Simulizi : Laiti Ningejua
Sehemu Ya Nne (4)
ILIPOISHIA...
“Mh! kweli yule mganga sio mtu wa mchezo mchezo.” Niliwaza baada ya kushuhudia upendo wa mume wangu ukiwa umefufuka kwa kasi ambayo sikutegemea kabisa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
ENDELEA...
Kwa kawaida chakula kinapoiva huwa kinapakuliwa kwenye hotpot kubwa halafu kinapelekwa sebuleni ili kila mtu aweze kujipakulia kiasi chake lakini ile siku haikuwa hivyo kwani baada ya chakula kuiva kwa bahati nzuri nilikuwa peke yangu jikoni, Fatuma na wanangu walikuwa sebuleni wanatazama tamthilia ambayo huwa wanapenda kuifuatilia nilitumia muda ule kuitia dawa niliyokuwa nimepatiwa na mganga katika sahani ya mume wangu. Chakula kingine nilikipakulia kwenye hotpot na kukipeleka sebuleni ili na sisi tukaweze kujipakulia. Iliniwia rahisi kutelekeza adhima yangu kwasababu pale nyumbani huwa tunakula kizungu kila mtu anapakua chakula ambacho anaweza kukimaliza. Nilikwenda chumbani kumwita Enrique wangu ili aje kula chakula ambacho kilikuwa kimeandaliwa na mke wake mpenzi. Mara baada tu ya kuanza kula chakula mume wangu alianza kukisifia chakula kwamba ni kitamu kupita kiasi.
“Chakula kitamu sana mke wangu hongera sana.”
“Asante.”
“Yaani kwa jinsi chakula kilivyo kitamu sitamani hata kumaliza kula.”
“Mbona cha kawaida tu honey!”
“Hapana leo umeonyesha ufundi wako wa mwisho.”
“Ok sweety, kula ushibe kabisa.” Nilizungumza huku moyoni nikimng’ong’a kwasababu nilikuwa nafahamu kuwa ni kalumanzira ndie alikuwa anafanya mambo. Tulimaliza kula na kwenda kulala, kusema kweli nilimshukuru Mungu kufanikisha lile zoezi gumu la kumuekea mume wangu dawa kwenye chakula bila kushtukiwa na mtu yeyote.
Kwa kadiri siku zilivyozidi kwenda ndivyo ambavyo nilizidi kushuhudia upendo wa mume wangu kwangu ambao haukuwa na mfano kwani kila mara aliniletea zawadi ambazo zilikuwa ni nzuri na za gharama kubwa. Upendo aliokuwa ananionyesha ni mkubwa kuliko hata ule wa kipindi cha uchumba wetu, ndani ya muda mfupi nilinawiri sana kwa matunzo makubwa niliyokuwa nikipatiwa na baba watoto wangu. Chochote nilichomwambia aniletee alijitahidi kwa hali na mali kunipatia kuniridhisha. Nilimpigia simu rafiki yangu Glory kumshukuru na kumweleza kwamba mambo yalikuwa yanakwenda vizuri bila tatizo lolote.
Uhusiano wangu na Fadhili uliendelea kama kawaida licha ya kupitia misukosuko kadhaa kwenye ndoa yangu, alisikitika sana nilipomweleza mambo mazito yaliyokuwa yamenisibu na alinionea huruma sana ila alihapa kutoniacha hadi mwisho wa maisha yake jambo ambalo lilinifanya niringe na kujivunia uzuri ambao nilikuwa nimejaliwa. Japokuwa sikuwa na kazi lakini sikuwai kuishiwa hata siku moja kwani nilipokuwa namwambia Enrique anipatie kiasi chochote cha pesa alinipa bila kuniuliza nakwenda kuzifanyia nini, kwahiyo nilizidi kujivinjari na Fadhili kwa kumpatia chochote anachohitaji ili asipatwe na shida yeyote kwasababu maumivu yake ni sawa na yangu. Kukosa kwangu kazi kulinipa muda mzuri zaidi wa kuweza kula maisha na mchepuko wangu kwasababu mara nyingi mume wangu anapokuwa anaelekea kazini mimi huwa naelekea kwa hawara wangu ambapo huwa nashinda kutwa nzima nikideka kifuani mwake. Kiherehere cha mume wangu kunigombeza na kunipiga pindi ninapochelewa kurudi nyumbani kilikwisha kabisa hivyo nilitengeneza tabia ya kurudi nyumbani kwangu usiku mara kwa mara kutokea kwa mchepuko wangu. Mabadiliko makubwa yaliyojitokeza katika familia yangu yalisababisha siku moja dada wa kazi akazungumza na mimi kumsifia mume wangu kwa jinsi alivyokuwa mpole.
***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
“Dada kweli baba sweetness kabadilika.”
“Kawaje.”
“Yani kawa mpole hadi raha.”
“Ndio hivo nimemwambia aache mambo ya kishamba kunichunga kama ng’ombe kwasababu mimi ni wake peke yake aondoe presha.”
“Ama kweli kaondoa presha.”
“Au wewe ulikuwa unafurahishwa na vurugu zake za kunigombeza kila mara kwa mambo yasiokuwa na maana.”
“Hapana nilikuwa sipendezwi kabisa.”
“Namshukuru Mungu nilipomuweka kitako kumweleza kwamba sifurahishwi na tabia yake alinielewa.”
“Kweli umejaliwa ushawishi wa hali ya juu sana.”
“Hahah! Ushawishi kajaliwa kila mwanamke sio mimi pekee hata wewe pia.” Ilkinibidi nimdanganye Fatuma kuhusu mabadiliko ya ghafla aliyoyashuhudia kwa mume wangu ili asizidi kushangaa.
Siku zilizidi kusonga huku nyumba yangu ikiwa imetawaliwa na amani. Watoto wangu Dylan na Logan ambao walikuwa masomoni Mombasa nchini Kenya walizidi kukua vizuri kiafya na kitaaluma wakati huo mwanangu Jordan bado alikuwa hajaanza shule kwasababu umri wake ulikuwa bado mdogo. Nilinunuliwa gari lingine aina ya Toyota mark x baada ya kulalamika nimechoshwa na Nissan Murano. Simu ya Fadhili ilikuwa ni mbovu inamsumbua na kusababisha mara kwa mara nisimpate hewani kwahiyo niliamua kumpatia ile simu yangu niliyokuwa nimeletewa na mume wangu kama zawadi kipindi aliporejea kutokea Zanzibar kikazi na mimi nilinunua simu nyingine ya bei ghali zaidi. Mawigi niliyokuwa navaa ni ya kuanzia laki mbili na kuendelea na pia nilikuwa sivai zaidi ya wiki moja. Maudhurio yangu katika maduka ya nguo yalitia fora mithili ya ruti za chooni kwasababu kila mara nilikuwa nafanya manunuzi ya nguo.
Kiukweli niliishi maisha kama ya mwanamitindo kwa namna nilivyokuwa napendeza kwa pesa nilizokuwa nikizichota kwa mume wangu. Nilipokuwa nikikatiza sehemu ambayo watu walikuwa wananifahamu walibaki vinywa wazi kushangaa kwa jinsi ambavyo nabadilika kila mara kwa mavazi ya bei kubwa kana kwamba nilikuwa nimeolewa na kigogo mkubwa serikalini. Starehe ilininogea kwasababu nilikataa kufunguliwa biashara nyingine kwa kuona kwamba kushinda dukani kutwa nzima kunaninyima mambo mengi kwahiyo niliamua kutumia kile kilichokuwa kikichumwa na laazizi wangu. Wanawake wenzangu walinionea wivu sana kwani na wao walitamani waume zao wawatunze kama ilivyokuwa kwangu lakini ilishindikana. Kwa jambo lolote lililofanyika pale nyumbani mimi ndie nilikuwa nina uwamuzi turufu na sio mume wangu kama ilivyokuwa awali, nilipokuwa nakohoa tu kidogo mume wangu alikuwa anatetemeka kuniuliza nahitaji nini. Bosi wa Fadhili ambae alikuwa nje ya nchi alimpa taharifa aondoke katika ile nyumba kwasababu alikuwa amempata mteja wa kuinunua. Ni taarifa ambayo niliipata siku moja nilipokwenda kumtembelea na kumkuta yupo katika hali ya uzuni wa hali ya juu kwasababu hakuwa na pakwenda.
***
“Usijali mpenzi nitakwenda kumshawishi mume wangu akupe nafasi nyingine.”
“Umechanganyikiwa?”
“Hapana.”
“Sasa utawezaje kumshirikisha mumeo jambo kama ilo ili hali unafahamu kabisa ananiwinda kama swala, au ndio unataka aniue?”
“Usiwe na wasiwasi yule kwangu hafurukuti wala hatapitapi.”
“Unamaanisha nini kusema hivyo?”
“Namaanisha kwamba hawezi kunikatalia endapo nitamtaka akusamehe na kukupa nafasi nyingine.”
“Nasikitika kukueleza kwamba sipo tayari kabisa kujaribu kuzichezea sharubu za simba.”
“Tafadhali dia naomba usiogope kwani hawezi kukufanya chochote naomba uniamini.”
“Kiukweli namwogopa sana mumeo pindi anapokuwa amepandwa na hasira.”
“Zile hasira zimekwisha kabisa sikuhizi hana lolote.”
“Mh! sawa bwana wewe fanya ufanyalo ila hakikisha kwamba sitadhurika.”
“Usijali bebi niachie ilo ni suala dogo kwangu nitahakikisha unarudi kufanya kazi nyumbani kwangu na utalipwa mshahara mzuri.”
“Yangu macho ila naomba uwe makini sana.”
Nilimshawishi mume wangu ili aweze kumsamehe Fadhili na pia ampe nafasi nyingine ya kurejea kazini kwasababu alikiri kujirekebisha, na kwa bahati nzuri alikubali kwahiyo yule masai ambae ndie alikuwa mlinzi kwa wakati ule tulimtimua na kurudi kwao Longido. Nilifurahi sana Olesaibulu kuweza kuondoka pale nyumbani kwangu kwasababu nilikuwa simpendi kabisa. Kitendo cha Fadhili kurudi pale nyumbani kilisababisha nipate urahisi wa kulifahidi penzi lake japokuwa nilikuwa sithubutu kumuingiza ndani kwangu kama ilivyokuwa mwanzoni kwasababu ya dada wa kazi ila nilikuwa najiibia kwenda kwenye chumba chake ambacho kipo jirani na getini na kupata dozi yangu ya fastafasta. Ule mchezo wa usiku kumtoroka mume wangu na kwenda getini kwa mlinzi ulirejea kama kawaida kutokana na tabia ya Enrique kulala kama mtu aliemeza dawa za usingizi. Kusema kweli ule mchepuko wangu ulikuwa ni kama pumnzi yangu ambayo huwezi kuitenganisha na mimi kwa jinsi ambavyo alikuwa wa muhimu kwangu.
***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Nilipata wazo la kumnunulia kiwanja hawara wangu ili kumdhihirishia kwamba nilikuwa na mapenzi mema kwake kwahiyo nilichachamaa kumuomba mume wangu pesa ambazo nilikuwa nazidunduliza na hatimae zilifika milioni 8 na kwenda kumnunulia kiwanja. Siku moja baada ya mume wangu kwenda kazini niliamua kumfanyia Fadhili surprise kwenda kumuonyesha kiwanja ambacho nilikuwa nimemnunulia.
Nilimchukua baada ya kumweleza kwamba kunamzigo nahitaji akanisaidie kupakia kwenye gari na ndipo nikaendesha gari moja kwa moja hadi maeneo ya Sorenyi jijini Arusha ambapo ndipo kiwanja kilipokuwepo.Mara baada ya kuona zawadi ambayo nilikuwa nimempatia alipandwa na hisia kali sana za furaha kwasababu hakutegemea kwamba ipo siku naweza nikamfanyia jambo kubwa namna ile katika maisha yake.
“Yani sijui nizungumze maneno gani yatakayoweza kufikisha shukrani zangu za dhati kwako mpenzi wangu.”
“Usijali nafanya haya yote kwasababu nakupenda sana.”
“Nakupenda pia.”
“Vipi lakini umepapenda?”
“Nimepapenda mno kwasababu kuna huduma zote za kijamii karibu.”
“Naomba usinisaliti Fadhili nitajiua?”
“Usijali siwezi kufanya hivyo kwasababu nakupenda sana.”
“Jitahidi pesa utakazokuwa unazipata kwenye mshahara wako uzipangilie vizuri ili uweze kununua vifaa vya ujenzi kusudi uanze kujenga mara moja kwasababu kiwanja tayari unacho.”
“Asante sana kiukweli nimepata moyo sana kwahiyo nakuahidi nitaweka mikakati kabambe ya kuanza ujenzi haraka.”
“Vizuri sana na pia usisite kunishirikisha jambo endapo utakwama kufaanikisha jambo fulani kwasababu fulani.”
“Nashukuru sana kwa msaada wako.”
“Hata hivyo huu ni mwanzo tu kuna mambo mengi mazuri nimeyapanga kwaajili yako cha msingi naomba ushirikiano wako wa nguvu.”
“Tupo pamoja mpenzi.”
“Poa.” Mazungumzo yetu yaliishia hapo na ndipo tukaingia kwenye gari kuanza safari ya kurudi nyumbani kwa haraka kwasababu wakati nilipoondoka sikumuaga dada wa kazi. Stori zote tulizokuwa tukipiga kwenye gari bado zilidhihirisha hisia za furaha alizokuwa nazo mchepuko wangu ambae hakutegemea kabisa kumiliki kiwanja kwa wakati ule.
Tulifika nyumbani salama na kukuta kila kitu kinakwenda sawa kabisa. Fatuma alikuwa tayari ameshaivisha chakula cha mchana kwahiyo nilikwenda bafuni kuoga ndipo nikarudi mezani kula chakula. Kiukweli nilikifurahia sana chakula kwasababu kilikuwa kitamu kupita maelezo na nilitamani wakati ule nilipokuwa nakula Fadhili angekuwa pembeni yangu nishuhudie anakula na kushiba lakini isingewezekana kutokana na uwepo wa dada wa kazi mule ndani. Nilipomaliza kula niliwasha gari na kwenda hadi Nakumat supermarket iliyopo Ngarenaro jijini Arusha kwaajili ya kununua mahitaji mbalimbali ya nyumbani kwangu. Nilifanya manunuzi ya bidhaa nilizokuwa nahitaji na kujaza buti la gari pamoja na siti ya nyuma ya gari langu kwasababu nilinunua vitu kwa jumla kuepuka usumbufu wa kwenda sokoni mara kwa mara. Baada ya kumaliza manunuzi ya bidhaa za ndani nilipitia mjini kati kwa sonara kununua saa, mkufu pamoja na hereni za dhahabu kwasababu nilizokuwa nazo nilikuwa nimezichoka. Nilifika kwa sonara ambae kila mara huwa nafanya manunuzi yangu ya vito kwake na nilifanikiwa kupata vitu nilivyokuwa nahitaji kwa thamani ya shilingi milioni 1 na laki 8.
Nilianza safari ya kurudi nyumbani kwa haraka kidogo kwasababu vitu nilivyokuwa nimenunua supermarket ndio vilikuwa vinakwenda kutumika ile siku. Nilifika salama na kumkuta mume wangu yupo sebuleni amekaa na wanae Jordan na Sweetness wanatizama runinga iliyokuwa inaonyesha kipindi cha bunge la jamuhuri ya muungano wa Tanzania.
“Habari za sahizi mume wangu.”
“Nzuri, pole.”
“Asante.”
“Pole mama.” Wanangu nao walinichangamkia kunipa pole.
“Asante wanangu.”
“Mama umeniletea chokoleti?” Jordan aliulizia zawadi kama kawaida yake.
“Ndio nimekuletea mwanangu.”
“Sawa mama.”
“Dada yupo wapi?” nilizungumza wakati naurusha ufunguo wa gari mezani.
“Yupo jikoni.” Sweetness alinijibu.
“Fatuma.” Niliita kwa sauti ya juu.
“Abee dada.”
“Kuna mizigo ipo kwenye gari fanya hima uingize ndani.”
“Sawa dada nimekwelewa.”
Chakula kiliiva na kutukuta bado tupo pale sebuleni tukiangalia vipindi mbalimbali vilivyokuwa vikirushwa kwenye runinga. Kutokana na mizunguko mingi niliyokuwa nayo ile siku nilijihisi kuchoka sana kwahiyo nilipomaliza kula nilikwenda moja kwa moja kujitupa kitandani na kumuacha mume wangu sebuleni akiendelea kufuatilia tamthilia fulani ambayo ilianza muda mfupi kabla ya kumaliza kula. Siku iliyofuata sikuwa na ratiba ya kutoka nyumbani kwangu kabisa kwahiyo nilishinda tu ndani kwangu nikitafakari mambo mbalimbali kuhusu maisha yangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
***
Miezi miwili baadae nilisafiri kwenda nchi ya jirani Kenya kwenda kuwachukuwa wanangu ambao walikuwa wamefunga shule kwa muda wa mwezi mmoja na wiki mbili. Nilifika katika shule waliyokuwa wanasoma na kuchukua ripoti yao ya masomo ambayo ilikuwa inaonyesha wao ndio walikuwa wanaongoza darasani kwa kufanya vizuri katika masomo yao. Nilifurahi sana na niliwaahidi tukifika nyumbani nitawapa zawadi kwasababu matokeo yao yalikuwa yamenifurahisha sana. Tulikwenda hadi kwa bibi yao mdogo ambae anaishi jijini Nairobi kwaajili ya kujiandaa kwa safari ya kurudi nyumbani Tanzania. Kesho yake mida ya saa nne asubuhi tulikwenda uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta na kuanza safari ya kurudi nyumbani huku nikiwa na furaha sana kwasababu nilikuwa nimewamiss wanangu kwa kitambo.
Tulifanikiwa kusafiri salama ndege ilitua katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro International airport (KIA) ambapo tulichukua usafiri mwingine ambao ulitufikisha nyumbani Arusha. Muda mfupi mara baada ya kutia timu nyumbani mume wangu nae alirejea akitokea kazini na kukuta nimeshawafikisha watoto nyumbani. Alifurahi sana alipowaona wanae wanakuwa na vizuri kimwili na kiakili na aliwaahidi pia kuwapa zawadi baada ya kuona ripoti zao za shule ambazo zilionyesha wao ndio walikuwa vinara darasani kwa kufanya vizuri katika masomo yote.
“Well done my sons.” (mmefanya vizuri sana wanangu.)
“Thank you dady.”
“Embu kila mmoja aniambie anahitaji zawadi gani ili kesho niweze kuwanunulia.”
I need novel (nahitaji kitabu cha hadithi.”
“And you Logan.” (Vipi wewe Logan unahitaji zawadi gani?)
“The same gift.” (Nahitaji zawadi kama ya Dylan.)
“Very good.” (vizuri sana.)
“Ok.”
“But I need to know why you need novels all of you.” (Nahitaji kufahamu kwanini wote munahitaji vitabu vya hadithi?)
“Mwalimu wa taaluma alitueleza kwamba hazina ya maarifa ipo katika vitabu kwahiyo hatuna budi kusoma vitabu vingi ili kuweza kupanua uelewa wetu, kwahiyo alitushauri huu muda wa likizo angalau tusome vitabu kadhaa vya hadithi kwasababu vitatuburudisha na pia tutajifunza mambo mengi yatakayotusaidia darasani na maishani.” Nilishikwa na butwaa nilipokuwa nikimsikiliza mwanangu Dylan alipokuwa anazungumza maneno ambayo yalikuwa ni tofauti kabisa na umri wake pamoja na darasa alilopo kwani ndio walikuwa wanaingia darasa la pili.
***
“Safi sana wanangu kesho asubuhi na mapema mtakwenda na mama yenu kwenye duka la vitabu ili muweze kununua vitabu mtakavyo.”
“Thank you dady.”
“Jitahidini zaidi na zaidi high school mtakwenda kusoma South Africa.”
“Ok dady.”
Siku iliyofuata niliongozana na wanangu hadi kwenye duka la vitabu lijulikanalo kwa jina la Book point lililopo katikati ya jiji la Arusha ambapo niliwanunulia vitabu mbalimbali vya hadithi kwa lugha ya Kiswahili na kiingereza. Kiukweli wanangu walikuwa wameshapandikiziwa tabia ya kupenda kusoma vitabu kwasababu walianza kusoma vitabu tangu tulipokuwa kwenye gari hadi tulipofika nyumbani na chakushangaza zaidi ni kwamba walikuwa na kasi kubwa sana katika usomaji wao jambo ambalo lilinifanya niringe na kujiona kweli ninawatoto werevu. Nilizidi kufurahi sana pale ambapo walikuwa wanasoma na kunihadithia walichokuwa wamekisoma na pia nilipata faraja kubwa baada ya dada yao kuiga ile tabia ya kusoma vitabu vya hadithi kwasababu mara nyingi yeye alikuwa anapambana na vitabu vya shule pekee. Mwishoni mwa wiki iliyofuata nilikwenda na wanangu kutembea katika hoteli ya kitalii ya Mount Meru ambapo walifurahi na watoto wengine kwa kuogelea pamoja na kucheza michezo mbalimbali hotelini pale.
“Mom we have real enjoyed.” (Kiukweli mama tumefurahi sana leo.) Dylan alizungumza na mimi wakati tulipokuwa kwenye gari kurudi nyumbani tukitokea hotelini.
“Sure.” (kweli?)
“Yeah we have enjoyed to the maximum.” (Ndio mama tumefurahi kupita kiasi) Logan alikazia kile kilichokuwa kimezungumzwa na mwenzie kunidhihirishia kwamba walifurahi sana ile siku.
“Ok my sons I love you.” (sawa wanangu, nawapenda sana.)
“We love you too mom.” (tunakupenda pia mama.)
Kila mara nilikuwa naulizwa na majirani kwamba watoto wangu wanasoma shule gani kutokana na sifa zao kuwa tofauti na za watoto wengine wa pale mtaani, wengi niliowaeleza shule walizokuwa wanasoma wanangu waliahidi kupeleka na wa kwao huko kwenda kupata yale maarifa ambayo waliyashuhudia kwa wanangu. Niliringa na kuvimba kichwa baada ya kuona majirani wakiumiza vichwa kuweza kuwa na familia kama yangu, kusema kweli pale kwangu tulikuwa tunaishi maisha ya kizungu kwasababu kwanza muda wote watoto wanazungumza kiingereza pamoja na kifaransa, baba yao vilevile alikuwa anazungumza vizuri sana lugha ya kiingereza, changamoto ilikuwa kwangu na kwa dada wa kazi ndio tulikuwa tunajiumauma kuzungumza kizungu.
Siku chache kabla ya kufungua shule niliongozana na wanangu kwenda nyumbani kwa kina mume wangu maeneo ya Meru kusalimia kwasababu tuliona sio vyema watoto wakarudi shule bila kwenda kuwasalimia babu na bibi. Walifurahi sana kuwaona wajukuu zao wakikuwa vizuri bila shida yeyote walishangaa sana kuona watoto wamebobea katika lugha ya kizungu ili hali hawaifahamu lugha mama hata kidogo jambo ambalo babu yao aliliponda na kusema kwamba linadidimiza mila na desturi za kwetu.
***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Baada ya kutoka nyumbani kwa wazazi wa mume wangu tulikwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa baba na mama yangu kusudi na wao wakawaone wajukuu zao ambao walikuwa wamebakiza siku chache warudi shuleni kuendelea na pilikapilika za kimasomo. Kwa bahati mbaya tulipofika hatukuwakuta nyumbani kwahiyo tulikaa pale nje kuwasubiri hadi waliporejea masaa mawili badae wakiwa na majembe mabegani mwao wakionekana kuchoka sana. Niliandaa chakula tukala tukashiba na baadae niliaga na kuondoka kwasababu muda ulikuwa umekwenda sana.
Niliwarudisha wanangu nchini Kenya kwaaajili ya kuendelea na masomo yao. Roho iliniuma sana kwa jinsi walivyokuwa wanamwaga machozi nilipokuwa nawaaga ili niweze kurudi nyumbani.
“No mom don’t go.” (usiondoke mama.) sauti ya Logan na mwenzie ilisikika huku wakilia kwa uchungu.
“Hapana wanangu mimi narudi nyumbani nyie bakini shule msome kwa bidii mtengeneze maisha yenu ya baadae.”
“We going to miss you mom.” (tutakumiss sana mama.)
“Msijali wanangu nitakuwa nakuja kila mara kuwatembelea pamoja na kuwaletea zawadi.”
“Ok mom have a good journey.” (sawa mama tunakutakia safari njema.)
“Thank you.”
“Bye.” Niliangana na wanangu na nilifunga safari ya kurudi nyumbani haraka kwasababu dada wa kazi aliniambia kwamba anahitaji kwenda kusalimia nyumbani kwao kwasababu alipata taarifa kwamba mama yake alikuwa ni mgonjwa kwahiyo nilimuomba kwanza awe na subira niwapeleke wanangu shule halafu nitakaporudi ndio aondoke kwenda kwao tanga kwa muda wa wiki moja. Nilipofika nyumbani kesho yake Fatuma aliondoka jijini Arusha kuelekea kwao. Kwa muda wa wiki moja nilikuwa mpweke sana kwasababu nilikuwa nimemzoea sana yule msichana kwasababu nilikuwa nikiishi nae kama ndugu yangu.
Niliamua kutumia nafasi ile kujivinjari na Fadhili kila siku mchana wakati mume wangu anapokuwa kazini. Kwa mapenzi niliyokuwa nikiyapata kwa mwanaume yule ingekuwa ninauwezo wa kubeba ujauzito mwingine ningebeba nizae kwasababu kuna msemo unasema kuwa hakuna chenye mwanzo kikakosa kuwa na mwisho kwahiyo naamini pia hata mapenzi yetu ipo siku yatafikia kikomo lakini nahitaji siku yatakapofika tamati niendelee kumkumbuka kwa kuwatazama watoto ambao nitakuwa nimezaa nae. Nampenda kuliko kitu chochote hapa chini ya jua na nipo tayari kupambana na mtu yeyote atakae thubutu kumnyooshea kidole kwa ubaya.
Matunzo niliyompatia ndani ya wiki moja ambayo tulikuwa huru kila siku asubuhi hadi jioni yalibadili mwonekano wa mchepuko wangu kwa kiasi fulani kuwa mzuri kwasababu kila siku nilikuwa namchemshia maziwa fresh asubuhi na jioni halafu anakula na mayai mawili ya kuku wa kienyeji, pamoja na hayo yote sikukubali kabisa baridi ya Arusha iendelee kumtesa kwahiyo nilikuwa nampashia maji ya kuoga kila wakati alipokuwa anakwenda bafuni, kiukweli alideka mithili ya mtoto kwa mamaye kwasababu nilikuwa nampenda na kumjali kuliko kitu chochote. Nguo za mume wangu zilikuwa zinafuliwa na dada wa kazi na wakati mwingine alikuwa anafua mwenyewe lakini nguo za hawara wangu mara nyingi huwa namfulia kwa siri kwasababu ya upendo wa dhati niliokuwa nao juu yake.
Wiki moja ilipokwisha Fatuma alirejea kazini kwake kutokea nyumbani kwao kumjulia hali mama yake na kusema kwamba anaendelea vizuri kiafya. Ndani ya wiki hiyohiyo nilimpeleka mwanangu Jordan kwenda kuanza elimu yake ya awali katika shule aliyokuwa anasoma dada yake kwasababu ulikuwa ndio msimu wa kupokea watoto wa elimu ya awali na darasa la kwanza. Hatukuthubutu kumpeleka nje ya nchi kama kaka zake kwasababu alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya kifua kila mara kwahiyo ndio sababu tuliona tuwe karibu nae kwaajili ya kumshuhulikia katika suala zima la matibabu. Tulizidi kuwatia moyo watoto wetu wasome kwa bidii kwa kuwapa kila hitaji la muhimu walilokuwa wanahitaji ili kuhakikisha kwamba wanafanya vizuri katika masomo yao. Siku zilizidi kusogea maisha yangu yakizidi kuwa ya furaha sana na familia yangu kwa ujumla.
Miezi minne baadae nilifurahi sana baada ya Fadhili kunijulisha kwamba amemwaga mchanga, kokoto pamoja na mawe ya kutosha katika kile kiwanja nilichokuwa nimemuhonga pia alinieleza kwamba anajipanga zaidi kutafuta pesa ili aweze kununua mahitaji mengine ili aweze kuanza ujenzi. Taarifa hiyo ilinipendeza sana kwasababu niliona kwamba anatamani siku moja na yeye awe na kwake kama wanaume wengine kwahiyo niliamua kutimiza ndoto yake kwa kumnunulia vitu vyote vilivyokuwa vimesalia na pia nilimkabidhi pesa ya kumlipa fundi ambapo jumala ya gharama zote ilikuwa ni milioni 7 na ujenzi ulianza mara moja.
Kwasababu mume wangu wakati wa mchana huwa kazini kwake kwahiyo nilimpa ruhusa kila siku ujenzi unapokuwa unaendele awe anakwenda kuwasimamia mafundi, ila nilimpa sharti moja la kurudi mapema kabla baba sweetness hajarejea nyumbani. Alifanya hivyo kwa moyo mmoja na ujenzi ulikuwa unakwenda kwa haraka sana, wakati mwingine nilikuwa namwambia apumzike halafu nakwenda kushinda na mafundi kuangalia ujenzi unavyokwenda.
Ndani yaa wiki moja na nusu nyumba yenye ukubwa wa rumu tatu za kulala pamoja na sebule ilifikia kwenye hatua ya kupauliwa hivyo ikabidi ujenzi usimame kwa muda ili nijipange zaidi kifedha kwasababu nilikuwa nataka ipauliwe kwa mabati ya Afrika ya kusini ili iweze kuwa na mvuto zaidi kama ilivyo nyumba nyingi za kisasa. Niliendelea kumpiga mume wangu mizinga ya maana ili nifanikishe adhma yangu ya kupaua ile nyumba kisasa zaidi.
Miezi mitatu baadae pesa ilipatikana ya kumalizia ujenzi kwahiyo nyumba ilipauliwa pamoja na kuvutiwa umeme, chini iliwekwa tailis ya gharama na ukutani ilipakwa rangi nzuri ya kuvutia. Mwonekano mzuri wa mjengo ule ulisababisha kila mtu aliekuwa akipita maeneo yale kupepesa macho kushangaa kutokana na jinsi ilivyokuwa inameremeta. Ujenzi ulipokamilika Fadhili alifurahi na kunishukuru sana kwa namna ambavyo nilijitoa kumsaidia kwa hali na mali kuhakikisha kwamba na yeye anapata sehemu nzuri ya kujisitiri kama watu wengine. Mimi pia nilifurahi nilipofanikisha kumaliza ujenzi wa nyumba yake kutokana na kwamba ni jambo ambalo lilikuwa linaniumiza kichwa kwa muda mrefu kwasababu nilikuwa sifurahishwi na maisha yake ya kuungaunga. Hayo yote na mengine mengi niliyomtendea Fadhili yalifanyika kwa siri kubwa kwani hakuna hata rafiki yangu mmoja niliyewai kumweleza kwamba nilikuwa nimemjengea nyumba yule mlinzi wangu kwasababu wengine wangeniona fala ila kutokana na kwamba mimi ndie nilikuwa najua ninachokipata kwa mtu yule niliona hakuna haja ya kumshirikisha shoti yangu hata mmoja kwasababu wanaweza kuanzisha maneno ya chini chini hatimae ikamfikia mume wangu au hata ndugu zake.
Fadhili aliendelea kufanya kazi pale nyumbani kwangu ingawa tayari alikuwa anamiliki mjengo wake wa maana ambao ulikuwa umekamilika kila kitu. Kwa jinsi nilivyokuwa nampenda mwanaume yule nilikuwa natamani kuitangazia dunia vile ambavyo sijiwezi kwake lakini ilishindikana kutokana na kwamba nilikuwa tayari ni mke wa mtu tena nilieolewa kwa ndoa ya kanisani. Kila mara nilikuwa najihisi kuwa na furaha sana pale ninapohisi uwepo wake maishani mwangu. Kwa namna ambavyo nampenda endapo ikatokea siku akanisaliti basi nafikiri nitayachukia kabisa mapenzi na sinta kaa nipende tena maishani mwangu kwasababu kwa kila namna nimejaribu kumuonyesha namna ambavyo moyo wangu umempa nafasi kubwa tofauti na kiumbe chochote kile hapa duniani.
Roho ilikuwa inaniuma sana pale ambapo nilikuwa naingia ndani kwenda kulala halafu namuacha mpenzi wangu getini akipigwa na baridi usiku kucha. Hapakuwa na namna yeyote ya kuweza kumuondoa getini kwasababu ndio kazi iliyokuwa imemuweka pale nyumbani kwangu kwahiyo nilizidi kumtia moyo aendelee kufanya kazi kwani ipo siku nitamtafutia kazi nyingine nzuri. Kipato kizuri cha mshahara alichokuwa anakipata pale nyumbani kwangu alikitumia vizuri katika kuboresha maisha yake zaidi na zaidi kwani aliweza kununua pikipiki ya biashara ambayo ilikuwa inamuingizia fedha kila siku, jambo ambalo lilinifurahisha sana kutokana na kwamba nilikuwa napenda kuona maendeleo yake kwasababu alikuwa ni mtu wa muhimu sana katika maisha yangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Siku zilisonga na hatimae Glory alimpata mwanaume mmoja fogo ambae alimpenda na wakaoana. Kwa bahati nzuri mume wake alikuwa amejenga maeneo ya PPF njiro kwahiyo ilisababisha kuwepo kwa urahisi wa kutembeleana kwasababu hapakuwa na umbali mrefu sana kufika kwake kama kipindi kile alipokuwa nyumbani kwao moshono. Baada ya sherehe ya harusi aliniomba nimsindikize kwa yule mganga ili akamtengeneze mume wake ili asiweze kumsaliti pia aweze kumfanyia mambo makubwa kama ambayo nilikuwa nikitendewa na mume wangu kwa wakati ule. Tulikwenda kwa mara nyingine kwa mganga Mbengwa nakumkuta anaendelea na shughuli zake za tiba kama kawaida. Alitukaribisha vizuri na alimpatia rafiki yangu dawa ambayo haikuwa tofauti sana na ile niliyokuwa nimepatiwa mara ya kwanza.
Mara baada ya huduma nilitoa shilingi laki moja kwenye pochi yangu na kumpatia kama shukrani kwa dawa nzuri aliyokuwa amenipatia siku ya kwanza nilipokwenda kwake kwani ilifanya kazi kama nilivyokuwa nataka. Alinishukuru sana ila alinipa msisitizo zaidi kuhusu ile hirizi kwamba nichunge sana mume wangu asijekuiona kwasababu kila kitu kitaharibika. Nilimuondoa shaka kwa kumweleza kwamba sehemu nilipokuwa nimeificha hawezi kabisa kuiona kwasababu ilikuwa kwenye sanduku langu la nguo. Tulirejea nyumbani kwa furaha sana kwasababu kile tulichokuwa tumekwenda kukifuatilia kwa mganga tulikuwa tumekifanikisha bila kikwazo chochote.
***
“Nashukuru sana kwa kampani yako shosti yangu.” sauti ya Glory ilisikika wakati tulipokuwa kwenye gari tukirejea majumbani mwetu.
“Usijali besti yangu nipo kwaajili yako.”
“Ngoja na mie nikajionee ufundi wa huyu mganga katika kumtengeneza mwanaume kwa maana nimechokaa kuadithiwa na wewe.”
Huyu mganga ni tishio, uwezi amini Enrique kanywea utafikiri kondoo alienyeshewa na mvua.”
“Unataka kunieleza kwamba ukorofi wote aliokuwa nao mume wako leo hii hana kauli kabisa juu yako.”
“Hana lolote mwanaume yule nimemuweka viganjani mwangu namchezea kama toi.”
“Kama ni kweli basi huyu kalimanzira ni noma.”
“We nenda kafanye mambo we mwenyewe utakuja kuniambia.”
“Sawa bwana.”
Nilimpeleka rafiki yangu hadi nyumbani kwake na baada ya hapo niliondoka kuelekea nyumbani kwangu ambapo nilifika na kukaa sebuleni kutazama runinga iliyokuwa inarusha kipindi nilichokuwa nakipenda. Baada ya muda mfupi nilisikia sauti ya wifi zangu wakizungumza na mlinzi wakati nilipokuwa ndani kwangu. Walikuwa na mazoea ya kuja kunitembelea kila mara lakini kiukweli nilikuwa sifurahishwi hata kidogo na ujio wao pale nyumbani kwangu kwasababu bado nilikuwa na kinyongo nao kwani waliwai kunivunjia heshima mbele ya Fadhili eti kwasababu nilichelewa kubeba ujauzito. Niliona hakuna haja ya kuendelea kuwachekea kinafiki ni bora niwadhihirishie kile kilichokuwa ndani ya moyo wangu. Hivyo basi waliponikuta ndani nilianza kuzungumza nao kwa lugha iliyojaa dharau na chuki ili tabia yao ya kuja nyumbani kwangu ikome kabisa kwasababu nilikuwa nawachukia kama kifo.
“Nyie mbwa koko kwanzia leo sitaki kuona hizo sura zenu mbaya hapa nyumbani kwangu.”
“Wifi naona sasa unavuka mipaka hata kama hututaki nyumbani kwako usitutukane hivyo.” Zubeda alinijibu haraka baada ya kuguswa na maneno yangu niliyokuwa nimeyatamka bila aibu wala chembe ya huruma.
“Narudia tena kwa herufi kubwa ninyi malaya sitaki kuwaona mbele ya macho yangu naomba muondoke mara moja kabla hamjapandisha mashetani yangu.”
“Malaya ni wewe mwenyewe uliekosa adabu, na kwa taarifa yako hatuondoki labda uondoke wewe kunguru mweusi.” Zubeda alizidi kujibizana na mimi huku mwenzie akinitazama kwa jicho la kunipandisha na kunishusha lakini sikutishika hata kidogo.
“Mfa maji siku zote haishi kutapatapa kwahiyo wala hamnisumbui kichwa changu nyie mashetani wakubwa.”
***
“Huna lolote mshenzi tu wewe.” Flora nae alizungumza baada ya kunisonya kwa dharau huku pua yake akiwa ameibinua juu mithili ya nguruwe mwenye njaa kali.
“Washenzi ni ninyi mlioshindwa kuishi kwa wanaume zenu mnabakia kuzurura mitaani utafikiri mmekuwa machinga.”
“Halafu huko unapoelekea ni kubaya utasababishaa tukupe kipigo mda sio mrefu mwanaizaya mkubwa wewe.” Zubeda alionekana kuendelea kuguswa sana na kauli yangu kwasababu ilikuwa na uhalisia wa asilimia mia moja.
“Mnanuksi nyie ndio maana mmechina kaogeeni maji ya magadi.”
“Kwataarifa yako tukimweleza kaka huu ushetani wako nakwambia atakutimua mchana kweupe.” Alizungumza Flora akifikiri bado kaka yao ni yule yule mwenye mbwembwe za fujo kwangu kama mwanzoni.
“Huyo mnaemtegemea kwangu haemi wala hatikisiki katulia tulii na kama hamuamini ngoja nimpigie simu muone atakavyokuja kuwaaibisha mbele yangu.” Nilizungumza wakati nilipokuwa nampigia simu mume wangu huku dada zake wakiwa pembeni yangu wameshika viuno wananitizama kwa hasira sana kana kwamba walikuwa wanataka kunimeza, kwa bahati nzuri simu iliita na kupokelewa muda uleule.
“Halo..o mp..enzi.” nilizungumza kwa kujifanyisha nalia huku simu yangu nikiwa nimeiweka sauti ya juu kabisa ili waweze kusikia mazungumzo yangu na kaka yao.
“Kuna nini kimetokea mke wangu mbona unalia?”
“Wadogo zako ndio wapo hapa nyumbani wananifanyia fujo.”
“Embu ngoja nakuja hapo sasahivi wambie wasiondoke tafadhali.” Baada ya hapo nilikata simu.
“Kwahiyo unafikiri labda atakapokuja atatufanya kitu gani?” sauti ya Flora ilisikika ikizungumza huku akizidi kuniangalia kwa sura ya ukali.
“Nyie subirini kama ambavyo kasema halafu akifika ndio mtapata majibu ya hayo maswali mnayoniuliza washenzi wakubwa ninyi.”
“Yani wewe mwanamke ni mpuuzi kuliko wanawake wote ambao nimewai kuwaona huku duniani.” Flora alizidi kuzungumza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
“Na bado upuuzi wangu hamjaufahamu vizuri ngoja kaka yenu aje ndio mtafahamu kiwango cha upuuzi wangu.” Niliendelea kubishana na wale wifi zangu kwa maneno machafu hadi mume wangu alipofika pale nyumbani akitokea kazini kwake. Niliposikia mlinzi anamfungulia geti nilianza kujiliza kwa kujifanyisha kusudi atakapofika na kuniona apandwe na hasira. Mara baada ya kulipaki gari alikuja kwa haraka hadi pale sebuleni na kunikuta bado nalijiza.
***
“Kwanini hamumueshimu wifi yenu?” swali hilo liliwalenga Flora na Zubeda ambao walianza kujitetea kwakusema kwamba mimi ndio nilikuwa nimewakosea heshima kwa kuanza kuzungumza nao kwa lugha ya matusi na dharau lakini mume wangu hakutaka kuelewa kabisa kile walichokuwa wanamweleza kwahiyo alivua mkanda wake wa ngozi uliokuwa kiunoni na kuanza kuwashushia kipigo cha mbwa mwizi mle ndani na hatimae aliwatimua na kuwapa onyo iwe mwanzo na mwisho kufika pale nyumbani kwangu. Moyo wangu ulitabasamu kwasababu kile alichokifanya Enrique ndicho ambacho nilichokuwa nimekusudia. Walipondoka mume wangu alianza kunibembeleza na kuniomba msamaha sana.
“Samahani sana mke wangu kwa hiki kilichojitokeza nakwahidi hautokaa ukishuhudie tena machoni mwako.”
“Wameniumiza sana.” nilizungumza huku nikijishika kiuno kana kwamba nilikuwa nimeumia sehemu hiyo.
“Pole sana mpenzi, ila na mimi nime
wapa kichapo kikali sana natumaini kwanzia leo watakuheshimu sana.”
“Kweli kabisa yani umewatwanga hadi nimefurahi mwenyewe.”
“Naomba utambue kwamba nipo tayari kupambana na mtu yeyote ambae atathubutu kukusumbua malikia wangu wa roho.”
“Nashukuriu sana mume wangu mpenzi, hakika hawa ndugu zako siwapendi kabisa kwasababu hawana hata chembe ya adabu tena nashukuru sana kwasababu umewapiga marufuku kuja hapa nyumbani kwangu.”
“Usijali, nakupenda sana.”
“Nakupenda pia honey wangu mwaaah!” nilizungumza wakati nampa busu la kinafiki shavuni mwake kwasababu sikuwa nikimaanisha kile nilichokuwa nimemtamkia. Baada ya hapo mume wangu alirudi kazini kwasababu alinieleza kwamba alikuwa kwenye kikao ila nilipompigia simu ya dharura alipewa dakika thelasini awe amesharudi kazini kwasababu alikuwa anasubiriwa ili kikao kiweze kuendelea.
“Ama kweli yule mganga ni fundi kama ingekuwa sio yeye Enrique angeanzia wapi kuhairisha kikao cha kazi kwa muda na kuja kuwashushia kipigo cha maana ndugu zake wa damu kisa mimi?” Niliwaza wakati nilipokuwa nimeketi peke yangu sebuleni natafakari tukio zima lililokuwa limetukia mda sio mrefu na kujikuta nahishia kufurahi sana kwasababu alifanya jambo ambalo lilinikosha sana. Nilihapa kuhakikisha mume wangu anavunja uhusiano wake na ndugu zake wote mpaka mama yake mzazi kwasababu nae nilikuwa namchukia kupita maelezo. Misaada yote ambayo mume wangu alikuwa anaitoa kwa baadhi ya ndugu zake nilizuia yote bila huruma.
Mipango yangu yote ya kuvuruga familia ya upande wa mume wangu ilikamilika baada ya mume wangu kugombana nao wote bila kujali walikuwa na umuhimu gani kwake. Ndugu zake wote walijenga chuki na familia yangu na hakuna hata mmoja aliekuwa anakuja kwangu kunisalimia isipokuwa rafiki yangu Glory pamoja na Doroth. Haikunipa presha wala sikujali kabisa kwasababu maisha yangu nilikuwa nayamudu barabara kwasababu mume wangu alikuwa na pesa kwahiyo siku zilizidi kusonga bila shida yeyote. Uwajibikaji mzuri pamoja na nidhamu ya kazi ilisababisha mume wangu kupandishwa cheo na kuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Vodacom kanda ya kaskazini jambo ambalo lilifanya kipato chake kizidi kuhimarika na maisha kuzidi kuwa matamu sana. Maisha yangu yalitawaliwa na mbwembwe za kubadili magari ya kifahari pamoja na vito vya thamani mwilini mwangu. Alizidi kuwekeza katika biashara mbalimbali ambazo aliajiri watu kwaajili ya kuzisimamia kusudi ziweze kukua kwa kasi kulingana na malengo tuliyokuwa tumejiwekea. Manufaa ya kupandishwa cheo kwa mume wangu yalimfikia pia na Fadhili kwasababu alizidi kula vinono ambavyo nilikuwa namchumia kiulaini kutoka kwenye mifuko ya mume wangu.
Kiukweli kwa mara ya kwanza nilipokuwa naanza mahusiano na Fadhili alikuwa bado ni mshamba sana lakini kwa kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga ndivyo ambavyo alikuwa anajanjaruka na kuwa kuwa na swaga kama za watoto wa mjini. Nguo zake za kiaskari muda wote zilikuwa ni safi na nadhifu kwani nilikuwa nikizifua na kuzipasi kila mara japo kuwa nilikuwa nafanya kwa kujiibia nisionekane na mtu yeyote. Muda wote alikua ananukia harufu ya marashi mbalimbali niliyokuwa namnunulia kwa pesa zangu, bado haikutosha kwani nguo zake zote hadi za ndani hakuna aliekuwa nafahamu gharama zake isipokuwa mimi pekee kwasababu ndie mtu ambae nilikuwa namnunulia katika maduka makubwa ya nguo za fasheni.
Pamoja na hayo yote niliyokuwa nimemfanyia lakini bado nilikuwa najiona kwamba sijafanikiwa kumfanyia jambo la maana sana katika maisha yake kutokana na upendo wa dhati niliokuwa nao kwake. Kungekuwa na uwezo wa kuweza kumkabidhi moyo wangu abaki nao basi ningefanya hivyo ili aweze kufahamu jinsi gani alivyo na nafasi ya kipekee kwangu. Kusema kweli ingekuwa kubadili mume ni kama namba ya siri ya kwenye m-pesa basi ningefanya hivyo kwa moyo mweupe kabisa ili niweze kuishi nae milele yote kwasababu ni mtu ambae nahisi pumzi zangu zitakata endapo atatoweka katika himaya yangu.
Ni mwanaume ambae nathubutu kusema ananiweza pindi tuwapo kitandani kwasababu huituliza hamu yangu yote na kuniacha nikiwa nimetosheka. Utamu wa penzi lake la dhati limefuta kabisa taswira ya mume wangu akilini mwangu na kunifanya nimuwaze yeye tu kila dakika usiku na mchana bila kuchoka. Hajaniteka kwa uchawi wala ndumba bali ni utashi aliojaliwa na Mwenyezi Mungu kucheza na hisia za mwanamke hadi akapagawa.
Asubuhi moja mara baada ya kuamka nilianza kujiandaa ili niweze kuelekea mjini kwenda kununua simu nyingine kwasababu niliyokuwa nayo ilikuwa imeshapitwa na wakati. Fatuma aliniomba kuzungumza na mimi kidogo kabla sijaondoka. Hivyo niliamua kusitisha zoezi la kuendelea kujiandaa kwa muda ili niweze kumsikiliza binti yule msikivu na mpole alikuwa na lipi la kunieleza.
“Samahani dada nahitaji kuzungumza na wewe kwa dakika mbili.” Maneno ya Fatuma yalinifanya nihisi labda kuna kitu anahitaji nimnunulie ndio maana alikuwa ananiingia kwa gia ile.
“Bila samahani mdogo wangu.”
“Kuna jambo nimeona nikushirikishe.”
***
“Zungumza tu usiogope.”
“Mwisho wa mwezi huu naomba niache kazi.” Kauli ya Fatuma ilinifanya nishtuke sana halafu muda huohuo nikaanza kuwaza harakaharaka kulikuwa na tatizo gani lililomshinikiza kuacha kazi kwa wakati ule wakati hapakuwa na hata dalili ya ugomvi kati yetu.
“Kwanini?” niliuliza huku macho yangu yakimshangaa kwa kuwa sikutarajia kusikia kauli kama ile kutoka kwake.
“Hakuna tatizo ila sababu ni kwamba nimempata mchumba ambae anahitaji kunioa.”
“Hongera sana.”
“Asante dada.”
“Mchumba ni wa wapi?”
“Anaishi Tanga ila ni mzaliwa wa Zanzibar.”
“Sawa nimekuelewa, ingawa nitakumiss sana mdogo wangu.”
“Nami pia nitakumiss ila cha msingi ni kuombeana uzima kwani Mungu akipenda tutaonana tena.”
“Kweli kabisa mdogo wangu.” Mwezi ulipofikia tamati aliondoka nyumbani kwangu na kuelekea kwao Tanga, nilizidi kuwasiliana nae kwa njia ya simu ambapo baada ya mwezi mwingine mmoja aliolewa kwa harusi ya kiislamu na huyo mchumba wake mwenye asili ya Kizanzibar. Kutokana na heshima aliyonionyesha kipindi alipokuwa kwangu nilimtumia shilingi milioni moja kama zawadi nono siku ya harusi yake kwasababu alikuwa ni binti anaependa kuwajibika ipasavyo katika majukumu yake kwa wakati husika. Ama kweli huyo mume aliekuwa amemuoa alikuwa amepata mke imara ambae ataweza kumsaidia kwa kiasi kikubwa kutimiza ndoto zao maishani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Kitendo cha dada wa kazi kuondoka pale nyumbani na kwenda kuolewa kilisababisha nipate wakati mzuri wa kuendelea kujivinjari na penzi la mchepuko kwasababu mume wangu anapokuwa amekwenda kazini utuacha wawili bila kujua anaeniacha nae anamsaidia kumega tunda lake. Tulikunywa na kula vitamu vya kurosti pindi tulipokuwa wawili huku tukitabasamu na kucheka kwa furaha sana kutokana na michezo ya kimahaba tuliyokuwa tukionyeshana. Tuliweka mikakati kabambe ya kufanya penzi letu liendelee kuwa la siri ili tusiweze kunaswa na mapaparazi na hatimae penzi letu kuingiwa na doa.
Ugomvi wa ndugu wa mume wangu na familia yangu ulifika pabaya kwasababu taharifa zilifika hadi nyumbani kwa wazazi wangu na kusababisha siku moja kupokea wito kutoka kwa mtu wa heshima ambae alitumwa na wazazi wangu kutoka nyumbani kwetu kwamba nahitajika haraka. Sikuwa na nguvu ya kukataa wito wa wazazi hivyo niliitikia kwa kufika siku ya pili yake nyumbani kwenda kuwasikiliza wazazi wangu walikuwa na lipi la kuzungumza na mimi binti yao mpendwa. Walihairisha shughuli zao za shamba ili waweze kuzungumza na mimi kwa muda mrefu kidogo kutokana na maneno ambayo walikuwa wameyasikia kwamba eti mimi nahusika kugombanisha familia ya mume wangu. Saa tatu na nusu asubuhi nilipaki gari yangu aina ya Toyota Land cruiser prado nje ya nyumba ya wazazi wangu.
***
“Karibu sana mwanangu.” Mama alinikaribisha huku akiweka shoka chini kwani alikuwa anapasua gogo lililokuwa pale nyumbani ili aweze kupata kuni za kupikia.
“Shkamoo mama.”
“Marahaba, hujambo mwanangu!” nilisalimiana na mama wakati alipokuwa akijifuta jasho jingi lililokuwa likimtirika kutokana na kazi ngumu aliyokua akiifanya kwa wakati ule. Nilitamani ningekuwa na uwezo nimsaidie kupasua lile gogo mara moja nimalize lakini haikuwezekana kwasababu nilikuwa nimevaa nimependeza.
“Pole kwa kazi.”
“Asante mwanangu.” Alinipokea mfuko niliokuwa nimeubeba halafu tukaongozana hadi sebuleni ambapo nilimkuta baba amekaa kwenye kiti anasikiliza redio yake ndogo ambayo ilikuwa inasikika kwa mbali kwasababu betri zilikuwa zimeishiwa chaji.
“Karibu binti yangu.”
“Shkamoo baba.”
“Marahaba.”
Mama alinimiminia chai kidogo iliyokuwa imebaki kwenye chupa halafu nikanywa pamoja na vipande kadhaa vya mihogo ya kuchemsha iliyokua imebaki. Baada ya hapo baba alianza kuzungumza kunieleza sababu iliyopelekea wakaniita niende pale nyumbani.
“Mwanangu kwa masikitiko makubwa tumepokea malalamiko kutoka kwa wakwe zako kwamba eti wewe binti yetu unamgombanisha mume wako na ndugu zake. Tumeumia sana na wala hatujaamini kwasababu tumekulelea katika misingi ya dini tukiamini kwamba siku zote katika maisha yako utakuwa na hofu ya Mungu ndani yako. Sasa nahitaji ukweli kutoka kwako kama kweli hiki tulichokisikia kinauhalisia ni bora ukatueleza sisi wazazi wako ili tuweze kutafuta suluhisho la haraka kabla ndoa yako haijafikia pabaya kwasababu hakuna kitu kibaya kama kuhishi na kijana wa watu wakati haelewani na ndugu zake.”
“Hapana wazazi wangu mimi sijafanya namna yeyote ya uchochezi kumgombanisha mume wangu na ndugu zake na wala sijawai kufikiria kufanya jambo kama ilo kwasababu nafahamu kabisa kwamba nitakuwa namkosea Mungu wangu. Nimejaribu kila njia kumshawishi mume wangu ili aweze kumaliza tofauti na ndugu zake lakini amekataa katakakata kwa madai kwamba ndugu zake wamejenga chuki na yeye baada ya kunioa mimi.” Nilizungumza maneno mengi kuwaongopea wazazi wangu ili wasiweze kufahamu ukweli upo wapi juu ya suala ambalo walikuwa wanataka kulifahamu kwa undani zaidi.
“Teddy.”
“Abee mama.”
***
“Ni laana mbaya sana kuwagombanisha ndugu wa mume ambao umewakuta wanapendana na wameshikana vema mithili ya sumaku na chuma, hivyo basi kama kweli unahusika halafu unatuficha naomba utambue kwamba laana hiyo itakutafuna wewe pamoja na kizazi chako.” Mama alizungumza maneno mazito sana hadi joto la mwili likaanza kupanda harakaharaka.
“Nimekwelewa mama ila naomba utambue kwamba mimi sihusiki kabisa katika ugomvi wa mume wangu na ndugu zake.”
“Unajua hata kama wewe huusiki katika ugomvi wao lakini ni vigumu watu kukuamini kwasababu mumeo alikuwa na mahusiano mazuri na ndugu zake kabla wewe hujaolewa na hilo lilijidhihirisha hata ile siku ya harusi yenu ambapo hata wewe nishahidi kwamba mlipata zawadi kedekede kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki wa mumeo jambo ambalo lilithibitisha uhusiano mzuri aliokuwa nao baba watoto wako hapo mwanzoni.” Baba alizidi kuzungumza na mimi maneno ambayo moja kwa moja yalionyesha kwamba hata wao walikuwa hawana imani na mimi.
“Ni kweli kabisa baba ila mimi sina hatia juu ya suala hilo.”
“Kama unachokizungumza kinaukweli ndani yake nakutakia kila la heri Mungu akubariki lakini kama unatuongopea hata sisi tuliokuzaa basi shauri yako.” Mama alizidi kuniporomoshea maneno ambayo yalikuwa yananichoma mtima mithili ya shoti ya umeme.
“Huo ndio ukweli wangu naomba mniamini.”
“Mimi baba yako ninachokueleza leo hii fanya kila namna kutafuta mahusiano mazuri na ndugu wa mumeo kwasababu hakuna mtu mwingine wa karibu ambae ataweza kuwasaidia endapo mtapatwa na matatizo isipokuwa hao ambao mnawaona hawafai kwa wakati huu. Ninafahamu vema kwamba mumeo anapesa za kumtosha kuendesha familia yenu vizuri lakini haina maana eti kwasababu mnajiweza kipesa basi ndio mgombane na ndugu jamaa na marafiki wanaowazunguka. Kuishi na jamii yako kwa maelewano na ushirikiano ni utajiri mkubwa kuliko wa fedha na dhahabu.” Maneno ya baba yalikuwa na uhalisia wa moja kwa moja lakini nilipuuzia na kuona kama alikuwa akighani shairi lenye beti nyingi mbele yangu.
“Nimekwelewa baba nitajitahidi kuufufua uhusiano mzuri uliokuwa umejengeka baina ya familia yangu na ndugu wa mume wangu.” Kauli hiyo ilinitoka ili kuwaridhisha wazazi wangu ambao walikuwa wananibananisha ili waweze kufahamu ukweli wa lile jambo walilokua wameelezwa na mzazi mwenzao kuhusiana na familia yangu na yao.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
“Mwanangu zingatia sana malezi tuliyokupa wakati ulipokuwa kwenye himaya yetu na pia uwalelee watoto wako katika njia ileile tuliyokulelea sisi kwasababu tulikujengea msingi mzuri ambao upo katika mpango wa Mungu.” Kiukweli hakuna siku ambayo mama alizungumza maneno mazito kama siku ile jambo ambalo lilinifanya nihisi maumivu ndani ya moyo wangu kwa namna ambavyo maneno yale yalikuwa yananigusa mubaashara bila chenga.
“Jambo la mwisho ninaloweza kukueleza ni kwamba kuwa na pesa na maisha mazuri haitoshi kuleta furaha ndani moyo wako bali furaha ya kweli hupatikana kwa kuwa na uhusiano mzuri na jamii inayokuzunguka.” Mazungumzo yetu yalifikia tamati na baada ya hapo niliwaaga na kuondoka kuelekea nyumbani kwangu kwenda kupumzika kwasababu nilijihisi kuchoka ghafla kutokana na mazungumzo yale kuwa na uzito wa hali ya juu kuliko ambavyo nilivyokuwa nafikiri.
Pamoja na mambo yote waliyoyazungumza wazazi wangu lakini bado sikuwa tayari kutengeneza uhusiano na ndugu wa mume wangu kwasababu niliona hakuna hata mmoja wao ambao alikuwa na upendo wa kweli kwangu zaidi sana walikuwa ni wanafiki. Moyo uliniuma sana wakati mwingine machozi yalinidondoka pale ambapo nilikuwa nikikumbuka tukio la wifi zangu kunipiga na kuniumiza vibaya. Nafsi yangu ilijenga chuki kali dhidi ya familia ya mume wangu kwasababu niliona wote walihusika katika tukio la kunidhalilisha.
Wadhamini wa ndoa wakishirikiana na watumishi mbalimbali kutoka katika kanisa nililokuwa nasali waliamua sikumoja kuja nyumbani kwangu kunitembelea kuzungumza na mimi baada ya kupata habari kwamba mimi ndie chanzo cha mfarakano baina ya mume wangu na ndugu zake. Kama ambavyo nilikuwa mbishi kwa wazazi wangu ndivyo ambavyo niliwabishia wale viongozi wa dini kwamba wale ndugu wa mume wangu hawanipendi ndio maana wameamua kunisingizia kwamba mimi ndie chanzo cha matatizo lakini sivyo.
Walizungumza mambo mbalimbali yenye hekima ya Mungu ndani yake pamoja na kutoa mifano kutoka katika Biblia takatifu kusudi niweze kuwa chachu ya kurejea kwa uelewano kati ya familia yangu na ndugu wa baba watoto wangu lakini nilionyesha kuwa na moyo mgumu. Pamoja na kwamba nilikuwa nawakatalia kuwa sina tofauti yeyote na ndugu wa mume wangu lakini maneno niliyokuwa nayazungumza yalidhihirisha kwamba moyo wangu ulikuwa umejaa chuki na hasira. Maongezi yetu yalidumu kwa takribani saa mbili lakini hatukuweza kufikia muwafaka mzuri kwahiyo walifunga kwa sala na kuondoka ila waliniachia ujumbe mzito sana kwamba niwaheshimu ndugu wa mume wangu la sivyo hasira ya Mungu itashuka juu yangu.
Nilipata wakati mgumu sana wakati nilipokuwa natafakari ule ujumbe lakini kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga ndivyo ambavyo nilikuwa nayachukulia kawaida mithili ya porojo za wanasiasa pindi wawapo jukwaani kunadi sera zao. Rafiki yangu Glory alinieleza kwamba ile ndio ilikuwa dawa tosha ya ndugu wa mume wenye viherehere na pia alinisisitiza niendelee kuwa na msimamo wangu kwasababu wao ndio walianza kulikoroga kwahiyo hawana budi kulinywa.
Rafiki yangu alinifanya niwe na moyo mgumu zaidi na kuendelea kupuuzia mahusia ya wazazi pamoja na ya viongozi wa dini kwahiyo niliendelea kupandikiza chuki katika moyo wa mume wangu dhidi ya ndugu zake hususani mama yake mzazi ambae ndie alikuwa akisambaza ujumbe wa ubaya wangu kwa watu mbalimbali. Kauli za chuki na dharau za mume wangu dhidi ya ndugu zake zilifika pabaya kwani ilipelekea hadi mama yake kumnenea maneno ya kumlaani kwasababu alichoshwa na nidhamu mbaya aliyokuwa akiionyesha kwake bila kujali kwamba alikuwa ni nani kwake. Kitendo cha mama yule kumtamkia mwanae maneno mabaya tena mbele yangu baada ya kufukuzwa pindi alipokuja nyumbani kwangu wala halikuniogopesha zaidi sana nilichukulia kawaida tu kwasababu nilikuwa namchukia sana mamamkwe wangu kiasi kwamba nilikuwa namuombea umauti umchukue kusudi nisiweze kumuona kabisa machoni pangu. Niliwaza kwamba endapo ataendelea kunifuatafuata nitamuendea kwa mganga nikamtoe roho yake ili niepuke kero zake za kunitangazia ubaya kwa ndugu jamaa na marafiki kwamba namshawishi mwanae agombane nao. Siku moja nikiwa na mume wangu kipenzi baada ya kutoka kwenye kikao cha wazazi katika shule waliyokuwa wanasoma wanangu Sweetness na Jordan tulipata wazo la kupitia nyumbani kwa wazazi wangu kwenda kuwasalimia kwasababu palikuwa ni jirani na pale shuleni. Mume wangu aliwanunulia zawadi nyingi sana ambazo zilijaa buti ya gari na baadhi tuliamishia katika siti ya nyuma ya gari.
***
Hata pale nilipomueleza kwamba ilikuwa inatosha aliniambia kwamba zilikuwa zimepita siku nyingi bila kwenda kuwasalimia wazazi kwahiyo hana budi kuwafungashia vilivyo. Alinunua kila kitu alichoona kinafaa na baada ya hapo tulianza safari ya kuelekea nyumbani kwetu ambapo tulifika na kuwakuta wazazi wapo wamepumzika kwenye kivuli cha mti mkubwa wa parachichi uliokuwepo pale nje kwetu. Mama alitukaribisha kwa furaha na ukarimu wa hali ya juu baada ya kusimama pale alipokuwa amekaa na baba na kuja kutulaki wakati tulipokuwa tunateremka kwenye gari letu la kifahari tulilokuwa tumenunua wiki tatu zilizopita.
“Karibuni sana wanangu.” Mama alizungumza na sisi baada ya kutufikia pale tulipokuwa tumeegesha gari letu.
“Asante sana mama shkamoo.” Enrique aliitikia wakati alipokuwa akishikana mikono na mama kwa heshima.
“Marahaba baba karibuni sana.”
“Asante mama.”
Enrique alitembea harakaharaka na kumfata baba pale chini kivulini alipokuwa amekaa na kwenda kumsalimia, mimi na mama tulibaki kushusha mizigo kwenye gari na kuingiza ndani. Japokuwa baada ya mume wangu kumsalimia baba alirudi kuja kutusaidia kwasababu kulikuwa na mizigo mizito kama vile gunia la mchele, sukari, ndoo kubwa ya mafuta na vitu vingine vizito kadha wa kadha ambavyo tusingeweza kuvimudu. Tulipomaliza kuingiza mizigo ndani tulikwenda pale ambapo baba alikuwa amekaa kwenye mkeka uliokuwa umetandikwa chini.
“Shkamoo baba.” Nilimsalimia baba kwa heshima kwasababu nilikuwa bado sijamsalimia.
“Marahaba mama hujambo.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
“Sijambo.”
“Karibuni sana.”
“Tunashukuru sana baba.”
“Mmekuja wakati mbaya kweli yani ndio tumemaliza kula mda sio mrefu.” Mama alizungumza wakati alipokuwa anachukua vyombo vya chakula vilivyokuwa pale tulipokuwa tumeketi na kuvipeleka kwenye beseni moja kuukuu sana iliyokuwa pembezoni mwa jiko lililokuwa na dalili za kuanguka kutokana na ukongwe. Kwa muonekano wa vyombo ilionyesha kwamba walikuwa wamekula ugali kwa maziwa ya mtindi kwasababu kulikuwa na sahani moja ambayo ilikuwa na kiporo kidogo cha ugali na pia kulikuwa na vikombe viwili vilivyokuwa vinaandamwa sana na inzi. Nilimshukuru Mungu baada ya kukuta wamemaliza kula kwasababu miongoni mwa vyakua ninavyovichukia huku duniani ni chakula cha aina ile.
***
“Usijali mama tutakula hata siku nyingine.”
“Mtatuwia radhi wanangu kwasababu ndio tunataka tuandae cha jioni.” Sauti ya mama ilisikika.
“Vipi baba habari za hapa.” Mume wangu aliuliza kwa shauku ya kutaka kufahamu maendeleo ya wazazi kwasababu hakuwa ameonana nao kwa kitambo kidogo.
“Za hapa kiukweli ni njema ingawa sio sana kwasababu najihisi kuumwa tangu wiki iliyopita lakini namshukuru Mungu bado ananikirimia zawadi ya uhai.”
“Pole sana mzee wangu, umeenda hospitali?”
“Hapana nimetumia tu dawa za asili.”
“Ingependeza zaidi kama ungeenda hospitali kupimwa ili tatizo linalokusumbua liweze kubainika.”
“Nimeugua katika kipindi kibaya sana kwasababu sikuwa na hata senti mfukoni mwangu ndio maana nimeshindwa kwenda hospitali na kuamua kutumia miti shamba kujitibu kama njia mbadala.”
“Pole sana baba ila kwa wakati mwingine msisite kufika nyumbani kwangu ili tuweze kuwapatia msaada wa haraka pale inapobidi kwasababu uwezo wa kuwasaidia tunao.
“Asante sana kijana wangu, vipi habari ya huko utokapo.”
“Njema kabisa, tumetoka shuleni kulikuwa na kikao cha wazazi ndio tukasema tupitie hapa nyumbani kuwajulia hali wazazi wetu.”
“Vizuri sana, wanaendeleaje na masomo yao hao wajukuu zangu.”
“Wanafanya vizuri.”
“Uwafikishie salamu zangu.”
“Hakuna shaka.”
Tuliendelea kuzungumza na wazazi pale nyumbani huku wakituhusia mambo mbalimbali katika maisha mpaka jioni kabisa ambapo tuliona tuondoke tuelekee nyumbani kwetu. Wakati tulipokuwa tunaaga kusudi tuweze kuondoka Enrique alimpatia baba fedha taslimu laki mbili kwaajili ya matibabu. Wazazi wangu walionyesha kufurahi sana kutokana na msaada ambao baba Sweetness aliwapatia. Walionyesha hisia zao za furaha kwa kututaamkia maneno ya baraka maishani mwetu.
***
“Mbarikiwe sana wanangu, Mwenyezi Mungu azidi kuwafungulia milango ya baraka maishani mwenu.” Baba alizungumza huku uso wake ukionyesha dhahiri kwamba alikuwa amefurahi. Na mimi wakati nilipokuwa nashikana na mama mkono kumuaga nilimpa shilingi elfu hamsini niliyokuwa nimeikunja bila baba kuona kusudi iweze kumsaidia katika mambo yake madogo madogo.
“Asanteni sana wazazi wangu.” Mume wangu alizidi kuwashukuru wazazi kwa ukarimu wa hali ya juu waliokuwa wameuonyesha mbele yetu.
“Karibuni sana.” mama aliendelea kutuonyesha ukarimu kwa kutukaribisha tena siku nyingine pale nyumbani.
“Tunashukuru sana.” baada ya hapo tulipanda kwenye gari na kuanza safari ya kurejea nyumbani kwetu njiro.
Tulipokuwa njiani tukirudi nyumbani tulikuwa tukizungumza mawili matatu na mume wangu na alionyesha kutokuridhishwa na maisha waliokuwa wakiishi wazazi wangu kwahiyo alitamani kufanya mabadiliko pale nyumbani kwa wazazi wangu.
“Unajua mke wangu nimeangalia maisha wanayoishi wazee hayajanifurahisha kabisa, kwanini tusiwaboreshee angalau kidogo na wao wajihisi kwamba wana watoto wanaowapenda na kuwajali.”
“Ni wazo zuri pia mume wangu, lakini ndugu zako wakisikia si ndio wataandika magazeti?”
“Usiwe na wasiwasi mke wangu kwasabaabu pesa natafuta mimi mwenyewe kwahiyo sina budi kuzipangilia mimi mwenyewe.”
“Poa dia mimi nipo na wewe bega kwa bega.”
“Hivi karibuni nitawajengea nyumba ndogo nzuri yenye mvuto.”
“Sawa.” Tuliweka mipango mingi kwaajili ya kuboresha maisha ya nyumbani kwetu wakati tulipokuwa kwenye gari tukielekea nyumbani.
Tulifika nyumbani salama ambapo nilianza kuandaa chakula cha jioni harakaharaka ili kiwahi kuiva watoto wale walale mapema kesho yake wadamke mapema wajiandae waende shule. Wakati nilipokuwa naendelea na shughuli ya kuandaa chakula ghafla nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu Glory akiwa analia kwa uchungu sana. Moyo wangu ulienda mbio mithili ya gari ya mashindano huku nikijiuliza maswali mengi sana kutokana na yowe alizokuwa anaangua mwenzangu kwenye simu. Nilijaribu kumbembeleza ili anyamaze anisimulie kilichokuwa kinamfanya amwage machozi kiasi kile lakini jitihada zangu ziligonga mwamba kwasababu hakuweza kunyamaza. Nilipoona nimeshindwa kumbembeleza niliamua kukata simu kusudi niweze kumalizia kuandaa chakula halafu ndio nimtafute lakini mara baada ya kukata simu alinipigia tena muda huohuo na kunifanya nijaribu kumsikiliza kwa mara nyingine kama ataweza kuzungumza jambo la kueleweka.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
“Nyamaza basi unisimulie kama kunauwezekano tuweze kutafuta ufumbuzi wa haraka juu ya tatizo lako.” Nilizungumza baada ya kupokea simu na kusikia kwa mara nyingine akiendelea kulia kwa uchungu kana kwamba alikuwa amefiwa na mtu wa muhimu sana maishani mwake. Kibaya zaidi sikufanikiwa kufahamu kilichokuwa kikimliza kwasababu alishindwa kabisa kumudu hisia kali za maumivu aliyokuwa nayo ndani ya moyo wake. Nilikosa amani kabisa nikawaza labda ni mambo ya kwa sangoma ndio yalikuwa yamemchachia na kuwa chanzo cha yeye kuangua kilio kikubwa namna ile. Zilikuwa ni hisia zangu ambazo hazikuweza kuthibitika kwasababu mlengwa alishindwa kunieleza kwa kinywa chake na kunifanya nibaki njia panda bila kujua cha kufanya.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment