IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
Glorious Worship Event (GWE) lilikuwa moja ya matamasha ya kusifu na kuabudu yaliyokuwa yakiandaliwa na kanisa kubwa nchini Tanzania, kanisa lililokuwa chini ya mchungaji mwenye upako, mchungaji mpakwa mafuta wa Bwana, Mchungaji Michael Yekonia wa Kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge jijini Dar es Salaam.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Vijana wengi kutoka katika makanisa mbalimbali walikuwa wakikutana katika Uwanja wa Taifa uliokuwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusifu na kumuabudu Mungu kisha kusikiliza maneno ya Mungu kwa dakika kadhaa kabla ya sifa na kuabudu kuendelea.
Wanachuo, wanafunzi waliosoma bweni waliomba ruhusa shuleni kwao ili kwenda kushiriki katika tukio hilo lililokuwa gumzo nchini Tanzania, tukio lililoripotiwa kila kona nchini Tanzania na kulifanya kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kuongeza idadi ya watu walioshiriki.
Vijana zaidi ya laki mbili walikuwa wakikusanyika uwanjani hapo, waimbaji mbalimbali wa kimataifa kutoka Afrika Kusini, Marekani, Nigeria, Botswama na nchi nyingine nyingi walifika katika tukio hilo ambapo kulikuwa na kazi moja ya kusifu na kuabudu tu.
Kwaya mbalimbali kutoka katika makanisa mengi jijini Dar es Salaam zilipewa nafasi za kuimba, waimbaji binafsi nao hawakuwa nyuma, kila mmoja aliyetaka kuimba siku hiyo ndiyo ilikuwa siku yake.
Kupitia tukio hilo kubwa, vijana wengi walikuwa wakionana, walijenga urafiki na hata wengine kujikuta wakiwa kwenye uhusiano wa kimapenzi ambao moja kwa moja yalileta ndoa. Tukio hilo lilipendwa, makanisani, vijana walilizungumzia mno, kila mmoja alitaka kushiriki, akutane na vijana wenzake na kisha kuanza kumuimbia Mungu.
Katika tukio la GWE la mwaka huo, zaidi ya vijana laki moja na nusu walikuwa wamefika uwanjani hapo, kila mmoja alifika akiwa na dhamira moja tu ya kumsifu na kumwabudu Mungu. Waliotaka kucheza kama watu waliochanganyikiwa, walifanya hivyo, waliotaka kusali mpaka kulia, wote walikuwa na uhuru.
Hakukuwa na utulivu, kila mmoja alicheza na kurukaruka, uwepo wa Mungu ulionekana mahali hapo, waliokuwa wagonjwa, kupitia nyimbo za sifa zilizokuwa zikiimbwa uwanjani hapo wakajikuta wakipokea uponyaji hata kabla kipindi cha maombezi kufika.
Miongoni mwa watu waliokuwa katika uwanja huo, ndani ya tukio hilo alikuwepo kijana mtanashati, kijana aliyekuwa na muonekano wenye fedha, sura ya upole, huyu aliitwa Laurence Mathew.
Kwa kumwangalia mara moja, usingepata wakati mgumu kugundua kwamba kijana huyo alikuwa na fedha au alitoka katika familia yenye fedha. Alikuwa na muonekano wa bei na hata mavazi yake aliyoyavaa yalikuwa ni ya bei mbaya.
Siku hiyo katika kipindi cha kusifu na kuabudu, hakutulia, alicheza mno, jasho lilimtoka, hakuangalia mavazi yake, hakuangalia kama alikuwa tajiri, alichokuwa akikifanya ni kucheza mpaka kuvua shati, alionekana kama kujitoa fahamu.
Hakukuwa na mtu aliyemwangalia mwenzake, kila mmoja alijali yake. Kwa Laurence ilionekana kuwa nafuu kwani kulikuwa na watu wengine ambao walicheza, walirukaruka mpaka nguo kuwavuka, hawakujali, walichokuwa wakikifanya ni kumsifu Mungu aliye hai.
“Bwana Yesu asifiweeeeee....” ilisikika sauti ya mchungaji Yekonia aliyesimama jukwaani.
“Ameeeeeeeeeeeen....” zilisikika sauti za watu wote waliokuwa uwanjani hapo, wakaanza kupiga vigelegele huku mikono yao ikiwa hewani.
“Leo ni siku ya kipekee sana, ni siku ambayo tumekuwa tukiisubiri kwa kipindi kirefu, leo ni siku ya kumkanyaga shetani, ni siku ya kuacha mizigo yetu msalabani, Yesu alipokufa, alibeba mizigo yetu na hata alipofufuka, bado akatuachia msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu,” alisema mchungaji Yekonia huku akiwaangalia watu waliokusanyika uwanjani hapo.
Hakuzungumza sana, hakutaka kupoteza muda wa watu uwanjani hapo, aliongea kwa dakika chache sana, akamkabidhi mtu wa sifa kipaza sauti kile kisha kuendelea kumsifu Mungu.
Wakati watu wakiendelea kumsifu Mungu, ghafla macho ya Laurence yakatua kwa msichana mmoja aliyesimama pembeni yake, kama hatua kumi kutoka alipokuwa, msichana huyo alikuwa akiimba huku akicheza, kwa kumwangalia usoni, alikuwa na uzuri wa ajabu.
Alifanana na mwanamuziki wa Marekani, Alicia Keys, uso wake ulionyesha kuwa na tabasamu pana lililomfanya kumvutia zaidi Laurence aliyebaki akiyatuliza macho yake kwa msichana huyo tu.
“Haleluyaaa...” alijikuta akisema Laurence, macho yake yaliganda kwa msichana yule.
Tayari akili yake ilikwishahama, kila alipomwangalia, tayari akaanza kupata maono, akajiona akisimama mbele ya kanisa, alikuwa amevaa suti na msichana huyo alivalia shela jeupe, walikuwa kanisani hapo kwa ajili ya tukio moja tu, kufunga ndoa na hatimaye kuwa mume na mke.
Akaulizwa kama alikuwa tayari kumuoa msichana huyo, jibu lake lilikuwa lilelile alilotaka kulitoa, ndiyo alikubali na hata alipoulizwa msichana huyo, hawakutofautiana jibu lake na Laurence, naye alikubali kuolewa.
Ghafla akatoka katika maono yale, akamwangalia vizuri msichana yule, alionekana kuwa msichana mpole, mwenye maisha duni kwani hata mavazi aliyoyavaa yalionyesha dhahiri kwamba msichana huyo hakuwa na maisha mazuri hata kidogo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Laurence hakutaka kusimama pale aliposimama, akajikuta akianza kupiga hatua za taratibu, tena huku akicheza mpaka karibu na msichana yule ambapo alipomwangalia vizuri, akagundua kwamba machozi yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake.
“Bwana Yesu asifiwe,” alisalimia Laurence, msichana yule hakusikia kutokana na kelele zilizokuwa uwanjani hapo.
“Bwana Yesu asifiweeee...” alimsalimia tena kwa sauti ya juu.
“Unasemaje?” aliuliza msichana yule.
“Nimekusalimia.”
“Sijambo,” alisema msichana yule huku akionekana kutokuisikia salamu ile.
Laurence hakutaka kuendelea kuzungumza na msichana yule, akajifanya kuwa bize kuimba kama wengine. Mawazo yake yalivurugika kabisa, akili yake ikahama, alihisi kuwa na mapenzi mazito juu ya msichana yule, kila alipomwangalia, aliona akimpenda kuliko mtu yeyote yule.
Alionekana kustahili kuwa mke wake wa ndoa, muonekano wake wa upole, sura nzuri vilikuwa vitu vilivyomchanganya vilivyo. Hakutaka kufuatilia tena kilichokuwa kikiendelea uwanjani hapo, mawazo yalimjaa juu ya msichana yule huku akiwa na hisia kali za mapenzi zikiutawala moyo wake.
Tamasha lile liliendelea mpaka lilipomalizika majira ya saa moja usiku. Mchungaji Yekonia akasimama na kisha kufunga kwa maombi mazito na kuwaruhusu watu kuondoka uwanjani hapo.
Laurence hakutaka kusubiri, alichokifanya ni kuanza kutafuta mazoea na msichana yule, kila alipoongea hiki au kuuliza kitu fulani, jibu alilopewa lilikuwa la kukatisha tamaa, lililoonyesha kwamba msichana huyo hakutaka kuulizwa zaidi.
“Unasali kanisa gani?”
“Mburahati.”
“TAG, Pentekoste au Anglikana?”
“TAG.”
Kila alichouliza, alijibiwa kifupi, tena huku uso wa msichana huyo ukionekana kuwa siriazi, hakuonekana kuwa tayari kuzungumza zaidi. Kwa Laurence, hali ilionekana kuwa mbaya, alishindwa kuelewa kama kweli angeweza kufanikiwa kuwa na msichana huyo au la.
Alichokuwa akikihitaji kwake si kuwa msichana wa kuwa naye siku kadhaa na kumuacha, alichokitaka ni kuwa naye, kufunga naye ndoa na kuwa mume na mke. Msichana huyo hakuonekana kuwa na habari, macho yake yaliangalia mbele, wakawa wamekwishafika nje, na walianza kuyafuata mageti na watu wengine.
“Binti...” aliita Laurence, msichana yule hakuitikia, akayageuza macho yake na kumwangalia Laurence usoni.
“Unaitwa nani?”
“Ili?”
“Kukufahamu tu mpendwa! Kwani kuna tatizo?” aliuliza Laurence.
Msichana yule hakujibu kitu, aliendelea kusonga mbele. Hakutaka kuzungumza na Laurence, kila alimwangalia, alikasirika kwa kuona kwamba alipotezewa muda wake. Japokuwa alikuwa ameegesha gari lake katika eneo la uwanja huo lakini Laurence hakulikumbuka, aliendelea kwenda na msichana yule ambaye alifika kituoni na kuanza kusubiria daladala.
“Unaishi wapi?” aliuliza Laurence.
“Wewe kaka vipi?”
“Jamani! Kwani kuna tatizo kama nikikufahamu zaidi mpendwa katika Bwana?”
“Aya! Naitwa Evadia,” alijibu msichana yule.
“Nashukuru kukufahamu. Ubarikiwe na Bwana,” alisema Laurence.
Wote wakajikuta wakikaa kituoni hapo kusubiri daladala. Laurence hakujua msichana huyo alikuwa akisubiri daladala za wapi. Usafiri ulikuwa ni wa shida kwani kulikuwa na watu wengi mno. Kila gari lililokuja kituoni hapo, liligombaniwa hivyo kukosa nafasi.
Waliendelea kusubiri. Evadia alikuwa akimshangaa Laurence, hakuwa akimfahamu mvulana yule, hakujua alihitaji nini. Japokuwa alionekana kuwa mvulana mwenye sura nzuri na ya upole lakini hakuwa amevutika.
Kila daladala aliyolifuata kwa ajili ya kupanda, alifuatwa na Laurence, alipoliacha, naye Laurence aliliacha. Evadia akawa na wasiwasi mno, alichokifanya ni kusogea pembeni kabisa ya kituo kile na kutulia, alitaka kuona kama Laurence angemfuata.
Moyo wa Laurence uliumia mno, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea. Moyo wake ulikuwa kwenye mapenzi ya dhati, hakuamini kuona kwamba msichana aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi yote hakuwa akimtaka, hakuwa akitamani kuzungumza naye.
Japokuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kumuona msichana huyo lakini moyo wake ulikufa na kuoza. Alichokifanya ni kusimama, alimwangalia Evadia kwa jicho la wizi, ilipokuja daladala ya kwenda Manzese kupitia Kigogo, Evadia akaifuata, akaingia ndani, naye Laurence akaingia. Akasahau kama aliliacha gari lake la thamani ya shilingi milioni mia na hamsini katika eneo la kuegesha magari pale Uwanja wa Taifa. Alikuwa bize kumfuatilia msichana huyo tu ambaye hakujua aliishi wapi..
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Abiria walikuwa wengi ndani ya gari, Laurence alishikilia bomba huku pembeni yake akiwepo Evadia ambaye alikuwa na maswali mengi juu ya mwanaume yule aliyekuwa akimuwinda tangu walipokuwa ndani ya Uwanja wa Taifa.
Hakutaka kuzungumza lolote na Laurence, alibaki kimya huku akisikilizia ni kitu gani kingefuata kwani kwa jinsi alivyoonekana Laurencce, hakuonekana kuwa mwanaume mwenye papara, kila alilokuwa akilifanya alionekana kuwa makini nalo.
“Umependeza Evadia,” alisema Laurence, hakuwa na kingine cha kusema zaidi ya kumsifia msichana huyo kwa kuamini kwamba pindi unapomsifia mwanamke, una asilimia kubwa za kumpata.
“Asante.”
“Unashuka wapi?” aliuliza Laurence.
“Mburahati.”
“Oooh! Sawa, ningependa nikufahamu zaidi,” alisema Laurence, watu waliokuwa karibu nao waliyasikia mazungumzo hayo japokuwa Laurence alijitahidi kuongea kwa sauti ya chini.
“Ili?”
“Basi tu, kuna mengi ya kuzungumza nawe.”
“Kuhusu nini?”
“Usiogope, niamini.”
“Hivi wewe kweli Mkristo au ulifika uwanjani kutafuta wanawake?” aliuliza Evadia huku akimkazia macho Laurence.
“Mimi?”
“Kwani naongea na nani?”
“Mimi ni Mkristo, sikwenda pale kutafuta mwanamke, nilikwenda kumsifu na kumuabudu Mungu,” alijibu Laurence.
“Sawa.”
“Evadia naomba unielewe. Mimi si kijana mhuni, sikukufuata kihuni, nimekuja kwako kama mtu anayejitambua, hicho unachokifikiria kichwani mwako juu yangu si kile kilichopo kwangu. Naomba tukae sehemu tuzungumze, hata kama utataka nije nyumbani kwenu, hakuna tatizo,” alisema Laurence.
“Uje nyumbani kwetu?”
“Ndiyo!”
“Kama nani?”
“Evadia, naomba usinifikirie vibaya,” alisema Laurence.
Kuanzia hapo Evadia hakutaka kuzungumza tena, alibaki kimya, kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele Laurence alijitahidi kumuongelesha lakini msichana huyo akawa kimya kabisa. Kwa muonekano wa nje Laurence alionekana kuwa mtu mzuri lakini hiyo haikuwa sababu ya Evadia kumuamini.
Safari iliendelea zaidi, Laurence hakunyamaza, alikuwa kinara wa kuongea japokuwa maswali yake yote aliyokuwa akiyauliza hakuwa akijibiwa. Gari lilipofika maeneo ya Mburahati Msikitini, Evadia akateremka, naye Laurence akateremka.
“Unahitaji nini kutoka kwangu?” aliuliza Evadia huku akimwangalia Laurance usoni.
“Kukuoa!”
“Unasemaje?” aliuliza Evadia huku akionekana kushtuka.
“Kwani haujanisikia mpendwa? Nahitaji kukuoa,” alisema Laurence.
Evadia akaonekana kukasirika, hakutaka kuendelea kusimama mahali hapo alichokifanya ni kuondoka kuelekea katika njia iliyokuwa na michanga mingi. Laurence hakusimama, akaanza kumfuata msichana huyo kama mkia.
Kila baada ya hatua ishirini, Evadia aligeuka nyuma, akaona bado Laurence alimfuatilia kwa nyuma. Safari iliendelea na baada ya dakika tano, msichana huyo akaanza kuifuata nyumba moja iliyochoka, kwa kuiangalia kwa nje tu ingekupa picha kwamba mtu aliyekuwa akiishi ndani ya nyumba hiyo alikuwa masikini mno.
Nje ya nyumba ile kulikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa akisuka ukili. Laurence hakutaka kusogea zaidi, akabaki akiwa amesimama kule mbali alipokuwa, hali waliyokuwa nayo watu wale iliunyong’onyeza moyo wake, akajikuta akiingiwa na huruma mno.
Msichana mwenye sura nzuri, msichana ambaye kwa kumwangalia tu hakutaka kujiuliza kama alistahili kuwa mke wake au la, maisha aliyokuwa akiishi yalikuwa ya kimasikini mno. Alipoiangalia nyumba ile, hakuamini kama kungekuwa na watu waliokuwa wakiishi humo.
Ilionekana kuwa kama kibanda fulani cha kufugia kuku. Sehemu nyingine ilijengwa kwa udongo lakini sehemu nyingine ilijengwa kwa matofali yaliyoonekana kuchoka sana. Bati lililotumia kuezeka nyumba ile lilichakaa, lilikuwa na kutu nyingi, kila alipoiangalia nyumba ile, kwa kifupi, alijisikia vibaya moyoni mwake.
Alipomuona Evadia akizungumza na mwanamke yule aliyekaa chini nje ya nyumba ile, hakutaka kusubiri zaidi, alichokifanya ni kugeuka na kurudi alipotoka. Hicho ndicho alichokuwa akikihitaji, alihitaji kupafahamu mahali alipokuwa akiishi Evadia.
Moyo wake ulimpenda mno, alitaka awe mke wake wa ndoa, kila alipomwangalia, sura ya kuvutia, aligundua kwamba msichana huyo alistahili kuwa mpenzi wake. Hivyo akaondoka zake na kujiahidi kurudi tena siku nyingine.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Laurence alikuwa na mawazo kichwani mwake, kazi zake za kila siku hazikufanyika, muda wote aikuwa na mawazo tele, alikuwa akimfikiria msichana aliyekutana naye jana yake ambaye kwake alionekana kuwa kama malaika.
Kila alipojigeuza huku na kule, taswira ya msichana yule ilionekana kichwani mwake, moyo wake ukavutwa, ukabuuzwa vilivyo, mapenzi mazito yaliendelea kuchipua moyoni mwake, hakutaka kitu kingine, hakuwa na hamu ya msichana mwingine, yule aliyekuwa akimfikiria alikuwa Evadia tu.
Usiku wa siku hiyo hata usingizi haukumjia inavyotakiwa, alikuwa akimfikiria msichana huyo tu, kwake, alikuwa tayari kukosa kitu chochote kile, afilisike na kurudi kama zamani, maisha ya kimasikini yaliyokuwa yamemtesa kwa kipindi chote lakini si kumkosa Evadia.
Alitaka kuwasiliana naye, alimuona siku moja tu lakini siku hiyohiyo ikaubadilisha moyo wake. Alikuwa msichana mrembo sana, aliyevutia, msichana mwenye umbo zuri, kitu kilichomhuzunisha ni kwamba msichana huyo alikulia katika maisha ya kimasikini.
Mungu hakumnyima kila kitu katika maisha yake, alimnyima utajiri lakini alimpa uzuri, kitu ambacho angebaki nacho milele na si kama utajiri ambao ungeweza kupotea siku yoyote ile. Kila alipotaka kulala, usingizi bado ulikataa kuja, alibaki akigalagala huku na kule mpaka ilipofika saa nane usiku ndipo usingizi ukamchukua.
Siku hiyo, kwa kuwa Evadia alimkaa sana kichwani, akafikia hatua ya kumuota msichana huyo, ndoto iliyomuonyesha kwamba walikuwa kanisani, alikuwa na suti nyeusi huku Evadia akiwa na shela jeupe lililomfanya kupendeza mno, ilikuwa siku ya harusi yao.
Laurence alifurahi mno lakini mara baada ya kushtuka kutoka usingizini na kugundua kwamba ile ilikuwa ndoto, alibaki na mawazo tele, moyo wake ukakosa raha kabisa.
Siku nyingine ilikuwa imeingia, Laurence akaamka kutoka kitandani, akajiandaa kwa ajili ya kwenda kazini. Alipomaliza kila kitu, akatoka ndani, akaelekea sehemu ya maegesho ya magari yake na kuchukua gari la kifahari, Ferrari Spider, gari ya gharama ambayo ilikuwa moja tu nchini Tanzania, akaingia ndani na kuondoka mahali hapo.
Laurence Mathew alikuwa miongoni mwa watu waliofanikiwa sana katika maisha yao. Alikuwa mkurugenzi wa kampuni kubwa ya Amazon Tyre ambayo ilikuwa ikihusika na uuzaji wa matairi Afrika Mashariki.
Kupitia biashara hiyo, akajikuta akitengeneza fedha, akanukia fedha na kuishi maisha ya kifahari. Katika maisha yake yote, alifikiria fedha, kila alipoamka asubuhi, kitu cha kwanza kabisa ambacho kilikuja kichwani mwake ni namna ambavyo angefanikiwa kupata fedha nyingi zaidi ya alizokuwa nazo kipindi hicho.
Kiu yake ya mafanikio, kiu yake ya kutamani kuwa bilionea mkubwa duniani ikamfanya kupambana sana, mbali na kuwa na kampuni hiyo, pia Laurence akaanzisha kampuni nyingine iliyokuwa ikishughulika na watalii katika mbuga mbalimbali za wanyama.
Kote huko, alikuwa katika harakati za kutafuta fedha, hakukubali kuona akishindwa, ili jambo lionekane kuwa kubwa na lililoshindikana, ilikuwa ni lazima alifanye, hakutaka kukata tamaa kwa kuliona jambo gumu na wakati hakuwahi kulifanya.
Akawa na fedha nyingi, akawa bilionea kijana. Wanawake wengi warembo walivyoona hivyo, wakaanza kumpapatikia lakini Laurence hakutaka kabisa kuwasikiliza. Alijua fika kwamba wasichana wengi walimfuata kwa kuwa alikuwa tajiri, aliwafahamu vilivyo hivyo akaamua kuachana nao kabisa.
Kiu yake ya mafanikio, kiu yake ya kutamani kuwa bilionea mkubwa duniani ikamfanya kupambana sana, mbali na kuwa na kampuni hiyo, pia Laurence akaanzisha kampuni nyingine iliyokuwa ikishughulika na watalii katika mbuga mbalimbali za wanyama.
Kote huko, alikuwa katika harakati za kutafuta fedha, hakukubali kuona akishindwa, ili jambo lionekane kuwa kubwa na lililoshindikana, ilikuwa ni lazima alifanye, hakutaka kukata tamaa kwa kuliona jambo gumu na wakati hakuwahi kulifanya.
Akawa na fedha nyingi, akawa bilionea kijana. Wanawake wengi warembo walivyoona hivyo, wakaanza kumpapatikia lakini Laurence hakutaka kabisa kuwasikiliza. Alijua fika kwamba wasichana wengi walimfuata kwa kuwa alikuwa tajiri, aliwafahamu vilivyo hivyo akaamua kuachana nao kabisa.
Utajiri wake haukupungua, ulizidi kuongezeka kila siku. Hakujiona, alikuwa mtu wa kuwasaidia watu wengine. Ndani ya miaka mitano tu, alikuwa na utajiri uliokadiriwa kuwa shilingi trilioni tano, tajiri mkubwa kabisa.
Kitu ambacho Laurence hakukitamani kabisa ni kujulikana, alihitaji kuwa huru, sura yake mitaani ilikuwa ngumu kujulikana. Siku nyingine ambazo alitamani sana kutembea mitaani, alivalia kawaida na kuingia mitaani, huko, alinunua karanga, alipanda daladala na kufanya mambo mengine pasipo watu kujua kwamba mtu waliyekuwa naye ndiye yule bilionea kijana aliyejijengea heshima.
Gari yake hiyo ya zaidi ya milioni mia tano alikuwa akiitumia kwenda nayo ofisini tu, alipofika huko, aliingia ofisini, alipotoka na kwenda kwenye mizunguko yake ya kawaida, aliomba gari la kawaida la mfanyakazi yeyote na kisha kuelekea mitaani, alipotaka kurudi nyumbani, aliingia ndani ya gari lake la kifahari na kurudi nyumbani.
“Hivi huyu Laurence ndiye nani? Sijawahi kumuona hata kidogo,” alisema jamaa mmoja, Laurence alikuwa pembeni ya meza ya magazeti, alikuwa akipitia magazeti.
“Hata mimi mwenyewe simfahamu, sura yake imekuwa adimu sana, kama Bakhresa” alisema jamaa mwingine.
“Kwani Laurence ndiye nani?” aliuliza Laurence huku akiwaangalia vijana wale usoni.
“Bilionea huyo! Nasikia jamaa nuksi sana, ana hela mpaka anapagawa,” alijibu jamaa mmoja.
“Kweli?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo! Kwani wewe haumfahamu?”
“Hapana!”
“Wewe mgeni nini hapa Tanzania?”
“Ni mwenyeji. Ila si umesema hata wewe haumfahamu?”
“Ndiyo! Nilimaanisha kwamba haujawahi kusikia chochote kuhusu yeye?”
“Hapana.”
“Basi umepitwa.”
Laurence alikuwa kwenye mizunguko yake kama kawaida, hakutaka kujiweka kama mtu mwenye fedha, alitaka kujua mambo mengi sana hivyo kutembea huku na kule, kuwa huru kulimfanya kuamini kwamba angeweza kujifunza mambo mengi sana.
Ombaomba waliokuwa mitaani walimsikitisha mno, hakuamini kama kulikuwa na watu waliokuwa na uhitaji wa namna ile, alihakikisha kwa kila ombaomba aliyekuwa akikutana naye, ilikuwa ni lazima kumsaidia kiasi fulani cha fedha.
Katika kipindi chote hicho alikuwa akimfikiria msichana ambaye alikutana naye siku chache zilizopita, Evadia, msichana mrembo aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati, msichana ambaye hakuona kama kulikuwa na mwingine zaidi yake.
Alizunguka sehemu mbalimbali pasipo kugundulika, alipoona kwamba alichoka sana, akaingia katika mghahawa wa chakula cha mama ntilie na kuanza kula. Alizungumza na watu wengi lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyegundua kwamba mtu huyo alikuwa bilionea, alipokula na kushiba tena huku akizungumza na watu mbalimbali kuhusu maisha kisha kuondoka zake.
Safari yake wakati huo ilikuwa ni kwenda Mburahati, mahali alipokuwa akiishi Evadia, alizikumbuka sana njia, hakutaka kupanda daladala, alifurahi kutembea mitaani, kuangalia mazingira na jinsi watu wengine walivyokuwa wakiishi.
Kutoka hapo alipokuwa mpaka Mburahati alichukua saa moja ndipo akafika Mburahati Msikitini na kisha kuingia mitaani. Alipita kwenye vichochoro vilevile, alipanda na kushuka, alizidi kusonga mbele mpaka alipofika katika nyumba ile kuukuu.
Alipoiona kwa mara ya pili, moyo wake ukamuuma zaidi, aliiangalia huku akilengwa na machozi, msichana ambaye alimfanya kutokulala vizuri usiku, msichana aliyemfanya kumfikiria sana, alikuwa akiishi katika nyumba ile iliyokuwa mbele yake.
“Shikamoo mama,” alimsalimia mwanamke aliyemkuta nje, mama yake Evadia ambaye alikuwa akisuka ukili.
“Marahaba mwanangu, hujambo?”
“Sijambo mama.”
Akayatuliza macho yake kwa mwanamke yule, alionekana kupigwa na maisha, alionekana ‘kuchoka’ mno. Moyo wake ulizidi kuumia, maisha aliyokuwa akiishi mwanamke yule yalimuumiza pia.
“Nimemkuta Evadia?” aliuliza Laurence.
“Ametoka, alikwenda hospitali.”
“Oooh! Sawa! Anaumwa?”
“Ndiyo!”
“Anaumwa nini?”
“Kwani wewe nani?”
“Rafiki yake.”
“Mmh! Sasa rafiki yake ndiyo asikwambie anaumwa nini?”
“Hahah! Sikutaka kumuuliza. Ila sidhani kama kuna tatizo endapo nikijua,” alisema Laurence.
“Utamuuliza mwenyewe akija.”
“Sawa! Atarudi muda gani?”
“Bado sijajua, ila atarudi tu,” alijibu mama yake Evadia.
Laurence hakutaka kuondoka mahali hapo, alibaki nyumbani hapo, alikaa katika mkeka huku akizungumza na mama yake Evadia ambaye muda wote alikuwa mtu wa mawazo tu, maisha aliyokuwa akiishi na binti yake yalimchanganya mno.
Laurence hakuuliza kitu chochote kile, kila alichokuwa akiambiwa, alikubaliana nacho hata kama kililazimika kuuliziwa maswali, hakutaka kufanya hivyo. Mawazo yake yalikuwa kwa Evadia tu, hakuwa na kitu kingine alichokuwa akikihitaji zaidi ya kumuona msichana huyo tu.
Muda ulizidi kwenda mbele, saa na dakika zilikatika, hakutaka kuondoka, alikuwa radhi kukaa hadi usiku wa manane lakini si kuondoka nyumbani hapo pasipo kumuona Evadia. Ilipofika saa mbili usiku, huku giza likiwa limetawala ndipo mama yake Evadia akamwambia kwamba alitakiwa kuondoka lakini Laurence akagoma.
“Haiwezekani mama, ni lazima nionane na Evadia leo,” alijibu Laurence.
“Kwani kuna nini?”
“Nataka nionane naye tu, wala usijali.”
“Sawa. Basi ngoja nikuletee chakula ule,” alisema mama yake Evadia.
“Sawa.”
Hakutaka kujivunga, aliletewa chakula, ulikuwa ugali na dagaa, pembeni kulikuwa na mchicha. Tangu awe bilionea hakuwahi kula chakula cha namna hiyo ila kwa sababu alikuwa amedhamiria kuishi maisha ya chini, akaamua kula.
Bado mama Evadia alikuwa na maswali mengi, kila alipomwangalia Laurence alishindwa kufahamu vizuri mwanaume huyo alikuwa nani. Ni kweli Evadia alikuwa na marafiki lakini hakuwahi kumuona mwanaume huyo hata siku moja.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila alipotaka kumuuliza, alibaki kimya, hakutaka kuuliza kitu chochote kile, akabaki na maswali yake moyoni.
Ilipofika saa 3:18 usiku, ndipo Evadia akatokea mahali hapo. Aliona nje ya nyumba yao kukiwa na watu wawili, mmoja alikuwa mama yake, alimtambua lakini mtu wa pili hakuweza kumtambua. Alionekana kuwa na hofu, hakujua mtu yule alikuwa nani na alifika hapo kufanya nini.
Akaanza kusogea karibu kwani kule mbali alipokuwa hakuwa akifahamu mtu huyo alikuwa nani. Mwanga wa koroboi uliokuwa ukiwaka ndiyo uliomfanya kugundua kwamba mtu aliyekuwa amekaa katika mkeka pamoja na mama yake alikuwa Laurence, mwanaume yule aliyemfuatilia siku chache zilizopita.
“Karibu Evadia,” alimkaribisha Laurence, Evadia hakujibu kitu zaidi ya kusalimia na kuingia ndani.
Moyo wa Laurence ukapoa, kitendo cha kumuona Evadia mahali hapo kiliufanya moyo wake kujisikia ahueni, hakuwa kwa siku kadhaa na kitendo cha kumuona tena mahali hapo kilimfanya kujisikia faraja.
Alimpenda, alimthamini, alitamani kuwa naye maisha yake yote. Kitendo cha kumuona mahali hapo kilimfanya kujisikia faraja, mapenzi aliyokuwa nayo kwa msichana huyo yakaongezeka zaidi.
“Kweli wewe ni rafiki yake?” aliuliza mama Evadia.
“Ndiyo!”
“Kweli?”
“Kweli tena.”
“Mbona hajazungumza hata na wewe?”
“Sijui! Inawezekana amechoka. Si ametoka hospitali? Inaelekea hajisikii vizuri,” alijitetea Laurence huku akijitahidi kuonyesha tabasamu pana usoni mwake.
Mama Evadia alionekana kuwa na wasiwasi, japokuwa Laurence aliongea kwa tabasamu pana tena huku akionekana kujiamini lakini mwanamke huyo akasimama na kuelekea ndani.
Lengo lake kubwa lilikuwa ni kumuita binti yake kwa kuamini kwamba inawezekana hakuwa amemtambua Laurence pale nje alipokuwa. Huku nyuma, mapigo ya moyo wa Laurence yalikuwa yakidunda kwa nguvu. Wakati mwingine alitamani kukimbia.
Walipendana kana kwamba hakukuwa na watu waliopendana kama walivyokuwa. Kila walipokuwa, walikuwa pamoja, walitembea pamoja huku wakati mwingine wakienda kutazama filamu pamoja.
Muonekano wao wa nje, walionekana kuwa watu waliopendana kwa mapenzi ya dhati kiasi kwamba kila mtu akahisi kwamba hakukuwa na kitu ambacho kingekuja kuwatenganisha, ukaribu wao ungeweza kwenda mbele zaidi mpaka pale ambapo wawili hao wangeoana na kuishi kama mke na mume.
Alikuwa ni kijana Dickson Maghembe na msichana aliyeitwa kwa jina la Evadia Johnson. Wawili hawa walikuwa gumzo kila walipokuwa. Japokuwa walikuwa wametoka katika familia tofauti lakini hakukuwa na mtu aliyeliangalia hilo, kila mtu alikuwa akimuona mwenzake sawa na alivyokuwa.
Evadia hakuwa msomi, aliishia darasa la saba baada ya baba yake kufariki dunia. Kuanzia hapo, hakusoma tena, maisha yake yakawa ni nyumbani tu huku akimtegemea mama yake ambaye alikuwa akifanya biashara ya mikeka aliyokuwa akiifuma yeye mwenyewe.
Kutokana na uzuri wake, wanaume wengi walimfuata Evadia, walimtaka kimapenzi kwa maneno matamu, kwa kutumia fedha lakini yote hayo yalionekana kuwa si lolote lile kwake. Alichokuwa akikiangalia ni mapenzi kwa Dickson tu, hakutaka kuwa na mwanaume yeyote yule katika maisha yake zaidi ya huyo mpenzi wake.
Dickson ambaye alikuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kila alipotoka chuoni ilikuwa ni lazima kupita nyumbani kwa kina Evadia na kuzungumza naye. Alimpenda, hapo alipokuwa akifika, alimchukua na kisha kuondoka naye kuelekea nyumbani kisha baadaye kumrudisha.
Wazazi walifahamiana, mara kwa mara walitembeleana, waliwahusia watoto wao kuhusu maisha, ni jinsi gani walitakiwa kuishi na kupenda mpaka pale watakapooana. Kila neno waliloambiwa, liliingia vichwani mwao na kutulia, ashki kubwa ya kupendana iliikamata mioyo yao, hawakuona kama kungekuwa na chochote kile ambacho kingewafanya kuachana.
“Dickson...” aliitwa Evadia.
“Ndiyo kipenzi.”
“Ninakupenda.”
“Najua hilo, ila haunishindi mimi!”
“Kweli?”
“Kwa nini nikudanganye. Ni lazima nikuoe, siwezi kukuacha maishani mwangu,” alisema Dickson huku akiachia tabasamu pana.
Waliahidiana mambo mengi, waliahidiana kuishi milele, waliahidiana kila kitu walichokiona kustahili kuingia katika mahusiano yao ya kimapenzi. Hakukuwa na mtu aliyetaka kumwacha mwenzake, kila siku waliendelea kuwa pamoja.
Wakati wakiyaongea hayo, walikuwa ufukweni, mapenzi yaliwachukua, walijikuta katika ulimwengu mwingine wa mahaba, wakiogelea katika dimbwi la mahaba na kila walipoangalia mbele, hawakuamini kama ingetokea siku moja wangeachana.
Mara baada ya kupita miaka mitatu ya uhusiano wao wa kimapenzi, hapo ndipo harakati za ndoa zikaanza kufanyika. Wakajipanga kwani hakukuwa na kitu chochote ambacho kingeweza kuwatenganisha au kuwazuia wao kufunga ndoa na kuishi pamoja.
“Evadia, ninakuahidi kwamba hakuna mwingine zaidi yako,” alisema Dickson huku akichia tabasamu pana.
“Na iwe hivyo mpenzi, ninatamani kuolewa nawe,” alisema Evadia, wakakumbatiana na kupigana mabusu mfululizo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati wakijiandaa na harusi, hapo ndipo baba yake Dickson alipomwambia kijana wake kwamba alitakiwa kuongeza elimu yake nchini Venezuela, hivyo alitakiwa kwenda huko haraka iwezekanavyo na mara atakaporudi nchini Tanzania basi mikakati ya ndoa iendelee na hatimaye wawili hao wafunge ndoa.
“Nitabaki na unyonge mpaka utakapotudi,” alisema Evadia, macho yake yalikuwa yakikusanya machozi.
“Najua mpenzi, hata mimi sitokuwa na furaha kamwe, hakika nitakuwaza wewe, sitoweza kuishi kwa furaha huku ukiwa mbali nami,” alisema Dickson, naye alionekana kuwa na huzuni mno.
Japokuwa walihuzunika lakini mwisho wa siku Dickson akaondoka na kuelekea nchini Venezuela. Kuwasiliana ilikuwa ni kwa tabu sana, kutokana na Evadia kutokupata elimu ipasavyo, hakuwa na akaunti ya barua pepe, hakuwa akitumia mtandao wowote ule wa kijamii, kitu pekee alichokuwa akikifahamu ni kutumia simu kwa kupiga na kutuma meseji tu.
Evadia alikosa raha, kila alipokuwa, alionekana kuwa na mawazo tele, hakuzoea kuwa mbali na mpenzi wake huyo, kila siku maisha yake yalikuwa ya huzuni mno. Wakati mwingine hakuwa akila chakula, mawazo yalitawala kichwani mwake, kila alipokaa, alimfikiria Dickson tu.
Siku zikaendelea kukatika, ni mara chache Dickson alikuwa akimpigia simu na kuzungumza naye na kitu pekee alichokuwa akimwambia ni kuwa mwaminifu mpaka pale ambapo angerudi tena nchini Tanzania.
“Nitakuwa muaminifu milele mpenzi,” alisikika Dickson.
“Nami nakuahidi uaminifu wangu,” alisema Evadia huku machozi yakimbubujika mashavuni mwake, hakika alisikia moyo ukimchoma mno.
Hayo ndiyo yalikuwa maneno waliyoambiana kila siku ambazo Dickson alipopiga simu. Mapenzi yaliendelea kuchipuka huku nchini Tanzania Evadia akiendelea kuwaambia marafiki zake wachache kwamba mara mpenzi wake atakaporudi nchini Tanzania basi wangeweza kuoana.
Baada ya miezi mingine kupita hapo ndipo mabadiliko yalipoanza kutokea, Dickson hakuwa mpigaji wa simu kama zamani na hata pale alipokuwa akipiga, stori zake zilikuwa za kawaida sana na hata kwenye umaliziaji wake, haukuwa kama ule uliokuwa kipindi cha nyuma.
“Nakupenda mpenzi,” alisema Evadia mara baada ya kuzungumza sana na Dickson ambaye kwa kumsikia tu, hakuonekana kuwa na raha.
“Asante...”
“Asante tena?”
“Ndiyo! Unataka nijibu nini tena?”
“Si kama zamani!”
“Kivipi?”
“Kwamba unanipenda pia,” alisema Evadia.
“Yaani neno hilo kila siku, acha kukariri Evadia,” alisema Dickson.
“Umeniita jina langu! Mungu wangu! Sijawahi kusikia ukiniita jina hilo miaka na miaka, imekuwaje?” aliuliza Evadia, alionekana kuchanganyikiwa.
“We ulitaka nikuite vipi?”
“Huwa unaniita mpenzi, imekuwaje tena?”
“Potezea.”
Aliposema neno hilo, Dickson hakutaka kuiacha simu hewani, alichokifanya ni kukata na kisha kuizima.
Evadia akachanganyikiwa, hakuamini kile kilichotokea, mpenzi wake, aliyempa thamani kubwa moyoni mwake, leo hii alikuwa akizungumza mambo yaliyompa maswali mengi kichwani mwake.
Akahisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake, machozi yakaanza kujikusanya machoni mwake na baada ya sekunde chache, yakaanza kububujika mashavuni mwake, hakika aliyasikia maumivu makali moyoni mwake.
Alikuwa na ndoto za kuolewa, zikafutika, alikuwa na ndoto za kupata maisha bora, nazo zikafutika, alihisi kuchanganyikiwa, mapenzi aliyokuwa nayo juu ya Dickson yalimzuzua mno na hata pale mambo yalipoanza kubadilika, alihisi kuchanganyikiwa.
Kauli za Dickson ambazo alizitoa siku hiyo zilimchanganya, akajiona kama akiukaribia uchizi, akabaki akibubujikwa na machozi, moyo wake ulimuuma mno. Hakujua kilichosababisha Dickson kubadilika ghafla namna hiyo, alibaki akijiuliza lakini mwisho wa siku hakupata jibu lolote lile.
Alibaki na maumivu moyoni mwake, hakutaka kumwambia mtu yeyote kile kilichokuwa kimetokea, hakutaka kumwambia mama yake wala wazazi wa Dickson kwa kuamini kwamba inawezekana siku hiyo ambayo alizungumza naye Dickson hakuwa na wakati mzuri, hivyo kuamini kwamba kama angepiga siku nyingine basi mambo yangekwenda kama yanavyotakiwa kwenda.
Usiri wenye kuumiza uliendelea kubaki moyoni mwake, hakutaka mtu yeyote yule afahamu. Baada ya kupita miezi miwili akapokea simu nyingine kutoka nchini Venezuela, alikuwa Dickson ambaye alimpa ujumbe mmoja mkubwa, ujumbe uliomsikitisha mno, alimwambia kwamba kama akipata mwanaume wa kumuoa, awe radhi kuolewa.
“Unasemaje?” aliuliza Evadia huku akionekana kushtuka.
“Kwani umesikia nini?”
“Nataka uniambie tena!”
“Kwani umekuwa kiziwi siku hizi?”
“Hapana, ila...”
“Hebu kuwa muelewa Evadia. Kama kuna mwanaume atajitokeza na kukwambia kwamba anataka kukuoa, usiichezee bahati hiyo, kuwa naye,” alisikika Dickson kwenye simu.
“Dickson...”
“Unasemaje?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwa nini unan....” aliuliza swali lakini hata kabla hajamaliza kuliuliza swali hilo, hapohapo akaanza kulia.
“Hebu acha utoto, sasa kipi kinakuliza? Kwani wewe ndiye wa kwanza kukataliwa? Nyamaza bwana, nitakuja na Luciana mwezi ujao, utamuona tu wifi yako,” alisikika Dickson na kukata simu.
Kulikuwa na watu wengi walioumizwa mioyoni mwao, wengine walilia na wengine kujiua kabisa, wengine wakakata tamaa ya kupendwa, hawakuyapenda mapenzi tena, waliwachukia wanaume na hata wanawake.
Maisha yalibadilika, wengine wakatishia kunywa sumu kutokana na maumivu makali ya kuachwa mapenzini, tena kwa watu waliokuwa wakiwapenda mno. Ingawa kulikuwa na wengi waliowahi kuumizwa mapenzini lakini kwa Evadia akahisi kwamba hakukuwa na mtu aliyepatwa na maumivu makali moyoni mwake kama alivyopata kipindi hicho.
Hakuamini kilichotokea, wakati mwingine alihisi kama yupo ndotoni na baada ya muda fulani angeamka kutoka usingizini, ukweli ni kwamba hakuwa ndotoni, kile kilichokuwa kikitokea, kilimtokea katika maisha yake, kilikuwa ni kitu halisi ambacho kilimuumiza mno.
Akakonda kwa mawazo, hakutaka kula, kila siku alipokuwa akiulizwa na mama yake tatizo lilikuwa nini, hakutaka kumwambia zaidi ya kumdanganya kwamba alikuwa akiumwa.
Moyo wake uliamini kwamba kuna siku Dickson angerudi na kumwambia kwamba alikuwa akimtania, alifanya vile kwa kuwa alitaka kujua ni kwa jinsi gani alikuwa akimpenda.
Alijipa moyo kila siku lakini pamoja na kujifariji sana, majibu yalikuwa yaleyale kwamba mwanaume huyo hakutaka kuwa naye kwa kuwa alimpata msichana mwingine aliyeitwa kwa jina la Luciana.
Hicho ndicho kilichokuwa kikimpa wakati mgumu Evadia, hali ya kuwa na mawazo mengi, wakati mwingine ikamfanya kuhisi kizunguzungu, alipokuwa akitembea mitaani, alianza kupepesuka na mwisho wa siku kuanguka chini, alipoinuka alijikuta akiwa kitandani tena huku amezungukwa na dripu zilizotundikwa juu yake.
Hali hiyo haikutokea mara moja au mara mbili, ndani ya mwezi huo ambao aliambiwa na Dickson kwamba alikuwa amempata mwanamke mwingine, kuanzia siku hiyo alikuwa kwenye hali mbaya, kuanguka na kuzimia ilitokea kwa zaidi ya mara tano kitu kilichompelekea mama yake kuwa na wasiwasi kwamba kulikuwa na tatizo.
“Evadia...”
“Abee mama.”
“Hebu niambie kuna nini.”
“Hakuna kitu.”
“Sasa kwa nini unaanguka mara kwa mara?”
“Sijui. Huwa ninajisikia kizunguzungu tu.”
“Mmmh!”
“Ndiyo hivyo!”
“Na umemwambia Dickson?’ aliuliza mama yake.
Hata kabla Evadia hajajibu swali hilo, akaanza kulia, mama yake alishtuka, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikimliza mtoto wake kiasi kile. Alijaribu kuuliza ili ajue sababu lakini hakupewa majibu zaidi ya msichana huyo kulia zaidi.
Siku zikaendelea kukatika, hakupokea simu nyingine kutoka kwa Dickson hali ilitoashiria kwamba kile kilichokuwa kimetokea, hakikuwa na utani hata mara moja, mwanaume huyo alikuwa amemaanisha alichokizungumza na kwamba alitakiwa kutafuta mwanaume mwingine wa kumuoa.
“Mama!”
“Unasemaje binti yangu?”
“Kuna kitu nataka kukwambia.”
“Kitu gani?”
“Kuhusu Dickson.”
“Amefanyaje?”
Hata kabla Evadia hakujibu swali hilo akaanza kulia, kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma, siku ambayo alipigiwa simu na mwanaume huyo kisha kuambiwa kwamba kama kungekuwa na mwanaume mwingine amemfuata kwa ahadi ya kumuoa basi akubaliane naye na huku siku nyingine akimwambia kwamba tayari alikuwa amepata mwanamke mwingine.
Alilia na kulia, mama yake alijaribu kumbembeleza na kumuuliza nini kilikuwa kinaendelea lakini hakujibu, aliendelea kulia, na aliponyamaza baada ya dakika tano kupita, hapo ndipo alipoamua kumwambia mama yake juu ya kilichokuwa kimetokea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mama yake hakuamini alichokuwa amekisikia, wakati mwingine alihisi kama alikuwa akimtania, alimjua vilivyo Dickson, jinsi alivyompenda binti yake, alifahamu ni kwa kipindi gani walikuwa wameweka ahadi ya kuoana na kuishi milele kama walivyokuwa wameambiana.
Kuambiwa kwamba mwanaume huyo alikuwa amepata mwanamke mwingine, hakika ilimchanganya na akashindwa kumwamini Evadia moja kwa moja.
“Haiwezekani,” alisema mama yake.
“Ndiyo hivyo mama! Dickson amepata mwanamke mwingine, anaitwa Luciana,” alisema Evadia.
“Dickson huyuhuyu?”
“Ndiyo mama!”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment