Simulizi : I Killed My Beloved One (Nilimuua Nimpendaye)
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ILIPOISHIA:
Askari wengine wawili wenye silaha walikuwa wakitufuata kwa nyuma, tukaishia kwenye geti kubwa la chuma ambapo yule askari alitoa funguo na kufungua kufuli kubwa lililokuwa linaning’inia, akafungua na mlango wa ndani kisha akanisukumia ndani, nikasikia mlango ukibamizwa nyuma yangu, ukifuatiwa na kelele za geti la chuma, akamalizia kwa kubana kufuli.
SASA ENDELEA...
Chumba kilikuwa kidogo, chenye harufu kali ya haja ndogo na kubwa, kikiwa hakina dirisha zaidi ya matundu madogo yaliyokuwa juu kabisa. Japokuwa kulikuwa na giza, niliweza kutambua kuwa mle ndani kulikuwa na watu wengi kwani nilisikia wakizungumza, huku wengine wakicheka.
Kwa kuwa ndiyo kwanza nilikuwa nimetoka nje kwenye mwanga, ilinichukua zaidi ya dakika mbili macho yangu kuzoea giza la mle ndani, nikiwa bado nimesimama vilevile kama nilivyoingia, nilianza kuona vizuri.
Japokuwa chumba kilikuwa kidogo, kulikuwa na watu wasiopungua ishirini ambao niligundua kuwa wote ni wanawake kwa jinsi walivyokuwa wanaongea. Nikawa natetemeka kwa hofu kubwa, kwa mara ya kwanza katika maisha yangu, nilikuwa nimeingia mahabusu, tena kwa kesi nzito ya mauaji.
“We mtoto kwa nini huamkii wakubwa zako,” nilimsikia mwanamke mmoja akiniuliza kwa ukali, harakaharaka nikaomba msamaha na kuwasalimu wote kwani niliamini hakuna anayelingana na mimi kiumri hata mmoja. Bado nilikuwa msichana mdogo ingawa shida nilizokuwa napitia maishani ndizo zilizonikomaza kabla hata ya muda wangu.
Licha ya kuwasalimu wote kwa heshima, hakuna hata mmoja aliyeitikia, nikawa nawasikia wengine wakitukana matusi mazitomazito huku wakinitisha kwamba watanifundisha adabu.
Nikiwa bado natetemeka, nilisogea taratibu kwa lengo la kutafuta sehemu ya kusimama vizuri lakini bila kukusudia, nikajikuta nikimkanyaga mtu aliyekuwa amelala sakafuni.
Kabla hata sijapata nafasi ya kumuomba msamaha, nilishtukia nikivutwa miguu kwa nguvu na yule mtu huku akiniporomoshea matusi mazito, nikadondoka chini kama mzigo na kumuangukia mtu mwingine, nikaanza kushambuliwa kama mpira wa kona. Wa kunipiga makofi walifanya hivyo, wa ngumi hali kadhalika, wengine wakawa wananifinya huku wengine wakinipiga mateke bila huruma.
Kwa kuwa bado majeraha niliyoyapata baada ya kupigwa na Jimmy yalikuwa bado hayajapoa, damu zilianza kunivuja tena kwa wingi, hali iliyowafanya wale mahabusu waniache, nikalala sakafuni huku nikilia kwa uchungu. Zile stori nilizokuwa nazisikia kuhusu uonevu na unyanyasaji mkubwa waliokuwa wanafanyiwa wanyonge wakiwa mahabusu au gerezani, sasa zilikuwa zikinitokea.
Nililia kwa uchungu sana lakini hakuna hata mmoja aliyejali, wengine wakaendelea kutukana matusi ya nguoni huku baadhi wakicheka kwa furaha.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mbona unaonekana bado mdogo sana, kwani umefanya kosa gani mpaka ukaletwa humu ndani?” nilisikia sauti ya mtu ikiniuliza, kwa taabu nikageuka na kumtazama aliyekuwa ananiuliza. Alikuwa ni mwanamke wa makamo, akiwa amenisogelea pale nilipokuwa nimelala huku damu nyingi zikinitoka.
Hata hivyo sikuweza kumjibu chochote kwani nilikuwa na donge kubwa shingoni lililosababisha nishindwe hata kuongea. Nikawa naendelea kulia kwa kwikwi kwani niliona kama naonewa bila sababu yoyote. Mambo yote yalikuwa yakitokea kwa kasi kubwa mno kiasi cha kunifanya nijihisi kama nipo kwenye ndoto ya kutisha lakini nitazinduka baadaye.
“Basi jikaze usilie, ukiingia humu inabidi ujifunze kuwa na roho ngumu,” alisema yule mwanamke huku akinisaidia kuinuka pale nilipokuwa nimelala na kuniegamiza ukutani, akapigwa na butwaa kwa jinsi nilivyokuwa natokwa na damu nyingi ambazo zililowesha nguo zangu zote na pale sakafuni.
Alipowaambia wenzake, kila mmoja alishtuka sana kwa jinsi nilivyokuwa nikitokwa na damu nyingi ukilinganisha na kipigo walichonipa. Ni kweli walinipiga lakini kama unavyojua mwanamke hata akikupiga ngumi, hawezi kukuumiza kiasi cha kufanya damu zitoke kwa wingi kama ilivyokuwa inatokea kwangu.
Hakuna aliyekuwa anajua kuwa niliingia nikiwa tayari nimejeruhiwa kisawasawa kutokana na kipigo nilichopata kutoka kwa Jimmy.
“Afande! Afande! Kuna mtu anataka kufa huku,” nilimsikia yule mwanamke akigonga geti kwa nguvu huku akipaza sauti. Aliendelea kutingisha geti kwa nguvu na muda mfupi baadaye, nilisikia funguo ikiingizwa kwenye kufuli kisha geti likafunguliwa.
“Yuko wapi?” nilimsikia askari mmoja akiuliza huku akimulika na tochi kali. Yule mwanamke akamleta mpaka pale nilipokuwa nimelala, aliponitazama tu, hakuhitaji kuongeza neno zaidi ya moja, akawaambia mahabusu wawili waniinue na kunitoa mpaka kaunta huku damu zikiendelea kunivuja kwa wingi.
Ilibidi nikimbizwe kwenye kituo cha afya cha Dokta Msangi kilichokuwa jirani na pale kituoni nikiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wa kike wawili, mikononi nikiwa na pingu mikononi. Nilipofikishwa, nilianza kupewa huduma ya kwanza ya kusafisha majeraha ambayo sasa yalikuwa yameanza kuvimba.
Nilisafishwa majeraha yote kwa kutumia dawa maalum, nikafungwa bandeji ili kuzuia damu isiendelee kunitoka kisha nikapewa na dawa za kutuliza maumivu. Baada ya hapo nilirudishwa tena pale kituoni nikiwa chini ya ulinzi mkali, nikaingizwa tena mahabusu.
Angalau sasa nilikuwa na ahueni kubwa kwani zile dawa nilizopewa zilinisaidia sana kupunguza maumivu. Nilipoingizwa tu mle mahabusu, yule mwanamke aliyenisaidia mara ya kwanza, alinipokea na kunionesha sehemu ya kukaa ambapo nilipata nafasi ya kuegamia ukuta uliokuwa umechorwachorwa na kuandikwa matusi mengi.
Kitu ambacho watu wengi hawakijui kuhusu mahabusu, ni kwamba ukiwa mle ndani, kupata nafasi ya kukaa sehemu ambayo unaweza kuegamia ukutani ni kama bahati, hasa kama mahabusu ni wengi kama ilivyokuwa siku hiyo.
Wale wababe tu ndiyo waliokuwa wakipata nafasi hizo, wanyonge wenzangu walikuwa wakikaa katikati, mahali ambapo mtu akisimama tu lazima akukanyage. Nilimshukuru sana yule mwanamke ambaye baadaye aliniambia kuwa anaitwa Bahati au mama wawili.
“Kwani wewe unaitwa nani?”
“Naitwa Eunice.”
“Enhee hebu niambie sasa, umefanya kosa gani mpaka ukaletwa humu ndani?” aliniuliza Bahati lakini sikuwa tayari kumjibu, nikajiinamia chini huku machozi yakianza kunitoka. Alirudia swali lake mara kadhaa lakini bado sikuwa tayari kumjibu chochote.
Akaamua kubadilisha mazungumzo na kuanza kunisimulia masaibu aliyokutana nayo, mpaka akatupwa lupango. Alichonisimulia kilinisisimua sana, nikasahau majanga yangu kwa muda.
Aliniambia kuwa alikuwa ameolewa na kubahatika kuzaa watoto wawili mapacha. Akasema awali mumewe alikuwa akimwambia kuwa anafanya kazi ya udereva teksi na alimuamini kwa sababu alikuwa akilifahamu gari alilokuwa analitumia.
“Siku nyingine alikuwa akikesha barabarani usiku kucha, akija asubuhi anakuja na fedha nyingi ambazo zilifanya tuishi maisha ya raha mustarehe,” alisema Bahati, akaongeza kwamba kumbe kuna jambo ambalo mumewe alikuwa akimficha kwa kipindi chote tangu wakutane na hilo ndiyo lililosababisha atupwe mahabusu.
“Kumbe mume wangu alikuwa jambazi, kuna wenzake alikuwa akishirikiana nao na walikuwa wakitumia gari lake kufanya ujambazi wa kutumia silaha usiku, siku moja wakafanya tukio kwenye kituo kimoja cha mafuta kilichopo Mbezi Beach, kwa bahati mbaya mwenzao mmoja akakamatwa na kuwataja wenzake.
“Mimi nikiwa sina hili wala lile, nikashangaa polisi wamekuja nyumbani kwetu, Kijitonyama na kuanza kupekua nyumba yetu. Kumbe mume wangu alikuwa akimiliki mpaka bunduki ingawa sikuwahi kuiona hata siku moja, wakaichukua na baadhi ya vitu walivyosema kuwa vilikuwa ni vya wizi.
“Kwa kuwa mume wangu tayari alishatoroka baada ya tukio hilo, ilibidi wanikamate mimi na kunileta humu eti mpaka mume wangu atakapopatikana. Wiki ya pili sasa nipo humu ndani,” alisema Bahati huku machozi yakimlengalenga. Nilimsikitikia sana kwani hakuwa na hatia yoyote ya kumfanya ateseke kiasi hicho.
“Haya na wewe nisimulie basi kilichokufanya ukaletwa humu,” aliniambia huku akijifuta machozi lakini bado sikuwa tayari kumwambia, nikamuomba anipe muda mpaka akili yangu itakapotulia. Nashukuru kwamba alinielewa, tukawa tunaendelea kuzungumza mambo mengine. Tulikatishwa na kelele za mlango wa mahabusu uliokuwa unafunguliwa, wote tukanyamaza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Eunice Ansbert” nilisikia jina langu likiitwa na askari wa kike, nikaitikia na kusimama huku nikitetemeka, safari hii nilikuwa makini nisimkanyage mtu yeyote na kusababisha nipigwe kama ilivyokuwa mwanzo.
“Twende huku,” alisema askari yule huku akimalizia kufunga geti, akanipeleka mpaka kwenye ofisi moja mlemle kituoni. Nilipoingia, macho yangu yaligongana na ya kaka yangu ambaye kwa ilivyoonesha, alikuwa akilia kwa muda mrefu kwani macho yake yalikuwa mekundu sana huku mishipa ya kichwani ikiwa imesimama.
Nilitaka kwenda kumkumbatia lakini yule askari alinizuia, akanielekeza kupiga magoti kwenye kona moja ya chumba kile. Mwanaume wa makamo aliyekuwa amekaa mbele ya meza kubwa, begani akiwa na nyota kadhaa, alikuwa akinitazama kwa macho ya udadisi, akiwa ni kama haamini.
Kwa mwonekano wake tu, nilijua lazima alikuwa ndiyo mkuu wa kituo. Ukiachilia mbali yeye na kaka, kulikuwa na watu wengine ambao sikuweza kuwatambua kwani sura zao zilikuwa ngeni kwangu. Mwanaume alikuwa mmoja na wanawake watatu, wote wakawa wananitazama huku kaka akiendelea kulia kwa kwikwi.
“Jimmy anaendeleaje kaka?”
“Amekufa, Jimmy amekufa Eunice,” kaka alisema huku akiendelea kuangua kilio, kauli ambayo ilikuwa kama mkuki ndani ya moyo wangu. Nilitamani kaka aniambie ananitania Jimmy hajafa lakini haikuwa hivyo. Nilibaki nimepigwa na bumbuwazi kwa muda nikiwa ni kama siamini.
“Na mama je?”
“Bado amelazwa, hali yake ipo vilevile kama ulivyomuacha,” alisema kaka huku akiendelea kulia, nikajikuta nimezama kwenye mawazo machungu.
“Eunice!” sauti nzito ya mkuu wa kituo ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye lindi la mawazo, akaniuliza swali ambalo lilikuwa gumu kwangu kulijibu kwa muda ule. Aliniuliza kwa nini nimemuua Jimmy? Nikabaki najing’atang’ata.
“Hawa ni wanaharakati na wanasheria kutoka Tamwa, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake, wameletwa na huyu ndugu yako. Nawapa dakika thelathini, waeleze kila kitu kuhusu kilichotokea ili kama kuna namna ya kukusaidia wajue wanaanzia wapi.
“Huwa siwapi watu nafasi kama hii lakini nikikutazama unafanana sana na mwanangu, napatwa na uchungu kama mzazi ndiyo maana nimetoa nafasi hii, watoto wa siku hizi sijui mmekumbwa na shetani gani,” alisema mkuu wa kituo, akainuka na kutoka nje, akatuacha mle ndani huku askari wawili wenye silaha wakiwa wamesimama mlangoni kwa nje.
Wakaanza kwa kujitambulisha upya, mmoja baada ya mwingine na kuniambia kwamba kaka yangu alikuwa ameenda ofisini kwao kuomba msaada baada ya kusikia kilichonipata hivyo walikuja hapo ili niwaeleze ilivyokuwa.
Haikuwa rahisi kuwaeleza ukweli kwani bado nilihisi hakuna mtu anayeweza kuninasua kutoka kwenye mkono wa sheria uliokuwa umeninasa. Ilibidi kaka awe mkali kidogo kwangu, akaniambia kama sitakuwa tayari kuwaeleza ukweli kwa kinywa changu mwenyewe, basi na yeye hatashughulika tena kunihangaikia kwa namna yoyote.
Kwa jinsi kaka yangu alivyokuwa anaongea kwa hisia, huku akiendelea kutokwa na machozi, sikuwa na namna zaidi ya kukubali kueleza ukweli. Nikaanza kwa kuwasimulia wanaharakati wale kuanzia siku ya kwanza nilivyokutana na Jimmy baada ya kufukuzwa ada shuleni.
Niliwaeleza jinsi nilivyoanza kujenga naye mazoea, jinsi alivyokuwa ananifuata nyumbani na kunipeleka sehemu za starehe na jinsi alivyofanikiwa kuuteka moyo wangu kiasi cha kujikuta nikimkabidhi mwili wangu.
“Unataka kusema hukuwahi kuwa na mwanaume mwingine yeyote kabla ya huyu Jimmy?”
“Sikuwahi hata mara moja, Jimmy ndiye aliyekuwa wa kwanza na ndiye aliyeutoa usichana wangu.”
“Wakati unakutana naye kimwili ulikuwa umeshatimiza umri wa miaka kumi na nane?”
“Hapana,” nilijibu huku nikiwa nimejiinamia kwa aibu, nikawaona wote wakiandika kitu fulani kwenye vitabu vyao kisha wakaniruhusu niendelee kueleza kilichofuatia.
Niliwaeleza kila kitu, sikuficha hata jambo moja. Niliwaeleza mabadiliko niliyoanza kuyaona kwenye mwili wangu baada ya kukutana kimwili na Jimmy, hali aliyokuwa nayo mama baada ya kugundua kuwa nina uhusiano na Jimmy na mlolongo wa matukio mengine yote yaliyofuata baada ya hapo.
“Umewahi kumfumania mara ngapi huyo Jimmy?”
“Sikumbuki vizuri lakini kwa kifupi baadaye niligundua kuwa alikuwa na wanawake wengi sana, tena wengine wakiwa wakubwa kabisa wenye uwezo wa kunizaa.”
“Nini kilitokea kuhusu ujauzito wako aliokupa?” mwanamke mmoja kati ya wale wanaharakati, aliniuliza swali ambalo liliupasua mno moyo wangu. Nilishindwa kuendelea, machozi yakawa yananibubujika kwa wingi mpaka waliponibembeleza na kunisihi nijikaze.
Niliwaeleza jinsi Jimmy alivyoandaa mpango wa kishetani wa kwenda kunitoa ujauzito, jinsi nilivyofanikiwa kuukwepa kwa mara ya kwanza na mbinu zote alizozitumia mpaka akatimiza azma yake.
“Unakumbuka mlienda kuitolea wapi hiyo mimba?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni kule mjini, nyumba nikiiona naweza kuikumbuka ingawa sikumbuki tulipita njia gani mpaka tukafika.”
“Ukioneshwa mtu aliyekutoa hiyo mimba unaweza kumkumbuka?”
“Ndiyo, namkumbuka vizuri kabisa,” nilijibu, nikawaona wakiandika tena maelezo yangu kisha kila mmoja akashusha pumzi ndefu, wakatazamana kisha wakaendelea kunihoji.
Nikamalizia kwa kueleza jinsi nilivyogundua kuwa Jimmy pia amewahi kuwa na uhusiano na mama yangu mzazi na jinsi mama alivyokiri kwetu kwamba alishirikiana na Jimmy kuyakatisha maisha ya baba yetu.
“Kwa hiyo baba yenu aliuawa na mama yenu kwa kushirikiana na Jimmy?”
“Mama anasema yeye hakujua kama Jimmy lengo lake ni kumuua baba kwani kama ni hivyo asingekubali, isipokuwa aliingizwa kwenye mchezo ambao hakuwa akiujua na mwisho ikawa ni kumpoteza baba yetu.”
“Tumeambiwa kuwa mama yenu amechanganyikiwa, nini kilichomtokea?”
“Mama hajachanganyikiwa isipokuwa amepatwa na matatizo ya kisaikolojia kwani ukikaa naye, kuna muda anazungumza vizuri kabisa na kuonesha jinsi nafsi yake ilivyo na hatia kutokana na alichomfanyia marehemu baba.”
Maelezo hayo yaliwashangaza sana wale wanaharakati, nikaona sura zao zimeanza kubadilika kutokana na maelezo yangu. Niliendelea kuwaeleza jinsi Jimmy alivyonivamia njiani wakati nikienda kuonana na mwanasaikolojia Dismas Lyasa kwa ajili ya kumsaidia mama.
Nikaeleza kila kitu, hatua kwa hatua, jinsi Jimmy alivyonipiga utafikiri anagombana na mwanaume mwenzake huku mwanamke wake akishangilia na mwisho, jinsi nilivyookota jiwe kwa lengo la kujihami na kumpiga nalo Jimmy kichwani.
Tayari dakika thelathini zilikuwa zimeisha, mkuu wa kituo akarudi na kututaka tuhitimishe mazungumzo kwani muda ulikuwa umeisha. Wale wanaharakati ambao sasa kila mmoja alikuwa akilengwalengwa na machozi kutokana na maelezo yangu, walimshukuru mkuu wa kituo kisha mmoja akanisogelea na kuniambia kwa sauti ya chini:
“Tutakupigania kwa kadiri ya uwezo wetu, kwa haya maelezo uliyotupa, naamini njia huko mbele ni nyepesi na hata ukipandishwa mahakamani, hutasomewa kesi ya mauaji kama zilivyo kesi za namna hiyo isipokuwa utasomewa kesi ya kuua bila kukusudia.
“Hukumu yake haizidi kifungo cha miaka mitatu, Mungu akusimamie,” alisema yule mwanamke kisha akanikumbatia na kunibusu kwenye paji la uso huku akionesha kulengwalengwa na machozi.
Maelezo yake yalinipa faraja kubwa sana kwenye moyo wangu. Japokuwa kifungo cha miaka mitatu hakikuwa kidogo lakini kilikuwa na afadhali kubwa kuliko miaka thelathini au kifungo cha maisha kabisa ambacho ndiyo hukumu ya mtu anayeua kwa kukusudia.
Niliagana nao wote huku nikiendelea kulia, ilipofika zamu ya kaka, tulikumbatiana kwa nguvu sana huku wote tukiangua vilio, akanibembeleza na kunifariji kwamba hayo yote yatapita na yatabaki kuwa historia kwenye maisha yetu.
Nilimuagiza anifikishie salamu zangu kwa mama na ajitahidi kuniletea maendeleo ya msiba wa Jimmy ili niwe najua kila kinachoendelea. Alinihikakikishia kuwa atafanya hivyo na atajitahidi kuwa ananiletea chakula kila siku asubuhi na jioni.
Bado tulikuwa tumekumbatiana tukiendelea kulia, tukaja kutenganishwa na askari walionichukua msobemsobe na kunirudisha mahabusu ambako kila mmoja alinishangaa kwa jinsi nilivyokuwa nalia kwa uchungu.
Mama wawili au Bahati, yule mwanamke aliyeonesha moyo wa kipekee kwangu, alisimama na kunipokea, akanishika na kunisogeza hadi pale nilipokuwa nimekaa awali, tukakaa na kuegamia ukuta huku mimi nikiendelea kulia kwa uchungu.
Kilio changu kilionekana kuwakera mahabusu wengine ambao walianza kuniporomoshea matusi ya nguoni na kuniambia hapo siyo mahali pa kudeka. Bahati alijaribu kuwatuliza lakini haikuwezekana, kila mtu alikuwa akitukana tusi lake, ikabidi nijikaze na kunyamaza.
Baada ya kukaa kimya kwa zaidi ya dakika kumi, Bahati aliniuliza nilichokutana nacho nilipotolewa mahabusu na sababu iliyofanya nilie kwa uchungu kiasi kile. Japokuwa alikuwa amenionesha moyo wa kipekee, bado sikuwa tayari kumueleza ukweli wa kesi iliyosababisha nikatupwa mahabusu.
Nilimdanganya kwamba nimepewa taarifa kwamba mama yangu anaumwa sana ndiyo maana nilikuwa nalia. Nilimuona amegundua kuwa namdanganya lakini hakutaka kuendelea kuniuliza maswali mengi, akawa ananipigisha stori za kawaida za maisha, hali ambayo ilinitoa kwenye huzuni niliyokuwa nayo.
Kitu ambacho watu wengi ambao hawajawahi kuingia mahabusu hawakijui, ukiwa mle ndani, inakuwa vigumu sana kufahamu muda, yaani huwezi kutofautisha kati ya asubuhi, mchana wala jioni, labda usiku unaweza kuugundua kwa sababu ya giza linaloonekana kupitia vidirisha vidogo.
Hakukuwa na mtu mwenye saa mle ndani, hali iliyotufanya tuishi kama tupo nje kabisa ya dunia. Pia jambo lingine ambalo wengi hawalijui, ukiwa mahabusu muda unaenda taratibu mno, yaani siku moja ukiwa ndani unaweza kuifananisha na hata siku mbili uraiani.
Jamani uhuru mzuri sana na huwezi kuona umuhimu wake mpaka siku uupoteze. Nawasihi sana watu ambao ndugu zao wapo mahabusu au gerezani kujitahidi kuwa wanawatembelea mara kwa mara na kuwapelekea mahitaji muhimu kama maji safi ya kunywa na vyakula bila kuchoka kwani hali ni mbaya sana, mimi nimejionea ndiyo maana nayasema haya.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mchana ule kaka hakuniletea chakula, nadhani ni kwa sababu ya ubize aliokuwa nao kwani ni yeye ndiye aliyetakiwa kuhakikisha wadogo zetu nyumbani wanakula, mama hospitalini anakula pamoja na mimi. Kwa bahati nzuri, ndugu wa mama wawili walimletea chakula ambacho alinikaribisha, tukala wote.
Baadaye sana kaka aliniletea chakula, akakikabidhi kwa askari ambaye alikuja kufungua lango la mahabusu na kuita jina langu, nikaenda kupokea kisha nikarudi kukaa na mama wawili ambapo tulikubaliana kwamba tusile muda ule mpaka baadaye kwani hatukuwa na njaa sana.
Tuliendelea kuzungumza mambo mbalimbali ya maisha, mama wawili akawa ananisimulia uzoefu mbalimbali wa maisha alioupata katika kipindi chote alichokuwa anaishi na mume wake. Kwa kweli nilijifunza mambo mengi sana.
Giza lilipoingia, tulikula chakula chetu kisha tukajilaza sakafuni. Sikumbuki nilipitiwa na usingizi saa ngapi lakini niliposhtuka, mahabusu wote walikuwa wamelala, wengine wakawa wanakoroma. Hewa ilikuwa nzito mno mle ndani, ukichanganya na joto la Dar, nilijihisi kama nipo kuzimu.
Niliutumia muda huo kusali na kumuomba Mungu wangu aoneshe miujiza. Maelezo niliyopewa na wale wanaharakati wa Tamwa walioletwa na kaka, yalianza kujirudia ndani ya kichwa changu, nikajisikia ahueni kubwa sana tofauti na wakati nikiingizwa humo ndani.
Nilisali kwa muda mrefu, nikajilaza tena sakafuni na usingizi wa maluweluwe ukanipitia. Nilikuja kuzinduka baadaye sana baada ya kusikia lango la kuingilia mahabusu likigongwa kwa nguvu, wote tukakurupuka na kusimama, askari wawili wakaingia na kuanza kutuita majina yaliyokuwa yameandikwa kwenye faili maalum.
Baada ya kila mtu kuitwa jina lake, wale askari walitoka na kutuacha kila mmoja akiendelea na shughuli zake. Niligundua kuwa tayari ni asubuhi kwani mwanga ulianza kuonekana kwenye kidirisha kidogo.
Saa kadhaa baadaye, niliitwa jina langu na askari mmoja, nikaenda getini ambapo alinikabidhi chupa ya chai pamoja na vitafunwa ambavyo bila hata kuuliza nilijua vimeletwa na kaka. Nilipokea na kurudi sehemu yangu, tukakaa na mama wawili na kuanza kunywa.
Tulipomaliza, niligundua kuwa ndani ya mfuko huo kulikuwa na karatasi lililokuwa na ujumbe ambao niliutambua kuwa unatoka kwa kaka kutokana na mwandiko wake, nikalitoa na kuanza kulisoma.
Ulikuwa ni ujumbe mrefu kutoka kwa kaka ambaye alinitaarifu kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa ya mazishi ya Jimmy. Akaniambia kuwa ndugu zake wamekuja juu sana na wanataka nichukuliwe hatua kali za kisheria kwa kukatisha maisha ya ndugu yao.
Sikuamini kwamba kweli huo ndiyo mwisho wa Jimmy na kwamba sitamuona tena maishani mwangu, nilishindwa kumalizia kuusoma ule ujumbe, nikauficha kwenye nguo niliyokuwa nimevaa na kuanza kulia kwa uchungu.
Yaani mpaka leo huwa nashindwa kuelewa kwamba zilikuwa ni akili za kitoto au ni mapenzi niliyokuwa nayo kwa Jimmy yaliyonifanya niwe kwenye hali ile? Eti licha ya yote niliyokuwa nimefanyiwa na Jimmy, roho iliniuma sana kugundua kuwa sitakuja kumuona tena kwenye maisha yangu.
Bado nilitamani kwamba siku zirudi nyuma ili nirekebishe makosa yangu lakini hilo halikuwezekana. Mama wawili alifanya kazi ya ziada kunituliza. Baadaye nilitulia na kuutoa ule ujumbe, nikaendelea kusoma kuanzia pale nilipokuwa nimeishia.
Kaka aliandika mambo mazito sana ambayo ama kwa hakika yalinishangaza. Aliniambia kuwa wale wanaharakati wa Tamwa, wanaendelea na kazi yao ambapo wamebaini kuwa siku chache baada ya baba kufariki dunia, kuna hamisho kubwa la mamilioni ya fedha lilifanyika kutoka kwenye akaunti yake ya benki kwenda kwenye akaunti ya Jimmy huku pia kukiwa na saini ya mama kwenye fomu ya benki ya kuhamisha fedha.
Pia aliniambia kuwa wamegundua kuwa baba alikuwa akijenga nyumba nyingine Mbezi ambayo ilikuwa imefikia hatua za mwisho lakini baada tu ya kufa, hati ikabadilishwa jina na kuandikwa la Jimmy huku shahidi akiwa mama.
Mwisho akaandika kuwa kumbe hata mafao ya baba yalikuwa tayari yameshatoka na mama alienda kusaini zaidi ya shilingi milioni arobaini na tisa ambazo zililipwa kama fidia kwa familia ya marehemu kutoa kwa kampuni aliyokuwa anafanyia kazi kwani alifariki akiwa kazini.
Baada ya kumaliza kuusoma ujumbe huo, nilibaki nimepigwa na butwaa nikiwa ni kama siamini kwani vitu vingi vipya vilikuwa vimeingia kwenye kichwa changu kwa mkupuo, kiasi cha kushindwa kuelewa nianze kulitafakari lipi.
Ule uchungu niliokuwa nao juu ya kifo cha Jimmy, uliyeyuka kama barafu juani, nikawa najiuliza maswali yaliyokosa majibu.
Nilijiuliza hivi Jimmy alikuwa na roho ya namna gani mpaka aisambaratishe familia yetu kwa kiasi kile? Yaani amuue baba yetu, atuchanganye kimapenzi mimi na mama yangu mzazi, ajimilikishe fedha zote zilizokuwa kwenye akaunti ya baba, ajimilikishe nyumba ya familia na kama hiyo haitoshi akombe mafao yote ya baba? Sikutaka kuamini kilichotokea.
Nilirudia kuusoma ujumbe ule kutoka kwa kaka zaidi ya mara tatu, nikajiinamia huku nikihisi kama moyo wangu ulikuwa unataka kusimama kutokana na maumivu niliyokuwa nayasikia. Nilijaribu kuivuta karibu taswira ya Jimmy kuanzia siku ya kwanza nilipokutana naye, nikalinganisha na ushetani alionifanyia.
Japokuwa ni kweli nilitokea kumpenda sana lakini baada ya kuyajua yote hayo, niliona kama adhabu aliyoipata haikumtosha. Nilitamani nipate nafasi hata ya kwenda kuhudhuria mazishi yake ili nikamalizie hasira na maumivu yangu kwenye maiti yake. Nikawa natetemeka kwa hasira mpaka mama wawili (Bahati) akanishtukia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwani una nini mdogo wangu? Kwa nini unakuwa msiri kiasi hicho? Ina maana bado huniamini?”
“Ha…ha…pa…na,” nilimjibu kwa kifupi huku nikiendelea kutetemeka kwa hasira iliyopitiliza. Sikuongea kitu chochote baada ya hapo, hata hamu ya kula ilipotea kabisa. Nakumbuka licha ya kaka kuniletea chakula cha mchana na cha jioni, sikuweza kula zaidi ya kumuachia kila kitu mama wawili ambaye naye ilibidi agawe chakula kwa mahabusu wengine ili kisiharibike.
Siku hiyo ilikuwa ndefu sana kwangu, ukichanganya na mazingira ya mahabusu, hakika niliionja Jehanam nikiwa bado nipo duniani. Hatimaye kesho yake, nilikuja kuitwa asubuhi na mapema mimi pamoja na mahabusu wengine kadhaa.
Tukaandikisha maelezo fulani kisha tukaambiwa tunapelekwa mahakamani. Nilisikia moyo ukinilipuka paaaa! Sikuwahi hata mara moja kuwaza kwamba ipo siku nitapelekwa mahakamani, tena kwa kesi nzito ya mauaji. Hata sikujua nini kitakachotokea mahakamani.
Mimi na baadhi ya mahabusu wenzangu tulipewa baadhi ya vitu vyetu ikiwemo viatu kisha tukatolewa na kupakizwa kwenye difenda chini ya ulinzi mkali, kila mmoja akiwa na pingu mikononi na safari ya kuelekea mahakamani ikaanza.
Gari lilianzia kwenye mahakama ya mwanzo, baadhi ya mahabusu wakashushwa na kuingizwa mahakamani kisha mimi na mahabusu wengine wawili tukaendelea na safari.
Tulipelekwa mpaka Mahakama ya Kisutu. Sikuwahi hata mara moja kuingia kwenye mahakama hiyo zaidi ya kuwa napita kwa mbali, tukateremshwa chini ya ulinzi mkali na kupelekwa mpaka kwenye chumba maalum kilichokuwa ndani ya mahakama hiyo. Bado nilikuwa natetemeka sana, nilitamani iwe ndoto lakini haikuwa hivyo.
Dakika kadhaa baadaye, nilikuja kuchukuliwa na askari wawili wa kike wenye silaha na kupelekwa kwenye chumba ambacho kesi yangu ilipangwa kusomwa. Tulipishana na askari magereza wengi ambao walikuwa wakiwatoa na kuwarudisha washtakiwa kwenye vyumba vya kusubiria kesi.
Pia niliwaona baadhi ya waandishi wa habari wakiwa na kamera zao mikononi. Sikupenda kupigwa picha na mtu yeyote, nikawa natembea kwa kujificha katikati ya wale askari. Nashukuru kwamba sikupigwa picha yoyote mpaka nilipoingizwa kwenye ukumbi wa mahakama.
Nikaenda kusimamishwa kwenye kizimba, pingu zikafunguliwa na wale askari wakasogea mita kadhaa kutoka pale kizimbani, nikabaki peke yangu. Kwa jinsi nilivyokuwa naogopa, sikuweza hata kuinua uso wangu na kuwatazama watu waliokuwa mahakamani mle, nikawa nimejiinamia huku machozi yakinitoka.
“Eunice! Eunice!” nilisikia sauti ambayo hata bila kuuliza nilijua ni ya kaka, nikajikakamua na kuinua uso wangu, nikamuona kaka akinipungia mkono kama ishara ya kunionesha kwamba alikuwepo mahakamani pale. Pembeni yake alikuwa ameambatana na wadogo zangu wengine ambapo nilipowatazama, kila mmoja alikuwa analia.
Upande wake wa kulia, niliwaona wale wanaharakati wa Tamwa wakiwa wamejipanga na kutulia, wote macho yao yakiwa kwangu. Mmoja kati yao alinionesha ishara kwamba nitulie na kila kitu kitakuwa sawa.
Muda mfupi baadaye, nilisikia askari mmoja akipaza sauti, watu wote wakasimama kisha nikamuona hakimu mwanamke aliyekuwa amevalia mavazi rasmi, akiingia kupitia mlango wa nyuma akiwa ameambatana na watu wengine kadhaa ambao harakaharaka niliwatambua kuwa ni mawakili na wazee wa mahakama.
Walipoingia na kukaa, watu wengine nao walikaa kwenye viti vyao kisha nikamuona wakili mmoja mwanamke akija pale kizimbani nilipokuwa nimesimama. Akanisogelea na kuniita jina langu kwa sauti ya chini.
Akaniambia kwamba yeye ni mwanasheria na wakili kutoka Tamwa, akaniambia kuwa yupo na wenzake watatu ambao alinioneshea kwa kidole mahali walipokuwa wamekaa, nao wakanipungia mikono kwa mbali.
“Kesi yako itakaposomwa, hutakiwi kujibu chochote, umenielewa Eunice?”
“Nimekuelewa mheshimiwa, ahsante kwa kuja kunitetea,” nilimjibu yule mwanasheria huku machozi yakianza upya kunitoka, akaondoka na kurudi kwenye kiti chake. Kwa kiasi fulani nilipata ahueni kubwa ndani ya moyo wangu baada ya kugundua kuwa kumbe sikuwa peke yangu katika janga lile.
Niliwatazama wale mawakili, nikamtazama kaka yangu na wadogo zangu kisha nikawatazama wale wanaharakati waliokuwa wamekaa siti moja na ndugu zangu, nikajikuta nikipata nguvu za ajabu. Nilijifuta machozi na kutulia pale kizimbani, mwendesha mashtaka wa serikali akasimama na kuanza kunisomea mashtaka yaliyokuwa yananikabili.
Kama nilivyoelekezwa na yule wakili, sikujibu kitu. Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi ile, akawaambia watu wote kwamba kwa kuwa mahakama ile haikuwa na hadhi ya kusikiliza kesi iliyokuwa inanikabili, sikutakiwa kujibu chochote. Akasema kwamba anaihamishia kesi yangu mahakama kuu ambapo alitaja tarehe mpya ya kuanza kusikilizwa rasmi kwa kesi yangu.
Baada ya hapo, aligonga nyundo mezani kisha watu wote wakasimama, akatoka yeye na jopo lake kisha nikaja kuchukuliwa na askari tofauti na wale walionipeleka ambao walikuwa wamevaa sare za askari magereza, wakanitoa mpaka nje na kwenda kunipandisha kwenye karandinga lililokuwa nje ya mahakama ile. Kwa mbali niliwaona kaka na wadogo zangu wakiwa wamekumbatiana huku wakilia, wale wanaharakati wa Tamwa pamoja na mawakili wangu wakawa wanawabembeleza huku wote wakinipungia mikono.
Nilijikuta nimezama kwenye mawazo machungu, machozi yakinibubujika kama chemchemi ya maji. Safari iliendelea huku nikiwa sina habari kabisa, akili yangu ilikuwa imehamia katika ulimwengu tofauti kabisa, ulimwengu wa machozi. Nilikuja kushtuka baada ya kuona lile karandinga likisimama na milango ya chuma ikianza kufunguliwa. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mimi na wenzangu kadhaa tukateremshwa kwenye karandinga hilo na askari waliokuwa wamevalia sare za askari magereza. Nikawa natazama huku na kule nikijiuliza pale ni wapi? Mara niliona maandishi yaliyoandikwa ukutani ambayo ndiyo yaliyonifanya nielewe kwamba kumbe tayari tulikuwa tumefika kwenye Gereza la Segerea.
Baada ya kuteremshwa kwenye karandinga, tulisimama na kujipanga mistari, wanawake upande wao na wanaume upande wao. Ukaguzi mdogo ukafanyika ambapo wote tuliitwa majina kisha tukaongozwa na askari wenye silaha kuelekea ndani ya gereza hilo ambalo nilikuwa nikisikia sifa zake tangu nilipokuwa mdogo.
Wanaume wakaingizwa upande wao na sisi tukapelekwa upande wetu. Kati ya watu wote, mimi ndiyo nilikuwa mdogo zaidi, hali iliyofanya kila tulipopita watu wote kunigeukia mimi na kunitazama kwa macho ya mshangao.
Nadhani walikuwa wakijiuliza nimefanya kosa gani katika umri ule niliokuwa nao lakini wala sikuwajali, nikawa nashangaa mazingira ya gereza huku tukiswagwa kama mifugo iliyokuwa ikiingizwa zizini.
Kitu nilichojifunza baada ya kuingia gerezani humo, jela siyo mahali pa masihara. Japokuwa awali nilikuwa nadhani mahabusu ndiyo sehemu mbaya zaidi, baada tu ya kuingia ndani ya gereza hilo nilielewa maana ya ule msemo usemao jela jeraha.
Sitaki sana kueleza mambo ambayo nilikutana nayo ndani ya gereza hilo kwani ni sawa na kutonesha donda ndani ya mtima wangu. Cha msingi tu nawaasa wenzangu kutovunja sheria za nchi, jambo linaloweza kusababisha wakatupwa gerezani kwani hakufai kabisa, bora uwe unasikia tu lakini usiombe yakukute.
Pia kwa wale wanaoingia gerezani kwa makosa ya bahati mbaya kama ilivyokuwa kwangu, au wale wanaosingiziwa, nawaombea kwa Mungu awape uvumilivu na ustahimilivu na kamwe wasikate tamaa kwani bado kuna maisha baada ya jela.
Jambo la msingi ni kuendelea kumuomba Mungu wakati wote na kujenga matumaini makubwa kwamba ipo siku watarudi tena uraiani na kuwa huru kama zamani. Kukata tamaa ni sumu kubwa sana kwa maisha hayo, afadhali huku uraiani hata ukikata tamaa bado maisha yanaweza kusonga mbele.
Jambo lingine nililojifunza, siyo wote wanaokwenda jela wana hatia. Yaani kama ingekuwa inaruhusiwa, ningewashauri waandishi wa habari na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu watembelee kwenye magereza na kuwahoji baadhi ya wafungwa sababu zilizowafanya wakajikuta wakiishia jela.
Huwezi kuamini, watu wengi wanatumikia vifungo kwa makosa ambayo hawakuyafanya ingawa wapo pia ambao kweli wanastahili kufungwa. Nafikiri ukosefu wa wanasheria wengi wanaozijua vizuri sheria ni miongoni mwa sababu za tatizo hilo.
Nitakuwa sijatenda haki kabisa kama sitamshukuru Bibi Jela, sijui jina lake halisi anaitwa nani lakini tulizoea kumuita kwa jina hilo. Japokuwa mama huyu ana sura ya kikatili lakini amejaaliwa moyo wa kipekee sana.
Nakumbuka siku moja tu baada ya kuingizwa gerezani, ‘niligumiana’ naye wakati wa chakula cha mchana, akanishangaa kwa muda mrefu na baadaye akaniita na kuniambia nimfuate, mkononi akiwa ameshika kirungu chake. Nilijua anaenda kuniadhibu kama nilivyoshuhudia akiwafanya baadhi ya wafungwa waliokuwa wanaonesha utovu wa nidhamu.
Alinipeleka pembeni kabisa na kuanza kunihoji kwa upole kuhusu kosa nililofanya mpaka nikapelekwa pale. Kwa kuwa nilikuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu, ilibidi niwe mkweli kwake. Nikamsimulia kila kitu kilichokuwa kimenitokea mpaka wakati ule.
Nilimuona akiumia sana ndani ya moyo wake, akaahidi kuwa pamoja na mimi kwa kipindi chote ambacho nitakuwa mle ndani. Ikawa muda wa chakula ukifika, ananichukulia chakula maalum walichokuwa wanapewa wafungwa wagonjwa ambacho kidogo kilikuwa na afadhali.
Sina uhakika kama bado anafanya kazi Segerea mpaka leo lakini popote alipo, namuombea kwa Mungu amzidishie na ampe maisha marefu.
Baada ya kukaa kwa muda wa siku saba, hatimaye siku ya kesi yangu kusomwa kwa mara nyingine iliwadia, tukatolewa pamoja na watuhumiwa wengine na kupelekwa Mahakama Kuu ya Tanzania, ile inayotazamana na bahari, katikati ya Jiji la Dar es Salaam, Posta (Kwa wenyeji wa Dar es Salaam watakuwa wananielewa vizuri).
Kama ilivyokuwa siku nilipopandishwa Kisutu, kaka alikuwepo mahakamani na wadogo zangu ambao siku hiyo walikuwa wamevaa nguo za shule. Nilijiuliza wameanza kwenda shule? Sikuwa na majibu. Kama kawaida, pembeni yao walikuwepo wale wanaharakati wa Tamwa waliokuwa na makabrasha mengi mikononi mwao.
Pia wale mawakili nao walikuwepo, wakiwa wamevalia mavazi yao maalum yaliyowafanya waonekane nadhifu sana. Baada tu ya kupandishwa kizimbani, niliwaona wote wakinipungia mikono lakini safari hii hakuna aliyekuwa na sura ya majonzi kama ilivyokuwa mwanzoni.
Kidogo nilijihisi ahueni ndani ya moyo wangu kwani kilichokuwa kinaniumiza zaidi awali, ilikuwa ni kuona jinsi watu wengine wanavyoumia kutokana na matatizo yangu, hasa wadogo zangu. Wakili mmoja alinisogelea na kuniita jina langu, akanipa mkono na kunisalimia kwa uchangamfu.
Akaniambia kuwa nitakapoulizwa chochote na jaji, ninyamaze kimya kama ilivyokuwa siku ya kwanza. Akanihakikishia kwamba kila kitu kitakwenda sawa kwani wamepata ushahidi wa kutosha kuhusu mambo yaliyokuwa yanafanywa na marehemu Jimmy. Akanihakikishia kuwa nitajionea mwenyewe kesi itakapoanza kusomwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilifurahi sana kusikia maneno hayo ya kutia moyo kutoka kwa yule wakili, alipomaliza kuzungumza na mimi alirudi kukaa na wenzake, nikawaona wote wakiwa na nyuso za furaha. Muda mfupi baadaye, askari mmoja alipaza sauti kisha watu wote wakasimama, jaji na jopo lake wakaingia na kwenda kukaa sehemu zao kisha kesi ikaanza kunguruma.
Taratibu za kimahakama zilianza kama kawaida ambapo mwendesha mashtaka wa serikali alinisomea mashtaka yaliyokuwa yananikabili mbele ya mahakama. Kesi ya msingi ikiwa ni ya mauaji.
Baada ya kumaliza kusoma jinsi tukio zima lilivyokuwa, maelezo ambayo hayakuwa na shaka hata kidogo kwani yalikuwa ndiyo uhalisia wenyewe wa jinsi tukio hilo lilivyokuwa, mwendesha mashtaka huyo alienda kukabidhi faili la kesi kwa jaji.
Pia nilimsikia akiiambia mahakama kuwa anakabidhi na vithibitisho vingine muhimu katika kesi hiyo, ikiwemo cheti cha daktari aliyeufanyia vipimo vya mwisho mwili wa marehemu, cheti cha kifo na ushahidi mwingine wa sauti ambao ulinishtua sana.
Yalikuwa ni mazungumzo yangu na Jimmy kwenye simu siku za nyuma kabla hajafa ambayo yalirekodiwa, nikajikuta natetemeka mno kwani kwa ushahidi huo, sikuamini kama naweza kuukwepa mkono wa sheria. Nakumbuka ni kweli nilizungumza maneno hayo lakini ilikuwa ni katika kipindi ambacho nilikuwa kwenye hali mbaya sana kiakili.
Ilikuwa ni katika kipindi ambacho nilitoa ujauzito kwa kurubuniwa na Jimmy lakini kibaya zaidi, madaktari walibaini kwamba kizazi changu kilikuwa kimeharibiwa katika zoezi hilo na kama hiyo haitoshi, mama yangu alikuwa ndiyo kwanza anafikishwa hospitalini kwa kile ambacho awali tuliamini kwamba amechanganyikiwa. Rekodi yenyewe ilikuwa hivi:
Jimmy: Nasikia unatishia kuniua si ndiyo?
Mimi: Ndiyo, lazima nikuue Jimmy, wewe ni muuaji tena shetani mkubwa, hakuna adhabu inayokufaa zaidi ya kifo.
Japokuwa nakumbuka tulizungumza mambo mengi siku hiyo, lakini kipande hicho kidogo tu ndicho kilichokuwa kimekatwa na kuchukuliwa kama ushahidi. Hata sijui waliwezaje kunasa mazungumzo hayo kwani nina uhakika wakati tunazungumza hakuna mtu mwingine aliyekuwa anatusikia.
Au inawezekana ndiyo mambo ya teknolojia ya kisasa kwenye sekta ya mawasiliano kwamba watu mnazungumza jambo leo mkijua ni siri yenu, kumbe kuna mitambo inarekodi kila kinachoendelea na siku ushahidi ukitakiwa, unapatikana bila tatizo. Ama kweli wapelelezi wana kazi kubwa sana.
Baada ya kuwasilisha ushahidi huo, mwendesha mashtaka huyo wa serikali ambaye mpaka leo sura yake naikumbuka vizuri kwani nilimfananisha na malaika mtoa roho siku hiyo japokuwa alikuwa akitimiza majukumu yake, aliinama kidogo mbele ya jaji kutoa heshima kisha akarudi na kuketi sehemu yake.
Ilifika zamu ya mawakili wa upande wa utetezi, nikamuona yule wakili wa kiume kati ya wale watatu waliokuwa wakinitetea, akisimama na kwenda kutoa heshima kwa jaji kisha akaanza kuwasilisha utetezi wake juu yangu.
Kitu ambacho lazima nikiseme ni kwamba, sheria ni kama mchezo fulani mzuri ambao ukiujua, ama kwa hakika unavutia mno. Nasema hivyo kwa sababu yule wakili aliposimama, alianza kuzungumza mambo ambayo yalinipa nguvu kubwa. Kila mtu aliyekuwa mle mahakamani, alitulia kimya kabisa wakati sheria zikichambuliwa kwa uzoefu wa hali ya juu.
Kwa mbali nikaanza kuuona upenyo wa kuiepuka adhabu kali iliyokuwa mbele yangu kwani wakili huyo alijenga hoja vizuri mno, kesi ikaanza kugeuka kutoka mimi kuwa mtuhumiwa mpaka kuwa muathirika namba moja wa unyanyasaji wa kijinsia.
Japokuwa wakati nakutana kimwili kwa mara ya kwanza na Jimmy, mwenyewe nilikuwa najiona nimeshakuwa mkubwa kumbe kisheria bado nilikuwa mtoto kwa sababu nilikuwa nimebakiza miezi miwili kabla ya kutimiza miaka 18.
Nikashangaa kugundua kuwa kumbe kisheria mwanaume akifanya mapenzi na msichana ambaye hajatimiza miaka 18, hata kama walikubaliana inahesabika kuwa ni ubakaji. Ili kuupa nguvu utetezi huo, wakili huyo alikuwa na cheti changu cha kuzaliwa mkononi, hata sijui alikipata wapi lakini nahisi ni kaka ndiyo alimpa.
Cheti hicho kikathibitisha kwamba ni kweli wakati nakutana na Jimmy kwa mara ya kwanza na kufanya naye mapenzi, sikuwa nimetimiza miaka 18 ingawa wakati nafanya tukio la kumpiga Jimmy na jiwe na kuyakatisha maisha yake, tayari nilikuwa nimetimiza umri huo na ndiyo maana nilipelekwa kwenye gereza la wakubwa na kupandishwa kwenye mahakama kubwa.
Pia wakili huyo alijenga hoja nyingine kadhaa, zote zikionekana kuwa na nguvu sana ikiwemo ile ya kusema nilimtishia Jimmy kifo nikiwa katika hali isiyo ya kawaida kiakili kwani nilikuwa nimetolewa ujauzito bila ridhaa yangu, jambo ambalo pia lilikuwa ni kosa kwa Jimmy na watu alioshirikiana nao.
Hata mazingira ya tukio lenyewe la kuyakatisha maisha ya Jimmy, yalijengewa hoja na kuonekana kuwa nilikuwa nikijihami kwa sababu Jimmy ndiye aliyeanza kunishambulia na kunijeruhi vibaya.
Pia ikaelezwa na wakili huyo kuwa sikuwa na lengo la kumuua na ndiyo maana sikubeba silaha yoyote na hata hilo jiwe lenyewe, nilimpiga nalo mara moja. Pia ikaelezwa kuwa yote hayo yalitokea nikiwa na msongo wa mawazo kwani mama yangu alikuwa akiteseka hospitalini na ikaelezwa kwamba mimi ndiye niliyekuwa naenda kumtafutia mtu wa kumpa tiba ya kisaikolojia.
Nilimuona hakimu akiwa bize kuandika maelezo hayo kutoka kwa wakili wangu kisha alipomaliza, alitoa heshima kwa jaji na kurudi kwenye kiti chake, nikamuona akipeana mikono na wenzake kama ishara ya kupongezana. Nilijikuta nikitokwa na machozi ya furaha kwani kwa jinsi wakili huyo alivyokuwa amejenga hoja nzito, hakukuwa na ubishi kuwa kesi itabadilishwa kutoka mauaji hadi kuua bila kukusudia.
Baada ya muda, nilimuona jaji na jopo lake la wazee wa mahakama wakiinuka, watu wote wakatangaziwa kwamba wakapumzike kwa dakika thelathini kisha watarudi tena kuendelea na kesi. Nafikiri jaji alifanya hivyo kwa lengo la kupata muda wa kwenda kujadiliana kuhusu mwenendo wa kesi hiyo.
Nikachukuliwa na kurudishwa kwenye chumba maalum ambako nilikaa mpaka dakika thelathini zilipoisha. Nikarudishwa tena kizimbani ambako nilikuta watu wote wakiwa wamesharejea na kukaa kwenye nafasi zao. Jaji akaanza kuieleza mahakama muafaka waliofikia.
Jaji huyo mwanamke, baada ya kurejea na jopo lake na kila mmoja kukaa sehemu yake, aliieleza mahakama kuwa baada ya kusikiliza pande zote mbili, upande wa mashtaka na upande wa utetezi, yeye pamoja na jopo la wanasheria na wazee wa mahakama, wamebaini kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kimakosa.
Akaeleza kuwa mazingira ya tukio yanaonesha kwamba haikuwa kesi ya mauaji ya kukusudia (murder) kama jalada lilivyokuwa limefikishwa kwake bali ilikuwa ni ya kuua bila kukusudia (manslaughter).
Akaagiza kwamba jalada la kesi yangu lirudishwe kwa mwendesha mashtaka mkuu wa serikali (DPP) kwa ajili ya marekebisho kwani lilifikishwa kwake kimakosa. Nilijikuta nikiinua mikono juu na kumshukuru Mungu kwani kile nilichokuwa nimeambiwa na wale mawakili waliokuwa wananitetea sasa kilikuwa kinaelekea kutimia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliikumbuka vizuri kauli yao kwamba wanaweza kunisaidia kunitetea kwa kadiri ya uwezo wao na kuigeuza kesi ya mauaji iliyokuwa inanikabili hadi kuwa kuua bila kukusudia ambayo adhabu yake haikuwa kubwa sana.
“Dhamana iko wazi kwa mshtakiwa, anatakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao ni wafanyakazi wa serikali ambao kila mmoja ataweka dhamana ya shilingi milioni ishirini, mshtakiwa hatatakiwa kutoka nje ya Jiji la Dar es Salaam bila idhini ya mahakama.
“Pia mshtakiwa atatakiwa kuripoti mahakamani hapa kila baada ya siku saba na kama ana hati ya kusafiria, anatakiwa kuikabidhi kwa msajili wa mahakama. Tarehe ya kuanza tena kusikilizwa kesi itatangazwa hapo baadaye,” alisema jaji na kugonga nyundo mezani, yeye na jopo lake wakainuka na kutoka kupitia mlango wa nyuma.
Nikiwa bado nimesimama kizimbani, nilijikuta nikitokwa na machozi nikiwa ni kama siamini kilichokuwa kinatokea.
Baada ya hakimu kutoka, niliwaona wale mawakili waliokuwa wakinitetea wakiinuka na kuelekea pale walipokuwa wamekaa wale wanasheria wa Tamwa pamoja na ndugu zangu.
Wakawa wanajadiliana kwa muda kisha nikamuona yule wakili aliyekuwa akinitetea akija pale kizimbani nilipokuwa nimesimama, machozi yakiendelea kunitoka, akaniambia nisiwe na wasiwasi wao wanaenda kwenye ofisi ya msajili wa mahakama kwa ajili ya kukamilisha taratibu za dhamana.
“Hata kama tukichelewa kidogo, usijali leo au kesho utarudi uraiani,” alisema huku akinishika begani, machozi yakawa yanaendelea kunitoka kwa wingi kwani hiyo ilikuwa ni sawa na ngamia kupenya kwenye tundu la sindano.
Nilimuona kaka na wadogo zangu nao wakikumbatiana kwa furaha kisha wote wakanigeukia, walipoona nalia, na wao walianza kutokwa na machozi. Nikaja kutolewa pale kizimbani na askari magereza ambao walinirudisha kwenye kile chumba cha kusubiria.
Nikakaa sakafuni huku moyo wangu ukiwa na matumaini makubwa kuliko wakati wowote katika maisha yangu. Nilimshukuru sana Mungu kwani ni kama alikuwa akijibu maombi yangu.
Eunice mimi ambaye awali nilikuwa nikikabiliwa na kesi nzito ya mauaji, leo nitoke kwa dhamana? Hakika kwangu ulikuwa ni muujiza mkubwa sana. Nadhani taratibu za dhamana zilikuwa ngumu kidogo kwani mpaka kesi zote zinamalizika kusomwa, bado sikuwa nimewaona wale mawakili wala wanasheria.
Mimi na watuhumiwa wengine tulitolewa na kupelekwa kwenye karandinga, tayari kwa safari ya kurejeshwa Segerea. Wakati napanda kwenye karandinga, niliwaona wale mawakili, wanasheria na ndugu zangu wote wakiwa wamejazana nje ya ofisi moja ambayo bila hata kuuliza nilijua ndiyo ya msajili wa mahakama.
Kwa pamoja wakageuka na kunitazama huku wakinipungia mikono ya kwa heri, wakawa wananioneshea ishara kwamba nisiwe na wasiwasi kwani wanashughulikia suala langu. Na mimi niliwapungia mikono kama ishara ya kuwashukuru kwa jinsi walivyojitolea kunisaidia.
Baada ya watuhumiwa wote kupandishwa kwenye karandinga, safari ya kuelekea Segerea ilianza huku nikiendelea kumshukuru Mungu, matumaini yakiwa yanazidi kuongezeka ndani ya moyo wangu.
Kwa kipindi kifupi tu nilichokuwa nikisota nyuma ya nondo, afya yangu ilikuwa imeporomoka kisawasawa. Nafikiri ni kwa sababu ya mawazo ambayo yalikuwa yakikitesa mno kichwa changu pamoja na hali halisi ya mahabusu na gerezani.
Hatimaye tulifika Segerea, tukateremshwa na kutenganishwa kama kawaida kisha kila mmoja akapelekwa sehemu yake. Nilipofika, jambo la kwanza ilikuwa ni kumshukuru Mungu wangu kwa miujiza yote aliyonitendea. Nilipiga magoti na kuanza kusali kwa unyenyekevu. Baada ya kumaliza, niliendelea na taratibu nyingine za maisha ya mle gerezani.
Niliona kama saa zinaenda taratibu kuliko siku nyingine zote. Hata hivyo, baadaye giza liliingia, nikawa nahesabu saa chache kabla ya kuja kutolewa rasmi na kurudi uraiani. Hatimaye siku ya pili iliwadia, asubuhi tulipoamka tu, nikaja kuitwa na kuambiwa kuwa nahitajika kwenye ofisi za mkuu wa gereza.
Harakaharaka niliongozana na askari magereza aliyekuja kuniita mpaka kwenye ofisi ya mkuu wa gereza ambapo niliwakuta wale wanasheria kutoka Tamwa wakiwa na wakili mmoja kati ya wale watatu pamoja na kaka yangu.
“Tumeshakamilisha taratibu zote za dhamana, tunaondoka na wewe,” alisema wakili wangu, nikashindwa kujizuia, nikamrukia na kumkumbatia kwa nguvu huku nikitokwa na machozi. Nilifanya hivyo kwa wale wengine wote na mwisho nikaishia kwenye mikono ya kaka ambapo hapo nilishindwa kukizuia kilio changu.
Wote tukawa tunalia kwa sauti utafikiri tumepokea habari ya msiba. Walituacha kwanza tumalize uchungu wetu kisha wakili wangu akanielekeza kwamba kuna nyaraka inabidi nizisaini kabla ya kuondoka.
Nilijifuta machozi na kuchukua kalamu, nikasaini mbele ya mkuu wa gereza kisha nikakabidhiwa vitu vyangu vichache nilivyovikabidhi siku naingia kisha tukatoka. Tulienda mpaka nje ambako gari maalum lilikuwa limepaki, wote tukaingia na safari ya kuondoka eneo hilo ikaanza.
Kila mtu alikuwa kimya kabisa ndani ya gari, mimi ndiyo nikawa wa kwanza kuuvunja ukimya kwa kumuuliza kaka kuhusu hali ya mama. Hakunijibu kitu zaidi ya kujiinamia, hali iliyoanza kunipa wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wangu.
Breki ya kwanza baada ya kutoka Segerea, ilikuwa ni nyumbani kwetu, mimi na kaka tukashuka kwenye gari huku wale wanasheria watatu na wakili mmoja wa Tamwa wakitufuata, tukaingia mpaka ndani ambapo walinisihi nitulie katika kipindi hicho, nisiwe natembeatemba hovyo na kama kuna mahali nataka kwenda, niwape taarifa kwanza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakamsisitiza kaka kuwa awe karibu na mimi na kamwe asiniache nitembee peke yangu kwa sababu za kiusalama. Niliwaelewa na kuwaahidi kutii walichoniambia, wakatuachia namba za simu za dharura na kutuambia tukikwama jambo lolote, tuwapigie simu mara moja.
Walituachia pia pesa za matumizi ambazo sikujua ni kiasi gani lakini zilikuwa nyingi kiasi, wakamkabidhi kaka na kumtaka ahakikishe anaisimamia vizuri nyumba yetu. Tuliwasindikiza kwa kuwapungia mikono mpaka walipoondoka na gari lao.
“Wadogo zangu wako wapi?”
“Wameenda shule.”
“Shule? Wameanza lini?”
“Mh! Nadhani wiki inaisha sasa.”
“Wanalipiwa na nani ada?”
“Tumesaidiwa na hawa wanasheria wa Tamwa, hata mimi ningeanza kwenda ila kwa sababu ya kusimamia mambo ya familia, nimeona nimalize kila kitu kwanza.”
“Ooh! Mungu Baba wa mbinguni, hakika wewe ni wa kipekee,” niliinua mikono na kutamka maneno hayo huku nikitokwa na machozi, tukakumbatiana na kaka na kuendelea kumshukuru Mungu kwa muujiza ule.
Ilibidi niende kwanza bafuni kuoga na kutoa nuksi zote nilizotoka nazo gerezani. Kaka alinielekeza kuwa niweke chumvi ya mezani kwenye maji ya kuoga ili kuvunja nguvu zote mbaya nilizotoka nazo gerezani. Sijui yeye alijifunzia wapi utaalamu huo ambao kwangu ulikuwa mgeni.
Baada ya hapo, nilienda chumbani na kubadilisha nguo, nikazikusanya zile nilizokuwa nimezivaa na kwenda kuzichoma moto. Angalau nikawa najihisi nimekuwa mtu mpya kabisa.
Bado nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua maendeleo ya mama kwani licha ya yote yaliyotokea, bado nilikuwa nikimpenda na kumheshimu na sikutaka kuona anaendelea kuteseka.
Nilimuuliza kaka kwa mara nyingine, kama ilivyokuwa mara ya kwanza, badala ya kunijibu alijiinamia kwa muda kisha akaniambia kuwa bado yupo hospitalini na hali yake siyo ya kuridhisha.
“Nataka nikamuone, naamini atafurahi sana kusikia nimetoka gerezani,” nilisema na kuendelea kumsisitiza kaka. Japokuwa alikuwa mgumu kidogo, nilipomng’ang’aniza sana, alikubali ila akaniambia inabidi nipumzike kwanza kidogo kisha ndiyo tuende.
Baada ya muda, tulianza kujiandaa ila kaka akaniambia inabidi nimsubiri hapohapo nyumbani akatafute Bajaj kwanza kwani hakutaka nionekane mitaani, jambo ambalo hata wale wanasheria wa Tamwa walilisisitiza kwa sababu ya usalama wangu.
Dakika kadhaa baadaye, kaka alirudi na Bajaj, dereva akaisogeza mpaka karibu na mlango, nikaingia nikiwa nimejitanda ushungi ulioacha sehemu ndogo tu ya sura yangu. Tukapanda na safari ya kuelekea hospitalini ikaanza.
Tulipofika, kaka alimlipa dereva Bajaj kisha tukashuka na kuingia hospitali. Kwa kuwa muda wa kuwaona wagonjwa ulikuwa umefika, hatukupata usumbufu wowote, tukawa tunaelekea wodini. Wakati tukiendelea kutembea, kaka aliniambia kuwa tukifika wodini, nijitahidi kujikaza na kuikubali hali nitakayokutana nayo.
Kauli hiyo ilinishangaza sana lakini sikutaka kuonesha wasiwasi wangu, akili yangu ikawa inanituma kuamini kwamba hali ya mama ilikuwa mbaya sana. Nikajikaza kama kaka alivyoniambia, tukawa tunazidi kusonga mbele kuelekea kwenye kwenye wodi ya wagonjwa wa akili.
Kwa kadiri tulivyokuwa tunazidi kusonga mbele, ndivyo mapigo ya moyo wangu yalivyokuwa yanazidi kuongezeka na hofu kunitawala. Sikujua nitamkuta mama katika hali gani hasa ukizingatia kuwa siku kadhaa zilikuwa zimepita bila kumuona.
Tulipofika kwenye mlango wa kuingilia kwenye wodi hiyo, sote tulisikia sauti ya mtu akipiga kelele kwa nguvu kutoka ndani ya wodi hiyo. Bila hata kuuliza, niliitambua sauti hiyo kuwa ni ya mama! Maskini! Nilijisikia vibaya sana. Nilimtazama kaka ambaye naye alinitazama, akanionesha ishara kwamba nizingatie alichoniambia.
Tulipoingia, macho yangu yalitua moja kwa moja kwa mtu aliyekuwa anapiga kelele. Nilishindwa kujizua kutoa machozi, mama alikuwa akifanya fujo kuliko kawaida. Alikuwa amesimama juu ya kitanda, mikononi na miguuni akiwa amefungwa kamba, nywele zikiwa timutimu.
Pia mwili wake ulikuwa umekongoroka kuliko kawaida, hakuwa mama yule ninayemjua. Niliongeza kasi, nikawapita watu wengine waliokuwa wanamshangaa mama, nikasogea mpaka kwenye kitanda chake. Hakuwa na habari, aliendelea kupiga kelele huku akizungumza mambo ambayo hakuna aliyekuwa anamuelewa.
“Mama! Mamaaa!”Nilisema huku nikimgusagusa miguuni, akanigeukia na kunitazama, nikamuona jinsi alivyokuwa amepigwa na butwaa. Hakuendelea tena kupiga kelele, akakaa kitandani taratibu huku akiendelea kunishangaa kama asiyeamini kilichotokea.
“Eunice! Ni wewe mwanangu?”
“Ni mimi mama,” nilisema huku nikilia kwa uchungu, sikujali hali aliyokuwa nayo, nilimkumbatia kwa nguvu, na yeye akawa anataka kunikumbatia lakini kamba alizofungwa mikononi zilimzuia, akawa analia kwa kwikwi huku akiniomba nimsamehe na kumsaidia kutoka kwenye yale mateso.
Kaka yangu naye alikuwa pembeni akiwa amejiinamia, watu wote waliokuwa wanamshangaa mama, wakaanza kunong’ona na kushangaa jinsi mama alivyobadilika ghafla baada ya kuniona. Waliosema damu nzito kuliko maji hawakukosea, uwepo wangu pale wodini ulimfanya mama atulie kabisa, akawa anaendelea kulia chinichini huku akinishangaa, akaniambia alishaamini kwamba sitaweza kutoka gerezani kutokana na kesi iliyokuwa inanikabili.
Ilibidi nianze kumueleza kilichotokea! Narudia kusema kuwa japokuwa watu wote walikuwa wakimuona mama kama amechanganyikiwa na hawezi kupona, mimi nilikuwa namtazama kwa jicho tofauti kabisa. Nilielewa kwa kina kilichomfanya awe kwenye hali hiyo na kwa sababu Mungu alinisaidia kurudi uraiani, nilijiapiza kuwa lazima nimsaidie.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilimsimulia mama kila kitu, akawa analia kwa kwikwi huku akijilaumu sana ndani ya nafsi yake. Alijiona kuwa na hatia kubwa sana na huenda ndiyo maana alikuwa anaonekana kama mwendawazimu. Nilizungumza naye kwa muda mrefu, nikimpa moyo na kumtaka akubaliane na hali halisi ya kilichotokea.
Baada ya kuona mama ametulia na hafanyi tena vurugu kama ilivyokuwa mwanzo, madaktari waliwapa maelekezo manesi waje kumfungua kamba baada ya kuwa nimewasihi kwa muda mrefu. Mama akafunguliwa zile kamba ambazo zilishaanza kuweka alama kwenye mikono na miguu yake.
Siku hiyo sikutaka kutoka kwenda sehemu yoyote, nilishinda kwenye wodi aliyokuwa amelazwa mama, tukiongea na kusimuliana mambo mengi ambayo kwa kiasi kikubwa yalimfanya mama aanze kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
Nilikuwa na kazi kubwa pia ya kumsafisha mama kwani ndani ya kipindi kifupi tu, alikuwa amebadilika kuliko kawaida. Nikamsuka nywele zake zilizokuwa timtim na kumkata kucha ambazo zilikuwa ndefu na chafu.
Pia nilimsimamia akaenda kuoga na kuvaa nguo nyingine safi. Angalau sasa akawa na mwonekano mzuri ingawa bado kuna muda alikuwa akiweweseka kama amerukwa na akili. Mpaka muda wa mimi kuondoka unafika, bado mama alikuwa hataki kabisa niondoke, akawa ananing’ang’ania kuwa tulale naye wodini.
Nilitumia ushawishi wa hali ya juu, akakubali niondoke kurudi nyumbani. Nikamuahidi kuwa kesho yake nitamfuata mtaalamu wa saikolojia, Dismass Lyassa kwa ajili ya kumpa tiba ya kisaikolojia ili aondokane na hali aliyokuwa nayo.
Kweli nilitoka wodini mpaka nje nilikomkuta kaka ananisubiri. Tukatoka mpaka nje ya hospitali ambapo kaka aliita Bajaj, tukapanda na safari ya kurudi nyumbani ikaanza huku kaka akinisifu kwa jinsi nilivyoweza kumtuliza mama.
Tulizungumza mambo mengi na kaka, tukakubaliana kuwa kesho yake asubuhi, tumfuate Lyassa na kwenda naye mpaka hospitalini hapo ili akatusaidie kumpa mama ushauri wa kisaikolojia utakaomsaidia kuondokana na hali aliyokuwa nayo.
Tulipofika nyumbani, tuliwakuta wadogo zangu wote wamesharudi kutoka shuleni. Waliponiona tu, walinikimbilia na kunikumbatia mwilini kwa furaha ya ajabu kwani tangu nitoke gerezani asubuhi, hatukuwa tumeonana kutokana na wao kuwa shuleni. Walinipa pole kwa yote yaliyotokea na kwa pamoja tukapiga magoti na kuanza kusali kumshukuru Mungu kwa miujiza yake.
Siku hiyo ilikuwa ya kipekee sana kwetu. Wadogo zangu walinisimulia jinsi walivyoanza kwenda shule na yote waliyokutana nayo. Nami niliwasimulia kwa kifupi yote niliyokutana nayo kuanzia siku ya kwanza nilipotokewa na balaa lile mpaka siku hiyo.
Kila mtu alikuwa ametulia wakati nikiwasimulia. Mpaka namaliza kuwasimulia kila mmoja alikuwa amelowa uso kwa machozi. Hata kaka yangu naye alikuwa na hali hiyohiyo.
Hata hivyo, nilimshukuru Mungu kwani angalau familia yetu ilianza kupata mwelekeo mpya baada ya kukosa dira tangu baba alipofariki. Baada ya kula chakula cha usiku, tulisali tena kisha tukaenda kulala.
Alfajiri kulipoanza kupambazuka tu, mimi ndiye niliyekuwa wa kwanza kuzinduka kutoka usingizini. Nikaamka na kuwaandalia wadogo zangu kifungua kinywa kisha nikawaamsha na kuanza kuwaandaa kwa ajili ya kwenda shuleni. Walifurahi sana kwani siku nyingi zilikuwa zimepita bila kupata upendo kutoka kwangu wala mama.
Walipoondoka, mimi na kaka tulijiandaa kisha tukaita Bajaj iliyotupeleka mpaka Ubungo River Side kwenye ofisi ya Dismass Lyassa. Tulipoingia ofisini kwake, tulipokelewa kwa uchangamfu na muda mfupi baadaye, tukapelekwa kuonana naye.
Nilifurahi sana kukutana ana kwa ana na Lyassa kwani kabla ya hapo, nilikuwa nikimsoma kwenye magazeti na vitabu tu alikokuwa anaandika kuhusu mambo mbalimbali ya kisaikolojia. Naye alitupokea vizuri sana, tukaanza kumueleza shida yetu.
Mimi ndiyo nilikuwa mzungumzaji mkuu, nikamsimulia kila kitu kuhusu familia yetu na mambo yote yaliyofanywa na mama. Kwa muda wote wakati nikiendelea kusimulia, Lyassa alikuwa makini kunisikiliza, huku na yeye akionesha kuguswa mno na maelezo yangu.
Nilipomaliza, wala hakuwa na mjadala, akakubali kuacha kila alichokuwa anakifanya na kuongozana na sisi mpaka hospitalini kwa lengo la kwenda kumuona mama.
Tulitoka ofisini kwake mpaka nje ambako dereva wa Bajaj alikuwa akitusubiri. Tukapanda na safari ya kuelekea hospitali ikaanza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tulipofika, ilibidi tukamilishe taratibu kadhaa za kiuongozi kabla ya Lyassa kuruhusiwa kwenda kuonana na mama. Tulipokamilisha kila kitu, tulienda mpaka wodini ambapo mama aliponiona tu, aliinuka kitandani kwake na kuja kunikumbatia kwa nguvu.
Akamkumbatia pia na kaka kisha tukamtambulisha kwa Lyassa. Baada ya utambulisho, Lyassa alimuomba mama tutoke nje ya wodi ile, kweli alikubali, nikamsaidia kumuandaa kisha tukaongozana naye mpaka nje, tukatafuta sehemu tulivu, chini ya kivuli cha mti tukakaa.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment