Simulizi : Maskini Mayasa
Sehemu Ya Pili (2)
Mayasa aliendelea kujifanya hana hisia zozote kwa Damaso yaani kwa asilimia mia moja kwa mwonekano tu alikuwa kama yupo na mzazi wake tena wa kike.
Waliendelea kupiga soga mpaka muda wa chakula cha mchana ulipofika. Damaso alienda kununua mboga na kuanza kupika kwa kutumia jiko la gesi ila Mayasa akaomba apike yeye.
Baada ya kupika, Mayasa na Damaso walikula pamoja huku kila mmoja akimtazama mwenzake kwa jicho la wizi na kila walipokutana walijikuta wakicheka na kutabasamu kwa pamoja. Damaso aliona njiwa wake anazidi kusogea kwenye mtego mwenyewe. Kuna wakati unaweza kusema Damaso alikuwa sawa na fisi, Fisi ni mnyama mwenye uchu wa nyama sana sana lakini shida yake ni uoga na kibaya zaidi kuwinda alikuwa hawezi.Kula kwake nyama ni mpaka mnyama afe mwenyewe ndipo aokote mzoga na kuula.
Baada ya kumaliza kula Mayasa alimshukuru Damaso kwa chakula ila Damaso kama kawaida yake 'mzee wa kuruka kamba' yeye alisema kuwa anayepaswa kushukuliwa ni Mayasa kwa kupika chakula kizuri.
Damaso alisema huku akinyanyua bilauri iliyojaa iliyojaa maji,
"hakika siku ya leo nimekula chakula kitamu sana ambacho sijawahi kula hata siku moja tangu nije hapa Nachingwea mjini, pongezi kwako Mayasa kwa chakula kitamu ambacho kinanipa hamu ya kuendelea kukila hata kama nimeshiba"
"Mmmmh ! Damaso unapenda kunivisha kilemba cha ukoka wewe!!"
Baada ya chakula hicho , Damaso alikuwa wa kwanza kukaa kwenye sofa kwani alijua Mayasa naye atakaa kwenye sofa, Damaso alifanya hivyo ili akae karibu na Mayasa apate nafasi ya kumwambia huku akiwa karibu naye sana. Unajua mara nyingi hisia huja kwa haraka watu wakiwa karibu; ndio maana mtu anayejijua ana hasira kali, akiwa na hasira sehemu yenye ugomvi huwa anajitenga pembeni kuepusha kukaa karibu na aliyegombana naye ili hasira zisimpande zaidi.
Damaso baada ya kukaa kwenye sofa na Mayasa naye aliweka vyombo mahala pake na akakaa kwenye sofa. Sofa ya Damaso ilikuwa ni ya kukaa watu wawili hivyo mara baada ya Mayasa kukaa karibu na Damaso wakawa wapo karibu sana kiasi kwamba sehemu za mapaja yao zilikuwa zikigusana. Kama ilivyo kawaida ya mbwa aonapo nyama huwa mate yanamtoka ,ndivyo ilivyokawa kwa Damaso wakati huo. Jogoo wa Damaso alikuwa teyari ameshapata moto na kumfamya aanze kuhangaika pa kutokea ili amuone koo. Damaso alijaribu kujizuia ili Mayasa asiweze kujua hali aliyokuwa nayo.
Ila kuna wakati waswahili waliwahi sema kuwa 'dalili za mvua ni mawingu', Mayasa alimuuliza Damaso,
"vipi mbona kama unahangaika ? au umeshiba sana?"
Wakati huo mapigo ya moyo wa Damaso yalikuwa yanapiga danadana kama zile za mchezaji hodari na hatari wa Real Madrid anayeitwa Ronaldo.
Damaso akamjibu Mayasa,
" unajua mimi nina tatizo moja ,,yaani nimezoea kulala baada ya kula.....ila usijali nitakuwa sawa muda sio mrefu"
"Ooh sasa si ulale tu maana mimi nipo karibu kuondoka mida hii"
Damaso alishtuka kwa jibu la Mayasa la kutaka kuondoka maana lengo lake la kumwambia alichomwitia bado halikutimia.
Damaso akajifanya kama hajasikia vile akamuuliza tena Mayasa "kundoka?"
"Ndio"
"Mmmh mapema yote hii ,unaharakia nini nyumbani kwako? "
"Si nimeshakuambia Damaso ninakaa na dada na shemeji, mimi sikai kwangu kama wewe"
Damaso akaamua kujitoa ufahamu kwa muda . Akaamua bora kufunguka tu kwa Mayasa kile kinachomsibu ndani ya nafsi yake. Damaso akamwambia Mayasa ,
" samahani Mayasa, je ninaweza kukuomba kitu?"
"Mmmmh , Damaso chumba chako wewe alafu unataka uniombe kitu mimi?"
Mayasa alijibu jibu ambalo lilipoteza kabisa lengo la Damaso. Ila Damaso bado akajikakamua tena akasema,
" mmmh Mayasa, hujanielewa sijamaanisha kukuomba vitu ambavyo vipo ndani ya chumba hiki, namaanisha kuwa nahitaji unisaidie kitu kutoka katika moyo wako kwa kutumia maneno ya kinywa chako"
"Mmmh !! Moyo wangu tena, enheee una maana gani kusema hivyo?"
"Wewe niambie tu kama unaweza kunisadia, alafu nikuambie kitu chenyewe"
"Aya niambie ila msaada wangu utategemea na kile utakachoniomba, kama nitaweza nitakusaidia, nitafanya hivyo ila kama sitaweza sitakusaidia, aya sema"
"Kabla sijasema kitu chenyewe, hivi Mayasa wewe haujahisi chochote kutoka kwangu kwa muda wote ambao tumefahamiana na wewe?"
"Mmh !! Damaso,kuhisi tena! Labda niseme tu ninachohisi wewe ni mtu mkarimu sana na unajali wenzako"
"Hayo yote sawa ila sikumaanisha hilo"
"Ni lipi sasa unamaanisha?"
"Mayasa naomba unisikilize kwa makini kidogo, unaweza ukashangaa sana maneno yangu lakini maneno yangu yana maana kubwa sana kwako na kwangu.....Kila siku nilikuwa nikiwaza ni wapi nitampata mwanamke ambaye atakuwa mke wangu na mama wa watoto wangu, niliumia sana kuona simpati yule anayendana na mimi ila leo nina furaha kuwa mbele ya mwanamke ambaye nimetokea kumpenda kwa muda mfupi tangu nimuone, mwanamke huyo sio mwingine anaitwa Mayasa,, Mayasa naomba nitamke rasmi kwako kuwa nakupenda sana na nakuhitaji sana uwe mke wangu na tujenge familia bora, tafadhali naomba unikubalie ombi langu, nahitaji kuwa na amani moyoni na ili niwe na amani ni wewe ndiye mwenye dhamana ya kuikamilisha amani ya moyo wangu....tafadhali tafadhali sana Mayasa,nakupenda sana sana tena sana!"
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya maelezo marefu, Damaso akamwachia kijiti Mayasa ili aweze kujibu alichokizungumza. Lakini ajabu iliyoje ni kwa upande wa Mayasa ambaye wala hakuonesha kushangaa kwa kile alichoambiwa na Damaso yaani alikuwa kama tu amesikia taarifa ambazo hazimhusu hata kidogo, jambo ambalo lilimtia hofu sana Damaso na kuanza kuhisi kama Mayasa atakuwa amedharau kile alichomwambia . Damaso akamuuliza Mayasa,
"hivi Mayasa umenielewa nilichokuambia au nirudie tena maelezo yangu?"
"Nimekusikiliza ila sijakuelewa ni wapi sasa unataka nikusaidie kitu, maana mwanzoni ulisema kuwa unahitaji nikusaidie kitu, sasa kwa maelezo yako mimi hata sijui nikusaidie nini"
Damaso alishangaa sana kauli ya Mayasa.Alijjuliza mwenyewe kichwani mwake,
" ina maana maelezo yote yale hajanielewa nataka nini kutoka kwake? Mbona nimeshamwambia kuwa ninampenda sana na ninahitaji awe mpenzi wangu? Huyu mwanamke ana lengo gani hasa?"
Damaso akakubali kuwa mtumwa akaamua kurudia lengo lake la msingi kwa Mayasa,maana waswahili wanasema,
"mtafutaji hachoki.....”
Ambapo ni sawa na ule msemo wa kiingereza unaosema ,
" it is not done until it done"
Damaso akasema,
" Mayasa unafanya makusudi, yaani kweli hujanielewa nimemaanisha nini?.....ila ngoja nirudie na hata ukiniambia nirudie mara kumi mimi nitarudia tu.....Nakupenda sana Mayasa nahitaji uwe mke wangu, je upo teyari?"
Mayasa akagutuka kidogo kisha akauliza,
"unanipenda?"
"Ndio tena sana"
"Mimi nilidhani baada ya kujua wote tunatoka kijiji kimoja basi wewe utakuwa kaka yangu, sasa unataka kunifanya niwe mkeo?"
"Sio tu uwe mke wangu, nahitaji pia unizalie watoto na tujenge familia bora na ya mfano kwa rika zetu na hata kwa hao wazee walioharibu familia zao kwa ujinga ama kwa uzembe wao"
Mayasa alikaa kimya kwa muda mfupi huku akitafakari amwambie nini Damaso. Wakati huo Damaso alimuwa ameshavurugwa teyari,kwa kuwa walikaribiana sana,Damaso aliinua kichwa cha Mayasa kwani wakati huo alikuwa amejiinamia chini,baada ya kumwinua Damaso alianza kumsogeza Mayasa karibu yake zaidi na huku na yeye akipeleka mdomo wake kwenye mashavu ya Mayasa ili ambusu, ghafla Mayasa alisimama huku akiwa amepandwa na jazba kubwa akasema,
"Kwa hiyo Damaso unataka kunibaka?hiyo midomo yako unaipeleka mashavuni mwangu ili iweje? Nitakuchukia milele ooooh...."
Damaso alijisikia vibaya sana na akawa mtu mwenye aibu sana baada ya kuulizwa swali hilo na Mayasa, na jogoo wake aliyekuwa anawika wika ovyo alinyamaza mwenyewe na kutulia kabisa. Damaso alijilaumu uamuzi wake wa harakaharaka ambao haukuzaa baraka bali aibu.
Mayasa akamuuliza tena Damaso "Nakuuliza tena Damaso, kwa hiyo umeniita kwako ili uje kunibaka?"
Kwa unyonge na upole wa hali ya juu Damaso akasema,
"Mayasa siwezi kukubaka wewe hata siku moja,kwanza nitaanzia wapi?"
Mayasa akadakia hapohapo hata kabla Damaso hajamaliza kusema "utaanzia wapi? Si ndo ulikuwa unaanza hapo!?"
"Hapana Mayasa sikuwa nataka kukubaka bali niliinua kichwa chako ili nikuone, maana nilikuwa nakuona umeinama sana chini,...ila yote hiyo ni kwa sababu nahitaji sana kuwa na wewe, tafazali sana Mayasa naomba unikubalie"
Mayasa alitulia kidogo kisha akakaa kwenye kitanda(muda huo hakukaa tena kwenye sofa kama alivyokaa mwanzo). Mayasa alimwangalia kidogo Damaso usoni kwake (Mayasa alifanya hivyo kwani aliwahi ambiwa na mwalimu wake ukitaka kumgundua mtu muongo mwangalie usoni kipindi unaongea naye utagundua kupitia wasiwasi aliokuwa nao) kisha akamuuliza Damaso swali,
" hivi una hisi mimi ndiye mtu sahihi kwako?"
"Kwa aslimia zote zilizopo duniani, wewe ndio mtu pekee unayeweza nipa furaha ya moyo wangu"
"Na umejuaje kuwa mimi ni sahihi kwako maana ni muda mchache tu tangu nikutane na wewe!!?"
"Mayasa, mapenzi hayana muda maalumu wa kuyathibitisha kama ndio muda wake,watu wanaopendana hukutana katika mazingira ambayo hata wao wenyewe hawayakuyatarajia,moyo wa mwanadamu ni kama sumaku ,huvuta na kuwa karibu kwa watu wanaendana nao.......Tangu nakutana na wewe nilikuangalia sana na nimegundua kuwa wewe una sifa zote ambazo wanawake wengi hawana za kuwa mke, sihitaji kuendelea kuumia ndio maana nimeamua kukuambia mapema tu ili ujue jinsi ninavyopata tabu ya nafsi ya kukufikiri wewe kila wakati, nakuhitaji sana zaidi ya unavyonifikilia"
"Mmmh !!! Damaso......"
"Mayasa niambie basi kama unanipenda basi"
Akiwa katika sura ya udadisi , Mayasa alimuuliza Damaso ,
"Je nikikuambia jibu wakati huu unahisi litakuwa sahihi? "
"Sasa unatakaje?"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nipe muda kidogo, nami nijipe nafasi ya kukufikiria ndani ya moyo wangu"
"Mmmmh,mpaka lini Mayasa,mwenzio nitazidi kuumia sana, naomba unijibu sasa hivi basi......"
"Damaso Damaso, kwa nini hunielewi?, Wewe ulianza kunifikilia mimi tangu siku zilizopita lakini mimi ndio kwanza unaniambia kitu kipya kabisa ambacho sikuwahi kukiwaza kabla ya leo, inabidi nami nikauulize moyo wangu kwa kutumia medula oblangata yangu ili nione kama moyo utachanua na kuachia nafasi ya kukaa Damaso au kama utasema hakuna nafasi hiyo,,lakini kama unataka nikujibu jibu lolote niambie nikujibu tu hapahapa......"
Damaso akaona isiwe tabu akakubali kuwa mshindwa katika hilo ilimradi tu amsimkwaze tena Mayasa, Damaso akasema,
"basi sawa Mayasa mimi nakuacha ukanifikilie ila nikuhakikishie tu kuwa Damaso ninafaa kuwa mume wako na nitakupenda sana, kama ukinipenda kamwe hutaliona chozi lako la uchungu litakalosababishwa na mimi"
Mayasa alikuwa anamsikiliza kwa makini sana huku akimwangalia usoni, Mayasa kamwambia Damaso kuwa anataka kuondoka na siku akiwa teyari kumjibu atamwambia.
Damaso akamkubalia na akampigia simu dereva bodaboda ili aje kumchukua Mayasa na kumrudisha kwake.
Mayasa alipofika nyumbani kwao. Aliingia moja kwa moja hadi chumbani kwake na kujilaza chali huku akitafakali juu ya kauli ya Damaso. Hakupata jibu harakaharaka la kumjibu Damaso. Kitu kilichomjia haraka haraka kichwani mwake ni kumshirikisha dada yake kwani ndiye mtu anayeishi naye na ndiye mwongozo wake kwa mambo yake mengi.
Nyakati za usiku wakati wanapata chakula cha usiku, Mayasa alimuuliza dada yake swali "Hivi dada ni wakati gani ni sahihi kwa mtu kuwa mke au mume?"
Dada yake na shemeji yake kwa pamoja wote walishtuka kwa pamoja kisha dada yake akamuuliza swali,
"unaposema wakati gani una maana gani?"
"Maana yangu ni muda upi, yaani mtu akiwa teyari amefanikiwa kimaisha au kipindi anatafuta maisha au muda wowote akimpata mchumba?"
Shemeji akatabasamu kisha akasema,
"shemu wangu vipi umempata nini!!?"
Mayasa akacheka kisha akasema , "hapana shem wangu nataka kujua tu"
Dada akatia neno lake "Mayasa mdogo kwa nijuavyo mimi mapenzi huwa hayana kanuni mara nyingi huwa yanachanua tu palipo na udongo wenye rutuba"
Shemeji wa Mayasa akadakia akasema,
" kwenye mapenzi ukiweka vigezo, ooooh mara niwe na nyumba mara sijui niwe na gari, nakuhakikishia utakaa miaka yote bila kuolewa wala kuoa"
Mayasa alikuwa akiangalia tu vita ya mawazo kati ya dada yake na shemu wake.
Mayasa akauliza swali
" kwa hiyo mtu akipendwa inabidi naye apendeke wakati huohuo?"
Mama vumi ,dada yake alicheka kidogo, kile kicheko cha umbea kisha akasemaakasema,
"Mayasa teyari huyu jamani ashapata, maana hata siku moja hajawahi zungumzia haya mambo......mmmh hebu tuambie mwenzetu umempata nani"
Baba vumi alicheka kisha akasema "mmmh mama vumi acha umbea wewe unataka mjue ili iweje"
Mayasa aligutuka kidogo lakini aliendelea kukaa kimya huku akiwaangalia tu lakini kichwani mwake akimfikilia Damaso alichosema na alijiuliza kama awaaambie au la, lakini alikuwa na hofu kidogo kwani ingawa walikuwa wanasema kwa matani lakini kiukweli teyari kuna mtu alikuwa amejitokeza kwa Mayasa.
Dada yake alihisi kitu akasema "Mayasa sema ukweli maana sisi ndio watu wako wa karibu wa hapa, ulichouliza leo umelenga nini hasa?"
Mayasa akaona hana sababu ya kuendelea kuficha kitu ikabidi afunguke tu , maana mficha magonjwa kifo humwumbua, Mayasa akasema,
"Jamani mimi nimekutana na kijana mmoja hivi ,amesema ananipenda sana na anataka kunioa"
Baba vumi akasema,
"si unaona mambo mazuri hayo, enhee shemu wangu nambie yuko wapi kaka yangu huyo?"
Mama vumi akiwa katika hali ya umakini akadakia,
"Afu wewe baba vumi unashabikia tu wakati unawajua watoto wa mjini hapa walivyo wahuni, kazi yao wanakupa mimba kisha wanakimbia"
"Sasa mke wangu si ndo tumuulize sasa huyo mtu ni wa wapi?"
Mayasa akadakia,
"jamani hamna sababu ya kubishana wala kulumbana wakati suala lenyewe mimi ndio nimelileta hapa, huyo kijana amesema yeye kwake ni kulekule mitaa yetu, kwao ni Luponda"
"Enhee kwa hiyo wewe umemwambia nini?" Dada yake alihoji.
"Nimemwambia kuwa siwezi kumpatia jibu langu mpaka nichanganue akili yangu juu yake ndipo nimpe jibu ambalo litakuwa bora sana"
Dada yake Mayasa akagutuka kidogo ,kisha akasema,
"Mdogo wangu Mayasa,sikiliza nikuambie kitu ,kwa sasa nakuomba malizia mafunzo yako ya ushonaji na hapo baadae ukimaliza utakuwa na uhuru wa kufanya maamuzi sahihi, kwa sababu unaweza kumkubalia alafu akakupa ujauzito kisha akakutelekeza na usijue nini cha kufanya na ikawa majuto ni mjukuu"
Baba Vumi akacheka sana kisha akasema ,
"mke wangu , kwa hiyo huyo kijana muda wote huo anamsubiri tu ndugu yako amalize mambo yake ndio amuoe??!! Haa haa unampoteza ndugu yako, kitu cha msingi hapa ni kumjua mtu mwenyewe kama kweli anampenda Mayasa na pia tumuulize Mayasa kama ana upendo kwa huyo kijana kisha tuone namna ya kuwaweka pamoja hawa kwani Mayasa ni mtu mzima sasa!!"
Baba Vumi akamuuliza Mayasa "kwani huyo mtu mwenyewe unampenda au?"
"yaani mimi sijui hata nifanye nini,sijui kama nampenda au simpendi maana najiona niponipo tu"
Baba Vumi alicheka sana kwani alikuwa anashangaa jibu la Mayasa yaani hajui kama mtu anampenda au la.Ila baadae Mayasa aliwaeleza kuwa mtu mwenyewe anaitwa Damaso na ndiye fundi ambaye aliwahi fika nyumbani kwao kutengeneza kitasa.
Dada na shemeji yake waliishiwa na maneno baada ya kusikia mtu mwenyewe ni yule fundi ambaye aliwatengenezea kitasa alafu akawa anakataa ela ya matengenezo wakabaki wanatazamana tu na kutabasamu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mama Vumi akasema ,
" kama kijana mwenyewe ndo huyo binafsi sina kipingamizi kwasababu nilimuona tu kwa jinsi anavyoongea ni kijana mwenye busara sana, yule ni mume haswaa!"
Maneno ya mama vumi yakapigiliwa msumari na baba Vumi ,
"kama ni huyo ,ooooh hata busara zake nafikiri ni nyingi kuliko zangu,ni aina ya wanaume wanaotafutwa na wanawake wengi hapa duniani na wasiwapate, kama amekuja kwako basi ni bahati kubwa sana shemu wangu"
"Kwa hiyo mnaniambiaje sasa?"
Mayasa aliwauliza.
Mama Vumi akasema,
"mimi sina ushauri juu ya nani awe mume wako,kwani moyo wako ndio unajua nini unataka, kama unamtaka huyo kijana, mwambie aje hapa nyumbani tumuone"
Baba Vumi naye alisisitizia maneno kama aliyoyasema mkewe na Mayasa aliona bora amwite Damaso aje nyumbani kwao.Mayasa ingawa alikuwa hajui moyo wake unasemaje kuhusu Damaso ila sifa za Damaso zilimpendeza sana na kila alipomkumbuka alijikuta akitabasamu lakini moyo wake bado ulikuwa upoupo tu kama mzoga wa mbwa,yaani haujui wapi uegemee.
Siku iliyofuata Mayasa alimpigia simu Damaso na kumwelekeza kuwa jumamosi au jumapili aende nyumbani kwao ili akaongee na dada yake. Kwa upande wa Damaso, alizipokea kwa furaha kubwa taarifa hizo za kuitwa nyumbani kwa Mayasa kwani moyo wake ulikuwa unamwitaji Mayasa kwa hali na mali ili awe mke wake,hata kama hakujua dada wa Mayasa anataka aseme nini lakini alifurahi kusikia anaitwa kwao Mayasa .
Siku ya jumapili asubuhi na mapema Damaso alimpigia simu Mayasa na kumwambia ataenda kwao siku hiyo mara baada ya kumaliza shughuli zake za usafi.
Mayasa naye kwa nafasi yake akawaambia dada na shemeji juu ya ujio wa Damaso.
Saa tano kamili asubuhi juu ya alama , Damaso aliwasili kwa Mayasa akiwa amevalia suluali yake nyeusi ya kitambaa na shati la mkono mifupi,huku akiwa amechomekea vizuri kama wapendavyo kuita watu 'mkanda nje'. Mayasa ndiye aliyempokea kwani mara baada ya kufika nyumbani kwa Mayasa, akiwa nje ya nyumba alimtumia sms Mayasa kuwa yeye yupo nje ndipo Mayasa akatoka nje na kumkaribisha.
Mama Vumi na Baba Vumi walimsalimu yule kijana(Damaso ) na kumuuliza mambo kazaa kuhusu maisha yake . Damaso aliongeza utulivu wakati anajibu maswali kitu ambacho kilimwongezea nafasi ya kupendwa na familia hiyo. Baba Vumi akasema,
"bwana Damaso sisi tumepata taarifa zako kutoka kwa Mayasa kuwa unahitaji kumchukua Mayasa akawe mkeo, je ni kweli?"
"Kabisaaa! ni kweli, hata Mayasa ni shahidi wa hili nilisemalo kwani yeye nilimweleza kila kitu kuhusu moyo wangu unawaza nini juu yake"
Baba vumi akamgeukia Mayasa na kumuuliza ,
"Mayasa umemsikia mwenzako ,je na wewe unasemaje?
"Mimi sina tatizo kwa kuwa nimefikilia wiki mzima jambo hili,na kugundua kuwa Damaso kweli ana lengo nami,kuna vitu vingi nimevipima kutoka kwake bila yeye kujua na nimejiridhisha anafaa kuwa mmoja miongoni mwa familia yetu".
Mayasa alimwamini Damaso kutokana na tabia yake ya upendo, na ndio maana wenye busara wanasema 'tabia njema ni silaha', lakini pia kilichomvutia Mayasa kwa Damaso ni usafi alionao Damaso,kuanzia yeye mwenyewe hadi ndani mwake mulipendeza sana na hivyo kumfanya Mayasa kuamini kuwa Damaso ni mtu ambaye anayejipenda kwa hiyo kuwa na mtu wa aina hiyo ni rahisi sana kumpenda na mwenzake.Katika maisha ukiwa na mwonekano mzuri yaani kujipenda hata kama huna kitu watu watakuogopa ila ukiwa mchafu mchafu watu watakuzarau na ndicho kilichotokea kwa Damaso,usafi wake umemfanya Mayasa kuvutiwa naye.
Mama Vumi akasema,
"mimi binafsi nimefurahishwa na jibu lako maana haya maamuzi ni yako mwenyewe na umesema kuwa umefanya uchunguzi juu ya upendo wa huyu kijana kwako na umesema ni sahihi, basi kilichobaki sasa ni huyu kijana kufanya mipango ya kujitambulisha kwa mzee Diko ili sasa watu wote wamtambue mume wa Mayasa"
Damaso alifurahi sana kusikia maneno ya mama Vumi na wote kwa pamoja walikubaliana kuwa Damaso sasa akawaambie wazazi wake ili mipango ya utambulisho itimie.
Damaso alirudi nyumbani kwake siku hiyo kwa furaha sana. Damaso alipanga kwenda nyumbani kwao kuwaelezea habari hizo kisha wafanye mipango ya kuonana na familia ya akina Mayasa. Jambo la kwanza Damaso alimpigia simu baba yake na kumwelekeza kila kitu, baba yake hakuwa na tatizo alibariki kila kitu na pia akampigia simu mama yake na kumweleza, pia mama yake hakuwa na pingamizi sana lakini yeye alisisitiza akawasikilize na babu na bibi yake wanasemaje kuhusu hilo jambo. Damaso aliona sasa kazi imeisha akapanga jumamosi ijayo aende huko kijijini kwao akawaeleze na kuyamaliza haya mambo mapema sana ili ajipatie jiko lake.
Wiki yote Damaso alitafuta pesa ya kwenda nayo huko kijiijini kwao kwani kama wataenda kujitambulisha ni lazima wabebe na pesa ambayo itakaa kwenye barua ,na kwa utamaduni wa kijijini kwao ni lazima kifanyike kitu kama hicho yaani huitwa pesa ya barua, kwa kipindi hicho sehemu nyingi ilizoeleka pesa ya barua ni shilingi elfu hamsini.
Siku ya ijumaa, siku moja kabla ya siku ambayo aliipanga kwa safari(jumamosi), Damaso alikuwa amepumzika chumbani kwake
wakati wa mchana alipitiwa na usingizi.Akiwa katika usingizi mzito Damaso aliota ndoto kama aliyowahi kuota siku chache zilizolizopita, kila kitu kilifanana na ndoto yake ya mwanzo lakini kwa ndoto ya siku hiyo kiliongezeka kitu kimoja.Siku hiyo aliota mke wake amejifungua watoto mapacha watatu lakini wote walikufa mara baada ya kujifungua. Damaso alishtuka kutoka usingizini na kujikuta yupo chini ya kitanda ingawa mwanzo alikuwa yupo juu ya kitanda.Hali hiyo haikumshangaza sana kwani alihisi labda alianguka kipindi anajigeuzageuza na hata ndoto yenyewe pia haikumshangaza wala kumtia hofu kwani hapo mwanzo aliambiwa na jirani yake kuwa mtu akiwa kwenye mawazo sana na kitu fulani basi hata ndotoni muda mwingine humtokea. Maneno ya jirani yake ndiyo yaliyompa ujasiri Damaso na kuamini kuwa ndoto zote alizoota zilikuwa ni za kawaida tu na wala sio kwamba labda zina ukweli fulani juu yake.
Ilipofika jioni ya siku hiyo, Damaso alienda kwa kina Mayasa ili akawaelekeze juu ya safari yake ya kwenda kijijini kwao. Alipofika aliwakuta na kuwaelekeza kila kitu jinsi alivyopanga, pia aliwaambia na Mayasa naye inabidi asafiri aende kijijini kwao ili siku atakayoenda Damaso kupeleka barua ya uchumba basi wakumte akiwa kwao.
Damaso alisafiri hadi kijijini kwao Mnero, alipofika alipokelewa vizuri na wazazi wa mama yake yaani babu na bibi yake. Damaso aliwasilimu na bila kukawia alikaa nao chini na kuzungumza lengo lake la kwenda huko huko kijijini .
Damaso alisema,
"bibi na babu yangu, mimi mjukuu wenu nimesikiliza kilio chenu cha mda mrefu na sasa nafurahi kusema kuwa nimempata mke ambaye atawazalia vitukuu, nampenda sana na ninafurahi kuwa na yeye ananipenda"
Babu na bibi yake Damaso walitazamana kisha wakatingisha kichwa kila mmoja kwa nafasi yake, baada ya hapo bibi akamuuliza DamasoDamaso
"Damaso mbona taarifa yako inakuja nusunusu?"
"Nusunusu !!? , kivipi bibi?"
Babu akadakia akasema,
" bibi yako anataka useme moja kwa moja, yaani huyo mke ni wa wapi? ni kabila gani? Wazazi wake ni akina nani?....hilo ndilo analotaka kusikia bibi yako"
"Haaa haaa ,,jamani hayo si ndo mambo yanayofuata baada ya taarifa yangu ya awali, nyie ndio kila kitu kwangu ni lazima niwaeleze, Huyo mwanamke anaitwa Mayasa na nimekutana naye huko mjini"
Babu na bibi wote walishangaa na kushtuka kwa pamoja walisema kwa mshangao ,
"mjini!!"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Ndio nimekutana naye Nachingwea mjini, mbona mnashtuka kwani kuna tatizo?"
"Huna adabu wewe mtoto!!....tena unajibu bila kuwa hata na aibu 'mjini'...sisi tulikuambia nini juu ya kuoa?, Neema huyu mtoto wa Nyaga jirani yetu mbona alikuwa anakusubiri wewe na tena wote sisi ni kabila moja alafu wewe unatuletea wahuni wa mjini huko, mjinga sana wewe mtoto"
bibi yake Damaso alifoka kwa hasira sana baada ya kusikia kuwa mke wake Damaso anakaa mjini, bibi huyo aliamini kuwa mtu akikaa mjini anakuwa mhuni na wala hana tabia mzuri. Bibi aliendelea tena mbele kusema ,
"kwanza watu wa mjini hawajui kufanya kazi, hawajui kulima!, hawajui kuchota maji! Hawajui kuwatunza ndugu wa familia yako!, lakini tazama huyu Neema alivyokuwa mfanya kazi hodari, ana nidhamu kwa kila mtu na uzuri zaidi ni jirani yetu na wote ni kabila moja, Damaso acha mambo ya kijinga, utamuoa Neema na ndio mke bora kwako, hayo mambo ya mjini mimi sitaki kusikia hapa na usirudie tena kuongea hilo mbele yangu"
Damaso alikaa kimya huku akimwangalia bibi yake akivyotokwa na povu mdomoni kwa kuongea sana. Damaso aliamini kuwa na busara hakuhitaji mtu awe na umri mkubwa bali ni kunahitaji kuwa na maarifa na ndio maana unaweza ukawa na umri mkubwa lakini usiwe na busara lakini ukakuta kijana mdogo tu lakini ana busara kuliko mzee,lakini hiyo haifanyi kuwapuuza wazee ambao hawana busara kwani wahenga wanasema ,
"jungu kuu halikosi ukoko na koti la babu halikosi chawa"
Babu yake alikuwa amekaa kimya tu, aliyekuwa anaongea sana ni bibi yake, na hivyo ndivyo ilivyokawa desturi ya familia hiyo, bibi ndio alikuwa ana nguvu sana ya kimaamuzi kuliko babu yake. Na hiki ndio kitu kilichowashangaza watu wengi sana pale kijijini kwao juu ya familia hii, yaani hata wanawake wa familia hiyo walikuwa wakiolewa tu basi wanakuwa ndio wasemaji wakuu kwa waume zao, watu walijiuliza sana kwa nini inatokea vitu kama hivyo lakini hawakupata majibu na waliishia kusema,
"sio bure kuna kitu tu"
Damaso akamuuliza bibi yake "kwa hiyo watu wote wanaokaa mjini ni wahuni?"
"Ni wahuni sana, kwani watumia madawa ya kulenya wanakaa wapi? Wanawake wanaojiuza wanakaa wapi? Majambazi wanakaa wapi? Vibaka wanakaa wapi? Mafisadi wa nchi hii wanakaa wapi? Na wengine wabaya wote wanakaa wapi unazani kama sio hukohuko mjini?"
"Sawa bibi yangu nimekuelewa ila Damaso mjukuu wenu anakaa hukohuko mjini kwa sasa ina maana naye sasa mumeweka kwenye kundi la wahuni?"
"Hapana, wewe Damaso umelelewa hapahapa na sisi, hivyo huwezi kuwa muhuni kwa sababu umetokea kijijini"
Damaso huku akiwa katika hali ya tabasamu akasema,
"Oooh kumbe anayetokea kijijini akienda mjini bado anakuwa na tabia njema!! Basi na mimi mke wangu matarajiwa anatokea kijijini tena hapo Ruponda jirani tu na kwetu, kwa hiyo wazee wangu ombi lenu la kutaka kuoa mwanamke wa kijijini bado lipo na nimelitimiza kuna swali?"
Babu na bibi walikaa kimya kidogo baada ya kusikia maneno ya Damaso, walishindwa wamjibu nini kingine juu ya Damaso kuoa mwanamke wa kijijini. Katika maisha kuna wakati unaweza ukatafuta kosa kwa mtu ili umkwamishe lakini usilione. Ila bibi yake Damaso alikuwa ni bibi asiyekubali kushindwa na watoti wake walimpachika jina na kumwita "Ashindikene" kwa lugha ya kiyao likiwa na maana ya "ameshindikana" ,Bibi Damaso akamwambia Damaso ,
"hata kama na yeye anatoka kijijini, sisi hatumjui na bila shaka hawezi kumzidi Neema kwa tabia njema hata siku moja"
Damaso akiwa katika ya kuchukia akamuuliza bibi yake ,
"kwa hiyo bibi .....wewe unataka niumoe nani?"
"Neema, hakuna mwingine tena hapa kila siku yeye ndio alikuwa anatuchotea maji na kama unavyotuona sisi bibi zako hatuna nguvu sasa za kwenda kuchota maji huko visimani, mjukuu wangu wakubwa ni jalala wasikilize wao kwani wanajua mengi kuliko wewe"
"Kumbe ulikuwa unazunguka zungukaaaa weee!, mara mjini hutaki kumbe unataka nimuoe Neema huyu binti jirani yetu ! ,, Ni jambo zuri sana wazee wangu kunishauri vitu vizuri kama hili jambo ambalo mmeniambia,kwani watu husema ukimuona nyani mzee basi ujue amekumbana na vikwazo vingi na wengine huenda mbali zaidi na kusema amekwepa mishale mingi hivyo naamini hata nyinyi pia mnajua vitu vingi kuhusu wanawake bora wa kuolewa kuliko mimi kwa sababu miaka yangu mimi labda nizidishe mara tatu au nne ndipo niikute yenu na mna kila sababu ya kunishauri jambo jema lolote nilifanyalo , lakini inapofika kwenye suala la maamuzi hilo linabaki kwangu na niseme tu teyari moyo wangu umechanua na kufungua milango kwa Mayasa na nyinyi hata mukimuoana huyo binti mtafurahi sana na pia ninaposema hayo ya Mayasa sina maana ya kwamba Neema ni mbaya au hana sifa za kuolewa,la hasha!! Maana yangu ni kuwa upendo ni sawa na mtu kupiga chafya, yaani ni tendo linalotokea kwa ghafla bila mtu kulipanga, ninavyojua na ndivyo ilivyo hata siku moja huwezi kupanga upendo wa ukweli, bali huja wenyewe na ilivyokuwa kwangu mimi kwa Mayasa yaani nimejikuta tu nampenda na kuhusu Neema wala sijawahi kufikilia hicho kitu kwani sina hata hisia naye na naamini hata nikikaa naye kamwe hatuwezi kudumu kwakuwa sitakuwa na unyenyekevu kwake bali ni maigizo tu ambayo kuna muda yatafika ukomo.......kwa hiyo babu na bibi, mimi nipo teyari kuoa na mke nimempata teyari , ujio wangu mkubwa nawaomba ikiwezekana babu anipeleke ndani ya siku mbili tatu hizi kwa wazazi wa Mayasa ili tukaunganishe familia zetu na kuwa kitu kimoja kwa maana ya kuwa kitu kimoja sasa"
Bibi yake alikuwa anatikisa kichwa kwa masikitiko sana kipindi Damaso anaongea, baadae bibi akasema ,
"yaani huko mjini kumekubadirisha sana, wewe Damaso ulikuwa mtu usiyenipinga yale ninayokuambia lakini leo nakushangaa sana yaani umekuwa mwongeaji sana na mpingaji wa kila jambo"
Babu baada ya ukimya sana akaamua kutia neno,
"akasema mke wangu hili jambo naomba tulizungumze usiku alafu asubuhi tutaongea na Kijana wetu Damaso"
Damaso aliwatahadharisha kuwa wajadili ila watumbue kuwa uamuzi utabaki kichwani mwake, hivyo wakati wakiendelea kujadili basi watambue kuwa wasije na wazo la kumuoa Neema.
***
Mayasa alifika nyumbani kwa wazazi wake salama. Baada ya kufika wazazi wake walishangaa sana kufika kwake bila taarifa na pia kwa ghafla.
Kabla hata Mayasa hajasema kitu, baba yake,Mzee Diko alisema "afadhali umefika mwenyewe ama kweli kila jambo lina wakati wake, kuna kijana alikuja hapa kutaka kukuoa na alitaka kuacha na barua kabisa ila tukamwambia asubiri mpaka wewe uje, kwa hiyo ni kama bahati vile, umefika wakati mwafaka"
Mayasa aliposikia habari hizo alifurahi sana kwani yeye alijua Damaso atakuwa alikuja nyumbani kwao na alijua kuwa Damaso hakuwa anatania bali kweli kabisa alitaka kumuoa.
Mayasa kwa harakaharaka aliuliza "Eeeh jamani vipi sasa kwa nini hamjamkubalia?"
Mzee Diko akasema,
"Mwanangu Mayasa hatukuweza kumkubalia kwasababu wewe wala hujamuona hivyo tuliona bora mpaka uje mwenyewe uli umuone kama atakufaa"
Mayasa aliona wazazi wake wameanza kuachana na mila zilizokwisha mda wake, maana hapo awali alikuwa mtu akitokea wa kutaka kuoa mmoja katika familia yetu basi ilikuwa baba ndiye anayeamua hivyo kwa upande wa anayechumbuiwa ilikuwa utake usitake ni lazima ukubali maamuzi ya mzee wao.
Baada ya kutulia kidogo Mayasa akasema ,
"Wazazi wangu , kipindi naendelea na mambo yangu yale ya ushonaji nilikutana na kijana ambaye amenitaka niwe mkewe na alifika hadi kwa dada akaongea naye, dada alimwambia aje huku nyumbani ili ajitambulishe na ajulikane rasmi.Huyo kijana ni wa hukuhuku kwenye hivi vijiji vyetu ila yupo mjini anfanya shughuli zake,sasa nilipofika na kuzikuta habari za huyo kijana kuwa alifika hapa wala sikuzishangaa sana kwani teyari nimekutana naye"
Mama Mayasa akasema "mwanangu umefanya jambo jema sana kuolewa na mtu anayetoka kijiji kimoja na wewe"
Wakati huohuo Mzee Diko akawaaga kuwa anaenda shambani na wakati anarudi atapita kwa familia ya yule kijana aliyefika kumchumbia Mayasa ili ampe taarifa za Mayasa kuwa teyari ameshafika mtu aliyekuwa anamuulizia na ikiwezekana basi kesho yake waende kwa Mzee Diko kuyamaliza hayo masuala. Mayasa alishangaa sana kwa jinsi wanavyosema wazazi wake(baba yake) kuhusu huyo kijana kwasababu yeye Mayasa anatambua fika kama Damaso anaishi kijiji cha jirani ila Mayasa alikuwa mpole kumsubiri tu maana kama siyo yeye macho yake basi yataona.
***
Asubuhi na mapema sana, Damaso aliamshwa na babu yake. Alipotoka nje ya chumba chake aliwakuta babu na bibi yake wakiwa sebuleni,aliwasilimia na kukaa kwenye mkeka.Damaso alishangaa sana kuwaona wazee hao wakiwa wenye tabasamu sana asubuhi hiyo. Babu akamwambia Damaso kuwa wapo teyari yeye akaoe huyo binti wa huko Ruponda aliyemtambulisha kwao kama Mayasa. Damaso aliendelea kuwashangaa sana na asijue nini walichojadili usiku mpaka siku hiyo wakakubali ombi lake la kutaka kuoa mtu mwingine kabisa tofauti na waliyomtaka wazee hao.Kilichomshangaza zaidi ni bibi yake amabaye alikuwa na tabia ya kung'ang'ania mambo, Damaso hakutaka kujua sana kuhusu walichojadili usiku lakini yeye aliangalia tu alichokitaka ni yeye kuruhusiwa kuoa mwanamke anayemtaka yeye mwenyewe.Babu yake Damaso ambaye alikuwa anatambulika sana kijijini hapo kwa jina la Mzee Nongwa, alimuuliza Damaso,
"vipi sasa tunaweza kwenda leo kwa wazazi wa huyo binti?"
"Na hilo ndilo lengo langu yaani umeniwahi tu kusema,natakiwa niwahi leo maana kule mjini kuna kazi nilipewa kuifanya hivyo nahitajika kutochelewa huku ili nikaimalize kwa wakati ili nijenge uaminifu kwa wateja wangu kwani sisi mafundi tuna sifa mbaya sana ya uongo, sasa lengo langu ni haya mambo yakamilike leo leo"
Mzee Nongwa akamwamabia hakuna tatizo, akamwelekeza Damaso achukue karatasi na kuandika yale ambayo alikuwa anayasema yeye Mzee Nongwa. Baada ya kumaliza kuandika wakachukua bahasha na kuiweka ile barua pamoja na shilingi elfu hamsini.
Baada ya kunywa chai, Damaso na babu yake walianza safari ya kwenda Ruponda kwa kutumia usafiri wa baiskeli. Walipofika Ruponda walianza kuulizia kwa Mzee Diko ni wapi na walimpata kijana mdogo hivi akawapeleka.
Asubuhi hiyohiyo nyumbani kwa mzee Diko walifika wageni.Mayasa alishangaa sana kumuona kijana ambaye siyo Damaso.
Mzee Diko ndiye aliyemtambulisha kijana huyo kwa Mayasa na kusema ,
"Mayasa huyu ndiye kijana aliyefika jana kukuulizia na jambo zuri leo amekuja tena hapa nyumbani kutoa pesa ya barua na hata hivyo kwa kuwa umesema mwenyewe kuwa mmekutana na kuyaongea basi sisi hatuna neno la kupinga zaidi ya kubariki tu mahusiano yenu"
Mayasa alishangaa sana na kujiuliza hivi kweli huyu ndio Damaso, lakini alijipa moyo wa subra na kujisemea moyoni labda ndio yeye kwa kuwa hajakaa sana na Damaso hivyo inawezekana sura yake bado hajaikariri usoni mwake. Simu ya Mayasa iliisha chaji pengine angejaribu kupiga namba ya Damaso ili aone kama ndio yeye.
”Mmh kwani mimi kipofu au? Huyu sio Damaso " mayasa alijisemea moyoni mwake.
Mzee wa yule kijana (mshenga) akaitoa barua palepale na kumkabidhi Mzee Diko. Mzee Diko aliamua kuingia ndani kuifungua barua na alikuta pesa shilingi laki moja pamoja na barua. Kisha akarudi sebuleni akawaambia kuwa barua yao imepokelewa na kwa upande wa mahali aliwaambia watoe shilingi laki saba pamoja na shuka mbili na koti moja na mbuzi mmoja.
Wakati wakiendelea kuongea ghafla uliingia ugeni mwingine na wageni hao walikuwa ni Damaso pamoja na babu yake.
Mayasa alishtuka baada ya kumuona Damaso halisi na hapo aliweza kumtambua bila shida yeyote kama ilivyokuwa kwa huyu kijana ambaye kwa wakati huo teyari barua yake ilishapokelewa na wazazi wake. Walikaribishwa na kukaa sebuleni nao. Wote walisalimiana, baada ya hapo , Wale wageni wa mwanzo kabisa walimuuliza Mzee Diko,
"Sasa Mzee Diko naona una wageni, je kuna kitu kingine cha kuendelea kukifanya au tayeri tumeshamaliza ili tukupe nafasi ya kuongea na wageni wako?"
"Kwa sasa kama munayo hiyo mahali mnaweza mkanipa sasa hivi na nyinyi mkaondoka na mke wenu"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wale jamaa kwa kuwa walikuwa wana uwezo walitoa laki tano hapohapo na kuhaidi watamalizia kiasi kilichobaki baada ya wiki moja lakini kabla Mzee Diko hajazipokea Mayasa akasema "baba na mama yangu niliwaambia kuhusu kijana mmoja ambaye nimekutana naye mjini......"hapo hapo akakatizwa na Mzee Diko "Mayasa si ndo huyu teyari!!!?, hayo unayotaka kuongea hayana msingi sana kwani teyari tumeshayamaliza hapa"
Damaso alishangaa sana kauli ya Mzee huyo ambaye hata kabla ya utambulisho alishajua teyari ndiye baba wa Mayasa.
Mayasa akasema tena,
"baba kuna jambo nataka kusema, ni kwamba niliyemzungumzia mimi sio huyo aliyetoa barua bali ni huyu aliyefika sasa hivi"
Watu wote waliokuwepo ndani humo walishangaa sana isipokuwa Mayasa mwenyewe.
Ndipo baba yake Mayasa akasema kwahiyo wewe ulikaa kimya mpaka tunapokea ela ya barua kwa nini hukusema sio huyu?"
"Jamani naomba mnisamehe yaani nilipofika hapa jana mliponiambia habari za kijana kuja kunichumbia nilijua ndiyo huyu Damaso kwani alisema atafika nyumbani, sasa nilipomuona huyu kijana nilishtuka lakini kwakuwa sijakaa mda mrefu sana na huyu Damaso na bado sijamkariri vizuri basi nilizani labda ndio yeye ndio maana sikusema kitu,naomba mnisamehe kwa usumbufu uliojitokeza na huyu ndiyo Damaso aliyenifanya nije kutoka mjini hadi hapa"
Mzee Diko alishangaa sana na akaona kama amehaibishwa vile na Mayasa na wala hakujua afanye nini kwa wakati huo, aliamua kuwauliza "sasa jamani tunafanyaje?"
Yule Mzee wa mwanzo aliyefika kabla ya akina Damaso alisema "sasa Mzee Diko si teyari umeshapokea barua yetu, yakupasa utupatie tu huyo binti yako na hawa kwa kuwa hawajatoa chochote, wakatafute sehemu nyingine"
Kauli hiyo ilibadiri hali ya hewa ndani ya nyumba ya mzee Diko.
Damaso na babu yake nao wakapigwa na butwaa, babu yake Damaso akasema,
“Damaso, bibi yako alishakuambia kuwa yupo Neema yule jirani yetu anakufaa,sasa ona tunavyodharirika hapa,hebu tuondoke hapa tuwaachie binti yao"
Damaso naye akiwa na hamaki akasema,
“Wewe Mayasa kwanini sasa umetupotezea muda wetu? Hivi mpaka unapokea pesa za hawa watu ulikuwa una maana gani? Ina maana kama leo tusingekuja hapa basi nisingejua chochote kinachoendelea”
Damaso na babu yake kwa hasira wakanyanyuka teyari kwa kuondoka.
Mayasa alipoona hivyo ,akaingilia kati ,akaamua kujishusha mbele yao ili Damaso asiondoke.
“Nisamehe Damaso,mimi sikujua kitu, wewe ndiye niliyekutarajia leo sio hawa, hapa hakuna hata mmoja ninayemjua ndio kwanza nimewaona Leo......"
”Hamna lolote mnajuana vizuri unataka kunizuga tu hapa Mayasa,niache niondoke ili mumalize shughuli yenu......"
"Hapana Damaso ,mimi sio mpumbavu kiasi hicho,nimekuja nyumbani kwa ajili yako"
Mzee Diko baada ya kuona hayo akasema,
“Sasa Wewe kijana lete hiyo barua yenu tuione alafu tutoe majibu hapahapa"
Mzee Nongwa,babu wa Damaso akamnong'oneza Damaso na kumwambia waondoke tu, ila Damaso akamwambia babu yake watoe tu barua yao kama Mzee Diko alivyosema.
Mzee Nongwa akaamua kumsikiliza mjukuu wake Damaso, akachukua barua na kumkabidhi Mzee Diko. Mzee Diko kama kawaida yake,akaingia chumbani kwake. Alipoifungua alikuta kuna shilingi elfu hamsini.
Mzee Diko akacheka mwenyewe kisha akajisemea mwenyewe,
"Yaani hawa watu hawana akili hata kidogo, wametoka huko walikotoka wamekuja hapa na viela vyao hivi visivyoeleweka huku wakidhani watampata mwanangu kwa bei chee, sasa wamenoa hawapati kitu hapa,nikitoka nje wataenda kunijua mimi ndio nani"
Hapo hapo akatoka nje na huku akiwa amechukia sana.
“Haiwezekani.....Haiwezekani wenzenu wametoa laki moja na hata hivyo wametoa laki tano zingine, alafu nyinyi mnatoa elfu hamsini? Mimi nilitegemea mtatoa zaidi ya walivyotoa hawa,sasa nyinyi mnatoa pungufu? Hapa hampati kitu tokeni tu, hawa mliowakuta ndio watachukua mke....”
Mayasa akadakia hapohapo,
“Baba wewe chukua tu hizo pesa zao ila mimi wala siendi kwa hao, nitaanzaje kumpenda mtu ambaye ndio kwanza namuona leo na hata sijawahi kufikiria kuwa na mtu kama huyo, Damaso ndiye atakayenioa”
“Weee nyamaza wewe mtoto, mimi ndiye nikiyekulea na shida niliapata mimi,sasa huyu kaja na elfu hamsini,yaani elfu hamsini ndio achukue mke? Kwani wewe ni kuku eti?”
Mzee Diko alifoka,lakini Mayasa akajibu tena,
“Kwa hiyo baba mimi thamani yangu ni laki moja?"
”hapana ,ila laki moja ni kubwa kuliko elfu hamsini"
“Baba, mimi sikubaliani na wewe,thamani yangu ni kubwa zaidi ya hiyo laki moja na naweza kusema haifanani na kitu chochote, hizi pesa zinatolewa kwa sababu ya utaratibu tu watu waliojiwekea hapo siku za swali, pesa si chochote kwenye upendo, pesa hazitakaa na mimi,kwa hiyo hata kama angetoa mia tano mimi ningeenda kwa Damaso, Damaso mimi ndio mke wako"
Damaso akatabasamu moyoni kwa maneno mazuri ya Mayasa.
Mama Mayasa naye akaona maneno ya mwanaye Mayasa ndio bora zaidi,akaamua kumshawishi mume wake wamkubalie tu Damaso hata kama ela yake haikuwa kubwa sana kama ya hao wengine.
"Mimi ndio baba wa mtoto huyu,maamuzi yangu huwa hayapingwi,kwanza hii tabia ya kunipinga mmeianza lini? Mimi ndio mwamuzi wa mwisho humu ndani hakuna aliyekuwa zaidi yangu hivyo basi mnatakiwa munisikilize mimi pekee na si vinginevyo"
"Baba mimi nishakuambia teyari, wewe chukua hayo malaki yako lakini mimi hawatanichukua, siwezi kwenda huko nisikokujua"
Mzee Diko alitia ngumu kidogo ila baadae akakubaliana nao baada ya kuna Mayasa na mama yake wameungana kumpinga na hawakuoñesha dalili zozote za kukubaliana naye. Akarudisha pesa za wale wengine na kuipokea barua ya Damaso.
Damaso akafurahi sana baada ya kuona kuanzia wakati huo teyari alikuwa anatambulika rasmi kama mume halali wa Mayasa. Mzee Diko na Mzee Nongwa wakakubaliana ela ya mahari na siku ya kuitoa pesa hiyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Damaso na babu yake baada ya kumaliza kila kitu wakaamua kuondoka. Walipofika nyumbani kwao walimkuta bibi Damaso akiwa amechukia sana.
"Enhee vipi?"
Bibi Damaso aliuliza,babu akajibu,
"Mambo safi tu, Damaso ashapata jiko na ataanza kulitumia muda sio mrefu"
"Msiniambie ujinga wenu huo, Neema alifika asubuhi mlivyoondoka tu,alikuja kumwangalia Damaso ili wayamalize kama tulivyopanga"
"Heee! Bibi yangu kwanini lakini unalazimisha mfupa kwenye chungu? Ukipasua chungu..."
"Mke wangu mambo yashaisha, habari za Neema sijui nani ,sasa hivi basi yameisha, kijana ashapata mtu wake,kama mbovu atajua yeye mwenyewe kwani yeye ndiye atakayekaanaye wala sio sisi"
Bibi Damaso hakujibu kitu, akaishia kufyonya tu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment