Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

THE LOVE YOU HAD BEFORE (PENZI ULILOKUWA NALO KABLA) - 4

 







    Simulizi : The Love You Had Before (Penzi Ulilokuwa Nalo Kabla)

    Sehemu Ya Nne (4)



    Maisha yakaanza upya, kutokana na maagizo aliyoyatoa Laurence, Matilda hakutakiwa kuishia hapo, alichoambiwa ni kwamba aendelee kumhudumia msichana huyo mpaka pale ambapo angekuwa mzima kabisa.

    Kiasi cha fedha walichokuwa nacho ndicho kilichomfanya mama Evadia kuanza kufanya biashara ambazo kwa kiasi fulani ziliwafanya kuwa katika maisha nafuu. Maisha yao yakaanza kuona dira, mama Evadia hakutaka kuishia hapo, alichokifanya ni kupamba zaidi, majirani wakashangaa, mabadiliko ya maisha yao yalikwenda kwa kasi mno.

    Siku zikakatika, Evadia akapata nafuu na kuanza kutembea, hakujisikia kizunguzungu kama kipindi cha nyuma, kwa kifupi, afya yake ilirudi katika hali ya kawaida.

    Katika kipindi chote alichokuwa akiendelea kupata matibabu nyumbani huku maisha yao yakiendelea kuimarika kutokana na fedha walizosaidiwa, Laurence hakuweza kuonekana nyumbani hapo.

    Hilo halikumtia wasiwasi mtu yeyote yule kwani walihisi kwamba kutokana na ugonjwa aliokuwa akiumwa, aliendelea kupata matibabu nyumbani kwake. Mama Evadia alionekana kujisahau, alianza kumsahau Laurence ambaye ndiye aliyefanya maisha ya binti yake kutengemaa.

    Kitendo cha Laurence kutoonekana, hakutaka hata kumpigia simu na kumuuliza aliendeleaje, kila siku alikuwa mtu wa kuwa bize tu, alifikiria kuhusu biashara zaidi kwani maisha ya shida aliyokuwa ameyapitia yalionekana kumfundisha mambo mengi mno.

    “Niliwasiliana na Laurence, anawasalimia, hali yake si nzuri kwa sasa, anasema kidonda bado kinamuuma,” alisema Matilda, alikuwa akizungumza na Evadia aliyekuwa na mama yake.

    “Masikini weeee, mpe pole sana. Ningekwenda kumuona leo ila sina muda, kuna mzigo fulani nitakwenda kuchukua baadaye, ila nikiwahi kurudi, nitakwenda kumuona, nitakupigia simu uje kunichukua,” alisema mama Evadia maneno yaliyomfanya Matilda kushtuka.

    “Sawa mama! Unaonaje tukienda kumsalimia Evadia?” aliuliza Matilda.

    “Bado sijawa vizuri, nikipona, nakuahidi nitakwenda,” alijibu Evadia.

    Kilichowachanganya ni fedha walizokuwa wakizipata, ziliwachanganya mno, hawakuwahi kuwa na fedha kama kipindi hicho, walichokiangalia ni kuendelea kufanya biashara kwa kuamini kwamba kama wasingeweza kuzisimamia biashara hizo basi mwisho wa siku wangerudi kule walipokuwa.

    Hawakuwa wakiishi Mburahati, walihama na kuhamia katika nyumba nzuri iliyokuwa Mabibo, nyumba yenye umeme ambayo ilikuwa na kila kitu ndani yake. Kama maagizo ya Laurence yalivyokuwa, hakutaka kumuona Matilda akikata mguu kwenda huko, bado aliwatembelea na hata siku nyingine kuwapa fedha japokuwa walikuwa na fedha ambazo ziliwafanya maisha yao kuwa vizuri.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Dickson alichanganyikiwa na penzi la Luciana, hakutaka kusikia kitu chochote kile, kila wakati alikuwa na msichana huyo, alimpenda kwa moyo wa dhati, hakutaka kumuacha na kila alipomwangalia, mbele yake aliyaona maisha ya milele ambayo wangeishi kama mume na mke.

    Siku zikakatika mpaka msichana huyo alipoondoka nchini Tanzania kuelekea Rwanda, huko, kama kawaida mapenzi yaliendelea, waliwasiliana kwenye simu na hata mitandaoni, kwa Dickson hakuonekana kuwa na wasiwasi kwa msichana huyo, alimwamini kwa kila kitu na kuona kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima mwisho wa siku waishi pamoja kama mke na mume.

    “Unakumbuka nilichokwambia?” aliuliza Dickosn.

    “Kuhusu nini?”

    “Harusi!”

    “Nakumbuka, ulisema lini vile?”

    “Mwaka ujao, ninataka kuishi nawe milele, hakuna kingine,” alisema Dickson.

    “Kweli?”

    “Ndiyo!”

    “Nashukuru mpenzi, nakupenda pia, ninatamani niishi nawe milele,” alisema msichana huyo maneno yaliyomfanya Dickson kusikia furaha moyoni mwake pasipo kukumbuka kwamba tabia ni kama ngozi ya mwili ambayo huwezi kuibadili.



    Kila kitu kilibadilika, hawakutaka kusikia la mtu yeyote yule, masikini akapata, akasahau alipotoka, akasahau juu ya mtu aliyewafanya kufika mahali hapo. Hakukuwa na mtu aliyemkumbuka mwanaume aliyeonekana kuwa masikini kwao, Laurence, siku za mwisho kuonana naye zilikuwa kipindi kile kule hospitali alipoamua kubadilisha figo yake na kumpa Evadia, baada ya hapo, hakukuwa na mtu aliyemkumbuka.

    Evadia alipona, alisahau juu ya mtu aliyemfanya kuwa na afya njema, kila alipokaa, maneno yake yalikuwa ni Mungu ndiye aliyemfanya kuwa mzima wa afya na si Laurence kwani kama Mungu angeamua afe, angekufa tu hata kama angebadilishwa figo.

    Biashara zao ziliendelea vizuri, walikwenda walipotaka na fedha walizokuwa wakikabidhiwa na Matilda ziliendelea kuyabadilisha maisha yao huku biashara zao zikiendelea vizuri kwa kuwaingizia kiasi kikubwa cha fedha.

    Maneno ambayo kila siku walimwambia Matilda ni kwamba kama kwenda kumuona Laurence, wangekwenda lakini si katika kipindi hicho kwani walikuwa bize mno na biashara na msichana Evadia alihitaji mapumziko zaidi, hivyo kama kwenda kumuona Laurence ambaye ilisemekana kwamba alikuwa hoi, isingewezekana kufanyika siku hiyo, alitakiwa kusubiri mpaka siku nyingine.

    “Kwani wewe unazipata wapi taarifa za Laurence?” aliuliza mama Evadia huku akimwangalia Matilda usoni.

    “Aliwahi kunielekeza anapoishi, mbali na hilo, ana namba yangu ya simu,” alijibu Matilda kwa sauti ya upole.

    “Oooh! Kumbe! Sawa!”

    “Sasa inakuwaje?”

    “Kuhusu?”

    “Kwenda kumuona!”

    “Bado tupo bize kwa sasa, ila tutakwenda tu.”

    Huo ulikuwa mwezi wa pili lakini hakukuwa na aliyesumbuka kusimama na kwenda kumuona Laurence ambaye walisikia juujuu tu kwamba alikuwa hoi kitandani.

    Waliendelea na maisha yao kama kawaida huku mwanamke yuleyule ambaye kipindi cha nyuma alikuwa akikaa nje akisuka ukili, leo hii aliendesha gari, kwao, maisha yalikwenda kasi sana.

    Mwezi wa tatu ulipoingia, siku moja wakaanza kusikia mlango ukigongwa tena mgongaji akigonga kifujofujo sana hali iliyowafanya Evadia na mama yake kuwa na hasira kwani ugongaji ule haukuwa wa kistaarabu hata mara kidogo.

    Mama Evadia akasimama na kutoka nje, akalifuata geti. Kwa kipindi hicho, Jua lilikuwa kali mno, alipolifikia geti, akalifungua, macho yake yakatua usoni mwa Laurence.

    “Shikamoo mama,” alisalimia Laurence huku akitoa tabasamu pana.

    Kabla ya kuitikia salamu ile, akaanza kuyapeleka macho yake chini mpaka juu, mwanaume aliyesimama mbele yake ndiye aliyemsaidia binti yake kuwa na afya mpaka kipindi hicho. Hakumpenda kijana huyo, hakutamani kumuona maishani mwake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alionekana kupigwa na maisha, alichoka, mavazi yake yalikuwa mabovu, kichwani alikuwa na nywele timutimu huku miguuni akiwa na kandambili zilizochoka sana, muonekano wake tu ulitosha kuonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa masikini.

    “Nani amekuelekeza hapa?” aliuliza mama Evadia hata kabla ya kuitikia salamu.

    “Kuna majirani zenu walinielekeza.”

    “Oooh! Sawa.”

    “Evadia yupo?”

    “Hayupo! Amesafiri.”

    “Amekwenda wapi?”

    “Moshi!”

    “Sawa mama! Nimechoka sana, naomba nipumzike ndani kwenye kivuli,” alisema Laurence huku akijionyesha kuchoka hasa.

    “Uingie ndani?”

    “Ndiyo!”

    “Utakaa na nani?”

    “Si na wewe mama.”

    “Hapana! Mimi natoka.”

    Mama Evadia alibadilika sana, fedha zikamtia jeuri hivyo hata Laurence kwake hakuonekana kuwa kitu, hakuwa na thamani hata mara moja. Hilo lilimuumiza sana Laurence, alijua fika kwamba mwanamke huyo hakuwa akitoka bali alisema hivyo kwa kuwa tu hakutaka aingie ndani.

    Moyo wake ulichoma kwa maumivu makali lakini hakuwa na jinsi, fedha zikambadilisha mwanamke huyo, alichokifanya ni kufunga geti na kurudi ndani huku akimwacha Laurence pale getini akiendelea kuchomwa na jua.

    Alipoingia ndani, akamfuata binti yake na kumwambia kuhusu Laurence, alifika mahali pale na kutaka kumuona lakini alikataa kwa kuwa hakuwa msafi, hakustahili kuingia ndani ya nyumba yao kwani angepachafua.

    “Hivi bado ananikumbuka?” aliuliza Evadia.

    “Anakukumbuka sana. Amechoka huyo, ungemuona, ungetema mate chini,” alisema mama Evadia.

    “Kweli?”

    “We acha tu. Mpaka anatisha.”

    Walikaa na kuanza kucheka, waligongesheana mikono kwa furaha tele. Mioyo yao ilibadilika, chuki kubwa ikajengeka kwa Laurence, alionekana si kitu tena, hata ule upendo aliokuwa nao uliompelekea kutolewa figo yake kwa ajili ya msichana huyo hakikuonekana kuwa kitu, hakikuonekana kuwa na thamani tena, fedha ziliwabadilisha wote wawili.

    Kwa upende wa Laurence, aliumia sana moyoni mwake, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, kitendo chake cha kutoa figo yake na kumpa msichana huyo hakikuonekana kuwa na thamani yoyote ile. Kilimuumiza moyo wake lakini hakuwa na jinsi.

    Huo ulikuwa mwanzo tu, hakutaka kukata tamaa, kila siku alifika nyumbani hapo lakini mama Evadia alipofungua geti na macho yake kugongana na ya Laurence, tayari alionekana kukasirika, hakukuwa na kitu kilichomuudhi kama kumuona mwanaume huyo nyumbani kwake.

    “Umefuata nini?” aliuliza huku akionekana kuwa na hasira.

    “Nimemfuata Evadia.”

    “Kwani umemuona?”

    “Hapana mama! Ninataka nimuone.”

    “Hayupo.”

    “Yupo wapi?”

    “Alikwishakufa kitambo sana,” alijibu mwanamke yule.

    “Naomba unionyeshee hata kaburi lake mama.”

    “Nenda Kinondoni, zunguka makaburi yote, utaliona tu,” alisema mama Evadia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Laurence aliendelea kuumia lakini hakuwa na cha kufanya zaidi ya kuondoka mahali hapo huku moyo wake ukimuuma sana. Alipiga hatua huku machozi yakimdondoka, hakukuwa na kitu kilichomuuma kama hicho.

    Alimpenda sana Evadia, hakutaka kumpoteza maishani mwake, alikuwa na thamani kuliko kitu chochote katika maisha yake lakini siku hiyo hakuonekana kuwa kitu chochote kile.

    Kulikuwa na vitu ambavyo vilimuumiza sana lakini hicho kilikuwa ni zaidi ya vyote. Hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, kuuficha ukweli kwamba alikuwa tajiri kulionekana kulififisha penzi lake kwa msichana Evadia.

    “Bosi! Imekuwaje tena?” aliuliza Matilda kwenye simu.

    “Wewe acha tu Matilda. Majanga.”

    “Kivipi?”

    “Nimefukuzwa, tena nimeambiwa kwamba Evadia amekufa.”

    “Kweli?”

    “Ndiyo! Yaani imeniuma sana. Kumbe fedha zinaweza kumbadilisha mtu namna hii?”

    “Ndiyo hivyo! Pole sana bosi. Kwa hiyo inakuwaje?”

    “Kuhusu nini?”

    “Kuwasaidia fedha, nisitishe?”

    “Hapana! Sipendi Evadia awe na maisha magumu. Ninampenda sana, ninapenda kumuona akiwa na furaha siku zote. Endelea kuwasaidia kwani hata biashara zao nahisi haziingizi kiasi kikubwa cha fedha,” alisema Laurence.

    “Basi sawa. Nitafanya hivyo bosi.”

    “Nitashukuru, ila kumbuka kwamba unatakiwa kuficha siri, kuanzia kwa wafanyakazi ofisini mpaka kwao wenyewe.”

    “Hakuna tatizo.”

    Alichokifanya Laurence ni kuchukua kalamu kisha kuanza kuandika barua ndefu. Hakupata nafasi ya kuzungumza na msichana huyo hivyo kitu pekee alichokiona ni kuzungumza naye kupitia maandishi tu.

    Alikaa chini na kufikiria ni jinsi gani alimpenda Evadia, alijaribu kukumbuka siku ya kwanza kumuona uwanja wa Taifa, alipoanza kuongea naye mpaka siku hiyo, hakika moyo wake ulimuuma mno, hivyo vitu vyote alitaka kuviandika katika barua hiyo kwa kuamini kwamba msichana huyo angeweza kukumbuka na kumuonea huruma.

    Akaanza kuandika huku moyo ukimuuma mno, utajiri wote aliokuwa nao ulionekana kuwa si kitu kwa kuwa tu msichana aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati hakuwa pamoja naye, alimkataa kwa kuwa alikuwa masikini, hakuwa na thamani maishani mwake.

    Alichukua muda wa saa moja kuandika barua hiyo yenye kurasa mbili, alipomaliza, akaifunga vilivyo kwenye bahasha kisha siku iliyofuata kuanza kuelekea huko Mabibo.

    Matilda alimpakiza ndani ya gari, walipokaribia, akateremka na kuanza kuelekea katika nyumba ile. Muonekano wake ulikuwa uleule kwamba kijana masikini asiyejiweza, mtu aliyepigwa sana na maisha, alipolifikia geti lile, kama kawaida akaanza kuligonga.

    “Jamani! Mbona unasumbua sana siku hizi?” aliuliza mama Evadia mara baada ya kufungua geti, alionekana kukasirika.

    “Mama! Ninampenda Evadia, kusumbuka kwangu hakukuanzia hapa, tangu kipindi kile cha nyuma,” alisema Laurence.

    “Aya nikusaidie nini?”

    “Najua kwamba Evadia yupo ndani, naomba umpe hii barua yake, sina mengi ya kuzungumza,” alisema Laurence huku akimgawia mwanamke huyo hiyo barua.

    “Sawa. Kuna kingine?”

    “Hakuna!”

    “Basi unaweza kwenda,” alisema mwanamke huyo na kulifunga geti.

    Mama Evadia akarudi ndani huku mkononi mwake akiwa na barua ile, alitaka kufahamu mwanaume huyo aliandika vitu gani, alipoingia ndani, akamfuata Evadia aliyekuwa chumbani akisikiliza muziki kisha kumgawia barua ile.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hii nini?”

    “Barua yako ameileta yule nguchiro wako,” alijibu mama yake.

    “Ila si ulimwambia nimekufa!”

    “Sasa yeye ameng’ang’ania kukufufua, nifanyeje!”

    “Sawa.”

    Alichokifanya Evadia ni kuanza kuifungua bahasha kisha kukutana na karatasi iliyokuwa imeandikwa kwa kirefu sana, japokuwa hakuwa msomaji wa maandishi mengi lakini alichokifanya ni kuanza kuisoma barua hiyo, kama mtu aliyejilazimisha, akaanza kulisoma neno moja baada ya jingine, mstari kwa mstari. Barua hiyo iliandikwa hivi....



    Kwako Evadia.

    Nakumbuka siku ya kwanza nilipokuona, hakika moyo wangu ulitokea kukupenda kuliko msichana yeyote yule. Ulikuwa msichana mrembo ambaye hakika sikujuta kukufuata mpaka ulipokuwa unaishi, sikuishia siku hiyo tu, ili kukuonyeshea kwamba nilikuwa nakupenda sana, niliendelea kukufuata mpaka pale ulipokubali kuwa wangu.

    Evadia, nini kimekukuta? Kwa nini unanifanyia hivi? Ninaumia, unajua ni jinsi gani ninakupenda, unajua ni kwa jinsi gani umekuwa msichana pekee katika maisha yangu. Niliamua kutoa figo yangu moja kwa ajili yako, sikutaka kukuona ukiteseka kitandani, sikutaka kukuona ukifa kitandani pale, kwa mapenzi yangu yote, nikaamua kutoa figo yangu kwa kuwa nilitaka kukuona ukiwa na afya njema, utabasamu kama zamani, na kwenye kucheka, ucheke pia.

    Kila kitu kimebadilika, upendo wangu mwingi umeonekana si kitu, matokeo yake, umeamua kuniacha kama nilivyo, tena mbaya zaidi nikiwa mgonjwa. Evadia, una figo mbili, kumbuka figo moja hiyo yenye nguvu ni yangu, kwa nini hutaki kunithamini? Kwa nini hutaki kunipenda tena?

    Gharama ya figo ilikuwa ni milioni ishirini, nilikudai chochote? Sikufanya hivyo, upendo wangu juu yako ulikuwa ni zaidi ya hiyo milioni ishirni, kwa nini umebadilika? Kwa nini umeamua kunifanyia hivi?

    Evadia, fedha si kitu, unaweza kuwa tajiri leo, ukabadilisha magari, ukawa na ndege yako lakini kesho ukawa mbeba mizigo katika soko fulani, ndiyo! Hayo ni maisha na wengi yamewatokea.

    Mama yako aliniambia kwamba umekufa, sikutaka kukubaliana naye kwa kuwa naamini upo hai ukitabasamu na kuringia figo yangu moja niliyokupa.

    Kama kweli upo hai, naomba ujue kwamba ninateseka kwa penzi lako, sijiwezi bila wewe, naomba uje kuniokoa masikini mimi kwani maisha yananipigika sana, nimekuwa sina kitu, sina pa kuomba msaada, ila kwa sababu kwa sasa maisha yako ni afadhali, naomba unikumbuke na mimi, kumbuka upendo wangu, kumbuka kwamba hakuna mwanamke ninayempenda maishani mwangu kama ninavyokupenda.

    Kama upo tayari, naomba urudi kwangu, naomba tutengeneze maisha pamoja. Siangalii fedha zenu, siangalii maisha yenu, ninachokiangalia ni upendo wa dhati nilionao juu yako.

    Nakupenda Evadia. Rudi kwangu.

    Mpweke, Laurence.



    Ilikuwa barua yenye kuhuzunisha sana, barua yenye kugusa moyo, barua ambayo kama angetumiwa mtu wa kawaida, angeamua kubadilisha maisha yake na kufanya kile kilichotakiwa kufanya lakini kwa Evadia, alipoisoma barua ile akabaki akitabasamu, maneno yaliyoandikwa hayakumchoma hata mara moja, alibaki akicheka, alipomaliza akaikunjakunja na kuichana, akazichukua hedifoni zake na kuziweka sikioni, kilichofuata ni kuendelea kusikiliza muziki.

    Moyo wake ulibadilika, mapenzi aliyokuwa nayo kabla yalipotea, hakumpenda tena Laurence, alimchukia kwa kuwa tu hakuwa na fedha, alisahau kwamba mwanaume huyohuyo aliamua kumpenda japokuwa nyumbani kwao maisha yao yalikuwa ya shida mno.

    Siku zikaendelea kukatika, mawazo ya Laurence akaanza kuyafuta kichwani mwake, hakutaka kumkumbuka, hakutaka kukumbuka lolote lile juu ya mwanaume huyo, kwa kifupi hakutaka hata kumuona.

    “Ameandikaje?” aliuliza mama yake.

    “Alikuwa analialia tu.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hebu niisome.”

    “Nishaichanachana, sina muda wa kuhifadhi uchafu,” alijibu Evadia.

    Kama kubadilika, alibadilika, hakutaka kusikia la mtu yeyote yule. Miezi miwili baadaye akapona kabisa na hivyo kumsaidia mama yake katika biashara zake alizokuwa akizifanya.

    Pamoja na mabaya yote hayo lakini ikawa kama Mungu amefungua milango ya baraka, waliingiza fedha, hawakuwa matajiri lakini waliweza kujikimu maisha yao na kiasi cha fedha kama milioni tano hakikuwapiga chenga kabisa.

    Alifanyiwa ubaya, alisahaulika lakini Laurence hakutaka kuacha kumsaidia msichana huyo, alimpenda kwa moyo wa dhati, alihakikisha kwamba maisha yake kila siku yanakuwa kama vile alivyotaka yawe.

    Hakutaka kutafuta msichana mwingine, kwake, Evadia alionekana kuwa kila kitu. Hakuacha kwenda nyumbani kwa msichana huyo, wakati mwingine alipofika huko na kugonga hodi, mama Evadia alipofungua mlango na macho yake kutua kwa Laurence, aliufunga mlango huo kwa dharau.

    Laurence hakuwa akiondoka, alichokifanya ni kubaki hapo nje, jua lilikuwa kali, alichokifanya ni kukaa hapohapo getini. Kwa jinsi alivyokuwa mchafu, watu waliokuwa wakipita nje walifikiri kwamba alikuwa ombaomba, hawakumjua kabisa kama alikuwa bilionea, kwao, mtu huyo alionekana kujaa umasikini mkubwa.

    Waliokuwa na fedha, walimsaidia hapohapo getini, hawakujua kama fedha hizo walikuwa wakimpa bilionea mkubwa. Laurence aliendelea kubaki getini, moyo wake ulijawa na hasira kali lakini hakutaka kuzionyesha, alitamani aingie ndani na kuwaambia kwamba yeye alikuwa bilionea na yule Laurence aliyekuwa akisikika mitaani na kuwa gumzo kutokana na utajiri wake alikuwa yeye lakini hakutaka kufanya hivyo, alitaka kuona mwisho wake ungekuwa upi.

    “Matilda, njoo huku kwa kina Evadia,” alimwambia Matilda kwenye simu.

    “Kuna nini bosi.”

    “Wewe njoo tu.”

    “Sawa bosi.”

    Laurence akakata simu na kuanza kumsubiri msichana huyo aweze kufika ili afanye kile alichotaka mafanyie. Ilipita nusu saa, gari aina ya Verrosa likafunga breki mbele ya nyumba hiyo na Matilda kuteremka, alipomuona Laurence pale chini alipokuwa, akabaki akishangaa, hakutegemea kumuona bosi wake mahali pale.

    “Nini kimetokea?” aliuliza Matilda huku akionekana kushangaa.

    “Yaani umesahau kama tunaigiza? Usihuzunike sana. Nimefungiwa mlango. Mama Evadia ametoka, aliponiona, akarudi ndani na kufunga mlango,” alisema Laurence.

    “Hapana! Haiwezekani.”

    “Ndiyo hivyo! Naomba upige hodi tena kwa honi ili aje kufungua tuingie ndani, tukifika humo, omba tuonane na Evadia,” alisema Laurence.

    “Sawa.”

    Hicho ndicho kilichotakiwa kufanywa, alichokifanya Matilda ni kurudi garini kisha kuanza kupiga hodi kwa kutumia honi ya gari. Wala hazikupita dakika nyingi, mama Evadia akatokea na kulifungua geti.

    Matilda akaingiza gari ndani ya nyumba hiyo, Laurence hakutaka kubaki nje, naye akatumia nafasi hiyohiyo kuingia ndani. Mama Evadia hakutaka kumwambia kitu chochote japokuwa alimwangalia kwa jicho kali lililoonyesha hasira kubwa kwani hakutaka kumuona hata kidogo.

    Matilda akateremka, uso wake ulijawa na tabasamu pana, akamsalimia Laurence kana kwamba hakuwahi kumuona kisha kumsogelea mama Evadia na kumsalimia pia.

    “Karibuni ndani,” alimkaribisha mama Evadia na wote kuanza kwenda ndani.

    Alichokifanya mama Evadia ni kuanza kuonyesha unafiki, akajifanya kumchangamkia Laurence ili Matilda asigundue kilichokuwa kikiendelea na wakati nyuma ya pazia, kila kitu kilichotokea kilijulikana na kila mtu.

    Wakaingia ndani, wakakaa kochini na kuanza kuzungumza mambo mengi. Muda wote huo mama Evadia aliendelea kulionyesha tabasamu pana usoni mwake. Alichokifanya Matilda ni kumuomba mwanamke huyo amuite Evadia, hilo halikuwa tatizo, hapohapo alipokaa, akamuita binti yake kwa sauti kubwa, akaitikia na kumwambia kwamba angekuja.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wala haikupita hata dakika moja, Evadia akatokea sebuleni hapo. Macho yake yalipotua kwa Laurence tu, akabaki akiwa na mshtuko mkubwa, hakuamini kumuona mahali hapo, ili kujifanya hajashtuka, akaanza kutoa tabasamu pana lakini mshtuko wake haukufichika usoni mwake.

    “Karibuni sana,” alisema Evadia huku akiwasogelea na kuwasalimia.

    Moyo wa Laurence ukapoa, hakuamini kama mpenzi wake alipona kabisa na kuwa mzima wa afya, akashindwa kuvumilia, hapohapo akasimama na kisha kumkumbatia kwa nguvu kama mtu ambaye hakutaka kumuacha aondoke zake.

    Mapenzi aliyokuwa nayo yalikuwa makubwa mno, alikuwa tayari kitu chochote kitokee lakini si kuona akimkosa msichana huyo ambaye hakuwa na habari naye kabisa.

    “Nimekukumbuka mpenzi,” alisema Laurence, tayari machozi ya hisia yakaanza kumtoka.

    “Nimekukumbuka pia,” alisema Evadia, lakini uso wake ulitofautiana na maneno aliyoyasema mahali hapo.

    Wakaanza kuzungumza, muda wote Laurence alikuwa akimwangalia Evadia, kila alipomtazama, alihisi mapenzi mazito moyoni mwake, alihisi kumpenda msichana huyo maradufu.

    Alichokifanya ni kuchukua simu yake, alitaka kurekodi sauti juu ya kila kitu ambacho kingesemwa mahali hapo, alitaka kubaki na kumbukumbu, ushahidi ambao hapo baadaye ungemfanya Evadia kulia sana, hivyo akaanza kurekodi.

    Matilda hakutaka kukaa sana, alichokifanya ni kuondoka kwani ndiyo meseji aliyoandikiwa kisiri na Laurence kwamba alitakiwa kuondoka, akaaga na kuondoka zake.

    Wakabaki watatu ndani ya nyumba, Evadia na mama yake wakaanza kumwangalia Laurence kwa macho ya chuki, hakukuwa na mtu aliyempenda kwa wakati huo kwa sababu tu alikuwa mtu masikini ambaye hakuwa na uwezo wowote ule.

    “Evadia...” aliita Laurence.

    “Nini?”

    “Mbona unanifanyia hivi mpenzi?” aliuliza.

    “Nani mpenzi wako?”

    “Wewe hapo.”

    “Tangu lini? Hivi mama hukumwambia kwamba ninataka kuolewa?” aliuliza Evadia.

    “Sikumwambia, nilisahau.”

    “Unataka kuolewa?”

    “Ndiyo! Tena ningetaka mchango wako,” alisema Evadia huku akimwangalia Laurence kwa macho ya chuki.

    “Evadia, mbona unaamua kunifanyia hivi?”

    “Hivi wewe mwanaume mbona unapenda kuishi kwa mazoea? Yaani unapenda kuishi kwa historia tu, hivi unafikiri kama zamani nilikuwa mpenzi wako basi mpaka sasa hivi ni mpenzi wako? Hebu acha maneno yako,” alisema Evadia na kumalizia na msonyo mmoja mkubwa.

    Maneno yalimuumiza moyo wake, maneno hayo yalimchoma, alihisi kitu chenye ncha kali, tena kikiwa cha moto kikiuchoma moyo wake, alisikia maumivu makubwa ya moyo, hakuamini kama kweli maneno yale aliyazungumza Evadia au mtu mwingine.

    “Unasemaje Evadia....”

    “Bwanaeeee...kwani hujanisikia,? Tangu lini umekuwa kiziwi.”

    “Evadia, kumbuka kwamba una figo yangu.”

    “Sasa nikishakumbuka?”

    “Nilifanya hivyo kwa kuwa ninakupenda.”

    “Kwani nilikulazimisha? Nilikulazimisha?”

    “Evadia mpenzi! Mbona umebadilika hivyo?”

    “Nimekuwaje? Mwekundu au wa njano? Halafu hilo neno la mpenzi unamwambia nani? Nani mpenzi wako? Nisikilize wewe masikini, sahau kila kitu kilichotokea kati yangu na wewe. Tena sahau kabisaaaa...” alisema Evadia huku akionekana kumaanisha alichokisema. Hapohapo Laurence akamgeukia mama Evadia.

    “Mama! Mbona Evadia kabadilika hivi?”

    “Nani mama yako?”

    “Jamani! Mbona mnakuwa hivi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakukuwa na mtu aliyejibu chochote, walichomwambia ni kwamba alitakiwa kuondoka nyumbani hapo mara moja. Laurence hakubisha alichokifanya ni kusimama na kutoka nje huku moyo wake ukiwa kwenye maumivu makali kwani kwa kile kilichokuwa kimetokea mahali pale, hakika hakuweza kukiamini huku wakati mwingine akihisi kama alikuwa ndotoni na baada ya dakika chache angeamka.



    Mapenzi yalikuwa motomoto, walipendana kwa mapenzi ya dhati hata pale msichana Luciana aliporudi nchini Rwanda, bado kila mmoja alijaribu kadiri ilivyowezekana kuwasiliana na mwenzake.

    Hakukuwa na kitu kilichowatenganisha, kila kilichokuwa kikiendelea katika maisha yao, walikikabidhi mikononi mwa Mungu ili mwisho wa siku wakutane tena na kufunga ndoa ambayo waliamini kwamba wasingeweza kutengana maisha yao yote.

    Luciana alikuwa na fedha, alijiona kuwa tajiri, hapohapo, alichokifanya ni kununua jumba kubwa katika mtaa mmoja wa kitajiri hukohuko Kigali, akanunua gari la thamani ambalo lilizua gumzo kubwa mitaani.

    Hilo hakutaka kuliangalia, alichokuwa akikitaka ni kuwaonyeshea watu kwamba alikuwa na fedha, alitoka nje ya nchi na kuvuna fedha nyingi, sasa katika kipindi hicho ndiyo ulikuwa muda wa kula matunda kwa kazi kubwa aliyokuwa akiifanya nchini Venezuela.

    Hakukatisha mawasiliano na Dickson, kila siku ilikuwa ni lazima kumpigia simu na kuzungumza naye. Uhusiano wao wa kimapenzi ulizidi kupanda juu, walizidi kupendana lakini baada ya miezi sita, hasa baada ya kukutana na mwanaume mwenye mchanganyiko wa mtu mweusi na uarabu, Luciana akajikuta akianza kupoteza dira katika penzi lake na Dickson.

    “Mmmh! Kumbe kuna wanaume wazuri namna hii, sijawahi kuona,” alisema Luciana huku akimwangalia mwanaume aliyesimama karibu na kaunta katika baa moja maarufu iitwayo Leopard ambayo ilikuwa katikati ya Jiji la Kigali.

    Kwa jina aliitwa Rahman Abdoulaziz, alikuwa kijana mtanashati ambaye baba yake, mzee Mohammed Abdoulaziz alikuwa Mwarabu kutoka nchini Oman huku mama yake akiwa Mtusi wa hapohapo Rwanda.

    Rahman alikuwa mzuri wa sura, wanawake wengi hapo Kigali walimpapatikia kwa kuwa ilisemekana yeye ndiye mwanaume mzuri kuliko wanaume wote waliokuwa katika jiji hilo.

    Rahman hakuwa mtu wa kupenda wanawake, alikuwa mtu wa kivyakevyake, wanawake waliokuwa wakimfuatilia, kila siku aliwatolea nje kwani alilelewa katika mazingira ya dini, hivyo hakutaka kufanya mambo ambayo yalionekana kama dhambi kubwa kwa Allah.

    Wanawake hawakuacha kumfuatilia huku na yeye hakuacha kuwakataa. Kila siku wanawake wapya waliibuka na kumtaka kimapenzi lakini msimamo wake ulikuwa uleule kwamba pepo ilikuwa muhimu kuliko mapenzi.

    Rahman alipoanza kuwa na marafiki wengi wa mitaani, hapo ndipo alipoanza kubadilika, wengi walimsifia kwamba alikuwa kijana mzuri hivyo kama alitaka kupata fedha kutoka kwa wanawake, basi uzuri wake ungekuwa chachu kubwa.

    Hilo likamfungua ubongo wake, hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kuanza kudili na wanawake waliokuwa wakimpapatikia ila fedha ndiyo kilikuwa kitu cha kwanza.

    Kulala kitanda kimoja na Rahman lilikuwa jambo zuri, kwa watoto wa matajiri hawakutaka kutulia, kila walipoambiwa kuhusu mwanaume huyo na kumuona, walikiri kwamba walikutana na mwanaume mzuri sana, hivyo wakataka kulala naye.

    Hakulala na mwanamke bila fedha, kama kulikuwa na machangudoa waliokuwa wakijiuza mitaani, basi naye kwa kipindi hicho akaamua kujiuza kwa wanawake hao ambao walimpa fedha nyingi kisha kulala naye.

    Kitendo cha Luciana kumuona Rahman hapo baa akachanganyikiwa, hakuamini kama nchini Rwanda kungekuwa na mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa Rahman, akashindwa kuvumilia, alimwangalia sana na mwisho wa siku kuanza kumfuata.

    “Unakwenda wapi Luciana?” aliuliza mmoja wa rafiki yake aliyekuwa akinywa naye.

    “Nakwenda kuzungumza na yule mwanaume,” alijibu.

    “Yupi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yule pale,” alisema huku akimnyooshea kidole Rahman.

    “Kumbe Rahman!”

    “Anaitwa nani?”

    “Rahman,” alijibu rafiki yake, hapohapo akawarudia kwanza apate kusikia mengi kuhusu mwanaume huyo.

    “Kumbe mnamfahamu?”

    “Kuna mwanamke asiyemfahamu Rahman hapa Kigali? Hakuna asiyemfahamu. Ndiye mwanaume mzuri kuliko wote, wewe mwenyewe si unamuona!” alisema rafiki yake.

    “Ndiyo! Namuona. Ana mpenzi?”

    “Mpenzi? Rahman awe na mpenzi! Huyo mpenzi hajitaki!”

    “Kwa nini?”

    “Mmmh! Anavyopendwa na wanawake, nadhani huyo mpenzi atakufa kwa presha,” alisema rafiki huyo.

    “Hilo tu?”

    “Si hilo tu. Kuna jingine.”

    “Lipi?”

    “Kama hauna hela, huwezi kuwa na mwanaume mzuri kama Rahman,” alisema rafiki huyo.

    “Kivipi?”

    “Huyo jamaa kakaa kifedha zaidi, halali na mwanamke bila fedha, yaani kama anajiuza,” alisema.

    Moyo wake ulikufa na kuoza kwa mwanaume huyo, hakutaka kusikia chochote kile, alichokitaka kwa wakati huo ni kuwa na mwanaume huyo tu. Kuhusu fedha kwake halikuwa tatizo hata kidogo, alikuwa nazo nyingi hivyo kummiliki mwanaume kama Rahman wala halikuwa tatizo kabisa.

    Alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kumfuata mwanaume huyo, alipomfikia, akasimama pembeni yake kisha kutoa tabasamu pana. Alipomwangalia vizuri kwa karibu ndipo akagundua kwamba mwanaume yule alikuwa na uzuri wa ajabu, damu yake ikaanza kuzunguka kwa kasi mwilini mwake, mapigo ya moyo yakawa yanadunda mno kiasi kwamba hata yeye mwenyewe akajishangaa.

    “Habari yako Rahman,” alisalimia Luciana.

    “Salama mrembo, karibu,” aliitikia Rahman huku akiachia tabasamu lililomfanya Luciana kuweweseka.

    “Asante. Naweza kuzungumza nawe?”

    “Kuzungumza nami?”

    “Ndiyo!”

    “Kuhusu nini?”

    “Mambo tu ya kawaida.”

    “Mmmh! Sawa. Nakupa dakika tano tu.”

    “Sawa. Tunaweza kwenda nje ya baa hii?”

    “Twende wapi sasa?”

    “Hata kwenye gari langu.”

    “Hakuna noma.”

    Rahman alikuwa mtu wa kupenda fedha, kwa jinsi alivyomuona Luciana, alijua kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima msichana huyo awe na fedha nyingi kwani kwa mtu aliyekuwa na fedha, hakika zisingeweza kujificha mwilini mwake.

    Alimtupia macho vizuri Luciana, alionekana kuwa msichana mrembo, mwenye fedha ambaye alivalia sketi fupi laini iliyoyafanya mapaja yake kuwa nje, juu alivalia blauzi laini huku ndani kukiwa kutupu kabisa kitu kilichofanya kifua chake kuonekana vizuri machoni mwa Rahman, mpaka kufika hapo, akachanganyikiwa.

    Wakatoka nje ya baa hiyo. Wakaelekea mpaka kwenye eneo la maegesho ya magari na kusimama nje ya gari moja la kifahari. Rahman alipoliona gari hilo, hakuamini macho yake, lilikuwa gari la kifahari lililoendeshwa na watu wenye fedha.

    Alizoea kuliona gari kama hilo kwenye video za wanamuziki nchini Marekani, hakuwahi kuliona laivu, kitendo cha kuliona gari hilo, akili yake ikamwambia kwamba mwanamke aliyesimama mbele yake hakuwa wa kawaida.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ingia tu,” alisema Luciana huku naye akizunguka mlango wa upande mwingine.

    Rahman akaufungua mlango na kuingia ndani. Harufu nzuri ndani ya gari lile likaifanya pua yake kuweweseka.

    Humo garini, Luciana hakutaka kuvumilia, alimwambia Rahman kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake kwamba alikuwa akimpenda sana, alimhitaji na kutaka kuwa mpenzi wake wa milele.

    Rahman hakuzungumza kitu, alibaki kimya. Kila alipomwangalia Luciana, kweli alikuwa msichana mrembo, alikuwa na fedha lakini tabia yake ya kukaa kimaslahi ilionekana kama kumharibia, hivyo alichokifikiria kwa haraka sana ni kumtalia Luciana.

    “Haiwezekani,” alisema Rahman.

    “Kwa nini?”

    “Siwezi kuwa na msichana wa kudumu, muda wa kuoa bado kabisa,” alisema Rahman kwa kujiamini.

    “Rahman, najua unachokifikiria, nimesikia mengi kuhusu wewe, jua kwamba ninajua mengi, nimeamua kukufuata wewe kwa sababu ninakupenda, u mwanaume mzuri mno, naomba uwe nami, naomba uwe mmiliki halali wa moyo wangu,” alisema Luciana huku akimwangalia mwanaume huyo usoni.

    “Kuwa na mimi?”

    “Ndiyo!”

    “Ni kitu kisichowezekana. Wewe unakuja kimapenzi na mambo ya kuishi milele na wakati mwenzako nipo kimaslahi, siwezi kuwa nawe,” alisema Rahman, alionekana kumaanisha, hapohapo akaufungua mlango kwa lengo la kutoka nje, kabla hajafanya hivyo, akashtukia akishikwa mkono na Luciana, alipogeuka, msichana huyo akamsogelea na kuanza kubadilishana naye mate ghafla.



    Dickson alichanganyikiwa, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea maishani mwake, alijaribu kumtafuta msichana wake, Luciana simuni lakini hakuwa akipatikana na hata hizo mara chache ambazo alipatikana, majibu yake yalikuwa tofauti na vile alivyokuwa akitegemea.

    Alimpenda sana, hakutaka kuwa na msichana mwingine katika maisha yake zaidi ya Luciana ambaye alimfanya kumuacha Evadia na kuwa naye. Kwake, maisha bila Luciana yalikuwa mateso makubwa, hivyo kitendo cha msichana huyo kutokueleweka simuni kulimchanganya mno.

    Hakuridhika, hakuishia hapo, aliendelea kumpigia simu msichana huyo na mara ya mwisho kabisa kuwasiliana naye, akafungiwa simu yake kitu kilichomuweka katika wakati mgumu mno.

    Alihangaika na kuhangaika, alijaribu kubadilisha simu yake lakini kitu kilichomuumiza zaidi hapo baadaye ni kwamba msichana huyo aliamua kubadilisha simu kitu kilichomsababishia maumivu makali ya mapenzi ambayo hayakuelezeka hata mara moja.

    Hakutaka wazazi wake wafahamu kitu chochote kile, yale maumivu makali, yalikuwa moyoni mwake, hakutaka kumwambia mtu yeyote. Kile kilichokuwa kikitokea kwa msichana Evadia ndicho kilichoanza kumtokea kipindi hicho.

    Hakutaka kurudi tena chuoni, hakuona kama angeweza kusoma na wakati alikuwa kwenye hali mbaya, mapenzi yalimtesa, yalimuonea na kumnyima fura ambayo alitarajia kuipata katika kipindi kifupi kijacho.

    Hakutaka kubaki nchini Tanzania, kitu alichokifanya ni kupanga safari ya kuelekea nchini rwanda, alichotaka kufahamu ni juu ya kilichokuwa kikiendelea kwa msichana Luciana kwani kuna kipindi alihisi kwamba msichana huyo alipobadilisha namba hiyo alisahau kuisevu namba yake.

    “Mbona upo hivyo?” aliuliza mama yake.

    “Nipo vipi?”

    “Unaonekana una mawazo. Halafu si leo tu, tangu juzi,” alisema mama yake.

    “Hakuna kitu mama.”

    “Sawa. Chuo vipi?”

    “Nitakwenda, ila si leo wala kesho.”

    “Kwa nini?”

    “Mama! Kuna safari nataka kwenda.”

    “Wapi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Rwanda, nataka niende kumsalimia Luciana,” alijibu Dickson.

    Huo ndiyo uamuzi aliouamua, tayari taratibu zote za safari alikwishazifanya na kitu pekee alichokuwa akikisubiria ni kuwaaga wazazi wake kisha kuondoka nyumbani hapo.

    Usiku, mama yake akamwambia baba yake juu ya kilichokuwa kimetokea kwamba kijana wao, Dickson aliamua kufunga safari kuelekea nchini Rwanda kuonana na mpenzi wake, mzee huyo alichokishangaa ni kwamba safari ilikuwa ghafla sana.

    “Kuna nini Dickson?” aliuliza baba yake.

    “Hakuna kitu.”

    “Mbona ghafla hivyo?”

    “Hakuna tatizo baba. Ninataka kumuona Luciana.”

    “Kuna amani lakini?”

    “Ipo, tena nyingi tu.”

    “Na chuo?”

    “Nitakwenda tu.”

    Hakukuwa na wa kumzuia, aliamua kuondoka nchini Tanzania na kuelekea Rwanda kwa kuwa alitaka kuonana na mpenzi wake. Japokuwa wazazi walijitahidi kumwambia maneno mengi ya kumzuia lakini Dickson hakuzuilika, hakutaka kusikia lolote lile, alichokuwa akikitaka ni kuelekea nchini Rwanda tu.

    Siku iliyofuata, mchana, akaanza safari ya kueleke uwanja wa ndege ambapo akapanda ndege na kuanza kuelekea nchini humo huku akiwa na mawazo lukuki.

    Hakuzungumza na mtu yeyote yule, abiria ambaye alikaa naye alijaribu kumuongelesha lakini majibu yake yalikuwa mafupi yaliyoonyesha kwamba alitakiwa kuachwa apumzike.

    Alichukua saa kumi mpaka kufika nchini Rwanda. Ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali, iliposimama, hapohapo abiria wakaanza kuteremka.

    Hakuwa mwenyeji sana hapo Kigali lakini siku ya kwanza aliyofika mahali hapo ilimfanya kukumbuka vilivyo kule alipoelekea na msichana Luciana, alichokifanya ni kuzifuata taksi kadhaa zilizokuwa pembeni na kuanza kuzungumza na dereva mmoja.

    “Naomba unipeleke Mwongozo,” alimwambia dereva huyo.

    “Hakuna tatizo, ingia.”

    “Ila kwanza nipeleke kwenye duka la kubadilisha fedha kisha twende huko.”

    “Hakuna tatizo.”

    Hapo ndipo safari ya kuelekea katika duka la kubadilishia fedha ilipoanza. Njiani, Dickson alikuwa na mawazo tele, alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa, kile kilichokuwa kikitokea katika maisha yake kilimchanganya mno.

    Mpaka taksi inasimama, hakuwa akijua, alikuwa kwenye lindi kubwa la mawazo. Dereva ndiye ambaye alimshtua kwamba tayari walikwishafika katika duka hilo hivyo angeendelea kufanya kile alichotaka kufanya.

    Kwa harakaharaka Dickson akateremka kutoka garini na kuanza kuelekea ndani ya duka lile ambapo akachukua fedha zake za Kitanzania na kisha kubadilisha kwa fedha za Rwanda kisha kurudi garini na kuanza safari ya kuelekea katika Mtaa wa Mwongozo.

    “Mbona una mawazo hivyo?” aliuliza dereva, wakati huo teksi ilisimama kwenye foleni.

    “Mapenzi yanauma sana.”

    “Kivipi tena? Kuna mtu kakutenda?”

    “Kuna mchumba wangu simuelewielewi kabisa, yaani yupoyupo tu,” alijibu Dickson.

    “Pole sana,” alisema dereva yule.

    Safari iliendelea mpaka walipofika katika mtaa huo ambapo kwa maelekezo ya Dickson, gari likasimama nje ya nyumba moja ambapo nje kulikuwa na mafundi waliokuwa wakirekebisha baadhi ya vitu katika nyumba hiyo.

    Dickson akateremka na kuelekea ndani. Alipofika huko, akakaribishwa na kutulia kitini. Alijulikana hapo nyumbani hivyo haikuwa kazi kubwa kuambiwa kwamba mchumba wake, Luciana hakuwa nyumbani muda huo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Amekwenda wapi?”

    “Alihama.”

    “Alihama? Amehamia wapi?”

    “Kivikile…”

    “Ndiyo wapi?”

    “Si mbali kutoka hapa. Kwani hakukwambia?” aliuliza mama Luciana.

    “Hapana! Nilipoteza simu na namba yake sikuwa nimeikariri,” alidanganya.

    “Basi hapa alihama, amenunua nyumba huko Kivikile, subiri nimwambie mtu akupeleke,” alisema mama Luciana.

    Dickson hakutaka kubaki mahali hapo, alipoletewa kijana ambaye alitakiwa kumpeleka alipokuwa akiishi Luciana, wakatoka nje na kuanza kuelekea huko.

    Moyo wake ulikuwa na presha kubwa ya kutaka kumuona Luciana, alimkumbuka mno, alimpenda, mapenzi aliyokuwa nayo moyoni juu ya msichana huyo yalikuwa hayaelezeki hata mara moja, kama ni baharini, tayari yalikuwa maji ya shingo.

    “Hivi kuna kitu gani kinaendelea?” aliuliza Dickson.

    “Wapi?”

    “Kwa Luciana, yaani simuelewielewi.”

    “Hakuna kitu kinachoendelea.”

    “Buka! Mimi ni mwanaume mwenzako, inakuwaje unanificha bwana, au unaona raha kuona nikiumia hivi?” aliuliza Dickson.

    “Kweli hakuna kitu.”

    “Buka, macho yako tu yanaonyesha jinsi unavyonidanganya, hebu shika hii kwanza,” alisema Dickson, hapohapo akatoa fedha ya Rwanda, Franc elfu moja na kumpa Buka.

    Hicho kilikuwa ni kiasi kikubwa cha fedha, hapohapo Buka akakichukua na kujiweka sawa kitini, hakutaka kuficha siri, fedha ilimpagawisha, akaamua kutoa siri.

    “Luciana ana mwanaume mwingine,” alisema Buka.

    “Ana mwanaume mwingine?”

    “Ndiyo! Mwarabu fulani hivi, tena huku tunapokwenda unaweza kukutana naye,” alisema Buka.

    “Kweli?”

    “Kwa nini nikudanganye na wakati umenipa hela? Kweli tena,” alisema Buka.

    Dickson akashusha pumzi nzito, hakuamini kile alichokisikia kutoka kwa Buka, akahisi presha ikipanda na kushuka, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, hakuamini kile alichokisikia kwamba mpenzi wake alikuwa kwenye uhusiano na mwanaume mwingine.

    Wakati akiwa ameshikwa na hasira, wivu ukiwa umemkaba kooni, hapohapo wakafika katika jumba la kifahari ambalo aliambiwa kwamba msichana wake, Luciana alikuwa akiishi, dereva akasimamisha na wao kuteremka, wakaanza kupiga hatua kuelekea getini.

    “Karibuni,” aliwakaribisha mlinzi aliyeshika bunduki.

    “Asante. Dada yupo?”

    “Yupo ndani kapumzika na shemeji.”

    “Naomba tukamuone.”

    “Subiri kwanza Buka, huyu nani?”

    “Mshikaji wangu!”

    “Mgeni wa nani?”

    “Dada!”

    “Hapana! Hatakiwi kuingia!”

    “Kwa nini sasa?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mama alimpigia simu Luciana na kumwambia ulikuwa unakuja na mgeni, hivyo aliniambia nisiwaruhusu kuingia, kama kuingia, ingia peke yako, ila huyu abaki,” alisema mlinzi.

    “Unasemaje?”

    “Ndiyo hivyo kaka! Hautakiwi kuingia, kama vipi rudini mlipotoka,” alisema Buka maneno yaliyomfanya Dickson kuumia kupita kawaida. Akahisi miguu ikikosa nguvu na mwili kumtetemeka. Akajiona kama muda wowote ule angekufa.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog