Simulizi : Penzi Bila Maumivu
Sehemu Ya Nne (4)
“Lakini Peter....”
“Lydia, nina moyo wa nyama, ninaumia kama wengine wanavyoumia, nisingeweza kuvumilia na ndiyo maana nimetoka Dar mpaka hapa kwa ajili yako tu, si mwingine, nimekuja kwa ajili yako, sikutaka kuona nikiendelea kuumia zaidi,” alisema Peter huku kwa mbali machozi yakianza kumlenga.
Maneno hayo aliyozungumza peter yaliuchoma moyo wa Lydia, akabaki akimwangalia tu pale kochini alipokuwa amekaa. Kwa mbali, hata naye machozi yakaanza kumlenga. Hapo ndipo alipogundua kwamba Peter alikuwa na upendo wa dhati kwake, hakuwa kama watu wengine ambao walitamani kuwa na mwanamke ili mradi, kwa Peter, alionekana kuwa tayari kufanya lolote lile lakini mwisho wa siku ampate.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Naomba unisamehe Peter, nilihisi tofauti na ulivyofanya,” alisema Lydia huku akianza kububujikwa na machozi.
“Ooppss...! Lydia, nimefanya hivi kwa kuwa ninakupenda, sitaki kukutania katika hili. Nimekuwa nikikufikiria sana na nisingekuwa tayari kukuacha ukiondoka, nilihitaji kukuonyeshea mapenzi ya dhati Lydia, hakukuwa na kingine zaidi ya hicho, ninakupenda mno,” alisema Peter huku akisimama na kuanza kumsogelea msichana huyo.
Lydia naye hakubaki pale alipokuwa, akapiga hatua kumsogelea Peter alipomfikia, wote wawili wakakumbatiana na kuanza kulia, upendo wa dhati ukaanza kuchipua moyoni mwa msichana Lydia, machozi yao yakaanza kulowanisha migongo yao. Huku wakiwa kwenye hisia kali za kimapenzi, mara mchungaji Marcus na mkewe wakatokea sebuleni hapo, kile walichokiona, kikawashtua.
Kila mmoja alistaajabu juu ya kile kilichokuwa kimetokea chumbani pale, walishindwa kuyaamini macho yao juu ya kile walichokuwa wakikiangalia, kiliwashangaza na hawakuamini kama Peter na Lydia walikuwa wamekumbatiana.
Peter na Lydia walikuwa wakibubujikwa na machozi yaliyolowanisha migongo yao, hisia kali zikawachoma wazazi hao na kugundua kwamba watoto hao walikuwa wakipendana kwa mapenzi ya dhati.
Hawakuongea kitu, walibaki wakiwaangalia tu, kwa kiasi fulani walibaki wakiwa na furaha kwani kumuona mtoto wa mchungaji akiwa amemkumbatia binti yao, kidogo wakafarijika mioyoni mwao.
“Ninakupenda Lydia,” alisema Peter, machozi yaliendelea kumbubujika mashavuni mwake huku akimwangalia Lydia usoni.
“Nakupenda pia Peter, naomba unisamehe kwa kila kitu kilichotokea,” alisema Lydia.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa uhusiano wao wa kimapenzi. Walipendana na kuthaminiana huku kila mmoja akimuahidi mwenzake kwamba angekuwa mwaminifu katika kipindi chote cha maisha yao.
Peter hakutaka kuwa msiri, alichokifanya ni kuwaambia wazazi wake kuhusu Lydia, walifurahi kusikia hivyo na wakatoa baraka kwa kila kitu kitakachotokea huku wakitahadharishwa kutokufanya mapenzi mpaka hapo watakapoona na kuwa mume na mke.
“Hilo si tatizo, hatutoweza kufanya,” alisema Peter.
Mpaka anaanza masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Peter alikuwa mwaminifu kwa asilimia mia moja japokuwa kulikuwa na wasichana wengi waliokuwa wakimfuatilia lakini bado uaminifu wake kwa Lydia haukupungua.
“Mchungaji, unamjua Tatiana?” aliuliza mwanachuo mmoja, alikuwa akimuuliza Peter ambaye katika kipindi chote alichokuwa chuoni hapo, alipenda kuishi kama mcha Mungu, kila wakati Biblia mkononi kiasi kwamba wanachuo wengine wakampachika jina la mchungaji.
Aliposikia jina la Tatiana, aliusikia moyo wake ukilipuka na kuanza kudunda kwa nguvu, hakutegemea kulisikia jina hilo katika maisha yake, damu ikaanza kutembea kwa kasi mishipani mwake huku akijikuta furaha yote aliyokuwa nayo ikianza kupotea, kumbukumbu juu ya msichana Tatiana zikaanza kujirudia kichwani mwake kama mkanda wa filamu.
“Umesemaje?”
“Tatiana anakuja. Aaah! Kumbe wewe mchungaji, utakuwa hamfahamu huyu,” alisema mwanachuo huyo huku akitoa kicheko cha chini.
Hakuwa akipenda miziki ambayo iliitwa ya kidunia, alipenda kusikiliza kwaya lakini hiyo haikutoshakabisa kutokumkumbuka Tatiana, alikumbuka jinsi alivyomuumiza kwa kutembea na mwanaume mwingine, tena kubusiana ukumbini huku akijua kwamba alikuwa amemuacha nchini Tanzania.
“Ndiye nani huyo?” akajifanya kuuliza.
Mwanamuziki mpya, ni noma sana, Mtanzania huyo!”
“Anaimba nyimbo za kidunia?”
“Hahahaha! Ndiyo!”
“Wala simfahamu!”
“Nilijua tu.”
Peter hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea darasani. Moyo wake ukawa kama umefukunyuliwafukunyuliwa, mawazo juu ya Tatiana yakaanza kumwandama tena.
Japokuwa kilikuwa kimepita kipindi cha miaka mitatu lakini akajikuta yale mapenzi aliyokuwa nayop juu ya msichana yule yakianza kurudi tena moyoni mwake. Aliichukia hali hiyo lakini hakuwa na jinsi kwani kila alivyokuwa akijilazimisha kuitoa, iliendelea kuwepo moyoni mwake.
Pasipo kupenda, naye akajikuta akianza kufuatilia kuhusu Tatiana. Mpaka siku ambayo msichana huyo alikuwa akiingia nchini Tanzania huku watu wakijipanga barabarani, naye alikuwa miongoni mwa watu hao.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila alipokuwa akimwangalia msichana huyo garini, moyo wake ulimuuma mno, alijikuta akimchukia sana zaidi ya alivyomchukia shetani. Akatamani apate bunduki na kmuua msichana huyo hapohapo garini.
“Nisamehe Mungu! Ninamchukia mno Tatiana,” alijikuta akisema.
Usiku wa siku hiyo, Peter alitulia chumbani kwake na kuanza kulia, ni kweli alimchukia mno Tatiana lakini akajikuta akimuomba Mungu msamaha kwa kile alichokuwa amekisema. Alichokifanya ni kumpigia simu mpenzi wake, Lydia kwani kila alipojaribu kuomba Mungu, hakujisikia kuwa katika hali ya kawaida.
“Una nini mpenzi? Mbona unalia?”
“Naomba unisaidie kuomba.”
“Kuna nini?”
“Nina chuki kali moyoni.”
“Chuki?”
“Ndiyo! Naomba unisaidie!”
“Unamchukia nani?”
“Tatiana!”
“Tatiana yupi?”
Peter hakujibu swali hilo, akaendelea kulia zaidi kwani kila alipomkumbuka msichana huyo, alizidi kuumia moyoni mwake.
Katika kipindi hicho kikaonekana kuwa kibaya kwake, kila alipofungulia televisheni, alikutana na matangazo yaliyomhusu Tatiana, kila aliposikiliza redio bado alisikia mengi kuhusu Tatiana.
Siku iliyofuata, matangazo yakaanza kubandikwa chuoni kwamba yule muimbaji aliyekuwa akiitetemesha dunia kwa kipindi hicho, Tatiana alitarajiwa kufika chuoni hapo. Peter alipoyaona matangazo hayo, moyo wake ukaumia mno. Hakutaka kumuona tena msichana huyo, mbaya zaidi, leo kulikuwa na mabango yaliyobandikwa kwamba msichana huyo angefika chuoni hapo.
Tatiana akawa gumzo chuoni, kila kona alizungumziwa yeye tu jambo lililomuuma mno Peter. Kuna kipindi alitamani kuwa mkuu wa chuo na asitishe ule ujio wa msichana huyo chuoni hapo kwani kwake hakupenda kabisa hilo litokee.
Mishemishe ziliendelea chuoni, maandalizi mazito yalipamba moto kwa ajili ya kumkaribisha mwanamuziki huyo aliyekuwa kipenzi cha watu wengi duniani. Kila mtu aliyesikia kwamba Tatiana alitarajiwa kwenda chuo kikuu, akakapanga kwenda huko kwa kuamini kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima Tatiana aimbe.
Wale waliokuwa Kibaha, Bagamoyo na sehemu nyingine zilizokuwa karibu na Jiji la Dar es Salaam wakafika jijini hapo kwa ajili ya kumuona msanii huyo aliyesifika kwa uzuri na sauti yake.
Siku ya ujio wake, japokuwa kulikuwa na ulinzi mkali uliokuwa umewekwa kwamba hakutakiwa kuingia mtu ambaye hakuwa mwanachuo wa chuo hicho lakini walishindwa kuwazuia watu hao, wakajikuta watu wote wakiingia chuoni hapo, tena hata wale wasiokuwa na vitambulisho.
Uwanja wa mpira chuoni hapo ukaonekana mdogo, watu wengi walikuwa wamejazana, jukwaa kubwa lilikuwa limewekwa na kupambwa vilivyo, kila mmoja alitaka kumshuhudia msichana huyo ambapo taarifa zaidi zilisema kwamba angeweza kutumbuiza.
“Mchungaji! Hata wewe?” alisikika mwanachuo mmoja wa kike, alikuwa akimwambia Peter.
“Hata mimi nini?”
“Upo hapa! Nilidhani upo nyumbani unatuandalia neno la kesho kanisani,” alisema msichana huyo, alikuwa akimtania Peter.
Peter hakutaka kuondoka, naye alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa uwanjani hapo ambao walitaka kumuona msichana huyo akiwa jukwaani. Japokuwa moyo wake ulimuuma mno lakini hakuthubutu kabisa kuondoka uwanjani hapo.
Dakika ziliendelea kukatika, watu walizidi kuongezeka zaidi mpaka kufikia watu zaidi ya elfu ishirini uwanjani hapo na hakukuwa na dalili za watu kukata. Ilipofika saa saba kamili mchana, ving’ora vikaanza kusikika, hakukuwa na maswali kwamba yule aliyekuwa akitarajiwa kuingia mahali hapo alikuwa nani.
Watu wakaanza kukimbilia kule kulipokuwa pa kuingilia, kila mtu alitaka kumuona Tatiana tu. Pikipiki mbili zilitangulia mbele na magari mengine kufuata, alionekana kuwa na msafara uliomkaribia rais wa nchi.
Watu wakaanza kupiga kelele huku wakiliimba jina lake ambalo lilionekana kuwa kero kwa Peter aliyekuwa akifuatilia kila kilichokuwa kikiendelea uwanjani hapo. Baada ya magari kusimama, Tatiana akashuka huku akiwa na Buffet kitu kilichoibua shangwe nyingi uwanjani hapo.
“Huyu demu mkali sana, sijui kwa nini sikuonana naye kabla ya kuwa supastaa!” alisikika akisema jamaa mmoja.
“Daah! Halafu Mzungu mwenyewe boya tu ndiye anamchukua dada yetu,” alisema jamaa mwingine.
Tatiana akaanza kupiga hatua kwenda jukwaani, alikuwa akipunga mikono yake hewani, watu walizidi kushangilia, moyoni mwa Peter, alitamani achimbe kaburi na kujizika kwani kila alipokuwa akimwangalia msichana huyo jukwaani, alizidi kuumia. “Ninakuchukia Tatiana,” alisema huku akiuma meno yake kwa hasira.
****
Nathan alimaanisha alipotamka kwamba mara ya kwanza kwamba alitaka kumuua msichana Tatiana, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, japokuwa kipindi kirefu kilipita lakini bado alikuwa na hasira mno na msichana huyo.
Hakutaka kuona akiendelea kuishi, kwa kile alichokuwa amemfanyia, alijiapiza kwamba ilikuwa ni lazima amuue hata kama angetumia kiasi gani cha fedha. Alichokifanya ni kuanza kumfuatilia kwani alikwishajua kwamba Petrov alishindwa hivyo alitaka kuingia kazini yeye mwenyewe.
Siku zikaendelea kukatika, hakuacha kumfuatilia msichana huyo, kila siku alihakikisha anaingia katika mitandao na kuona msichana huyo alikuwa akifanya nini kwa kipindi hicho kwani kila siku aliuhisi moyo wake ukiwaka moto kwa hasira.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alimuacha Dassy kwa ajili ya msichana huyo, aliumia sana kwani alipanga mambo mengi na msichana Dassy lakini mwisho wa siku, kila kitu kikabadilika, ndoto alizokuwa nazo kwa msichana huyo zikapotea kwa sababu ya Tatiana, hakutaka kuona akishindwa kumuua msichana huyo.
“I will kill her myself,” (nitamuua mimi mwenyewe) alisema mara baada ya kuona kwamba kwa mara ya kwanza msichana huyo alitarajiwa kwenda nchini Tanzania.
Hakutaka kukubali, hiyo kwake ikawa nafasi pekee ya kutaka kufanya kile alichotaka kukifanya, hivyo akajiandaa kwa ajili ya kwenda nchini Tanzania ili kukamilisha kile alichokuwa amekipanga.
Ndani ya ndege alikuwa na presha kubwa, alijiona akichelewa kufika nchini Tanzania, alitamani kasi iongezeke na hatimaye ajikute nchini Tanzania akiwa amewahi kabisa kwa ajili ya kumuua msichana huyo.
Ndege ilichukua masaa kumi na moja na ndipo ikaanza kuingia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere. Iliposimama, hakutaka kusubiri, akaanza kuteremka na abiria wengine na kufauta taratibu zote alizotakiwa kufuata kama abiria.
Alipotoka nje ya jengo la uwanja huo, akachukua teksi ambayo ilimpeleka mpaka katika Hoteli ya Serena ambapo akateremka na kuchukua chumba. Chumbani, akili yake haikutulia, muda wote alikuwa akifikiria kufanya mauaji tu.
Zilibakia siku mbili hata kabla Tatiana hajaingia nchini Tanzania hivyo alichokifanya ni kuanza kutafuta bastola ndogo kwa ajili ya kufanya kazi aliyotaka kuifanya. Kazi haikuwa nyepesi hata mara moja kwani hakuwa akifahamu sehemu zozote nchini Tanzania ambapo kungemfanya kupata bastola kwa urahisi sana, hivyo baada ya kutafuta kwa kipindi kirefu, akaona njia nyepesi ya kumuua msichana huyo ilikuwa ni humohumo hotelini alipokuwa amefikia.
Alichokifanya ni kusikilizia juu ya hoteli ambayo angefikia msihana huyo ambapo aliamini kwamba angefanikiwa kufanya mauaji hayo, hivyo moyo wake ukabaki na kimuemue.
“Anatajia kuingia lini?” ilisikika sauti simuni, alikuwa akizungumza na Petrov.
“Kesho!”
“Nataka nije Tanzania.”
“Unasemaje?”
“Nataka kuja kumalizia pale nilipoachia,” alisikika Petrov.
Japokuwa Nathan alikuwa amefika nchini Tanzania kwa ajili ya kukamilisha kazi aliyokuwa ameipanga kwa kuwa Petrov alishindwa, mwanaume huyo naye hakutaka kubaki Liberia, kiasi cha fedha alichokuwa amelipwa pasipo kazi kufanyika ikamuuma sana hivyo akataka kusafiri kwenda nchini Tanzania.
Usafiri wake ulikuwa ni wa meli kubwa ya mizigo, kuna kipindi aliteremka na kupanda boti iendayo kasi huku lengo likiwa ni kufika nchini Tanzania pasipo kukamatwa.
Kwa Nathan, mambo yalikwenda kama alivyotaka, mpaka siku ambayo Tatiana alikuwa akishuka kutoka kwenye ndege na kuanza kuelekea hotelini alikuwa akifuatilia kila hatua, alionekana kuwa na hasira mno, kila alipomwangalia msichana huyo, alitamani kumuua.
Msafara huo mkubwa ukaishia katika Hoteli ya Blue Pearl, hapo ndipo Nathan alipotaka kufanya mauaji yake, hivyo alipoona kwamba msichana huyo amechukua chumba hotelini hapo, na yeye akaenda kuchukua chumba.
“Utakaa muda gani?” aliuliza msichana wa mapokezini.
“Wiki moja.”
“Naomba passport yako,” alimwambia Nathan, akampatia.
“Sawa. Karibu sana, jisikie huru,” alisema msichana wa mapokezi, akamuita kijana ambaye akabeba mizigo yake na kuanza kuelekea kwenye lifti kwa ajili ya kupanda juu mpaka kilipokuwa chumba chake.
Walipofika katika ghorofa iliyokuwa na chumba chake, akateremka na kijana yule kisha kuanza kukifuata. Akachukua kadi maalumu ya kufungua milango na kuipitisha kwenye kimashine kidogo na mlango kufunguka.
“Nashukuru sana,” alimwambia kijana aliyembebea mizigo, akaingiza mkono mfukoni na kutoa dola kumi na kumpatia.
“Nashukuru pia.”
“Ila samahani.”
“Bila samahani.”
“Hivi naye Tatiana yupo hoteli hii?”
“Yeah! Yupo, amefika leo mchana.”
“Daah! Nitatamani kumuona, nimesafiri kutoka Marekani mpaka hapa kwa ajili yake, ninatamani sana nimuone,” alisema Nathan.
“Nafikiri utamuona tu.”
“Utaweza kunisaidia?”
“Kumuona Tatiana?”
“Hapana! Yaani kama nitakuwa na uhitaji wa baadhi ya vitu.”
“Hakuna tatizo. Namba yangu hii,” alisema mhudumu yule huku akimpa kikaratasi kilichokuwa na namba yake.
Alihitaji msaada, alijua kwamba asingeweza kufanya kila kitu peke yake hivyo kulikuwa na baadhi ya vitu ambavyo angehitaji kununuliwa na kijana huyo kwani hakujua mahali kulipokuwa na maduka.
Usiku wa siku hiyo, hakulala, alikuwa akifikiria ni kwa namna gani angefanikiwa kufanya kile alichotaka kukifanya, kile kilichomfanya kusafiri kutoka nchini Liberia mpaka nchini Tanzania. Alijipa moyo kwamba angefanikiwa kufanya kile alichopanga kukifanya hivyo alitaka kusubiri muda ufike ili akamilishe.
Alikosa bunduki, hivyo aliona kitu kizuri kufanya mauaji ni kumuua Tatiana kwa sumu tu kitu kilichoonekana kuwa chepesi sana kufanyika, tena kingefanyika pasipo kugundulika. ***** “Ninawapenda Watanzania wenzangu,” alisema Tatiana, watu wote waliokuwa uwanjani wakapiga kelele za shangwe.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku hiyo alikuwa akizungumza mbele ya maelfu ya Watanzania kwa mara ya kwanza. Msichana huyo alionekana kuwa mrembo mno, watu hawakuamini kila walipokumbuka kwamba alikuwa msichana masikini aliyetoka mkoani Shinyanga, tena vijijini huku akiwa kipofu.
Hapo ndipo walipoamini kwamba fedha zilikuwa na uwezo wa kumbadilisha mtu yeyote yule, kila alipokuwa, Tatiana alionekana kuwa mtu mwenye fedha nyingi, aliishi ndani ya maisha ya kifahari, alitembelea fedha, kila alipopumua, wakati mwingine alihisia akipumulia fedha tu.
Peter ambaye alikuwa miongoni mwa maelfu ya watu waliokuwa uwanjani hapo aliendelea kufuatilia kila kitu, moyo wake uliumia mno, hakuamini kama msichana yule aliyesimama jukwaani aliwahi kuwa mpenzi wake aliyempenda kwa penzi la dhati.
Akabaki akimwangalia huku akionekana kuumia mno moyoni mwake. Kuna wakati alijikuta akibubujikwa na machozi, aliyafuta na kuendelea kumtazama msichana yule.
“Nawashukuru sana....basi acha iwe muda wa picha,” alisema Tatiana na kuelekea kulipokuwa na viti na kutulia.
Watu hawakutaka kutulia, waliposikia kwamba Tatiana alitaka kupiga picha na watu waliokusanyika mahali hapo, kila mtu akajiandaa vilivyo, kila mmoja alitaka kuwa mbele ili aweze kupiga picha na msichana huyo.
Japokuwa mkuu wa chuo alikuwa akizungumza, hakukuwa na mwanachuo aliyemsikiliza, walichokuwa wakikitaka mahali hapo ni kupiga picha na msichana huyo tu. Tatiana alichukulia kila kitu kuwa kawaida, hakufikiria kuhusu fujo ambazo zingetokea mahali hapo, alichikfanya mara baada ya mkuu wa chuo kumaliza ni kuteremka jukwaani, walinzi walitaka kumzuia, akawakataza kwa kuamini kwamba Watanzania walikuwa watu wa amani.
Alipofika chini, watu wakaanza kumsogelea na kila mmoja kung’ang’ania kupiga naye picha. Zilionekana kama fujo fulani lakini kwa Tatiana alikuwa akijsikia furaha tu, waliokuwa na kamera au simu zenye kamera ni miale ya kamera tu ndiyo iliyokuwa ikimulika.
Watu wengi wakamvamia huku wakimshika huku na kule, wengine wakijipiga naye picha, wala hazikupita dakika nyingi, Tatiana akaanza kuhisi kitu, ghafla, hata kabla hajajua ni kitu gani kilikuwa kimetokea, akaanza kuona giza mbele yake hali iliyomfanya kila mtu kumshangaa, hata Buffet ambaye alikuwa kule jukwaani, akaonekana kugundua kitu kwani msichana huyo aliyekuwa katikati ya watu waliokuwa wamemzunguka alionekana kuwa tofauti.
“Damu...damu...damu....” zilisikika kelele, kila mtu aliyesikia hivyo akasogea pembeni.
Buffet akashtuka, maprofesa wakashtuka mara baada ya kusikia wanachuo wakipiga kelele kusema kwamba waliona damu, kwa harakaharaka wakaanza kushuka jukwaani kumfuata Tatiana kwani tayari alianza kulegea na hapohapo akaanguka chini, damu zilikuwa zikimtoka, nguo nzima ililowanishwa na damu.
“Sogea pembeni, sogea pembeni,” alisema Buffet mara baada ya kufika pale chini.
Tatiana alikuwa hoi chini, damu zilikuwa zikimtoka, kitu cha kwanza kabisa alichokifanya Buffet ni kuchukua shati lake kwa ajili ya kuzuia damu iliyokuwa ikimtoka Tatiana.
Ubavuni mwake, upande wa kushoto alikuwa amechomwa kisu huku mkono wake maeneo ya kiwiko kwa mbele alichanwa na kisu hicho hali iliyoufanya mshipa wake wa damu ambao ulidhibiti mkono na vidole kuchanwa vibaya na hiuvyo kusababisha damu nyingi kuanza kumtoka.
Hakukuwa na mtu aliyefahamu ni nani alikuwa amemchoma kisu msiahcna huyo. Hapohapo polisi wakaanza kuzunguka huku na kule kuona kama wangeweza kumpata mtu aliyekuwa na kisu mkononi lakini hawakuweza kumpata mtu yeyote yule.
Tatiana aliugulia maumivu pale chini, kadiri muda ulivyozidi kwenda ndivyo damu zile zilipozidi kumtoka. Buffet akachanganyikiwa, alijitahidi sana kuzizuia damu za Tatiana kutoka lakini hazikuweza kukata, bado ziliendelea kumtoka mfululizo hali iliyomaanisha kwamba kama wasingefanya haraka iwezekanavyo basi msichana huyo angeweza kufariki dunia.
Kwa haraka sana gari likasogezwa, akapakizwa na kisha kuanza kupelekwa katika Hospitali ya Marie Stoppes ambayo haikuwa mbali na chuo hicho. Ndani ya gari, bado damu ziliendelea kumtoka Tatiana, kila mmoja akaona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa msichana huyo kuvuta pumzi ya dunia hii.
Hasira ilimkaba Peter kwa kiwango cha mwisho kabisa kiasi kwamba akashindwa kuvumilia, kila aliposimama mahali pale alihisi akishindwa kabisa kuzizuia hasira zake, hakutaka kuendelea kubaki hapo kwani kila alipokuwa akimwangalia Tatiana aliyekuwa amekaa kule jukwaani, alishikwa na hasira zaidi.
Akaondoka uwanjani hapo, kitu alichokuwa amedhamiria siku hiyo kilikuwa ni kumuua msichana huyo tu, alipoondoka, safari yake iliishia nje ya eneo la chuo, karibu na geti la kuingilia Mlimani City upande wa Chuo cha Ardhi ambapo kulikuwa na vibanda vingi, akakifuata kibanda kimoja na kununua kisu ambacho akataka kinolewe kabisa.
“Ni lazima nimuue, aliniumiza sana, siwezi kumuacha,” alijisemea Peter na kuondoka mahali hapo kurudi chuoni.
Alipofika, akakificha vizuri kisu chake kiunoni kwa kulishusha zaidi shati lake na kisha kukaa katikati ya wanachuo waliokuwa pale uwanjani. Mpaka Tatiana anasimama na kuanza kuzungumza, tayari hasira alizokuwa nazo zilimkaba kooni kabisa na akashindwa kuvumilia.
Tatiana alianza kwa kuongea mambo mengi, wanachuo walikuwa wakipiga makofi, kuna wengine aliwasikia wakiusifia uzuri wa msichana yule, kuna wengine walikuwa wakizungumza mengi kuhusu Tatiana lakini Peter hakutaka kujali, lengo alilokuwa ameliweka kichwani mwake ni kumuua msichana huyo tu.
Muda wa kupiga picha ulipofika, naye akajichanganya katikati ya watu, akamfuata Tatiana kwa nyuma. Kutokana na idadi kubwa ya watu kumzongazonga Tatiana, hakukuwa na mtu aliyemuona pale alipotoa kisu kisiri, akamsogelea Tatiana, watu walipoendelea kusukumana, akamchoma msichana huyo kisu cha ubavuni kisha kumkata mkononi, sehemu alipoamini kulikuwa na mshipa mkubwa wa damu ukipita.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipofanya hivyo, hakutaka kukaa, kwa haraka sana akakiweka kisu kiunoni na kuondoka mahali hapo kabla hajashtukiwa na mtu yeyote yule. Kilichotokea nyuma, hakutaka kukifuatilia kwani alijua iwe isiwe ilikuwa ni lazima Tatiana afe.
“Mchungaji,” aliita msichana mmoja, alikuwa amemuona Peter akielekea darasani.
“Naam!”
“Una damu tumboni,” alisema msichana yule,
Peter akaangalia, akaona kweli alikuwa na damu zilizotoka kwenye kisu kile alichokificha, hazikuwa nyingi ila kutokana na shati jeupe alilolivaa, zilionekana vizuri.
“Mungu wangu! Kumbe nimechunika!”
“Vipi tena.”
“Nilijaribu kuruka zile seng’enge!”
“Hahha! Wewe si wa kwanza, wengi washawahi kujichana nazo, nenda kanawe,” alisema msichana yule.
Peter akashusha pumzi, alichokifanya ni kwenda bafuni na kisha kunawa, akalivua shati lake na kuondoka kuelekea katika chumba alichokuwa akiishi mmoja wa rafiki yake na kuchukua shati kisha kuondoka katika mazingira ya chuo.
Moyo wake ukawa na furaha mno, hakuamini kama angeweza kufanikisha kile alichokuwa amekipanga, kila alipokuwa, alikenua, aliona kufanya jambo moja kubwa tena kwa ujasiri mkubwa mno. Kila alipokuwa, tabasamu pana lilikuwa usoni mwake.
Kile alichokuwa amekifanya, kwake kikaonekana kuwa sahihi, hakutaka kumuomba Mungu msamaha kwa dhambi aliyokuwa ameifanya, wakati mwingine, alijipa haki ya kufanya jambo lile kwa kisingizio cha Tatiana alistahili kufanyiwa unyama kama ule.
***** “Jamani kuna nini tena?” aliuliza nesi.
“Mchukueni kwanza.”
“Kwanza tuambieni nini kimetokea,” alisema nesi yule, hakuwa akijua kama wale waliomleta Tatiana alikuwepo na mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Slaam.
“Nesi! Mazungumzo baadae, okoa maisha kwanza.”
“Amefanya nini? PF3 iko wapi?” aliuliza nesi yule.
Hali ya Tatiana iliendelea kuwa mbaya, wasingeweza kubaki pale nje huku wakizungumza na nesi yule, walichokifanya ni kuingia ndani huku kila mmoja akionekana kuchanganyikiwa.
Kila mtu aliyemuona Tatiana, alibaki akisikitika, damu ziliendelea kumtoka mfululizo hali iliyoonyesha kwamba muda wowote ule angeweza kufariki dunia jambo ambalo hakukuwa na mtu aliyetaka kuliona,
Walipofika mapokezini, wakamtambulisha Tatiana, kila mtu aliyesikia akashtuka, kwa haraka wakamchukua na kumpeleka katika chumba cha upasuaji ambapo huko kazi ikaanza rasmi.
Buffet na mkuu wa chuo pamoja na baadhi ya wanachuo waliotangulizana nao walibaki nje, kila mmoja alionekana kuwa na mawazo, tukio lililokuwa limetokea lilimstaajabisha kila mtu kwani hakukuwa na tukio kama hilo ambalo liliwahi kutokea tangu chuo hicho kianzishwe.
Buffet ndiye aliyeonakana kuchanganyikiwa zaidi, kila alipokaa, alikuwa akiongea peke yake tu. Hakukuwa na mtu aliyemuongelesha mwenzake kwa kipindi hicho, kila mmoja akabaki na lake moyoni mwake.
Madaktari walijifunugia ndani ya chumba kile cha upasuaji wakimshughulikia Tatiana, baada ya dakika ishirini, tayari waandishi wa habari wakafika hospitalini hapo kwa ajili ya kutaka kuchukua matukio yaliyokuwa yakiendelea.
“Imekuwajekuwaje tena?” aliuliza Consolatha, mwandishi mahiri kutoka katika Gazeti la Undani.
“Naomba mtuache kwanza, hali haipoa sawa.”
“Amekufa?”
“Consolatha, maneno gani hayo unayozungumza!” alisema mwanachuo mmoja, kutokana na umaarufu wa mwandishi huyo kwenye habari za udaku, alikuwa akijulikana sana.
Kila daktari aliyekuwa akitoka ndani ya chumba kile, alifuatwa na wanachuo hao akiwemo Buffet wakitaka kujua kile kilichokuwa kikiendelea ndani juu ya hali ya Tatiana. Hakukuwa na mtu yeyote aliyezungumza lolote lile ila nyuso zao zilionyesha dhahiri kwamba hali ndani haikuwa nzuri hata mara moja.
Hapo ndipo walipoanza kujiuliza juu ya mtu aliyefanya tukio lile, hawakumjua zaidi ya kushtukia msichana huyo akitokwa na damu tu, Umati mkubwa wa wanafunzi waliokuwa wamemzunguka ndiyo uliowafanya kutokugundua ni nani aliyekuwa amefanya jambo lile.
“Ni lazima uchunguzi ufanyike, hii ni aibu kubwa professa,” alisema mwanachuo mmoja, alikuwa akimwambia professa.
“Ndiyo hivyo! Hivi ilikuwajekuwaje?”
“Hata mimi sikuona vizuri, nilishtukia akitokwa damu.”
“Hii ni hatari sana. Ni lazima aliyefanya unyama huu apatikane, tunataka kujua na sababu pia,” alisema professa.
Taarifa za kuchomwa kisu kwa Tatiana zikaanza kusambaa kama upepo, mitandaoni, watu wakawa wa kwanza kuziandika kitu kilichopeleka kusambazwa duniani kwa haraka sana. Kila mtu aliyezisoma taarifa hizo alipigwa na mshangao, hawakuamini kile kilichokuwa kimetokea, nchi ambayo watu waliita kuwa ya amani, kutokea kitendo kama kile cha kikatili kilishusha heshima ya nchi.
Duniani kukawa gumzo, nchi ya Tanzania ikaanza kusikika tena kutokana na kile kilichokuwa kimetokea. Hapo ndipo watu walipogundua kwamba msichana huyo alikuwa na maadui wengi duniani hivyo alitakiwa kupewa ulinzi wa nguvu.
Tukio hilo lilifananishwa na lile la gari kulipuka kwa bomu nchini Marekani huku akiwa ndani ya gari hilo na rafiki yake. Kwa sababu katika tukio hilo mhusika alijulikana kwamba ni Petrov, hivyo hata katika tukio hilo lililotokea, watu wakajua kwamba kulikuwa na mkono wa Petrov.
“Ila huyu jamaa kwa nini anafanya hivi?” aliuliza jamaa mmoja.
“Hata mimi sijui.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jeshi la Polisi la Tanzania halikukaa kimya, kwa kile kilichotokea kilimaanisha kwamba nchi hiyo ilikuwa ikiingia kwenye aibu kubwa kimataifa hivyo amri kutolewa kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima mtu aliyefanya kitu hicho ajulikane na kukamatwa kisha kufikishwa katika vyombo vya habari haraka sana.
Chuoni hakukukalika, kila kona kulikuwa na gumzo kuhusu kile kilichokuwa kimetokea. Kila mmoja alihuzunika, hawakuamini kama kungekuwa na mwanachuo ambaye angefanya kitu kama kile kwani kila walipoangalia na kufuatilia, hawakuona kama msichana Tatiana aliwahi kuishi Dar es Salaam, makazi yake yalikuwa Shinyanga kijijini, je huyo adui alikuwa nani?
“Huyu atakuwa yule Mrusi! Hivi anamtafutia nini huyu demu?’ aliuliza mwanachuo mmoja.
“Warusi wana roho mbaya sana, hawaangalii sababu, wao wanachotaka kuua tu, hakuna kingine,” alisema jamaa mwingine.
Hiyo ndiyo ikawa habari ya mjini, kila kona tukio hilo lilikuwa likizungumziwa tu. Redioni, taarifa hizo zilitangazwa huku magazeti yote ambayo yalitarajiwa kutoka siku inayofuata, yalionekana kuwa na habari hiyo kwa ukubwa zaidi, hivyo watu wakapanga kuyanunua ili wajue ukweli.
“Dokta! Tuambie ukweli!” alisema professa huku akiinuka kitini.
“Ukweli gani?”
“Juu ya Tatiana. Masaa matano yamepita, hatujui lolote lile,” alisema Professa.
“Naomba twendeni ofisini,” alisema dokta.
Hawakutaka kuchelewa, walichokifanya, wote wakaanza kumfuata daktari yule ambaye alipiga hatua za harakaharaka kuelekea ofisini mwake. Kwa muonekano aliokuwa nao tu ulionyesha kwamba kulikuwa na jambo baya lililokuwa limetokea mule chumbani hivyo kila mmoja akashikwa na hofu moyoni mwake.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa tayari kupokea taarifa zozote mbaya, walimpenda Tatiana, hawakutaka kuona mschana huyo akifariki dunia kwani bado alionekana kuwa na kazi kubwa ya kuendelea kuitangaza nchi ya Tanzania.
Baada ya kufika ofisini, daktari yule akakifuata kiti chake na kutulia. Akaanza kuwaangalia watu wale, kwa mbali, machozi yakaanza kumlenga, kila mtu akahofia, hasa Buffet ambaye akashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.
******
“Hali yake ni mbaya sana, mshipa mkubwa unaopeleka damu na ambao unavidhibiti vidole vyake umechanika,” alisema dokta huyo aliyekuwa na kibati kidogo pembeni ya kifua chake katika koti lake kilichoandikwa Dk. Henry.
“Kwa hiyo atapona?” aliuliza Buffet huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Naweza nikasema hamsini kwa hamsini. Ule ni mshipa muhimu sana, umechanika kiasi kwamba amepoteza kiasi kikubwa mno cha damu,” alisema Dk. Henry na kuendelea:
“Hali imeonekana kuwa mbaya zaidi tumboni, kisu kile kilizama na kuchana nyama zinazoshikilia mbavu kiasi kwamba kimeifanya damu kuvilia ndani ya tumbo lake hali ambayo inayoonyesha ni ya hatari sana, inaweza kumletea matatizo zaidi hata kifo chake,” alisema Dk. Henry huku akimwangalia kila mtu usoni.
Maneno aliyowaambia yaliwashtua mno, yaliongeza huzuni kwa Buffet ambaye bado alikuwa na mapenzi ya dhati kwa msichana wake ambaye aliamini kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima amuoe hapo baadae.
Dk. Henry hakutaka kuishia hapo, aliwapa maelezo ya kutosha kwamba hali ya Tatiana ilikuwa mbaya sana, tangu kipindi alichozimia, mpaka katika kipindi hicho hakuwa amerudiwa na fahamu. Alikuwa kwenye hali mbaya mno, kwa kumwangalia kwa nje tu ungeweza kugundua kwamba Tatiana alikuwa kwenye hali hiyo.
Buffet hakutaka kusikia kitu chochote, alichokuwa akikitaka ni kumuona msichana huyo tu. Aliambiwa kuwa hali ya binti huyo haikuwa nzuri lakini hakukubali, alihitaji kumuona msichana huyo hivyohivyo.
Dk. Henry hakuwa na jinsi, kama alivyokuwa ametaka, hakuweza kuzuia, alichokifanya ni kuwachukua kisha kuwapeleka katika chumba alicholazwa Tatiana. Kitendo cha Buffet kumuona mpenzi wake akiwa hoi kitandani, machozi yaliyokuwa yakimbubujika yakaongezeka zaidi.
Tatiana alikuwa kimya kitandani, alipumua kwa kusaidiwa na mashine ya oksijeni, kwa juu yake, kulikuwa na dripu moja ya damu na nyingine ya maji ambazo zote hizo zilikuwa zikiingia mwilini mwake.
Kwa jinsi alivyoonekana kitandani pale, alimsikitisha kila mmoja, mamumivu moyoni mwa Buffet yakaongezeka zaidi, hakuamini kile alichokuwa akikiona mbele yake. Kwa hatua fupifupi huku machozi yakiendelea kumbubujika, akaanza kumsogelea msichana yule, alipomfikia, akainama na kumbusu katika paji lake la uso.
Alijikuta akishikwa na hasira za ghafla, akaanza kuwa na kisasi kikubwa moyoni mwake juu ya mtu aliyesababisha yale yote hali iliyomfanya kuhisi ni Petrov kwani huyo ndiye aliyekuwa akiyaweka maisha ya mchumba wake katika hali ya hatari.
Alijiapiza kumtafuta mtu huyo kwa gharama zozote zile na kumkamata kisha kumuuapopote pale kwa ajili ya kuupoza moyo wake ambao kila siku ulikuwa kwenye majonzi mazito.
Tatiana hakuinuka kitandani pale, alikuwa amepoteza fahamu huku akipumua kwa msaada wa mashine ya oksijeni. Siku zikaendelea kukatika, siku ya pili ikaingia, ya tatu ikajisogeza na mwisho wa siku wiki kukatika lakini bado hali ya msichana huyo ilikuwa mbaya kitandani pale.
Kila siku madaktari walijitahidi kuhakikisha kwamba Tatiana anapona kabisa lakini jambo hilo likawa gumu kwani kidonda alichokuwa amekipata mbavuni kiliendelea kuongezeka hali iliyoyahatarisha zaidi maisha yake.
“Ni lazima tumuhamishie Muhimbili,” alisema Dk. Henry.
“Hapa mmeshindwa?” aliuliza Professa.
“Hali ni mbaya zaidi, hatutakiwi kukaa naye sana, pale kuna wataalamu wengi na vifaa vyenye uwezo, nahisi watamsaidia,” alisema Dk. Henry.
Hawakuwa na cha kufanya zaidi ya kile walichokuwa wameambiwa. Siku iliyofuata, gari la wagonjwa likaandaliwa na hatimaye Tatiana kutolewa hospitalini tayari kuingizwa ndani ya gari huku akiwa juu ya machela ili safari ya kwenda Muhimbili ianze.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu walijazana kwa wingi hospitalini hapo, wengi walimuona Tatiana akiwa kitandani, walihuzunika huku wengine wakilia kabisa, hawakuamini kile walichokuwa wakikiona kwamba msichana mrembo aliyebarikiwa kuwa tajiri baada ya kutoka kwenye umasikini, leo hii maisha yake yalikuwa juu ya kitanda.
Waandishi waliokuwa mahali hapo, kutoka kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi wakaanza kumpiga picha huku wakiwahoji baadhi ya watu waliokuwa mahali hapo ambapo wengi wakaanza kuelezea hisia zao juu ya kile kilichokuwa kimetokea.
“Inaniuma sana, ni lazima huyu mtu apatikane,” alisema mwanamke mmoja miongoni mwa wale wengi waliokuwa wamekusanyika hospitalini hapo.
Kila mmoja alizungumza lake lakini wote walikuwa na maneno yaliyofanana kwamba walitamani kuona mtu aliyefanya tukio lile akikamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani kutokana na kile kitendo alichokuwa amekifanya.
Watu wakapigiana simu na kupeana taarifa kwamba Tatiana alikuwa njiani kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hivyo watu wengi kuanza kukusanyika hospitalini hapo kwa ajili ya kuona kile kilichokuwa kikiendelea.
King’ora kilikuwa kikipigwa kutoka katika gari lile la wagonjwa, watu wakapaki magari yao pembeni na kulipisha gari lile lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi hali iliyowafanya watu kushangaa kwani hata kama lilikuwa gari la wagonjwa lakini haikutakiwa kuendeshwa kwa mwendo wa kasi namna ile kwani lingesababisha ajali endapo taili lingepata pancha ya ghafla.
Ndani ya gari lile, Buffet alibaki akimwangalia Tatiana, kama kulia alilia sana lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika, kitendo cha Tatiana kulala kitandani pale kilimuumiza moyo wake hali iliyomfanya kila wakati kujiapiza kwamba ilikuwa ni lazima aliyefanya tukio lile akamatwe na kisha kulipa kisasi kwa kile kilichokuwa kimetokea.
“Nitampata tu,” alijisemea Buffet huku akiwa mwenye hasira kali.
Hawakuchukua muda mrefu wakaanza kuingia katika eneo la hospitali hiyo, gari hilo lilipoonekana kwa mbali tu, watu wakajua ndiyo lile lililombeba Tatiana hivyo kuanza kulisogelea huku watu wengine wakilipiga picha mfululizo.
Polisi waliokuwa mahali hapo walijitahidi kuzuia ghasia zilizotaka kufanyika kwani kila mmoja alikuwa aking’ang’ania kumuona msichana huyo aliyekuwa hoi kitandani. Hakukuwa na shughuli zilizoendelea, japokuwa kulikuwa na walinzi getini lakini hawakutosha kuwazuia mamia ya watu walioingia hospitalini hapo wakitaka kumuona msichana huyo mrembo.
“Jaribuni kuwazuia,” alisema daktari huku akijiandaa kuufungua mlango wa gari lile.
“Mkuu! Hiyo si kazi nyepesi kabisa, watu hawa hatutoweza kuwazuia, tupo sita, wao wapo zaidi ya mia tano, tutawezaje sasa?” alihoji mlinzi mmoja.
Hata wale watu waliokuwa katika wodi nyingine kama ile ya watoto na watu waliokuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya moyo, wakafika kule ilipokuwa gari ile ya wagonjwa kwani walisikia kwamba Tatiana angefika mahali hapo.
Mlango ukafunguliwa, muda wote watu walikuwa bize wakipiga picha juu ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Buffet akateremka, flashi za kamera zikaongezeka. Machela iliposhushwa, kila mtu akataka kusogea ili aweze kumuona Tatiana kwa karibu kabisa.
Wanawake wakashindwa kuvumilia, kile walichokiona kiliwaumiza mno, hawakuamini kama mwisho wa msichana yule ungekuwa namna ile. Machela ile ikaanza kusukumwa mpaka ndani ya jengo la hospitali hiyo ambapo jopo la madaktari kumi wakakutana kwa ajili ya kuizungumzia hali ya Tatiana, walitakiwa kupambana kufa na kupona lakini mwisho wa siku msichana huyo apone kabisa.
“Ripoti kutoka Marie Stoppes inasemaje?” aliuliza Dk. Kobe.
“Amechanika mshipa mkubwa wa damu pia amechanwa nyama zinazoshikilia mbavu mwilini mwake,” alijibu Dk. Mwaki huku akiwa ameshika karatasi tatu zilizokuwa na ripoti juu ya hali ya Tatiana.
Kila daktari alishikwa na hofu, hali aliyokuwa nayo Tatiana ilimuogopesha kila mmoja na kuona kwamba kama wasingepambana vya kutosha basi msichana huyo angeweza kufariki dunia. Kikao hicho kilichukua nusu saa tu, wakatawanyika na kuanza kazi mara moja huku jukumu kubwa la kuhakikisha Tatiana anarudi katika hali ya kawaida akipewa Dk. Kimario ambaye alikuwa bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo.
Hali ya Tatiana haikubadilika, japokuwa alipewa dawa za kuweza kukausha kidonda kikubwa alichokipata ubavuni mara baada ya kuchomwa kisu lakini kidonda kile hakikuacha kuvuja damu hali iliyomfanya kutokupata nafuu hata kidogo.
Kila siku ilikuwa ni lazima madaktari waendelee kumchunguza na kumpatia matibabu makubwa ili kuyaokoa maisha yake lakini hakukuwa na kitu kilichosaidia kwani bado kidonda kile kiliendelea kuhatarisha maisha yake kwa asilimia mia moja.
“Hapa tutashindwa, ni lazima tufanye kitu,” alishauri Dk. Kimario, mpaka kutamka maneno hayo, hakuona kama kungekuwa na jambo jingine la kufanya.
“Kitu gani?”
“Huyu mtu asafirishwe na kupelekwa India katika Hospitali ya Ganga yenye wataalamu wa mgonjwa kama huyu,” alijibu huku akionekana kuwa na uhakika.
“Yaani inamaanisha sisi tumeshindwa kabisa?”
“Hiyo ndiyo maana yangu. Sijawahi kushindwa lakini hali ya mgonjwa hasa kile kidonda kutokupona, imenitia hofu sana,” alisema Dk. Kimario.
Walichokifanya ni kumuita Buffet na kumwambia kile walichokuwa wameambiwa kwamba ili kuokoa maisha ya Tatiana ilikuwa ni lazima wamsafirishe na kumpeleka nchini India ambapo huko angepatiwa matibabu makubwa na kumrudisha katika hali ya kwaida.
“Kwa nini tusimpeleke Marekani?” aliuliza Buffet.
“Hapana! India ndiyo kwenye madaktari mabingwa na wagonjwa wa namna hii wamekuwa wakitibiwa sana huko. Tumejadili na kuona ni lazima apelekwe huko,” alisema Dk. Kimario.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Buffet hakuwa na pingamizi, akakubaliana nao kwamba ilikuwa ni lazima mpenzi wake asafirishwe na kupelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu.
“Mungu! Naomba umuokoe Tatiana kwani akifa, nitakuwa na hasira zaidi na mtuhumiwa,” alisema Buffet huku akiyauma meno yake kwa hasira.
Kijiji cha Chibe hakikuwa kijiji tena, mabadiliko makubwa yaliyokuwa yametokea yalimshangaza kila mtu aliyekwenda kukiangalia. Kipindi cha nyuma kilitawaliwa na nyumba za nyasi huku kukiwa na nyumba moja tu ambayo iliezekwa kwa bati.
Kwa wakatihuo Chibe ile iliyokuwa kipindi cha nyuma haikuwa hii ya sasa, majengo makubwa yalijengwa, kukawa na mabomba mengi ya maji yaliyopitishwa chini, umeme wa kutosha ulikuwepo, yote haya yalifanywa na msichana Tatiana katika kipindi alichokuwa nchini Marekani.
Heshima kwa wazazi wake ikaongezeka zaidi. Wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali wakafika kijijini hapo na kuwekeza kwa kufungua maduka makubwa, soko kubwa na vitu vingine vingi ambavyo vyote hivyo vilikifanya eneo la kijiji kile kuongezeka zaidi.
Hakukuwa na matatizo ya afya tena, kulikuwa na hospitali kubwa ambapo madawa yote yalipatikana, kulikuwa na wauguzi waliokuwa na ubora zaidi, kwa kifupi, kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Tatiana aliamua kuyabadilisha maisha ya watu wa kijiji hicho.
Katika siku ambayo Tatiana alikaribia kutua nchini Tanzania, tayari taarifa zikasambazwa, wazazi wake na wanakijiji wengine wakawa na shauku kubwa ya kutaka kumuona msichana huyo ambaye alipoondoka nchini nchini Tanzania, tayari miaka mitatu na nusu ilikuwa imepita pasipo kurudi.
“Kumbe anarudi?”
“Ndiyo! Nimesikia anafika kesho.”
“Na atafika na huku?”
“Sasa si ndiyo kwao! Kwa nini tena asifike?”
Walikuwa wanakiji wawili waliokuwa wakizungumza, taarifa za kufika kwa Tatiana nchini Tanzania zilijulikana dunia nzima hivyo Watanzania wakajipanga kwa ajili ya kumpokea ndugu yao. Siku hiyo ilipofika, wanakijiji wakapewa taarifa kwamba tayari msichana huyo alikuwa ameingia nchini Tanzania na ndani ya wiki hiyo, angefika kijijini hapo alipozaliwa.
Kila mmoja akajisikia wa thamani moyoni mwake, kitendo cha kijiji hicho kutangazwa zaidi na zaidi kiliwaongezea umaarufu mkubwa hivyo wakawa na kiu ya kumuona msichana huyo akiingia ndani ya Kijiji cha Chibe.
“Unasemaje?”
“Nimesikia alitaka kuuawa?”
“Alitaka kuuawa? Kivipi tena? Yaani yeye mwenyewe alitaka auawe?”
“Hapana! Kuna mtu amemchoma kisu.”
“Wapi?”
“Hukohuko Mjini Dar es Salaam,” alisema mwanakijiji mmoja.
Kila mmoja alishtuka, hawakuamini kile kilichokuwa kimetokea kwamba msichana Tatiana alichomwa kisu akiwa Dar es Salaam akizungumza na wanachuo wa chuo kikuu.
Bi Frida alilia sana, hakuamini kile kilichotokea hivyo kumwambia mume wake kwamba iwe isiwe ni lazima waelekee jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumuona binti yao kipenzi. Hawakutaka kuendelea kukaa Chibe, walichokifanya ni kuondoka na kuelekea Dar.
Njiani ndani ya ndege, muda wote bi Frida alikuwa akilia tu, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, kila alipomkumbuka binti yake kipenzi, alijisikia maumivu makali mno. Mzee Sangiwa akawa na kazi kubwa ya kumbembeleza mke wake ambaye hakunyamaza kabisa.
“Nyamaza mke wangu! Ngoja tufike kwanza,” alisema mzee Sangiwa.
Walichukua masaa mawili mpaka kufika Dar es Salaam ambapo moja kwa moja wakaenda kuchukua chumba hotelini na kisha kuanza kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo huko wakapelekwa moja kwa moja mpaka kwa Dk. Kimario ambaye akawachukua na kwenda naye ofisini huku akiwa na Buffet ambaye kwao alikuwa mgeni ila walijua fika kwamba alikuwa akitembea na binti yao baada ya kuachana na Smith ambaye ndiye walikuwa wakimfahamu.
“Afadhali mmefika,” alisema Dk. Kimario.
“Asante. Ila nini kinaendelea?”
“Ni kwamba binti yenu alichomwa kisu.”
“Vyote tunajua, tunahitaji kujua nini kinaendelea baada ya yeye kuchomwa kisu?” aliuliza mzee Sangiwa.
“Tumejaribu kumtibia lakini hali imekuwa ngumu zaidi hivyo ni lazima asafirishwe.”
“Kwenda wapi?”
“India.”
“Lini?”
“Kesho!”
Bi Frida akazidi kulia zaidi, hakuamini kama kweli mwanaye alitakiwa kusafirishwa na kupelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu. Hapo ndipo walipojua kwamba kweli tatizo alilokuwa amelipata binti yao lilikuwa kubwa na lingeweza hata kupoteza maisha yake.
Mioyo yao iliumia lakini hawakuwa na jinsi, walitakiwa kukubaliana na ukweli kwamba binti yao alitakiwa kusafirishwa na kuelekea nchini India kwa ajili ya matibabu.
“Na sisi tunakwenda.”
“Kama mnataka kwenda sawa ila si kwa kesho. Tayari tushafanya maandalizi, tiketi zishapatikana, kama mnataka kwenda nafikiri inatakiwa kufanyika keshokutwa,” alisema Dk. Kimario.
Huo ndiyo uamuzi uliofikiwa, japokuwa hawakutakiwa kuondoka kesho yake lakini wakaomba ruhusa ya kutaka kumuona binti yao, hilo wala halikuwa tatizo, wakachukuliwa na kupelekwa katika chumba alicholazwa Tatiana.
Walipofika hapo, macho yao yalipotua kwa msichana huyo, mzee Sangiwa ambaye macho yake yalikuwa makavu, akashangaa kuona yakianza kulengwalengwa na machozi na ndani ya sekunde kumi tu, machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alihisi maumivu makali ya moyo, kwa jinsi binti yake alivyokuwa kimya kitandani pale, alijikuta akikata tanmaa ya kuona akinyanyuka tena kitandani pale. Wakamsogelea, bi Frida alikuwa hoi, tayari machozi yaliyokuwa yamekauka kwa muda yakaanza kububujika tena mashavuni mwake.
Picha ile iliyokuwa ikionekana mbele yake ilimuumiza mno, hakuamini kama binti yake aliyempenda kwa moyo wote, msichana aliyetokea kuwasaidia wao kama wazazi wao na kijiji kizima alikuwa kimya kitandani.
“Tatiana amka mwanangu,” alisema bi Frida huku akiendelea kububujikwa na machozi ya uchungu.
Bandeji kubwa ilifungwa tumboni mwake huku bandeji nyingine kubwa ikifungwa kwa wingi ubavuni mwake ambapo hapo ndipo kulipokuwa na jeraha lile la kuchomwa kwa kisu. Mbali na hiyo, hata mkono wake wa kushoto kulikuwa na bandeji nyingine ambayo kwa mbali ilionekana kuchafuliwa kwa damu zilizokuwa zikiendelea kumtoka japo kwa taratibu sana.
“Dokta, mwananagu ataamka lini?” aliuliza mzee Sangiwa huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ataamka tu.”
“Lini?”
“Hatujajua, ila India ndioyo watatuambia kila kitu. Tumejitahidi sana kuokoa maisha yake, tunatumaini ataamka tu,” alisema Dk. Kimario.
Japokuwa walikuwa na huzuni sana, kulia sana lakini hiyo haikutosha kumuinua Tatiana kitandani pale. Watu walijazana mno hospitalini, kila mtu aliyefika mahali hapo alitaka kuingia ndani ya chumba kile kwa ajili ya kumuona mwanamuziki huyu aliyekuwa hoi kitandani.
Hospitali ya Muhimbili ikatembelewa na masupastaa wengi kutoka sehemu nyingine nyingi hasa katika nchi za jirani, kila aliyefika mahali pale na kumuona Tatiana pale kitandani, alihuzunika na kuona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa msichana huyo.
“Dokta! Atapona kweli?” aliuliza Golden, mwanamuziki aliyekuwa na jina kubwa nchini Tanzania kipindi hicho.
“Kupona atapona, ila itabidi apelekwe India, vinginevyo, tutashindwa kuyaokoa maisha yake,” alisema Dk. Kimario.
Mbali na wasanii, pia walifika mpaka viongozi wa nchi, mawaziri mbalimbali akiwemo rais na balozi wa Marekani, wote walifika mahali hapo kwa ajili ya kumjulia hali Tatiana ambaye hakuwa na habari juu ya watu walioingia na kutoka chumbani humo.
Maandalizi yaliendelea kufanyika na siku iliyofuata, tayari safari ilitakiwa kuanza kuelekea nchini India. Ndege ya Shirika la Ndege la Indians Airlines ndiyo iliyowabeba na kuanza safari ya kuelekea nchini humo.
Buffet alitulia kitini, hakuwa mbali na mahali ambapo mpenzi wake alipokuwa, alitamani kukaa karibu naye ili hata kama kungetokea muujiza kwa msichana huyo kufumbua macho, basi yeye awe wa kwanza kuona hilo likitendeka.
Safari aliiona kuwa ndefu mno, alitamani wafike nchini India haraka iwezekanavyo kwani hali ya Tatiana ilizidi kuwa mbaya kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele.
Baada ya masaa ishirini na tatu, ndege ikaanza kuingia ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ghandhi na moja kwa moja akuanza kuelekea katika Hospitali ya Ganga ambayo haikuwa mbali kutoka uwanjani hapo.
Walichukua dakika ishirini mpaka kufika katika hospitali hiyo ambapo machela ikashushwa kisha kuanza kusukumwa kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo. Wakati madaktari walipoona kwamba mtu waliyemtarajia amefika, jopo zima la madaktari ishirini wakakutana katika chumba chao huku wakiwa na ripoti iliyokuwa imetumwa kutoka nchini Tanzania, walipofika kwenye chumba hicho, kitu cha kwanza kila mtu akapewa ripoti ile na kuanza kuipitia.
“Kuna kazi kubwa mbele yetu,” alisema Dk. Muntesh, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake hospitalini hapo.
“Ila nadhani tutafanikiwa na kuiletea heshima nchi hii, hasa kuitangaza hospitali hii,” alisema daktari mwingine, Dk. Kandesh.
“Hilo ndiyo lengo letu. Cha msingi tuanze kazi,” alisema Dk. Madesh ambaye akakabidhiwa jukumu hilo na kusaidiana na madaktari wengine wawili. Kazi ikaanza mara moja huku Buffet akiwa na uhakika kwamba mpenziwake angeweza kupona.
*****
Moyo wa Peter ukaridhika kutokana na kile alichokuwa amekifanya, kitendo cha kumchoma kisu Tatiana na kulazwa hospitalini huku akiwa na lengo la kummaliza kabisa lilimfurahisha mno. Alijiona kutenda haki kwani kile alichofanyiwa na msichana yule hakikuweza kusahaulika moyoni mwake.
Chuki yake haikupungua, kila alipomfikiria msichana huyo, bado alijiona kuwa na kila sababu kuweza kummaliza kabisa. Aliposikia kwamba msichana yule alipelekwa hospitalini na hali yake ilikuwa mbaya, alifurahi mno.
Japokuwa alikuwa amefanya kitu hicho kibaya lakini moyo wake haukuacha kumuomba Mungu, kila siku alipiga magoti chini na kusali, alikwenda kanisani kila alipohitajikahuku wakati mwingine akihubiri neno la Mungu kanisani humo.
Kile alichokuwa amekifanya, wala hakikuonekana kuwa dhambi, kila aliposimama mbele ya watu na kuhubiri kisha kukumbuka tukio lile la kumchoma Tatiana kisu, aliona kama alistahili kufanya vile kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Magazeti na vyombo vingine vya habari viliendelea kutoa taarifa kwamba hali ya msichana yule ilikuwa mbaya mno na hivyo isingewezekana kutibiwa nchini Tanzania, alitakiwa kusafirishwa na kupelekwa nchini India.
Taarifa zote alikuwa akizifuatilia lakini bado alitaka kuona msichana huyo akiendelea kuteseka kitandani kwani hakukuwa na kitu kingine ambacho alitakiwa kukipata zaidi ya kile.
“Afi tu!” alijisemea huku akionekana kuwa na hasira.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nathan alifuatilia kila kitu, mara baada ya kuambiwa juu ya chumba alichokuwa amechukua Tatiana, akajiandaa kwa ajili ya kummaliza msichana huyo. Kitu cha kwanza kabisa alichokifikiria ni kumpa kinywaji kilichokuwa na sumu ili atakapokunywa aweze kufa.
Wazo hilo lilikaa akilini mwake lakini kuna kipindi akajiona mjinga kwani angeweza vipi kumpa kinywaji msichana huyo? Kitu cha pili ambacho kilimjia kichwani mwake ni kumpiga risasi Tatiana, pia ugumu katika hilo ukajitokeza juu ya mahali ambapo angeweza kupata bastola kwa ajili ya kumpiga msichana huyo risasi, napo akakosa jibu.
Kitu cha mwisho kabisa kilichokuja akilini mwake ni kumuua msichana huyo kwa kumchomachoma na kisu. Hilo likawa wazo zuri lililopokelewa kwa mikono miwili kichwani mwake, hakukuwa na kazi kubwa ya kupata kisu kwani humohumo hotelini angeweza kukipata na hivyo kumuua Tatiana.
Usiku hakulala, alikuwa akifikiria namna atakavyomuua msichana huyo na kisha kukimbia, hata kama kukamatwa, akamatwe wakati amekwishamuua na kuuridhisha moyo wake. Akajiandaa vilivyo, asubuhi ilipofika, akamuita kijana yule aliyekuwa amemuhudumia na kumuagiza kumletea kisu.
“Cha nini tena?” aliuliza kijana yule.
“Nina kazi nacho.”
“Hapana bwana, haiwezekani, huwa haturuhusiwi kumpa kisu mteja,” alisema kijana yule.
Japokuwa alimuahidi kwamba angemsaidia kwa kila kitu lakini hilo likawa gumu kufanyika, mhudumu yule hakutaka kumpa kisu Nathan kwani moja ya sheria ya hoteli hiyo haikuruhusu kitu kama hicho kifanyike.
Alibembeleza na kubembeleza lakini msimamo wa mhudumu yule ulikuwa uleule kwamba kisu hakikutoka. Nathan hakutaka kubembeleza sana, alichokifanya ni kutoka nje ya hoteli ile na kwenda kule kulipokuwa kunapaki daladala nyingi, katika Kituo cha Ubungo Terminal.
Alikuwa na uhakika kwamba huko angeweza kupata kisu, alipozungukazunguka huku na kule, akafanikiwa kupata kisu kwa muuza vyombo vya ndani ambapo akampatia kiasi cha shilingi elfu kumi, pasipo kuomba chenji yake akaondoka zake.
Kila kitu alichokuwa akikitaka kilikamilika. Kwa wakati huo alikuwa tayari kwa kila kitu, alikuwa radhi kuona akikamatwa na polisi na kufungwa lakini mwisho wa siku alitaka kuhakikisha msichana huyo akifariki dunia.
“I will kill her by using this knife,” (nitamuua kwa kutumia kisu hiki) alijisemea Nathan wakati anakiangalia kisu kile.
Siku hiyo ndiyo alipanga kufanya kile alichotaka kukifanya. Hakutaka kuchelewa, japokuwa Petrov alimwambia kwamba alikuwa njiani kuja nchini Tanzania lakini hakutaka kumsubiria, alitaka kufanya kila kitu kivyakevyake kwa kuamini kwamba kama nafasi alikuwa ameipata nchini Marekani lakini hakuifanyia kazi, hivyo kwake aliuona kuwa uzembe mkubwa mno.
Siku hiyo, kila wakati alikuwa akimuita mhudumu yule ambaye alimzoea na kumuulizia kama Tatiana alikuwa amefika au la. Kila alipomuuliza, alimwambia kwamba hakufika na kama angefika angemwambia ili azungumze naye.
“I will let you know, brother,” (Nitakujulisha, kaka) alisema mhudumu yule.
Muda haukusubiri, uliendelea kusonga mbele huku Nathan akiwa kwenye presha kubwa ya kutaka kuonana na Tatiana ili aweze kumuua na kurudi zake nchini Liberia au hata kama kukamatwa, akamatwe lakini akiwa tayari amemuua msichana huyo.
Ilipofika saa tatu usiku, hakukuwa na dalili za kumuona Tatiana hotelini hapo, akashindwa kuelewa ni kitu gani kilichokuwa kimetokea, alichokifanya ni kumuita mhudumu yule kwa lengo la kutaka kujua ukweli juu ya kilichokuwa kimetokea, kama alifika na kuingia kimyakimya au la!.
“Haujapata taarifa?” aliuliza mhudumu yule.
“Taarifa gani?”
“Tatiana ameuawa!”
“Tatiana ameuawa? Na nani? Wapi? Saa ngapi?” aliuliza Nathan maswali manne mfululizo.
“Alikwenda chuo, kuna mtu alimchoma kisu.”
“Nani?”
“Mpaka sasa hivi haijajulikana. Angalia kwenye televisheni,” alisema mhudumu yule.
Nathan hakutaka kusubiri kule chini, alichokifanya ni kupandisha lifti harakaharaka ili aweze kuingia chumbani kwake na kuangalia kwenye televisheni kile kilichokuwa kimetokea, alipofika tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kufungua CNN na kuangalia, habari zilizofika punde ziliendelea kuionyeshwa juu ya kile kilichokuwa kikiendelea nchini Tanzania.
“Nani aliyefanya hivi?” alijiuliza huku akiwa haelewielewi,” alisema Nathan huku akiikodolea macho televisheni ile.
Moyo wake haukufurahia hata kidogo, japokuwa alichokiona ndicho kile alichotaka kukifanya lakini hakufurahia kabisa, alitaka kukifanya kile kwa mikono yake na si kufanyiwa na mtu mwingine.
“Huu ni upumbavu, nitakwenda hata hospitalini, lakini ni lazima nimuue kwa mkono wangu,” alisema Nathan huku akionekana kuwa na hasira, wala hazikupita siku nyingi, akapata taarifa kwamba Tatiana alikuwa amesafirishwa na kuelekea nchini India kwa ajili ya matibabu.
Hakutaka kukubali, alihitaji kumaliza kazi hiyo haraka iwezekanavyo, mara baada ya kujua kwamba msichana huyo alitarajia kupata matibabu katika Hospitali ya Ganga, baada ya wiki moja naye akapanda ndege kuelekea huko, hakukubali kurudi nchini Liberia kabla ya kutimiza kile alichokitaka. Alidhamiria kumuua msichana huyo.
Madaktari wa Hospitali ya Ganga walijitahidi usiku na mchana kuhakikisha kwamba Tatiana anapona na kurudi katika hali yake ya kawaida. Hakukuwa na mtu aliyelala, walipishana ndani ya chumba kile kwa zamu huku kila mmoja akijitahidi hata kushauri juu ya kile kilichotakiwa kufanyika.
Kitu cha kwanza kabisa ambacho walikifanya ni kuhakikisha kwamba ile damu iliyokuwa inavuja ubavuni inakatika kwani kama ingeendelea vile ilikuwa ni lazima kumwagikia tumboni na hatimaye kupata matatizo zaidi, hivyo wakaanza kulishughulikia suala hilo.
“Tunahitaji kwanza kuua wadudu, lete dawa ya Cristapen,” alisema Dk. Mandesh ambaye ndiye yule aliyepewa jukumu zito la kuhakikisha kwamba msichana Tatiana anarudi katika hali yake ya kawaida.
Akakabidhiwa dawa ile na kisha kuanza kuipulizia ndani ya tumbo la Tatiana kwa kupitia katika jeraha lile alilolipata kwani kabla ya kufanya chochote kile ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba wadudu wote ambao wangeweza kupita kupitia jeraha lile wanadhibitiwa haraka iwezekanavyo.
Baada ya kuhakikisha kwamba wamefanikiwa kufanya hivyo, mikasi zaidi iliandaliwa kwani kitu kingine walichotakiwa kufanya ni kuchunguza kidonda kile hasa katika nyama zile zilizokuwa zimechanwa na kisu kile.
“Hili ni tatizo kubwa sana, nahisi kunyunyizia dawa ya Cristapen haitoshi, ngoja tuikate kabisa damu hii,” alisema Dk. Mandesh na kisha kufanya hicho alichokuwa amekisema, shughuli ya kukata damu ile ikaanza mara moja.
Nathan akatua nchini India katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Coimbatore iliokuwa katika Jiji la Coimbatore. Alipoteremka, akaanza kupiga hatua kuelekea nje ya uwanja huo ambapo akachukua begi lake na kisha kuanza kupiga hatua nje ya jengo la uwanja huo.
“Where to brother?” (Unakwenda wapi kaka?) aliuliza dereva teksi mmoja aliyekuwa amesimama pembeni ya teksi yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Do you know any seven star hotel?” (Unaijua hoteli yoyote ya nyota saba?) aliuliza Nathan.
“Yaap brother! What about Sea Clif Hotel?” (Ndiyo kaka! Unaonaje Hoteli ya Sea Clif?)
“Where is it located?” (Ipo eneo gani?)
“Almost one kilometre from here?” (Kama kilometa moja kutoka hapa)
“And, do you know Ganga hospital?” (Unaifahamu Hospitali ya Ganga?)
“Yaap!”
“Where is it located?” (Ipo eneo gani?)
“That one....” (Ile pale) alisema dereva yule huku akiinyooshea kidole hospitali hiyo, haikuwa karibu, ila kwa kuwa ilikuwa na ghorofa kubwa lililoonekana mpaka hapo, dereva akaona bora amuonyeshee.
Nathan akaridhika, alichokifanya ni kumwambia dereva waelekee katika hospitali ile ambapo malipo yake yalikuwa ni rupii kumi tu. Wakaingia garini na safari kuanza. Japokuwa drevea alikuwa akileta uchangamfu mkubwa lakini kwa Nathan, aliamua kutulia kwani kichwa chake ilikuwa na mawazo mengi.
Alisumbuka sana mpaka kufika nchini Tanzania, alipokuwa hapo, bado alihitaji kusafiri tena kuelekea nchini India ambapo huko ndipo alipopanga kufanya mauaji yake. Bado chuki kubwa dhidi ya Tatiana ilikuwa moyoni mwake, hakumpenda msichana yule na alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile ili mradi afe tu.
Hawakuchukua muda mrefu sana wakawa wamekwishafika katika hospitali hiyo ambapo Nathan akaanza kuiangalia kwa makini, hakutaka kuteremka kutoka garini, alibaki humo huku akiiangalia tu.
“Ndiyo hapa,” alisema dereva yule.
“Ok! Nashukuru! Kuna hoteli hapa karibu?”
“Ndiyo! Ila si nyota saba.”
“Nipeleke hiyohiyo, hata kama nyota tano,” alisema Nathan na kuanza kupelekwa huko. Walipofika, wakateremka na kisha kuelekea mapokezini ambapo akachukua chumba na kufuata lifti kupandisha chumbani kwake.
Huko, muda wote macho yake yalikuwa dirishani, alikuwa akifuatilia kwa karibu kila kilichokuwa kikiendelea nje ya hospitali ile. Kama kawaida, kutokana na umaarufu mkubwa aliokuwa nao Tatiana, Wahindi wengi wakiwemo waandishi wa habari walikuwa wamekusanyika nje ya jengo la hospitali ile kwa lengo la kuingia ndani ili waweze kumuona Tatiana.
“Hapa patafaa sana, ngoja nianze kutafuta njia ya kuingia ndani ya hospitali ile. Nitaingia kama daktari, ngoja nitafute kile kitu kinachohitajika,” alisema Nathan.
Kitu chepesi ambacho aliona kama kingefanyika basi kingempa nafasi kubwa ya kumuua Tatiana ni kuingia ndani ya chumba kile huku akiwa na mavazi ya kidaktari ambayo aliamini kwamba kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angeweza kumgundua kwani hospitali hiyo ilikuwa na madaktari wengi mpaka wengine kutokujuana.
Siku iliyofuata, Nathan akaondoka kuelekea mitaani ambapo huko akaanza kuzungukazunguka kwenye maduka makubwa kwa ajili ya kununua mavazi kama ya kidaktari kwa ajili ya kukamilishia kile alichotaka kukifanya.
Kwa kuwa alikuwa na fedha za kutosha, tena akitokea katika familia ya bilionea mmoja nchini Liberia, kuhusu kununua mavazi hayo kwa gharama kubwa wala hakukuwa na tatizo lolote lile, alipoyanunua mavazi hayo, akanunua na mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo iitwayo stetoscope kisha kurudi hotelini.
Usiku mzima alikuwa akijifikiria namna ya kuingia hospitalini mule na kufanya kile alichokikusudia pasipo kugundulika na mtu yeyote yule. Mchana wa siku hiyo, akaelekea katika hospitali ile ambapo bado waliendelea kujazana huku kila mmoja akitaka kumuona Tatiana ambaye uwepo wake ndani ya hospitali ile ulimpa umaarufu mkubwa hata zaidi ya waziri mkuu wa nchi hiyo.
Nathan hakutaka kuingilia mlango wa mbele, alitaka kuingilia mlango wa nyuma kabisa, hiyo yote ilikuwa ni kufanya upelelezi wake kama kulikuwa na ulinzi mkali mahali pale.
Hakukuwa na mtu aliyemuona, na hata wale waliomuona, hawakuwa wakihusika chochote kile na hospitali hiyo hivyo hawakujishughulisha naye kabisa. Huku akiwa ameufikia mlango wa kuingia ndani, mara akashtuka kusikia akiitwa.
“You!! Where you go?” (Unakwenda wapi?) aliuliza mlinzi kwa Kingereza kibovu.
“I’ve gota patient in here,” (Nina mgonjwa humu) alijibu Nathan.
“You no go there, this is not entering,” (Usiende huko, hii si sehemu ya kuingilia) alisema mlinzi huyo huku akiendelea kuiharibu lugha hiyo pasipo kujali chochote kile.
Hicho ndicho alichotaka kukifahamu mahali hapo, alitaka kufahamu ni ulinzi wa aina gani ulikuwepo. Alichokifanya mara baada ya kuambiwa kutoka kule ni kurudi na kuelekea kule kulipokuwa na watu wengi ambao walikuwa wakisubiri ruhusa ya daktari kuingia hospitalini.
“Hamuwezi kuingia wote, wengine bakini, zamu kwa zamu,” alisema daktari mmoja, alikuwa akiwaambia watu zaidi ya mia nne waliokuwa wamekusanyika mbele yake.
Watu wakagawanywa, wengine walitakiwa kuingia ndani lakini wengine walitakiwa kubaki kwani walikuwa wengi mno, hivyo wangeingia zamu kwa zamu. Hilo halikuwa tatizo, walichokuwa wakikitaka ni kuingia ndani tu na kumuona msichana huyo aliyekuwa akiteseka kitandani.
Ndani ya hospitali hiyo, madaktari walikuwa wamejitahidi sana kumtibu Tatiana kiasi kwamba kikafika kipindi wakaona kwamba walifikia mwisho. Walitumia ujuzi wao wote, kidogo Tatiana akaanza kuonyesha nafuu, yaani kile kidonda alichokuwa nacho kikaanza kukauka hali iliyoonyesha kwamba muda wowote ule msichana yule angeweza kurudiwa na fahamu.
“Kidogo kuna nafuu,” alisema Dk. Mandesh na kisha kuwashukuru madaktari wenzake kwa kazi kubwa waliyokuwa wameifanya mpaka hatua ile ya kidonda kile kuanza kukauka.
Buffet hakuwa na cha kushukuru zaidi, kama ni maneno ya shukrani, alihakikishia anawapa kila siku kwani kwa jinsi alivyowaona madaktari wale, walikuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba mgonjwa yule akipona. Kuna wakati walikataa kula, walikataa kupumzika kwa ajili ya Tatiana kitu ambacho kwa Buffet kilionekana kuwa zaidi ya kujitolea, hivyo shukrani hazikumuisha mdomoni mwake.
Baada ya kuandaliwa vizuri kwa ajili ya watu kumuona Tatiana, wakaruhusiwa kuingia zamu kwa zamu katika chumba kimoja kilichokuwa kimetwngwa ghorofani kabisa na hakukuhitajika kelele za aina yoyote ile.
Kila mtu aliyeingia ndani ya chumba kile, hakuruhusiwa kuingia na viatu vyake, alitakiwa kuviacha mlangoni ambapo hapo walipewa viatu vingine ambavyo hata kama ungetembea vipi, usingeweza kusababisha kelele zozote zile.
Kila mtu aliyemuona Tatiana kitandani pale, alibaki akilia, hakuamini kile alichokuwa akikiona. Msichana mrembo, mwanamuziki aliyejizolea umaarufu mkubwa alikuwa kitandani kimya kabisa.
“She is too young to die,” (Ni mdogo mno kufa) alisikika mwanamke mmoja ambaye alishindwa kuyazuia machozi yake kububujika mashavuni mwake.
Miongoni mwa watu walioingia ndani ya chumba kile alikuwemo Nathan ambaye baada ya kumuona Tatiana kitandani pale, hakuwa kama watu wengine, hakuwa na huzuni hata kidogo tena wakati mwingine alijiona akishikwa na hamu ya kumsogelea msichana yule kitandani pale na kumuua, bado kile alichofanyiwa kipindi cha nyuma kilizidi kuutafuta moyo wake.
“I will kill this bitch by mtyself,” (Nitamuua huyu malaya mimi mwenyewe,” (Alijisemea Nathan huku akiyapitisha macho yake usoni mwa msichana huyo.
Ulinzi ulikuwa wa kutosha mahali hapo, mbali na polisi waliokuwa nje ya mlango wa chumba hicho, pia wengine walikuwa ndani kuhakikisha kila kitu kinakwenda salama. Taarifa za kuchomwa kisu kwa msichana huyo zilijulikana kila kona duniani hivyo waliamini kwamba piga ua ilikuwa ni lazima wauaji wasafiri kuelekea hiko India kwa ajili ya kummaliza palepale kitandani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipomaliza kumwangalia Tatiana, hakutaka kukaa sana, hakutaka kuzoeleka sana hivyo alichokifanya ni kuondoka hospitalini hapo. Alipofika hotelini, akajilaza kitandani, hasira kali ilimkaba kooni mwake, hakumpenda kabisa Tatiana na alimchukia zaidi ya alivyomchukia shetani.
Hakurudi tena hospitalini, alichokifanya ni kukaa hotelini kwa siku mbili kisha siku iliyofuata, akaanza kufanya mchakato wa kutafuta namna vitambulisho vya madaktari hospitalini pale vilivyokuwa.
Hilo wala haikumpa shida kwani ndani ya masaa matatu tu, tayari kila kitu kilikuwa kimekamilika na ni safari ya kwenda huko tu ndiyo ambayo alikuwa akiisubiri.
Siku ya kufanya tukio ilipofika, akaondoka hotelini huku akiwa na kibegi kidogo mgongoni. Hakukuwa na mtu aliyemtilia shaka hasa alipoingia hospitalini kwa kuwa alionekana kama watu wengine ambao walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kuwaletea vyakula wagonjwa wao.
Wakati alipokuwa akienda huko, hakutaka kwenda mchana, alikwenda usiku kwani alihofia macho ya watu wengi waliokuwa mchana katika siku aliyokuja na ndiyo maana aliamua kuja usiku ambapo aliamini pia hakukuwa na watu wengi.
Alipoingia ndani, kitu cha kwanza alichokifanya ni kwenda chooni ambapo huko, kwa haraka sana akavaa koti kubwa, akachukua mashine ya stetoscope, akaining’iniza shingon, akachukua mafaili yake, akayashikilia mkononi, akachukua sindano iliyokuwa na sumu ya Mephromethomphy ambayo hutumika kuulia wadudu msituni, sumu iliyokuwa na nguvu kubwa ya kuua kwa kipindi kifupi hasa inapoingia katika mshipa wa damu wa binadamu, ilikuwa moja ya sumu ambayo haikutakiwa kuuzwa kipindi hicho, hata Nathan aliipata kimagumashi. “Hapa nina uhakika sitoweza kugundulika,” alisema Nathan huku akivaa miwani ya macho hali iliyomfanya hata muonekano wake kubadilika. Mbali na hivyo, akakipachika kitambulisho upande wake wa kushoto kilichoonyesha jina la Dr. Stephen Show. Akawa na uhakika wa kuingia chumbani, hivyo akaanza kuelekea huko huku akijiamini
Ilikuwa ngumu mno kugundua kwamba mtu aliyekuwa akija mbele yao hakuwa daktari. Nathan alitembea kwa kujiamini huku kila wakati akiangalia mafaili yake hali iliyowafanya polisi wote kuona kwamba mtu huyo alikuwa daktari kweli.
Alitembea kwa kujiamini, miwani yake, mavazi na ile mashine aliyokuwa ameining’iniza shingoni iliwafanya polisi wote kuwa na uhakika kwamba Nathan alikuwa daktari.
Alitembea mpaka alipofika katika mlango wa chumba kile, hakusimama, japokuwa polisi walitamani kumsimamisha lakini wakajikuta wakipuuzia na hivyo kumruhusu kuingia ndani ya chumba kile.
Hiyo ilikuwa nafasi nzuri kwa Nathan, hakuamini kama angeruhusiwa kirahisi namna ile, akakishika kitasa na kisha kuingia ndani huku akionekana kuwa mwenye furaha kubwa kwa kuwa aliona hiyo ndiyo nafasi ya kukamilisha kile alichotaka kukifanya.
“Karibu daktari...” alisikia akikaribishwa ndani ya chumba hicho, akageuka nyuma na macho yake kutua kwa Buffet aliyekuwa pembeni mwa kitanda cha Tatiana.
“Asante sana, anaendeleaje?” aliuliza Nathan huku akiiweka vizuri miwani yake.
“Kidogo hali yake inaonekana kuwa nzuri japokuwa bado hajarudiwa na fahamu,” alisema Buffet huku akisogea pembeni.
Alichokifanya Nathan ni kutoa sindano katika koti lake na kumtaka Buffet aondoke ndani ya chumba kile ili aendelee na kazi yake. Kwa mbali Buffet alionyesha mshtuko lakini akajipa moyo kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile.
Hata kabla hajatoka ndani ya chumba hicho akaanza kujiuliza maswali kuhusu bomba la sindano ile kwamba ilikuwaje daktari mkubwa kama yule, tena ndani ya hospitali kubwa namna ile kuja na kutoa bomba la sindano katika koti lake?
Yeye mwenyewe alikuwa daktari lakini kitu kama kile hakikuwa kikikubalika kabisa, sindano ilitakiwa itolewe kutoka kwenye boksi lake na ndipo daktari achukue dawa na kumchoma mgonjwa, kile kilichoendelea, hakikuonekana kuwa sahihi.
“Vipi?” aliuliza Nathan huku akimwangalia Buffet usoni.
“Daktari....”
“Nenda nje niendelee na kazi yangu...” alisema Nathan huku akimkazia macho Buffet, akajitahidi kuonyesha tabasamu pana
Japokuwa moyo wake haukumtuma kwenda nje lakini hakuwa na jinsi, alijua ni kwa namna gani madaktari walikuwa bize hasa anapokuwa mgonjwa ambaye ana tatizo kubwa, alichokifanya ni kutii tu kwani hakukuwa na kitu kingine zaidi ya hicho.
Buffet akakaa katika benchi kubwa la chumba lililowekwa nje, kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi na alikuwa akijiuliza maswali mengi juu ya kile kilichokuwa kimetokea, huku akiwa kwenye mawazo hayo, ghafla akatokea Dk. Mandesh ambaye uso wake ulionyesha tabasamu kwa mbali.
“Mbona upo hapa?” aliuliza Dk. Mandesh.
“Kuna daktari anamhudumia mgonjwa.”
“Kuna daktari anamhudumia mgonjwa?” aliuliza Dk. Mandesh huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo!”
“Daktari gani?”
“Simjui.”
Ni kama Dk. Mandesh akashtuka kitu fulani, alichokifanya ni kuugsogelea mlango ule na kisha kutaka kuufungua, mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani. Daktari huyo akaanza kupigha hodi huku akihitaji kufunguliwa lakini mlango haukufunguliwa.
Polisi waliokuwa pembeni ambao walipewa jukumu la kulinda chumba kile wakasogea kule alipokuwa Dk. Mandesh na Buffet kutaka kujua kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo.
“Kuna nini dokta?” aliuliza mlinzi mmoja.
“Ni nani aliingia humu?” aliuliza Dk. Mandesh.
“Kuna daktari mmoja hivi.”
“Yupi?”
“Kiukweli simjui, ila ni daktari.”
“Hapana! Huyo atakuwa si daktari. Hakuna daktari anayeruhusiwa kuingia humu zaidi ya wale tuliokuja kabla,” alisema Dk. Mandesh.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila mmoja akashtuka, maneno aliyoyaongea daktari yule yalimshtua kila mmoja na kugundua kwamba kulikuwa na tatizo limetokea hivyo nao kuanza kuugonga mlango ule uliokuwa umefungwa kwa ndani.
“Vipi?”
“Mlango haufunguki. Mungu wangu! Ni nani tena?” aliuliza Dk. Mandesh huku akionekana kushangaa.
Wazo moja tu ndiyo lililowajia vichwani mwao kwamba watumie mlango wa nyuma ya chumba kile. Hawakutaka kusubiri, huku kila mmoja akionekana kuchanganyikiwa, wakaanza kukimbia kuelekea kwenye upande wa pili wa chumba kile.
Walipofika huko, mlango haukuwa umefungwa, ulikuwa wazi kabisa, wakaingia moja kwa moja ndani. Picha waliyoiona kitandani pale iliwashtua mno. Tatiana alikuwa akirusha miguu yake huku na kule, mapovu mazito yalikuwa yakimtoka mdomoni kama mtu aliyekuwa akikaribia kukata roho.
Kila mmoja akachanganyikiwa, Buffet hakuweza kuvumilia kuiangalia picha ile, akajikuta akipiga magoti na kuanza kulia. Mtu aliyesemekana kuwa daktari ambaye aliingia ndani ya chumba kile aliharibu kila kitu, hapo wakagundua kwamba mtu huyo hakuwa daktari kama alivyuokuwa bali alikuwa muuaji ambaye alitaka kumuua Tatiana.
“Naomba uokoe maisha yake! Naomba uokoe maisha yake,” alisema Buffet huku akilia.
Alikuwa daktari mzoefu tena aliyeaminika sana nchini Marekani lakini ndani ya chumba hicho, kwa jinsi alivyokuwa amechanganyikiwa, akasahau kabisa kwamba hata naye alikuwa daktari hivyo suala la kumtibu mtu lingewezekana kwa asilimia mia moja.
Alichokifanya Dk. Mandesh hata kabla ya kumtibu Tatiana, akalichukua bomba la sindano lililokuwa chini na kulinusa ili aweze kujua lilikuwa na sumu aina gani kwani aliamini kwamba sumu iliyokuwemo ndani ya bomba lile la sindano ndiyo iliyotumika kumchoma Tatiana.
“Mungu wangu! Mephromethomphy!” alisema Dk. Mandesh huku Tatiana akiendelea kukukuruka kitandani pale, alikuwa akikaribia kukata roho.
****
Bado moyo wake ulikuwa na hasira mno, alikunja ndita usoni mwake huku akimwangalia Tatiana kitandani pale, hakumpenda hata kidogo na hata aliposhika lile bomba la sindano, alidhamiria kumchoma msichana huyo na kisha kuondoka kwa kuamini kwamba msichana yule angekufa kwani sumu ile ilikuwa na nguvu mno.
Alichokifanya kabla ya kufanya chochote kile ni kuufuata mlango na kisha kuufunga kwa kutumia kiloki kidogo kilichokuwa kwenye kitasa kisha kumrudia Tatiana kitandani pale na kuanza kumwangalia tena.
Kwa jinsi hasira kali zilivyokuwa zimemkaba kooni mwake, akashindwa kuvumilia, hapohapo akajikuta akianza kulia kwa uchungu. Machozi yakabubujika mashavuni mwake kwani kitendo cha kumuona msichana yule mahali pale, tayari kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma kama mkanda wa filamu, hivyo hakuona jinsi zaidi ya kumuua tu.
Akaingiza mkono wake katika mfuko wa pili wa koti lake na kisha kutoa chupa ndogo iliyokuwa na sumu ile ya
Mephromethomphy, akachukua sindano ile na kisha kuchoma katika kikopo kile kisha kuivuta sumu ile.
“Ni lazima ufe malaya mkubwa,” alisema Nathan huku akiwa na hasira mno.
Huku akiwa na hasira zilizomkaba kooni, hapohapo akaanza kusikia mtu akigonga mlango na kutaka kuingia ndani. Tayari akaona kwamba kama asingefanya kile kilichokuwa kimemleta ndani basi angeweza kukamatwa kirahisi, alichokifanya ni kumchoma Tatiana sindano ile.
Msichana huyo akaanza kubadilika kitandani pale, akaanza kurusha miguu na mikono yake huku na kule, mapovu yakaanza kumtoka mdomoni, hali ile iliyokuwa ikitokea, ilimfurahisha mno Nathan.
“Bora ufe malaya mkubwa, haya ndiyo matunda ya usaliti wako,” alisema Nathan huku akionekana kuwa mwenye hasira kubwa. Alichokifanya mara baada ya kuona Tatiana akiwa kwenye hali ile ni kuondoka kupitia mlango wa nyuma huku akiwa na uhakika kwamba msichana huyo angefariki dunia.
“Bora nimekamilisha kazi,” alisema Nathan huku akiwa kwenye mwendo wa kasi kuelekea nje ya jengo la hospitali ile.
Japokuwa alikuwa akitembea kwa harakaharakla na kuonekana mgeni machoni mwa walinzi waliokuwa wakirandaranda huku na kule lakini hakukuwa na mtu aliyemsimamisha na kumuuliza kwani muonekano wake tu aliokuwa nao ulionyesha kwamba alikuwa daktari, hivyo watu wakampisha pasipo kujua kwamba mtu huyo alikuwa muuaji
Sumu ya Mephromethomphy ilizidi kumuweka kwenye hali mbaya, Tatiana aliendelea kurusha miguu na mikono yake huku na kule na mapovu yakimtoka kwa wingi mdomoni. Dk. Mandesh akachanganyikiwa, sumu ile iliyokuwa imeingia katika mishipa ya damu ya Tatiana ilikuwa hatari sana na ingeweza kumuua wakati wowote ule.
“Nipe Cyclomethius...” alisema Dk. Mandesh.
Cyclomethius ilikuwa dawa yenye nguvu ya kuondoa sumu mwilini mwa mwanadamu hasa katika damu yake. Kwa haraka sana Buffet akachukua chupa iliyokuwa na dawa hiyo na kisha kumpa Dk. Mandesh ambaye akachoma sindano katika chupa ile na kisha kuivuta dawa ile kwa kutumia sindano na kumchoma Tatiana kitandani pale.
Kila mmoja kwa wakati huo alikuwa akimuomba Mungu juu ya hali ya msichana huyo kwani kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo alivyozidi kurusharusha mikono na miguu yake huku na kule.
Huku wakiendelea kumhudumia Tatiana, madaktari wengine wakafika nje ya mlango ule ambapo walipogonga, ukafunguliwa na kisha kuingia. Hali waliyoikuta hata wao iliwashangaza mno kwani hawakutegemea kuona kitu kama hicho kikitokea.
“Kuna nini?” aliuliza daktari mmoja miongoni mwa watatu walioingia chumbani humo.
“Kuna mtu alikuja kumchoma sindano yenye sumu.”
“Nani?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hata mimi simjui. Hawa wanasema kwamba ni daktari.” Alisema Dk. Mandesh huku akiisikilizia hali ya Tatiana mara baada ya kumchoma sindano ile.
Taarifa zikaanza kutolewa kwamba kulikuwa na mtu aliyeingia hospitalini hapo na kujifanya daktari huku akiwa na lengo la kumuua Tatiana. Kila aliyezisikia taarifa zile alishtuka, bila juhudi kubwa iliyofanywa na Dk. Mandesh basi msichana Tatiana angeweza kufariki dunia.
Kila mtu akashangaa na kuona kwamba ulinzi wa hospitali hiyo ulikuwa mdogo mno kiasi kwamba kulikuwa na mtu ambaye aliingia huku akiwa na lengo la kumuua Tatiana. Watu wakaanza kutoa maoni yao kwamba Tatiana alitakiwa kuhamishwa hospitalini hapo na kupelekwa katika hospitali nyingine ili kuyaokoa maisha yake.
“Haitowezekana kuhamishwa,” alisema daktari mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Rajiv.
“Na kwa nini hamkuweka ulinzi wa kutosha hospitalini hapa?” aliuliza mwandishi wa habari.
“Ulinzi upo wa kutosha, na ukitaka kuamini, baadae njoo kwa lengo la kufanya mambo yako uone,” alisema Dk. Rajiv huku akionekana kukasirika kutokana na maswali aliyokuwa akiulizwa.
“Na Tatiana anaendeleaje?”
“Sijui.”
Dk. Rajiv hakutaka kuendelea kuhojiwa, alishikwa na hasira mno kwani maswali ya mwandishi yule hakuona kama alitakiwa kuulizwa kwa kuwa yalionyesha udhaifu mkubwa wa hospitali yake.
Kwa kuwa hospitali hiyo ilikuwa na kamera ndogo za CCTV, walichokifanya ni kwenda kuangalia ili kumuona huyo mtu ambaye aliingia ndani ya hospitali hiyo kwa lengo la kumuua Tatiana. Hilo wala halikuwa tatizo hata kidogo, wataalamu wa IT wakafanya kazi yao na mwisho wa siku Nathan kuonekana akitembea kwa kujiamini mpaka katika chumba kile.
“Chukueni picha yake, anahitajika sana,” alisema Dk. Rajiv na vijana wale wa IT kufanya hivyo.
Hicho ndicho kilichofanyika, picha ya Nathan ikachukuliwa, wakaziprinti na kisha kuwapa walinzi na baadhi ya madaktari huku wakiwaambia kwamba ilikuwa ni lazima suala hilo libaki na kuwa siri kwani walijua kwamba mara muuaji huyo atakaposikia kwamba Tatiana hakufariki, lazima angerudi tena.
Masaa yaliendelea kukatika, hali ya Tatiana ikaanza kurudi katika hali ya kawaida kama aliyokuwa nayo kabla ya kuwekewa sumu ile. Mapigo yake ya moyo yakarudi kawaida japokuwa bado hakurudiwa na fahamu.
Pongezi zote zilikwenda kwa Dk. Mandesh ambaye ndiye aliyehakikisha kwamba mgonjwa wake anapatiwa matibabu ya nguvu na hatimaye kuwa kama zamani.
Maswali yakaanza kuulizwa juu ya sababu iliyowafanya watu kutaka kumuua Tatiana. Hawakujua tatizo lilikuwa nini mpaka msichana huyo kutaka kuuawa mara tatu, mara ya kwanza ilikuwa nchini Marekani ambapo gari lake lililipouliwa kwa bomu, mara ya pili nchini Tanzania alipochomwa kisu na mara ya tatu kuwa hapo nchini India.
Kila mmoja akaona kwamba kulikuwa na tatizo nyuma ya pazia, kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea ambacho hakukuwa na mtu yeyote yule aliyefahamu zaidi ya Tatiana na watu waliotaka kumuua. Wengi walimuonea huruma kwani walijua kwamba hizo zilikuwa hujuma kutoka kwa watu wengine ambao hawakutaka kuona maendeleo ya msichana huyo.
Hakukuwa na aliyefahamu kuhusu usaliti wa mapenzi aliokuwa ameufanya, wanaume wawili walitaka kumuua kwa kuwa tu aliwasaliti kitu kilichowafanya kuwa na hasira mno dhidi yake.
“Ila zitakuwa fitina tu,” alisikika jamaa mmoja aliyekuwa ameshika Gazeti la Ijumaa.
“Ila hata mimi nahisi hivyo! Jamaniiiii...mbona wanataka kutuulia mtu wetu? Mbona wana wivu sana hawa watu?” aliuliza mwanamke mmoja, alionekana kuwa kwenye mapenzi ya dhati kwa Tatiana.
Tanzania hakukukalika, kila mtu alikuwa akimzungumzia Tatiana aliyeonekana kuwa na bahati mbaya kutokana na yale yaliyokuwa yakitokea, kuna wakati walihisi kwamba bado mpenzi wake wa zamani, Smith alikuwa akimwandama, alitaka kumuua kutokana na kile kilichokuwa kimetokea, kuachwa solemba na kuamua kuwa na mwanaume mwingine.
Kila mmoja aliandika maoni yake katika mitandao ya kijamii, hisia zao kali ndizo zilizoonyesha kwamba ni kwa kiasi gani walikuwa wakimpenda Tatiana ambaye alikuwa na sura ya upole, inawezekana kuliko watu wote duniani.
“Kwani anaendeleaje?”
“Kwani gazeti wameandikaje?”
“Kwamba yupo salama sasa hivi! Hivi ni kweli au wanataka kutupoza tu?”
“Inawezekana ikawa kweli,” alisema mwanamke mmoja.
Watu wengi wakaanza kumuombea uzima Tatiana, hali yake bado haikuwa imetengemaa na kuna watu waliendelea kumtafuta ili wamuue. Mpaka kufikia hatua hiyo, tayari wakajua kwamba msichana huyo alitakiwa kupewa ulinzi mkubwa ili yasimkute balaa aliyokuwa akitaka kukutana nayo.
Hospitalini hapo, ulinzi ukaongezwa zaidi, kile kilichotokea kilionekana kuwa kosa kubwa mno hivyo walitaka kuhakikisha kwamba kila kitu kinakuwa salama. Polisi waliokuwa na bunduki zaidi ya watano walikuwepo nje ya chumba kile.
Nje ya jengo hilo getini, polisi waliongezeka tena huku wakiwa na picha za Nathan kisiri kwani hawakutaka mtu yeyote yule agundue hilo. Kila aliyepita, alikuwa akikaguliwa haswa, haikujalisha kama alikuwa akienda kumwangalia mgonjwa wake au la.
*****
Nathan aliendelea kufikiria kuhusu Tatiana, kichwa chake kiimuuma mno na hakuamini kile alichokuwa akikiona kwamba msichana huyo hakufariki dunia, aliokolewa katika hatua za mwisho kabisa katika kipindi alichokuwa akitokwa na mapovu mdomoni.
Moyo wake ukawaka kwa hasira, hakuamini kile alichokuwa akikiona kwenye televisheni kwamba alijitahidi kufanya kila kitu kwa umakini mkubwa lakini mwisho wa siku hakufanikiwa juu ya kile alichokuwa amekipanga.
Nathan hakutaka kukubali, hakutaka kuona msichana huyo akiendelea kuwa hai kwani kwa jinsi alivyoona, hakustahili kabisa kuvuta pumzi ya dunia hii, hivyo akajipanga kupeleka mashambulizi kama kawaida yake.
Kwa mara huii ya pili kuingia ndani ya hospitali ile, hakutaka kujifanya kama daktari bali alitaka kujifanya mwandishi wa habari kutoka katika Shrika kubwa la Habari Duniani, CNN. Alichokifanya ni kuingia katika Mtandao wa Google ambapo huko akaona jinsi vitambulisho vya wafanyakazi wa shirika hilo vilivyokuwa na hivyo kutengeneza vyake.
Zoezi hilo lilitumia msaa manne, akapewa kitambulisho chake kilichokuwa na picha yake kisha kununua kamera kubwa, vyote hivyo alikuwa akivifanya ili aweze kupata ruhusa ya kuingia ndani ya chumba kile kwa kisingizio cha kumpiga picha Tatiana kisha kutumia nafasi hiyohiyo kumuua.
Nathan alifanya maandalizi yote mpaka akawa na nguo za CNN ambapo alipozivaa na kuanza kuelekea katika hospitali ile, hakukuwa na mtu yeyote alyeweza kugundua kwamba mtu huyo hakuwa mwandishi kama alivyoonekana bali alikuwa muuaji.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Getini, walinzi hawakuwa na maswali naye, wakamruhusu kuingia ndani, kama kawaida yake, alitembea kwa kujiamini sana kiasi kwamba alijipa uhakika kwamba siku hiyo angekamilisha kile alichotaka kukifanya.
Akaingia ndani ya jengo hilo, walinzi na polisi wote waliokuwa hospitalini hapo, hakukuwa hata na mmoja aliyekuwa na habari naye jambo lililompa urahasi mno kupita na kuelekea kule kilipokuwa chumba kile.
Alipofika katika korido iliyokuwa na chumba kile, alipotoa kitambulisho na kuwaonyesha kwamba alikuwa mfanyakazi kutoka katika Shirika la Habari la CNN, hakukuwa na polisi yeyote yule aliyemuuliza maswali zaidi, wakamuuliza shida yake ambapo akawaeleza kwamba alitaka kumuona Tatiana na kumpiga picha ili wafuasi wake wapate kujua hali yake ilikuwaje kipindi hicho.
“Hakuna tatizo, karibu sana mwandishi, huwa tunaziheshimu sana kazi zenu, hasa nyie CNN na BBC, ila kama wangekuwa waandishi wengine, tusingekuruhusu,” alisema polisi mmoja huku akitoa tabasamu pana.
Ugumu ambao aliufikiria Nathan kipindi cha nyuma haukuwepo hata mara moja. Akaruhusiwa na kuanza kuufuata mlango wa kuingia ndani ya chumba kile. Alipofika humo, alijua kwamba Buffet angekuwemo chumbani humo lakini kitu cha ajabu, mwanaume huyo hakuwepo hivyo kumsogelea Tatiana pale kitandani alipokuwa amelala, na hapohapo akafungua zipu ya begi lake alilobebea kamera na kutoa kisu kilichokuwa na ncha kali, akajiandaa kumuua Tatiana kitandani pale.
Ulinzi imara ulikuwa umeimarishwa, kila polisi aliyekuwemo ndani ya hospitali hiyo alikuwa na picha ya Nathan hivyo isingekuwa na ugumu wowote ule kumgundua katika kipindi alichokuwa akifika hospitalini hapo na kujifanya mwandishi wa habari kutoka CNN.
Walimgundua mapema sana na taarifa zikatolewa haraka kwamba hawakutakiwa kuonyesha ishara zozote zile za kumshtua, walitakiwa kumuonyeshea upendo wowote ule huku hata Buffet akiambiwa kwamba hakutakiwa kukaa karibu na chumba kile.
Hali ambayo alionyeshewa ikampa uhakika kwamba hakugundulika hivyo kutokuwa na wasiwasi kabisa, akajua kwamba iwe isiwe ni lazima kufanya mauaji kama alivyokuwa amepanga.
Taarifa zikapelekwa mpaka ndani ya hospitali ile, Dk. Rajiv akapewa taarifa kwamba yule muuaji alikuwa amefika hospitalini hapo, na wakati huu hakujifanya daktari bali alijifanya kuwa mwandishi wa habari kutoka CNN.
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi pekee ya kujitangaza duniani kwamba ulinzi wao ulikuwa imara na hata mara ya kwanza kile kilichokuwa kimetokea, kilitokea kwa bahati mbaya tu, hivyo akawaambia baadhi ya polisi waingie ndani ya chumba alichokuwa Tatiana na wajifiche huku wakimsikilizia yule muuaji.
“Pia kumbukeni kutokumuonyesha tofauti zozote zile,” alisema Dk. Rajiv.
Hakutaka kuendelea kufanya kazi zake, akabaki akisikilizia kile kilichokuwa kikiendelea. Moyoni alimuomba Mungu aweze kufanya kama kile alichotaka kukifanya, muuaji akamatwe na hatimaye afikishwe mbele ya sheria.
Nathan alikishikilia kisu mkononi mwake, alisimama umbali wa kama hatua nne kutoka kilipokuwa kitanda cha Tatiana. Kila alipokuwa akimwangalia msichana huyo kitandani pale, hasira zilimshika zaidi, hakupenda kumuona akiendelea kupumua hata kama alikuwa kwenye hali ya mateso makali namna ile.
Hata kabla hajaanza kupiga hatua kumsogelea zaidi, ghafla akasikia watu wakitoka nyuma ya kabati la kuwekea dawa walipokuwa wamejificha, walikuwa polisi wenye bunduki mikononi mwao, Nathan akapigwa na mshtuko mkubwa, watu wenye bunduki walisimama mbele yake, bunduki zikiwa zimemuelekezea yeye huku akiwa na kisu mkononi mwake.
“Upo chini ya ulinzi,” alisema polisi mmoja.
“Nyanyua mikono juu,” alisema polisi mwingine.
Walijua kwamba Nathan alikuwa na kisu mkononi mwake, walichokifanya ni kumuwahi na kisha kumlaza chini kwani walijua kwamba endapo wasingefanya hivyo basi kwa kasi ya ajabu angeweza kumchoma kisu msichana huyo hapo kitandani.
“Niacheni nimuueeee...niacheni nimuueeee malaya huyu...” alisema Nathan huku akiwa amelazwa chini.
“Hebu nyamaza huko.”
“Niacheniiii...ameniumiza sana mpumbavu huyuuuu....”
Hakukuwa na aliyemsikiliza, kelele zile alizokuwa akizipiga ndizo zilizowafanya polisi waliokuwa nje kujua kwamba tayari kile walichokuwa wamekipanga kilifanikiwa, walichokifanya ni kuingia ndani ya chumba kile huku wakitangulizana na Buffet aliyekuwa akimwangalia Nathan kwa macho ya chuki mno.
Japokuwa alikuwa akizungumza maneno mengi lakini hakuweza kuachiwa, alibebwa mzobemzobe na kupelekwa nje ya chumba kile huku Buffet ambaye hakuongea kitu chochote kile akibaki chumbani mule huku akimwangalia mpenzi wake, Tatiana.
Kule alipopelekwa, Nathan aliwekwa katika chumba kimoja kilichokuwa na giza totoro, kilionekana kama stoo ambapo kulikuwa na harufu kali ya madawa kitu kilichoonekana kuwa mateso makubwa ambayo hakuwahi kuyapata maishani mwake.
Alibaki chumbani humo usiku mzima, hakukuwa na mtu aliyeshughulika naye chochote kile, alifungiwa na madaktari kuendelea na shughuli zao huku pale nje wakimuacha polisi mmoja aliyeendelea kulinda huku akiwa na bunduki mkononi mwake.
Walichokifanya, hawakutaka kumpeleka kituoni wakati huo, walijua kwamba endapo angekwenda kituoni wasingeweza kumpata tena hivyo nao walichukua nafasi hiyo kumpa mateso na ndipo baadae achukuliwe na kupelekwa katika kituo kikubwa cha polisi.
“Get me out of here...” (Nitoeni humu) alipiga kelele Nathan lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyejali, bado giza na idadi kubwa ya mbu iliendelea kumtesa chumbani mule.
Nathan aliendelea kuwa na hasira mno, hakuamini kama alishindwa kutekeleza kile alichokuwa amekipanga mwanzo, alijikuta akilia tu chumbani humo kwani hasira kali alizokuwa nazo juu ya Tatiana zilimkaba kooni.
Siku iliyofuata, mlango ukafunguliwa, polisi wanne waliokuwa na bunduki wakaingia chumbani humo na kisha kumchukua huku nje ya chumba hicho wakibaki polisi wawili. Nathan alionekana kuwa kama gaidi mkubwa aliyetakiwa kuwekewa ulinzi wa uhakika kwani vinginevyo angeweza kutoroka.
“Kuweni makini, ndiye huyohuyo aliyelipua gari kule Marekani,” alisema polisi mmoja, wenzake wote wakashikilia vizuri bunduki zao.
Taarifa zilikuwa zimezagaa kila kona kwamba yule mtu aliyetaka kumuua Tatiana siku mbili zilizopita alikuwa amekamatwa na hivyo alikuwa akipelekwa polisi kwa ajili ya mahojiani kisha kupelekwa mahakamani ambapo angeshtakiwa kwa kosa la kukusudia kuua.
Waandishi wa habari hawakutaka kukaa mbali, kwa kuwa walizipata taarifa hizo tangu usiku, hivyo asubuhi na mapema walikuwepo hospitalini hapo kwa ajili ya kupiga picha kila kitu ambacho kingeendelea kwa mtuhumiwa yule.
Wakati Nathan akitolewa ndani ya hospitali ile, tayari flashi za kamera zikaanza kummulika mfululizo, aliipeleka mikono yake ili asionekana sura lakini polisi walikuwa wakiishusha na kuiacha sura yake wazi ili ionekane vizuri.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hebu shusha mikono yako hapa!” alisema polsi mmoja huku akimshusha mikono ile Nathan.
Hakuwa na jinsi, alikuwa chini ya ulinzi na alitakiwa kufanya kile walichotaka polisi wale akifanye, hivyo akashushwa mikono ile na kuendelea kupigwa picha.
Hakukuwa na mtu aliyeamini kama yule kijana ndiye aliyetaka kumuua Tatiana. Alionekana kuwa kijana mpole, mzuri wa sura ambaye hakufanana kabisa na muuaji yeyote yule duniani. Maswali yakaanza kumiminika kama Nathan ndiye aliyetaka kumuua Tatiana au polisi walikuwa wamecheza mchezo fulani ili hospitali ile irudishe heshima kama iliyokuwa nayo mwanzo.
“Mbona ni kijana mzuri tu,” alisema mwanamke mmoja.
“Hata mimi nashangaa, siamini kabisa.”
“Hapana kuna kitu.”
“Unahisi kuna nini?”
“Polisi hawa, wanaweza wakawa wamecheza mchezo na madaktari.”
“Una uhakika hicho kinaweza kutokea?”
“Kwa nini kisiweze? Kila mmoja anaangalia tumbo lake tu,” alisema mwanamke yule.
Kitu kilichowavutia zaidi watu ni kwamba kijana huyo alitaka kumuua Tatiana huku akijifanya kuwa mwandishi wa habari kutoka katika Shirika la Habari la CNN. Watu wengi waliamini kwamba Nathan alikuwa mwandishi kweli kwani muonekano wake ulionekana mtu fulani aliyekuwa na uwezo kifedha.
Wakati tetesi zile zikizidi kuenea kwamba inawezekana Nathan alikuwa mtangazaji kweli, mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo la habari, bwana Swan akatoa tamko kwamba hawakuwa na mfanyakazi mwenye jina hilo, kwa kuwa nao walikuwa wamechafuliwa, akaahidi kwamba ni lazima nao wangekwenda kushitaki.
“Huyu ataozea jela aiseee...hapa haponi,” alisema polisi mmoja huku akimwangalia Nathan aliyekuwa ameinama garini akilia.
“Huo ndiyo ukweli. Gaidi la kimataifa hili,” aliongezea polisi mwingine.
Bado moyo wa Nathan ulijuta, alishindwa kujua ni mahali gani alikosea mpaka kujikuta akikamatwa na polisi kisha kuanza kupelekwa kituoni huku akiwa hajatimiza lengo lake la kumuua Tatiana.
Alijaribu kuwaeleza polisi kwale kwamba alitaka kumuua Tatiana kutokana na usaliti mbaya aliokuwa amemfanyia lakini hakukuwa na yeyote aliyemuelewa, wote hao walimuona kuwa mtu mbaya ambaye alitakiwa kiufungwa hata kifungo cha maisha jela.
Safari ile ilichukua dakika kumi huku wakisindikizwa na magari mengi ya polisi mpaka walipofika kituoni ambapo Nathan akateremshwa huku akiwa na pingu mikononi kisha kuingizwa ndani ya jengo la kituo hicho. Macho yake yalikuwa mekundu kwa sababu ya kulia sana, hakuamini kabisa kama kweli alikamatwa hata kabla hajatekeleza mpango wake wa kumuua Tatiana. Moyoni alijuta.
*****
Taarifa za kukamatwa kwa Nathan ziliendelea kutapakaa dunia nzima, Waliberia wakachanganyikiwa, walimfahamu Nathan kama kijana mtulivu, mpole ambaye alipendwa na wanawake wengi kutokana na uzuri wake.
Alikuwa mtoto wa bilionea mkubwa nchini humo lakini kamwe hakuwa na majivuno. Alipendwa na watu wengi na hata wale wachache waliokuwa wakimchukia walifanya siri mioyoni mwao kwani miongoni mwa watu waliopenda kusaidia watu wengine, Nathan alikuwa mmojawapo.
Kitendo cha kukamatwa kwake baada ya kugundulika kwamba ndiye aliyetaka kumuua msichana Tatiana, Waliberia wengi walikataa hilo na kuamini kwamba kulikuwa na nguvu ya mtu fulani juu ya tukio lile kwani mtu kama Nathan asingeweza kufanya kitu kama kile kutokana na upole mwingi aliokuwa nao.
Wazazi wake wakachanganyikiwa mara baada ya kupata taarifa hizo. Nyumbani hakukukalika, siku hiyohiyo wakapanda ndani ya ndege yao binafsi na kuanza kuelekea nchini India kwa ajili ya kumuona kijana wao kwani mara ya mwisho aliwaaga kwamba alikuwa akienda nchini Nigeria, sasa kwa nini awe nchini India?
“Nakumbuka alituambia anakwenda Nigeria,” alisema baba yake.
“Ndivyo alivyoaga.”
“Sasa iweje awe India?”
“Hata mimi nahangaa, nahisi kuna kitu,” alisema mama yake.
Kila mmoja alichanganyikiwa, hawakuamini kile kilichokuwa kikiendelea kwamba kijana wao alikuwa amekamatwa na hivyo kufikishwa mbele ya sheria huku akiwa na kesi iliyofunguliwa jalada lisemalo kwamba alikuwa na kesi ya kutaka kuua.
Ndege ilikata mawingu na ndani ya masaa sita ikaanza kuingia nchini India. Walipoteremka kutoka ndani ya ndege, hali ya hewa ilikuwa ni ya joto mno ambapo wakaanza kutembea mpaka kwenye gari lililokuwa limewafuata na kisha kuondoka na kuelekea hotelini hata kabla ya kwenda kuonana na mtoto wao.
Hotelini hakukukalika, kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuona Nathan kiasi kwamba hawakutaka kukaa sana na hivyo kuulizia sehemu alipokuwa amewekwa na kisha kuelekea huko huku kila mmoja akiwa amechanganyikiwa.
“Tunahitaji kumuona kijana wetu,” alisema baba yake Nathan alikuwa akizungumza na polisi.
“Nani?”
“Nathan.”
“Nyie ni wakina nani?”
“Wazazi wake.”
“Hamruhusiwi kumuona.”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Kisa?”
“Nyie jueni kwamba hamruhusiwi kumuona,” alisema polisi aliyekuwa kaunta maneno ambayo yaliungwa mkono na kila polisi.
Baba yake Nathan hakutaka kuhangaika, alichokifanya ni kunyanyua simu yake na kuanza kupekua majina kadhaa yaliyokuwa humo, alipolipata jina alilokuwa akilitaka, akabonyeza kitufe cha kupiga simu na baada ya sekunde kumi, mtu wa upande wa pili akapokea simu, alikuwa swahiba wake mkubwa, waziri mkuu wa nchi hiyo na kuanza kuzungumza naye.
Alimwambia mengi tu lakini kubwa zaidi ni yeye kuzuiliwa kumuona mtoto wake. Hilo wala halikuwa tatizo kubwa, akaambiwa ampe simu mkuu wa kituo hicho ambaye baada ya kukabidhiwa akaanza kufokewa kama mtoto kwa kile kilichokuwa kimetokea kituoni kwake.
“Samahani mzee,” alisema mkuu wa kituo baada ya simu kukatwa.
“Hakuna cha samahani, nionyesheni kijana wangu haraka,” alisema baba yake Nathan na hapohapo wakachukuliwa na kupelekwa ndani ya chumba kimoja kwa heshima kubwa na kuambiwa kusubiri hapo.
Wala haukuchukua muda mrefu, Nathan akaletwa chumbani hapo. Hakuwa amejeruhiwa, hakupigwa hata kidogo. Akawekwa kwenye kiti huku akiwa amefungwa pingu. Hapohapo baba yake akaagiza afunguliwe zile pingu kitendo kilichofanyika haraka sana.
“Nathan, nini kimetokea?” aliuliza baba yake.
“Baba! Unamkumbuka yule mwanamke aliyenifanya nimuache Dassy?”
“Ndiyo!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiye huyu niliyetaka kumuua!”
“Unasemaje?”
“Ndiye huyuhuyu niliyetaka kumuua. Ameniumiza sana, hatakiwi kuishi hata mara moja,” alisema Nathan huku machozi yakianza kumbubujika mashavuni mwake.
“Nathan....”
“Baba! Ameniumiza sana, nimemuacha mwanamke aliyekuwa akinipenda kwa moyo wa dhati, halafu leo anafanya hivi! Anafanya hivi ili iweje? Baba, nina hasira naye mno,” alisema Nathan huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikisema.
Mama yake akashindwa kuvumilia, naye akajikuta akibubujikwa na machozi kwani kitendo cha kuyaona machozi ya mtoto wake kilimuumiza mno moyoni mwake. Alimpenda sana, hakutaka kumuona akilia, hakukuwa na mtu aliyekuwa akimpenda kama Nathan.
Muda huo, Nathan akaanza kusimulia kila kitu kilichotokea tangu siku ya kwanza alipokutana na Tatiana na kile kilichoendelea katika maisha yao ambapo kwake ilionekana kama maisha yaliyojaa maumivu makali mno.
“Unataka tukufanyie nini?” aliuliza baba yake.
“Chochote kile ili nitoke na kumuua Tatiana.”
“Hapana! Hatutaki utoke na kumuua huyo malaya. Naomba uachane naye na urudi kwa Dassy,” alisema baba yake.
“Ataweza kukubali?”
“Hana tatizo. Amekuwa na maisha yenye majonzi siku zote, amekuwa akilia sana, amekataa kuolewa na mwanaume mwingine, aliwaambia wazazi wake kwamba kama hatoolewa na wewe, kamwe hatoweza kuolewa na mwanaume mwingine yeyote yule na ni bora aishi hivyohivyo maishani mwake bila mume. Nathan, Dassy anakupenda mno, achana na huyu malaya, rudi kwa Dassy,” alisema mama yake huku akiyafuta machzoi yake.
“Ila Tatiana amaniumiza mama!”
“Mungu atamlipia. Hautakiwi kulipiza mabaya kwa mabaya, haujawahi kusoma hivyo kwenye Biblia?” aliuliza mama yake.
“Nishasoma mama.”
“Achana naye na urudi kwa Dassy,” alisema baba yake.
Moyo wake ulimchukia mno Tatiana lakini hakuwa na jinsi, maneno waliyoyaongea wazazi wake yakaanza kuubadilisha moyo wake na hatimaye kukubaliana nao kwamba mara atakapoachiwa huru basi atarudi nchini Liberia na kuungana na msichana wake wa kipindi cha nyuma, Dassy na hatimaye aweze kumuoa.
Siku hiyo alirudishwa tena sero ambapo baada ya siku mbili akapelekwa mahakamani. Huko, ni rushwa na uswahiba wa ba ba yake ndiyo uliokuwa umekolea kiasi kwamba mwisho wa siku Nathan hakuonekana kuwa na hatia yoyote lile kwani ushahidi haukuwa umejitosheleza na hivyo kushinda kesi katika mazingira yaliyojaa utata mwingi.
Alichokifanya baada ya kushinda kesi hiyo ni kurudi nchini Liberia. Japokuwa magazeti mengi yaliandika juu ya utata huo lakini hakukuwa na watu waliopeleka kesi hiyo tena mahakamani hivyo Nathan kuwa huru kwa asilimia mia moja.
“Dassy!” alimuita msichana wake, Dassy akayainua macho na kumwangalia Nathan machoni.
“Naomba unisamehe kwa yote niliyotenda, ninaahidi kukupenda kwa moyo wangu wote,” alisema Nathan huku akibubujikwa na machozi.
Dassy hakupindua kwa Nathan, alimpenda kwa moyo wote. Kitendo alichokuwa amefanyiwa kilikuwa kibaya lakini hakutaka kukumbuka chochote kile, akaamua kumsamehe Nathan na baada ya mwezi mmoja wawili hao wakafunga ndoa kanisani na kuwa mke na mume.
“Nitakupenda milele,” alisema Nathan huku uso wake tu ukionyesha kumaanisha alichokuwa akikisema.
“Nitakupenda pia,” alisema Dassy na kisha kukumbatiana.
****
Japokuwa moyo wake haukuridhika kama alivyotaka lakini hakuwa na jinsi, akaamua kuachana na Tatiana kwani kwa kile alichokifanya moyo wake ulimwambia kwamba lingekuwa fundisho kwa msichana huyo katika maisha yake yote.
Akawa bize na masomo na baada ya kumaliza mwaka mmoja uliobakia tu, akaanza kufanya mipango ya kusomea uchungaji kwani hakutaka tena kujichanganyachanganya kama alivyokuwa akifanya.
Chuki aliyokuwa nayo dhidi ya Tatiana, akaamua kuitoa na kutengeneza maisha yake na Mungu. Alidhamiria kwa moyo mmoja kumtumikia Mungu, baada ya kukubaliana na mchumba wake, Lydia, moja kwa moja Peter akaanza masomo katika Chuo cha Biblia kilichokuwa Dodoma.
Penzi lake kwa msichana Lydia lilizidi kuongezeka, katika maisha yake yote, msichana huyo alikuwa kila kitu. Mara kwa mara walipokuwa likizo, ilikuwa ni lazima kuwasiliana na Lydia na kisha kumfuata mkoani Morogoro ambapo walikuwa wote katika kipindi chote pasipo kufanya mapenzi, walitaka kufanya hivyo mpaka watakapoingia ndani ya ndoa.
Baada ya mwaka wa kwanza chuoni kumalizika, hapo ndipo alipopata mdhamini ambaye alitaka kumsomesha katika Chuo cha Biblia cha Holly Jehovah kilichokuwa ndani ya Jiji la Toronto nchini Canada.
Hiyo ilikuwa ni nafasi yake ya kipekee ambayo hakutaka kuiona ikipita. Kwa kuwa alikuwa ameandaliwa kila kitu, kilichokuwa kimebaki kilikuwa ni safari tu. Akawaambia wazazi wake, wote hawakuamini, walijua fika kwamba kijana wao alikuwa na ndoto za kufika mbali, alikuwa na kiu ya kuwa mchungaji mkubwa hapo baadae.
“Tunamshukuru Mungu kwa hilo, hakika baraka zake ni za milele,” alisema baba yake, mchungaji Lazaro.
Hakukuwa na cha kusubiri, baada ya wiki moja, wazazi wake na mchumba wake, Lydia wakamsindikiza mpaka uwanja wa ndege ambapo akaingia ndani ya ndege ya Shirika la Alliance Air na safari ya kuelekea nchini Canada kuanza.
Njiani, Peter alikuwa na furaha tele, hakukuwa na kitu alichokuwa akikipenda kama kwenda kuchukua digrii yake ya kwanza nchini humo. Alijiona kupewa heshima kubwa ambayo isingeweza kusahaulika maishani mwake.
Alipofika nchini Canada, akapokelewa uwanjani hapo kwa gari la chuo na kisha kuanza kupelekwa kilipokuwa chuo cha Holly Jehovah. Njiani, macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule, kila kitu alichokuwa akikiona mbele yake kilimshangaza kwani hakuwahi kuwa kwenye nchi nzuri kama ilivyokuwa Canada.
Moyo wake ulifurahi sana, akajikuta akianza kumshuru Mungu mulemule ndani ya gari kwani kile kilichokuwa kikitokea kwake kilionekana kuwa kama muujiza ambao hakuutegemea kabisa maishani mwake.
Baada ya kuchukua dakika ishirini njiani, gari likaanza kuingia ndani ya eneo la chuo hicho. Kilikuwa miongoni mwa vyuo vikubwa vya dini, kilijengwa vizuri na kilikuwa na eneo kubwa la kupumzikia na hata kujisomea.
Alipoteremka kutoka garini tu, Peter akainyanyua mikono yake juu na kuanza kumshukuru Mungu. Hapo ndipo alipoanza safari ndefu ya kumtumikia Mungu maishani mwake, hakutaka kukumbuka kitu chochote kilichotokea, alichokuwa akikitaka ni kuwa karibu na Mungu tu.
**** CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilichukua mwezi mmoja na nusu na ndipo Tatiana akayafumbua macho yake kitandani pale. Mwili wake ulipungua mno, alionekana kuchoka kupita kawaida. Mtu wa kwanza kabisa kumuona msichana huyo wakati amefumbua macho alikuwa nesi ambaye kwa furaha kubwa akatoka chumbani mule na kwenda nje.
“Vipi?” aliuliza Buffet ambaye alikuwa amekaa kitini, kasi aliyotoka nayo nesi yule ilimbidi ashangae na kumuuliza.
‘Tatiana...”
“Amefanya nini?” aliuliza lakini nesi hakujibu swali hilo, akakimbia kuelekea katika ofisi ya Dk. Mundesh.
Buffet akashikwa na hofu, akahisi kwamba inawezekana Tatiana akawa amefariki dunia, akajikuta moyo wake ukianza kudunda kwa hofu kubwa, ila mbali na hofu hiyo, akaanza kujiuliza juu ya tabasamu alilokuwa amelitoa nesi huyo wakati akimpa taarifa, akahisi kwamba inawezekana Tatiana alikuwa amefumbua macho.
Hakutaka kubaki kitini pale, alichokifanya ni kukimbilia chumbani, akapiga hatua kuelekea katika kitanda alichokuwa Tatiana, kile alichohisi ndicho kilichotokea, Tatiana alikuwa macho, alikuwa akiangalia huku na kule japokuwa hakuonekana kuwa na nguvu.
“Tatiana mpenzi...” alijikuta akiita Buffet huku machozi yakianza kumbubujika mashavuni mwake.
Hakuamini kile alichokuwa akikiona, baada ya mwezi miezi karibia miwili kuwa kimya kitandani, hatimaye mwisho wa siku Tatiana akayafumbua macho yake na kuona tena. Kwa Buffet, wakati mwingine alihisi kama yupo katika usingizi wa kifo ambapo baada ya muda angeshtuka kutoka kitandani, kilichokuwa kikitokea, hakikuwa ndoto, lilikuwa tukio halisi lililotokea katika maisha yake.
Tatiana hakuzungumza chochote kile, Buffet alibaki akimwangalia mpaka pale Dk. Mandesh alipofika chumbani mule akiwa na manesi wengine. Kila mmoja akaonekana kufurahia maendeleao ya Tatiana, hapohapo wakamuona Buffet atoke chumbani mule ili wafanye kazi yao.
“Usihofu, kazi imekamilika, amini kwamba atarudi kama alivyokuwa mwanzo,” alisema Dk. Mandesh huku akionekana kuwa na furaha tele.
****
Mzee Sangiwa na mkewe wakafika nchini India, walifurahia kile walichokuwa wamekutana nacho kwamba binti yao mpendwa alikuwa amerudiwa na fahamu. Hizo ndizo stori zilizosambaa duniani kwamba mwanamuziki yule aliyekuwa amepoteza fahamu, alikuwa amerudiwa na fahamu.
Ilikuwa fuiraha kwa kila mtu aliyeipata habari hiyo, watu wengi wakiwemo masupastaa wakajitolea kumtembelea nchini India na kumjulia hali kwani maendeleo yake yalimshangaza kila mtu kwani wengi walidhani kwamba angekufa kitandani.
Siku zikakatika, wiki zikakatika na hatimaye Tatiana akarudi katika hali yake ya kawaida, akawa na nguvu na hivyo kuruhusiwa kurudi nchini Tanzania kuendelea na majukumu yake.
Kama kawaida Watanzania wakajikusanya uwanja wa ndege kwa ajili ya kumpokea na kumpongeza kwa namna alivyoweza kupambana kitandani mpaka kuwa kama alivyokuwa kipindi hicho.
Alipoanza kuteremka ndani ya ndege, kelele za watu zikaanza kusikika uwanjani hapo, japokuwa Tatiana alionekana kukonda sana lakini wala hakukuwa na mtu aliyejali, kitendo cha kuonekana akiwa mzima wa afya kilimfurahisha kila mtu aliyekuwa akimwangalia.
Baada ya kupokelewa, akapelekwa hotelini na wazazi wake ambapo baada ya siku mbili safari ya kuelekea Shinyanga ikaanza. Katika kila kona aliyotokeza, watu walikuwa wakishangilia, hakukuwa na aliyeruhusiwa kupiga picha na msichana huyo tena kwani waliogopa kutokea kitu kama kile kilichotokea chuo kikuu.
“Ninahitaji kuolewa,” alisema Tatiana, alikuwa amewaweka wazazi wake kwenye kikao cha usiku, alitaka kuzungumza nao kuhusu mipango yake ya ndoa na Buffet.
“Umeamua kutoka moyoni?”
“Ndiyo baba! Ninataka kuolewa sasa,” alisema Tatiana.
“Hakuna tatizo, sisi kama wazazi, tunaruhusu hilo kwa moyo mmoja,’ alisema mzee Sangiwa.
Huo ndiyo uamuzi aliokuwa ameamua, hakutaka kuishi na Buffet kama wapenzi tu badala yake alitaka kuolewa kabisa. Taarifa zilipoanza kutangazwa kuhusu ndoa hiyo, kila mmoja alifurahia huku wengine wakitamani kuona hasuri hiyo itakavyofanyika.
Ili kama maandalizi, baada ya kurudi nchini Marekani, Tatiana akaitwa katika majarida mbalimbali kwa ajili ya kupiga picha, alifanyiwa mambo mengi hata zaidi ya alivyofanyiwa Kim Kardashian wakati alipotaka kuolewa na Kanye West.
Jina lake lilikuwa kubwa mno, hivyo watu walipoona majarida mengi yakiwa na picha zake kwa mbele huku amevaa shela, kila mmoja akayapapatikia na kuyanunua kwa wingi. Hakukuwa na mwanamuziki aliyekuwa akipendwa sana duniani kama Tatiana.
“Ninakupenda Buffet! Ninakupenda mume wangu mtarajiwa,” alisema Tatiana huku akiwa na furaha mno, hakuamini kama alikuwa akienda kuolewa mwaka wa pili mara baada ya kupata jina kubwa duniani.
“Ninakupenda pia, ninakuahidi kukuoa kipenzi,” alisema Buffet huku akionekana kuwa na furaha.
Wakati tetesi juu ya harusi hizo zikiendelea kusikika kote duniani, ndicho kilikuwa kipindi ambacho albamu yake ya kwanza iitwayo Love Revenge ilipokuwa ikitoka hivyo kuanzisha ziara maalumu iliyopewa jina la Last Trip ambapo alipanga kutembea nchi mbalimbali kwa ajili ya kuitangaza.
Tatiana alifanya kila alichoweza, hakutaka kubaki alipokuwa, bado aliendelea kukusanya fedha, katika kila tamasha alilokuwa akilifanya, watu walikuwa wakijazana, tiketi zilikwishaisha katika sehemu zote ambazo alitarajiwa kwenda kufanya tamasha huko.
“Ni nchi tatu ndizo zilizobaki, Ujerumani, Romania na Finland,” alisema Tatiana, wakati huo walikuwa nchini Uingereza.
“Kote tutakuwa pamoja. Hivi nilishawahi kukwambia kwamba baba yangu ni Mjerumani?” aliuliza Buffet.
“Hapana!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Baba yangu ni Mjerumani, mama yangu ni Mmarekani, kwa hiyo tunakwenda nyumbani,” alisema Buffet huku akionekana kuwa na futraha.
“Nitafurahi kuwaona mashemeji zangu,” alisema Tatiana pasipo kujua kwamba kile kitakachotokea nchini humo ndicho kilichobadilisha maisha yake yote, kitu kilichomfanya kulia kila siku na hata wakati mwingine kutamani kujiua.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment