Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

SONONEKO - 3

 







    Simulizi : Sononeko

    Sehemu Ya Tatu (3)



    ILIPOISHIA



    Je, hivi yeye aliumbwa kuipata tabu hii ambayo alikuwa akiipata. Hivi hakustahili kuipata furaha katika maisha yake. Je, ni nani wa kuisababisha furaha katika maisha yake?



    Hakika nilikuwa ni mimi. Mwanaume ambaye nilikuwa sijui kupenda ninapopendwa wala kumjali mtu anayenipenda na kunijali.



    SASA ENDELEA



    Aliponiona katika hali ile, Rose aliinuka kutoka pale zuliani alipokuwa ameketi na kuja kitandani nilipokuwa nimelala. Aliniinua na kunilaza katika kifua chake huku akiwa amenikumbatia kwa upendo.



    Nililihisi fukuto la joto lililokuwa likitoka katika kifua chake. Joto hili lilinikumbusha mbali sana hasa nyakati za mwanzo za mapenzi yetu. Dah! Ni miaka mingi nyuma kipindi ambapo penzi letu lilikuwa motomoto. Nilikumbuka mbali sana siku hiyo.

    ***************

    Nilikuwa nimepigika hasa na kupondeka vilivyo. Yaani kama kipigo cha aina ile kingeendelea kwa dakika tano mbele basi ingebaki historia kwamba hapa duniani palikuwa na kibaka mmoja maarufu sana aliyekuwa akiitwa Stanley.



    Ni kweli nilikuwa ni kibaka maarufu sana katika jiji hili la Kano. Nilikwishawahifungwa jela kama mara tatu hivi lakini ilionekana kwamba wizi ilikuwa ni fani ambayo ilikuwa damuni mwangu na kuiacha ilikuwa ni ndoto.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Leo mchana katika mtaa huu wa Downtown nilifanikiwa kukwapua pochi la dada mmoja mrembo ambaye alikuwa akishuka katika gari lake kwa lengo la kwenda madukani kufanya manunuzi.

    Ile anauweka mguu chini, mzee mzima nikawa nimekwishampitia na kumkwapua pochi lake alilokuwa amelishika mkononi.



    Kilikuwa ni kitendo cha haraka sana ambacho hata yeye hakukitegemea. Akili yake ilipokuwa inakaa sawa na kuelewa kwamba alikuwa ameporwa, mimi ndiyo nilikuwa nataka kutokomea kabisa kutoka katika mtaa ule.



    “Mwiziiiiiiiiiiiiiiii! Jamani mwiziiiiiiiii!” Yule dada alipiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa raia wema.



    Watu walikuwa wamekwishaniona na kwa kuwa walikuwa wakinifahamu na walikuwa wamenichoka, walianza kula sahani moja na mimi kwa lengo la kunimaliza kabisa endapo wangenitia mikononi.



    Siku ile ilikuwa ni mbaya sana kwangu kwani wananchi walionesha ushirikiano wa kutosha. Kila mtaa niliokuwa ninakwenda mbele yangu nilkutana na kundi kubwa la wananchi wenye hasira kali. Nikawekwa kati nikiwa sina njia yoyote ya kujiokoa.



    Nikajua leo ndio leo mzee mzima nilikuwa nakufa huku najiona. Na nilifahamu ya kwamba leo lazima ningekaangwa na kiberiti kwani baadhi ya watu niliwaona na matairi ya gari pamoja na vidumu kadhaa vilivyojaa mafuta aina ya petrol.



    Na sikujua vitu hivi vilitafutwa wakati gani. Ama kweli wananchi walikuwa wako chapchap mpaka basi.



    Shughuli ikaanza. Mvua ya kipigo ikaanza kuniangukia kwa ghafla bila hata ya maelezo. Nilipigwa ngumi ya mdomo ambayo iliichanachana kabisa midomo yangu ya juu na chini. Nikashushwa na jiwe la mgongoni ambalo lilinipeleka chini kabisa na kunilaza chali.



    Ukafuatia mguu mzito ambao ulitua kwa nguvu juu ya tumbo langu na kunisababishia maumivu makali sana. Baada ya hapo zikaanza kufuata mvua za bakora, mawe mapanga na kila aina ya silaha.



    Hakika nilichakaa siku ile na hata angelikuja mama yangu mzazi ambaye alinibeba tumboni miezi sita asingeweza kunitambua hata kidogo kwa hali niliyokuwa nayo. Ni kwa kudra za mwenyezi Mungu nilikuwa bado ninaendelea kuishi.



    Ghafla nilisimamishwa na mikono yenye nguvu ya mwananchi mmoja na kisha nikavishwa matairi mawili ya gari huku wananchi wakishabikia na kupiga kelele za kuchochea kwamba nichomwe moto.



    Nikatupwa chini bila ya huruma huku nikiwa nimevishwa yale matairi. Ghafla nikahisi kimiminika kikitua juu ya mwili wangu na kunizidishia maumivu makali kutoka katika majeraha ambayo nilikuwa nimeyapata.



    Harufu ya kimiminika hiki ilinifanya nigundue kwamba yalikuwa ni mafuta aina ya petroli.



    Nilimwomba mwenyezi Mungu anisamehe dhambi zangu zote ambazo nimewahi kuzifanya katika maisha yangu na pia aniepushe kutoka katika harufu hii ya kifo ambayo nilikuwa naivuta kwa sasa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Na pia kimyakimya nilimwahidi mwenyezi Mungu ya kwamba endapo ningepona leo basi wizi kwangu ingekuwa ni historia. Ningeacha kabisa.



    “Jamani naomba mwacheni msimchome moto!” Ilikuwa ni sauti ya mwanamke ambaye alikuwa akishuka katika gari lililofika maeneo yale muda ule.



    Nilijitahidi kuuinua uso wangu na kumtazama yule malaika aliyekuwa akitaka kuninusuru kutoka katika mkono wa mauti.

    Nilishangaa kuona ni yule mwanamke ambaye nilimkwapulia pochi lake. Mh! Mbona ajabu.



    “Haiwezekaniiiiiii! Haiwezekaniiiiii! Huyu ni kibaka mzoefu na huwa anatusumbua sana leo lazima tumpotezeeeee!” wananchi wenye hasira walilalamika kwa kupaza sauti.



    “Jamani ndugu zangu mimi ndiye niliyeibiwa. Kwa adhabu mliyompa sidhani kama atarudia tabia hii ya wizi. Tuwe na ubinadamu basi ndugu zangu kwani huyu ni binadamu mwenzetu”.



    “Msameheni kwani Mungu ameagiza upendo baina yetu”. Aliongea yule dada maneno ambayo yalikuwa ni kweli tupu kwani kwa kipigo nilichokipata pale niliapa kutoirudia tena shughuli hii ya wizi.



    Yaaini ilikuwa ni ajabu kabisa na nilitambua kwamba mwanamke huyu alikuwa ni roho wa Mungu aliyetumwa kuja kunihubiria niache shughuli hii mbaya ya wizi. Alifanikiwa kuwashawishi wananchi wale wenye hasira kali wakaniacha huru.



    Wakasaidiana kunibeba na kunilaza katika viti vya nyuma vya gari la kifahari la dada yule aina ya Toyota “VX”. Akaliwasha gari lile na safari ya kuelekea hospitali ikaanza.



    Kiukweli nilikuwa katika hali mbaya sana na kama ungepita muda wa saa moja bila ya kupata matibabu basi ningeweza kukata roho.

    Kwa takribani ya muda wa dakika kumi na tano tulikuwa tumekwishawasili katika viunga vya Hospitali ya Taifa ya Kano.



    Gari liliwekwa katika maegesho ya hospitali ile na manesi wakaja na vitanda vya kubebea wagonjwa na kunilaza juu yake.



    “Naomba mumsaidie mgonjwa wangu huyu tafadhali” Aliongea yule dada huku akiwa na wasiwasi mkubwa juu ya usalama wa maisha yangu.



    “Ondoa shaka dada yangu kwani hapa amefika katika mikono salama kabisa. Mungu ni mkubwa na atatusaidia kumjaalia mgonjwa afya bora.



    Nilikimbizwa haraka haraka kwa kubururwa juu ya kitanda kile cha kubebea wagonjwa kupelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi. Hali yangu ilikuwa inatisha kwa kweli.



    Baada ya uchunguzi wa kina wa daktari ilionekana kwamba nilitakiwa kufanyiwa upasuaji mdogo wa taya kwani lilikuwa limevunjika.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Na pia ilibidi niongezewe damu kwani majeraha niliyoyapata yalisababisha kupungukiwa na damu kwa kiasi kikubwa. Hii ilitokana na kutokwa na damu kwa wingi toka mahali pa tukio mpaka hapa hospitali.



    Bila ya kuupoteza wakati zaidi nilikimbizwa katika chumba cha upasuaji ambako ulifanyika upasuaji wa kulitengeneza taya langu. Kwa muda wote huo fahamu nilikuwa sina kabisa.

    *********

    “Unaendelea vipi kwa sasa kaka yangu?” Aliniuliza yule dada baada ya wiki moja ya matibabu pale hospitalini pindi alipokuja kunitembelea.



    “Kwa sasa naendelea vyema kabisa na daktari ameniambia kwamba kama hali itaendelea hivi hivi basi ndani ya siku tano zijazo nitaruhusiwa kurudi nyumbani”. Nilimjibu yule dada mfadhili na mwokozi wa uhai wangu huku nikiwa na aibu kubwa sana kutokana na kitendo ambacho nilimfanyia siku zile.



    “Ninaitwa Rose Bisenga, sijui mwenzangu waitwa nani?” Yule dada kwa mara ya kwanza alijitambulisha kwangu baada ya kuona hali yangu imetengamaa kidogo kwa kufanya mazungumzo mafupi hata ya utambulisho tu.



    “Mimi ninaitwa Stanley”. Nilimjibu Rose huku aibu ikiwa bado haibanduki usoni mwangu kwa sababu mambo niliyomfanyia kwa kweli yaliniumbua.



    “Nafurahi kuona hali yako ikitengamaa vyema, mungu ni mkubwa na atajalia iendelee kuimarika zaidi”. Rose aliongea kwa kunifariji.



    “Nashukuru sana dada Rose kwa moyo wako wa huruma na hisani. Mungu azidi kukushushia baraka”. Nilimwambia Rose maneno ambayo yalitoka katika uvungu wa moyo wangu.



    “Usijali kwani ni kawaida kwa binadamu kufadhiliana”. Alinijibu kwa sauti tamu na nyororo iliyoyakuna masikio yangu na kunipa faraja.



    “Lakini ni binadamu wachache sana wenye moyo wa fadhila kama wako hasa kwa mambo maovu ambayo nilikutendea”. Niliongea kwa sauti yenye majuto ndani yake.



    “Usijali na jisikie huru kabisa”. Rose alijibu.

    ***************





    “Hizi ni dawa ambazo utahakikisha anakunywa kila siku. Hii utampa kutwa mara tatu nah ii nyingine ni kutwa mara moja. Hii ya maji utahakikisha anaipata kutwa mara mbili. Baada ya mwezi hakikisha unamrudisha hapa hospitali kwa minajili ya kumchunguza afya yake”.



    “Pia kama kutatokea mabadiliko yoyote ya afya yake usisite kumleta hapa hospitali. Nawatakia kila la kheri”. Daktari alikuwa akimpa maagizo Rose mara baada ya mimi kuruhusiwa kutoka pale hospitali.



    “Nashukuru sana dokta kwa msaada mkubwa ambao mmetupatia katika kuifanya afya ya ndugu yangu kutengamaa. Mungu awabariki sana na kuwazidishia katika kila mlifanyalo”.



    “Usijali dada yangu na unakaribishwa hapa kwa wakati mwingine tena kwa msaada wowote wa kitabibu”. Aliongea daktari yule wa kiume ambaye ndiye aliyenishughulikia katika kuupigania uhai wangu usiniponyeke kutokana na majeraha niliyoyapata siku ile ya kipigo.



    “Ahsante sana”. Aliongea Rose huku akija katika kitanda nilichokuwepo na kunisaidia kuinuka.



    “Twende zetu Stanley kwani tumekwishaipata rukhsa ya daktari”. Aliongea Rose huku akinikongoja kuelekea katika mlango wa wadi ile ambayo nililazwam mlango ambao ulitutoa nje kabisa.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kule nje nilikongojwa kuelekea katika maegesho ya magari ambako Rose alinipeleka mpaka ambako alipaki gari lake la kifahari aina ya V8.



    Niliingizwa ndani ya gari lile mara baada ya kufunguliwa mlango huku nikisindikizwa na sauti tamu ya mrembo yule, “Pole sana Stanley”.



    “Ahsante sana dada Rose. Sielewi hata namna ya kukushukuru kwa ukarimu wako kwani nilikwishachungulia kabu……” Nilikatizwa kauli yangu na sauti ya Rose huku akiwa amekiweka kidole chake kimoja mdomoni.



    “Shiiiiiiiiiiiiiiiii! Nilikwishakukataza Stanley. Nilikwambia wala usiwaze kwa hili kwani binadamu yeyote anaweza kulitenda hili katika kipindi kile kutokana na hali uliyokuwa nayo”. Aliongea Rose.



    Aliliwasha gari na kisha akalirudisha nyuma. Baada ya kupata nafasi nzuri akaingiza gia ambayo ililifanya gari lianze kusonga mbele na kutuondoa kutoka katika majengo yale ya hospitali.



    “Sasa inakuwaje? Nyumbani kwako ni wapi?”. Rose aliniuliza swali ambalo lilikuwa ni tata kwangu kwani katika miaka yote mingi niliyoishi katika jiji hili sijawahi kuwa na mahali ambapo nitapaita ni nyumbani.



    “Mh! Mimi nyumbani kwangu ni popote!” Nilimjibu Rose jibu ambalo lilimchanganya kabisa kwani hakuelewa ni nini nilikuwa namaanisha kwa kusema vile.



    “He! Una maana gani Stanley, mbona sikuelewi?” Aliuliza Rose huku akiibadili gia ya lile V8.



    “Ni historia ndefu sana dada Rose. Mimi sijawahi kuwa na nyumba. Maisha yangu yote nimekuwa nikiyaendesha kwa kulala katika mabaraza ya majumba ya watu na maduka pia”.



    “Sijawahi kuwa na kazi muhimu zaidi ya hii ya uporaji ambayo mara nyingi imekuwa ikinipa matatizo makubwa kama hili ambalo nimelipata sasa”. Niliongea huku machozi yakinitiririka.



    Maneno yale yalimchoma sana Rose ambaye alishikwa na huzuni ambayo ilionekana katika macho yake.



    Alipunguza mwendo wa gari na kulipaki pembeni.



    “Pole sana Stanley. Naweza kukuuliza swali moja zaidi kama hutajali” Aliongea Rose huku akinitazama usoni.



    “Uliza tu Rose wala usiwe na wasiwasi”. Nilimjibu Rose huku nikiwa ninayakwepesha macho yangu kwa soni.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hivi kwa nini siku ile ulinipora mkoba wangu?” Lilikuwa ni swali ambalo hata sikulitegemea kutoka kwa dada huyu. Nilihisi anaweza kunipeleka polisi.



    “Nisamehe dada yangu usinipeleke polisi kwani nitakufa mimi. Ni maisha magumu ndiyo yaliyonisababisha nikuibie dada yangu kwani siku ile nilikuwa na njaa ya kutokula kwa muda wa siku mbili”.



    “Nihurumie sana dada yangu. Nimekosa mimi na sitarudia”. Niliyatapika yote yaliyokuwa moyoni mwangu kwa lengo la kumshawishi Rose asinipeleke polisi.



    Kwa kweli leo hii niliyajutia matendo yangu na kuapa mbele za Mungu kwamba nitaacha wizi na sitarudia tena. Nilipiga magoti ndani ya lile gari huku nikimwomba radhi Rose.



    Rose alijisikia huzuni sana kwa yale aliyokuwa akiyasikia kutoka kwangu. Moyo wake ulimuuma kwa shida ambazo nilikuwa nikikumbana nazo maishani.



    “Stanley mimi nilikwisha kusamehe na ndiyo maana waniona niko hapa mpaka leo. Nahitaji kukusaidia Stanley. Je, wasemaje?” Aliongea Rose



    Unajua kwa takribani sekunde kama nane hivi sikuweza kuamini masikio yangu kile ambacho yalikuwa yakikisikia. Kunisaidia? Mimi Stanley? Niliamini usemi wa wahenga usemao Mungu hamtupi mja wake.



    “Dada yangu siamini masikio yangu. Kwa muda mrefu nimekuwa ni adui wa binadamu wote kutokana na matendo yangu. Nahisi wewe ni malaika uliyetumwa na Mungu kwani toka umeniokoa kutoka katika kifo siku ile nimeamini kwamba Mungu yupo”.



    “Ninashukuru sana dada yangu kwa msaada wako lakini nahisi nitakuwa mzigo kwako kutokana na historia ya maisha yangu ya wizi”. Niliongea maneno ambayo yalitoka moyoni mwangu kabisa.



    “Hapana Stanley. Kamwe huwezi kuwa mzigo kwangu. Ninao uwezo wa kukusaidia. Pia sina hofu na wewe kwani najua kwa sasa umejirekebisha na yaliyopita yatabaki kuwa historia. Mungu ni mkubwa na daima anatenda. Acha nikusaidie Stanley”. Aliongea Rose huku akiliwasha gari lake na kushika barabara kuu.



    Safari yetu ikaendelea.



    Hatua ya kwanza ya safari yetu ilikuwa ni kwenye maduka ya kifahari ya nguo. Huko nilinunuliwa nguo nyingi na za gharama za juu ambazo sikuwahi kuota kwamba nami katika maisha yangu nitakuja kuzivaa katika mwili wangu ukiachilia mbali kuzijaribu tu.



    Nikanunuliwa viatu jozi nne ambavyo vilikuwa na thamani ya juu sana. Ama kweli nyota ya jaha iliniangukia siku ile.



    Baada ya hapo nilipelekwa katika saluni ya kisasa ambako nilirekebishwa nywele ambazo hapo awali zilikuwa shaghalabaghala huku zikiwa zimenyolewa sehemu iliyokuwa na jeraha tu.

    *************

    “Karibu sana Stanley hapa ndipo nyumbani kwangu”. Nilikaribishwa na Rose katika jumba moja kubwa sana la kifahari ambalo lilikuwa ni mithili ya yale ambayo huwa tunayaona katika filamu za kizungu.



    “Dah! Humu ndimo unamoishi dada Rose? Aiseh! Ni kuzuri sana”. Niliongea nikionekana wazi nikiwa ni mshamba wa kutupwa.



    Na hiyo ilikuwa ni hali halisi licha ya kuishi katika jiji hili la Kano lakini sikuwahi kuingia katika majengo ya namna hii zaidi ya kuyaangalia kwa nje na kwenye picha labda.



    “Ahsante na hapa ndipo utakapokuwa unaishi Stanley. Uwe huru sana kwani mimi ninaishi peke yangu pamoja na watumishi wawili tu wa ndani”. Aliongea Rose kwa sauti yake ile ile ya upole na tamu kuisikiliza masikioni.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ahsante sana dada Rose sijui nitakulipa nini kwa unayonitendea. Mungu akubariki sana dada”. Niliongea nikimaanisha nilichokuwa nikikiongea.

    *****************

    Kwa kweli toka wakati ule nilikuwa siamini kile ambacho kilikuwa kinanitokea. Yaani mimi Stanley, fukara wa kutupwa ambaye nilikuwa sina hata hakika ya kupata mlo kwa siku kuishi maisha ya kifahari namna ile katika lile kasri la kifahari?



    Ama kweli mwenyezi Mungu hamtupi mja wake. Usemi huu ulikuwa ni kweli tupu isiyo na shaka hata kidogo.



    Sasa niliyaona kabisa maisha yakianza kuninyookea. Sasa nami nilianza kuyaonja maisha ambayo watu wengine walikuwa wakiyaishi na kuyaona ni ya kawaida kabisa wakati kwa wengine ilikuwa ni ndoto hata kuyanusa maisha ya namna hii. Ama kweli binadamu hatufanani.



    Sasa nilimwona Rose kwamba alikuwa ni malaika ambaye alitumwa na Mungu kuja kunikomboa katika lindi la umasikini ambamo niliuwa nimetopea. Hakika kilio changu sasa kilikuwa kimesikika kwa jalali.



    Siku zilizidi kukatika kama upepo vile huku mimi nikiendelea kuyatafuna maisha ya kifahari katika kasri lile la kifahari la Rose.



    Nilikuwa nikiishi kama mfalme huku Rose akiwa ananijali sana na kunifanya nisahau maisha ya tabu na umasikini ambayo nilikuwa nimeishi kwa muda mrefu sana tangu utoto wangu.



    Kila ambacho nilikihitaji basi Rose alinitimizia bila ya kinyongo. Maisha yalikuwa ya raha sana kwa upande wangu kwani nilinawiri sana.



    Kwa sasa nilionekana ni mwanaume nadhifu sana na mwenye mvuto wa pekee machoni pa wengi. Sikuwa Stanley yule wa kipindi kile ambaye alikuwa ni kibaka maarufu hapa jijini Kano na kuchukiwa na wengi.



    Wakazi wengi wa jiji la Kano walinishangaa sana kwa hali ambayo nilikuwa nayo kwa sasa. Hawakupenda kuyaamini macho yao. Waliamini kwamba kila binadamu ana bahati yake.



    Rose alinichukua na kuniweka katika moja ya kampuni yake ya uuzaji wa vipuri vya magari. Hii ilikuwa ni baada ya kuridhika nami kwamba nilikuwa nimebadilika tabia na ningemudu kusaidia katika kampuni yake.



    Nami sikutaka kumwangusha mfadhili wangu huyu hata kidogo. Niliamua kuchapa kazi vilivyo mpaka yeye mwenyewe alifurahi sana.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sikuyapenda kabisa maisha ya kifukara ambayo nilikuwa nikiishi hapo awali. Maisha yale yalikuwa si mazuri. Ni maisha ambayo sidhani kama kuna mtu yeyote pia ambaye anapenda kuyaishi. Sikupenda kurudi huko kamwe.

    ****************



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog