Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

MTU WA UFUKWENI (THE BEACH MAN) - 1

 





    IMEANDIKWA NA : ANDREW MHINA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Mtu Wa Ufukweni (The Beach Man)

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa ni kama ndoto ya mchana! Ndoto yenye kila aina ya dalili ya kuondoka na kubakia na kumbukumbu ya muda mfupi sana kwa baadhi ya mabaki ya ndoto hiyo. Nilijaribu kufikicha macho yangu ili kuhakikisha yale yaliyoko mbele yangu!.. Bado vitu vyote vilikuwepo! Lile jumba la fahari lilikuwa limetulia mbele ya macho yangu, wakati bwawa la kuogelea likiwa karibu yangu mahali nilipokuwa nimeketi.

    Mazingira ya mahali hapa ni mazuri ajabu! Majani mafupi yaliyokatwa kwa mashine maalumu, bustani nzuri za maua na miti ya kimvuli iliyokuwa ikitingishwa taratibu na upepo, vilitoa burudani ya pekee. Niliamka taratibu pale nilipokuwa na kusogelea banda la magari. Nilikuwa nataka tena kuamini kuwa mali hizi zote zilikuwa ni za kwangu. Magari matatu ya fahari yalikuwa yametulia mahali pake. Haikuwa ndoto wala wazimu kwa mimi kushangaa mali zangu mwenyewe!

    Historia yangu ndiyo iliyonilazimisha kuangalia mambo haya kama ndoto ya mchana. Historia yangu inanifanya nisiamini japo ndio niko ndani ya ukweli wa yale ninayoona kuwa ni ndoto. Mara simu yangu ya mkononi inaita! Niliitoa mfukoni na kuiangalia nione ni nani alikuwa akipiga. Nikiwa kando ya banda la magari nilipokea simu ile, alikuwa ni Jobiso Baro, mmoja wa waandaaji wa filamu mashuhuri nchini mwetu. Muda mrefu sana alikuwa akinishawishi kucheza filamu ya matukio yaliyopita katika maisha yangu.

    Nilisita kufanya hivyo mara nyingi, sio kwamba kulikuwa na ubaya kucheza sinema ya maisha yangu la hasha! Bali nilikosa mahali hasa pa kuanzia katika mikasa yangu niliyopitia. Nilikuwa natafuta namna ya kuanza kuielezea historia yangu, kusudi nisije nikaacha chochote cha muhimu kuwekwa kwenye sinema hiyo.

    Muda nao ulikuwa umenibana sana kwa sababu nilikuwa na majukumu ya kusimamia makampuni yangu mapya, ambayo nilitakiwa kila wakati niwepo mahakamani, kusudi nishughulikie kubadilisha jina la umiliki kutoka mmiliki wa kwanza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kutafuta wakili binafsi nalo lilikuwa swala la muhimu, lakini ni nani wakili atakayefaa kusimama na mimi katika mwendo mzima wa maisha yangu na mali zangu? Maswali mengi na mambo mchanganyiko vilibebana ndani ya kichwa changu hata nikawa sina muda wa kutosha kutoa maamuzi sahihi kwa vyote. Wafanyakazi wangu wa ndani ninashukuru sana kwamba walikuwa wakinielewa, hasa nilipowaambia kuwa nataka utulivu wa kutosha. Walifanya kazi zao mapema na kuniachia nafasi ya utulivu katika eneo la bustani yangu, iliyopo karibu na bwawa hili la kuogelea.

    Mahali hapa huwa ninapatumia kupumzikia, wakati nikitoka ofisini na kutafuta utulivu wa kipi kianze kati ya majukumu yangu mengi niliyokuwa nayo. Pamoja na kwamba umepita muda wa miezi mitatu tangu niwe mmiliki wa mali hizi, lakini kila siku kwangu niliona kama ni ndoto ndefu.

    Ndoto iliyotawala katika usiku wote bila kubadilika! Ndoto iliyofanana sana na ukweli halisi! Ndoto labda iliyokuwa na mapitio yaliyofanania na yale ya mawazo ya Alinacha wa kitabu cha Alfu lela u lela au siku elfu na moja! Tofauti moja ya ndoto yangu na Alinacha ni kwamba mwenzangu alikuwa akiwaza na kupotelea katika mawazo yake ya kiutajiri na usultani.

    Lakini kwangu ni kwamba ninaishi kabisa ndani ya ndoto hizo. Ndoto zenye vitu vinavyoshikika na amri zinazotekelezeka! Naam! Ndoto ya mchana lakini iliyodumu kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu! Nilifikia mahali pa kukata shauri kukubaliana na ukweli uliopo, kuwa hii sio ndoto bali ni jambo halisi limetokea. Sababu ya kuyafananisha maisha haya na ndoto ni kwamba sikutegemea kuwa iko siku nitafikia vilele hivi vya mafanikio.

    Taratibu nilipeleka simu ile sikioni mwangu na kuanza kuitikia:“Haloo Jobiso!”….“Habari Mheshimiwa!” Alijibu Jobiso…kisha akaendelea “Nimetaka kukujulia hali tu, pia nina jambo la muhimu kidogo nikujulishe.” Alisema Jobiso sauti yake ikisikika kama mtu mwenye haraka. “Jambo gani Jobiso! Mbona unaonekana kama unataka kukimbia uko sawa?” Nilimwambia kwa mshangao.“Niko sawa mheshimiwa, lakini nilitaka kama una nafasi tuanze yale mahojiano kusudi niandaye vipande vya Sinema yako.”Alisema kwa utulivu.

    “Mbona una haraka sana Jobiso! Bado sijawa tayari kutokana na mibanano ya mambo yangu. Sijaandaa chochote nitaanzia wapi?” Nilimjibu kwa msisitizo kidogo. “Mheshimiwa nimekuambia hivyo kwa sababu baada ya mwezi mmoja nitakuwa nchini marekani kwa masomo. Leo hii mkurugenzi wangu ametoa ofa kwa wafanya kazi wake bora kwenda masomoni, ili kupanua ujuzi zaidi.

    Mimi nimetokea kutangazwa kuwa mmoja wa wafanyakazi bora.”Jobiso alielezea kwa hamasa kuonyesha jinsi alivyovutiwa na ofa aliyopewa ya kwenda nchini Marekani. “Hongera sana bwana mdogo! Nimekuelewa, lakini unadhani kuna haja ya kufanya haraka juu ya sinema yangu? Maana sioni kwamba hata nikikuhadithia itaweza kuchezwa kwa kipindi hicho kifupi.

    Nilimwambia kwa utulivu lakini nikitia msisitizo kuwa kazi ile haikuhitaji haraka kiasi hicho. “Kaka niruhusu tu nije mengi tutaongelea huko. Ninajaribu kuangalia uwezekano wa kufanya jambo kwa wakati. Unakumbuka waswahili na ule msemo wao maarufu?” Aliuliza huku akijiandaa kuachia kicheko chake cha uzushi. “Ndio nakumbuka kuwa linalowezekana leo lisingoje kesho.” Nilimjibu.Basi naomba nije ili tuangalie ni wapi pa kuanzia.” Alisema kwa shauku baada ya kuijibu methali yake. Nilifikiri kidogo nini cha kufanya kutokana na kutokujiandaa vema juu ya hili, lakini niliafikiana naye aje nyumbani.

    “Basi dogo unaweza kuja wakati huu maana mimi nipo tu nyumbani.” Nilimwambia na kukata simu, baada ya yeye kupokea ukaribisho huo kama mtu aliyeokota kipande cha almasi! Nilijisogeza katika ngazi za kupandia kuelekea katika mlango unaonipeleka hadi kwenye sebule kubwa nzuri,sebule iliyojaa kila aina ya vifaa vya thamani.

    Kando ya sebule hiyo kuna chumba maalumu nilichokiteua kiwe ofisi yangu. Chumba hiki kimejengwa kwa aina yake. Ofisi yangu hii ina kila aina ya vifaa vya kielektroniki, vya kunasia sauti na kamera za kuchukulia matukio mbalimbali. Nimeamua kutumia chumba hiki kwa ajili ya mahojiano yangu na Jobiso Baro, juu ya maandalizi ya sinema yangu.



    * * *

    Ulikuwa ni usiku wa manane kukiwa na manyunyu ya mvua kiasi na upepo wa hapa na pale. Nyota zilikuwa zimefichwa na mawingu meusi yanayoashiria mvua kubwa kunyesha. kijiji cha Makuyuni kilikuwa kimya isipokuwa sauti za watu wachache waliokuwa wakikohoa ndani ya nyumba zao na kilio cha mtoto aliyekuwa aidha anataka kunyonya, au ni deko la kijinga tu,kwa baadhi ya watoto.

    Hali ilikuwa tofauti katika nyumba moja. Ni katika nyumba aliyokuwa akiishi bwana Kimbe na mkewe bi Nacharo. Mke wa Kimbe alikuwa katika wakati mgumu sana wa kutaka kujifungua. Hali hii ilikuja sambamba na ugumu wa maisha. Hakukuwa na hata senti moja mifukoni mwa Kimbe. Hakuwa hata na rafiki mmoja wa kumwendea usiku huo, hii ni kutokana na madeni aliyokuwa nayo katika kijiji hicho.

    Hali ilikuwa ni mbaya kwa ujumla kiasi cha kumfanya akose jinsi ya kufanya. Maumivu ya uzazi yalikuwa ni makubwa kwa mkewe kiasi cha kupiga kelele hafifu, akitarajia kupata msaada. Baada ya muda mrefu kupita bi. Nacharo alifanikiwa kujifungua peke yake akiwa chumbani kwake! Kwa ujuzi kidogo wa kidaktari kuhusu mambo ya uzazi, bwana Kimbe alifaulu kumzalisha mkewe. Hali hii ilileta unafuu kutokana na gharama za hospitali ambazo wasingeweza kuzimudu.

    Walimshukuru Mungu kwa kuwapigania, lakini kukabaki jambo moja kubwa ambalo ni la lazima. Mama mtoto alihitaji chakula na mafuta ya kutosha kwa ajili ya uzazi. Hiyo ilimfanya Kimbe aende kusaka kibarua baada ya mapambazuka baada ya kumwandalia mkewe uji. Kwa ugumu wa aina yake maisha yaliendelea na mtoto aliendelea kukuwa japo kwa udhaifu sana. Mtoto huyu alikuwa wa Kiume ambaye walimwita Ramsoni. Ramsoni ni jina la rafiki yake bwana Kimbe waliyeonana nchini India wakati Kimbe akichukuwa kozi yake ya udaktari. Ramson na Kimbe walikuwa wanafunzi wote katika chuo hicho cha Udaktari.

    Wote walikuwa wakichukuwa kozi moja katika kitengo cha mifupa na upasuaji. Walitokea kuelewana sana mpaka mwisho waliachana kwa masikitiko makubwa baada ya kumaliza kozi hiyo. Mwishowe waliishia kupeana anuani na kuahidiana kuandikiana barua. Waliachana uwanja wa ndege kila mmoja akipanda ndege ya kurudi kwao, Ramson alirudi kwao Uholanzi. Kimbe alikuwa daktari mzuri sana katika kitengo cha Moi katika hosptali kuu ya Taifa Muhimbili Dar es Salaam. Kwa miaka mitatu mfululizo alifanya kazi hiyo kwa amani hadi siku aliyofukuzwa kazi yake, hii ilitokana na kusingiziwa kuchukuwa rushwa kwa mmoja wa wagonjwa wake. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sheria ya hospitali hii ilikuwa kali sana juu ya wala rushwa, sababu hii ilimfanya Dr.Kimbe afukuzwe baada ya kupewa malipo yake ya NSSF. Malipo ambayo hayakukidhi mambo mengi, zaidi ya kujenga nyumba yake ndogo kijijini hapa. Shamba lake alilopewa na babu yake kwa upande wa mama yake, ndilo lililowasaidia kupata chakula kidogo.

    Lakini kama balaa kwa upande wake mjomba wake alimnyang’anya shamba hilo,akitumia kisingizio kuwa hakuwa na haki ya kurithi shamba hilo, kwa kuwa yeye hana ukoo na upande huo wa ujombani. Hali hii ilimwacha mtupu wakati huo akiwa tayari ameoa mkewe huyo.Dr. Kimbe hakutaka kurudi kwa wazazi wake baada ya kufukuzwa kazi, kutokana na aibu juu ya kashfa yake hiyo na kuhofia hasira za baba yake kutokana na jinsi alivyomsomesha kwa gharama kubwa.

    Babayake Dr.Kimbe alikuwa na fahari kubwa baada ya mwanaye kurudi kutoka nchini India akiwa na shahada ya udaktari kwa upande huo wa upasuaji. Sherehe zilizofanyika kijijini hapo kwa kumpokea mtoto wake vilimtofautisha na wakaazi wote wa kijiji chao. Baba yake Dr. Kimbe anaitwa mzee Kihedu ambaye aliishi katika kijiji cha Taabu yanini kilichopo nje kidogo ya mji wa Tanga katika njia kuu ya kuelekea nchini Kenya.

    Watu wote kijijini hapo walimwonea wivu mzee Kihedu kwa kuwa na mtoto msomi na mwenye kazi yenye kipato kikubwa. Sherehe hiyo iliweka alama za wivu kwa baadhi yawanakijiji katika mioyo yao. Baada ya sherehe hiyo minong’ono ya masengenyo ilikuwa imetapakaa kila mahali katika kijiji hicho. Maneno kuwa mzee Kihedu na mkewe Bi. Namkunda walikuwa wakiringa yalikuwa ni mengi lakini hayakupatilizwa.

    Mzee Kihedu alimtuliza mkewe asiyafuatilie maneno hayo kwani hayana maana. Wao walijua kuwa kumsomesha mtoto wao ulikuwa ni wajibu wao. Na kila mtu alipaswa kufanya hivyo kwa familia yake kwa ajili ya maendeleo yake. Hilo halikumtisha na alimtahadharisha mkewe kutofuatilia chochote juu ya maneno ya majirani zao kusudi wasijenge uhasama zaidi. Busara ya kunyamaza ilimfanya ashinde na kurudisha hali ya urafiki kwa wale waliojaribu kujitenga nao kutokana na wivu.

    Kila wakati Dr.Kimbe alikuja nyumbani kwao na kuwasalimia wazazi wake huku akiwaachia kiasi kizuri cha fedha kwa ajili ya kulimia mashamba yao. Furaha yao ilizidi baada ya mtoto wao wa pekee kutaka kuoa. Walimsimamia kwa mambo yote na kumwozesha kwa furaha. Hatua hii ilifurahiwa sana na wazazi wake na baadhi ya wanakijiji.

    Sherehe yake iliweka historia nyingine kwa kuwa ya fahari. Mbuge wa jimbo lao alihudhuria sherehe hiyo akiongozana na mkuu wa wilaya na marafiki zao. Msururu wa magari uliokuwepo wakati wa kuja na kuondoka baada ya harusi ni alama nyingine kubwa iliyowekwa katika historia ya wanakijini hao. Vyote hivi vilimfanya Dr. Kimbe kugoma kurudi kijijini kwao mara baada ya kufukuzwa kazina kutangazwa katika Hospitali zote.

    Kosa hilo ambalo kiukweli halikuwa la kwake lilimtia fedheha kubwa na kumfanya akose amani katika maisha yake. Baada ya kutoka Dar-es Salaam aliazimia kushukia Korogwe katika kijiji cha Makuyuni alikokuwa amepewa shamba na babu yake mzaa mama yake. Alipangisha nyumba kijijini hapo wakati akishughulikia Ujenzi wa nyumba yake ndogo. Baada ya miezi sita alihamia kwenye nyumba yake ya vyumba viwili na sebule. wakati huo akiwa analima shamba alilopewa urithi na babu yake.

    Taarifa za kufukuzwa kazi wazazi wake walizipata baada ya miezi miwili. Aliwaambia kwa njia ya barua na kuwataarifu kuwa yeye yuko makuyuni na kamwe asingekuja kijijini hapo kwa hali yake aliyonayo. aliogopa fedheha kwake na kwa wazazi wake waliojinyima kumsomesha. Taarifa hiyo iliwafadhaisha lakini wangefanyaje? waliendelea kumwombea mtoto wao ili apate kazi nyingine ya maana kuliko kutegemea kilimo cha mkono. Kiwango cha Elimu alichokuwa nacho hakikustahili kumfanya arudi kijijini kutegemea jembe la mkono. Mwaka wa pili baada ya kuwepo kijijini makuyuni, Mjomba wake aliyezaliwa na mama yake alikuja juu na kudai apewe shamba la baba yake. Maneno makali na kutishia kumpeleka mahakamani, vilimfanya Dr. Kimbe akubali kuachia shamba hilo. Hali hiyo ilisababishwa pia na kukosa japo maandishi kidogo kutoka kwa babu yake kuwa alimrithisha yeye. Kwa ujumla ni kwamba alipewa shamba hilo kwa kauli tupu isiyo na ushahidi wa maandishi.

    Baada ya kunyang’anywa shamba lake alibadilika na kuwa zaidi ya maskini, kwani hakuwa na maarifa mengine zaidi. Hali yake ilikuwa mbaya sana, hadi kumpelekea mtoto wake Ramson kuzaliwa katika mazingira magumu kiasi hicho. Hali ya madeni ilizidi kuwa mbaya kiasi kutokana na vibarua alivyofanya vya shamba kutokukithi mahitaji yao. Hali hii ilisababisha mtoto wao kupata ugonjwa wa Utapiamlo. Mzee Kihedu alilia machozi siku aliyowatembelea kijijini hapo, hakuamini kumwona mwanaye katika hali hiyo. Mwisho wa yote aliamua kumshauri arudi kijijini Taabu ya nini.

    “Baba kwakweli ningetamani nirudi, lakini nakwepa macho ya watu. Nitawaangalia vipi wanakijiji walioniona niko juu kimaisha na sasa narudi nikiwa na hali hii? Rafiki zangu niliowazidi elimu baada ya wao kufeli mitihani ya kujiunga na Elimu ya Sekondari, nitawaambia nini wakati nikijiunga nao tena kijijini kulima na kuchunga mbuzi? Na wewe baba yangu utajisikiaje baada ya kuhangaika kwa ajili yangu, mpaka kuuza baadhi ya mashamba yako kwa ajili ya kunisomesha?

    Utasema nini tena wakati ukidhihakiwa na rafiki zako kwenye vijiwe vya kahawa jioni? Hapana baba Mimi sirudi huko.” Alisema Dr.Kimbe. Maneno haya yalikuwa na ukweli wote lakini Mzee Kihedu hakuyajali yote hayo. “Kimbe wewe ni mwanangu, hapa yuko mkaza mwanangu na mjukuu wangu. Uthamani wa maisha yenu umezidi hayo maneno, ambayo yatachukua muda mfupi tu na watu watayaona ya kawaida. Isitoshe wewe una marafiki wengi nje ya nchi, unaweza kuwaandikia na baadaye ukapata kazi nzuri zaidi ya hiyo uliyoachishwa.

    Kumbuka mimi ni Mzee sasa na mama yako. Ninani atakayeangalia mashamba yako na mifugo iliyopo? Twende na ujifanye huyaoni wala kuyasikia maneno ya wanakijiji, kwa faida yako mwenyewe. Unadhani mjukuu wangu atakuwa katika hali gani baadaye ukiendelea hivi? Hebu tafuta mteja wa nyumba yako umuuzie na uondoke hapa urudi nyumbani sawa!” Alisema mzee Kihedu. Mwisho wa Yote Dr. Kimbe alikubali kuondoka kijijini Makuyuni na kuuza nyumba yake na mwishowe akarudi Kijijini Taabu yanini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maisha yalikuwa sio mabaya katika familia hii, mwaka umepita sasa tangu Bwana Kimbe afike kijijini hapa. Mashamba yalisimamiwa vema na mifugo ilistawi sana na kuongezeka. Bidii yake katika kazi viliwafumba midomo wambea wote waliokuwa wakijaribu kufuatilia maisha yake. Hakuwa akionekana kwenye vilabu vya pombe wala kwenye kijiwe kama wengine wanavyofanya kila siku. Yeye na mke wake na wazazi wake ndio marafiki wakubwa. Mfumo wake wa maisha ya ukimya na uchapakazi vilimletea furaha na heshima kwa watu wengi.

    Mafanikio yalikuja kwa kasi sana na kubadilisha afya zao zilizokuwa dhaifu kwa ugumu wa maisha walipokuwa Makuyuni. Kila wiki walikuwa wakikutanika pamoja na wazazi wao kwa ajili ya kikao cha familia kujadili mambo ya maendeleo yao. Ramsoni alishakuwa na kufikia umri wa kupelekwa kwenye shule ya Chekechea. Miaka minne ilitosha kumfanya ajiunge na shule hiyo. Kwa ujumla ni kwamba maisha yalirudi kuwa mazuri kwa Dr. Kimbe na familia yake.

    Kwa Upande wa Mzee Kihedu alijawa na furaha kwa kuungana na mwanae kijijini hapo kuliko hata alipokuwa kazini. Mazao yaliongezeka mara nyingi zaidi ya alipokuwa peke yake. Bidii na utaalamu wa kilimo pamoja na ubunifu wa mambo aliokuwa nao Dr. Kimbe, vilimfanya awe mbali sana kimaendeleo kuliko wanakijiji wote. Wengi wa wanakijiji walikuwa wakitegemea minazi yao tu. Lakini yeye alilima mazao mbalimbali na kufuga mifugo mingi mbalimbali.

    Ni kweli kilikuwa ni kilimo cha mkono lakini alikifanya kwa ubunifu mkubwa. Wafanyakazi wa shambani walirahisisha kazi na kusababisha maendeleo kwa familia hizo mbili. “Kwakweli baba ninafuraha sana katika maisha yangu mpaka hapa.” Dr.Kimbe alimwambia baba yake jioni moja wakati walipokuwa kwenye kikao cha familia. “Ndio Mwanangu! Hata mimi ninakuona umebadilika sana na unatufurahisha mimi na mama yako.” Alisema Mzee Kihedu huku akionyesha tabasamu la ushindi.

    “Kwa kweli mwanangu furaha yangu na baba yako ni kubwa sana, kwani hata upweke hatuna tena. Pia ninafurahi niko na mkaza mwanangu hapa na tunashirikiana vizuri. Mjukuu wetu Ramson naye anatufanya tufurahie maisha kwa uchangamfu wake.”Wote walitabasamu na kutoa miguno kuashiria kumkubalia mama kwa maneno yake. “Labda ungetueleza juu ya furaha yako maana ni wewe uliyeanzisha mazungumzo haya.”

    Alisema Mzee Kihedu akimgeukia mwanae ili asikie kutoka kwake zaidi. “Unajua Baba niliathirika sana kifikra baada ya kuachishwa kazi? Kwa mawazo yangu nilijua kuwa sasa nimekwisha!Mbaya sana ni taarifa zangu za kufukuzwa kazi zilivyosambazwa katika Hospitali zote nchini. Hii ilinifanya nikose ujanja hata wa kuomba kazi mahali popote. Kuchanganyikiwa kwangu kukanifanya niamue kujiweka mbali sana na watu wanaonijua. Niliona aibu sana kurudi tena hapa kijijini.

    Akili zangu kidogo zilizobaki nikachanganya na za mke wangu, zikatuelekeza kwenda kujificha Makuyuni. Shamba alilonipa babu Sengasu, likawa sababu ya mimi kwenda kujihifadhi kijijini pale, ili nilime na kuendesha maisha yangu na familia. Balaa jingine ni pale mjomba chambo alipokuja na kuninyang’anya shamba lile. Kwakweli nilijiona kama ambaye ulimwengu wote umeniinamia na kunidhihaki!

    Sikuona kwamba maisha yangu yalikuwa na mwelekeo tena, kwani huku kijijini sikuwa ninafikiri habari yake. Sikutaka fedheha ya kudhihakiwa na watu walionijua hali yangu hapo mwanzo.”Alisema Dr. Kimbe kwa hisia kali.“Nilikuona siku nilipokuja kukutaka urudi nyumbani.” Alisema mzee Kihedu kisha akakohoa na kuendelea tena.. “Hofu yako kwa wanakijiji kuwa watakuonaje ilikuwa na ukweli wa asilimia ishirini tu. Asilimia nyingi zilikuwa zikisimamia haki ya wewe kurudi nyumbani kwenu.” Waswahili wana msemo usemao: “Ng’ombe akivunjika mguu, hujikokota na kurudi kwao.”

    Hapa ni kwako! Mkataa kwao ni mtumwa! Angalia ulivyotaka kujifanya mtumwa, kwa kwenda kuishi mahali pengine na kutegemea shamba ambalo ulipewa bila hata kipande cha karatasi, kukudhibitisha kuwa ni lako. Hebu tuachane na hayo ilimradi uko nyumbani sasa. Vipi kisima watu wako wameshamaliza kukichimba?” Alihitimisha kwa swali mzee Kihedu na kuingiza mada nyingine.

    Kwakweli kisima bado hakijakamilika inavyoonekana maji yako chini sana, inabidi waendelee kuchimba kusudi tupate unafuu kwa ajili ya umwagiliaji wa mazao.” Alisema Dr.Kimbe. “Ramson mmemwacha amelala au anachora mapicha yake?” Aliuliza Mzee Kihedu baada ya ukimya mfupi. Alikuwa akipenda sana kuwa na mjukuu wake karibu mara zote lakini Ramson alipenda kujitenga mwenyewe muda mwingi huku akijisomea na kuchora mapicha mbalimbali.

    Japo alikuwa ni mdogo lakini alikuwa anaonyesha kuwa na kipaji hasa cha uchoraji na akili nyingi darasani kwao. “Nilimwacha amelala alisema kuwa alikuwa anasikia usingizi.” Alijibu mke wa Kimbe kwa mara ya kwanza katika kikao chao hicho. “Vizuri mwache alale amefanya kazi kubwa sana leo. Unajua alipotoka tu shuleni tuliungana kwenda shamba la minazi, aliwasimamia mbuzi wakati mimi nikisimamia watu wa kuangua nazi.

    Mpaka tunarudi jioni hii yuko hoi kwa kukimbizana na mbuzi.” Aliongea hayo kwa sifa kidogo Mzee Kihedu na wote walicheka. Mwisho wa yote waliagana kwa sala kusudi wakalale. “Kwa hiyo kesho utakuwa kule kwenye kisima au fundi atasimamia hiyo kazi?” Aliuliza mzee kihedu akitaka kujua ratiba ya kesho yake.

    “Baba unajua kazi usipoisimamia mwenyewe haiendi? Inabidi niwepo pale, vibarua wanaendelea na kazi yao kwenye shamba la Mtimbwani. Labda wakija na kusema wamemaliza kazi nitaenda haraka na pikipiki ili nikakague kazi yao kabla sijawalipa.” Alisema Kimbe huku akiusogelea mlango.

    “Kesho nitakwenda na Ramson akaone kisima kinavyochimbwa.” Alimalizia. Sawa tu ila keshokutwa tutakwenda naye mjini Tanga, nataka kumtembeza maeneo mbalimbali, maana naenda kununua baadhi ya mahitaji ya nyumbani.” Alisema Mzee kihedu.

    “Sawa baba nawatakia usiku mwema baba na mama.” aliaga. “Asante na nyinyi pia.” Walijibu Mzee Kihedu na mkewe kwa pamoja. Walitoka Kimbe na mkewe na kuelekea kwenye nyumba yao iliyoko kama mita mia mbili kutoka Nyumbani kwa Mzee Kihedu.



    * * *

    Mapambazuko ya siku hii yaliambatana na mvua za hapa na pale. Hali ya hewa ilikuwa hairuhusu kwenda kokote, lakini kutokana na kazi nyingi za muhimu ililazimu Dr. Kimbe atoke na mkewe kwa ajili ya kusimamia uchimbaji wa kisima. Baada ya hapo alipanga kwenda Mtimbwani kuwaangalia vibarua wa shambani, kama wamemaliza kazi yao. Ramson naye alipenda kuambatana na wazazi wake japo alitakiwa aende kwa babu kutokana na hali ya mvua. hawakutaka kumlazimisha kubaki kwa babu kutokana na msimamo wake. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kufunga milango ya nyumba waliondoka na kuelekea taratibu njia iendayo shambani kwao. Mazungumzo ya hapa na pale yaliwafanya waingie barabarani kutaka kuvuka kwenda ng’ambo ya pili bila kuangalia. Mara walisikia sauti ya Ramsoni akiita “mamaaa babaaa gariiiiiiiiii!!!”… Wakati wanageuka ili kumwangalia Ramson walikumbana na gari na mizigo likiwa hatua tatu mbele yao.

    Milio ya breki za gari hilo iliwachanganya wakashindwa kufanya lolote na mwishowe gari hilo liliwagonga vibaya! Dreva wa gari hilo alijaribu kwa bidii zake zote kuwakwepa lakini kwa sababu ilikuwa kwenye kona hakuweza kuwaona wakiwa mbali, bidii zake zote hazikufua dafu badala yakealiishia kuwagonga na gari ikaserereka na kugonga mnazi kisha likazima.

    Dreva aliteremka kwenye gari na kumkuta mtoto amewakumbatia wazazi wake wakiwa wametapakaa damu na sehemu nyingine hazitazamiki. Kelele zile za gari na Sauti za hamaki viliwavuta watu wengi kijijini. Wapita njia na wanakijiji walikusanyika kwa haraka na kuja kushuhudia ajali ile mbaya.

    Kwa haraka walimwondoa mtoto Ramson juu ya miili ya wazazi wake alikuwa analia kwa uchungu mkubwa. Mwanzoni walifikiri kuwa na yeye pia aliumia kwa jinsi alivyotapakaa damu lakini baadaye wakagundua kuwa alikuwa hajaguswa popote. Walimweka kando na kukusanya maiti zile na kuita gari ndogo kwa ajili ya kuzipeleka Hospitali ya mkoa. Mzee Kihedu na mkewe walipata taarifa ya ajali hiyo wakiwa njiani kuelekea kwenye shamba lao la minazi. Taarifa kuwa Kimbe na mkewe walikuwa wamepoteza maisha viliwachanganya akili na kuwatesa sana moyoni.



    * * *

    Ilikuwa ni halaiki ya watu katika msiba huo. Watu walikuwa wakikanyagana katika eneo la mazishi. Magari yalijaa katika maeneo mbalimbali, marafiki wengi walioko pande mbalimbali walihudhuria baada ya kupata taarifa za Msiba huo wa kusikitisha. Vilio vya maombolezo vililipuka mara tu baada ya kuyaona makaburi, yaliyochimbwa karibu karibu kwa ajili ya Kimbe na mkewe Bi Nacharo.

    Ilisikitisha sana lakini kila mmoja alikubaliana na matokeo hayo kwa sababu kazi ya Mungu haina makosa siku zote.Mchungaji Tito alikuwa akitoa mahubiri kwa watu waliokuwa mazishini, kulionekana kukiwa na utulivu wa hali ya juu Isipokuwa vilio vya hapa na pale vya akina mama.

    “Ndugu zangu ni kweli kabisa msiba huu umetupa huzuni nyingi sana, kwani umemgusa kila mmoja wetu. Bwana Kimbe na bi Nacharo walikuwa ni watu wema sana na wenye ushirikiano na kila mtu hapa kijijini. Lakini tukiangalia Maandiko Matakatifu yanasema kuwa, Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake za kuishi sio nyingi. Nazo zimejaa taabu. Ukweli wa maneno haya unadhibitika kila siku, watu wanakufa. Hii inaonyesha kuwa dunia hii sio ya kutegemea sana. Sio mahali pa kuishi milele. Tukiangalia vizuri maandiko yanatuonyesha kuwa mbele yetu kuna njia mbili. Njia ya kwenda mbinguni na njia ya kwenda jehanum. Njia hizi zote zinategemea uchaguzi wa mtu mwenyewe. Ukichagua kwenda mbinguni utaishi katika maisha ya kumcha Mungu. Utajiepusha na mambo mabaya na kutenda mema kwa msaada wa Mungu.

    Kwa hiyo kila mmoja ajue kuyatengeneza maisha yake kabla hajapatwa na mauti kama ndugu zetu hawa.” Alisema Mchungaji Tito katika mahubiri yake. watu wengi walikuwa wametulia kimya wakisikiliza hotuba hiyo. Mchungaji anawataka ndugu wa karibu wawasindikize marehemu, kwa kutupa mchanga kila mmoja kwa zamu katika makaburi yote mawili.

    Alifanya hivyo ili kukomboa wakati kwani makaburi hayo yalichimbwa katika eneo moja. Baada ya zoezi hilo Mchungaji alichukuwa mchanga kiasi na kutupa ndani ya kaburi huku akisema maneno haya:“Umetoka mavumbini na mavumbini umerudi,Bwana ametoa na Bwana ametwaa Jina lake libarikiwe. kisha akafanya hivyo kwa kaburi la Bi Nacharo, mwishowe akamalizia kwa sala maalumu Hatimaye ibada ya mazishi iliishana watu walitawanyika.

    Mzee Kihedu na mke wake pamoja na Mjukuu wao Ramson walibaki na majonzi makubwa sana. Kubembelezwa hakukufaa kitu kwani Kimbe kwao ndiye aliyekuwa kila kitu. Alikuwa ni mtoto wao wa Pekee ambaye walimtegemea kusimamia mali walizokuwa nazo. Lakini mwisho wa yote walikubaliana na ukweli kuwa Mungu amewapenda zaidi. Walijikusanya tena kuweza kuendelea na maisha ya kawaida. Hali ilikuwa tofauti kwa Ramson kwani vifo vya wazazi wake aliviona kwa macho yake mwenyewe. Mara kwa mara aliota hali hiyo na wakati mwingine ilimjia katika mawazo yake kana kwamba inatokea sasa hivi. Majonzi yake hayakuisha mapema maana alikumbuka kila saa upendo wa wazazi wake.

    Babu yake na bibi yake walimfanya asiwaze kwa kumtendea mambo mazuri ya kumshangaza kila wakati,kusudi asahau msiba ule lakini haikusaidia sana. Alizidisha Utulivu kwa kutafakari kwa kina mambo yaliyomtokea. aliwapenda sana babu na bibi yake. Walichukuwa nafasi ya wazazi wake lakini bado pengo lao lilikuwa wazi kabisa siku zote.

    Pamoja na yote hayo aliendelea vizuri na masomo yake ya Chekechea, mwaka uliofuata alitarajiwa kujiunga na darasa la kwanza katika Shule iliyokuwepo kijijini hapo. Alikuwa na akili katika masomo yake na pia alikuwa na kipaji maalumu cha kuchora akiwa katika umri huo mdogo. Babu na bibi yake walimfurahia sana. Waliishi naye kama mtoto wao na sio mjukuu. walikuwa wanamchukulia kama Kimbe wao aliyefariki ghafla kwa ajali.



    Ilianza kama mzaha sana unaoumiza moyo. Mzaha wa kitoto uliofanywa na watoto wenyewe wakati wa michezo yao ya kitoto: “Mwizi”! hayo ni maneno yaliyotamkwa na mmoja wa vijana kwenye kundi moja lililojadili unadhifu wa Mmoja wao kijijini hapo. Kila wakati vijana hao waliumiza vichwa vyao kutafuta nini cha kufanya ili wamharibie kijana huyo mpole na mwenye bidii.

    Mioyo yao iliuma kwa wivu juu ya maendeleo ya Kijana mwenzao. Hali ya uvivu ilishamiri kwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho. Wengi walipokea urithi kutoka kwa wazazi wao na babu zao mashamba makubwa ya Minazi. Kwa hiyo hawakuona haja sana ya kushughulika na kazi za mikono zaidi ya kuwa na vishamba vidogo tu vya kulima mazao ya kukithi mahitaji ya chakula.

    Wengi walikuwa wakikaa tu vijiweni na wengine kwenye vilabu vya pombe ya mnazi na kucheza bao, huku wakingojea kuvuna nazi tu zinapokomaa. Tabia ya wazazi ikachukuliwa na watoto wao kizazi hadi kizazi mpaka ikazoeleka. Mazoea haya ya kukaa tu na kucheza kwa kutegemea kurithi mali za wazazi ambao nao walirithi toka kwa wazazi wao ilifanyika kama ugonjwa. Hali hii iliwakumba hata wale ambao hawana kitu cha maana cha kurithi pindi wazazi wao wanapoondoka katika dunia hii. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ugonjwa huu wenye jina maarufu lijulikanalo kama “Uvivu” liliwafanya vijana wote wakae tu vijiweni bila kazi. Hali hii haikukemewa na wazazi wao kwa sababu nao pia walikuwa hivyo hivyo. Kutokana na kukaa bila kazi tabia nyingi huzaliwa. Tabia ya kukaa vijiweni zilizaa maovu mengi sana yakiwepo utumiaji wa bangi, hatimaye madawa mengine ya kulevya. Tabia hizi nazo zikazaa udokozi na hatimaye wizi wa mifugo, ubakaji na mambo mengine kama hayo. kwa ujumla vijana wengi wakawa na magenge ya siri.

    Magenge yaliyosababisha maovu mbalimbali kijijini hapo na vijiji vya Jirani. Lakini katika kijiji hiki aliishi kijana mmoja aliyekuwa tofauti na wengine. Kijana huyu si mwingine ila ni Ramson Kimbe! Upole wake na uchapa kazi vilimfanya awe tofauti kwa kila kitu. Umaridadi wake katika mavazi na maendeleo yake katika masomo, pamoja na mafanikio ya familia yake, vilimfanya awe tofauti sana. Kijana huyu ambaye anaishi na babu na bibi yake alikuwa na msimamo wa maisha yake binafsi.

    Hakuridhika na mali za babu yake, japo alijua kuwa yeye ndiye mrithi wa mali hizo. Kutoridhika kwake kulimfanya azidishe bidii kwa masomo yake na kazi za shambani. Japo alikuwa na umri mdogo lakini alijitahidi kufanya kazi mbalimbali akisaidiana na babu yake. Alikuwa na mashamba yake mwenyewe aliyoyasimamia kwa kuyalima na kuweka vibarua, kazi ambayo babu yake alimsaidia.

    Akiwa darasa la tano alikuwa ni kinara kwa umaridadi shuleni kwao na katika masomo alikuwa akiongoza pia. Umaridadi wake na ufahamu mkubwa katika mambo mbalimbali, vilimfanya apendwe na waalimu na watu mbalimbali kijijini hapo. Sifa zake hizo zilimfanya pia kupata maadui wengi wakiwepo vijana wenzake na watu wazima, waliokuwa na husuda kutokana na maendeleo yake.

    Mambo haya yote yakifanyika bila yeye kujua lolote. Maisha kwake yaliendelea kama kawaida. Aliendelea kupanda na kuwa zaidi ya jana kila siku kutokana na mafanikio yake. Hakutaka kukaa vigenge wala majungu, kutokana na tabia yake hii alikosa marafiki kabisa. Vijana wengi walikuwa wavivu sana na wenye tabia mbaya. Kila aliyejaribu kuwa rafiki yake alimshauri kufanya kazi kwa bidii, ili kutengeneza hali ya maendeleo kwake binafsi na kijiji chao. Alipenda sana kuangalia maisha yajayo na kwamba matayarisho ya maisha bora ya sasa na ya baadaye yanamhitaji mtu mwenyewe.

    Bidii na ubunifu kwa kazi ni sehemu ya maendeleo hayo yanayotamaniwa na wengi. Sera zake hizo zikaonekana kama Hadithi za ajabu kwa vijana wa rika lake, kwani walijua majukumu yote kwa umri wao yanabebwa na wazazi wao. “Kujitwisha majukumu mazito ya kufikiria maisha ukiwa mdogo, ni kujibebesha mzigo usiokuhusu.” Hayo ni baadhi ya maneno ya marafiki za Ramson waliokuwa wakimshauri apunguze harakati zake za kuyasaka maisha bora. Umri wake ukilinganishwa na mambo aliyokuwa akiyafikiria waliona kuwa havikulingana kabisa na yeye.

    Pia ukichukulia kuwa Babu yake mzee Kihedu alikuwa ni tajiri wa mashamba na mifugo. Mali zote alizokuwa nazo Mzee Kihedu zote zilikuwa za Ramson, kwakuwa Mzee huyo hakuwa na mtoto mwingine zaidi ya baba yake Ramson ambaye ni marehemu kwa sasa. Hata babu yake alikuwa akimshauri atulie na kuangalia masomo tu kwa kuwa kila kitu kipo sawa ila Ramson aliendelea na msimamo wake na bidii katika mashamba hasa kusimamia na kufanya kazi.

    Mwisho wa yote Mzee alinyamaza kwani hakuona kama kuna tatizo kwakuwa katika masomo Ramson hajawahi kupoteza maks zake. Alishikilia namba moja kwa kila mtihani na kazi za nyumbani alikuwa yuko vizuri. Kutokana na bidii yake babu yake alikuwa akimnunulia nguo nzuri sana kila mara hadi kusheheneza mavazi tele ya thamani. Nguo na viatu vya shule alinunuliwa pea nyingi. Alikuwa akibadilisha viatu kila siku na nguo zake za shule zilikuwa safi kila mara.

    Mara kwa mara alipewa zawadi ya kuwa Mwanafunzi msafi shuleni kwao. Na mtaani mara tu baada ya kumaliza kazi zake za shamba alikuwa akivaa mavazi mazuri na mifukoni mwake hakupungukiwa na hela. Pamoja na yote hayo Ramson hakuwahi kujihusisha na tabia za uhuni. Wasichana wengi walimfuata wakimtaka urafiki, mitaani na hata shuleni, lakini alibaki kuwaheshimu kama dada zake tu.

    Kati ya mambo aliyoyazingatia ni pamoja na wosia wa babu yake aliokuwa anamwambia kila wakati kuwa: “Mambo yote mazuri ni mazuri kwa wakati wake, ukiyaharakisha yanakuwa machungu kuliko shubiri!”Pia mzee huyo alikuwa anamwonyesha baadhi ya vijana kijijini hapo wanaougua ukimwi na wale waliopoteza maisha yao kwa sababu ya kuharakisha mambo. Haya yalikuwa mausia mema kabisa na kwa busara alizokuwa nazo Ramson alizingatia na kujiepusha na mambo yote mabaya.



    * * * * *CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nimesema hilo wazo nililotoa linafaa sana kumbambikizia huyu mwendawazimu! Unajua kama tutasema kuwa ni mwizi hiyo inaweza ikakubaliwa na watu wengi kwa sababu ya jinsi anavyopiga pamba za ghali kila mara.” Alisema kijana mmoja aitwaye Rafa katika moja ya vikao vyao vya kutaka kumharibia Ramson sifa. “Lakini wewe hujafikiri vizuri juu ya wazo lako hili! Nakwambia mwanangu hapo umekurupuka; hebu angalia mwenyewe jamaa alivyo na bidii katika kazi ninani asiyejua hilo? Kama tukiulizwa kuwa tuna ushahidi gani tuna lipi la kuonyesha?”

    Alimaliza kwa hoja Abuu kijana aliyekuwa akijihusisha na biashara ya kuuza misokoto ya bangi kwa wahuni wote kijijini hapo. “Aaaa! Hilo mwanangu mbona rahisi? hujaona mtu akibebeshwa zigo la bangi na kuhukumiwa kwenda jela mvua kadhaa kumbe msala ulikuwa sio wake kabisa? Sawa kabisa Mchizi! unajua hapa la maana ili huyu mtoto asizidi kutunyanyasa na kuonekana sisi hatuna inshu kutokana na mambo yake kuwa safi inabidi kumchomea nguru! Hebu basi Tumsikilize bwana mipango tuone mbinu zake atakazotuambia.” Alisema Alen aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo aliyekuwa amekaa kimya muda wote.

    Wote walimgeukia Beka ambaye alisifika kwa kutoa mawazo ya hapo kwa hapo na yenye viwango vikubwa. Huyu bwana alikuwa na akili nyingi sana katika kupanga mambo mabaya! mipango ya kuiba na hata kuua. Kuna wakati waliwahi kufanya uhalifu katika duka la mhindi kijiji cha tatu kutoka kilipo kijiji chao. Waliiba mashine ya kukatia miti iitwayo Chensoo!

    Walipogundua kuwa mfanyakazi yule amewagundua walikwenda kuificha mashine ile na kurudi kinyemela ili kumfuatilia wajue kuwa atafanya nini! Walipofikawakamkuta amemwamsha mhindi na walikuwa katika harakati za kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi. “Umesema iko nafahamu miji ote ee”! Aliuliza mhindi huyo. “Ndiyo mzee nawafahamu wote wako kijiji kile anakoishi Kishori!”

    “Basi kimbia bana nenda ambia polisi wao nakamata miji ote sawa?” Mhindi alimwamrisha aliamrisha mfanyakazi wake aitwaye Kihoba.Naye alianza safari usiku huo akielekea Kituo cha polisi. Kituo cha Polisi kilikuwa umbali kama wa dakika tano hivi. Baada ya kutoka aliteremka kilima kidogo kwa tahadhari, lakini kabla hajaenda mbali alivamiwa na kundi la akina Beka na asubuhi yake alikutwa amekufa kando ya njia. Msako wa kutafuta wauaji haukufanikiwa na mhindi yule wala hakujitokeza kuzungumzia habari za wizi uliofanyika dukani kwake. Hii ilisababisha uchunguzi kukosa mwelekeo mzuri. “Tunakusikiliza Beka.” Alen alimshtua Beka kwenye lindi la ukimya akiwa anatafakari njia ya kufanya. “Okay! Nimeona kwa wakati huu tunaweza kufuatilia nyendo za kijana mahali atakapokuwa kesho baada ya kutoka shule. Kisha tutajua la kufanya baada ya hapo. Kwa sasa inabidi tumtume dogo Sam ili afuatilie hilo halafu akitujulisha ratiba yake ya kesho usiku huu huu tutajua la kufanya sawa?” Wote wakakubaliana na Sam alitumwa kumfuatilia.



    * * * *

    Baadhi ya wanakijiji walikuwa wamemzunguka Ramson akiwa shambani kwao. Zogo lilikuwa limetanda mahali hapo kila mmoja akitoa shutuma kwake na wengine wakitaka kumpiga. Chini yake kulikuwa na mfuko wa nailoni wenye vitu mbalimbali vya dukani; mzigo uliosemekana kuwa Ramson aliuiba dukani kwa Mpemba. Ramson alivimba uson kwa kipigo na alichaniwa nguo zake katika kurupushani ya kumlazimisha kubeba mzigo ule na kuelekea Kituoni.

    “Jamani siwezi kubeba mzigo huu, sio wangu na sijahusika kuiba vitu hivi.” alijitetea Ramson huku akilia kwa uchungu. “Kijana usitutanie kabisa beba mzigo wako na uongoze njia twende kituoni; tulizani ni kijana mpole na mchapakazi kumbe ni mwizi tu!”Alisema jamaa mmoja aliyekuwa mstari wa mbele katika kutoa adhabu kwa Ramson.Mwishowe walimnyanyua kwa nguvu na kumbebesha mzigo ule huku wakimpiga vibao na wengine wakimchapa kwa fimbo. Walimfikisha kituoni na kumfungulia jalada na hatimae wakamwingiza mahabusu.

    Ramson alikuwa katika wakati mgumu sana, sio kwa kipigo alichokipata bali kwa uzushi aliofanyiwa. Katika maisha yake hajawahi hata kufikiri kuhusu wizi. Mpaka kufikia umri alionao alikuwa ameshayamudu maisha yake kuliko hata baadhi ya wakaazi wa kijiji hicho. Mbali na mashamba mengi aliyokuwa nayo babu yake na mifugo, mbali na kuwa urithi wote wa mali hizo ni wake, lakini yeye mwenyewe alikuwa akisimamia mashamba ya marehemu baba yake kwa bidii sana.

    Alikuwa na maisha mazuri na hakuwahi kupungukiwa na kitu. Huo ndio ukweli binafsi wa maisha yake, ukweli unaojulikana na baadhi ya wanakijiji, ukweli ambao umefumbiwa macho na masikio ili kumdidimiza katika shimo la takataka na kuuchafua utu wake. Moyo wa Ramson uliuma sana kuliko maumivu yenyewe, kwa kupakwa matope na kuharibiwa sifa yake aliyojaribu kujitengenezea kwa umakini mkubwa. Hili ni doa lisiloweza kufutika kwa baadhi ya vichwa vya watu. Uelewa wa mambo kwa watu unatofautiana kulingana na fikra kuwa tofauti.

    Jambo moja zuri sana linaweza kufanyika kati ya watu, lakini uzuri wake ukapatiwa tafsiri nyingi na watu waliopo. Wengine watasema ni zuri sana wengine watatoa kasoro uzuri wake na wengine watasema ni baya. “Haiwezekani nizushiwe mambo mabaya kiasi hiki! ina maana watu hawaoni badii yangu na uadilifu wangu ndani ya kijiji hiki?” Hivyo ndivyo alivyokuwa akitafakari Ramsoni katika chumba kidogo cha mahabusu kilichokuwa na harufu mbaya ya mikojo. Hali ya mawazo mbalimbali yalipita kichwani mwake akiwa hajui la kufanya katika kiza hicho kigeni katika maisha yake. Alijiona akiwa katika kona mbaya sana! kona iliyokusudiwa kuharibu mipango ya maisha yake ya baadaye.

    Mawazo ya kuwa mtu maarufu mwema na mwenye kusababisha maendeleo kwa nchi yake viligeuka kuwa ndoto ya mwendawazimu. Kashfa ya wizi ilimvunja nguvu kabisa na kumwathiri kifikra. Aliwakumbuka wazazi wake aliotaka kuwaenzi katika maisha yake kwa kuwa mtu mchapakazi na msomi.

    Alifikiri juu ya bidii zake katika kazi na uaminifu wake kwa jamii iliyopo kijijini hapo. Baadaye alishindwa kuelewa kuwa ninani aliyeleta mzigo ule pale shambani tenandani ya kibanda chake cha kupumzikia baada ya kazi? Hofu ilimkamata alipofikiria kuwa babu yake atakapopata habari hizi atamchukuliaje? moyo wake uliuma sana na ghafla machozi yalimtoka kwa huzuni kubwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    * * * *

    “Nafikiri tuna sababu ya kujipongeza maana yule mtanashati ameingia matatani!” Alisema Beka kwa majivuno huku akiwasha msokoto wa bangi. “Ule mchezo ulikuwa kiboko mtu wangu. Pale hachomoki au mnasemaje masela wangu!” Aliropoka Alen mkuu wao wa kundi.

    “Unajua watu wengi huingia matatani hivihivi kwa kubambikiziwa kesi bila wao kuhusika?” Alisema Abuu kisha akaendelea. unajua kwanini watu wangu wa nguvu? Ninakumbuka kupata taarifa nyingi ndani aidha ya mitandao na hata kwenye Televisheni zikizungumzia habari za matukio yaliyowapeleka watu wengi gerezani au kukutanishwa na kitanzi.

    Kesi hizo si za kweli bali wamebebeshwa tu kama hivi! Upelelezi mwingine unafanyika juu juu tu na kuacha ukweli wa jambo ukipepea na kupotea machoni mwa sheria dhidi ya mtuhumiwa. Wengi walipewa mizigo ya madawa ya kulevya kwenye mabegi yao ya safari bila wao kujua. Wanapofika Airport wanashangaa wakati wakiingizwa matatani.

    Ili ujue kweli wamebambikiwa ni pale mtu anapokiri kuwa mizigo ile ni yakwake wakati wachunguzi wakishaipima na kuona kuwa kuna madawa ya kulevya. Hawezi kukana begi lake wakati anajua halina chochote ndani kibaya, baadaye watu hawa hufunguliwa mashtaka na kufungwa kizembe sana, kumbe hawakuhusika. Mchezo huu kaucheza vizuri sana Beka kwa yule mtoto wa marehemu!” Alisema Rama kwa Utani zaidi huku akisababisha wengine kuangua kicheko cha dhihaka.

    “Ninakumbuka jinsi Nilivyomfuatilia baada ya kuiba pale kwenye duka la mpemba. Nilibeba ule mzigo nikifuatana na dogo Sam kumfuatilia kijana mpaka shambani kwao. Alipofika hakukaa sana kwenye kibanda alitoka na kuelekea kwenye kisima chao ili achomeke mpira wa kunyweshea. Kwakweli yule kijana nimemhusudu sana kwa bidii zake. Kuna wakati ninafikiri kufuata nyayo zake lakini ninajiona nimeshachelewa.

    Kuanza kugumu heri mwenzetu ameyakuta yametayarishwa na babu yake na marehemu baba yake. Sasa ukiambiwa wewe uanze mpaka kufikia hatua ile utasota sana na siajabu usifikie kutokana na kukosa zana za kazi na mtaji. Baada ya kumwona akienda kuchomeka mpira kisimani, niliingiza ule mzigo kwenye kibanda chake na kutoka mbio. Nilimpigia mpemba nikiwa njiani karibu na kijijini kumwarifu kuwa baadhi ya bidhaa za dukani kwake zimefichwa kwenye shamba la Mzee Kihedu na kijana wake ndiye mwizi.”

    Alihitimisha Rama sehemu ya taarifa ya kazi aliyopewa na kundi lile. “Enhee! Mpemba alivyokuuliza wewe ninani ulimjibuje?” Aliuliza Alen. “Swali hilo aliuliza mwanzoni wakati akipokea simu, lakini aliposikia taarifa za kupatikana kwa baadhi ya mali zake akasita ili asikilize kwa makini.

    Mwishoni ndio akauliza kwani ninaongea nanani?! Nililisikia sana swali hilo ila nilikata simu kabla sijajibu lolote.” Umefanya vizuri dogo ila hakikisha namba yako unaibadilisha mapema kwa sababu inaweza ikagundulika tukaingia matatani.” Alisema Aleni kwa msisitizo.



    * * *

    Mawazo yake yalikatishwa ghafla sana kwa kishindo cha kufunguliwa kwa mlango wa chuma wa mahabusu hiyo. Mara baada ya kufunguliwa mlango kwa makeke ya aina yake askari mmoja mweusi na mwenye macho makali alijitokeza na kuita Ramson Kimbe!” Ndani ya chumba kile cha mahabusu hakikuwa na wahalifu wengine..

    Hivyo Ramson aliitika na kusimama. “Njoo nje mara moja.” Aliamrisha askari yule na Ramsoni alimfuata mpaka mapokezi. Moyo wake uliruka mapigo kama mawili mfululizo baada ya kumwona babu yake amekaa kwenye kiti akimsubiri. Uso wake wa upole lakini wenye aina fulani ya mshangao ulimtuliza kidogo Ramson na kumsalimia kwa unyonge kidogo. “Shikamoo babu.”

    “Marahaba Mjukuu wangu, pole sana kwa matatizo. Nimekuja kukutolea dhamana mengine tutakwenda kuyaongelea nyumbani.” Baada ya Ramson kukabidhiwa vitu vyake, wakaanza safari ya kurudi nyumbani. Njiani walikuwa kimya sana. Kila mmoja akiwaza lake moyoni kati ya Ramsoni na babu yake. Nyumbani walimkuta Bibi akiwa katika majonzi ya aina yake huku akiwa kashika tama.

    Alipomwona Mzee Kihedu na mjukuu wake alishangilia sana! “Ooo mjukuu wangu! pole sana kwa matatizo!” Alimkumbatia mjukuu wake na kumshika mkono na kuingia naye ndani. ..Kisha akaendelea..“Pole sana Ramson kwa matatizo. Tunajua jinsi tunavyochukiwa katika kijiji hiki cha Tabu ya nini! Hizo zote ni njama tu za watu wabaya wanaoyachukia maendeleo yetu.”

    Alisema bibi sauti ya majonzi akionyesha kuwa alikuwa na mzigo mzito sana moyoni mwake. “Usiogope Ramsoni tutafanya mpango kesi hii haitaenda mahakamani, niko tayari kutoa kiasi chochote cha fedha kulipa, lakini sitakuwa tayari uathirike kisaikolojia.” Alisema babu kwa msisitizo na kumfanya Ramson apate nafuu kubwa moyoni mwake kwa kujua kuwa kumbe familia yake haijaamini njama za maadui zake.

    Hii ilimpa nguvu hata ya kuelezea jinsi ilivyotukia. “Kwakweli sijajua ninani walionifanyia njama hizi, maana wamesababisha jina langu kuchafuka kabisa kijijini hapa.” Hilo usijali sana Kijana wetu njama zao zitafichuka na ukweli utajulikana na wewe utabaki msafi kama ulivyo!”

    Hakuna ubaya unaodumu katika vita kati yake na wema. Wema ni kama nuru na ubaya ni kama vile giza. Giza linatoroka na kupotelea mbali pale nuru inapotokea. Waswahili wana msemo wao wa busara usemao”“Ukweli ukisimama uongo hujitenga.” Iko siku Mabaya yanayofanyika kijijini hapa yatabainika, na wabaya wote na njama zao Watawekwa wazi.” Babu Kihedu alisema hayo kwa uchungu mkubwa.

    “Nenda kaoge mjukuu wangu ubadili nguo ili upate chakula.” Bibi alimwambia mjukuu wake. Ramson alifanya hivyo huku akipata moyo wa matumaini kwa maneno ya babu na bibi yake. Baada ya matayarisho yote alipata chakula na kwenda kupumzika. Mzee Kihedu alirudi Kituoni asubuhi ya pili na kukutana na mkuu wa kituo. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nia yake ni ili mambo hayo yasiende mahakamani. Mpemba aliitwa na kutakiwa wayamalize kwa kulipwa vitu vilivyoibiwa. Baada ya kuzungumza machache Mzee kihedu alimwambia Mpemba:“Iko siku Ammi utajagundua wabaya wako. Ninakumbuka wakati Ramsoni akiwa Chekechea ulivunjiwa duka lako hadi ukaanza upya kujenga na kulianzisha tena. Hali hii ilijirudia mara nyingi na wahalifu hawajawahi kutiwa ndani.

    Leo Mjukuu wangu ndio anabambikiwa tatizo hili la wizi. inaniuma sana.” Alisema Mzee Kihedu kwa masikitiko.“Lakini Mzee kihedu kumbuka anayeshikwa na manyoya ndiye mwizi wa kuku; kwa hiyo usilalamike zaidi ya kulipa gharama na kukaa vema na mjukuu wako umkanye tabia zake hizi.Alimalizia Mpemba kwa maneno yake yanayoonyesha kutokuamini maneno ya Mzee Kihedu. Mzee Kihedu alilipa vitu vile vilivyotolewa kizibiti na gharama za mlango uliovunjwa kisha akaondoka kituoni hapo.



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog