Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

A LIVING DREAM ( NDOTO INAYOISHI ) - 5

 







    Simulizi : A Living Dream ( Ndoto Inayoishi )

    Sehemu Ya Tano (5)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Mwaka wa pili wa masomo yake ya Biblia ukakatika na hatimae kumaliza kabisa na kupewa cheti chake kutoka kwa askofu mkuu wa dhehebu lake. Alikuwa na furaha isiyo kifani, alimkumbatia mke wake na kupiga picha kadhaa, kwao, ilionekana kuwa furaha kubwa.

    Kwa muda, wakasahau tatizo walilokuwa nalo kwamba hawakuwa na mtoto, waliendelea kuyafurahia maisha mpaka waliporudi Dar es Salaam huku Emmanuel akiwa na cheti chake mkononi.

    Baada ya miezi miwili, akapewa Kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge ili aweze kuliongoza, kwake ilikuwa furaha zaidi, japokuwa alikuwa na washirika wachache lakini hakuonekana kujali.

    Kutokana na upako aliokuwa nao, watu wakaanza kujaa kanisani kwake. Kuponywa kwa wagonjwa na wenye matatizo mbalimbali kuliwafanya watu wengi kumiminika kanisani hapo.

    Ndani ya miezi kadhaa, tayari alikuwa na washirika sitini ambao wote walikwenda hapo kutokana na upako mkubwa aliokuwa nao. Hakutaka kuacha kumwabudu Mungu, aliendelea kumuabudu kama kawaida yake japokuwa alikuwa akipitia katika mapito mazito.

    “Mume wangu,” aliita mke wake.

    “Unasemaje mke wangu.”

    “Najisikia kizunguzungu,” alisema Luciana.

    “Tatizo nini?”

    “Sijui, naomba unipeleke hospitali.”

    “Hali hiyo imeanza lini tena?”

    “Toka asubuhi. Naomba uje unipeleke hospitali,” alisema Luciana.

    Japokuwa alikuwa na kazi nzito ya kuandaa andiko la siku ya Jumapili, hakutaka kujali, akaifunika Biblia na kisha kuelekea chumbani kuchukua ufunguo wa gari, akarudi sebuleni hapo, akamchukua mke wake na kulifuata gari na kuondoka nyumbani hapo.

    Breki ya kwanza ilikuwa katika Hospitali ya Kinondoni, walipofika hapo, Luciana hakuonekana kuwa na tatizo lolote lile, mwili wake ulionekana kuwa mzima wa afya.

    “Ana tatizo gani?” aliuliza Emmanuel.

    “Mkeo mjamzito.”

    Kwanza Emmanuel akashtuka, hakuamini kile alichokuwa amekisikia, akamwangalia dokta vizuri, alihisi kama ni sauti iliyosikika kichwani mwake lakini si sauti ya daktari yule.

    “Umeongea wewe au nimesikia sauti kichwani mwangu?” aliuliza Emmanuel.

    “Kuongea nini?”

    “Kwamba mke wangu mjauzito.”

    “Ni mimi! Ndiye niliyekwambia kwamba mkeo mjauzito, hatukuw......” alisema dokta huyo lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, Emmanuel akaanza kuongea kwa sauti kubwa.

    “Mungu ametenda....Mungu ametenda....dokta! Mungu wangu ni mkuu! Ametenda...” alisema Emmanuel huku akimuinua dokta kitini na kumkumbatia kwa furaha.

    Kwake ulionekana kama muujiza, hakuamini kwamba hatimae, mke wake aliyekuwa na tatizo kubwa la kizazi, mwisho wa siku akawa amepata ujauzito. Akabaki akimshukuru Mungu na hata baadae aliporuhusiwa kumuona mke wake, hakuweza kuizuia furaha yake, machozi yakaanza kumbubujika, wakashikana mikono na kuanza kumshukuru Mungu.

    ****

    Baada ya miezi sita kukatika, tena huku tumbo lake likiwa linaonekana vizuri, ndipo mchungaji Emmanuel akaalikwa katika mkutano mkoani Dodoma. Matangazo yakabandikwa kila kona kwamba mkutano mkubwa wa Injili ujulikanao kama Delivarence (Ukombozi) unatarajiwa kufanyika mkoani hapo katika Uwanja wa Mpira wa Jamhuri

    Mkutano ulifanyika kwa mafanikio makubwa lakini wakati walipokuwa wakirudi jijini Dar es Salaam, ndipo ajali kubwa ikatokea baada ya kupigiwa simu kwa namba ambayo hawakuielewa vizuri, namba iliyokuwa ikitumiwa na majini, namba ambayo ungeipokea tu, ilikuwa ni lazima ufe, ndiyo namba ambayo Luciana aliipokea na mwisho wa siku kupata ajali mbaya ya gari.

    *****

    Hali ilikuwa inatisha, ripoti za madaktari kutoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilisema kwamba majeruhi waliumizwa vibaya vichwani mwao na hivyo walitakiwa kufanyiwa oparesheni hasa baada ya miili yao kuchunguzwa kwa kupitia mashine kubwa ya T Scan.

    Zoezi la kufanya uchunguzi huo lilikuwa la gharama sana hivyo fedha zilihitajika haraka iwezekanavyo ili oparesheni ifanyike. Washirika wa Kanisa la Praise And Worship wakiongozwa na askofu wao wakachanga kiasi cha fedha kilichokuwa kikihitajika na matibabu kuanza rasmi.

    Uchunguzi ulipofanyika katika mashine ya T Scan, ilionyesha kwamba kulikuwa na madonge makubwa ya damu yalikuwa yameganda vichwani na hivyo yalitakiwa kutolewa haraka iwezekanavyo.

    “Hili jambo linatakiwa kufanyika ndani ya siku moja tu kabla hawajapatwa na matatizo zaidi,” alisema Dk. Abdallah Issa, daktari bingwa wa upasuaji hospitalini hapo.

    Washirika na ndugu za wagonjwa hawakutaka kuondoka, walitaka kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea ndani ya chumba cha upasuaji. Madaktari walikuwa makini na kazi zao, walichokifanya ni kuwachukua Emmanuel na mkewe kisha kuvichana vichwa vyao, wakachukua kitochi kidogo na kuanza kuchungulia ndani ya kichwa ili kuona madonge ya damu yaliyokuwa yameganda.

    Ilionekana kuwa kazi kubwa, madaktari walikuwa wametulia wakiifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa mno. Walichukua masaa nane, upasuaji ukakamilika, wakaziba sehemu ambayo waliiachana huku madonge yale ya damu yakiwa yametolewa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “What is going on? What about operation? Is it successful done? We want to see her,” (Nini kinaendelea? Upasuaji ulikuwaje? Ulifanyika kwa mafanikio? Tunataka kumuona) aliuliza askofu mara baada ya oparesheni hiyo kufanyika, alionekana kuwa na wasiwasi mwingi.

    “It is successful done, you have to wait for twelve hours, you can go now and be back tomorrow” (Imefanyika kwa mafanikio, mnatakiwa kusubiri kwa masaa kumi na mbili, mnaweza kuondoka na kurudi kesho) alisema Dk. Abdallah aliyetoka katika chumba cha upasuaji.

    Hawakuwa na jinsi, walichokifanya ni kuondoka hospitalini hapo huku ikiwa tayari imetimia saa 2 usiku. Kila mmoja alikuwa na mawazo, mioyoni mwao walikuwa wakiendelea kuwaombea majeruhi hao waweze kurudi katika hali zao za kawaida.

    “Mungu naomba uwaponye!” alisema mama yake Luciana huku akiwa amepiga magoti chumbani kwake, tayari mashavu yake yalilowanishwa na machozi yaliyokuwa yakimtoka.

    Siku iliyofuata, asubuhi na mapema wazazi wa majeruhi hao walikuwa hospitalini hapo. Walitulia katika viti vya watu wanaosubiria wagonjwa, alipotokea Dk. Abdallah na kuwaona, akawataka kumfuata ambapo akaenda nao mpaka katika chumba kile walicholazwa.

    Kama walivyoletwa ndivyo walivyokuwa kitandani pale, kila mmoja akashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kuwabubujika mashavuni mwao kwani picha waliyokuwa wakiiona iliwaumiza mno.

    Emmanuel na Luciana, vichwa vyao vilikuwa vimefungwa bandeji huku puani wakiwa na mashine iliyowasaidia kupumua.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha waliyokuwa wakiishi. Siku ya kwanza ikakatika, siku ya pili ikaingia na kukatika, mpaka wiki inamalizika, bado Emmanuel na mkewe hawakuwa wamefumbua macho.

    “Watakufa?” aliuliza mama yake Emmanuel huku akionekana kuwa na hofu.

    “Hapana, hawawezi kufa, Mungu wetu ni mkuu, atawaponya tu,” alisema askofu aliyeonekana kuwa na imani kubwa.

    Makanisani watu walizidi kuomba, hali waliyokuwa nayo wagonjwa wale iliendelea kuwatisha, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa na matumaini ya wagonjwa wale kuinuka vitandani na kuendelea na maisha yao kama kawaida.

    Wenye kulia, walilia mno, wenye kusononeka, walisononeka mtu lakini pamoja na kufanya vitu vyote hivyo, wawili hao hawakuweza kufumbua macho vitandani pale.

    Watu wengine wakasafiri kutoka katika mikoa mbalimbali na kufika Dar es Salaam kwa ajili ya kuwajulia hali lakini mbaya zaidi, kila kitu kilikuwa vilevile, hakukuwa na unafuu wowote ule hali iliyowaumiza kupita kawaida.

    “Au wamekufa ila madaktari wanatudanganya?” aliuliza mshirika mmoja, mwezi wa pili ulikuwa umepita lakini watu wale walibaki vilevile, hawakukufumbua macho yao, na hata kula, walitumia mipira maalumu iliyokuwa ikibadilishwa kila siku kwa gharama ya shilingi elfu thelathini kila mmoja, fedha zote hizo zilichangwa kutoka katika makanisa mbalimbali.

    “Sidhani kama wanaweza kutuficha kitu kama hicho, nadhani hakuna aliyekufa,” alijibu mshirika mmoja.

    ****

    Patrick hakutaka kuwa mbali, kila kitu kilichokuwa kikiendelea, alikifuatilia kwa karibu mno. Alikuwa na moyo wa kulipa kisasi tu, japokuwa alifanyiwa usaliti miaka saba iliyopita lakini bado moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali.

    Hakujisikia amani, kitendo cha kuwaona wawili hao wakiwa wanaendelea na maisha yao vitandani huku wakiwa hoi aliumia mno. Hakukuwa na kitu alichokuwa akikitaka kama kuona wawili hao wakiuawa palepale kitandani, yaani kama wamelala katika usingizi wa kifo, wasiweze kuamka tena.

    Hakujisikia hukumu wala huzuni juu ya wagonjwa wale, moyo wake ulifarijika mno na hivyo alitaka kuwamaliza wote wawili vitandani pale. Kwa sababu alikuwa akijulikana na wazazi wa watu hao, alichokifanya ni kuwatafuta watu ambao wangeweza kufanya kazi yake tena kwa malipo mazuri kabisa.

    “Wapo wapi hao watu?” aliuliza mmoja wa kijana aliyekuwa katika kundi la Black Mimi.

    “Hospitalini, nataka mfanye kazi, kuwamaliza tu, basi, hapo nitaridhika,” alisema Patrick.

    “Una kiasi gani?”

    “Kwani malipo yenu yapo vipi?”



    “Milioni mbili kila kichwa.”

    “Hakuna noma, ila kazi itafanyika?”

    “Ndiyo, itafanyika kwa uhakika, tuamini.”

    “Sawa. Mtanipa taarifa, nitawaleteeni picha zao na vilevile nitawaambia vyumba walipolazwa, vingine, mtajua nyie namna ya kufanya kazi yenu,” alisema Patrick.

    Baada ya siku mbili, vijana hao walikuwa na kila kitu kilichohitajika katika kukamilisha kazi zao, walichokifanya ni kuanza mara moja.

    Kwa sababu walikuwa wamekwishaambiwa kila kitu, wala haikuwa ngumu, siku ya kwanza tu, walichokifanya ni kwenda katika hospitali hiyo, walichokuwa wakikitaka ni kusoma ramani na kujua hali ilikuwaje.

    “Nyie ni washirika wa kanisa gani?” aliuliza askofu mara baada ya vijana wawili kutokea hospitalini hapo na kuomba nao wawaone wagonjwa.

    “Praise And Worship kutoka mkoani Morogoro kwa mchungaji Mpanda,” alijibu kijana mmoja.

    “Sawa. Subiri, wanawaandaa kasha tutaingia kuwaona.”

    Zaidi ya washirika arobaini walikuwa wamekusanyika nje ya chumba kile kikubwa, kila mmoja alitaka kuwaona wagonjwa hao waliokuwa wakienda mwezi wa tatu pasipo kufumbua macho yao. Waliokuwa na maua, walikuwa nayo na hata wale waliokuwa na uwezo wa kununua kadi za kuwatakia pole, nao walikuwa nazo mikononi mwao.

    Madaktari walipomaliza kuwaandaa, wakawaomba watu hao waingie ndani ya chumba kile kwa zamu. Emmanuel na mkewe Luciana walikuwa kimya vitandani pale, miili yao ilidhoofika mno kana kwamba walikuwa wakiugua Ugonjwa wa UKIMWI.

    Walitia huruma, kila mtu aliyekuwa akiwaangalia, alishindwa kuvumilia, alijikuta akibuibujikwa na machozi. Mateso makubwa yalikuwa yakiendelea kitandani pale. Japokuwa washirika walijitahidi sana kuomba Mungu lakini kuna kipindi kikafika wakaona ni kama walikuwa wakimpigia kelele kwani hakukuwa na mabadiliko yoyote yale.

    “Askofu, njoo tuzungumze kwanza, kuna tatizo,” alisema Dk. Abdallah, alimchukua askofu na kwenda naye pembeni.

    “Kuna tatizo gani?”

    “Luciana.”

    “Amefanyaje?”

    “Si unajua ana mimba?”

    “Ndiyo.”

    “Ishatimia mwezi wa tisa, tumeangalia na kugundua kwamba bado mtoto ni mzima, ila sasa….”

    “Kuna nini?”

    “Ooopsss….anatakiwa kufanyiwa oparesheni kwa ajili ya kumtoa mtoto huyo. Ila kuna mawili.”

    “Mawili yapi hayo?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Anaweza kufa au kupona. Kufa ni asilimia sabini ila kupona ni asilimia thelathini. Kama kuomba, naomba muombe sana na Mungu wenu awasaidie, mana’ke ni asilimia kumi na tano tu ya watu wanaokuwa katika hali hii hupona,” alisema Dk. Abdallah, kijasho chembamba cha hofu kikaanza kumtoka askofu. Mwili wake ukaanza kumtetemeka, akajikuta akishusha pumzi ndefu kwani hata uso wa daktari yule ulionyesha wasiwasi mkubwa.

    “Wa kwanza kufa ni Luciana…..” ilisikika sauti moyoni mwake, japokuwa alijaribu kuikemea kwa kuamini kwamba ilikuwa ni sauti ya shetani, lakini bado sauti ile iliendelea kumsisitiza kwamba mtu wa kwanza aliyetakiwa kufa ni Luciana.

    ****

    Askofu alijaribu kukemea, alikemea zaidi na zaidi lakini bado sauti ile haikutoka kichwani mwake, aliisikia vilivyo ikiendelea kumwambia kwamba mtu wa kwanza kufa alikuwa Luciana. Hakuweza kujua kama sauti hiyo ilikuwa ni ya Mungu, yake au ya shetani.

    Alizungumza na Dk. Abdallah kwa kipindi kirefu na kisha kutoka ndani ya ofisi ile na kuwafuata washirika wake walipokuwa. Hakuonekana kuwa na furaha, kwa kumwangalia tu wala usingeweza kujiuliza kama mtu huyo alikuwa na mawazo au la.

    “Njooni tukemee,” alisema askofu, alikuwa akiwaambia washirika mbalimbali waliokusanyika mahali hapo, walichokifanya ni kushikana mikono na kuanza kukemea.

    Baada ya hapo, akawaelezea washirika hao kile kilichokuwa kikiendelea kwamba ujauzito wa Luciana ulifikia muda wa kujifungua na hivyo alitakiwa kufanyiwa oparesheni.

    “Ni kitu kibaya sana kumzalisha mtu na wakati hana fahamu, cha msingi tuendelee kumuomba Mungu tu,” alisema mshirika mmoja huku akionekana kuwa na hofu usoni mwake.

    ****

    Vijana wawili waliojifanya kuwa madaktari waliovalia makoti yao marefu wakaingia ndani ya eneo la hospitali hiyo. Kwa kuwaangalia tu usingeweza kugundua kwamba vijana hao hawakuwa madaktari kama walivyokuwa kwani mbali na makoti meupe waliyokuwa nayo, shingoni walikuwa na mashine za kusikilizia mapigo ya moyo huku mikononi mwao wakiwa na mafaili makubwa.

    Kila aliyewaona aliwapa heshima waliyostahili huku watu wengine wakiwafuata na kutaka kusikilizwa. Hawakuwa na habari nao, walichokuwa wakikitaka ni kutekeleza mpango mzito waliokuwa nao, kumuua Emmanuel na mkewe, Luciana waliokuwa hoi kitandani.

    Walipofika nje ya chumba kile, washirika kadhaa walikuwepo mahali hapo, mlango ulikuwa umefungwa na hakukuwa na mtu yeyote aliyeruhusiwa kuingia kwani Luciana alitakiwa kuhamishwa na kupelekwa katika chumba cha kujifungulia, ‘labour’.

    Walipowaona madaktari hao feki, hawakuweza kugundua, walichokifanya ni kuwapisha njia ili waweze kuingia ndani ya chumba kile na kuendelea na kazi zao. Japokuwa askofu aliwahi kuzungumza na vijana hao tena katika kipindi walichokuja na kujifanya washirika kutoka katika Kanisa la Praise And Worship lililopo Morogoro lakini kwa kipindi hicho hakuweza kukumbuka chochote kile.

    Walipoingia ndani, kijana mmoja akachukua sindano yake kutoka kwenye mfuko wa koti lake na kisha kumsogelea Emmanuel pale alipolala. Hakuonekana kuwa na huruma, kazi kubwa aliyokuwa amepewa ni kuwaua watu hao pasipo kuuliza swali lolote kwamba walifanya nini na kwa nini walitakiwa kufa.

    Sindano ile ilikuwa na sumu iitwayo Meprothiagro, sumu kali iliyokuwa na uwezo wa kumkausha mtu yeyote ndani ya masaa mawili tu. Alichokifanya, akaichukua dripu ya maji iliyotundikwa juu ya Emmanuel na kisha kuichoma na sindano ile, alipomaliza, akafanya hivyohivyo kwa Luciana.

    “Ishaanza kuingia,” alisema kijana mmoja.

    “Basi tusepe, si ndiyo mtaalamu alituambia tufanye hivi tu?”

    “Ndiyo.”

    “Basi tuondoke kabla madaktari hawajafika na kuwa msala.”

    Hakukuwa na muda wa kupoteza mahali hapo, walichokifanya ni kuufungua mlango na kuanza kuondoka mahali hapo. Washirika wakawa na maswali yasiyokuwa na majibu. Madaktari wale feki waliokuwa wameingia walitumia muda mdogo mno kufanya kazi tofauti na siku nyingine.

    Walikwishazoea kwamba madaktari wanapoingia humo, huchukua zaidi ya saa moja na ndipo hutoka, ila kwa siku ile, madaktari wale walichukua muda mfupi sana kana kwamba wagonjwa walikuwa wamerudiwa na fahamu.

    “Wagonjwa wanaendeleaje?” aliuliza askofu.

    “Wanaendelea vizuri, muda si mrefu watazinduka.”

    “Kweli?”

    “Ndiyo!”

    “Amen! Utukufu kwa Mungu,” alisema askofu huyo huku akiinua mikono yake juu na kutoa ishara ya kumshukuru Mungu.

    Madaktari feki hao wakaondoka huku wakiwa wamewaacha watu katika matumaini makubwa kwa kuona kwamba wagonjwa hao wangeweza kupona muda wowote ule. Walikaa kwa takribani dakika kumi, Dk. Abdallah akafika huku akiwa ameongozana na madaktari wenzake.

    “Leo tumechelewa kuja kwa kuwa tulikuwa kwenye kikao kuhusu wagonjwa wenu, tunataka tuwahudumie vizuri na tufanye kila linalowezekana kuhakikisha kwamba wanapona kabisa” alisema dokta huyo huku washirika wote wakiwa kimya.

    “Sawa dokta, ila kulikuwa na madaktari wengine walikuja, wamesema kwamba wagonjwa wanaendelea vizuri, tunamshukuru Mungu kwa hilo,” alisema askofu huku akionekana kuwa na furaha.

    “Unasemaje?”

    “Kuna madaktari walikuja.”

    “Madaktari?”

    “Ndiyo!”

    “Madaktari gani?”

    “Wawili, walikuja na kuingia ndani, wakawajulia hali wagonjwa na kisha kuondoka.”

    “Mmmh!”

    “Vipi tena? Mbona unaguna?”

    “Hao madaktari! Madaktari wote tuliokuwa tunahusika na kuwahudumia wagonjwa hawa tulikuwa kwenye kikao, sasa hao ni madaktari gani?” aliuliza Dk. Abdallah.

    Wasiwasi wake ukaibua hofu kwa wahirika wote akiwemo askofu mwenyewe. Kitendo cha kusema kwamba kulikuwa na madaktari waliokuwa wamekuja na kisha kuwahudumia wagonjwa hao na kuondoka, kilimshtua.

    Kwa haraka pasipo kupoteza muda Dk. Abdallah na wenzake wakaingia ndani ya chumba kile, kitu cha kwanza walichokifanya ni kuwaangalia kama walikuwa na mabadiliko yoyote yale. Mapigo yao ya moyo yalidunda kama kawaida lakini hilo halikuwafanya kuona kwamba kila kitu kilikuwa salama.

    “Kuna kitu, hebu yachukue haya maji ya kwenye dripu,” alisema Dk. Abdallah, dokta mwingine akafanya hivyo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Wakachukua hizo dripu na kuweka dripu nyingine na hizo kwenda nazo maabara kwa ajili ya vipimo. Walipofika huko, hawakutaka kupoteza muda, wakaanza kufanya kila kitu kilichotakiwa kufanyika, na dakika kumi na tano baadae ikagundulika kwamba kuliwekwa sumu iliyokuwa na nguvu ya kuua kwa kuukausha mwili.

    “Give me Physolodin NH2,” alisema Dk. Abdallah na kuletewa dawa hiyo.

    Physolodin NH2 ilikuwa moja ya dawa yenye nguvu ambayo ilitumika zaidi katika kuua sumu nyingi zilizokuwa zikiingizwa katika mwili wa binadamu. Ilikuwa dawa kali ya kupambana na sumu hizo na kama mtu aliyewekewa dawa hiyo hakuwa na sumu yoyote ile mwilini mwake, basi mtu huyo angeweza kupata matatizo makubwa, hivyo madaktari kuwa makini sana kutumia dawa hiyo kwa wagonjwa wao.

    “Vipi hapo?”

    “Joto limeanza kupanda.”





    “Hebu wawekeeni Sychrophine 13, changanyeni na MorphyneHP,” alisema Dk. Abdallah na kisha madaktari wenzake kufanya kama walivyoambiwa kwa kuchanganya dawa hizo katika dripu zile.

    Hakukuwa na mtu aliyekuwa na amani, kila mmoja alikuwa na wasiwasi tele kwa kuona kwamba jambo la hatari lingeweza kuwatokea wagonjwa hao, kufariki dunia kutokana na sumu kali waliyokuwa wamewekewa ambayo husahambulia zaidi damu huku ikipenya mpaka ubongoni.

    Walijitahidi kwa kadiri walivyoweza lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote yale. Hofu ikazidi kuwaingia kwamba watu hao wangeweza kufariki kwa kuhisi kwamba walikuwa wamekwishachelewa sana mpaka sumu hiyo kuingia mwilini zaidi.

    “Vipi hali zao?” aliuliza Dk. Abdallah.

    “Hali ni mbaya dokta, nahisi tulichelewa.”

    “Hapana. Mmewawekea dawa kama nilivyoagiza?”

    “Ndiyo dokta, si uliona tulivyofanya kama tulivyoagiza!”

    Wala haukuchukua muda mrefu. Emmanuel na Luciana wakaanza kutingishika vitandani pale, walionekana kama watu waliotarajia kukata roho muda wowote ule. Madaktari wakachanganyikiwa, yaani juhudi zote walizokuwa wamezifanya, mwisho wa siku hazikuweza kubadilisha kitu chochote kile.

    Wakajitahidi kuwaongezea dawa nyingine zaidi lakini hali ikawa kimya, mapigo ya moyo yakaanza kupungua, miili yao ikaanza kupoatwa na ubaridi hali iliyowafanya kuhofia na kukata tamaa kwamba ndani ya dakika chach, wawili hao wangeitwa marehemu.

    “Mungu wasaidie,” alijikuta akisema Dk. Abdallah, pamoja na utaalamu wake wote, wa kusoma kwa zaidi ya miaka kumi, naye alionekana kukata tamaa, alijua kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kila kitu, kama kushindwa, alikuwa amekwishashindwa.

    ****

    Walitumia ujuzi wao wote kuyaokoa maisha ya wagonjwa waliokuwa wamewekewa sumu katika dripu za maji. Walionekana kama wafu wanaopumulia mashine za hewa safi.

    Hakukuwa na msaada mwingine ambao wangeweza kuufanya, kama kujitahidi, walijitahidi mpaka pumzi ya mwisho lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika. Mapigo yao ya moyo, yakaonekana kuanza kushuka taratibu huku miili yao ikianza kuwa ya baridi hali iliyowafanya kuwa katika hali mbaya na madaktari kugundua kwamba muda wowote ule wagonjwa wale wangeweza kufa.

    Madaktari wote wakatoka ndani ya chumba kile, walikuwa wamenyong’onyea na hakukuwa na yeyote aliyekuwa radhi kuzungumza na washirika wale. Wangewaambia nini? Je lingekuwa jambo jepesi kuwaambia kwamba wagonjwa wao walikuwa katika hatua za mwisho kuishi katika dunia hii? Je wangewaambia kwamba wagonjwa wao waliwekewa sumu kwa ajili ya kuyakatisha maisha yao? Je wangeweza kuwaambia kwamba walijitahidi kuyaokoa maisha yao lakini kila kitu kilionekana kwenda ukingoni? Hakika wasingeweza kufanya hivyo,.

    “Dokta....” aliita askofu lakini tofauti na siku nyingine, Dk. Abdallah hakugeuka nyuma, aliendelea kusonga mbele.

    Askofu hakutaka kubaki mahali hapo, hakuonekana kukubaliana na kile kilichokuwa kikiendelea, alitaka kufahamu ni kitu gani kilitokea mpaka kuwa katika hali hiyo. Alijua kwamba wagonjwa wale walikuwa kwenye hali mbaya mno, na pengine walikuwa wamekwishakufa, lakini pamoja na hiyo yote, alitaka kufahamu kila kitu.

    #Watakao share leo simulizi hii kutumiwa simulizi nzima inayofuata kabla ya kesho share ujiachie na sehemu inayofuata

    ITAENDELEA SIKU YA KESHO HAPA HAPA

    Kasi yake ya kukimbia ikaishia ndani ya ofisi ya Dk. Abdallah. Dokta huyo alikuwa nyuma ya meza yake, alionekana kuwa na mawazo mno hali iliyompelekea kujua kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kimeendelea ndani ya chumba kile.

    “Dokta kuna nini huko?” aliuliza askofu huku akionekana kuwa na hofu.

    “Hali imekuwa mbaya.”

    “Kivipi?”

    “Hao watu walioingia, hawakuwa madaktari, bali walikuwa watu wabaya waliotaka kuwamaliza wagonjwa,” alisema Dk. Abdallah.

    “Mungu wangu!”

    “Ndiyo hivyo. Nisingependa kukwambia hili lakini wakati mwingine nahisi kwamba natakiwa kukwambia ili uelewe kile kinachoendelea, wagonjwa wapo kwenye hali mbaya mno kiasi kwamba muda wowote ule....”alisema Dk. Abdallah na kubaki kimya.

    “Muda wowote nini?”

    “Wanaweza kufariki,” alisema Dk. Abdallah kinyonge.

    Moyo wa askofu ukanyong’onyea, hakuamini kile alichokuwa amekisikia, alimwangalia Dk. Abdallah mara mbilimbili. Kichwa chake kikaanza kujiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu, pasipo kutarajia, akajikuta akianza kububujikwa na machozi mashavuni mwake.

    Hakutaka kuendelea kubaki ndani ya chumba kile na daktari ambaye alionekana kukata tamaa, alichokifanya ni kutoka na kuelekea nje ya chumba kile, kule walipokuwa washirika wengine.

    Uso wake ulionyesha kila kitu kwamba hakuwa sawa kitu kilichowafanya washirika wengine kuhuzunika kwa kujua kwamba kuna jambo baya lililokuwa limetokea.

    “Kuna nini?” baba yake Luciana aliuliza huku naye akionekana kuwa kwenye sintofahamu.

    “Njooni tuombe,” alisema askofu na kuanza kuomba tena.

    ****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Japokuwa sumu ile ilikuwa imeingizwa miilini mwao kwa kupitia mishipa yao lakini dawa walizozitumia madaktari wale kuiondoa sumu ile iliwasaidia mno kwani kwa kiasi fulani, baada ya mapigo ya moyo kushuka, masaa matatu baadae mapigo yakaanza kurudi tena na kuwa kawaida.

    Waliendelea kubaki kitandani wakiwa kimya mpaka Dk. Abdallaha alipoingia na kuanza kuwasogelea. Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kuanza kusikiliza mapigo ya mioyo yao, kitu kilichoonekana kumshangaza, mapigo yao yalikuwa yakidunda kawaida tofauti na siku zilizopita.

    Hakuamini, akawaangalia vizuri, hakuwa akiamini kile alichokuwa amekiona, alichokifanya ni kuwaambia madaktari wenzake muujiza uliokuwa umetokea, kila mmoja akawa na furaha moyoni mwake.

    Askofu na washirika wake waliporudi kwa mara nyingine tena, wakapewa taarifa kwamba wagonjwa wao walikuwa wakiendelea vizuri japokuwa waliwekewa sumu katika miili yao, sumu ambayo kwa namna moja au nyingine ndiyo ilionekana kuwa dawa ya kuwafanya kuwa katika hali hiyo.

    Bado madaktari waliendelea kufuatilia maendeleo yao hasa Luciana ambaye alikuwa na ujauzito uliofikisha miezi tisa. Walikuwa wakimchukua vipimo ili kujua ni siku gani ambayo mtoto angekuwa tayari tumboni kwa ajili ya kutolewa

    Siku zikaendelea kukatika, baada ya wiki moja, madaktari wakamchukua Luciana na kumpeleka katika chumba cha kujifungulia. Huko ndipo kazi ya kumtoa mtoto wake tumboni ikaanza kufanyika.

    Haikuwa kazi nyepesi, walichukua zaidi ya masaa manne na ndipo wakafanikiwa kumtoa mtoto wa kike tumboni mwake, mtoto aliyeonekana kuwa na afya njema iliyowaridhisha madaktari wote.

    “Mungu ametenda!” alisema Dk. Msuya huku akimchukua mtoto yule na madaktari wengine wakianza kazi ya kumshona Luciana.

    Mtoto alikuwa akipiga kelele mno, alikuwa akilia kwa sauti ya juu iliyowafanya washirika waliokuwa nje ya chumba kile kuanza kushangailia, hawakuamini kama Luciana angeweza kujifungua salama kutokana na hali aliyokuwa nayo.

    Japokuwa alikuwa mtoto mdogo ambaye hakutakiwa kuangaliwa na watu wengi lakini washirika wale hawakutaka kukubali, walichokitaka ni kumuona mtoto huyo hata kabla wazazi wake hawajaamka katika usingizi wa kifo.

    “Kazuriiii....” alisikika msichana mmoja akiwaambia wenzake huku akimwangalia mtoto yule.

    “Amefanana na mama yake, aiseeeee,” aliongezea msichana mwingine.

    Siku zikaendelea kukatika huku washirika hao wakifika hospitali hapo kila siku. Baada ya miezi miwili kukatika, hatimae Emmanuel na mke wake wakaanza kurejewa na fahamu zao.

    Mtu wa kwanza kabisa kurudiwa na fahamu alikuwa Emmanuel, aliyafumbua macho yake na kuangalia huku na kule. Kitendo cha kuona dripu ikiwa imetundikwa kwa juu tu akajua kwamba hapo alipokuwa ilikuwa ni hospitali.

    Macho yake hayakutulia, japokuwa yalifumbuka kwa tabu lakini akaanza kuyapepesa huku na kule. Aliwaona manesi wakiendelea kufanya usafi, alitamani kuwaita lakini sauti yake haikutoka kabisa.

    Hakuutikisa mwili wake, alibaki kitandani hapo huku akitamani kuwaita manesi hao. Kitendo cha manesi hao kuyapeleka macho yake na kumuona Emmanuel amerudiwa na fahamu, kitu cha kwanza wakapiga kelele na mmoja wao kutoka chumbani mule kumfuata dokta kumwambia kile kilichokuwa kimetokea chumbani mule.

    Japokuwa muda ulikuwa umekwenda sana lakini Dk. Abdallah alikuwa hospitalini pale, kitendo cha kuitwa na kuambiwa kwamba Emmanuel alikuwa ameyafumbua macho yake, kilimshtua hivyo kuinuka kitini na kwenda kuhakikisha kwa macho yake.

    Alipofika, akajikuta akimshukuru Mungu kwa muujiza mkubwa aliokuwa ameufanya. Walichokifanya ni kuendelea kumhudumia kwa kumuongezea dripu nyingine ya maji huku wakiendelea kumsikilizia Luciana.

    Askofu aliporudi hospitalini hapo na washirika wake, walipopewa taarifa kwamba Emmanuel alikuwa ameyafumbua macho yake, wakashtuka, wakaanza kumshukuru Mungu kwa muujiza mkubwa aliokuwa ameufanya.

    Kama kuomba, waliomba sana, walitegemea muujiza kutokea lakini muda ulikwenda sana kiasi kwamba wakaanza kukata tamaa. Leo hii, watu waliokuwa wakiwaombea kila siku, mmojawapo alikuwa ameyafumbua macho yake kitu kilichoonekana kuwa muujiza mkubwa.

    “Asante Yesu! Daaah! Kama naota,” alisema askofu huyo, moyo wake ulimshangilia Mungu.

    Baada ya siku mbili, Luciana naye akarudiwa na fahamu, akayafumbua macho yake na kuanza kuyapepesa huku na kule. Hakufahamu pale alipokuwa zaidi ya kuona dripu ikiwa imetundikwa juu yake.

    ****

    Patrick akawa na uhakika kwamba vijana aliokuwa amewatuma walifanya kama alivyotaka wafanye, hakuwa na wasiwasi hata kidogo kwani moyo wake ulimwambia kwamba kazi aliyokuwa amewapa, tayari ilikuwa imekamilika.

    Kitu alichotaka kukisikia mahali hapo ni kile kilichokuwa kimeendelea, kwamba watu aliotaka wafe, wamekufa na hivyo kuendelea na maisha yake, kwani hakukuwa na kitu kilichokuwa na uzito moyoni mwake kama kisasi.

    Hakuwapenda hata siku moja, alijiona kuwa mtu mwenye bahati mbaya katika ulimwengu huu, kukataliwa na msichana mrembo kama Luciana kilimuumiza moyoni mwake.

    Baada ya siku mbili, vijana wale aliowatuma wakafika nyumbani kwake na kumwambia kwamba kazi ilifanyika, waliwawekea sumu katika dripu zile na hivyo ajiandae kupokea taarifa za msiba.

    “Mmefanikisha?”

    “Kabisa bosi, wewe jiandae kupokea taarifa za msiba, hatujajua mazishi yatafanyikia wapi,” alisema kijana mmoja huku akionekana kuwa na uhakika juu ya kile alichokuwa akikizungumza.

    “Nashukuru sana, sasa nitaishi kwa amani,” alisema Patrick.

    Alichokifanya ni kuingia chumbani kwake ambapo huko akachukua kiasi cha fedha kilichokuwa kimebakia na kuwamalizia vijana wale. Bado moyo wake uliendelea kuwa na furaha na kujiona kwamba hakukuwa na siku ambayo alikuwa na furaha kubwa kama siku hiyo.

    Maisha yakaendelea, hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote ule na hata kutaka kuwasiliana na wazazi wa Luciana, hakutaka kabisa.

    Baada ya wiki moja, Patrick akaanza kupata mabadiliko. Kitu cha kwanza kabisa, moyo wake ukakosa amani, katika kila kitu alichokifanya, akakosa raha kabisa. Alijitahidi kufanya mambo ambayo kila siku aliamini kwamba yalimpa furaha lakini hakukuweza kubadilika kitu chochote kile, bado aliendelea kuwa vilevile.

    “Kuna nini ndani yangu? Mbona sina furaha na amani?” alijiuliza lakini akakosa jibu.

    Alichokifanya ni kuwapigia simu wazazi wake na kuwauliza kama kila kitu kipo sawa, wote wakamwambia kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile, tena jambo zuri ni kwamba biashara yao ya mazao ilikwenda vizuri kabisa.

    “Mama!” alijikuta akiita.

    “Unasemaje?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Nahisi nina tatizo,” alisema Patrick, wakati huo walikuwa wakizungumzia simuni.

    “Tatizo gani?”

    “Sijajua.”

    “Sasa kwa nini useme una tatizo?”

    “Sijisikii amani moyoni, sina furaha, kila ninachotaka kufanya, sina amani kabisa,” alisema Patrick.

    “Tatizo nini?”

    “Sijajua mama. Yaani nimechanganyikiwa.”

    Alikuwa na fedha, mali na kila kitu alichokuwa akikihitaji kwa wakati huo, alikuwa nacho. Alikumbuka kila kitu alichokuwa nacho na hata fedha ambazo zilikuwa zikiingia katika akaunti yake kutokana na biashara alizokuwa akizifanya, pamoja na hayo yote hakuwa na furaha kabisa.

    Wiki mbili baadae, Patrick akafanikiwa kumpata msichana mrembo wa sura, mwenye umbo zuri ambaye kama ungefanikiwa kumuona, usingethubutu kusema kwamba alikuwa mzuri, aliitwa Getrude.

    Alikutana na msichana huyu katika mihangaiko yake ya kila siku, akatokea kumpenda na kwa sababu umri ulikuwa umekwenda sana, akaamua kumwambia kwamba alitaka kumuoa.

    Sharti la kwanza kabisa aliloliweka msichana huyo ni kwenda kuwaona wazazi wake kwani kulikuwa na wanaume wengi waliotumia tekniki ya kutaka kuoa kupata wasichana.

    Kwa Patrick wala halikuwa tatizo, kwa kuwa alidhamiria na kile alichokuwa akikitaka, akaenda kuwaona wazazi hao ambao nao wakamwambia lingekuwa jambo jema kama angeanza kwenda kanisani, akafanya hivyo.



    Pamoja na mambo yote hayo, bado furaha haikurudi moyoni mwake. Kuna kipindi alikuwa akikaa peke yake, Biblia mkononi na kuanza kufikiria tatizo lilikuwa nini. Alikumbuka kwamba inawezekana kwa sababu aliwaua Emmanuel na Luciana ndiyo lilikuwa chanzo, hivyo akaanza kuomba sana, alikemea na kukemea lakini hali iliendelea kubaki vilevile, amani haikurudi moyoni mwake.

    “Mchungaji....” alimuita mchungaji wake.

    “Unasemaje Patrick.”

    “Sina amani moyoni.”

    “Kwa nini?”

    “Sijui kabisa.”

    “Nini kilitokea?”

    Kile kilichotokea kilikuwa siri yake, hakutaka kumwambia mtu yeyote yule, alijua kwamba alifanya jambo baya la uuaji na hivyo alitaka kila kitu kiendelee kuwa siri yake.

    Hakutaka kumwambia mchungaji, alichomwambia ni kwamba aondoke na arudi tena kumsimulia kilichotokea katika maisha yake. Hakutaka kurudi mwezi huo, baada ya mwezi mmoja kupita, hapo ndipo Patrick akarudi kwa mchungaji na kuanza kumuelezea kila kilichotokea.

    “Una moyo mchungaji?” aliuliza Patrick kwa sauti ndogo.

    “Nina moyo, wewe niambie nini kilitokea, inawezekana hicho ndicho kinachokuskosesha amani,” alisema mchungaji, hapohapo Patrick akaanza kulia.

    ****

    Hakunyamaza, bado aliendelea kulia kwa uchungu. Huo ndiyo ulikuwa wakati wake wa kutubu dhambi zake zote alizokuwa amezifanya. Japokuwa wakati mwingine alikuwa akisali peke yake chumbani na kumuomba msamaha Mungu, lakini aliona suala la kuusema uovu wake na kisha kuomba msamaha lilikuwa jambo jema.

    Alihadithia kila kitu kilichotokea katika maisha yake, toka siku ya kwanza alipokutana na Luciana, kuwekeana ahadi chini ya mbuyu na kisha kuelekea Dar. Hakuacha kitu chochote kilichotokea kati yeye na msichana huyo, mpaka siku zile alizokuwa akisalitiwa, mapenzi kupungua na hata barua zake kutokujibiwa, kila kitu alikiweka wazi.

    Aliendelea mbele zaidi mpaka siku zile alizoamua kwenda Mjini Bagamoyo, akasimama chini ya mbuyu na kisha kuanza kulalamika juu ya kile kilichokuwa kimetokea na msichana yule jini kumtokea na kumueleza kilichokuwa kimetokea.

    “Aliamua kumpa adhabu ya kuwa kichaa, Luciana akapata ukichaa ghafla,” alisema Patrick huku akilia, alikuwa akiongea kwa sauti ndogo na iliyoeleweka sana.

    “Baada ya hapo, kipi kilitokea?” aliuliza mchungaji.

    “Sijajua, ila baada ya miaka mit6ano, Emmanuel akataka kumuoa Luciana.”

    “Alimuoa?”

    “Alimuoa ila si siku ile kwani nilipinga harusi hiyo isifanyike,” alisema Patrick.

    Aliamua kufunguka kila kitu kilichotokea, japokuwa aliumia sana lakini hakutaka kunyamaza kwa kuamini kwamba baada ya kusimulia hayo, angeweza kujisikia amani moyoni mwake.

    Aliendelea kusimulia kwa mtindo wa kuulizwa maswali na mchungaji na kisha kuyajibu. Aliamua kuweka wazi hivyo hata suala lake la kumuua Emmanuel na Luciana aliliweka wazi pasipo kusitasita.

    “Kwa hiyo uliamua kuwaua?”

    “Ndiyo mchungaji! Hiki kitu kimekuwa kikiniumiza sana moyoni mwangu,” alisema Patrick huku akijitahidi kuyazuia machozi yake yasitoke tena.

    Kitu alichokijua ni kwamba Emmanuel na mke wake walikuwa wameuawa hospitalini. Kila siku akawa mtu wa kuomba msamaha huku akimsihi Mungu amsamehe kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea kwani kwa wakati huo, moyo wake uliamua kubadilika kabisa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Siku zikaendelea kukatika, aliendelea kumtumikia Mungu katika roho na kweli. Japokuwa alikuwa mtu mzuri machoni pa wanadamu lakini bado moyo wake uliendelea kuwa vilevile, hakujisikia amani hata kidogo.

    Aliumia, hakujua ni kitu gani alitakiwa kukifanya, kama kuomba aliomba sana lakini bado hakukuwa na mabadiliko yoyote yale. Siku zikaendelea kukatika mapaka pale alipoamua kumuoa mchumba wake, Getrude, harusi iliyohudhuriwa na watu wengi wakiwepo wafanyabashara wakubwa Tanzania.

    “Hatimae nimekuoa, hakika sikutaka kukuchezea,” alisema Patrick huku akionekana kuwa na furaha.

    “Sikuwa nikikuamini na ndiyo maana nikakwambia uende kuwaona wazazi wangu,” alisema Getrude.

    ****

    Hali ya Emmanuel na mkewe ziliendelea kutengemaa na baada ya mwezi mmoja, wakaweza kufumbua midomo yao na kuanza kuzungumza tena. Ulikuwa muujiza mkubwa, washirika hawakuweza kuamini kama baada ya miezi mingi kupita hatimae watu hao waliweza kufumbua midomo yao na kuzungumza tena.

    Wakamshukuru Mungu kwa kila kitu kilichotokea. Zilipita siku kadhaa, watu hao wakaanza kutembea tena. Mbali na furaha ya kupona na kuanza kurudi katika hali zao za kawaida, walikuwa na furaha zaidi hasa mara baada ya kusikia kwamba walikuwa na mtoto wa kike.

    “Ataitwa Glory, acha tumpe Mungu utukufu kwa kila kitu kilichotokea kwani pasipo neema yake, tusingekuwa hapa,” alisema Emmanuel.

    Waliendelea kubaki hospitalini, na baada ya kujisikia wapo vizuri kabisa, wakaruhusiwa na kurudi nyumbani. Huko, wakaanza kumshukuru Mungu na baada ya wiki moja, wakarudi tena kanisani na kuendelea na huduma kama kawaida.

    ****

    “Kumbe wapo hai? Imekuwaje? Hawakufa? Nini kilitokea?” yalikuwa maswali kadhaa yaliyokuja mfululizo kichwani mwake mara baada ya kuliona tangazo kwamba kungekuwa na mkutano mkubwa ambao ulitarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Jangwani huku mhubiri mashuhuri, Emmanuel Kihampa akitarajia kutoa huduma katika mkutano huo.

    Patrick alikuwa amelishika tangazo hilo mikononi mwake, hakuamini kile alichokuwa akikona kwamba watu ambao aliamini kuwa walikufa hospitalini, leo hii walikuwa hai na waliandaa mkutano mkubwa wa Injili.

    Alichokifanya ni kuinuka. Alionekana kuwa na furaha kubwa, hakuamini macho yake kabisa. Akatoka chumbani alipokuwa amekaa na kuelekea sebuleni ambapo akamkuta mke wake akiangalia televisheni.

    Hakutaka kuzungumza kitu, akaanza kupiga hatua kuelekea nje huku tangazo lile likiwa mikononi mwake.

    “Kuna nini?” aliuliza Getrude.

    “Kuna sehemu nakwenda mke wangu.”

    “Wapi?”

    “Subiri! Nitakwambia nikirudi.”

    “Mume wangu....”

    “Nina haraka mke wan.....” alisema Patrick lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, akatoka nje. Akaelekea katika sehemu ya maegesho ya magari na kuchukua gari lake na kuondoka mahali hapo.

    Huku akiwa njiani, akachukua simu yake na kumpigia mchungaji wake ili amwambie mahali alipokuwa akiishi mchungaji Emmanuel, akaambiwa kwamba alikuwa akiishi Kijitonyama, akaelekea huko.

    Kwa kuwa mpangilio wa nyumba ulikuwa mzuri, hakupotea, alijikuta akiegesha gari nje ya nyumba hiyo, alipopiga honi, geti likafunguliwa na mlinzi.

    “Habari yako!” alimsalimia mlinzi.

    “Salama, nikusaidie nini?”

    “Nahitaji kumuona mchungaji.”

    “Sawa. Nimwambie anauliziwa na nani?”

    “Patrick.”

    Mlinzi akaondoka mahali hapo, Patrick alibaki garini huku akiwa na mawazo tele. Hakuamini kama Emmanuel angeweza kumsikiliza mara baada ya mambo yote mabaya aliyowahi kumtendea na mkewe.

    Wala haukuchukua muda mrefu, geti likafunguliwa na kuambiwa aingie, akaliingiza gari ndani ambapo macho yake yakagongana na ya watu aliokuwa akiwachukia kipindi cha nyuma, Emmanuel na mkewe, Luciana huku wakiwa wamembeba mtoto wao kipenzi.

    Patrick akalipaki gari na kuteremka. Pamoja na kuwafanyia mambo mengi mabaya, nyuso za watu hao zilitawaliwa na tabasamu pana lililomtia moyo kwa kuona kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile.

    Hiyo ilikuwa siku ya kipekee, hakuwa na chuki tena, aliwapenda kwa kuwa maisha yake yalibadilishwa. Katika hali ambayo hakuitegemea, moyo wake ukarudi katika hali ya kawaida, hali ya kutokuwa na amani, furaha ikatoweka kabisa, akajikuta akianza kulia.

    Ilikuwa ni siku ya kuomba msamaha, kwa kila kitu alichokuwa akikiongea, alibaki akilia tu, alibubujikwa na machozi kwa kiwango kikubwa sana lakini mwisho wa siku, akasamahewa.

    “Mungu husamehe na sisi hatutakiwi kukaa na visasi au vinyongo mioyoni mwetu. Tunajua kwamba haukuwa wewe, kulikuwa na nguvu fulani iliyokuwa ikikusukuma kufanya mambo yale, kwa moyo mmoja, tumekusamehe Patrick,” alisema Emmanuel.

    “Nashukuru sana,” alisema Patick na kuwakumbatia.

    Kila kitu kilichotokea katika maisha yake, kikasahaulika, akaanza upya, furaha ikaongezeka katika maisha yake, hakuwa na huzuni tena, hakujutia alichokuwa amekifanya kipindi cha nyuma kwa kuwa alihitajika kusahau kila kitu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Baada ya miezi kumi, mke wake, Getrude akajifungua mtoto wa kiume na kumpa jina la Godbless kwa kuamini kwamba Mungu alikuwa amembariki. Hakutaka kukumbuka kitu chochote kile alimuacha Luciana akiendelea na maisha na mumewe huku naye akiendelea kumtumikia Mungu katika maisha yake na familia yake.



    MWISHO



0 comments:

Post a Comment

Blog