IMEANDIKWA NA : NEA MAKALA
*********************************************************************************
Simulizi : Mvua Ya Huba
Sehemu Ya Kwanza (1)
Toka kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu Mungu aliona binadamu hapaswi kuishi peke yake, hivyo akamfanya mtu mke kutoka ubavu wa mtu mume. Na hiyo ikawa ndiyo ndoa ya kwanza iliyopewa maagizo ya kuujaza ulimwengu na kutawala kila kitu kilichomo. Ndoa inamaana Zaidi ya sherehe, ndoa huusisha nyoyo mbili zilizoridhiana si kwa pesa au uzuri bali ni ule upendo wandani ambao Mungu mwenyewe ndiye chimbuko.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni chereko na nderemo nyingi ndani ya kanisa kuu la Mt. Patrick, Mjini Morogoro. Watu walikuwa wengi wakishuhudia wawili wanaopendana wakifunga pingu za maisha.
"Lucas unampokea Lucy awe mke wako, tena waahidi kuwa mwaminifu kwake, katika taabu na raha, katika ugonjwa na afya, umpende na kumuheshimu siku zote za maisha yako?"
“Ndiyo nimekubali”
"Lucy unampokea Lucas awe mume wako, tena waahidi kuwa mwaminifu kwake, katika taabu na raha, katika ugonjwa na afya, umpende na kumuheshimu siku zote za maisha yako?"
“Ndiyo nimekubali”
“Ukubaliano wenu huo mliouonesha mbele ya kanisa, Bwana na authibitishe kwa wema wake, apende kuwazidishia wingi wa Baraka zake. Alivyounganisha mungu, mwanadamu asiyatenganishe”.
Padre akauthibitisha muungano ule kwa kuwafunga stola, kanisa zima liliyoyoma kwa makofi na vigerere. Wazazi wa pande zote mbili walionesha nyuso za tabasamu wakati wote, machozi ya furaha yalitiririka katika nyuso zao. Lucas ambaye ni Luteni kanali wa jeshi nchini alivalia suti yake ya kijeshi yenye rangi nyeupe na yenye mapambo ya rangi mbali mbali, Lucy yeye alivaa shera jeupe lililoburuzika mpaka chini na kufanya muonekano wa tausi.
Hakika wawili hawa wamechaguana, Lucas ni mvulana mtanashati sana, aliye na umakini mkubwa katika kila alichokifanya. Lucy yeye ni daktari bingwa wa upasuaji. Umakini katika kazi yake ukamfanya awe ni mwanamke aliyeokoa maisha ya watu wengi na mwenye mafanikio makubwa mno. Ndoa hii ilionekana kama Baraka kutoka kwa mwenyezi Mungu sababu wawili hao kwa kiasi kikubwa kazi zao zilihusu usalama wa Binadamu.
Mizinga ya kijeshi ilipigwa nje ya ukumbi, wanajeshi wote walisimama kutoa heshima kwa Lucas pamoja na mkewe, kisha shampeni zikafunguliwa na wakawamwagia maharusi. Hakika ilikuwa ni siku ya furaha sana ambayo si rahisi kufutika vichwani mwa kila mtu aliyehudhuria mahali hapo.
Sherehe ilimalizika majira ya 6:20 usiku, wawili hao wakaingia kwenye gari tayari kwa ajili ya kuelekea kwenye nyumba yao mpya iliyopo maeneo ya Bigwa, hawakuitaji dereva. Lucas aliamua kuendesha mwenyewe huku mke wake kipenzi akiwa pembeni yake. Walisindikizwa na nyimbo laini kutoka kwa Peabo Bryson akishirikiana vyema kabisa na Roberta Flack “Tonight I celebrate my love”
Tonight I celebrate my love for you
It seems the natural thing to do
Tonight no one's gonna find us
We'll leave the world behind us
When I make love to you
Tonight I celebrate my love for you
And hope that deep inside you'll feel it too
Tonight, our spirits will be climbing
To a sky filled up with diamonds
When I make love to you tonight
Tonight I celebrate my love for you
And that midnight sun is gonna come shining through
Tonight there'll be no distance between us
What I want most to do is to get close to you tonight
Tonight I celebrate my love for you
And soon this old world will seem brand new
Tonight we will both discover
How friends turn into lovers
When I make love to you
Tonight I celebrate my love for you
And the midnight sun is gonna come shining through
Tonight there'll be no distance between us
What I want most to do is to get close to you
Wakati nyimbo hiyo ikiendelea na wawili hao wakiifatisha kuimba kwa kupokezana, ghafla mbele yao kukatokea roli kubwa lililokuwa kwenye mwendo mkali sana, dereva wa roli aliwasha taa zote za mbele hivyo Lucas akashindwa kuona vizuri. Wazo la kufunga breki likamjia lakini kila alipojaribu breki zilikataa, kengele ya hatari ikagonga kichwani mwake akamtazama mkewe ambaye hakuwa anaelewa lolote linaloendelea.
“Lucy mke wangu,” Lucas aliita.
“Abeee! Mahabuba”
“Wewe ni mwanamke mzuri kuliko wote ambao macho yangu yamebahatika kuwaona, nakupenda sana,” alisema Lucas huku akishirikia usukani kwa mkono mmoja na kumshika lucy mkono ambao ulikuwa na pete ya ndoa.
“Nakupenda Zaidi mume wangu,” Lucy akajibu na kusogea alipo mumewe na kuanza kumbusu.
Lucas akamsisitiza mkewe afunge mkanda vizuri kisha akamtaka afumbe macho kwa haraka, Lucy hakuelewa kilichotokea baada ya hapo Zaidi ya kuhisi gari kuyumba mwisho kukawa kimya.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
BAADA YA WIKI 2
Lucy anafungua macho yake na kujikuta yupo katika mazingira hasiyo yaelewa, akajitazama vizuri akakuta amewekewa dripu ya maji, kichwa kikamuuma sana. Kwa mbali akamuona mama yake akiwa amekaa. Mama alipoona binti yake amerejewa na fahamu akafurahi mno, akasogea hadi alipolala bintiye,
“Pole mwanangu! Wajisikiaje sasa?”
“Aah! Najisikia vizuri tuu mama,” alijibu Lucy.
“Haya subiri basi nikamuite daktari aje kukuangalia”
Mama yake na Lucy akatoka na kwenda kumuita daktari ambaye dakika chache baadae akawa tayari ameshafika na kumfanyia vipimo Lucy.
“Kwa sasa anahitaji kupumzika, natumai baada ya wiki 2 atakuwa salama kabisa,” alisema daktari.
“Ah! Daktari wiki 2 nyingi mno, kesho kutwa natakiwa niende Cuba nikamalizie masomo yangu ya udaktari,” alisema Lucy.
Maneno hayo yalimshtua mama yake na hata daktari mwenyewe alishtuka, akahisi hali ya utofauti kidogo kwa Lucy.
Mama yake akamsogelea binti yake na kumtazama kwa makini Zaidi ,
“Mama unaniangalia nini, nashangaa likizo hii imekuwa fupi mno ila nitakupeza sana, mwambie daktari aniandikie dawa nitazimalizia nyumbani”.
Maskini Lucy ajali ilimsababisha akapoteza kumbukumbu za miaka 5, hakuweza kukumbuka kama alishaolewa hakukumbuka kitu chochote kuhusiana na maisha yake ya miaka 5. Daktari akamuita mama yake Lucy ofisini kwa maongezi Zaidi,
“Mwanao amejigonga sehemu ya nyuma ya ubongo wake, hii imepelekea yeye kupoteza kumbukumbu za kipindi Fulani cha maisha yake, angalizo ninalokupa usimlazimishe akakumbuka kilichotokea,” alisema daktari.
“Sawa nimekuelewa”
“Unaweza ukaenda nae nyumbani kwa sasa”
Mama aliwapigia simu nyumbani kuwajulisha kila kitu kilichojili, usafi mkubwa ukafanyika, wakaficha vitu vyote ambavyo kwa namna moja au nyingine vingeweza kusumbua akili ya Lucy. Lucy akafikia bafuni kisha baadae akaingia chumbani kwake kwa ajili ya kupumzika, akasogea kwenye dressing table yake akashangaa kuona mabadiriko kidogo,
“Mhmhmh! Mama hivi vitu vyote kaweka nani?” aliuliza Lucy kwa sauti.
“Aah! Dada yako huyo utamuweza alivinunua kipindi uko hospitali,” mama alijibu.
Lucy akapekua kwenye mkoba wake akakuta pete ya ndoa, alishangaa sana lakini akajikuta akiipenda pete ile na kuamua kuivaa bila kuuliza lolote. Mama yake alipoingia akashikwa na bumbuazi kuona bintiye amevaa pete ile,
“Wee Lucy nini hiko?” aliuliza mama.
“Aah! Nimekuta hii pete kwenye mkoba wangu alafu hata sijui ni ya nani ila nimejikuta nimeipenda tuu na kuamua kuivaa”
Mama akamtazama binti yake kwa huzuni sana, taratibu machozi yakamdondoka Lucy akashuhudia ilo na akainuka kumsogelea mama yake,
“Mama mbona walia! Unatatizo gani?”
“Nalia kwa furaha tuu kukuona mwanangu ukirejea katika hali ya kawaida,” alijibu mama.
“Hivi mama baba ameshanikatia tiketi kweli maana siku zimeisha,” aliuliza Lucy.
“Ndio mwanangu ameshakata”.
*******************************
Hali ya Lucas ilikuwa mbaya mno, hakuweza kurejewa na fahamu toka siku ambayo alipata ajali, wazazi wake wakawa karibu naye muda wote huku wakimuomba Mungu anyooshe mkono wa uponyaji kwa kijana wao. Wakati wazazi na ndugu wengine wa Lucas wakiwa wamekaa kwenye benchi lililopo karibu na chumba alicholazwa lucas wakamuona Lucy akiongozana na mama yake wakija eneo hilo. Bila kutarajia wote wakasimama huku nyuso zao zikaonesha tabasamu, hakika familia hiyo ilimpenda sana Lucy na walifurahi mno wawili wale kuoana. Wote waliosimama kumlaki Lucy walishangaa kuona Lucy akiwapita kama hawajui, alipofika katikati ya mlango alipolazwa Lucas ghafla akajikuta akisimama na machozi yakimtoka bila kuelewa nini hasa kilichokuwa kikimliza, akatazama kwenye mlango ule uliokuwa na kioo kilichoonesha kila kitu kilichomo ndani, akamuona Lucas akiwa amefungwa bandeji nyingi mno na akipumua kwa mashine. Akasogea hadi walipo wazazi na ndugu wa Lucas,
“Habari zenu!”
“Nzuri tuu!”
“Shikamooni”
“Marahaba! Mwanangu” aliitikia mama Lucas huku machozi yakimtiririka.
“Poleni sana kwa kuuguza, japo siwafahamu na simfahamu mgonjwa ila nimejikuta nikiguswa sana, hadi machozi kunitoka,” alisema Lucy.
Mama Lucy alipoona mwanae amesimama na kuongea na ile familia bila kujua kuwa wale ni wakwe zake, akatembea kwa haraka na kumshika mkono, kisha akawaomba radhi ile familia na kuingia na Lucy chumba cha daktari.
“Ahh! Mama si ungeacha niongee nao walau kidogo, alafu sijui kwa nini nahisi kama vile nawafahamu,” alisema Lucy.
“Mama tupishe kidogo nataka nimfanyie vipimo,” alisema daktari.
“Sawa dokta haina shida,” alisema mama Lucy na kutoka nje.
Alipofika nje akaenda ilipo familia ya kina Lucas, akajikuta Analia pia pindi macho yake yalipotua kwa mama Lucas,
“Lucy wangu hakumbuki chochote kile kilichotokea, daktari amesema alipata mshtuko kidogo uliyemuathiri mfumo wake wa ubongo. Naomba mvumilieni kidogo naamini ipo siku atarejesha kumbukumbu na kuja kuungana nanyi katika kumuuguza mume wake,” alisema mama Lucy.
Watu wote walimuhurumia sana, wakamfariji na kuahidi kushirikiana naye hadi pale kumbukumbu za binti yake zitakaporejea, pia wakaahidi kutokusema lolote lile kwa Lucy ambaye bado alikuwa kwenye msitu wa giza asielewe njia hipi ni sahihi.
Baada ya vipimo kukamilika Lucy akatoka na alipofika kwenye mlango ule ambapo ndani yake Lucas alilazwa akasimama tena, akasogea hadi kwenye kioo na kutazama ndani, machozi yakamtoka hadi mwenyewe akajishangaa kwanini Analia. Alipotazama kwenye benchi akamuona mama yake ikiwa anazungumza na mama yake Lucas akawasogelea na kukaka kisha akasema,
“Mama Kwani huyu mgonjwa ana uhusiano gani name, mbona kila ninapomtazama nahisi kuumia sana moyoni?”
“Mhmhmh! Mwanangu binadamu tumeumbiwa moyo wa kuwahurumia wenzetu, hiyo hali ni ya kawaida tuu mwanangu,” alijibu mama yake Lucas.
“Nahisi kama nina mtu wa muhimu sana katika maisha yangu ila mbona sikumbuki, mama hivi ni kweli nimepoteza kumbukumbu?” aliuliza Lucy.
“Ni kweli mwanangu huu ni mwaka 2017 na wewe kumbukumbu zako zimeishia mwaka 2012”
“Bila shaka kuna watu wengi tuu ambao siwakumbuki”
“Ndiyo mwanangu kikubwa fata ushauri wa daktari kumbukumbu zako zitarudi taratibu,” alisema mama yake Lucy.
“Naomba niingie ndani nikamuone mgonjwa huyu,” alisema Lucy.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mama Lucy na mama yake Lucas wakatazamana wasijue wamjibu nini, lakini kabla hawajasema lolote Lucy akawa tayari ameshaingia kwenye kile chumba na kumsogelea Lucas,
“Hey! Amka basi mbona watu wengi wanahuzunika kwa sababu yako, mama yako, baba yako, wadogo zako na ndugu zako, marafiki pia wote wanakuja kukutazama ila wewe umelala tuu ata kuamka hutaki. Wewe ni wathamani sana katika maisha yao usiwatende hivi,” alisema Lucy.
Wakati akiongea hayo mama yake pamoja na mama yake Lucas nao wakaingia na kumsikiliza, wote wakajikuta wakiangusha chozi, Lucy alipogeuza shingo akakuta mama Lucas Analia mno,
“Wewe sio mtu mzuri, unawezaje kumliza mama yako, embu amka basi mama yako afurahi kidogo,” aliendelea kuzungumza Lucy.
Lucas ni kama alikuwa akisikia kile alichoambiwa kwani aliweza kukunjua mkono wake na kumshika Lucy, tukio lile likawa la kushangaza mno. Lucy akafurahi mno,
“Ameamka! Oneni! amenishika mkono wangu!”
Kabla hajaongea Zaidi alishangazwa kuona Lucas akiwa na pete iliyofanana na ile aliyoivaa yeye, akazilinganisha na kuona kuwa zinafanana kwa kila kitu,
“Mbona ana pete kama hii niliyoivaa mimi?” aliuliza Lucy.
Mama yake ikabidi amshike mkono na kumtoa nje,
“Mwache mgonjwa apumzike na wewe pia unahitaji kupumzika hivyo twende nyumbani,” alisema mama Lucy.
“Lakini mama mbona hujanijibu swali langu! Kwanini nina pete inayofanana na aliyoivaa yule mkaka”
“Jamani Lucy wewe kuwa muelewa basi, pete zipo nyingi na inatokea watu wakavaa zinazofanana, kama ilivyo kwa nguo, viatu hata mikoba,” mama Lucy alijibu kwa ukari kidogo.
Walipofika nje kabisa ya hospitali hali ya hewa ikabadirika, wingu zito likatandana, upepo mkali ukavuma, wakatembea kwa haraka sehemu ambayo walipaki gari yao lakini kabla hawajaingia Lucy akasita akatazama barabarani na kushuhudia gari zikigongana uso kwa uso. Mwili ukahisi kupigwa na shoti kama ya umeme, akasimama huku akiduwaa, machozi yakamtiririka japo hayakuonekana kutokana na mvua iliyoanza kunyesha.
“Wee Lucy huoni mvua hiyo, embu ingia kwenye gari tuondoke,” alisema mama Lucy.
Lucy hakusikia lolote lile aliloambiwa na mama yake, kumbukumbu ya matukio ya nyuma ikaanza kutiririka kichwani mwake, akakumbuka jinsi alivyokutana na Lucas, walivyoanza mahusiano yao, walivyotambulishana kwa wazazi, alivyohitimu mafunzo yake ya udaktari na kuwa bingwa katika maswala ya upasuaji. Akaikumbuka pia ile siku walivyoweka kiapo kanisani, akakumbuka jinsi walivyokuwa wakiimba ile nyimbo ya “Tonight I celebrate my love” akakumbuka lile busu alilompa mume wake wakiwa kwenye gari, akaikumbuka ile kauli ya mumewe ya kumtaka afunge vizuri mkanda kisha afumbe macho, akakumbuka mtikisiko aliousikia.
Mama Lucy akashuka kwenye gari na kumsogelea mwanae akakuta ni mtu aliye kuwa mbali kimawazo, akatazama kule alipokuwa akitazama binti yake na kushuhudi ajali ile iliyotokea,
“Lucy mwanangu!”
“Mama mume wangu!”
Lucy alisema kauli hiyo huku akitimua mbiyo kurudi ndani ya hospitali, alikimbia mno huku akigongana na baadhi ya watu ambao wengi wakafikiri labda binti huyo amekumbwa na matatizo ya akili. Akafika katika chumba ambacho mumewe amelazwa akashangaa kumuona mama mkwe wake akilia na kugalagala chini. Akasogea na kupishana na wauguzi waliofunika mwili vizuri tayari kwa kwenda kuhifadhiwa kwenye chumba maalumu. Lucy akajikuta anaishiwa nguvu na kukaa chini. Alihisi maumivu makali ambayo kiukweli siwezi kuyaelezea ili ndugu msomaji uweze kuelewa, mama yake alipofika akashikwa na mshtuko kuona binti yake akiwa katika hali ile. Alipomtazama mama yake Lucas akapata picha ya kila kilichotokea, akasogea kwa haraka alipo mwanae,
“Mama mume wangu hayupo, sitomuona teena mimi,” alisema Lucy huku machozi yakimbubujika.
“Basi mwanangu usilie ni kazi ya Mungu,” mama akasema.
“Kazi ya Mungu ni kuonea watu kama sisi, mama hata ndoa yangu sijaifurahia amemchukua mume wangu, anichukue basi na mimi,” alizidi kulalama Lucy.
Taarifa ya msiba ikasambaa na ndugu walio karibu wakawahi hospitali, kuwachukua Lucy, mama yake pamoja na mama yake mkwe. Ndugu hawakuangaika kwenye taratibu za mazishi sababu Lucas alikuwa ni afisa wa jeshi hivyo yote yalikuwa chini ya jeshi.
***********************************
Miezi mitatu baadae Lucy akawa bado ni mtu wa kulia na kumlalamikia Mungu juu ya kifo cha mume wake, Lucy msichana aliyejaliwa umbo lenye kuvutia na rangi yenye kung’aa sana. Vyote hivyo vilipotea, Lucy alikonda mno na rangi yake ikafifia, hakuwa na muda wa kula mpaka alazimishwe, na hakuwa na muda wakutunza nywele zake kama ilivyokuwa kipindi cha awali.
“Lucy mwanangu wakati umefika sasa, mshukuru Mungu na ujaribu kusahau yaliyopita,” alisema mama yake Lucas.
“Hapana mama, siwezi kumsahau mume wangu, kuanzia leo sitokula chochote wala kunywa chochote hadi huyo Mungu aliyemchukua mume wangu anichukue na mimi,” alisema Lucy.
“Hapana mwanangu kusema hivyo ni sawa na kukufuru, Njia za Mungu si za binadamu na jua kila linalotokea Mungu anamakusudi nalo, hata mimi nimeumia sana kumpoteza mwanangu tena unajua kuwa yeye ni mtoto wangu wa pili lakini nimeshamuachia Mungu hivyo nawe jitahidi mwanangu,” alisema mama Lucas.
Lucy hakutaka kuelewa lolote aliloambiwa, aliendelea kumlaumu Mungu kwa maumivu ambayo anayapitia. Siku moja akaamua atoke na kwenda lilipo kaburi la mumewe, akapiga magoti pembeni na kuanza kuomba, Hakuwa na nguvu ya kupiga magoti kwa muda mrefu hivyo akajikuta akianguka pembeni ya kaburi la mumewe. Mvua ikaanza kunyesha na taratibu akahisi macho yanaishiwa nguvu mwishowe giza likatawala asiweze kuona wala kutambua lolote.
Tanganyika, mwaka 1917
Lucy akafumbua macho yake na kujikuta yupo katika dunia asiyoielewa, watu walionekana ni watofauti sana na wale aliowazoea kuwaona siku zote,
“Hatimaye Mwenda umeamka, jambo la heri hili,” alisema mama mmoja aliyevalia kibwewe cha ngozi na juu alifunika sehemu ya maziwa yake kwa kitambaa cheusi kilichochakaa mno.
“Mungu wangu! Nipo wapi tena au namimi ndio nimeshakufa, mbona sura hizi ni kama za watu wa zamani sana,” alijiuliza Lucy moyoni lakini asipate majibu ya maswali yake.
“Embu kunywa hii dawa itafanya mwili wako urejewe na nguvu kwa haraka,” alisema yule mama.
Lucy akapokea dawa ile iliyokuwa kwenye kibuyu na kuanza kuinywa ila hakuweza kumeza hata fundo moja akajikuta anaitema maana ilikuwa chungu mno, akashangaa mavazi aliyovaa. Akashangaa hata sehemu aliyolala, kumbukumbu yake ya mwisho ni alikuwa juu ya kaburi la mume wake.
“Huku ni wapi na wewe ni nani?” aliuliza Lucy.
“Jamani Mwenda, mimi mama yako mkubwa umenisahau inamaana?”.
Jibu hilo likamchanganya Zaidi Lucy ambaye alishangaa kwanza kuitwa Mwenda, pili alimshangaa yule mwanamke aliyedai kuwa ni mama yake mkubwa. Wakati akiendelea kuwaza hayo akasikia ngoma ikipigwa kwa nguvu, yule mwanamke aliyekuwa naye akatoka nje kwa kasi na Lucy naye akaamua kumfata, akasogea ulipo mkusanyiko wa watu na wote wakainama kutoa heshima kwa mtu ambaye kwa haraka Lucy aligundua kuwa mtu yule ni chifu.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndugu wananchi, wazungu wameendelea kututesa sana, sasa tunalazimika kulima mashamba yao pasipo kupewa ujira wowote, vijana wetu wakiume wameendelea kutekwa na kupelekwa utumwani, hatujui hali hii itaisha lini. Kitu ambacho nawasihi tuzidi kushirikiana na kila mmoja awe mlinzi wa mwenzie,” alisema Chifu.
Lucy akahisi kama vile yupo katika maigizo ya filamu ya kiasili, akatazama kila kona ili aone kama kuna kamera na waongozaji lakini hakuona kitu hicho. Nguvu zilimuisha akachanganyikiwa asijue atarudi vipi katika dunia aliyoizoea yeye.
“Samahani kaka, hivi hao wazungu wanaowanyanyasa wanatoka taifa gani,” aliuliza Lucy kwa mmoja wa wavulana waliosimama eneo hilo.
Swali la Lucy likazua mshangao kwa watu wote kwani katika zama hizo msichana aliyefikia umri wa kuolewa ilikuwa ni marufuku kumsemesha mwanaume asiye mume wake. Wazee wakahamaki kuona lile tukio,
“Mwenda nini unafanya? Umesahau kama wewe ni mchumba wa mtu kwa nini umsemeshe mwanaume mwingine?” aliongea mama mmoja ambaye Lucy hakuwa anamfahamu.
“Kwani ni dhambi kuuliza?”
Alijikuta akipokea kofi zito toka kwa mama yule, kisha mama huyo akapiga magoti na kuomba radhi kwa wazee wa sehemu ile,
“Nastahili mimi adhabu sikumfunza binti yangu vyema, tafadhari msiyaguse maisha yake,” alisema mwanamke yule.
Lucy akachanganyikiwa Zaidi alipogundua kuwa huyo ndiye mama yake, alihisi yupo ndotoni na kujipa moyo hayo yote yatapita pindi tu asubuhi itakavyofika.
“Hivi wee mwana unanitaka nini mimi, wajeremane watusumbue bado nawewe unataka usababishe matatizo mengine,” alifoka mama Mwenda au mama Lucy wa miaka hiyo.
Lucy akashangaa mno kusikia wajeremane, akavuta kumbukumbu na kujua kuwa mama yake alimaanisha wajerumani,
“Germany!?” Lucy aliongea kwa mshangao.
“Unaongea lugha gani wewe?”
Lucy akawa kama hakiamini kile ambacho akili yake inamwambia kila akipiga mahesabu ya utawala wa kijerumani aligundua kuwa ulikuwa kuanzia miaka ya 1880 hadi miaka ya karibu na katikati mwa 1900 kabla ya vita ya pili ya dunia dunia.
“Hao vijana wanaochukuliwa hapa wanapelekwa wapi?” akauliza Lucy.
“Tunasikia tuu wanasafirishwa na kupewa mafunzo ya kijeshi kisha wanaenda kupambana vita”
Lucy akakaa chini baada ya kugundua kuwa amerudishwa miaka 1000 nyuma na kipindi alichokuwepo kilikuwa kipindi cha vita ya kwanza ya dunia.
“Yamewezekanaje haya! Mimi kuwa kipindi hiki cha vita ya kwanza ya dunia, toka katika dunia ile ya kidigitali, hii itakuwa ndoto lazima, nikiamka kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Lucy.
Mama yake hakuelewa lolote lililosemwa na Mwenda, akafikiri labda mwanae anaweza akawa amechanganyikiwa kutokana na kuugua kwa muda mrefu.
“Mwanangu! mchumba wako Mogela, amekuletea zawadi nyingi kipindi ulichokuwa unaumwa, ila kwa bahati mbaya naye, amechukuliwa kwenda kupigana vita vya wajerumani, lakini atarudi hivyo lazima utunze ahadi yenu”.
Lucy akajikuta akicheka asijue ajibu nini, kila alipolisikia jina la Mogela ndivyo alivyojikuta akicheka Zaidi asiamini Kama anamchumba mwenye kuitwa jina la ajabu hivyo.
***************
Kilikuwa ni kipindi cha mwezi Juni, Mwezi ambao ulikuwa na baridi iliyoambatana na upepo mkali mno. Hali hiyo ilifanya mazao mengi kuharibika ukizingatia ulikuwa ni mwezi wa mavuno. Lucy ambaye ndiye mwenda hakuweza kulizoea baridi hilo akajikuta akishikwa na vichomi, kaya nyingi zikalalamika kwa uongozi wa juu kuhusiana na baridi ile ambayo iliwarahisishia wajerumani kuwakamata vijana wao kwa urahisi na kuwapeleka vitani.
Wazee wakila koo wakakaa na kuitisha kikao cha watu wote, kama ilivyokawaida tarumbeta iliyoambatana na ngoma ikapigwa na watu wakakusanyika.
“Ndugu wananchi baridi na upepo vimekuwa kero kubwa katika utendaji wetu wa shughuli mbalimbali, hivyo basi ni lazima tuiombe mizimu ituondolee hii adha,” alisema chifu.
Watu wakashangilia kwa makofi na vigelele, bila kupoteza muda akaandaliwa binti mmoja ambaye hakuwahi kumjua mwanaume na kijana mmoja wa kiume ambaye naye hakuwahi kumjua mwanamke. Mwanamke akakabidhiwa chungu kilichojaa maji na mwanaume akakabidhiwa jembe pamoja na gunia, Kisha wawili hao wakaanza safari ya kwenda katikati ya msitu mnene.
Wakatembea Zaidi ya saa tatu, hatimaye wakawasili sehemu waliyoikusudia, yule msichana akatua kile chungu na mvulana akaingia porini Zaidi kumsaka mnyama anayefahamika kwa jina la ndezi au digigi. Mvulana yule akafanikiwa kumkamata ndezi akamuweka kwenye gunia na kurudi alipo msichana. Kisha akachimba udongo na kuuanza kuuvuruga kwa kuchanganya na yale maji, papo hapo upepo mkali ukaanza kuvuma na kutikisa miti. Mvulana akamchukuwa ndezi akiwa ndani ya gunia na kumuingiza ndani ya kile chungu kilichosimamishwa vizuri.
Upepo uliendelea kuvuma kwa kasi mwishoe ukaanza kuingia ndani ya kile chungu na baada ya dakika 10 hali ikawa shwari. Mvulana yule akasiliba ule udogo kwenye mdomo wa chungu kile kuhakikisha ule upepo hautoki na hatimaye safari ya kurejea kijijini kwao ikaanza.
Wanakaya wote bado wakawa wamekusanyika kwa pamoja kuwasubiri mashujaa wao, ulikuwa ni usiku wa saa nne, siku hiyo mbalamwezi iling’aa na kufanya kila kitu kuonekana kwa uwazi. Kwa mbali mashujaa wawili wakaonekana wakiwa kwenye njia kuu ya kuingia kijijini kwao, tarumbeta ikapigwa na kufanya watu wote kuamka na kuanza kushangilia. Dakika chache baadae wakawa wamewasili na chifu akasimama na kuzungumza,
“Inaonekana bado mizimu ipo upande wetu, sasa tutaanza mafunzo rasmi ya kujilinda dhidi ya maadui zetu. Tuendelee kushika miiko yetu, ushirikiano na upendo uzidi kutawala miongoni mwetu”.
Hayo yote yalionekana Kama sinema kwenye fikra za Lucy, hakutaka kusadiki hata kidogo kuwa ndio uhalisia wa maisha aliyo nayo.
Dar es Salaam, Tanzania, 2017
Ni katika hospitali ya kijeshi Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam, Madaktari wanaangaika kuyanusuru maisha ya Lucy ambaye alionekana kuwa na hali mbaya Zaidi. Lucy hakuweza kurejewa na fahamu kwa takribani majuma matatu hali iliyozua hofu kubwa kwa ndugu zake wa karibu.
“Mwanao yupo katika hali ya koma na hii ni baada ya kupata mtikisiko kidogo kwenye ubongo wake wa nyuma, aah! siwezi kusema ni lini hasa atarejewa na fahamu,”
“Je inaweza ikatuchukua juma lingine au mwezi mwengine?”
“Mhmhm! Uponaji wa ubongo hufanyika taratibu mno, inaweza kutuchukua miezi na hata mwaka”
“Daktari naomba umsaidie binti yangu arejee katika hali ya kawaida”
“Tumeshafanya yote yaliyo ndani ya uwezo wetu ila usiache kumshirikisha Mungu wako, naamini atafanya njia” alisema daktari na kuondoka.
Baba yake Lucy akasogea hadi alipolala mwanaye akamtazama sana na chozi likamdondoka. Mzee yule aliumia sana kuona binti yake akiwa katika hali hiyo.
“Hivi kweli Lucy unataka kuniacha na kuungana na mumeo, nionee huruma baba yako, fumbua macho mwanangu, nini shida baba yako niko hapa,” alisema baba huyo huku akifuta machozi.
“Mume wangu! Yatosha sasa, Lucy wetu ataamka siku si nyingi, tuzidi kumuombea” alisema mama Lucy.
********************
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mkuu nimepokea taarifa ya upelelezi juu ya ajali ya Lucas na mkewe, ila inaonesha kuwa ajali ilipangwa”
“Nini?”
“Ndio hivyo mkuu ajali imepangwa na mmoja kati yetu maana breki za gari zilikatwa kabla ya sherehe kuisha,”
“Sasa ni nani huyo aliyesababisha kifo cha luteni wetu?” aliuliza mkuu wa kitengo cha jeshi la anga ambalo Lucas alikuwa akifanyia kazi.
“Hilo ndilo fumbo tunalopaswa kulitafutia majibu kwa sasa” alisema Chodo ambaye naye alikuwa mmoja wa wanajeshi waliyopewa kazi ya kufatilia kwa karibu Zaidi ajali ile, iliyogharimu maisha ya Luteni kanali.
“Fatilia hili swala kwa umakini mkubwa na usiri wa hali ya juu, mbali na sisi nani mwingine anayejua kuhusu hii ripoti?”
“Askari mmoja wa usalama wa barabarani,” alijibu Chodo.
“Sawa mjulishe kuwa kitengo chetu kitafatilia kwa undani Zaidi swala hili”
Ajali aliyoipata Lucas ilikuwa na siri nzito nyuma yake, hakuna aliyeweza kuelewa ni nani hasa muhusika wa tukio hilo maana wote walionekana wema.
Tanganyika, 1917
Ni alasiri moja tulivu iliyopambwa na mawingu mepesi, Mwenda ambaye ndiye Lucy aliambata na baadhi ya wasichana wa lika lake kuelekea msituni kwa lengo la kukata kuni. Wenzake walimuona kuwa wa tofauti sana, hawakumzoea vile, Mwenda aliyekuwa mpole na mkimya sasa amegeuka kuwa muongeaji na hasiye na hata lepe la uoga.
“Yaani mwenda toka uteleze na kuanguka mtoni, nahisi akili zako zimebadirika,” alisema Nyamtambo.
“Mhmh! Mimi lini nimeanguka mtoni?” aliuliza Mwenda.
“Duuh! Nyamtambo achana na hayo maswali tuliambiwa kuwa hakumbuki baadhi ya mambo toka ile siku aliyoteleza mtoni,” alidakia msichana mwingine.
Kauli ile ikamfanya Mwenda avute kumbukumbu hadi mwaka 2017, akaikumbuka ajali aliyoipata akiwa na mume wake. Akakumbuka kauli ya mama yake kuwa amepoteza kumbukumbu za takribani miaka mitano. Akahisi kuishiwa nguvu asijue aseme nini hili wale wenzie waweze kumuelewa, ukweli alikuwa mgeni kabisa katika dunia hiyo ambayo yeye alizoea kuisoma katika vitabu kipindi alipokuwa shuleni.
“Inamaana hadi huku nilipata ajali? Je wakati Napata ajali hiyo nilikuwa peke yangu au na mtu mwingine?” alijiuliza Lucy asipate jibu.
Akawatazama wale wasichana wenzake, kisha akapiga moyo konde na kuamua kuuliza,
“Jamani ni kweli sikumbuki chochote toka nilivyoteleza mtoni, je! mnaweza kuniambia siku hiyo nilikuwa na nani?”
Nyamtambo na wenzake wakatazamana kisha wakacheka kwa pamoja, wakamtazama Lucy wasijue la kumwambia.
“Mhmhm! Utajua kila lililotukia siku kumbukumbu zako zitakaporejea,” alisema Nyamtambo.
Zoezi la kukata kuni likaanza, kila mmoja akawa anahangaika kuhakikisha anafunga kuni za kutosha kwa kutumia walau siku tatu. Lucy alikuwa bado akitafakari maneno waliyosema wenzake, akawaza atawezaje kuishi kama Mwenda pasipo kujua huyo Mwenda alikuwa ni mtu wa aina gani.
Wakati akiendelea kutafakari hayo ghafla hali ya hewa ikabadirika, mawingu yakatanda na kufanya jua kufifia, Nyamtambo na wenzake wakamtazama Mwenda kwa hofu. Wakamkimbilia na kumvuta chini ya mti mmoja mkubwa.
“vipi mbona mmenileta hapa?”
“Mhmh! Inamaana kweli Mwenda umesahau hadi vitu unavyoviogopa,” aliuliza Nyamtambo.
“Una maana gani?”
“wewe haupatani na mvua hata kidogo”
“Mhmhm! You can’t be seriously…. Mimi niogope mvua?”
Wenzake walizidi kuduwazwa na maneno ya Mwenda maana walizoea kumuona mwenda akishikwa na homa hata kupoteza fahamu pindi mvua inyeshapo. Hayo yote yalikuwa mapya kwao,
“Itukuzwe Mizimu ya mababu zetu, Mwenda japo huna kumbukumbu ila napenda ulivyo sasa,” alisema Nzasa.
Mvua ikaanza kunyesha, Mwenda hakutaka kusubili ikatike akanyanyua kuni zake na kujitwika kichwani kisha akaanza safari ya kurudi nyumbani akifuatiwa na wenzake. Kabla hawajafika mbali sana wakasikia mtu akipiga ukunga na kuomba apishwe, wote wakasimama pembeni na kuacha njia katikati. Mwenda hakuwa amesikia hilo yule kijana aliyekuwa akikimbia kwa kasi bila kuangalia vizuri mbele akajikuta akimvaa mwenda na kula naye mweleka. Kijana huyo alikuwa mwepesi Zaidi kwani alimka na kuendelea na safari yake bila kutia neno, Mwenda alichukia mno akasimama na kupaza sauti,
“Hivi watu wa huku kwa nini umekosa ustaharabu? Unampalamia mtu hata kuomba radhi unashindwa!”
Kauli ile iliwafanya wenzake wazidi kumshangaa Mwenda, kwa mara nyingine tena akarudia kosa la kumsemesha mwanaume ambaye hajamuoa. Kijana yule akasimama na kugeuka kumtazama Mwenda. Mapigo ya moyo yaliongezeka ghafla pindi sura ya kijana yule ilipotua kwenye ubongo wa Mwenda, akajikuta akitimua mbio na kwenda kumkumbata yule kijana huku akilia kwa kwikwi.
“Lucas mume wangu! Kumbe upo huku, kwanini uliniacha wakati unajua kuwa nisingeweza kuishi bila ya wewe,” alisema Mwenda.
Kijana yule akamshangaa sana Mwenda, akajitoa mikononi mwake na kumsukuma pembeni,
“Hivi unakielewa unachokifanya wewe?” aliuliza kijana yule kwa ukali.
Nyamtambo na wenzake wakapiga magoti na kuomba radhi kwa niaba ya Mwenda.
“tunajua si sahihi kwa sisi kuzungumza nawe ila tafadhali usichukue hatua yeyote juu ya huyu mwenzetu, maana ana matatizo kidogo ya akili” alisema Nyamtambo.
“Jamani mimi nina akili zangu timamu, najua kupambanua baya na jema, wewe ni Lucas wangu nina uhakika. Kwanini unanikana, usinitende hivi”.
Ukweli kijana yule alishabihana na Lucas kwa kila kitu, kuanzia sauti, mwendo na muonekano swala ambalo lilimfanya Mwenda au Lucy aone kuwa amekutana na mumewe. Changamoto ni kwamba kijana yule hamtambui Mwenda na hakuwahi kumuona kabla hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza.
“sawa nimewaelewa kweli akili zake hazipo sawa, sitosema wala kufanya lolote juu yake endeleeni na safari yenu”
Nyamtambo na wenzie walimshukuru kijana yule ambaye hawakuweza kumuuliza hata jina lake, wakamuonya Mwenda na kumtaka aongeze umakini kwa kila jambo ambalo alikusudia kulifanya.
Njia nzima Mwenda hakuwa na raha, aliamini kwa asilimia zote kuwa Yule aliyemuona ndiye kipenzi cha moyo wake. Hali hiyo ikawalazimu wenzake wamsindikize hadi nyumbani kisha wakamuelezea mama yake Mwenda kila kilichotokea, mama alistaajabu sana, akashindwa kumuelewa mwanawe.
“Mwenda haya ninayo yasikia ni kweli?”
“Ndiyo mama nimemuona mume wangu kwa macho yangu!”
“Wewe mwana wewe! Mbona unanivuruga kiasi hiki? Mwanangu ujaolewa bado huyo mume unayemzungumzia ni yupi?”
Mwenda au Lucy akatafakari sana kauli ya mama yake, akaona ni kweli kuwa amesababisha mambo mengi ya hatari kwa maisha yake. Akamtazama mama huyo anayeongea kwa uchungu mno, kisha akaingia ndani akabadili nguo na kujilaza kwenye kitanda ambacho kilitengenezwa kwa kutumia miti na kamba.
“Huyu mwenda alikuwa ni mtu wa namna gani hasa! Kama mimi nimeshika nafasi yake huku yeye atakuwa wapi? Mhmhm! Hivi hii kweli ni ndoto? Mbona usiku umekuwa mrefu hivi?” alijiuliza Lucy asipate majibu.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kipindi cha mavuno kuisha kukaandaliwa sherehe ambayo iliwakutanisha watu wa kaya zote, sherehe hiyo ililenga katika kuishukuru mizimu iliyoweza kuwasaidia hadi kuwa na mavuno mengi ghalani. Pombe nyingi za kienyeji zikatengenezwa huku vijana wa kiume wakileta wanyama wa mwituni watakao tumika kama kitoweo. Sherehe ilianza kwa ibada maalumu na kutoa sadaka ya wanyama na nafaka katika jiwe moja kubwa lililotumika kwa ajili ya matambiko. Kisha ubani ukachomwa na wote wakainama kifudifudi na kusujudu.
Mambo hayo yalikuwa mapya kabisa kwa lucy ambaye alisikia tuu kuwa kuna matambiko ila hakuwai kuyashuhudia. Lucy aliyelelewa katika imani ya kikristo hakutaka kusadiki yale yaliyofanyika. Ibada ikamalizika watu wote wakarejea uwanjani , wote wakala na kunywa. Vikundi mbalimbali vya burudani vikatumbuiza kwa zamu. Wapo waliocheza ngoma, wapo waliopambana na wapo, walioshindana kukimbia. Katika hali isiyotarajiwa mmoja kati ya wakimbiaji akateleza na kuanguka, anguko lake lilikuwa baya mno, watu wote wakasimama na kutazama kama atawea kuinuka pale chini alipo. Kijana Yule hakuwa na nguvu ya kuinuka zaidi ya kupiga piga miguu kama mtu anayeugua kifafa, bila kutarajia Lucy au Mwenda akatoka mbio na kuingia katikati ya uwanja, akamsogelea huyo mkimbiza upepo na kukuta anatoa damu nyingi puani, alipomtazama vizuri akakuta ulimi umejikunja na kuzuia sehemu ya koo yaani ulikuwa kama unataka umezwe. Bila kupoteza muda akashika taya za Yule kijana na kuzitanua kidogo, kisha akatumia vidole vyake viwili kuutoa ule ulimi na kuuweka sawa. Watu wakamzunguka wasielewe nini anachokifanya,
“Yupo salama kwa sasa, ila anahitaji tiba zaidi tusaidiane kumpeleka hospitali,” alisema Lucy.
Neno hospitali lilikuwa jipya sana masikioni mwa wananchi wa Sanzani, hakuna aliyeelwa nini Lucy anamaanisha. Wazee wakaamuru kijana Yule abebwe na kupelekwa kwa tabibu wa kijiji, maneno yakazuka juu ya matukio anayoyafanya Mwenda. Amri ikatoka na mwenda akahitajika mbele ya baraza la wazee siku iliyofatia.
Mwenda hakuwa na hofu yeyote aliposimamishwa mbele ya wazee hao, alionekana mwenye kujiamini kupita maelezo. Kabla ya shtaka lake kusemwa akakuta kuna mzozo mwingine ukiendelea juu wa mwanaume mmoja aliyemlaumu mkewe kumzalia watoto wa kike tupu. Kesi ile ikamfanya Mwenda atabasamu tuu.
“Mimi siwezi kuendelea kuishi tena na huyu mwanamke! Haiwezekani huyu mtoto wa sita naye kazaliwa wa kike”
Kesi ilikuwa ngumu mbele ya wazee wale waliokuwa na upeo mfupi juu ya maswala ya biolojia wakajikuta wakifikia uamuzi wa kumtaka Yule mlalamikaji kuoa mke mwingine ambaye atakayempa hitaji la moyo wake. Mweda hakuona kama ile ni haki akasimama na kuomba ridhaa ya kuongea, wazee walizidi kumshangaa sana binti Yule mbali na kuwa na shtaka bado aliendelea kuvunja miiko. Mama yake alimzuia lakini Mwenda hakusikiaa akasimama na kupaza sauti,
“Maamuzi yenu yana uwalakini kidogo! Hamkutenda haki,” alisema Mwenda huku akisogea karibu kabisa na wazee wale.
Mama yake aliinamisha uso asione aibu ile binti yake anayoisababisha, hakuwa na ujasiri wa kuwatazama wazee wale.
“Wewe ni nani hasa unayekosoa maamuzi ya baraza?” alisema mzee mmoja kwa ukali.
“Askari mtoeni huyu hapa na hata shtaka lake hatutolisikiliza tutatoa adhabu moja kwa moja,” alisema mzee mwingine.
“Kuna tofauti gani kati yenu na wajerumani? Kama mnaweza kunikatili hivi mimi niliye na asili ya kwenu, je si zaidi kwa wajerumani? Dunia niliyotoka mimi ilikuwa na uhuru wa kuongea, kila mtu alipewa nafasi ya kutetea haki yake. Je ninyi hamtamani Sanzani yetu iwe kama dunia hiyo!” alisema Lucy.
Wazee wakavutika kumsikiliza binti Yule, askari wakaamuliwa kumuacha aongee kwanza ndipo wamchukue.
“Huyu mama hana kosa lolote kama ingekuwa kulaumiwa basi wewe baba ndiye ungestahili kushtakiwa kwa kushindwa kumfanya mkeo kupata watoto wakiume. Kwa asili mwanaume ana mbegu mbili ya kike na ya kiume wakati mwanamke akiwa na ya kike pekee, sasa kama mwanaume akitoa mbegu kabla ya yai kurushwa, mbegu za kiume hufa baada ya saa 24 yaani mapema zaidi ya zile za kike ambazo zenyewe hudumu kwa saa 72. Inavyoonesha wawili hao walikuwa wakikutana faragha saa kadhaa kabla ya yai kurushwa na hayo ndiyo matokeo,” alisema Mwenda.
Wazee wakamtazama binti Yule na kuona kuwa anakitu cha tofauti ambacho hawawezi kukipata kwa msichanaa mwingine yeyote hapo kijijini.
“Sisi hatuelewi iko unachokizungumza na wala hakipo katika kumbukumbu na miiko yetu, binti unawezaje kuzungumza mambo ya aibu mbele ya kadamnasi kubwa hii?”
“Hayo si mambo ya aibu ila ndiyo uhalisia wa mwili wa binadamu, suluhisho mimi nitawaelekeza baadhi ya mambo na naamini mtoto watakayempata atakuwa wa kiume, lakini swala la huyu kuoa tena si sawa maana tatizo linaweza kuwa vile vile,” alisema Mwenda.
Hali ya chifu ilizidi kuwa mbaya kiasi cha kumchanganya mke mkubwa wa chifu, kikao cha dharula kikaitishwa na wazee wote wakakusanyika. Mke wa chifu akaenda ukumbini huku akiwa mwenye majonzi tele. Wazee wakasimama kutoa heshima zao na wakakaa baada ya mke wa chifu.
“Ndugu zangu wa Sanzani! Hali ya chifu wetu siyo ya kuridhisha, tumejaribu kila njia lakini naona juhudi zangu zimefika ukingoni. Binafsi siwezi kukaa pasi na kufanya lolote katika kupunguza maumivu anayoyasikia” alisema Mke wa chifu.
Mzee mmoja mwenye umri kati ya miaka 70 na 80 akasimama na kuomba ridhaa ya kuzungumza jambo, mke wa chifu akamruhusu.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Uishi miaka mingi enh Malkia wetu! Katika Sanzani yetu tuna hazina ya kipekee ambayo kama tukiitumia vyema naamini mtukufu chifu wetu atarejea katika hali ya kawaida” alisema mzee huyo huku akimtazama malkia kwa umakini wa hali ya juu.
“Hazina hipi hiyo unayoizungumzia wewe?” aliuliza Malkia.
“Mwenda ndiye hazina ninayoizungumzia, binti huyu amejaaliwa kuwa na kipawa cha pekee hasa katika kutatua matatizo yahusuyo mwili wa binadamu, tumpe nafasi naamini atakuwa msaada mkubwa kwa chifu” alisema mzee huyo.
Jina la Mwenda likamchefua Zaidi malkia hakutaka kusikia lolote kuhusu msichana huyo aliyeitaji kuuona mwili wa mume wake kinyume na miiko waliyorithishwa. Malkia akatafakari kidogo kisha akafungua kinywa chake na kunena,
“Je ni halali kwa mwanamke kuona sehemu ya mwili wa mwanaume bila wawili hao kuwa na uhusiano wa ndoa takatifu?”
“Ni chukizo kubwa mbele yetu na hata kwa mizimu ya sanzani!” wote wakajibu kwa sauti moja.
“Huyo mwenda unayemzungumzia hapa anahitaji kuona sehemu ya mwili wa chifu ili amtibu je hilo linaruhusiwa?”
“Ni dhambi kubwa isiyosameheka…!” balaza la wazee likajibu tena kwa sauti moja.
“Ndio maana nikasema hapo awali kuwa jitihada zangu zimefikia ukingoni, siwezi kuruhusu huyo Mwenda atazame mwili wa mtukufu chifu Lukemo!” alisema malkia.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment