Search This Blog

Friday, November 18, 2022

IANGALIE TULEANE - 3

 






Simulizi :Iangalie Tuleane
Sehemu Ya Tatu (3)




Shamrashamra zilienea kote, ila kwa watu wa mzee Tualike pekee, wengine waliohudhuria ambao walikuwa hawampendi walitulia kusikiliza kinachoendelea. Ilipofika saa 9:59 mlango wa ofisi uliotengenezewa kwa aluminium ulifunguliwa, wanaume wanne na wanawake wawili waliovaa madela na nikabu walijitokeza wakipita katikati ya washangiliaji kuondoka eneo hilo. Waliibua sintofahamu kwa watu, hadi shamrashamra zilizokuwa zinaendelea kusimama kwa muda, ila wao hawakujali, waliendelea na safari huku wakipongezana. Sintofahamu yao ilikoma baada ya mlango ulivyofunguliwa kwa mara nyingine, kisha Mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi, mzee Anthony Kumwembe kutokeza.



Mara tu alivyoonekana, alilakiwa na watu wa vyombo vya habari, kwa kupigwa picha za mnato na video kama watoto wadogo wakiwa mchezoni. Wale washangiliaji nao waliongeza shangwe kana kwamba tayari mzee Tualike kawa Mwenyekiti. Ilichukua dakika nane shangwe kumalizika kisha mzee Kumwembe kuanza kuzungumza na halaiki hiyo iliyokusanyika mahali hapo. Hakikukosekana chombo cha habari kilichorusha mubashara tukio hilo, watu waliomo majumbani mwao washuhudie kinachoendelea.

“Habarini za jioni?” Mzee Kumwembe alisalimia.

“Nzuriiii!”

“Nashukuru. Nauona uzuri wenu, basi Mungu aendelee kufanya hivyo hadi mwisho wa maisha yenu.”

“Aminaaaa!”

“Aaah!...leo ni siku ya fahari kijijini kwetu, ambayo inaweka historia katika kuelekea mabadiliko ya serikali yetu. Kwa muda mrefu tulikuwa na zoezi la uchukuaji na urudishaji wa fomu kwa watu wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za kiutendaji wa serikali, hatimaye leo tumefikia tamati. Natamka rasmi kuanzia sasa kufunga zoezi hilo, na kutaja orodha ya watu waliotia nia kwa nafasi moja tu ya uenyekiti wa serikali ya kijiji, hizo zingine zitatajwa sehemu husika, hususani zile za mtaa. Kwa kipindi chote hicho, tangu nafasi zilivyotangazwa, nafasi ya uenyekiti, imewaniwa na watu wawili, nao ni; Mzee Tualike Misifa, mgombea mwenza wake ni Zullea Kasinde. Mtu wa pili, ni Bi. Mwema Asononekaye, mgombea mwenza Mchungaji Chilombo Saad.”

“Heeee!” Ndilo neno pekee lililosikika toka kwenye ile halaiki iliyokuwa inamsikiliza. Mshangao huo ulitoka kwa watu wanaompenda na kumuunga mkono mzee Tualike, lakini watu wachache wamchukiao waliopo hapo walijawa shangwe baada ya kupatikana mpinzani wa kushindana naye. Ilikuwa sintofahamu ya nguvu, si kwao tu bali hata kwa mzee Tualike aliyekuwa anafuatilia tukio hilo kupitia runinga alistaajabu na wapambe wake.

“Inawezekana vipi?” Aliuliza.

“Hii ni kali mzee wetu. Tutakabiliana naye vipi?”

“Aiseee, hata kutekwa atekwe huyu mtu. Maana ule mpango nilionao nikiingia madarakani anaufahamu fika.”

“Unataka hilo jambo lifanyike kwa sasa?”

“Ndiyo. Kabla hajapanda jukwaani na kufukua makaburi.”

“Aaah!...fanya subra. Tukifanya kwa siku za hivi karibuni, watu watahisi moja kwa moja wewe ni mhusika. Acha kwanza aanze kufanya kampeni ndipo tupange mpango mzuri wa kumuondoa. Tena mpango rahisi sana, kukifanyia hitilafu chombo cha usafiri atachokuwa anatumia.”

“Hamna shida kanitibua sana akili yangu huyu mwanamke. Sitojali kama mama wa wanangu, ninachohitaji alambe mchanga na huyo kinyago wake anayeongozana naye.”







Kesho yake ni habari “mume na mke” kuwania nafasi ya uenyekiti. Kijiji kizima habari hiyo ndiyo ilikuwa na nguvu zaidi ya zingine, kwani magazeti na majarida karibu yote, kurasa ya mbele yalipambwa na habari zao, jinsi watakavyochuana vikali wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi. Hata vipindi vya midahalo ya asubuhi radioni na runingani ilikuwa ya kisiasa ambapo wataalamu tofauti tofauti wa siasa walialikwa kutoa mitazamo namna itavyokuwa. Kampeni pia zilianza jioni ya siku hii, mzee Tualike ndiyo mtu wa kwanza kuzindua, mkutano wake ulifurika watu, watu wengi sana kiasi kwamba uwanja hakutosheleza. Alisindikizwa na wanaye, watu wengine wanaounda kundi lake na baadhi ya viongozi wa serikali, hasa Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, mzee Kasoyaga.



Alimwaga sera zake, wananchi wazielewe kwa kusaidiana na hao waliomsindikiza ili wazielewe na wafahamu nini atachofanya pindi aingiapo madarakani. Mambo yalikuwa ni moto, kwani kila mmoja aliyepanda jukwaani alipambanua barabara vipaumbele kuhakikisha ufahamu unakuwa wa kutosha kwa wananchi.

“Mkitoka hapa muwe na kumbukumbu, kuanzia leo hadi siku ya uchaguzi itakapowadia, siku unayoenda kupiga kura. Na hiyo siku msifanye makosa, mpatieni kura mzee Tualike, mzalendo wa kweli, aliyesaidia harakati nyingi ndani ya kijiji chetu na vile vinavyotuzunguka. Huyu ndiye mtu atayetuletea maendeleo ya kweli. Mmesikia vipaumbele vyake, kwamba atatoa huduma ya elimu bure, afya kwa wazee bure, ataanzisha na kufufua viwanda vyetu ili tuwe na bidhaa zinazotengenezwa hapa kijijini kwetu. Sasa mnamtaka mtu gani zaidi ya huyu,” alisema mzee Kasoyaga katika sehemu ya hotuba yake.

“Huyo ndiyo Mwenyekiti wetu, hatuwezi kuongozwa na mwanamke siyeee,” wananchi waliropoka, wakifurahia hotuba.



Saa 12 jioni mkutano uliahirishwa hadi siku inayofuata. Mwitikio wa wananchi uliwahakikishia ushindi unaenda kwao, mapema kabla vituo havijafungwa. Hata sera zao walizohubiri ziliwapa matumaini ya ushindi, kuwa ni bora na kama zitaendana na mpinzani wake, za mpinzani hazitokuwa bora sana kama za kwao. Siku ya pili, kampeni iliendelea mtaa mwingine, na ndiyo siku ambayo Bi. Mwema naye alizindua kampeni zake, ila hakuzindulia Tuleane, alizindulia kijiji cha Majini, ambacho ni kisiwa na miaka ya nyuma kilikuwa na muungano na Tuleane kwa idara fulani, ila baadaye ulivunjwa baada ya wawakilishi toka mitaa yote ya vijiji hivyo kutofautiana katika maamuzi ya Mwenyekiti wa Jamhuri ya muungano katika kijiji cha Majini na thamani ya Mwenyekiti wa kijiji cha Majini ndani ya Tuleane. Ila waliacha idara moja iwe kwenye muungano, idara ya ulinzi na usalama.



Hakupata watu wengi katika mkutano wake, idadi ndogo ya watu wapatikanao ndani ya kijiji hicho kulinganisha na mzee Tualike kule Tuleane, ila kwa upande wa huko walionekana kuwa ni wengi. Naye alisindikizwa na wapambe wake, na baadhi pia ya viongozi wa serikali wampendao. Hawakuacha kukubalika na wananchi wa kijiji hicho, tena zaidi ya mzee Tualike, kwa jinsi ambavyo walipokelewa. Mkutano ukaanza rasmi saa 10 jioni, kiongozi mmoja baada ya mwingine akawa anapanda jukwaani kunadi wagombea walioko kampani moja na Bi. Mwema kwa upande wa Majini kisha baadaye alifuatia Bi. Mwema.

“Majini oyeee!”

“Oyeeeeee!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Nashukuru sana kwa ukarimu wenu na mapokezi makubwa mliyotupatia, niwaahidi kuwa sitowaangusha. Niwe Mwenyekiti nisiwe Mwenyekiti, nitakuwa bega moja nanyi, wananchi na viongozi wa serikali mtakaowachagua. Watangulizi wangu wamesema mengi sana, ambayo ndiyo vipaumbele vyetu, vilivyopo ndani ya kitabu cha sera yetu, hiki hapa...” alisema Bi. Mwema huku akinyanyua juu kitabu cha sera kuwaonesha wananchi kwa sekunde kadhaa, kisha alikirejesha na kuendelea.

“...nina moja kubwa la kulizungumza ambalo wenzangu hawajalizungumza ila limo ndani ya hiki kitabu. Nianze kwa kuwauliza kabla sijaenda kwenye hiyo hoja. Wanamajini, hamhitaji tena muungano?”

“Tunahitajiiiiiiiii!” Wananchi waliitikia.

“Basi chagueni hawa watu tuliowanadi huku kwenu, ili nikichaguliwa kule Tuleane, nijadiliane vizuri na hawa wenzangu namna ya kurudisha muungano ulio bora wenye kujali maslahi ya kila pande. Wanamajini, endapo nitabahatika kuwa Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Tuleane, nitarudisha muungano, wenye kujali maslahi ya pande zote tofauti na wale wenzangu wanaoshindwa hata kutamka kuhusu neno muungano. Ninahitaji kurejesha yale yote ambayo yalipata kuwa ndani ya muungano, na sio muungano huu uliopo sasa, unaotoa manufaa upande mmoja. Vijiji vyetu vinahitaji kuendelea kuwa kwenye muungano, tena muungano wa kipekee kabisa tofauti na muungano uliopata kuwa mwanzo, nikiwa na maana inabidi tuwe na serikali pekee inayohusika na mambo ya muungano, hivyo Majini itakuwa na serikali yake na Tuleane pia serikali yake na tutakuwa na hiyo ya muungano. Majini oyeee...”

“Oyeeeeee!”

“Tupeni kura, tuwafanyie haya tunayowaahidi.”



Pindi Bi. Mwema anaendelea na mkutano wake katika moja ya mtaa kijijini Majini, mzee Tualike naye alikuwa moja ya mtaa Tuleane akinadi sera zake na kuuza vitabu vya sera kwa wananchi waliohudhuria mkutanoni. Watu wengi walinunua, ili wafahamu kiundani namna sera zilivyopangwa na mikakati itayotumika kutekeleza. Bi. Mwema naye, na kampani lake walifanya mauzo ya vitabu vya sera, Majini na Tuleane pia, ambako aliwaachia mawakala wake, wananchi wanunue kabla ya uzinduzi wa kampeni ambayo aliitaraji kuifanya siku iliyofuata baada ya kuhitimisha Majini.



Kikao kilivyohitimishwa walirejea Tuleane, wakiwaacha wananchi na shauku kubwa ya kufikia siku ya uchaguzi wafanye maamuzi. Shauku hiyo haikuwa kwa wananchi wa kijiji cha Majini pekee, hapana! Hata Watuleane pia, walipendezwa mno na sera zake, hususani ya kurejesha muungano na kutengeneza serikali tatu. Wengi wao walikuwa wanafuatilia hotuba yake kwenye vyombo vya habari vilivyokuwa vinarusha mubashara pamoja na kusoma vitabu vya sera walivyonunua. Watu wa Tualike walifuatilia hotuba yake usiku, kupitia vipindi vya taarifa ya habari, matukio na mitandao ya kijamii, pasipo na kusahau vitabu kwa wale walionunua.

“Hapa kanena,” baadhi yao walisifia waliyovutiwa na hoja zake.

“Tena sana. Huyu mama ana akili na maono ya mbali sana. Kwa hiki nitampatia kura yangu.”



Mzee Tualike naye alifuatilia, jambo lililopelekea kumuongezea hasira kila sera ilivyokuwa inatamkwa. Zilishabihiana na zake, lakini zingine hazikuwemo na ndizo zilizompandisha hasira zaidi.

“Vipi vitabu vilishaisha?” Aliuliza mzee Tualike, akifanya maongezi na mtu wa upande wa pili wa simu.

“Hapana. Vimebaki baadhi,” alijibu yule aliyoko upande wa pili.

“Sitisheni kuuza. Nataka tuvifanyie marekebisho, tuongeze baadhi ya sera, kama hii ya muungano. Nahisi tusipofanya hivyo huyu mama atatupiga bao.”

“Sahihi kabisa. Na vipi kuhusu tulivyoviuza?”

“Fanyeni jitihada virudishwe.”

Simu ikakatwa.



Usiku huohuo, likatolewa tangazo la marekebisho ya kitabu cha sera cha mgombea, mzee Tualike Misifa. Na kuwaomba wananchi wote walionunua warejeshe baada ya marekebisho kumalizika wapatiwe vitabu vingine. Baadaye vile vilivyosalia viliamriwa kuchomwa, na zoezi hilo kufanyika. Sintofahamu ikatamalaki, kwa wanunuzi imekuaje lakini hawakupata muafaka zaidi ya kufanya jinsi tangazo lilivyotolewa. Ambapo wanunuzi walihitajika kupeleka vitabu vyao kwa wakala maalumu walioteuliwa kuvipokea. Asilimia kubwa walirudisha, navyo vikachomwa moto, huku ikiandaliwa sera nyingine iliyo na sera zilezile zilizoko kwenye kitabu cha awali na kuongezwa zingine ambazo hazikuwepo.



Baada ya siku mbili kitabu kipya cha sera kilitoka mtaani na manunuzi kuendelea, huku wale wa awali waliopata kununua wakipewa bure. Hawakukosekana watu waliofanya ukosoaji na upongezaji, ila wengi wao walikuwa wakosoaji walivyogundua ameiga baadhi ya sera toka kwenye kitabu cha Bi. Mwema.



Kampeni zilizidi kusonga mbele, kwa nguvu kubwa kutegemeana na namna wanavyokubalika kila mtaa wanaoenda. Japo kulikuwa na makundi ila wananchi wengi walionekana kumkubali Bi. Mwema.



Walivutiwa na sera, na mikakati ya kipekee aliyojiwekea ya utekelezaji aingiapo madarakani. Hata waliokuwa wanavutiwa na Mzee Tualike siku za mbeleni walianza kuhama kumuunga mkono, kitendo kilichozidisha ghadhabu. Kila kona ya mtaa ni Bi. Mwema tu, ndiye aliyeonekana kukubalika tofauti na ilivyotarajiwa, kwamba Mzee Tualike atakuwa juu ya mkewe sababu ya uanaharakati wake. Si watoto, vijana ama wazee, wimbo wao ulikuwa mmoja tu, hitajio lao ni Bi. Mwema.



Juu ya sera nzuri alizonazo, kitu kingine kilichomuongezea kupendwa ni jinsia. Kijiji cha Tuleane kilikuwa na wanawake wengi kuliko wanaume. Wanawake wenzake hawakuhitaji kumuangusha kwa namna yoyote japo palipata kutawaliwa na imani ya udhaifu, kwamba mwanamke ni mdhaifu kuliko mwanaume hivyo atashindwa kuongoza kijiji. Walihitaji kuonesha uhodari wa mwanamke, juu ya dhana zinazoenezwa, ni namna gani nao wanaweza wakipewa nyazfa kubwa kuziongoza.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Viroja vingine vya namna hii viliendelea kuibuliwa kila uchao, wao hawakujali, waliziba masikio na kuongeza hamasa ya kuendelea kukubalika. Wazi! Dalili za ushindi zilionekana kwenda kwa Bi. Mwema. Jitihada alizozionesha jukwaani na kufuatia historia ya kiutendaji kipindi cha nyuma iliendelea kumpa chati. Baadaye vilianza vitendo vya wivu na hiyana, kwa kuzuiawa kufanya mikutano katika viwanja vizuri ambavyo mzee Tualike aliruhusiwa kufanyia na watu wa serikali. Muda mwingine alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi na sungusungu aongezapo dakika katika mikutano yake. Alifanyiwa visa, ili ikiwezekana apoteze sifa na nguvu ya kupendwa kwa wananchi, huku mipango ya kumuondoa ikiendelea kuratibiwa.



Kila siku nguvu kubwa ya dola ilitumika kwake, pasi na kujua kama wanamuongezea nguvu ya kukubalika zaidi nao kuishusha sifa yao. Hawakujua wakifanyacho wanapunguza imani ya kupendwa, walichojali ni maslahi wayapatayo kwa muda huo, huku wakitengeneza hali tete ya kudumu upande wao.







“Ushafikia wakati wa kufanya lile jambo.” alisema mzee Tualike pindi akiwa na wanaye wameketi sebuleni jioni moja baada ya kurudi toka kwenye kampeni.

“Yes! Tunasubiri amri yako,” wanaye nao walichangia hoja.

“Hadi kufikia jioni ya siku ya kesho, nahitaji nisikie wakiitwa majina mengine.”

“Worry out our father, we have prepared for that job.”

“Thanks! I’m sure you don’t let me down.”



Punde baada ya kumaliza maongezi na vijana wake aliwasiliana na mzee Kasoyaga kumtaarifu alichodhamiria ili uratibu uliopangwa utekelezwe. Asubuhi ya siku iliyofuata, vijana wawili wa mgambo, ambao waliagizwa kumkamata Awetu, waliungana na Jipendekezo na Majungu hadi katika moja ya jengo kuukuu litumikalo kwa utengenezaji wa vyombo vya moto, gereji, lililoko nje kidogo ya kijiji ambako vyombo vya usafiri vitumiwavyo na Bi. Mwema hufanyiwa ukarabati kila siku mara baada ya kumaliza mikutano yake. Hii ilikuwa gereji ya kipekee nzuri, ambayo inaaminiwa na hutumiwa na watu mbalimbali watakapo huduma ya vyombo vyao, kwani hata magari ya taasisi za serikali na jeshi la mgambo hutumia.



Dhamira ya ujio wao ilikuwa moja tu, kuhakikisha usafiri utumiwao na Bi. Mwema unafanyiwa hitilafu ili umsababishie ajali itayoondoa uhai wake. Hakuna mtu aliyewahisi kama nia yao ni ovu, kwani vijana wa sungusungu walikuwa hawatambuliki machoni kwa watu wengi, zaidi ya viongozi wa juu wa jeshi lao na viongozi wa juu wa serikali. Walikuwa walinzi wa siri wa Mwenyekiti, “Chairman Secret Service” (CSS) hivyo ni ngumu kuhisiwa. Jipendekezo na Majungu pia hawakuweza kuhisiwa sababu hata nao vyombo vyao wafanyiavyo kampeni huleta hapo. Moja kwa moja wahudumu wa gereji walijua wamekuja kuangalia usafiri huku wale walioongozana ni wageni wao, ilhali ndiyo wanyama waliokuja kufanya tukio.



Tena walikaribishwa kwa heshima zote, na meneja mkuu wa gereji hiyo. Baada ya maongezi mafupi yaliyoanza kwa salamu walipelekwa kuangalia maendeleo ya vyombo vyao. Mzunguko ulikuwa mfupi kuyafikia, waliyakugua walivyoridhika nayo walimpongeza meneja kwa kazi nzuri inayoendelea.

“Meneja! Acha tukupe pongezi kwa kazi nzuri. Tumefarijika sana, nahisi hata mzee atafurahi tukimfikishia taarifa hii.”

“Nami nashukuru sana. Tutaendelea kuwa pamoja katika kila jambo.”

“Sawa. Ila tuna ombi, kama hautojali unaweza kutusaidia.”

“Lipi tena ndugu zangu?”

“Tuko na hawa wageni wetu wako na usafiri wao, una hitilafu kidogo hivyo wanaomba eneo waufanyie kazi ili tujumuike nao kwenye kampeni jioni ya leo.”

“Hamna shida waulete tu. Tuna maeneo mengi sana ya wazi.”

“Ahsante sana.”

“Okay! Haina shida.”



Hatimaye waliagana kisha Jipendekezo na Majungu waliondoka na kuwaacha wale vijana wa sungusungu. Baada ya muda mfupi, usafiri wao uliletwa, walitafuta eneo zuri wakalipaki. Ambapo ni karibu na gari itumiwayo na Bi. Mwema. Haraka sana walipanga boksi uvunguni, lililotokeza uvungu wa gari ya Bi. Mwema ndipo wao wakafuatia kuingia mmoja mmoja kupitia kwenye gari yao. Kijana wa kwanza alivyoingia aliserereka hadi chini ya gari ya Bi. Mwema pasi na watu kumuona, kwani ilikuwa rahisi kuitambua gari hiyo tokana na bendera iliyokuwa inapeperusha juu yenye picha ya Bi. Mkubwa huyo. Pasi na chelea walianza kushughulika, kwani walikuja na zana zao ambazo walizihifadhi kwenye kibegi kidogo cha mgongoni chenye mkanda mmoja. Ila pale waliposhindwa kushughulikia kifaa kwa ukosefu wa zana mmoja wao alitoka kwenda kuomba.



Waliifanya kazi hiyo karibia muda wa saa moja, walipojihakikishia washakamilisha kila walilohitaji, waliondoka kwenda kwa meneja kushukuru, kisha wakaondoka eneo hilo. Wakati huo tayari gari la Bi. Mwema sehemu zinazoshikilia breki walishazilegeza, kwamba dereva akishakanyaga kwa muda mrefu ikate breki kisha ipoteze mwelekeo. Walivyoondoka, walienda moja kwa moja kwa mzee Kasoyaga, mkuu wao wa kazi kumhabarisha juu ya utekelezaji wa kile walichoagizwa ulivyokamilika. Kila kinachoendelea katika mpango wao kikishakamilika mzee Kasoyaga hakuweza kukaa nalo moyoni, haraka naye humfikishia mzee Tualike. Hivyo, vijana wake wa siri wa ulinzi walivyomtaarifu, alimtaarifu mzee Tualike pia, habari iliyopelekea tabasamu pana kwao na kutengeneza sherehe kimoyomoyo kufurahia kumuondoa Bi. Mwema, hasimu wake namba moja katika ulingo wa siasa.

“Kwani, leo anaelekea wapi kufanya mkutano wake?”

“Atakuwa Misawaji,”

“Kule kwenye barabara iliyo na miteremko na kona kali?”

“Yeah! Ni huko.”

“Basi kwisha habari yake.” ilikuwa sehemu ya maongezi yao.



Saa 9:46 alasiri Bi. Mwema na kampani yake walizuru gereji tayari kwa safari ya kuelekea katika mtaa waliopaswa kufanya kampeni siku hiyo. Dereva aliifuata gari, aliingia ndani na kuitekenya, ndipo wengine walifuatia kuingia. Taratibu ilianza kuacha eneo hilo huku watu waliomo ndani wakiaga kwa kuwapungia mkono wahudumu wa gereji waliokuwa wamejipanga mstari mmoja kuwashangilia.

“Safari njema mama. Tunakutakia mkutano mwema muendako.”

“Amina!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Walivyolifikia lango kuu la kuingilia walipandisha juu vioo, dereva alizidi kukanyaga mafuta, lakini kwa mbali ilisikika sauti fulani ikiwasimamisha. Ila ilishindwa kusikika vizuri kama ni wao ndiyo waitwao ama watu wengine. Baada ya kusikika kwa muda mrefu dereva ilibidi aangalie kulikoni, kupitia kioo cha pembezoni mwa gari, kwani hakuwa amefunga kioo cha upande wake mpaka mwisho, wakati huo akihimizwa azidi kuongeza mwendo wapate kuwahi kule wanakoelekea. Sauti hiyo ilikuwa ya mtoto mdogo apataye umri wa miaka kumi, mmoja miongoni mwa watoa huduma wa gereji hiyo akiwa kakamatia spana na suruali yake kubwa iliyokuwa inampwaya, hivyo haikuwa na nguvu ya kusikika na kufika mbali sana. Baadhi ya wenzake ilibidi wamsaidie, ndipo dereva akapata uthibitisho wa kuwa wao ndiyo waitwao, akaamua kusimamisha gari.

“Mbona umesimama?” watu wote wa ndani walimuuliza.

“Kuna mtu hapo nyuma kwa muda mrefu sana ameonekana kutusimamisha. Kwa hiyo acha tumsikilize kwanza.”



Kwa juhudi za mbio alizofanya hatimaye aliwafikia huku akiwa anahema vibaya mno.

“Pole sana kijana,” alisema dereva.

“Ah... Ahsante. Kio...kiongozi wenu anaitwa.”

“Na nani?”

“Meneja!”

“Mmmh!... Ana nini tena? Wakati tulikuwa naye muda mfupi uliopita?” Bi. Mwema alidakia.

“Sijui. Ila amenituma niwaambie hivyo.”



Pasipo kupoteza muda, Bi. Mwema aliteremka na kuongozana na kijana huyo hadi ofisi ya meneja, ambapo alimkuta meneja na wageni wengine wawili wa jinsia ya kike walionekana fika si wenyeji wa kijiji chao. Kutokana na muonekano wao, walikuwa na rangi ya ngozi tofauti na asili ya watu waishio Tuleane. Asili ya ngozi ya wana Tuleane ilikuwa nyeusi wao nyeupe. Alivuta kiti na kuketi huku akionekana mwenye uharaka.

“Samahani kwa usumbufu. Kuna hawa watu ni wageni wako,” alisema meneja akiwaonyesha wale wanawake kwa mkono wake wa kuume.

Bi. Mwema aligeuka na kuwaangalia kwa mara nyingine, kisha ile hali ya uharaka akaituliza kuwasikiliza.

“Sisi ni washirika wa dhehebu la Angalikana toka Kalipinde. Tulibahatika kuja ofisini kwako asubuhi ya leo hatukubahatika kukukuta. Pasipo kupoteza muda, twende moja kwa moja kwenye lengo. Ujio wetu una lengo moja, tukiwa kama watumishi wa Mungu tupendao maendeleo, dhehebu letu, limeona vyema kukusaidia katika harakati zako za kampeni. Ambapo tumedhamiria kukupatia msaada wa usafiri wa kukusaidia katika harakati endapo utapenda. Dhehebu letu, kupitia taasisi yake ya wanawake tumependezwa na jitihada na uthubutu uliouonesha, hivyo tukaona si vibaya kama tutakuunga mkono kufanikisha kile ulichoamua kama mwanamke mwenzetu.”



Kimya kidogo kilipita, huku Bi. Mwema akionekana kukumbuka jambo, baada ya kuhitimisha kumbukumbu zake ndipo akafungua mdomo kuzungumza.

“Nashukuru sana kwa maana nilikuwa na uhaba wa usafiri pamoja na ubovu wa chombo chetu, kiasi kwamba tulishindwa kufika baadhi ya sehemu ambazo ni muhimu kufikiwa. Kwa msaada wenu, naimani yale maeneo sasa tutayafikia,” alisema Bi. Mwema huku akitoa mkono kuwapongeza.



Maongezi yalivyomalizika baada ya kusaini baadhi ya nyaraka walitoka kwenda kuangalia huo usafiri ambao alikabidhiwa. Magari mawili, aina ya Toyota VX. Makabidhiano yalivyomalizika alirejea mahali alikowaacha wenzake na kuwahadithia kilichtokea. Kila mmoja alifurahi, furaha waliyoiweka wazi kwa vicheko na tabasamu zenye mvuto usoni.

“Dereva washa gari tuondoke tuwahi kuanza mapema mkutano wetu,” alisema Bi. Mwema akiwa anafunga mkanda.



Dereva akatekeleza agizo.









Mchungaji Chilombo alifanikiwa kuingia hifadhini hadi kwenye gari ile aliyoiendea mwanzo. Alipanda kwenye tairi kisha kuangalia kitu walichokuwa wakikitafuta, ambacho kimefichwa na kufanikiwa kukiona kikiwa chini kabisa ya reli za kichukuzi za chini, machela. Kitu alichokiona kilikuwa ni flash, pasipo na ajizi alikitambua ndicho kitu pekee ambacho kilikuwa kinamaanishwa kwenye ujumbe waliouokota. Alipohakikisha ndicho kitu pekee, alirejea mahali alipowaacha wenzake baada ya kuagana na walinzi. Kabla hata hajaulizwa, alifikia kuwaonesha alichokuta hali iliyowafanya wapeane pongezi kisha kuianza safari ya kurudi nyumbani kwa MJM Zimbwa.



Hawakupitia sehemu yoyote, moja kwa moja walipiga hatua hadi nyumbani kwa MJM Zimbwa na kufanikiwa kumkuta akiwa nje ya nyumba ambapo alikuwa akilisha mifugo wake ambao ni ndege aina ya njiwa. Pembeni yake waliketi wanawake wawili wakipembua mchele. Walikuwa ni Bi. Mwema na mwanaye, Laumio. MJM Zimbwa ndiye aliwakamata jioni ile walivyokuwa wanaiba shambani mwake, hivyo baada ya kuwatambua ilibidi awasaidie kwa kuishi nao nyumbani kwake. Walistaajabu! Hadi Bi. Mwema na Laumio pia walipatwa na hali hiyo kwa sababu ya kufumaniwa, jambo ambalo hawakulihitaji wala hawakutarajia kuwa wataonwa na watu zaidi ya mwenyeji wao.

“Ondoeni shaka, hawa ni watu wema kwenu, hakika yangu hawawezi fichua siri ya uwepo wenu hapa kijijini,” alisema MJM Zimbwa, baada ya kuuona mshangao wao.



Hali ilivyotulia kwa pamoja waliingia ndani kuzungumza. Mch. Chilombo ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu, kwa kuanza kumpasha MJM Zimbwa maendeleo ya kile walichojadili mwanzo kisha akaendelea na dhamira kuu waliyonayo ya kumtafuta mtu wa kupingana na mzee Tualike kwenye uchaguzi uliopo mbele yao. Hapo walikuwa na maongezi marefu, kwani yule waliyemhitaji agombee alipingana nao, ambaye ni Bi. Mwema kwa nguvu hadi ilifikia hatua ya kunyanyuka kuondoka kwenye maongezi hayo. Jitihada za ushawishi za muda mrefu ndizo zilizomrubuni kumrudisha na kukubaliana na dhamira ya kina Mch. Chilombo. Makubaliano yalivyopita kwa pamoja walifurahia, baadaye Mch. Chilombo aliitoa ile flash na kuwaomba waichunguze ili kujua kilichomo ndani na wapate kufahamu.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

MJM Zimbwa aliifuata kompyuta mpakato chumbani kwake, flash ikawekwa na kufunguliwa lakini isivyo bahati ilikuwa na nywila ambalo ni neno la siri ili kuyafikia yaliyomo. Hamu ya kuendelea kufahamu kilichomo iliishia hapo, kwani, walitambua miongoni mwao hamna mtu mwenye uwezo wa kujua nywila ya kufungulia kifaa hicho kitunzacho taarifa. Ukizingatia mhusika hayuko duniani, angeliwepo ingeliwarahisishia kumuuliza. Hata kujaribu bahati, kwa kubahatisha hawakuhitaji, wangesumbuka pasi na sababu, ila iliwajengea shauku ya kutafuta namna nyingine ilimradi waifungue. Namna waliyofikiria ni kumtafuta mtaalamu mwenye uwezo wa kushughulika na vifaa hivyo. Mtaalamu wa IT (Information Technology).

“Mbona mnahangaika sana?” Aliuliza Laumio baada ya kuona hangaiko nyingi walizokuwa wanaendelea nazo MJM Zimbwa na wenzake. Wakati huo alikuwa amelala kwenye kitanda kilichotengenezwa kwa kamba, akiwa anacheza na paka. Ikambidi ainuke aangalie wanachofanya.

“Mihangaiko mama yetu, katika hizi harakati za kupambana na baba yako,” Mooja alijibu.

“Hawezi kuwa baba yangu kwa sasa, mwanaume katili aliyekosa haya, wa kazi gani? Halafu hiyo flash mbona kama ya Awetu,” aliendelea kuuliza baada ya kuona alama fulani iliyochorwa juu ya flash iliyosomeka AMBWL.

“Umejuaje? Ndiyo yenyewe.”

“Hiyo alama hapo juu ndiyo niliyopelekea kuifahamu. Hicho ndicho kinawafanya mhangaike?”

“Eeh! Inahitaji neno la siri.”

“Andikeni Albinism.” alisema Laumio kisha alirudi zake kitandani kuendelea kucheza na paka.



Hawakukawia. Neno waliloambiwa liliingizwa na hatimaye kufunguka. Wakalikuta faili moja tu, lililosomeka “mpango wa siri” andiko lililovutia kuendelea kufuatilia kilichomo. Walifungua, wakakutana na faili jingine lililoandikwa “Andiko la Bi. Mwema” walivyofungua hapo, walikutana na habari ndefu yenye kurasa kumi. Kila ukurasa ilikuwa unaelezea jambo moja. Taratibu walianza kusoma ujumbe ulioandikwa kila kurasa kulingana na pointi zilivyopangwa, lakini hawakufika mwisho walighairisha, sababu walikuwa hawaelewi kinachomaanishwa, ilibidi wawaite Bi. Mwema na Laumio wawafafanulie.



Mshituko ndicho kitu cha kwanza kilichowapata mara baada ya ujumbe huo, ila sio kwa muda mrefu. Muda mfupi tu, wakaungana na wenzao kwa maana ndio waliokuwa na ufahamu wa kutosha. Bi. Mwema alianza kuwaelezea ujumbe mmoja baada ya mwingine na uhusika wake katika mpango huo wa siri ulioandaliwa na familia ya mzee Tualike. Laumio akiwa anakazia maelezo kidogo sehemu ambayo mama yake alisahau. Haikumchukua muda mrefu kuhitimisha, alikuwa anaeleza kwa ufupi na maelezo yaliyojitosheleza, yaliyowahamasisha wote na kuongeza uchungu wa kutekeleza walichokubaliana kwa uharaka.

“Sikuwa na nia yoyote katika maisha yangu ambayo nilitarajia kugombea uongozi wowote unaohusiana na serikali yetu, ila baada ya kuukumbuka huu mpango, umenipa mshawasha wa kugombea. Hata kama sitabahatika kuchaguliwa ila niuambie umma, lengo la mzee Tualike endapo akichaguliwa.”

“Aiseee!...hiki kitu ni kibaya sana. Lazima tuizuie hii hata kama atafanikiwa kuchaguliwa.”

“Sahihi kabisa. Haina haja ya kuwaogopa hawa sungusungu wetu, kwani nao ni raia wa kijiji hiki kama sisi. Hivyo kama tumeamua basi tujidhatiti hadi hatua ya mwisho, sio tunaanzisha kisha tunawaachia raia wapambane nao. Tuwe nao bega kwa bega kwenye kila hatua.”

“Nalo ni neno. Tuhakikishe hilo linafanyika,” wote walikubaliana, kwa sura zilizojaa tabasamu pana kana kwamba hakuna shida yoyote inayowakabili, ama ambazo zilishawapata na kuwaweka sehemu mbaya kimaisha.



Andiko lenye mpango wa siri ulioandaliwa na mzee Tualike miaka kadhaa nyuma katika harakati za kuelekea kuwa Mwenyekiti wa katika kijiji cha Tuleane unawafanya kuongeza nguvu ya ushirikiano ili wauzuie. Amepanga kuutumia punde tu baada ya kuingia madarakani. Andiko hilo lenye mjumuisho wa mambo kumi, huku mambo mawili ndiyo yakiwa makubwa mengine yaliyobakia, yanawapelekea kuongeza nguvu ya ufikiri wa namna ya kuuzuia mpango huo usitekelezeke. Jambo la kwanza la mpango huo ni mabadiliko ya katiba, amepanga kuongeza muda wa kuwa madarakani toka ule ulioko kwenye katiba kwa wakati huo, miaka minne hadi aliyotaka yeye mwenyewe.



Mpango huo unasema wazi, kupitia dokezo la pili, pale aingiapo madarakani kuandaa kundi la viongozi na vijana wa mtaani kuandaa hoja ya kuongeza muda wa viongozi wanaochaguliwa na wananchi madarakani. Toka miaka minne hadi kutokuwa na ukomo wa kugombea, ikiwa na maana kama ataacha kugombea basi ni kwa ridhaa yake. Akipenda basi hata mwisho wa maisha yake. Jambo la pili, linaweka wazi “kuvunja vikundi vya kiharakati” vinavyoongozwa na wapinzani wa serikali, ili mipango yao waamuapo pasitokee mtu wa kuweka kizuizi. Hizo ndizo dondoo kubwa, ambazo iliwabidi washughulike nazo kwa udi na uvumba, na sehemu mbadala waliyohitaji kuyabainisha haya ni siku ya mwisho wa kampeni.



Siku ya mwisho ya kuhitimisha zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu wao ndio walienda kuchukua, dakika za mwisho, karibu kabisa na muda wa kufunga. Walichukua, wakakamilisha kujaza na kuirejesha kisha kuondoka taratibu zote zilivyokamilika. Kampeni zilivyoanza walijikita kueneza sera na kufanya ushawishi mkubwa ili wananchi wavutike kuwachagua siku ya uchaguzi. Hamasa waliyoipata toka kwa wananchi iliwaongezea morali ya kujidhatiti vilivyo kusonga nao pamoja hadi siku ya mwisho itayowaibua washindi na kuweka historia ya mageuzi tangu kijiji hicho kilivyojikomboa mikononi mwa utawala wa kijiji cha Mamba.



Sekunde, dakika na masaa yalizidi kukatika na kubakia siku chache za kuhitimisha zoezi la kampeni. Siku mbili tu zilibakia. Hapa hamu ilizidi kuongezeka pande zote. Wananchi na viongozi wahutubiaji kutumia majukwaa kuhitimisha kampeni kwa uzuri wa kutoa hotuba zilizo bora na zenye viwango vya kusikilizwa muda wote hata pale uchaguzi utapomalizika. Hamu hiyo iliwahimiza kuanza mikutano yao ya kampeni mapema tofauti na mwanzo, hata sekunde moja tu, kwao ilikuwa sawa na kupoteza siku nzima. Sekunde moja ilikuwa na umuhimu mkubwa kwao, hawakuhitaji iende bure pasipo na kitu cha msingi chenye kuwapatia kura. Ndiyo maana, Bi. Mwema alivyoitwa na meneja wa gereji, awali alichukia sana, kwani aliona anapoteza muda mwingi usio na manufaa.



Chuki yake iliisha alivyokabidhiwa zawadi ya magari mawili na wahisani kutoka kijiji kingine, washiriki wa dini, dhehebu la Angalikana. Masista pia. Zawadi iliondoa fundo alilotengeneza. Tabasamu likachanua, alishindwa kulizuia na kuwapa mshawasha wenzake alivyorudi garini. Hakuwa na haja ya kuwaficha, aliwahadithia kila kitu kisha akamhimiza dereva awashe gari waondoke. Dereva hakujadili, alitii kauli ya bosi wake na kuanza safari ya kuondoka.

“Kwanini tusitumie hizo gari mpya tulizopewa?” Ilisikika sauti ya Laumio kutoka kiti cha nyuma alipoketi, kauli iliyomfanya dereva asimamishe gari ghafla, wajadiliane.

“Bhana! Tunachelewa, achaneni na hilo wazo,” Bi. Mwema alichangia hoja.

“Mama! Kwanini unapenda shida? Unataka tubanane humu wakati kuna vyombo vizuri vipo na vimekuja kwa ajili ya kutumika. Hili ndilo tatizo letu, tunapenda kujitesa.”

“Hayo magari tutayatumia siku ya mwisho.”

“Hapana. Tufanye mwanao anavyotaka, tuanze leo.” Mch. Chilombo naye alichangia.





http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Okay! Tufanye hivyo mnavyotaka ila tunapoteza muda.”

“Hamna shida kuhusu hilo, wananchi watatuelewa tu hata kama tutakuwa tushachelewa.”



* ***



Hatimaye walibadili gari, waliiacha ile watumiayo siku zote na kuzitumia zile mpya walizozawadiwa kutokana na harakati zao. Safari nzima ilikuwa tamu, upya wa gari walizotumia tena wakiwa wachache kwenye kila gari tofauti na awali walivyobanana uliwafanya watokwe na tabasamu la safari nzima hadi wanafika eneo husika walilopaswa kufanyia mkutano. Hii ndiyo siku ambayo walidhamiria kuanza kuuweka wazi mpango wa siri ulioandaliwa na mzee Tualike. Mkutano ulivyoanza mmoja baada ya mwingine alipanda jukwaani kuhubiri, kukazia sera zao walizoanza nazo kipindi cha nyuma. Mtu wa mwisho kupanda jukwaani kuhutubia alikuwa Bi. Mwema. Umati ulilipuka shangwe, pindi alivyokuwa anapanda, mkononi akiwa kakamatia faili lililo na karatasi zilizoandikwa ule mpango.

“Leo tumekuja kuwapa siri. Tunataka mjue namna serikali yetu inawasaidia watu wenye nia ovu na kijiji chetu kwa kulinda maslahi yao. Mkononi mwangu, ninazo nyaraka za siri, zenye andiko la mpango wa siri ulioratibiwa na mzee Tualike miaka ya nyuma kwa ajili ya kuutumia sasa apatapo kuwa Mwenyekiti. Siku zote tumekuwa mstari wa mbele kuwataka hawa watu wasipewe madaraka, hiki nitachozungumza leo ndiyo sababu iliyotufanya tuongee kila siku, tukitaka muwakatae hawa watu. Leo tunazungumza hapa, kesho jiandaeni kusoma taarifa nitakayoisoma hapa magazetini.”

“Mama tuambie...!” walisema wananchi.

“Wale ndugu zetu wa upande wa pili si watu wazuri, sio wazuri hata kidogo. Hizi karatasi zote mnazoniona nazo zina mipango miwili iliyopangwa na wao pindi nasi tuko kwenye familia ile, lakini hatukuutambua hadi pale tulipochukua jukumu la kutoroka, na kukopi baadhi ya nyaraka za siri zenye mipango mbalimbali, lakini hii tunayowaambia leo ndiyo mikubwa zaidi ya mingine. Ndugu wananchi, wale watu, msiwachague, wana nia ya kuvuruga amani na upendo wa kijiji chetu. Wamepanga, endapo watafanikiwa kuingia madarakani, watabadilisha katiba yetu kwa kuweka muda wa utawala toka miaka hii iliyopo hadi kutokuwa na kikomo cha utawala. Je, hawa sio watu wabaya?” Aliuliza Bi. Mwema wakati huo baadhi ya maneno aliyokuwa anatamka yalishindwa kusikika vizuri kutokana na kipaza sauti kuzima zima.



Aliendelea kuelezea hadi pointi nyingine iliyofuata, ya kuvunja vikundi vya kiharakati ili pale atapokuwa madarakani akiamua kutenda jambo, asitokee mtu yeyote wa kupingana naye anachoamua. Habari hiyo ilikuwa mpya masikioni mwa wananchi waliokusanyika hapo kusikiliza, iliibua ulizo, kwa kila mmoja kujiuliza kama kuna ukweli wowote juu ya kile wanachosikia ama ni kampeni tu.

“Hiki niongeacho, siongei kwa sababu nahitaji kura zenu, hapana! Hii ni habari ya kweli. Na laiti kama Awetu angelikuwepo leo hii, angelithibitisha hili, ama alipaswa kuwa mtu wa kwanza kuliweka hadharani, ila ilishindikana kwa sababu ya figisu alizofanyiwa. Kuanzia ile siku ya sherehe ya kuhitimu elimu ya msingi, na zingine zilizofuatia hadi alivyokumbwa na umauti. Hiki nilichozungumza ndicho alipaswa kukizungumza ile siku ya mahafali yao, lakini alishindwa kufanikisha, alitafuta siku nyingine amalizie ilishindikana pia.”



Mnamo saa kumi na mbili jioni mkutano uliahirishwa, watu walianza kutawanyika lakini wakiwa na sintofahamu kubwa kwa kile walichosikia. Hatimaye hoja hizo ziliibua majadiliano mazito, karibu kijiji kizima, kwani mitaa ambayo kikao hicho hakikufanyika walisikiliza kwa njia ya vyombo vya habari hasa redio, runinga na mitandao ya kijamii. Baadhi ya wananchi waliamini, hususani walioko upande wa Bi. Mwema, ila wale wa mzee Tualike hawakuafikiana na habari hiyo, waliona kama hoja za kawaida zitumiwazo na wanasiasa watafutapo huruma kwa wananchi, ambao hawakufungamana na upande wowote. Baadhi waliamini, wengine nao hawakuamini, hivyo ilijenga mgawanyiko mkubwa, huku asilimia kubwa wakiamini kilichoongelewa.



Upande wa mzee Tualike mambo hayakuwa shwari, toka walivyoanza mkutano wao wa kampeni hadi wanamaliza hakuna taarifa yoyote waliyoisikia kuhusu Bi. Mwema na watu wake kama wao walivyotaraji. Baadaye walivyojaribu kuulizia walipewa habari namna mwanamke huyo anavyoungurumisha jukwaani kwa kutoa mipango yao mizito ya siri.

“Unasema kwamba?” Aliuliza mzee Tualike, simu ikiwa sikioni, akizungumza na mtu wa upande wa pili.

“Ndiyo hivyo mzee, mwanamama leo katema cheche zinazowahusu ambazo hajawahi kutamka mahali popote. Tena kaahidi kutoa gazetini.”

“Zinasemaje?”

“Kaanika mpango wenu wa kutaka kubadili katiba na kuvunja vikundi vya kiharakati.”

“Eeeeeeh!”

“Ni hivyo, kama huamini subiri kesho uone gazetini, ama ingia mtandaoni uangalie vipande vya video.”

“Nimekuelewa!...nimekuelewa...!” Alisema Tualike na kukata simu.



Alivyokata tu simu, aliingia kwenye mtandao wa YouTube athibitishe alichoambiwa. Alivikuta. Kila kipande alichoangalia kilikuwa moto, na hakuthubutu hata kumaliza kutazama vipande vyote. Hakufikisha hata dakika moja kwa kila kipande alichoangalia kwani vilimpandisha hasira na kuzidisha chuki dhidi yao. Hakuvumilia! Muda huohuo alianga na mzee Kasoyaga. Mzee Kasoyaga aligeuka kuwa mtumwa wa mzee Tualike, kulipa fadhila alizofanyiwa kipindi cha nyuma toka alivyoanza kuwania nafasi mbalimbali za kiuongozi ngazi za chini hadi hatua ya uenyekiti aliyonayo. Sababu alishakuwa na ufahamu tosha wa uzuri na ubaya wa mzee huyo, alijua ni nini kinaweza kikamsibu pale atapopingana naye ilhali alishasaidiwa kipindi kilichopita kwa nyanja zote.

“Imekuwaje hajapatwa na kile tulichopanga?” Aliuliza mzee Tualike baada ya kupashana habari.

“Kwa taarifa nilizonazo, walibadili usafari, wamezawadiwa magari mapya, hayo ndiyo walitumia.”

“Etiiiiiiiiii!”

“Hee! Wamefanya hivyo.”

“Kwa hiyo tutafanyaje?”

“Niachie kazi, nitamnyoosha, hana uwezo kutuzidi.”



Simu ilivyokatwa, mzee Kasoyaga aliunga upande mwingine, kuwasiliana na vijana wake wa kazi wa siku zote ambao ni Sabaya na Maroda. Aliwapa maagizo fulani yaliyowasukuma muda huo waondoke kwenda nyumbani kwa MJM Zimbwa, kwani ilishafahamika kuwa Bi. Mwema anaishi huko. Lengo la ujio wao lilikuwa ni moja tu, kumkamata na kundi lake kwa ujumla ikiwezekana, kama watashindwa kukamata watu wote, wamkamate Bi. Mwema na Laumio. Safari yao ilikuwa himahima, hadi wanawasili eneo husika, walibisha hodi iliyoitikiwa sekunde chache baada ya kusikika mtu akiitikia kisha kufungua mlango.



Waliingia ndani baada ya kukaribishwa, na kufikia sebuleni ambapo watu wengine walikuwepo pia. Baadaya kusalimiana walijitambulisha na kueleza lengo la ujio wao, wakati huo MJM Zimbwa hakuwepo. Laiti angelikuwepo ingeliwapatia wakati mgumu wa kutimiza nia yao, sababu alishawahi kuwa Mkuu wao kipindi cha nyuma. Wasingeweza kuwakamata mbele yake, na angeliweza kuwazuia. Kutokuwepo kwake iliwarahisishia kuwakamata wote kwa kosa la kutoa maneno yenye uchochezi na uvunjifu wa amani na kuondoka nao kwa haraka kabla MJM Zimbwa hajawakuta.



Wakati wanaondoka watu watokao chombo cha ukusanyaji kodi ya kijiji BOKOTU (Bodi ya Kodi Tuleane) nao walifika mahali hapo, kushikilia gari alizozawadiwa Bi. Mwema na masista wa Angalikana kwa kosa la kutolipia ushuru. Walibaki kuduwaa, kwanini serikali inaamua kuwakandamiza pasi na kosa lolote lakini hakukuwa na uwezo wa kujitetea zaidi ya kuafiki kile kilichowapata, huku wakiambatanishwa na maneno mengi yaliyojaa vitisho wakileta ukaidi. Hatimaye walipelekwa kituo kikuu cha mgambo, na kuwekwa mahabusu huku gari nazo zikipelekwa ofisi ya bodi ya BOKOTU kwa ushikiliaji wakati wakisubiri amri nyingine.



Limekuwa jambo la kawaida sana, serikali ya Tuleane kuweka vizingiti kwa wanaharakati wanaoenda kinyume na matakwa yao, ama vibaraka wa serikali. Wamekuwa wakifanya hivyo, kupunguza nguvu na matarajio ya kuendelea na harakati wanazoanzisha. Asilimia kubwa huundiwa kesi zisizo na msingi, ili kuwapotezea muda na vibaraka kulinda nafasi zao zisiharibiwe. Sio kesi tu, kujeruhiwa na kuuwawa navyo ni miongoni mwa mambo ya kawaida kwa watu wa aina hii, hasa wale wabishi walioshindikana kwenye kesi wanazofunguliwa. Wapo ambao hushambuliwa na hujeruhiwa, wengine huuwawa na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika wa uovu huo.



Katika mambo haya, chombo kinachohusika na ulinzi na usalama, jeshi la mgambo, hushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo huku likitengeneza mazingira ya wazi ya uonevu, kuwaaminisha wananchi kuwa wapinzani wa serikali ni wachochezi, hawapati huduma za kisheria inavyotakiwa. Mazingira haya pia, hutoa ishara zote, watu wa idara nyeti za serikali kuwa wahusika wa vitendo vibaya vinavyotokea. Hiyo yote inachangiwa na ukimya wa muda mrefu katika utoaji wa maamuzi ya uhalifu mkubwa utokeapo, kwa wanaharakati ama watendaji wa mgambo wanapokuwa wahusika. Lengo hilo hufanyika ili kulinda maslahi ya mtu, au kikundi fulani kinachopigia upatu serikali. Wakati wa sasa mambo yako tofauti na awali ndani ya jeshi la mgambo la Tuleane, sio Tuleane tu, hata vijiji vingine pia, kwa kushindwa kudumisha na kuziongoza amri bali amri ndizo huwaongoza wao, zile zitokazo juu.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Viongozi wengi wameshindwa kutambua thamani ya mwananchi, mchangiaji mkubwa wa kodi na mambo mengine yanayoiwezesha serikali kuwa imara kwa kila nyanja. Wanasahau, kuwa huyu ndiyo anayewapa wadhifa wa wao kupokea pesa nyingi zitokanazo na jasho lao, na muda mwingine hudiriki kuiba pia, tena sio kiwango kidogo cha pesa, hapana! Kiwango kikubwa tu, huku wakishindwa kuchukuliwa hatua, hata ya kufikishwa mbele ya vyombo vya kisheria na endapo watafikishwa kesi itasikilizwa baadaye hufutwa. Pia wanakosa huruma ya kutambua ni namna gani wananchi walihangaika katika shughuli zao wakachangia pesa hizo kupitia viushuru lukuki waviwekavyo kila sehemu. Mwananchi amekuwa jalala, na chanzo kikuu cha kushibisha matumbo yao, hali isiyovumilika na kuhitajika mahali popote, ila wananchi wenyewe wanashindwa kulibainisha hili, nakuweka wazi matakwa yao ya kutowahitaji sababu ya uoga.



Nao wanasahau kuwa ndiyo wenye mamlaka kijijini hapo, kwa kuhofia kupoteza uhai wao. Wanaendelea kuruhusu uonevu, kwa sababu wanashindwa kutambua thamani waliyonayo, wanaishia kushangaa na kutoa malalamiko ya chinichini waonapo maovu. Wanashindwa kuinuka kukemea na kuchukua maamuzi sahihi ya kukabiliana. Mzee Kasoyaga alikuwa anafanya haya kwa lengo la kumsaidia Mzee Tualike, aliyempigania miaka ya nyuma katika nafasi mbalimbali za kiuongozi kuanzia zile za chini hadi aliyonayo sasa. Alihitaji ushindi unaenda kwake, na si kwa mtu mwingine kama wananchi walivyoonesha mapendo yao.







Japo ilikuwa ni usiku ila baadhi ya majirani walishuhudia kinachoendelea, hivyo MJM Zimbwa alivyorejea iliwapa urahisi wa kumwambia wapi wenzake waliko. Habari aliyoipata haikumshtua sana, sababu ya ufahamu wake wa kutosha juu ya matendo ya dola kwa wanaharakati wanaokinzana naye. Japo alikuwa mstaafu wa serikali, tena katika nafasi nyeti kiuongozi lakini hakuwa na mapendo yoyote na serikali kutokana na udhalilishaji aliotendewa miaka ya nyuma ya kufukuzwa nafasi ya ukuu wa mgambo kabla muda wake wa ustaafu haujafika, kisa tu alipishana kauli na Mwenyekiti wa kijiji, mzee Kasoyaga.



Alichofanya, baada ya kupata taarifa, aliwasiliana na mwanasheria ili akawasaidie kina Bi. Mwema. Kweli! Mwanamama, aitwaye Dkt. Emmakulata Mbunda, mwanasheria na wakili msomi alienda kituo kikuu cha mgambo usiku huo ili kutoa msaada kwa watu alioambiwa, lakini mgambo aliowakuta walimzuia kuingia ndani. Baadhi yao walimzuia, mmoja wao alisogea pembeni kidogo na kuonekana kufanya mawasiliano.

“Amekuja mwanasheria wa MJM Zimbwa, alisema amekuja kuwaona wateja wake, ila tumemzuia.”

“Mzuieni kabisa, asifanikiwe kuonana nao, halafu baadaye fanyeni jitihada za kuwahamisha kituo.”

“Nimekuelewa.” Alimalizia kwa kusema hivyo mgambo kisha alikata simu.



Jitihada za kumzuia zilifikia hatua ya kutishiwa na bunduki, aina ya pump action ili aondoke kituoni hapo. Jambo lililopelekea naye kupandwa na hasira kama mbogo.

“Mnanizuiaje kuonana na wateja wangu? Sheria ipi inawapa mamlaka hayo?”

“Njoo kesho asubuhi mama, usiku hatuwezi kukuruhusu.”

“Mniambie vifungu vya sheria, sio kwenda kwa hoja. Nataka tuende kisheria.”

“Mama! Hatubadilishi kauli, kama unataka kutumia sheria nenda mahakamani. Hapa ni amri tu.”

“Sababu hamna taaluma ya sheria, japo mnatumikia sheria ndiyo maana mnatanguliza amri. Ila leo mtafahamu nini maana ya sheria,” alisema Dkt. Emmakulata huku akisogea pembeni na kutoa kilongalonga kwenye mkoba wake.



Mgambo aliyekuwa anabishana nao ghafla alitoweka eneo lile, kwa kupotelea ndani ya kituo kisha kufunga mlango. Dkt. Emmakulata naye hakuchukua muda mrefu kumaliza maongezi yake, mara baada ya muda jopo la watu wanne walifika kituoni pale alipoketi. Walikuwa wanasheria wenzake. Aliwaeleza kila kitu kuhusu ujio wake mahali hapo na mambo yaliyomsibu mara baada ya kufika.

“Watakuzuiaje?” Walimuuliza kwa pamoja.

“Hata sielewi hawa jamaa lengo lao ni lipi.”

“Twendeni tukawaone.”



Waliondoka kuelekea ndani ya kituo, ila hawakufanikiwa kuingia kwa sababu mlango ulishafungwa. Na walivyojaribu kuomba wafunguliwe, hawakujibiwa. Iliwabidi waondoke baada ya kuona hamna dalili za wao kuruhusiwa kuonana na kina Bi. Mwema ili wapate maelezo yao wajue namna ya kuwatetea. Wakakubaliana, asubuhi ya siku inayofuata wakutane mahali hapo. Kulivyopambazuka, wakafanya hivyo! Mapema sana, asubuhi waliwasili kituoni kulilia mustakabali wa Bi. Mwema na watu wake. Wakati huo tayari taarifa za kukamatwa kwao zilishaenea mtaani, karibia kijiji kizima. Jambo lililowasukuma wale watu wawapendao wakusanyike kituoni, kushinikiza watolewe.



Siku hii walifanikiwa kuingia kisha kuonana na Mkuu wa kituo na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa kituoni hapo ili kuangalia namna ya kuwasaidia. Kikubwa walitaka wapatiwe dhamana ila waliambulia ugumu wa kutotekelezwa hitajio lao kwani mgambo walikuwa wanatii amri ya mtu ambaye ni mzee Kasoyaga. Wananchi nao kila dakika walizidi kuongezeka, hata wale wampendao mzee Tualike, ambao walifika kushuhudia hatma ya wanaharakati hao.



Mkusanyiko ulizidi kuwa mkubwa, kila dakika ilivyozidi kusonga mbele ndipo mamia ya wananchi walifika. Kwa hasira, walikizunguka kituo, kwa umbali fulani ambapo mgambo hawakusita kuwadhibiti japo walikuwa wanafanyiwa vitendo vya hapa na pale, kama vile kurushiwa mawe, miti na chupa zilizo na ujazo wa mikojo kutokana na hasira kali waliyonayo.



Mle ndani jopo la mawakili watano, likiongozwa na Dkt. Emmakulata walizunguka karibu ofisi zote za jingo. Muda mwingine waliketi eneo la mapumziko kusubiri maelezo na uwezekano wa kukamilishwa takwa lao lakini dalili zilikosekana za kuwaaminisha kuwa wanaweza kutimiza hicho kitu kwa wakati. Ilifikia hatua, walitamani kutembeza makofi kwa mgambo waliowapatia huduma, kwani dhahiri walionesha mazingira ya kutowajali na kutii matakwa yao.

“Hawa jamaa mbona siwaelewi?”

“Acha tu, ila sheria itachukua mkondo wake hata kama watatuchelewesha. Inaonekana wanapata maelekezo kutoka kwa mtu fulani.”

“Na vipi ulishaonana na huyo Mkuu wao wa hii kanda?”

“Kajifungia ofisini, na kila ninavyompigia simu hapokei.”

“Hakuna shida, sheria itaamua leo. Wanataka kuikalia? Wataona wakipatacho.”



Ilikuwa sehemu ya maongezi ya mawakili hao wakimsubiri Mrakibu wa jeshi la mgambo kanda ya kati inayojumuisha mitaa minne ya kijiji cha Tuleane. Hali haikutulia, ilichafuka, na yote ni kwa sababu wanamgambo walikuwa wanatekeleza amri iliyotolewa na mtu, na si kufuata utaratibu unavyotakiwa. Ilichangia kuwaweka kwenye wakati mgumu, kiasi kwamba ilifikia hatua walitumia nguvu kubwa kujikinga na vitendo vilivyoanzishwa na wale mawakili pasi na sahau waliokusanyika nje ya kituo. Hawakusita kupiga mabomu, ya kishindo na moshi pia, ili kuwatawanya mamia ya watu waliokusanyika.



Wakati hayo yanaendelea, mzee Kasoyaga alikuwa ofisini kwake—ofisi kuu ya kijiji, akiendelea na majukumu kama ilivyo ada. Tukio lililojiri alilishuhudia kwa njia ya picha za mnato pamoja na video alizokuwa anatumiwa na walinzi wake wa siri, sanjari na wale mgambo walioko kituoni. Wakati wakiomba maelekezo nini cha kufanya. Shinikizo lililokuwepo kutoka kwa wananchi lilimsukuma kutoa amri za kinyama na zisizo na utu. Upande wa pili pia, alikuwa anafanya mawasiliano kila baada ya muda na mstaafu MJM Zimbwa ili amuondoe mwanasheria wake na wale wengine kituoni. Alitaka kabisa kwa udi na uvumba Bi. Mwema na watu wake wasiondolewe. Kauli ilikuwa ngumu kukubalika. MJM Zimbwa alikataa katakata kumtoa kwa kigezo cha kutoingilia biashara ya mtu ilhali naye alikuwa sehemu ya msaada. Ila kwa wakati huo hakuhitaji kutambulika na viongozi wa serikali kama yupo upande wa upinzani.



Kitendo cha kukataliwa kilimpa hisia za uhusika wa MJM Zimbwa katika tukio. Hakuhitaji wazo hilo limtawale akilini mwake. Hakulipa nafasi kwa muda huo. Aliahidi kulifanyia kazi siku zijazo, lakini ilimfanya apandwe na hasira kali akijiuliza, kwanini kakataliwa wakati ndiye mtawala?

“Hao vimbelembele piga hata risasi,” Amri ilitoka.

“Ndiyo kiongozi. Na vipi kuhusu wale watu?”

“Wako kituoni ama mlishawatoa jana?”

“Tuliwatoa, wako ofisini kwa kamanda.”

“Waacheni huko hadi saa kumi jioni ndipo muwaachie, tena kwa dhamana ya kiwango kikubwa cha pesa.”

“Hakuna shida mheshimiwa, tutatekeleza hilo.”



Kauli iliyotoka kwa mzee Kasoyaga, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, ndiyo iliyotekelezwa na mgambo walioko kituoni na walinzi wake wa siri. Hivyo kituoni paliwaka, kila mwananchi aliyeonekana kimbelembele kushadadia Bi. Mwema na wenziye waachiwe alishambuliwa kwa mabomu ya machozi. Muda mwingine hata risasi za moto alipoonekana ameweza kuhimili moshi wa mabomu. Ndani nako, sehemu waliyohifadhiwa Bi. Mwema na watu wake, hali haikuwa shwari. Waliteswa, sio kwa kupigwa, hapana, bali kwa kunyimwa mahitaji ya msingi, hasa chakula na maji. Toka walivyoingia, ni mlo mmoja tu walibahatika kuupata asubuhi, tena chakula kilichokosa ubora, kisichoiva, kilichowatengenezea mazingira magumu ya ulaji. Maji walikuwa wanaletewa lita tatu tu, kwa watu wote watano, lengo ni kuwadhoofisha ili waachane na kile walichopanga kufanya. Hakika, walidhoofika kwani kiu na njaa iliyowakumba, iliwafanya wasahau harakati zao na kuwaza namna ya kupata shibe na hali hiyo kufika mwisho.

Fika walifahamu, wanafanyiwa hayo sababu ya kuvumbua mabaya wanayotaraji kuyafanya, kwa lengo la kuwasaidia wana Tuleane. Ila hawakukata tamaa, walijipa moyo lazima wahakikishe wanatimiza walichoanza nacho. Saa 10 jioni, kama oda ilivyotoka, walitolewa kwenye vyumba walivyofungiwa wakapelekwa kituoni. Zikafanyika taratibu fulani baadaye wakaachiwa kwa dhamana, iliyogharimu kiwango kikubwa cha pesa. Walivyotoka tu kituoni, wakaomba wapatiwe chakula, baada ya hapo wakafunga safari kuelekea ofisi ya Bokotu, kufuatilia gari zao, zilizokamatwa. Wafuasi waliokusanyika kituoni wakawa nyuma yao kuwasindikiza, huku wakiimba nyimbo lukuki za kuwasifu kuwa ni mashujaa wa kweli wanaopaswa kupewa kijiji chao kuongoza.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Safari haikuwa ndefu sana, takribani mita mia tano, maana ofisi hazikuwa mbali na kituo kikuu cha mgambo kilipo. Muda waliofika, ofisi ilikuwa bado haijafungwa, hivyo mmoja wao, ambaye ni Bi. Mwema alifanikiwa kuingia ndani akiambatana na jopo la wanasheria. Walitaka kujua taratibu zinakuwaje ili wapate gari zao, maana walikuwa hawadaiwi. Sababu kila lililotokea ni la kuamriwa huku nako ubabaishaji ulikuwa mwingi zaidi ya kituoni. Kwani amri ilishatoka kuwa hakuna kurudishiwa magari yao siku hiyo hadi siku inayofuata. Lengo, kama watalazimika kufanya kampeni, wafanyie gari yao ya zamani, ambayo ilishakuwa na hitilafu. Baada ya mzunguko wa muda mrefu, hatimaye waliamua kuahirisha ili muda uliobakia wawahi kufanya kampeni, japo muda ulishayoyoma.



Hawakuhitaji kubadili nguo, walidhamiria kwenda walivyo kwenye mtaa ambao kampeni ilipaswa kufanyika. Wakapitia gereji, walikoiacha gari waliyokuwa wanatumia awali. Kisha wakajipanga tayari kwa safari kuanza.



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog