Simulizi : Ninge
Sehemu Ya Pili (2)
GARI ile ya polisi ilifika pale huku polisi wakiruka kutoka katika gari ile hata kabla haijasimama vizuri kisha wanne kati yao wakanivamia pale nilipokuwa na kuanza kunizongazonga, mimi sikuwa na la kujitetea zaidi ya kuendelea kuwa nimepiga magoti huku nikiwa nimenyoosha mikono yangu juu.
Walinichukua na kunifunga pingu mikono ile ambayo bado ilikuwa inayo maumivu ya kufungwa na zile kamba katika namna ya mateso makali.
Walinipakiza kwenye gari shuhuda mimi na wakata kuondoka ila nikaona niwasihi jambo moja ambalo nilijua kuwa kwa namna yoyote ile walikuwa hawajalifahamu bado.
‘’Afande.. afande naomba unisikilize afande’’ nilimsihi askari ambaye alionekana kuwa kiongozi wa ule msafara.
‘’unataka kusema nini wewe muuaji… unaua mama yako..’’ alinifokea.
‘’A fande, huko porini afande, afande huko porini kuna mtu ameuwawa, ni kiongozi, ni mtu maarufu fulani hivi nawasihi sana kabla hamjaondoka na mimi naomba mlitambue jambo hilo pia.. kuna watu wamefanya mauaji adfande sio mimi nina mashaka ni hao wamemuua mama yangu…’’ nilijielza upesiupesi yote niliyohisi nafaa kujielza ili kujitoa katika kitanzi kile kilichokuwa mbele yangu.
‘’Watu gani, wenzako wamekukimbia tayari.. wamekukimbia na utahukumiwa ukiwa peke yako.’’ Alinijibu huku akitaka kuondoka zake, CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
‘’Hapana afande nawaomba sana twende huko porini..’’
Kwa kawaida huwa sio jambo la kawaida kabisa kwa askari kumsikiliza mtuhumiwa na kufuata anayowashauri, ilikuwa hivi pia kwangu. Hawakunielewa hata kidogo badala yake askari mmoja alijaribisha kirungu chake katika mwili wangu na kunitia maumivu makali na gari likaondoka.
Gari liliondoka kwa mwendo wa kasi lakini baadaye mwendo ulipungua kutokana na ubovu wa barabara uliokikabili kijiji chetu. Nilikuwa katika majonzi, kwa mara ya kwanza kabisa katika maisha yangu nilikuwa nimevikwa pingu na mbaya zaidi ilikuwa ni kwa kosa la mauaji.
Safari ile ilikuwa mbaya kupita zote tangu nilipoanza kusafiri na nilikuwa nikiona kama ni safari ya kuelekea katika moto wa milele.
Nilijaribu kuwatazama wale askari kwa jicho la huruma lakini hii haikusaidia kitu.
Baadaye mbele gari likasimama, hapa nikaona maaskari wawili wanashuka akabaki mmoja tu pale katika ile karandika, ni hapo nilipoipenyeza shingo yangu katika bomba na kuweza kuona nje, jicho langu lilikutana na mojawapo ya sura ambazo niliziona usiku uliopita zikihusika katika kutoa uhai wa yule bwana aliyewaelezea ni wapi kipo walichokuwa wakikitafuta.
‘’Afande.. afande..’’ nilimuita huku nikiogopa sana.
‘’Afande tafadhali nisikilize afande..’’ niliendelea kumsihi askari aliyekuwa amebaki ambaye baadaye nilikuja kumtambua kwa jina la saimoni.
‘’Unasemaje wewe dogo, hapa mndo umefika dogo mengineyo utajibu mahakamani..’’ alinijibu.
‘’Afandee…’’ sasa nilimuita kwa ukali hadi kastaajabu.
‘akanitazama kwa jicho la kisharishari, akatazama huku na kule bila shaka alihitaji kuchukua kirungu chake……
‘’Afande sio muda wa kutumia silaha nisikilize afande nakuomba..’’ nilimweleza.
‘’Haya sema…’’ alinijibu huku akijiweka sawa.
‘’afande hao watu mbele yetu, jana usiku wamemuua…. Yes nimemkumbuka jina wamemuua Gadna Mselemu…. Wamemuua na nilishuhudia kwa macho yangu, afande nakusihi kama mdogo wako nifiche wasinione wananisaka waniue maana nilishuhudia kila walichokifanya kwa Gadna…..’’ nilimweleza kwa sauti ya kusihi.
Afande saimoni akatabasamu kidogo, kisha akacheka kwa dharau.
‘’ngoja niwaite wakuone kabisa…..’’ alisema huku akipanda katika bomba ili aweze kufanya alichokusudia.
‘’nikiwa na pingu yangu mikononi nilimshika mguu wake na kumsihi sana asifanye vile.
‘’afande naongea nikiwa na akili zangu timamu, afande wakiniona wataniua na mtaukosa ushahidi, afande wanaihujumu nchi hao… kama hauniami piga simu ya gadna uzungumze naye…. Afande gadna ameuwawa’’ nilimsihi zaidi.
Kusihi kwangu katika namna moja ama nyingine kulimfanya yule afande atulie kidogo, kisha akavua koti lake akanipa nijifunike.
Nilijifunika na hapo nikamsikia akimuita afande mwingine aitwaye afande wanchera, alipoitika nikaitambua kuwa ni ile sauti ya mkuu wa ule msafara.
Nikiwa katika kona moja nimetulia nikiuficha uso wangu niliwasikia wakizungumza na nikasikia yule afande wanchera akisema kuwa watu wale ni wapelelezi wapo katika kijiji hicho kwa ajili ya kumtafuta mtuhumiwa wa mauaji aliyetoroka kutoka nchi jirani ya Kenya.
Niliomba sana afande saimoni aweze kumuelezea juu ya nilichomweleza, hata kabla sijamaliza kuwaza hivyo nikamsikia akimgusia juu ya nilichomweleza.
‘wakati wanazungumza nikaisikia sauti kwa mbali.
‘’waheshimiwa tunaomba tuikaguea gari yenu kwa ajili ya kujiridhisha tu maana kila gari tunalikagua kwa idhini tuliyopewa na serikali…’’ sauti ile niliisikia usiku uliopita.
Sasa dua ikawa ni kwamba wasiruhusiwe kutukagua maana kuniona kwao tu kungebadili kila kitu pale tulipokuwa.
Sikuwa nikijua sheria zozote zile ikiwa askari nao wanaweza kukaguliwa gari lao ikiwa ruhusa imetoka ngazi za juu kabisa.
‘’wale watu ni akina nani hasa jamani eeh..’’ nilijiuliza sana huku nikiombea nisijekuwa na mwisho mbaya kabisa kuishia katika mikono yao.
‘’mna mashaka na sisi kuwa tumemuhifadhi mtu huyo ama…’’ sauti ya afande wanchera kiongozi wa msafara ule ilihoji.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
‘’hapana afande tunahitaji kujiridhisha….’’
Nikaona hii hali inaweza kuwa mbaya kisha nikajikuta nasema NINGE… ili nisiseme ninge nikaamua kuzungumza.
‘’afande saimoni waombe muongee na aliyewaagiza, waongo hao.. ni waongo afande…’’ nilizungumza.
‘’kaa kimya kimburu wewe…..’’ alifoka afande wanchera lakini licha ya kufoka alisema kile nilichomuomba.
‘’maafisa tunaomba mtupatie mkuu wenu tuzungumze naye kama hamtajali…’’ wanchera aliwaomba.
‘’ina maana hamuamini kama tupo katika kazi ama..’’ alijibu.
‘’kama nyie hamuamini kama sisi hatuwezi kutunza muhalifu wenu kwanini basi mnataka sisi tuwaamini tu kuwa mmeagizwa kufanya kazi huku… vitambulisho pekee havitoshi…’’ alijibu kwa jeuri afande wanchera.
Kimya kikatanda, bila shaka kama ni moshi sasa ulikuwa umeanza kufuka na kilichokuwa kinaenda kufuata ni moto.
Mbaya zaidi moto huu ulikuwa unakuja kuwaka mimi nikiwa na pingu mikononi, ningejiokoa kessy mimi.
Baada ya kimya cha kama dakika moja hivi yule bwana akajibu kuwa simu ipo katika gari lao na anaenda kuifuata. Nikazisikia hatua akiondoka.
Nikajitutumua tena nikazungumza.
‘’maafande wanazo silaha si watu wazuri wamemuua gadna wanataka kupoteza ushahidi wawekeni chini ya ulinzi.. nawasihi.’’ Nilizungumza huku natetemeka
‘’acha kutufundisha kazi pumbavu wewe…’’ alijibu kwa ukali wanchera lakini baada ya kujibu nikamsikia akimwambia afande saimoni aingie garini na kuchukua silaha.
Nilijikuta Napata nafasi ya kutabasamu, yaani kushauriwa hataki lakini ushauri anauchukua.
Nikajikuta natamani kuwa askari, nikaapa kuwa kama nikitoka salama nitafanya kila niwezalo niwe askari.
Nikausikia mlango ukifunguliwa na kisha kufungwa. Bila shaka silaha zilikuwa tayari.
‘’Hatutapiga simu, na tutakagua gari lenu..’’ ilisikika sauti mpya, sauti ambayo hata usiku ule niliiskia.
Aliyoyaongea yalimaanisha kuwa liwalo sasa na liwe……
Nilitetemeka sana…..
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
JIFUNZE.
HAKI ni neno moja jepesi sana kutamka lakini kiundani ni neno kubwa sana, HAKI yako mwenyewe inaweza kupindishwa na kuitwa kosa. Halafu kosa likanyooshwa na kuitwa HAKI.
Askari wetu wanatokwa jasho kutupigania tuzipate haki zetu, lakini wapo maaskari wachache kati ya hao wengi wanazipindisha haki zetu kwa maksudi kabisa. Kisa kikuu kikiwa ni RUSHWA….
EPUKA RUSHWA SASA NI ADUI WA HAKI…
Nilikuwa nasimuliwa tu hapo zamani kuwa risasi nikipigwa hewani ama hata kuelekea upande ambao haupo wewe muhusika wa kuusikia mlio ule basi utaisikia kana kwamba imepigwa katika sikio lako, na hiki ndicho kilichonitokea mimi.
Ulisikika mlio mkali wa risasi, nikahisi ile risasi imepigwa kuja nilipokuwa nimeketi kwa kujificha nyuma ya lile gari.
Hata sikumbuki ni wakati gani ambao nilivua lile koti la afande saimoni na kulitupa mbali, huku nikitokwa na mayowe ya hofu nikajirusha hovyo katika lile gari na kujikuta nikijibamiza vibaya katika bomba ngumu za vyuma zilizokuwa zimeizunguka gari ile.
Kilichonifanya nikose stamina zaidi na kuumia vibaya zilikuwa ni zile chuma zapingu katika mikono yangu.
Hapo ndipo nikakiri kuwa hakuna kitu kizuri na cha bure kabisa duniani kama uhuru na amani.
Laiti ningejua kuwa haya yote yatakuja kutokea basi kamwe nisingekubali jua la utosi liwake kabla sijaifikisha taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa.
Lakini nilikuwa nimechelewa tayari.
Nilipasuka katika sehemu ya mbele ya kichwa changu, damu ikawa inanivuja, na hapo nikasikia onyo kutoka nje.
‘’Mkileta jeuri tena tunafyatua hiyo miguu yenu…’’ ilifoka sauti ya wale maadui, sasa bila shaka wale maaskari walikuwa wamekubaliana na maneno yangu kuwa wale waliotusimamisha hawakuwa watu wema hata kidogo bali wanyama kabisa.
Acha nilisifie jeshi letu la polisi kwa hili, simaanishi wamekamilika la, wana mapungufu yao mengi tu lakini nitaanzaje kuzungumzia mapungufu tu wakati nilipata kushuhudia na ukakamavu wao.
Hawakuwa legelege nilimsikia afande wanchera akinong’ona amri kadhaa hivi halafu kwa pamoja wakahesabu moja hadi kufikia tano na hapo mapambano yakaanza ya kutupiana risasi.
Zilisikika kelele za vilio na miguno ya maumivu, lakini milio ya risasi ikitawala zaidi.
Na ghafla gari likaondolewa kwa kasi sana, nikiwa bado nimepigwa butwaa mara mle ndanbi akajirusha na kuingia ndani afande wanchera kisha saimon akafuata, wote wakiwa makini kabisa na silaha zao.
Milio iliendelea kusikika huku ikisindikizwa na matusi makali, nilikuwa natetemeka sana kwa sababu mambo kama hayo nilizoea kuyaona kwenye filamu za mapigano tu.
Gari ilienda kwa kasi sana huku ikiruka huku na kule, kwa sababu mimi nilikuwa ninazo pingu mkononi hata sikuweza kujishikiza vizuri, nilibamizwa huku na kule huku nikishindwa kuidhibiti ile damu iliyokuwa inavuja.
‘’Wanaharamu wakubwa hawa… wameua kijana wetu mmoja…’’ afande Wanchera alizungumza huku macho yake yakiwa makini sana kutazama kila kona.
Wakati bado hali haijawa tulivu mara ulisikika mlio mkali sana, kilikuwa ni kishindo kikubwa kuja katika gari yetu. Nikayumbishwa na kujibamiza katika kuta za ile gari ambazo zilikuwa vyuma tupu.
Nikapatwa na kizunguzungu halafu nikaona giza likijongea huku kizunguzungu kikiongezeka kwa kasi na kunifanya niione gari kama inazunguka.
Na mara ukasikika mlio mwingine mkubwa tena na hapo sikutambua ni kitu gani tena kilikuwa kinaendelea.
******
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa kama ndoto vile ambayo ikageuka kuwa katika uhalisia, nilihisi baridi kali katika mwili wangu, nilijiona nipo katika kitanda lakini sikuwa naliona shuka kwa sababu nilikuwa nimeyafumba macho na sikutaka kuyafumbua, nilijaribu kupapasa huku na kule ili niweze kulipata shuka na kujifunika, nilipapasa lakini kila nilipojaribu kuupeleka mkono mmoja nilishangaa na mkono wa pili ukilazimisha kwenda pamoja na mkono wa kwanza.
Nikapapasa lakini bado sikuweza kulipata shuka.
Ule uzembe wa kugoma kufumbua macho kwa sababu usingizi utakata niliupuuza na kuamua kufumbua macho.
Nikafumbua macho na kuangaza.
Lahaula, sikuwa sikuwa kitandani nilikuwa nipo katika majani tena machafu na lilikuwa giza ambalo lilipunguzwa maka,li na mwezi uliokuwa umeng’ara vyema.
Nilipojitazama mkononi nilikuwa ninazo pingu.
Nilikurupuka kutoka pale huku nikipiga makelele ya uoga.
Sikujua eneo ambalo nilikuwepo.
Ile napiga kelele na kuanza kukimbia nikasikia nikipewa onyo kuwa nisijaribu kukimbia.
Mungu wangu…… onyo lilelile kama nililopewa na wale watu wabaya kabisa ambao niliwashuhudia wakimuua Gadna kwa mateso makali.
Sikutaka kusimama, na hilo likawa kosa langu. Ile naendelea kupiga hatua mara nikahisi kitu kizito sana kikiuponda mguu wangu wa kulia, nikarusha na kutua mbali kama mzigo.
Nilijaribu kusimama tena lakini sikuweza hata kuutikisa ule mguu wa kulia.
Nikawa nalia kama mtoto mdogo wakati wanafika pale waliokuwa wamenipa onyo lile na kuanza kunimulika na tochi zao.
Nilikuwa sina la kusema zaidi ya kuhema juu juu huku nikitokwa na kilio cha uchungu.
‘’Wewe ni nani…’’ waliniuliza wawili kwa pamoja.
‘’Nisameheni jamani…. Mimi si mtu mbaya…’’ nilijitetea.
‘’Hizo pingu kakuvesha nani…’’
‘’Nimevishwa na maaskari ila sina kosa jamani,… wamekosea tu…. Nisameheni..’’ niliwasihi. Wakati huo tochi zao zikiyamulika macho yangu na kunifanya nisione vyema mbele.
Kimya kikatanda wakanong’onezana kitu na baadaye mmoja akanibeba begani kama mzigo wakaondoka na mimi nisijue hata ni wapi walipokuwa wananipeleka.
Nilitambua sasa kuwa sikuwa na namna nyingine tena ya kujiokoa wala kuwashawishi lolote.
Na vile nilikuwa nayapitia maumivu makali haswa nilitamani hata kufa dakika hizohizo ili nisiendelee kuumia.
Walinifikisha hadi katika gari dogo aina ya NADIA, wakaniingiza huko na hapo nikakutana na mtu aliyekuwa na vifaa kadhaa kama daktari, akaanza kutibu jeraha langu la mguuni.
Hapo ndipo nilipotambua kuwa kumbe nilipigwa risasi wakati ule nilipokuwa najaribu kukimbia.
Wakati naendelea kutibiwa waliendelea kuniuliza maswali kadha wa kadha juu ya kisa cha kufikia pale nilipokuwa, niliogopa sana kuwaeleza kuwa nilishuhudiia kifo cha Gadna na wauaji kadhaa nawatambua, niliogopa sana kwa sababu tu sikuwa na imani na watu hawa pia.
‘’Chagua moja bwana mdogo, tukuache hapa na pingu zako askari wafike na kukuchukua ukafie jela ama tuondoke na wewe tukafanye kazi, maana bado una nguvu za kufanya kazi.’’ Aliniuliza bwana mmoja kwa utulivu huku akipuliza hewani moshi wa sigara yake.
Sikujifikiria sana katika kujibu, maana kiasi cha kuachwa pale katika giza lile nene ilimaanisha kuwa lolote laweza kutokea, aidha kushambuliwa na wanyama wakali ama hata kukutwa na watu wengi9ne wabaya.
Nikajikuta nakubali kuondoka nao, wakati huo hata sijui wanajihusisha na nini.
Sikujua kuwa ninaondoka nao kwenda mbali kabisa.
Na hiyo kazi waliyokuwa wameniahidi ilikuwa kazi ambayo sikuwahi kutegemea kuifanya maishani mwangu lakini tayari nilikuwa nimefanya makosa nililazimika kukubalianana kila kitu.
Baada ya kufungwa lile jeraha wakanidunga sindano ambayo sikujua ni ya nini, nikaanza kushambuliwa na jinamizi la usingizi hadi niliposinzia……
Sijui yalipita masaa mangapi lakini nilikuja kurejewa na fahamu nikiwa peke yangu katika nyumba kubwa nisiyoifahamu….CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa kimya sana nyumba ile, nilitazama huku na huku na kujihakikishia kuwa nilikuwa peke yangu eneo lile.
Hawa ni akina nani…. Nilijiuliza, lakini wa kunijibu hakuwepo.
Nikayatazama maisha yangu ndani ya siku chache hizi yalivyoingia katika historia ya ajabu kiasi kile…..
Nilitikisa kichwa na kisha nikazungumza kwa sauti ya chini.
Ama kwa hakika hakuna aijuaye kesho hata yule mtunzi wa kalenda…..
Hata mimi sikuwa nimefahamu kuwa kesho yangu itakuwa ya aina ile.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment