Simulizi : I Killed My Beloved One (Nilimuua Nimpendaye)
Sehemu Ya Tatu (3)
Japo alikuwa akizungumza kwa taabu, huku akilia, niliweza kumuelewa ambapo aliniambia kwamba wanaume ni watu wabaya sana wanaoweza kufanya ukajuta kuzaliwa. Aliongea mambo mengi kwa mafumbo, nilijitahidi kuwa makini lakini mengine nilikuwa siyaelewi.
Haikuwa kawaida kwa mama kuzungumza kwa busara kiasi hicho kwani tangu kifo cha baba, tulizoea kumsikia akifoka muda mwingi. Moyoni nikaanza kupatwa na wasiwasi kwani niliwahi kusikia kwamba ukiona mgonjwa anaongea sana, ujue anakaribia kuaga dunia. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mama! Mamaa! Usiondoke mama,” nilisema huku nikitokwa na machozi kwani mama alikuwa akiongea kwa uchungu sana kama mtu anayetaka kukata roho. Cha ajabu, alinijibu kwamba hafi ila cha moto anakiona, nikamuuliza alikuwa anamaanisha nini kusema vile lakini bado aliendelea kuongea kwa mafumbo.
Ilibidi niende kumuita nesi na kumpa taarifa kwamba mama amezinduka, harakaharaka alikuja kwenye kitanda chake na kuanza kumpima vipimo mbalimbali, akaniambia kwamba bado akili zake zilikuwa hazijatulia hivyo alihitaji zaidi muda wa kupumzika.
Akampa dawa za usingizi lakini kabla hajalala, aliniita na kuniambia kitu kilichozidi kunichanganya. Aliniambia kwamba Jimmy hakuwa mwanaume sahihi kwangu na kwamba nikipuuzia alichoniambia, ipo siku nitajuta.
Nilishindwa kuelewa yeye amemfahamia wapi Jimmy wangu kiasi cha kunitolea maneno kama hayo. Nilitamani kumdadisi zaidi lakini nesi aliniambia kwamba nimuache apumzike, sekunde chache baadaye akapitiwa na usingizi mzito na kuniacha nikiwa na maswali mengi yaliyokosa majibu.
Japokuwa ilikuwa ni usiku sana, sikukubali kirahisi, nilichukua simu yangu ambayo muda wote nilikuwa nimeificha, nikatafuta namba za Jimmy na kuanza kumpigia. Cha ajabu, japokuwa ilikuwa ni usiku sana, namba yake ilionesha kwamba inatumika. Niliendelea kumpigia zaidi ya mara tatu lakini bado majibu yalikuwa yaleyale.
“Namba ya simu unayopiga, inatumika kwa sasa, tafadhali jaribu tena baadaye.” Nilishindwa kuelewa Jimmy alikuwa akizungumza na nani usiku wote huo, akili nyingine ilinituma kuamini kwamba huenda anaongea na watu anaofanya nao kazi.
Nilipojaribu kuipiga kwa mara ya nne, simu iliita, nikajikuta nikitabasamu kwani nilikuwa na uhakika kwamba Jimmy atapokea lakini haikuwa hivyo. Simu iliita mpaka ikakata yenyewe. Nilipojaribu kupiga tena, haikuwa ikipatikana hewani kuonesha kwamba ilikuwa imezimwa. Nilijaribu tena na tena lakini bado majibu yalikuwa yaleyale kwamba haipatikani.
Nilijisikia vibaya sana ndani ya moyo wangu, sikupata jibu kwa nini Jimmy ananidharau kiasi hicho kwani tangu nilipokutana naye kimwili kwa mara ya pili, alibadilika mno. Hakuwa tena yule Jimmy ninayemjua, mpole, mcheshi na mwenye sauti ya kubembeleza. Alibadilika na kuwa mtu tofauti kabisa.
Sikulala usiku huo, niliwaza mpaka kichwa kikaanza kuniuma. Kauli aliyoniambia mama kwamba Jimmy hakuwa mwanaume sahihi kwangu ilikuwa ikijirudiarudia akilini mwangu, nikaendelea kujiuliza maswali yaliyokosa majibu.
Nilichokipanga ni kwamba asubuhi kukipambazuka, kaka akija kunipokea kukaa na mgonjwa, niende moja kwa moja nyumbani kwa Jimmy ili kujua kinachofanya akatae kupokea simu zangu. Nilikuwa tayari kumuomba msamaha ili kama kuna kosa lolote nililomfanyia anisamehe.
Sijui tuite ni ulimbukeni au ushamba wa mapenzi! Mwenzenu niliamini siwezi tena kuishi bila Jimmy kwa jinsi nilivyokuwa nampenda. Niliamini yeye ndiyo kila kitu kwenye maisha yangu na nikaapa kulipigania penzi langu kwa kadiri ya uwezo wangu wote.
Mpaka jogoo la kwanza linawika, nilikuwa bado sijapata hata lepe la usingizi, nikaamka na kuanza kujinyoosha huku macho yakiwa yamevimba kutokana na kukosa usingizi usiku kucha. Kwa bahati nzuri, kaka aliwahi sana kuja kunipokea siku hiyo, nikafurahi kwani nilijua nitapata muda mzuri wa kumuwahi Jimmy kabla hajaondoka.
Harakaharaka niliagana na kaka kwa kisingizio kuwa nawahi nyumbani kwenda kupumzika kwani sijalala usiku kucha hasa baada ya mama kurudiwa na fahamu zake. Nikatoka mpaka kituo cha daladala, nikasubiri usafiri na baada ya muda, tayari nikawa nipo ndani ya daladala, mawazo yangu yote yakiwa kwa Jimmy.
Niliwaza kwamba nikifika na kuzungumza naye, tukilimaliza tatizo nitalala kwake mpaka mchana ambapo nitaenda nyumbani kuwaandalia ndugu zangu chakula pamoja na cha mgonjwa.
Ilipogonga saa kumi na mbili, tayari nilikuwa mbele ya nyumba ya Jimmy, nikajaribu kumpigia simu ambapo kama kawaida, iliita bila kupokelewa. Nilizidi kujisikia vibaya lakini nikajua muda si mrefu nitaonana na Jimmy ili kumaliza tofauti kati yetu.
Nilienda kujaribu kugonga geti lakini napo sikupata majibu yoyote, ikabidi nitafute sehemu na kukaa kusubiri mpaka atakapokuwa anatoka. Kwa jinsi nilivyokuwa na usingizi, nilipokaa kwenye ukuta wa nyumba ya jirani ambayo ilikuwa haijamalizika kujengwa, nilianza kusinzia hapohapo.
Nilishtushwa na mlio wa geti lililokuwa linafunguliwa, nikaamka na kusogea pembeni kuangalia kama kweli aliyekuwa anafungua mlango ni Jimmy kwani niliogopa kukutwa na mtu mwingine tofauti na Jimmy. Nikajibanza kwenye ukuta nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kumuona aliyekuwa anafungua geti.
Mara nilimuona Jimmy akitoka, akiwa amevaa nguo za kulalia, sijui ni kitu gani kilinitokea kwani ghafla nilijikuta nikitabasamu na kusahau maudhi yote aliyonifanyia, nikawa nafikiria jinsi atakavyonikumbatia kwa mahaba kama ilivyokuwa siku ile ya kwanza.
Ghafla furaha yangu ilitibuka baada ya kuona mwanamke mwingine akitoka, akaenda kumkumbatia Jimmy na kumbusu huku nikishuhudia. Mapigo yangu ya moyo yalibadilika ghafla, yakaanza kwenda mbio kuliko kawaida. Japokuwa ilikuwa ni asubuhi, nilijikuta nikitokwa na kijasho chembamba.
Kwa kuwa sikuwa mbali na getini, niliweza kumuona vizuri mwanamke huyo. Alikuwa ni mwanamke mnene, mrefu wastani, usoni akiwa amejichubua kiasi cha ngozi yake kubadilika na kuwa nyekundu. Kiumri alikuwa mtu mzima sana na alipishana mno na Jimmy. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ungeweza kudhani ni mtu na mama yake au shangazi yake. Kwa macho yangu nikawashuhudia wakibusiana midomoni, Jimmy akaenda kutoa gari na kabla ya kumpakiza, niliwaona tena wakikumbatiana kimahaba kama wapenzi wa siku nyingi walioshibana. Nilijikuta nikitetemeka kama nimemwagiwa maji yenye barafu.
Nilifumbua mdomo wangu na kumuita Jimmy lakini sauti haikutoka, moyoni nikajihisi kama nimechomwa na kitu chenye ncha kali kutokana na maumivu niliyokuwa nayahisi. Sikuwahi kuumia moyoni kama siku hiyo, miguu ikaniisha nguvu na machozi yakawa yanaulowanisha uso wangu kama chemchemi ya maji.
Taratibu nikakaa chini na kujikunyata kama kifaranga cha kuku kilichonyeshewa na mvua, nikawa nalia kwa kwikwi huku nikihisi kama roho inataka kutoka. Narudia tena, sijawahi kuhisi maumivu ndani ya moyo wangu kama niliyoyahisi siku hiyo! Nilihisi dunia nzima imenielemea, nikatamani ardhi ipasuke na kunimeza.
“Kwa nini Jimmy! Kwa nini umeuvunja moyo wangu Jimmy! Nimekukosea nini kustahili adhabu kali kiasi hiki?” nilisema huku nikiendelea kujikunyata, ile baridi ya asubuhi sasa ilikuwa imeongezeka maradufu na kunifanya nijihisi kama nipo ndani ya jokofu.
Baada ya kukaa pale chini kwa takribani dakika ishirini nikiendelea kuomboleza, nilisikia muungurumo wa gari likija pale nyumbani kwa Jimmy. Hata sijui akili yangu ilikuwa inawaza nini kwani ghafla nilijifuta machozi na kusimama nikijitahidi kujikaza kama hakuna kilichotokea.
“Nimekusamehe Jimmy, bado nakupenda! Sipo tayari kukupoteza,” nilisema kwa sauti ya chini wakati gari la Jimmy likisogea taratibu. Eti licha ya yote niliyoyashuhudia, bado moyo wangu ulikuwa tayari kumsamehe Jimmy. Nilitamani kama ashuke kwenye gari na kuja kunikumbatia kisha aniambie neno lolote zuri! Mapenzi haya, sina hamu!
Tofauti na nilivyotegemea, japokuwa Jimmy aliniona kwani nilikuwa nimesimama sehemu ya wazi ili anione kwa urahisi, alijifanya hajaniona, akanipita na gari lake hadi karibu na mlango wa nyumba yake, akateremka harakaharaka na kufungua mlango wa upande wa pili.
Kwa macho yangu nikamshuhudia msichana mwingine akishuka, ambaye kiumri hatukupishana sana, tena akiwa amevaa sare za shule na mgongoni akiwa amebeba begi la madaftari.
“Karibu sana mpenzi, jisikie upo nyumbani,” nilimsikia Jimmy akimwambia yule msichana, akamshika mkono na kumsaidia kuteremka kwenye gari, akamkumbatia na kumbusu kisha akamuongoza kuingia ndani.
Ufuska ulioje! Yaani ndani ya muda mfupi tu, tayari nilimshuhudia Jimmy akimtoa mwanamke aliyeonesha kwamba alilala naye usiku kucha na muda mfupi baadaye, akaja na mwingine, tena mwanafunzi! Kweli dunia ina mambo.
Alipomuingiza ndani, alirudi na kuliingiza gari lake sehemu ya maegesho huku akiendelea kupuuza uwepo wangu mahali pale. Kwa mara nyingine nikasikia moyo ukinipasuka ‘pyaaa!’, nikajikaza na kumuita Jimmy kwa sauti ya kukatakata.
Alinisogelea kwa dharau na kuniuliza nilikuwa nataka nini? Nikajikakamua huku machozi yakiendelea kunibubujika, nikamwambia mama yangu anaumwa ndiyo maana nimewahi nyumbani kwake asubuhi ile. Nilitumia gia hiyo nikiamini anaweza kunionea huruma na kukaa na mimi japo kwa dakika chache.
“Sasa kwani mimi ndiyo daktari? Hebu niondolee uchuro wako, unalia umesikia kuna msiba hapa? Nakuomba uondoke haraka,” alisema Jimmy kwa sauti ya ukali, akiwa amenikazia macho kuonesha kuwa hakuwa na hata chembe ya masihara.
Nilishangaa kugundua kuwa Jimmy ana sauti ya ukali kiasi kile kwani awali sikuwahi kumsikia, niliamini sauti yake ni ile ya upole na kubembeleza kama alivyonizoesha.
Hata sura yake ilikuwa imebadilika kabisa, machozi yakazidi kunitoka nikiwa siamini kilichokuwa kinanitokea.
“Kosa langu ni lipi kwako Jimmy mpaka kustahili maumivu makali kiasi hiki? Jimmy… nimekukosea nini mi…” nilishindwa kumalizia sentensi yangu, nikahisi maumivu makali kwenye kifua changu, upande wa kushoto kwenye moyo mpaka nikalazimika kujishika sehemu hiyo na kuinama chini.
Nilitamani kila kitu kiwe ndoto lakini haikuwa hivyo, ghafla nikaanza kuhisi kizunguzungu kikali, nikaanguka chini kama mzigo, puuh! Kwa mbali nikasikia hatua za Jimmy akiondoka kisha akabamiza geti kwa nguvu.
Sikuelewa tena kilichoendelea mpaka baadaye nilipozinduka na kujikuta nimelazwa chini ya mti, watu wawili wakinipepea.Nilipozinduka tu, nilihisi maumivu makali ya kichwa na sehemu nyingine za mwili wangu, nikajaribu kuinuka lakini nikashindwa, nikaendelea kulala huku nikijaribu kukumbuka kilichonitokea.
Nikakumbuka kila kitu, hali iliyonifanya nilie kwa uchungu sana, wale watu wakawa wanajaribu kunibembeleza na kunisihi ninyamaze kwani nitajiumiza zaidi.
Baada ya kukaa kwa muda mrefu, baadaye nilipata nguvu za kuinuka, nikakaa kitako na kuanza kujifuta vumbi usoni. Bado nilikuwa jirani na nyumbani kwa Jimmy kwani niliweza kuiona nyumba yake.
“Kwani kumetokea nini dada?” mmoja kati ya wale watu wawili aliniuliza lakini nilishindwa kumjibu zaidi ya kuendelea kutokwa na machozi. Kitu pekee nilichowaomba ni kuniitia Bajaj au bodaboda. Nashukuru kwamba nilikuwa na fedha zangu za akiba kwenye mfuko wa kaptura niliyokuwa nimeivaa ndani.
Nawashukuru sana watu wale kwani walinisaidia kuniinua pale chini, mmoja akanipa kitambaa chake nijifute vumbi usoni, wakanisaidia kutembea mpaka mtaa wa pili kulipokuwa na kituo cha Bajaj na bodaboda.
Nikajikokota na kupanda kwenye Bajaj na kumuelekeza dereva sehemu ya kunipeleka, nikawashukuru sana wale wasamaria wema kisha safari ya kurudi nyumbani ikaanza. Njia nzima niliendelea kulia huku nikilitaja jina la Jimmy.
Nilipofika nyumbani, nilishuka na kumlipa dereva wa Bajaj fedha zake, kwa taabu nikajikongoja mpaka ndani. Kwa bahati nzuri wadogo zangu walikuwa wakicheza nyuma ya nyumba hivyo hawakuniona wakati nikiingia, nikapitiliza bafuni ambapo nilijimwagia maji kuondoa vumbi mwilini mwangu kisha nikaenda kujifungia chumbani kwangu.
“Jimmy! Nisamehe mpenzi wangu kama nimekukosea, bado nakupenda mwenzio, tafadhali usinitese Jimmy! Ziko wapi ahadi zako?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Japokuwa nilikuwa na usingizi mkali uliosababishwa na kukesha hospitalini nikimuuguza mama, sikuweza kulala hata kidogo, nikawa najigalagaza kitandani, nikiwa nimeukumbatia mto wangu, machozi yakinitoka kiasi cha kulowanisha mto na shuka nililokuwa nimetandika.
Nikiwa naendelea kuomboleza, ghafla nilianza kuhisi hali ya ajabu, mdomo ulijaa mate na muda mfupi baadaye, nikahisiki chefuchefu kikali. Nilijikaza na kutaka kukimbilia bafuni lakini kabla sijafika, nilianza kutapika mfululizo mpaka nikaishiwa nguvu.
“Dada una nini? Mbona unatapika?”
“Nahisi ni homa, nisaidie kunipeleka bafuni nikanawe,” nilimwambia mdogo wangu aliyekuwa wa kwanza kugundua kwamba nimetapika sana koridoni, akaniinua na kunisaidia kutembea mpaka bafuni, nilipoingia nilianza tena kutapika, namshukuru mdogo wangu alinisaidia sana.
Akarudi kwenye korido na kusafisha sehemu zote nilizokuwa nimechafua kisha akarudi bafuni ambapo alinisaidia kujisafisha kisha akanirudisha chumbani. Nikajipumzisha kitandani huku maswali mengi yakianza kupita ndani ya kichwa changu.
Nilijiuliza ni kitu gani kilichosababisha nitapike vile? Hata kama ingekuwa ni homa, huwa nikiugua homa sitapiki kiasi hicho, nikaanza kuwa na wasiwasi ndani ya nafsi yangu.
Hata hivyo, mawazo hayo hayakudumu sana kichwani mwangu, nikaanza kulikumbuka tukio alilonifanyia Jimmy muda mfupi uliopita, nilishindwa kujizuia, nikaanza tena kulia kwa uchungu.
Nilikuja kuzinduliwa kutoka kwenye dimbwi la mawazo machungu na sauti za watu waliokuwa wanaongea nje ya nyumba yetu. Bila hata kuuliza nilijua mama amerudi kwani niliwasikia wadogo zangu wakimsalimia kwa uchangamfu.
Nikawa na uhakika kuwa tayari mama alisharuhusiwa kutoka hospitalini hasa baada ya kurejewa na fahamu zake usiku uliopita. Japokuwa nilikuwa na furaha kwa mama kurudi nyumbani lakini nilikuwa na wakati mgumu sana wa kuzificha hisia zangu.
Kwa jinsi mama alivyokuwa ananielewa, niliamini atashtukia mchezo mzima haraka sana, jambo ambalo sikuwa tayari kuona linatokea. Nikajikaza na kuamka, nikaenda kumsalimia mama ambaye aliponiona tu, swali la kwanza aliniuliza kwa nini macho yangu yalikuwa mekundu sana.
“Usingizi mama, si unajua usiku sikulala na sasa hivi nashindwa kupata usingizi vizuri kwa sababu ya joto,” nilidanganya, mdogo wangu akakazia kwa kumwambia mama kwamba pia nilikuwa natapika.
“Unatapika?”
“Mmh! Nahisi mbu wamening’ata kule hospitalini, inaweza kuwa ni malaria,” nilizidi kudanganya, mama akashauri kuwa ni bora nikapime haraka na kumeza dawa kabla hali haijawa mbaya. Akaingia ndani kwa kujikongoja mpaka sebuleni ambapo alikaa wakati mimi na kaka tulisaidiana kuingiza vitu walivyotoka navyo hospitali.
Tulikaa na mama kwa muda pale sebuleni, akawa anatushukuru kwa jinsi tulivyomuuguza kwa upendo. Baada ya muda, alituomba akapumzike kwani bado mwili wake haukuwa na nguvu, tukamsaidia kumpeleka mpaka chumbani kwake ambapo aliendelea kupumzika.
Kwa kuwa nilikuwa naujua vizuri ukali wa mama, ile simu aliyonipokonya, niliwahi kuirudisha palepale alipokuwa ameificha huku nikifuta meseji zote nilizokuwa namtumia Jimmy ili asije akagundua kuwa nilikaidia amri yake na kuchukua tena simu ile.
Nashukuru Mungu hilo lilifanikiwa vizuri, nikarudi chumbani kwangu ambako nilijifungia na kuendelea kuomboleza vitendo nilivyofanyiwa na Jimmy. Kilichozidi kunipa wasiwasi, ile hali ya kujihisi kichefuchefu iliendelea kunirudia mara kwa mara.
“Nimenasa ujauzito nini? Lakini haiwezekani, yaani kufanya mara mbili tu ndiyo nibebe mimba?” niliwaza na kujipa moyo mwenyewe, siku ya kwanza ikapita huku bado nikiwa na huzuni kubwa ndani ya moyo wangu.
Wiki moja baadaye, hali yangu ilizidi kuwa mbaya, licha ya kutumia dozi ya malaria, bado kichefuchefu hakikuisha, safari hii kikawa kinaambatana na homa za hapa na pale huku pia nikianza kuchagua aina za vyakula. Nilipendelea kuweka ndimu kwenye kila kitu, mpaka kwenye chai.
Kwa kuwa nilikuwa nakula peke yangu chumbani kwa kisingizio cha kwamba naumwa, hakuna aliyeshtukia haraka mchezo huo. Siku nyingine, nilikuwa nikimwaga chakula chote nilichoandaliwa kupitia dirishani kwani nilipoteza kabisa hamu ya kula baadhi ya vyakula na kupendelea kula maembe mabichi na ndimu.
Hofu kwamba nimenasa ujauzito ikazidi kuniingia kwani nilikumbuka jinsi mwalimu wa somo la Bailojia shuleni alivyotufundisha kuhusu dalili za mama mjamzito.
Baada ya kukaa kwa hofu kwa siku kadhaa, niliamua kujitoa mhanga. Kwa kuwa tulikuwa tumefundishwa pia na mwalimu namna ya kumpima mama mjamzito bila kumpeleka hospitali, nilipata wazo nililoona linafaa.
Nikatoka na kwenda kwenye duka la madawa lililokuwa jirani na pale nyumbani kwetu, nikaomba kipimo cha mimba au Pregnancy Test kama kilivyokuwa kikiitwa kitaalamu. Nikarudi chumbani kwangu na kuanza kufuata maelekezo ya namna ya kukitumia kipimo hicho.
Nilijisaidia haja ndogo kwenye kikopo, nikakifungua kile kipimo na kukitumbukiza kwenye kopo lenye kiwango kidogo cha haja ndogo kisha nikakaa na kusubiri kwa dakika kadhaa. Nilipoenda kukiangalia baada ya dakika kumi kupita, moyo wangu ulilipuka paah!
Mistari miwili ya rangi nyekundu ilikuwa imejitokea upande wa juu wa kipimo hicho, kuonesha kwamba tayari nilikuwa nimenasa ujauzito. Kwa mahesabu ya harakaharaka, nilijua ujauzito huo utakuwa na wiki mbili.
“Mungu wangu! Mimbaaa… lazima ni ya Jimmy tu, sasa itakuwaje?” nilisema huku nikikaa chini na kujishika mikono kichwani. Ilikuwa ni habari mbaya kupindukia kwangu.
Ukiachilia mbali umri wangu mdogo ambao haukuniruhusu kubeba ujauzito, pia mwanaume aliyekuwa amenipachika ujauzito huo, Jimmy alinikataa vibaya na kuendelea kufanya ufuska na wanawake wengine, wakubwa kwa wadogo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nitakuwa mgeni wa nani mimi? Nitamwambia nini mama yangu? Watu watanionaje hapa mtaani? Fedha za ada zikipatikana shuleni nako itakuwaje?” nilijiuliza maswali mengi yaliyofanya nijihisi kama nimemwagiwa maji ya moto kichwani. Nilishindwa kujizuia, nikaanza kulia kwa sauti kama mtu aliyepokea taarifa za msiba.
Mara nikasikia mlango wa chumba changu ukigongwa huku sauti ya mama ikisikika kutokea nje.
“Eunice! Eunice fungua mlango,” mama alisema huku akigonga. Harakaharaka nikakificha kile kipimo cha ujauzito pamoja na kopo lililokuwa na haja ndogo, nikajifuta machozi na kwenda kufungua mlango, mama akaingia.
“Vipi unaendeleaje?” mama aliniuliza huku akisogea na kukaa kwenye kitanda changu.
“Naendelea vizuri mama,” nilimjibu huku nikijaribu kuvaa tabasamu hafifu kupoteza ushahidi kwamba nilikuwa nalia. Alipokaa kitandani, alianza kwa kunishukuru tena kwa jinsi nilivyosimama kama mama wa familia kwa kipindi chote alichokuwa anaumwa.
Akaniambia amegundua kuwa hata akifa leo au kesho, ninaweza kuwaongoza vizuri wadogo zangu. Licha ya sifa alizokuwa ananimwagia, akili yangu ilikuwa mbali mno, nikiwaza juu ya janga nililokuwa nimelichuma na namna ya kulitatua.
“Nimepata mkopo kwa ajili ya kuwalipia ada ya shule lakini itabidi mhame kule mlikokuwa mnasoma kwa sababu ada yake ni kubwa sana, mtahamia hapa karibu na mtakuwa mnasoma shule ya kutwa,” mama aliniambia.
Badala ya kuifurahia taarifa hiyo, nilijihisi kuishiwa nguvu kabisa lakini nilijikaza ili mama asigundue chochote. Tulizungumza mambo mengi, kikubwa mama aliendelea kuomba radhi kwa jinsi alivyoshindwa kuiongoza familia yetu tangu kifo cha baba.
“Wewe ni mwanamke kama mimi, kwa kuwa unakuwa mkubwa, utayaona mwanangu, naomba sana unisamehe na uniombee pia msamaha kwa kaka yako na wadogo zako, najihisi mwenye hatia sana kwa kukubali kurubunika,” mama alisema huku akiwa anatokwa na machozi.
“Kurubunika? Kivipi? Ni kipi hasa kinachofanya uyajutie maisha yako kiasi hiki?”
“Nilirubuniwa nikarubunika, wanaume ni viumbe hatari sana. Najuta sana mwanangu, mimi ndiyo chanzo cha familia hii kuyumba, tazama sasa mnavyopata shida, hii yote ni kwa sababu ya ujinga wangu,” mama alisema huku akiendelea kulia. Kiukweli nilibaki njia panda na bado nilikuwa sielewi maana ya nahau na mafumbo aliyonipa.
Mama aliinuka huku akiendelea kulia na kuondoka kurudi chumbani kwake, akaniacha na mawazo lukuki. Nilijaribu kuunganisha matukio kuhusu mwenendo wa mama na kilichokuwa kinamsumbua lakini bado sikupata picha ya alichokuwa anamaanisha.
Mawazo juu ya mama yalipotea haraka kichwani mwangu kama moshi upoteleavyo angani, nikaanza kufikiria janga lililokuwa linanikabili. Taarifa aliyonipa mama kwamba tuanze kujiandaa kwenda shule, ilizidi kunitia hofu ndani ya moyo wangu kwani nilijua shule nyingi zina utaratibu wa kuwapima wanafunzi wa kike ujauzito.
Wazo pekee ambalo niliona linafaa kwa wakati huo ilikuwa ni kumfuata Jimmy na kumueleza ukweli kwamba amenipa ujauzito kabla siri hiyo haijavuja. Nikapanga kwamba nikifika nyumbani kwake, nitaomba kuzungumza naye kwa heshima na atakapokubali nitamueleza kwa upole kwamba licha ya kunitoa usichana wangu, pia alikuwa amenipa ujauzito.
Niliamini Jimmy akisikia nina ujauzito wake, atafurahi na kuamua kurudiana na mimi kwani mara kwa mara kabla sijampa mwili wangu, alikuwa akiniambia kwamba anapenda siku moja nimzalie watoto wazuri kama mimi.
Katika kumbukumbu zangu, ilionesha kwamba Jimmy hakutamka maneno hayo mara moja, mara kwa mara alikuwa akinisifia kwamba mimi ni mzuri sana na akinioa, atapenda nimzalie watoto wazuri, jambo litakalomfanya awe na furaha siku zote za maisha yake.
Niwaeleze kwa kifupi kwamba licha ya umri wangu mdogo, mwenzenu Mungu amenijalia uzuri wa kipekee kwani kiukweli mimi ni mzuri sana. Nimejaliwa mvuto wa aina yake kuanzia usoni mpaka miguuni, ngozi yangu yenye rangi ya ung’avu wa asili, macho yangu mazuri na kifua changu kilichojaa vizuri ni sifa zinazonifanya niwe na mvuto wa kipekee.
Yote tisa, kumi ni shepu ya kipekee niliyojaliwa. Mwili wangu umejengeka kikekike hasa na kukaribia kufanana na namba nane, nadhani nimerithi kutoka kwa mama yangu ambaye licha ya kuwa mtu mzima, bado ana mvuto sana.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa mtu yeyote kugundua uzuri wangu kwa haraka kwani nilifundishwa tangu nikiwa mdogo kuvaa mavazi ya staha na kujisitiri vizuri. Wengi waliishia kuisifia sura yangu tu na mara kwa mara nilipopita kwenye mkusanyiko wa wavulana, walikuwa wakinikonyeza na kunionesha ishara ambazo sikuwa nazifurahia.
Hata hivyo, tofauti na wasichana wengi wazuri waliokuwa wanautumia vibaya urembo waliojaliwa kwa kufanya mambo yasiyofaa mbele za jamii, mimi kamwe sikuutumia vibaya urembo wangu na ndiyo maana licha ya kukumbana na vikwazo vingi, nilifanikiwa kuvishinda vyote na Jimmy ndiyo alikuwa mwanaume wangu wa kwanza maishani.
“Akiukubali huu ujauzito wangu, nipo tayari hata kuacha shule, nampenda sana Jimmy na natamani niwe mke wake wa ndoa,”niliwaza wakati nikitoka nyumbani kimyakimya bila mtu yeyote kujua ninakokwenda. Nilienda mpaka kwenye kituo cha bodaboda na Bajaj, nikapanda moja na kumuelekeza dereva wapi pa kunipeleka.
Kwa kuwa bado nilikuwa na fedha za kutosha nilizokuwa nahongwa na Jimmy, matumizi madogomadogo kama nauli hayakunipiga chenga. Baada ya kukatiza mitaa mingi, hatimaye tulifika nyumbani kwa Jimmy, nikamlipa dereva wa bodaboda, akaondoka na kuniacha pale nje nikitafakari namna ya kuingia ndani kwa Jimmy.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Eeeh! Mungu nisaidie Jimmy aukubali huu ujauzito wake, nampenda sana na nataka kuanzisha naye familia,” nilisema huku nikiwa nimelishika tumbo langu kwa mikono miwili, machozi yakitiririka na kuulowanisha uso wangu.
Naendelea kusema sijui zilikuwa ni akili za kitoto, ushamba wa mapenzi au kitu gani kwani mwenzenu nilikuwa nimeshamsamehe Jimmy kwa yote yaliyotokea na nilikuwa na matumaini makubwa kwamba ataurudisha moyo wake nyuma na kunionea huruma. Nilitokea kumpenda sana kiasi kwamba niliamini bila yeye, siwezi kuishi wala kufanya chochote!
Taratibu nikaanza kusogea kwenye geti la kuingilia nyumbani kwa Jimmy huku nikiwa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu, nikajivuta mpaka nilipolifikia, nikabonyeza kitufe cha kengele kilichokuwa ukutani.
Nilipoona kimya, niligonga geti kwa mikono yangu, kwa mbali nikaanza kusikia hatua za mtu akitembea kuja getini, mapigo ya moyo yakazidi kunienda kasi, akilini nikapanga kwamba Jimmy akifungua tu mlango, nitampigia magoti kwa heshima na kumuomba anisikilize shida yangu.
Vishindo vya mtu aliyekuwa akitembea kuja getini viliongezeka, mara nikasikia mtu akifungua kitasa kwa funguo kisha geti likafunguliwa. Tofauti na nilivyotegemea, nilikutana na sura ya mwanamke ambaye sikuwahi kumuona, akiwa amejifunga taulo la Jimmy kifuani.
Uso ukanishuka kwa haya kwani tayari nilishajiandaa kukutana na Jimmy na nilishavaa uso ambao niliamini akiniona atanionea huruma.
“Nikusaidie nini?” sauti ya nyodo kutoka kwa mwanamke huyo ambaye kwa kumkadiria alikuwa na umri wa miaka kati ya ishirini na sita hadi thelathini ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye dimbwi la mawazo. Nilishindwa cha kujibu, nikashangaa machozi yakinibubujika kama chemchemi ya maji.
“Mbona hujibu? Nakuuliza nikusaidie nini? Au umeleta taarifa za msiba?” yule mwanamke alizidi kunisanifu huku akiwa ameshika kiuno kwa dharau. Akili ya haraka ilinijia kwamba kulia hakuwezi kunisaidia chochote kwa wakati ule, ikabidi nijikaze kisabuni.
“Naomba kuonana na Jimmy tafadhali,” nilisema kwa sauti ya upole huku nikijifuta machozi kwa kiganja cha mkono wangu. Japokuwa nilijikaza lakini ukweli ni kwamba niliumia sana ndani ya moyo wangu.
Jimmy! Mwanaume niliyetokea kumpenda kwa moyo wangu wote na kumruhusu kuwa wa kwanza kuujua mwili wangu aligeuka na kuwa mwiba mkali kwenye moyo wangu.
“Jimmy hayupo, kama una maagizo yoyote niachie mimi nitamfikishia,” alijibu yule dada huku akinipindishia mdomo na kuendelea kunioneshea dharau ya hali ya juu. Sikufurahishwa na dharau zake hata kidogo kwani tayari nilikuwa na mzigo mzito ndani ya kichwa changu.
“Dada tafadhali, sina shida ya kupigizana kelele na wewe, najua Jimmy yupo ndani. Naomba kuonana naye,” nilisema kwa sauti ya ukali kidogo kwani nilihisi nikiendelea kumchekea yule mwanamke hawezi kuniruhusu kuonana na Jimmy.
“Nimeshakwambia hayupo, wewe vipi? Kama unataka msaada hapa siyo nyumba ya kusaidia yatima na wasiojiweza,” alisema yule dada kwa nyodo huku akitaka kubamiza geti na kulifunga, nikamuwahi na kulishika geti kwa nguvu, tukaanza kusukumana huku tukiendelea kurushiana maneno makali.
Kwa jinsi nilivyokuwa na hasira na maisha, nilimsukuma kwa nguvu, geti likamgonga usoni na kumfanya aanguke chini, akapiga kelele zilizomshtua Jimmy aliyekuwa ndani. Wakati huo tayari nilishaingia ndani ya geti, nikawa namsubiri yule mwanamke ainuke ili nimshikishe adabu.
Sijui niliupata wapi ujasiri huo kwani katika historia ya maisha yangu mimi siyo mgomvi kabisa na sijawahi kugombana na mtu. Japokuwa alikuwa amenizidi sana umri, nilipanga kumalizia hasira zangu zote kwake. Ni kama alijua kilichokuwa ndani ya akili yangu kwani alipoinuka, alikimbilia ndani.
Wakati anapandisha ngazi, Jimmy alitoka ndani kwa kasi, na yeye akiwa amejifunga taulo tu. Akapigwa na butwaa kumuona mwanamke wake amechafuka mwili mzima kwa vumbi, huku mimi nikiwa nimesimama jirani na geti, nikihema kwa nguvu.
Alimuamuru mwanamke wake kuingia ndani huku akimpa pole, akashuka kwenye ngazi na kuanza kutembea kwa kasi kuja pale nilipokuwa nimesimama. Japokuwa alionesha wazi kwamba alikuwa anakuja kisharishari, wala sikutetereka, nikasimama kwa ukakamavu.
Alinisogelea mpaka mwilini, akaniuliza kwa ukali: “Kwa nini unakuja kunifanyia fujo nyumbani kwangu?” Sikumjibu kitu kwani kiukweli wala sikuwa nimekuja kufanya fujo bali mwanamke wake ndiye aliyeanza kunikorofisha na kunitolea maneno ya kuudhi.
Jimmy alirudia swali lake lakini sikumjibu kitu, nikahisi donge likinikaba kooni na kunifanya nianze kutokwa na machozi kwa wingi. Nadhani hali ile ilimfanya Jimmy anionee huruma kwani alishusha pumzi ndefu na kugeuka nyuma kuangalia kama yule mwanamke alikuwa akitutazama.
Zile hasira zake zikayeyuka kama theluji iyeyukavyo juani. Kwa sauti ya chini akaniuliza kilichonipeleka pale nyumbani kwake.
“Nina ujauzito wako Jimmy,” nilisema huku nikiendelea kulia kwa uchungu.
“Unasemaaa… ujauzito? Eunice… una wazimu au umechanganyikiwa?” mshtuko alioupata Jimmy ulijionesha waziwazi kwenye uso wake, akawa anababaika kama mtu anayeng’atwa na siafu, mara ajishike kichwani, mara kifuani na kiunoni! Utulivu ulimuisha kabisa, akawa ananitazama kama asiyeamini nilichomwambia.
“Naomba uondoke nyumbani kwangu haraka! Unataka kuniletea matatizo si ndiyo? Ondoka haraka kabla sijakufanya kitu kibaya malaya mkubwa wewe.”
“Sasa unanifukuza niende wapi Jimmy? Nimeshakwambia nina ujauzito wako, na hakuna mwanaume anayeujua mwili wangu zaidi yako, ningekuwa malaya usingenikuta na usichana wangu,” nilisema huku nikiendelea kulia lakini haikusaidia kitu, Jimmy alinikokota mpaka nje, akanisukuma kwa nguvu kisha akabamiza geti na kulifunga kwa funguo.
Nilitamani kila kitu kiwe ndoto lakini haikuwa hivyo. Sikuamini hata kidogo kama Jimmy anaweza kugeuka na kuwa mnyama kiasi hicho. Nilibaki nimelala palepale nilipoangukia huku nikilia kwa uchungu kuliko kawaida.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baadaye nilipopata nguvu, niliinuka na kuondoka eneo hilo, nikaenda mpaka kwenye kituo cha Bajaj na bodaboda huku nikijikaza mtu yeyote asijue kilichokuwa kinaendelea. Nikapanda bodaboda iliyonipeleka mpaka nyumbani. Nikashuka na kuanza kutembea kuelekea nyumbani.
“Mbona umechafuka hivyo? Halafu inaonesha kama ulikuwa unalia, kuna tatizo?” mama alinidaka juujuu kwa maswali ambayo nilishindwa kuyajibu, ikabidi nimdanganye kwamba nilianguka ghafla baada ya kuhisi kizunguzungu wakati nikitoka kufuata madaftari kwa rafiki yangu Nancy aliyekuwa anaishi mtaa wa pili.
Mama alitingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana na mimi ingawa bado alionesha kuwa na wasiwasi mkubwa juu ya maelezo yangu. Harakaharaka nikaingia chumbani kwangu na kuvua nguo zilizochafuka, nikaenda bafuni kuoga kisha nikarudi na kujitupa kitandani, nikaendelea kulia kwa uchungu huku nikiwa sijui nini hatima ya maisha yangu na kiumbe kilichokuwa ndani ya tumbo langu.
Sikutoka nje kabisa, hata chakula siku hiyo nilikataa kwa kisingizio kwamba naumwa. Ilipofika majira ya saa nne za usiku, simu yangu ambayo sasa mama alishanirudishia na kunipa uhuru wa kuitumia, iliita mfululizo. Nikainuka kichovu na kwenda kuichukua.
Sikuamini macho yangu kugundua kuwa aliyekuwa ananipigia ni Jimmy. Mapigo ya moyo wangu yakawa yanaenda mbio, nikawa nahisi kama nipo ndotoni. Nikajikaza na kuipokea, kweli alikuwa ni Jimmy.
“Haloo Eunice!” Jimmy aliongea kwa uchangamfu baada ya kupokea simu.
Kwa jinsi alivyokuwa amenichangamkia, alinikumbusha siku za mwanzo za uhusiano wetu, ile hofu iliyokuwa imetanda kwenye moyo wangu ikayeyuka kama theluji iyeyukavyo juani.
Alianza kwa kuniomba radhi akisema anaijutia nafsi yake kwa yote aliyonifanyia. Akaniambia anahisi alikuwa amerogwa kwani alikuwa hajielewi kabisa kiasi cha kugeuka mkatili na mtesaji wa nafsi yangu.
Hata sijui nini kilitokea kwani wakati Jimmy akiendelea kuniongelesha kwenye simu kwa sauti yake ya kipole, machozi yalianza kunitoka kwa wingi, nikapiga magoti na kuinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu kwa muujiza uliokuwa unaendelea.
Nilifurahi sana kwa Jimmy kuyaelewa makosa yake mapema na kuamua kujirudi kwangu, machozi yakaendelea kunitoka kwa wingi wakati Jimmy akiendelea kunipamba kwa maneno mazuri na kuniomba nimsamehe kwa yote yaliyotokea.
Aliponiuliza kama nimeupokea msamaha wake, harakaharaka nilimjibu kwamba nimeupokea na nimekubali kumsamehe kwa moyo mkunjufu. Hata sielewi kichwa changu kilikuwa kinawaza nini kwani kitendo kile cha Jimmy kunipigia simu kilinifanya nisahau yote aliyonifanyia na kumsamehe kutoka ndani kabisa ya moyo wangu.
“Kwa hiyo kesho tunaweza kuonana?”
“Saa ngapi?”
“Asubuhi nitakuja kukuchukua nyumbani kwenu,” alisema Jimmy kwa sauti ya mahaba, nikakubali harakaharaka huku tabasamu hafifu likichanua usoni kwangu. akarudia kuniomba msamaha kisha akakata simu, siwezi kueleza jinsi nilivyojisikia furaha ndani ya moyo wangu, nilikuwa ni kama nimefufuka kutoka katika wafu.
Niliinuka kitandani na kuanza kurukaruka chumbani kwangu kama mwendawazimu, nikashusha pumzi ndefu na kurudi tena kitandani, nikaukumbatia mto wangu huku hisia juu ya penzi la Jimmy zikirudi kwa kasi ndani ya mtima wangu.
Nilitamani saa ziende haraka ili nionane na Jimmy wangu. Hata ile hamu ya kula iliyokuwa imepotea kwa kipindi kirefu, ilirudi na kunifanya nitoke na kwenda jikoni kutafuta chochote cha kutia mdomoni, nilipopata nikarudi chumbani na kuanza kula huku nikisikiliza muziki kutoka kwenye simu yangu mpaka usingizi uliponipitia.
Kesho yake asubuhi niliwahi kuamka na kuanza kujiandaa, nikajipamba vizuri na kujipulizia marashi mazuri ili kumfurahisha Jimmy atakaponiona, nikachagua gauni zuri lililokuwa linanikaa vizuri mwilini, nikawa najikagua kwenye kioo.
Kwa jinsi nilivyokuwa nimejipamba, ukichanganya na uzuri wa sura na umbo langu, nilipendeza si mchezo. Nikawa na uhakika kwamba Jimmy atakaponiona tena, atabadili mawazo yake na kuachana na wanawake zake wote ambao hakuna aliyekuwa ananifikia kwa uzuri hata mmoja.
Nilipomaliza kujiandaa, nilimtumia meseji Jimmy, akaniambia yupo njiani anakuja. Sikutaka mama au mtu yeyote ajue ninakokwenda, nikatoka kwa kujifichaficha na kupotelea mitaani bila mtu yeyote kuniona. Nilienda mpaka sehemu ile ambayo tulikuwa tukikutania na Jimmy. Muda mfupi baadaye, nikamuona akija akiwa ndani ya gari la kifahari, huku uso wake ukiwa umejawa na tabasamu.
Alisimamisha gari na kushuka, akanifuata na kunisabahi kwa uchangamfu, akanishika mkono na kuniongoza hadi kwenye gari, akanifungulia mlango na kunisaidia kupanda. Nilijihisi kama mtoto wa mfalme kwa jinsi alivyokuwa ananinyenyekea.
Na yeye aliingia ndani ya gari lakini hakuliwasha haraka, tukawa tunazungumza mambo mawili matatu ambapo alirudia tena kuniomba msamaha na kuniambia ameamua kufungua ukurasa mpya wa mapenzi kwa sababu amegundua kuwa nampenda kwa dhati. Muda wote nilijiinamia kwa aibu za kikekike.
Akawasha gari kisha tukaondoka eneo lile. Tofauti na nilivyotegemea, hatukwenda nyumbani kwake kama ilivyokuwa kawaida, akaendesha gari mpaka Manzese, tulipofika kituo kiitwacho Bakhresa, alipaki gari pembeni ya barabara kisha akatoa simu yake na kuanza kuzungumza na mtu wa upande wa pili.
Kwa jinsi mazungumzo yao yalivyokuwa, ni kama Jimmy alikuwa akiulizia ramani ya mahali tulikokuwa tunakwenda, baada ya kueleweshwa vizuri, aliwasha gari tena kisha tukaiacha barabara ya lami na kuingia ndanindani. Tuliendelea kukata mitaa ya Manzese mpaka tulipo fika kwenye baa moja ya uswahilini.
“Kuna mtu namsubiri, njoo tunywe japo soda hapa baa,” alisema Jimmy wakati akipaki gari vizuri, tukashuka na kwenda hadi kwenye baa hiyo, mimi nikaagiza soda wakati Jimmy aliagiza maji makubwa ya Kilimanjaro, tukaanza kunywa taratibu huku Jimmy akionesha kuwa bize na simu yake. Sikujali sana hasa baada ya kuniambia kuwa kuna mtu anamsubiri.
“Samahani naomba nikusumbue kidogo mpenzi wangu,” Jimmy aliniambia huku akitoa noti ya shilingi elfu kumi, akaniambia anaomba nikamnunulie vocha kwenye duka lililokuwa jirani. Nikainuka na kwenda mpaka dukani, baada ya muda mfupi nikarudi na kumpa vocha yake, tukaendelea kunywa vinywaji vyetu.
Baada ya dakika chache, mwanaume mmoja mrefu wastani, mwenye mvi chache kichwani alifika pale tulipokuwa tumekaa, akasalimiana na Jimmy kwa uchangamfu kama watu waliokuwa wanafahamiana tangu zamani, akanisabahi na mimi kisha akakaa.
“Mtu mwenyewe ndiyo huyu?” aliuliza yule mtu huku akinitazama vizuri, Jimmy akatingisha kichwa kama ishara ya kumkubalia. Jimmy akanipa ishara kwamba niongozane naye, nilikubali kwani sikutaka kumuudhi Jimmy ingawa sikuelewa tunaenda wapi. Niliposimama, nilihisi kichwa changu kikiwa kizito sana kama mtu niliyekunywa pombe.
“Kwani tunaenda wapi?”
“Jimmy hajakwambia?” aliniuliza yule mwanaume huku tukizidi kukata vichochoro, tukatokezea kwenye jengo moja kuukuu ambalo kwa ndani lilikuwa na vifaa kama hospitali.
Wakati naingia, nilihisi kichwa kinazidi kuwa kizito, yule mwanaume akanishika mkono na kuniingiza mpaka chumba cha ndani huku nikisikia usingizi wa ajabu.
“Hebu lala hapa,” alisema yule mtu huku akivaa koti kama la kidaktari na kuanza kukusanya vifaa vingi vya chuma, mikasi, pamba pamoja na madawa ambayo sikuyaelewa.
Nilibaki natetemeka huku usingizi nao ukinizidi kiasi cha kuanza kupepesuka, nilitamani kumuuliza yule mtu ambaye niligundua kuwa ni daktari kinachoendelea lakini mdomo ulikuwa mzito. Kutokana na usingizi mzito uliokuwa unanielemea, nilijilaza mwenyewe kwenye kile kitanda.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikiwa katika hali ya kuleweshwa na usingizi, huku nikihisi kichwa kuwa kizito kuliko kawaida, nilijitahidi kujikaza nisilale kwani bado sikujua pale ni wapi na Jimmy na yule daktari walikuwa na mpango gani na mimi. Pia nilijishangaa kwa nini hali yangu imebadilika ghafla kiasi cha kuhisi usingizi mzito kiasi hicho.
“Au ni ile soda niliyokunywa? Lakini tangu lini soda ikalewesha? Au… au…” nilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. Sikutaka kabisa kumhisi vibaya Jimmy kwamba anaweza kuwa amenichanganyia kitu kwenye soda yangu.
Akili yangu ilikataa kabisa, nikawa nahisi labda ni hali ya kawaida inayosababishwa na ujauzito wangu mchanga. Wakati nikiendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, yule daktari naye aliendelea kukusanya vyuma vingi, mikasi, sindano, pamba pamoja na madawa mengi.
“Jiandae nikuchome sindano ya nusu kaputi, bila hivyo utasikia maumivu makali sana,” alisema yule daktari huku akivuta dawa kwa kutumia bomba la sindano. Japokuwa nilikuwa na hali mbaya, sikukubali kirahisi kuchomwa sindano nikitaka kwanza anipe maelezo ya kutosha kwani nilihisi kuna jambo la hatari linalotaka kunitokea.
“Punguza usumbufu basi, mbona maswali yamekuwa mengi? Au hutaki tukitoe hicho kimimba chako?” daktari aling’aka baada ya kuona namuuliza maswali mengi.
“Whaaat?” (Niniiii?) niliuliza kwa mshtuko nikiwa ni kama siamini nilichokisikia, hata sijui nilipata wapi nguvu kwani niliinuka kwa kasi na kusimama huku nikiyumbayumba, mapigo ya moyo yakawa yananienda kasi kuliko kawaida. Ni hapo ndipo nilipogundua mchezo mzima uliokuwa unataka kuendelea. Kumbe Jimmy alinileta pale kwa lengo la kuutoa ujauzito wangu! Sikutaka kuamini.
Yule daktari naye alibaki amepigwa na butwaa kwani inavyoonekana, alikuwa hajui kama sina taarifa ya kinachotaka kutokea. Kwa jinsi nyumba hiyo ilivyokuwa, nilijua nikijilegeza anaweza kunichoma sindano ya usingizi kwa nguvu kisha akaendelea na kazi yake, jambo ambalo sikuwa tayari kuona linatokea.
Akili ya haraka niliyoipata ilikuwa ni kutoka mbio mpaka nje ambako ningeomba msaada kwa wasamaria wema. Kwa kasi ya ajabu, nikamzunguka yule daktari na kukimbilia mlangoni, nikaufungua mlango ambao tayari ulishafungwa kwa funguo, nikatoka mbio huku nikipepesuka.
Nashukuru Mungu yule daktari wala hakushughulika kunikimbiza kwani hata sijui ingekuwaje. Nikaendelea kutimua mbio mpaka nilipotoka nje ya jengo lile, sikutaka kurudi kule nilikomuacha Jimmy, nikaanza kukimbia ovyo mitaani huku nikiwa sielewi naenda wapi.
Nilikimbia huku nikipepesuka kama mlevi mpaka nilipotokea mtaa wa pili, kila mtu niliyekuwa napishana naye alikuwa ananishangaa lakini sikujali. Moja kwa moja nilienda mpaka kwenye duka moja, haraka nikaagiza maziwa fresh ya kwenye boksi pamoja na maji chupa kubwa.
Kwa bahati nzuri nilikuwa nimetembea na fedha za akiba. Nikaanza kugida maziwa kwa fujo kwani sasa nilishapata picha kwamba Jimmy aliniwekea kitu kwenye soda ili kunipumbaza akili. Nilimaliza boksi zima la maziwa, nikafungua na chupa ya maji na kuanza kunywa mfululizo.
Sikujali watu walioanza kukusanyika na kunishangaa, nilichotaka ilikuwa ni kukata ile sumu iliyonilewesha kwani nakumbuka tuliwahi kufundishwa shuleni namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa mtu aliyenywesha madawa ya kulevya au sumu.
Nilikunywa maji mengi mpaka nikahisi tumbo limejaa, nikakaa kwenye benchi lililokuwa nje ya duka hilo na kwa mbali nikaanza kuhisi ahueni kubwa. Niliendelea kukaa huku nikijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, nikapata picha kwamba kumbe hata Jimmy aliponipigia simu na kujifanya ananiomba msamaha, hakuwa amemaanisha bali alitaka tu kutimiza ushetani wake.
Nilijiapiza kuwa hata kama nimepata ujauzito bila kutarajia, tena nikiwa na umri mdogo na wakati huohuo aliyenipa huo ujauzito amenikana, kamwe sitajaribu kuutoa hata iweje. Nilikuwa nafahamu vizuri madhara ya kutoa mimba na hatari zake kwa hiyo sikuwa tayari kabisa.
Baada ya kukaa na kutulia kwa karibu nusu saa, nilipata akili za kuondoka kurudi nyumbani. Kwa kuwa nilikuwa nimeingia ndanindani sana, sikujua hata
ramani ya kutokea hivyo ikabidi niombe msaada wa kuelekezwa barabarani.
Kwa bahati nzuri, muuza duka alikubali kunisindikiza mpaka kituoni baada ya kuhisi sikuwa katika hali ya kawaida, tukakatiza kwenye mitaa mingi ya Manzese na hatimaye tukatokea kwenye Viwanja vya Bakhresa, angalau nikawa nimepata ramani.
Nilimshukuru sana yule muuza duka ingawa kila alipojaribu kunidadisi, sikuwa tayari kumueleza chochote. Nilipanda daladala na safari ya kurudi nyumbani ikaanza huku mawazo yakiendelea kunitesa kichwani kiasi cha kunifanya nionekane kama nimechanganyikiwa.
Kwa bahati nzuri nilifika salama nyumbani ingawa bado kichwa kilikuwa kikiniuma sana, nikapitiliza chumbani kwangu kulala. Nilipojitupa kitandani tu, nilipitiwa na usingizi mzito kuliko kawaida. Nilikuja kuzinduka jioni, nikaamka na kwenda kujimwagia maji, angalau nikawa najihisi ahueni kubwa tofauti na mwanzo.
Kwa kuwa hata kichwa changu kilikuwa kimetulia, tofauti na mwanzo ambapo nilikuwa nahisi maruweruwe, nilianza kutafakari kwa kina kilichotokea. Roho iliniuma sana kugundua kuwa Jimmy alikuwa na roho mbaya kiasi cha kufikia hatua ya kuhatarisha maisha yangu kwa maslahi yake binafsi.
Mwili ulinisisimka mno huku nikiwa siamini kama nimekivuka kizingiti kile, nikajishika tumboni huku nikiendelea kutafakari, machozi yakaanza kunitoka. Jimmy aligeuka na kuwa mwiba mkali kwenye maisha yangu mpaka nikawa najuta.
Lawama zangu nilizielekeza kwa mama kwa sababu kama angekuwa makini kusimamia vizuri fedha za marehemu baba, angeweza kutulipia ada bila matatizo kama zamani na huenda hata nisingekutana na Jimmy.
Nakumbuka vizuri kuwa nilikutana naye kwa mara ya kwanza nikiwa narudi shuleni baada ya kufukuzwa kutokana na kukosa ada. Nilikumbuka vizuri jinsi nilivyokuwa na mawazo siku hiyo mpaka nikajikuta naingia barabarani na kunusurika kugongwa na gari la Jimmy. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nililia sana kwa uchungu wakati kumbukumbu hizo zikipita ndani ya kichwa changu. Nilizinduka kutoka kwenye dimbwi la mawazo baada ya ujumbe mfupi kuingia kwenye simu yangu, nikaichukua na kujifuta machozi kwanza kisha nikaufungua.
Moyo wangu ulilipuka baada ya kugundua kuwa ulikuwa umetoka kwa Jimmy, akinilaumu sana na kutishia hata kuyakatisha maisha yangu endapo nitaendelea kukataa kuutoa ujauzito niliokuwa nao.
Nilirudia kuisoma meseji hiyo zaidi ya mara tatu nikiwa ni kama siamini. Jimmy alikuwa amenitolea maneno machafu na vitisho ambavyo vilinifanya nikose kabisa amani ndani ya nafsi yangu.
Nilitamani kwenda kumwambia mama ukweli wangu wote na kila kitu kilichokuwa kinaendelea kwani maji yalikuwa yamenifika shingoni hasa baada ya Jimmy kutishia kuwa nikiendelea kukataa kutoa mimba, yupo tayari hata kuniua. Hata hivyo, nilishindwa kwenda kumwambia mama kwa kuhofia ukali wake, nikabaki njia panda.
Nikiwa naendelea kuwaza huku nikiwa sijui nini hatima yangu, simu yangu ilianza kuita mfululizo, hata hivyo wala sikujishughulisha nayo kwani sikutaka kuzungumza na mtu yeyote kwa muda huo. Nilihitaji kukaa peke yangu, nilihisi kama dunia nzima inajua kilichonipata hali iliyonifanya nianze kusikia aibu hata kutoka nje.
Simu iliendelea kuita, nikawa sina ujanja zaidi ya kuichukua, nilipotazama namba ya mpigaji, mapigo ya moyo wangu yalilipuka baada ya kugundua kuwa ni Jimmy. Nilijishauri mara kadhaa kwamba nipokee au niache mpaka simu ikakata.
Sekunde chache baadaye, ikaanza tena kuita, nikapiga moyo konde na kuipokea ingawa sikutaka kuzungumza chochote. Nilipopokea tu, sauti ya ukali ya Jimmy ilisikika:
“Huwezi kunikwepa, nitafanya kila liwezekanalo kuhakikisha unakufa kama ukiendelea kukataa kuutoa huo ujauzito, unataka nikaozee jela? Lazima nikupoteze. Kabla sijakupoteza, usalama wako ni kukubali kwenda kufanya ‘abortion’, ukipuuzia utakiona cha moto.”
Nilihisi mwili wote ukiniisha nguvu, vitisho vya Jimmy sasa vilikuwa vimefikia mahali ambapo sikuwa na ujanja tena zaidi ya kuamua jambo moja; nimweleze mama ukweli ili suala hilo lishughulikiwe katika ngazi ya familia au nikubali kutimiza alichokuwa anakitaka ili yaishe.
Nikiwa bado naendelea kuwaza, simu ilianza tena kuita, mpigaji alikuwa ni yuleyule, Jimmy. Kutokana na hofu niliyokuwa nayo, niliamua kuizima kabisa, nikatoa betri na laini, kila kimoja nikakitupia upande wake. Nilijilaza kitandani huku mawazo yakiendelea kukisakama kichwa changu mithili ya mtu aliyebebeshwa chungu cha moto.
Niliendelea kuwaza mpaka nikajikuta nimepitiwa na usingizi bila kula chochote kama ilivyokuwa kawaida yangu tangu nilipopata ujauzito huo. Nililala kwa muda mrefu mpaka kesho yake.
Nilikuja kuzinduka alfajiri na mapema, nikaamka na kukaa kitandani, mawazo yakiendelea kukisumbua kichwa changu. Niliwaza mambo mengi sana mpaka nikajihisi kama naelekea kuchanganyikiwa. Nilijikongoja na kuamka, nikakusanya betri, laini na simu yangu kisha nikaviunganisha.
Nilipowasha simu tu, ujumbe mfupi wa maneno uliingia, nilipotazama namba ya mtumaji, mapigo ya moyo yalinilipuka baada ya kugundua kuwa ni Jimmy. Nilisita kuufungua ujumbe huo kwa muda, baadaye nikapiga moyo konde na kuufungua ujumbe huo.
Tofauti na nilivyotegemea kwamba nitakutana na ujumbe wa vitisho kama kawaida, nilikutana na meseji iliyonifanya nihisi kama nipo ndotoni. Ulikuwa ni ujumbe mrefu kutoka kwa Jimmy akiniambia kwamba amegundua kuwa anafanya makosa makubwa kunilazimisha kufanya jambo ambalo mwenyewe nilikuwa silitaki.
Akaandika kwamba anaomba sana nimsaidie kwani endapo itafahamika kwamba nina ujauzito na yeye ndiyo mhusika, nitasababisha afungwe jela miaka thelathini, jambo ambalo lingempoteza kabisa kimaisha. Akanibembeleza kwamba yupo tayari kurudiana na mimi na kunifanyia chochote ninachokitaka ilimradi tu nikubaliane na anachokitaka.
Nilishusha pumzi ndefu baada ya kumaliza kusoma ujumbe huo, nikarudia tena mara ya pili na ya tatu nikiwa ni kama siamini. Kutokana na kitendo alichonifanyia mara ya kwanza cha kujifanya amerudiana na mimi kumbe alikuwa anataka kunitoa ujauzito bila mwenyewe kujua, nilijikuta nikipoteza imani naye.
“Najua anataka nikubali tu kutoa huu ujauzito, wala hana mapenzi na mimi na huenda hilo likishatimia atarudia tabia yake kama zamani,” niliwaza nikiwa pale kitandani, nikavuta shuka na kujifunika tena, nikaendelea kuwaza kwani sikujua niamue nini.
Mara simu yangu ilianza kuita, nilipoangalia mpigaji alikuwa ni Jimmy, nikapokea na kunyamaza ili nimsikie alikuwa anataka kusema nini. Kwa sauti ya upole, iliyoonesha kwamba ndiyo kwanza amezinduka kutoka usingizini, Jimmy alinisalimu na bila hata kusubiri majibu, alianza kuongea akiyarudia maneno aliyoyaandika kwenye ile meseji.
Niweke wazi kuwa miongoni mwa vitu vilivyokuwa vinanifanya nishindwe kuwa na msimamo, ni nguvu ya ushawishi aliyokuwa nayo Jimmy. Yaani alijaliwa uwezo wa kipekee wa kumlainisha mwanamke kwa maneno matamu na kumfanya atimize alichokuwa anakitaka kwa urahisi.
Aliongea kwa upole utafikiri siyo yule aliyekuwa akinitishia maisha saa chache zilizopita, alinibembeleza kwa maneno matamu huku akinifanya nimuonee huruma yeye badala ya kujionea huruma mimi. Alizungumza kwa muda wa kama dakika mbili nikiwa sijamjibu neno hata moja, alipomaliza aliniuliza kama nimemuelewa na nimekubali.
Nilijikuta nikikubali kila kitu alichoniambia, nikamsikia akicheka kwa sauti ya chini kisha akaniambia atanipigia simu baadaye ili tupange vizuri nini cha kufanya kisha akakata simu. Japokuwa alishakata simu, nilibaki nimeishikilia ya kwangu sikioni kwa zaidi ya dakika nzima, nikashusha pumzi ndefu na kuamka.
Nikaenda mbele ya kioo changu kikubwa na kuanza kujitazama huku nikiwa nimejishika tumboni. Hata sijui kwa nini nilimkubalia Jimmy kwamba nipo tayari kwenda kuutoa ujauzito wangu kwani nilishajiwekea dhamira kwamba kamwe siwezi kufanya kitendo hicho cha hatari.
“Nisamehe mwanangu, nakupenda sana lakini nadhani muda wako ulikuwa bado haujafika, samahani sana,” nilisema huku machozi yakinitoka, nikiamini kiumbe kilichokuwa tumboni mwangu kilikuwa kikinisikia nilichokuwa nakisema.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Maneno matamu ya Jimmy yalinifanya niwe tayari kuuhatarisha uhai wangu eti kisa kumnusuru asije akafungwa miaka thelathini jela kwa kosa la kunipa mimi mwanafunzi ujauzito. Mpaka leo huwa nakijutia sana kitendo hicho kwani kilifungua ukurasa mpya wa mateso kwenye maisha yangu.
Naamini kama ningeomba ushauri kwa mama yangu au kwa mtu yeyote aliyenizidi umri, huenda angenipa mawazo ya namna ya kukabiliana na tatizo hilo kuliko uamuzi ambao niliuchukua. Jimmy alitumia kigezo cha umri wangu mdogo na mapenzi yangu kwake kunirubuni na kuweka doa kwenye maisha yangu ambalo mpaka leo haliwezi kufutika.
Ilipofika majira ya kama saa nne hivi asubuhi, Jimmy alinipigia simu na kuniambia nianze kujiandaa huku akisisitiza kuwa safari hii hatutaenda kwenye hospitali za vichochoroni bali atanipeleka kwenye hospitali kubwa yenye madaktari wenye uzoefu na kazi ya kutoa mimba.
Huku nikitetemeka, nilianza kujiandaa, nikaenda kuoga kisha nikavaa gauni langu zuri, nikajiangalia kwenye kioo kwa dakika kadhaa, nilijikuta nikitokwa na machozi huku nikiendelea kutetemeka.
Sikuwahi kufikiri hata mara moja kwamba ipo siku na mimi nitaingia katika orodha ya wauaji kwa kukatisha maisha ya kiumbe kilichokuwa ndani ya tumbo langu.
“Eeh Mungu nisamehe, sina cha kufanya zaidi ya kukubali alichokisema Jimmy,” nilisali huku machozi yakiendelea kunitoka. Nikatoka na kuanza kuelekea sehemu ya kukutania na Jimmy.
“Eunice! Eunice! Mbona unalia? Kuna tatizo?” mama aliniuliza wakati nikiwa nimeshafika mita kadhaa kutoka nyumbani, moyo wangu ukalipuka mno kugundua kuwa kumbe mama alikuwa akinitazama muda wote.
“Kwani unaenda wapi? Hebu njoo kwanza,” mama alisema huku akiteremka kwenye ngazi, nikabaki nimesimama palepale kama nimemwagiwa maji ya baridi. Mama alinisogelea na kunishika mkono, akanitazama usoni.
“Una nini mwanangu? Mbona sikuelewi?” alisema huku akinishika mkono na kuanza kunirudisha ndani lakini bado sikuwa tayari kumweleza kilichokuwa ndani ya moyo wangu. Alipoendelea kuniuliza, ilibidi nimdanganye kwamba nasikia kichwa kinaniuma sana.
“Sasa ulitaka uende mwenyewe hospitali? Ukizidiwa itakuwaje?” mama aliniuliza, nikabaki nimejiinamia. Alienda kufungua kabati na kunitolea vidonge vya kupunguza maumivu, akaniambia nikapumzike chumbani kwangu na kama hali hiyo ikiendelea, basi atanipeleka hospitali.
Akaniambia kwamba kama mawazo ya kutokwenda shule kwa kipindi kirefu kwa kukosa ada ndiyo yaliyosababisha kichwa kiniume, nisiwe na wasiwasi kwani kila kitu kitaenda vizuri baada ya siku chache kama alivyoahidi tangu mwanzo.
Nilirudi chumbani kwangu lakini bado sikuwa na amani, taarifa kuhusu shule zilizidi kuniongezea presha, mara simu ya yangu ikaanza kuita, nilipotazama namba ya mpigaji, alikuwa ni Jimmy.
“Uko wapi? Mi nimeshafika kitambo nakusubiri eneo letu lilelile,” alisema Jimmy kisha simu ikakatwa. Nilishusha pumzi ndefu, nikawa natafakari nini cha kufanya. Japokuwa nilikuwa naogopa sana lakini upande mwingine nilitaka kumfurahisha Jimmy. Niliamini kwamba nikikubali kutoa ujauzito wangu, tutarudiana kimapenzi kama mwenyewe alivyosema.
Nilipokumbuka suala hilo, nikajikuta napata nguvu za ajabu, nikatumia ujanja wa hali ya juu na hatimaye nikafanikiwa kutoka tena, nikapitia njia ya nyumanyuma na kupotelea mitaani, nikaenda mpaka sehemu ile Jimmy aliponiambia ananisubiri.
Cha ajabu alinipokea kwa uchangamfu sana, akanikumbatia na kunibusu shingoni, jambo ambalo lilinifariji na kuamini kwamba ni kweli alikuwa akitaka kurudiana na mimi. Akanifungulia mlango wa gari huku akiendelea kuzungumza na mimi kwa upole na ucheshi.
Akawasha gari na tukaondoka kwa mwendo wa kasi huku muziki laini ukituburudisha. Sikuongea chochote kwani hofu niliyokuwa nayo ilikuwa haielezeki, akaendesha gari mpaka tulipotokezea kwenye barabara ya lami. Safari hii alinipeleka Posta, gari likasimama mbele ya ofisi moja nzuri.
Tukateremka kwenye gari huku nikizidi kutetemeka kwa hofu, Jimmy akawa ananifariji na kuniambia nisiwe na wasiwasi kwani hakuna tatizo lolote kutoa ujauzito hasa ukiwa mdogo kama wangu. Hata hivyo, bado niliendelea kutetemeka kwa hofu na kwa kadiri nilivyokuwa napiga hatua kwenda mbele ndivyo hofu ilivyozidi.
Tuliingia na kwenda mpaka mapokezi, tukamkuta msichana aliyekuwa amevaa kama nesi aliyeonesha kufahamiana na Jimmy kutokana na jinsi alivyomchangamkia. Akatuelekeza tupande ngazi mpaka ghorofani. Tulipokelewa na mwanaume mtu mzima aliyekuwa amevalia koti la kidaktari.
Naye ilionesha anafahamiana sana na Jimmy na tayari walishazungumza kuhusu mimi kwani mwanaume huyo hakuniuliza chochote zaidi ya salamu. Baada ya muda, yule daktari alinichukua mpaka ndani ya chumba kilichokuwa na kitanda na vifaa vingine kama hospitali.
Nilishangaa sana kwani jengo hilo ukilitazama kwa nje, halikuwa na dalili yoyote kuonesha kwamba ndani kulikuwa kukifanyika ukatili huo. Niliendelea kutetemeka huku nikifikiria mara kadhaa kuhusu uamuzi wangu wa kukubali. Yule daktari akavuta dawa kutoka kwenye kichupa kwa kutumia bomba la sindano kisha akaja kunichoma.
Muda mfupi baadaye nikaanza kuhisi usingizi mzito, nikalala palepale kitandani na sikuelewa tena kilichoendelea.
Nilikuja kuzinduka baadaye sana na kujikuta nimelala kwenye chumba kingine, tofauti kabisa na kile cha mwanzo. Sikuwa na nguo hata moja mwilini zaidi ya shuka jeupe nililokuwa nimefunikwa.
“Unajisikiaje binti,” sauti ya daktari ilinishtua, nikajaribu kugeuka ili nimtazame vizuri, ni hapo ndipo nilipogundua kilichotokea kwani tumbo lilianza kuniuma sana kiasi cha kunifanya nianze kupiga kelele.
“Pole, maumivu hayo ni ya muda tu, hizi dawa utakuwa unakunywa kwa ajili ya kusafisha tumbo,” alisema daktari huyo huku akinipa furushi la vidonge na dawa za maji. Nilijaribu kuinuka lakini bado maumivu yalikuwa makali sana, hasa chini ya kitovu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ngoja nikuchome sindano ya ganzi,” alisema daktari huyo. Angalau maumivu yalipungua baada ya kuchomwa sindano ya ganzi, akanionesha nguo zangu kisha akatoka ili kunipa nafasi ya kuvaa. Nilijizoazoa na kuteremka kitandani, nikavaa nguo zangu, nikafungua mlango ambapo nilimuona yule daktari akiwa amekaa na Jimmy wakizungumza.
Jimmy aliinuka haraka na kuja kunishika mkono, akanisaidia kuteremka kwenye ngazi mpaka chini, akanipeleka kwenye gari huku akinipa pole nyingi na kunisifia eti kwa kumuokoa kutoka kwenye mdomo wa mamba. Alinisaidia kuingia kwneye gari na safari ya kuondoka ikaanza. Kwa muda huo sikuwa nikihisi maumivu makali kwani bado sindano ya ganzi ilikuwa ikifanya kazi.
Alinipeleka mpaka karibu kabisa na nyumbani, sehemu ambayo huwa tunakutania kila siku. Akafungua ‘dash board’ ya gari na kutoa burungutu la noti nyekundunyekundu, akaniambia eti nitakuwa nanunua juisi na matunda ili kurudisha damu zilizopotea.
Sikumjibu kitu zaidi ya kutingisha kichwa, nikaanza kutembea taratibu huku nikiwa nimeinama kidogo kwa mbele kutokana na maumivu ya tumbo ambayo sasa nilianza kuyasikia, nadhani sindano ya ganzi ilianza kuisha nguvu.
Nilitembea kwa kujikongoja mpaka nilipofika nyumbani, nikakuta mama na ndugu zangu wapo sebuleni wakila chakula cha mchana, nikapitiliza chumbani kwangu kimyakimya na kujitupa kitandani, machozi yakaanza kunitoka.
“Eeeh Mungu nisamehe kwa ukatili nilioufanya, sikukusudia ila sikuwa na njia nyingine,” nilisema huku nikiendelea kulia kwa uchungu. Narudia tena kusema kwamba sikuwahi hata siku moja kuhisi kwamba inaweza kutokea nikafanya kitendo cha kikatili kama hicho.
Kutoa mimba kwangu ilikuwa ni dhambi kubwa sawa na kuua na siku zote nilijiapiza kuwa kamwe sitajaribu kufanya mchezo huo lakini sasa na mimi tayari nilikuwa nimeingia katika orodha ya wasichana waliowahi kutoa mimba, tena nikiwa na umri mdogo kabisa.
Niliendelea kulia huku nikijihisi ni mwenye hatia kubwa mpaka nilipopitiwa na usingizi. Nilikuja kuzinduka baada ya kuhisi mama akinitingisha huku akiniita jina langu.
Kumbe wakati naingia chumbani sikukumbuka hata kufunga mlango, kwa bahati nzuri dawa za kusafisha tumbo nilizopewa pamoja na fedha nilikuwa nimezificha kwenye begi langu kwani bila hivyo mama angegundua mchezo kamili.
“Kwani ulikuwa wapi muda wote?” mama aliniuliza, nikamdanganya kwamba nilikuwa nyumba ya jirani kuazima daftari kwa rafiki yangu tuliyekuwa tukisoma wote kidato kimoja. Japokuwa mama aligundua kwamba namdanganya, hakutaka kuendelea kunihoji zaidi.
“Hee! Hiki nini tena mwenzetu?” mama alishtuka kupita kiasi baada ya kuona kitu kisicho cha kawaida kitandani kwangu. Na mimi nilishtuka na kuinuka kidogo nikitaka kujua mama alikuwa ameona nini. Nilipigwa na mshtuko usio na kifani baada ya kugundua kuwa kumbe wakati nimelala damu zilikuwa zikinitoka bila mwenyewe kujua.
“Aaa… oooh samahani, naona nimeingia kwenye siku zangu ghafla,” nilimdanganya mama huku nikibabaika, akaendelea kunitumbulia macho akiwa ni kama haamini alichokiona.
“Yaani hapo ulipo una utoto gani uingie kwenye siku zako bila mwenyewe kujijua? Kwani hukuona dalili? Ungekuwa mbele za watu huoni kama ni aibu kubwa hiyo,” mama aliendelea kunisema huku akiwa ameamini kwamba kweli nilikuwa nimeingia kwenye siku zangu.
Maskini! Hakujua kuwa muda mfupi uliopita nimetoka kufanya ‘abortion’. Nilijikaza kisabuni ili kuhakikisha mama anaendelea kuamini uongo wangu, nikainuka na kutoka haraka kwenda bafuni. Japokuwa tumbo lilikuwa linaniuma sana, nilijikaza ili mama asizidi kunishtukia.
Nilipoenda bafuni hata mimi nilichanganyikiwa mno kwani damu zilikuwa zikinitoka kwa wingi kiasi cha kulowanisha kabisa nguo zangu huku tumbo nalo likizidi kuchachamaa. Nilitumia muda mrefu bafuni, baadaye nikatoka na kwenda chumbani kwangu. Nashukuru mama alishaondoka na kwenda kuendelea na shughuli zake.
Nikatoa shuka ambalo sasa lilikuwa halitamaniki na kwenda kuliloweka bafuni, nikarudi na kusafisha chumba changu, nikatandika shuka jingine kisha nikajisitiri vizuri kwa ‘mambo yetu’ yale ili nisiendelee kuchafua nguo, naamini wanawake wenzangu wananielewa vizuri ninachomaanisha.
Kwa kuwa tumbo lilikuwa likiniuma sana, nilitoa dawa za kutuliza maumivu, nikanywa na kuendelea kupumzika. Kidogo hofu ilipungua kwani mama alishaamini kwamba natumikia siku zangu hivyo nilikuwa na uhakika hawezi kunisumbua kwa maswali mpaka siku nne zitakapoisha kwani hiyo ndiyo ilikuwa kawaida yangu kila mwezi.
Licha ya kunywa dawa za kutuliza maumivu, tumbo liliendelea kuniuma mno, kila nilipojaribu kulala nikiamini nitapitiwa na usingizi, hali ilikuwa tofauti kwani sikupata usingizi zaidi ya kuendelea kuugulia maumivu makali, masikini Eunice mimi! Nilijuta.
Siku hiyo sikula chochote zaidi ya juisi na maji kutokana na maumivu niliyokuwa nayahisi, ikafika muda nikalazimika kunywa vidonge vya usingizi ili nilale lakini bado haikusaidia chochote.
Kilichozidi kunitia hofu ni kwamba kila baada ya muda mfupi, nilikuwa nikienda kubadilisha mambo yetu yale kutokana na kuzidiwa na kasi ya mvua zilizokuwa zinanyesha kisawasawa. Ndani ya muda mfupi tu, tayari nilishabadilisha zaidi ya mara nne lakini bado kasi ilikuwa ikizidi kuongezeka.
Ilibidi nimpigie simu Jimmy ili nimueleze hali halisi, kwa bahati nzuri alipokea.
“Tumbo linaniuma sana na zinanitoka kwa wingi Jimmy, nahisi mpaka mwili unaishiwa nguvu.”
“Pole, ila dokta alisema ni hali ya kawaida, jikaze mpaka asubuhi tutajua cha kufanya, pole sana,” alisema Jimmy, kauli ambayo kidogo ilinipa matumaini. Sijui kwa nini, japokuwa nilikuwa na hali mbaya lakini kitendo cha kusikia sauti ya Jimmy tu, nilihisi ahueni kubwa, nikaachia tabasamu hafifu, tukaagana kisha simu ikakatwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hata hivyo, muda mfupi baadaye hali ilirudi kuwa ileile, tumbo likawa linazidi kuniuma, uzalendo ukanishinda na kuanza kuugulia kwa sauti, hali iliyomshtua mama, akaja mpaka chumbani kwangu.
“Mbona unaugulia hivyo mwanangu tofauti na siku zote ukiwa kwenye kalenda, leo imekuwaje?”
“Hata si…siju..ii mama,” nilimjibu mama huku nikiendelea kujinyonganyonga kutokana na maumivu. Hali iliendelea hivyo kwa muda mrefu, ikabidi mama ahame chumbani kwake na kuja kulala na mimi, akachemsha maji ya moto ambayo aliyatumia kunichua tumboni lakini bado hali ilizidi kuwa mbaya.
Ilifika muda nikaanza kusikia kizunguzungu, nahisi ni kwa sababu ya kupoteza damu nyingi. Hali iliendelea hivyo, kizunguzungu kikazidi safari hii kikiambatana na maumivu ya kichwa, ikafika mahali, nikawa naona giza tu mbele yangu. Sikuelewa tena kilichoendelea.
Nilikuja kuzinduka baadaye sana na kujikuta nikiwa kwenye mazingira tofauti kabisa na nyumbani. Nilikuwa nimelala juu ya kitanda kilichotandikwa mashuka meupe, nikatulia na kuanza kujiuliza pale ni wapi na nimefikaje. Nilipotazama vizuri, niligundua kuwa nilikuwa nimetundikiwa chupa ya damu.
“Mungu wangu,” nilijisemea ndani ya moyo wangu, nilipogeuza kichwa nilimuona mama akiwa amekaa pembeni yangu, amejishika tama na kuinamisha kichwa chake chini kuonesha kwamba alikuwa amezama kwenye dimbwi la mawazo.
Nilishtuka mno kugundua kuwa nipo hospitalini, nikajua siri yangu imetoka kwani lazima madaktari walinipima na kugundua kuwa nimetoa ujauzito. Niliendelea kumtazama mama ambaye hakuwa na habari kama nimesharejewa na fahamu.
Kwa jinsi alivyokuwa na majonzi, nilihisi huenda ameshajua kila kitu, mapigo ya moyo wangu yakawa yananienda mbio kuliko kawaida. Nilipojaribu kuinuka, nilishindwa kutokana na maumivu makali ya tumbo niliyokuwa nayahisi, mama akashtuka na kunisogelea.
“Mama! Hapa ni wapi?” nilimuuliza nikitaka kuhakikisha tu kwani tayari nilishajua kuwa nipo hospitali.
“Tupo hospitali mwanangu, unajisikiaje?”
“Bado tumbo linaniuma, kwani ilikuwaje mpaka nikaletwa hapa?” nilimuuliza mama kwa sauti ya chini, lengo langu likiwa ni kutaka kujua kama ameshaujua ukweli au la! Badala ya kunijibu, mama alijiinamia na nilipomtazama vizuri, niligundua kwamba alikuwa akilia. Ikabidi nitulie kwanza kwani ilivyoonesha tayari alikuwa akiujua ukweli.
“Eunice mwanangu, kwa nini umeharibika kiasi hiki? Wewe ni wa kwenda kutoa ujauzito halafu unanificha mimi mama yako?” mama alisema huku akilia kwa uchungu mno. Mapigo ya moyo yalinilipuka na kuanza kunienda mbio kupita kawaida, nilijikuta nikiishiwa nguvu kabisa, sikutaka tena kumtazama mama usoni.
“Ni…sa..mehe.. ma…ma,” nilisema kwa kubabaika huku na mimi nikianza kulia. Nilijisikia vibaya sana siku hiyo, mama aliendelea kunisemea maneno makali na kutishia kuniachia laana kama sitamtaja mhusika wa ujauzito huo na mahali nilikoenda kuutolea.
Akaniambia kwamba nimshukuru sana Mungu wangu kwani daktari aliyenipokea alikuwa akifahamiana naye vinginevyo ningekuwa chini ya ulinzi wa polisi kwa kosa la kufanya mauaji ya kichanga kilichokuwa ndani ya tumbo langu.
Mama aliendelea kuongea maneno mengi, akijilaumu na kunilaumu mimi, wakati mwingine akimlaumu Mungu kwa yote yaliyokuwa yakitokea kwenye maisha yetu. Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza kwa uchungu, nilishindwa kuendelea kumficha chochote.
Ikabidi nimueleze yote kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Nilipomtajia kwamba Jimmy ndiye aliyekuwa mhusika wa yote hayo, alipigwa na butwaa akiwa ni kama haamini alichokisikia, akabaki amekodoa macho kwa sekunde kadhaa.
Cha ajabu, hakuendelea kusema chochote, akainuka kimyakimya pale alipokuwa amekaa na kuanza kutembea taratibu kuelekea nje, kichwa akiwa amekiinamisha chini. Hakurudi wala sikumuona tena kwenye wodi niliyokuwa nimelazwa, baadaye akaja kaka yangu ambaye sasa ndiye aliyechukua jukumu la kuendelea kuniuguza.
“Dokta anasemaje? Nitapona kweli maana bado nasikia tumbo linaniuma.”
“Mh! Tusubiri maana nilimsikia mama akisema kuwa dokta aliyekutoa ujauzito alifanya makosa na kuikata mishipa ya damu kwenye kuta za kizazi chako ndiyo maana ulipoteza damu nyingi,” alisema kaka yangu, taarifa zilizoushtua mno moyo wangu.
“Mungu wangu, sasa kama amenitoboa kizazi si ndiyo mwanzo wa ugumba huu? Nitakuja kubahatika kupata mtoto kweli maishani mwangu,” niliwaza huku nikionekana kuzama kwenye dimbwi la mawazo machungu. Maelezo aliyonipa kaka yaliufanya moyo wangu ufe ganzi kwa hofu.
Kwa bahati nzuri, muda mfupi baadaye daktari alikuja kuangalia maendeleo yangu, nikaanza kumhoji maswali mengi ili angalau anipe jibu litakalofufua matumaini kwenye moyo wangu. Hata hivyo, haikuwa kama nilivyotegemea.
Nilipoanza kumuuliza, alinijibu kwamba kwa kuwa nimejitakia mwenyewe, madhara yoyote yatakayonitokea yananistahili na hakuna wa kumlaumu. Hakuwa mpole kwangu kama walivyo madaktari wengi, aliendelea kunishutumu kwa kuhatarisha maisha yangu nikiwa bado na umri mdogo sana.
“Umemuumiza sana mama yako, unakimbilia wapi mpaka kuanza mapenzi ukiwa na umri mdogo kiasi hicho? Watoto wa siku hizi bwana, mnaacha kukazania masomo mnaendekeza mapenzi, haya ndiyo matokeo yake sasa,” alisema daktari huyo kwa ukali.
Nililia sana, nikagundua kuwa kumbe nilikuwa nimefanya dhambi kubwa sana pengine kuliko hata nilivyokuwa nafikiria. Niliwasikia wagonjwa wengine waliokuwa wamelazwa jirani na mimi wakianza kunisema kwa sauti za chinichini huku wote wakinitazama.
Kwa hali ilivyoonekana, walikuwa wanajua kuwa nipo hospitalini hapo kutokana na kutoa mimba, jambo lililozidi kunifanya nijione mwenye hatia kubwa kwa wanadamu na kwa Mungu, nikaendelea kulia kwa uchungu huku kaka yangu akiwa ndiye mtu pekee aliyekuwa akinifariji.
Baadaye alikuja muuguzi mwingine wa kike ambaye alionekana kuguswa na kilichonitokea, akaja kunibadilisha chupa ya damu, akatoa ile iliyokuwa imeisha na kunitundikia nyingine, akawa ananifariji na kuniambia nimuombe Mungu kizazi changu kiwe hakijaharibika sana kwani kama ni hivyo, hakutakuwa na namna nyingine yeyote zaidi ya kukitoa.
“Mnitoe kizazi? Halafu itakuwaje sasa?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Huwa tunafanya hivyo kwa sababu wanawake wengi hasa wanafunzi, huwa wanaenda kutolea mimba vichochoroni au kwa madaktari wasio na utaalamu wa kutosha na matokeo yake, huharibiwa vizazi vyao jambo linalosababisha wakiletwa hapa tusiwe na namna ya kuwasaidia zaidi ya kuwatoa vizazi,” alisema nesi huyo kwa upole, akazidi kunichanganya kichwa changu.
Alipoondoka nililia sana, nikamuomba kaka yangu anipe simu yangu, nikajikaza kisabuni na kutafuta namba za Jimmy, nikamuendea hewani huku nikiendelea kulia. Hata hivyo, simu iliita tu bila kupokelewa kwa muda mrefu. Sikuchoka, nikaendelea kupiga tena na tena, baadaye simu ikapokelewa lakini cha ajabu, nilikutana na sauti ya mwanamke.
“We nani mbona unasumbua sana?”
“Samahani, namuomba mwenye simu,” nilisema huku nikijikaza nisiendelee kulia.
“Sema shida yako, ukinipata mimi ni sawa tu na kumpata mwenye hii simu.”
“Dada tafadhali naomba kuongea na Jimmy?”
“Nimekwambia eleza shida yako, kama huwezi kata simu na usipige tena,” alisema yule mwanamke kwa nyodo kisha akakata simu. Kitendo hicho kilikuwa sawa na kunichoma mkuki ndani ya moyo wangu, uchungu niliokuwa nausikia awali sasa ulizidi maradufu, maumivu nayo yakaongezeka mpaka ikafika mahali nikahisi nataka kufa.
“Eunice vipi? Jikaze dadaangu, utakuwa sawa usijali dada,” alisema kaka kwa sauti ya chini, akawa anaendelea kunifariji kwa maneno ya kunitia nguvu lakini haikusaidia kitu. Kwa mara ya kwanza nilijikuta nikimchukia Jimmy kupita kiasi.
Yeye ndiye aliyekuwa chanzo cha yote kwani bila kunishinikiza nikatoe ujauzito huo, mwenyewe nilikuwa tayari kuilea mimba mpaka itimize miezi tisa kisha kukileta kiumbe kipya duniani, kwa namna yoyote ile.
Nilitegemea kuwa baada ya kutimiza alichokuwa anakitaka, angenirudia kama mwenyewe alivyoahidi, kunionesha mapenzi makubwa kuliko awali na kunijali kwa moyo wake wote. Sasa iweje wakati mwenzake nikiwa kwenye maumivu makali kiasi hiki, yeye aendelee na ufuska wake? Nilijiuliza na kujikuta nikizidi kumchukia.
“Lazima atayalipia haya yote, siwezi kukubali,” nilijikuta nikitamka kwa sauti ya juu, kaka akashtuka na kuanza kuniuliza nilikuwa namaanisha nini na nilikuwa namzungumzia nani. Sikuweza kumjibu chochote zaidi ya kuendelea kulia.
Nikiwa katika maumivu makali, simu yangu ilianza kuita na nilipoangalia namba ya mpigaji, alikuwa ni Jimmy, nikaacha kila nilichokuwa nakifanya na kuipokea, nikataka nimsikie Jimmy atasema nini.
“Haloo! Sikia Eunice,” alisema Jimmy, nikashusha pumzi ndefu na kutega masikio yangu ili kumsikiliza alichokuwa anataka kukisema.
“Nilikuwa sijawahi kukwambia ukweli lakini leo nadhani ndiyo siku muafaka. Mimi nina mke na kwa kipindi chote hicho alikuwa masomoni, sasa amerudi na tunaendelea na maisha yetu.
“Hakuna mwanamke ninayempenda kama yeye, nyie wengine mlikuwa wapita njia tu, naomba kuanzia leo usinipigie simu wala kunisumbua kwa sababu mke wangu hapendi, nafikiri umenielewa,” alisema Jimmy na kabla hata sijamjibu chochote, alikata simu.
Kwa jinsi nilivyokuwa na jazba, nilijikuta nikiivurumisha ile simu ukutani, hata sijui nilipata wapi nguvu, ikapasukapasuka vipande na kuzusha hali ya tafrani mle wodini. Nikawa naendelea kupiga kelele kama mtu aliyechanganyikiwa.
Ilibidi manesi waitwe haraka, wakanizunguka pale kitandani na kunishika kwa nguvu, mmoja akanidunga sindano ya usingizi. Muda mfupi baadaye, nilipitiwa na usingizi mzito. Nilipokuja kuzinduka, nilijikuta nimehamishwa pale nilipokuwa nimelazwa awali na kupelekwa kwenye wodi ya peke yangu.
Pembeni yangu alikuwa amekaa kaka yangu ambaye alikuwa amejiinamia, aliposikia napiga chafya akafurahi na kunisogelea, akawa ananiuliza najisikiaje na akawa ananisihi niachane na hasira zisizo na msingi, nilitingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana naye huku machozi yakinilengalenga.
“Mama yuko wapi?”
“Mama anaumwa sana, analalamikia maumivu makali ya kichwa kiasi kwamba hawezi kufanya chochote.”
“Mungu wangu, najua haya yote ni kwa sababu yangu, hata sijui mwisho wa yote ni nini,” nilisema kwa huzuni. Mambo yaliyokuwa yakitokea, nilianza kugundua kuwa yapo nje ya uwezo wangu. Nilitamani dunia ipasuke inimeze kwani kosa moja nililolifanya, lilizua matatizo makubwa kuliko kawaida.
Niliendelea kujilaumu mwenyewe kwa kukubali kulaghaiwa na Jimmy, chuki dhidi yake ikazidi kunipanda.
Siku ya kwanza ilipita, nikawa naendelea na matibabu huku bado maumivu ya tumbo yakizidi kunitesa. Siku ya pili, nilianza kutokewa na hali ya ajabu. Licha ya tumbo kuendelea kunitesa sana, nilianza kutokwa na uchafu unaotoa harufu mbaya mithili ya kitu kilichooza sehemu zangu za siri.
Niliogopa mno, nesi alipokuja kunichoma sindano nikamueleza hali hiyo, na yeye akaonesha kushtuka na akanieleza kuwa hiyo ni dalili mbaya inayoonesha kuna kitu hakipo sawa kwenye kizazi changu.
“Mungu wangu, isije kuwa kizazi changu kimeharibika kama alivyosema yule nesi jana!” niliwaza huku nikiwa na hofu kubwa mno ndani ya moyo wangu. Kama ni kweli kizazi changu kilikuwa kimeharibika, maana yake wangenifanyia oparesheni kukitoa, jambo ambalo lilimaanisha kuwa siwezi kuja kupata tena ujauzito wala kuzaa. Ilikuwa ni zaidi ya maumivu!
Yule nesi alitoka na kwenda kumuita daktari yuleyule aliyekuwa akinitolea maneno makali jana yake, akaja naye mpaka kwenye kitanda nilichokuwa nimelazwa na kuanza kunichunguza kwa umakini. Akampa maelekezo yule nesi achukue sampuli kidogo ya uchafu niliokuwa nautoa kwa ajili ya kwenda kuufanyia kipimo kiitwacho Pap Smear.
“Dada tumuombe Mungu isije kuwa hilo tatizo tunalolihisi, yaani hata sijui itakuwaje,” alisema nesi yule kwa huruma, akanichukua vipimo na kuondoka navyo kuelekea maabara. Nilibaki nimejikunyata kama kifaranga cha kuku kilichonyeshewa na mvua, nikiomba Mungu afanye miujiza yake.
Hilo likiwa bado halijafika mwisho, kaka yangu alikuja na taarifa zilizozidi kuupondaponda moyo wangu. Alikuja na taarifa kwamba hali ya mama ilibadilika ghafla, akawa anapayuka na kuongea mambo yasiyoeleweka kama mwendawazimu.
“Kwa hiyo yuko wapi?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tumemleta hapahapa hospitali ila yeye amelazwa kule kwenye wodi ya watu wenye matatizo ya akili,” alisema kaka yangu huku na yeye akilengwalengwa na machozi.
“Unasemaaa? Mama amechanganyikiwa akili? Mungu wangu,” nilisema kwa mshtuko nikiwa ni kama siamini kaka alichoniambia. Hata sikujua mwisho wa yote hayo utakuwa nini, ama kwa hakika familia yetu ilikuwa ikipitia kipindi kigumu mno.
Mara mlango wa wodi ulifunguliwa, nikawaona nesi na daktari wakija huku mkononi wakiwa na faili ambalo hata bila kuuliza nilijua ni la majibu ya vipimo vyangu. Moyo ukanilipuka paah!
“Binti, pole sana,” alisema daktari huku akifungua faili lililokuwa na majibu yangu, akanitazama kwa muda kisha akashusha pumzi ndefu na kumgeukia yule nesi aliyekuwa ameongozana naye, wakapeana ishara kisha daktari akanigeukia na kuniuliza mahali aliko mama.
“Inabidi mama yako ndiyo aje ili tumpe majibu yako, hatuwezi kukupa wewe kutokana na hali yako.”
“Mama anaumwa, nipeni mimi au kama haiwezekani, mpeni kaka yangu,” nilisema, daktari akatazamana na yule nesi kisha wakapeana ishara fulani ambayo mimi sikuielewa. Kaka yangu naye alikuwa amesimama pembeni, akiwa haelewi chochote kilichokuwa kinaendelea.
“Wewe ndiyo kaka yake huyu mgonjwa?” daktari alimuuliza kaka, akatingisha kichwa kukubaliana na alichoulizwa.
“Tuna taarifa mbaya kuhusu mdogo wako.”
“Taarifa mbaya? Kuhusu nini?”
“Mdogo wako ana matatizo makubwa kwenye kizazi chake. Inavyoonesha daktari aliyemtoa ujauzito alifanya makosa makubwa na kukiharibu kizazi chake.”
“Mungu wangu! Kwa hiyo?”
“Inabidi afanyiwe upasuaji wa kutolewa kizazi ili kunusuru asizidi kupata matatizo zaidi.”
Kauli ya daktari ilipenya kama mkuki ndani ya moyo wangu, nikawa ni kama siamini alichokisema. Nitolewe kizazi? Sikuwahi kuogopa kama siku hiyo. Kwa tafsiri nyepesi, huo ndiyo ungekuwa mwisho wangu wa kupata ujauzito au mtoto. Hiyo ilimaanisha kwamba ningeishi kama mgumba kwa kipindi chote cha maisha yangu kilichobaki, jambo ambalo sikuwa tayari kuona linatokea.
Niliwatazama daktari na nesi kwa zamu, nikawa ni kama siamini nilichokisikia, nikamtazama kaka yangu ambaye alikuwa amejiinamia, machozi yakiwa yanamlengalenga.
“Daktari kwani hakuna namna nyingine ya kunisaidia?” nilimuuliza yule daktari huku nikilengwalengwa na machozi. Sikutaka kuamini kwamba huo ndiyo mwisho wangu wa kuishi maisha ya kawaida, nilibaki na majuto makubwa ndani ya moyo wangu.
“Hakuna namna nyingine binti, tukikuacha hivyo utakufa,” alisema daktari huku akionesha kutokuwa na masihara hata kidogo, akageuka na kuondoka huku yule nesi akimfuata kwa nyuma. Nilibaki nimeduwaa kwa muda, nikiwa ni kama siamini kilichokuwa kinatokea.
“Umeamua nini dada?” kaka yangu alinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo, nikashindwa hata kumjibu zaidi ya kuanza kulia kwa uchungu. Akanisogelea na kuanza kunibembeleza huku akiongea maneno ya kunifariji.
“Kila jambo lina sababu yake dada, wala usilie sana na kumlaumu Mungu, kubali kwamba ana malengo na wewe ndiyo maana haya yote yanatokea,” alisema kaka lakini maneno yake yalikuwa yakiingilia sikio moja na kutokea lingine. Sikuwa tayari kuona natolewa kizazi, akilini nilipanga kufanya chochote kinachowezekana kuzuia hali ile.
Mawazo ambayo niliyapata akilini mwangu, ilikuwa ni kutoroka hospitalini na kukimbilia kusikojulikana kukwepa kilichokuwa mbele yangu. Niliona ni bora niendelee kuteseka kwa kuumwa tumbo na kutokwa na uchafu tumboni kuliko kukubali kutolewa kizazi changu.
Kaka aliendelea kunifariji kwa muda mrefu lakini wala sikuwa nikimsikiliza, nilizama kwenye dimbi la mawazo machungu huku nikijilaumu sana kwa upumbavu niliokuwa nimeufanya.
“Mbona naongea na wewe lakini inaonesha upo mbali kimawazo?”
“Kaka tafadhali naomba niache kwanza, akili yangu haipo sawa kabisa.”
“Sawa, ngoja basi nikamuangalie mama,” alisema kaka, nikazinduka kutoka kwenye lindi la mawazo na kuanza kufikiria kuhusu janga lingine lililokuwa linatukabili, mama alikuwa amechanganyikiwa, sababu kubwa ikiwa ni mimi.
“Naomba tuende wote.”
“Hapana, we pumzika tu mpaka hiyo dripu iishe,” alisema kaka, akainuka na kuondoka, nikabaki peke yangu huku mawazo yakiendelea kuniandama. Kuna muda nilifikiria kwamba ni bora nife ili kukimbia matatizo makubwa yaliyokuwa yananiandama lakini akili nyingine ikaniambia huo haukuwa uamuzi sahihi.
“Kila tatizo lina njia yake ya kutokea,” maneno aliyokuwa akipenda kuyazungumza marehemu baba, yalijirudia ndani ya kichwa changu, kidogo nikapata ahueni. Nikachukua simu yangu na kujaribu tena kumpigia simu Jimmy lakini kama ilivyokuwa mara ya kwanza, alipokea tena mke wake.
Safari hii hakuwa na hata chembe ya uungwana, alianza kunivurumishia matusi mazito, tena ya nguoni huku akinitahadharisha kuacha kuipiga namba ya mumewe na kama nikiendelea, atanifanyia kitu kibaya ambacho sitakisahau maishani mwangu.
Hasira nilizokuwa nazo dhidi ya Jimmy zilinibadilisha mno, sikukubali kutukanwa kiasi kile, na mimi nikaanza kumjibu yule mwanamke huku nikimtolea vitisho kwamba nipo tayari kufanya chochote ili kumkomesha Jimmy.
Maneno yangu yalionesha kumgusa yule mwanamke, ghafla akawa mpole na kuanza kuniuliza kwa nini nataka kumdhuru Jimmy, nikamjibu kijeuri kwamba hayo mambo hayamhusu lakini lazima nimshikishe adabu, hata ikibidi kumuua nipo tayari.
“Dada punguza hasira, hebu nieleze kwani amekufanyia nini mpaka unafikia hatua ya kutoa maneno makali kiasi hicho?”
“Wewe si unajifanya jeuri, sasa subiri kupokea mzoga wa mumeo, mwambie kwamba alichokifanya kwangu hakina msamaha, lazima nimshikishe adabu,” nilisema huku nikitetemeka kwa hasira kisha nikakata simu. Yule mwanamke alionekana kuogopa sana kwani sikuwa na masihara hata kidogo, akaanza kunipigia simu mfululizo lakini sikupokea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya muda mrefu kupita, simu ikiendelea kuita mfululizo, niliamua kuipokea lakini tofauti na awali , safari hii alikuwa ni Jimmy mwenyewe, nikashusha pumzi ndefu na kumuuliza alichokuwa anakitaka. Nilikuwa nimebadilika mno, roho ya kisasi ikiwa imenijaa rohoni kupita kiasi.
“Nasikia unatishia kuniua si ndiyo?”
“Ndiyo, lazima nikuue Jimmy, wewe ni muuaji tena shetani mkubwa, hakuna adhabu inayokufaa zaidi ya kifo.”
“Kuniua mimi huwezi, pesa zangu zinanilinda kila ninapokwenda na ili kukuonesha kwamba mimi ni jeuri zaidi yako, naenda kukuchukulia RB polisi uje kukamatwa,” alisema Jimmy kwa nyodo lakini wala sikutishika. Kwa hali niliyokuwa nimefikia, moyo wangu ulikuwa umekufa ganzi kabisa, nilikuwa tayari kwa lolote.
Jimmy alipoona sitishiki na maneno yake, alikata simu, hasira juu yake zikazidi kunipanda huku nikijiapiza kuwa lazima nilipize kisasi. Mambo yote yaliyokuwa yananitokea, kuanzia kuharibika kwa kizazi changu mpaka kuchanganyikiwa akili kwa mama, chanzo kilikuwa ni Jimmy.
Basi afadhali angeonesha kunijali na kuwa upande wangu katika matatizo makubwa niliyokuwa napitia, bado aliendelea kuwa kikwazo kikubwa na kuutesa moyo wangu. Hakika nilichoka na kweli nilipania kufanya kitu ili kukomesha watu wenye tabia kama za Jimmy.
Baada ya dripu yangu kuisha, nesi alikuja kunitoa, kabla hajanitundikia nyingine, nilimuomba nikamtazame mama yangu kwanza kwani kwa mujibu wa kaka, hali yake ilikuwa mbaya na alikuwa amelazwa kwenye wodi ya wagonjwa wa akili.
Yule nesi aliniruhusu, nikasimama huku nikisikia maumivu makali ya tumbo, nikajikaza na kuanza kujikongoja kuelekea kwenye wodi ya wagonjwa wa akili kama nilivyokuwa nimeelekezwa na yule nesi. Kwa bahati nzuri, nilipofika nilimkuta kaka amekaa nje ya wodi hiyo, akiwa amejiinamia huku akionesha kuzama kwenye dimbwi la mawazo machungu.
Aliponiona alishtuka, akasimama na kunisaidia kukaa kwani nilikuwa nikiugulia maumivu makali ya tumbo, akaniuliza kama nilikuwa nimeruhusiwa kutoka wodini au nilifosi. Nilimuelewesha kuwa nesi amenipa ruhusa baada ya dripu yangu kuisha.
“Mama ana hali mbaya sana, halafu anaongea maneno ambayo mimi hata siyaelewi na sitaki kuamini, twende ukajionee mwenyewe,” kaka alisema, akanisaidia kusimama na kunishika mkono, nikajikongoja na kuingia ndani ya wodi ya wagonjwa wa akili wanawake ambayo ilikuwa na vurugu nyingi.
Kaka akaniongoza mpaka kwenye kitanda alichokuwa amelazwa mama. Sikuamini macho yangu, mama alikuwa amelala kitandani na kufungwa kamba mikononi na miguuni. Muda mwingi alikuwa akifurukuta akitaka kujifungua zile kamba lakini haikuwezekana.
Aliponiona tu, alitulia na kunitazama usoni kama anayevuta kumbukumbu mimi ni nani, mara akaniita jina langu na kuanza kulia kwa uchungu.
“Nisamehe mwanangu, mimi ndiyo nilihusika na kifo cha baba yenu, naijutia sana nafsi yangu, nilikubali kurubuniwa na mtu niliyeamini kwamba ananipenda kuliko alivyokuwa akinipenda baba yenu lakini yaliyotokea namuachia Mungu,” alisema mama huku akiendelea kulia kwa uchungu.
Nilimtazama kaka nikiwa ni kama siamini alichokuwa anakisema mama, akaniambia kuwa mara kwa mara amekuwa akizungumza maneno hayo lakini akaniambia tusimuamini kwani huenda anasema hivyo kutokana na kuchanganyikiwa akili.
Japokuwa nilikubaliana na kaka lakini tayari kengele ya hatari ililia ndani ya kichwa changu. Nilianza kuunganisha matukio mengi kuanzia siku ya mazishi ya baba ambapo polisi walifika nyumbani kwetu na kuanza kuwahoji baadhi ya watu kwa kile walichokisema kuwa ni kupeleleza chanzo cha mauaji ya baba.
Nakumbuka jinsi nilivyoshtuka siku hiyo kwani awali tuliaminishwa kuwa baba alikufa kwa ajali kazini akiwa kwenye kazi zake za uinjinia lakini nikashangaa kusikia polisi wakisema kuwa aliuawa na mtu asiyejulikana.
Sikuishia hapo, niliendelea kuunganisha matukio, jinsi mama alivyobadilika baada ya kifo cha baba, alivyokuwa anaondoka asubuhi sana akiwa amejipodoa kisawasawa na kurudi usiku, tena akiwa amelewa, tabia ambayo hakuwa nayo enzi za uhai wa baba. Pia nilikumbuka jinsi mama alivyofuja mali za marehemu baba ikiwemo fedha nyingi zilizokuwa benki, malipo ya mirathi na mali nyingine ambazo zingeweza kutusaidia maishani.
Nilikumbuka pia jinsi alivyoendelea na hali hiyo kwa muda kabla mambo hayajabadilika na kumfanya muda mwingi awe anajifungia chumbani kwake akionesha kuwa na mawazo mengi kama mtu aliyetokewa na tukio ambalo hakulitegemea.
Niliunganisha matukio yote hayo mpaka jinsi mama alivyoshtuka baada ya kugundua kuwa nilikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Jimmy, jinsi alivyonionya juu ya mwanaume huyo na yote yaliyofuatia. Nikajikuta napata picha tofauti kabisa kichwani mwangu.
Sikutaka kumpuuza mama kama kaka alivyokuwa ananiambia bali nilijikuta napata shauku kubwa ya kufahamu mambo mengi kutoka kwa mama ambaye kila mtu alikuwa akimuona kama mwendawazimu. Nilimuomba kaka atoke nje na kutupisha mimi na mama tuzungumze.
Alikubali ingawa alinisisitiza kuwa endapo atanisihi nimfungue kamba, nisikubali kwani walipata shida kubwa kumfunga, nikatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye. Alipoondoka, nilimsogelea mama huku nikijikaza kutokana na maumivu ya tumbo ambayo ama kwa hakika yalikuwa yakinitesa.
“Unasema ulihusika kumuua baba?”
“Ndiyo Eunice, wanaume wabaya sana, kuna mtu alinihadaa na kuniambia kuwa baba yenu ananipotezea muda, akaniambia tukifanikisha kumuua, atanionesha vitu nilivyokuwa navikosa kwa kipindi kirefu maishani mwangu. Sijui ni shetani gani aliniingia,” mama alisema huku akiangua kilio cha uchungu kila baada ya kuongea maneno machache.
“Kwa hiyo baba hakufa kwenye ajali kazini kama ulivyotuambia?”
“Haikuwa ajali bali ni mpango wa kifo ambao ulipangwa ili ionekane kuwa ni ajali lakini kwa bahati mbaya au nzuri, ukaenda tofauti na kuwafanya polisi na baadhi ya watu waliokuwa eneo la tukio washtukie mchezo.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unaweza kunitajia huyo mwanaume aliyehusika kwenye mpango wa kumuua baba?” nilimuuliza mama huku nikiwa nimemkazia macho, sikuwa na hata chembe ya masihara kwa sababu niliamini mama yangu hana makosa isipokuwa huyo mtu aliyemshawishi kisha kumuacha kwenye mataa ndiye adui yetu. Licha ya kumuuliza hivyo mama, hakuwa tayari kunijibu zaidi ya kuendelea kulia.
Nilizidi kumbana, ikafika mahali nikacharuka kama mbogo na kumshinikiza kuwa lazima amtaje vinginevyo nitaenda kuwaambia polisi kila kitu ili waje kumkamata.
“Ni Jimmy!”
“Whaaaat? Jimmy huyuhuyu ninayemjua?” nilisema kwa mshtuko nikiwa ni kama siamini nilichokisikia, nilitamani iwe ndoto.
Nilibaki nimeduwaa kwa sekunde kadhaa, nikiwa siamini kabisa kile kilichosemwa na mama. Alinihakikishia kuwa ni Jimmy huyohuyo niliyekuwa namfahamu ndiye aliyehusika.
Akaniambia kuwa ndiyo maana alipogundua kuwa nilikuwa na uhusiano na mwanaume huyo, alikuwa mkali sana kiasi cha kunipiga na kunijeruhi vibaya. Akaeleza jinsi alivyojisikia vibaya kuchangia mwanaume na mimi mwanaye wa kumzaa.
Nilishindwa kuendelea kumsikiliza, nikatoka mbiombio mpaka nje ambapo nilianza kuangua kilio kama niliyepokea taarifa za msiba. Nililia sana kiasi cha kuwafanya watu waliokuwa hospitalini hapo, kujaa na kunizunguka. Ilibidi kaka anichukue na kunirudisha wodini, nikamuona akizungumza kitu na nesi.
Muda mfupi baadaye, yule nesi aliyekuwa akinihudumia, alikuja kitandani kwangu akiwa na bomba la sindano lililokuwa na dawa ndani yake. Akaniandaa vizuri na kunichoma huku nikiendelea kulia kwa uchungu, nikaanza kusikia usingizi mzito na muda mfupi baadaye, nikalala fofofo.
Sikujua nimelala kwa muda gani lakini nilipokuja kurejewa na fahamu zangu, ilikuwa ni usiku, wodi yote ikiwa kimya kabisa. Pembeni yangu, kaka yangu alikuwa amekaa akiwa amejiinamia. Alipoona nimezinduka, alisimama haraka na kunisogelea pale nilipokuwa nimelala, dripu ikiendelea kutiririka kuingia ndani ya mishipa yangu.
“Unaendeleaje dada?”
“Nahisi kichwa kizito sana.”
“Pole, nafikiri ni kwa sababu ya dawa ya usingizi uliyochomwa.”
“Dawa ya usingizi?”
“Ndiyo! Nilipoona una hali ile, nilienda kumuomba nesi akuchome dawa ya usingizi ili utulie kwani ulikuwa na hali mbaya, pole sana na nakuhakikishia kila kitu kitakuwa sawa,” alisema kaka kwa sauti ya upole, nikajikuta machozi yakianza tena kunitiririka hasa wakati kumbukumbu za kilichotokea zilipoanza kunirudia.
Nilitamani ardhi ipasuke na kunimeza, nilitamani siku zirudi nyuma niyafute yote yaliyotokea, sikujua nitamtazama vipi mama yangu baada ya kuujua ukweli huo. Pia chuki dhidi ya Jimmy ilizidi kuwa kubwa ndani ya moyo wangu, kila nilipomfikiria mapigo ya moyo wangu yalikuwa yakinienda kasi kuliko kawaida.
Kaka aliendelea kunifariji, angalau nikaanza kuona kama kila kilichotokea ni kawaida ingawa hali hiyo ilikuwa ikija kwa muda mfupi tu, baada ya hapo mambo yalikuwa ni yaleyale. Namshukuru Mungu nilipoamka siku ya pili, maumivu ya tumbo yalikuwa yamepungua sana na hata uchafu haukuendelea kunitoka.
Japokuwa daktari alinisisitiza kuwa ni lazima nifanyiwe upasuaji wa kuondoa kizazi changu ili kuzuia madhara zaidi, nilikataa na kumwambia kuwa endapo nitazidiwa tena, nitarudi mwenyewe kwa ajili ya kazi hiyo, nikawa namuomba aniruhusu nikaendelee kujiuguza nyumbani.
Japokuwa haikuwa rahisi kukubaliana na mimi, nilipomng’ang’aniza daktari na kumueleza kuwa nilikuwa na matatizo makubwa ya kifamilia, alikubali kunipa ‘discharge’ ingawa alinisisitiza niwe naenda hospitali kila baada ya siku tatu.
Nilimshukuru sana na dripu yangu ilipoisha tu, niliruhusiwa kutoka hospitalini. Japokuwa bado nilikuwa sijapona lakini nilikuwa na ahueni kubwa ukilinganisha na wakati nafikishwa hospitalini hapo. Nikaandikiwa dawa za kuendelea kutumia nikiwa nyumbani huku daktari akirudia kunisisitiza tena na tena kuwa nirudi hospitalini hapo kila baada ya siku tatu.
Kaka alinisaidia kukusanya vitu vyangu, alipomaliza tuliondoka hospitalini hapo, sikutaka kwenda kwenye wodi aliyokuwa amelazwa mama kwani nilijua nitaenda kukitonesha kidonda changu ambacho bado kilikuwa hakijapona. Kaka akanisindikiza mpaka nyumbani ambako nilienda kwanza kuoga kisha nikaenda kupumzika chumbani kwangu.
Baada ya kuhakikisha nipo salama, kaka aliniacha mikononi mwa ndugu zangu wengine kisha yeye akaondoka kurudi hospitalini kuendelea kumuuguza mama. Nilipumzika kwa muda mrefu, ndugu zangu wakaniandalia chakula laini, nikala kidogo na kuendelea kupumzika huku akili zangu zikiwaza kitu kimoja tu, kisasi.
“Nikipata nguvu tu, lazima nimshikishe adabu Jimmy, atawajibika kwa yote aliyoyafanya,” niliwaza nikiwa nimejilaza kitandani.
Siku zilizidi kusonga mbele, hali yangu ikazidi kuimarika huku mama akiendelea kuteseka hospitali. Maumivu ya tumbo yakapungua kabisa na sasa nikawa na uwezo wa kutembea vizuri na hata kukimbia. Nilimshukuru sana Mungu wangu ingawa sikuwa na uhakika kama kizazi changu nacho kilikuwa kimepona.
Hakuna kitu nilichokuwa nakiogopa kama kuwa mgumba, nikawa namuomba Mungu wangu aniepushie mbali janga hilo. Baada ya siku tatu kupita, nilirudi hospitali kama nilivyoambiwa na daktari. Nikafanyiwa vipimo mbalimbali ambapo daktari aliniambia kuwa naendelea vizuri.
Akanipa dawa nyingine za kuendelea kutumia kisha baada ya kumalizana naye, nikaenda kumuangalia mama ambaye bado alikuwa amelazwa kwenye wodi ya wagonjwa wa akili.
Nilipofika, hali niliyomkuta nayo mama ilinisikitisha mno. Mama alikuwa amedhoofika kupita kiasi, yaani ndani ya siku chache tu ambazo nilikuwa sijamwona, aliisha na kubaki kama mtu aliyeugua kwa kipindi kirefu. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nesi aliyekuwa akiwahudumia, alinieleza kuwa eti mama ameweka mgomo wa kula kuanzia alipofikishwa hospitalini hapo na kwamba walikuwa wakijitahidi kumlisha kwa kutumia mipira maalum, tena akiwa amelala.
Kwa kweli niliumia sana, nilimtazama kaka ambaye muda mwingi alikuwa akishinda pembeni ya kitanda cha mama, nikamuona na yeye akiwa amejiinamia kwa huzuni.
“Haya yote chanzo ni mimi, tazama familia yangu inateketea kwa ujinga wangu, ni bora nife,” mama alisema kwa taabu, kauli iliyotushtua mno mimi na kaka, tukaanza kumbembeleza na kumsihi aache kufikiria kifo, tukamhakikishia kwamba tutakuwa naye pamoja mpaka mwisho wa matatizo yaliyokuwa yanaisumbua familia yetu.
Japokuwa mama alikuwa akionekana kama amechanganyikiwa, ukweli ni kwamba hakuwa amechanganyikiwa isipokuwa kichwa chake kilikuwa kimeelemewa na msongo wa mawazo na matatizo chungu nzima ambayo hakuwa na uwezo wa kuyahimili.
Nilitamani kutokee muujiza wa kumfanya aone kila kitu kuwa cha kawaida ili aruhusiwe kutoka hospitalini tukaanze kuijenga upya familia yetu lakini kwa ilivyoonesha, alikuwa akihitaji msaada mkubwa ili kumtoa kwenye hali hiyo.
“Kaka unaonaje tukimtafuta mtaalamu wa saikolojia kwa ajili ya kumsaidia mama?”
“Ni wazo zuri lakini si unajua kila kitu ni pesa?”
“Ni kweli lakini mimi kuna fedha kidogo nimebakiwa nazo, naamini zitatosha,” nilisema.
Kauli hiyo ilionesha kufufua matumaini mapya kwenye moyo wa kaka yangu. Tulikubaliana kazi hiyo tuifanye siku hiyohiyo kwani vinginevyo tungempoteza mama huku tukishuhudia.
Kwa kuwa mimi nilikuwa naifahamu ofisi ya mshauri mahiri wa saikolojia, Dismas Lyasa iliyokuwa Riverside, Ubungo jijini Dar es Salaam kwa wakati huo, niliamua kufunga safari kwa ajili ya kwenda kumuomba amsaidie mama. Japokuwa bado sikuwa ‘fiti’ kisawasawa, nilijikongoja hivyohivyo, nikamuacha kaka akiendelea kumuuguza mama.
Nikatoka mpaka nje kwenye kituo cha daladala, nikapanda za kuelekea Ubungo na safari ikaanza. Sikuwa naifahamu vizuri ofisi yake lakini kwa msaada wa ramani niliyoipata kwenye moja ya vitabu vyake vya saikolojia, niliamini nitafika.
Nilishuka Ubungo na kuvuka barabara nikapita kwenye taa za kuongozea magari na kuanza kutembea taratibu kuelekea Riverside. Nikawa natembea pembeni ya barabara, nikavuka daraja la Ubungo na kuvuka kituo cha daladala chenye vurugu nyingi. Nikawa naendelea kutembea taratibu pembeni ya barabara.
Ghafla nikashtushwa na gari lililofunga breki za ghafla pembeni yangu. Nilipogeuka na kulitazama huku mapigo yakinienda mbio, nililitambua kuwa linafanana sana na gari la Jimmy. Sikuwa nimekosea, nikamuona Jimmy akishuka na kuanza kunifuata kwa kasi, akionesha waziwazi kwamba alikuja kwa shari.
Nyuma yake, mwanamke ambaye simfahamu naye alifungua mlango, akawa anamfuata Jimmy kwa nyuma huku akijifunga vizuri nguo zake.
Nikajua nimepatikana, nilitamani kukimbia lakini nilikuwa nimechelewa, Jimmy akawa ameshafika. Nikawa natetemeka kwa hofu huku nikiwa sijui wamepanga kunifanya kitu gani.
“Wewe kinyago ndiyo unatishia kuniua? Nimekuja sasa, niue,” alisema Jimmy kwa sauti ya ukali huku akizidi kunisogelea. Mwanamke wake naye alinisogelea mpaka mwilini, akawa anamuunga mkono Jimmy kwa kila alichokuwa anakisema.
“Kinajifanya kinajua kutuma meseji za vitisho kijitu chenyewe hata kwenye mkono hakijai,” alisema mwanamke huyo, kufumba na kufumbua akanikwida nguo niliyokuwa nimeivaa.
Bado nilikuwa natetemeka nikiwa sijui wamepanga kunifanya nini. Nilipoona mambo ya kushikana mwilini yameanza, nikajua mwisho wake hauwezi kuwa mzuri. Kwa bahati nzuri, nilifanikiwa kuchoropoka, nikawa najaribu kukimbia lakini kabla sijafika mbali, Jimmy alinichota mtama kwa nguvu, nikadondoka kwenye lami puuh!
Sikuamini kama Jimmy anaweza kukosa hata chembe ya huruma kwangu, hasa ukizingatia kuwa bado nilikuwa sijapona tumbo ambalo yeye mwenyewe ndiye aliyenipeleka kutoa ujauzito na kunisababishia matatizo makubwa.
Kibaya zaidi, eneo tulilokuwepo lilikuwa jeupe sana na hakukuwa na mtu yeyote jirani anayeweza kunisaidia. Watu walikuwa mbali kutoka pale tulipokuwepo na hata nilipopiga kelele kutokana na maumivu niliyoyapata baada ya kuangukia tumbo, ni wachache tu ndiyo waliogeuka.
Kwa kuwa niliangukia tumbo ambalo bado lilikuwa halijapona, nilijisikia maumivu makali mno, hata hivyo nikajikaza kisabuni na kujaribu kusimama, Jimmy na mwanamke wake walikuwa wamesimama mita chache kutoka pale nilipokuwa, wakionesha kufurahia mateso niliyokuwa nayapata.
Huku nikichechemea, nikiwa nimeinama na kujishika tumbo, nilianza tena kutimua mbali lakini kama ilivyokuwa mara ya kwanza, Jimmy alinirukia na kunipiga tena teke lililonirusha juu, nikaanguka chini kama furushi. Hakuishia hapo, alikuna na kunikalia kifuani, akaanza kunivurumishia ngumi za usoni kama anayepigana na mwanaume mwenzake.
Akawa ananitolea vitisho kuwa nikiendelea kumfuatilia maisha yake, ataniua. Nililia sana lakini hata hivyo, hakukuwa na msaada wowote, Jimmy akawa anaendelea kunisulubu kwa hasira bila huruma. Mwanamke wake aliendelea kushadadia, jambo lililozidi kumpa Jimmy kichwa.
Hakujali kwamba tayari ameshanijeruhi vibaya usoni kiasi cha kusababisha damu nyingi ziwe zinanitoka mdomoni na puani, akaendelea kunipiga kwa hasira. Akili pekee iliyonijia, ilikuwa ni kufanya kila ninachoweza kujinusuru kwani kwa jinsi alivyokuwa ananipiga, ningelemaa angeweza kuniua.
Nilimdaka mkono wake mmoja, nikauvutia mdomoni na kuanza kumng’ata kwa nguvu zangu zote. Nilitumia nguvu kubwa mpaka nikahisi nimemchana mkononi lakini bado sikumuachia, akaacha kunipiga na kuanza kupiga kelele. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mwanamke wake alikuja na kuanza kumsaidia, nikamuachia Jimmy ambaye alisogea pembeni na kuanza kuangalia eneo nililomng’ata. Na mimi nilitumia muda huo kusimama, uso wote ukiwa unachuruzika damu, nikamuona Jimmy akinifuata kwa mara nyingine kwa lengo la kuendelea kunipiga, jambo ambalo sikuwa tayari kuona linatokea.
Sijui nilipata wapi nguvu, nikainama na kuokota jiwe kubwa lililokuwa kando ya barabara, nikalinyanyua juu na kuanza kumtishia Jimmy kwamba akinisogelea nampiga nalo lakini hakujali, akaruka kwa lengo la kuniangusha chini lakini kabla hajatimiza azma yake, nilimrushia lile jiwe kwa nguvu zote, likampata kichwani kisawasawa.
Kwa macho yangu nilimshuhudia Jimmy akianguka chini kama mzigo, akatulia tuli huku damu nyingi zikimtoka kichwani. Purukushani zile zilizodumu kwa dakika kadhaa, zilifanya watu wengi waliokuwa mbali, kuanza kutimua mbio kuja pale tulipokuwepo.
Dakika kadhaa baadaye, umati mkubwa wa watu ukawa umetuzunguka, mimi nikiwa nimepigwa na butwaa, nikiwa siamini kilichotokea, damu nyingi zikinitoka mdomoni na puani na Jimmy akiwa amelala chini. Yule mwanamke wake sikumuona tena, nikaanza kusikia kelele za watu wakisema: “Ameua! Ameua!”
Nilitamani kila kitu kiwe ndoto lakini haikuwa hivyo.
“Kwani imekuwaje?”
“Huyu dada kamuua mtu, wote tumemuona akimpiga na jiwe kubwa kichwani.”
“Dada yupi?”
“Huyo unayemuona mbele yako,” niliwasikia baadhi ya mashuhuda wa tukio lile wakimwambia mwanaume mmoja wa makamo aliyekuwa amevalia kizibao kilichokuwa na maandishi mgongoni yaliyosomeka Polisi Jamii.
Sikupata hata muda wa kujitetea kwani nilikuwa ni kama nimerukwa na akili. Kila nilipokuwa namtazama Jimmy ambaye alikuwa amelala chini damu nyingi zikiendelea kumtoka, nilikuwa ni kama siamini kilichotokea, nikahisi nipo kwenye njozi za kutisha.
“Kaa chini,” alisema yule mwanaume kwa sauti ya juu. Moyo ukanilipuka kwa nguvu kisha taratibu nikatii alichoniambia. Akamsogelea Jimmy pale alipokuwa amelala na kumgusa kifuani kusikiliza mapigo yake ya moyo. Nilimkazia macho yule polisi jamii kwani nilijua naweza kugundua kama Jimmy bado anapumua au la kwa kuzisoma hisia zake kupitia uso wake.
Nikamuona amekodoa macho na kuduwaa kwa sekunde kadhaa mara baada ya kukigusa kifua cha Jimmy, nikaelewa moja kwa moja kwamba mapigo ya moyo wake yalikuwa chini sana au huenda yalikuwa yamesimama kabisa, jambo ambalo bado nilikuwa sitaki litokee. Nilitamani wale watu waliokuwa wamenizunguka wamuinue Jimmy na kumkimbiza hospitali lakini haikuwa hivyo, nikazidi kuchanganyikiwa.
Kelele za watu waliokuwa wanazidi kuongezeka eneo lile, zilizidi kunipandisha wazimu, nikawa natetemeka mwili mzima huku nikijaribu kuwatazama wale watu kama kuna hata mmoja ambaye nilikuwa namfahamu ili angalau anisaidie.
Sura zote zilikuwa ngeni, yule polisi jamii ambaye naye alibaki ameduwaa pembeni ya mwili wa Jimmy baada ya kumpima mapigo ya moyo, akaanza kunihoji maswali ambayo hakuna hata moja nililolielewa.
Siyo kwamba alikuwa akiniuliza kwa lugha ngeni, hapana! Akili zangu zilikuwa zimehama kabisa kiasi kwamba sikuwa naelewa chochote zaidi ya kuwaza juu ya hatima ya Jimmy na kitakachonipata kama kweli alikuwa amekufa.
Damu ziliendelea kunitoka kwenye majeraha niliyokuwa nayo lakini sikujali wala sikusikia maumivu yoyote kwani mwili wangu ulikuwa umekufa ganzi. Nikamuona yule polisi jamii akibonyeza namba fulani kwenye simu yake ya mkononi, akaanza kuongea lakini hata sikujua anaongea nini na nani japokuwa alikuwa karibu yangu.
Japokuwa ni kweli Jimmy alikuwa amenikosea kwa kipindi kirefu na kunifanyia mambo ambayo ama kwa hakika hakuna binadamu mwenye hisia za kawaida angeweza kuyavumilia, niliona kama hakustahili kupatwa na yale yaliyotokea.
Ni kweli nilishajiapiza mara kadhaa kuwa lazima nimuue Jimmy kwa aliyonifanyia lakini sijui kwa nini nilijihisi kuwa na hatia kubwa kiasi hicho ndani ya moyo wangu. Nafikiri ni kwa sababu mwenzenu bado nilikuwa nampenda sana na nilikuwa na matumaini makubwa kwamba ipo siku atakuja kubadilika na kunikubali niwe mke wa maisha yake. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilizinduka kutoka kwenye dimbwi la mawazo baada ya kusikia muungurumo wa pikipiki ikipenya katikati ya umati mkubwa wa watu ambao wote walikuwa wakikanyagana kwa lengo la kunishuhudia.
Muda mfupi baadaye, askari wawili wanaotumia pikipiki ambao wengi hupenda kuwaita Tigo, walifika na kupaki pikipiki yao, wakashuka wakiwa na bunduki mikononi mwao. Moja kwa moja nikawaona wakizungumza na yule polisi jamii ambaye aliwaeleza kwa kifupi kilichotokea kisha wakanisogelea.
Bila hata kuniuliza chochote, mmoja kati yao alitoa pingu kiunoni na kuninyanyua pale chini nilipokuwa nimekalishwa, akanifunga kwa nyuma na kunikalisha tena. Nikamuona yule mwingine akitoa zile simu wanazotumia polisi (radio call) na kuanza kuzungumza na upande wa pili.
Haukupita muda mrefu, gari la polisi likaja eneo lile, askari kadhaa waliokuwa wamevaa ‘gloves’ kwenye mikono yao wakateremka wakiwa na machela na kumbeba Jimmy kisha wakamlaza kwenye ile machela yao na kumpandisha kwenye difenda.
Askari mmoja wa kike akaja na kuninyanyua pale nilipokuwa nimekalishwa, akanipandisha kwenye difenda ambapo nilikalishwa katikati ya askari wenye silaha, Jimmy akiwa pembeni yangu. Gari likaondoka kwa kasi huku umati mkubwa wa watu waliokuwa wamefurika wakipiga kelele na kuniita muuaji.
Kwa mara ya kwanza tangu tukio hilo litokee, nikajikuta nikishindwa kujizuia na kuanza kulia kwa uchungu huku nikitamani muda urudi nyuma japo kwa dakika chache tu ili nirekebishe yote yaliyotokea.
Safari yangu ya kuelekea ofisini kwa mwanasaikolojia maarufu, Dismas Lyasa kwa ajili ya kumuomba msaada wa kumsaidia mama ambaye alikuwa amechanganyikiwa akili kutokana na kuzidiwa na msongo wa mawazo, ikawa imeishia hapo. Nililia sana nilipomfikiria mama yangu na hali aliyokuwa nayo wodini lakini sikuwa na cha kufanya.
Breki ya kwanza ilikuwa ni kwenye Kituo cha Polisi Urafiki ambacho ndicho kilichokuwa kinahudumia maeneo yote ya kuanzia Ubungo, Kimara, Shekilango na baadhi ya sehemu za Sinza na vitongoji vyake, ukiachilia mbali kile kidogo kilichokuwa ndani ya stendi ya mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo.
Ni kama polisi walikuwa wakiwasiliana kwani gari liliposimama tu, askari kadhaa wenye silaha walilizunguka, nikanyanyuliwa mzobemzobe na kusukumizwa chini lakini kabla hata sijatua, tayari nilikuwa mikononi mwa askari mmoja mwanamke ambaye mpaka leo namkumbuka ingawa sikupata nafasi ya kulijua jina lake.
Japokuwa alikuwa ni mwanamke, alikuwa na mwili mkubwa wenye nguvu, usoni akiwa na rangi nyeusi tii! Nafikiri ni mwenyeji wa Kanda ya Ziwa. Akanidaka juujuu na kuanza kunikokota kwa nguvu kuelekea ndani ya kituo hicho, huku wenzake wakiwa pembeni, kila mmoja akiwa ameninyooshea bunduki yake.
Sikuamini kama Eunice mimi leo hii nilikuwa nadhibitiwa kama jambazi au muuaji mzoefu. Nikazungushwa nyuma ya kaunta na kukalishwa chini huku nikisindikizwa na vibao vya hapa na pale, kila mmoja akiniita muuaji.
Nikasikia ile difenda ikiondoka kwa kasi, bila hata kuuliza nikajua Jimmy anakimbizwa hospitali. Nikaanza kuhojiwa na yule askari mwanamke ambaye alianza kwa kuniuliza jina langu, umri, kabila, makazi na maswali mengine kama hayo huku akiandika maelezo yangu kwenye faili la rangi ya kaki.
Baada ya kuhojiwa kwa muda mrefu kuhusu historia yangu, yule askari wa kike alinisimamisha pale chini nilipokuwa nimekaa, akanipa kalamu na kuniambia nisaini kwenye yale maelezo aliyokuwa ameyaandika.
Kilichonishangaza ni kwamba hakuniuliza chochote kuhusu kilichotokea kati yangu na Jimmy, nafasi ambayo nilikuwa naisubiri kwa hamu kwani niliamini endapo nikipewa nafasi ya kujieleza, mtu yeyote ambaye atanisikiliza atanionea huruma.
“Vua viatu, mkanda kama unao, mtandio na hizo hereni zako. Kama una kitu chochote mfukoni nikabidhi,” alisema yule askari huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara. Nikavua viatu, mkanda na hereni kisha nikatoa kitambulisho cha shule ambacho nilikuwa natembea nacho japo nilikuwa siendelei na masomo.
Nikatoa fedha nilizokuwa nazo ambazo nilipanga kwenda kumpa mshauri nasaha na mwanasaikolojia, Dismas Lyasa kwa ajili ya matibabu ya kisaikolojia ya mama, nikatoa na simu, nikamkabidhi yule askari ambaye alichukua bahasha na kuviweka vitu vyote kisha akavibana pamoja, juu yake akaandika jina langu na kuweka kwenye droo zilizokuwa pale kaunta.
“Twende huku,” alisema huku akinivuta mkono kwa nguvu, wale askari wengine wakawa wanaendelea kunitolea vitisho kuwa huko ninakopelekwa ndiko kunakonifaa. Kwa kadiri tulivyokuwa tunaelekea ndani ndivyo hewa ilivyozidi kuwa nzito, nikawa nasikia harufu kali ya haja ndogo na kubwa ambayo ilizidi kuniongezea hofu kwenye moyo wangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Askari wengine wawili wenye silaha walikuwa wakitufuata kwa nyuma, tukaishia kwenye geti kubwa la chuma ambapo yule askari alitoa funguo na kufungua kufuli kubwa lililokuwa linaning’inia, akafungua na mlango wa ndani kisha akanisukumia ndani, nikasikia mlango ukibamizwa nyuma yangu, ukifuatiwa na kelele za geti la chuma, akamalizia kwa kubana kufuli.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment