Search This Blog

Friday, November 18, 2022

MASKINI MAYASA - 5

 





    Simulizi : Maskini Mayasa

    Sehemu Ya Tano (5)





    ***



    Kijana ambaye alikutana na Neema,kama walivyokubaliana ,jioni walitafutana na kukutana. Neema ndiye aliyemwambia kijana huyo aende kwake. Kijana alipofika kwa Neema,alikaa moja kwa moja kitandani maana chumba hakikuwa na sofa wala kiti, hakukuwa na chochote cha kukalia zaidi ya kitanda tu.

    “Nambie Neema,kitambo sana ila naona mwana anakaribia kuja duniani sasa.....”

    “Wewe Bahati si ulinikimbia nilipokuambia nina mimba yako sasa nimembambikiza mtu na sasa yeye ndiye anayehudumia kila kitu......”

    “Hamna,wala sio hivyo,mimi sikukimbia, sema tu harakati na mihangaiko ndio ilinifanya wakati ule nikatae ila ulikuwa ujinga tu, naamini hiki ni kiumbe changu na wala hakuna utata juu ya hilo,sasa sioni sababu ya wewe kuendelea kung'ang'ania baba ambaye sio halali..”

    Neema alitulia kimya baada ya maneno ya Bahati. Neema alikumbuka jinsi walivyoachana na Bahati wakiwa kijijini kwao. Mimba ni kweli ilikuwa ya Bahati na wala sio Damaso. Neema aliamua kufanya mipango na kumlazimisha bibi Damaso amwite Damaso mpaka wakutane na mimba ionekane ya Damaso. Neema aliyafanya haya yote ili kuepusha aibu ya kuonekana mimba haina baba kwani Bahati alitoroka na hata kuhusu mimba alisema kuwa haisiki nayo. Bibi Damaso naye kwa tamaa na hulka zake bila hata kujua akaingia kichwa kichwa na kumwingiza Damaso kwenye mkenge. Damaso akawa anahudumia mimba ambayo sio yake bila kujua.

    Neema alikumbuka yote yaliyopita,akaamua kumuuliza Bahati ,

    “Sasa itakuwaje maana sasa hivi nimeshampachika mtu huu ujauzito na yeye ndiye anayehudumia?”

    “Swali zuri sana, kwa sasa naomba muache jamaa aendelee kukuhudumia hadi utakapojifungua alafu mimi nitajitokeza na kudai mtoto wangu na kama ikitokea ubishi basi tutavitafuta vipimo vya DNA kokote kule ili tuangalie ni nani hasa baba wa mtoto, na naamini hatuwezi kufikia huko kwani ni lazima atakayezaliwa atakopi sura yangu.....”

    “Sasa si bora sasa hivi ungejitokeza ili mwenzako asiendelee kujua ana mtoto wakati hana chake hapa....”

    “Hiyo sawa! Lakini kwa sasa mimi wala siko vizuri sana, ningekuwa nipo poa basi hata leo hii ningekuchukua, wewe na mimi inabidi tuwe kitu kimoja,na hii siri anayeijua ni mimi na wewe na ndio maana nakusisitizia kuwa kitu kimoja huyo mtu mwache aendelee kulea kwa mapenzi yake lakini mwisho wa siku kidume najitokeza alafu nachukua mtoto kiulaini kabisa.....wajinga ndio waliwao daima.... ”

    “Lakini Bahati hili jambo huoni kama linaweza kutuletea shida?”

    “Neema acha kuwa na mawazo ya kijinga, hivi wewe utajisikiaje moyoni mwako kwamba baba halali nipo lakini unamwacha mwanao anacheza na baba ambaye siye? Amka toka usingizini ,achana naye mimi ndiye mwenyewe”

    Neema akalainika na maneno ya Bahati,hivyo wakakubaliana kuwa kama Bahati alivyopendekeza. Damaso aliendelea kuhudumia mimba zote huku akiamini anakaribia kuwa baba wa watoto wawili. Kipato chake kidogo alikibana hivyohivyo na kuendelea na huduma kwa Mayasa na Neema,



    Siku moja Mayasa akiwa yupo kliniki alishangaa kumuona Neema naye akija hapo. Mwanzo alipomuona alijua amemfananisha lakini aliposogea karibu yake alimuona vizuri kuwa ndiye yeye. Neema alikuwa ameongozana na Bahati na kwa jinsi walivyokawa wanaonekana siku hiyo,wala huwezi kuuliza swali kuwa hao wanauhusiano gani. Walionekana dhahiri ni wapenzi.

    Mayasa alishangaa sana kumuona mtu ambaye aliambiwa na mume wake Damaso kuwa yupo kijijini lakini alimuona siku hiyo tena akiwa na mwanamume mwingine. Tukio hilo lilimchanganya sana Mayasa. Wakati akiwa anaendelea kushangaa ,Neema naye alienda moja kwa moja kukaa pembeni ya Mayasa. Neema akajifanya hajamuona Mayasa. Mayasa akamshika begani Neema ,kisha akamsalimu. Neema aligeuka na kumtazama Mayasa,hakujibu kitu akaishia kubinua mdomo tu. Mayasa alitamani sana kumuuliza anakaa wapi na mtu ambaye amefuatana naye ni nani lakini aliona kama atazalisha jambo lingine ambalo halikuwepo hapo awali. Mayasa alipomaliza mambo yake akaondoka na akaenda kujibanza sehemu fulani ili amtazame kwa makini Neema. Baadae akumuona Neema akiwa na Bahati wanatoka pamoja na kufurahi pamoja. Hata maneno ambayo walikuwa wanayaongea yalikuwa yanaonesha ni wapenzi.

    “Huyu mtoto akizaliwa basi jina lake litakuwa Bahati kama langu, maana amepata bahati ya kulelewa na baba wawili,mmoja fake na mwingine ni original ambaye ndiye mimi”

    Bahati alijinasibu mbele ya Neema ,wakati huo Mayasa akiwa anawasikia vizuri kila walilokuwa wanaongea. Mayasa akagundua kuwa Damaso anachezewa mchezo mbaya, anaaminishwa mimba ni yake kumbe si kweli. Mayasa akaamua kujitokeza mbele yao kwa lengo la kumshushua Neema na aache mara moja tabia ya kumlaghai Damaso.

    “Kumbe wewe dada ni mjinga na kahaba sana,kumbe mume wangu ndio unachuma alafu unakuja kutumia nawanaume mwingine huku ukimdanganya mume wangu, nimewasikiliza maneno yenu yote,siku zote mwisho ubaya ni aibu, leo ndio umefika mwisho wako,achana kabisa na mume wangu na hili jambo naenda kumwambia Damaso leo leo.... ”

    Mayasa alimtahadharisha Neema kuhusu mume wake, Neema alibinua midomo kwa dharau na kejeli kwa maneno ya Mayasa. Alimpuuza na alitamani sana apigane naye lakini wakati huo tumbo lilikuwa kubwa sana.

    Bahati akamsogelea Mayasa na kumtandika vibao viwili na huku akimsemea maneno mabaya,Mayasa alitaka kujaribu kurusha mikono yake kwa Bahati lakini Bahati akamdaka na kumuogezea kofi lingine.

    “Yasiyo kuhusu ukiyafuatilia yatakusumbua sana, siku nyingine ukiona jambo halikuhusu achana nalo hata kama linakuumiza moyo.....pilipili usiyoila yakuwashia nini?”

    Neema alimwambia Mayasa na wakati huohuo yeye na Bahati wakashika njia na kupotea zao. Mayasa aliwaangalia hadi walivyopotea kabisa machoni pake ndipo na yeye akashika njia kuelekea kwake. Alipofika kwake, alimsubiri Damaso hadi alivyorudi ndipo akaamua kumuuliza Damaso kuhusu Neema wapi aliko. Damaso alishtuka lakini bado aliendelea kuficha ukweli, yeye alisema kuwa bado yupo huko kijijini kwao. Baada ya Damaso kujieleza sana,Mayasa akasema,

    “Kama kweli yupo kijijini ,basi haina haja ya kuendelea tena kuongea nilichokiona leo huko hospitali”

    “Vipi kwani umeona nini?”

    “Aaah basi haina maana kwani teyari nilichokiona kingekuwa na maana kama Neema angekuwa yupo hapa mjini, ila kwa kuwa yupo kijijini basi tuache tu.....”

    Damaso akaonesha wasiwasi kwa kile alichokisema Mayasa,akamwambia Mayasa aseme tu alichokiona,Mayasa alipoona Damaso analazimisha sana,akamuuliza swali,

    “Vipi kwani Damaso mbona unanilazimisha sana? Au kuna jambo umenificha ambalo ninastahili kulijua?”

    “Mmmh! Wala hamna jambo lolote....”

    “Sasa?”

    “nataka nijue tu umeona kitu gani huko....”

    “Unajua Damaso iko hivi, sio kila siku uongo utakuokoa katika jambo fulani, uongo kuna wakati unatakiwa ukae pembeni na ukweli uchukue nafasi ambayo itapelekea kufungua milango kwa jambo ambalo limefichika na linahitaji ufumbuzi, unaweza ukawa unadanganya jambo fulani kwa kudhani kuwa unajiokoa au unaepusha jambo fulani kumbe ndio ikawa unajiongezea balaa....”

    “Kwa hiyo unamaanisha kuwa haya ninayokuambia ni ya uongo?”

    “Wala sina maana hiyo nilikuwa natoa mfano tu.....”

    Damaso akiwa bado anatafakari na huku akijiandaa kusema jambo, Mayasa akasema tena,

    “Aaah! Jamani Damaso ngoja tuyaache hayo, tuongee habari zingine.....Ngoja tuongee habari za hospitali, Daktari amesema ninaendelea vizuri sana na hata aliyepo tumboni naye anaendelea vizuri ila ameniambia niongeze mazoezi tu .....”

    Damaso alitikisa kichwa akiashiria anamwitikia alichokuwa anakisema Mayasa lakini moyoni mwake alikuwa anajiuliza kimetokea kitu gani kati ya Neema na Mayasa. Alianza kuhisi pengine wamekutana na Neema wakiwa hospitali. Damaso hakujua kuna jambo gani la zaidi ambalo amekumbana nalo Mayasa. Alitamani sana kumsikia Mayasa anamwambia jambo lenyewe lakini kutokana na tabia yake ya kusema uongo kuhusu Neema ilimnyima kabisa uhuru wa kuendelea kuuliza kuhusu jambo hilo. Damaso alipopata mpenyo akamtafuta Neema kwenye simu, alipompata akamuuliza kama alionana na Mayasa siku hiyo, lakini majibu ya Neema yalikuwa ya maudhi sana na mkato, alionesha wazi hakutaka kuwa teyari kuulizwa swali kama hilo. Damaso akakata simu,akaona bora aende kwa Neema wakati huohuo.

    Alimuaga Mayasa kuwa anaenda kuangalia mpira, Mayasa hakuwa na shida yeyote, akamwacha Damaso aende tu. Damaso hakuchukua usafiri wowote, alitembea kwa miguu kuelekea alikompangia Neema.

    Wakati Damaso yupo njiani, Neema alikuwa yupo chumbani kwake na Bahati wakipiga stori huku wakicheka na kufurahi sana. Damaso alitembea hadi akafika mlangoni kwa Neema, hakutaka kuhodisha kwa kuwa alijua ni kwake. Neema na Bahati walikuwa kitandani tena wakiwa katika hali ya kimahaba sana, hata Bahati alikuwa hana shati juu,alilivua. Damaso akashika kitasa na kuanza kukinyonga ili mlango ufunguke..







    Damaso baada kunyonga kitasa, mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani. Akaacha akatulia,akataka achukue simu yake alafu ampigie Neema lakini kabla hajafanya hivyo akasikia sauti zinatoka kwa ndani. Akatulia mlangoni huku akitega sikio kwa umakini sana. Kuna muda sauti ilikuwa inapenya hadi nje lakini muda mwingine kulikuwa na ukimya tu. Mbaya zaidi dirisha lilikuwa kwa nyuma ,hivyo mpaka uzunguke ndipo uweze kuchungulia. Akaamua kugonga mlango kwa nguvu huku akiita jina la Neema. Neema aliijua sauti ya Damaso, akajiridhisha baada kuchungulia katika tundu la ufunguo na kumuona Damaso.

    Neema akamwambia Bahati avae shati lake harakaharaka,alafu atajifanya ni kaka yake. Baada ya Bahati kuvaa shati, Neema akauliza ni nani anayegonga mlango,jibu lilikuwa ni Damaso. Neema akaufungua mlango. Damaso akazama ndani kwa haraka sana. Akamkuta Bahati amekaa kitandani lakini sura yake ikiwa ipo kiunyonge sana. Damaso hata kabla ya salamu akaamua kumuuliza Bahati ni nani. Bahati kabla hata hajajibu, Neema akamuuliza swali Damaso,

    “Mmmmh! Damaso ina maana haumjui huyu? Mbona amekaa sana pale nyumbani? Ni mtoto wa shangazi ,kwa hiyo ni shemeji yako”

    Damaso hakujibu kitu, alimwangalia Bahati huku akili yake ikionekana wazi ipo katika mtinginyo wa mawazo. Akamsalimia Bahati kwa kumshika mkono, alafu akamuuliza jina lake. Baada ya kujibiwa ,bado Damaso alikuwa hayupo sawa, alikuwa anajiuliza kama hao ni wanandugu kwa nini sasa walijifungia mlango. Neema alijua Damaso bado yupo katika wimbi la mawazo, akaamua kujikomba ili kumtuliza,

    “Vipi Damaso mbona unaonekana mwenye maswali mengi sana? Au unajiuliza kwa nini mlango tuliufunga kwa ndani?”

    Damaso akajibu hamna kitu anachowaza yupo sawa tu, Neema akasema tena,

    “Kama unajiuliza kwanini mlango tuliufunga kwa ndani,jibu lake ni kuwa hapa yaani kuna watoto wa huyo mama mpangaji mwenzetu huwa wanaingia sana alafu ni wasumbufu sana, kuna muda unakuta wanaingia wakiwa na michanga miguuni pamoja na matope, huwa wanachafua ndani,kwa hiyo niliamua kufunga ili tumalize maongezi yetu kwa uhuru na kuelewana pia na chumba kisichafuliwe”

    Hapo angalau sasa Damaso alianza kuonekana ana tabasamu katika sura yake, hofu ikaanza kumwondoka na kuamini kuwa ni kaka yake wala hamna lolote lingine. Damaso akamuuliza tena kuhusu Mayasa kama walikutana naye siku hiyo lakini majibu yalikuwa kama yaleyale ya mwanzo ,alishindwa kujua Mayasa aliona kitu gani siku hiyo alivyokuwa kliniki, akaamua kuliacha jambo hilo na akawaaga ili aondoke.

    “Sasa Neema mimi nilipita tu hapa kukusalimu, ngoja niwaache ili muendelee kuongea”

    Neema naye akamwitikia harakaharaka ili tu aondoke na hao waendelee na mambo yao. Damaso akaondoka. Akiwa njiani alikutana na mama fulani ambaye anakaa katika nyumba anayokaa Neema, mama huyo alimfahamu Damaso kwani kuna siku aliwahi kutambulishwa na Neema kuwa ndiye mume wake. Walisalimiana na Damaso alafu baadae mama huyo akamuuliza swali Damaso,

    “Hivi yule binti wa pale nyumbani ni mkeo kabisa kabisa au ....?

    “Ni mke wangu,vipi mbona swali hilo?”

    “Aaaah! Hata hamna kitu, bado upo naye au mmeachana?”

    “Nipo naye hadi kesho....”

    “Mawazo yangu mliachana......”

    “Kwa nini unawaza hivyo?”

    “Siku namuona yupo na kijana fulani hivi basi ndio nikajua mmeachana na sasa yupo na yule kijana”

    “Hapana bado nipo naye, yule kijana ni kaka yake tu"

    “Kaka yake?!!”

    Mama huyo alishangaa sana jibu la Damaso kuwa ni kaka yake wakati anawaona kila siku wanalala pamoja na wana asilimia mia moja za kuwa wapenzi. Damaso akajibu tena kuwa ni kaka yake. Mama huyo alitamani kumwambia ukweli Damaso lakini akaona atamwaribia mwenzake, maana hata yeye mwenyewe ingawa alikuwa anakaa na bwana lakini bado alikuwa ana michepuko miwili. Hakutaka kuendelea kuongea zaidi, akaamua kuagana naye na kila mmoja akaendelea na safari yake.

    Damaso akarejea kwake na kuendelea na shughuli zingine. Siku zilisonga mbele hadi ikafika hatua Neema anahesabiwa siku tu ili aweze kuongeza binadamu katika hii dunia yenye kila aina ya ubaya na udhurumati. Baba wa mtoto aliyekuwa anajulikana na watu wa wanaoishi nao alikuwa ni Damaso lakini kiasilia na mwenyewe hasa ni Bahati. Hata Damaso naye alianza kuwa na matumaini ya kuitwa baba. Siri hii alikuwa nayo Bahati ,Neema na Mayasa ambaye aliwahi kuwasikia wakiteta juu ya jambo hilo. Mayasa kila alipojaribu kumwelezea kuhusu juu ya utata uliojitokeza kuhusu mimba ,Damaso hakutaka kabisa kusikia kuhusu suala hilo na hii ilichagizwa na bibi yake ambaye mara kwa mara alikuwa anapiga simu na kumwimiza amtunze Neema pamoja na mimba yake.

    Siku ya kujifungua iliwadia na Neema akapelekwa hospitali kwa ajili ya kujifungu. Kwa msaada wake Mungu mwenyewe, Neema alijifungua salama mtoto wa kiume. Baada ya kutoka hospitali ,walienda hadi kijijini kwao. Bibi Damaso ndiye aliyekuwa anashugulika mambo mengi huku akifurahi baada ya kuona adhma yake imetimia. Kadri siku zilivyozidi kwenda ,sura ya mtoto wala haikuonesha dalili za kufanana na Damaso. Minong'ono ya majirani ilianza lakini minong'ono hiyo wala haikumfikia Neema wala Damaso wala bibi Damaso,hivyo kila mmoja aliendelea na jambo lake na maisha yake.

    Baada ya Neema kuwa sawa na kuwa na nguvu, alirejea mjini kwa ajili ya kuendelea na maisha kama kawaida. Bahati naye alikuwa anamsubiri kwa hamu kubwa sana. Mtoto alikuwa anafanana sana na Bahati, hakufanana hata kimoja na Damaso. Kama kawaida,mchezo ukawa unaendelea, Damaso anapeleka huduma na Bahati naye hivyohivyo.

    Siku moja Bahati akamwambia Neema ,

    “Neema sasa umefika wakati wa kujua mbivu na mbichi, kila mmoja achukue kilicho chake, hatuwezi kuendelea kuishi hivi kama watumwa kwa kutokuwa na uhuru na maisha yetu, mtoto amezaliwa na mwenyewe umeona kila kitu kachukua cha kwangu, yaani hii ni kopi yangu kabisa, umefika wakati sasa Damaso aambiwe ukweli ili asiwe anakuja kuja hapa.....”

    “Mmmh! Sasa wewe unashauri nini?”

    “Mpigie simu, akija hapa mwambie kuwa mimi ndiye baba na hana chake hapa, wewe mchane tu ukweli wake....”

    “Kuambiwa ataambiwa lakini sio kwa ghafla kiasi hicho, bora ajue kidogo kidogo”

    Bahati akajifanya kukasirika,alafu akasema,

    “Neema, kumbe wewe unampenda Damaso na mimi unanizingua tu, hadi leo hutaki kumwambia unasubiri nini? Hivi wewe hujui kama Damaso ana mke? Unadhani atakuoa wewe? Yule teyari ana maisha yake na wewe unatakiwa uwe na maisha yako, mimi Bahati ndiyo ninayestahili kuishi na wewe, kama hutaki kumwambia ,nitaenda kumwambia mwenyewe na mambo nikayavuruge mwenyewe”

    “Wewe tulia,mimi ndiye niliucheza mchezo na nitaumaliza mchezo sasa hofu yako nini?”

    “Haiwezekani miezi inazidi kukatika tu alafu wewe upo kimya, kama inashindikana niambie mimi niangalie ustaraabu mwingine maana naona kama nampigia gitaa mbuzi vile...”

    “Basi sawa leo nitampigia simu, akija hapa nitamwambia unachotaka ili uridhike, mimi wala simpendi yule ,ni bibi yake tu ndiye aliyenifanya nikutane naye wala sio mimi,wewe ndiye mwanaume wangu wa kwanza na bila shaka utakuwa wa mwisho”

    Bahati akatabasamu baada ya kusikia kauli ya Neema, na muda huohuo Damaso alipigiwa simu na Neema huku akiambiwa aende kuna tatizo limetokea. Damaso alikuwa kazini kwake,haraka sana akaenda kwa Neema. Alimkuta Neema yupo na Bahati,hakushangaa sana kwani teyari alikuwa anamfahamu Bahati kama shemeji yake. Neema alimsalimu Damaso na baada ya hapo Neema akasema,

    “Samahani sana Damaso kwa haya nitakayokueleza sasa hivi, kwanza kabla sijasema lolote nakuomba mwangalie mtoto alafu mtazame na huyu Bahati alafu niambie umegundua kitu gani......”

    Damaso akamtazama mtoto na Bahati, walikuwa wanafanana sana, Damaso akakumbuka kuwa Bahati ni kaka wa Neema hivyo Damaso akajibu,

    “Yeah nimewaona ,wamefanana sana”

    “Umegundua nini?”

    Neema aliuliza,Damaso akajibu,

    “Nimegundua ni kweli Bahati ni ndugu yenu na ndio maana mtoto kafanana naye”

    Neema akatabasamu kisha akasema,

    “Pole umepotea, na bado upo gizani. Ngoja leo nikutoe gizani na nikuweke kwenye nuru.Bibi yako ndiye aliyetufanya sisi tukutane ila kiukweli moyo wangu wala haupo kwako, huyu unayemuona ndiye.......”

    Kabla hata hajamaliza kusema, Simu ya Damaso ilianza kuita, akaipokea na kupewa taarifa za Mayasa kuzidiwa hivyo anahitajika aende hospitali kwa kujifungua mtoto. Aliyepiga simu alikuwa ni dada yake Mayasa.Muda huohuo Damaso akampigia simu dereva wa tax na kumwambia awahi kwenda kumchukua Mayasa kwake na kumpeleka hospotali.

    Baada ya dakika tano hivi, dada yake Mayasa alipiga tena simu kuwa wapo njiani wanaelekea hospitali, Damaso yeye akawajibu kuwa naye atakuwa njiani hivyo watakutana hospitalini hukouko. Baada ya kukata simu,Damaso akamgeukia Neema kisha akamuuliza,

    “Unajua mimi sijaelewa kitu,yaani unamaanisha nini kwa haya unayoyazungumza?”

    Bahati akadakia hapohapo,

    “Yaani maana yake ni kuwa huyu mtoto sio wako,mimi ndiye baba yake na mwenyewe si umeona tulivyofanana sana, kwa hiyo kaka hapa huna chako, nimevumilia na nimeshindwa leo nimeamua kukuambia ukweli tu ili ujue na usiendelee kutoa gharama ambazo si za lazima....”

    Damaso akazidi kuchanganywa,kabla hata hajasema kitu ,simu yake iliita tena. Alikuwa ni mama Vumi akimhimiza Damaso kuwahi hosptalini kwani kuna mambo yanahitajika haraka sana. Damaso akaamua kuwaaga huku akiwaambia atarudi tena muda sio mrefu ili aelezwe vizuri kuhusu mambo hayo kwani hakuwaelewa kabisa walichokuwa wanakiongea. Damaso akachukua bodaboda na kuwahi hospitali.





    Walipofika hospitalini, Damaso akashuka haraka kwenye pikipiki na kuwahi ndani katika Ward ya wajawazito ili akaonane na mama Vumi. Alipotembea kama hatua kumi hivi, dereva wa bodaboda akamwita Damaso na kumkumbusha kuwa alikuwa hajalipa pesa. Damaso akageuka na kurudi kisha akampatia pesa yake.

    Sehemu ambayo walikuwepo ilikuwa ni lango kuu la kuingia katika hospitali ya wilaya Nachingwea, sasa wakati Damaso anageuka ,hakujua kama nyuma kuna gari linakuja. Alipogeuka alikutana na gari la kubeba wagonjwa(ambulance) ambalo lilikuwa linakuja kwa kasi sana,gari hilo lilikuwa limebeba majeruhi wa ajali ,ndio maana hata mwendo wake ulikuwa wa kasi sana. Gari lilimgonga Damaso na likamsukuma hadi akaenda kujibamiza ukutani. Damaso alipoteza fahamu palepale, wakamchukua na kumkimbiza kwa daktari.

    Kwa Daktari alipofika ,akatundikiwa dripu ya maji lakini bado alikuwa hajapata fahamu. Walijaribu kumpapasa mfukoni ili waangalie kama ana simu ili wawatafute ndugu zake,lakini hawakuiona. Simu ya Damaso ilipotea wakati amerushwa na gari ,mtu aliyeiokota angalau alikuwa mstaarabu ,Kwa kuwa hakumjua mwenyewe wala hakuizima hadi alipopigiwa na mama Vumi. Mtu huyo naye alikuwa anaenda hospitali kuwaangalia ndugu zake ambao walikuwa wamelazwa katika hospitali hiyo. Baada ya kupokea simu ya mama Vumi alisema kuwa simu ameiokota. Walipoendelea kuongea zaidi walijua kuwa wote wapo mitaa hiyo hiyo,hivyo baada ya muda walikutana na simu ya Damaso ikabaki mikononi mwa Mama Vumi.

    Mama Vumi hakujua Damaso atakuwa wapi, hivyo akaenda kukaaa nje ya ward ya wajawazito huku akiangaza macho ili aangalie kama atamuona Damaso. Lakini hadi jua linazama hakufanikiwa kumuona. Usiku wa saa nne, Mayasa alifanikiwa kujifungua salama mtoto wa kiume, mtoto huyo alikuwa na asili ya kihindi.Yaani ukimwangalia alikuwa hana tofauti na muhindi yeyote yule, Manesi waliosaidia kufanikisha walijua kuwa baba wa mtoto ni muhindi. Mayasa alimwangalia mtoto wake, alikuwa ni muhindi asilia, hata mama Vumi naye alimuona mtoto, japo ilikuwa ni furaha lakini kwa upande wa pili kulikuwa na hudhuni kubwa. Mayasa hakujua cha kufanya nini, aliendelea kusubiri tu aone kitakachojiri. Baadae mama Vumi akamwambia habari za Damaso kuhusu simu yake na kutomuona hadi dakika hiyo.

    Mpaka inafika asubuhi Damaso bado alikuwa hajapata fahamu. Daktari aliyempokea Damaso baada ya kuona hakuna ndugu aliyejitokeza akaamua kumchukua na kumwamisha hospitali , alimwamisha kutoka Nachingwea hadi mkoa wa Mtwara katika hospitali ya Ndanda. Kwakuwa yeye alikuwa dokta,jambo hilo lilimfanya apokelewe kwa haraka na mgonjwa wake akaanza kupata matibabu mara moja. Daktari huyo alimkabidhi kwa daktari mwenzake ambaye wanafahamiana alafu yeye akarejea kazini kwake kuendelea na kazi zake.

    Jitihada zilifanyika asubuhi hiyo na baada ya muda mchache tu, Damaso alipata fahamu. Alifumbua macho ingawa kusema alikuwa hawezi. Akataka kunyanyuka lakini daktari alimshika na kumwambia atulie kidogo. Damaso akatulia na kuendelea kulala hapo hapo kitandani lakini kumbukumbu za kukumbuka kilichompata bado zilikuwa hazijarejea.



    Kwa upande wa akina Mayasa nao jioni yake waliruhusiwa kurudi nyumbani. Walifikia nyumbani kwa Damaso, ikawalazimu kuwapa taarifa kwao kwani kuna mambo ya mila ambayo yalitakiwa yafanyike. Mpaka giza linazama ,bado Damaso alikuwa hajarudi, hawakuwa na hofu sana kwani waliamini Damaso atarudi muda sio mrefu. Kila aliehodisha chumba cha Mayasa, moyo wa Mayasa ulikuwa unadunda kwa hofu sana ,alikuwa anadhani Damaso ndiye anayekuja.

    Usiku wote walijaribu kubuni njia ipi ni bora ambayo watamweleza Damaso ili aelewe na jambo hilo liishe. Kila njia walioibuni walikuta ina madhara mengi kuliko faida ,mwishowe walichoka na wakaamua kutulia kusubiri kwa yatakayotokea siku za usoni. Baba Vumi naye alipofika , alishangaa sana baada ya kumuona mtoto huyo, ila yeye akaamua kutulia hadi Damaso mwenyewe atakapokuja. Siku iliisha ,Damaso hakutokea. Asubuhi yake ,watu wa kijijini kwao walifika kwa Mayasa kwa lengo la kumuona mtoto. Mama Mayasa ndiye aliyefika na upande wa Damaso, bibi Damaso ndiye aliyefika. Safari ilikuwa ya bahati sana kwani wote kwa pamoja walifika wakati mmoja.

    Walipofika kwa Mayasa,waliingia chumbani huku kila mmoja akiwa na shauku ya kumuona mjukuu wake. Mtoto wa Mayasa alikuwa amelazwa kitandani, mama Mayasa akaenda hadi alipolala mtoto na akamfunua mtoto na kumuangalia. Moyo wake ulifanya paaa! baada ya kuiona sura ya mtoto, akamuuliza Mayasa,

    “Yuko wapi sasa?”

    “Damaso hajarudi tangu juzi....”

    “Sio Damaso, namuulizia mjukuu wangu....”

    “Heee! Mama jamani, si ndio huyo umemnyanyua?”

    “Huyu?”

    “Ndio.....Mama”

    “Mmmh!”

    Mama Mayasa alipigwa na butwaa kwa kuona mtoto ambaye hafanani na wazazi wake wote wala ndugu zake wengine. Bibi Damaso naye akamshika mtoto ili amwangalie, alipomuona tu naye akashtuka,na kuuliza swali ambalo lilimtoka tu bila kupanga,

    “Huyu ni mzungu?"

    Mama Mayasa naye akadakia hapohapo,

    “Yaani hata mimi nilitaka kuuliza hapo, huyu ni mzungu au ?”

    Mayasa akajifanya kucheka, kisha akasema,

    “Sasa jamani kiumbe imekuja jana tu hapa duniani, si lazima awe hivyo mweupe hata kama baadae atakuwa mweusi.....”

    “Mmmh! Aya bana nimepata mjukuu mzungu”

    Mama Mayasa akasema baada majibu ya Mayasa.Baadae bibi Damaso akauliza swali kwa Mayasa huku akimuulizia kuhusu Damaso. Mama Vumi muda wote huo alikuwa pembeni na yupo kimya tu ,akaamua kuwaelezea kinagaubaga kuhusu Damaso. Alipomaliza maelezo hayo, Mama Mayasa akauliza,

    “Kwa maana hiyo baba mkwe wangu Damaso ndio kusema bado hajamuona nwanaye?”

    “Ndio......”

    Mama Vumi akajibu. Wakati huohuo simu ya Mayasa ilianza kuita,alikuwa ni Damaso kwani baada ya kumbukumbuku zake kurejea ,aliweza kukumbuka vizuri jinsi tukio lilivyotokea. Uzuri namba ya Mayasa alikuwa nayo kichwani, hivyo aliazima simu na kumpigia. Mayasa akaipokea simu ingawa namba zilikuwa mpya kwake.

    “Haloo Mayasa, Damaso naongea hapa.....”

    “Heee Damaso uko wapi jamani.....”

    “Nipo salama, vipi mambo yameenda vizuri?”

    “Ndio.....uko wapi?”

    “Usihofu nitakujuza, hebu niambie mtoto amekopi sura ya nani? Yako au Yangu....ila najua atakuwa amekopi sura yangu kwani huyo ni mwanangu...”









    Mayasa alishikwa na kigugumizi kujibu swali hilo. Alitulia kama nusu dakika hivi bila kujibu. Damaso akamuuliza tena swali lilelile, Mayasa akajibu kuwa atamaliza uhondo akimwambia mapema kuhusu sura ya mwanaye, hivyo alimwambia atulie hadi hapo atakaporejea ndipo ataenda kumuona yeye mwenyewe.Damaso naye akatulia kwani aliamini kuwa mtoto ni wake na yupo tu muda wote, baadae Damaso akamwelezea kuhusu yaliyompata na sehemu alipokuwepo. Mayasa alipomaliza kuongea naye ,akawapasha na wenzake kuhusu taarifa za Damaso, kila mmoja alishangaa sana juu ya taarifa hizo. Bibi Damaso akamtafuta mjomba wake Damaso na kumwambia aende alikolazwa ili akamwangalie hali yake.

    Alipofika huko alimkuta hali yake si nzuri sana, na hata daktari alimwandikia rufaa ,hivyo damaso na mjomba wake wakafanya safari ya kutoka Mtwara hadi Dar es salaam kwa ajili ya matibabu zaidi maana alionekana moyo wake ulipatwa na mshtuko baada ya kugongwa hivyo mapigo ya moyo yalibadilika. Walipofika Dar es salaam walienda hadi katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete na matibabu yakaanza mara moja.

    Siku zikasogea huku Damaso akiwa bado hajamuona mtoto wake. Wakati huohuo mtoto alzidi kukua na kuchukua sura ya Sunir. Hata majirani wa Mayasa walianza mingong'ono kuhusu mtoto huyo. Ndugu wa Mayasa walikaa kikao na kuanza kumjadili mtoto huyo. Kila mmoja alitoa mawazo yake lakini wengi walisema kuwa mtoto sio wa Damaso na Damaso akirejea tu basi watampasha juu ya mambo hayo na ikiwezekana basi huo ndio utakuwa mwisho wao. Hata ndugu wa Mayasa mwenyewe nao walikuwa wanawasiwasi juu ya mtoto wa Mayasa ,walijaribu kumbana sana Mayasa ili aeleze ukweli kabla hajarudi Damaso lakini ilishindikana kwani hakuwa teyari teyari kumwambia mtu kitu chochote kuhusu mtoto wake, siri bado ilibaki moyoni kwa Mama Vumi na Mayasa mwenyewe.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku moja mume wa mama Vumi,shemeji wa Mayasa,alimbana sana mke wake ili aseme kuhusu mtoto wa Mayasa. Mama Vumi akaamua kumwambia mume wake kuhusu jinsi mimba alivyoipata hadi anapata mtoto muhindi. Baba Vumi alihamaki sana kwa maamuzi ambayo mama Vumi aliyafanya kwa jambo ambalo lilimkabiri Mayasa.

    “Mmefanya ujinga ambao hauvumiliki hata kidogo, kwanini msingemwambia Damaso au kama Damaso mliona mtaaharibu basi mungeniambia hata mimi kabla hata haya mambo hayajawa makubwa kiasi hiki, sasa na huyu Mayasa ,yaani mpaka anaenda kukutana na huyo Sunir na wewe unamsindikiza kwenye huo ujinga au na wewe ulipata bwana hukohuko.......”

    Baba Vumi alihamaki na wakati huohuo mama Vumi naye akadakia hapohapo kujisalimisha,

    “Mimi sijui jamani, hiyo siku aliyoenda hakuniambia ,mimi nilikuja kujua baada ya yeye kwenda na huko na ilipotokea mimba, ila hayo mengine mimi siyajui”

    “Hamna wewe muongo, unajua kila kitu, mbona haya mengine amekushiriisha kwa nini na hilo usijue?"

    “Heee! Jamani baba Vumi kwa hiyo kukuambia ukweli leo ndio imekuwa kosa?”

    “Kosa lako ni kukaa kimya muda mrefu bila kunishirikisha, yaani zaidi ya mwaka sasa mimi sijui kitu, na inawezekana una siri nyingi sana zinazonihusu hata mimi, yaani kuanzia sasa nitaishi na wewe kwa makini sana....”

    “Mmmmh!”

    “Wewe sema tu mmmh! Leo nampigia simu Damaso namwambia huu ujinga wenu, yule ni ndugu yangu bwana,japo si wa damu....”

    “Jamani baba Vumi usimwambie kwanza....”

    “Nitamwambia yote....”

    Baba Vumi alipomaliza kusema hivyo akatoka nje ya nyumba yake na akachukua simu kisha akampigia simu Damaso, alimuulizia hali, Damaso alisema kuwa yupo mbioni kurudi Lindi kwani hali yake imeshaimarika na sasa yupo vizuri kwa kuendelea na kazi zake. Baada ya hapo baba Vumi akamuuliza swali Damaso ambalo lilimfanya naye ashangae kidogo, Baba Vumi aliuliza,

    “Je unamjua mtu anayeitwa Sunir?”

    “Namjua, vipi....”

    “Unamjuaje?”

    “Ni mpangaji mwenzangu....”

    “Yuko wapi sasa hivi?”

    “Mmmmh kaka unanitisha kweli, mbona maswali mengi sana kulikoni? Ila huyo jamaa aliko sasa sifahamu kwani ni zaidi ya mwaka sasa sijamuona,yeye alishahama pale nyumbani zamani sana...

    .enhee nambie”

    “Aaaah kumbe ndio maana...sasa ukirudi nitakujuza kuhusu huyo mtu”

    “Ok sawa, vipi lakini ulimuona mwanangu?”

    “Yeah nimemuona”

    “Eti nasikia nimetoa kitu cheupe kweli kweli”

    “Eeeh ni kweli kaka”

    Baba Vumi hakutaka kumwambia mapema Damaso kuhusu Mayasa hivyo akaamua kuyakatisha mazungumzo hayo na wakaagana kisha akakata simu. Kuna mpangaji mmoja ambaye alikuwa anakaa katika nyumba wanayokaa akina Mayasa,yeye alikuwa rafiki wa Sunir ,siku ambayo alimuona mtoto wa Mayasa, alibaini ni sura ya Sunir kabisa. Hakuishia hapo, akaamua kushika simu yake na kumpigia Sunir,

    “Baba Sunir.....Vipi kaka”

    “Kama kawa jamaa yangu, Wanasemaje Nachingwea?”

    “Huku heri kabisa na amani tele, ila mapya ndio mengi!”

    “Mmmmh! Ushaanza mambo yako, leo una lipi tena?”

    “Kabla sijaanza na ubuyu wa huku, hebu nikuulize swali kaka....Hivi huyu mke wa Damaso ushampitia nini kaka...”

    “Haahaa ,hamna kaka...."

    "Sema ukweli kaka kama uliwahi,mambo yashaharibika huku”

    “Aaah ! Mara moja tu si unajua tena mzee”

    “Basi kama ni hivyo baba umeacha kopi yako huku.....”

    “kopi gani tena?”

    “Mayasa ana mtoto ,kila kitu amekopi kwako!”

    “Usiniambie baba....”

    “Habari ndiyo hiyo...”

    “Vipi sasa yule jamaa yake amesemaje au imekuwaje hapo?”

    “Hapa Damaso hayupo na hajamuona mtoto wake, nasikia anarudi wiki hii...”

    “Daaah ndio hivyo kumbe...najua jamaa akirudi hawezi kumwelewa Mayasa hata kidogo.Mimi nakuja kumchukua kiumbe changu kwanza dingi ananichosha sana kuhusu mtoto”

    “Daah weee njoo tu, tuyajenge"

    Sunir naye akaahidi kuja kwa ajili ya kumchukua mwanaye wiki hiyohiyo. Na ndiyo wiki ambayo Damaso naye atarejea.



    Baada ya siku mbili, Damaso akapiga simu na kuwaambia kuwa kesho yake atarudi kwani teyari yupo safi. Ndugu zake Damaso hasa bibi na babu yake wakasema kesho yake atawakuta kwake wakimsubiri ili wamuone. Kesho yake ,Damaso na mjomba wake wakapanda gari la kwenda kwao Nachingwea wakitokea Dar es salaam.

    Majira ya saa tisa ,teyari Damaso alikanyaga ardhi ya Nachingwea teyari kwenda kumuona mwanaye kutoka kwa Mayasa. Wakachukua usafiri wa boda boda hadi kwao ambapo walimkuta bibi na babu Damaso pamoja na baba na mama Vumi.

    Wakati huohuo ,Sunir naye alikuwa ameshaingia Nachingwea, naye akapanda bodaboda kuelekea kwa kina Mayasa ili akamuone mtoto wake.







    Damaso alipoingia tu kabla hata ya salamu alitupa macho yake kitandani ambapo alikutana na mtoto muhindi. Alipomuona alidhani kuwa ni mtoto wa jirani tu au kuna mtu alikuja na kumuacha. Akajaribu kuangalia tena pembeni ,hakuona kitu, akawaangalia watu wote ambao wapo ndani ya chumba hicho lakini hakumuona mtoto. Mayasa akajua fika kuwa Damaso anamtafuta mtoto wake ingawa teyari ameshamuona. Baadae Mayasa akamsalimu Damaso na watu wengine wote wakafanya hivyohivyo. Baada ya hapo, Damaso akauliza swali,

    “Mtoto yuko wapi?”

    Watu wote wakatazamana baada ya kusikia swali hilo, bibi Damaso akajibu,

    “Heee wewe Damaso,hujamuona au? Si huyo hapo mzungu wako, mwangalie afu utuambie amefanana na nani kati yetu”

    “Huyu ndiye mwanangu?”

    Damaso akajikuta anauliza swali baada ya kuambiwa kuwa huyo ndiye mwanaye. Damaso akauliza tena kwa Mayasa,

    “Eti Mayasa ni kweli kuwa huyu ndiye mwanangu?”

    Kiunyonge sana ,Mayasa akatingisha kichwa kuashiria kuwa ndiye huyo huyo.

    Damaso ni kama alikuwa anaona maigizo vile,mawazo ambayo yalifika kichwani mwake ni kuwa pengine walimficha mtoto na walikuwa wanataka kufamfanyia surprise . Hakufikiria chochote kama huyo mtoto ndiye wa Mayasa.

    “Aaah ! Jamani eeeh nipeni huyo mtoto, msinifanyie hivyo .....mjue mie nina hamu sana ya kumuona mwanangu jamani"

    Damaso alisema huku akimwangalia Mayasa ambaye sura yake haikuonesha furaha hata kidogo. Baba Vumi naye akatia neno lake,

    “Kaka huyu ndiye mtoto wako unayemwitaji, wala hakuna mwingine,ni huyu huyu”

    Damaso akasogea tena alipo mtoto ,kila alipojaribu kumwangalia ,hakuona tofauti na mwanzo, bado aliendelea kuwa mhindi vilevile. Na alipomwangalia zaidi aliona mtoto kama amefanana na Sunir vile. Damaso bado hakuamini kama huyo ndiye,akauliza tena swali kwa Mayasa ,

    “Hivi huyu mtoto si muhindi kabisa huyu? Mimi ni muhindi au wewe ni muhindi? Imekuwaje sasa uwe na mtoto kama huyu”

    Maswali yaliulizwa harakaharaka kwa Mayasa, Mayasa hakujua aanze na swali gani, aliendelea kukaa kimya, wakati huohuo bibi Damaso akasema huku akimtazama Damaso,

    “Damaso mimi nilishakuambia kuhusu huyu mke ,wewe ukabisha, sasa angalia leo haya mambo aliyokufanyia......Neema ndiye angekufaa wewe sio takataka hii....”

    Mama Vumi baada ya kusikia ndugu yake anaitwa takataka, alichukia sana ,hali ya kuwa anajua hayo yote chanzo ni yeye. Akaamua kurusha neno kwa bibi Damaso,

    “Bibi samahani sana, ndugu yangu sio takataka hata kidogo.....tena nikisikia tena unamwita hivyo humu ndani patachimbika sasa hivi.....”

    Bibi Damaso naye akahamaki,akataka kurusha ngumi kwa mama Vumi,lakini Damaso akaiwahi na kuidaka.

    “Jamani mbona mnanivuruga? Nimetoka hospitali leo kuja kumuona mwanangu alafu mambo mnayonionesha naona mnazidi kunivuruga....”

    Damaso aliongea alafu akachukua maji na kunywa. Bibi Damaso wakati huo alikuwa amekasirika sana ,akasema,

    “Damaso......huu ukoo uliutoa wapi? Umemsikia huyu shemeji yako alivyoniambia? Mimi naondoka siwezi kuendelea kubaki ndani humu, huyu ni mtoto mdogo sana ,hawezi kuniambia mimi maneno kama haya“

    Mjomba wa Damaso alikaa kimya,hakusema kitu chochote kwani mama yake bibi Damaso alikuwa anamjua vizuri sana kwa ukorofi na maneno mabovu. Babu Damaso naye alikaa kimya huku akimwangalia tu mkewe alivyokuwa anacharuka. Damaso alipoona mambo hayaeleweki,akatoka nje ya chumba alafu akazunguka nyuma ya nyumba. Akakaa kwenye gogo ambalo lilikuwepo hapo nje. Wakati amekaa hapo, Sunir naye alikuwa anakuja, Sunir ndiye aliyekuwa wa kwanza kumuona Damaso, akamwambia dereva bodaboda abadirishe njia ili asionane na Damaso kwanza kabla hajaonana na rafiki yake.

    Damaso alikaa kama dakika mbili hivi, akaona bora aende kwa Neema ili akamalizie mazugumzo yake, maana siku ya kwanza hakumwelewa kabisa na Bahati wake. Akaanza kutembea mdogomdogo kuelekea kwa Neema. Alipofika alikuta chumba kimefungwa. Alihodisha bila majibu. Damaso akafikiri pengine Neema atakuwa ameenda dukani, akatulia kidogo.

    Kuna mama jirani na Neema,ambaye siku moja aliwahi kumwambia Damaso kuhusu Neema kuwa analala na kijana mwingine, alimuona Damaso, akaamua kumsogelea Damaso,

    “Mambo Damaso.....”

    “Safi”

    “Vipi mbona sura yako ipo hivyo?”

    “Ipoje?”

    “Haina furaha, imejaa mfadhaiko..”

    “Aaah hamna, kawaida tu”

    “Noana umekuja kumwangalia Neema aliyechukuliwa na kaka yake...”

    “Kaka yake? Kaka yake yupi?”

    “Wewe si ndio uliyesema kuwa yule kijana ni kaka yake? Basi ninavyokuambia hapa mwenzio amehama hapa na hayupo”

    Damaso akashtuka na kuyatumbua macho,akauliza swali,

    “Amehamia wapi?”

    “Mmmmmh! Mimi sijui....”

    Damaso aliendelea kujiuliza na kushangaa kuhama kwake Neema, hapo akaanza kuamini kuwa ni kweli mtoto wa Neema hakuwa wake, kwani asingeweza kuhama bila kumpa taarifa. Kwa bahati nzuri Mama mwenye nyumba naye alifika siku hiyo, alimwita Damaso na kumkabidhi funguo za chumba chake. Alafu akamwambia,

    “Damaso mwanangu, hizi funguo amenipa Neema,ameniambia kuwa ukija hapa nikupe wewe ,yeye alisema kuwa amehama ila hakuniambia anaenda wapi,kwa hiyo funguo zako hizi hapa”

    Damaso akazichukua funguo kisha akaelekea kwenye chumba chake, hata kabla hajafika mbali,mama mwenye nyumba alimwita tena Damaso,Damaso akageuka na kurudi tena alipo huyo mama.

    “Kuna jambo nimekumbuka aliniambia Neema.....Neema alisema kuwa wala usiangaike kumtafuta na amesema hajachukua kitu chako chochote, lakini pia amesema yote aliyokuambia kuhusu mtoto ,ndio ipo hivyo na wala hakuwa kwenye utani”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Damaso damu ikamsisimuka baada ya maneno ya mama mwenye nyumba, akachanganyikiwa sana. Mama mwenye nyumba akampa pole Damaso na Damaso akasonga mbele kwenye chumba chake. Alifungua chumba na kweli alikuta kila kitu ambacho alikinunua.Neema hakuchukua hata kijiko. Damaso alikaa kitandani kama dakika tano alafu akatoka nje na kukifunga chumba. Akaamua kurudi tena kwake ambapo huko alikuta kuna ugomvi unaendelea kati ya bibi Damaso na Mama Vumi.

    “Mchawi na mnafiki mkubwa wewe bibi, bora ufe tu....haya yote umesababisha wewe alafu hapa unajifanya hujui,nyoka mkubwa wewe......”

    Mama Vumi alimwambia bibi Damaso na wakati huo alikuwa anatoka ndani kwenda nje ndipo akakutana na Damaso mlangoni. Maneno aliyosema mama Vumi ,Damaso aliyasikia, hivyo akamtaka mama Vumi kurudia tena maneno yake. Bila kupepesa macho wala kumumunya ulimi, mama Vumi aliyarudia maneno yake tena huku akisisitiza na kusema,

    “Damaso huyu bibi yako ni mtu mbaya sana, ni mchawi na ni muuaji, kama unaona ninamsingizia bibi yako basi tafuta muda utaona nilichokisema ni kweli”

    Bibi Damaso naye akaweka neno lake,

    “Damaso mjukuu wangu, hawa watu wamepanga kitu gani sijui, labda wanataka wakuue, maana huyu anatutukana na huyo mkeo anakuzalia mzungu, yaani maana yake mtoto sio wako....Damaso fanya maamuzi ya haraka”

    Baada ya maneno hayo, Damaso naye akahamaki akaanza kumhoji Mayasa kuhusu mtoto. Mayasa hakujibu kitu zaidi ya kulia tu. Kila alichomhoji, hakujibu.

    “Niambie huyu mtoto umempata wapi, vinginevyo sasa hivi unaondoka kwenu....”

    Kabla hajaongea tena mtu mwingine, mlango wa chumba chao uligongwa,Damaso akaruhusu mtu aingie,Sunir akaingia. Mapigo ya moyo wa Mayasa yakaongezeka mara dufu, yakawa yanadunda kama mapigo ya ngoma. Sunir akasema,

    “Habari za jioni nyote, mimi naitwa Sunir Gandir, mtoto pekee wa kiume wa Mr Gandir, nimekuja kuleta majibu ya maswali mnayojiuliza, kwanza kabisa nianze na swali la Damaso la mwisho ambalo nimelisikia , jibu lake ni kuwa mtoto amemtoa kwangu, na mimi ndiye baba yake.......”







    Damaso akasimama sawa sawa na kumkazia macho Sunir. Maneno ya Sunir yakazua tafrani katika chumba hicho.

    “Unasemaje wewe?”

    Damaso alijikuta likimtoka swali ambalo hakukusudia kuuliza. Sunir akaendelea mbele tena kuongea,

    “Najua watu mnashangaa lakini niwaambie tu wala msishangae sana, haya ni mambo ya kawaida tu ,makosa madogo madogo kwenye ndoa au mahusiano hutokea, halikuwa kusudio langu la kutaka kuharibu mapenzi ya Mayasa na Damaso lakini tamaa za mwili zilinifanya nikutane na Mayasa na hatimaye likatokea hili linaloendelea sasa, mimi nimekuja kumchukua mwanangu alafu hayo mengine mtaendelea wenyewe.”

    Baada ya kumaliza kusema tu, alishtuka ngumi limetua mgongoni kwake kutoka kwa Damaso. Damaso akarusha ngumi lingine kichwani kwa Sunir, Sunir hakurudisha ngumi wala hakukasirika. Baba Vumi akamshika mkono Damaso na kumwambia atulie. Sunir akasema,

    “Mwache anipige kwani ana haki ya kufanya hivyo, lakini hata ukinipiga kutwa nzima bado hakuna utakachobadirisha, mtoto ataendelea kuwa wangu tu, mimi naondoka zangu lakini nitarudi tena kwa ajili ya kumchukua mwanangu, leo nimekuja tu kujionesha ili nijibu swali lililokuwa linawasumbua akilini mwenu kuhusu mtoto aliyezaliwa, samahani sana bro Damaso ,hii imetokea kwa bahati mbaya sana......mpende mke wako kwani nina uhakika anakupenda sana tena sana”

    Baada ya kumaliza kusema hayo Sunir akaondoka zake na kuacha hali ya hewa ikiwa imechafuka chumbani humo. Damaso naye wakati huohuo akamwambia Mayasa naye ambebe mtoto wake kisha atoke chumbani kwake muda huohuo. Baba Vumi akajaribu kumtuliza Damaso ili apunguze hasira lakini ndio ikawa kama amechochea mkaa wa moto, Damaso akazidi kung'aka, hakutaka kabisa kumsikiliza yeyote, akafungua mlango na kumwonesha Mayasa mlango wa kutokea. Mayasa alikuwa anatokwa na machozi, Damaso akasema,

    “Mayasa naomba uondoke humu ndani sasa hivi, yaani nikiendelea kukuona basi bila shaka jera itakuwa sehemu yangu ya kudumu na wewe utabadirisha makazi ya kawaida ya binadamu na kuishi kuzimu, sasa ili kuepusha hilo lisitokee naomba uondoke”

    Mama Vumi akambeba mtoto wa Mayasa alafu akamwambia Mayasa waondoke. Mama Vumi alifanya hivyo kwani kwa wakati huo teyari alishamuona Damaso amechukia sana na hakuwa teyari kumsikiliza mtu yeyote. Mayasa na mama Vumi wakatoka na kuondoka kuelekea nyumbani kwake. Baba Vumi alibaki ndani huku akimtuliza Damaso. Baadae nae akaondoka na kumwacha Damaso na ndugu zake. Bibi Damaso akamsifu sana Damaso kwa kumfukuza Mayasa maana amefanya jambo ambalo limemdharirisha yeye pamoja na ukoo wote. Akamwambia Damaso sasa huo ni wakati wake wa kwenda kumchukua Neema na kuishi naye. Jambo hilo ni kama lilizidisha hasira kwa Damaso, akamwambia kuwa hata huyo Neema naye mtoto ambaye amejifungua ni wa mtu mwingine si wake.Bibi Damaso akajifanya kushangaa jambo hilo, Damaso alijua bibi yake ndiye aliyefanya wakutane na Neema, hakutaka hata kumwambia lolote. Aliamua kuacha tu jambo hilo huku akipanga siku nyingine ataenda kumwambia. Siku hiyohiyo bibi na babu Damaso waliondoka na kwenda kijijini kwao. Hata mjomba wake nae aliondoka na akabaki Damaso peke yake.

    Mayasa alipofika kwa Mama Vumi ,hakuweza kutulia alikuwa analia tu, kilio ambacho hakina sauti. Mama Vumi dada yake ndiye aliyefanya kazi ya kumtuliza lakini haikuwa kazi rahisi.

    Siku mbili zilikatika Mayasa akiwa nyumbani kwa dada yake, Sunir alifanya kila namna hadi akapajua nyumbani kwa dada wa Mayasa. Alifika huko na kukutana na Mayasa , siku hiyo alimkuta Mayasa na mtoto wake pekee. Mayasa akaeleza hisia zake kwa Sunir huku akionesha wazi kuwa anamlaumu sana Sunir kwa kumwingiza kwenye matatizo.

    “Miongoni mwa watu ambao sipendi hata kuwaona ni wewe Sunir, wewe ni mwanaume ambaye umenisababishia matatizo makubwa sana, yaani umeyarudisha nyuma maisha yangu badala ya kusonga mbele, nilikuwa na Damaso na leo sipo naye tena kisa ni wewe, yaani hata sijui kwanini nilikutana na shetani kama wewe.....”

    Mayasa aliongea kwa hisia kali sana mbele ya Sunir, Sunir alijua Mayasa ameumia sana na amechukia sana lakini hakuna litakalobadirika ,teyari kila kitu kilishafanyika na hakuna namna ya kubadiri yaliyopita. Mawazo yakaja harakaharaka kichwani mwa Sunir ,akaona kama Damaso amemuacha basi yeye amchukue Mayasa pamoja na mwanaye ili wakaishi pamoja Dar es salaam. Sunir akamwambia Mayasa jambo hilo, Mayasa hakulijibu kwani bado mawazo yake yalikuwa kwa Damaso na kichwani mwake alikuwa anafikiria juu ya kwenda kuomba msamaha.

    Sunir akaamua kumwambia Mayasa kuwa aendelee kufikiria jambo hilo kwa siku kadhaa alafu ampe jibu,baada ya hapo Sunir akaondoka zake. Siku hiyohiyo jioni Mayasa alimpigia simu Damaso na kumwitaji waonane. Damaso alikataa kabisa, Mayasa akaamua kuomba msamaha kwa njia ya simu hivyohivyo lakini Damaso hakusikia lolote. Mayasa akamtumia baba Vumi kwenda kuomba msamaha kwa Damaso lakini naye aligonga mwamba. Kilichomfanya Damaso akatae Samahani ya Mayasa ni maneno ya ndugu zake pamoja na wapangaji wenzake na jambo ambalo lilitia ugumu moyo wa Damaso ni suala la Mayasa kuwa na mtoto tena mtoto mwenyewe ni muhindi ambaye kila mtu atajua kuwa mtoto huyo sio wake.

    Ndani ya wiki moja kila siku Mayasa alikuwa anamuomba msamaha Damaso lakini haukukubalika. Mayasa alikata tamaa ya kuwa naye tena Damaso, Mayasa akaamua kumwambia Sunir kuwa yupo teyari kuishi na yeye, alimwambia dada yake kuhusu jambo hilo,dada yake alijibu kuwa yeye hana mamlaka na jambo hilo,akamwambia awaambie wazazi wao. Mayasa alitumia simu kuwaambia jambo hilo lakini majibu ya wazazi wao hayakuwa pamoja na Mayasa, walikataa sana juu ya yeye kwenda kwa Sunir. Wazazi wa Mayasa tangu litokee suala la Mayasa kupata mtoto muhindi ni kama walimsusa hivi, wazazi wake waliona wameaibishwa sana kwani jambo hilo lilizagaa kijiji chote.

    Mayasa akaendelea kuishi kwa dada yake kama wiki mbili hivi, maisha yalibadirika sana, alionekana kama mzigo tu kwa dada yake kwani hata ule upendo wa mwanzo uliisha kabisa. Mayasa akalitambua hilo. Sasa akaona huo ndio wakati mwafaka wa yeye kwenda kuishi na Sunir maana ndugu zake wengi walishaanza kumtenga hata dada yake ambaye alikuwa tegemeo lake. Kwakuwa alikuwa na namba za Sunir akaamua kumpigia na kumwambia aende kumchukua. Wakati huo Sunir alikuwa amerudi Dar es salaam, Sunir akaamua kumtumia nauli Mayasa. Mayasa alikata tiketi bila kumshirikisha yeyote.Alifanya hivyo kwa sababu aliona akimwambia dada yake hawatamkubaria kwani teyari walishakataa jambo hilo. Asubuhi na mapema hata kabla watu hawajaamka, Neema akachukua begi lake na kuondoka. Alifika kituo cha mabasi na akakaa kwenye siti yake.







    Mida ya saa kumi na mbili gari likaanza kuondoka. Safari ikaanza mara moja kutoka Nachingwea kuelekea jijini Dar es salaam. Hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kabisa kwenda Dar es salaam. Safari ilikuwa nzuri kwa upande wake kwani mwanaye wala hakumsumbua njiani kulialia. Majira ya saa tisa teyari alishaingia Mbagala kituo cha kwanza kabisa ,alitulia kwani yeye aliambiwa kuwa akashukie kituo cha Temeke Sudan. Abiria wa Mbagala walipomalizika kushuka, gari likasonga mbele hadi wakafika Temeke Sudani. Hapo sasa akampigia simu Sunir na kumwambia yupo Sudani. Baada ya dakika ishirini tu, Sunir alifika na kumpokea Mayasa pamoja na mwanaye.

    Wakatoka hapo na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Sunir. Sunir alikuwa anaishi na wazazi wake maeneo ya Mbezi. Walipofika wa kwanza kupokelewa alikuwa ni mtoto, hakuna aliyemjali Mayasa ,watu wote aliowakuta walimshabikia mtoto tu, Mayasa aliona pengine walikuwa na hamu kubwa ya kumuona mtoto. Akatulia kwenye sofa na kusubiri utaratibu mwingine ambao utaendelea.

    Watu wote aliowakuta ndani walikuwa wahindi isipokuwa yeye tu ndiye aliyekuwa mwafrika, walikuwa wanaongea kihindi tu baadae sana ndipo wakaanza kumsemesha Mayasa kwa lugha ya kiswahili. Wakamsalimu naye akawasalimia. Sunir alikuwa ndani ,alipotoka nje akaamua kumtambulisha Mayasa kwao.

    “Jamani huyu ndiye Mayasa muliyepata kumsikia, ndiye mama wa huyo mtoto, bila shaka wala hofu nyote mmempenda na tutaishi naye hapa......(akageukia upande wa Mayasa na akaanza kuwatambulisha ndugu zake)....Mayasa huyu ndiye mama yangu, hawa ni dada zangu na huyu ni bibi yangu na baba ndiye huyu”

    Mayasa alikuwa anatingisha kichwa tu kuashiria anaelewa yale anayoambiwa na Sunir. Mayasa kila alipojaribu kuangalia sura za watu aliowakuta aliona ni sura ambazo zilikuwa kama hazikubaliani na maelezo ya Sunir. Hakufikiria kuuliza kwani alijua pengine ndivyo walivyo. Usiku ulipofika ,Mayasa alipewa chakula vizuri tu na baadae akaoneshwa chumba cha kulala.

    Watu wote wakaenda kulala ,Sunir chumba chake na Mayasa chumba chake.

    Siku zilikatika na kutimia kama wiki hivi tangu Mayasa ayaanze maisha mapya nyumbani kwa Sunir. Mambo yalianza kubadirika kwa upande wa Mayasa. Mama yake Sunir alimwambia Mayasa,

    “Kuanzia leo kazi yako kila ukiamka asubuhi ni kufanya usafi nyumba mzima, ndani na nje, alafu chakula kitapikwa na wewe kila siku labda itokee tu nimejisikia mwenyewe kupika au mwingine wa nyumba hii, kwa hiyo unatakiwa uelewe kuwa kazi zote zinazohusu nyumba hii zitakuwa zinafanywa na wewe”

    Mayasa akaitikia na kulikubali hilo, lakini moyoni alishaanza kuona tabu imeanza kuingia. Kila siku ndio ilikuwa kazi yake hiyo na ikifika jioni alikuwa anachoka sana. Sunir alikuwa hajui kitu kuhusu Mayasa kama anafanyishwa kazi kutwa nzima kwani yeye kila siku hutoka asubuhi na baba yake kwenda kariokoo kwenye duka lao vifaa vya umeme. Hivyo hakujua chochote kilichokuwa kinaendelea kwa Mayasa. Mayasa alikosa amani kabisa, hakuwa na furaha kwenye nyumba ya akina Sunir. Mbaya zaidi tangu aende Dar es salaam hakuwahi kutoka nje ya geti la nyumba hiyo. Kwa hiyo hakuwa anaijua sehemu nyingine yeyote zaidi ya hapohapo.

    Siku moja Sunir aliamua kumchukua Mayasa na mwanaye kisha wakatoka nje ya nyumba yao. Walienda kutembea ufukweni mwa bahari ya hindi. Siku hiyo Mayasa alipata wasaa wa kuzungumza na Sunir. Alimweleza kila lililokuwa linamsumbua akilini mwake. Alianza kumuuliza swali,

    “Sunir kuna jambo linanichanganya sana, tangu nimefika pale kwenu nimegundua kuwa maisha yenu ni mazuri sana yaani pesa zipo , sasa kinachonishangaza ni kwanini kule Nachingwea ulipanga nyumba alafu maisha yako yalikuwa ya kawaida sana?”

    Sunir akatabasamu kisha akajibu kuwa yeye huwa anapenda sana kuishi na jamii ya watu wa kawaida, ingawa ilikuwa ngumu sana kuruhusiwa ila alilazimisha hadi akatoka kwake na kwenda kupanga, baadae kwa utani Sunir akasema,

    “labda nilienda kupanga pale ili nikutane na wewe.....”

    Mayasa akatabasamu alafu akamuuliza tena Sunir,

    “Sunir....Hivi ulivyosema kuwa tuje kuishi pamoja kwako ndio kama vile tunavyoishi au kuna siku tutaishi pamoja yaani mume na mke?”

    Sunir akajishika kidevu chake,kisha akajibu kuwa mpango wake ni kuishi na yeye kama mke. Sunir akasema,

    “Matatizo yako yote yanayokupata pengine yamesababiswa na mimi mara baada ya kukutana na wewe, Mayasa nataka nikuambie kuwa nitaishi na wewe ,siwezi kukutupa hata kidogo,nakuhakikishia nitairejesha furaha yako”

    Mayasa akatumia nafasi hiyo kumweleza juu ya manyanyaso anayoyapata kutoka kwa ndugu zake hadi anafikia hatua ya kukosa amani na kuanza kufikiria kurudi kwake. Sunir akashangaa sana, alikuwa hayajui hayo yote kama alikuwa anafanyiwa Mayasa. Sunir akamwambia kuwa atafanya kila namna wakae pamoja. Waliongea mambo mengi sana hadi ilipofika jioni na kuamua kurudi nyumbani.

    Walimkuta mama Sunir amechukia sana ,aliwauliza walikuwa wapi na kwanini wamechelewa. Sunir akamjibu mama yake kuwa walikuwa kwenye matembezi ya kawaida tu. Mama Sunir akamwambia Sunir kuwa wakati wanaenda kulala itabidi abaki ili waongee naye.

    Muda ulipofika Sunir akawekwa kikaangoni, ndugu zake wote walikuwepo isipokuwa Mayasa tu ambaye aliamliwa aende chumbani ili asisikie kitakachozungumzwa. Sunir aliulizwa na mama yake kuwa ana mpango gani na Mayasa. Sunir alijibu kuwa lengo lake ni kukaa naye kama mke wake baada ya taratibu zote kutimia. Ndugu zake wote walisikitika sana,mama Sunir akasema,

    “Wewe mtoto usituletee balaa hapa, huyu mwanamke mchafu mchafu awe mkeo? Mjinga sana wewe , wanawake wa maana wamejaa kila kona, pale kwa mzee Gulam wapo, Kule kwa Patel wapo na huyu jirani yetu Sanjay naye ana watoto,huyu mwanamke amekupa nini au ndio ushapewa mambo ya kiswahili teyari.....nakupa wiki moja mrudishe kwao huyu mwanamke kama mtoto nitamlea mwenyewe”

    Wote wakamuunga mkono mama Sunir, Sunir akasema,

    “Ni vipofu pekee ndio watakaochaguliwa vitu, iwe mke au kitu chochote, mimi Sunir Mungu amenibariki na akanipa macho mawili yanayoona karibu na mbali, nitachagua pale macho yangu yatakapoona, nimemuona Mayasa sio hizo takataka zingine mnazozisema, alafu nimesikia huwa mnamtesa sana yaani mnafanyisha kazi kama vile mfanyakazi wenu, sio jambo zuri mwogopeni Mungu wenu!”

    Mama sunir akajua hayo yote yanatokea kwa sababu ya Mayasa hivyo akajisemea moyoni kuwa atafanya kila namna ili Mayasa aondoke katika nyumba hiyo. Sunir akaamua kutoka na kwenda chumbani kwake baada ya kuona kikao chenyewe kilikuwa cha kutaka kumfanya amtenge Mayasa.

    Asubuhi yake ilipofika ,kama kawaida Sunir na baba yake wakatoka na kwenda kazini kwao kwa kila siku. Mama Sunir sasa akaanza kazi yake rasmi ya kuhakikisha Mayasa anatoka katika nyumba hiyo. Mama Sunir akamwita Mayasa, Mayasa akatoka nje na kumsalimia mama Sunir, mama Sunir hakuitikia badala yake, akamuonesha rundo la nguo nyingi sana alafu akamwambia azifue na akimaliza aingie jikoni kutayarisha chai. Wakati huo huo dada zake Sunir nao walitoka na nguo zao nyingi wakaongeza ,zikawa nyingi zaidi.

    Mayasa akataka kusema neno lakini alizuiwa na mama Sunir. Akaamua kukusanya nguo na kwenda kuzifua. Mtoto wake akaanza kulia,akaacha kufua ili akamchukue ila mama Sunir akamkataza na kumwambia hana mtoto,yeye ndio akaenda kumchukua na kumbembeleza.Mayasa akaendelea kufua hadi alipomaliza na kuingia jikoni kutayarisha chai.





    Mayasa alipomaliza kupika chai akajua kazi amemaliza, akaingia chumbani na kujilaza maana alikuwa amechoka sana. Alilala kama dakika tano hivi, ghafla akaona mlango wa chumba chake unafunguliwa. Alikuwa ni mama Sunir,

    “Yaani wewe kinyago unajilaza hapa sasa hivi ili iweje? Unataka kazi akufanyie nani? Haya amka twende huku ukanitengenezee juice....”

    Mama Sunir alimwambia Mayasa na akamshika mkono na kumvuta harakaharaka. Mayasa alijaribu kujitetea lakini ndio ikawa kama ameongeza moto , sasa hayakuwa maneno tena ,akaanza kupigwa. Mayasa alitoa machozi, lakini machozi yake yalikuwa sawa na machozi ya samaki, hakuna aliyejari kulia kwake badala yake ndio waliongeza kipondo na maneno yenye kukashfu na kuudhi. Maskini Mayasa! hakuwa na mkombozi wala msaidizi, alijilaumu sana kwa maamuzi yake ya haraka ya kutoka kwake na kuja nyumbani kwa Sunir. Siku zote majuto ni mjukuu! Ningejua huja baada ya safari. Machozi yakiwa yanamlenga, akaanza kufanya kazi aliyoelekezwa, akaifanya hadi akamaliza. Alipomaliza akaoneshwa kazi nyingine nayo akaifanya hadi akamaliza.

    Jioni ilipofika ,Sunir aliporejea alimkuta Mayasa akiwa amechoka sana na hata furaha hakuwa nayo. Sunir alimuuliza Mayasa kulikoni, lakini Mayasa hakusema kwani mama Sunir alimwambia kuwa kama akimwambia Sunir yale anayofanyiwa basi hakika huo ndio utakuwa mwisho wa maisha yake. Mama Sunir aliwahi kumwonesha Mayasa bastola ya mume wake, hicho ndicho kilimfanya Mayasa aogope zaidi, hivyo alivyoulizwa na Sunir hakusema lolote alilofanyiwa zaidi ya kusema kuwa yupo vizuri na hamna lolote.



    Mwezi mmoja ulipita Mayasa akiwa anaishi katika mateso. Sunir kila alipojaribu kutaka kuama kwake, wazazi wake walikataa na huku wakimwambia kuwa kama anataka kufanya hivyo basi atakuwa amejitoa mojakwamoja kwao na asitegemee kupata msaada wowote. Sunir alipata kigugumizi kufanya maamuzi juu ya jambo hilo. Mayasa alijaribu kumshawishi sana Sunir kutoka hapo na wakaishi sehemu nyingine lakini jitihada zake ziligonga mwamba. Mayasa alibaini kuwa tatizo kubwa ni ndugu zake Sunir, na hata kama watakaa pamoja basi mambo yatakuwa yaleyale ya uonevu upande wake. Alianza kufikiria namna ya kujitoa kwenye mikono ya watu hao kwa jitihada zake mwenyewe. Wakati Mayasa akiwaza hilo na ndugu wa Sunir nao walikuwa wanawaza yao. Mama Sunir alimtesa sana ndani ya mwezi lakini hakuona dalili za Mayasa kutoka hapo. Mama Sunir siku moja alinunua sumu. Alikusudia kumtilia kwenye chakula ili afe tu maana hakutaka kabisa kumuona Mayasa anakuwa mmoja wa familia yake kama Sunir anavyotaka.

    Siku hiyo mama Sunir alitengeneza juice mwenyewe, hata Mayasa naye alishangaa sana, haikuwa kawaida yake kufanya jambo kama hilo. Hata mezani yeye ndiye aliyeandaa na hata wakati wa chakula alimfurahia sana Mayasa. Siku zote kicheko cha mnafiki huwa hakikawii kwisha, ila tabasamu la mwenye haki hudumu milele. Kicheko cha mama Sunir na tabasamu lake alilolionesha siku hiyo lilimtia shaka Mayasa, Mayasa akaanza kuwa naye makini katika kila hatua atakayoifanya siku hiyo. Yeye ndiye aliyeenda kutia juice kwenye bilauri zote. Kwenye bilauri ya Mayasa ndio akatia sumu. Bilauri hiyo akaitenga pembeni, alafu akachukua bilauri zingine zote na kuzipeleka mezani,akagawa bilauri kwa kila mtu, Mayasa ndiye akakosa, mama Sunir akajifanya kumtuma dada yake Sunir ili akachukue . Mama Sunir aliyafanya haya yote ili tu kuonesha kuwa ana upendo wa dhati kwa Mayasa ili Sunir aone kuwa kama anaambiwa kuwa anaonewa basi ni uongo. Dada yake Sunir akaenda hadi jikoni ambako ndiko kulikokuwa na bilauri. Aliikuta bilauri imejaa juice kushinda hata yake. Yeye naye akaanza kuingiwa na wivu, siku zote roho mbaya haijengi, akaona njia pekee ya kumkomoa Mayasa basi anywe juice yote. Hakujua kama mama yake ametia sumu, alikunywa juice yote alafu akaosha bilauri kisha akatia juice nyingine kidogo sana alafu akaongeza maji mengi sana ikajaa hadi juu.

    Akachukua juice na kumkabidhi Mayasa. Mama Sunir moyo wake ulichanua kwa furaha sana,alijua sasa kazi imeisha. Kidudumtu aliyekuwa anamsumbua, habari yake inaenda kufika mwisho. Mayasa aliangalia juice aliyopewa ilikuwa nyepesi sana tofauti na za wenzake , alipata hofu kuinywa lakini baadae akasema liwalo na liwe kila kitu kimeshapangwa na Mungu, binadamu ni kama bendera tu,akanyanyua bilauri na kuinywa juice. Mama Sunir akatabasamu sana, akajua kazi imeisha. Akasubiri kama dakika tano hivi ili aone kitatokea nini.

    Alishangaa kumuona mwanaye anaanza kulalamika tumbo linamuuma. Mayasa alikuwa yupo vizuri tu wala hakuonesha dalili za kuumwa tumbo wala kuumwa chochote. Mtoto huyo alizidi kulalamika sana kuwa tumbo linamuuma sana. Mama Sunir akamuuliza kama kuna kitu amekula,

    “Wewe mwanangu umekula nini?”

    Kwa tabu sana, dada yake Sunir akajibu,

    “Na...hisi ni juice, nimekunywa nyi...ngi sana”

    “Umekunywa ile juice niliyokutuma ya Mayasa?”

    “Ndi...o nime....kunywa....yote...nikamtilia maji ndio nikampa”

    Mama Sunir akashtuka sana baada ya kauli ya mwanaye, akajua kuwa teyari ameshakunywa sumu.

    “Aaah! Mwanangu umekunywa sumu jamani.....”

    Mama Sunir alijikuta akisema kwa sauti kubwa ambayo ilipelekea hadi Mayasa kuisikia na watu wote wakasikia. Wakachukua maziwa na kunywesha na wakati huohuo teyari Sunir alikuwa ameshatoa gari nje teyari kwa kumpeleka hospitali. Nyumba yote akabaki Mayasa na bibi wa Sunir tu ,wengine wote wakaenda hospitali.

    Mayasa alifikiria sana kuhusu tukio hilo, akaona hanabudi kupotea machoni pa mama Sunir maana alibaini kuwa yeye ni kikwazo kikubwa sana katika familia hiyo. Mfupa ukilazimisha kwenye chungu unaweza ukapasua na chungu chenyewe. Mayasa akaona atumie muda huohuo kutoroka hata kabla hawajarudi hospitali. Mayasa akaenda chumbani kwake na akamlaza mtoto alafu akamwambia,

    “Mwanangu mimi mama yako nakuacha hapa , ninaondoka na kwenda kusikojulikana, najua bado unanihitaji sana mama yako lakini sina namna ya kufanya , ipo siku yeyote tutakutana, baki salama mwanangu!”

    Katika chumba cha Mayasa kulikuwa na madaftari mengi , hivyo akaamua kuchukua moja na kuchana karatasi kisha akaandika ujumbe alafu akaenda kuupenyeza chini ya mlango wa Sunir. Baada ya kufanya hayo yote, Mayasa akatoka nje na wakati huo ilikuwa teyari usiku na giza limeshaanza kuingia. Mayasa akaanza kutembea huku akiwa hajui anakoenda.







    Alitembea kuelekea mbele kwa mbele huku akifuata barabara ya lami ambayo ilikuwepo pembezoni mwa nyumba ya kina Sunir. Alitembea sana huku asijue mwisho wa safari yake upoje. Njiani alipishana na gari la kina Sunir, yeye alilijua lakini waliomo garini hawakumuona. Alitembea hadi akafika sehemu akakuta kuna kituo cha daladala. Akaenda hadi katika kibanda cha abiria ,akatafuta sehemu akaketi.





    Sunir na ndugu zake wengine walirejea kwao ,Mayasa hawakumkuta ,walimtafuta kila mahari katika nyumba hiyo lakini hawakumuona. Ila mtoto walimkuta akiwa amelazwa katika kitanda ambacho huwa kinalaliwa na Mayasa. Nguo karibu zote walizikuta. Bibi alipoulizwa kuhusu Mayasa hakuwa na jibu kwani hakumuona wakati anatoka. Sunir akaingia chumbani kwake, alipoingia alikutana na karatasi iliyokunjwa ,akaiokota na kuifunua. Akakuta imeandikwa, akaanza kuisoma, karatasi ilikuwa imeandikwa hivi,

    “Sunir...nimeamua kuondoka kwenu ili nisiharibu amani ya ndugu zako, sijui niendako na wala sijui nitakumbana na nini usiku huu, ila bora shari nitakayokutana nayo usiku huu kuliko shari nitakayokutana nayo kutoka kwa ndugu zako. Mimi sikuja kwako eti kwa sababu nilikupenda,la hasha! Nilikuja kwako baada ya kuona Damaso ameniacha, nilitarajia kuipata furaha pengine nikiwa na wewe lakini nimeongeza uchungu ndani ya nafsi yangu,mateso niliyoyapata hapo yanatosha sasa! Hata kama tungekaa pamoja ,amani na furaha kwetu ingekuwa ndoto tu kwani vikwazo ni vingi sana. Nimegundua kuwa sina thamani yeyote mbele ya ndugu zako,ngoja niondoke niende kokote pengine kuna watu watatambua thamani yangu. Sijui Mungu amenipangia nini kwenye haya maisha lakini najua kuna jambo anataka nijifunze kutokana na changamoto hizi. Nilitamani kuondoka na mwanangu lakini najua ningempa shida tu kwani hata niendako sikujui. Mtunze mwanangu najua ipo siku tutaonana tena, mimi Mayasa!”

    Sunir alimaliza kusoma maandishi hayo na machozi yakaanza kumtoka, mwanzo alijizuia lakini kadri alivyokuwa anakumbuka maneno ya Mayasa, machozi yalizidi kumtoka. Sasa haikuwa machozi tu bali na sauti ya kilio cha chinichini kilichoambatana na uchungu kilianza kusikika. Hata baba yake Sunir alisikia na akaenda chumbani kwa Sunir. Alimkuta ameshika karatasi, akaichukua naye akaisoma. Alipomaliza kusoma akamshangaa sana Sunir ni kitu gani kilichomfanya alie. Sunir hakuongea neno lolote mbele ya baba yake. Baba yake akatoka nje na ile karatasi kisha akamuonesha na mama Sunir. Mama Sunir alipomaliza kusoma, akatabasamu sana, akajua mpango wake umetimia. Na uzuri mtoto wake aliyekunywa juice yenye sumu alikuwa anaendelea vizuri sana maana walimwaisha hospitali mapema hivyo madaktari waliiondoa sumu yote kwa haraka sana. Sunir aliumia sana lakini baadae akaona atulie tu kwani basi hilo ndio teyari limeshatokea. Alitamani atoke usiku huo huo akamtafute Mayasa lakini hakujua wapi aanzie, akaamua kumwomba Mungu tu amlinde na mabaya yote usiku huo na huko anakoelekea asipatwe na tatizo lolote.



    Mayasa alikaa kwenye kituo cha daladala kwa muda wa kama lisaa limoja hivi huku asijue wapi aende. Mayasa alijiuliza arudi kwa Sunir au asonge mbele. Moyo wake hukutaka tena kurudi nyuma hasa alipokumbuka mama sunir alipokusudia kumuua kwa kitumia sumu . Mayasa alikumbuka siku ambayo alifika Dar es salaam alishuka kwenye kituo cha Sudani kilichopo Temeke. Akili ya Mayasa ikamwelekeza kufanya utaratibu wa kufika huko kwani huko ndiko iliko njia ya kurudi nyumbani kwake Lindi. Hakuwa na hata hela yeyote ambayo ingeweza kumfikisha Temeke. Akaamua kwenda kwa jirani yake ambaye naye alikuwa anasubiri daladala. Aliyemwendea hakuwa na hiyana aliingia mfukoni na kutoa noti ya shilingi elfu moja kisha akampatia Mayasa. Mayasa akashukuru sana, gari la Temeke lilipofika akapanda na kuianza safari ya Temeke. Alikaa kwenye siti ya nyuma kabisa,baada ya konda kuchukua nauli,Mayasa aliwaza na kuwazua hadi akapitiwa na usingizi hapohapo. Gari lilifika Temeke ,abiria walishuka. Mayasa alikuwa bado amelala ,hakujua kama teyari ameshafika na kwakuwa alikuwa amekaa nyuma kabisa ,hakuna ambaye alimuona. Konda wa gari hilo akajua watu wote wameshuka ,akafunga mlango wa gari na kumruhusu dereva wake waondoke. Hawakutaka kupakia abiria tena kwani teyari ilikuwa usiku sana hivyo wakaamua kwenda kuliegesha gari ili wajiandae kwa ajili ya siku inayofuata.

    Baada ya kuliegesha sehemu na kuhesabu mapato yao, konda wa gari akaanza kufanya usafi ndani ya gari. Alipofika siti ya mwisho alishangaa kumkuta mtu, haraka sana akamwita dereva wake kuja kumuona. Mayasa alikuwa bado amelala. Dereva akasema kuwa itakuwa amejisahau kutokana na usingizi ambao alikuwa nao. Wakamwamsha, Mayasa akaamka kwa kushtuka sana, baada ya kutazama mbele, macho yake yalikutana na wanaume wawili.Wakamtuliza na kumwambia kuwa wao ni dereva na konda. Hapo ndipo akili zikarejea kuwa alipanda gari. Akawauliza kuwa ni wapi hapo, wakamjibu kuwa ni Temeke. Alipoulizwa yeye kuwa alitakiwa ashuke wapi,Mayasa hakuwa na jibu lolote. Mayasa akaamua kuwaomba kama inawezekana basi wamwache alale ndani ya gari alafu asubuhi atatoka maana usiku huo alikuwa hajui ataenda wapi. Konda akamuuliza Mayasa nyumbani kwake ni wapi , pia Mayasa hakuwa na jibu zaidi ya kuendelea kuwaomba tu wamkubalie alale ndani ya gari maana hakuwa na pa kwenda usiku huo.

    Konda akamwita pembeni dereva wake na kumwambia wamsaidie sehemu ya kulala kwa usiku huo alafu asubuhi ikifika atajua mwenyewe pa kwenda maana alionekana mtu mwenye matatizo sana. Wakamwambia Mayasa kuwa kulala kwenye gari ni hatari sana maana sehemu yenyewe ilikuwa na mbu wakubwa wanaofanana na inzi kwa unene hivyo wangeweza kumsababishia malaria. Wakamwambia wataenda kumtafutia hifadhi kwa usiku huo na asubuhi ataenda na safari zake. Wakatoka hapo wakaenda hadi nyumbani kwa Konda, konda alipanga chumba kimoja. Konda akamwonesha chumba Mayasa alafu yeye akaenda kulala nyumba ya wageni(gest).

    Hata dereva naye alimshangaa konda siku hiyo maana tabia ya konda huyo ilikuwa ya kiuni sana, hakufikiria kama angemwacha salama Mayasa usiku huo,alijua atamwambia walale wote kitanda kimoja. Mayasa akaingia chumbani na kulala. Konda huyo wakati yupo gest akafikiria mtu mwenyewe hamjui ndio kwanza wameonana siku hiyohiyo alafu amemwachia chumba chake na vitu vyake vyote.

    “Aisee leo nimefanya ujinga sana, vipi akitoroka na mali zangu itakuwaje? Nitamuona wapi? Na hata polisi nitaripoti kwa njia gani? Si kila mmoja atanishangaa sana na kuniona mimi ni mjinga sana? Ngoja nirudi haraka nyumbani nikamwambie tulale wote kama hataki basi atajua pa kwenda usiku huuhuu"

    Konda aliwaza kisha akaondoka na kurudi haraka nyumba aliyopanga. Alikuta chumba kimefungwa kwa ndani na alipochungulia alimwona Mayasa akiwa amelala. Akahodisha mara kadhaa lakini Mayasa alikuwa bado amelala tu. Akarudia tena kumwamsha na hapo sasa akaamka. Akafungua mlango baada ya kusikia sauti ya konda. Konda akaingia chumbani na kuwasha taa kisha akakaa kwenye sofa ambayo ilikuwepo ndani humo.







    Konda alimwangalia Mayasa alimuona ana dalili za usingizi na uchovu sana. Akabaini kuwa Mayasa hakuwa na lengo lolote baya kwake, kwani teyari alishaanza kulala na kama angekuwa ana lengo lolote baya basi wala asingelala mapema kiasi hicho. Konda akaamua kumuongopea Mayasa ,

    “Dada samahani kwa kukuamsha ,najua teyari ulishaanza kulala na usingizi ulishakupata, nilitaka nikalale gest ila kwa bahati mbaya sana nimekuta vyumba vimejaa, sasa mimi nitalala hapa kwenye sofa na wewe endelea kulala hapo hapo kwenye kitanda”

    Mayasa hakutaka kumhoji sana konda, akaamua kumwitikia tu kwa kichwa alafu akapanda kitandani huku akiwa na nguo zake zote mwilini mwake, hakuvua nguo hata moja. Ingawa Mayasa alikubali kulala moyoni alikuwa anawaza sana juu ya konda kama angeweza kumwambia au kumfanya kitu chochote kibaya.

    Upande wa konda yeye hakuwaza chochote juu ya Mayasa na hii ilichangiwa na jinsi Mayasa alivyokuwa anaonekana na jinsi alivyokuwa anajibu. Kila mmoja alipitiwa na usingizi. Konda alishtuka saa kumi na moja alfajiri baada ya alamu aliyotega kupiga na kumwamsha. Akajiandaa kwa ajiri ya kwenda kuanza harakati zake za kusaka tonge. Alipomaliza akataka kumwamsha Mayasa ,lakini alimwonea huruma maana bado alikuwa yupo usingizini. Akajiuliza sana jinsi ya kufanya lakini mwishowe akapata ufumbuzi. Akachukua karatasi na kuandika ujumbe kisha akauacha kitandani pembeni na alipolala Mayasa. Alafu akaondoka.

    Mayasa alipoamka jua teyari lilikuwa limeanza kuchomoza. Hakumkuta mwenyeji wake , alipoangalia pembeni yake akaona kuna karatasi imeandikwa ,akaichukua na kuanza kuisoma,

    “Dada nimeshindwa kukuamsha kwani nilikuona bado umelala, mimi nimetoka ,nipo kwenye kazi yangu, tafadhali nakuomba funga mlango utakapotoka alafu funguo weka chini ya kapeti ambalo lipo nje ya mlango, hapo kwenye sofa nimekuwekea 5000 ,ichukue itakusaidia kwa nauli na kifungua kinywa”

    Mayasa alipomaliza kusoma,akaangalia kwenye sofa na kweli aliiona noti ya shilingi elfu tano. Alimuona mtu huyo ni mwenye moyo wa pekee sana kwani amemuamini sana hadi amefikia hatua ya kumwambia afunge mlango akiwa peke yake bila kujua kama atachukua kitu chochote ndani mwake. Akafungua mlango na kuitafuta bafu iliko, akaoga maji na kurudi chumbani akajiandaa teyari kwa kuondoka. Alifanya kama alivyoambiwa kisha akatoka nje na kushika barabara ya lami. Alitembea hadi akafika maeneo ya Temeke hospitali. Akaanza kuulizia kituo cha Sudan kipo wapi ili apate gari la kwenda Nachingwea. Akaoneshwa , kabla hata hajafika huko ,alikumbuka kuwa alikuwa na picha ndogo ya mwanaye ameisahau nyumbani kwa konda, kwakuwa hapakuwa mbali sana na hapo akaamua kurudi ili akaichukue picha hiyo maana huo ndio ukumbusho wake pekee uliobaki mara baada ya kumwacha mwanaye kwa akina Sunir.

    Alipofika alikuta mlango upo wazi. Akahodisha na akamuona konda. Konda akamkaribisha ndani. Wakasalimiana, lakini mkononi konda alikuwa ameshika picha ambayo ndiyo alikuwa anaifuata. Mayasa akamwambia konda kuwa alikuwa anaifuata picha hiyo. Konda akamkabidhi picha Mayasa. Mayasa akaaga na kuanza kuondoka. Konda alitafakari sana, akaamua kumuita Mayasa hata kabla hajafika mbali. Mayasa akarudi.

    “Dada samahani sana, unajua hii ni kama bahati, gari letu limeharibika na lipo kwa fundi, sasa sikutegemea kama nitakuona tena muda huu,nilijua utakuwa umeshaondoka teyari, hivi huyo wa kwenye picha ni nani? Na ukitoka hapa unaelekea wapi?”

    “Huyu ni mwanagu na ninaelekea nyumbani sasa.....”

    “Samahani, hivi unaishi wapi?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mayasa alisita kutoa jibu haraka, baadae akasema,

    “Lindi”

    “Lindi? Lindi hii ya mkoa au?”

    “Ndio”

    “Kwa hiyo sasa hivi unaenda lindi?”

    “Ndio”

    “Aaah unajua unanichanganya, yaani sijaelewa kitu, vipi ile jana ulikuwa unatokea wapi?”

    “Mbezi”

    “Yaani bado, sijaelewa ,kuna kitu kinakosekana kwenye maelezo yako, hebu naomba unifafanulie kuhusu wewe kama hutojali....”

    “Hata hamna kitu kingine zaidi ya nilichokueleza, sasa hivi nikitoka hapa naenda nyumbani Lindi....”

    “Mmmmh! Samahani dada japo sijakaa sana darasani kusomea masuala ya saikolojia lakini sura yako nikiiangalia naona kuna kitu ndani yake ambacho kinakusumbua, ila kama hakuna basi haina shida safari njema....”

    “Aya asante kwa heri.....”

    Mayasa akaanza kuondoka , Konda akamwita tena alafu akamwambia,

    “Japo sikufahamu na wala sijui chochote kuhusu wewe,nahisi moyo wangu hautaridhika ikiwa kama hautajua una tatizo gani, tafadhali hebu niambie japo kwa uchache sana kuhusu wewe....”

    Mayasa akaona bora amwambie tu kwanini yupo hapo na ilikuwaje hadi akafika Dar es salaam. Alimweleza kila kitu ingawa sio vyote ila konda alielewa. Konda akasikitika sana na akamwambia Mayasa kuwa asubiri siku hiyo afanye kazi alafu jioni atakavyorudi atampa nauli ya kufika kwake Lindi. Mayasa akakubali kubaki ili apate nauli ya kufika kwake.

    Hapo sasa undugu wao ukaanza,wakajitambulisha majina yao kila mmoja kwa mwenzake. Konda alimwonesha Mayasa sehemu ya kununua chakula maana yeye alikuwa hapiki, Baadae konda akamuaga Mayasa na kwenda kuangalia gari lao kama limetengenezwa ili waendelee na kazi. Mayasa akabaki chumbani peke yake, hakuwa na kazi nyingine ya kufanya zaidi ya kuangalia runinga na kulala tu. Muda wa kula alienda sehemu ambayo alioneshwa na akanunua chakula kisha akaenda kula chumbani kwa konda. Baada ya kula, kama kawaida aliendelea kuangalia runinga hadi akapitiwa na usingizi.

    Mayasa aliamka majira ya usiku kama saa moja hivi , akaenda tena kununua chakula na kukila.Akatulia tena kitandani kuangalia runinga hadi Konda aliporejea majira ya saa nne usiku ikielekea saa tano.

    “Vipi umeboreka sana?”

    Konda aliuliza baada ya kuingia ndani tu na kumkuta Mayasa akiwa anaangalia TV.

    “Hapana sio sana....”

    Mayasa alijibu alafu akampa pole Konda maana alionekana amechoka sana. Konda alishukuru kwa kusema asante. Mayasa akasubiri aone kama atapewa nauli ya kurudi kwake. Konda alienda kuoga, aliporudi akamwambia Mayasa kuwa kwa siku hiyo biashara haikwenda vizuri sana kwani hata mapato waliyopata yaliishia kuwa hesabu ya bosi wao(mmiliki wa gari lao) , kwahiyo akamuomba Mayasa aendelee kuvumilia hadi siku inayofuata ndipo atapata nauli kama mambo yakienda vizuri yaani biashara ikiwa nzuri. Mayasa alikubaliana na Konda, kama kawaida muda wa kulala ulipofika Mayasa alilala kwenye kitanda na Konda alilala kwenye sofa.

    Asubuhi na mapema kama kawaida Konda aliamka na kwenda kwenye kazi yake. Mezani aliacha shilingi elfu tano ambayo ni kwa ajili ya Mayasa imsadidie kwa chakula kwa siku hiyo. Kama kawaida Mayasa alishinda ndani tu kutwa nzima hadi aliporudi Konda jioni, lakini siku hiyo Konda aliwahi kurudi sana. Alirudi saa moja jioni, Mayasa alijua kuwa Konda amerudi mapema ili awahi kumpatia nauli yake na yeye apate kujiandaa na safari. Konda alionekana mchomvu sana, alikuwa amenyong'onyea. Konda akamwambia Mayasa kuwa anaumwa ndio maana amewahi kurudi siku hiyo. Alikuwa ametoka hospitali na amepewa dawa za malaria kwani baada ya kupimwa aliambiwa kuwa anaumwa malaria. Alikuwa anajisikia baridi sana, akapanda kitandani na kujifunika shuka. Mayasa alienda sehemu wanapouza chakula na akanunua chakula kwa ajili yake na kwa ajili ya konda. Konda hakula kabisa kwani alikuwa hajisikii hamu yeyote ya chakula. Konda alimwambia Mayasa,

    “Dada leo pesa ilikuwa ngumu sana, lakini kwakuwa nilikuhaidi kuwa nitakupatia nauli, nilifanya kila namna ya kukopa kwa rafiki zangu na nimefanikiwa kupata hii elfu thelathini....Kwa hiyo chukua ili kesho uwahi na safari yako”

    Mayasa akapokea na kumshukuru sana Konda. Muda wa kulala Konda akaamka kitandani na kumpisha Mayasa, yeye akaenda kulala kwenye sofa. Mayasa akiwa kitandani alikuwa anamshuhudia konda jinsi alivyokuwa anapata tabu kuwafukuza mbu. Mayasa akaona bora yeye akalale kwenye sofa alafu Konda akalale kwenye kitanda ambako kuna neti. Konda naye akamwonea huruma Mayasa, basi wakakubaliana kulala wote kitandani.

    Mayasa alikubali kulala pamoja na Konda kitanda kimoja kwani teyari alishamuona Konda hakuwa na lengo lolote baya. Walilala mbali mbali sana, usingizi ukawachukua na kulala fofofo. Hakuna aliyejua kama anajivingirisha na kusogea kwa mwenzake. Majira ya saa kumi na moja kasoro, alam ikaanza kuita kwenye simu ya konda. Wote wakaamka baada ya mlio wa alamu. Walipoamka, wote walijikuta kila mmoja mkono wake upo kwa mwenzake na walikuwa wamekumbatiana. Zaidi ya dakika moja walibaki wametazamana na bado wakiwa wamekumbatiana.





    Kila mmoja alibaki akimshangaa mwenzake ,kukumbatiana kwao kukazua tabasamu ndani ya mioyo yao na sura zao. Miili ikahitajiana, hakuna aliyepanga iwe hivyo lakini mazingira hatarishi ambayo waliyatengeneza wao wenyewe yakapelekea kufanya kitu ambacho hawakutarajia kukifanya kabla. Mwili wa binadamu umeumbwa kuwa dhaifu, unaweza ukasema jambo fulani hulifanyi lakini siku ukisogea mazingira hayo ambayo yana jambo hilo unaweza ukajikuta unalifanya bila kutegemea. Ndio maana watalaam wa masuala ya theolojia wanasema kuwa roho ndio inakuwa ipo radhi kuacha jambo baya lakini mwili wa binadamu huwa dhaifu sana na kushindwa kuendana na roho. Mayasa na Konda walijikuta wanaingia katika uwanja wa mpira ambao huwa na wachezaji wawili tu,hakuna refa wala mashabiki wala kocha. Mayasa na Konda wao ndio wakawa wachezaji, refa, kocha na watazamaji.

    Mchezo waliocheza ukawafanya kila mmoja asahau alichokipanga. Mayasa akasahau kama ana safari na Konda naye akasahau kama anaumwa malaria na hata hivyo alitakiwa aende kwenye kazi yake. Walipomaliza waliendelea kulala hadi ilipofika majira ya saa moja asubuhi wakati teyari jua limeshaanza kuchomoza. Konda alimpigia simu dereva wake na akamwambia kuwa hajisikii vizuri hivyo hataenda siku hiyo.

    Siku hiyo iliisha kwa wawili hao kushinda ndani huku wakipiga stori za maisha yao. Konda akamshawishi Mayasa kubaki ili aendelee kuishi naye hapo nyumbani. Mayasa naye bila kuchanganya akili zake akafuata mwili wake,akakubali kubaki na Konda.

    Maisha yakaanza sasa ya mke na mume kati ya konda na Mayasa. Konda alinunua kila kitu ndani ambacho kingeweza kumfaa Mayasa kupika mwenyewe pasi na kununua chakula migahawani. Siku zilisonga mbele maisha yakiwa ya furaha na amani sana. Tabasamu ambalo lilipotea moyoni kwa Mayasa sasa aliweza kuliona japo sio sana ila angalau moyo wake ulichanua kwa amani na furaha.

    Maisha yakaendelea hivyo, Mayasa akaanza kuijua na baadhi ya mitaa ya Temeke kama Tandika,Wailes,na kwingineko. Habari za nyumbani kwake alizisahau kabisa. Konda alifanikiwa kumbadiri kabisa Mayasa kutoka kwenye hudhuni na kuwa na furaha. Miezi mitatu ilipita Mayasa akiwa na Konda. Konda aliamini sasa amepata mke aliyemwitaji. Aliwataarifu ndugu zake kuhusu Mayasa. Kilichobaki ni upande wa ndugu wa Mayasa nao kujua. Ugumu uliotokea ni jinsi ya kupata mawasiliano ya ndugu wa Mayasa kwani Mayasa simu aliiacha kwa kina Sunir ambayo ilikuwa na namba za ndugu zake. Walichopanga ni kupanga safari hadi nyumbani kwa Mayasa ili wakaone namna ya kuunganisha uhusiano wao.

    Baada ya wiki moja safari ilipangwa ya kwenda Lindi. Ndugu zake Konda walikuwa wanakaa Morogoro, wao walibariki safari hiyo kupitia simu ambayo alipiga Konda alipowataarifu juu ya safari hiyo. Safari ya Lindi ilianza mara moja na walifanikiwa kufika salama Nachingwea mjini. Waliposhuka garini , Mayasa alijiuliza mwenyewe wapi aanze kwenda kati ya kwa dada yake au kijijini kwao moja kwa moja. Akaona bora aanze kwa dada yake mama Vumi. Wakachukua usafiri hadi kwa mama Vumi. Bahati nzuri walipofika tu, mama na baba Vumi ndio walikuwa wanaingia. Mayasa alikuwa amebadirika ,mwili wake ulianza kunawiri na hata ngozi yake ilikuwa nyororo . Kichwani alisuka rasta na kumfanya apendeze sana. Mama Vumi na baba Vumi walimkaribisha ndani Mayasa na Konda. Mayasa akawasalimu na kumtambulisha Konda kwao. Akaeleza kila kitu kuhusu ujio wake. Mama Vumi alitamani amuulize Mayasa alikuwa wapi muda wote ambao hajaonekana kwao ila aliona ataharibu mambo, akaona asubiri muda ambao atakuwa peke yake. Siku hiyo walikubaliana watalala hapo alafu kesho yake ndipo wataenda kijijini kwa wazazi wao. Ilipofika usiku, wakati konda anaoga maji ndipo mama Vumi akaanza kumwambia Mayasa kuhusu Damaso jinsi alivyoangaika kumtafuta kila mahali na asimpate. Lengo la kutafutwa kwa Mayasa lilikuwa ni kutaka kujenga upya mahusiano yao ambayo yaliyumba hapo awali. Japo Mayasa alikuwa na upendo kwa Damaso lakini alimwambia dada yake kuwa kwa wakati huo, Konda ndiye aliyekuwa kila kitu kwake. Dada yake hakutaka kubishana sana na ndugu yake, akaamua kumwacha afanye analoona linafaa kwenye maisha yake mwenyewe.

    Siku iliyofuata Mayasa na Konda wakaondoka na kwenda kwa wazazi wa Mayasa. Wazazi wake walimpokea kwa furaha sana maana tangu aondoke kwao hawakuwa na mawasiliano naye tena ndio hadi wanamuona siku hiyo. Baada ya salamu, Mayasa akawaomba msamaha wazazi wake kwa kuondoka kwao bila kuaga. Wazazi wake hawakuwa na hiyana, walikubali msamaha wa Mayasa. Baada ya hilo kufanyika, Mayasa akamtambulisha rasmi Konda kwa wazazi wake na kwa nini amefika naye nyumbani hapo. Wazazi wake walishangaa sana lakini kushangaa kwao kulikuwa ni moyoni hivyo konda na Mayasa hawakuona chochote. Baadae mama Mayasa akamwita Mayasa ndani na kuwaacha baba na Konda nje wakiendelea na stori.

    “Mwanangu, hivi Damaso yuko wapi?”

    Mama alimuuliza Mayasa. Mayasa akajibu.

    “Sijui aliko.....”

    “Sasa na huyu uliyemleta vipi tena?”

    “Mama nyinyi wenyewe ni mashahidi, Damaso aliniacha ,sasa mimi ningefanyaje? Na huyu mtu wala sio mbaya sana ni mwema tu, amenisaidia sana hadi leo unaniona hapa....”

    “Mmmh! Mwanangu jamani....kwa hiyo umemkubalia kwa sababu amekusaidia? Na vipi akitokea kijana mwingine akikusaidia chochote naye utamkubalia?”

    “Hapana, si hivyo! Haina maana kwamba kwa sababu amenisaidia ndio nimemkubalia,la hasha! nimeona tu ana huruma na upendo”

    “Mmmmh! Aya! Ila sasa akitokea tena Damaso na kuja hapa kukutafuta itakuwaje? Maana siku za mwanzo aliwahi kuja kukuulizia.......”

    “Hawezi kuja hata kidogo, kwa jambo lile lililotokea hawezi kunitaka tena”

    “Sawaa......Ila je akitokea tena utafanyaje?”

    “Heee! Mama jamani ,hawezi kutokea tena, kwanza hata akitokea wala haina shida, hatukufunga ndoa sisi....”

    Mama Mayasa akaishia hapo kumuuliza maswali, akamtaka kumsimulia zaidi kuhusu Konda, hapo ndipo Mayasa akafunguka juu ya safari yake kuanzia anatoka kwao hadi anaenda Dar es salaam na kukutana na Konda. Mama alionesha wasiwasi waje juu ya konda lakini Mayasa alimtoa kabisa kwenye hofu na shaka. Akamtuliza mama yake kwa kummwagia sifa kedekede Konda. Kwa shingo upande mama alimkubalia Mayasa kuwa na Konda ingawa hofu yake kubwa ilikuwa ni muda ambao walikutana na Konda ulikuwa mfupi sana kwa yeye Mayasa kuweza kujua kwa undani tabia za Konda huyo. Mayasa akatoka nje alafu mama akamwita baba Mayasa wakajadili ndani, wakakubaliana kuwa kwa kuwa huyo Konda yeye(Mayasa) ndiye anamjua basi wamruhusu tu na ukizingatia Damaso naye alishamtenga Mayasa baada tu ya kujifungua mtoto mhindi. Walikubaliana mambo ya mahali na siku ambayo ataileta. Baada ya siku moja Mayasa na Konda walirudi mjini kwa dada yake.

    Siku ambayo Mayasa na Konda walifika mjini kwa mara ya kwanza wakitokea Dar es salaam, baba Vumi alimpa taarifa Damaso kuwa Mayasa amerudi. Wakati huo Damaso alikuwa Mtwara kwenye kazi zake. Kutokana na taarifa ya baba Vumi, Damaso aliomba ruhusa kwa wenzake na kwenda moja kwa moja kwa wazazi wa Mayasa kwani alidhani ndio atakuwa huko. Walipishana, Damaso anaenda kijijini na Mayasa anaenda mjini.Wazazi wa Mayasa walimwambia Damaso kuwa Mayasa sasa amepata mchumba mpya kwani yeye alishamuacha. Damaso hakutaka kubishana nao sana, akaamua kuondoka. Akampigia simu Baba Vumi na kumuuliza tena kuhusu Mayasa. Baba Vumi alimwambia kuwa yupo kwake na jamaa yake. Damaso naye muda huohuo akapata usafiri kutoka kijijini hadi mjini. Alipofika mjini, alienda moja kwa moja kwa nyumbani kwa Baba Vumi. Alimkuta nje Mayasa akiwa na dada yake. Moyo wa Mayasa ulipatwa na mshtuko sana baada ya kumuona Damaso, Mama Vumi naye akapagawa akajua kishanuka. Damaso alikuwa anahema sana,alionekana alikuwa ana shauku ya kutaka kumuona Mayasa. Mayasa naye aliyakumbuka maneno ya mama yake ,“Ikitokea Damaso anakuja tena kwako utafanyaje?” Sasa maneno ya mama yake yalionekana dhahiri katika uhalisia. Wakati huohuo Baba Damaso na Konda nao walikuwa wanaingia kwani walitoka kidogo kwenda kutembea.







    Damaso akamsalimia Mayasa, Mayasa akaitikia lakini kwa uoga sana yaani hakujiamini kabisa. Damaso akawasalimu na wengine wote na konda naye akiwemo. Baada ya hapo Damaso akamuuliza Mayasa alikuwa wapi kwa muda wote ambao alikuwa hayupo kwake. Mayasa hata kabla hajaanza kujibu simu ya konda iliita hivyo alitoka pembeni kidogo kupokea na kuongea. Hapo sasa Mayasa akapata upenyo wa kuzungumza na kumjibu Damaso japo kwa uchache sana. Damaso alianza kumwambia Mayasa habari zake na jinsi alivyopata tabu kumtafuta bila mafanikio, Mayasa alipoona Damaso anazidi kuongea kuhusu mahusiano yao akaamua kumwambia Damaso kuwa watakutana baadae kuzungumza maana mazingira hayakuruhusu kuongea mambo hayo. Konda naye alimaliza kuongea na simu na akarudi kijumuika na wenzake.

    “Nimesikia una mchumba Mayasa, je ni kweli?”

    Damaso alikuwa na shauku ya kutaka kujua harakaharaka juu ya mambo hayo. Mayasa akajibu,

    “Ndivyo hivyo ,ni sahihi kabisa.....”

    “Unasemaje?”

    Damaso aliuliza kana kwamba hajasikia alivyojibu Mayasa. Mayasa akajibu tena vilevile na huku akitabasamu na kumwonesha Konda kuwa ndiye mchumba mwenyewe.

    “Kwani Mayasa huyu ni nani? Mbona anakuuliza maswali mara mbilimbili?”

    Konda naye aliamua kuingilia kati baada ya kuona Damaso anazidi kuchanja mbuga katika maswali tena hasa ya ndani kabisa. Damaso alikuwa kama amepaniki vile akaanza kuhamaki,Damaso akamwangalia Konda alafu akasema,

    “Wewe nani hadi unamuuliza maswali mke wangu kuhusu mimi?........kaa kimya haya mambo hayakuhusu wala usiyaingilie”

    Mayasa baada ya kusikia kauli ya Damaso ,akaingilia kati ili kumtuliza Konda,

    “Baby usiwe na hofu, huyu ndio yule kijana niliyekupa taarifa zake kuhusu kutengana hadi nikakutana na wewe,sasa sijui amefuata nini kutoka kwangu ila msamehe tu maana hajui alitendalo”

    Damaso alichukia sana baada ya kujibiwa hivyo na Mayasa , alitamani amrukie mzima mzima. Damaso hakutaka kuamini kabisa kama maneno anayoyatamka Mayasa yalikuwa yanatoka mdomoni kwake. Maana Mayasa aliyemfahamu yeye sio huyo ambaye alikuwa na majibu ya namna hiyo.

    “Ni wewe Mayasa unayenijibu hivi au labda ni mzimu wake?”

    “Heee! Damaso ndugu yangu mbona unatia huruma kiasi hicho? Usichoeleewa hapa ni kipi? Wewe nenda kaendelee na maisha yako nami niache niendelee na maisha yangu niliyoyachagua”

    Damaso alitaka anyanyue mkono ili amtandike Mayasa lakini baba Vumi aliona hivyo akawahi na kumshika mkono Damaso alafu akatoka naye hapo na kuanza kumsihi asifanye lolote kwani atazalisha jambo lingine ambalo mwanzo halikuwepo. Baada ya kutoka naye kabisa maeneo ya nyumbani kwa baba Vumi ,Baba Vumi akamwambia Damaso,

    “Ndugu yangu Damaso hasira ni hasara siku zote, fikiria pale unampiga halafu anapata madhara, hivi huoni kuwa unataka kusababisha matatizo zaidi?Alafu inaonesha huamini kabisa kama yule ndiye Mayasa uliyemfahamu......Damaso hapo sasa ndio unatakiwa utambue kuwa hakuna binadamu ambaye huwa anakuwa na tabia ya kudumu, binadamu hubadirika kila siku , ndio maana mara kadhaa dini zimefundisha kuwa usimtumini mwanadamu yeyote, nakusihi tulia , mara nyingi anayejikwaa na kuanguka basi akiamka huwa mwangarifu sana pale atembeapo, sasa mimi sioni sababu ya wewe kuendelea kubishana na Mayasa, mwache akapambane na dunia, Siku zote mkataa pema pabaya panamwita”

    Damaso alimsikiliza kwa makini sana baba Vumi, alimwelewa sana na hasira zake zote zikaisha. Hata hivyo Damaso alitamani sana akutane na Mayasa kwani kuna mambo ya msingi anataka amweleze, akamuomba baba Vumi kama anaweza basi afanye kila namna akutane na Mayasa ili amweleze masuala kadhaa yaliyotokea baada ya wao kutengana.

    Baba Vumi na Damaso wakapanga njia ambayo ingeweza kumfanya Mayasa akutane na Damaso bila yeye kujua kama anaenda kukutana naye maana Mayasa alionekana hataki tena kusikia habari za Damaso. Hivyo basi waliona njia rahisi ya kumtoa ni kumwambia kuwa anaitwa na fundi wake Mr Makalanga. Damaso na Baba Vumi wakaachana alafu Damaso akaenda kukaa jirani na ofisi ya Mr Makalanga ,sehemu ambayo Mayasa alikuwa anajifunza kushona nguo. Baba Vumi alivyofika nyumbani kwake, akamungopea Mayasa kuwa amekutana na fundi wake Mr Makalanga na anamtaka aende ofisini kwake kabla hajaondoka Dar. Mayasa akajua kweli, kwa kuwa siku inayofuata alipanga waondoke Dar basi Mayasa ikabidi atumie muda huohuo kwenda kumuona fundi wake. Akapanda bodaboda na kwenda kwa fundi wake. Alipofika , Damaso akamuona Mayasa ,akamsogelea na kumwita , Mayasa hakutaka kwenda kwa Damaso hivyo Damaso akalazimika kumsogelea zaidi alafu akamwambia kuwa aliyekuwa anamwita ni yeye Damaso na wala sio mwingine, aliambiwa kama anaitwa na fundi ili tu afanye haraka ya kuja. Damaso akamuomba sana Mayasa watafute sehemu ili waongee. Kwa shingo upande, Mayasa alikubali, wakaenda katika sehemu ambayo inayouzwa vinywaji ambayo ilikuwa karibu yao. Wakatafuta sehemu wakakaa. Damaso akaanza kumweleza Mayasa kuhusu bibi yake.

    Akamwambia kuwa bibi yake ameshafariki. Hapo kidogo angalau Mayasa akatulia na kuendelea kumsikiliza kwa makini Damaso. Damaso akaendelea kueleza kuwa bibi yake alikamatwa katika nyumba ya kijana mmoja huko kijijini kwao akiwa anawanga,sasa huyo kijana alikuwa ameweka zindiko katika nyumba yake hivyo baada ya kukamatwa kuna vitu alimpa na bila shaka hivyo ndivyo vilimfanya afariki. Baada ya bibi Damaso kukamatwa akiwa anawanga,kuanzia asubuhi yake akaanza kuumwa. Kila wakimwambia wampeleke hospitali aligoma na kukataa katakata. Lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya sana, siku moja alimwita Damaso na kumwambia,

    “Mjukuu wangu Damaso mimi bibi yako siwezi kupona tena, nimekuwa mchawi kwa muda mrefu sana, nimekuwa nikiwaroga majirani zangu na hata ndugu zangu, nimekuroga sana pamoja na yule mke wako ndio maana hata mimba za mkeo zilikuwa zinatoka kila anaposhika ujauzito hiyo yote ilikuwa kazi yangu, lakini sasa ujanja wangu wote umekwisha, siponi ,ninaenda kufa sasa ....neno langu kwako kamrudishe mke wako Mayasa ili uendelee kuishi naye, nisamehe sana Damaso, mwambie na Mayasa anisamehe kwa niliyomfanyia......Yote niliyowafanyia hayakuwa na faida kwangu zaidi ya kukuumiza mjukuu wangu Damaso, narudia tena nisamehe.....”

    Baada ya kumwambia hayo Damaso,lisaa limoja mbele Bibi Damaso akakata roho na habari zake zikaenea kijiji kizima kuwa amekufa kwa sababu ya uchawi. Damaso akaendelea kumweleza Mayasa kuwa baada ya hapo alifanya kila jitihada za kumtafuta lakini hakufanikiwa kumpata. Damaso huku akiwa mwenye utulivu sana akasema,

    “Mayasa sasa nimetambua kuwa chanzo cha haya yote alikuwa ni bibi yangu,hata yule Neema ambaye alikuwa na mimba baadae nikagundua kuwa mimba haikuwa yangu na aliyesababisha ni huyohuyo bibi yangu. Nilikutafuta kwa lengo la kutaka kukuambia haya na turejeshe mapenzi yetu kama yalivyokuwa hapo awali, Nilisikitika sana baada ya kukutafuta na kukukosa, lakini leo tumeonana na sasa turudi nyumbani tikaufungue ukurasa mpya wa maisha yetu baada ya hizi changamoto zilizotokea”

    Muda wote huo Mayasa hakusema neno lolote,alikuwa yupo kimya, alipoona Damaso amemaliza kusema naye akatia neno lake,

    “Damaso,hakuna marefu yasiyo na ncha, pengine mwisho wetu teyari umefikia, uliponifukuza kwako kipindi kile ,nililia na kuhudhunika sana, lakini kwa sasa siwezi kurudiana na wewe ,mimi nimepata mchumba na hata wewe mwenyewe umeshamuona teyari,Kwa hiyo mimi na wewe sasa hivi ni kama hatujuani tu, endelea na maisha yako nami niendelee na maisha yangu....“

    “Mayasa....Siku zote huwezi kujua umuhimu wa kitu fulani mpaka siku moja itokee unakihitaji lakini hakipo karibu nawe, tangu uondoke nyumbani nimekuwa mpweke sana, nimegundua wewe una umuhimu sana katika maisha yangu,Yule jamaa yako sidhani kama anakuhitaji kama ninavyokuhitaji mimi. Mayasa unatakiwa utambue kuwa mwanaume yeyote anapompenda mwanamke kitu cha kwanza kufikiria ni ngono(kufanya naye mapenzi) na si vinginevyo, hata kama atakuambia maneno mengi mazuri ikiwemo suala la ndoa , hayo yote atayasema ili tu afanye nawe mapenzi na baada ya hapo anaweza akakutupa au ikatokea kweli akatamani akuoe, mimi najua kwa muda mfupi uliokutana na jamaa ,sina hakika kama kweli alikufuata kwa lengo la ndoa, najua atakutumia na akimaliza haja zake basi atakufanya kama kalai linavyotupwa baada ya kukamilisha ujenzi , mimi najua unajua jinsi ninavyokupenda, Mayasa rudi nyumbani......”

    “Siwezi kurudi tena kwako....”

    Baada ya jibu hilo ,Mayasa akaanza kunyanyuka ili aondoke, Damaso akamshika mkono na kumwambia,

    “Usikivu nao ni kipimo cha busara, sijamaliza kusema wewe unataka kuondoka....Kwa hiyo ina maana sasa hivi hata kunisikiliza tu hutaki? Zile busara zako umezipeleka wapi?”

    Mayasa akakaa chini alafu akasema,

    “Aya ongea nakusikiliza.....”

    Damaso akamwangalia Mayasa na akatambua kuwa hadi kufikia hatua hiyo Mayasa hakuwa teyari kumsikiliza na hata kama atamsikiliza basi yatakuwa yanaingia sikio hili alafu yanatokea sikio lingine. Damaso akamwambia Mayasa,

    “Hivi ni jinamizi gani limekupata wewe? Mimi ninashukuru sana kwakuwa adhma yangu ya kukutana na wewe na kukuambia niliyopanga nikuambie teyari nimeshakuambia, siwezi kukulazimisha uwe na mimi lakini naamini ukinikosa mimi basi utakuwa umekosa bonge la bwana, sijisifii ila ninajijua na hata wewe unajua, Mayasa naomba uniambie neno lako la mwisho, je upo teyari kurudi nyumbani?”

    “Nirudi kwako alafu yule nimpeleke wapi?”

    “Mayasa....Mayasa hilo litafuata baada ya kujibu nilichokuuliza, je upo teyari kurudi nyumbani tukaishi wote kama zamani?”

    Kabla hata hajajibu simu yake iliita ,alikuwa ni Konda,akapokea. Konda alimuuliza Mayasa yuko wapi mbona anachelewa sana, Mayasa aliongopa kuwa bado yupo kwa fundi wake. Baada ya kukata simu, Damaso akasema,

    “Kama ingekuwa huyo mtu wako yuko moyoni basi wala usingemdanganya kuhusu mahali ulipo, hiyo ni ishara tosha kuwa hayupo moyoni mwako bali ni tamaa za mwili tu ndizo zimekufanya uwe naye, Mayasa narudia tena je upo teyari kurudi nyumbani?”

    “Nirudi kwako kufuata nini?”

    “Mayasa nimeshakuambia,naomba tukaishi kama zamani, naomba jibu lako la mwisho, je upo teyari kuungana nami ?”





    Mayasa akamwangalia Damaso bila kusema kitu. Akatulia kama dakika mbili hivi huku akichezea simu yake alafu akamwambia Damaso kuwa kuwa pamoja naye tena hilo ni jambo gumu sana na haliwezi kutokea.Damaso alikuwa king'ang'anizi sana hapo sasa Mayasa hakusubili tena maneno yeyote kutoka kwa Damaso, akanyanyuka na kuondoka. Mayasa alirudi kwa dada yake . Aliwakuta wote wakiwa wamekaa nje. Naye akajumuika nao.

    Damaso aliendelea kukaa alipoachwa na Mayasa kama dakika ishirini mbele. Aliwaza na kuwazua kuhusu Mayasa. Japo aliumia lakini hakuwa na budi kumtoa akilini Mayasa kwani Mayasa teyari ameshafanya maamuzi mengine kabisa tofauti na yale aliyofikiria. Damaso akaona bora arudi kazini kwake kuendelea na kazi zake. Siku ya pili yake Damaso akasafiri hadi Mtwara kuendelea na majukumu yake ya kazi na Mayasa naye na Konda wake wakasafiri siku iliyofuata kurudi jijini Dar es salaam. Maisha ya wawili hao yaliendelea wakiwa na furaha sana. Mayasa akaona hayo ndiyo maisha ambayo alikuwa anayawaza. Changamoto ilikuwa moja tu ya kutokaa muda mrefu na mpenzi wake Konda, hii ni kwa sababu Konda alikuwa anatoka saa kumi na moja asubuhi na kurejea saa tano hadi sita usiku. Hivyo muda ambao alikuwa anakutana nae ulikuwa hauzidi masaa manane. Hali hiyo Mayasa aliivumilia huku akiamini siku moja itaisha kama ilivyoisha suala la Damaso na bibi yake hali kadhalika na suala la Sunir na mwanaye.

    Mayasa akajuana na wapangaji wenzake tena wakampachika na jina wakawa wanamuita mama Konda. Maisha yakaenda hivyo na Mayasa akawa amezoeleka hata nyumba ya jirani huko wakawa wanamjua. Baada ya mwezi mmoja , Mayasa alikuwa anashona nguo nje tu ya nyumba aliyokuwa anaishi. Alianza kupata wateja kwani eneo ambalo alikuwa anakaa hakukuwa na fundi mwingine wa kushona hivyo wateja walimiminika kwake kwa wingi. Siku zilivyozidi kusonga mbele , Konda akajadili na Mayasa juu ya kupata mtoto. Tangu apate ujauzito wa Sunir, Mayasa alianza kuwa makini katika suala la kushika mimba. Hakutaka kushika mimba haraka kwani tangu ajifungue mtoto wa Sunir haikupita hata mwaka hivyo alimwambia Konda aendelee kusubiri kidogo mpaka akae sawa. Konda alikubali ingawa alikuwa na shauku kubwa sana ya kuitwa baba.

    Mambo kangaja huenda yakaja, siku zilisonga mbele wawili hao wakiwa pamoja. Siku moja Mayasa aliona mguu wake unawasha sana kuanzia kwenye goti hadi kwenye wayo. Hakutilia maanani ,aliona pengine ni mdudu tu amempanda na kusababisha muwasho. Alijiwasha kama dakika tano hivi baadae ukatulia. Siku iliyofuata ukaanza tena kuwasha. Kama kawaida ulikuwa kwenye hali hiyo kwa muda fulani alafu baadae ukatulia. Kadri siku zilivyozidi kusonga mbele ndipo muwasho ulivyozidi kuongezeka. Sasa mguu haukuwasha tu, ukaanza kutoa na majimaji na maumivu kwa mbali sana yakaanza kusikika. Konda alimpa pesa Mayasa ya kwenda hospitali, baada ya kwenda huko akapatiwa dawa na daktari na akaanza kuitumia. Alipata nafuu, lakini baada ya wiki moja hali ya mwanzo ikajirudia tena. Maumivu yakaongezeka hadi akawa anakosa usingizi kabisa. Hospitali walienda tena, wakafanya vipimo na kama kawaida akapewa dawa za kutumia. Dawa alianza kuzitumia lakini hakupata ahueni hata kidogo. Konda akaanza kuamini imani za kishirikina kwamba pengine Mayasa amerogwa na Damaso baada ya kukataliwa hata alipomwambia Mayasa kuhusu hilo Mayasa naye akasadiki kwamba yaweza kuwa kweli amerogwa. Wakapanga safari hadi Bagamoyo kwenda kwa mganga wa kienyeji. Mayasa akatoa maelezo yake kwa mganga kuhusu mguu na Konda naye akaongezea kuhusu Damaso. Mganga akafanya mambo yake, baada ya kuona kazi yake imerahisishwa na Konda aliposimulia habari za Mayasa na Damaso , naye akapita mulemule. Akawaambia kuwa ni huyohuyo Damaso ndiye aliyesababisha hayo. Mayasa akaanzisha chuki kali kwa Damaso ,aliamini maneno ya mganga kuwa Damaso ndiye aliyesababisha. Mganga akatoa dawa na kuwapa maelekezo namna ya kuitumia. Kama ilivyo kawaida, Konda akaacha pesa kwa mganga huyo kisha wakarejea Dar es salaam na kuianza tiba ya mganga huyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mayasa aliitumia dawa aliyopewa kwa mganga kwa muda wa wiki moja lakini matokeo hayakuwa mazuri sana. Bado maumivu yalikuwa yaleyale, kwakuwa namba ya mganga walichukuwa ,Mayasa alimpigia simu na kumweleza hali yake, mganga akamwambia kuwa aendelee kuvumilia kwani dawa inafanya kazi. Mayasa alivumilia lakini hakuona matunda yake. Mwanzo mguu ulikuwa unatoa majimaji ya kawaida tu, lakini baadae ukaanza kutoa majimaji yaliyoambatana na harufu. Harufu ilianza kuwa ya kawaida lakini baadae harufu ikaongezeka mara dufu. Harufu ikawa kali sana, Mayasa akakosa amani kabisa, ile furaha ambayo mwanzo alikuwa nayo ilianza kupotea taratibu, sura yake haikuonesha tabasamu ,tabasamu lote likapotea. Konda naye akaanza kuona hilo ni balaa, naye akakosa amani kabisa. Tabia ya furaha ni kutodumu katika maisha ya mwanadamu, furaha huja na kutoweka. Majirani wa Mayasa hawakumsogelea tena Mayasa, kutokana na harufu iliyokuwa inatoka katika mguu wake. Konda naye hakulala usiku kucha kutokana na harufu hiyo. Hawakujua wafanye nini maana hospitali wameenda na kwa waganga wa kienyeji pia wameenda lakini hamna matokea mazuri.

    Rafiki zake konda walifika kumwangalia Mayasa , walimuonea huruma Konda, alafu wakaanza kumwambia bora ambwage tu maana wanawake wazima wenye afya safi ambao hawana harufu wako wengi sana. Rafiki yake mmoja alimwambia,

    “Kaka acha ubwege .....miezi inakatika bado unaendelea kuuguza mgonjwa ambaye hujui atapona lini na hata ugonjwa anaoumwa bado haujui, kaka wanawake wapo kila kona kwanini unaendelea kukaa na mtu ambaye anatoa harufu kama mzoga? Achana naye mzee !ataendelea kumaliza pesa zako tu bila sababu ya msingi....kwanza vyuma vimekaza kinoma jamaa yangu...piga chini”

    Maneno ya rafiki zake yalikuwa mengi sana. Hata familia yake iliposikia habari hizo wakamwambia kuwa aachane naye. Siku moja mama yake Konda alimwambia Konda,

    “Sasa mwanangu huyo mwanamke hata hujamuoa bado ,teyari ameanza kukuletea shida. Na vipi ukimuoa? Sisemi kwamba watu hawaumwi lakini huyo mmmmh! Kwanza hata ugonjwa wenyewe haujulikani anaumwa nini, bora matatizo yawakute mkiwa kwenye ndoa yanavumilika lakini hapo mmmmmmh! Hapana.”

    Maneno ya mama na rafiki zake yakaondoa kabisa wazo la Konda la kutaka kuendelea kukaa na Mayasa. Konda akamwambia Mayasa inabidi arudi kwake Lindi ili akajiuguze, Mayasa hakukubali jambo hilo, kwani aliona watu wakwao watamshangaa sana akiwa katika hali hiyo. Konda akaona bora atumie ile mbinu ya akufukuzaye hakuambii toka. Akaanza kutorudi akitoka, anakaa hukohuko siku mbili hadi tatu ndipo anarudi kwake. Hali ya Mayasa ikazidi kuwa mbaya,mguu haukuwasha ila kero ilikuwa harufu mbaya. Konda alifanya hivyo kama wiki hivi, Mayasa akaamua kumuuliza,

    “Kwa hiyo kwa sababu ninaumwa ndio hunitaki tena? Mbona pale mwanzoni tulikuwa tunalala wote kitanda kimoja lakini siku hizi sikuoni ?”

    Konda akajibu,

    “Mayasa wakati naanza na wewe wala haukuwa hivi na kama ungekuwa hivi wala usingekuwa na mimi, nilivyokuona mwanzo sivyo ninavyokuona sasa, siwezi kuvumilia shida kama hizi, bora uondoke tu, hivi ni nani anayeweza kuvumilia kuishi na mtu anayetoa harufu mbaya kama wewe? Hakuna na hatatokea....”

    “Yaani leo unaongea hivyo kweli, ni wewe au mwingine?”

    “Sio leo tu hata kesho na siku zote zinazofuata nitaongea hivyo, leo nakupa nauli ya kwenda kwenu, kesho nitakavyorudi hapa nisikukute”

    Konda akachukua nauli na kuiacha kitandani alafu akaondoka. Mayasa akaanza kulia sana. Lakini kilio chake kilikuwa sawa na kilio cha samaki, hakuna aliyejua wala kusikia kilio chake. Kila alichofikiria aliona hakina maana. Akafikiria kujiua lakini nafsi ilikataa kabisa. Binadamu watakupenda kwa sababu ya vitu fulani fulani ambavyo unavyo, siku ikitokea umepoteza kimojawapo hapo upendo utaanza kupoa. Mapenzi ya Konda kwa Mayasa yaliisha kwa sababu ya ugonjwa wake.Pengine labda upendo unaoanza bila vigezo ndio pekee utakaodumu kwa kuwa ni moyo ndio ulioamua na si vinginevyo.

    Mayasa alifikiria kwenda kwa Sunir lakini huko aliona ndio majanga kabisa na kurudi kwao Lindi aliona aibu jinsi alivyokuwa anatoa harufu, akaamua kubaki hapo hapo. Konda aliporudi siku ya pili yake usiku bado alimkuta. Siku ya hiyo Konda alifika na mwanamke mwingine. Mayasa hapo sasa akajuwa teyari hatakiwi tena. Lakini kuondoka aligoma. Konda na mwanamke wake wakaondoka. Asubuhi ilipofika Konda alitafuta mgambo na akawatuma wakamwondoe Mayasa kwa nguvu. Mayasa akaondolewa kwa nguvu na kwenda kupandishwa gari la kwao Lindi. Abiria aliyekaa naye aliamua kuhama siti kwa harufu kali ya Mayasa. Mayasa alifika Nachingwea na akaenda moja kwa moja kwa dada yake. Dada yake alifadhaika sana baada ya kuiona hali ya Mayasa.

    Dada yake akamchukuwa na kumpeleka hosptali ya wilaya. Akapatiwa kitanda na kulazwa. Matibabu hayakuwa mazuri sana kwani pesa ya kutosha haikuwepo. Taarifa zikafika kijijini kwao ,wazazi nao wakafika kumuona. Mayasa alikuwa analia hata kuhadithia hakuweza zaidi ya kusema “Damaso anajua”, Mayasa alikuwa anayaamini maneno ya mganga wake. Damaso akatafutwa na kuletwa hospitali. Alipomuona Mayasa katika hali hiyo alishtuka sana, hakujuwa amepatwa na nini. Akawauliza anaumwa kitu gani lakini hakuna aliyejua kwani hata vipimo hakupatiwa kutokana na kutokuwa na pesa. Damaso akaambiwa kuwa Mayasa amesema kuwa yeye anajua anachoumwa. Damaso hakuwaelewa ,akaona cha msingi ni kuwasaidia kwanza kumtimbu alafu mengine yatafuata. Damaso akachukuwa akiba yake yote na kumwamisha hospitali na kumpeleka hospitali kubwa zaidi , Mayasa akapelekwa hospitali ya Ndanda Mission kwa ajili ya matibabu zaidi.





    Damaso alimuomba sana daktari aweze kumsaidia

    Mayasa kwa juhudi zake zote ili aweze kupona na kurejea katika hali yake ya mwanzo. Daktari alimjibu Damaso asiwe na wasiwasi kwani wao kazi yao ni kutibu na Mungu ndiye anayeponya hivyo asiwe na wasiwasi atapona tu. Damaso alitulia kusubiri wataalamu

    wafanye kazi yao. Mayasa alipelekwa chumba cha X-ray, akapiga picha mguu wake na madaktari wakaanza kuchunguza kuanzia hapo. Wakamfanyia na vipimo vigine vingi,wakabaini tatizo. Ndani ya mguu wa Mayasa ilionekana kuna kipande kidogo cha chuma kimekaa katika nyama. Wakamfanyia upasuaji na kukiondoa na wakayasafisha majimaji yote ambayo yalikuwa yanatoa harufu kali sana. Baada ya hapo akapelekwa kwenye ward kulazwa.

    Mayasa baada ya kuambiwa kuwa alikuwa na kipande cha chuma katika mguu wake, alikumbuka siku moja wakati anatembea barabarani akielekea sokoni kuna muda alijikwaa alafu akaangukia sehemu chakavu yenye vyuma vidogovidogo vingi sana na baada ya kuanguka alihisi kuna kitu kimemchoma mguuni ila alipoangalia hakukiona. Baada ya wiki moja kupita ndipo akaanza kupata muwasho na maumivu. Alikumbuka alivyomchukia Damaso kwa kuamini kuwa yeye ndiye kasababisha lakini kumbe si yeye! Mzaniaye ndiye kumbe siye! Chuki alizojenga kwa Damaso zilikuwa za bure.

    Mayasa akawaza jinsi alivyoenda hospitalini ila kwa kuwa hawakuwa na pesa basi aliishia kupewa dawa tu bila vipimo stahiki. Mawazo yakaanza kupandana kichwani mwa Mayasa kuhusu pesa. Je pesa inaokoa uhai,swali hili lilijaa akilini mwa Mayasa, akawaza kama kusingekuwa na pesa za matibabu inamaana mguu wake ungeendelea kuoza na kutoa harufu ila pesa za Damaso zimefanikiwa kuokoa uhai wake, bado mawazo yakazidi kulandalanda kichwani mwake huku akijihoji mwenyewe lakini kama pesa inaokoa uhai wa mwanadamu mbona kuna watu wenye pesa nyingi na wanatibiwa hospitali nzuri na bado wanakufa? Pengine yupo anayeokoa uhai zaidi ya hizo pesa. Mayasa akazidi kuwaza kama kuna mtu ambaye anatakiwa afanyiwe matibabu ya figo na akawa hana pesa alafu baada ya muda akafariki kutokana na kukosa matibabu

    na hapo vipi,amefariki kwa sababu ya kukosa pesa ya matibabu ama ? Vipi angekuwa na pesa na angepata matibabu na tatizo lake kuisha? Mayasa aliwaza sana hadi akaja kushtuliwa na ndugu zake ambao waliruhusiwa na daktari kuja kumuona. Mayasa alipomuona Damaso ,moyo wake ulijawa na aibu ya yale aliyomwazia.

    Damaso alijawa na furaha baada ya kuona madktari wameweza kugundua tatizo na hatimaye Mayasa amepata nafuu. Wazazi wa Mayasa walimshukuru sana Damaso kwa kuokoa maisha ya mtoto wao kwa kiasi cha pesa alichotoa. Damaso akiwa mwenye tabasamu akajibu,

    “Si mimi wa kushukuriwa, ni Mungu mwenyewe ndiye ameamua iwe hivyo!”

    Baba Mayasa mzee Diko akasema kuwa yeye anashukuriwa kwa sababu ndiye aliyefanikisha Mayasa kupata nafuu.Damaso akasema tena,

    “Hata kama ni mimi niliyetoa pesa,lakini sikuwa na uwezo wa kumtibu huyu wala kumponya, mara ngapi tumesikia viongozi kadhaa wakitibiwa nje ya nchi kwa pesa nyingi lakini bado matibabu hayakufanikiwa? Basi bila shaka mimi si wa kushukuriwa hata kidogo, mpeni sifa Mungu wenu aliyemponya mwana wenu!”

    Baada ya Damaso kujibu hivyo wakaendelea kuongea na mgonjwa huku wakimuuliza chuma kiliingiaje,Mayasa akawasimulia jinsi chuma kilivyoingia mwilini mwake. Wiki moja ilipita Mayasa akiwa hospitali na hatimaye Mayasa alipata nafuu kabisa sasa ilibaki jeraha la kidonda kupona. Waliruhusiwa kurudi nyumbani . Damaso naye akawaacha na kuendelea na shughuli zake. Baada ya miezi miwili Mayasa alipona kabisa na kuwa kama zamani. Alimuona Damaso ni mtu wa kipekee sana,kwani pamoja na hayo yote aliyomfanyia na kwenda kwa Konda bado tu aliweza kumsaidia na kuokoa maisha yake.

    Mayasa aliamini kuwa hakuna binadamu anayeijua kesho yake,kila dakika ukutanayo na mtu yeyote basi hutakiwa kuonesha dalili zozote za dharau. Mayasa alipoamua kuyakabidhi maisha yake kwa konda,hakujuwa kabisa kama Damaso atakuja kuwa mkombozi wake. Hakika usitupe mti baada ya kumtupa jongoo!.

    Mayasa alienda nyumbani kwa Damaso kwa ajili ya kwenda kumuomba msamaha na kumshukuru kwa ajili ya kile alichomfanyia hadi mguu wake ukapona kabisa. Baada ya kufika nyumbani kwa Damaso, hakumkuta kwani kwani muda huo alikuwa yupo kazini kwake. Alienda kuangalia sehemu ambayo hapo mwanzo walikuwa wanaweka funguo. Aliikuta ,akataka kufungua lakini kabla hata hajafungua alimuona Damaso akiwa anakuja tena huku akiwa na mwanamke mwingine. Akaacha funguo harakaharaka , moyo wake ukaanza kuumia na ukajawa na wivu sana. Alidhani kuwa aliyefuatana na Damaso atakuwa mchumba wa Damaso.

    Damaso alifika kwake na kumkuta Mayasa akiwa nje ya chumba chake. Akaufungua mlango na kumkaribisha ndani. Yule mwanamke naye akaingia ndani na kumwambia ampatie kile alichofuata. Damaso akachukua nguo zake zote chafu na kumpatia mwanamke huyo. Baada ya hapo akamsalimia Mayasa. Wakati huo ,Mayasa alikuwa amesononeka sana, kwani alikuwa anajua Damaso atakuwa amepata mwanamke mwingine ambaye ndiye huyo amekuja kuchukua nguo zake na kwenda kumfulia. Mayasa akaitikia salama ya Damaso na kisha kumweleza jinsi gani moyo wake ulivyojawa na shukrani kwa alichomfanyia na huku akimweleza jinsi alivyokuwa anammwazia vibaya wakati alipokuwa anaumwa.

    Mayasa baada ya kueleza maelezo yake marefu yaliyojaa hisia za moyoni, Damaso naye akasema,

    “Matatizo yanapotokea mara nyingi huwa mawazo mabaya nayo huja hasa pale unapojaribu kutafuta ufumbuzi wa tatizo na ukashindwa kulipata, hapo unaweza ukakufuru, ukagombana na marafiki na hata kutengana na ndugu zako wa karibu, Mayasa...... , tatizo linapotokea hutakiwi kabisa kukata tamaa kwani ukikata tamaa huo ndio mwanzo wa kufanya dhambi maana hapo utaanza kukufuru na kuwaza mambo mabaya. Hatuna chochote tunachomiliki ambacho tunaweza tukajisifu nacho sisi binadamu, hivyo kila hatua tuipitiayo basi hatuna budi kumshukuru Mungu maana yeye ndiye anayejua kesho yetu, mimi sina kinyongo na wewe na wala na yeyote, furaha yangu ni kukuona ukiwa unafuraha”

    Mayasa akamsikiliza Damaso kwa maneno yake mazuri alafu baada ya hapo akamwambia Damaso,

    “Moyo wangu unajuta sana kwa maamuzi yangu niliyoyafanya hapo mwanzo, sasa nimetambua kwanini wahenga walisema kuruka agana na nyoga! Mimi niliruka shimo bila kuagana na nyonga matokeo yake nikatumbikia shimoni,nafurahi kuona huna kinyongo nami,lakini kuna jambo nimeumia sana....Nilidhani kuwa bado kumbe teyari ......”

    Damaso akadakia na kuuliza teyari kitu gani. Mayasa akajibu,

    “Damaso nimetambua kuwa maisha yangu bila wewe sitaweza kwani wewe ndiye unayetambua matatizo yangu kiundani na upendo wako kwangu ni mkubwa, nilikuwa nakusudia kukuomba msamaha ili niishi na wewe kama mwanzo lakini nimemuona mwanamke na bila shaka huyu ndiye mke wako”

    Damaso akatabasamu sana kisha akamwambia Mayasa kuwa huyo mwanamke sio wake bali ni mwanamke ambaye huwa anamfulia nguo zake na kumlipa. Mayasa akatabasamu baada ya kusikia hilo. Mayasa akamuomba Damaso juu ya kukaa naye tena. Damaso hakuwa na shida kwani hata yeye bado alikuwa na mapenzi ya dhati kwa Mayasa ni matatizo tu ndiyo ambayo yaliwafanya watengane. Kwakuwa walikaa muda mrefu bila kukutana, Damaso alimwambia Mayasa waende kuangalia afya zao. Majibu yalikuwa mazuri kwa kila mmoja.

    Sasa hawakutaka tena kuishi kama washkaji, mipango ya harusi ilifanyika na baada ya mwezi mmoja ,ndoa ilifungwa na watu wakafurahi sana. Maisha yao yakaongezeka furaha kwani baada ya mwaka mmoja tangu wafunge ndoa teyari walikuwa wana mtoto mmoja wa kike. Miaka kumi ilipita wakiwa ndani ya ndoa na familia iliongezeka na kuwa kubwa, sasa watoto walikuwa watatu. Na maisha ya kupanga yalikoma kwani teyari walikuwa wamepata nyumba yao. Japo ilikuwa ngumu lakini siku moja Sunir aliweza kwenda Lindi kuangalia kama anaweza kumuona Mayasa. Sababu ya kufanya hivyo ni mwanaye kuulizia sana kuhusu mama yake. Sunir alipofika Lindi alienda moja kwa moja kwa dada yake Mayasa kumuulizia Mayasa. Dada yake alipata hofu kumwelekeza lakini Sunir alijipambanua kuwa lengo lake ni mwanaye aliyefika naye kumwona mama yake. Dada alimpeleka nyumbani kwa Mayasa. Mayasa alimuona Sunir na mwanaye ,wakaonana na kusalimiana. Mtoto wa Sunir akafurahi kumuona mama yake na Mayasa halikadhalika. Baadae Sunir na mwanaye wakarejea Dar es Salaam na Mayasa naye akaendelea na maisha yake pamoja na mumewe kwa upendo na amani tele.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    *MWISHO*







    Changamoto humfanya mtu kuwa bora zaidi ya alivyokuwa mwanzo, hatupaswi kukata tamaa kwa kila changamoto tutakayokutana nayo,Kikubwa ni kuendelea kumuomba Mungu awe kiongozi wetu siku zote za maisha yetu.

0 comments:

Post a Comment

Blog