Simulizi : Dead Love ( Penzi Lililokufa )
Sehemu Ya Tatu (3)
“Aaah... eeeh unajua...” alibabaika msichana huyo huku akionesha wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wake.
“Nimeshakwambia mimi ni rafiki yako na usinifiche kitu chochote, nakuomba sana kuwa huru kuzungumza na mimi,” alisema Abdallah huku akiendelea kumtazama Karen kwa macho ya huruma.
Awali alihisi huenda msichana huyo alikuwa na tabia mbaya ya kupenda sana wanaume ndiyo maana aliishia kuwa changudoa lakini maelezo hayo aliyompa ya jinsi alivyojikuta akiingia kwenye biashara hiyo, yalimfanya aanze kumtazama kwa macho ya huruma.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Karen alishusha pumzi ndefu na kuinua uso wake ambao muda wote alikuwa ameuinamisha, akamtazama Abdallah huku michirizi ya machozi ikiwa imejichora kuanzia kwenye macho yake kushuka mashavuni, kuonesha kwamba alikuwa akilia.
“Sijawahi kwenda kupima Ukimwi na siwezi kufanya hivyo hata siku moja.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Mwenyewe najua mapito niliyopitia, siwezi kuwa salama labda kwa kudra za Mwenyezi Mungu, isitoshe sijajiandaa kupokea majibu mabaya, naweza kufa kwa mawazo bure,” alisema msichana huyo na kusababisha mapigo ya moyo wa Abdallah yalipuke na kuanza kumwenda kasi kuliko kawaida.
Kwa tafsiri nyepesi, kama msichana huyo alikuwa ‘ameukanyaga’, na yeye alikuwa tayari ameambukizwa kwani walipokutana kimwili hawakutumia kinga na kama iliwezekana kwa gonjwa la zinaa kumpata, isingeshindikana kwa Ukimwi.
“Sasa kama ulikuwa unajijua kwamba haupo salama, kwa nini tulipofanya mapenzi hukutaka tutumie kinga?”
“Jamani Abdallah, unanilaumu bure. Kwani kati ya mwanaume na mwanamke nani anayetakiwa kuamua kutumia kinga au kutotumia?”
“Ni wajibu wa kila mmoja, tena kama wewe ndiyo ulitakiwa unitahadharishe mapema kwamba nitumie kinga kwa sababu wewe unakutana na wanaume wengi.”
“Hata wenzako watakushangaa, maisha haya unaweza kukutana na mwanamke hujui historia yake halafu ukaingia kichwakichwa bila kinga? Wanaofanya hivyo ni wale waliojikatia tamaa ya maisha lakini kwa kijana mwenye ndoto nyingi kama wewe, huo ni upumbavu wa hali ya juu.”
“Kwa hiyo mimi mpumbavu?”
“Sikia Abdallah, kama lengo la kunitafuta usiku huu ni kuja kunibebesha mzigo wa lawama, basi niache niondoke zangu, inaonekana huna lengo la kunisaidia na najuta sijui kwa nini nimekwambia ukweli wa maisha yangu,” alisema Karen huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara kwenye uso wake, akainuka na kuanza kutembea harakaharaka kuelekea mlangoni akitaka kufungua na kuondoka.
Japokuwa ilikuwa ni usiku wa manane msichana huyo hakujali chochote, akawa anataka kuondoka. Abdallah aliyajua makosa yake, haraka akainuka na kwenda kumshika mkono huku akimsihi apunguze jazba na waendelee kuzungumza.
Kwa kuwa alikuwa na uwezo mkubwa wa kumbembeleza mwanamke hata pale anapokasirika, Abdallah alifanikiwa kumtuliza msichana huyo, akarudi na kukaa, mazungumzo yakaendelea.
“Siku ile nilipoenda kupima na kukutwa na ugonjwa wa zinaa, daktari alishauri kwamba nikuchukue na wewe ukaendelee kutibiwa.”
“Siwezi kwenda hospitali Abdallah, kama kweli nina gonjwa la zinaa nasubiri dalili zianze kuonekana kisha nitaenda duka la madawa kununua dawa zangu ambazo nazijua mwenyewe, sina haja ya kwenda hospitali,” alisema msichana huyo na kusababisha Abdallah aishiwe cha kuzungumza.
Ukimya mrefu ulipita kati yao, Abdallah akijilaumu ndani ya nafsi yake kwa kumuamini msichana huyo bila kumjua kwa undani na kujikuta akifanya naye mapenzi bila kinga. Karen naye aliendelea kuwaza yake, huku akijiuliza kama kweli kijana huyo mtanashati alikuwa na lengo la kumsaidia au alikuwa anamchora.
“Muda unazidi kwenda Abdallah, naomba uniache mi niende zangu kwangu.”
“Hapana Karen, huwezi kwenda sehemu yoyote. Hustahili kuishi aina ya maisha unayoishi, hebu simama na ujitazame pale kwenye kioo jinsi ulivyo mrembo! Hukuzaliwa kuja kuwa changudoa Karen,” alisema Abdallah kwa sauti iliyojaa hisia nzito.
Bila aibu msichana huyo akasimama na kusogea kwenye kioo kilichokuwa pale sebuleni, akavua kitenge alichokuwa amejifunga na kubakia na kinguo chake kilichoyaacha wazi mapaja yake, alichokuwa amekivaa akiwa kwenye biashara yake ya uchangudoa.
“Hahaa! Kwani mi mzuri eeh?” alisema Karen huku uso wake ukijawa na tabasamu la ghafla, alijishika kiuno na kuanza kujigeuzageuza pale kwenye kioo huku akiendelea kutabasamu.
Japokuwa Abdallah alikuwa kwenye dimbwi la mawazo machungu, moyo wake ukiwa na hofu kubwa kwamba ameambukizwa Virusi vya Ukimwi na msichana huyo, alijikuta akitabasamu.
“Hebu niwashie muziki nikuoneshe ninavyojua kucheza,” alisema msichana huyo huku akionesha kufurahishwa sana na maneno aliyoambiwa na Abdallah ya kumsifia kwamba yeye ni mrembo kwani hakuwa akikumbuka mara ya mwisho aliambiwa lini maneno mazuri kama hayo.
Abdallah aliinuka na kwenda kumuwashia redio yake ya kisasa iliyokuwa pale sebuleni, akamuwekea CD iliyokuwa na wimbo wa mwanamuziki mahiri wa nchini Marekani, Beyonce Knowles uitwao Single Lady kama mwenyewe alivyokuwa ameomba.
Japokuwa ilikuwa tayari ni usiku sana na watu wengi walikuwa wamelala, Karen alianza kuonesha umahiri mkubwa wa kucheza wimbo huo mithili ya Beyonce mwenyewe huku akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake. Usingeweza kuamini kwamba wawili hao muda mfupi uliopita, walikuwa kwenye mvutano mkubwa kila mmoja akisimamia msimamo wake.
Baada ya wimbo huo kuisha, Karen alimshukuru Abdallah kwa kumkumbatia na kumbusu huku akiendelea kuchekacheka.
“Sasa mimi nitalala wapi?”
“Utalala na mimi chumbani kwangu.”
“Huogopi kulala na changudoa? Nitakuambukiza tena ngoma,” alisema msichana huyo na kuachia kicheko cha chinichini kilichomfanya Abdallah aanze kubadilika kihisia. Ile hofu aliyokuwa nayo iliyeyuka kama theluji iyeyukavyo juani, alishaamua liwalo na liwe kwani kama ni maji yalishamwagika, akamshika kiuno na kufungua mlango wa chumbani, wakaingia wote na kuubamiza mlango nyuma yao
Muda mfupi baadaye, wote walikuwa kama walivyotoka kwenye matumbo ya mama zao, kila mmoja akionekana kuelea kwenye hisia nzito za huba. Kama ilivyokuwa mara ya kwanza walipokutana, ufundi mkubwa aliokuwa nao Karen ulimfanya Abdallah ajihisi kama yupo kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akawa anatoa miguno ya hapa na pale wakati mikono laini ya msichana huyo ikivinjari taratibu na kwa ufundi mkubwa kwenye mwili wa Abdallah, huku akimwagia mvua ya mabusu ya hapa na pale. Pumzi zikawa zinamtoka nusunusu.
Msichana huyo aliendelea na manjonjo yake huku Abdallah akizidi kuwa taaban lakini ghafla kijana huyo alishtuka kama mtu aliyekuwa usingizini na hisia zake zikazima kama mshumaa uzimavyo gizani kwenye upepo mkali.
“Vipi?” aliuliza Karen kwa sauti ya kunong’ona, Abdallah ikabidi avunge kwamba alikuwa ameanza kupitiwa na usingizi ndiyo maana ameshtuka kiasi hicho.
“Basi tulia mpenzi wangu, umenifurahisha sana kwa jinsi ulivyoonesha kunijali kwa siku ya leo, nataka nikupe zawadi ya penzi tamu kama shukrani kwako kwani hajawahi kutokea mtu mwenye moyo kama wako kwenye maisha yangu,” alisema Karen huku akiendelea na vituko vya hapa na pale.
Hata hivyo, licha ya kuendelea na manjonjo ya hapa na pale na kumchombeza kwa maneno matamu, Abdallah hakuzama tena kwenye hisia za mapenzi, sanasana mapigo ya moyo yaliendelea kumwenda mbio huku kijasho chembamba kikimtoka.
Kilichomshtua akiwa amezama kwenye hisia nzito za mapenzi, ni pale alipokumbuka kwamba msichana huyo aliyekuwa akikaribia kufanya naye mapenzi, ndiye aliyemuambukiza ugonjwa wa zinaa ambao mpaka muda huo ulikuwa bado haujapona na alikuwa akiendelea kutumia dozi.
Alikumbuka pia kwamba muda mfupi uliopita, alitoka kumshuhudia msichana huyo akiwa anafanya biashara haramu ya kuuza mwili wake, hisia kwamba Karen alikuwa na Virusi vya Ukimwi ndizo zilizokizonga kichwa chake na kumtoa kwenye hisia tamu za mapenzi alizokuwa akiogelea ndani yake.
“Jamani vipi tena? Mbona hutulii,” Karen alimuuliza Abdallah baada ya kuona bado anaendelea kuhangaika, ikabidi aendelee kumdanganya na kuficha kilichokuwa kikipita ndani ya kichwa chake.
“Basi twende ukaoge kwanza huenda ukarudi kwenye hali yako ya kawaida,” alisema msichana huyo na kuinuka, akachukua taulo moja na kujifunga kisha akampa lingine Abdallah na kuelekea pamoja bafuni huku akiendelea kumfanyia vituko vya hapa na pale vya kimahaba.
Hata hivyo, bado ilikuwa ni sawa na kazi bure, licha ya msichana huyo kuoga naye na kuendelea kumfanyia mashamsham ya mapenzi, hisia za Abdallah hazikuweza kurudi kabisa. Kila mara alikuwa akivuta picha kichwani mwake na kujiona akiwa amedhoofika na kubaki mifupa mitupu kutokana na kushambuliwa na Virusi vya Ukimwi.
Wakarudi chumbani ambapo ilibidi Abdallah amuombe apumzike kidogo kisha wataendelea na walichokusudia kukifanya. Kwa kuwa muda ulikuwa umeenda sana na kila mmoja alikuwa amechoshwa na pilikapilika za usiku huo, walipolala walipitiwa na usingizi mzito.
Abdallah ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzinduka kutoka usingizini na kujikuta akiwa amelala na Karen, tena wakiwa wamegandana kama ruba. Alijaribu kuvuta kumbukumbu zake kama hawajakutana kimwili na alipojiridhisha, aliamka na kuelekea bafuni.
Huku nyuma, Karen naye aliamka na kukaa kitandani. Abdallah alipotoka bafuni, walisalimiana kisha msichana huyo naye akaenda kuoga. Huku nyuma, Abdallah alijiandaa harakaharaka kwani hakutaka kabisa kufanya tena mapenzi na msichana huyo, bado hofu ya kuambukizwa Virusi vya Ukimwi ilikuwa ikikitesa kichwa chake.
“Naenda kazini mara moja, naomba usiondoke nikukute hapahapa,” alisema Abdallah huku akimalizia kujiandaa. Msichana huyo ilibidi akubaliane naye kwani ilionesha kwamba ana nia ya dhati ya kumsaidia, ukizingatia kwamba na yeye hakuwa akiyapenda maisha ya kujiuza kutokana na hatari alizokuwa akikutana nazo kila kukicha.
Abdallah alienda kudanganya kazini kwao kwamba amepata dharura, akapewa ruhusa na kuahidi kurudi muda mfupi baadaye. Akilini mwake alikuwa akifikiria jambo moja tu, kwenda na msichana huyo hospitali ili wote wawili wakapime afya zao.
“Nikijikuta nimeshaathirika, nitajiua hata kwa kujirusha ghorofani lakini kama nipo salama na yeye yupo salama, nitambadilisha sana mpaka watu watashangaa, nataka aje kuwa mke wangu,” aliwaza Abdallah wakati akiwa kwenye bodaboda, akirudi nyumbani huku mkononi akiwa amebeba vitafunwa kwa ajili ya kwenda kupata kifungua kinywa.
Hata hivyo, hakujua ni mbinu gani anayoweza kuitumia ili msichana huyo akubali kupima kwa hiyari yake. Muda mfupi baadaye, alikuwa tayari ameshawasili nyumbani kwake na kumkuta Karen akimsubiri.
Baada ya kupata kifungua kinywa pamoja, Abdallah alianza kuingiza mistari yake kujaribu kumshawishi msichana huyo akubali kwenda kupima Virusi vya Ukimwi na kutibiwa gonjwa la zinaa ambalo bado alikuwa nalo.
Hata hivyo, kama mwenyewe alivyokuwa amehisi, haikuwa kazi nyepesi kumshawishi msichana huyo akubali. Ilimchukua zaidi ya saa tatu kumbembeleza huku akimuahidi kuwa hata akikutwa ameambukizwa, atamtunza na kuishi naye pamoja kwenye nyumba yake.
Baadaye msichana huyo alikubali kwa shingo upande, wote wakajiandaa kisha Abdallah akampa suruali yake na tisheti avae kwani hakuwa na nguo anazoweza kuzivaa mchana barabarani, zile alizokuja nazo jana yake zilikuwa maalum kwa kazi ya uchangudoa.
Wakatoka na kuelekea Hospitali ya Marie Stopes huku msichana huyo akionekana kuwa tayari kwa lolote. Hali ilikuwa mbaya kwa Abdallah ambaye alikuwa akitetemeka mno na kujiapiza kuwa akikutwa na ngoma, ni bora ajiue kuliko kuteseka kwa kukonda na kudhoofika.
Walipofika hospitalini, waliingizwa kwanza kwenye chumba maalum cha ushauri nasaha ambapo walikutana na mtaalamu wa kazi hiyo aliyefanikiwa kwa kiasi kikubwa kumtuliza Abdallah mpaka akawa tayari kupokea majibu ya aina yoyote.
Wote wawili walichukuliwa vipimo na kupelekwa sehemu maalum ya kusubiria majibu, wakakaa huku kila mmoja akiwa kimya kabisa. Abdallah alionesha kuwa mbali mno kimawazo kiasi cha kuyafanya macho yake yabadilike rangi na kuwa mekundu. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Majuto makubwa yalikuwa yakimuandama kwa kukubali kufanya mapenzi na msichana huyo bila kinga mara ya kwanza walipokutana bila kujua kwamba mwenzake alikuwa changudoa.
Baada ya dakika kadhaa, wote wawili waliitwa kwenye chumba cha ushauri nasaha ambapo swali la kwanza waliloulizwa na yule daktari waliyemkuta, ilikuwa ni kama wanataka kupewa majibu yao kwa pamoja au kila mmoja anataka kupewa majibu yake peke yake.
Abdallah na Karen walijadiliana kidogo kisha wakafikia muafaka kwamba wapewe majibu yao kwa pamoja, mapigo ya moyo ya kila mmoja yakaanza kwenda mbio kuliko kawaida.
“Dokta ngoja kwanza nakuja, naenda toilet mara moja,” alisema Karen huku akionesha kuchanganyikiwa mno, japokuwa kiyoyozi kilikuwa kikipuliza kwa sana ndani ya ofisi hiyo, msichana huyo alikuwa akitokwa na kijasho chembamba.
Msichana huyo aliposimama, Abdallah naye alisimama kwa madai kwamba anamsindikiza, Karen akajaribu kukataa lakini Abdallah ambaye naye alikuwa akitetemeka, akawa king’ang’anizi. Wakatoka wote na kuelekea kwenye korido ya kuelekea chooni.
“Nahisi kama moyo wangu unataka kusimama,” Karen alisema huku akijipepea kwa mkono wake.
“Hata mimi najisikia vibaya sana, hata sijui itakuwaje.”
“Kwa nini tusiondoke tuachane na hayo majibu tutakuja kupima siku nyingine tukiwa tumejiandaa,” Karen alijaribu kumuingizaAbdallah kwenye mtego lakini kijana huyo akashikilia msimamo, akasema kama ni maji tayari walishayavulia nguo hivyo hawana budi kuyaoga.
Karen alijaribu kumshawishi Abdallah lakini alipoona amekuwa mgumu kukubaliana naye, hakuwa na ujanja zaidi ya kukubali kurudi kwenye chumba cha ushauri nasaha kwa ajili ya kuchukua majibu yao.
Hata chooni hawakufika tena, wakarudi ambapo walimkuta daktari akiwa amekaa palepale walipomuacha, karatasi za majibu zikiwa mkononi mwake.
“Mbona mnaonekana hamjiamini jamani? Eeeh! Kaeni chini mtulie,” alisema daktari huyo huku tabasamu likiwa limeupamba uso wake, angalau mioyo ya Abdallah na Karen ikatulia kwani kwa ilivyoonesha, hakukuwa na majibu mabaya vinginevyo daktari asingetabasamu.
Walikaa huku kila mmoja akivuta na kutoa pumzi ndefundefu, daktari akawatazama mmojammoja kisha akauliza aanze kutoa majibu ya nani.
“Ladies first!” (Wanawake kwanza) Abdallah alidakia na kusababisha daktari acheke, akajiweka vizuri kitini na kuanza kusoma majibu ya Karen. Kabla hata hajamaliza kuyasoma, Karen aliruka pale kwenye kiti alichokuwa amekaa na kusimama, akamkumbatia Abdallah kwa nguvu huku akipaza sauti:
“Siamini! Siamini kama sijaukanyaga,” alisema huku akirukaruka kwa furaha akiwa haamini kabisa. Kwake huo ulikuwa ni zaidi ya muujiza, kukutwa yupo ‘HIV Negative’? Hakuyaamini masikio yake.
“Lakini pamoja na kuwa huna maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, inaonesha una ugonjwa sugu wa zinaa ambao inatakiwa ukitoka hapa ukaanze kutumia dozi nitakayokuandikia kwa siku saba bila kukosa hata siku moja,” alisisitiza daktari, Karen akawa anaendelea kufurahi.
Ilifika zamu ya Abdallah ambapo kama ilivyokuwa kwa Karen, naye majibu yalionesha kuwa ni ‘HIV Negative’ yakimaanisha alikuwa salama dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi. Tofauti na Karen, Abdallah alipopewa majibu hayo, alianza kuangua kilio mpaka akapiga magoti chini.
“Ahsante Mungu kwa kuniokoa, Alhamdulillah,” alisema huku akiinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu. Aliendelea kulia kwa dakika kadhaa huku machozi yakimtoka kwa wingi kama chemchemi ya maji.
“Tuko salama baba, inuka unikumbatie,” alisema Karen huku akimshika Abdallah na kumuinua pale chini, wakakumbatiana kwa nguvu huku Abdallah akiendelea kulia. Baada ya kutulia, daktari aliwakalisha chini na kuanza kuwapa ushauri wa jinsi ya kuishi maisha salama.
“Kila mmoja ajitahidi kuwa mwaminifu kwa mwenzake, siku hizi dunia imeharibika sana, ni rahisi sana kupata maradhi, mkishindwa basi tumieni kinga,” alisema daktari huyo kisha akamuandikia Karen dawa za kutumia kutibu ugonjwa wake uliokuwa ukimtafuna ndani kwa ndani.
Walitoka mpaka nje ya hospitali hiyo, kila mmoja akiwa haamini kama wamenusurika kutoka kwenye mdomo wa mamba. Wakakumbatiana tena na kubusiana midomoni. Hawakuwa na muda wa kupoteza, walikodi Bajaj iliyowarudisha mpaka Mikocheni ambapo walipofika, jambo la kwanza ilikuwa ni Karen kuanza kutumia dozi aliyopewa.
“Nisamehe sana Abdallah kwa yote yaliyotokea, najua siku ya leo ilikuwa ngumu sana kwako lakini nashukuru Mungu mpaka sasa hivi roho ya kila mmoja imetulia. Nakushukuru kwa kunionesha nuru maishani mwangu,” alisema msichana huyo baada ya kutoka kuoga na kumkuta Abdallah akiandika jambo kwenye kitabu chake cha kumbukumbu (diary).
“Usijali Karen, naomba ukae tuzungumze,” alisema Abdallah huku akifunga diary yake, akashusha pumzi ndefu na kumuangalia msichana huyo ambaye kwa muda huo alikuwa amejifunga khanga moja tu akitokea kuoga.
Akakaa na mazungumzo yakaanza ambapo Abdallah alimueleza ukweli kwamba aliamua kumfuatilia ili aujue ukweli wake kwa sababu alitokea kumpenda sana na hakuwa tayari kumpoteza.
“Nakupenda sana Karen na nakuomba ukubali kutulia na mimi, nitakupa kila unachokitaka lakini sitaki urudie kazi yako ya uchangudoa,” alisema Abdallah kwa hisia nzito, msichana huyo akawa anatingisha kichwa kumkubalia alichokuwa anakisema.
“Hata mimi nimekuwa mjinga kwako kwa sababu nakupenda Abdallah, nashukuru Mungu afya zetu zipo salama, nakupenda sana na nipo tayari kutulia na wewe,” alisema msichana huyo kwa sauti ya upole, akasimama na kumshika mkono Abdallah na kumuinua, wakakumbatiana na kugusanisha ndimi zao.
Taratibu wakaanza kukokotana kuelekea chumbani huku wakiendelea kumwagiana mvua ya mabusu, kila mmoja akionesha kuzama kwenye dimbwi la mahaba ya dhati.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nakupenda sana Karen, nataka kuyabadilisha maisha yako.”
“Nakupenda pia Ibra, nashukuru kwa kunionesha njia,” alisema msichana huyo kwa sauti iliyokuwa ikitokea puani, mapigo ya moyo ya kila mmoja yalikuwa yakienda kasi mno huku kila mmoja akionekana kuukamia mpambano huo usiokuwa na jezi.
Dakika chache baadaye, kilichokuwa kinasikika ndani ya chumba hicho, ilikuwa ni sauti za miguno ya hapa na pale wakati wawili hao wakiogelea kwenye bahari yenye kina kirefu cha huba.
Kazi ilikuwa moja tu siku hiyo, kila baada ya mapumziko mafupi, wawili hao walikuwa wakirejea tena dimbani mpaka wakawa hoi. Siku hiyo ilikuwa ya kipekee mno kwao kwani walifanikiwa kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wao.
Abdallah hakuweza tena kurejea kazini, siku nzima walishinda ndani mpaka kesho yake ambapo kama kawaida, Abdallah alijiandaa kwa ajili ya kuelekea kazini huku akimkabidhi msichana huyo fedha za matumizi.
Karen alimshukuru sana Abdallah, wakaagana vizuri na kijana huyo akatoka kuelekea kazini huku akiwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake kwani sasa alikuwa na uhakika wa afya yake na mapenzi ya dhati kutoka kwa Karen.
Kazini hakukaa sana kwani muda wote alikuwa akimfikiria Karen. Kwa mara nyingine akatunga uongo na kuomba ruhusa, akaondoka bila kumpa taarifa yoyote Karen kwa lengo la kwenda kumfanyia ‘sapraiz’.
Hata alipofika nyumbani kwake, hakupiga hodi bali alifungua mlango kimyakimya na kunyata kuingia ndani kwa lengo la kumfurahisha mpenzi wake huyo. Hata hivyo, alipoangaza macho sebuleni hakumuona, ikabidi aelekee chumbani ambapo alipofungua mlango, alijikuta akipigwa na butwaa kubwa kutokana na alichokiona.
“Karen! Karen,” alisema Abdallah huku akiharakisha kumuinamia pale sakafuni alipokuwa amekaa na kuegamia ukingo wa kitanda. Alishindwa kuelewa amepatwa na nini kwani alipoingia, alimkuta amekaa sakafuni, kichwa chake akiwa amekiinamisha huku mate mengi yakimtoka.
Wakati akiendelea kumtingisha, alishtuka kuona damu zikimchuruzika kwenye mkono wake wa kushoto, akazidi kuchanganyikiwa. Wakati akiendelea kuhaha huku na kule, aliona kitu kilichozidi kumchanganya zaidi. Pale msichana huyo alipokuwa amekaa, pembeni palikuwa na bomba la sindano lililotumika.
Kwa umakini mkubwa akalichukua na kulichunguza vizuri, akagundua ndiyo lililosababisha msichana huyo awe anavuja damu kwenye mkono wake kwani kwa ilivyoonesha alijichoma mwenyewe kwani juu kidogo ya sehemu iliyokuwa inatoka damu, alikuwa amejifunga kwa kitambaa.
Bado alishindwa kuelewa muunganiko wa vitu hivyo vyote kwa pamoja, aliendelea kulishangaa lile bomba la sindano na kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. Akili ya haraka aliyoipata, ilikuwa ni kukimbia nje kutafuta msaada wa kumkimbiza msichana huyo hospitalini kwani bado hakuwa na uwezo wa kuongea wala kufanya chochote.
Alitoka mpaka nje ambapo alikimbilia kwenye kituo cha Bajaj kilichokuwa jirani na anapoishi, akaomba msaada kwa dereva mmoja ambaye aliwasha Bajaj yake haraka na kuelekea mpaka kwenye mlango wa nyumba aliyokuwa anaishi kijana huyo.
“Kwani kuna nini?”
“Mke wangu amezidiwa ghafla, naomba unisaidie kumkimbiza hospitalini,” alisema Abdallah huku akionesha kuchanganyikiwa mno. Akaingia ndani na yule dereva wa Bajaj mpaka chumbani ambapo walisaidiana kumbeba na kumtoa nje.
“Huyu ndiyo mke wako?”
“Ndiyo, kwani vipi?”
“Kama namfahamu huyu dada.”
“Halafu umesema amezidiwa na nini?”
“Bro maswali mengi ya nini? Hebu tusaidiane kwanza kumkimbiza hospitalini mengine yatafuata,” alisema Abdallah huku akionekana kuchanganyikiwa kabisa. Dereva huyo wa Bajaj hakuwa na cha kufanya zaidi ya kumsaidia kumtoa msichana huyo mpaka nje.
Wakasaidiana kumpakiza kwenye Bajaj kisha kwa kasi kubwa wakaondoka na safari ya kuelekea hospitalini ikaanza. Muda mfupi baadaye, tayari walikuwa ameshafika, huku bado Karen akiwa na hali ileile kama mwanzo.
Walipokelewa na manesi ambao walimlaza msichana huyo kwenye kitanda cha magurudumu na kumkimbiza wodini.
“Unasema nini kimempata?”
“Asubuhi alikuwa mzima kabisa, nilipotoka kwenda kazini huku nyuma sijui kumetokea nini lakini niliporudi ndiyo nikamkuta akiwa kwenye hali hii.”
“Mbona vipimo havionesha kama ana tatizo lolote?” daktari aliyekuwa akimhudumia msichana huyo alimuuliza Abdallah baada ya vipimo vya awali kuonesha kwamba msichana huyo hakuwa na tatizo lolote kubwa.
Baada ya kushindwa kuelewana, ilibidi amuite Abdallah pembeni na kuanza kuzungumza naye kwa sauti ya chini.
“Mkeo anatumia madawa ya kulevya?”
“Madawa ya kulevya?”
“Ndiyo kwa sababu ana dalili zote za mtu aliyetoka kujidunga madawa ya kulevya, kwani unaweza kunieleza mazingira uliyomkuta nayo?” alisema daktari huyo na kumfanya Abdallah abaki ameduwaa, akiwa haamini kabisa alichokuwa anakisikia.
Aliunganisha matukio harakaharaka, akakumbuka alivyokuta bomba la sindano likiwa pembeni yake, akajua alichokuwa anakisema daktari lazima kitakuwa na ukweli.
“Karen anatumia madawa ya kulevya? Mungu wangu,” alisema Abdallah huku akijishika mdomoni.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tunahisi tu lakini majibu ndiyo yatakayosema ukweli kwa hiyo shaka ondoa,” alisema daktari na kuondoka kurudi wodini, akamuacha Abdallah akiwa bado amepigwa na butwaa, akiwa haamini kabisa.
“Nina mkosi gani mimi?” alisema Abdallah huku machozi yakianza kumlengalenga. Kwa kipindi kifupi tu tangu aanze uhusiano wa kimapenzi na Karen, mambo mengi sana yalikuwa yametokea kiasi cha kumfanya muda mwingine ahisi kwamba yupo ndotoni au anaangalia filamu ya kusisimua.
Aliendelea kutafakari kwa muda mrefu, mawazo machungu yakipita ndani ya kichwa chake kiasi cha kuyafanya machozi yawe yanamtoka bila mwenyewe kujijua.
“Kaka vipi mbona unalia? Kuna tatizo,” nesi mmoja aliyekuwa amebeba sinia lenye vifaa vya tiba, alimuuliza Abdallah baada ya kumkuta amesimama palepale alipoachwa na yule daktari.
Kauli hiyo ndiyo iliyomzindua Abdallah kutoka kwenye dimbwi la mawazo machungu, harakaharaka akatoa kitambaa mfukoni na kuanza kujifuta machozi huku akitembea taratibu kuondoka eneo hilo.
“Jamani kaka si naongea na wewe? Mbona hunijibu?” yule nesi aliongea tena kwa upole, Abdallah akamjibu kwa kifupi tu kwamba hali ya mgonjwa wake haikuwa nzuri ndiyo maana alikuwa na mawazo kiasi hicho.
“Usijali, atapona tu,” alisema nesi huyo huku akiendelea na shughuli zake kwani ilivyoonesha Abdallah hakuwa tayari kuzungumza naye kwa wakati huo. Abdallah alienda kukaa kwenye mabenchi maalum na kuendelea kuwaza, maswali mengi yakikisumbua kichwa chake.
Muda mfupi baadaye, yule daktari aliyekuwa akizungumza na Abdallah mara ya kwanza, alimfuata tena pale alipokuwa amejiinamia.
“Nifuate,” alisema daktari huyo huku mkononi akiwa ameshika faili. Abdallah aliinuka na kumfuata, wakaenda mpaka kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Karen, dripu ikiendelea kutiririka kwa kasi kuingia kwenye mshipa wake wa mkononi kwa ajili ya kwenda kupunguza ukali wa madawa ya kulevya aliyotumia.
“Vipimo vinaonesha kwamba amejiovadozi Heroine kwa hiyo nilichokihisi awali sikuwa nimekosea,” alisema daktari huyo, Abdallah akawa anatingisha kichwa kwa masikitiko huku machozi yakianza tena kumlengalenga. Kwa muda wote huo, Karen alikuwa haelewi chochote kilichokuwa kinaendelea, alikuwa amelala pale kitandani huku udenda mwingi ukiendelea kumtoka.
“Hutakiwi kulia kijana, ulisema huyu ni nani yako?”
“Ni mchumba wangu.”
“Mko pamoja kwa muda gani?”
“Siyo muda mrefu, ndiyo kwanza tupo kwenye hatua za awali.”
“Unatakiwa kumsaidia aondokane na matumizi ya madawa ya kulevya.”
“Nitamsaidiaje sasa dokta?”
“Inabidi tusubiri kwanza sumu ya madawa ikishapungua atazinduka. Akizinduka usioneshe kumshangaa wala kumlaumu, muonee huruma na tafuta muda ambao atakuwa ametulia uzungumze naye akubali kuanza matibabu ya dawa ya methadone.”
“Methadone ndiyo nini?”
“Ni dawa maalum ya kuwasaidia watumiaji wa madawa ya kulevya kuondokana na tatizo hilo bila kupata madhara.
“Unajua hakuna kitu kigumu kama kuacha kutumia madawa ya kulevya lakini ukimpeleka kwa wataalamu wa madawa ya kulevya waliopo Mwananyamala au Hospitali ya Muhimbili, watamsaidia lakini lazima mwenyewe kwanza akubali kusaidiwa,” alisema daktari huyo, Abdallah akashusha pumzi ndefu na kumgeukia tena Karen pale kitandani.
Daktari huyo aliendelea kumpa Abdallah somo la namna ya kumsaidia Karen kuondokana na tatizo la utumiaji wa madawa ya kulevya.
“Wakiwa wanaendelea kujadiliana, Karen aliupiga chafya mfululizo na kufumbua macho, akawa anashangaashangaa pale ni wapi na amefikaje.”
“Abdallah,” aliita Karen kwa sauti ya kiteja, akamsogelea na kumuinamia pale kitandani huku mkono mmoja akimgusa shingoni kupima joto la mwili wake.”
“Unaendeleaje mpenzi wangu,” Abdallah alijikaza kiume na kumuuliza msichana huyo.
“Kwani hapa ni wapi na nimefikaje?” alisema Karen kwa sauti ya kilevi.
“Hapa ni hospitali, ulipata matatizo kidogo lakini usijali utakuwa sawa,” alisema Abdallah kwa sauti ya kubembeleza, msichana huyo akaanza kuchekacheka mwenyewe kuonesha kwamba bado madawa yalikuwa yakiendelea kufanya kazi.
“Kwa hiyo nani kanileta hapa? Halafu wewe si uliondoka kwenda kazini? Imekuwaje?” alihoji msichana huyo huku akiendelea kuchekacheka mwenyewe. Ilibidi Abdallah amuelezee kuanzia mwanzo ilivyokuwa, Karen akawa anaendelea kucheka kwa furaha huku muda mwingine akizungumza mambo yasiyoeleweka.
Baada ya daktari kuridhishwa na maendeleo yake, aliwaruhusu kuondoka huku akimsisitiza Abdallah kufanyia kazi alichomwambia. Kwa kuwa alikuwa na namba za simu za yule dereva wa Bajaj aliyemsaidia kumpeleka hospitali, Abdallah alimpigia simu na muda mfupi baadaye aliwafuata.
Akawarudisha mpaka nyumbani kwa Abdallah ambapo msichana huyo alikuwa wa kwanza kuteremka kwenye Bajaj, akaingia ndani wakati Abdallah akitoa fedha za kumlipa dereva huyo wa Bajaj ambaye alimsaidia sana.
“Umesikia broo, wewe ni mwanaume mwenzangu mi siwezi kukuacha upotee huku unajiona. Huyu demu nimekwambia mi namfahamu, anajiuza huyu na hata mimi nimeshawahi kumnunua ingawa yeye hanikumbuki, kuwa makini broo,” alisema yule dereva wa Bajaj na kumfanya Abdallah ashtuke.
Kilichomshtua haikuwa kusikia kwamba msichana huyo anajiuza kwani yeye mwenyewe amewahi kumshuhudia kwa macho yake lakini alishtuka kugundua kuwa hata yeye alikuwa anamfahamu. Alibaki ameganda kwa sekunde kadhaa palepale kisha akamjibu kwa kifupi dereva huyo kwamba anashukuru kwa kumpa taarifa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sasa kama huyu anajua si mtaa mzima watakuwa wanajua? Nitaonekanaje mbele ya jamii kuishi na mwanamke ambaye kila mmoja anafahamu kwamba anajiuza?” Abdallah alijiuliza akiwa bado ameganda palepale nje.
Akaanza kueleza jinsi alivyojikuta akiingia kwenye janga hilo, hatua kwa hatua huku akisisitiza kwamba alikuwa anateseka sana kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya lakini hakuwa na uwezo wa kuachana nayo.
SASA ENDELEA...
Ilikuwa ni stori nyingine ya kusikitisha kwenye maisha ya Karen. Abdallah alimsikiliza kwa makini wakati akisimulia jinsi alivyojikuta akiingiakwenye janga la matumizi ya madawa ya kulevya. Kwa mujibu wa maelezo yake, haikuwa hiyari yake bali alijikuta akiingizwa bila mwenyewe kupenda.
“Nateseka sana Abdallah, kama kuna njia nisaidie mwenzio,” alisema msichana huyo na kumkumbatia Abdallah kwa nguvu huku machozi yakimtoka kwa wingi na kumlowanisha Abdallah kifuani.
“Upo tayari kusaidiwa?”
“Nipo tayari mpenzi wangu, hata ukisema sasa hivi,” alisema Karen na kumfanya Abdallah atabasamu. Hakuna kitu alichokuwa anatamani kitokee kama Karen kurudi kwenye hali yake ya kawaida na kuwa mwanamke bora wa kujenga naye familia.
Baada ya mazungumzo marefu, wawili hao walikubaliana kwamba kesho yake, jambo la kwanza litakuwa ni kwenda kwenye Hospitali ya Mwananyamala kukutana na madaktari waliokuwa wakifanya kazi ya kuwatibu waathirika wa madawa ya kulevya.
Walilala pamoja kwa mahaba makubwa, muda wote wakiwa wamegandana kama ruba. Yale mawazo yaliyokuwa yakikitesa kichwa cha Abdallah sasa yalikuwa yamepungua sana baada ya msichana huyo kukubali mwenyewe kwenda kutibiwa.
Asubuhi kulipopambazuka, Abdallah aliwahi kuamka na kwenda kuripoti kazini kwao kwanza kisha akarudi nyumbani na kumchukua Karen, safari ya kuelekea Hospitali ya Mwananyamala ikaanza.
Walipofika Mwananyamala, walieleza shida yao mapokezi ambapo nesi waliyemkuta aliwaelekeza kwenda kuonana na Dokta Kyaruzi, bingwa wa matibabu kwa waathirika wa matumizi ya madawa ya kulevya.
Mwanaume wa makamo, aliyekuwa amevalia miwani na kuishusha kidogo, alikuwa amekaa nyuma ya meza kwenye ofisi namba 8, ukutani kukiwa na picha mbalimbali zilizokuwa zikieleza madhara ya utumiaji wa madawa ya kulevya na namna ya kuondokana na uraibu.
Ilibidi Abdallah ndiyo awe mzungumzaji mkuu ambapo baada ya kumsalimia daktari huyo aliyewapokea kwa uchangamfu, alieleza kilichosababisha wakafika hospitalini hapo. Baada ya maelezo ya kutosha kutoka kwa Abdallah, daktari huyo alimuomba atoke nje ili abaki na Karen pekee, jambo ambalo alilikubali.
Walipobaki wawili, Dokta Kyaruzi alianza kumhoji Karen kwa kina kuhusu historia yake ya matumizi ya madawa ya kulevya, kuanzia jinsi alivyoanza, aina ya madawa anayotumia na kiwango anachotumia kila siku.
Maelezo yake yalimshangaza mno Dokta Kyaruzi kwani licha ya urembo na umri mdogo aliokuwa nao msichana huyo, alikuwa amekubuhu kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, akitumia dozi kubwa ambayo ingeweza hata kusababisha siku moja akafa kifo cha ghafla.
“Umeamua mwenyewe kuja kupata matibabu au ni shinikizo kutoka kwa mchumba wako?”
“Hapana dokta nimeamua mwenyewe,” alisema Karen, mazungumzo yakaendelea ambapo daktari huyo alianza kwa kumueleza jinsi madawa ya kulevya yanavyofanya kazi mwilini. Akaendelea kumueleza namna madawa hayo yanavyouathiri ubongo na kumfanya mtumiaji aendelee kutumia kwa kipindi chote cha maisha yake.
Mwisho alimueleza madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya na mbinu za kuachana nayo. Akamueleza ukweli kwamba hakuna kazi ngumu kama kujitoa kwenye janga la matumizi ya madawa ya kulevya.
“Usipokuwa na moyo wa dhati haitakuwa kazi nyepesi kuachana nayo. Wengi huwa wanaanza vizuri lakini baadaye wanashindwa na kujikuta wakiendelea kutumia. Naomba na wewe usiwe miongoni mwa watu wa aina hiyo,” alisema Dokta Kyaruzi, Karen akawa anatingisha kichwa kuonesha kukubaliana na kile alichokuwa anaambiwa.
Baada ya mazungumzo yaliyochukua zaidi ya dakika arobaini, Dokta Kyaruzi alimuita Abdallah ambaye kwa muda wote alikuwa nje akisubiri, akamshirikisha juu ya walichokubaliana na kumuomba awe karibu na Karen kwa kipindi chote ambacho atakuwa akipata matibabu kwa ajili ya kuondokana na tatizo lililokuwa linamsumbua.
“Itabidi kila siku awe anakuja hapa hospitalini kunywa dawa ya methadone, hatakiwi kukosa hata siku moja.”
“Sasa dokta kwa nini usitupe dawa nyingi ili awe anatumia nyumbani?”
“Hapana, hizi dawa ni hatari na zinatakiwa kutumiwa chini ya uangalizi maalum kwani zinafanya kazi kama madawa ya kulevya na kuna baadhi wanazitumia kama madawa ya kulevya,” alisema daktari huyo na kuendelea kuwaelewesha jinsi dawa hizo zinavyofanya kazi.
“Unajua tatizo kubwa kwa mtumiaji wa madawa ya kulevya, asipopata dozi anashikwa na arosto, bila shaka Karen unaelewa ninapozungumzia arosto,” alisema daktari huyo, Karen akawa anatingisha kichwa kukubaliana na alichokuwa anakisema.
“Sasa hizi dawa zinaenda kumaliza kabisa arosto kwa hiyo hata usipotumia madawa ya kulevya hutapatwa na arosto,” alisema Dokta Kyaruzi kisha akatoa boksi lililokuwa na dawa hizo na kumpa Karen pamoja na maji ili anywe.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Huu ndiyo utakuwa utaratibu wetu, kuna wenzako wengi tu wanatumia hii dozi, kadiri utakavyokuwa unakuja ndivyo utakavyokuwa unakutana nao,” alisema Dokta Kyaruzi kisha akatoa faili maalum ambapo aliandika maelezo yote muhimu kuhusu Karen.
Huo ukawa mwanzo wa msichana huyo kutumia dawa za methadone ili kuondokana na tatizo hilo la matumizi ya madawa ya kulevya. Baada ya kumaliza kila kitu hospitalini hapo, waliianza safari ya kurudi nyumbani lakini kilichomshangaza Abdallah, wakiwa njiani, wanaume wengi walikuwa wakimsalimia Karen, tena wengine wakimuita kwa jina lake.
“Wamekujuaje? Halafu mbona wote ni wanaume?” alihoji Abdallah lakini Karen hakuwa na jibu.
...
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment