Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

PENZI KABLA YA KIFO - 1

 













    IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



    *********************************************************************************

    Simulizi : Penzi Kabla Ya Kifo

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    “Kwani inahusu?”

    “Subiri kwanza...usipaniki Elizabeth, kuna swali nataka kukuuliza.”

    “Nimesema sihitaji maswali.”

    “Lakini Elizabeth! Unajua Tanzania inakuheshimu sana, sasa imekuwaje mpaka ukavaa vile? Tena mbele za watu, watoto wote Tanzania walikuwa wakiangalia kipindi kile, ukajianika tu na vivazi vyako vya uchuro.”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwani kuna tatizo? Mbona nyie mnakuwa washamba sana, mbona wakina J.Lo hamuwaambii? Juzikati Kim Kardashian alivaa vilevile, mlimwambia? Au kisa amefanya Elizabeth? Hebu nitolee uchuro wako huo, kama hauna hela, sema nikupe, kama hauna cha kuandika, kaandike kuhusu mama yako,” alisikika msichana mrembo Elizabeth, baada ya kutamka maneno hayo, akaingia ndani ya gari lake la kifahari, Ferrari 458 Spiderlenye gharama zaidi ya milioni mia nne na kuondoka zake.

    Elizabeth DicksonMarcel alikuwa mwanamitindo aliyekuwa na jina kubwa Afrika, alifanikiwa zaidi, alibuni mavazi yake mwenyewe na kuyasambaza nchi mbalimbali duniani kiasi kwamba akatengeneza jina na kumfanya kuwa maarufu mkubwa hata zaidi ya mwanamke yeyote yule barani Afrika.

    Mara kwa mara alikuwa mtu wa kuonekana kwenye magazeti, maisha yake yaliyojaa vituko yaliwashangaza watu wengi kiasi kwamba hawakujua kitu alichokitafuta kwani kama jina kubwa, alikuwa nalo, kama ni fedha, alikuwa nazo na za kutosha kabisa na kumfanya kuwa bilionea.

    Waandishi wa habari hawakumuacha, japokuwa kila siku alisema kwamba anachukia kufuatiliwa na waandishi hao lakini hawakuacha kumfuatilia, kila walipomuona baa akinywa na mwanaume, habari yake iliandikwa, walipomuona akiingia kwenye gari la mwanaume mwingine, pia habari hiyo ikaandikwa.

    Japokuwa hakuishiwa vituko, lakini Elizabeth alitokea kupendwa mno, watu walimheshimu kwa kuwa alikuwa mtafutaji sana, kichwa chake kilikuwa na akili ya kutafuta fedha, kila alipokaa, alifikiria fedha na hata wanaume alikuwa akitoka nao kimapenzi, ni wale waliokuwa na fedha tu ambao aliamini wangeweza kumpa njia nyingi za kutafuta za kutafuta fedha hizo.

    Kitu kilichowashangaza watu wengi ni kwamba Elizabeth hakuwa mtu wa kuvaa mavazi ya heshima, kila siku alivalia nguo fupi sana, mapaja yalikuwa wazi au kuvaa nguo alizozibuni ambazo zilionyesha asilimia tisini ya mwili wake.

    “Huyu Elizabeth anakera sana, anavaa mavazi mafupi tu, yananikera lakini nashangaa nampenda sana, na ukiniuliza nampendea nini, wala sijui, mimi nampenda tu” alisema msichana mmoja, alikuwa shabiki mkubwa wa Elizabeth.

    “Hata mimi nampenda sana! Sijali uvaaji wake, hata akitembea mtupu mitaani, wala sijali, mimi nampenda tu,” alisema msichana mwingine.

    Pamoja na kupenda sana kujianika kwa mavazi yake mafupi na yenye kuonyesha umbo lake kwa asilimia kubwa lakini huyu Elizabeth alikuwa na moyo wa huruma, alipenda kuwasikiliza watu waliokuwa na shida mbalimbali na kuwasaidia kitu kilichompa heshima kubwa japokuwa maisha yake ya upande wa pili yalikuwa hovyo.

    Kila siku watu mbalimbali waliokuwa na matatizo kiafya walifika nje ya nyumba yake ya kifahari iliyokuwa Mbezi Beach, walihitaji msaada wake. Wengine walitoka mikoani wakiwa na matatizo makubwa ambayo yalihitaji kiasi kikubwa cha fedha hospitalini.

    Kutokana na moyo wa huruma aliokuwa nao Elizabeth, wala hakuwa mbinafsi, kila aliyefika nyumbani kwake, alimsaidia pasipo kuangalia ngozi au tofauti za kidini, kwake, kila mtu alionekana kuwa sawa.

    Baada ya kusaidia watu kwa kipindi kirefu, akaamua kuanzisha hospitali yake binafsi kwa ajili ya wagonjwa wa moyo tu. Alijua kwamba mamia ya Watanzania walikufa kwa magonjwa ya moyo, hivyo alivyotaka ni kuwa na hospitali ya magonjwa hayo ili wagonjwa watibiwe hapo na si kusafirishwa kwenda India kama ilivyokuwa.

    Jina lake lilikua kila siku, wasichana wengi wakampenda na hivyo nao kutamani sana kuwa na umaarufu na akili ya kutafuta fedha kama aliyokuwa nayo Elizabeth. Hakuruhusu jina lake liingie kwenye bidhaa yoyote ile pasipo kupewa fedha, alijua kwamba jina lake lilikuwa biashara kubwa, lilikuwa na thamani kubwa na liliwavuta watu wengi kununua kitu ambacho kilihusisha jina na picha yake, hivyo akalitumia vilivyo.

    Ingawa alikuwa na jina kubwa, kuwa na utajiri mkubwa lakini mpaka kipindi hicho Elizabeth hakufanikiwa kupata mtoto. Hicho ndicho kilikuwa kilio chake cha kila siku, alijitahidi kuzianika hisia zake katika vyombo vya habari huku akilia lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika kabisa.

    Alijuta, kuna kipindi alimlaumu Mungu kwamba alimuonea lakini kila alipofikiria kwamba kulikuwa na wanawake waliopata watoto kisha watoto kufariki, akajikuta akibadilisha mawazo yake na kumshukuru Mungu.

    Moyo wake uliteseka, usiku alipokuwa peke yake kitandani, muda mwingi ulikuwa ni kufikiria ni kwa namna gani angeweza kupata mtoto. Alitembea na wanaume wengi, wenye fedha lakini hakufanikiwa kupata mtoto.

    Akatembelea kwa waganga wengi, kila mtu aliyejitangaza kwamba angeweza kumtibu tatizo lake alimfuata lakini hakukuwa na matumaini yoyote yale. Akaamua kuachana na waganga wa jadi na hivyo kusafiri mpaka Ulaya, huko akafanyiwa uchunguzi, kila kitu kilionekana kuwa sawa, hata madaktari walipoona kwamba hashiki mimba walishindwa kufahamu tatizo lilikuwa nini, walishangaa lakini bado msichana Elizabeth hakuweza kupata mtoto.

    “Au niokoke kama zamani? Ngoja nifanye hivyo!”

    Huo ndiyo uamuzi alioufikia, akaamua kuokoka huku lengo lake likiwa ni kupata mtoto lakini bado hakufanikiwa, hali ilikuwa vilevile, hakuweza kupata mtoto kitu kilichomfanya kulia usiku kucha.

    “Candy! Tatizo langu nini?” aliuliza Elizabeth huku akilia.

    “Usilie Elizabeth! Kuna siku utapata mtoto, niamini,” alisema Candy.

    “Una uhakika?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo! Ninaamini utakuja kupata mtoto, wewe vumilia tu,” alisema Candy.

    Huyo ndiye alikuwa rafiki wake wa kufa na kuzikana, hakukuwa na mtu mwingine aliyekuwa karibu naye kama msichana Candy. Popote alipokuwa, alikuwa na msichana huyo na popote pale alipokwenda, Candy alikuwa pembeni yake.

    Alijua mambo yake mengi kuhusuElizabeth, alifahamu leo aligombana na nani na kesho alikuwa na mwanaume gani. Hitaji kubwa la Elizabeth, mzigo mkubwa aliokuwa nao ulikuwa wake pia, walishibana kuliko marafiki wote.

    “Candy....” aliita Elizabeth.

    “Unasemaje?”

    “Umemuona mwanaume yule tuliyepishana naye?”

    “Yupi?”

    “Yule aliyevalia suti nyeusi.”

    “Hapana! Kafanyaje?”

    “Ni mzuri mno! Alivyotabasamu ameufanya moyo wangu kushtuka sana.”

    “Kwa hiyo turudi?”

    “Hapana! Tuendelee na shughuli zetu tu,” alisema Elizabeth.

    Wakati huo walikuwa Mlimani City, walikwenda kufanya manunuzi yao ya kawaida. Wakati wanaingia ndani ya jengo hilo kubwa ndipo walipopishana na jamaa huyo.

    Elizabeth alimwangalia kwa sekunde kadhaa, alikuwa mwanaume mzuri wa sura, aliyemvutia mno, alivalia miwani huku mkononi akiwa ameshika mfuko uliojaza vitu alivyotoka kununua.

    Elizabeth akashindwa kuvumilia, naye akatoa tabasamu pana ambalo aliamini kwamba hakukuwa na mtu aliyemuona, kisha kupishana.

    Utulivu ukapotea ndani ya duka hilo kubwa, watu waliokuwa mahali hapo mara baada ya kumuona Elizabeth, wakaanza kumfuata huku wengine wakitaka kupiga naye picha. Alikuwa msichana maarufu sana, kukutana naye sehemu ilikuwa ni bahati kubwa kwani wengi walikuwa wakimuona magazetini na mitandaoni tu.

    “Kwachaaaa...kwachaaa...” ilisikika miale ya kamera, kila mtu alikuwa bize kumfuata Elizabeth.





    Watu waliokuwa wakiendelea na shughulia zao, wakaziacha na kisha kumsogelea Elizabeth na kutaka kupiga naye picha tu. Ilionekana kuwa usumbufu, japokuwa alikuwa amefika dukani hapo kwa ajili ya kufanya manunuzi yake binafsi, uwepo wa watu wengi waliokuwa wakimfuata kila alipokwenda, ulimkera.

    Hakujali wala hakuringa, kila aliyetaka kupiga naye picha, akafanya hivyo, baadaye kabisa, akaingia ndani ya duka kubwa la nguo na kisha kununua nguo kadhaa na kuondoka mahali hapo huku akifuatwa na kundi la watu nyuma yake.

    “Candy!”

    “Abee!”

    “Mwanaume mwenyewe yule pale amesimama nje ya gari lake,” alisema Elizabeth huku akimwangalia mwanaume yule aliyeonekana nadhifu mno, alikuwa akizungumza kwenye simu huku akiwa ameliegemea gari lake la gharama, Hammer nyekundu.

    “Ngoja nimfuate nikazungumze naye.”

    “Elizabeth, huoni watu wanavyokuangalia?”

    “Hata kama, siogopi chochote kile, acha nimfuate,” alisema Elizabeth,

    Hakutaka kuvumilia, moyo wake ulikwishakufa na kuoza kwa mwanaume huyo ambaye alimuona mara moja tu na kumpenda, akaanza kumsogelea, mapigo ya moyo yaliongezeka, alitaka kumwambia ukweli, hakutaka kuvumilia kuona akiteseka, alichokuwa akikihitaji kilikuwa ni mapenzi kutoka kwa mwanaume huyo.

    Japokuwa alikuwa amezunguka kwa wanaume wengi pasipo kupata mtoto yeyote yule, akashindwa kujizuia, alipokuwa akimwangalia mwanaume huyo, moyo wake ulimwambia kwamba angeweza kupata mtoto kupitia huyo, hivyo alitaka kuhakikisha anamwambia ukweli kwamba anampenda, hata kama angemkataa, lakini alitaka kumwambia ukweli ili awe huru.

    Wakati akiendelea kumsogelea huku watu wengi wakimfuata, akiwa amebakiza hatua ishirini kabla hajamfikia, mara mlango wa gari aliloegemea mwanaume yule ukafunguliwa, mwanamke mmoja akateremka, alikuwa mzuri wa sura, alivutia, alimbeba mtoto wake mdogo, akamfuata mwanaume yule na kusimama pembeni yake, akazungumza naye kidogo, wakaingia garini.

    Hakukuwa na siku Elizabeth aliyoumia kama siku hiyo, hakujua kama yule mwanamke aliyeteremka kutoka garini alikuwa mke wa yule mwanaume au rafiki yake. Akahisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake, akabaki amesimama huku akiliangalia lile gari ambalo liliwashwa na kuondoka mahali hapo.

    “Haiwezekani!” alisema Elizabeth, hapohapo akalifuata gari lake la kifahari, akaufungua mlango na kuingia ndani.

    “Vipi Elizabeth!”

    “Mwanaume yule anafaa kuwa mume wangu! Sitaki mwanaume mwingine zaidi ya yule,” alisema Elizabeth huku akionekana kuchanganyikiwa, hapohapo akawasha gari na kisha kuanza kulifuata gari lile, akili yake kwa wakati huo ilichanganyikiwa mno. Donge kubwa la mapenzi likaung’ang’ania moyo wake.

    Elizabeth hakukubali, moyo wake ulikufa na kuoza, hakutaka kuona mwanaume mzuri kama yule akimkosa, alitaka kumpata, awe mume wake wa dhati kwa kuamini kwamba ingewezekana hata kupata mtoto kwa mwanaume huyo.

    Aliendesha gari kwa kasi kidogo kuelekea Mwenge kupitia kwenye Barabara ya Sam Nujoma, walikuwa wakiendelea kulifuatilia gari lile ambalo liliendeshwa kwa mwendo wa kasi kuelekea Mwenge. Hawakutaka kulipita, waliendelea kulifuatilia mpaka lilipochukua Barabara ya Bagamoyo kuelekea Mbezi Beach.

    Kilichomuuma ni uwepo wa mwanamke yule garini mule, hakujua kama alikuwa mkewe au dada yake, moyo wake uliumia mno mpaka yeye mwenyewe kujishangaa.

    Siku ya kwanza tu kumuona mwanaume yule, akatokea kumpenda na hata alipomuona na mwanamke mwingine, akahisi kuwa na wivu mkali moyoni mwake.

    “Candy!”

    “Abeee!”

    “Hivi yule mwanamke ni nani?”

    “Sijui! Labda mkewe,” alisema Candy pasipo kujua ni kwa namna gani jibu lake lilivyomuumiza Elizabeth.

    “Haiwezekani! Hawezi kuwa na mume mzuri kiasi kile, yule anatakiwa kuwa na mwanamke mzuri kama mimi,” alisema Elizabeth.

    “Ndiyo! Ila utafanya nini kama utagundua kwamba yule ni mkewe?”

    “Tutaona, chochote nitaweza kufanya, hata kama kutumia utajiri wangu wote! Nipo radhi, ili mradi nimpate tu” alisema Elizabeth.

    Alimaanisha alichokisema, hakuwa na utani hata kidogo. Kila alipomfikiria mwanaume yule, moyo wake ulimpenda mno. Waliendelea kulifuatilia gari lile, lilipofika Afrikana, gari likakata kona na kuchukua barabara ya upande wa kulia. Nao walikuwa nyuma kama kawaida.

    Alichohitaji kujua ni mahali alipoishi mwanaume yule, alikuwa makini barabarani, kila walipopita, kwa kuwa gari lake lilikuwa la kifahari na lilijulikana sehemu nyingi, watu walikuwa wakilipiga picha tu.

    Mbele wakakutana na makutano ya barabara, gari halikuchukua barabara nyingine zaidi ya kusonga mbele, lilipofika lilipokuwa likielekea, taa zikaanza kuwaka kuashiria kwamba lilitakiwa kuingia katika jumba moja kubwa la kifahari. Dereva akaanza kupiga honi.

    Hicho ndicho alichotaka kuona, alipoona hivyo, akaridhika na hivyo kugeuza gari, kwa sababu alijua mahali alipokuwa akiishi mwanaume yule, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo.

    “Tuondoke, nishapafahamu! Nitarudi siku nyingine,” alisema Elizabeth na kisha kuondoka mahali hapo.

    Siku hiyo ilikuwa ni ya kumfikiria mwanaume yule tu, hakuwa akimfahamu lakini alijihisi kuwa na mapenzi mazito juu yake. Kitandani, hakulala kama siku nyingine, alipofumba macho, taswira ya mwanaume yule ilimjia kichwani mwake kitu kilichompa wakati mgumu kupatwa na usingizi.

    Alikuja kupatwa na usingizi saa saba usiku, muda wote huo alikuwa akiendelea kumfikiria tu. Alipoamka saa tatu asubuhi, kitu cha kwanza kabisa ni kumpigia simu Candy na kumtaka kufika nyumbani kwake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ninataka unisindikize sehemu,” alimwambia rafiki yake huyo.

    “Wapi tena?”

    “Kule kwa jana, ninataka kuonana na yule mwanaume leo hiihii,” alisema Elizabeth.

    “Mmh!”

    “Mbona unaguna.”

    “Tutamuona vipi?”

    “Wewe twende tu,” alisema Elizabeth.

    Alikuwa rafiki yake mkubwa ambaye kwa kifupi ungeweza kusema kwamba ndiye aliyemuweka mjini, Candy hakuwa na jinsi, akakubaliana naye na hatimaye safari ya kuelekea Afrikana kuanza.

    Hawakutaka kutumia gari walilotumia jana yake, wakabadilisha gari kwani lile lilijulikana mno kwa kuwa hakukuwa na mtu aliyekuwa akiendesha gari la thamani nchini Tanzania zaidi yake, gari lile likawa nembo, kila lilipoonekana, watu walijua kwamba mahali hapo kulikuwa na Elizabeth.

    Hawakuchukua muda mrefu, wakafika walipokuwa wakienda. Alichokifanya Elizabeth ni kuteremka na kisha kuwafuata wanaume kadhaa waliokuwa pembezoni mwa bahari ili kuwauliza.

    “Za saa hizi!” aliwasalimia.

    “Aaah! Elizabeth!”

    “Ndiyo mimi! Samahanini kama nitawapotezea muda wenu.”

    “Hakuna tatizo mrembo!”

    “Ninauliza ni nani anaishi nyumba ile pale,” alisema Elizabeth huku akiinyooshea kidole nyumba ile.

    “Kuna jamaa fulani hivi anaitwa Edson, mmiliki wa ile hoteli kubwa ya Amazon Five ya kule Upanga, yeye ndiye anaishi mule.”

    “Ana mke?”

    “Ndiyo, tena na mtoto mmoja.”

    “Sawa. Ofisi yake ipo wapi?”

    “Ipo pale kwenye Jengo la Ubungo Plaza, pia ni meneja wa Kampuni ya Ndege ya Flying 15, ukifika hapo, ukimuulizia, utaambiwa alipo,” alisema kijana mmoja.

    “Umesema anaitwa Edson?”

    “Ndiyo! Edson Gwamanya.”

    “Nashukuru!”

    Hakutaka kuwaacha vijana wale hivihivi kwani walionekana kuwa msaada mkubwa mno kwake, hivyo akawapa fedha ili wagawane. Hiyo haikutosha, walichokiomba ni kupiganaye picha, hilo wala halikuwa tatizo, akapiga nao picha na kuondoka huku akiwaacha wakiwa na furaha mno.

    Kidogo moyo wake ukaridhika, kitendo cha kuambiwa mahali alipokuwa akifanyia kazi Edson kidogo ilimridhisha, hakutaka kulaza damu, alichokifanya ni kuelekea huko huku akiwa na furaha mno.

    Walitumia dakika arobaini mpaka kufika katika jengo refu la Ubungo Plaza ambapo wakateremka na kuanza kuelekea ndani. Kila mtu aliyemuona Elizabeth, alibaki akimkodolea macho, msichana huyo alikuwa na mvuto mkubwa mno, kila alipopita, watu walikuwa bize kumwangalia tu.

    “Samahani! Ninamuulizia Edson Gwamanya,” alisema Elizabeth, alikuwa akizungumza na msichana mmoja ndani ya jengo hilo.

    “Yupo ghorofa ya saba,” alisema msichana yule na kumpa maelekezo zaidi ya kufika huko.

    Hawakutaka kupoteza muda, wakaelekea sehemu ya kupanda lifti na kusubiri kwa nje. Watu hawakuchoka kumwangalia, kila aliyemuona, alibaki akimkodolea macho huku wengine wakishindwa kuvumilia na kujikuta wakimsalimia huku nyuso zao zikitawaliwa na tabasamu pana.

    Lifti ilipofika chini, ikafunguka, wakapanda na kuanza kupanda juu. Moyo wa Elizabeth ukaanza kudunda kwa nguvu, hakujiamini kabisa, alijikuta akianza kutetemeka kwani kukutana na mwanaume huyo kwa mara ya pili kulimtia hofu moyoni mwake.

    Lifti ilipofika ghorofa ya saba, ikasimama na kisha kuteremka. Macho yao yakatua katika mlango ulioandikwa Flying 15, wakaanza kupiga hatua kuufuata mlango huo, muda wote huo mapigo ya moyo wa Elizabeth yalizidi kudunda zaidi, hakuonekana kujiamini hata mara moja.

    “Subiri kwanza,” alisema Elizabeth, alimsimamisha Candy.

    “Kuna nini?”

    “Mbona nahofia hivi?”

    “Jamani! Hebu jipe nguvu, tuumalizie huu mkia, tushamla ng’ombe mzima,” alisema Candy, Elizabeth akashusha pumzi nzito.

    Wakapiga hatua mpaka walipoufikia mlango ule na kisha kuufungua, mtu wa kwanza kukutana naye alikuwa sekretari ambaye walimsalimia na kisha kukaa katika viti vilivyokuwa mahali hapo.

    Kipindi chote sekretari yule alibaki akimwangalia Elizabeth, alikutana na msichana aliyekuwa supastaa, aliyependwa na wanawake wengi, kila alipomtazama, alijisikia raha moyoni mwake.

    “Karibuni sana,” alisema sekretari huku akitoa tabasamu pana.

    “Ahsante. Tunaweza kumuona meneja?”

    “Hakuna tatizo.”

    Alichokifanya sekretari ni kuchukua ile simu ya mezani na kisha kumpigia meneja wake, wala simu haikuita kwa kipidi kirefu, ikapokelewa na Edson ambapo akamwambia kwamba awaruhusu wageni hao waingie ndani.

    Waliporuhusiwa, wakaanza kuufuata mlango wa kuingia ndani ya ofisi ile. Candy alikuwa mbele huku Elizabeth ambaye ndiye aliyekuwa na shida ya kuonana na mwanaume huyo akiwa nyuma.

    Walipoingia tu, kitendo cha Elizabeth kumuona Edson, mapigo ya moyo wake yakaongeza kasi ya kudunda, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, kila alipomwangalia Edson ambaye uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, uzuri aliokuwa nao ukazidi kuongezeka huku Elizabeth akahisi kama yupo ndotoni, kukukutana na mwanaume mzuri kama alivyokuwa Edson ilikuwa moja ya tukio lisiloaminika machoni mwake.

    “Karibu,” aliwakaribisha Edson, kitendo cha Elizabeth kuisikia sauti ya Edson tu, akahisi ngoma za masikio yake zikianza kucheza. Alifarijika kupita kawaida.

    Alimini kwamba duniani kulikuwa na wanaume wengi, ila hakukuwa na mwanaume aliyemzidi uzuri yule aliyekuwa mbele yake, yule aliyeonyesha tabasamu huku akionekana kuwa mtu mchangamfu mno, Edson.

    Kila alipomwangalia, alihisi akimpenda zaidi ya alivyokuwa akimpenda kabla, sura yake ilimvutia na kila alipoendelea kumwangalia, aliamini kwamba hakukuwa na mwanamke yeyote aliyestahili kuwa na mwanaume huyo zaidi yake.

    Alitamani kupata nafasi zaidi ya kuzungumza naye, amwambie ukweli juu ya alivyokuwa akijisikia, hata kama atakataliwa, ajue lakini si kuona mwanaume huyo akipita huku mwanamke mwingine ambaye kwake alionekana kutokuwa na hadhi ya kutembea naye akiwa ameolewa na kuwekwa ndani kabisa.

    “Huyu namfahamu, anaitwa Elizabeth! Sijui wewe unaitwa nani?’ aliuliza Edson, muda wote uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana.

    “Naitwa Candy!”

    “Ok! Karibu sana!”

    “Ahsante. “





    Wote wakanyamaza, walikuwa kama watu waliosakiziana kuzungumza. Japokuwa Elizabeth alikuwa na hamu kubwa ya kumwambia Edson alivyokuwa akijisikia moyoni mwake lakini kwa wakati huo, kila kitu kikasahaulika.

    “Mnazionaje huduma zetu?” aliuliza Edson baada ya kuona ukimya wa muda mrefu.

    “Ni nzuri mno, ninapenda kusafiri na ndege zetu, ninazipenda sana, ni safi, zina uwezo, nawapongeza sana,” alisema Elizabeth, hakuwahi kupanda ndege za Shirika hilo la ndege lakini aliamua tu kusifia tu.

    “Ahsante sana Elizabeth, pia ninapenda ubunifu wako, ni mzuri sana, u mwanamke wa tofauti sana, unajitoa kwenye kutafuta chapaa, hakika kila mwanaume anatamani kuwa na mwanamke kama wewe,” alisema Edson na kumalizia kwa tabasamu pana.

    Wakati wakizungumza hayo, mawazo ya Elizabeth yalihama kabisa, alichokiona ndani ya moyo wake ni kwamba alikuwa na Edson sehemu fulani, ndani ya chumba huku wakiwa wamelala na kufanya kila kitu usiku huo huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha mno.

    “Elizabeth...” aliita Candy baada ya kumuona rafiki yake akiwa kimya, tena kwenye lundo la mawazo.

    “Abeee!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Edson hakuzungumza kitu, alivyoona namna msichana huyo alivyoshtuka kutoka katika lindi la mawazo, alibaki akicheka tu. Hata yeye alimkubali sana Elizabeth, alikuwa msichana mrembo lakini kamwe hakutaka kumsaliti mke wake.

    “Nitahitaji unibunie vazi moja zuri la kike, vazi ambalo halijawahi kutokea nchini Tanzania, ninataka iwe zawadi kwa mke wangu,” alisema Edson.

    “Hakuna tatizo, nitafanya hivyo, nakuahidi utalipenda,” alisema Elizabeth.

    Japokuwa naye alirudisha jibu kwa tabasamu pana lakini moyo wake haukuwa na furaha hata kidogo, kile alichokuwa amejiuliza, alipata jibu la uhakika, achana na wale vijana waliokuwa ufukweni, kitendo cha kujua kwamba mwanaume huyo alikuwa ameoa, kilimuumiza sana, akahisi kama kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake.

    “Naombeni niende washroom kwanza,” alisema Candy, Elizabeth akashtuka.

    “Ooh! Hakuna tatizo, mwambie dada hapo akueleze,” alisema Edson.

    Candy akasimama na kutoka ndani ya ofisi hiyo. Kitendo cha kubaki wawili ndani ya ofisi ile, hapo ndipo Elizabeth akagundua kwamba Candy alifanya vile ili kuwaacha wawili hao peke yao, yaani Elizabeth atupe ndoano yake na hatimaye kumnasa Edson.

    Akabaki kimya kwa muda, alikuwa akijifikiria ni kitu gani alitakiwa kumwambia Edson. Alikumbuka kwamba usiku uliopita hakulala kwa raha kwa kuwa tu mawazo juu ya mwanaume huyo yalimsumbua mno. Siku hiyo, Edson alikuwa mbele yake, kwa muonekano wake tu, ulionyesha kwamba alikuwa tayari kusikia chochote kile kutoka kwake.

    “Edson...” aliita Elizabeth.

    “Niambie.”

    “Unajitahidi sana kwenye ufanyaji wako wa kazi, nimekufuatilia kwa kipindi kirefu, hakika wewe ni mchapakazi,” alisema Elizabeth.

    “Ahsante sana Elizabeth! Hata wewe pia, una jina kubwa, pia unajitoa sana, hakika unastahili kuwa hapo ulipo,” alisema Edson.

    Mpaka Candy anarudi ndani ya ofisi hiyo, hakukuwa na cha maana kilichoendelea zaidi ya mazungumzo ya kawaida tu. Elizabeth aliumia kwani alipewa muda wa dakika kumi nzima lakini hakuzigusia hisia zake kwa mwanaume huyo.

    Mpaka wanaaga na kuondoka huku wakiwa wamebadilishana namba za simu, Elizabeth hakuamini kama mikwara yake yote aliyokuwa nayo kabla angeweza kunywea mara atakapokutana na mwanaume huyo.

    “Vipi? Ulimwambia?”

    “Hapana!”

    “Eeeh! Hukumwambia tena?”

    “Niliogopa, yaani mapigo ya moyo yalinidunda sana,” alisema Elizabeth.

    “Jamani! Yaani presha yote ile ya jana na leo umeibuka kapa?”

    “Yaani wewe acha tu shoga yangu! Sijui kwa nini.”

    Waliendelea kuzungumza mpaka wakaingia ndani ya gari, Elizabeth alitamani arudi ofisini mule na kumwambia Edson namna alivyojisikia moyoni mwake lakini hakukuwa na nafasi hiyo tena,.

    “Ila namba ya simu si umeipata, sasa maliza kila kitu huko,” alisema Candy.

    Kuwa na namba ya Edson kulimpa moyo kwamba angeweza kumpata mwanaume huyo. Kila wakati alikuwa mtu wa kuiangalia namba ile, alitamani kupiga na kuzungumza naye, japo aisikie sauti yake tu aridhike lakini aliona kwamba jioni ndiyo ungekuwa muda mzuri wa kuzungumza naye.

    Saa ziliendelea kukatika, ilipofika saa 12 jioni, akachukua simu yake na kisha kuiangalia namba ile, hakutaka kukubali, alichokifanya ni kuanza kumpigia Edson. Simu haikuita sana, ikapokelewa na sauti ya Edson kusikika.

    “Hallo!”

    “Hallo Edson, u mzima?”

    “Nipo poa Eliza. Mlifika salama?”

    “Yeah! Nimefurahia mapokezi yako! Mungu akubariki,” alisema Elizabeth.

    “Amen!”

    “Sawa. Bye bye!”

    “Bye!”

    Alikuwa akipanga mistari mingi ya kumwambia Edson lakini kitu cha ajabu alipompigia simu, maneno yale yote yalifutika kichwani mwake jambo lililomfanya wakati mwingine kujiona mjinga.

    Siku hiyo ikakatika hivyohivyo, alikuwa na mawazo mengi juu ya mwanaume huyo. Kesho yake, asubuhiasubuhi, muda ambao alijua kwamba Edson alikuwa kazini akampigia simu na kuanza kuzungumza naye, akaomba miadi ya kuonana naye kwa mara nyingine ili amgawie kitabu kilichokuwa na nguo mbalimbali ambazo aliona kwamba staili moja ingemvutia hivyo kushonewa mke wake.

    “Sawa! Njoo ofisini, ila wahi, saa sita nitaingia kikaoni,” alisema Edson.

    “Nipe nusu saa.”

    Hakutaka kuchelewa, hata hakutaka kumpa taarifa Candy, kwa kuwa alikuwa amekwishaoga asubuhi hiyo, alichokifanya ni kuanza kuelekea huko Ubungo kwa ajili ya kuonana na Edson tu.

    Kama kawaida watu hawakuacha kumshangaa, alikuwa mtu maarufu mno na kuonana naye ilikuwa ni bahati sana, kila alipopita, aliangaliwa mpaka mwenyewe kujisikia aibu lakini hakujali.

    Akapanda lifti na kwenda mpaka kwenye ofisi ya Edson, alipofika, moja kwa moja akaruhusiwa na kuingia ndani. Alipoyakutanisha macho yake na Edson tu, hapohapo mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu, kwa siku hiyo, alijipanga vilivyo, hakutaka kushindwa hata mara moja, alihitaji kumwambia ukweli mwanaume huyo.

    “Umependeza sana,” alisema Edson huku akimpa mkono.

    “Ahsante sana.”

    Walizungumza mawili matatu na kisha Elizabeth kuchukua kitabu kile kilichokuwa na picha kadhaa za mavazi na kumsogelea Edson kule alipokuwa, kuizunguka meza na kusimama karibu yake kisha kukiweka kitabu kile mezani, kwa jinsi mapigo yake ya moyo yalivyokuwa yakidunda, hata Edson aliyasikia kwa mbali.

    “Elizabeth! Upo sawa?”

    “Kwa nini?”

    “Hapana! Nimeuliza tu!”

    “Nipo sawa!”

    “Basi hakuna tatizo! Haya nionyeshee sasa,” alisema Edson, wakati huo, mawazo ya Elizabeth hayakuwa hapo kabisa, alikuwa akijifikiria namna ya kumuingia mwanaume huyo. Walikuwa wawili tu ofisini, tena karibukaribu mno. Hiyo akaiona kuwa nafasi yake kumaliza mchezo.

    “Edson.....”

    “Naam.”

    “Unanukia vizuri kweli!”

    “Ahsante!”

    “Unatumia pafyumu gani?”

    “The Prince...”

    “Waooo! Ya kiume?”

    “Ndiyo! Nililetewa na mke wangu kutoka Uholanzi! Naipenda sana, hata ikiisha, huwa ananiagizia,” alisema Edson.

    Elizabeth akabaki kimya kwa muda, mapigo ya moyo wake yalikuwa yakidunda kwa nguvu mno, Edson alibaki akikiangalia kitabu kile lakini uwepo wa msichana yule pembeni yake, tena kwa ukaribu kabisa kulimnyima amani.

    Alitamani kumwambia atoke lakini aliuona mdomo wake kuwa mzito kufanya hivyo, alichokifanya ni kubaki kimya tu huku macho yake yakikiangalia kitabu kile.

    Kulikuwa na picha za mavazi mengi yaliyomvutia, aliyoamini kwamba kwa namna moja ama nyingine mkewe angeyapenda sana, alichokifanya ni kuchagua moja na kisha kumwambia Elizabeth kwamba lingekuwa jambo zuri sana kama angeshona vazi hilo.

    “Umelipenda?”

    “Yeah!”

    “Nashukuru! Nitakufanyia kazi hiyo! Ila kuna jingine.”

    “Lipi?”

    “Naweza kuonana nawe baadaye?”

    “Baadaye?”

    “Ndiyo!”

    “Kuna nini?”

    “Haujanijibu swali langu!”

    “Inategemea na muda!”

    “Jioni, hata saa kumi na mbili.”

    “Mmmh!”

    “Nini?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nitaangalia, ila sidhani, nitahitaji kurudi nyumbani kukaa na familia yangu!” alisema Edson huku akionekana kumaanisha alichokisema.

    Moyo wa Elizabeth ulikuwa na wasiwasi mno, alitamani sana kumwambia mwanaume huyo juu ya kilekilichokuwa kikiendelea kwamba alimpenda sana lakini hakujua ni wapi alitakiwa kuanzia.

    Alibaki kimya huku akionekana kama kuna jambo kubwa alikuwa akilifikiria mahali hapo. Edson alibaki kimya akimwangalia msichana huyo. Ni kweli alikuwa mrembo, alivutia kwa kila mwanaume ambaye angebahatika kumuona lakini kwake yeye, alimuona kuwa msichana wa kawaida, mawazo yake yote yalikuwa kwa mkewe tu.

    Elizabeth alipoona ameshindwa kabisa, akaamua kuondoka ofisini hapo na kurudi nyumbani kwake. Huko, aliendelea kujuta, alipata nafasi hiyo kwa mara ya pili lakini bado hakumwambia mwanaume huyo ukweli wa moyo wake.

    Alichokifanya ilipofika jioni ni kumpigia simu na kumwambia kwamba walitakiwa kuonana, kitu kilichomuuma sana ni pale alipomwambia kwamba alitakiwa kurudi nyumbani haraka kwani alihitaji kukaa na famiia yake, baada ya hapo, simu ikakatwa.

    “Edson....Edson...nakupenda Edson...nahitaji uwe wangu Edson...” alisema Elizabeth huku machozi yauchungu yaliyojaa mapenzi yakianza kumbubujika mashavuni mwake.

    Hakukuwa na kitu kilichobadilika, kama siku nyingine, usiku wa siku hiyo alikuwa na mawazo tele, nyumbani hakukukalika, kila wakati alimfikiria mwanaume huyo kiasi kwamba alihisi angechanganyikiwa na mawazo aliyokuwa nayo.

    Kesho yake alichokifanya ni kuelekea dukani ambapo huko akanunua maua mazuri na kadi za mapenzi kisha kununua cd ambayo aliingiza nyimbo nzuri za mapenzi huku kukiwa na kipande cha karatasi kilichobeba ujumbe mzito.

    Hakuwa na kingine alichoweza kukifanya, kama kumwambia kwa mdomo, alishindwa, hivyo aliona njia nyepesi ni kuufikisha ujumbe wake kwa kutumia maandishi na vile vitu vingine alivyonunua.

    Siku hiyohiyo baada ya kukamilisha kila kitu, akachukua gari lake mpaka katika ofisi ya Edson na kumwachia sekretari kile alichokuwa amekibeba kwa ajili ya mwanaume yule aliyeuteka moyo wake kisha kuondoka zake.

    Hakujua ni kitu gani ambacho kingetokea, hakujua Edson angechukulia vipi kile alichokuwa amekifanya, kwake, aliona kwamba ile ndiyo ingekuwa njia nyepesi ya kuuteka moyo wa mwanaume huyo ambaye alikuwa na mke na mtoto wake mdogo, kwa Elizabeth, hilo wala hakutaka kujali.



    “Kuna mzigo wako bosi.”

    “Kutoka wapi?”

    “Kwa Elizabeth!”

    “Waoo! Yaani kashamaliza kushona?”

    “Sijui!”

    Alichokifanya sekretari yule ni kuchukua ule fuko uliokuwa na urembo mwingi kisha kumpa bosi wake. Edson akauchukua na kuanza kuelekea nao ndani. Alichokijua yeye ni kwamba mule ndani kulikuwa na nguo aliyomwambia Elizabeth amshonee kwa ajili ya mkewe.

    Alipofika ofisini, akaufungua mfuko ule na kuanza kutoa vitu vilivyopo ndani. Kwanza akashtuka, hakuamini kile alichokiona kwa mara ya kwanza, kitu ambacho kilikuwa cha kwanza kutoka ndani ya mfuko ule yalikuwa ni maua mekundu mawili.

    Akashtuka, akayaangalia maua yale vizuri, alionekana kama mtu aliyeshangazwa na hali ile, hakuishia hapo, akatoa vitu vingine, akakutana na kadi, alipoifungua tu, akasoma ujumbe uliokuwepo, ulikuwa ni wa kimapenzi.

    “Mungu wangu!”

    Kitu cha kingine kukitoa kilikuwa ni kipande cha karatasi, akakichukua na kisha kukifungua ndani. Kilikuwa na ujumbe mfupi ulioandikwa kwa mwandiko mzuri wa kike, maneno yaliyopangiliwa, machache na yaliyokuwa na ujumbe mfupi tu yaliyosomeka.

    Edson....

    CD imejieleza kila kitu.

    Elizabeth.

    Hapo ndipo alipoingiza mkono wake ndani ya mfuko ule, akakutana na cd moja ambayo akaichukua na kisha kuichomeka katika mlango wa laptop yake na kisha kuchukua hedifoni na kuanza kusikiliza.

    Cd ile ilikuwa na nyimbo kadhaa zilizoimbwa na waimbaji wengi wa Kimarekani, kulikuwa na Wimbo wa Fly Without Wings wa West Life, Just Go wa Lionel Rich na Never Let You Go wa Justin Bieber.

    Edson alizisikiliza nyimbo zile zote ambazo aliambiwa kwamba zilikuwa na ujumbe kuhusu kile alichokuwa akikihisi moyoni mwake juu yake. Nyimbo zote hizo zilikuwa na ujumbe mkali wa mapenzi, alipozisikiliza, alihisi kitu cha tofauti moyoni mwake.

    Hakikuwa mapenzi,ilikuwa ni chuki kubwa kwa msichana huyo, kwa kile alichokifanya, aliona kama alivuka mipaka kwani hakutegemea msichana kama Elizabeth kufanya jambo hilo ambalo aliliona kama kuingiliwa katika maisha yake na wakati alikuwa na mke aliyempenda kuliko wanawake wote.

    “Hebu subiri kwanza, kumbe hanijui,” alisema Edson kwa hasira.

    Hakutaka kupoteza muda, hapohapo akachukua simu yake, moyo wake uliwaka kwa hasira, alijiona ghafla akimchukia Elizabeth, japokuwa alikuwa msichana maarufu, mwenye fedha na mrembo mno lakini hiyo haikuwa sababu ya kumfanya kumsaliti mke wake.

    Simu ikaanza kuita, akawa na hamu ya kuisikia sauti ya msichana huyo, alitaka amtukane na kumuonya kwa kile alichokuwa amekifanya. Hakupendezwa nacho hata kidogo. Simu iliita na kuita lakini haikupokelewa, akakunja uso wake kwa hasira.

    Simu ile ikaita mpaka ikakata, hasira zikampanda zaidi. Alichokifanya ni kutoka ofisini kwake, hakutaka kukaa, kazi zisingefanyika hata mara moja, alichokitaka ni kumfuata msichana huyo nyumbani kwake, hata kama hakutaka kupokea simu, aliamini kwamba endapo angekwenda nyumbani basi angeweza kumkuta, hicho ndicho alichokifanya.

    “Kumbe huyu hanijui, sasa subiri....” alisema Edson huku akiwa na hasira kali kama mbogo. Akawasha gari na kuanza kuelekea nyumbani kwa Elizabeth aliyekuwa akiishi hukohuko Mbezi Beach.

    *****

    Simu ya Edson ilipokuwa ikiita, aliiona sana, alikuwa akiiangalia simu yake tu pasipo kuipokea. Moyo wake ulijawa na hofu kubwa, hakujua kama upigaji wa simu ile ulikuwa ni wa amani au kulikuwa na tatizo.

    Kila alipotaka kuipokea, mapigo yake ya moyo yalimdunda mno, alitetemeka mwili huku uso wake ukionekana kama mtu aliyekosa amani, akabaki akiiangalia mpaka simu hiyo ilipokatika.

    Alikwishajua kwamba mwanaume huyo alikuwa amepata kile alichomwachia sekretari, hakujua kama alifurahia au alichukia, hakujua maana ya kumpigia simu wakati ule, akabaki akitetemeka tu.

    “Vipi tena?” aliuliza Candy aliyekuwa amefika nyumbani hapo asubuhiasubuhi.

    “Hakuna kitu.”

    “Nani anakupigia simu?”

    “Edson!”

    “Sasa mbona hupokei?”

    “Naogopa!”

    “Kwa nini?”

    “Mmmh! Wewe acha tu!’

    Walibaki wakizungumza mengi, bado Elizabeth aliendelea kumwambia Candy juu ya hisia zake za kimapenzi kwa Edson kwamba alikuwa hali, halali, alichokuwa akikihitaji ni penzi la dhati kutoka kwa mwanaume huyo tu.

    “Candy! Nikwambie kitu?”

    “Niambie.”

    “Nilikwenda ofisini kwa Edson!”

    “Lini?”

    “Leo hiihii.”

    “Kufanya nini?”

    “Nilimpelekea vitu ambavyo vilionyesha ni kwa namna gani ninampenda, jamaniiii, hivi yule mwanaume kaniwekea dawa gani? Mbona nimedata hivi?” aliuliza Elizabeth huku tabasamu pana likionekana usoni mwake.

    Wakati wanazungumza mengi kuhusu Edson, mara wakasikia mlio wa honi kutoka nje ya nyumba hiyo, kitu cha kwanza alichokifanya Elizabeth ni kuchungulia dirishani, mlinzi alikwenda na kufungua geti, hakufungua geti kubwa, akafungua dogo.

    “Candy!” aliita Elizabeth kwa mshtuko.

    “Nini?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Edson!” alijibu Elizabeth huku akionekana kuwa na wasiwasi mahali hapo.

    Edson hakutaka kuzungumza chochote na mlinzi, ndiyo kwanza akamsukumia pembeni na kisha kuelekea ndani ya nyumba hiyo ya kifahari. Alipoufikia mlango, akakishika kitasa na kukifungua, akaingia ndani, macho yake yakatua kwa wasichana wawili, Elizabeth na Candy.

    Alichokifanya ni kumtupia Elizabeth ule mfuko aliokuwa amemletea ambao ndani yake ulikuwa na vile vitu alivyokuwa amempa. Alipofanya hivyo, akageuka na kuanza kupiga hatua kutoka nje, alipoufikia mlango wa sebule hiyo, hata kabla hajaufungua akageuka nyuma.

    “Nisikilize wewe malaya!” alisema Edson, alionekana kufura kwa hasira, Elizabeth akawa anatetemeka tu.

    “Kuanzia leo, sitaki unizoee kabisa, yaani sitaki unizoee hata mara moja. Siyo unajiona wewe ni malaya basi unafikiri dunia nzima wapo kama wewe. Ukinifuatilia tena, nitakupiga risasi mpumbavu weeee...” alisema Edson huku akionekana kuwa na hasira mno, alipomaliza, akaufungua mlango na kuondoka zake.

    Elizabeth alibaki akiwa amesimama kama nguzo ya umeme, hakuamini kile kilichotokea, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, hakutingishika, alibaki vilevile na ghafla machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.

    Hakutegemea kama kweli mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati angeweza kumfanyia kitendo kama kile. Alitamani hilo liwe moja ya tukio lililotokea ndotoni, alitamani kusikia rafiki yake Candy akimwamsha na kumwambia kwamba asubuhi ilikwishafika na hivyo walitakiwa kuendelea na ratiba nyingine kama kawaida.

    Kile kilichotokea, hakikuwa ndoto, ni kweli mwanaume aliyekuwa akimpenda, Edson alikuwa amefika nyumbani hapo na kumtupia mfuko uliokuwa na vitu vya mapenzi alivyompelekea kama kumuonyeshea ni jinsi gani alimpenda, ni kweli alimwambia maneno machache kwamba asidiriki kumtafuta hata mara moja.

    Elizabeth hakuamini hata kidogo, akajikuta akilisogelea kochi na kisha kutulia, sauti ya kilio kilichotoka mahali hapo kilikuwa kikubwa kilichomfanya hata Candy mwenyewe kushtuka. Ni kweli alikwishawahi kumsikia rafiki yake huyo akilia, lakini sauti ya kilio alichokitoa siku hiyo ilikuwa ni ya juu mno.

    “Nyamaza Elizabeth....” alisema Candy huku akijaribu kumbembeleza.

    Elizabeth hakunyamaza, aliendelea kulia, alipoona anabembelezwa sana huku moyo wake ukiendelea kuumia zaidi, akasimama na kuelekea chumbani kwake ambapo huko akajilaza kitandani na kuendelea kulia.

    Hakukuwa na siku ambayo moyo wake uliumia kama siku hiyo, alipoona kwamba mapenzi aliyokuwa nayo juu ya Edson yalikuwa makubwa mno, akajilazimisha kuiingiza chuki moyoni mwake lakini jambo hilo halikuwezakana kabisa, bado aliona kuwa na mapenzi mazito kwa mwanaume huyo.

    Siku hiyo hakutaka kutoka, hakutaka kuufungua mlango wa chumbani kwake. Japokuwa Candy alipiga sana hodi huku akimsisitizia aufungue mlango lakini hakufanya hivyo, aliendelea kubaki chumbani humo huku akilia.

    Usiku, hakulala, alikesha huku mawazo yake yakiwa kwa Edson tu. Kila wakati aliishika simu ile na kuiangalia namba ya Edson, alitamani kumpigia na kuzungumza naye, japokuwa alikuwa ametukanwa lakini hilo wala halikuwa tatizo, vitisho vyote alivyokuwa amepewa kwake havikumuogopesha.

    Hakutaka kujiuliza mara mbilimbili, hapohapo akampigia simu Edson huku saa yake ikimwambia kwamba tayari ilikuwa ni saa tano usiku. Simu ile ikaanza kuita, haikupokelewa, iliita na kuita mpaka ikakata.

    Hakutaka kuacha, alichokifanya ni kupiga tena, yote hayo, alikuwa akitaka kuzungumza na Edson tu kwani bado moyo wake ulikataa kabisa kumtoa mwanaume huyo. Mara ya pili wala simu haikuita sana, ikapokelewa na sauti ya Edson kusikika.

    “Hallo!” iliita.

    “Hallo Edson.”

    “Wewe Elizabeth! Nilikwambiaje?”

    “Nimeshindwa kuvumilia, kama unataka kuniua njoo uniue tu, siwezi kuona nikikukosa, nakupenda sana,” alisema Elizabeth huku akianza kulia.

    “Nimekwambia hivi....”

    “Ninakupenda Edson, ninahitaji uwe mpenzi wangu!”

    “Hivi wewe mwanamke umechanganyikiwa?”

    “Ndiyo! Nimechanganyikiwa kwa mapenzi yako, naomba unihurumie Edson....” alisema Elizabeth huku akiendelea kulia.

    Huku akiendelea kuishikilia simu, akahisi kulikuwa na mtu alimpokonya mwanaume huyo simu ile, wakati akikaa kusikilizia, mara akasikia sauti ya mwanamke ikianza kuita kwenye simu. Hakutaka kujiuliza, alijua kwamba huyo alikuwa mkewe Edson, hakukata simu, alitaka kusikiliza angesemaje.

    “Mbona unatusumbua sana Elizabeth! Hivi haukumuelewa Edson?” aliuliza mke kwa sauti iliyosikika kama mtu mwenye wivu mkali.

    “Ninajua! Ila ninampenda mumeo!”

    “Unasemaje?”

    “Ninampenda mumeo! Ni mwanaume wangu wa ndoto, sipendi kulificha hili, mwambie kwamba ninampenda sana,” alisema Elizabeth huku kilio cha kwikwi kikisikika, hakuongea sana, akakata simu hiyo na kuanza kulia kwa sauti kubwa iliyozuiliwa na mto alioulalia kwa staili ya kuufunika uso wake.





    Mapenzi ni upofu, ndivyo ilivyokuwa kwa msichana Elizabeth. Alikuwa na jina kubwa, alipendwa na watu wengi, kila alichokifanya, kilionekanakuwa baraka, alifanya biashara nyingi zilizomfanya kuwa bilionea, alijikusanyia kiasi kikubwa cha fedha na kuwa mwanamke aliyekuwa na fedha kuliko wanawake wote barani Afrika, lakini pamoja na kuwa na vitu vyote hivyo, mapenzi yalimtesa, mapenzi yalimliza kila siku.

    Mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, hakumpenda kama alivyokuwa akimpenda, aliutesa moyo wake, alishindwa kujizuia. Kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, mapenzi yalimtesa, kuanzia siku hiyo ambapo alimpigia simu na mwisho wa siku kuzungumza na mke wa Edson, hakutaka kuwasiliana naye tena.

    Akabaki akiuuguza moyo wake tu, hakufanya kazi nyingine, kila kitu alikisimamisha kwa kuwa moyo wake haukuwa kwenye mudi ya kufanya kitu chochote kile.

    Siku ziliendelea kukatika, bado alikuwa na hamu ya kupata mtoto, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, hakuwa na tatizo lolote kiafya, alikuwa mzima kabisa lakini kitu cha ajabu, hakuweza kupata mtoto.

    Kila alipowaona wanawake wengine wakiwa na watoto wao, moyo wake ulimuuma mno, alitamani naye kupata mtoto kama wengine, ampende na kumlea kwa mapenzi ya dhati. Alilia usiku mzima, kila alipokumbuka kwamba alitembea na wanaume wengi pasipo kupata mtoto, alizidi kuumia.

    Baada ya miezi miwili kupita, hatimaye maumivu yakawa yamepungua, hakumkumbuka tena Edson, aliamua kuachana naye na kufanya ishu zake nyingine. Safari hazikuisha, hakuwa mtu wa kutulia, leo alikuwa akienda nchi hii na siku nyingine alikwenda nchi nyingine.

    Hivyo ndivyo maisha yake yalivyokuwa kwa kipindi kirefu. Katika siku ambayo alibuni mavazi ya kike aliyoyaita kwa jina la ELIZYAA, watu wengi walikusanyika ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee kulipokuwa kukifanyika uzinduzi wa mavazi hayo ya kike.

    Kila mtu aliyeyaona, aliyapenda, yalikuwa mavazi yaliyobuniwa kwa ustadi mkubwa ambayo yalistahili kuvaliwa na mwanamke yeyote, sehemu yoyote ile pasipo kujali kama ilikuwa sehemu iliyotakiwa kuvaliwa mavazi ya heshima au la.

    Hayo yakawa mafanikio yake makubwa, hakuamini pale alipohitajika kueleka nchini Morocoo kwa ajili ya kufanya uzinduzi wa mavazi hayo kwani kwa mara ya kwanza bilionea kutoka nchini humo, Alhamdul Rasheed alipoyaona katika mitandao mbalimbali, aliyapenda na hivyo kuwasiliana na Elizabeth.

    “Nataka tufanye biashara! Upo tayari?” aliuliza Rasheed kwenye simu.

    “Nipo tayari!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ninataka nifanye uzinduzi wa mavazi yako huku Morocco ila kwa makubaliano fulani,” alisema Rasheed.

    “Makubaliano gani?”

    “Asilimia ishirini iwe kwangu, upo tayari?”

    “Mbona kubwa hivyo?”

    “Basi kumi na tano!”

    “Sawa! Hakuna tatizo.”

    Elizabeth alijifunza mambo mengi katika biashara kwamba hauwezi kufanikiwa kama kila kitu utataka ufanye peke yako. Ili ufanikiwe zaidi, ilikuwa ni lazima kuchangia vitu fulani na watu wengine, hivyo ndivyo ilivyokuwa.

    Alijulikana dunia nzima kutoka na bidhaa zake alizokuwa akiziuza lakini ili kujulikana zaidi alitakiwa kufanya biashara hizo na watu wengine. Hakuangalia ni kiasi gani Rasheed angepata, alichokijali ni kwamba angeweza kulitangaza jina lake zaidi na hivyo kupata kiasi kikubwa cha fedha.

    Hakuwahi kumuona Rasheed, alikuwa amewasiliana naye kwenye simu tu, alipanga kwenda nchini Morocco kwa ajili ya kuonana naye na kupanga jinsi mambo yatakavyokuwa, hivyo baada ya wiki moja, kila kitu kilipokamilika, akaanza safari yakuelekea huko kwa ndege ya kukodi.

    Baada ya saa kadhaa, ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mogador uliokuwa katika Jiji la Marrakech nchini Morocco. Kwa kuwa tiketi yake ilisomeka kama mtu maalumu, VIP, akapitishwa katika mlango wanaotakiwa kupita watu hao huku akiwa na begi lake kisha kuelekezwa mahali walipokuwa wenyeji wake walipokuwa wakimsubiri.

    “Karibu Morocco,” alimkaribisha mwanaume mmoja wa Kiarabu, alikuwa amevaa kanzu ndefu nyeupe na kilemba kilichokuwa na kamba fulani kichwani.

    “Ahsante sana,” aliitikia Elizabeth na kuanza kuelekea nje na mwanaume yule wa Kiarabu.

    Safari yao iliishia nje ya uwanja ule, alipoangalia huku na kule, kulikuwa na magari mengi ya kifahari ambayo yalipaki mahali hapo. Mazingira mazuri ya eneo hilo yalimfurahisha kwa kuwa yalivutia mno machoni mwake, kila alipoyaangalia alijikuta akiachia tabasamu pana.

    Wakalifuata moja ya magari ya kifahari yaliyokuwa mahali hapo kisha kuingia. Ilikuwa gari moja kubwa aina ya Jeep lililokuwa na rangi nyeusi. Ndani ya gari lile kulikuwa na muonekano uliomshangaza mno, alilipenda na kujikuta safari nzima akitoa tabasamu pana tu.

    Ni kweli aliwahi kukutana na magari mengi ya kifahari huku yeye mwenyewe akiwa anamiliki gari lenye thamani kubwa lakini katika maisha yake yote hakuwahi kukutana na gari kama lile aliloingia, akabaki akiliangalia tu.

    “Ni gari zuri sijawahi kuona,” alijisemea Elizabeth.

    Gari lile hakulikuwa likiwashwa kwa ufunguo, ilikuwa ikitumika sauti ya mmiliki wa gari hilo ambayo ilirekodiwa katika chombo maalumu alichokuwa nacho dereva yule ambapo mara baada ya sauti ile kusikika ikiamuru gari liwake, likawaka na dereva kushikilia usukani.

    “Hili gari ni la nani?” alijikuta akiuliza.

    “Mbona umeuliza hivyo?”

    “Ninataka kujua tu. Ni la Rasheed?”

    “Hahaha!”

    “Mbona unacheka sasa?”

    “Utajua tu. Kwanza unamfahamu Rasheed mwenyewe?”

    “Hapana!”

    “Aisee! Kwa hiyo nikikwambia mimi ndiye Rasheed!”

    “Hahaha! Nahisi sitoamini.”

    “Kwa nini?”

    “Basi tu.”

    Safari iliendelea mbele, Elizabeth alikuwa na hamu kubwa ya kumfahamu huyo Rasheed, kitu kilichojenga akilini mwake ni kwamba alikuwa mmoja wa watu wenye fedha nyingi kitu kilichomchanganya kabisa.

    Alijua kamba dereva yule alikuwa na mambo mengi ambayo angeweza kumwambia kuhusu Rasheed lakini alikuwa akimficha, alichokifanya ni kuendelea kumwambia kwamba alihitaji kumfahamu huyo Rasheed mwenyewe kwani alihisi moyo wake kuwa na kiu kubwa.

    “Utamjua tu,” hilo ndilo jibu alilopewa kila wakati alipokuwa akiuliza.

    Safari iliendelea mpaka walipofika katika mtaa uliokuwa na majumba mengi ya kifahari, kwa kuuangalia tu wala usingesumbuka kujiuliza juu ya watu waliokuwa wakiishi ndani ya mtaa huo, walikuwa ni watu wenye fedha kwani hata magari waliyokuwa wakipishana nayo yalikuwa ni ya kifahari mno.

    Gari lile likaenda na kusimama nje ya geti moja kubwa, ndani yake kulikuwa na jumba kubwa la kifahari. Alichokifanya dereva yule ni kuchukua rimoti kisha kuibonyeza kwa kuielekezea katika geti lile, hapohapo likajifungua na kisha kuliingiza gari lile.

    Mazingira aliyoyakuta ndani ya eneo la jumba hilo la kifahari yalimshangaza, kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea, bustani kubwa ya maua, magari ya kifahari zaidi ya lile alilokuwa amepokelewa nalo, kila kitu alichokuwa akikiangalia ndani ya eneo la jumba lile la kifahari, alibaki akishangaa tu.

    “Tumefika!” alisema dereva yule na wote kuteremka.

    Wakaingia mpaka ndani ya jumba lile, kila kitu alichokiona, Elizabeth alibaki akishangaa tu. Vyombo vingi vilivyokuwa ndani ya jumba hilo vilinakshiwa kwa dhahabu, kwa muonekano aliokuwa ameukuta, ulimwambia kwamba mwanaume aliyekuwa akiishi humo alikuwa mtu mwenye fedha nyingi mno.

    “Karibu sana. Ngoja nikaendelee na majukumu,” alisema dereva yule.

    “Sasa mbona unaniacha! Huyo Rasheed yupo wapi?” aliuliza Elizabeth.

    “Anakuja. Wala usijali.”

    “Sawa!”

    Akabaki sebuleni pale peke yake, macho hayakutulia, alikuwa akiangalia huku na kule, kila kitu alichokuwa akikiona kilikuwa kigeni machoni mwake. Alikuwa mwanamke bilionea, aliyeogelea sana fedha lakini kile alichokuwa amekutana nacho kilimshangaza mno.

    Wala hazikupita dakika nyingi, mara mwanaume fulani akatokea sebuleni hapo. Alikuwa Mwarabu, aliyevalia kanzu ndefu, usoni hakuwa kama watu wengine, hakuwa na ndevu hata moja, nywele zake alizinyoa kwa staili ya panki, alivalia miwani, alipofika mahali hapo, akavua miwani na kubaki akiangalia na Elizabeth.

    Elizabeth akashtuka, aliwahi kusikia stori nyingi kuhusu malaika kwamba vilikuwa viumbe vizuri mno huku akimuomba sana Mungu japo naye akutane na malaika hao ili kuona walikuwa wazuri namna gani.

    Siku hiyo alihisi kwamba Mungu alijibu maombi yake, mwanaume aliyesimama mbele yake alikuwa mzuri mno. Alipomwangalia, moyo wake ukaanza kudunda kwa nguvu, hakuamini kama duniani kulikuwa na mwanaume mzuri kama alivyokuwa yule Mwarabu aliyekuja sebuleni pale, akajikuta akianza kutoa tabasamu pana.

    “You are welcome Elizabeth! I am the one who contacted you yesterday,”(Karibu sana Elizabeth! Mimi ndiye niliyewasiliana nawe jana) alisema mwanaume yule, Elizabeth akazidi kutabasamu.

    “It’s my pleasure to meet you,” (Ni furaha yangu kukutana nawe) alisema Elizabeth kwa sauti nzuri ambayo hakuwahi kuitumia kumwambia mwanaume yeyote yule, tayari moyo wake ukaanza kufa na kuoza, alitamani japo mwanaume yule amwambie tu kwamba alikuwa akimpenda. Hakika alimhitaji, alikuwa mzuri hata zaidi ya Edson. Mwanaume huyo alikuwa Rasheed.







    Kwa jina aliitwa Alhamdul Rasheed. Alikuwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka ishirini na tano lakini alikuwa miongoni mwa matajiri wakubwa nchini Morocco. Alimiliki visima viwili vya mafuta nchini Qatar ambavyo vilimuingizia fedha nyingi mno.

    Utajiri wake ulikadiriwa kuwa dola bilioni 40 ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni themanini. Rasheed alikuwa fedha, alikuwa akiishi maisha ya kifahari, alipendwa na watu wengi kwa kuwa alikuwa kijana mdogo ambaye kila siku ndoto zake zilikuwa ni kuwaona vijana wengine kama yeye wakifanikiwa na kuwa mabilionea.

    Kila mwaka wakati wa siku yake ya kuzaliwa alikuwa akigawa kiasi cha dola milioni moja kwa vijana mbalimbali ambao walikuwa na ndoto za kuwa na fedha kama alivyokuwa nayo yeye.

    Alifungua vituo vingi kwa ajili ya kuwafundisha watu masuala ya ujasiriamali huku wakati mwingine akiingia gharama ya kuwaita walimu kutoka nje ya nchi ambao walikuwa na uwezo mkubwa kuhusu ujasiriamali.

    Aliwawapenda watu wa nchini kwake, hakutaka kuona watu wakiendelea kuwa masikini na wakati alikuwa na uwezo wa kuwafanya wawe matajiri wakubwa. Utu wake na wema ndiyo uliochochea mapenzi makubwa kwa watu mbalimbali kiasi kwamba kila lilipotajwa jina la Alhamdul Rasheed, watu walikuwa wakishangilia kwa shangwe.

    Kwa kuwa alikuwa mbunifu mzuri wa mavazi, hata alipopata utajiri, hakutaka kuiacha kazi hiyo, mara kwa mara alikuwa akienda katika kumbi mbalimbali zilipofanyika shoo za ubunifu na kuangalia kipi kilikuwa kikiendelea.

    Wanawake warembo waliokuwemo huko, walimpenda kwa kuwa hata sura yake ilikuwa na mvuto mno. Hakuwa mtu wa wanawake, japokuwa aliamini kwamba alikuwa mzuri sana lakini mbali na uzuri huo wanawake hao walihitaji fedha, walitaka kuwa naye kwa kuwa walimuona kuwa ni tajiri mkubwa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kichwa chake kilifikiria fedha, hakutaka kuyaweka mapenzi mbele, kila alipokaa, alifikiria noti za dola tu. Siku zikaendelea kukatika wasichana waliendelea kujigonga lakini badada ya kutembea nao, alitaka kujikusanyia fedha.

    Msichana Elizaeth alipoibuka, akaanza kumfuatilia, alikuwa msichana mrembo ambaye baadaye akasadikiwa kwamba alikuwa msichana maarufu Afrika Mashariki.

    Alichokifanya ni kumfuatilia kwani aligundua kwamba mbali na umaarufu aliokuwa nao, msichana huyo alikuwa na kitu cha ziada, akili ya kutafuta fedha kama aliyokuwa nayo.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog