Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

A LIVING DREAM ( NDOTO INAYOISHI ) - 4

 







    Simulizi : A Living Dream ( Ndoto Inayoishi )

    Sehemu Ya Nne (4)



    Uchawi ulichukua nafasi yake, kila kitu kilichokuwa kikitokea, yule jini aliyekuwa akiishi katika mbuyu kule Baamoyo alikuwa akishuhudi kila kitu. Alichukizwa na hali iliyokuwa ikiendelea, alikumbuka kwamba Patrick na Luciana waliahidiana mengi chini ya mbuyu miaka kadhaa iliyopita hivyo hakutaka kuona hali yoyote ya usaliti ikitokea, na kama ingetokea basi angetoa adhabu, ndivyo ilivyokuwa kwa Luciana.

    Alichukizwa na kitendo kile na hivyo asingeweza kumsamehe msichana huyo. Mbali na kumpa ukichaa lakini bado hakuonekana kuridhika. Kitendo kilichotokea kanisani kwamba msichana huyo alikuwa akiolewa na Emmanuel kilimkasirisha mno, hivyo akataka kummaliza kabisa.

    Patrick alivyokuwa akitoka nje huku akionekana kuwa na maumivu mno ndicho kipindi ambacho jini huyo akaamua kubadilisha kila kitu kanisani humo. Hasira zake zikawaka na hivyo akataka kumuua Luciana ili kama kukosa basi wakose wote.

    Kitendo chake cha kusimama mlangoni na kisha kumnyooshea kidole Luciana, hapohapo msichana huyo akaanguka chini, mapigo yake ya moyo yakashuka kwa kiasi kikubwa hali iliyomfanya kila mtu mahali hapo kuingiwa na hofu.

    “Vipi?” aliuliza Emmanuel huku akionekana kuchanganyikiwa.

    “Tumpelekeni hospitali.”

    “Lakini moyo vipi?”

    “Mapigo yanaendelea kushuka tu. Jamani, huyu mtu anaweza kufa....tumkimbizeni hospitalini kwani hata mwili wake umekwishaanza kuwa wa baridi” alisema baba Luciana.

    Tayari hali iya hewa ikachafuka kanisani, watu wote wakapigwa na butwaa, hawakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea kanisani hapo, kitendo cha Luciana kudondoka kilimpa hofu kila mmoja.

    Walipompakiza ndani ya gari tu, safari ya kuelekea hospitalini ikaanza. Kila mmoja akawa na presha, muda wote ndani ya gari hilo, Emmanuel alikuwa amekiegemeza kichwa cha Luciana mapajani mwake.

    Machozi yalikuwa yakimbubujika tu, kila wakati alikuwa akigusa mapigo yake ya moyo kuona kama alikuwa mzima au la. Bado mapigo ya moyo yaliendelea kudunda kwa taratibu, tena kwa mbali mno kuonyesha kwamba muda wowote ule yangeweza kusimama na Luciana kufariki dunia.

    “Dereva, ongeza kasi, tunakwenda hospitalini na si harusini,” alisema Emmanuel huku akionekana kuchukizwa na kasi ya dereva yule.

    “Foleni mkuu.”

    “Vunja sheria, kama kutatokea tatizo, nitazungumza nao.”

    “Kwa hiyo nipite njia ya watembea kwa miguu?”

    “Ndiyo! Pita hukohuko.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Dereva hakutaka kuhofia tena, kwa sababu alikwishaambiwa avunje sheria wala halikuwa tatizo kwake, alichokifanya ni kuingia katika njia hiyo tena huku akiwa katika mwendo wa kasi.

    Japokuwa watu walilalamika na wengine kutukana lakini dereva hakuonekana kujali, alichokifanya ni kupiga gia, kukanyaga mafuta huku akishikilia vema usukani wa gari lile.

    Ndani ya dakika kadhaa, wakafika katika Hospitali ya St. Monica iliyokuwa Upanga ambapo wakamteremsha na kumuingiza ndani ya hospitali hiyo. Manesi waliokuwa mahali hapo wakaonekana kumshangaa Luciana, bado alikuwa na shela lake huku mume wake mtarajiwa akiwa pembeni yake.

    Akapakizwa juu ya machela na kuanza kusukumwa kuelekea ndani. Emmanuel hakutaka kukaa mbali na Luciana, alikuwa pembeni yake huku akili yake yote ikiwa juu ya mapigo ya moyo wa Luciana tu.

    “Naomba mumsaidie, naomba mumsaidie mke wangu,” alisema Emmanuel.

    “Sawa. Usijali, atapona tu. Subiri hapa,” alisema nesi mmoja wakati machela ile wakiingiza ndani ya chumba kimoja kilichokuwa na maneno yaliyosomeka ICU mlangoni.

    “Nesi! Usifunge mlango, subiri kwanza,” alisema Emmanuel.

    “Kuna nini?”

    “Naomba niingie ndani.”

    “Haiwezekani, subiri hapahapa nje.”

    “Nataka kufuatilia kila hatua, hata akifa, afe mbele ya macho yangu.”

    “Nani kakwambia atakufa? Usijali, hatokufa.”

    “Una uhakika?”

    “Ndiyo! Subiri hapahapa.”

    “Daah! Sawa!”

    Wote wakabaki nje ya chumba hicho, Emmanuel hakutaka kuzungumza kitu chochote, kichwa chake kilikuwa kimechanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilikuwa kimeendelea.

    Hasira zake zote zikahamia kwa Patrick, alijua kwamba mwanaume yule ndiye aliyesababisha kila kitu kilichotokea, kwani pasipo yeye, aliamini kwamba mpenzi wake, Luciana asingeweza kuanguka pasipo sababu yoyote ile.

    Walichukua kama dakika mbili, daktari mmoja mwenye koti kubwa jeupe na mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo ikiwa shingoni mwake, akaingia ndani ya chumba hicho pasipo kuzungumza na mtu yeyote yule.

    Waliendelea kuwa nje ya chumba kile kwa zaidi ya masaa mawili, mara mlango ukafunguliwa na daktari yule kutoka nje. Kila mmoja akasimama na kuanza kumwangalia, uso wake ulionekana kuwa tofauti na ulivyokuwa kabla.

    Alivyoingia, kwa mbali alionekana kuwa kawaida lakini kipindi hiki alipokuwa ametoka ndani ya chumba kile, alionekana kunyong’onyea mno.

    “Kuna nini?” hilo lilikuwa swali la kwanza alilouliza Emmanuel huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa.

    “Mbona mmemchelewesha hivyo?” aliuliza daktari yule.

    “Imekuwaje? Mmeyaokoa maisha yake?” aliuliza Emmanuel, mahali hapo alionekana kuwa mzungumzaji mkuu.

    “Mmmh! Hali ni mbaya sana.”

    “Imekuwaje?”

    Ooppss!” dokta yule alijikuta akishusha pumzi ndefu na nzito, kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

    ****

    Muonekano wa daktari yule uliwapa mashaka, sura yake ilionyesha kuwa na majonzi mengi na walikuwa na uhakika kwamba kulikuwa na jambo baya lililotokea ndani ya chumba kile, hasa Luciana kufariki dunia.

    Walibaki wakimwangalia daktari yule, kwa muonekano alionekana kuwa na jambo kubwa alilotaka kuwaambia lakini hakujua ni kwa namna gani angeweza kufikisha ujumbe ule uliokuwa ukimkera moyoni mwake.

    “Vipi dokta, tuambie tu uk....” alisema Emmanuel lakini hata hajamalizia sentensi yake, akajikuta akianza kulia.

    Alimpenda Luciana na hakutaka kusikia kitu chochote kibaya kutoka kwake, alimthamini kwa kuwa alijua ndiye alikuwa msichana pekee aliyeufanya moyo wake kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa asilimia mia moja.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Hakutaka Luciana apatwe na tatizo lolote lile, alimuomba Mungu aendelee kuwa mzima na kama kufa, afe lakini akiwa tayari amekwishamuoa na si katika kipindi kama hicho, hata kama alikuwa kichaa, hilo wala hakuonekana kulijali.

    “Njooni ofisini,” alisema daktari na hapohapo pasipo kupoteza muda wakaanza kumfuata.

    Walipofika, akawakaribisha vitini na kuanza kuwatazama nyusoni mwao. Ni kweli daktari alionekana kuwa na donge kubwa lililomshika kooni hivyo alitaka kuzungumza nao angalau ajisikie amani.

    “Mgonjwa wenu hana tatizo lolote lile,” alisema daktari huku akiwaangalia.

    “Unasemaje?”

    “Mgonjwa wenu hana tatizo hata kidogo.”

    “Haiwezekani, alianguka ghafla kanisani, tena alipokuwa akifunga ndoa,” alisema baba yake Luciana.

    “Ndiyo hivyo, mapigo yake ya moyo yapo vilevile, hayashuki wala hayapandi, ninachokishauri, mpelekeni kwenye nyumba za ibada, nahisi atapona kabisa, si mnajua haya magonjwa ya kienyeji huwa hayaonekani katika vifaa vyetu,” alisema daktari yule.

    “Sawa.”

    Huo ndiyo ushauri uliotolewa, hakukuwa na kitu kingine kilichotakiwa kufanywa zaidi ya watu hao kumpeleka Luciana katika nyumba moja ya ibada kwa ajili ya kufanyiwa maombezi. Ilionekana kwamba alikuwa na tatizo kubwa ambalo kwa dawa hizi za kibinadamu, wasingeweza kumtibu hata mara moja hivyo kulitakiwa kufanyika njia nyingine kabisa.

    Hawakutaka kusubiri, walichokifanya ni kwenda katika Kanisa la Praise And Worship lililokuwa chini ya mchungaji Kimario.

    Walipofika katika eneo la kanisa hilo, wkateremka kwenye gari na kuanza kupiga hatua kuelekea ndani ya kanisa hilo, walipofika mlangoni tu, ghafla nguvu za ajabu zikamuingia Luciana, katika hali wasiyoitegemea, wote waliokuwa wamemshika, wakarushwa huko na yeye kuanguka chini, Luciana akaanza kurusha miguu yake huku na kule, mapovu yakaanza kumtoka mdomoni, watu wote waliokuwa kanisani mule wakabaki wakishangaa tu.

    ****

    “Ebwanaeeee, umesikia ishu iliyotokea kule mbuyuni? Ni noma, kuna mwanamke kaamka na kujikuta pale na wakati usiku uliopita alilala chumbani kwake,” alisema jamaa mmoja.

    “Acha utani.”

    “Kweli tena. Achana na huyo, kuna mwingine alipita karibu akadondoka, hivi kwa nini huu mbuyu tusiukate,” alihoji jamaa huyohuyo.

    “Hilo ndilo la maana, kama vipi tukamshirikishe mwenyekiti wa serikali za mtaa,” alisema jamaa mwingine.

    Bado mambo ya ajabu yalikuwa yakiendelea kutoka mjini Bagamoyo, mbuyu ule ulioaminika kuwa wa kichawi uliendelea kuwatesa watu kama kawaida. Hakukuwa na amani, watu wengi waliokuwa waikilala vyumbani mwao, mwisho wa siku walijikuta wakiwa nje.

    Hali ilitisha na kila siku hofu zilizidi kuongezeka. Matukio hayo ya ajabu ndiyo yaliyowapekea watu kuwa na uamuzi mmoja tu, kuukata ule mbuyu na maisha kuendelea.

    Jambo hilo likafanyika, vijana watano wenye nguvu wakaandaliwa, wakapewa mashoka na kisha kuanza kazi mara moja. Ilikuwa ni moja ya kazi kubwa mno, kila walipojaribu kuukata mbuyu ule, haukukatika, waliona kama wakipiga kitu kilichokuwa na chembechembe ya vyuma.

    Watu hao waliendelea kujaribu kuukata mbuyu ule huku wananchi wakiongezeka na kushuhudia kile kilichokuwa kikiendelea, kazi ile kubwa iliendelea kufanyika lakini hakukuwa na kilichoendelea zaidi ya mbuyu ule kuendelea kuwa imara.

    Baada ya siku mbili, vijana wale waliokuwa wakiukata ule mbuyu na kushindwa kuuangusha, wakaanza kuumwa ghafla, miili yao ikaanza kutokwa na malengelenge jambo lililowafanya kuwapeleka hospitalini lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika zaidi ya kufariki dunia.

    Siku ya mazishi yao, mambo ya ajabu yaliendelea kutokea, makaburi yao yote, yalikuwa yamejaa maji na wakati hakukuwa na mvua yoyote ile iliyonyesha. Waganga wakahitajika na kuanza kufanya uganga wao lakini maji yale yaliyokuwa yakitokea makaburini hayakupungua, bado yaliendelea kuwa vilevile hivyo wakaamua kuwazika hivyohivyo.

    Mara baada ya siku kadhaa tangu watu waamue kuukata mti ule, kuna kijana akaonekana chini ya mbuyu ule huku akilalamika mno, hawakujua alikuwa akizungumza na nani lakini kwa jinsi alivyokuwa akiongea, kulikuwa na mtu pembeni yake japokuwa hawakuwa wakimuona.

    Alizungumza kwa dakika kadhaa na kisha kuondoka huku akionekana kuwa na majonzi mno. Alipoondokea, hakukuwa na mtu aliyefahamu lakini baada ya siku kadhaa, mara ule mbuyu ukaanza kufuka moshi mkubwa kiasi kwamba hata mtu aliyesimama mbali alipouona moshi ule, alifikiri kwamba nyumba ilikuwa ikiteketea kwa moto.

    Watu wakaanza kukimbilia kule kulipokuwa kukifuka moshi, kuna wengine walikwenda na ndoo za maji kwa ajili ya kuuzima moto ule, ila cha ajabu walipofika kule, hawakukuta nyumba yoyote zaidi ya ule mbuyu uliokuwa ukiteketea moto.

    “Mungu wangu!” alisikika mwanaume mmoja, hakuwa akiamini kile kilichokuwa kikitokea, mwanaume huyo, alikuwa miongoni mwa wachawi wakubwa hapo mjini Bagamoyo.

    Kila mtu akapigwa na butwaa!

    ****

    Emmanuel na wazazi wa Luciana wakawa wamesimama pembeni, kilichokuwa kimetokea kiliwashtua, Luciana alikuwa chini huku akirusha mikono yake huku na kule na mapovu yakimtoka mdomoni, kelele zilikuwa zikisikika kutoka kwake kwamba alikuwa akiungua kitu kilicholifanya kanisa lile kuzidi kukemea zaidi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Moshi mkubwa ukaanza kutoka mwilini mwake, ukaanza kutanda kanisani mule hali iliyowapeleka watu kuzidi kuumea huku wakiongozwa na mchungaji wa kanisa lile.

    “Ninakukemea kwa jina la Yesu! Mtoke binti huyu, pepo wa ukichaa, pepo wa magonjwa, kwa jina la Yesu mtoke binti huyu....” alikemea mchungaji yule.

    Kanisa zima likafuka moshi mzito, kilichokuwa kikitokea hakikuaminika, mwili wa Luciana ukaanza kutoa ungaunga uliopukutika chini huku miguu yake ikianza kuvimba na baada ya muda kuacha.

    Kila kitu kilichokuwa kikitokea, Emmanuel alikishuhudia kwa macho yake. Maombi yale yalichukua kwa takribani dakika arobaini na tano, Luciana akabaki kimya, hakukuwa na sauti yoyote iliyosikika kutoka kwake, alikuwa kama mtu aliyekufa.

    “Mleteni mbele, shetani hana ujanja hata mara moja kwa Mungu wetu aliye hai,” alisema mchungaji na hapohapo watu wakambeba Luciana na kumpeleka mbele, kitu cha ajabu, hata ule moshi ukakatika ghafla.

    Hapo, mchungaji hakunyamaza, aliendelea kuomba huku akinena kwa lugha, wala hazikuchukua dakika nyingi, Luciana akayafumbua macho yake. Kwanza akaonekana kushangaa, alijikuta akiwa amezungukwa na watu wengi waliokuwa wakimfanyia maombi, alipoyageuza macho yake kuangalia huku na kule, yakatua kwa Emmanuel aliyekuwa akimshangaa.

    “Emmanuel....” aliita Luciana huku akijitahidi kuinuka, Emmanuel akamsaidia kumuinua.

    “Mpenzi wangu!”



    “Kuna nini tena? Hapa wapi? Mbona nimezungukwa na watu wengi? Mungu wangu! Nimefikaje kanisani na wakati nilikuwa darasani nikijiandaa kufanya mtihani? Emmanuel, nirudishe shuleni nikaanze kufanya mtihani,” alisema Emmanuel, alikuwa akimwambia mpenzi wake huku akionekana kuchanganyikiwa.

    Emmanuel akabaki akisikitika tu, maneno aliyokuwa akiambiwa na mpenzi wake, matukio yake yalitokea miaka mitano iliyopita, kipindi alichoingiwa na mapepo na kuwa kichaa. Kumbukumbu zake zilimwambia hivyo na wala hakujua kile kilichokuwa kimetokea.

    Emmanuel hakumwambia kitu, machozi ya furaha yalikuwa yakimbubujika, kitendo cha kumuona mpenzi wake akiwa amerudiwa na fahamu na kuwa kama alivyokuwa kipindi cha nyuma, alijisikia kutaka kurukaruka kwa furaha.

    “Emmanuel, mbona nina shela? Mbona sijavaa sare zangu za shule?” aliuliza Luciana.

    Kila kitu alichokuwa akikizungumza kilimfanya kuonekana kwamba hakuwa akifahamu kile kilichokuwa kimetokea. Emmanuel hakuwa na jinsi, kwa furaha kubwa aliyokuwa nayo, akajikuta akimsogelea Luciana na kisha kumkumbatia kwa furaha.

    “Umerudi mpenzi,” alisema Emmanuel kwa furaha.

    “Kutoka wapi mpenzi? Nilisafiri?”

    “Hapana. Mungu ametenda, ni kwa kipindi kirefu nimekuwa nikisubiri kitu hiki kitokee, hatimae kimetokea,” alisema Emmanuel huku machozi yake yaliyokuwa yakimbubujika mashavuni kuulowanisha mgongo wa Luciana.

    Alichokifanya mchungaji ni kumpa nafasi Emmanuel kuelezea kitu gani kilichokuwa kimetokea mpaka msaichana huyo kuletwa kanisani hapo huku akiwa kwenye hali hiyo. Emmanuel akasimama mbele kabisa kanisani, machozi yaliendelea kububujika mashavuni mwake, kila kilichokuwa kimetokea, hakuwa akiamini kama Mungu alikuwa ametenda muujiza.

    Hapo ndipo alipoanza kulihadithia kanisa juu ya kile kitu kilichokuwa kimetokea miaka mitano iliyopita, tangu siku ya kwanza kwa msichana huyo kuingiwa na mapepo na mwisho wa siku kupelekwa hospitalini na kuwekwa katika vyumba maalumu vya wagonjwa wa vichaa.

    Hakuishia hapo, aliendelea kulielezea kanisa kwamba pamoja na kuwa katika hali hiyo, bado alitaka kumuoa kwa sababu alikuwa na mapenzi ya kweli kwake. Baada ya miaka mitano kupita, hatimae akawaambia wazazi wake kwamba alikuwa akitaka kumuoa msichana huyo.

    Kila kitu kilichoendelea baada ya hapo, Emmanuel alikiweka wazi, Luciana akabaki akilia tu, hakuamini kile alichokuwa akikisikia. Kila mtu kanisani mule akamshangaa Emmanuel huku wasichana wengi wakitamani kuwa na mwanaume kama yeye.

    “Hilo shela, hii suti, vyote vinamaanisha kwamba tulikuwa katika hatua ya mwisho kufunga ndoa, nisingeweza kukuacha, nilitaka niwe nawe maisha yangu yote,” alisema Emmanuel huku akimwangalia Luciana.

    Luciana akashindwa kuvumilia, akajikuta akipiga hatua na kumkumbatia Emmanuel, kila kitu alichokiongea kanisani hapo, kikaaminika kwani hata wazazi wake walikuwepo mahali hapo na walionekana kuufahamu ukweli wote aliokuwa akiuzungumzia mpenzi wake.

    “Mchungaji, tulikamilisha kila kitu, lilikuwa limebakia tendo moja tu kabla ya kufunga ndoa, tunaweza kuendelea kanisani kwako? Ninatamani kuishi na Luciana kama mke wangu,” alisema Emmanuel.

    “Koh koh koh!”mchungaji alianza kwa kukohoa na kuendelea:

    “Hakuna tatizo, ila itatubidi tusubiri mpaka baadae kwani nitahitaji kuwa na cheti cha ndoa pia,” alisema mchungaji huyo kwani alitaka kuwasiliana na mchungaji yule aliyetaka kuwafungisha ndoa kwa ajili ya kupatiwa cheti cha ndoa ili wawili hao waweze kuweka sahihi zao.

    ****

    Kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo watu walivyozidi kuongezeka karibu na mbuyu ule. Hawakuamini kile kilichokuwa kikiendelea kwamba mbuyu wa kichawi ulikuwa ukifuka moshi mwingi huku kelele zikisikika mahali hapo.

    Huo ukaonekana kama muujiza, hakukuwa na mtu aliyejua kilichokuwa kikiendelea mpaka hali kuwa ile. Moshi haukupungua, ulizidi kuongezeka zaidi kiasi kwamba watu wengi wakayahofia maisha yao kwa kuhisi kwamba mambo yangeweza kuwa mabaya zaidi.

    “Mmmh! Huu mbuyu vipi? Mbona unazidi kufuka moshi, yasije kuwa majini tu!” alisema kijana mmoja, bado moshi uliendelea kufuka kama kawaida.

    Hakukuwa na mtu aliyefahamu ni kitu gani kilitokea, ghafla, ule mbuyu mkubwa ukatandwa na moshi mwingi zaidi kiasi kwamba haukuweza kuonekana zaidi ya moshi ule, hali hiyo ilichukua zaidi ya dakika tano, moshi ulipoanza kukata, ghafla, mbuyu ule haukuonekana, kilichoonekana ni nyoka mkubwa wa rangi nyekundu, watu kuona hivyo, wakaanza kukimbia.

    Kila mtu mtuakataka kuyaokoa maisha yake, wale wasiokuwa na mbio, wakajikuta wakiangushwa chini na kukanyagwakanyagwa, hata wale waliokuwa na watoto, wakajikuta wakiawaacha, kila mtu alitaka kuyaokoa maisha yake. Cha ajabu, nyoka yule mkubwa akapotea sehemu ile, watu walipoangalia, hata mbuyu haukuonekana sehemu ile, yaani ilikuwa wazi kabisa.

    ****

    Wiki ziliendelea kukatika, mwezi ukamalizika na hatimae mwaka wa kwanza kupotea. Patrick aliendelea kuwa na mawazo juu ya msichana aliyewahi kuwa mpenzi wake, Luciana. Mwaka huo ukapita na mwingine kuingia, maumivu moyoni mwake hayakuisha, kila alipokuwa akikumbuka yale yaliyotokea katika maisha yake ya nyuma na msichana Luciana, aliumia mno.

    Yalikuwa ni zaidi ya maumivu, hakuamini kama kipindi chote kile alichokuwa amepoteza na msichana huyo, mwisho wa siku hakuweza kumuoa, matokeo yake alikuja kuolewa na mtu mwingine kabisa.

    Kama kulia, alilia mno. Kipindi cha nyuma alipata taarifa kwamba Luciana hakuwa tena kichaa bali alipona kwani alifanyiwa maombezi kanisani na mwisho wa siku kuwa mzima wa afya. Alichokifanya, huku akionekana kuwa na hasira mno, akaanza kwenda Bagamoyo chini ya ule mbuyu ili kujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Alipofika Bagamoyo, akaanza kuelekea katika Mtaa wa Magomeni kulipokuwa na huo mbuyu mkubwa, alipofika, kitu ambacho kilimshangaza, mbuyu haukuwepo jambo lililomfanya kunyong’onyea.

    Japokuwa tayari kipindi cha miaka miwili ilikuwa imepita lakini lilikuwa jambo lisilojengeka kichwani mwake kwamba mbuyu ule ulikuwa umekatwa. Aliufahamu fika, alijua kwamba watu waliuogopa vilivyo tangu miaka hiyo hivyo lilikuwa jambo gumu kuukata mbuyu huo.

    Alibaki akikaa chini huku hajui ni kitu gani kilikuwa kimetokea. Hakuacha kujiuliza maswali lakini kila swali alilojiuliza, hakupata jibu lolote lile. Fikra iliyomjia kichwani ni kuhisi kwamba inawezekana alikuwa amepotea njia, hivyo njia ile aliyokuwa amepita nayo haikuwa yenyewe.

    “Lakini ile nyumba nyekundu si ile pale! Na uwanja si ule kule, sasa nini kimetokea? Mbuyu uko wapi?” alijiuliza lakini akakosa jibu.

    Hakutaka kukaa na maswali mengi, alichokifanya ni kuwafuata vijana waliokuwa wamekaa kijiweni kwa lengo la kuwauliza.

    “Samahani, kuna jambo ningependa kuwauliza,” alisema Patrick mara baada ya salamu.

    “Uliza tu kaka.”

    “Nakumbuka hapa kulikuwa na mbuyu, upo wapi? Ulikatwa au?”

    “Duuh! Yaani stori ilitapakaa Bagamoyo nzima, wewe mgeni nini?” aliuliza jamaa mmoja.

    “Yeah! Nimetoka Dar.”

    “Unafikiri ule ulikuwa mbuyu basi! Haukuwa mbuyu bali ulikuwa nyoka mkubwa,” alisema jamaa mwingine.

    “Mnamaanisha nini, sijawaelewa.”

    Hapo ndipo vijana wale walipoanza kumuhadithia Patrick kile kilichokuwa kimetokea. Aliyategesha masikio yake vizuri na kuendelea kuwasikiliza vijana wale walioongea kila kitu pasipo kubakisha kitu chochote kile.

    Patrick hakuamini kile alichokuwa akikisikia. Kuambiwa kwamba mbuyu ule haukuwa mbuyu bali ulikuwa nyoka mkubwa kilimshangaza mno. Alifika hapo Bagamoyo kwa kuwa alikuwa akihitaji msaada mkubwa kutoka kwa mbuyu ule kwani tayari mambo yake ya mapenzi yalikuwa yakimsumbua lakini kile kitu alichokuwa amekifuata kule, hakukipata.

    Hakutaka kuendelea kukaa Bagamoyo, alichokifanya ni kuondoka na kurudi Dar. Njiani, alikuwa na mawazo mengi na hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya. Hakumpenda tena Luciana, alikuwa miongoni mwa watu aliokuwa wakiwachukia mno, alichokifanya ni kutafuta njia zaidi za kuweza kummaliza, moyo wa mapenzi ukapotea na moyo wa mauaji kumuingia.

    Alipofika Dar, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuonana na rafiki yake wa siku nyingi, huyu aliitwa Michael ambaye alimuahadithia kila kitu na hata uamuzi aliokuwa ameufikiria.

    “Kwa hiyo unataka kumuua?”

    “Ndiyo. Ila nisijulikane.”

    “Kwa hiyo unamaanisha kienyeji?”

    “Ndiyo! Yaani nisijulikane tu.”

    “Kuna sehemu nitakupeleka.”

    “Wapi?”

    “Usijali, wewe twende tu, utapajua hukohuko.”

    “Hakuna tatizo.”

    Wakaondoka kuelekea huko.

    ****

    Maisha yalikuwa ya raha, hakukuwa na shida yoyote, Emmanuel na mke wake, Luciana walipendana mno. Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo mapenzi yao yalivyozidi kuongezeka, hawakutaka kukumbuka kitu chochote kile, kila kilichokuwa kimetokea katika maisha yao ya nyuma, wakaamua kukisahau.

    Baada ya kukaa kwa miezi sita ndani ya ndoa, Emmanuel akahisi kuwa na uhitaji wa kumtumikia Mungu na kuwa mchungaji, hakutaka kukaa kimya, kwa kuwa aliyaona maono hayo toka ndotoni, akaamua kumwambia mke wake.

    Halikuwa tatizo, alichokifanya ni kuwasiliana na mchungaji wake, mchungaji Christopher Mwangole na kumwambia kile kilichokuwa kimemtokea katika maono, alimwambia dhamira yake ya kutaka kuwa mchungaji, akakubaliwa hivyo kushauriwa kwenda kuusomea mkoani Dodoma, kilipokuwa Chuo Kikuu cha Biblia Tanzania.

    Siku ya kuondoka, moyo wake ulimuuma mno, alibaki akimwangalia mke wake huku akiwa na maumivu makali ya moyo, hakupenda kumuacha katika hali hiyo, alihitaji kuwa naye karibu kadiri ilivyowezekana lakini katika kipindi hicho, hakuwa na jinsi, ilimbidi kuondoka kuelekea chuoni.

    Huko, akaanza masomo yake. Kila siku akawa mtu wa kuwasiliana na mke wake, haikuwahi kupita hata siku moja asiwasiliane naye, alijitengea ratiba yake maalumu ya kuzungumza naye simuni.

    Alimfariji kwamba miezi sita ya ‘semister’ya kwanza ilikuwa fupi hivyo angeweza kurudi tena nyumbani na kuungana naye. Kila mmoja alimkumbuka mwenzake na alitaka kumuona kwa mara nyingine tena.

    Baada ya miezi sita, yaani mwaka mmoja upite tangu wafunge ndoa, akarudi nyumbani kwake, ilikuwa furaha mno, akajikuta akimkumbatia mke wake huku akibubujikwa na machozi ya furaha.

    “Miezi sita imekuwa kama miaka kumi,” Emmanuel alimwambia mke wake, Luciana.

    “Kwangu ni zaidi ya karne nzima, nilikukumbuka mpenzi wangu,” alisema Luciana na kuendelea kukumbatiana.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao ya kila siku, hawakutaka kuwa mbali mbali, walitamani kila siku waendelee kuwa pamoja na hata kipindi hicho cha likizo, kwao kilionekana kuwa kidogo mno.

    Japokuwa waliishi kwa furaha, mapenzi kemkem lakini kulikuwa na jambo moja lililowatatiza maishani mwao, nalo ni mtoto. Walifanya kila jitihada ili waweze kupata mtoto lakini likaonekana kuwa jambo gumu kutokea. Walishinda kitandani huku juhudi zikiendelea kuongezeka lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika, tatizo lilikuwa lilelile kwamba mtoto hakupatikana.

    Walichokifanya ni kwenda hospitalini, huko, wakaomba kuonana na daktari ambaye baada ya kuelezewa kwa kirefu akagundua kwamba Luciana ndiye alikuwa na tatizo, hivyo akawaita ndani na kuanza kuwapa elimu.

    “Sababu zipo nyingi kama vile mirija kuziba kitaalamu fallopian blockage, matatizo ya kutokupevuka kwa mayai ya mwanamke kitabibu hali hiyo huitwa ovulation disorder na kuota vinyama kwenye mji wa mimba yaani endometriosis na kuwahi kusimama hedhi au early menopause.

    “Sababu nyingine za kutoshika mimba ni kuwa na uvimbe kwenye kizazi kitaalamu huitwa uterine fibroid, kuharibika kwa tezi la mayai (polycystic ovary syndrome), kizazi kushikana na viungo vingine vya uzazi (pelvic adhesions),” alisema dokta huyo.

    Wote walikuwa kimya wakimsikiliza, kila neno aliloongea liliwaingia vichwani mwao. Baada ya kuwapa ushauri mrefu, mwisho wa siku akawapa njia ya kulitatua tatizo hilo.

    Walirudi nyumbani wakiwa na furaha tele huku kila mmoja akiwa na uhakika kwamba wangeweza kupata mtoto. Shughuli zao ziliendelea mpaka Emmanuel alipomaliza likizo yake na hivyo kurudi chuoni.

    Aliendelea kusoma huku kila siku akimuombea mke wake aweze kupata ujauzito. Kwa sababu siku aliyokuwa ameondoka nyumbani ndiyo ilikuwa miongoni mwa siku za kushika ujauzito, alifanya kila aliwezalo usiku kitu kilichomfanya kwa muda huo kujua kwamba inawezekana dalili zimeanza kuonekana.

    “Vipi mke wangu? Mungu ametenda?” aliuliza Emmanuel.

    “Hapana. Bado sijaona dalili yoyote ile.”

    “Hata kutapika?”

    “Bado.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Kizunguzungu je?”

    “Bado.”

    “Na hata kichefuchefu?”

    “Bado kabisa, yaani nahisi ni tatizo kubwa.”

    Emmanuel akanyong’onyea, hakuamini kile alichokuwa amekisikia, mke wake kuchukua kipindi kirefu namna ile pasipo kupata mimba kilimchanganya. Akajikuta akikesha akiomba ili naye apate kuwa na mtoto.

    Wakati mwingine alihisi kwamba Mungu hakusikia maombi yake kwani hadi mwaka wa pili ulipoingia, bado hali ilikuwa ileile tu, dalili za mimba hazikuonekana, akachanganyikiwa zaidi.

    ****

    Mambo yalibadilika, imani za kishirikina zikaanza kujengeka mioyoni mwa watu, watu wengi wakatolewa kafara huku wengine wakizikwa hai, maalbino wakauawa na wengine kukatwa viungo vyao kwa kuwa ilihisiwa kwamba viungo hivyo vilikuwa na nguvu ya kuvuta utajiri.

    Upendo wa watu ukapungua, maisha ya mtu mwingine hayakuonekana kuwa na thamani kabisa, wengine wakawa ladhi kuwaua watu wengi lakini mwisho wa siku waendeshe magari ya kifahari na kupiga misele mitaani.

    Makanisa ya kishetani yakaanzishwa, mengine yaliwataka watu wasali wakiwa uchi, mengine yaliwataka watu watoe kafara za damu kila walipokwenda kanisani huku mengine yakiwataka watu kufanya mapenzi makanisani humo, yaani ilikuwa shaghalabaghala.

    Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele ndivyo ambavyo mambo mengi ya kishirikina yalipozidi kutokea. Dunia ikatawaliwa na ushirikina mkubwa, shetani akajipatia nguvu na kuanza kuwatesa watu wengi.

    Manukato mengi yakatengenezwa kuzimu, nguo za kike asilimia nyingi zilitengenezwa huko huku zikiwekewa nyuzi maalumu kwa ajili ya kuwavuta wanaume, kuwaumbia tamaa na mwisho wa siku kulala nao.

    Wakati ndege nyingi zilipokuwa angani zilipotea na kutokuonekana, Wazungu walijitahidi kufanya kila liwezekanalo kuzipata lakini mwisho wa siku hawakuambulia kitu zaidi ya kusikia tetesi tu kutoka kwa wanasayansi kwamba ndege zilipotea sana katika Bahari ya Java, sehemu ndogo baharini iliyokuwa na mvutano mkubwa nchini Indonesia.



    Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba ni ushirikina ndiyo uliokuwa ukifanya kazi yake katika kipindi chote hicho. Dunia ilibadilika na watu wengi wakaanza kuamini uchawi, wengine wakajitokeza na kudai kwamba kulikuwa na makundi ya wasanii ambao waliyaendsha maisha yao kitajiri baada ya kujiunga na dini iliyokuwa ikimuabudu shetani.

    Baada ya siku kuendelea kukatika huku imani za kishirikina zikiendelea kuchachamaa mioyoni mwa watu hapo ndipo zilipoanza kusikika tetesi kwamba kulikuwa na namba za simu zilizokuwa zikipigwa simuni, kama ukiziona na kuzipokea, hapohapo unafariki dunia.

    Kama zilivyokuwa tetesi za ndege, ndivyo zilivyokuwa tetesi hizo pia. Zilianza kusambaa nchini Marekani lakini baada ya kipindi cha mwezi mmoja, kampuni moja ya simu nchini Marekani ikathibitisha kwamba hizo hazikuwa tetesi bali zilikuwa taarifa kamili.

    Watu wakaanza kuhofia, namba hizo ambazo mpaka katika kipindi hicho hazikujulikana ni zipi zikaonekana kuwa tishio kwa watu wote nchini Marekani. Kila aliyepigiwa simu kwa namba ngeni, hakuipokea simu ile kwa kuamini kwamba namba hiyo ndiyo ilikuwa ileile kutoka kuzimu.

    Wanachuo wanne kutoka katika Chuo cha Mississippi nchini Marekani walifariki dunia huku walipofuatwa vyumbani mwao, simu zilionekana pembeni huku masikio yao yakitoka damu.

    Vifo hivyo havikuishia hapo tu, viliendelea kusambaa sehemu mbalimbali na mpaka mwezi mmoja wa tetesi za namba hiyo ziliongezeka na tayari watu zaidi ya elfu moja nchini Marekani walikuwa wamekwishafariki dunia.

    “Did you see the numbers?” (Uliziona hizo namba?) aliuliza jamaa mmoja.

    “No! I just heard of them but I didn’t see them. How do they look like?” (Hapana! Nilizisikia lakini sijawahi kuziona. Hivi zipo vipi?) aliuliza jamaa mwingine.

    “I don’t know,” (Sifahamu)

    Zilipita wiki kadhaa ndipo namba zilizoonekana kuwa chanzo zikatajwa kwamba ni +255901009999. Kitu cha kwanza kabisa kilichofanyika ni kuangalia ‘code’ za nchi ambayo ilianzia na +255. Kwenye kuangalia kwao, wakagundua kwamba namba hizo zilikuwa ‘code’ kutoka nchini Tanzania.

    Hawakuwa na cha kufanya zaidi ya watu kupewa taarifa kwamba hawakutakiwa kupokea simu iliyokuwa ikipigwa na namba hiyo. Watu wakaishi kwa hofu na hata wale waliokuwa na ndugu zao kutoka nchini Tanzania wakashikwa na hofu kiasi kwamba hata walipokuwa wakipigiwa simu na ndugu zao, hawakuwa wakizipokea simu hizo.

    Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo namba hiyo ilizidi kutikisa dunia. Watu waliendelea kufariki huku tetesi zikisema kwamba kila mtu aliyekuwa akifariki, alinyoywa damu na hivyo kuwa kinywaji kule kuzimu.

    Namba hizo hazikuishia nchini Marekani tu, zikaanza kusambaa mpaka katika nchi za jirani kama Canada, Mexico, Costa Rica na sehemu zingine. Hofu ikaendelea kuikumba dunia, kutokana na namba hizo kuwa tata, watu wengine wakaamua kutokutumia simu kabisa.

    Baada ya kipindi kirefu, dhahama hilo likatawala dunia nzima. Kwa nchini Tanzania, hali ilionekana kuwa ngumu zaidi kwani namba iliyokuwa ikitumika ilikuwa na ‘code’ zilezile zilizokuwa zikitumika nchini Tanzania.

    “Sasa jamani huku si kuuana,” alisema jamaa mmoja huku akionekana kuwa na hofu moyoni mwake.

    “Hapa inabidi serikali ifanye jambo, kama tumeshindwa kuwashughulikia mafisadi, basi tumshughulikie hata mtu anayetumia namba hii,” alisema jamaa mwingine huku akionekana kukasirika.

    “Kaka, hili jambo gumu, hujasoma mpaka Marekani imewasumbua, sasa kama wao imewasumbua, vipi kuhusu sisi?” alihoji jamaa mwingine.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Watu waliendelea kufariki, simu hiyo ya hatari ilikuwa ikiendelea kupigwa, kwa kila mtu aliyeiona na kuitambua kwamba simu hiyo ilitoka wapi, hakuipokea ila tatizo lilikuwa kwa wale ambao hawakuwa wameitambua, hasa wale wasiokuwa na muda wa kupitia vyombo vya habari, waliendelea kupukutika.

    Si makanisani wala misikitini, kote huko wakajikusanya na kuanza kumuomba Mungu awasaidie katika hilo lakini jambo hilo likaonekana kuwa gumu, si kwamba Mungu hakuwasikia, ila kutokana na uovu mwingi uliokuwa ukifanyika, hakukuonekana kuwa na msaada wowote ule.

    *****

    Patrick na Michael wakafika sehemu iliyokuwa na pori kubwa, hapo wakateremka kutoka garini na kuanza kutembea kuingia ndani zaidi, walipofika umbali fulani, macho yao yakaona kijumba fulani cha udongo, hakikuwa na bati wala hakikujengwa na matofali, walichokifanya ni kuanza kukisogelea.

    Kulikuwa porini, penye kuogopesha sana lakini Michael hakuonekana kuhofia chochote kile, hiyo haikuwa siku yake ya kwanza kufika hapo, alikwishazoea kufika na ndiyo maana siku hiyo aliamua kumleta rafiki yake kwa ajili ya kupata kile alichotaka kukipata.

    Walipofika ndani, wakamkuta mwanaume mmoja mzee sana ambaye kwa kumtazama tu, alistahili kuitwa babu. Wakaambiwa wakae chini na hapo ndipo Patrick alipotakiwa kuelezea kile alichokuwa akikitaka.

    Hakufika kitu chochote, alimwambia mganga yule kwamba lengo lake la kufika mahali hapo ni kwamba alitaka kumuua mtu ambaye alimfanyia kitu kibaya katika maisha yake, japokuwa kilikuwa kimepita kipindi kirefu lakini moyo wake haukutaka kusahau na alikumbuka kila kitu na kuzidi kuumia.

    “Anaitwa nani?”

    “Luciana.”

    “Sawa. Jichane hapo kidoleni kisha tumbukiza damu yako ndani ya chungu hicho chenye maji,” alisema mganga huyo huku akimpa Patrick kisu ambapo alifanya kama alivyotakiwa kufanya.

    “Chukua kisu hicho, damu yako imeendana na mimi na ndiyo maana sitaki kuzungumza nawe mengi, nitakufanyia kazi yako, kisha utakachotakiwa ni kunipa kile unachoona ninastahili kupewa kwa kazi niifanyayo, hata kama itakuwa ni fedha tena shilingi hamsini, bado nitashukuru,” alisema mganga yule.

    Patrick akachukua kisu kile.

    ****

    Mganga akaanza kuongea maneno yake yasiyoeleweka, kitu alichokuwa akikitaka ni kuiona picha ya Luciana kwenye maji yale na Patrick achome kisu katika maji hayo ili msichana huyo afariki dunia.

    Kitu cha ajabu ambacho hata mganga mwenyewe hakukielewa, alipomaliza kuongea maneno yake, sura ya Luciana haikutokea katika maji yale kitu kilichomshtua kwani haikuwa kawaida, kwa miaka ishirini aliifanya kazi hiyo lakini jambo hilo halikuwahi kutokea.

    “Vipi?” aliuliza Michael.

    “Subiri! Hebu ngoja nianze tena, inawezekana kuna maneno nilisahau,” alisema mganga yule na kuanza kuongea maneno yake yaleyale tena kwa ufasaha mkubwa.



    Hakikubadilika kitu, bado sura ya Luciana haikutokea katika maji yale. Maswali mengi yakaanza kumiminika kichwani mwake kwamba inawezekanaje hali kama hiyo kutokea? Tena katika kipindi kama hicho? Kila alipojiuliza, akakosa jibu.

    Mganga akatambua kwamba Luciana alikuwa na nguvu nyingine zilizokuwa kubwa kuliko zake, na kitu alichokihisi ni kwamba alitumia uchawi uliokuwa na nguvu kuliko zake. Hakutaka kushindwa, alichokifanya ni kuwachukua na kuwapeleka porini.

    Walipofika huko, wakausogelea mti mmoja mkubwa uliokuwa na tunguli nyingi kwa chini ambazo zote zilifungwa kwa kitambaa chekundu kwa juu.

    Hiyo ndiyo ilikuwa sehemu yake aliyoitegemea, hata kama mtu alitumia nguvu gani, alikuwa na uhakika wa kushinda. Uchawi huo wa uliokuwa kwenye mti huo haukuwa na masihala, watu wote waliokuwa wakishindikana ndani ya chumba chake, alifanikiwa kwa urahisi sana mara anapokwenda katika mti huo.

    “Hapa tutafanikiwa tu,” alisema mganga maneno yaliyoanza kuwatia faraja.

    “Kweli mkuu?”

    “Ndiyo! Hakuna kinachoshindikana hapa, yaani asilimia mia moja tunammaliza,” alisema mganga huyo.

    “Tutashukuru sana,” alisema Michael.

    Kazi ikaanza upya, mganga yule, kama kawaida yake akaanza kuzungumza maneno mbalimbali aliyokuwa akiyatumia kila siku chini ya mti ule. Kulikuwa na karai lililokuwa na maji ndani yake yaliyochanganywa na damu, lengo lake lilikuwa ni kuongea maneno yale na mwisho wa siku picha ya Luciana kutokea, kitu cha ajabu, haikuweza kutokea.

    Jasho lilimtoka, mwili ukaanza kumtetemeka, alijitahidi kwa nguvu zote laini majibu yaliendelea kubaki yaleyale tu, sura ya Luciana haikuweza kutokea.

    “Huyu mtu mchawi,” alisema mganga huku akionekana kuhamaki.

    “Mchawi? Hapana! Luciana siyo mchawi, na sijui kama anaujua uchawi,” alisema Patrick.

    “Labda haujamchunguza. Dalili zinaonyesha kwamba yeye ni jini!”

    “Jini?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Ndiyo!”

    “Hapana mganga.”

    “Usibishane na mganga, mimi ndiyo nakwambia hivyo.”

    “Mganga, si kwamba nakubishia ila nakwambia ukweli, Luciana si mchawi,” alisema Patrick.

    Walibaki wakibishana lakini hakukuwa na makubaliano yaliyowekwa, kila mmoja kuzungumza lake. Mganga alichanganyikiwa, alichowaambia Patrick na Michael ni kuondoka mahali hapo, hilo wala halikuwa tatizo, wakaondoka.

    ****

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog