Simulizi : Juliana
Sehemu Ya Tano (5)
Safari yao ikaishia katika Ufukwe wa Coco ambapo ndipo alipotaka kufanya mauaji ndani ya gari kabla ya kumchoma kisu kisha kumtupa huku akimshikisha kisu hicho ili kuonyesha kwamba mwanamke huyo alijiua kwa kujichoma kisu.
Gari liliposimama, Juliana akabaki akishangaa, hakujua sababu iliyomfanya mumewe kusimamisha gari mahali kama hapo. Hakuwa na hofu naye kwani alihisi kila kitu kilikuwa salama kabisa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati akifikiria hayo tayari Gideon akaanza kukishika kisu chake kilichokuwa kiunoni, alitaka kummaliza Juliana hapohapo garini kisha kumtoa na kumshikisha kisu kile kuonyesha kwamba alijimaliza mwenyewe.
“Moja, mbili, tat…” alihesabu kabisa.
Wakati akihesabu, ghafla akasikia simu yake ikianza kuita, akashtuka, haraka sana akaichukua kutoka mfukoni mwake na kuipeleka sikioni hata bila kuangalia mpigaji alikuwa nani.
“Umemaliza?” ilisikika sauti ya Juliet kwenye simu.
“Bado!”
“Kwa hiyo umeshindwa? Basi usinijuejue,” ilisikika sauti hiyo.
“Hapana! Sijashindwa! Naomba dakika chache kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Gideon huku akionekana kuogopa kumpoteza msichana mrembo kama Juliet.
Wakati akizungumza na Juliet kwenye simu, Juliana alibaki akimwangalia, mumewe alikuwa akizungumza kwa kukatishakatisha maneno kitu kilichoonekana kuwa na hofu kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
Gideon alitumia sekunde chache, alipomaliza, akashusha pumzi nzito, akajigusa kiunoni kuangalia kama kisu chake kilikuwepo, alikiona na hivyo kujiandaa kukichukua kwa ajili ya kumchoma Juliana.
Hata kabla hajafanya hivyo, simu yake ikaanza kuita tena. Moyo wake ukapiga paaa kwani alijua kabisa kwamba mpigaji alikuwa Juliet, haraka sana akaichukua na kuipeleka sikioni.
“Nimekwambia nipe dakika chache,” alisema Gideon mara baada ya kuipokea simu.
“Kaka! Kuna tatizo nyumbani...” Ilisikika sauti ya Halima, msichana wa kazi aliyekuwa naye nyumbani kwake.
“Kuna tatizo?”
“Ndiyo! Jesca anaumwa sana, mwili wake umeanza kushika joto mno,” alisikika Halima.
“Nani? Jesca? Anaumwa sana? Mwili umeshika joto?’ aliuliza Gideon mfululizo.
Gideon alichanganyikiwa, hakuamini alichokuwa amekisikia kwamba mtoto wake wa pekee, Jesca alikuwa akiumwa mno usiku huo. Japokuwa alikuwa kwenye hatua za mwisho kumuua mke wake ndani ya gari, hakutaka kufanya hivyo bali akakiacha kisu chake, akawaha gari na kuondoka mahali hapo.
Juliana aliishiwa nguvu, aliposikia kwamba mtoto wake alikuwa akiumwa alichanganyikiwa, alimpenda mno, alikuwa kwenye maumivu makali, familia yake ndiyo ilikuwa kila kitu, alimuuliza mumewe mara kwa mara kuhusu Jesca lakini hakujibu kitu kwani naye alichanganyikiwa mno.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika nyumbani, harakaharaka wakateremka na kuanza kuelekea ndani. Japokuwa Juliana alikuwa akiumwa sana lakini akajikaza mpaka kufika chumbani ambapo wakamkuta mfanyakazi akiwa na mtoto sebuleni huku akimbembeleza anyamaze kwani alikuwa akilia sana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tatizo nini?” aliuliza Gideon huku akimshika Jesca.
“Sijui ila nadhani ni maralia. Mwili wake umechemka sana,” alisema mfanyakazi huyo.
“Jesca...Jesca tatizo nini mama?” aliuliza Juliana huku naye akimgusa mtoto huyo kupima joto la mwili wake.
Alikuwa kwenye hali mbaya, Jesca hakujibu chochote kile zaidi ya kuendelea kulia. Hawakutaka kubaki mahali hapo, haraka sana wakamchukua, wakampakiza ndani ya gari na kuanza kuondoka mahali hapo.
Garini, kila mmoja alikuwa kimya, Juliana alimpakata mtoto wake huku mumewe akiendesha gari hilo. Gideon akasahau kabisa kuhusu Juliet, wakati huo kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mtoto wake aliyekuwa kwenye hali mbaya tu.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika hospitalini ambapo moja kwa moja wakateremka na kuanza kuelekea ndani huku wakiwa wamembeba mtoto huyo. Manesi walipowaona, wakaleta machela, wakampakiza na kuanza kuelekea ndani.
Walikwenda mpaka katika chumba kimoja kilichoandikwa ICU kwa nje na kuambiwa wasubiri hapo.
Hawakutulia kwenye mabenchi yaliyokuwa mahali hapo, walitaka kujua kile kilichokuwa kikiendelea humo ndani.
Baada ya saa moja, mlango ukafunguliwa na mwanaume mmoja mnene aliyekuwa na koti jeupe na kuwaambia kwamba mtoto wao alishikwa na maraliia kali hivyo walitakiwa kuondoka na kumuacha hapo apumzike kwanza.
“Siwezi kuondoka na kumuacha mtoto wangu!” alisema Juliana huku akimwangalia daktari.
“Sawa. Ila hutoweza kumuona kwa kipindi hiki!”
“Haina shida. Ila kuondoka mahali hapa siwezi,” alisema Juliana.
Alimaanisha, ilikuwa vigumu kuondoka na wakati mtoto wake alikuwa kwenye hali mbaya kupita kawaida. Vile alivyosema ndivyo alivyomaanisha kwamba kamwe asingeweza kuondoka mahali hapo hapo na wakati mtoto wake alikuwa kwenye hali mbaya kupita kawaida.
Kwa sababu muda ulikuwa umekwenda sana, Gideon akaondoka kwa ajili ya kununua chakula, alipofika ndani ya gari tu, simu yake ikaanza kuita na alipoangalia jina la mpigaji, alikuwa Juliet, kwanza moyo wake ukapiga kwa nguvu, hakutegemea kwamba msichana huyo angepiga tena simu huku akiwa hajafanya kile walichokuwa wamekubaliana.
“Umekwishamuua?” lilikuwa swali la kwanza hata kabla ya salamu.
“Bado!”
“Bado? Kwa nini? Hutaki kuishi na mimi? Mbona hutaki kunisikiliza? Mbona hutaki kufanya ninachotaka ukifanye hubby?” aliuliza Juliet huku akijifanya kulia kwenye simu.
Kwa jinsi moyo wake ulivyokuwa ukimpenda msichana huyo, Gideon akajisikia vibaya moyoni mwake, alijiona kama mkosaji mkubwa. Alitamani kumuomba msamaha kwani kilio chake kiliuumiza mno moyo wake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwa nini lakini hubby?”
“Naomba unisamehe! Kuna tatizo liilitokea,” alisema Gideon.
“Tatizo gani?”
“Mtoto wangu anaumwa sana. Tumemleta hospitalini. Ila nilikuwa katika hatua za mwisho kukamilisha mpango wetu,” alisema Gideon.
“Kwa hiyo akiwa anaumwa ndiyo mama yake hawezi kufa?” aliuliza Juliet huku akionekana kuwa na hasira.
“Hapana!”
“Kumbe tusemeje? Mimi najua hunipendi tu! Najua unataka kunichezea,” alisema Juliet huku akilia kitu kilichomfanya Gideon kusikia uchungu mno kwenye simu.
Alitamani hata kumpigia magoti msichana huyo, alikuwa akimpenda mno na alikuwa na hamu ya kufanya kile alichotakiwa kufanya ili kumpa furaha lakini kutokana na hali ilivyokuwa nyumbani hapo alishindwa kabisa.
Alimuelewesha lakini msichana huyo hakutaka kuelewa hata kidogo, alichokuwa akikitaka ni kuona Juliana anakufa haraka sana mahali popote pale atakapokuwa.
Juliana hakuwa na furaha, moyo wake ulikuwa umeumia kupita kawaida, alilia usiku na mchana, alikuwa kwenye mateso makali, kansa ilimuumiza, wakati akiyaugulia maumivu hayo, upande mwingine mtoto wake alikuwa mgonjwa.
Hakujua amlilie nani, hakujua sababu ya Mungu kuamua kumuadhibu kwa namna hiyo. Hakuwa na raha, hakula chakula chochote kile, kila wakati alikuwa mtu wa kusikitika na kumuuliza Mungu kwa nini yeye?
Japokuwa alikuwa nyumbani lakini kila siku asubuhi alikuwa hospitalini kwa ajili ya kumuona mtoto wake, Jesca. Kila alipokuwa akimuona kitandani, alihisi moyo wake kuwa kwenye maumivu makali, hakupenda kumuona katika hali hiyo, ilimuumiza mno kiasi kwamba wakati mwingine alihisi kama angepata ugonjwa wa presha.
“Mungu! Naomba usimchukue mtoto wangu, itaniuma sana Mungu,” alisema Juliana huku machozi yakimtoka, wakati huo alikuwa mbele ya kitanda alicholala mtoto wake, kwa jinsi alivyokuwa kimya kitanani pale, alionekana kama tayari alikwishafriki dunia.
“Mke wangu! Acha kulia, Jesca atapona tu,” alisema Gideon huku akimwangalia mke wake.
“Inaniuma! Kwa nini Mungu anataka kumchukua mtoto wangu? Ninamuhitaji, yeye ni faraja yangu, yeye ni kila kitu kwangu,” alisema Juliana huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.
“Usilie mke wangu! Ninaamini Mungu atafanya jambo,” alisema Gideon.
Alijaribu kumfariji sana mke wake lakini mwanamke huyo hakufarijika, kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, kila alipomuona mtoto wake kitandani pale, moyo wake ulichoma na kuchoma.
Siku zikakatika, baada ya siku tatu ndipo Jesca akarejewa na nguvu na kuanza kuzungumza tena. Kila mmoja alifurahi, nyuso zao zikatawaliwa na tabasamu pana, kwao, kwa kile kilichokuwa kimetokea ilikuwa kama muujiza fulani mkubwa.
“Unajisikiaje?” aliuliza Juliana huku akimwangalia mtoto wake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tumbo linauma mama!”
“Pole sana! Mungu ni mponyaji, atakuponya tu,” alisema Juliana huku akimwangalia mtoto wake.
“Kweli mama?”
“Ndiyo! Unakumbuka mwalimu wa Sunday School alisemaje?”
“Mungu ni mponyaji!”
“Basi jua atakuponya tu!”
Julieth alikasirika, moyo wake uliuma mno, hakuamini kama mwanaume ambaye kila siku alisema kwamba alimpenda kwa moyo wa dhati hakufanya kile alichokuwa amemwambia.
Moyo wake ulichoma, alichohitaji ni kumuona Juliana akifa haraka iwezekanavyo ili yeye aende ndani ya jumba la kifahari na kuishi na Gideon.
Kila siku masikio yake yalikuwa katika simu yake, alitaka kusikia kama mwanamke huyo alikufa au la. Siku zilikatika lakini kila alipopigiwa simu alisalimiwa na kuambiwa kwamba bado mauaji hayakuwa yamefanyika.
Alichukia, alimlaumu Gideon na kumwambia kwamba hakuwa akimpenda na ndiyo maana hakumfurahisha kwa kufanya kile alichokitaka kifanyike haraka iwezekanavyo.
Alivyoona kwamba Gideon ameshindwa kabisa kumuua kwa kumchoma kisu, akaomba kuonana naye kwani kuna kitu alitaka kumpa ambacho aliamini kuwa kingemfanya kuifanya kazi ile kwa urahisi zaidi.
Wakapanga sehemu na muda, walipoonana, msichana huyo akampa sumu ya cyanide na kumwambia kwamba alipaswa kumuwekea kwenye chakula kwani kumchoma kisu tu alishindwa.
“Haina shida! Sasa hivi utafurahi na moyo wako,” alisema Gideon huku akiichukua sumu hiyo.
Moyo wake ulibadilishwa na msichana huyo, aliona kabisa akiwa na chuki kali dhidi ya mke wake wa ndoa, alimuahidi kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kumuua Juliana ilimradi tu aishi na Juliet.
Akaondoka huku akiahidi kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima amuwekee sumu Juliana na kufariki dunia.
Alipokuwa njiani, akili yake ilikuwa ikifirikiria ni kwa jinsi gani angetimiza kile alichokuwa ameambiwa.
“Nitamuua hata leo hii!” alisema Gideon huku akiwa njiani kuelekea nyumbani.
Hakuchukua muda mrefu akafika nyumbani kwake, akalipaki gari sehemu ya maegesho na kuelekea ndani.
Alipofika sebuleni, akapigwa na mshangao baada ya kumuona Jesca akiwa nyumbani.
Ilikuwa ni kama sapraizi kwake kwani tangu alipoondoka nyumbani hapo mtoto huyo alikuwa hospitalini. Alibaki akiwa ameduwaa, Juliana na Jesca wote walikuwa kwenye nyuso zenye tabasamu huku wakimwangalia.
“Dad!” aliita Jesca huku akiwa na tabasamu pana.
“We wanted to surprise you!” (tulitaka tukusapraizi) alisema Juliana huku akimwangalia mume wake.
“Well, you succeeded,” (Vizuri, mmefanikiwa) alisema Gideon huku akiwafuata.
Tangu mke wake alipoanza kuumwa, siku hiyo alimuona mke wake kuwa tofauti kabisa, tabasamu alilokuwa akilionyesha usoni mwake lilionyesha kabisa kwamba mwanamke huyo alikuwa na penzi la kweli kwake.
Akabaki akiwa amesimama huku macho yake yakiwaangalia wote wawili. Wakati akiwa anaendelea kufikiria mambo mengi kuhusu mke wake, Jesca akasimama, akamfuata na kumkumbatia.
“Dad! Come back to us pleseee,” (baba! Turudie tafadhali) alisema Jesca huku akianza kulia.
Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, hakujua kama mtoto wake huyo alijua kilichokuwa kikiendelea au la. Ghafla, katika hali ambayo hata yeye mwenyewe aliishangaa, mwili wake ukaanza kutetemeka na kijasho chembamba kuanza kumtoka.
Aliguswa moyoni mwake, alimshika mtoto wake huku akimwangalia mke wake aliyekuwa kochini, bado tabasamu pana lilikuwa likionekana usoni mwake.
Hapo ndipo akaanza kujiuliza juu ya kile kilichokuwa kimetokea, kwa nini alitaka kumuua Juliana? Kulikuwa na ubaya wowoote aliomtendea mpaka kutaka kuchukua hatua ngumu kiasi hicho.
Wakati akijiuliza hivyo, kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma kabisa tangu siku ambayo alikutana na msichana huyo, alivyokuwa akimuhitaji na mwisho wa siku kufanikiwa kuwa naye na kumuoa.
Upendo wote ulikwenda wapi? Yaani kipi kilimfanya mpaka kuchukua uamuzi wa kukubaliana na Juliet kumuua mke wake? Kuna baya alilomtendea? Kama hakuna, kwa nini aliamua kukubaliana na msichana huyo?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati akijiuliza yote hayo, akaanza kumfikiria mtoto wake. Hii ilimaanisha kwamba kama angemuua Juliana mtoto Jesca angebaki akiwa hana mama. Nani angempa mapenzi yale aliyokuwa akiyapata kutoka kwa mama yake? Juliet angeweza? Msichana huyo alikuwa na umri mdogo, binti mbichi, je, angeweza kuishi na Jesca na kumpa mapenzi yote ambayo mke wake alikuwa akimpa?
Miguu yake ikaanza kuishiwa nguvu, akakaa kwenye kochi, mashavu yake yalilowanishwa na machozi, aliumia, alijiona kuwa mkosaji kwani mke wake huyo hakuwa amemkosea kitu chochote kile zaidi ya kumwambia kwamba kila siku alitamani kumuona akiwa na furaha tele.
“Nisamehe mke wangu!” alisema Gideon huku akisimama na kumfuata mke wake.
Juliana hakujua kilichokuwa kikiendelea, alimwangalia mume wake huku akiwa na maswali mengi juu ya sababuu iliyomfanya kulia namna ile.
Alipomfikia, wakakumbatiana.
“Nilitaka kukuua!” alisema Gideon, hakuwa na jinsi, alimwambia ukweli mke wake kwamba alitaka kumuua kwa kuwa tu alikuwa na tamaa ya kuwa na mwanamke mwingine.
Juliana ilimuuma lakini hakuwa na la kufanya, alifurahi kwa sababu tu mume wake alijiweka wazi, kwa jinsi alivyokuwa akilia ilionyesha ni kwa jinsi gani alikuwa ameumia kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Akamuomba msamaha mke wake, alimwambia kwamba shetani alikuwa amemuingia na ndiyo maana alifanya maamuzi ya kijinga ya kutaka kumuacha na kumchukua mwanamke mwingine.
“Nimekusamehe mume wangu kama tu umeligundua kosa lako,” alisema Juliana huku akimwangalia mume wake huyo aliyekuwa akibubujikwa na machozi.
Akasimama na kumkumbatia, moyo wake ukaridhika, akajisikia amani, hakutaka kachana na Juliet hivihivi, alichokifanya ni kumpigia simu na kumwambia kwamba aliifanya kazi aliyokuwa amempa na hivyo alitaka kuonana naye katika Hoteli ya Lion kwa ajili ya kuzungumzia maisha yao ambayo yangeendelea baada ya kumuua mke wake.
“Umemuua kweli?” aliuliza msichana huyo kwenye simu.
“Ndiyo! Tuonane tuzungumzie maisha yetu mapya,” alisema Gideon.
“Sawa. Nakupenda sana mume wangu! Nakupenda sana kwa kunisikiliza,” alisema Juliet na simu kukatwa.
Alipanga mipango na mke wake, japokuwa hakuwa katika hali nzuri lakini alimuomba kujikaza kwani alitaka kumpeleka huko hotelini kuonana na Juliet, msichana aliyetaka afe kwa gharama yoyote ile.
Kwa kuvumilia maumivu, Juliana akakubaliana na mumewe, wakaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika hoteli hiyo ambapo akachukua chumba na kwenda na mkewe.
Wakatulia huko, muda mwingi alikuwa akimpigia simu Juliet kwa lengo la kumsisitiza kwamba alitakiwa kuonana naye haraka sana. Hilo halikuwa tatizo, baada ya dakika ishirini, msichana huyo akafika na kwenda ndani ya chumba hicho alichoambiwa kwamba Gideon alikuwepo akimsubiri.
Alipoingia na macho yake kutua kwa mwanaume huyo, akamfuata na kumkumbatia kwa furaha. Gideon hakuonyesha tofauti yoyote ile, naye akamkumbatia huku mke wake, Juliet akiwa bafuni akisubiri muda wa kuambiwa atoke.
“Hongera sana kwa kazi nzito!” alisema Juliet huku akiachia tabasamu.
“Nashukuru! Ila ningependa kwanza nikwambie kitu kimoja,” alisema Gideon.
“Kitu gani hubby?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ninampenda mke wangu!” alisema Gideon.
“Unampenda mke wako? Kashakufa tayari! Tuanze maisha mapya hubby!” alisema Juliet.
“Hapana! Mke wangu hajafa.”
“Hajafa?”
“Juliet! Ninampenda mke wangu. Hujui tulipotoka, nilimpenda kwa kipindi kirefu sana, tangu tulipokuwa shuleni. Nilikuwa masikini, mwanamke yule alinipenda hivyo hivyo, sikuwa na kitu, alinionyeshea mapenzi ya dhati. Nilimthamini sana.
Uliponiambia nimuue, nilikubaliana nawe, sikukumbuka kitu chochote kile kuhusu mimi na yeye,” alisema Gideon na kuendelea:
“Ni mwanamke mzuri, hajawahi kunikosea, ananipenda. Juliet! Mke wangu ni mke mwema, sikuweza kumuua mwanamke yule, ni mzuri sana, mcha Mungu! Nitamuua vipi? Siwezi!
Nikwambie tu Juliet, ninampenda mke wangu, ninampenda sana, haijalishi ni mgonjwa, ninampenda mno, ninampenda kwa kiasi kwamba siwezi kuelezea. Kama ulitarajia nimuue, hicho ni kitu ambacho hakiwezi kutokea, siwezi kumuua mwanamke ninayempenda toka moyoni mwangu,” alisema Gideon huku machozi yakimtiririka mashavuni mwake.
Juliet alivimba kwa hasira, hakuamini kile alichokisikia, alimwamini Gideon na kuona kwamba angefanya kile alichomwambia akifanye lakini matokeo yake akamwambia kwamba hakukifanya kwa kuwa tu alikuwa akimpenda mke wake.
Hata kabla msichana huyo hajasema kitu chochote, Gideon akasimama na kwenda kuufungua mlango wa bafu na Juliana kutoka. Kama ilivyokuwa kwa mumewe, hata na yeye machozi yalikuwa yakimtiririka mashavuni mwake kwani alikuwa akisikia kila kitu kilichokuwa kikiendelea huko.
“Juliet! Mwangalie mke wangu, angalia uzuri wake, huyu mwanamke ana moyo wa chuma, ni mwanamke ambaye kila mwanaume duniani anatamani kuwa naye. Unawezaje kumuua mwanamke kama huyu? Hakuna mwanaume kichaa wa kufanya hivyo, kila mmoja anatamani kuwa na mtu kama Juliana,” alisema Gideon na kuendelea:
“Juliet! Ninampenda mno mke wangu, ni mrembo, sikuwahi kuukupenda, sikuwahi kupenda mwanamke zaidi ya huyu, wewe nilikutamani tu, ukweli sikuwahi kukupenda hata siku moja moyoni mwangu! Nilikutamani tu Juliet,” alisema Gideon.
Juliet alishindwa kuvumilia, akasimama kutoka pale alipokuwa amekaa, akaufuata mlango, akaufungua na kutoka ndani ya chumba hicho.
Moyo wake ulisikia maumivu makali, hakuamini kama kwa kipindi chote hicho alichokuwa na mwanaume huyo kumbe hakuwahi kumpenda zaidi ya kumtamani tu.
Gideon hakujali, akamwangalia mke wake usoni na kumwambia kwa mara nyingine tena kwamba alikuwa akimpenda mno na kamwe asingeweza kufanya ujinga kama alioufanya kipindi hicho. Akamkumbatia na kumpiga mabusu mfululizo mashavuni mwake na baada ya dakika kadhaa, wakaondoka hotelini hapo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Maisha yakabadilika, mapenzi yakarudi, wakapendana zaidi, Gideon akawa karibu na mkewe, akamfanyia mambo mengi kama mkewe mpaka pale miaka mitano ilipokatika na mwanamke huyo kufariki dunia kwa ugonjwa wa kansa iliyokuwa ikimtesa kwa miaka mingi.
Juliana akabaki kichwani mwa Gideon, alimthamini na kila wiki ilikuwa ni lazima kwenda katika kaburi la mke wake na kukaa pambeni kama kumuenzi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment