Simulizi : Mvua Ya Huba
Sehemu Ya Pili (2)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baraza likawa kimya kwa muda kila mmoja akitafakari ni kwa namna gani anaweza kutoa wazo litalosaidia katika kuokoa maisha ya Chifu. Mtoto wa kwanza wa chifu ambaye alikuwa eneo hilo akasimama na kusogea hadi alipo mama yake, akainamisha kichwa chake ishara ya kutoa heshima kisha akawatazama wazee waliokusanyika mahala hapo, akakohoa kidogo na kuanza kuongea,
“Sioni haja ya sisi kuumiza sana kichwa, Mwenda ni raia mtiifu na mzalendo katika Sanzani yetu hivyo basi napendekeza aungane na mtukufu chifu katika ndoa takatifu ili aweze kumtibu”
Balaza la wazee likaridhia hilo bila pingamizi lolote, Malkia akapendekeza siku iliyofuata saa tisa alasiri kuwa mahususi kwa ajili ya ndoa hiyo.
**************************
Taarifa zikasambaa kwa watu wote wa Sanzani, mama yake Mwenda alifurahi mno kusikia mwanae anatakiwa kuwa mke wa kumi na nne wa chifu Lukemo. Kwake ilikuwa ni heshima kubwa ambayo hakuwahi kuifikilia, akaridhia bila kipingamizi na kuhaidi kutoa ushirikiano wake wakati wowote.
Mwenda hakujua lolote linaloendelea nje ya chumba alichofungiwa, baada ya kitambo kidogo kupita Lukoha akafungua mlango kisha akainamisha kichwa kutoa heshima zake kwa Mwenda. Jambo hilo likamshtua sana Mwenda hakujua lina maana gani,
“Nitakusindikiza hadi nyumbani kwenu na mengine utayajua ukifika huko” alisema Lukoha.
Mwenda alifurahi mno kuongozana na mwanaume yule ambaye kwa kiasi kikubwa aliuteka moyo wake, walipofika nje Mwenda akaona punda aliwekwa nakshi mbalimbali amesimama. Lukoha akamuashiria Mwenda kupanda yule punda kisha taratibu safari ya kurejea nyumbani kwao ikaanza.
“Sikupata muda mwingi wa kuwa karibu na Lucas katika dunia ile, akhsante Mungu kwa kunileta huku ninafuraha sasa” alisema Mwenda kwa sauti ya chini ambayo haikusikika popote.
Kwa mara ya kwanza msichana huyo akajikuta akitoa shukrani toka alipokumbwa na maswahibu ya kufiwa na mume wake katika ile dunia nyingine. Hakutamani kurejea kule tena, akatamani abaki karibu na Lukoha mwanaume aliyeshahabiana na mumewe kwa kila kitu na aliamini kuwa huyo ndiye wake.
Safari iliendelea hatimaye wakawasili nyumbani kwa kina Mwenda, mazingira hayakuwa kama vile alivyoyaacha watu walionekana wengi kuliko kawaida. Maswali mengi yakaanza kutiririka kichwani mwake hasiyapatie majibu kwa wakati huo.
Mama yake alipomuona bintiye amewasili akasogea kumlaki kwa nderemo na vifijo, wanawake waliokuwa eneo hilo nao wakaungana na mama Mwenda katika kumlaki binti yake. Nyimbo mbalimbali zikaimbwa na kwa heshima kubwa wanawake wakajilaza chini na kumtaka Mwenda apite juu ya migongo yao. Hali hiyo ikamchukiza Zaidi Mwenda ambaye bado alikuwa kwenye kiza kinene asiweze kudadavua japo kwa kinaga ubaga juu ya hayo yanayoendelea.
“Hongera mwanangu..! Hongera mwanangu….! Umekuwa sasa!” alisema mama Mwenda kwa furaha tele.
“Mama haya yote yana maana gani?” aliuliza Mwenda.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Swali lile likamfanya mama Mwenda aduwae kwa sekunde kadhaa, hakujua kama mwanae hajui lolote, akamtazama kisha akacheka kwa nguvu. Watu wote wakaendelea kushangilia kwa vigelegele na makofi. Hali hiyo ikamfanya Mwenda achukie Zaidi, akageuka nyuma kumtazama Lukoha lakini hakumuona, akaangaza huku na huko lakini hakupata kumtia machoni. Mwenda akarudi nyuma kwa haraka ili amatazame nje ya ua lakini kabla hajafika popote akazuiliwa,
“Mwenda mwanangu wewe ni nuru mpya ya Sanzani kwa sasa huruhusiwi kufanya lolote hadi ndoa yako itakapopita” alisema mama yake Mwenda.
“Mhmhm! Mama ndoa gani unayoimaanisha?” aliuliza mwenda kwa mshangao mkubwa.
“Mwanangu kesho majira ya alasiri utaungana na chifu Lukemo katika ndoa takatifu na baada ya hapo utakuwa na jukumu jipya la kumuhudumia mumeo”
“Mhmh! Mama unamaanisha kwamba mimi natakiwa niwe mke wa 14 wa chifu”
“Ndio mwanangu hii ni bahati ambayo wasichana wengi wa rika lako uitamani bila mafanikio” alisema mama yake Mwenda.
“Mama unawezaje kukubali mimi niolewe na mwanaume ambaye sijawahi kumfikilia akilini mwangu isitoshe yule ni kama baba au babu yangu, siwezi kuolewa nawe”.
Kauli hiyo ikamfanya mama yake akae chini na kupiga piga ardhi huku akisota kwenda upande mmoja hadi mwingine,
“Baba Mwenda wee! Unayashuhudia haya kweli mwanao anayonifanyia mimi, uwii mtoto huyu kweli wangu” alisema mama Mwenda huku machozi yakianza kumtiririka.
Kwa desturi za watu wa Sanzani msichana aliyechaguliwa kuungana na chifu katika ndoa ni sawa na Baraka kuu kwa familia hiyo na kaya nyingine jirani. Kitendo cha kukataa ni sawa na kuikatalia mizimu ambayo wamekuwa wakiiamini mihongo kwa mihongo, karne kwa karne toka enzi za mababu waliopita na kuanzisha desturi hizo. Adhabu yake huwa ni kifo si kwa binti pekee bali ukoo mzima, swala hili likamfanya mama yake Mwenda ahisi kama yupo katikati ya ndoto aitake kusadiki kile anachokisikia toka kwa mwanae.
“Wewe Mwenda nafikiri hujui unalotaka kufanya labda tu nikuonye kama mama yako anakuchekea mimi sina mzaha hata kidogo, hatutaki mkosi kwenye ukoo wetu wewe utaolewa utake usitake” aliongea mwanamke mmoja ambaye mwenda hakuwa akimfahamu.
“mhmh! Wewe ni nani hasa hata kuwa na haki juu ya maamuzi yangu?” aliuliza Mwenda.
Watu wote walistahajabishwa na swali hilo, hakuna aliyesadiki kuwa kweli mwenda haelewi au anafanya makusudi. Bila kupata majibu ya kuridhisha mwenda akashikwa na wanawake waliokuwa na nguvu na kumfungia ndani. Taratibu nyingine zikaendelea kama zilivyopangwa.
“Mama mwenda wala usiwaze sana kuhusu haya si unajua bado binti yako kumbukumbu hazijakaa sawa, mimi naamini kadri muda unavyozidi kwenda atagundua makosa yake”
Maneno yale yakamfariji sana mama Mwenda aliyeanza kupoteza tumaini juu ya bintiye. Akarejea walipo wenzake na waendelea na taratibu nyingine za kimila.
***********
Hayawi hayawi sasa yamekuwa lile jambo lililokuwa likisubiliwa kwa hamu limewadiwa, watu wote wa sanzani wakakusanyika katika uwanja mkubwa kushuhudia tukio la Mwenda kufunga ndoa na chifu ambaye kwa Muda huo alikuwa na hali mbaya kiasi cha kutoelewa nini kinaendelea.
“Ndugu zangu wa Sanzani muda mfupi ujao tutaanza kufanya ibada ya kuiomba mizimu iridhie muungano kati ya Mwenda binti Magari na chifu wetu mtukufu Lukemo, kutokana na chifu kutojisikia vizuri jukumu lake litachukuliwa na mzaliwa wake wa kwanza,” alisema mzee mmoja ambaye ndiye mkuu wa mila na ibada zote za mizimu ya Sanzani.
Mtoto wa chifu akajongea mbele ya madhabahu iliyotahayarishwa mahususi kwa ajili ya tukio hilo na akaketi kumsubili Mwenda. Muda mfupi baadae Mwenda akisindikizwa na mama yake pamoja na ndugu zake wengine wakawa tayari eneo hilo shangwe nyingi zikaanza tarumbeta ikapulizwa kila mmoja akasimama. Machozi yakambubujika Mwenda kwani hakuitamani ile ndoa, akafikiri afanye nini mbele ya jamii ile iliyokusanyika kushuhudia tukio lile la kihistoria. Kwa mara nyingine tena akainua macho yake angani na kusema.
“eenh! Mungu najua sistahili kusema haya ninayotaka kusema, nimekukosea sana, pamoja na hayo yote mimi bado ni mtoto wako naomba niepushe na hili sitoliweza hakika”
Alipomaliza kutamka hayo akajikuta yupo uso kwa uso na mtoto wa chifu aliyefahamika kwa jina la Ng’arika, Mwenda aliduwaa sana kumuona Ng’arika kwani sura ile haikuwa ngeni machoni pake. Akavuta kumbukumbu ili ajue ni wapi hasa alipomuona huyo mwanaume aliyesimama mbele yake, kumbukumbu zikamchukua hadi siku ya harusi yake akakumbuka kuwa ni mmoja kati ya watu waliokuwa kitengo kimoja na mumewe Lucas. Maswali mengi yakazidi kutiririka kichwani mwake asipate kujibiwa.
“Mwenda utaunganishwa na chifu kupitia uzao wake wa kwanza ambao ndio huo uliosimama mbele yako,” alisema kiongozi wa ibada.
Mwenda akawa bado hasadiki akatamani kusema jambo lakini akashindwa, akageuza shingo yake kuangaza watu waliopo mahali pale akashangaa kumuona Lukoha akiwa ameinamisha kichwa chake asiweze kumtazama. Mwenda alichukia mno, akaendelea kuongea na Mungu wake kwa sauti ya chini,
“Haya yote yana umuhimu gani? Mbona mtu mwenyewe anikumbuki? Mungu mbona ni mimi tu kila wakati”
Kabla hajaendelea kuongea Zaidi, muongozaji wa ibada akamtaka mwenda asogee na kuketi mkabala na Ng’arika, mwenda akafanya hivyo. Muda ukawadia na ibada ikaanza, wakati huo hali ya hewa nayo ikabadirika wingu zito likatanda, mvua nyepesi ikaanza kunyesha na kufanya watu wa Sanzani washangilie wakiamini kuwa tukio hilo limeridhiwa na mizimu. Ukafika wakati wa kuwaunganisha wawili wale, ubani ukachomwa, muongozaji wa ibada akawataka Ng’arika na Mwenda wasimame nao wakatii, akawashikisha mikono ishara ya kuwaunganisha papo hapo Mwenda akakumbuka alivyounganishwa na mumewe katika dunia ile ya mwaka 2017. Machozi yakamtoka akiamini kuwa kila kitu kimefikia hatamu, akageuza shingo yake kumtazama Lukoha akakuta naye akimtazama huku uso wake ukionesha kufadhaika mno kiasi kwamba chozi likamtiririka pasi na mwenyewe kuelewa. Tukio hilo likamuachia maswali mengi Mwenda, kwa mbali akasikia akiitwa,
“Lucy….! Lucy….! Lucy….! Lucy….!”
Mwenda alishangaa kusikia jina lile katika dunia ile, akaangaza huku na huko kumtafuta mtu anayemuita lakini asimuone na kadri mshale wa sekunde ulivyozidi kusogea ndivyo sauti ile ilivyozidi kuongezeka kiasi cha kumuumiza masikio. Watu waliojumuika kushuhudia harusi ile wakamshangaa mwenda wasijue amekumbwa na nini. Ng’arika akamsogelea Mwenda na kutaka kumshika mkono lakini kabla hilo alijatimia Mwenda akaanguka na kupoteza fahamu.
Kadamnasi yote ikasimama kwa tahayaruki kwani ni aghalabu mno kwa tukio lile kutokea hasa kwa siku ya furaha kama ile. Kiongozi wa ibada akawataka watu watulie kwani kila kitu hutokea kwa mapenzi na matakwa ya mizimu, hivyo lazima kutakuwa na sababu hata kwa lile lililotokea. Mwenda akabebwa kwa haraka na kupelekwa kwa tabibu wa chifu.
**************************
Mwenda anafumbua macho yake na kujikuta yupo katika chumba ambacho hakukielewa, akaendelea kudadisi walau atambue ni wapi hasa alipo lakini asifanikiwe, akatazama mikono yake akakuta ametundikiwa dripu ya maji, alihisi shida kidogo katika upumuaji wake na alipojichunguza akakuta amewekewa mashine ya kupumulia. Tukio la mwisho katika kumbukumbu zake ni siku ya harusi na akaikumbuka sauti iliyokuwa ikimuita na baada ya hapo hakujua kilichoendelea.
“Mhmh! Nilipoteza fahamu ila hivi vitu vyote vimetokea wapi? Sanzani haina hospitali wala vifaa tiba” alijiuliza Lucy.
Alipoendelea kutazama akagundua kuwa yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi, akaendelea kutafakari na kujiuliza Zaidi.
“Bila shaka hii ni dunia ile niliyeizoea mimi, ila hii ndoto au nimerejea kweli mahala nilipopazoea”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati akiendelea kutafakari hayo akaona mlango ukifunguliwa akaamua kufumba macho yake ili ajue nini kitafanyika. Akiwa amefumba macho akaisikia sauti ya mama yake,
“Lucy mwanangu najua ipo siku utainuka katika kitanda hiki cha maudhi, nmeupeza ucheshi wako, vituko na tabasamu lako, nakupenda sana mwanangu”
Maneno hayo yakamfanya Lucy afumbue macho yake na kumtazama mama yake ambaye machozi yalilowesha mashavu yake, akatabasamu na kunyanyua mkono wake na kumgusa.
“Nakupenda pia mama”
Mama Lucy hakuamini alichosikia akafikicha macho yake ahakiki ni kweli maneno yale yalitoka kinywani kwa bintiye au ni mawazo yake.
“Nimekupeza mama, mwanao ni mzima”
Mama yake na Lucy akamkumbatia bintiye kwa furaha sana, wote kwa pamoja wakajikuta wakilia na katika kipindi hiko hiko daktari akaingia, alishangazwa kidogo na maendeleo ya Lucy. Akamfanyia vipimo na kuona kuwa yupo sawa kiafya. Lucy alijishangaa kwani alihisi amekonda mno tofauti na alivyokuwa katika dunia ile ya miaka 1000 nyuma.
“Mom! Am I dreaming? (Mama hii ni ndoto au kweli?)
“You’re not dreaming my love (haupo ndotoni mwanangu)
Daktari akamtazama Lucy na mama yake kisha akawaambia,
“Japo sikuona tatizo lolote katika vipimo nilivyomfanyia ila siwezi kumruhusu kwa sasa naomba mvute subira hadi kesho, ili usiku huu tuendelee kuitazamia hali yake”
“Daktari mwanangu anazaidi ya mwezi katika chumba hiki binafsi sioni haja yay eye kuendelea kuwa hapa mpe nafasi ya kuungana na familia yake kwa siku hii” alisema mama Lucy.
Daktari akafikiri kwa kina kisha akamtazama Lucy kwa macho ya udadisi, akamuangalia tena mama yake Lucy kisha akasema,
“Sawa nitatimiza haja ya moyo wako, ila itakulazimu uwe naye karibu muda wote maana chochote kinaweza kutokea”
Mama yake lucy alifurahi mno kuona bintiye akirejea katika mazingira aliyoyazoea. Nyumbani kila mmoja akawa na shahuku ya kumuona Lucy wakaandaa tafrija fupi ya kumkaribisha. Walipofika nyumbani wakapokelewa kwa makofi na vigelele huku ndugu, jamaa na marafiki wa Lucy na hata wa marehemu mumewe wakiwa eneo hilo.
“Karibu tena mwanangu!” alisema baba Lucy.
Lucy alifurahishwa sana na mapokezi yale kila mmoja alimsogelea na kumkumbatia kwa ukarimu. Lucy aliangusha machozi ya faraja yaliyochanganyika na furaha kuu, hakujua aseme nini litalofaa kuwa kama shukrani zake. Wakati akiendelea kufikiri huku akiwatazama watu wale waliokusanyika mahala hapo. Moyo ukaripuka kwa mshtuko baada ya kumuona mtoto wa kwanza wa chifu lukemo ambaye alisimama kwa niaba ya baba yake hili kupitisha ndoa ile. Mapigo ya moyo yakaenda kasi na mama yake akagundua kuwa bintiye hayupo sawa. Akamsogelea na kumuuliza,
“Nini shida mwanangu”
“Mama mtoto wa chifu Lukemo amefata nini hapa?”
“Mhmhm! Lucy chifu Lukemo ndiye nani?”
“Mama yule kiongozi wa Sanzani?”
“Sanzani ndiyo wapi?”
“Mama! Sanzani ilikuepo miaka elfu moja iliyopita?”
Mama Lucy alihishiwa nguvu kabisa akapata na mashaka juu ya maswali ya bintiye akahisi uhenda matatizo aliyoyapitia yameleta athari kidogo katika akili yake.
“Nahisi umechoka sasa mwanangu! Ngoja nikusindikize ndani ukapumzike na baba yako atatoa neno kwa wageni hawa”
“Mama mbona hunijibu swali langu yule ni Ng’arika mtoto wa kwanza wa chifu Lukemo” alisema Lucy huku akionesha mkono wake kwa mmoja kati ya wageni waliopo eneo hilo.
Mama akatazama kisha akatabasamu alipooneshwa huyo kijana ambaye Lucy aliamini ni Ng’arika, akamshika mkono na kusogea nae hadi walipo vijana wale.
“Mwanangu hawa wote wanafanya kazi katika kitengo alichokuwa akifanya marehemu mumeo na huyu ni Cassian rafiki mkubwa sana wa mumeo”
Lucy alishangaa kidogo kuona hata katika dunia ya 2017 bado kuna mtu aliyekuwepo miaka 1000 nyuma na alikuwa karibu na mtu aliyefanana na mumewe. Shughuli iliendelea kwa watu kupata chakula cha jioni na mwishoe wazazi wa Lucy wakatoa shukrani zao na kila mmoja akarejea katika makazi yake.
****************
Baada ya siku kadhaa kupita, mama Lucy akiwa karibu Zaidi na bintiye, akashangazwa na tabia ngeni na ya kushangaza iliyojengeka kwa lucy toka aliporejewa na fahamu. Mama aliendelea kutafakari lakini asipate majibu kwa haraka, Lucy amekuwa na vitu vya kushangaza muda mwingi alipenda kukaa kwenye miti au bustani iliyoizunguka nyumba hiyo tofauti na awali ambapo muda mwingi alipenda kukaa chumbani kwake na kuangalia filamu au kusoma vitabu mbalimbali. Mama alistaajabishwa Zaidi na maongezi ya mwanae kwani mambo yote aliyoyazungumza yalihusu juu ya miaka elfu moja iliyopita ambayo kiuhalisia hakuwepo.
Siku moja mama yake Lucy akaamua amchukue bintiye na kwenda kwenye eneo la hifadhi ya taifa ambapo kulikuwa na vivutio vya misitu na wanyama wadogo wadogo. Lucy alifurahia sana safari hiyo,
“Mama huku yaani kama Sanzani, hii milima, hii misitu, hawa ndege yaani kila kitu ni kama kule tuu!” alisema Lucy.
“Mhmh! Mwanangu japo nimekuzaa na kukulea hadi kufikia hapo ulipo lakini nahisi kwa siku za hivi karibuni umekuwa mgeni nisiyekufahamu” alisema mama Lucy.
“Mhmhm! Mama hata watu wa Sanzani walisema maneno hayo hayo”
“Naomba unijuze japo kwa kinaga ubaga hiyo Sanzani unayoizungumzia wewe ipoje?”
Lucy hakuwa na namna Zaidi ya kumuelezea mama yake kila kitu, kuanzia siku ya kwanza hadi siku ile ambayo alitakiwa kuungana na chifu Lukemo katika ndoa tukufu. Mama alicheka mno na kumuona mwanaye kama anamuadithia simulizi za kale.
“Mhmhm! Wewe Lucy mbona wanihadithia mambo ambayo yalishaandikwa kwenye vitabu”
“Mama hii sio simulizi ni kweli nimeyashuhudia kwa macho yangu”
“Lucy itabidi kesho turudi hospitali maana naona unahitaji kufanyiwa uchunguzi Zaidi, wewe ni binti mdogo bado hata miaka 30 hujafika unanieleza kuwa ulikuepo miaka elfu moja iliyopita hili si jambo la kawaida”
“Mama japo nipo huku lakini roho inaniuma kwanini Mume wangu anajifanya hanikumbuki na anakubali kabisa mimi nifunge ndoa na mtu mwingine”
Hadi kufika hapo mama aliamini kabisa mwanaye hayupo sawa kiakili, akakumbuka maneno ya daktari kuwa alitakiwa kutazamwa kwa ukaribu Zaidi. Akawaza itakuaje endapo kama mwanae atachanganyikiwa Zaidi wakiwa eneo hilo. Akaogopa mno akamshika Lucy mkono ambaye alionesha kutotamani kuondoka eneo hilo.
“Mwanangu muda wa kurejea nyumbani umefika, twende sasa!”
“Hapana mama mimi sitamani kurudi nyumbani nahisi hapa ndio mahala sahihi kwangu.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana mwanangu huwezi kubaki eneo hili, nataka niendelee kuwa karibu zaidi na wewe”
“Sioni raha yeyote ya kuwa nyumbani bila ya kumuona mume wangu”
“Mungu ametupa uwezo wa kusahau maumivu na mahangaiko tuliyopitia, pia ametupa nafasi ya kuinuka pale tulipoanguka na kuanza safari upya. Mwanangu wewe si dhaifu kiasi cha kushindwa kusahau yaliyopita na kuanza maisha mapya. Natamani siku moja uishi kwa furaha na uupe moyo wako nafasi ya kupenda tena”.
“Mama mume wangu hajafa bado anaishi na siwezi kumpenda mtu mwingine angali yeye yu hai”
“Lucy umekutwa na nini wewe!” aliuliza mama kwa mshangao mkubwa.
Lucy hakujibu kitu zaidi ya kutabasamu, hadi hapo mama aliamini kwa kiasi kikubwa kuwa bintiye hayupo sawa kiakili.
***************
“Hivyo ndivyo ilivyokuwa daktari toka siku aliporejesha fahamu zake mpaka leo hii ninapozungumza nawe” alisema mama Lucy ambaye aliamua kwenda kuonana na daktari kumuelezea kila kilichojiri kwa bintiye.
“Mhmh! Kiukweli sio rahisi mtu kusadiki hayo mambo uliyoniambia na katika miaka yangu yote ya kufanya kazi kama daktari wa akili hili kwangu ni jambo jipya. Lakini mimi nafikiri haya yote yametokea sababu binti yako yu mpweke mno, nafikiri kuna ulazima wa yeye kuwa na mwenza atakayeweza kumsahaulisha yaliyomkuta”.
“Natamani iwe hivyo lakini sizani kama litawezekana, mwanangu ameufunga moyo wake na hataki kutazama pengine”
“Hakuna lishindikanalo ndani ya muda, tuvute subira kidogo kila kitu kitakuwa sawa” alisema daktari.
Mama aliridhia maneno ya daktari na kurejea nyumbani huku akitafakari ni kwa namna ipi anaweza kumsaidia bintiye.
******************
Luis ni kijana mwenye ndoto za kuwa muimbaji mkubwa nchini na duniani kwa ujumla katika mtindo wa R&B. luis amejaliwa sauti nzuri ambayo imekuwa kivutio kwa mashabiki wake wachache wa mji wa Morogoro. Umahiri wake katika upigaji wa gitaa ulimuongezea sifa nyingine iliyompa fursa ya kufanya maonesho katika hotel na kumbi mbalimbali za Morogoro.
Kilikuwa ni kipindi cha msimu wa sikukuu ya wapendanao, baba Lucy aliamua kuichukua familia yake na kwenda nayo katika Hotel moja kwa ajili ya chajio, watu walikuwa wengi siku hiyo na burudani mbalimbali zikatolewa.
Ikafika zamu ya Luis kupanda jukwaani na kuwaburudisha wateja walio eneo hilo, akapewa kiti kirefu na kusogezewa kipaza sauti kisha akakohoa kidogo na kusema.
“Katika maisha nimejifunza vitu vingi lakini lililokubwa zaidi ni kusamehe na kusahau, wahenga wanasema hewala sio utumwa, kuna mambo tunalazimika kuyaacha na kuyasahau hata kama hatupendi ili tuweze kupokea yaliyo mapya na bora zaidi. Mapenzi ni sawa na mashua na maisha ni sawa na bahari, kama ilivyo kwa mashua kupitia misukosuko mingi baharini ndivyo ilivyo katika mapenzi utapitia misukosuko mingi mpaka siku ambayo utayoiacha hii dunia”.
Ukumbi mzima ukatawaliwa na ukimya wa hali ya juu huku kila mmoja akivutwa na maneno ya Luis ambayo kiuhalisia yaligusa nyoyo za wengi. Lucy alikua akisikiliza lakini alionesha kama kutokubali maneno yale,
“Mhmh! mahangaiko ya mapenzi bado yapo hata kama ukitoka kwenye dunia hii, Sanzani pia kuna wanaoteseka na mapenzi huu ni uongo ulio dhahiri” alisema Lucy Lakini hamna aliyemzingatia maana wote akili zao zilikuwa jukwaani alipo Luis.
“Tone moja la sukari haliwezi kubadili radha ya maji ya bahari na wala tone moja la maji ya mvua aliwezi kuongeza ukubwa wa bahari lakini tone hilo hilo moja lituapo kwa mtu mwenye kiu huleta burudisho japo kwa kiasi kidogo. Wapo waliokata tamaa na kufunga nyoyo zao wakiamini Mungu ndivyo alivyowapangia. Ninapoenda kuimba nyimbo naomba ufanye mabadiriko”
Alisema Luis na kuanza kuimba, nyimbo ile ilimgusa sana Lucy akajikuta akisimama huku machozi yakimtiririka. Akafungua pochi yake na kutoa noti kumi za elfu kumi na kwenda kumtuza Luis, watu wengine wakainuka na kuungana na Lucy katika tukio hilo ambalo lilimpa hamasa ya kuimba Zaidi Luis. Hadi alipomaliza kuimba Luis alijikuta akiwa na pesa zisizopungua milioni moja. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupata kiasi hiko cha pesa toka alipoanza kuimba kwenye kumbi mbalimbali za starehe.
Luis aliwashukuru watu wote na kutoka jukwaani huku akisindikizwa na pongezi nyingi, wengi walifurahia sana tumbuizo lile.
“Haya bhana tumalizane kabisa maana leo umezikusanya mno”
“Mhmh! Beka hata kupumzika sijapumzika tayari unazungumzia habari za mtonyo”
“Pesa kwanza! Nilipe deni niachane nawe kwa Amani”
“Daah poa kaka!” alisema Luis huku akitoa noti tatu za shilingi elfu kumi na kumkabidhi Beka.
“Ahh! Lui enh hapa unazingua sasa!” alisema Beka.
“Kivipi?”
“Hizi pigo za ajabu ujue, mtonyo wangu umekaa nao karibu miezi mitatu leo umezikusanya unarudishaje kavu, weka cha usumbufu”
Luis hakuwa na namna Zaidi ya kumuongezea noti nyingine ya elfu kumi Beka. Beka akaipokea kwa tabasamu.
“Hapa kiroho safi! Kama vipi tutasomana kesho” alisema Beka kwa lugha ya kiuni na kuondoka eneo hilo huku akimuacha Luis akiangaza huku na huko kutafuta usafiri.
Wakati akiendelea kuangaza akasikia mtu akimuuliza.
“Vipi kijana unaelekea wapi?”
“Ah! Mzee mimi naelekea Kigurunyembe”
“Basi ingia kwenye gari tukupe lift maana sisi tunaelekea Bigwa” alisema mzee huyo.
Luis alifurahi sana kwake ilikuwa kama bahati kupanda katika gari ile ya kifahari aina ya Range, alipoingia akakuta ni familia japo hakuwa anawafahamu ila aliona upendo mkubwa uliopo kati yao. Alitamani sana kama angekuwa mmoja kati ya wanafamilia wale.
“Kijana unakipaji sana!” alisema baba yake Lucy.
“Nashukuru mzee wangu” alijibu Luis.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hii unayoiona hapa ni familia yangu na huyu ni binti yangu yeye ni daktari mkubwa wa upasuaji, na huyu ni dada yake yeye ni mfanyakazi katika shirika moja la ndege na makazi yake ni jijini Dar es Salaam, huyu ndiyo wa ubani wangu yaani mama wa watoto hawa. Sijui wewe mwenzetu tunakufahamu kwa jina na kupitia uimbaji wako mengine hatuyatambui,” alisema baba Lucy.
Luis akahisi kushikwa na kigugumizi hakuelewa aanzie wapi kujielezea, akashusha pumzi ndefu kidogo kisha akasema,
“Sikubahatika kuwa na elimu ya darasani isipokuwa ile niliyofunzwa na wazazi wangu, sauti na mikono kwangu ndiyo ofisi, nategemea hivi kuishi”.
“Unaishi na nani?”
“Na baba yangu”
“Vipi kuhusu mama yako na je hauna ndugu wengine?”
Luis akashindwa kujibu swali hilo akajikuta akitokwa na machozi asijue nini aseme, maana mdomo wake uligoma kabisa kufunguka.
“Ni stori ndefu mzee wangu ambayo sitoweza kuimaliza kwa leo lakini ndugu niliyenaye ni baba yangu pekee, mama sikubahatika kumfahamu na sijui kama angali hai au mfu” alisema Luis.
Baba yake Lucy hakutaka kuhoji zaidi kwani aliiona huzuni iliyojaa katika maisha ya kijana huyo, akafungua moja kati ya bahasha na kutoa namba za simu;
“Kijana ukiwa na nafasi naomba unitafute kupitia namba hizo”
“Sawa nashukuru mzee wangu”
Luis akafikishwa hadi nyumbani kwao hakukuwa na watu walioshuhudia hilo maana ulikuwa ni usiku mnene. Akawashukuru tena na kuingia ndani kwake, nao wakageuza gari tayari kwa kuendelea na safari. Usiku huo Luis alitingwa na mawazo sana akakumbuka yale maswali aliyokuwa akiulizwa na mzee Yule kuhusu ndugu na mama yake. Ukweli hakuwa na majibu sahihi ya maswali hayo, hakuweza kuwatambua ndugu zake wala mama yake.
“Kwanini baba hakuniambia lolote kuhusu mama yangu na kwanini hata siku moja sijawahi kuona akienda au kutembelewa na ndugu wa aina yeyote? Nahisi kuna ukweli nisioufahamu, Mungu mpe nguvu baba yangu naamini atanijuza kila kitu,” alisema Luis
********************
Baada ya juma juma kupita, Luis alialikwa nyumbani kwa kina Lucy, aliduazwa na ukubwa wa nyumba ile iliyopangiliwa vyema. Nyumba ya kina lucy imezungukwa na bustani iliyochanganyika na miti mbalimbali. Mazingira hayo yalimvutia sana Luis. Akajikuta akiomba ridhaa ya kukaa nje bustanini badala ya ndani, wenyeji wake wakaridhia ombi la Luis na wakahaidi kuungana naye muda si mrefu.
Luis akasogea sehemu yenye miti na kuendelea kuangaza kila kona kwa mbali macho yake yakatua kwa Lucy ambaye alikuwa akitabasamu na kuongea mwenyewe. Luis alishangazwa na jambo hilo akaongeza hatua za miguu yake na kumkaribia zaidi Lucy.
“Habari yako dada!” alisema Luis.
“Nzuri tuu!” aliitika Lucy.
“Nina siku nyingi kweli sijacheka, je unaweza kuniambia kinachokufurahisha ili nami nifurahi”
“Kaka samahani! Katika Sanzani yetu ni mwiko kwa mwanamke kuzungumza na mwanaume hasiyemuoa”
“Mhmhm! Sanzani ni wapi?”
“Ni sehemu niliyeishi miaka elfu moja iliyopita”
Luis hakuitaji muendelezo wa maongezi yale akajikuta akicheka muda huohuo kutokana na maelezo ya Lucy.
“Basi umeshinda dada sikutegemea kama unaweza kunichekesha kwa muda mfupi hivi”
“Kipi kilichokuchekesha”
“Maneno yako”
“Hivi kwanini kila mtu nikimwambia habari za miaka elfu moja iliyopita hataki kunisadiki! Je unajua kama nilitaka kuolewa na chifu Lukemo”
“Mhmh! Dada eenh! Hizo kamba zako sasa zimezidi”
“Sio kamba ila ni kweli”
Luis akamuangalia sana Lucy akagundua kuwa lile alilokuwa akiliongea alilimaanisha hakukuwa na hata chembe ya utani ndani yake.
“Yawezekanaje haya! Au msichana huyu anamatatizo ya akili?” alijiuliza Luis.
“Vipi mbona kama unataka kusema jambo”
“Hapana dada”
Waliendela kuongea japo Luis akawa na wakati mgumu zaidi kumuelewa Lucy, muda mfupi baadae mama yake Lucy naye akajumuika nao.
“Karibu mama!” alisema Luis.
“Akhsante mwanangu”
“Sikupata nafasi ya kusoma historia ya darasani lakini dada hapa ananisimulia kila kitu”
Mama yake Lucy alitabasamu tuu hakutaka kusema lolote juu ya hayo, akamwangalia mwanae pia akamwangalia na Luis kisha akasema,
“Nahisi damu zetu zimeendana, kiukweli najihisi furaha na amani moyoni mwangu, nitakuwa mama yako kuanzia leo”
Luis hakuamini aliposikia maneno hayo, toka alipozaliwa hadi kufikia umri huo hakuwahi kutamka neno mama, akafikiri mara mbili kabla hajajibu japo swali jingine liliibuka moyoni mwake juu ya ukarimu ule anaofanyiwa na wanafamilia ile.
“Mama mimi nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu, binafsi sina kipingamizi, naomba kwanza nizungumze na baba yangu kisha atakalo niambia nitakujuza” alisema Luis.
“hilo halina shida”
************************
Familia ya kina Lucas wanapokea taharifa ambayo kidogo inawaacha katika mkanganyiko pasi na kuelewa nini wafanye. Habari ya kupangwa kwa ajali iliwashtusha na kuwauzunisha mno.
“Siwezi kulifumbia macho hili kwa gharama yeyote ile nitahakikisha aliyesababisha mauti ya mwanangu naye analipa,” alisema baba yake Lucas kwa hasira mno.
“Mzee hauna shida ya kuumiza kichwa kwani tayari swala hili lipo ofisini na uchunguzi umeanza, kwa sasa naomba mtulie na tutakapofikia hatutosita kuwajuza” alisema Chodo.
Baba yake Lucas akaona ni vyema amjuze mzazi mwenzie juu ya kilichojificha nyuma ya maswahibu yale. Kwa pamoja wakakubaliana kutosema popote hadi uchunguzi utakapokamilika.
***************
Jioni moja Luis alienda nyumbani kwa kina Lucy ili aweze kutoa majibu juu ya kile alichoombwa, bahati mbaya hakufanikiwa kuwakuta wenyeji wake Zaidi ya Lucy aliyekaa upweke bustanini. Baada ya salamu Luis akaketi mkabala kabisa na msichana huyo, akatumia sekunde kadhaa kumuangalia Lucy kisha akamsemesha,
“Leo nataka tuzungumze lakini ni lazima tutumie falsafa”
“Hahahaha! Niko vizuri kwenye falsafa huwezi nishinda mimi”
“Kweli eenh!”
“Ndio! Nikikushinda lazima unizawadie”
“Sawa nami nikikushinda lazima ufanye hivyo hivyo”
“Ayah! Anza sasa” alisema Lucy.
Luis akakohoa kidogo kuweka sawa koo lake kisha akatazama angani na kuvuta hisia mithiri ya mtu anayeitaji kukumbuka jambo, akafungua kinywa chake na kusema
“Hisia hizi zina maana gani! Mimi ni msafiri nisiyejua hatamu ya safari, tumezaliwa katika dunia mbili tofauti hivyo siwezi kukupenda. Palipo na mvua ya huba hapakosi jua la mwiba na palipokauka panatamani kunyeshewa”.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mimi ni msafiri nisiyetamani kati na hatamu ya safari, nimezaliwa zama za kale lakini bado ni kijana mamboleo, nimenyeshewa mvua ya huba nimelowa kwa shurba. Asali ni chungu Zaidi ya shubiri, hisia hizi zinamaana gani, tumezaliwa dunia mbili tofauti siwezi kukupenda,” alisema Lucy.
Luis aliduwazwa na jibu la Lucy, hakufikiria kama binti huyo anaweza kuwa haraka katika kufafanua mafumbo na kuyajibu. Akampigia makofi ishara ya kumpongeza;
“Machoni kama kuku wa kisasa, fikrani mithili ya sungura, eenh malkia uliyejaliwa fani ya utabibu, kwanini uko mbali sogea unitibu”
“Hakuna marefu yasiyo na ncha, kila kilicho hai ni lazima kufa………”
Kauli hii ikamfanya Lucy ashindwe kuendelea kuzungumza, akahisi mwili kushikwa ganzi na wala hakuelewa imekuaje hadi yeye kuzungumza vile. Luis akauona mfadhaiko ule, akacheka sana hadi kuanguka chini, Lucy akachukia kidogo;
“Nini kikuchekechasho?”
“nipe tuzo yangu”
“Tuzo gani?”
“Si tumekubaliana kuwa mshindi atapewa tuzo”
“Kwani nani kasema kuwa nimeshindwa”
“Matendo huongea Zaidi ya maneno, muonekano wako umenidhihirishia ushindi wangu”
“Hapana sijashindwa turudie tena”
“Muda sio rafiki ilikuwa kiangazi sasa masika”
“Sawa sema unataka nikupe nini?”
“Kesho nitakualika kwa chakula cha mchana nyumbani kwangu”
“Sawa” alijibu Lucy.
Wakati maongezi hayo yakiendelea mama Lucy alikuwa kwa mbali akiwatazama, alihisi kufarijika kwa kiasi kikubwa kwani kijana yule amemfanya bintiye kuonekana mtu.
“Kweli kila shetani na mbuyu wake, Lucy hakuelewana na yeyote kati yetu lakini kwa kijana yule ambaye hana hata mwezi ameweza kutengeneza urafiki thabiti, Luis nafikiri wewe ni malaika uliyeletwa kuirejesha furaha iliyopotea katika familia hii” alisema mama Lucy huku machozi ya faraja yakimtoka.
Siku iliyofatia Lucy ikamlazimu atimize ahadi aliyoiweka kwa Luis, akaingia ndani ya gari lakini kabla hajawasha akakumbuka siku aliyopata ajali na mumewe, akajikuta akiogopa mno na kutoka nje ya gari. Akaamua atafute usafiri wa bajaji ambao ulimpeleka moja kwa moja hadi mtaa wa pili kigurunyembe ambapo Luis alikuwa akiishi. Lucy aliyashangaa mazingira yale ambayo kwa asilimia kubwa watu waliojenga makazi hapo ni wakipato cha chini na ni wachache waliojaliwa kipato cha kati. Luis alifurahi mno kumuona Lucy ambaye aliteka akili za watu wengi wa eneo hilo, wengi walishangaa nyumba ile kupata mgeni kwani haikuwa kawaida,
“Sitaki kujua maoni yako juu ya mahala hapa, ila ndipo tulipojaaliwa kujistiri mimi na baba yangu, karibu sana,” alisema Luis huku akimpokea Lucy mkoba wake wenye rangi ya samawati.
“Akhsante sana” alijibu Lucy na kuingia ndani.
Baba yake Luis ni mgonjwa wa muda mrefu sana, Luis amejitahidi kuhangaika katika hospitali mbalimbali bila mafanikio. Mzee huyo anasumbulia na kansa ya mapafu lakini siku zote alivumilia maumivu yake na kumkaza kijana wake huku akimsii asilegee na kuyumbishwa juu ya matatizo yake. Mzee huyo aliufurahia sana ugeni ule,
“Shikamoo baba” alisema Lucy.
“Marhaba mwanangu” alijibu baba yake Luis.
“Baba huyu ni rafiki yangu anaitwa Lucy”
“Mhmh! Mwanangu lini umejifunza uongo?”
“Kivipi baba?”
“Huyu rafiki yako au ndiyo mkwe”
“Duuh! Baba”
“Sema tuu maana vijana nyie mna visa kweli”
Baba yake Luis alikuwa mcheshi sana kama mwanae, kwa pamoja wakajikuta wakicheka. Pamoja na furaha iliyojengeka usoni mwa mzee yule lakini hakuweza kuficha maradhi yanayomsibu, kwani mara nyingi alipokohoa alikohoa damu. Lucy alikuwa mwepesi kulibaini hilo, hakuweza kuvumilia akauliza,
“Baba unaonekana umedhoofika kwa maradhi waweza niambia kipi kinachokusibu”
“Hahahaha! Mwanangu uzee unamambo mengi usijali sana kuhusu mimi” alisema mzee huyo.
Lucy alijitahidi kuelewa kile alichoambiwa lakini alimuhurumia sana kwani dalili ya kukohoa damu inaonesha kuwa yupo katika hatua ya mwisho ya kuumwa.
“Leo nimefarijika sana kuona mwanangu akiwa na rafiki mwema, naamini hata nikiondoka katika hii dunia kuna watu wataomkimbilia na kumsaidia”
“Mhmh! Mzee usije ukaaribu sherehe yetu, leo ni siku ya kufurahi hayo mambo utaongea siku nyingine,” alisema Luis kiutani.
Baba yake alitabasamu huku akijua fika mwanae hawezi kuukubali ukweli kuwa siku si nyingi watatengana huku wakitumai kukutana katika maisha ya roho.
Luis aliandaa chakula na wote wakajumuika kula, kisha baadae akamuaga baba yake kuwa anaenda sehemu ya makumbusho iliyopo eneo hilo la kigurunyembe. Kiuhalisia Kigurunyembe ina maana ya “kiguru twende” neno hili lilitumika enzi za ukoloni ambapo watumwa walipofika eneo hilo walijikaza hili wasiweze kutupwa katika shimo ambalo lilikuwa kama jalala kwa watumwa waliochoka. Walifika eneo lililokuwa na picha za watumwa, kumbukumbu zikarudi hadi Sanzani, ambapo vijana wengi wakiume walichukuliwa utumwa na kupewa mafunzo ya kijeshi hili kupambana kama maaskari wa kijerumani.
“Matukio haya yamekuwa historia kwa huku ila katika Sanzani ni vitu ambavyo vinatokea” alisema Lucy.
“Umeanza eenh! Na kamba zako”
“Kwa hiyo utaki amini kama mimi nilikuepo miaka hiyo iliyopita”
“Sawa nimesadiki ulikuwepo, niambie unamiaka mingapi kwa sasa”
“28”
“Ongeza na hiyo elfu moja unayoisema”
“Mhmhm! Itakuwa 1028”
“Khaa sasa wewe mtu au jini?”
“Nini?”
“Umenisikia bhana ila kiburi tuu, hamna binadamu anayeweza kufikisha umri huo”
“Ndio mimi sasa”
“Kwa hiyo wewe bibi”
“Nani bibi?”
“Wewe hapo ajuza wa miaka 1028”
Waliendelea kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya kihistoria huku wakitaniana hadi jua lilipozama kisha kwa pamoja wakarejea nyumbani na Lucy akamuaga baba yake Luis huku akimuahidi kuja kumtembelea siku nyingine. Luis alimsindikiza Lucy hadi alipopata usafiri kisha naye akarudi nyumbani, kabla hajaingia ndani akahisi simu yake ikiita alipoitazama akakuta ni namba hasiyoitambua. Bila kupoteza muda akabonyeza kitufe cha kupokelea na kuiweka sikioni,
“Wewe ni gugu uliyeota kwenye shamba langu, siwezi kuvuna nilichopanda kama nitakuacha uendelee kumea” ilisikika sauti uliyo upande wa pili wa simu.
“Sijaelewa unamaanisha nini”
“Acha hiko ambacho umekianzisha sasa kitagharimu maisha yako na hata ya huyo baba yako”
“Wewe ni nani kwani?” alizidi kuuliza Luis.
“Mimi nipo na nitaendelea kuwepo popote uendako hadi nihakikishe nakutoa kwenye shamba langu”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Simu ile ikamuacha njia panda Luis asiweze kung'amua nini maana ya maongezi yale, aliogopa mno akafikiri kwa kina lakini hasipate majibu juu ya sababu ya uadui huo.
"Mhm! inamaana ukaribu wangu na familia ya kina Lucy ndiyo umesababisha haya au kuna jambo lingine ambalo mimi silifahamu" alijiuliza Luis.
Kwa wakati ule hakutaka kuumiza kichwa zaidi akaamua avute subira ili aone kama jambo lile litarijudia tena. Akageuka nyuma na kuangalia kila kona ili aweze kuona kama kweli kuna mtu anayemfatilia lakini hakuambulia kitu.
Akaingia ndani na kumkuta baba yake amepitiwa na usingizi hakutaka kumsumbua zaidi ya kumuweka vizuri kisha naye akaingia chumbani kwake na kujipumzisha. Nyumba ya kina Luis ni ya kawaida iliyojengwa kwa matofari ya kuchoma ikiwa na jumla ya vyumba vinne na sebule iliwatosha sana kwa mahitaji yao.
*****************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment