Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

NISAMEHE LATIFA - 5

   







    Simulizi : Nisamehe Latifa

    Sehemu Ya Tano (5)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ulikuwa ni muda wa kuhangaika, kujutia kile kilichotokea na pia huo ulikuwa muda wa kulia na kusaga meno. Msichana aliyekuwa amemkataa ndiye aliyekuwa gumzo duniani, ndiye aliyesemekana kuwa na utajiri mkubwa kuliko vijana wote waliokuwa na umri chini ya miaka thelathini.

    Ibrahim aliumia moyoni mwake, mafanikio ya Latifa yaliuumiza mno moyo wake, akawa mtu aliyekosa raha, amani na furaha, kila alipokuwa akikaa, alijikuta akijilaumu kwa ujinga aliokuwa ameufanya.

    Latifa alikuwa msichna mzuri, mwerevu, mwenye akili na kuchanganua mambo, mbali na sifa hizo zote, msichana huyo alikuwa na sifa moja kubwa kwamba alikuwa akimpenda. Alipewa upendo wote, alithaminiwa kwa kiwango cha juu kabisa lakini badala ya kuupokea upendo ule, baada ya kuona namna gani alithaminiwa, mwisho wa siku akaona vyote hivyo havikuwa na thamani, upendo haikuwa sababu ya kuendelea kumpenda, akaamua kumuacha, akaamua kumliza, akaupa kidonda moyo wa msichana huyo, pasipo kuwa na huruma, akamwambia achukue taimu yake na yeye abaki na Nusrat, msichana aliyeamini kwamba angeishi naye milele.

    Kama kulikuwa na watu waliokuwa na maumivu makali duniani, Ibrahim alikuwa wa kwanza, alilia, macho yakawa mekundu, alijuta na kujuta lakini ukweli haukubadilika, kila kitu kilibaki kilekile kwamba aliacha nazi, akajiona mjanja wa kuchagua na mwisho wa siku mikono yake ikaangukia kwa koroma.

    Nusrat, yule msichana mrembo, yule msichana aliyemwambia kwamba angempenda miaka yote, leo hii alikuwa akiishi naye kimagumashi, maisha na wanaume wengine yakamteka na mwisho wa siku kujikuta akitumia muda mchache sana kuwa naye.

    Ibrahim hakuficha, alimwambia mzee Deo juu ya Latifa, yule msichana mrembo aliyekuwa akivuma sana, msichana aliyekuwa bilionea.

    “Msichana mwenyewe huyu hapa,” alisema Ibrahim, alikuwa akimwambia mzee Deo.

    “Msichana gani?”

    “Yule niliyemuacha kwa ajili ya huyu fisi,” alisema Ibrahim.

    “Unamaanisha Latifa?”

    “Ndiyo!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa ilikuwaje mpaka ukamuacha mwanamke bilionea?”

    “Ni ujinga, kipindi kile hakuwa na kitu, alikuwa msichana aliyejielewa, ila huyu nguchiro akanishawishi mpaka nikawa naye,” alisema Ibrahim huku akishindwa kulizuia chozi lake kububujika mashavuni mwake.

    “Pole sana aisee! Latifa ni msichana mrembo, kama ningekuwepo siku hiyo, hakika ningekupiga vibao, kwa mbali anafanana na Nahra kipindi kile alichokuwa msichana wangu,” alisema mzee Deo.

    “Nahra huyo mwanamke uliyezaa naye?”

    “Ndiyo! Ila duniani mara nyingi watu huwa wawiliwawili,” alisema mzee Deo pasipo kujua kama yule aliyekuwa akimzungumzia alikuwa binti yake wa damu.

    Ibrahim alijitolea kumsaidia mzee Deo, mara baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, kitu cha kwanza alichokifanya ni kumpeleka nyumbani kwake huku mzee huyo akiwa na mguu moja.

    Japokuwa mke wake alikasirika sana juu ya ujio huo lakini Ibrahim hakutaka kujali, alijisikia kumsaidia mzee huyo siku zote za maisha yake. Siku ambayo mzee huyo alikuja nyumbani hapo, mke wake, Nusrat alilalamika sana mpaka kufikia hatua ya kutaka kupigana lakini msimamo wa Ibrahim ukawa huohuo kwamba mzee Deo hakutakiwa kuondoka nyumbani hapo.

    Baada ya siku kadhaa, wakapata taarifa kwamba Latifa alikuja nchini Tanzania na safari yake ilianzia mkoani Kigoma. Moyo wake ulifarijika mno, alitamani kuonana na msichana huyo, si kwa lengo la kumwambia wawe pamoja, kitu alichokitaka ni msamaha kutoka kwa binti huyo tu.

    Alimsubiria kwa hamu kubwa, mpaka siku ambayo ilitangazwa kwamba msichana huyo aliingia jijini Dar es Salaam na watu zaidi ya elfu kumi walikwenda kumpokea uwanja wa ndege.

    Ibrahmi hakutaka kukaa nyumbani, alitaka kwenda huko, naye awe mmoja wa watu waliokwenda kumpokeaLatifa. Kutokana na idadi kubwa ya watu, hakupata nafasi ya kufika mbele kabisa, alisimama kwa mbali huku akimwangalia msichana huyo ambaye alikuwa na mwanaume asiyemfahamu kabisa, moyo wake ulimwambia kwamba mwanaume huyo alikuwa mpenzi wake.

    Ibrahim hakumsogelea, hakutaka kuonekana, kumuona Latifa, moyo wake ukaridhika kabisa, alichokifanya ni kugeuka na kurudi nyumbani. Njiani mawazo yalimsumbua mno, hakuamini kama kweli Latifa alikuwa vile aliyokuwa, kila alipokuwa akiufikiria ubilionea aliokuwa nao na umaarufu, aliona kwamba hata yeye pia angekuwa bilionea kwani wangechangia utajiri huo.

    Alipofika nyumbani, alishangaa kuona mzee Deo akiwa nje, alikuwa akililia kama mtoto mdogo, damu zilikuwa zimetapakaa kila kona, mguu wake ambao ulikuwa haujapona inavyotakiwa ulikuwa umetoneshwa.

    Ibrahim alipomuona, akamkimbilia kule alipokuwa, akainama na kumwangalia mzee huyo ambaye alikuwa na kipande cha mguu kutokana na kukatwa kwa sababu ya kansa. Alishindwa kuvumilia, akajikuta akitokwa na machozi.

    “Vipi tena?” aliuliza Ibrahim.

    “Mke wako.”

    “Kafanya nini?” aliuliza Ibrahim huku akionekana kuwa na hasira.

    “Amenifukuza kwako, kanitupa hapa nje,” alisema mzee Deo.

    “Hebu subiri!”

    Ibrahim akasimama na kuufuata mlango, akataka kuufungua lakini mlango haukufunguka, ulikuwa umefungwa kwa ufunguo. Wakati akiendelea kuugonga, hapohapo kwa chini akaona kikaratasi kikiwa kimepenyezwa chini mlangoni, akakichukua na kuanza kukisoma, kiliandikwa maneno machache sana yaliyosomeka ‘Sitaki nimuone huyo mzee mchafu nyumbani kwangu! Ukijifanya kiburi, hata wewe utaondoka, hujachangia hata tofali humu.’

    Ibrahim akahisi moyo wake ukichomwa na kitu chenye ncha kali, aliumia mno, alijikuta akikunja ngumu na kukichanachana kikaratasi kile. Maneno yaliyoandikwa katika karatasi ile yalikuwa ya kweli kabisa kwamba hakuchangia hata tofali ndani ya nyumba ile.

    Ibrahim akamfuata mzee Deo, akamnyanyua na kuanza kuondoka naye. Mzee huyo alikuwa na maumivu makali, bado damu zilikuwa zikimtoka katika kipande cha mguu alichokuwa nacho, alichokifanya ni kumpeleka hospitali.



    Safari ya kwenda Dar es Salaam ikaanza rasmi, ndani ya ndege bado Latifa alionekana kuwa na mawazo lukuki, penzi lake kwa Dominick lilichanya kiasi kwamba akawa haoni wala hasikii.

    Walipofika Dar, idadi ya watu elfu kumi walikuwa wamefika uwanjani hapo, ndege ile ilipoanza kutua, kila mmoja alionekana kuwa na furaha, vibendera vidogo vikaanza kupepewa, watu waliovalia fulana zilizokuwa na picha za Latifa wakajisogeza mbele kabisa.

    Uwanjani hapo Latifa alikuwa amepewa heshima kubwa mno, Waziri Mkuu, bwana Abdallah Kibonde alikuwa amefika kwa ajili ya kumpokea msichana huyo huku kukiwa na kundi la watoto watatu ambao waliletwa kwa ajili ya kumkabidhi maua kama ishara ya heshima na kumpenda.

    Kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo na pote alipopita Latifa kilikuwa kikirushwa laivu katika mashirika mbalimbali ya habari kama CNN, BBC, Aljazeera na mengine mengi kwani huyu Latifa alikuwa mtu mwenye nguvu kwa kipindi hicho, mtu aliyeleta mapinduzi makubwa mno.

    Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Dominick alikuwa akikifuatilia kwa karibu zaidi. Alifurahi kuwa karibu na Latifa, kwake, alionekana kuwa msichana mwenye nyota kubwa ya kupendwa.

    Miongoni mwa watu wengi waliokuwepo mahali hapo, walikuwa waandishi wa habari ambao mikono yao ilikuwa na kamera na walikuwa wakiendelea kufanya kazi yao ya kupiga picha kwa kila kilichokuwa kikiendelea.

    Kila mmoja akafurahia, kumuona Latifa nchini Tanzania, ndani ya nchi aliyozaliwa kulimfurahisha kila mtu. Katika kipindi cha nyuma, aliondoka nchini Tanzania kama mtu wa kawaida, hakukuwa na mtu aliyemthamini, alionekana kuwa si kitu ila leo hii alikuwa amerudi tena, alipokelewa kishujaa zaidi ya walivyokuwa wakipokelewa viongozi wengine.

    “Unajisikiaje kuwa Tanzania?” aliuliza mwandishi wa habari.

    “Sina la kuongea, naomba mniache, moyo wangu una furaha mno,” alisema Latifa huku akionekana mwenye furaha mno, machozi yalikuwa yakimbubujika.

    Hapohapo akachukuliwa na kuingizwa ndani ya gari la waziri huyo kisha safari ya kuelekea hotelini kuanza. Garini, Latifa alijisikia fahari mno, maisha yake yakaanza kurudi nyuma, kipindi alichokuwa akiishi Manzese kwa mama yake mlezi, bi Semeni aliyekuwa kaka yake mzee Issa ambaye kila siku alimchukulia kuwa baba yake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Leo hii alikuwa ndani ya gari la heshima, miongoni mwa magari yaliyopandwa na viongozi wakubwa nchini. Moyo wake ulifurahi mno, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, wakati mwingine alihisi yupo ndotoni.

    “Latifa...” aliita waziri, bwana Kibonde.

    “Ndiyo mheshimiwa.”

    “Umeliletea sifa taifa hili, japokuwa Wamarekani wamekuwa wakikung’ang’ania lakini utaendelea kuwa Mtanzania,” alisema bwana Kibonde.

    “Nashukuru sana! Ninajisikia kupendwa, ninapenda na kuvutiwa kwa kila kitu kinachotokea katika maisha yangu, kama nilivyowasaidia watu wengine, ningependa niwasaidie na Watanzania pia,” alisema Latifa huku akiachia tabasamu.

    “Mama yupo hai?”

    “Hapana! Alifariki miaka mingi iliyopita baada ya kuugua Ugonjwa wa UKIMWI, niliambiwa kwamba alikuwa mlevi mno,” alijibu Latifa na kubaki kimya, machozi yakaanza kumlenga.

    “Pole sana! Na vipi baba?”

    “Sijajua yupo wapi, nahisi amekwishakufa!”

    “Kwa nini uhisi?”

    “Sikuwahi kumuona, niliambiwa na baba yangu mlezi kwamba baba alimfukuza mama baada ya kugundua kwamba alikuwa mjauzito, tena hapo ni baada ya mama kufukuzwa nyumbani na wazazi wake kisha alikuwa na mimba ya mtu mweusi,” alisema Latifa.

    “Pole sana! Kwa hiyo hujui kama baba yako yupo hai au la?”

    “Sijui chochote kile.”

    Waliendelea kuzungumza ndani ya gari, Dominick ambaye naye alipewa heshima kubwa alikuwa ndani ya gari hilo, hakuzungumza chochote kile, alibaki kimya huku masikio yake yakiwa makini kusikiliza na ubongo wake kuwa makini kukariri.

    Safari ile iliendelea mpaka walipofika katika Hoteli ya Kilimanjaro, wakateremka na kisha kuingia ndani. Hakukuwa na wateja wengi, wale waliokuwepo, walitakiwa kubaki haohao na hata wale waliotaka kupanga hotelini, hawakuruhusiwa mpaka Latifa atakapoondoka.

    Ratiba ilikuwa imekwishapangwa, Latifa alitakiwa kukaa hapo hotelini mpaka kesho yake ambapo angechukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, huko, angefanya ziara ya kuzungukazunguka kwa wagonjwa kisha baadaye kupelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala na mwisho kabisa kuitwa katika Kituo cha Televisheni cha Global.

    Mawazo juu ya Dominick hayakuisha, picha ya mtu huyo ilikuwa ikimjia kichwani, alimpenda mno, hakutaka kumwambia ukweli kwani alikumbuka maneno aliyomwambia nchini Senegal kwamba asije siku akamwambia kwamba alikuwa akimpenda.

    Usiku ulikuwa mrefu, alibaki akiwa amekumbatia mto tu huku mwili wake ukianza kumtetemeka, hakuwa na hamu ya kuwa na mwanaume mwingine, aliyekuwa akimtaka kipindi hicho alikuwa Dominick tu.

    Baada ya kukaa mpaka saa saba usiku, Latifa akashindwa kuvumilia, alichokifanya ni kuchukua simu yake na kwenda sehemu ya majina, akaanza kulitafuta jina la Dominick.

    “Mungu! Naomba anielewe,” alisema Latifa.

    Alipoliona jina la Dominick, hapohapo akapiga namba hiyo na simu kuanza kuita. Wakati ikiwa inaita, mwili wake ukaanza kumtetemeka, japokuwa kulikuwa na kiyoyozi kilichokuwa kikifanya kazi lakini kijasho chembemba kikaanza kumtoka.

    “Hallo!” aliita Dominick kwenye simu.

    “Hallo Dominick, naomba uje chumbani,” alisema Latifa kwa sauti ndogo.

    “Kuna nini?”

    “Wewe njoo tu!”

    “Kuna amani lakini?”

    “Ipo, tena nyingi tu, naomba uje,” alisema Latifa.

    “Sawa!” alijibu Dominick na kukata simu.

    Moyo wake ukapoa, akajisikia amani moyoni mwake, muda huo, usiku huo ulitulia alikuwa akimsubiri mwanaume aliyekuwa na mapenzi naye, Dominick afike chumbani humo.

    Mara akasikia mlago ukigongwa, akashusha pumzi ndefu, akasimama na kuanza kuufuata mlango, alivalia nguo laini ya kulalia iliyoyafanya maungo yake kuonekana vilivyo, akaufuata mlango na kuufungua, alipomuona Dominick tu, mapigo ya moyo wake yakaanza kuongeza kasi, akahisi kama moyo ungeweza kuchomoka.

    “Karibu,” Latifa alimkaribishaDominick.

    “Ahsante.”

    Dominick akaingia ndani, yeye mwenyewe alichanganyikiwa, vazi alilovaa msichana huyo lilimuweka kwenye wakati mgumu, kila kitu maungoni mwake kilionekana wazi, wazimu ukampanda, kila alipojitahidi kujikaza kiume, akashindwa kabisa.

    “Umependeza,” alisema Dominick, alishindwa kuvumilia, japokuwa lilikuwa ni vazi la kulalia tu lakini akakosa maneno, akaona bora asifie hivyohivyo tu.

    “Na hili vazi?” aliuliza Latifa.

    “Ndiyo! Koh koh koh...u mzuri sana Latifa,” alisema Dominick na kujikoholesha, akili yake ilihama, alichokuwa akikifikiria ni mapenzi tu.

    “Nashukuru!”

    Latifa alifikiri kazi ingekuwa kubwa, alijipanga vilivyo lakini mara baada ya Dominick kuingia humo ndani, akagundua kwamba kazi ilikuwa nyepesi mno, hata kumsukuma mlevi katika mteremko wa mlima ilikuwa ngumu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alichokifanya Latifa ni kumsogelea Dominick pale alipokaa, kabla mwanaume huyo hajajiandaa, akashtukia akivamiwa na Latifa, mwisho wa siku wakajikuta wakiangukia kitandani, kilichoendelea, kilichotokea, hakukuwa kingine zaidi ya sauti ya kitanda na mihemo ya mahaba kusikika tu.

    Asubuhi kila mtu alikuwa hoi, hawakulala usiku kucha, walikesha huku wakibusiana huku na kule. Baada ya kuamka, ilipofika saa moja na nusu wakaletewa kifungua kinywa na kuanza kunywa.

    Walifanyiana mapenzi ya njiwa, walilishana, walibusiana na kukumbatiana, muda mwingi Dominick alikuwa akimpakata Latifa na kumbusu kadiri alivyoweza.

    “Siamini,” alisema Dominick.

    “Huamini nini?”

    “Eti na mimi nimelala na bilionea!”

    “Haha! Hebu acha maneno yako kipenzi, niite Latifa tu jamani, hilo bilionea, wala silipendi kuitwa na mtu kama wewe,” alisema Latifa kwa sauti laini, ya mahaba, yenye kumtoa nyoka pangoni, sauti iliyozitetemesha ngoma za masikio ya Dominick.

    Ilipofika saa mbili na nusu wakapigiwa simu na kuambiwa kwamba muda ulikuwa umefika hivyo walitakiwa kuanza ziara ya kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

    Wakajiandaa na walipomaliza wakatoka ndani na kuelekea mapokezi ambapo huko wakakutana na dereva wa waziri ambaye akawachukua na kuanza kwenda huko huku wakitangulizana na Waziri Kibonde ambaye walimkuta garini.

    Hawakuchukua muda mrefu, wakafika katika hospitali hiyo na moja kwa moja kuanza kile kilichokuwa kimempeleka nchini Tanzania. Kila alichokifanya, Dominick alikuwa akikichukua kwa kamera yake, bado alikuwa kwenye utengenezaji wa makala yake.

    Baada ya kuzunguka huku na kule, kuwaona wagonjwa waliokuwa wakiteseka vitandani, Latifa akatoa msaada wa kiasi cha shilingi milioni mia tano ili kisaidie katika ununuaji wa dawa na kujenga maabara nyingine hospitalini hapo. Walipomaliza, wakaelekea katika Hospitali ya Mwananyamala, huko, alifanya kama alivyofanya Muhimbili na kuahidi kutoa kiasi kama kile kwa ajili ya utengenezaji wa maabara na kunua dawa kwa ajili ya wagonjwa katika hospitali hiyo.

    “Tunashukuru kwa kila kitu. Nini kinafuata?” alisema Waziri Kibonde na kuuliza.

    “Ahsante kwa kila kitu pia, tunatakiwa kwenda kwenye Kituo cha Televisheni cha Global kwa ajili ya mahojiano, baada ya hapo, nadhani tutakwenda kupumzika,” alisema Latifa.

    “Sawa! Ila kuna kitu.”

    “Kipi?”

    “Rais amenipigia simu, amesema kwamba umealikwa ikulu kwenye chakula cha usiku na familia yako,” alisema waziri.

    “Unasemaje?”

    “Ndiyo hivyohivyo! Umealikwa.”

    “Kweli?”

    “Ndiyo!”

    “Ikulu?”

    “Hapohapo mjengoni.”

    Latifa hakuamini, kile alichokuwa ameambiwa hakutarajia kukisikia. Leo hii aliambiwa kwamba alihitajika kwenda ikulu, hakuamini, msichana aliyekulia kwenye maisha ya kimasikini, leo hii alikaribishwa ikulu, kwake ilikuwa ni faraja tele.

    “Nimefurahi, nitakuja,” alisema Latifa



    Bi Rachel alikuwa na furaha tele, kila alipomwangalia Latifa ambaye alifika nchini Tanzania kwa ajili ya ziara yake ya kuwatembelea Watanzania wengine, moyo wake ukafarijika mno.

    Kila wakati alikuwa akitazama televisheni, alimkumbuka msichana huyo, aliishi naye, yeye ndiye aliyempeleka nchini Marekani ambapo huko alisoma na binti yake, Dorcas, leo hii, yule Latifa masikini, mtoto aliyezaliwa na mwanamke mnywa gongo alikuwa maarufu duniani, tena mwenye fedha nyingi.

    Baada ya Latifa kutembelea hospitali hizo, akapigiwa simu na msichana huyo na kumwambia kwamba alitakiwa kujiandaa kwani walitakiwa kuonana katika Ofisi za Kituo cha Televisheni cha Global kwa ajili ya kuzungumza mengi.

    Bi Rachel alifurahi kusikia hivyo, akahisi kuthaminiwa zaidi ya mtu yeyote yule. Alichokifanya ni kuwasiliana na mzee Issa, na bi Semeni ambao hao ndiyo waliomlea Latifa kule Manzese, ila katika kipindi hicho, hata nao maisha yao yalikuwa mazuri hasa mara baada ya Latifa kuwa bilionea.

    Wakafika katika jengo la kituo hicho cha televisheni na kuanza kumsubiria. Wafanyakazi wa kampuni hiyo walipoambiwa kwamba watu hao waliokuja walikuwa ndegu zake na Latifa, walijisikia wivu sana kwa kuona walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na bahati kubwa maishani mwao.

    Ilipofika saa sita mchana, gari la kifahari likaanza kuingia katika eneo la kituo hicho, mlango ukafunguliwa na Latifa kuteremka, akaanza kutembea kuelekea ndani ya jengo hilo. Alipoingia ndani na kuwaona ndugu zake, kwa futaha akawakimbilia na kuwakumbatia, machozi ya furaha yakaanza kumtoka.

    “Nashukuru sana mama, nashukuru sana mama kwa msaada wako, bila wewe, nisingekuwa hapa,” alisema Latifa huku akiwa amemkumbatia bi Rachel.

    “Usijali Latifa, nilifanya yote kwa kuwa nilihisi kukusaidia,” alisema bi Rachel.

    Wafanyakazi wote waliokuwa mahali hapo wakaanza kuwaangalia watu hao, kumuona Latifa katika ofisi zao walijisikia fahari sana, wengine wakachukua nafasi hiyo kupiga naye picha na kuzirusha mitandaoni.

    Baada ya kumaliza ishu ya kupiga picha na wafanyakazi, akaitwa katika chumba kimoja ambacho kilikuwa maalumu kwa ajili ya kufanya interview ambayo ingerushwa moja kwa moja kwenye televisheni.

    “Karibu Latifa,” alikaribishwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akaanza kufanyiwa maandalizi kwa ajili ya uchukuaji video, muda huo, ndugu zake walikuwa pembeni wakifuatilia kila kitu, walionekana kuwa na furaha mno. Dominick hakuacha kuchukua kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo, bado aliendelea na mchakato wake wa kumtengenezea makala msichana huyo. Baada ya kumaliza, akaitwa mbele ya kamera na kuanza kuhojiwa.

    Latifa akaanza kusimulia historia ya maisha yake tangu alipofukuzwa mama yake ambayo historia yake alisimuliwa na mzee Issa, alisimulia kila kitu, baada ya kutimuliwa nyumbani kwa mama yake kisa alikuwa na mimba ya mtu mweusi, akakimbilia kwa mwanaume aliyempa ujauzito ule ambaye naye huyo aliamua kumtimua nyumbani kwake.

    Ilikuwa simulizi yenye kuhuzinisha, wakati mwingine alipokuwa akisimulia, alitabasamu, kuna kipindi alifika, alibubujikwa na machozi na kuendelea mbele. Hakutaka kuacha kitu, alimzungumzia Ibrahim, jinsi alivyoutesa moyo wake, alivyomuacha mbele ya msichana mmoja wa Kiarabu, aliumia, alikosa raha, akakata tamaa ya kupenda hivyo kurudi nchini Marekani.

    Alipofika huko, akasimulia kuhusu Liban, kila alipokuwa akiwazungumzia watu hao wawili, machozi yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake, aliumia mno, aliteseka moyoni mwake mpaka kipindi kingine alitamani kufa, afe ili asiweze kuteseka tena.

    “Pole sana Latifa,” alisema mtangazaji aliyekuwa akimhoji.

    “Ahsante sana, ila ni maisha, Mungu anaporuhusu jambo fulani litokee, huwa anakupa na mlango wa kutokea,” alisema msichana huyo.

    Kipindi hicho kilichukua saa moja, alipomaliza, akasimama na kumfuata mzee Issa, akamkumbatia huku akibubujikwa na machozi mashavuni mwake, alipotoka mikononi mwake, akamfuata bi Semeni na kumkumbatia pia.

    “Samahani Latifa,” alisema msichana mmoja, alikuwa mfanyakazi wa hapo.

    “Bila samahani.”

    “Kuna mtu anakuulizia hapo getini.”

    “Nani?”

    “Anaitwa Ibrahim, amesema kwamba unamfahamu,” alijibu msichana yule.

    Latifa alipolisikia jina hilo, moyo wake ukapiga paaaa, akakunja uso wa hasira, machozi yakaanza kumbubujika tena, kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma kama mkanda wa filamu.

    *****

    Kwa mara ya kwanza Kituo cha Televisheni cha Global kilitangaza kwa kusema kwamba siku ya Ijumaa kungekuwa na mahojiano maalumu na msichana bilionea mwenye asili ya Kitanzania ambaye alikuwa akiishi nchini Marekani, Latifa Issa kama alivyojulikana.

    Kila mtu akatamani kukiangalia kipindi hicho kilichotarajia kuruka majira ya saa tisa alasiri. Watu wakaambiana, wakasambaziana taarifa kwamba msichana huyo bilionea, aliyeleta tumaini kubwa duniani hasa kwa wagonjwa wa kansa angehojiwa moja kwa moja kwenye televisheni.

    Kila mtu alitaka kumsikiliza, kila mtu alitaka kusikia historia ya maisha yake kwamba alianzia wapi, alipitia wapi na wapi mpaka kuwa vile alivyokuwa kipindi hicho. Kila kona, stori ilikuwa moja tu kuhusu Latifa, matangazo yakatangazwa sana, watu wakashikwa na hamu kubwa ya kumsikiliza msichana huyo mrembo.

    Kati ya watu waliokuwa na hamu ya kumsikiliza Latifa alikuwa Ibrahim, alijua kwamba angeumia hasa mara baada ya kumsikia msichana huyo akizungumzia kile kilichopita, hakutaka kujali sana, alichoamua kipindi hicho ni kumsikiliza tu.

    Kwa kuwa alikuwa amekwishamwambia mzee Deo kuhusu Latifa, alichokifanya ni kumwambia kwamba msichana yule aliyekuwa amemkataa alitarajiwa kuhojiwa katika televisheni, hivyo akawa na hamu ya kutaka kumuona.

    Siku hiyo ambayo ndiyo ilitakiwa kuonyeshwa kwa kipindi hicho, Ibrahim akaamua kumchukua mzee huyo na kumpeleka nyumbani kwake, hakumuhofia mke wake, alijua kwamba mwanamke huyo alikuwa mkorofi lakini kwenye suala la Latifa, hakutaka kusikia chochote kile.

    “Umemleta kufanya nini humu?” aliuliza Nusrat huku akionekana kuwa na hasira, mbaya zaidi akaziba hata pua yake kumaanisha kwamba alikuwa akisikia harufu mbaya.

    “Nimemleta, nataka kumuonyeshea yule msichana aliyenipenda, nikaamua kumuacha kwa ajili yako shetani,” alisema Ibrahim kwa kiburi.

    “Ndani ya nyumba yangu?”

    “Wewe mjinga nini, hebu tupishe, na ole wako ulete za kuleta, ndugu zako watakuta maiti tu humu ndani,” alisema Ibrahim, hata Nusrat alipomwangalia mumewe, alijua kwamba siku hiyo alikuwa tofauti, kama ni ng’ombe basi aliota mapembe.

    Ibrahim akamchukua mzee Deo na kwenda kutulia naye kochini, akachukua rimoti ya televisheni na kisha kuiawasha. Mzee Deo alikaa kitini, hakujisikia kuangalia, hakuwa na amani kabisa kwani jinsi alivyokuwa akimwangalia Nusrat ambaye alikaa pembeni kabisa, alionekana kuwa na hasira mno.

    Latifa alivyoonyeshwa kwenye televisheni, Ibrahim akajikuta akianza kububujikwa na machozi, moyo wake uliumia, kila alipokuwa akimwangalia msichana yule, akagundua kwamba aliitupa almasi jangwani na kuokota bati.

    Msichana huyo mrembo, mwenye muonekano wa fedha akaanza kusimulia historia ya maisha yake. Kila mmoja akabaki kimya akimsikiliza, alianza kusimulia kuanzia mbali, tangu mama yake alipofukuzwa nyumbani kwao, alipokwenda nyumbani kwa mpenzi wake, Deo kisha kumfukuza, alionekana kuumia mno.

    Mzee Deo aliposikia historia aliyokuwa akiisimulia Latifa, akashtuka, akaanza kumwangalia Latifa, akasimama kutoka katika kochi lile na kuisogelea televisheni, kila mmoja mule ndani akabaki akimshangaa.

    “Ibrahim....” aliita mzee Deo, machozi yakaanza kumtoka.

    “Nipo mzee....”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Latifa ni binti yangu!” alisema mzee Deo huku akionekana kushangaa, Ibrahim akashtuka, si yeye tu, hata Nusratakashtuka.

    “Unasemaje?”

    “Kumbe Latifa ndiye mtoto wangu aliyezaliwa na Nahra,” alisema mzee Deo.

    Hapo ndipo Ibrahim alipoanza kukumbuka mahojiano yale, alikumbuka Latifa alimtaja mtu aliyeitwa Nahra na Deo, wazazi wake waliokuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi mpaka baba yake alipomfukuza mama yake.

    Mahojiano yale akayaunganisha na historia aliyowahi kusimuliwa na mzee huyo kwamba zamani alikuwa na mwanamke wa Kihindi, alimpa ujauzito lakini baadaye akafukuzwa nyumbani kwao, na alipokuja kwake, naye alimfukuza ila ni kwa sababu tu alitishiwa kuuawa na ndugu zake Nahra kwa kutumiwa watu waliokuwa na bunduki, na kama asingemfukuza basi angeuawa yeye.

    “Ni mtoto wangu! Kumbe Latifa ni mtoto wangu!” alisema mzee Deo huku akijifuta machozi.

    Ibrahim alishindwa kuamini, wakati mwingine alifikiri kwamba alikuwa ndotoni, katika kipindi chote alichokuwa akiishi na huyo mzee, alivyokuwa akizungumza naye kumbe alikuwa mzazi wa msichana aliyekuwa amemuacha, Latifa.

    Latifa hakuwa na kipindi kirefu katika kituo kile, alichokifanya Ibrahim ni kumwambia kwamba ilikuwa ni lazima kumfuata Latifa huko na kumwambia ukweli kwamba alikuwa na baba yake nyumbani kwake.

    “Ngoja nikamlete uzungumze naye,” alisema Latifa.

    “Atakubali kuja?”

    “Atakuja tu. Subiri,” alisema Ibrahim huku akionekana kuchanganyikiwa, hakutaka kuchelewa, akaondoka kuelekea huko, tena alikuwa akikimbia kwa kasi ajabu.



    Jina la Ibrahim lilimchanganya, hakuamini kama kweli aliitwa na msichana yule kwa kuwa alikuwa akihitajika na mtu aliyejitambulisha kwa jina hilo. Huku akionekana kuwa na hasira, akatoka pamoja na ndugu zake kuonana na huyo mtu.

    Alipofika, alipomwangalia Ibrahim, akajikuta akiingiwa na huruma, aliyesimama mbele yake alikuwa Ibrahim, yuleyule kijana aliyekuwa amemtesa na kumkataa kipindi cha nyuma, ila hali aliyokuwa nayo, ilimtia huruma mno.

    “Ibarhim,” alijikuta akimuita kijana huyo aliyeonekana kupigwa na maisha.

    “Latifa...” aliita Ibrahim, tayari machozi yakaanza kumbubujika, hata naye kumbukumbu za nyuma zikaanza kujirudia kichwani mwake.

    “Umefuata nini?” aliuliza Latifa huku akiwa amesiamam.

    “Kwanza naomba unisamehe kwa yote yaliyotokea, dunia imeniadhibu kwa kile nilichokufanyia,” alisema Ibrahim.

    Japokuwa alijiahidi kwamba asingeweza kumsamehe mwanaume huyo lakini hakuwa na jinsi, kwa namna ambavyo alionekana mahali hapo, ilionyesha kabisa kwamba maisha yalimpiga, hivyo hakutaka kumwadhibu tena, alichokifanya ni kuukunjua moyo wake na kumsamehe kwa kila kitu kilichotokea.

    “Nimekusamehe Ibrahim, dunia imekufunza,” alisema Latifa.

    “Kuna kitu ninahitaji kutoka kwako.”

    “Kitu gani?”

    “Baba yako anateseka Latifa, kila ulichoambiwa ni kweli kilitokea, ila naye ana historia ya tofauti na hiyo uliyokuwa nayo,” alisema Ibrahim, alikuwa amemsogelea kidogo, kila mtu akashtuka.

    “Baba yangu?”

    “Ndiyo!”

    “Nani?”

    “Mzee Deo!”

    “Hapana! Baba yangu kashakufa!”

    “Una uhakika? Ulionyeshewa kaburi lake? Au hata picha yake unayo”

    “Ibrahim, baba yangu! Haiwezekani!”

    “Latifa, huu ndiyo muda wa kuusikia ukweli, twende ukamuone baba yako, ameteseka sana, kansa ya mguu ilisababisha kukatwa mguu wake, twende ukamuone, atafurahi kama akikuona,” alisema Ibrahim.

    “Baba yangu......” alisema Latifa, sauti ya kilio chake ikaanza kusikika.

    “Ni kweli, yupo hai, hana pa kuishi, amekuwa akiteseka miaka yote, alikuwa ombaomba mitaani, alifukuzwa kila sehemu. Nimekuwa nikiishi naye kwa kipindi kirefu pasipo kujua kwamba ni baba yako, historia aliyonisimulia, ni hiyohiyo ambayo umesimulia japokuwa kuna kitu ambacho haukukifahamu, si wewe tu bali hata marehemu mama yako hakukifahamu, nimemsaidia sana mpaka kufikia kipindi hiki. Naomba twende ukamuone, tuwahi, namjua mke wangu, anaweza hata kumuua,” alisema Ibrahim.

    “Kumuua! Amuue baba yangu!”

    “Ni mwanamke mwenye roho mbaya! Twende Latifa,” alisema Ibrahim, hawakutaka kusubiri, waliposikia kwamba mke wa Ibrahim angeweza kumuua mzee Deo, wote wakaingia ndani ya gari na kuanza kuelekea huko.

    Garini, bado Ibrahim aliendelea kumuomba msamaha msichana huyo, alijutia matendo aliyoyafanya, hakuomba msamaha kwa kuwa Latifa alikuwa msichana bilionea, aliomba msamaha kwa kuwa alihitaji kusamehewa kwa yote aliyoyafanya.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ibrahi...nime...kus...ame..he..” alisema Latifa huku akilia.

    Walichukua dakika kumi njiani ndipo walipofika alipokuwa akiishi Ibrahim. Kwa kuwa nyumba ilizungushiwa ukuta huku ikiwa na geti kubwa, Ibrahim akateremka na kwenda kulifungua geti lile ili gari liingizwe ndani.

    Kitu cha ajabu alipofika katika eneo la nyumba hiyo, akapiga uyowe mkubwa, mbele yake alikuwepo mzee Deo, alikuwa hoi chini, kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, muda huo napo damu zilikuwa zikimtoka katika kipande cha mguu wake, Nusrat alikuwa amemtoa ndani ya nyumba yake.

    Latifa na watu wengine waliposikia uyowe huo, wakahomoka kutoka garini, wakajua kwamba kulikuwa na kitu ndani ya nyumba hiyo, walipolifungua geti dogo na kuingia ndani, wakamkuta Ibrahim akiwa amemshika mzee Deo aliyekuwa chini huku akilia, mzee huyo alikuwa hoi, damu ziliendelea kumtoka katika kipande chake cha mguu na alikuwa akilia kwa maumivu makali.

    Wote wakamfuata, kila mtu aliyemwangalia, sura yake ilifanana na Latifa kwa mbali, hakukuwa na mtu aliyekuwa na ubishi kwamba mzee yule alikuwa mzazi wa Latifa.

    Latifa akajikuta akianza kulia, hasira ikamkaba kooni dhidi ya Nusrat, alionekana kuwa na hasira mno.

    “Hanijui, yaani pamoja na kuniumiza bado ananiumizia baba yangu! Atanitambua mimi ni nani,” alisema Latifa huku kwa kumwangalia tu ungegundua ni jinsi gani alikuwa na hasira.

    Walichokifanya ni kumchukua na kumpeleka hospitalini huku Latifa akiahidi kwamba ni lazima angemuonyesha Nusrat yeye alikuwa nani.

    ****

    Latifa alikuwa akilia tu, kila alipomwangalia baba yake, moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama alikuwa kwenye hali ile. Watu wengine walimbembeleza anyamaze lakini hakunyamaza, hasira kali dhidi ya Nusrat ilimkamata mpaka kufikia kiasi cha kukunya ngumi.

    Kitendo cha kupigwa baba yake na kuumizwa namna ile kulimuongezea hasira ya kumchukia Nusrat ambaye miaka michache nyuma alimuumiza kwa kumchukulia mwanaume wake, hakuonekana kuridhika, leo hii alimpigia baba yake.

    “Nitamuonyesha,” alisema Latifa huku akionekana kuwa na hasira kali.

    Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Japokuwa kipindi cha nyuma alisema kwamba baba yake alikuwa miongoni mwa watu aliokuwa akiwachukia kwa kuwa tu alkimfukuza mama yake lakini wakati alipokuwa akimwangalia, mateso aliyoyapata, chuki yote dhidi yake aliyokuwa nayo ikaondoka na huruma kumuingia.

    Manesi waliokuwa na machela wakasogea lilipokuwa gari lile na kumpajndisha mzee Deo juu ya machela ile na kuanza kusukumwa kwenda kwenye chumba kimoja kilichoandikwa Theatre. Walipofika nje ya chumba kile, wakazuiliwa.

    Watu waliokuwa wamegundua kwamba msichana aliyekuwa mbele yao alikuwa Latifa walibaki wakishangaa, hawakuamini kama kweli yule aliyesimama mbele yao alikuwa ndiye au alikuwa msichana mwingine aliyefanana naye.

    “Inawezekana ndiyo yeye,” alisema jamaa mmoja huku akimwangalia Latifa ambaye machozi yalikuwa yakimbubujika tu.

    “Labda! Ila awe hapa anafanya nini?”

    “Sijui, hebu tusogee karibu zaidi tumuone.”

    Kila aliyepita, hakuacha kumshangaa Latifa aliyekuwa akilia tu. Ibrahim alikuwa kimya, moyo wake ulimuuma, alimzoea sana mzee Deo, alikuwa rafiki yake mkubwa, alimpenda pasipo kujua kwamba mzee huyo alikuwa mzazi wa msichana aliyemuacha kipindi cha nyuma, Latifa.

    Madaktari wakawa wanapishana mlangoni, wengine waliingia na wengine kutoka. Mgonjwa aliyeletwa kwao alionekana kuwa wa maana sana, ilikuwa ni bora kuleta utani kwa mgonjwa mwingine lakini baba yake Latifa.

    Baada ya msaa mawili, mlango ukafunguliwa na daktari kutoka, akawaita watu hao ofisini kwake kwa lengo la kuzungumza nao. Walipofika huko, akawaweka chini.

    “Hali ya mgonjwa si mbaya, alitoneshwa tu kidonda chake,” alisema Dk. Mimi, mwanamke mzuri mwenye umbo la kuvutia.

    “Ila ninataka kuzungumza naye, naweza kufanya hivyo?”

    “Hakuna tatizo, unaweza ila kama baada ya saa moja hivi, atahitaji muda wa kupumzika,” alisema Dk. Mimi.

    “Sawa!”

    Kusubiri halikuwa tatizo kabisa, alitaka kumsikia baba yake akizungumza kile alichokuwa akitaka kuzungumza. Alitaka kusikia kile ambacho hakuwa amekisikia kuhusu mama yake, kile alichosema Ibrahim kwamba mzee huyo alikuwa na la ziada.

    “Nyamaza Latifa,” alisema Dominick huku akimvuta Latifa upande wake.

    Walitulia kwa muda wa saa moja na ndipo walipoambiwa kwamba wangeweza kumuona mgonjwa wao. Wakainuka na kuingia ndani. Latifa alipomuona baba yake kitandani pale, uso wake ukajawa na tabasamu pana na kuanza kumsogelea.

    Moyo wake ukaingiwa na hisia kali, ukapatwa na furaha kubwa kiasi kwamba alishindwa kuliuia tabasamu lake kutawala usoni mwake.

    “Baba...”

    “Naam mwanangu.”

    “Nini kilitokea?”

    “Maisha, maisha yalinipiga na ndiyo maana nipo hivi,” alijibu mzee Deo.

    Latifa akanyamaza, akamsogelea baba yake kitandani pale na kumbusu katika shavu la uso huku machozi ya furaha yakimbubujika mashavuni mwake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Umefanana sana na mama yako,” alisema mzee Deo.

    “Nani? Mimi?”

    “Ndiyo! Mama yako alikuwa mrembo kama ulivyo,” alisema mzee Deo.

    “Sasa kwa nini ulimfukuza wakati alipokuwa na mimba yako?”

    “Nilimpenda sana mama yako, nilijitolea kwa kila kitu, nilitaka niishi naye japokuwa nyumbani kwao hawakuwa wakinipenda kisa tu nilikuwa mtu mweusi. Alipofukuzwa kwao, akakosa pa kwenda, alichoamua ni kuja nyumbani kwangu.

    “Hata kabla hajafika, tayari wazazi wake waliwatuma watu wawili, walikuja huku wakiwa na bunduki, waliniambia kwamba endapo ningempokea mama yako na kuishi naye, hakika wangeniua, na waliniambia kabisa kwamba walitumwa na wazazi wake,” alisema mzee Deo na kuendelea:

    “Niliogopa sana, niliona kweli ningeuawa, nilichokifanya ni kumfukuza Nahra huku nikiumia moyoni. Sikufanya vile kwa kuwa sikuwa nikimpenda, la hasha! Nilifanya vile kwa kuwa nyuma yangu niliwekewa bunduki. Alipoondoka, sikukaa nyumbani, niliondoka kwenda kumtafuta, usiku mzima nilimtafuta kila kona, ila sikufanikiwa kumpata, huo ukawa mwisho wa kuonana naye,” alisema mzee Deo, tayari naye machozi yalianza kumbubujika.

    Watu wote waliokuwa mahali pale walikuwa kimya wakimsikiliza, mzee huyo alitia huruma kitandani pale, alionekana kukosa nguvu na alikuwa mtu aliyekosa tumaini kabisa.

    “Nisamehe Latifa,” alisema mzee Deo.

    “Nimekusamehe baba! Kila kitu kilichopita, kimepita, ni lazima tugange yajayo,” alisema Latifa, hapohapo akayapeleka macho yake usoni mwa Ibrahim aliyekuwa kimya.

    “Ulimfahamu vipi Ibrahim?”

    “Ni mtu ambaye amenisaidia sana, bila yeye nafikiri leo hii nisingekutana na wewe. Alinionyeshea upendo mkubwa sana, sikuamini kama kuna watu wenye roho nzuri kama alivyokuwa yeye. Nimekuwa naye kipindi chote, nilipopata tatizo, alinisaidia kwa fedha kidogo aliyokuwa nayo.

    “Hakujua kama mimi ni baba yako, alinionyeshea upendo kwa kuwa aliona nastahili kufanyiwa hivyo japokuwa mke wake alikuwa ni tatizo kubwa. Binti yangu! Ibrahim alinihadithia kila kitu kuhusu wewe hata kabla hajajua kama mimi ni mzazi wako, naomba umsamehe, inawezekana mambo yote anayopitia, shida zote anazozipata ni kwa ajili ya laana yako, msamehe na sahau kila kitu,” alisema mzee Deo.

    Latifa akayapeleka tena macho yake kwa Ibrahim, alipanga kutokusamehe katika maisha yake lakini kila alipokuwa akimwangalia, bado mwanaume huyo alionekana kuhitaji msamaha.

    Alionekana kupigika katika maisha yake, alitia huruma lakini pamoja na hayo yote, alifanya kazi kubwa sana kumlea baba yake. Hakuwa na fedha za kutosha lakini nkiasi hichohicho kidogo alikitumia kwa ajili ya kumtibu baba yake, hakika alifganya jambo kubwa lililohitaji sifa kubwa kutoka kwake.

    Hakuongea kitu, alichokifanya ni kumsogelea na kumkumbatia. Wote wawili walikuwa wakibubujikwa na machozi. Latifa hakuwa na jinsi, aliukana moyo wake na kumsamehe mwanaume huyo aliyeonekana kuhitaji sana msamaha.

    “Nisamehe Latifa.”

    “Nimekusamehe Ibrahim, Ahsante kwa yote uliyomfanyia baba yangu,” alisema Latifa huku akijifuta machozi.

    “Naomba umsamehe Nusrat pia! Ni mwanamke mpumbavu asiyejua lile analolifanya. Naomba umsamehe.”

    “Nimsamehe Nusrat?”

    “Ndiyo!”

    “Kwa hivi alivyomfanyia baba yangu?”

    “Latifa! Hebu sahau kwanza. Wewe ni mtu mkubwa na mwenye heshima, tazama dunia nzima inakutazama wewe, usiposamehe, vipi wale vijana wanaotaka kuwa kama wewe? Nao watakapokosewa hawatakiwi kukosea kisa wewe haukusamehe? Vipi kuhusu wale watoto wanaotaka kuwa kama Latifa, kweli nao hawatakiwi kusamehe? Samahe saba mara sabini, au umesahau hilo?” aliuliza Ibrahim.

    “Nakumbuka.”

    “Basi naomba umsamehe!”

    “Nimemsamehe!”

    “Nashukuru!”

    Huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha mapya, Latifa hakuwa na kinyongo, moyo wake ulilainika na hakutaka kuwa na kingo na mtu yeyote yule, alichokiamua ni kumsahmehe kila mtu aliyewahi kumfanyia ubaya kwa makusudi au bahati mbaya.

    Alikuwa mtu mwenye mafanikio, bilionea, alichokifanya ni kumsafirisha baba yake nchini Marekani, alitaka akatibiwe huko na kuishi naye hukohuko. Kwa Ibrahim, japokuwa alimfanyia mambo mabaya nyuma hakutaka kumuacha hivihivi, aliamua kumsaidia kama alivyomsaidia baba yake.

    Akamnunulia nyumba kubwa Mbezi Beach na kumgawia kiasi cha shilingi milioni mia tatu kwa ajili ya kufanya biashara zake kitu ambacho kwa Ibrahim kilikuwa kitu kikubwa, baada ya wiki moja, akaamua kumpa talaka Nusrat na kumuoa mwanamke mwingine na kuishi naye nyumbani kwake huku akifungua biashara kubwa.

    Kwa Latifa, akaamua kufunga ndoa ya kishria Dominick na watu hao kuishi pamoja kwa amani ni na upendo ambapo baada ya miaka miwili, wakafanikiwa kupata mtoto wa kiume waliyemuita kwa jina la Godlove.

    Dawa yake ya kansa ya Morphimousis iliendelea kutikisa duniani, watu waliokuwa na magonjwa ya aina hiyo waliendelea kutibiwa na kupona. Aliendelea kuingiza kiasi kikubwa cha fedha, utajiri wake ukazidi kuongezeka maradufu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya miaka mitano kupita, wakapata mtoto wa pili wa kike waliyempa jina la Cecilia. Latifa alikuwa na furaha tele, moyo wake ulikuwa na amani, hakuwa na kinyongo na mtu yeyote, maisha yake yalikuwa ya furaha tele.



    MWISHO....



    Nashukuruni sana kwa kuifuatilia simulizi hii. Mungu awabariki.


0 comments:

Post a Comment

Blog