Simulizi : Mvua Ya Huba
Sehemu Ya Nne (4)
Wakati Mwenda akiongea hayo hali ya Lukoha ikabadirika akahisi baridi kali mno iliyomfanya atetemeke mwili mzima. Mwenda akaongeza kuni lakini haikufaa kitu, njia iliyobaki ni kumkaribia Zaidi Lukoha na kumkumbatia ili kuruhusu joto la mwili wake limsaidie. Mwili wa Mwenda ukasisimka kuliko kawaida kwani alilikumbuka vyema kumbatio la mumewe ambalo halikuwa tofauti na hilo alilomkumbatia Lukoha.
“Tulia hivi hadi baridi litakapopungua” alisema Mwenda.
“Malkia wangu kwa nini wafanya yote haya kwa mtumishi wako” alisema Lukoha.
“Umeyaokoa maisha yangu na ni wakati wangu wa kulipa fadhira,” alijibu Mwenda.
Lukoha alijikuta akihisi hali ya tofauti kwa mara ya kwanza kwani katika maisha yake yote hakuwahi kukumbatiwa vile, alichozoea yeye ni kushika jambia au upinde na mshale kupambana na maadui na hata wanyama wakali waliotaka kusababisha madhara. Akaipenda hali ile naye akanyanyua mikono yake bila kuelewa akashikilia kiuno cha Mwenda, Mwenda akashtuka kidogo na wakajikuta wakitazamana bila kusemeshana. Nyoyo zao zikavurugika mithili ya kimbunga na kufanya waheme kuliko kawaida,
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nafikiri sumu imeathiri mfumo wangu wa upumuaji kwanini moyo unadunda hivi?” alisema Lukoha ambaye hakujua kuwa hali ile ilitokea kwa sababu ya sumaku ya huba iliyoanza kuwavuta wawili wale.
“Natamani sumu hii ikuue kabisa nami niwe mtu pekee wa kukuzika” alisema mwenda ambaye alishajua kuwa sumu ile si ya nyoka ila ya huba.
Lukoha alishtuka sana kusikia kauli ile toka kwa malkia huyo, hakuelewa hasa nini kilimaanishwa toka katika sentensi hiyo.
“Malkia wangu usinichoke haraka hivyo hadi kutamani nife, bado nina deni la kukulinda,” alisema Lukoha.
Mwenda akatabsamu na kumuangalia Lukoha kwa macho maregevu Zaidi ambayo bado yalizidi kumduwaza Lukoha.
“Hivi ushawahi kumpenda mtu na kutokutamani hasitoweke mbele ya upeo wa macho na fahamu zako?”
“Ndiyo”
“Unaweza kuniambia kuwa mtu huyo alikuwa ni wa namna gani?”
“Kwangu mtu niliyempenda na kutotamani kumpoteza ni chifu Lukemo pekee, baada ya wazazi wangu kuchukuliwa na kuangamizwa na wajerumani yeye pekee ndiye aliyekuwa kila kitu kwangu”
Mwenda alishtuka kidogo kusikia habari ya wazazi wa Lukoha kufariki, akajiuliza kama kuna uhusiano wowote wa maisha yajao na maisha yaliyopita. Kama katika dunia ile ya karne ya 21 wazazi wake wanaishi je na yeye haishi je si sawa katika dunia hii kuwa wazazi wake bado wanaishi, hakutaka kusema lolote juu ya hilo. Akarudi katika mada yake ya msingi,
“Pole kwa yaliyokukuta ila swali langu lilikuwa na shabaha ya kumpenda mtu wa jinsia kama yangu na kutamani kujenga naye familia”
“Hilo bado halijatokea kwangu”
Usiku ule wakaongea mengi sana huku wakiwa bado wamekumbatiana hamna aliyekuwa tayari kumuachia mwenzie.
BAADA YA SIKU TATU
Mambo hayakuwa shwari kwa Sanzani kwani chifu Majariwa alishafika na kupewa taarifa juu ya kurithishwa mke wa kaka yake. Alifurahi sana na akatamani amuone huyo mke wake, watu wakaagizwa kumwita Mwenda lakini hawakumuona, na hapo ndipo taarifa ya Lukoha kutoroka na Mwenda ikaenea Sanzani nzima. Watu wengi wakahojiwa na wote wakatoa jibu kuwa siku 6 zilizopita waliwaona wawili hao wakitoka na kufata njia iliyoelekea kwa mama yake Mwenda.
Chifu Ng’arika hakuamini kama Lukoha anaweza kufanya hilo jambo la kutoroka na Mwenda akaagiza askari na watu wote wa Sanzani kutoa taharifa endapo watawaona wawili hao. Hadi siku ya sita inaingia hakuna aliyefanikiwa kugundua kuwa wawili hao wametokomea wapi, Chifu Ng’arika akaita kikao cha dhalura kilichowahusisha wazee, washauri na viongozi wa ibada za mizimu.
“Ndugu zangu Lukoha amefaya jambo moja la aibu sana katika Sanzani yetu yeye si wa kutoroka na mke wa chifu, nimewaita hapa ili tushauriane tufanye nini juu ya hawa wawili” alisema chifu.
“Chifu mtukufu! Hamna adhabu inayowastahili hao tofauti na kifo maana wamevunja miiko ya mizimu na hata tamaduni zetu za Sanzani,” alisema mzee mmoja na wenzake wote kumuunga mkono.
“Sasa natoa agizo popote atakapoonekana Lukoha na huyo Mwenda wapigwe mpaka kuuawa na vichwa vyao viletwe hapa,” alisema chifu Ng’arika kwa jazba mno.
“Hapana chifu! Mimi nafikiri wakamatwe wakiwa wazima na adhabu hiyo ifanyike hapa adharani ili kila mmoja ajifunze na hasifikirie kurudia upuuzi huu” aliongea kiongozi mmoja wa ibada za mizimu.
Balaza likaridhia na chifu akatoa amri hiyo mpya kwa askari na watu wote ambao wakaahidiwa zawadi na cheo kikubwa katika utawala wa Sanzani endapo watafanikisha kuwapata wawili hao.
*************
Lukoha na Mwenda wakajikuta wakizoeana sana kwa wakati huo mfupi na hawakujua lolote linaloendelea,
“Nafikiri sasa tunaweza kuondoka” alisema Lukoha baada ya kuridhika juu ya afya yake.
“Sawa ila sijajua hapa tupo katika milki ipi na tunaanzia wapi safari yetu” alisema Mwenda.
Lukoha akamtaka Mwenda asubiri kidogo kisha yeye akatoka kufanya uchunguzi akatembea Zaidi na kukutana na kundi kubwa la watu, akasimama na kuwasalimu kwa heshima,
“Habari za muda huu”
“Njema japo sio sana”
“Vipi umekumbwa na matatizo yeyote mtokapo?” aliuliza Lukoha.
“Aah! Kuna mpuuzi mmoja huko Sanzani inasemekana amtoroka na mke wa chifu, hivyo askari wapo kila kona wakiwasaka na sisi tumezuiliwa kuingia Sanzani ndiyo tunarejea kwetu biashara imeshindikana”
Lukoha akashtuka sana hakuamini kama mambo yanaweza kuwa magumu kiasi kile, akaendelea kuwahoji,
“Mhmh! Wanauhakika gani kama kweli huyo mtu ametoroka na mke wa chifu?”
“Wewe kijana una maswali ya maudhi kweli nenda mwenyewe ukajionee watu wote wapo msituni maana atakayefanikiwa kuwapata atapewa zawadi na cheo kikubwa katika milki ya sanzani”
“Kweli itabidi na mimi nianze kuwasaka hao watu maana zawadi na cheo sio kitu kidogo” alisema Lukoha ili hasiweze kugundulika kwa wafanya biashara wale.
“Haya juhudi zako ndiyo mafanikio yako” alijibu mmoja kati ya wafanyabiashara wale.
“Na watu hao watapata adhabu gani?”
“Kifo ndiyo halali yao”
Jibu hilo lilimuogopesha sana Lukoha akageuka na kukimbia kurejea kule alipomuacha Mwenda, alipofika akakuta mazingira yakiwa kimya mno, akaishangaa ile hali akamwita Mwenda lakini hakuitika. Wakati akiendelea kumtafuta Mwenda akahisi kupigwa na kitu kizito kichwani kisha akaanguka chini na kupoteza fahamu.
******************
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lukoha aliporejewa na fahamu akajikuta amefungwa kamba miguuni na mikononi, hakuwa na shaka Zaidi ya kujua kuwa tayari alishakamatwa na askari wa jeshi la Sanzani, lakini kila alipoiangalia hiyo sehemu hakuwa anaielewa. Muda mfupi baadae akaja kijana mmoja ambaye alionekana kutoka katika familia ya daraja la juu akatoa amri kwa askari walio eneo hilo kuwa afunguliwe na apelekwe mbele ya chifu. Lukoha akafunikwa uso kwa kitambaa cheusi kisha akapelekwa sehemu aliyokusudiwa kufikishwa,
“Mtukufu chifu tumewakamata wawili hawa wakiwa katika pango la hazina ya milki hii, nafikiri uhenda wakawa ni maadui walioagizwa kuja kuchunguza siri zetu, naomba adhabu kali itolewe juu yao,” alisema kijana yule ambaye mara ya kwanza alitoa amri juu ya kufunguliwa kwa Lukoha na kupelekwa eneo hilo.
Chifu akasimama kisha akakohoa na kutazama watu wote waliokusanyika mahala hapo, akashuka toka sehemu iliyo juu na kusogea hadi alipo Lukoha. Mwenda alipata nafasi ya kumtazama vizuri chifu yule, sura yake haikuwa ngeni kabisa akajaribu kukumbuka ni wapi hasa alipoiona sura ile hakuweza kukumbuka.
“Katika tawala hii ya Uchindile ni mwiko sana kutoa siri ya hazina, bila shaka wananchi wote mnaelewa hili, ninapowatazama wawili hawa ni wazi si wenyeji wa mahala hapa na sina shaka juu ya hawa kuwa wapelelezi. Adhabu yangu ni moja tuu dawa ya adui…”
“Ni kifo” waliitikia watu wote.
Lukoha akafungwa mikono yake nyuma kisha akasogezwa katika shimo moja lenye nyoka wenye sumu kali ambalo lilitumika kutoa adhabu kwa wote waliohukumiwa kifo. Mwenda akafikiri namna ya kumsaidia hakuipata akawaza tena na kumbukumbu ikampeleka hadi katika dunia ile ya 2017 ambapo sura ya chifu Mtambala ilifanana kabisa na sura ya baba yake Lucas, Mwenda akajikuta akipaza sauti na kumuita chifu. Chifu akageuka na kusogea alipo Mwenda, akashuhudia machozi yakidondoka toka kwa binti huyo,
“Huwezi kutufanyia ukatili huu bila ya kutupa nafasi ya kujieleza” alisema Mwenda.
“Wewe ni nani hasa” aliuliza chifu.
“Ukitaka kujua kuhusu mimi zuia hilo uliloamuru lifanyike maana unaweza kuja kujijutia maisha yako yote”
“Unanitisha?”
“Sikutishi ila nakuomba simamisha kwanza hilo jambo kwanza hauna ushahidi wa kutosha wa kututia sisi hatiani” alisema Mwenda.
“Unawezaje kumjibu chifu wetu hivyo, naye adhabu yake ni kifo msogezeni kwenye shimo la mauti,” alisema kijana yule ambaye bado utambulisho wake haukufahamika kwa wakati huo.
“Hapana mwacheni! Anaonekana ni msichana wa tofauti kidogo”
“Chifu Mtambala sifa zako zimeenea ndani na hata nje ya mipaka ya Uchindile, sisi ni watu wa Sanzani bado maamuzi yako yana walakini”
Chifu alishtuka sana aliposikia kuwa watu wale wametokea Sanzani, akarudi nyuma na akatoa amri Lukoha asitumbukizwe kwenye shimo lile la mauti nao wakatii.
“Kiongozi wa mahusiano ya nje unataharifa gani kutoka Sanzani” aliuliza Chifu.
“Tumepokea taharifa kuwa aliyekuwa mlinzi wa marehemu chifu Lukemo ametoroka na mke wa chifu hivyo Sanzani kwa sasa haijatulia askari wapo kila kona kuwasaka wasaliti hao na kuwafikisha mbele ya chifu ili kupokea adhabu yao” alisema kiongozi huyo aliyohusika katika maswala ya mahusiano ya tawala na milki za jirani.
Kauli hiyo ikamshtua Mwenda kwani hakuwa anajua hilo jambo, akajikuta akikaa chini bila kupenda chifu akapata jibu la moja kwa moja kuwa watu wanaotafutwa ni hao wawili.
“Chui akijivika ngozi ya kondoo atabaki kuwa chui na kamwe hawezi kuwa kondoo hata iweje, sasa nimegundua kuwa wawili nyie ni wasaliti hivyo itapendeza Zaidi kama nitawarejesha Sanzani” alisema chifu.
“Huwezi kufanya hivyo kwa mtoto wako!” Mwenda alijikuta akisema bila kutarajia.
Chifu Mtambala akashangaa juu ya lile maana ni kweli alipotezana na mtoto wake miaka mingi iliyopita, kwa haraka sana akasogea alipo Lukoha na kumvua kitambaa kile, hakuyaamini macho yake alipomuona kijana huyo.
“Lukoha…!”
“Baba..!”
Chifu akasahau kama yupo katika mkusanyiko mkubwa wa watu waliokuwa wakiisubiri hukumu ya wawili wale. Msaidizi wa chifu alipoona hali ile ikabidi asimame na kuwataka watu watawanyike kurejea majumbani kwao na kitakachojiri watataharifiwa. Watu wakatii na kutawanyika japo minong’ono ya chinichini iliendelea.
*********
“Nasikia kijana yule ametoroka na mke wa chifu wa Sanzani”
“Wewe hata mimi nimelisikia hilo sasa kwanini chifu abadili maamuzi”
“Mimi najua sababu ya chifu kubadili maamuzi”
“Tuambie sababu ni nini”
“Kijana yule ni mtoto wa pili wa chifu Mtambala ambaye alipotezana naye miaka mingi iliyopita”
“Wewe unasema ukweli?”
“Ndiyo hivyo ila kwa usalama wetu ni vyema haya mambo yakaishia hapa”
Yalikuwa maongezi kati ya wakulima waliokutana njiani baada ya kumaliza shughuli zao za shambani na kurejea majumbani mwao.
Jioni ya siku hiyo chifu Mtambala akatenga muda wake kukaa na familia yake yote, wote wakakusanyika isipokuwa mama yake.
“Baba mbona mama simuoni?”
“Mwanangu mama yako yupo, kwa sasa kuna mambo anayashughulikia na atakuwa nje ya Uchindile kwa muda wa juma moja”
“Nina hamu sana ya kuonana naye”
“Utamuona vuta subira kidogo”
“Sawa baba” akajibu Lukoha.
Chifu Mtambala akatoa utambulisho kwa ndugu zake wengine waliopo hapo nao wakafurahi kuungana na ndugu yao huyo ambao hawakuwa wakimfahamu. Chifu Mtambala anajumla ya wake 6 na watoto 22 huku wakiume wakiwa 8 na wakike wakiwa 14. Kama ilivyo katika tawala nyingi za kipindi hiko kila mke alikuwa na kaya yake hivyo Lukoha yeye alikuwa ni mtoto wa pili kwa mke wa kwanza wa chifu Mtambala.
“Natamani kufahamu Zaidi kuhusu binti huyu, maana kila nikimtazama naona ni watofauti sana” alisema chifu Mtambala.
Lukoha akamuelezea baba yake kila kitu kuhusu Mwenda kuanzia siku ya kwanza waliponana, jinsi walivyosaidiana hadi kufika mahala hapo.
“Mwanangu binti huyu anafaa kuwa mke wako” alisema Chifu Mtambala baada ya kusikia simulizi ya Lukoha.
“Mhmh! Baba unalolizungumza haliwezekani hata kidogo mimi ni kama mtumishi wake naye ni malkia kwangu”
“Lukoha amini husiamini wawili ninyi mnapendana na sio dhambi kama mtaweka wazi hisia zenu, baba yako sasa nina nguvu naweza kukuunga mkono kwa lolote lile, nikotayari kutuma watu Sanzani ili kuwepo mazungumzo ya Amani na kuwaruuhusu wawili ninyi kuwa pamoja” alisema baba yake na Lukoha.
“Baba nayatamani hayo yote unayoyasema ila sijajua moyo wa Mwenda unawaza nini”
“Usiku wa leo usipite bila kuweka wazi hisia zako kwako”
Lukoha akaridhia na kutoka alipo baba yake moja kwa moja hadi katika chumba alichopo Mwenda, akabisha hodi na baada ya muda mfupi akaruhusiwa kuingia ndani. Lukoha akapatwa na kigugumizi macho yake yalipotua kwa Mwenda, hakujua atamke neno gani.
“Mhmh! Kweli wenye ndoa wanakazi kweli yaani ndio maana machifu wanatumia amri, naanzaje sasa kumwambia” alijiuliza Lukoha.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mwenda akabaki akimtazama Lukoha na kutabasamu kwani jinsi alivyokuwa akibabaika alishagundua nini kusudio la moyo wa Lukoha. Akamsogelea na kumkumbatia kisha akamwambia,
“Usiogope sema nakusikiliza”
“Malkia wangu! Mimi nina……” Lukoha alishindwa kumalizia kauli yake.
“Huna haja ya kusema lolote, kuku ni wako ya nini kumshikia manati wewe ni mume wangu hata katika maisha yajao”
“Asante kwa kuufunza moyo wangu kudunda, nimeelewa maana halisi ya mapenzi, sitamani kukupoteza hata kwa sekunde chache, natumai tutahalalishwa na kuishi kama mke na mume,” alisema Lukoha.
**************
Msafara wa wajumbe wa chifu Mtambala kuelekea Sanzani ili kuomba uhalali juu ya Mwenda na Lukoha ukawasili na kupokelewa na chifu Ng’arika. Ombi lile likasemwa pindi tu balaza la wazee na viongozi wa ibada walipowasili. Ghazabu kuu ikamshika chifu Ng’arika na kuona kuwa amedharaulika.
“Nilikuwa nikimuheshimu chifu Mtambala kwa miaka mingi sana lakini swala hili la kuwataka watuhumiwa wetu siwezi kulikubali” alisema chifu.
“Mtukufu chifu, mtawala wetu hajawahi kumdharau yeyote awe mkubwa au mdogo, ila yeye upenda kumsikiliza kila mmoja na kuheshimu mawazo yao. Hii inamfanya kuwa mtawala wa kipekee katika ukanda huu wa mashariki, kwetu ndoa hufanyika kwa wawili walioridhiana japo katika ardhi hii ni tofauti”
“Basi..! ishia hapo hapo nyie ni wakina nani hasa hadi mkosoe miiko yetu, je mmekuja kuitukana mizimu ya Sanzani? Ninauwezo wa kuwaua hapa hapa na nisipate lawama. Nakutuma kwa huyo mpuuzi mwenzio mwambie nahitaji watuhumiwa wangu hapa tofauti na hapo sitosita kutangaza vita na nina uhakika nitawaamgamiza na kuichukua Uchindile kuwa katika Milki ya Sanzani” alisema chifu Ng’arika kwa jazba sana.
Balaza likalipuka kwa minong’ono wapo waliomuunga mkono chifu na wapo wachache waliopingana naye japo hawakuwa na ujasiri wa kuzungumza. Mjumbe wa chifu Mtambala akapiga magoti na kuinama ishara ya kusujudu ili kutoa heshima kwa chifu Ng’arika kisha akageuka na kuondoka eneo hilo.
Huku nyuma majadiliano kati ya chifu na balaza lake yakaendelea, kiukweli chifu alikasirishwa mno, hakutaka kubadili maamuzi yake.
“Kama juma moja litapita bila watuhumiwa hao kuletwa hapa, nitaliongoza jeshi na kuiangamiza uchindile yote,” alisema Ng’arika.
“Mtukufu chifu nafikiri si busara kutumia nguvu kuliko hekima, tuvute subira na tusikilizane vita inamatokeo hasi hata kama tutashinda lakini bado tutakuwa tumepoteza nguvu na kumbuka wajerumani bado wanatuwinda” alisema mzee mmoja.
Kauli hiyo ikamfanya chifu Ng’arika avute upinde uliokuwa na mshale akauachia na kulenga sehemu ya moyo ya mzee huyo, papo hapo akaanguka na kupoteza maisha. Toka kujengwa kwa misingi ya Sanzani hakukuwahi kutokea jambo hilo kila mmoja alimshangaa sana chifu Ng’arika,
“Kuanzia leo kauli yangu itakuwa ya mwisho sitaki tena kusikia matusi na yeyote atakayenipinga atafata njia yam zee huyo” alisema Ng’arika na kuondoka eneo hilo.
“Jamani hili lililofanyika hapa naomba libaki kuwa siri, tukilipeleka kwa wananchi tutapata wakati mgumu Zaidi” alisema mshauri mkuu wa chifu.
“Tutaieleza vipi familia yam zee huyu? Unayajua maumivu ya kuondokea na mtu unayempenda na kumthamini? Mzee huyu ana mke, watoto na wajukuu ambao wamezoea kumuona leo tutawaambia kipenzi chao hakipo duniani je tutawatajia sababu gani?” aliuliza mzee mwingine.
“Kwa sasa tusiongee lolote na wakiwauliza waambieni ameagizwa kwa tawala jirani kushughulikia mambo nyeti walau kutokea hapo tutakuwa na la kuongea”
Balaza likakubaliana hivyo kisha kila mtu akaondoka na kurejea katika shughuli zake za kila siku.
**************
“Nauona mwisho wa Sanzani kama Mwenda atarejea hapa, binti huyu ni kama moto ukiutumia vyema uleta faida na ukiutumia vibaya husababisha madhara. Namna pekee ya Sanzani kubaki salama ni kumuachia binti huyu aende” alisema Kiongozi wa ibada ya mizimu pia alikuwa mtaalamu wa maswala ya unajimu.
“Unafikiri kwa nini chifu aliamua kufanya jambo lile?” aliuliza mnajimu msaidizi.
“Chifu hakutaka kuonekana dhaifu mbele ya baba ya watu wake ukizingatia ndio kwanza ameingia katika utawala na amefanya hivi ili kujenga Imani kwa chifu Majariwa”
“Nini hatima ya haya yote?”
“Hatima ni kupotea kwa Sanzani kwa maana wawili wale wananyota kali na zenye ushawishi mkubwa mno, kitendo cha kuwaadhibu kitaigawa Sanzani katika makundi mawili na kudhoofisha ulinzi wetu, hiyo itakuwa fursa kwa vibaraka wa wajerumani kufanya kazi yao na mwisho kuleta maafa”
“Nini sasa kifanyike?”
“Tunatakiwa tumzuie chifu Ng’arika kufanya alichokusudia maana tukio la kumwaga damu isiyo na hatia limewaghazibisha mizimu”
Wanajimu hao waliamua kupeleka mawazo yao kwa wazee wengine hili waone ni kwa namna gani wanaweza kuikoa hatima ya Sanzani. Kweli wawili wanaopendana wanapoungana hata Mungu mwenyewe husimama katikati yao.
Taarifa za kukataliwa kwa ombi la kuharalisha uhusiano kati ya Lukoha na Mwenda ikamfikia chifu Mtambala akahuzunika sana kushindwa jambo lile.
“Na amesema kama watuhumiwa hawa hawatafikishwa Sanzani basi ni sawa na sisi kutangaza vita naye” alisema Kibaraka aliyetumwa Sanzani.
“Sikuwahi kufikiria kama Ng’arika ni mpumbavu kiasi hiki, hatuna cha kupoteza endapo vita ikitokea ila bado hatuna sababu ya kumwaga damu zisizo na hatia. Na hii itakuwa nafasi ya pekee kwa wajerumani kuteka milki zetu ili kuzuia hayo yote nitawarudisha wawili hawa Sanzani naamini watapata namna ya kujitetea” alisema Chifu Mtambala.
“Hapana chifu kufanya hivyo ni sawa na kuwatengenezea kaburi, tusikubaliane na matakwa ya chifu Ng’arika” alisema mzee mmoja ambaye naye alikuwa na nafasi ya juu katika maamuzi yahusuyo Uchindile.
“Najua ukomavu na udhaifu wa Sanzani, toka nikiwa mdogo nimekuzwa kuwa mlinzi hodari wa milki ile, hamna kitakachonikuta naungana na wazo la mtukufu Chifu na nawaahidi nitarejea na mke wangu” alisema Lukoha.
Wazee wote waliupenda ujasiri wa Lukoha na kuridhia yeye kurejea Sanzani. Lukoha akamueleza Mwenda kila kitu naye akaaridhia ilo, wakapewa askari ishirini ambao waliwasindikiza hadi kwenye mipaka ya tawala ya Sanzani.
***************************
Chifu Ng’arika alikuwa hapo tayari na jeshi lake akaamuru Lukoha afungwe mikono na miguu na kupelekwa sehemu ya hukumu pia akatoa agizo hilo hilo kwa Mwenda. Watu wengi walijipanga njiani wapo walio wahurumia na kusema ni uonevu na wapo waliowadhiaki kwa maneno ya kashfa.
Chifu Majariwa alikuwa sehemu ya hukumu akiwa na shahuku kubwa ya kumuona Mwenda mwanamke aliyeandaliwa kwa ajili yake. Msafara ukafika sehemu hiyo na chifu Majariwa akasimama kwa ghazabu mno baada ya macho kutua kwa Lukoha. Watu wengi wakakusanyika eneo hilo hili kushuhudia adhabu itakayotolewa kwa wawili hao.
“Kwanza nafurahi maana sikutarajia Uchindile wangeniogopa na kuniheshimu hivi hata kuniletea watu hawa waliotenda usaliti katika ardhi hii, mleteni Mwenda hapa,” alisema Chifu Ng’arika.
Askari wakamleta Mwenda na kumsimamisha mkabala na Lukoha, Chifu Majariwa alipouona uzuri wa Mwenda uchu wa kulipata penzi la binti huyo ukamshika. Hakutaka tena adhabu yeyote imkute binti yule bila yay eye kufaidi Penzi Lake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Leo hii wawili hawa watachinjwa na vichwa vyao vitaning’inizwa kwenye lango kuu la kuingia Sanzani kwa kufanya hivi itakuwa fundisho kwa wote mnaotamani kufanya upumbavu kama huu. Kilicho cha chifu kitabaki kuwa cha chifu si mlinzi wala si mtu wa kawaida mwenye ruhusa ya kukikaribia” aliendelea kuseama Chifu Ng’arika.
Lukoha akasogezwa sehemu ya machinjio akavikwa kitambaa cheusi kisha mtu aliyefunika uso wake huku akishikilia upanga ulio na makali akamsogelea. Mwenda akahuzunika sana moyoni mwake hakuelewa ni kwa namna gani anaweza kumnusuru Lukoha toka katika mahuti yale yaliyokuwa karibu mno.
“Tafadhali chifu mtukufu usitoe uhai wa kijana huyo, mimi ndiye mwenye hatia, niko radhi kufanya lolote” alisema Mwenda.
Kauli hiyo ikampa nguvu chifu Majariwa ambaye muda wote alikuwa akitafuta nafasi hili aweze kutekeleza mpango wake.
“Eti amesema kuwa yuko radhi kufanya lolote?” aliuliza chifu Majariwa kama mtu anayehitaji kuhakikisha kile alichokisikia kwanza.
“Ndiyo niko radhi hata kufa hili Lukoha apone”
Chifu Majariwa akatoka sehemu ya juu na kushuka hadi chini kisha akamnyanyua Mwenda ambaye uso wake uliloa kwa machozi. Akasogea karibu na sikio kisha akamwambia,
“Nitayasaidia maisha ya Lukoha endapo utaridhia kutumikia urithi alioniachia marehemu kaka yangu”
Mwenda akasogea nyuma na kumtazama usoni chifu Majariwa, moyo ulipata na mshtuko Zaidi alipoona chifu majariwa amefanana na Izack kwa kila kitu.
“Nini hiki? Inamaana niko ndotoni au ni kweli haya mambo yanatokea huyu ni Izack kwa hakika” alisema Mwenda bila kusikika na yeyote yule.
“Sina muda wa kupoteza watu wote wanakutazama hatima ya maisha ya Lukoha yapo mikononi mwako” alisema Chifu Majariwa.
“Sawa nimekubali” alijibu Mwenda.
Majariwa akacheka kwa sauti kubwa iliyowashtua watu wote wa Sanzani kisha akasogea hadi kwa chifu Ng’arika na kumwambia,
“Bado nina nafasi ya kuamua adhabu itakayomfaa mwanamke huyu, ukizingatia ni mali yangu. Aidha bado nina maamuzi juu ya mtu aliyemfanya mke wangu kukosea hivyo chaguo langu sio kifo”.
Ng’arika alishangaa mno kusikia kauli toka kwa baba yake mdogo, kwa mara nyingine akahisi kuingiliwa katika maamuzi yake.
“Unawezaje kuvuruga mila na desturi za Sanzani? Nakuheshimu kwa sababu unadamu sawa na ya baba yangu, huyu hafai kuwa mke na yule hafai kuwa mlinzi wote ni wasaliti lazima wauawe” alisema Ng’arika kwa jazba.
Hali ile ya kutokuelewana ikawapa nafasi wanajimu na wazee wengine kuona ile hatari waliyokuwa wakiizungumzia juu ya hatima ya Sanzani. Kama wawili wale watagombana Sanzani itazidi kutengeneza uadui na tawala nyingi za jirani ambazo kama zitaungana ni rahisi kuiangusha na kuipoteza kabisa Sanzani.
“Wewe bado mtoto mdogo sana kwangu! Fanya kama nilivyosema jua kuwa Mwenda ni mali yangu hamna mwenye ruhusa ya kumfanya chochote”
Kauli hiyo ikamfanya chifu Ng’arika ashindwe kujizua na kuchomoa jambia na kujeruhi mkono wa chifu Majariwa. Askari waliongozana na Majariwa walivyoona hayo nao wakaingilia kati, sasa kukawa na ugomvi kati ya baba na mwana.
“Niliwaambia nyota za watu wale wawili ni kali mno japo nilitegemea mahafa lakini sikujua itakuwa kwa namna hii, njia pekee ya kutatua tatizo lile ni kuwaachia wawili wale waondoke katika ardhi hii ya Sanzani” alisema mnajimu Mkuu.
Watu walipoona tafrani ile kila mmoja akaanza kutimua mbio ili kunusuru maisha yako kama pande mbili zile zitaamua kupambana. Wakaagizwa vijana kumi waliokuwa wakilinda maeneo ya ibada ya mizimu wakawachukua Mwenda na Lukoha, wakawatoa hadi nje ya mipaka ya Sanzani kishwa wakawaambia,
“Msishawishike kurejea Sanzani tena, nendeni mkaishi kwa Amani mizimu imewaridhia”
“Nini kitatokea endapo tutarejea?” akauliza Lukoha.
“Uwepo wenu umesababisha mpasuko kuanzia kwa wananchi hadi watala, suluhu pekee ya wao kuungana ni nyinyi kutokomea kusikojulikana. Muda sio rafiki ondokeni hapa” alisema mmoja kati ya askari wale waliopewa jukumu la kuhakikisha Mwenda na Lukoha wanatoka katika ardhi ya Sanzani wakiwa salama.
Askari wa chifu Majariwa wakashika silaha zao tayari kupambana na kikosi cha askari wa chifu Ng’arika, papo hapo anga likabadirika na kuwa jeusi kisha upepo mkali uliombatana na radi ukatokea na kuwatawanya askari wale. Hali ile ilidumu kwa muda wa saa mbili, baadaye hali ikawa shwari na Ng’arika akarejea katika hali yake ya kawaida japo Chifu Majaliwa bado alijawa na ghazabu juu ya tukio alilofanyiwa.
Baada ya tukio hilo ndipo chifu Ng’arika alipokea taharifa juu ya kutoweka kwa watumiwa wake, akashangaa Zaidi juu ya jambo hili akahisi uhenda baba yake mdogo ndiye aliyepanga hayo yote. Akatoka akiongozana na askari wake ambao wakizunguka nyumba aliyokuwa chifu Majariwa na kumtaka wazungumze.
“Kunidharau haikutosha sasa umeamua kuwatorosha kabisa” alisema Ng’arika.
“Wametoroka?” aliuliza Chifu Majaliwa kwa mshangao.
“Nikuulize wewe umewatoroshea wapi?” alijibu Ng’arika.
“Hapana hawez kutoroka na mke wangu” alisema chifu Majariwa huku akizunguka bila kuelewa anataka kuelekea wapi.
Chifu Majaliwa alilogwa na uzuri wa Mwenda hakuwahi kuona binti mrembo na mwenye kujiamini kiasi kile. Aliona msichana yule anasifa na vigezo vyote vya kuwa mke wake,
“Niongezee kikosi usiku huu naanza safari ya kumsaka mke wangu popote alipo na nakuahidi nitakuletea kichwa cha yule mpumbavu aliyetoroka naye” alisema chifu Majaliwa.
*******************
Mwenda na Lukoha walitembea umbali mrefu sana, walipoona usiku umekuwa mzito sana wakaamua wapumzike kwenye pacha ya mkuyu. Lukoha alimsaidia kumvuta Mwenda na hatimaye akafanikiwa kukaa vyema,
“Mahali hapa ni salama kwetu kwa usiku huu adui yeyote atakayekuja eneo hili tutakuwa wa kwanza kumuona kabla yake” alisema Lukoha.
“Niko tayari kwa kulipigania penzi hili naamini hamna wakututenganisha” alijibu Mwenda.
“Natamani kukuche haraka tuwahi kufika Uchindile na tupate Baraka kutoka kwa wazee ili tuishi kama mume na mke”
“Mungu atatimiza hitaji la nyoyo zetu”
Waliendelea kuzungumza na Lukoha akawa wakwanza kupitiwa na usingizi, Mwenda akayatafakari matukio yanayomkuta katika dunia hii ya miaka 1000 nyuma akajaribu kuoanisha na matukio yaliyomkuta katika dunia ile ya 2017.
“Nafikiri kuna kitu Mungu anataka kunionesha chifu Majaliwa analandana sana na Izack na Lukoha analandana na mume wangu Lucas, lazima kunakitu ambacho sikifahamu baina ya watu hawa wawili” alisema Mwenda.
Mwenda alizama kabisa katika lindi la mawazo akashtushwa na kelele za watu, alipotazama umbali kama wa mita mia mbili akaona vienge vya moto vilivyowasaidia watu wale waliokuwa kama wakitafuta kitu kilichopotea. Kwa haraka akamuamsha Lukoha naye akatumia uzoefu wake wa kijeshi na kugundua kuwa walikuwa ni askari wa Sanzani.
“Bila shaka chifu Ng’arika bado anataka kutuadhibu, tuondoke hapa kabla hawajatufikia” alisema Lukoha.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakashuka kwenye mti ule wa mkuyu na kuanza kukimbia kulekea magharibi ambapo Uchindile inapatikana. Walikimbia kwa nguvu mno lakini juhudi zao hazikuzaa matunda kwani walijikuta wakiingia katika mtego wa askari wale.
“Mbio za sakafuni siku zote huishia ukingoni, Lukoha uliyepewa sifa tele kwa uhodari wako katika mapambano leo umekuwa mdogo kama sisimizi. Subili jua litakapochomoza utakumbana na adhabu yako” alisema kapteni wa jeshi hilo la Sanzani.
*************
Lukoha na Mwenda wakawekwa chini ya Ulinzi hadi mawio kisha wakasafirishwa hadi juu ya mlima uliopo eneo hilo ambapo chifu Majaliwa aliweka kambi. Chifu alifurahi mno alipomuona Mwenda akawaamuru wamfungulie binti yule na kumleta karibu yake.
“Hatimaye umerudi kwangu Malkia, pumzika na tumuadhibu yule mpuuzi” alisema chifu Majaliwa.
“Usifanye hiko ulichopanga Lukoha ni mume wangu na Mungu ndiye shahidi hakuna wa kututenganisha,” alisema Mwenda.
Chifu Majaliwa akachukia mno akaamuru Lukoha apigwe hadi pale Mwenda atakapokubali kuwa mke wake, bila huruma askari wakamshushia kipigo kama mnyama aliyedhuru watu. Mwenda alihisi maumivu makali ambayo hakuweza kuyastahimili akatoka na kwenda kumkumbatia Lukoha aliyekuwa katika mateso makali. Askari wakamtoa Mwenda kwa nguvu na kumuacha Lukoha peke yake kisha chifu Majaliwa akashika upinde na mshale akaunyoosha kwa Lukoha na kuuachia, Mshale ule ukachoma Lukoha tumboni papo hapo Lukoha akaanguka chini akamtazama Mwenda aliyekuwa akilia bila kupata msaada wowote.
“Mwenda wewe ni mwanamke mzuri kuliko wote ambao macho yangu yamebahatika kuwaona, nakupenda sana”
Kauli hiyo ikamliza Zaidi Mwenda kwani pia ndiyo ilikuwa kauli ya mwisho kabla ya yeye na mumewe Lucas kupata ajali. Mwenda alilia mno hakuwa na wakumsaidia wala kumbembeleza, akajikuta akipata nguvu ya ajali akampiga mmoja wa askari na kumnyang’anya jambia ambalo akataka kumchoma nalo chifu Majaliwa. Kabla hajatimiza azma yake askari wakamuahi na kumzuia mwenda akapaza sauti yake na kusema,
“Ipo siku haya uliyonifanyia nitayalipiza, lazima nikuue….Nitakuua tuu”
Papo hapo upepo mkali ukatokea na ardhi ikatetemeka, hakuna aliyeweza kuona kilichotokea, Mwenda akahisi nguvu kumuisha akaanguka chini na kupoteza fahamu.
**************
“Niachieni lazima nimuue, nitamuua tuu…” alisema Lucy na kuzinduka toka katika usingizi mzito huku akiwa aanahema mithiri ya mtu aliyekuwa akikimbia.
“Vipi mwanangu wajionaje na hali” aliuliza mama yake Lucy ambaye muda wote alikuwa na binti yake chumbani hapo.
“Mama Wamemuua mume wangu siwezi kukubali lazima na wao niwaue” alisema Lucy.
Kauli ile ikamchanganya kidogo mama yake Lucy na kuona mwanae amerejewa na tatizo lake la kuongea vitu vya ajabu. Akamshika mikono na kumsihi atulie,
“Mwanangu mumeo alishafariki siku nyingi zilizopita na wewe sasa ni mchumba wa mtu”
“Hapana mama mume wangu wamemuua leo na nimeshuhudia kwa macho yangu”
Lucy aliendelea kusumbua huku akisisitiza kuwa mumewe ameuawa, akamsha machungu yaliyopoa na kusahaulika. Ikabidi daktari apigiwe simu na kuja hapo nyumbani akamfanyia vipimo Lucy lakini hakuona tatizo lolote, ikabidi amchome sindano iliyompa usingizi.
“Tunaamini kuwa mtu aliye nusu mfu nusu hai, roho yake utembea na kukutana na mambo mengi, nafikiri mwanao ni muathirika wa hilo hivyo kuweni makini na kila kitu anachokisema kinaweza kuwa na ukweli na pia kinaweza kuwa cha uongo ni hatari sana kama mambo haya yatatoka nje” alisema Daktari.
“Sawa nitajitahidi kumchunga binti yangu”
Izack akapata taharifa juu ya Lucy kurejewa na fahamu akafurahi sana, akaacha shughuli zake na kwenda kumuona mwanamke huyo ambaye kiukweli alimpenda sana. Alipofika alimkuta akiwa bado amelala hakutaka kuondoka akasubili hadi atakapoamka.
“Lucy wangu yuko hivi toka tukio la mume wake kufariki, shukrani nyingi kwako kwani ulimfanya binti yetu kuwa katika hali nzuri na nakuomba uvumilie kwa kipindi hiki kwani najua atasumbua” alisema mama yake Lucy.
Wakati wakiongea hayo Lucy akaamka toka usingizini, akainuka na kukaa kitako akatazama lakini hakuona mtu hapo chumbani ikabidi ashuke kitandani na kuusogelea mlango akaufungua na kutoka nje ya chumba, akatazama kila kona kwa mbali akamuona mama yake aliyekuwa akizungumza na mtu ambaye hakumfahamu.
“Mama!” Lucy akaita.
Mama akaisikia sauti ya bintiye akainuka kwa haraka na kwenda kumshika kwani hakuwa na nguvu, Izack naye akaona ni wakati wake wa kuonana na Lucy. Lucy akapiga kelele alipoiona sura ya Izack akawa kama anataka kuongea kitu lakini akashindwa, akiwa bado mikononi mwa mama yake akapoteza fahamu.
“Mhmh! Ni ajabu kidogo kwani alipoiona tu sura yako amepoteza fahamu tena, sijui zitarejea muda gani yawezekana ikatulazimu tusubiri wiki au mwezi kama ilivyokuwa awali, kwa sasa nenda ukapumzike nitakujulisha kwa kila hatua atakayofikia” alisema mama yake Lucy.
Izack akaondoka huku akiwa na mawazo tele juu ya lile tukio la Lucy kupiga kelele alipomuona, hakujua nini hasa kilichomkuta mwanamke yule aliyeutesa moyo wake kwa muda mrefu. Akajipa moyo na kuamini kila kitu kitakuwa sawa kadri ya muda uendavyo.
***************
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Luis hakujua lolote linaloendelea kwa Lucy, toka siku ile aliyofukuzwa hakutaka kufatilia japo moyo wake ulitamani sana kujua hali ya Lucy. Hakuwa na ujasiri wa kufanya lolote kwani alisadiki kuwa Lucy alishakuwa mali ya Izack. Baba yake Luis alijua kila kinachomsibu mwanaye akajaribu kumshauri kuwa aende kumjulia hali, Luis akaupokea ushauri ule wa baba yake na kuamua kuitumia jioni moja kwenda kumtembelea.
Alipofika akasita sana kuingia ndani maneno ya baba na mama yake Lucy yakawa bado yanazunguka kichwani mwake.
“Kijana tulikupokea na kukuona kama mtoto wetu ila kwa haya sitojutia kukwambia ondoka katika nyumba yangu na sihitaji kukuona maana huna nia njema na familia hii. Nilizani wewe ni nuru uliyekuja kuiangaza familia hii ila sivyonilivyofikiri maana umekuwa giza unayeitaji kuipoteza furaha iliyotawala hapa Luis nenda na usifikirie kurudi tena hapa”
Maneno hayo yakamfanya abadili uamuzi wake na kurudi alipotoka kabla hata hajaingia ndani wala kumuona Lucy. Wakati anaondoka akaona gari la baba yake Lucy likiwa linakuja mbele yake, Luis hakulijali akaendelea na safari, lilipomkaribia likapunguza mwenda na hatimaye kusimama kabisa. Luis akalitazama na kuona mlango ukifunguliwa, hakuamini aliposhuhudia Lucy akishuka kwenye gari lile na kuja upande alipo yeye. Luis akawa kama ameshikwa na bumbuazi kwani ni ukweli usio na kificho alimpeza sana binti yule.
“Kweli hunipendi!” alisema Lucy baada ya kumsalimu Luis.
“kwanini wasema hivyo”
“Toka nimeumwa sikusikia yeyote aliyesema kuwa umekuja kunitazama”
Sentensi hiyo ikamshtua Luis ambaye hakuwa anajua kama Lucy alikuwa akiumwa hakujua ajitetee vipi hili Lucy amuelewe.
“Duuh! Kwanza nisamehe sana maana sikuwa najua kuwa ulikuwa mgonjwa” alisema Luis.
“Sawa usijali! Ila nilipata nafasi ya kurudi Sanzani na niliyoyaona huko nahisi yanauhusiano mkubwa na yaliyonitokea hata yatakayonitokea siku zijazo, natamani kuongea nawe kiurefu Zaidi ila mazingira si rafiki, kama hutojali naomba twende nyumbani” alisema Lucy.
“Samahani! Muda pia si rafiki unaijua vyema hali ya baba yangu, naomba kesho uje naamini tutapata nafasi ya kuongea Zaidi” alisema Luis.
“Sawa haina shida”
Wakapeana mikono ishara ya kuagana, macho ya Luis yakatua kwenye vidole vya Lucy akashangaa kutoiona pete ya uchumba. Akashindwa kuuliza lolote kwa Lucy kwa wakati huo,
“Mhmh! Inamaana tukio la kuvishwa pete halikufanyika! Nani alizuia jambo hilo au mama na baba yake Lucy wameyafanyia kazi yale niliyowaambia? Au kuna mambo mengine yamejitokeza? Natakiwa niwe makini Zaidi kwa wakati huu”
Alisema Luis kwa sauti ya chini huku akitembea baada ya kuagana na Lucy huku wakiahidiana kuonana siku inayofuata kwa maongezi Zaidi. Kwa upande mwingine Luis alipata nguvu mpya kwa kuona Lucy hana pete yeyote mkononi mwako na upande mwingine alihofu usalama wa maisha ya baba yake.
***********
Saa zikaenda kwa kasi hatimaye Machweo ya siku mpya yakafika, Luis hakuwaza lolote Zaidi ya kuwa na shahuku kubwa ya kuonana na lucy kama walivyoahidiana. Akafanya shughuli za nyumbani hapo kwa haraka na umakini Zaidi, baba yake akamshangaa mwanaye kwani haikuwa kawaida,
“Mhmh! Kwa usafi huu lazima leo kutakuwa na ugeni mkubwa” alisema baba yake Luis.
“Ndiyo na wala sitaki kukwambia nani anakuja wewe subili utamshuhudia mwenyewe” alijibu Luis.
“Haya yangu mimi macho tu”
Luis akaendelea kusafisha kila kona ya nyumba, akapanga vitu katika namna ya kuvutia, alipoona kila kitu kiko kama alivyokusudia akaenda bafuni kuweka mwili wake safi kisha akaa sebuleni tayari kwa kuupokea ugeni ambao muda wowote ungewasili. Luis akasikia muungurumo wa gari nje ya nyumba yao akaamka kwa furaha akijua kuwa Lucy tayari amekwisha wasili japo alishangaa kuwa ni mapema Zaidi ya alivyotarajia. Akamtazama baba yake kisha akatabasamu,
“Baba tabasamu kidogo mgeni tayari amekwishawadia” alisema Luis huku akiusogelea mlango uliokuwa ukigongwa kwa nguvu.
Luis akashika kitasa cha mlango na kugeuka kumtazama baba yake kisha taratibu akaufungua na kupataza sauti yake,
“Surprise…………………!”
Alijikuta akikatisha alichotaka kusema hasa baada ya kuona sura ya baba yake ikibadirika na kuwa kama mtu anayeogopa.
“Baba! Lucy huyu mbona wamuogopa tena?”
Baba yake Luis akaanza kukohoa mfululizo na kuanza kupumua kwa shida, Luis akageuza shingo yake na kutazama ni nani hasa aliyemkaribisha na kufanya hali ya baba yake kuwa mbaya Zaidi. Akaona watu waliofunika nyuso zao huku wakiwa wameshikilia silaha za jadi na za kisasa. Alishtuka sana kabla hajauliza lolote akapigwa kofi lililompeleka mpaka chini, Luis akakimbilia kwa baba yake ambaye hali yake ilibadilika mno. Akachukua dawa iliyopembeni na kutaka kumnywesha baba yake lakini kabla hajafanya hivyo wale watu wakamsogelea na kumiga tena na ile dawa ikamwagika,
“Mbona sina uadui na mtu mwataka nini kwangu?” aliuliza Luis.
“Roho yako” akajibu mmoja kati ya wale watu watano.
“Nimewakosea nini?”
Luis hakujibiwa Zaidi ya kupigwa na ubapa wa panga, kisha wakamsogelea baba yake na kumwangusha chini, Luis aliumia mno kushuhudia tukio lile. Akajikuta akipata nguvu na kumvamia mmoja kati yao na kumpiga mweleka. Akajitahidi kupambana nao lakini nguvu yake ilikuwa ndogo kwani alijikuta akidhibitiwa vilivyo, yule aliyepigwa mweleka na Luis akaamka kwa hasira na kuchukua panga kisha akalishusha katika mkono wa Luis. Wakati jambo hilo linaendelea Lucy naye akawa ndiyo anawasili na kukutana na unyama ule.
Akapiga yowe lililowashtua watu waliokuwa nje na hata waliokuwa ndani waliogopa sana, Wakamsogelea Lucy kwa haraka ambaye alishindwa kufanya lolote kutoka na hofu iliyomshika, wakampiga sehemu ya shingo ulipo mshipa wa fahamu na papo hapo Lucy akaanguka chini na kupoteza fahamu.
“Oyah! Tuondokeni hapa huyu mwanamke kashaharibu mpango”
“Tunaondokaje kizembe tuwapige risasi”
“Hapana huyu mwanamke hatakiwi kuuwawa ni mali ya bosi”
Nje watu wakasogea ilipo nyumba ya kina Luis na kugundua uhalifu uliokuwa ukiendelea ndani, wananchi wakachukua zana mbalimbali tayari kwa kupambana. Majambazi yale yalipofika nje yakapiga risasi hewani na kufanya watu waogope na kuanza kutimua mbio hovyo, hata hivyo wapo wachache waliamua kujitoa muhanga kwa kuwashambulia kwa mawe. Gari lao liliharibiwa vibaya hata wao kujeruhiwa, hawakutaka kuacha ushahidi wowote nyuma pia waliogopa kuua raia wasiokuwa katika mpango wa kuuawa. Jambo hilo liliwapa ugumu Zaidi katika harakati zao za kutoroka eneo hilo.
“Tumezidiwa tuifanye nini?” alisema mmoja kati ya wahalifu wale.
“Tutupia mbinu B, mimi nitaingia na kuwasha gari”
“Sawa”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mbinu B ilikuwa ni kurusha mabomu ya machozi, ilo likawasaidia kwani watu wote walitawanyika kutafuta namna ya kuzuia mfukuto waliohusikia machoni mwao. Majambazi yale yakafanikiwa kutoweka eneo hilo.
Huku nyuma Luis hakujiweza kwa lolote maana alipigwa na kujeruhiwa vibaya sana, Lucy akatoka nje kuomba msaada lakini hakubahatika kumuona yeyote. Akarejea ndani na kumuangalia baba yake Luis naye alikuwa na hali mbaya sana, wazo la kupiga simu polisi likamjia na baada ya dakika ishirini askari wakawasili eneo hilo. Luis na baba yake wakapakizwa kwenye gari na kupelekwa hospitalini, Lucy akabaki kidogo ili kuisaidia polisi katika uchunguzi wao.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment