Simulizi : Mtu Wa Ufukweni (The Beach Man)
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni kesi ambayo ilikosa mahali pa kusimamia. Kesi Isiyo na ushahidi wowote wala mwelekeo hasa. Baadaye uchunguzi ulifanywa na Polisi haukuona kuwa Ramson alihusika kwa lolote. Ilionekana kwamba muuaji ni Dr. Jackson ambaye alimpiga risasi mkewe na kutaka kumuua Ramson badala yake risasi ikampiga ya mguuni. Baadaye alijipiga risasi ya kichwa mwenyewe. Uchunguzi wa alama za vidole kwenye bastola ile uliona kuwa mtumiaji wa silaha hiyo alikuwa ni Jackson mwenyewe.
Wakati upelelezi wa haya yote unafanyika, Ramson alikuwa Hospitali akitibiwa akiwa chini ya ulinzi. Mpaka anapata nafuu kubwa kwenye jeraha lake la mguu, upelelezi ulimwondoa kwenye shutuma na baadaye walimwachia huru. Ramson alitoka Hospital asijue la kufanya. Ila alikumbuka kuwa karatasi zile alizificha sana baada ya kukabidhiwa na marehemu Dr Jackson.
Alipoingia kwenye gari la Jackson aligundua picha na vyeti. Picha zile zilimwonyesha yeye akiwa na mke wa Dr. Jackson wakiogelea na nyingine zilizokuwa na ushahidi pia vitu vte hivyo alivificha pamoja na zile hela. Alifanya hivyo kusudi kuondoa ushahidi wa yeye kuhusishwa na vifo vya Dr. Jackson na mkewe.
Hii pekee ndiyo iliyomweka mbali na kesi ya mauaji hayo. Baada ya yote hayo Wafanya kazi wake walipokuja aliwaaagiza wampeleke mtoto kwa mmoja wa rafiki zake. Simu aliyompigia rafiki yake huyo ilimfanya akubali kumtunza mtoto huyo, hadi hapo mambo yatakapotulia. Katika maficho alikozificha karatasi zile na fedha alizokabidhiwa na Marehemu Mary palikuwa salama. Baada ya kurudi akiwa huru alikuta vitu vikiwa vile vile kama alivyoweka.
Alikaa na kuamua kusoma makaratasi yale aliyopewa na Dr. Jackson, maana tangu apewe hajawahi kuyapitia na hakujua kuwa yalihusu nini! Mwili ulimsisimka sana baada yakusoma kichwa cha habari! Maneno yaliyofuata yalimfanya apanue mdomo kwa mshangao! Kila hatua aliyoipiga katika kusoma maneno yaliyopo pale, vilimfanya aduwae! Ilikuwa ni zaidi ya habari! Ilimshangaza na kumshtusha kwani ndani ya karatasi zile Dr.Jackson alirudia kusema kuwa, hakuwa na budi kufa kwa sababu hataweza kustahimili kuishi bila Mary mkewe!
Na pia asingevumilia kupata hukumu ya mauaji ya mkewe ambayo mwenyewe hakukusudia kufanya hivyo. Lakini jambo la msingi ni kwamba hakuwa na ndugu hata mmoja, ila wazazi wake tu ambao wako kijijini nao ni wazee sana. Kwa hiyo ameamua kumrithisha Ramson mali zake zote, ambazo ni pamoja na mahotel mawili ya kitalii yaliyopo Lushoto mjini.
Makampuni ya usafirishaji iliyopo jijini Dar es Salaam. Mashamba mawili yenye heka kumi kila moja, moja likiwa Lushoto na jingine likiwa Korogwe Pia kulikuwa na nyumba tatu; Moja ikiwa hapo mjini Tanga na nyingine ikiwa Arusha na nyingine ilikuwa Ostabay Dar es Salaam.
Fedha zilizoko Bank zilikuwa ni Shilingi milioni mia sita na hamsini. Mwisho wa yote akamwambia atafute wakili kwa sababu yeye pamoja na mali zote hizo hakuwahi kuweka wakili binafsi. Wakili atakayemweka amsimamie katika kubadilisha hati za umiliki wa mali zake, kutoka jina la Dr. Jackson Kigoi kwenda jina lake yaani Ramson. Hakujua aanzie wapi baada ya kuona mambo hayo.
Alimshangaa sana Dr. Jackson kwa moyo wake wa ajabu! Alikaa na kuangalia jinsi ya kufuatilia mambo ya sheria kwa ajili ya kuwakilisha barua ile. Alijua kuwa ile ndiyo itakayomsaidia pindi atakapoifikisha kwa mwanasheria. Alijua kuwa huko atapata mwongozo wa namna ya kusimamia mali zile za Marehemu Dr.Jackson. Akili hazikutulia kabisa! Alikuwa na mchanganyiko wa mawazo.
Moyo wake ulikuwa umejaa huzuni na mawazo mengi, kwa mtihani mkubwa sana aliopewa na Dr. Jackson. Kwa ujumla alikuwa hajui aanzie wapi ili kuziweka malizote zile chini ya himaya yake. Kichwa kilijaamambo mengi na baadaye alijikuta akipitiwa na Usingizi. Usingizi huu uliomchukuwa muda mrefu kabla ya kuamka na kutafuta jibu la mitihani iliyopo mbele yake.
Ramson Aliingia ndani baada ya kufunguliwa mlango! Aliitikia salamu ya dada aliyemfungulia mlango na kuingia ndani. Sebuleni alimkuta mzee Kigoi akiwa amekaa na mkewe. baada ya salamu Ramson akaanza mazungumzo. “Wazee wangu naomba sana mnisamehe kwa kusababisha kifo cha Dr. Jackson!”
Nikijieleza ni habari ndefu sana lakini naomba mnisamehe sana kwa yote wazee wangu.” Alisema hayo huku akilia machozi mbele ya wazee hao. ..kisha akaendelea: “Mimi ndiye Ramson mmiliki wa ufukwe wa mwahako ambako Dr. Jackson na mkewe walipofia. Nimetafuta sana nijue mahali mlipo wazee wangu mpaka nimefika leo. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baba na mama naombeni mnisamehe juu ya yote yaliyotokea.” Alihitimisha na kunyamaza kimya ili asikie kile wazee hao watakachosema. “Kijana Hebu inuka ukae na ufute kabisa machozi yako.” Alisema Mzee Kigoi na Ramson akanyanyuka na kukaa kwenye kochi lililokuwa kando yake; alipokuwa ametulia Mzee Kigoi aliendelea: “Huwezi kuomba msamaha kwa kazi ya Mungu kijana.
Mimi ninavyojua ni kwamba Mwanangu Jackson alikufa kwa siku zake! Potelea mbali kama kulikuwa na sababu gani lakini ninachojua ni kwamba kifo chochote hakikosi sababu au mlango wa kupitia. Wewe uwe na amani kabisa sioni wapi umekosea katika msiba huu.” Alisema Mzee Kigoi na kumtazama mkewe aliyekuwa kimya wakati wote.
“Kijana mimi na baba yako hapa ni wazee sasa. mambo mengi tumepitia na wasawahili wanasema: “Kuishi kwingi ni kuona mengi. Tunajua mengi na tumejifunza mambo ya ajabu sana katika maisha yetu haya. Tunajua kuwa kifo chochote kinapompata mtu kinatafuta pa kupitia tu. Pia kifo hicho hakiji hadi wakati wa mtu uwe umefika. Kama wakati haujafika kifo hukaa mbali kabisa na wala Jackson na mkewe wasingelikufa. Lakini ninavyojua ni kwamba kila jambo hupangwa na mwenyezi Mungu. Asingepanga mtoto wetu asingelikufa.
Kwa hiyo mwanangu uwe na amani tu.” Alisema hivyo mke wa mzee Kigoi akimwondoa wasiwasi Ramson. “Asanteni sana wazazi wangu.” Baada ya hapo Ramson aliwasomea ile karatasi aliyopewa na Dr. Jackson kisha baada ya hapo akasema: “Wazazi wangu kuja kwangu hapa kuwatafuta ni ili pia niwaachie jukumu hili. Kwangu mimi sistahili kurithi hata shilingi moja. Nitasimama pamoja na wewe baba katika kuhakikisha kuwa mali hizi zote zinaingia mikononi mwako.” Alisema Ramson akiwa kashikilia karatasi ile. “Kijana wewe ni mtu wa ajabu sana!! Alifoka Mzee kigoi,
“Sijaona mtu mwenye busara kama wewe katika maisha yangu! Wenzio wanalilia mali mpaka kudiriki kushikilia silaha na kumwaga damu za watu wewe unapewa kihalali mali hizi na unazikataa!” Aliongea kwa mshangao mkubwa Mzee Kigoi na kumgeukia mkewe ambaye naye aliishia kuguna tu na kutoa tabasamu la mshangao. .. kisha akaendelea “Mimi na mama yako tunakupokea rasmi leo kuwa mtoto wetu. Mali zote hizo utazisimamia wewe!”
Kama marehemu Jackson amefikiria mpaka akaamua kukuandikia maneno haya juu ya mali zake zote, moja kwa moja amekuidhinisha kuwa mtoto wetu badala yake. Huna haja ya kutupa sisi mzigo ambao hatutauweza. Uzee tulionao huu tutaweza wapi kuingia kila mahali kutafuta sijui hati gani za umiliki wa vitu hivyo?
Sisi kwa moyo wote tunakupa baraka zote, kama alivyofanya ndugu yako nenda kashughulikie hayo mambo. Ikiwa kuna mahali nitatakiwa kuja kudhibitisha lolote nitafanya hivyo. Jukumu lako litabaki kututunza sisi wazazi wako kama alikuwa akifanya marehemu kaka yako sawa?” Alihitimisha Mzee Kigoi na mama alimuunga mkono.Baada ya hapo Ramson akaagana nao na kuingia Rasmi katika michakato na majukumu mapya.
Kila kitu kilienda kama kilivyopangwa. Wazazi wa Dr. Jackson walihamishwa kutoka kijijini na kupewa nyumba nzuri na ya kifahari Mjini. Ramson aliwawekea wafanyakazi wa kuwahudumia kwa kila kitu. Hoteli ziliendelea vizuri na makampuni yote. ufukwe nao ulitengenezwa na kuwa bora sana kwa kujengewa mahoteli ya kifahari ya kulala watalii.
Maboti mapya na ya kisasa yalinunuliwa. Kijiji cha Tabu yanini mkutano mkubwa ulifanyika. Ramson aliamua kufanya mambo ya kimaendeleo; ikiwa ni pamoja na kuweka mabomba ya maji badala ya visima na kujenga Hospitali kubwa na nzuri kabisa. Historia iligeuka na kumfanya Ramson kuwa mtu wa thamani kubwa anayetegemewa kwa mambo mengi.
Babu yake Ramson aliona fahari kubwa sana Baada ya kukamilishiwa nyumba yake mpya na nzuri kijijini hapo. Kwa ujumla Ramson alikuwa ndiye mfadhili katika kijiji cha Taabu yanini. Aligeuka na kuwa gumzo katika nchi yote, kwa kusababisha maendeleo na mabadiliko katika fukwe. Wengi walijaribu kuiga katika kutengeneza baadhi ya fukwe, hivyo alifanyika cheche yenye kuleta moto mkubwa wa maendeleo, katika fukwe za pwani ya bahari na hata katika maziwa makuu nchini Tanzania.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
* * *
“Hiyo ndiyo Historia kamili ya maisha yangu!” Nilisema huku nikimtazama Jobiso Baro usoni. Alikuwa ameduwazwa na safari yangu ya maisha jinsi ilivyokuwa na mabonde na milima mikali! Hakutaka kabisa kuikatisha hadithi yangu ya maisha kwa kuonyesha uchomvu! Niliushangaa uvumilivu wake. “Pole sana Brother na hongera sana kwa mafanikio makubwa uliyoyapata.
Ninakuahidi kwamba maandalizi ya Vipande vya Sinema yatakuwa tayari ndani ya wiki hii. Nitakuletea vipande vyako vya kuhusika na kazi itaanza mara moja.” Alisema Jobiso Baro kwa uhakika wakati akikusanya vifaa vyake vya kazi.” Kama tulioagana wote tulitazama saa. Mimi niliguna na mwenzangu alipiga mluzi wa mshangao! Kumbe nilitumia masaa kumi na mbili kusimulia Historia ya maisha yangu!
MWISHO
0 comments:
Post a Comment