Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

A LIVING DREAM ( NDOTO INAYOISHI ) - 2

 







    Simulizi : A Living Dream ( Ndoto Inayoishi )

    Sehemu Ya Pili (2)



    Kila siku Luciana alikuwa mtu wa kuumia tu, alimpenda sana mpenzi wake, Patrick lakini suala la Emmanuel kuingilia kati lilimpa wakati mgumu. Alijitahidi kutokumfikiria Emmanuel lakini kila siku alikuwa kama mtu anayejisumbua kutokana na mvulana huyo kuchukua asilimia kubwa moyoni mwake.

    Mapenzi bila mawasiliano, mapenzi ya mbali yalionekana kama kutaka kumuua nyoka kwa fimbo ya mbali, yaani wakati unakwenda kuichukua tu, mwenzako kashaondoka.

    Hivyo ndivyo ilivyokuwa katika kipindi hicho, mapenzi yale ya mbali yalionekana kutokusaidia kitu chochote kile. Akahisi kabisa kwamba Patrick alikuwa akianza kufutika moyoni mwake na Emmanuel kuanza kumuingia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Alibahatika kumuona siku moja tu, tena wakati alipokuwa akicheza mpira, ila siku hiyo moja ndiyo iliyobadilisha kila kitu moyoni mwake. Mapenzi yaliendelea kumkimbiza kila siku.

    Hakuwa akilala kwa raha, alikuwa mtu wa kujigeuza huku na kule tu. Alipokuwa akigeuka upande wa kushoto, Emmanuel alikuwa akionekana, alipokuwa akigeuka upande wa kulia kitandani hapo, Emmanuel alikuwa akionekana na hata alipokuwa akilala kifudifudi, bado tu Emmanuel alikuwa akionekana na kila alipokuwa akiamua kulala chali, alimuona Emmanuel akija juu yake na kumlalia.

    Luciana alijiona kuwa kwenye uamuzi mgumu, hakufikiria kama kitendo chake cha kuja Jijini Dar es Salaam kingeweza kubadilisha kila kitu likiwepo suala lake la kutaka kumsaliti Patrirk.

    Wiki nzima alikaa kwenye mawazo mengi, hakuwa akipenda mpira lakini kutokana na moyo wake kutekwa na Emmanuel, akajikuta akianza kuwa mfuasi mzuri wa mpira wa miguu shuleni hapo.

    Kila alipokuwa akimwangalia Emmanuel, moyo wake uliburudika, hakuwa ameongea naye lakini kwa jinsi alivyomtazama, alionekana kuwa kijana mcheshi na mwenye maneno mengi ambaye hata kama angekaa na msichana yeyote yule basi ilikuwa ni lazima afurahie.

    Kutokana na moyo wake kumruhusu Emmanuel kuchukua nafasi zaidi ya Patrick, akajikuta akianza kuingiwa na wivu. Alikumbuka kwamba aliambiwa na rafiki yake Joah kwamba Emmanuel alikuwa katika mahusiano na msichana aliyeitwa kwa jina la Hadija, kila alipokuwa akimuona mvulana huyo akiwa na Hadija, moyo wake uliumia kupita kawaida.

    “Sasa kwa ninaumia nini? Hivi kweli siwezi kusema imetosha na niendelee na mapenzi na mpenzi wangu Patrick?” alijiuliza Luciana lakini hiyo haikuweza kuubadilisha moyo wake, bado alikuwa akijisikia kuwa na Emmanuel tu.

    Maneno yake, malalamiko yake hayakuweza kubadilisha kitu chochote kile, bado aliendelea kumfikiria mvulana huyo ambaye kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo alivyozidi kumfikiria zaidi.

    “Ninakuchukia Emmanuel, ninakuchukia Emmanuel,” alisema Luciana huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikisema.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Maneno yake hayakuweza kuubadilisha moyo wake, bado aliendelea kumpenda Emmanuel. Kuna kipindi ambacho Luciana aliona hakukuwa na sababu ya kumuona Emmanuel, kila ilipokuwa ikitokea mechi, alijifanya kuwa bize kusoma lakini bado mvulana huyo aliendelea kuwa moyoni mwake.

    Alikosa amani, mapenzi yalimuendesha kupita kawaida. Alipoona hali hiyo inaendelea zaidi, hapo ndipo alipoamua kuanza tena kwenda kuangalia kila mechi ambayo Shule ya Azania ilikuwa ikicheza.

    Kitendo cha kumuona Emmanuel kwa mara nyingine, moyo wake ukatulia, akahisi anampenda zaidi, akawa hoi kwa mvulana ambaye hakuwa na habari naye.

    Siku zikaendelea kukatika, hata mawasiliano yake na mpenzi wake, Patrick yakawa yamepungua kabisa. Kila alipokuwa akiandikiwa barua, alijiahidi kurudisha majibu lakini akawa kimya.

    Hakujali kitu chochote kile, Patrick alianza kufutika moyoni mwake, na katika kipindi hicho alikuwa ameanza kuingia mwanaume mwingine kabisa, Emmanuel.

    “Joah, ninaomba unisaidie kitu kimoja,” Luciana alimwambia Joah, yule rafiki yake aliyempa taarifa kwamba Emmanuel alikuwa katika mahusiano na msichana aitwaye Hadija.

    “Nikusaidie nini?”

    “Kuna mwanaume nataka kuonana naye,” alisema Luciana, kwa muonekano wake tu, alionekana kuzidiwa na mapenzi.

    “Eeeh! Mwanaume gani tena?”

    “Emmanuel.”

    “Mmmh! Una hatari wewe.”

    “Hatari ya nini?”

    “Si unamzungumzia yule Emmanuel bwana wake na Hadija?”

    “Ndiyo huyohuyo.”

    “Unamtaka?”

    “Nahisi moyo wangu unaniambia hivyo.”

    “Unataka tushushuliwe?”

    “Na nani?”

    “Hivi unamjua Hadija humjui?”

    “Yupoje?”

    “Ana fujo sana, sitaki kushushuliwa, kama unataka nenda wewe mwenyewe,” alisema Joah.



    Kila msichana alikuwa akimuogopa Hadija, hakuonekana kuwa msichana wa kawaida, kwa sababu alikuwa amekulia maisha ya Uswahili, Temeke, Hadija alijua namna ya kumchambua mwanamke mara wanapokuwa katika ugomvi.

    Kutokana na maneno yake ya uswahili na kuzoea kushinda katika vigodoro, Hadija alionekana kuwa msichana wa ajabu, hakumuogopa mtu yeyote yule, maneno yake ya shombo yaliwafanya wasichana wenzake kumuogopa.

    Luciana hakutaka kukubali, alikuwa amekwishazama katika mapenzi ya Emmanuel, hakuogopa vitisho vya Hadija, kitu alichokuwa akikihitaji ni kuwa na Emmanuel tu.

    Siku ambayo aliamua kujipanga ikawadia, siku hiyo hakutaka kusikia kitu chochote kile, alichokuwa akikihitaji ni kuongea na mvulana huyo tu.

    Kama kuumia alikwishaumia sana, alitaka kuyapoza maumivu yake na njia sahihi ya kufanya hivyo ilikuwa ni kumuita Emmanuel na kuongea naye tu.

    “Hata kama nitachambuliwa, sitojali,” alijisemea Luciana, alichoamua ni kumsubiria Emmanuel ili aweze kuongea naye tu.

    Ilipofika saa nane kamili, kengele ya kuondoka nyumbani ikagongwa, kwa harakaharaka Luciana akachukua begi lake na kutoka nje ya eneo la shule. Siku hiyo hakutaka kuongea na mtu yeyote yule, kile alichokuwa akikitaka ni kuongea na mvulana huyo tu.

    Alipofika nje, kama bahati ilikuwa upande wake, wanafunzi wa Shule ya Azania nao wakaanza kutoka. Luciana akajipa uvumilivu wa kumsubiri mvulana huyo. Wanafunzi walimpita huku yeye akiwa amesimama katika ukuta uliokuwa umechorwa matangazo mengi kuhusiana na kujikinga na magonjwa hatari likiwepo UKIMWI.

    Baada ya dakika ishirini kusimama katika ukuta huo, kwa mbali akamuona mvulana ambaye kwa kumwangalia tu, aligundua kwamba alikuwa Emmanuel japokuwa alikuwa amempa mgongo.

    Mapigo yake ya moyo yakaanza kumdunda, akaanza kuogopa, alipoona kwamba aliteseka kwa muda wa miezi miwili kwa ajili ya kuongea na mvulana huyo, akapiga moyo konde na kisha kuanza kumfuata.

    Mapigo yake ya moyo yaliendelea kudunda zaidi na zaidi, amani ya moyo wake ikamtoka, kichwa chake kikaanza kufikiria mengi kwamba kama angemfikia basi angeweza kuongea naye na kumwambia mambo mengi kuhusiana na mapenzi.

    Huku zikiwa zimebakia hatua kumi kabla ya kumfikia, Luciana akasimama, akaanza kujiuliza kama lilikuwa jambo jema kumfuata au la. Akaupiga moyo konde kwa mara nyingine, akaendelea kumfuata, alipomfikia, akamshika bega, kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

    “Emmanuel....” Luciana akaita, Emmanuel akageuka na kuanza kumwangalia Luciana usoni, kwa mshtuko alioupata Luciana, alikaribia kuzimia, presha ilikuwa imekwishapanda huku moyo ukidunda mithiri ya kutaka kuchomoka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Niambie miss,” aliitikia Emmanuel, Luciana akaanza kusisimkwa, vinyweleo vikamsimama, alitamani kukimbia. Hata kabla hajaongea kitu chochote kile, Hadija akatokea.

    ****

    Luciana hakuongea kitu, alibaki kimya huku akionekana kuwa na hofu kubwa, kumuona Emmanuel mahali hapo, tena akiwa katika uso wa tabasamu, alijisikia furaha moyoni mwake.

    Kitu pekee ambacho kwa kiasi fulani kiliiondoa furaha ile aliyokuwa nayo ni ujio wa ghafla wa Hadija, msichana aliyeambiwa kwamba alikuwa akitembea na Emmanuel lakini pia alikuwa msichana mbabe, mwenye matusi na ukorofi wa hali ya juu.

    “Mambo!” alijikuta akimsalimia Emmanuel.

    Hadija aliyekuwa pembeni, akasogea karibu zaidi. Sura yake ilionekana kuwa na hasira nyingi, aliyauma meno yake kwa kwani muonekano wa Luciana ulionyesha kwamba msichana huyo alikuwa na hisia za kimapenzi kwa mvulana wake.

    “Poa!” alijibu Emmanuel huku akiachia tabasamu pana.

    Hadija hakutaka kupoteza muda, alijiona kama akichelewa kufanya kile alichokusudia kukifanya mahali hapo. Akapiga hatua zaidi na kuwasogelea, akaanza kumwangalia Luciana kwa macho ya dharau na kuanza kutoa misonyo.

    “Hadija! Sitaki ugomvi,” alisema Emmanuel huku akionekana kubadilika.

    Aliishi na Hadija kwa kipindi kirefu, alimfahamu, hakuwa msichana wa maneno mengi, alikuwa akifanya vitendo vingi vikiwepo vya kumpiga mtu ambaye alihisi kwamba alitaka kumchukulia mvulana wake.

    Luciana hakuwa msichana wa kwanza, yeye alikuwa kama wa nne. Kulikuwa na wasichana wengi walitaka kufanya kama vile alivyotaka kufanya Luciana lakini mwisho wa siku, wakajikuta wakitukanwa, wakivamiwa na kupigwa na msichana huyo.

    Emmanuel akabaki akimwangalia Luciana, kwa kumwangalia usoni tu, msichana huyo alikuwa mpole na mkimya huku akionekana kuwa na ufahamu mkubwa. Hakuonekana kuwa mchokozi au mgomvi, muonekano wake ungekufanya kugundua kwamba msichana huyo alizaliwa katika familia iliyozingatia misingi yote ya dini.

    “Hivi wanaume wote hapa shuleni wamekwisha?” aliuliza Hadija, hakutaka kusikia kitu chochote kile, tayari hisia zake zilimuonyeshea kwamba msichana huyo alitaka kufanya kitu kibaya cha kulipoteza penzi lake.

    “Hadija utanikera,” alisema Emmanuel huku akionekana kukasirika.

    Luciana hakuongea kitu, nafasi hiyo ya kukaa kimya ikamfanya Hadija kukasirika zaidi. Alikwishazoea kwamba kwa kila mtu aliyekuwa akimsema ilikuwa ni lazima mtu huyo azungumze chochote na kuanza kugombana.

    Kitendo cha Luciana kubaki kimya, kwake akakifananisha na dharau, hapo ndipo alipoamua kumvamia na kuanza kumpiga.

    Wanafunzi waliokuwa pembeni hawakutaka kupitwa, wakasogea karibu na kushuhudia ugomvi ule. Luciana hakurusha ngumi wala kofi, alikuwa akivutwa huku na kule na kupigwa mfululizo.

    Emmanuel hakutaka kukubali, alichokifanya ni kuingilia kati. Ngumi nyingine zilimpata yeye lakini hakutaka kujali, alijitahidi kumtoa Hadija na kufanikiwa, Luciana akabaki hoi, hata shati lake la shule lilikuwa limechanwa.

    “Wewe malaya nitakuua! Unafikiri nina masihala, uliza shule nzima utaambiwa mimi ni nani,” alisema Hadija huku akitukana mfululizo.



    Luciana hakuongea kitu, alishindwa kuvumilia, akaanza kububujikwa na machozi. Vibao na ngumi zilizompata zilimuumiza, uso wake ukaanza kuvimba huku damu zikianza kuonekana katika lipsi za mdomo wake.

    “Niachieeeee....nimesema niachie Emmanuel,” alisema Hadija huku akitaka kutoka katika mikono ya mvulana huyo.

    “Nisikilize Hadija!”

    “Nini? Unataka kuniambia nini?”

    “Subiri kwanza, mbona unakuwa na hasira hivyo? Kwa nini umempiga mtoto wa watu?” aliuliza Emmanuel kwa sauti ya chini.

    “Unamtetea? Nauliza unamtetea?” aliuliza Hadija. Muda wote alikuwa akiongea kwa sauti ya juu mpaka matemate kuanza kumtoka.

    “Subiri kwanza, usijifanye chizi, kwa nini umempiga msichana wa watu?” aliuliza Emmanuel kiupole.

    “Nimesema niache nimuonyeshe adabu,”

    Emmanuel alikuwa kijana mpole, mkimya, hakuwa mgomvi hali iliyowafanya watu wengine kumpa jina la mchungaji. Alipendwa shuleni hapo na kila mtu, aliheshimiwa mno lakini mara baada ya kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi na msichana Hadija, kila kitu kikaonekana kubadilka.

    Hakuwahi kupigana maishani mwake lakini kitendo alichokifanya Hadija kilimkasirisha, pasipo kutarajia, akajikuta akianza kumpiga msichana huyo.

    “Eeh! Mchungaji anaua!” alisikika mwanafunzi mmoja, watu wote waliokuwa wakipita barabarani wakaanza kusogea kule kuona vizuri kilichokuwa kikiendelea.

    “Muue kabisa, amezoea huyo, kama angetaka wa kwake peke yake si angemuumba au angeutafuta mgomba,” ilisikika sauti ya msichana mmoja na wengine kuisapoti kwa kuipigi kelele.

    Japokuwa Hadija alikuwa akilia, Emmanuel hakuonekana kujali, mtu mpole ambaye hakuna mtu aliyefikiri kwamba kuna siku angeweza kumpiga mtu, muda huo alibadilika, alikuwa na hasira kupita kawaida, hakutaka kushikwa na mtu yeyote, kwa sababu Hadija ndiye alikuwa sababu, aliendelea kumshushia kipigo.

    Kipigo kile kikali kikawashtua wanafunzi waliokuwa wakishangilia, wakaona kwamba Emmanuel angewea kumuua msichana yule, walichokifanya ni kuwasogelea na kumshika mvulana huyo aliyeonekana kuwa na hasira kali mpaka mishipa ya shingo kumsimama.

    Kila alipotaka kuongea kitu, alishindwa, mwisho wa siku akajikuta akilia tu. Moyo wake ulikuwa kwenye hasira kali mno, kila alipokuwa akimwangalia Hadija, alitamani kumuongezea kipigo kwani hata picha za nyuma alipokuwa akiwapiga wanafunzi wengine zilimrudia, hivyo alitamani kuendelea kumpiga zaidi.

    “Please forgive her,” (Tafadhali! Naomba umsamehe!) alisema Luciana huku akimshika Emmanuel mkono.

    “Did you get hurt?” (Umeumia?) aliuliza Emmanuel.

    “Ofcourse! But please forgive her,” (Ndiyo! Lakini tafadhali naomba umsamehe) alisema Luciana.

    “But why did she do this to you? I am fed up of her,” (Lakini kwa nini amekufanyia hivi? Nimechoshwa naye) alisema Emmanuel huku akionekana kuanza kupoa kutoka kwenye hasira kali alizokuwa nazo.

    Siku hiyo ndiyo ulikuwa mwisho wa uhusiano wa kimapenzi baina ya Emmanuel na Hadija. Japokuwa mara kwa mara msichana huyo alikuwa akimfuata kijana huyo na kumuomba msamaha, alimsamehe lakini hakutaka kuwa naye tena.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Hadija aliumia, akaanza kuzichukia hasira zake, hakuamini kama hizo ndizo zilizosababisha kumpoteza Emmanuel wake. Mara kwa mara alikuwa akimfuata na kumuomba msamaha lakini Emmanuel alikuwa mwanaume mwenye msimamo mkali, hakutaka kuwa naye tena.

    Siku zikaendelea kukatika, huku uhusiano wake na Hadija ukiendelea kufa, ndipo alipoanza kuwa karibu na Luciana. Kila siku alikuwa akionana naye alikuwa akimuuliza swali lilelile kama aliumia au la.

    Maswali ya kujirudia, ukaribu wao, taratibu Emmanuel akajikuta akianza kumuingiza msichana huyo moyoni mwake, mapenzi yakaanza kumteka, kwa Hadija, hakutaka kuzama moja kwa moja kwani alihisi kama alikuwa akijilazimisha kwa msichana huyo, lakini kwa Luciana, aliuhisi moyo wake kupenda kwa penzi la dhati....ila hakujua kama msichana huyo alikuwa na mvulana wake aitwaye Patrick aliyekuwa mkoani Tabora masomoni.

    ***

    Emmanuel hakutaka kujificha tena, moyoni mwake alijiona kuwa na mapenzi mazito kwa Luciana, hivyo hakutaka kuendelea kuugulia, kitu alichokifanya ni kupanga siku ambayo angemwambia ukweli kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.

    Siku ambayo alipanga kuzungumza naye alijipanga vilivyo, alihakikisha kila kitu kinakaa sawa na kwenda shuleni kwa ajili ya kuzungumza na Luciana.

    Alipofika shuleni, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumtafuta Luciana, kila siku alikuwa na kawaida ya kuonana naye katika Kituo cha Fire lakini siku hiyo hali ilikuwa tofauti, kila alipokuwa akimsubiri, hakutokea.

    Tayari akashikwa na wasiwasi kwa kudhani kwamba Luciana hakuwa amekuja shuleni, lakini pamoja na hayo yote, hakutaka kuondoka, aliendelea kuvumilia kwa kuamini kwamba angeweza kuonana naye.

    “Mambo!” ilisikika sauti ya msichana nyuma yake, alipogeuka, macho yake yakagongana na Luciana.

    “Waoooo! Umependeza!” alisema Emmanuel huku akimwangalia Luciana ambaye uso wake ulijawa na tabasamu tu.

    “Asante. Umenisubiria sana?”

    “Hapana! Na mimi ndiyo kwanza nimefika sasa hivi,” alisema Emmanuel japokuwa alijua kwamba alimsubiria sana, hakutaka kumwambia ukweli.

    Wakaondoka kituoni hapo na kwenda shuleni. Japokuwa walikuwa wakiongea mambo mengi lakini kichwa cha Emmanuel kilifikiria namna ya kuufikisha ujumbe wake kwa Luciana, hakujua ni kwa namna gani angeweza kumwambia na kueleweka.

    “Luciana...”

    “Abeeee....”

    “Kuna kitu nataka kukwambia. Unaniruhusu?” alisema Emmanuel.

    “Hakuna tatizo. Kitu gani?”

    “Ooppss...” akajikuta akishusha pumzi nzito.

    “Kitu gani?” aliuliza kwa mara nyingine.

    “Ni muda mrefu sana nimekuwa nikijifikiria juu ya su....” alisema Emmanuel lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, wakajikuta wakiwa wamekwishafika katika geti la Shule ya Wasichana ya Jangwani.

    Kwa jinsi mapigo ya moyo wa Emmanuel ulivyokuwa ukidunda, akaona afadhali walikuwa wamefika katika geti hilo kwani hakuwa na nguvu za kuendelea kumwambia Luciana juu ya lile lililokuwa likiusibu moyo wake.

    Kati ya hatua kumi alizotakiwa kupiga, hiyo ndiyo ilikuwa hatua ya kwanza kabisa, akajipa nguvu kwamba angeweza kufanya vizuri zaidi katika siku nyingine kuliko siku hiyo. Wakaagana na kila mtu kuingia katika geti la shule yake.

    Darasani hakukusomeka, kila wakati Emmanuel alikuwa na mawazo juu ya msichana huyo, kwake, alimuona kuwa msichana mwenye uzuri wa ajabu kupita kawaida. Kila alipokaa na kuanza kuufikiria uzuri wake, akabaki akifurahia tu.

    Kama alivyojiahidi kwamba siku hiyo angemueleza ukweli kilichokuwa kikimsibu moyoni mwake, alipoonana naye muda wa kutoka shuleni akaamua kumueleza ukweli.

    “Ninaogopa.”

    “Unaogopa nini Luciana?”

    “Namuogopa Hadija.”

    “Unamuogopea nini?”

    “Akijua...”

    “Atafanyaje?”

    “Atanipiga, hukumbuki siku ile?”

    “Lakini nishamuacha, nilishamwambia asinijuejue, simpendi,” alisema Emmanuel.

    “Imeanza lini?”

    “Toka siku ile, yaani mimi na yeye hatuivi chungu kimoja.”

    “Sawa, naomba muda wa kujifikiria.”

    “Mmmh!”

    “Nini tena?”

    “Itawezekana kweli?”

    “Nitakujibu!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Siku hiyo Emmanuel alijiona kushusha mzigo mzito kutoka kichwani mwake, hakuamini kama alifanikiwa kumwambia Luciana ukweli wa moyo wake. Kila alipokaa, kichwa chake kilikuwa kikifikiria jibu ambalo angeweza kupewa na Luciana kama alikubaliana naye au la.

    Kwa Luciana, moyo wake ulikuwa kwenye wakati mgumu, alijua fika kwamba alimpenda Emmanuel lakini suala la Patrick bado lilimuumiza kichwa chake.

    Hakujua ni kitu gani alichotakiwa kukifanya, suala la kuwa n Emmanuel lilimaanisha kwamba Patrick ndiyo ingekuwa basi tena. Kila wakati alipokuwa akikaa, alijipa matumaini kwamba hata Patrick mwenyewe aliamua kuachana naye hasa kila barua aliyokuwa akiandika hakuwa akiijibu.

    “Acha niwe na Emmanuel tu, sina jinsi.”

    Huo ndiyo uamuzi wa mwisho ambao aliufikiria, akaamua kuwa na Emmanuel na mapenzi yakaanza rasmi.

    Walipenda na kuthaminiana, japokuwa si mara zote walikuwa wakionana lakini kwa siku zile walizokuwa pamoja, walionyesheana kwamba walikuwa wakipendana mno.

    Mapenzi yakawa mapenzi, wakapelekana mpaka nyumbani, wakatambulishana kwamba walikuwa marafiki wa kufa na kuzikana. Wazazi wote wakakubaliana nao, na kwa sababu hawakuwa wakimfahamu Patrick, kwao ikaonekana kuwa shwari.

    Baada ya wanafunzi wa kidato cha sita kumaliza mtihani, huku Lucian akiwa amekaa shuleni tena huku moyo wake ukiwa na hamu kubwa ya kuongea na Emmanuel, akasikia akiitwa na rafiki yake, Joah na alipomfuata, akamwambia kwamba kulikuwa na mwanaume alikuwa akimuulizia getini.

    “Nani? Emmanuel?” aliuliza Luciana.

    “Hapana.”

    “Sasa ni nani?”

    “Sijui! Wala simjui!”

    Luciana akawa na maswali mengi juu ya mvulana aliyekuwa akimuulizia, hakutaka kubaki pale alipokuwa, alichokifanya ni kwenda kule alipokuwa akihitajika. Hakuamini macho yake mara baada ya kufika hapo na kumuona mtu aliyekuwa akimuulizia, alikuwa Patrick.

    “Patrick....” alijikuta akiita Luciana, aliuhisi mwili wake kupigwa ganzi.

    “Ndiye mimi mpenzi! Nimerudi tena,” alisema Patrick huku tabasamu pana likiwa usoni mwake.

    “Umerudi lini?”

    “Jana, sikutaka kukufahamisha, nilitaka kukufanyia surprise,” alisema Patrick, alisimama nje ya gari alilokuja nalo huku uso wake ukipendezeshwa kwa tabasamu pana.

    “Ooppss....” Luciana akajikuta akishusha pumzi ndefu na nzito, kichwa chake kikaanza kumfikiria Emmanuel.

    ****

    Kuna kipindi Luciana alihisi yupo katika usingizi mzito wa kifo na baada ya muda angeshtuka na kujikuta kitandani, kile kilichokuwa kimetokea, hakikuweza kuaminika mbele yake.

    Mvulana aliyekuwa mpenzi wake, aliyemthamini na kumpenda na hata kumpa shauku ya kwenda Dar es Salaam, leo hii alikuwa mbele yake kwa mara nyingine tena baada ya mara ya mwisho kuonana mjini Bagamoyo, lakini tatizo lilikuwa pale alipohisi moyo wake haukuwa kwa mvulana huyo.

    Mawazo mengi yalimjaa moyoni mwake, hakujua ni kitu gani alitakiwa kumwambia PAtrick, alihisi halikuwa jambo rahisi kumwambia kwamba alikuwa amepata mvulana mwingine hivyo alitakiwa kutafuta msichana mwingine kwani moyoni mwake hakuwa na nafasi tena.

    Japokuwa huo ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe, lakini alihofia kumwambia Patrick kwamba hakutaka kuwa naye tena, alijua ni kwa jinsi gani mvulana huyo alikuwa na upendo mkubwa, alijua ni kwa namna gani alisubiri kwa kipindi kirefu kuwa naye kwa mara nyingine, ubaya ni kwamba alikuja muda mbaya, muda ambao alitakiwa kuukumbuka ule msemo kwamba “Fimbo ya mbali haiwezi kuua nyoka’



    “Naomba usogee karibu mpenzi,” alisema Patrick huku akiachia tabasamu pana.

    “Kusogea karibu yako?”

    “Ndiyo laazizi, nimekukumbuka mno,” alisema Patrick.

    “Hapana! Siwezi!”

    “Kwa nini tena?”

    Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi nzuri ya kumwambia kwamba alikuwa amekwishapata mvulana mwingine, lakini kila alipomwangalia Patrick, alijihisi kuwa binadamu mwenye huruma nyingi kuliko binadamu wote duniani.

    “Huoni kama nina nguo za shule! Mbaya zaidi upo katika himaya ya shule yetu,” alisema Luciana.

    Sababu hiyo ikamridhisha Patrick hivyo hakutaka kukaa sana, akaondoka shuleni hapo.

    Luciana akawa na mawazo, alijiona kupitia kwenye wakati mgumu kuliko nyakati zote alizowahi kupita katika maisha yake. Hakuwa na raha tena, Patrick aliharibu kila kitu moyoni mwake.

    “Kuna nini Luciana?” aliuliza Emmanuel mara baada ya kukutana naye.

    “Hakuna kitu mpenzi.”

    “Haiwezekani! Huwa haupo hivyo, hebu niambie kuna nini.”

    “Hakuna kitu. Kweli tena hakuna kitu, nahisi naumwaumwa, hasa kichwa, tena upande huu,” alisema Luciana huku akikishika kisogo chake.

    “Pole sana. Umekunywa dawa?”

    “Yeah!”

    “Basi nenda nyumbani ukapumzike, nitakuja kukuona usiku,” alisema Emmanuel.

    “Sawa.”

    Hakujua ni wapi alitakiwa kuomba ushauri juu ya kile kilichokuwa kikiendelea kutokea maishani mwake. Wavulana wawili ambao wote walikuwa wazuri kwa sura waliuweka moyo wake katika wakati mgumu.

    Moyo wake ukagawanyika, upande mmoja ulimwambia kwamba Patrick alikuwa bora zaidi kwa sababu alikuwa mwanaume wake wa kwanza lakini upande mwingine ambao ulikuwa mkubwa zaidi, ukamwambia kwamba Emmanuel alikuwa bora zaidi kwa kuwa alikuja wakati alipokuwa na uhitaji wa kuwa na furaha zaidi.

    Aliendelea kuishi katika hali hiyo mpaka pale Patrick alipopafahamu alipokuwa akiishi na hivyo kuanza kufika nyumbani hapo na kuendelea kumsisitizia kwamba alikuwa akimpenda mno na alihitaji kuwa naye.

    Kwa Luciana, ni kama alikuwa kigeugeu, kila alipokuwa akizungumza na Patrick, alimuonyeshea upendo wa kinafiki lakini moyo wake ulikuwa kwa Emmanuel. Moyo wake ukawa na donge moja kubwa, donge ambalo aliamini kwamba kuna siku angelitema kwa Patrick pasipo kujali kama mvulana huyo angeumia au la.

    “Nikwambie kitu Patrick,” aLuciana alimwambia Patrick.

    “Niambie! Kuna nini?” aliuliza Patrick huku akiwa ameachia tabasamu pana.

    “Ooppss..!!” luciana akashusha pumzi ndefu na nzito.

    Walikuwa katika baa moja, ulikuwa ni usiku wa saa mbili, hakukuwa na watu wengi sana sehemu hiyo na kila mtu aliyekuwepo mahali hapo alikuwa akiendelea na mambo yake pasipo kumjali mwenzake.

    Siku hiyo ndiyo ambayo Luciana alipanga kumwambia Emmanuel ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake. Hakutaka kumficha tena, hakutaka kukaa na donge zito moyoni ambalo kila siku lilikuwa likimfurukuta tu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Tatizo lilikuja pale alipokuwa akimwangalia mvulana huyo. Moyo wake ulimkataza kabisa kumruhusu kufanya kile alichokuwa amekipanga kwani uliamini kwamba yangekuwa maumivu mazito kwa Patrick na angeweza kufanya kitu chochote kile kulinusuru penzi hilo.

    Emmanuel hakuwa kimya, kama kawaida yake, mara kwa mara alikuwa akimpigia simu Luciana lakini msichana huyo hakutaka kabisa kuipokea, alikuwa akikiangalia kioo cha simu ile huku jina la mpigaji lililosomeka ‘The Only One’ likionekana lakini hakuipokea kabisa, cha zaidi, akaigeuzia chini, yaani kioo kikawa chini.

    “Najua unanipenda sana Patrick,” alisema Luciana, alikuwa akijizungushazungusha tu.

    “Tena zaidi ya sana, si unakumbuka hata ile siku ya kwanza kukuona kule Bagamoyo, hakika upendo wangu haukupungua hata kidogo,” alisema Emmanuel.

    “Lakini Patrick....”

    “Unasemaje kipenzi?”

    “Mungu wangu! Sijui niseme nini!”

    “Niambie chochote tu. Nataka nianze chuo, nikisoma kwa miaka mitatu nataka kukuoa kabisa,” alisema Patrick.

    “Ishu siyo ndoa Patrick.”

    “Kumbe ishu ni nini?”

    “Moyo wangu!”

    “Umefanya nini?”

    “Ooppss..!!”

    “Niambie.”

    “Haupo kwako tena,” alisema Luciana.

    Kwanza Patrick akabaki kimya, akafikicha macho yake na kumwangalia vizuri Luciana, hakuyaamini maneno yale aliyokuwa ameyaongea, alitaka kusikia tena kuona kama msichana yule alikuwa amemaanisha kile alichokuwa amekizungumza au la, alipomuuliza, Luciana hakupindisha maneno, aliendelea kumwambia vilevile kwamba moyo wake haukuwa kwake.

    Kuna matukio mengi yanapotokea, mtu unahisi kwamba utakuwa kwenye ndoto moja ya kusisimua ambayo itakupeleka kutamani kuamka, na unatokea kumshukuru Mungu sana kwa kuona kwamba kile kilichokuwa kikiendelea, kumbe kilikuwa katika ulimwengu mwingine kabisa, hivyo ndivyo alivyotamani Patrick iwe.

    Hakuamini. Picha ya kwanza kabisa kumjia kichwani mwake, ni ile siku ya kwanza ambayo alikutana na msichana huyo mjini Bagamoyo, urembo wake na hata ile ahadi waliyowekeana hukohuko huku ule mbuyu ukiwa shahidi, tena huku wakiwa wameyaandika majina yao, hakika ilikuwa ni zaidi ya maumivu.

    “Luciana! Umechanganyikiwa?” aliuliza Patrick huku akionekana kutokuamini.

    “Hapana! Nina akili timamu, ulipokuwa shule, nilimpata mvulana mwingine, anaitwa Emmanuel,” alisema Luciana kwa kujiamini.

    “Impossible...haiwezekani kabisa. Unakumbuka kule Bagamoyo, unaukumbuka ule mbuyu, unakumbuka tulizungumza nini na mbuyu ukawa shahidi?” aliuliza Patrick huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa, macho yake yakageuka na kuwa mekundu, alitamani kulia.

    “Nakumbuka kila kitu. Kwa nini niendelee kukufariji na wakati moyo wangu haupo kwako tena?” aliuliza Luciana.

    Si Patrick tu aliyeumia, bali hata Luciana mwenyewe alisikia maumivu makubwa moyoni mwake. Hapo ndipo alipogundua kwamba alikuwa na chembechembe za mapenzi kwa Patrick. Kila neno alilokuwa akilizungumza, hakutaka kulizungumza ila kulikuwa na nguvu ya ziada iliyomwambia kwamba alitakiwa kumwambia hivyo.

    “Yaani pamoja na muda wote nilioupoteza Luciana?”

    “Ndiyo!”

    “Yaani pamoja na upendo mkubwa niliokuwa nao Luciana?”

    “Ndiyo! Naomba utafute msichana mwingine Patrick, kiukweli, moyo wan...” alisema Luciana lakini Patrick akaingilia.

    “Kila kitu kina gharama Lucy...kila kitu kina gharama, chochote kitakachotokea, ule mbuyu utakuwa shahidi wetu,” alisema Patrick, akasimama na kuondoka mahali hapo.

    Yalikuwa ni zaidi ya maumivu moyoni mwake, macho yake mekundu yakaanza kumwaga machozi mfululizo. Moyo wake uliumia kupita kawaida, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea.

    Alipoteza muda wake mwingi kwa ajili ya msichana huyo, alimfikiria katika kipindi chote alichokuwa shuleni lakini mbaya zaidi, alimwandikia barua nyingi mno, hapo ndipo alipopata jibu kwamba kwa nini barua zake hazikujibiwa.

    Hakutaka kutembea, alikuwa akikimbia kulifuata gari lake, alipolifikia, akaufungua mlango na kuingia ndani. Hapo ndipo alipogundua kwamba mapenzi yanauma, hapo ndipo alipogundua kwa nini watu wengine waliamua kujiua au kuua kwa ajili ya mapenzi.

    Yaani Luciana yuleyule, msichana yuleyule aliyesimama naye chini ya mbuyu na kumwambia kwamba alikuwa akimpenda, msichana yuleyule aliyeahidiana naye ahadi nyingi kwamba wangeoana na hatimae kuishi kama mume na mke, msichana yuleyule ambaye aliamua kuwakataa wasichana wengine kwa ajili yake, leo hii, alimwambia kwamba hamtaki, kwa sababu tu alikuwa amepata mwanaume mwingine. Patrick alijisikia kuua.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    ****

    Ulikuwa ni moja ya mibuyu mikubwa mjini Bagamoyo ambapo watu wengi walikuwa wakifika hapo kwa ajili ya kuweka tambiko au kuzungumza maneno mabaya hasa kwa maadui zao au wale wenye roho mbaya kuutumia mbuyu huo kwa ajili ya kuwapotezea bahati wale waliokuwa wakiwaonea wivu.

    Mara kwa mara wale waliokuwa wakiamini katika uchawi, wale waliokuwa wakiuthamini uchawi kuliko kitu kingine walikuwa wakifika mbuyuni hapo na kufanya kile walichokuwa wakikitaka kukifanya hasa kwa ubaya.

    Ulikuwa mbuyu mbaya uliojaa laana, ulikuwa mbuyu mbaya uliokuwa ukiwapotezea watu bahati. Mchana, ulionekana kama mbuyu mzuri wa kukaa chini yake na kuleta kivuli kizuri lakini kwa usiku, mbuyu ule ulikuwa ukitumika kama makazi ya wachawi wote wa Mkoa wa Pwani.

    Kundi kubwa la wachawi kutoka katika Mkoa wa Pwani walikuwa wakikutana chini ya mbuyu ule na kucheza uchi huku wakati mwingine wakitumia sehemu hiyo kama sehemu hiyo kunywa damu za watu waliozipata kutoka katika ajali mbalimbali zilizokuwa zikitokea.

    Mbuyu huo ulikuwa maarufu kuliko kitu chochote kile mjini Bagamoyo, umaarufu wa mbuyu ule ulikuwa mkubwa hata zaidi ya watu kumfahamu rais wao wa nchi. Japokuwa kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakiuogopa mbuyu huo, lakini kuna wengine walikuwa wakiufuata na kufanya mambo yao mengine.

    Halikuwa jambo la ajabu kukuta nazi, kuku aliyechinjwa chini ya mbuyu huo uliokuwa ukitisha sana kila ilipofika usiku. Nguvu kubwa za kichawi ziliuandama jambo lililoongeza hofu kwa wakazi wengi.

    Kuna kipindi zilienea tetesi kwamba kulikuwa na mwanamke mzuri, aliyekuwa akivutia ambaye alipenda sana kukaa karibu na mbuyu ule na wanaume waliovutiwa naye na kumfuata, waliuawa na kunyonywa damu.

    Zilikuwa tetesi zilizovuma sana, vyombo vya habari vikatangaza sana, watu wakahofia mno na kutotaka hata kuuona.

    Pamoja na vitisho vyote hivyo, bado Patrick na Luciana walifika chini ya mbuyu huo kila usiku na kufanya vile walivyotaka kuvifanya. Chini ya mbuyu huo ndipo walipowekeana ahadi kwamba wasingeweza kuachana na kama ingetokea kuachana, basi yule ambaye amemuacha mwenzake asiweze kuishi kwa furaha katika maisha yake ya uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine na hatimae mwisho wa mwaka kufa.

    Mbali na kuwekeana ahadi hiyo, wawili hao wakawekeana agano la damu kwa kuchanana na wembe kisha kila mmoja kulamba damu ya mwenzake. Mbuyu huo wa ajabu ukawa shahidi, majini yote yaliyokuwa yakizunguka karibu na eneo lile la mbuyu yakawa mashahidi kwa kile kilichokuwa kimetokea.

    Patrick na Luciana walipendana na kuaminiana kwamba kusingekuwa na mtu yeyote kati yao ambaye angeweza kumsaliti mwenzake, kwa jinsi mapenzi yalivyokuwa yakiwaendesha, walihisi kama wangeishi milele.

    Kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea, Patrick akabaki akizikumbuka zile siku zote ambazo alitumia na Luciana kuwa chini ya mti na hata kuwekeana ahadi kwamba wangeishi milele na kusingekuwa na yeyote ambaye angewatenganisha.

    “Leo hii Lucy amesahau kila kitu!” alisema Patrick huku akilia kama mtoto mdogo.

    “Yaani amesahau kipi tuliwekeana chini ya mbuyu, kasahau kila kitu, Luciana....kwa nini lakini? Kwa nini umes.....” alisema Patrick lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake akaanza kulia.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake ya kila siku, kila alipomkumbuka Luciana, alikuwa akilia tu. Walifanya mambo mengi matamu lakini mwisho wa kila kitu, hawakuwa pamoja tena.

    Mara baada ya kukaa kwa wiki moja huku moyo wake ukiwa kwenye maumivu makali mno, Patrick akaamua kwenda mjini Bagamoyo, hakwenda huko kwa ajili ya kuwasalimia ndugu, jamaa na marafiki bali alikwenda huko kwa kuwa alitaka kuulalamikia mbuyu kwa kile kilichokuwa kimetokea.

    Usiku wa saa mbili, Patrick alikuwa chini ya mbuyu huo. Uwepo wake mahali hapo ukaanza kumkumbusha mbali, alikumbuka kila kitu alichokuwa akifanya na msichana yule, alikumbuka mambo mengi yaliyomfanya kulia zaidi.

    “Amenisaliti, amevunja ahadi yangu,” alisema Patrick huku machozi yakimbubujika mashavuni mwake, alikuwa amepiga magoti huku akikipigapiga kifua chake.

    Hakujua ni kitu gani kilichokuwa kimeendelea, mara upepo mkali ukaanza kuvuma mahali hapo, kwanza akaogopa na kutamani kukimbia lakini kila alipotaka kufanya hivyo, miguu yake ikawa mizito kuinuka.

    Upepo ule uliendelea kuvuma zaidi, majani yaliyokuwa pembezoni mwa mbuyu ule yakaanza kama kutoa sauti ambazo hakuzielewa zilisemaje zaidi ya kumuongezea hofu zaidi.

    Huku akiwa mwenye hofu kubwa, ghafla, akatokea msichana mrembo, msichana wa Kiarabu ambaye kwa kumwangalia tu, alikuwa na umbo zuri lililoyachanganya macho yake.

    “Wewe nani?” aliuliza Patrick huku akionekana kuwa na hofu moyoni.

    “Nilikuwepo,” alisema msichana yule.

    “Ulikuwepo! Wapi?”

    “Siku mlipokuja kuwekeana ahadi hapa, na hata mlipoweka agano la damu, nilikuwepo,” alisema msichana yule huku akionekana kuwa na majonzi, naye, kwa jinsi alivyoonekana, alikuwa kama mtu anayekaribia kulia.

    “Ulikuwepo siku ile? Luciana amenisaliti, kama ulikuwepo, bora twende ukamkumbushe, yaani kasahau kila kitu,” alisema Patrick huku akimsogelea msichana yule.

    “Hapana! Sitoweza kwenda, kama amevunja ahadi mliyowekana, ni lazima aadhibiwe,” alisema msichana yule huku akionekana kumaanisha alichokuwa akikisema.

    “Utampa adhabu gani?”

    “Tutamuua.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com*

    “Hapana! Ninampenda Luciana, naomba usimuue, ninampenda Luciana wangu, mpe adhabu yoyote lakini si kumuua,” alisema Patrick huku akianza kulia tena.

    “Unataka tumfanye nini?”

    “Chochote kile, lakini si kumuua.”

    “Kama hatutomuua, basi tutamfanya kichaa katika maisha yake yote hapa duniani, kwa kuwa mliweka ahadi chini ya mbuyu huu, na sisi ndiyo tutakaohusika katika kutoa adhabu,” alisema msichana yule, upepo uliokuwa umetulia, ukaanza kuvuma tena, kukasikika kuwa na kelele nyingi mahali hapo mpaka Patrick akaziba masikio yake, ghafla, msichana yule, akapotea!

    ****



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog