Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

MTU WA UFUKWENI (THE BEACH MAN) - 4

 







    Simulizi : Mtu Wa Ufukweni (The Beach Man)

    Sehemu Ya Nne (4)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilipita miaka miwili baada ya uhusiano wa Ramson na Mary. Mtoto alishazaliwa na tayari alikuwa na zaidi ya mwaka mmoja. Alikuwa ni mtoto wa kiume aliyeitwa Lameck. Mara kwa mara Mary alikuwa anaenda Ufukweni na mtoto huyo, akiwa kaongozana Irene rafiki yake. Hata uhusiano wa kimapenzi kati ya Mary na Ramson uliendelea kwa namna ya usiri. Siku moja walipokuwa ufukweni walikuwa na mazungumzo kuhusu mtoto.

    “Naona mtoto amekuwa mkubwa sasa, unafikiri ni lini utanimalizia hela zangu ili nimsahau kabisa?” Alisema Ramson huku akimwangalia mtoto wake aliyekuwa amebebwa na Irene. Irene na Lameck walikaa kwenye viti umbali wa mita mia moja, wakati Mary na Ramson wakiwa kwenye mazungumzo yao. “Hilo lisikupe shida Ramson nadhani yote tulishayamaliza kwenye mkataba wetu, nilikwambia usubiri kiasi kilichobaki nikupatie wakati Dr Jackson akirudi nchini.

    Ninaamini kuwa unakumbuka hilo.” Alisema Mary kwa namna ya umakini sana huku akimtazama Ramson machoni ili maneno yale yamwingie sawasawa. “Ni sawa Mary lakini jamaa amekaa sana huko au ameongeza tena muda wa masomo yake?” Ramson Aliropoka! “Ramson naamini wewe ni mtu makini sana na unajua kila kitu sina nilichokuficha! Nilikwambia kuwa Dr. Jackson atakaa nchini Uingereza kwa muda wa miaka mitatu.

    Mpaka sasa ana miaka miwili na miezi saba. Miezi mitatu tu imebaki atarudi na kila kitu kitaenda kama tulivyopanga sawa?” Alisema Mary. “Sawa Mary nimekuelewa.” Alisema Ramson. “Nashukuru kwa kunielewa Ramson sasa ninaona ni wakati wa kurudi nyumbani kwaheri tutaonana siku nyingine.” Alisema Mary na kusimama kisha akaanza kupiga hatua kumfuata Rafiki yake Irene.

    “Sawa nitakupigia simu tuangalie namna ya kuonana tena siku mbili hizi sawa?” Ramson Alimwambia Mary. “Sawa.” Alisema Mary bila kugeuka na baada ya hapo Mary na Irene walinyanyuka na kuelekea lilipo gari lao. Irene alimpungia Ramson Mkono wa kwaheri wakati Mary akilitoa gari ufukweni hapo.



    * * *

    Yalikuwa ni mapokezi mazuri sana yaliyofanywa na watu wachache na wa muhimu katika Uwanja wa ndege. Uwanja huu wa Mwalimu J.K.Nyerere, ulifurika watu wengi jioni hii miongoni mwa watu waliokuwa hapa walikuwa ni Dr.Mudy, Mary na Mtoto Lameck. Dr. Mudy ni rafiki yake Dr.Jackson alikuwepo uwanjani hapa pamoja na Mary na mtoto Lameck ili kumpokea Dr. Jackson. Leo ilikuwa ndiyo siku ya kurudi kwa Dr. Jackson nyumbani Tanzania.

    Alikuwa na furaha sana kurudi tena nyumbani, baada ya kuishi kwa muda mrefu mbali na familia yake. Zaidi sana kilichomfurahisha ni juu ya kuzaliwa kwa mtoto Lameck. Shauku ya kumwona mtoto wake ilikuwa kubwa sana. Moyo wake ulikuwa na shauku kubwa sana ya kumwona mkewe mpenzi Mary.

    Hakupata picha furaha atakayoipata pindi atakapowaona Mke wake na mtoto wake. Aliona kama ndoto na baraka ya pekee sana kwa familia yake kuongezeka. Shauku yake ilizidi baada ya ndege kutua katika uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere. Aliona mchakato wa kukaguliwa mizigo kama inayochelewesha kuonana kwake na familia yake.

    Uvumilivu wake ulimsaidia mpaka zoezi hilo likaisha, baada ya hapo akasogelea maeneo ya mapokezi na ndipo alipomwona mke wake na mtoto. Furaha yake ilikuwa kubwa sana kuwaona naye mkewe akiwa na mtoto wake alimkimbilia mumewe na kumkumbatia kwa furaha. “Woooooow!!! Mume wangu mpenzi! Nimefurahi sana kukutana tena.” Alisema Mary akimwachia mumewe baada ya kukumbatiana kwa muda mrefu.

    “Mimi ni zaidi mke wangu. Nilikuwa ninaona kama ndege imesimama angani maana nilikuwa na hamu sana ya kuwaona na mtoto wangu mpenzi.” Alisema Dr.Jackson huku akimchukuwa mtoto toka kwa mama yake. “Vipi baba hujambo?” Dr.Jackson alimsalimia mtoto wake. Mara hiyo hiyo alijitokeza Dr.Mudy!“Mzee UK imekukubali sana!” Alisema Dr.Mudy huku akimgusa rafiki yake begani.“Oooohoo! Dr. Mudy!” Alifoka Dr. Jackson kwa furaha!“Ee bwana nimekusahau ghafla naona kitambi kinaanza kutafuta njia mzee!! Inaelekea bongo mambo mazuri sana.” Alisema Dr.Jackson kwa furaha sana baada ya kumwona rafiki yake Mudy.

    “Karibu sana rafiki yangu tumekumiss sana mtu wangu.” Alisema Dr.Mudy huku wakiongozana kwenda kwenye gari aliyokuja nayo Mary. Baada ya Dr. Jackson na mkewe na mtoto wao kupanda ndani ya gari, Dr. Mudy naye aliifuata gari yake na kuingia ndani tayari kwa safari ya kwenda nyumbani kwa Dr. Jackson Ostabay mahali ambapo Dr.Jackson alipanga kukaa na mkewe kwa siku tatu ndipo warejee jijini Tanga. Walipofika walizungumza mawili matatu wakati wakipata vinywaji kisha Dr.Mudy aliaga.

    “Jamani sasa na mimi ngoja nirudi nyumbani tutaonana kesho baada ya wewe kupumzika ili tuulizane habari za UK. vizuri.” Alisema Dr. Mudy. “Sawa ndugu yangu wewe nenda ukalale kesho jioni itabidi uje ili tuogee mengi.” Alisema Dr. Jackson huku akinyanyuka na kuingia ndani baada ya muda alitoka na mfuko mdogo na kumkabidhi Mudy.“Hii ni zawadi yako Rafiki yangu.

    Ninajua kuwa wewe ni mlevi sana wa vitu hivi.” Alisema Dr. Jackson. “Aiiiiiisee Loptop!.. Kwakweli siamini macho yangu!” Alisema Dr.Mudy kwa mshangao wa furaha! “Ndio nimekuletea rafiki yangu japo ucheze cheze Game!” Alisema Dr. Jackson huku akicheka. “Usifanye utani rafiki yangu unajua umenipa zawadi nzuri sana? Hapa Internate kwa sana na Game inapigwa vilevile! Alisema Dr. Mudy kwa utani. “Sawa ndugu yangu tuonane kesho basi alisema Dr. Jackson huku akimtoa nje ya geti na baadaye rafiki yake huyo aliondoka akiwa na furaha tele.

    Dr.Jackson na mkewe walikuwa na furaha sana hasa Jackson kwa kumwona mtoto aliyeamini kuwa ni mtoto wake. “Nafurahi sana kumwona mwanangu mpendwa Lameck. Kwakweli hatimaye leo aibu ya kuwa hatuna mtoto imefutika kabisa. Nimepata mrithi wa mali hizi na mtu muhimu wa kuendeleza mali zetu.” Alisema Dr. Jackson kwa furaha isiyo na kifani. Alikuwa akicheza na mtoto wake kwa muda mpaka akaanza kusinzia. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alinyanyuka na kwenda kumlaza kwenye kitanda chake. Waliongea mambo mengi sana wakiulizana hiki na kile kwa zamu. Baada ya muda mrefu wote walijikuta wamepitiwa na usingizi. Kwa Jackson furaha ilikuwa kubwa sana kwa kuungana na mke na Mtoto wake. Aliyafurahia maisha kwa namna ya ajabu sana.

    Ila kwa mkewe alikuwa na siri moyoni mwake. siri nzito ambayo kama ikifichuka na kujulikana kwa Mumewe Italeta adhari kubwa sana katika maisha yake. Siri hii ilikuwa ni kama bomu. Bomu linaloweza kuangamiza kabisa familia yake iwapo litalipuka. Moyo wake haukuwa na raha hata pale ambapo mumewe alionyesha furaha yeye alikuwa akifanya maigizo tu.

    Roho yake ilikuwa inamsuta kila saa anapomwangalia mtoto wake na kumwangalia mumewe jinsi alivyokuwa akimfurahia. Kwa namna Alivyokuwa haikuchukuwa muda mrefu Dr. Jakson alimgundua mkewe kuwa hakuwa na furaha sana ila alichukulia tu kuwa labda ni hali ya uchovu, au alikuwa huenda hajisikii vizuri. Zawadi alizompa zilimfurahisha sana Mary hivyo kumfanya asahau ile hali ya mwanzoni.

    Kesho yake walifunga safari kurudi uwanja wa ndege tayari kwa safari ya Tanga ambako ndipo walipoweka makaazi yao ya kudumu. Walifurahia sana kuwepo Tanga baada ya dakika arobaini kuwepo angani wakielekea katika mji huo. Kwakuwa walifika mapema Siku yao ilikuwa ni njema sana na wakati wa jioni ulipofika waliamua kwenda kupunga upepo baharini. Mwahako ndiko walikojichagulia maana walipapenda sana. Walipofika walikuwa na wakati mzuri sana wa kupumzika ufukweni hapo, huku wakizungumza hili na lile kwa furaha. Mazungumzo yao kati yake na Mudy yalihusu masomo.

    Walikumbushana mengi baada ya hapo hasa walipokuwa wakisomea nchini India miaka kumi iliyopita. Ramson aliwahudumia kama kawaida kwa vinywaji huku akimtupia Mary jicho la wizi. Mary alikuwa mtulivu sana jioni hii. Baadaye waliondoka na kurudi mjini wenye furaha kubwa. Kwa Ramson alikuwa na kidonda moyoni cha wivu, ambacho hakufikiria hapo mwanzo kuwa mapenzi yalikuwa yamebeba vitu kama hivyo.

    Kwake kumwona Mary amekaa na mumewe na kukumbatiwa, moyo wake ulipata tabu sana kwa wivu wa kimapenzi. Tangu akiwa mdogo hakuwahi kushiriki mapenzi na mwanamke yeyote, kwa hiyo hakujua kuwa ndani ya mapenzi kuna kitu kibaya sana kiitwacho wivu. Alikuwa anasikia tu kwa watu kuhusu mambo ya wivu wa kimapenzi, kwake aliona ni ujinga wa hali ya juu sana kumwonea mwanamke wivu. Leo imekuwa zaidi ya kituko kwa kumwonea wivu mke ambaye hakuwa wa kwake. Alipotaka kupotezea hali hiyo iliibuka kama moto! Ilikuwa haiepukiki.

    Kingine kilikuwa ni mtoto wake Lameck. Hakupenda kumwona yuko mikononi mwa baba mwingine, wakati yeye yupo. Hali ile ilimsukuma aone heri kuhamia mahali pengine ili awe salama. Aliona kwamba ikiwa ataendelea kuwepo mahali hapo iko siku kingetokea kitu cha ajabu. Hizo zilikuwa ni fikra tu zilizopita kichwani kwake na kumpa namna ya kuondokana na shari.

    Alijua atakapokuwa nje ya Tanga atasahau taabu hizo, zinazosababishwa na wivu kwa Mary na Uchungu wa mtoto wake.“Lakini huyu mwanamke atakaponipatia hela zilizobaki kwake sitapata taabu kuwa mbali na ufukwe huu.” Alijisemea…“Kumwachia mtu mahali hapa apaendeleze na mimi kwenda mbali kwa miaka miwili ama mitatu kutanipa nafasi ya kusahau kila kitu.” Aliendelea kujipa ushauri ambao kwake ulikuwa wa busara sana.

    Ramson aliendelea na shughuli zake akiwa tayari katika kujipanga kuondoka, maana aliamini kuwa Mary hatakawia kumkabidhi kiasi cha shilingi millioni kumi zilizobaki kwenye mapatano yao. Kichwani kwake aliwafikiria marafiki zake na kuangalia japo ampate mmoja atakayemwamini ili amwachie biashara zake ufukweni hapo. Alipanga akipata hela zake kutoka kwa Mary na kuchanganya na nyingine zilizoko Bank, aweze kwenda kuanzisha biashara eneo jingine ndani ya nchi hii, au nje ya nchi ikibidi.

    Mawazo yake yaliendelea hadi alipokuwa kitandani usiku. Kutokana na mawazo mengi usiku huo aliotandoto nyingi sana za kutisha na zisizoeleweka vizuri. Ilimradi alikuwa katika changamoto ya pekee juu ya tatizo lake jipya. Hata ilipofika asubuhi hakuwa na raha hasa kwa kukosa japo simu kutoka kwa Mary ya kumjulisha kuhusu fedha zake kuwa atamletea lini. Kujitenga kwa Mary kulimpa mtihani mkubwa sana kwani alizoea ukaribu wake. Jambo jingine lililokuwa linampa shida ni juu ya Patano lao kuhusu kiasi cha fedha za malipo ya mwisho.

    Mary hakumjulisha hata juu ya mumewe kuwa alikuwa amerudi hivyo ilimpa shida kujua kuwa Dr.Jackson ameingia lini nchini. Mawazo yaliendelea kupandana kichwani kwake na kumfanya aone kuwa Mary anataka kumgeuka juu ya mpango waliopatana. Lililomtatiza ni kukosa mawasiliano na Mary, hasa kwa kujulishwa tu juu ya mpango wao baada ya mumewe kurudi.

    Kwa siku nzima alikosa rahasana na akashindwa kufanya jambo lolote la maana. Muda wote alikuwa akiguna tu na kukosa mwelekeo wa kufanya hata kazi zake kwa umakini. kazi muhimu alimpatia kijana wake azisimamie na kuwaongoza wafanyakazi wenzie wachache, kufanya usafi na kuweka eneo lile katika hali ya kuvutia wateja. Moyo wake ulikuwa ukimwuma sana kila alipokuwa akifikiria habari ya Mary na mtoto wake.

    * * *

    Ulikuwa ni usiku wa saa sita simu ya Mary ilipoita. Alikuwa kitandani, Mumewe alikuwa amelala fofofo! Mary alipoangalia kwenye kioo cha simu, alikutana na Jina Ramson! Haraka sana aliondoka kitandani hapo na kuelekea sebuleni na kuipokea simu ile. “Ramson unasemaje usiku huu wote? Aliuliza Mary kwa hamaki.

    “Unanilazimisha wewe Mary kufanya hiv,i sio makusudio yangu! Tangu mumeo amerudi huonyeshi hata dalili ya kutimiza ahadi tuliyowekeana, hupigi simu wala ujumbe mfupi hutumi.” Alisema Ramson kwa kulalamika. “Samahani sana Ramson kwa hilo lakini kumbuka kuwa simu na ujumbe mfupi kwangu ni hatari sana. Dr. anakuwa na simu yangu kila wakati. Sipati mpenyo mwingine wowote.” Alijibu Mary kwa kujitetea.

    “Kwa hapo Mary huwezi kunidanganya! ikiwa anakuwa na simu yako kila saa mbona umepokea wewe wakati huu? Potelea mbali kuhusu hayo yote, la msingi nahitaji uniambie ni lini utanipa hela zangu zilizobaki?” Aliuliza Ramson bila mzaha. “Naomba Ramson nivumilie ili nilifanyie kazi jambo hilo.” Alisema Mary kwa kubembeleza. “Siwezi kuvumilia zaidi ya hapa!” Alisema Ramson kwa hasira. “Ramson nitakuja kesho tutaongea vizuri sawa?” CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mary alisema maneno hayo kwa kunong’ona baada ya kusikia sauti ya mumewe kutoka chumbani akikohoa; kisha akakata simu. Ramson aliduwaa lakini ahadi ya kwamba Mary atakuja ufukwenikesho yake, ilimvutia japo bado kuna hatari alikuwa anaihisi katika jambo hilo. Alikuwa hana hamu tena kuendelea kuwepo mahali hapo, kutokana na matatizo yaliyopo.

    Alihofia maisha yake kukatizwa kutokana na uhusiano huo mbaya uliozaa matunda ya mtoto. Alijua kuwa kwa vyovyote Dr. Jackson anaweza kufanya vipimo vya DNA ikiwa tu atashtukia jambo fulani kwa mtoto. Baada ya kugundua lazima hatari ingefuata maana asingevumilia. Kwa mawazo hayo Ramson alikusudia apewe hela zake ili aondoke kabisa katika mji huo.

    Kuhusu biashara zake na mradi wake kwa ujumla ufukweni hapo, angeuacha kwa marafiki zake. Kuchelewa kwa Mary kumpatia hela zake ni kumfanya akaribie kwenye mdomo wa mamba; kitu ambacho ni hatari kubwa sana kwake. Alisubiri siku ya pili yake aone uaminifu wa Mary juu ya ahadi yake.

    Mapambazuko ya siku hii yaliambatana na hamu ya kumwona Mary. Kila wakati alikuwa anaangalia njia, kuona labda Mary angekuja wakati huo. Kila aliposikia muungurumo wa gari aligeuka upesi akifikiri ni Mary amekuja. Hali hii iliendelea kwa muda mrefu sana, mpaka kufikia mchana wa siku hiyo. Kuna muda alifikia kukata tamaa kabisa juu ya ujio wake ufukweni hapo.

    * * *

    Usiku kabla ya kulala Dr. Jackson alimwambia mkewe ajiandaye kwa safari ya kesho yake. “Mke wangu ni siku nyingi sana nimekuwa nje ya nchi. Alisema Dr. Jackson akakohoa kidogo kisha akaendelea.. “Natamani kesho twende Lushoto, Tukaangalie Hotel zetu na maendeleo yake. utakuwa wakati wetu mzuri sana wakwenda kupumzika, baada ya kutengana kwa muda mrefu.”

    Alitoa wazo Dr. Jackson.“Mume wangu nashukuru kwa wazo lako zuri, nadhani hilo halina tatizo kabisa nitajiandaa.” Alijibu Mary kisha akaenda kabatini kuandaa nguo chache za kwake na za mumewe. Baada ya kuzifunga vizuri kwenye mabegi alirudi kitandani na kuungana na mumewe. Waliongea mengi na hatimaye wote walipitiwa na usingizi.

    kilichomwamsha Mary ilikuwa ni simu iliyopigwa na Ramson. Alijua kuwa kama atayachukulia kimzaha malalamiko ya Ramson yangemharibia. Jambo aliloona ni la lazima ni kutafuta kisingizio cha kutokwenda Lushoto na mumewe. Mwisho wa yote akaona kujifanya mgonjwa ndiyo njia pekee itakayompa mwanya wa kubaki.

    Baada ya muda alianza kujiliza akijifanya anaumwa na Tumbo. Hata mumewe alipoamka alimkuta mkewe katika hali hiyo.Alipohoji tatizo Mary alisema kuwa anaumwa na tumbo. “Kama linakuuma sana basi nikupeleke ukapimwe Hospital ijulikane kuwa ni nini?” Alisema mumewe kwa msisitizo akimhimiza mkewe ajiandae waende Hospitali. “Usiwe na wasiwasi mume wangu hali hii sio ya kwenda Hospital.” Ni majira yake na halitadumu kwa muda mrefu zaidi ya siku mbili tu ya tatu linatulia kabisa. Alisema Mary na mumewe alimwelewa.

    “Sawa mke wangu nimekuelewa sasa itabidi basi Lushoto niende peke yangu? Nitakuja baada ya siku mbili kwa kuwa Hoteli zote mbili kuzikagua ni kazi kubwa.” Alisema Dr. Jackson. Sawa mume wangu ila siku mbili nitakukosa sana! Japo pia kuna umuhimu mkubwa wa kutembelea Hotel zetu, maana kwakweli taarifa za kupewa tu hazitoshi.” Mary aliongea hivyo na baada ya muda alimwandalia mumewe chai mezani. Baada ya kuoga na kunywa chai hiyo alipakiza begi lake kwenye gari na kumuaga mkewe na kumbusu mtoto kisha akaondoka zake.



    * * *

    Asubuhi baada ya mumewe kuondoka, Mary alimpigia Ramson Simu kuwa anakuja. Ramson alifurahi kuwa hatimaye atapewa fedha zake. Mnamo saa tano za asubuhi Mary alikuwa barabarani kwenda Mwahako Beach. Mwendo wake ulikuwa wa kasi sana lakini alipofika mwakidila alikutana na ajali ya pikipiki na baiskeli watu wengi walikusanyika mahali hapo kwa wingi.

    Kwakuwa waliogongana walikuwa wamelala barabarani aliteremka ili aone majeruhi hao. Baada ya muda majeruhi wale waliondolewa na kuruhusu magari kupita. Dr. Mudy aliyekuwa akitoka Pangani alipita mahali pale kwa kasi lakini macho yake yalimwona Mary Mke wa rafiki yake. Kwanza alianza kuiona gari yake na kisha baada ya kuangalia sana akamwona Mary akielekea iliko gari yake.

    Alipopita kidogo alisimamisha gari kando ya barabara na kuangalia mwelekeo wa shemeji yake. Alipomwona akipinda kushoto mahali ilipo Mwakidila sokoni alijua kuwa alikuwa akielekea Mwahako Beach. Baada ya kuona hivyo ilimsikitisha sana maana alijua kuwa rafiki yake Dr. Jackson alikuwa akiibiwa na Beach Man. Hali hiyo ilimtia uchungu kutokana na taarifa aliyopewa na rafiki yake Jackson, kuwa alikuwa aende Lushoto na mkewe lakini tatizo ni kwamba mkewe alikuwa akiumwa.

    Hali hii hakuivumilia badala yake alipiga simu ya Dr. Jackson. Halo ndugu yangu mambo vipi? Alisalimia Mudy baada ya simu kupokelewa. “Aisee ni nzuri sana kwema Pangani?” Aliuliza Dr. Jackson. “Pangani ni kwema nimeshamaliza shughuli zangu ila sasa niko hapa Mwang’ombe napita mahakamani hapa narudi Mjini.” Alisema Mudy.

    “Sawa ndugu yangu mimi nilishafika Lushoto kitambo ninapitia mahesabu na kukagua mazingira ya Hoteli zangu.“Jackson alisema na mara hiyo simu ikakatika. Alijaribu kuipiga lakini alikutana na ujumbe ukisema: “Asante kwa kutumia mtandao wa voda com. Namba unayopiga kwa sasa haipatikani tafadhali jaribu tena baadaye.”

    Dr. Mudy alitaka kuwakilisha ujumbe wake wa kimbea kuhusu kukutana na mke wa rafiki yake akielekea Beach. Ni mazungumzo mengi ya Jackson yaliyosababisha chaji yake iliyokuwa kidogo kwenye simu yake kwisha. Simu yake ilizima kabla hajawakilisha ujumbe huo. Aliendelea mbele akipania kuwa baada ya kuweka chaji kwenye simu yake basi angemweleza rafiki yake mambo yote.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    * * *

    Mary alifika ufukweni na Ramson alimpa mapokezi ya aina yake kwani walijumuika katika kukumbushia uhusiano wao. Baada ya zoezi lao Ramson aliuliza juu ya mpango wao waliopatana. “Mary uvumilivu unanishinda siwezi kuvumilia kukuona uko na mumeo na mtoto wangu. Ninachotaka kuanzia sasa nipate ule mzigo uliobaki nijue cha kufanya. Hiyo peke yake itakuwa ndio dawa ya kustiri siri yetu.” Alisema Ramson kwa Msisitizo.

    “Ramson nimekuelewa mpenzi wangu lakini nimekuja kukuambia kuwa naomba usubiri kidogo tu kuna mambo nayarekebisha kusudi nikupe ule uzigo tuliopatana.” Mary alisema kwa upole. “Lakini Mary kumbuka kuwa ulisema jamaa akija tu utanipatia na sasa tangu aje ni wiki imeshaisha sio mapatano yetu. ila kama unavyosema ni muda mfupi naombaufanye hivyo kabla mambo hayajawa mabaya.

    Nataka niondoke katika mji huu kwa muda usiojulikana.” Alisema Ramson.” “Usiwe na wasiwasi nitatimiza kila tulichoongea, nipe siku tatu tu tangu leo.” Alisema Mary kwa uhakika. “Kwa sababu umesema mwenyewe kuwa ni baada tu ya siku tatu naomba isivuke hapo. Kwa sababu sina amani moyoni mwangu juu ya maisha yangu.

    Utanielewa vibaya ikiwa hutatimiza ahadi yako ndani ya siku hizo. Najua niko hatarini kwa sababu nawaelewa madaktari walivyo! Iko siku atashtuka kuwa mtoto sio wa kwake na kama akienda kwenye vipimo vya vinasaba kitakakachotokea ni siri kuwa wazi.” Alisema Ramson huku akionyesha hofu katika macho yake. “Ramson nitajitahidi nifanikiwe ndani ya siku hizo.” Alisema Mary huku akinyanyuka na kuaga kuwa anarudi nyumbani.”

    “Zingatia hayo na uwe makini sana kwa kila jambo. usifanye papara katika kila pointi. Kosa moja tu litaifanya siri yetu kuwa hadharani.” Alitahadharisha Ramsoni. “Hakuna wasi wasi niko makini Ramson.” Alijibu Mary huku akiishilia ndani ya gari lake, baadaye akaliwasha na kuliondoa taratibu Ufukweni hapo. Mawazo yalipandana kwa Mary na kumsababisha kuwa na huzuni, iliyochanganyika na majuto.

    Siri hii imekuwa kikwazo sana ndani ya maisha yake. Hakuwa tena na raha katika maisha kama ilivyokuwa hapo mwanzo.Hitaji la kupata mtoto na tamaa ya kimapenzi, imemwingiza katika hatari kubwa katika maisha yake. Nisawa kabisa kuwa alimpenda sana Ramson, lakini haikuwa zaidi ya mapenzi tu aliyoyataka kwake. Ndoa yake hakutaka kuipoteza kabisa hivyo alitamani kuilinda, kwa namna yoyote ile ya gharama.

    Lakini dalili zinavyoonyesha mpaka hapo ni kwamba kuna dalili za siri hiyo kuvuja, kutokana na uharaka wa Ramson katika madai yake. Alijuta sana kumwambia Ramson kuwa alikuwa na mimba yake. Alikumbuka jinsi alivyopata furaha ya ghafla baada ya kupewa majibu ya vipimo na Daktari. Furaha yake ilimnyima simile hivyo akajikuta anaropoka na kumpa nafasi ya utawala Ramson, katika nafsi yake na maisha yake kwa ujumla.

    “Umefanya kosa kubwa sana rafiki yangu kumwambia Ramson kuhusu huo ujauzito. Hiyo inaweza kukugharimu mambo mengi katika kuilinda siri hii.”

    Alikumbuka maneno ya rafiki yake Irene, pindi tu alipomwambia kuwa amemjulisha Ramson juu ya ujauzito ule kuwa ni wake. Mpaka sasa kengele za tahadhari zilikuwa zikipigwa masaa ishirini na nne! Hali ya mashaka ilitawala kila wakati pindi tu anapofikiria jinsi ya kucheza katika pande zote mbili, kwa Ramson na mumewe.

    Alijikuta yuko njia panda kwa ujumla. “Zingatia hayo na uwe makini kwa kila jambo, Usifanye papara katika kila pointi! Kosa moja tu litaifanya siri yetu kuwa hadharani!” Aliyakumbuka maneno ya Ramson ya mwisho wakati wanaachana. Hakuwa na hakika kuwa hatafanya kosa katika harakati zake za kuihifadhi siri hii; hasa ukizingatia kuwa pande zote alikuwa anawindwa!

    Alikuwa na majukumu ya kawaida kwa mumewe na kwa Ramson. Kutoa Shilingi milioni kumi na kumpa Ramson halikuwa jambo kubwa sana wakati mumewe akiwa yuko masomoni. Lakini kutoa kiasi hicho cha fedha wakati mumewe akiwepo ni mtihani mkubwa sana, ambao umebeba hatari kubwa sana, kama hautafanywa kwa uangalifu.

    Ubaya wenyewe ni kwamba pande zote mbili zitamwangukia kwa hasira kubwa sana bila huruma. Hayo yalikuwa ni mawazo ya kweli yaliyokuwa yakipita katika kichwa cha Mary. Kwakweli hakuwa na nafuu wala faraja kwa yote hayo; bali yalimtaka kuwa macho sana katika pande zote mbili. Kwa wakati huu Presha ilikuwa kwenye kulilipa deni la Ramson. Baada ya hapo abaki salama akiyalea mapenzi yake kwa mumewe. Tatizo kubwa lilikuwa ni Ramson na deni lake peke yake. Mawazo yake yalikuwa juu sana kutafuta jinsi ya kutatua tatizo hilo kwa busara.

    * * *

    Dr. Mudy alipofika nyumbani jambo la kwanza alikimbilia kwenye soketi ya umeme, ili kuchaji simu yake kusudi aweze kumpa rafiki yake habari juu ya Shemeji yake. Moyo wake ulikuwa na dukuduku bayasana, ambalo lilihitajika kutolewa mahali husika ili apate nafuu. Jamaa huyu huwa hawezi kuvumilia anapoona neno. Rafiki zake wengi walikuwa wakimshauri aachane na kazi ya udaktari, badala yake awe mwandishi wa habari wa magazeti ya udaku! Pendekezo hilo la rafiki zake lilikuwa sahihi, kwa sababu Dr. Mudy alikuwa hakai na jambo.

    Anapoona jambo ambalo sio zuri, hulisimamia na kulitolea habari zake mahali husika. Mara tatu aliweza kutoa taarifa kuhusu Madaktari wenzake, waliokuwa wakijihusisha na kutoa mimba za wanafunzi. Madaktari hao walikamatwa na kufungwa kifungo cha miaka ishirini kila mmoja baada ya kubainika wakifanya tendo hilo. Leo hii yupo nyumbani kwake akiwa na harakati za kuchomeka simu kwenye chaji, lakini hali haikuruhusu kwani umeme ulikuwa umekatika.

    Kidogo alitahayari kutokana na zoezi lake kukwamishwa na kukosekana kwa umeme. “Lakini ni kwa muda tu, umeme ukirudi nitachaji na kumwambia rafiki yangu habari hizi.” Alijisemea kimoyomoyo huku akielekea chumbani kwake na kuingia bafuni ili ajimwagie maji kuondoa uchomvu wa safari.

    Baada ya kumaliza kuoga aliporudi chumbani kwake ili kuvaa nguo alikuta umeme umesharudi. Kwa haraka alichukuwa simu yake na kuiweka kwenye chaji. Baada ya hapo alirudi na kumalizia kuvaa, kisha akarudi na kuwasha simu ikiwa kwenye chaja na kutafuta namba ya Dr. Jackson. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hata hivyo bahati haikuwa upande wake, kwa sababu simu ilikuwa haipatikani alijaribu tena ikawa vile vile. “Mmmmmh! huu umbea utachacha sasa! kama angepokea ningempasha habari zikiwa bado za motomoto, lakini inavyoonekana leo sikulalia mkono mzuri. Jamaa tunapishana tu nikitaka kufikisha umbea wangu kunatokea vikwazo!” Alilalamika Dr. Mudy huku akijaribu kupiga kwa mara nyingine ambayo ilijibiwa vilevile kuwa namba haipatikani labda ajaribu tena baadaye! “Hakuna neno ataifungua tu simu yake.

    Na mimi sitaki kumtumia ujumbe mfupi wala nini! Nataka nimpigie na kumwambia kila kitu neno kwa neno.” Aliendelea kusema peke yake mawazoni huku akiwa ameshushuka kwa kukosa nafasi ya kubwagiza habari zile. Habari ambazo alizitunza kwa muda mrefu sana ila tu alikuwa akizitafutia ushahidi wa kutosha.

    Alitayarisha ushahidi wa namna zote na kupata vigezo mbalimbali vya kuusema umbea ule kwa Jackson. Uchunguzi wake wa kina na ufuatiliaji wa mambo na kuhifadhi ushahidi ni sehemu ya kipaji chake. Hii ndio maana baadhi ya marafiki zake walimpendekeza kuwa alifaa sana kuwa mwandishi wa habari.

    Kwa upande wa Mary aliweka ushahidi wa siku nyingi, hivyo kuifanya habari kamili juu ya kuibiwa kwa rafiki yakeiwe imeiva. Hii ndiyo sababu iliyopelekea kuhangaika sana ili kumpata Dr. Jackson, kusudi ampe habari kamili. Mahangaiko yake hayakufua dafu kwa siku ile, hivyo alilala nayo tena bila mafanikio.

    * * *

    Dr. Jackson alifika salama Lushoto na ukaguzi wa Hotel zake ulifanyika mara tu baada ya kufika. “Inaonekana mnafanya vizuri kazi zenu au sio Meneja?” Alisema Dr.Jackson baada tu ya kuingia kwenye Ofisi ya meneja wa Hotel mojawapo kati ya mbili alizonazo. Ni kweli Mzee tunajitahidi kufanya vizuri.” Alijibu Meneja kwa unyenyekevu. “Nimeona mazingira ya nje ni mazuri watu wa kukatia majani kwenye bustani wamefanya vizuri bwawa la kuogelea liko katika hali ya usafi, kadhalika bwawa la samaki pia naona linatunzwa vema, maana naona samaki wamekuwa wengi sana.

    Hayo ni machache ya mambo niliyoyaona mazuri. Hongera sana Meneja kwa kazi yako nzuri.” Alisema Dr. Jackson huku akimpa mkono Meneja kusindikiza pongezi zake. “Asante Bosi kwa kuyaona hayo. Tunajitahidi kufanya vizuri kwa sababu wageni ni wengi kutoka Ulaya; wanakuja kulala hapa wengine wanakaa kwa mkataba, wa mwezi mpaka miezi mitatu.

    Wanapokuja watu hawa kinachowavutia ni mazingira kwanza ya Hotel. Bwawa la kuogelea bwawa la samaki na vivutio vinginevyo, ikiwepo bustani ya mboga mboga na bustani ya matunda. Mpangilio wa vitu hivyo huwafanya waje hapa na kutaka kuishi hapa, ikiwa muda wao wa kukaa hapa ni mrefu.” Alisema Meneja kwa kirefu akielezea jinsi biashara zinavyoenda vizuri.

    “Unataka kuniambia kuwa tangu niondoke nchini wamekuja watalii mara ngapi kwenye Hotel zetu?” Aliuliza Dr. Jackson. “Unajua mzee miaka mitatu sio mchezo! Inabidi niangalie kwenye kitabu kusudi nikupe idadi hasa za wageni wetu.” Alisema Meneja na huku akifungua kabati la vitabu vya wageni na taarifa za kila siku. Kisha akaendelea… “Unaona sasa! Kwenye kitabu cha kupokea wageni kinaonyesha kuwa ni zaidi ya mara ishirini tumeingia mkataba na wageni toka nje ya nchi wa kukaa kwa muda mrefu. Wengine walikaa wiki mbili wengine walichukuwa Hoteli nzima kwa miezi mitatu.

    Hawa hapa walikaa kwa miezi miwili. waliokaa kwa muda wa miezi miwili miwili walikuwa watalii kutoka Nchini Marekani. Watalii hawa walikuja kuendesha semina za mambo ya ukimwi. Walichukuwa Hoteli nzima kwa muda wote huo. Wengine walitoka Austaralia hawa walikuja kufanya utafiti wa wadudu wanaoeneza magonjwa, kwa wanyama kama vile Ng’ombe, mbuzi na kondoo.

    Hawa walikuwa watu mia moja na kumi, hivyo iliwalazimu kuchukuwa Hotel nzima waliobaki tuliwapeleka kwenye Hotel yetu nyingine. Kwa ujumla Bosi hao ndio wageni wetu waliotutembelea katika kipindi chote hicho.” Alisema Meneja huku akimalizia kuweka idadi kamili, katika karatasi moja na kumkabidhi bosi wake.

    Kiasi cha fedha kwenye akaunt kimefikia shilingi ngapi kulingana na kazi zilizofanyika?” Aliuliza Dr. Jackson. Fedha zote zilizoko Bank nimekuwa nimeorodhesha kwenye kitabu cha mahesabu. Nimejitahidi kuhifadhi risiti za manunuzi ya vitu vya matumizi, faida nimeweka kwenye Akaunti. Kumbukumbu nimeweka kwenye kitabu hiki.” Alionyesha kitabu kikubwa cheusi. Alisema Meneja. Kiasi chote cha akiba iliyoko Bank ni hii hapa. Alimwonyesha kila kitu jinsi alivyotunza mahesabu.

    Baada ya kumpa kitabu cha akiba iliyopo, alimpa kitabu kingine cha mchanganuo wa mapato na matumizi. Mwisho wa yote Dr. Alimpongeza sana Meneja wake kwa kufanya kazi nzuri sana. “Kazi yako ni nzuri sana. Endelea na shughuli mimi ninataka nikamilishe kuangalia Hotel ile nyingine. Nahitajika nirudi mjini Tanga maana nahitajiwa kazini.” Alisema Dr. Jackson. “

    Ila bosi nimekuwa nikijiuliza kila siku mambo mengi sana ninakosa majibu. Wewe ni tajiri sana mwenye Miradi mingi kiasi hiki, lakini bado unafanya kazi ya kuajiriwa! Kwanini usitulie ukaangalia miradi yako?” Samahani bosi kama nitakuwa nimeingilia maisha yako binafsi.” Alisema Meneja wakati wanaagana.

    “Bila samahani ni watu wengi wananiuliza swali hilo sio wewe tu. Unajua kazi ya Udaktari ni sehemu ya wito kwa ajili ya kuwasaidia binadamu wenzetu? Aliuliza kisha akaendelea. “Wito ni kitu cha ajabu sana, humuendesha mtu kwa ndani ya nafsi yake na mtu huyo akakosa maamuzi sahihi zaidi ya kuutimiza wito huo. Ndani yangu ninasukumwa na huruma kwa watu wanaoteseka kwa magonjwa.

    Nikiwa nje ya kazi hii ninajiona kama sijakamilika, ikiwa tu sijafanya jukumu langu la kuwasaidia watu wanaoteseka. Hilo ndilo linalonisumbua na kunifanya niendelee kuwepo kazini. Hata kama ningekuwa na utajiri kiasi gani hauwezi kunifanya nikaacha kufanya kazi yangu ya Udaktari.” Alisema Dr. Jackson na kumalizia kwa kumpa mkono wa kwaheri Meneja wake. Asante mzee kwa kunijibu. Una moyo wa ajabu sana Bosi wangu.”

    Alimaliziakuzungumza wakati Dr. akifunga mkanda na kuliwasha gari kisha kuliondoa kwa mwendo wa taratibu. Njiani aliwapungia mkono wafanya kazi wake waliokuwa wakifanya usafi na kuendelea na safari yake. Ukaguzi wa hoteli yake nyingine, ulikuwa ni hali kadhalika na baada ya kumaliza kukagua kila kitu aliondoka jioni ya siku ya pili tangu afike Wilayani hapo.

    Fedha zilikuwa ni nyingi za faida alizozipata kwa kipindi chote hicho kiasi kwamba alifikiri kuanzisha mradi mwingine mkubwa sana. Alijaribu kufikiri akiwa kwenye gari lake, huku akipiga mluzi taratibu kufuatisha mziki uliokuwa ukipigwa na Mwanamuziki Mbiliabel.

    * * *CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mary baada ya kurudi kutoka ufukweni alijipanga na kumpigia rafiki yake Irene simu kusudi waonane. “Kwani una haraka sana ya kuonana na mimi sasa hivi? Kama unaweza kusubiri niende mara moja Bank maana kuna Fedha zinatakiwa za marejesho Pride.” Alisema Irene baada ya Mary kumwambia anataka waonane ndani ya muda huo. “Mazungumzo yangu ni marefu na yanahitaji tuyaongee mapema sijui utafanyaje?” Aliuliza Mary kwa sauti ya chini yenye dalili kuwa amebanwa sana na jambo.

    Irene kwa kuzingatia uzito huo aliouonyesha rafiki yake akamwambia: “Kwani kuna tatizo gani rafiki yangu? au mambo yameharibika?” Alisema Irene akisukumia na utani ambao ulifanana na ukweli. “Ninashukuru kama umekubali tuonane mengine tutaongea tukikutana.” Alisema Mary na kukata simu. Baada ya hapo aliingia kwenye gari lake na kuanza safari kuelekea kwa Irene.

    Alienda kwa mwendo wa kasi kusudi amwahi rafiki yake. muda haukuwa mrefu sana alifika nyumbani kwake na kumkuta Irene Sebulen akiwa kakaa mkao wa kutaka kuondoka. “Wooooow Mary” Alisema Irene na kumkubatia rafiki yake… “Karibu sana naona leo huko kwenye hali yako ya ucheshi unanini” Alisema Irene baada ya kumkaribisha Mary kwenye moja ya sofa.

    “Sio hali mbaya sana, ilibidi tu nikuone japo tupeane maarifa. Alisema Mary kwa unyonge. “Kuhusu nini sasa?” Aliuliza Irene akiwa na shauku ya kujua. “Rafiki yangu sasa hivi niko njia panda na sijui ni njia gani nitapita ili niokoke! Mpaka sasa Ramson ananidai kile kiasi cha shilingi millioni kumi, na amenikalia kooni kwelikweli hana utani kabisa. Lengo la Ramson anataka akimbie mji maana hana uhakika na maisha yake kama anavyodai mwenyewe. Nimempa siku tatu za kumlipa hela hizo, lakini mpaka sasa bado sijajua nitaanzia wapi kumwomba Mume wangu kiasi chote hicho.”

    Alisema Mary katika hali ya majonzi akihitaji ushauri kutoka kwa Irene rafiki yake. “Pole sana Mary! Labda utakuwa unakumbuka maneno yangu, nilikuambia tangu mwanzo kuwa hukupaswa kumwambia Ramson kuwa una mimba yake. Ungezingatia yote haya yasingelitokea.” Irene alimwambia Mary kwa masikitiko.

    “Ni kweli rafiki yangu lakini Waswahili wanasema: “Maji yakishamwagika hayazoleki.” Nimejuta sana juu ya hilo na kila wakati ninakumbuka ushauri wako, lakini majuto yangu hayawezi kubadilisha lolote kwa sasa. Kinachotakiwa ni kupata njia mpya ya jinsi ya kujikwamua kutokana na matatizo haya, nishauri ndugu yangu!” Alisema Mary kwa uchomvu wa mawazo. “Sawa rafiki yangu labda twende katika Pointi yenyewe.

    Jioni Mr. wako atakaporudi ongea naye umwambie kuwa, kuna biashara tumeamua kuifanya ya kuleta vipodozi na kuviuza kwa jumla. Na kwamba bidhaa hizo tunazitoa nchini China. Mpe mchanganuo mzima wa mtaji unaohitajika na faida zitakazopatikana kutokana na biashara hizo. Kwa sasa tuandae mchanganuo huo, kisha nitauprint na kukupatia ili ukampe mumeo.”… Alisema Irene kisha akameza mate wakati huo Mary alikuwa amemtazama tu usoni.

    “Kwenye huo mchanganuo nitaweka kiasi cha mtaji kama milioni Thelathini na tiketi itakuwa ni shilingi million tano. Mpaka kufikia hapo mimi hela zangu nitakuwa nazo tayari, kwa hiyo utamwambia kuwa ulikuwa unamsubiri kusudi umweleze jinsi tulivyopatana.” Alisema Ireni huku akimwangalia Mary usoni kuona kwamba maneno yale yamemwingia.

    “Hapo umenipa njia. Kweli ninavyomjua ni kwamba hawezi kugoma, ila anachotaka mara nyingi ni kupewa mchanganuo wa kile kinachohitajika kufanywa. Unanishauri baada ya kupewa hela hizo nifanyeje?” Aliuliza Mary. “Ufanyeje tena!?” Alisema Irene kwa kushangaa!...“Lengo la yote haya ni ili upate hela za kumlipa Ramson!

    Ninavyofahamu ni kwamba mumeo hakufuatilii katika miradi yako wala biashara zako. Kwa hiyo kwako ni njia nzuri sana ya kuondoa tatizo lililopo la huyu Ramson.Si ndiyo shida iliyopo kwa sasa?” Alisema Irene huku akitabasamu. “Hapo mwenzangu umenisaidia sana rafiki yangu.”

    Alisema Mary huku akiungana na rafiki yake katika kutabasamu. Wewe ni Mbunifu sana wa mambo! Hiyo ni mbinu kabambe ambayo itanisaidia kuniondoa kwenye matatizo, Asante sana rafiki yangu.” Alisema Mary huku akionyesha uso wa matumaini. Irene alinyanyuka na kuingia ofisini kwake.“Jichukulie mwenyewe juisi hapo Frijini wakati nikiandaa Mchanganuo sawa?” Alisema kabla hajaingia na baadaye akatokomea ndani.



    Ilikuwa ni ujumbe mfupi uliomshtua kwenye mawazo yake. Mawazo muhimu sana ya kupangilia namna ya kuanza mradi mkubwa, kulingana na fedha nyingi alizopata. Wimbo wa Mbiliabeli uliendelea kujirudia kweye Redio huku Dr. Jackson akiutolea kibwagizo kwa mluzi!Alichukuwa simu yake huku akiwa amekasirika kidogo. Baada ya kuifungua simu yake akakuta ujumbe mfupi kutoka kwa Dr.Mudy.

    Ujumbe wenyewe ulikuwa na maneno machache sana, yaliyosomeka hivi: “Rafiki yangu kama umerudi fanya kila njia tuonane kwenye Hoteli ya Mkonge jioni hii, kuna habari nyeti sana nikuambie. Zingatia kuwa ni muhimu.”

    Baada ya kusoma akairudisha simu mahali pake huku akiwaza ninini anachoitiwa na rafiki yake? “Ni jambo gani hilo la Muhimu tena?” Alijiuliza Dr. Jackson huku akikerwa na wito huo bila kujua kuwa unahusu nini.” Alifika nyumbani alasiri akiwa na uchomvu wa safari. Jioni hii alimkuta mkewe amechangamka sana. Lakini hakutaka kukaa sana maana wakati alioambiwa wakutane na Mudy ulikuwa umefika.

    “Mbona unaondoka mapema kiasi hiki hata hujapumzika? halafu nina mazungumzo mazuri sana ambayo ungeyafurahia mume wangu.” Alisema Mary kwa hali ya deko.“Sawa Honey nitakaporudi baadaye tutakaa tuongee sawa? Kwa sasa nimeitwa na rafiki yangu Mudy amesema kuwa ana mambo muhimu sana ya kuzungumza na mimi.” Dr.Jackson alisema kwa kusihi ili apate nafasi ya kwenda kumwona Mudy.

    “Mtoto yuko wapi?” Aliuliza kwa kumalizia akitaka kutoka. “Yuko chumba cha michezo anacheza.” Alijibu Mary. Mara hiyo Dr. Jackson akarudi na kuingia chumba cha michezo, alimkuta Lameck anachezea magari yake ya kitoto. Jambo Lameck? Alisema Dr. Jackson na Lameck akaitika na kumsalimia baba yake. Jackson alimbeba na kumpa zawadi alizomnunulia, kisha akatoka na kuingia kwenye gari kisha, akaiondoa kwa mwendo wa kasi kidogo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alifika mkonge baada ya muda mfupi maana kutoka mahali alipoishi na Hotelini hapo sio mbali sana. Baada ya kupaki gari mahali pake aliondoka na kwenda kwenye bustani iliyopo nyuma ya Hoteli hiyo kubwa. Kufika hapo alimkuta rafiki yake akiwa anamsubiri. “Kumbe umeshafika!” Jackson aliuliza huku akishangaa. “Zamani sana mbona?” Alisema Mudy huku akinyanyuka kwenye kiti na kumsalimia rafiki yake.

    Baada ya kupeana mikono walikaa na wakati huo huo mhudumu alikuwa ameshafika kutaka kuwahudumia. “Niletee Malta Guiness ile isiyo na kilevi sawa?” Alisema Dr. Jackson. “Na mimi vilevile aliagizia Mudy na mara hiyo mhudumu akaenda kuwachukulia vinywaji. “Habari za Lushoto rafiki yangu?” Mudy aliuliza wakati akijiweka sawa kwenye kiti. “Habari sio mbaya ni nzuri sana rafiki yangu.Lushoto ni kuzuri sana baridi ya kule kama Uingereza nilikotoka.

    Mazingira ya kijani na misitu vimenifanya nijisikie vizuri sana kwa siku hizi mbili. Ninatamani baada ya kustaafu kazi ya udokta nihamie Lushoto nikamalizie uzee wangu huko.” Alisema Dr. Jackson kwa hisia kali. Mara mhudumu alifika na makopo mawili ya Malta Guiness na kuwawekea na glasi kisha akaondoka. “Haya rafiki yangu nimekuja unipe habari ulizosema kuwa ni nyeti.

    Kiukweli nimechoka sana nilitakiwa niwe niko kitandani nimepumzika saa hizi.” Alisema Jackson. “Sawa kabisa naona ni vizuri kwenda katika jambo lenyewe.” Alisema Mudy kisha akakohoa kisha akaendelea….”Nina jambo ambalo kwa siku nyingi nimelifanyia utafiti na baadaye nikaona kuwa sio vema kukaa nalo bila kukuambia.” Alitulia kidogo kuona kama maneno yake yanapokelewa namna gani.

    kisha akaendelea tena… “Unajua yule Beach Man sio mtu mzuri kwako? Alianza kwa swali ili kuchokoza shauku ya Jackson ya kutaka kujua zaidi. “Sio Mtu mzuri kwangu kivipi?... Usizunguuke sema moja kwa moja hivyo ndivyo ninavyokuambiaga mara nyingi, kuwa kama una habari niambie kabisa. Namna hiyo unaweza kumsababishia mtu shinikizo la damu bila sababu ya msingi sawa?” Aling’aka Dr. Jackson kwa sauti ya juu kidogo. “Nimekuelewa ndugu yangu ila usiwe mkali. “ Habari yenyewe ni kwamba yule Jamaa ana uhusiano wa kimapenzi na shemeji yaani mkeo!” Alisema Mudy huku akimtazama Jackson jinsi atakavyozipokea habari zile.

    “Nashukuru rafiki yangu kwa kunipa hizo habari.” Alisema Jackson kwa kujikaza na kuzuia hasira ambayo haijulikani ikiwa ni kwa ajili ya Mudy, au huyo Ramson aliyeambiwa. “Lakini habari zenyewe hizo kwangu siwezi kuziamini kabisa, hata ungeniambia kwa Lugha gani. Mimi na Mary tumetoka mbali sana! Mbali kiasi kwamba chochote unachokisema kuhusu yeye kunisaliti ni kama unaongea Kichina, ambacho sikielewi hata ungefafanua namna gani! Labda nikuage kwa sababu sitaki kusikia zaidi kuhusu hilo ngoja nikapumzike…

    ”Kwa heri.” Alisema na kunyanyuka kwenye kiti na kuelekea kwenye gari lake. Dr. Mudy alijisikia vibaya sana kwa kutokueleweka kwa rafiki yake. Alijaribu kumzuia lakini haikusaidia lolote. Hata kinywaji Dr. Jackson alikiacha hapo bila hata kukifungua. “Rudi rafiki yangu sijawahi kuzusha jambo lolote kwako na habari hii nina ushahidi nayo.” Alisema Mudy lakini ilikuwa kama anayempigia mbuzi gitaa ili aserebuke, badala yake mbuzi aliendelea kula majani!

    Dr.Jackson alielekea kwenye gari yake, kisha baada ya kuingia aliiwasha na kuiondoa kwa kasi kuelekea nyumbani kwake. Njiani alikuwa anafikiria mengi sana kuhusiana na taarifa ile. Upendo wake kwa mkewe ulikuwa juu sana. Yuko tayari kupigana na mtu kama tu wataongea kinyume na mkewe. Dr. Mudy kwake aligeuka adui baada tu ya kumsikia akisema habari kuhusu mkewe.

    Maneno yake yalijirudia kwenye mawazo yake kama jinamizi: “Habari zenyewe ni kwamba yule jamaa ana uhusiano wa kimapenzi na shemeji yaani mkeo.”Maneno haya yalikuwa mafupi lakini yanayoumiza sana kuliko hata risasi. Moyo unaumia vibaya sana kuliko maumivu ya mwili. Moyo unapoumia kila kitu kinasimama, maana maumivu yake hushirikiana na kichwa chenyewe. Mudy alimuumiza sana kwa habari zake hizo. “Ningejua kuwa habari zenyewe ni za hivyo nisingeitikia wito wake.” Alijisemea moyoni wakati alipokuwa akipiga honi ya gari kwa ajili ya kuingia ndani ya nyumba yake.



    * * *

    Mazungumzo kati ya Dr. Jackson na mkewe yalifikia mwafaka kuwa Mary atapewa shilingi milioni kumi, kusudi aongezee mwenyewe kiasi kilichobakia; ili Irene aende kufungasha bidhaa nchini China. Hii ni baada ya Mary kujieleza sana na kuonyesha mchanganuo wote wa biashara hiyo. “Fedha yote nitakupatia kesho kutwa maana kesho nitakuwa kazini kuna mwanamke ambaye nimepangiwa kumfanyia upasuaji. Na kama zoezi hilo likimalizika mapema saa saba kamili nitakuwa na kikao na uongozi wa Hospital, kuna mambo muhimu ya kuweka sawa kikazi.

    “Ninakuahidi kuwa kesho kutwa mapema sana nitakwenda kukutolea hela hiyo kwenye Akaunti ya Hotel sawa?” Alisema Dr. Jackson kwa upole.“Sawa mume wangu mpenzi asante sana kwa kunijali.” Alisema Mary akifurahia mafanikio hayo na kumpongeza rafiki yake Irene kwa ushauri wake.

    “Usijali wewe ni mke wangu. Unadhani mali hizi zote ni za nani kama sio zetu wote pamoja na mtoto wetu?” Alisema Dr. Jackson kwa sauti ya upole sana. Alipotaja habari za mtoto alikuwa kama ametonesha kidonda kwa Mary. Mary alikumbuka vizuri tahadhari ya Ramson, isitoshe kesho yake ndio ulikuwa mwisho wa kumpelekea fedha zake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ila alijipa moyo kuwa mara tu ifikapo keshokutwa majira ya saa sita, atakuwa mbele ya Ramson akimpatia Fedha zake zote. Alijua tendo hilo litaondoa shida zote na kumfanya ayafurahie tena maisha yake na mumewe. Hilo ndilo jambo la muhimu sana kwa kuirejesha furaha yake na uhuru moyoni mwake.

    Dr. Jackson naye alihuzunika sana moyoni mwake kwa kupata habari za ajabu ajabu kutoka kwa Rafiki yake Mudy. Japokuwa hakuziamini kabisa lakini zilikuwa zinamsumbua kila saa. Moyo wake ulimwuma kwa uchungu kila anapofikiri kuhusu habari zile. Kila wakati alikuwa akijiuliza kama ikitokea kuwa ni kweli mkewe anamsaliti kwa Ramson angejisikiaje? Mahesabu hayo ya ndani kwa ndani yalimfanya kila wakati kukosa raha kabisa.

    Naye alijiwekea ahadi ya kutafiti habari zile kwa kina.Kwa fikra zake aliamini kuwa habari zile ni uongo mtupu hazina ukweli wowote. Lakini kwa kujiridhisha ilikuwa ni lazima azifanyie utafiti. Kila mmoja kati yake na Mary alikuwa na fikra zake tofauti na mwenziye.

    Fikra zao zikilenga kutafuta ubora wa maisha yao ya ndoa. Mawazo hayo yaliendelea hadi pale walipopotelea ndani ya usingizi mzito. Kila mmoja aliingia katika ndoto mbalimbali zilizousukuma usiku ule hata ikafikia asubuhi. Waliamka wenye mawazo tofauti japo kila mmoja alionyesha furaha kwa mwenzake. Kila mmoja alimpenda mwenzake, kwa dhati.

    Jackson aliona ili furaha yake itimie ni pale atakapofanya upelelezi na kugundua kuwa maneno ya rafiki yake yalikuwa ni majungu tu. Hakutaka kuyakubali moja kwa moja na pia hakutaka kuyachukulia mzaha. Kwa upande wa Mary alitaka amlipe Ramson hela zake, kusudi awe huru na vitisho vyake. Hakutaka ndoa yake iingie kwenye matatizo. Alijua kuwa pindi tu atakapomlipa Ramson itampa nafasi ya kuhama kama alivyomweleza mwenyewe. Ikitokea hivyo itampa nafasi nzuri ya kuyafurahia mapenzi yake huku moyoni akiwa huru kwa asilimia nyingi na mumewe.

    * * *

    Ulikuwa ni usiku wa matumaini kwa Mary. Usiku mwingine uliotanguliwa na mchana uliokuwa na mishemishe nyingi, zilizoambatana na kikao kati yake na Irene. Kikao hiki kilikuwa ni kwa ajili ya kutoa asante kwa ushauri alioupokea kutoka kwake. Ushauri uliosababisha Mumewe kuahidi kumpatia kiasi cha shilingi milioni kumi.

    “Rafiki yangu sina cha kufanya kwako zaidi ya kukushukuru kwa kunisaidia mbinu hizi. Shinikizo la damu liliniandama wakati wote, hivyo mawazo yalipandana kiasi kwamba sikuweza hata kuwaza kiusahihi.” Alisema Mary kwa furaha na matumaini. “Usijali rafiki yangu ni jukumu langu kukusaidia wakati wa taabu.” Alisema Irene.

    Kuna ule msemo usemao: “Akufaaye wakati wa dhiki ndiye rafiki wa kweli, Leo nimedhibitisha maneno hayo kwako. Alisema Mary.. Ila sasa mwenzangu leo ndio siku niliyotakiwa kumpelekea Ramson mzigo wake, wakati ahadi yenyewe nimepewa ya kesho. Sijui nifanyeje?” Alisema Mary kwa wasiwasi kidogo. “Usiwe na wasiwasi kesho sio mbali. Mtengenezee Mshtukizo au kwa lugha ya wenzetu Surprise!

    Vile anavyofikiri sivyo wakati anafikia kuona kama mambo yamekwama ndipo unapomtokea kwa ghafla na kumkabidhi mzigo wake sawa?” Alisema Irene na Mary akaona ushauri huo ni sawa tu kwa sababu hakukuwa na njia nyingine zaidi. Baada ya mazungumzo hayo waliagana. Mary alirudi nyumbani ikiwa tayari jioni imeshafika. Alimkuta msichana wa kazi akimwogesha mtoto naye aliingia jikoni na kuandaa chakula kwa ajili ya familia.

    Mengi yaliyofanyika ndani ya siku hiyo yalimchosha na kumfanya awe na usingizi. Lakini ilibidi ajikaze kwa ajili ya kumsubiri mumewe mpaka atakaporudi. Mnamo saa tatu kamili mumewe alirudi akiwa amebeba zawadi mbalimbali. Vitu hivyo walisaidiana kuviingiza ndani na baada ya kutulia alimwandalia mumewe chakula.

    Baada ya kumaliza kila kitu waliingia chumbani kwa ajili ya kupumzika. Hali ya uchomvu ilikuwa imemwandama Mary hivyo alitangulia kupitiwa na usingizini wakati mumewe akiingia kazini katika kupanga malengo yake ya miradi. Dr. Jackson alitaka kuanza mradi mwingine mkubwa lakini alikuwa hajapanga kuwa ni mradi gani.

    Usiku huo aliamua kupanga na kuamua kuwa ni mradi gani auanzishe baada ya kupata faida zilizojilimbikiza kwa miaka mitatu. Fedha za Hoteli zilikuwa ni nyingi hivyo zilitosha kufanyia mradi wowote mkubwa. Usingizi ulikata na pale ulipojaribu kuja aliuzimisha na kahawa chungu. Mawazo yake yaligombana ndani kwa ndani wakati alipokuwa akifikiria aina tofauti ya miradi, alizidi kuzama ndani ili kufanya uamuzi sahihi.

    Ilipofika saa sita na nusu alishtuliwa na mlio wa simu ya Mkewe. Alivumilia kuona kuwa mwenyewe ataamka kuipokea lakini Mary alikuwa amelala usingizi mzito. Ili kuondoa kero kutokana na kelele hizo aliamua kuichukuwa ili aone ninani mpigaji. Mwanzoni alidhani Irene anampigia rafiki yake kwa ajili ya mpango yao ya kibiashara. Lakini alishtuka alipoona Jina la Ramson kwenye kioo cha simu!

    Mawazo ya Dr. Jackson yalienda mbali sana! Iweje Ramson ampigie mkewe simu usiku huu?! Kabla hajaipokea akawa amekubaliana na maneno ya Mudy. Taratibu aliminya kitufe cha kupokelea na kuwa kimya ili asikie mpigaji anataka nini. Mara Sauti ya Ramson ikasikiika upande wa pili:

    “Mary Mpenzi hii ni mara ya pili kuniahidi na matokeo yake kumbe umeamua kunidanganya! Patano letu lilikuwa leo mchana uniletee shilingi milioni kumi zangu ili niondoke katika mji huu. Kumbuka nilikwambia kuwa zile Milioni kumi ulizonipatia miaka mitatu iliyopita bado nimeziweka kusudi zinisaidie huko nitakakokimbilia kuanzisha mradi mwingine. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tatizo ni kwamba huelewi kuwa ninakabiliwa na hatari kiasi gani nikiendelea kuwepo hapa. Sasa ninataka uchague mawili kwa sasa, kuniletea Fedha zangu mchana wa siku ya kesho au uniletee mtoto wangu. Sitanii Mary!..Labda utajua kuwa sifanyi utani pale utakaposhindwa kuniletea hela zangu hapo kesho kwaheri!”

    Baada ya maneno hayo makali simu ikakatika. Dr. Jackson alishituka sana kusikia maneno hayo! Moyo wake ulimuuma sana baada ya kugundua hata mtoto Lameck ni wa Ramson! Ujasiri na uvumilivu ndio uliomfanya asimwamshe mkewe wala yeye mwenyewe asifanye jambo la ajabu katika kipindi hicho kigumu kwake!

    Taratibu hasira zake zilitengeneza machozi huku moyo wake ukiachia maumivu ya aina yake! “Kumbe Lameck sio mtoto wangu, kumbe fedha nilizoambiwa kuwa ni za biashara ni kwa ajili ya kumpatia Ramson ili kuficha siri kuhusu mtoto! Kweli nimefanywa bwege kwa kiasi kikubwa sana!” Dr. Jackson aliendelea kujiwazia huku akiuguza moyo wake uliokuwa na maumivu kama kidonda.

    Mawazo ya kupanga miradi yakabadilika ghafla badala yake akaanza kupanga jinsi ya kufanya katika janga hili. Alijua kuwa busara ilihitajika kwa kiwango cha juu sana. Kuchukulia papara suala hili ilikuwa ni hatari sana. Kwa Jackson busara aliiwekea kiwango cha juu sana katika kufanya maamuzi. Aliona mengi yaliyofanywa na watu bila kufikiri jinsi yalivyoleta hasara, katika maisha ya watu hao.

    Alimkumbuka rafiki yake Chido aliyeamua bila busara kuua mkewe na hatimaye kujiua mwenyewe, eti kwa sababu alimfumania na House boy wao. Mawazo yake yalimkumbusha jamaa mmoja aliyeitwa Alen aliyekuwa akimiliki biashara nyingi zikiwepo vituo saba vya mafuta ya magari. Jamaa huyu aligundua kuwa rafiki yake mpenzi alikuwa na uhusiano na mkewe na kwamba kati ya watoto aliokuwa nao wanne, wawili walikuwa wa huyo rafiki yake.

    Huyo naye alichukuwa maamuzi ya kuwaua watoto wote wa jamaa yake na kumwua mkewe kwa bastola,kisha akakimbia. Baadaye Alen alikamatwa na Polisi akiwa mafichoni na kupelekwa mahakamani. Mahakama ilimkuta na hatia hatimaye alihukumiwa kifungo cha maisha Gerezani. Mali zake alizozisumbukia kwa muda mrefu kwa taabu, aliziacha huku maisha yake yakiwa nyuma ya nondo akiteseka bila kikomo. Haya yote yalipita katika kichwa cha Dr. Jackson. Alifikiria kwa kina kitu cha kufanya ili asilete madhara kwa mtu yeyote.

    Mwishowe akaona vema kuwa asubuhi akatoe hela zote alizozitaka mkewe na kumkabidhi. Hizo ndizo zitakazomfanya awabambe pale watakapokutana kwa ajili ya kukabidhiana. Kwa njia hiyo Wezi wake watajihukumu wenyewe na huo unaweza kuwa ndio mwisho wa mkewe kumsaliti. Busara aliyoibuni ni kwamba baada ya kuwakuta jinsi watakavyobabaika na kuomba msamaha mwisho wa yote atatangaza msamaha kwao, bila kusababisha madhara kwa yeyote.

    Moyo wa Dr. Jackson uliuma sana kwa fedheha atakayoipata hasa itakapojulikana kwa watu kuwa mtoto aliyekuwa anajivuna naye sio wa kwake. Hali hiyo tena ikaibua maumivu katika moyo wake na maamuzi ya kwanza yakatibuka na kukosa uamuzi sahihi, juu ya jambo hilo.

    Machozi yalimtoka pindi alipokuwa akimwangalia mkewe aliyekuwa katikati ya usingizi. Mwisho wa yote alipitisha uamuzi aliouona ni wa Busara zaidi. Alipoangalia saa yake alikuta ilikuwa ni saa kumi na moja alfajiri. Alikesha hapo kitini akiwa amechanganyikiwa kutokana na mlundikano wa mambo. Mary aliamka alifajiri hiyo baada ya simu yake kupiga Alam. Ulikuwa ni wakati wa kuanza majukumu yake ya kumwandalia mumewe chai kusudi awahi kwenda kwenye mizunguko ya siku hiyo.

    “Heey! inamaana leo hujalala kabisa! Mbona uko vilevile na nguo zako ulizotoka nazo kazini jana?” Aliuliza Mary kwa mshangao. “Ni kweli sijalala kabisa nimekuwa na mambo mengi sana usiku huu.” Alijibu kwa upole sana Dr. Jackson akiwa kajiinamia mezani, akijifanya kuwa anapitia mahesabu kwenye karatasi.

    Lengo lake lilikuwa kuficha uso wake uliokuwa na majonzi. Sawa mume wangu pole sana kwa kazi hiyo nzito, ila ungejipumzisha japo kidogo kazi haziishi. Mwili ndio huo huo, wenyewe hauna spea unatakiwa uupumzishe, kusudi upate nguvu kwa ajili ya kufanya mambo mengine.” Alishauri Mary na kuingia maliwatoni kujiandaa, kwa ajili ya kuanza majukumu yake.

    Jackson hakujibu neno ila baada ya mkewe kutoka bafuni,naye aliinuka na kwenda kuoga. kisha akajiandaa na kumuaga mkewe kuwa anaondoka. “Si usubiri kidogo nikuandalie chai mume wangu?” Alisema Mary. “Nina suala muhimu naenda kuweka sawa ofisini kusudi niwe huru baadaye kwenda Bank; nikichelewa naweza nisipate muda wa kufanya mapatano yetu.” Alisema Dr. Jackson na kutoka huku akielekea lilipo gari lake alipanda ndani na kuliondoa gari kwa mwendo wa taratibu.



    * * * *

    Dr. Mudy alifurahi kumwona rafiki yake amemtembelea asubuhi hiyo. “Karibu ndugu yangu mbona asubuhi sana kwema huko?” Aliuliza Mudy akijaribu kuchangamka kwa rafiki yake. “Kwema tu kwani ni mara ya kwanza kuja hapa asubuhi kama hivi?” Aliuliza Dr. Jackson kisha alinyoosha mkono ili kusalimiana na rafiki yake. Walishikana mikono na kusalimiana, kisha Mudy akamkaribisha rafiki yake sebuleni.

    Baada ya kukaa kwenye kiti Dr. Jackson alimwambia rafiki yake: “Rafiki yangu nimeamini kile ulichokisema. Nimefanya upelelezi baadaye nimedhibitisha jambo lile kuwa ni kweli.” Alisema hivyo kisha akatulia kidogo… kisha akamweleza kila kilichotokea usiku wa jana yake. Dr.Mudy alikuwa anasikiliza kwa makini sana. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Lakini rafiki yangu una moyo wa uvumilivu sana. mtu mwingine angeshafanya mambo ya ajabu kwa hasira. Sasa ulikuwa unataka nikupe ushirikiano gani baada ya kugundua mambo hayo?” Aliuliza Dr. Mudy kwa utulivu. “Kwako nimekuja ili unipe ushahidi ulionao juu ya swala hili kusudi nipate nyongeza ya hayo niliyoyashuhudia jana.” Alisema Dr. Jackson. “Sawa rafiki yangu.” Alisema Mudy kisha akaenda jikoni kumwita mkewe na kumtaka awaletee kahawa. Kisha akarudi kwenye kiti chake na baada ya hapo akaendelea na mazungumzo..

    ”Unajua tangu mtoto anazaliwa nilijua kabisa kuwa hakuwa wa kwako. Ila nilinyamaza sikutaka kukuchanganya maana ulikuwa masomoni. Hali hiyo ilininyima rahasana na baadaye nilifuatilia ili nijiridhishe katika mashaka yangu. Kufuatilia kwangu nyendo za shemeji za kila wakati za ufukweni, kukazaa matunda.Siku moja nilienda ufukweni nikawaona Ramson na shemeji wakiwa wanaogelea. Hali hiyo ikanifanya nichukuwe picha kadhaa za ushahidi.

    Haikuishia hapo niliendelea kupeleleza na kugundua mengi sana. Mengi ya kutosha ambayo nayo niliyapiga picha. Lakini pia baadaye nikakumbuka tukio la ajali mbaya uliyoipata nchini India, tulipokuwa pamoja masomoni. Baada ya ajali ile ya piki piki uliyoipata baada ya kugongwa na gari, ulipopimwa ulionekana kuwa hungeweza kupata mtoto katika maisha yako. Ushahidi wa hilo ni vyeti hivi vya Hospitali uliyotibiwa. Wakati unapatiwa matibabu ulikuwa hujitambui, kwa namna hiyo kila kitu nilihusishwa mimi kama ndugu yako.

    Majibu hayo ya vipimo usingelivikumbuka kwa sababu wakati yanatolewa wewe ulikuwa mahututi kitandani. Nilipewa vyeti vyako na kwa bahati nikasahau kukupatia, nilihifadhi kwenye begi langu. Nilishanga nilipopata habari kuwa Shemeji alikuwa mjamzito. Ndipo nikakumbuka maneno ya Daktari kule India. Kumbukumbu yangu ilinipeleka kwenye cheti nikaamua kukitafuta. Baadaye Mungu sio Athumani nilikipata.

    Hiki ndio cheti chako kinachodhibitisha kuwa huwezi kupata mtoto!” Dr. Mudy alimwonyesha rafiki yake cheti hicho… na kumfanya Dr. Jackson aendelee kupigwa na butwaa!..Kisha akaendelea.“Kwa hiyo mpaka hapo nyongeza yangu ni hiyo na ushahidi wangu ni huo hapo. Moyo uliniuma pindi nilipokumbuka jinsi mama alivyokuwa akimsema vibaya mkeo kuwa ni mgumba.

    Hali hii ikanipa kuona kuwa labda shemeji alifikia mahali akapimwa na kuonekana kuwa hakuwa na matatizo hivyo akaamua kuzaa nje ya ndoa na kuificha siri hiyo japo kwa fedha ili kuficha aibu yake na yako katika ndoa yenu. Ndio maana akaamua kufanya hivyo!” Alisema Mudy akiwa katika hali ya kumtetea Shemeji yake kusudi rafiki yake asimchukulie maamuzi magumu.”

    Hayo niachie mwenyewe acha kumtetea! Dr. Jackson alisema huku akikiangalia kile cheti na picha alizopigwa mkewe akiwa na Ramson Ufukweni. Mara alisikia nyayo za shemeji yake yaani mke wa Mudy akija mezani akaficha zile picha chini ya meza. Mke wa Mudy alimsalimia shemeji yake kwa uchangamfu sana na baadaye alimkaribisha kahawa. Baada ya kuwamiminia kwenye vikombe. Jackson alishukuru kwa kahawa na kuendelea na mazungumzo yake na Dr.Mudy.

    “Jambo hilo la kuanza kumtetea shemeji yako achana nalo kabisa. Niachie mimi mchezo mzima nitajua nifanyeje sawa?” Alisema Dr. Jackson wakati akimalizia kahawa yake na kisha alinyanyuka akiwa kashikilia ushahidi wa picha na cheti chake baadaye akaaga kuwa anaondoka. “Sawa rafiki yangu lakini hupaswi kuchukuwa hatua yoyote mbaya. Ninakuamini sana kuwa wewe ni mtu jasiri unayeweza kuvumilia mambo magumu katika maisha.

    Sitaamini macho yangu kama utaonyesha kubadilika katika tabia yako ya mwanzoni. Jikaze na uendelee kuwa jasiri na mvumilivu ili mambo haya yamalizike kwa usalama. Naamini baada ya hapo amani itakuwa kubwa katika maisha yenu.Ninasema hivyo kwa sababu ninajua hii ni bahati mbaya tu.” Alisema Mudy maneno ya busara sana kwa rafiki yake baada ya kumwona akiwa na hasira kali. “Okay nimekuelewa nitakuona jioni kukupa michapo kuhusu kile kitakachotokea maana nataka niwafanye wakutane leo.”

    Alisema Dr. Jackson huku akiingia ndani ya gari lake na kuliondoa baada ya kuangalia saa yake ya mkononi. Neno la mwisho alilosema Dr. Jackson, Mudy hakulielewa kuwa alikuwa na maanisha nini kusema kuwa alikuwa anataka awafanye wakutane ufukweni leo. Mudy alikumbuka kumpungia mkono rafiki yake wakati akiwaamechelewa sana; badala yake aliona vumbi kiasi lililoonyesha kuwa rafiki yake alishatokomea.



    * * *

    Mary alifurahi sana kupatiwa mzigo wa hela na mumewe. Woooow! nafurahi sana Mume wangu kuona kwamba unanijali kiasi hiki. Asante kwa kuwa Mume mwema kwangu.” Alisema Mary wakati akizipokea hela hizo. “Usijali ni kawaida tu kwa mume kumjali mkewe.

    Ila sikai kuna mahali nakimbia nimekuletea tu hizi hela kusudi umpelekee rafiki yako, awahi kufanya utaratibu wa safari ya China au sio?” Aliuliza Dr. Jackson wakati akitoka na kuelekea iliko gari yake. Kwa Mary ilikuwa ni nafuu kwake kuona Mumewe kaondoka ili apate mpenyo wa kupeleka hela zile kwa Ramson. Alijiandaa haraka haraka na baada ya muda alianza safari kuelekea Ufukweni.

    Mwendo wake ulikuwa wa kasi sana wakati akienda ufukweni kwani alijua kuwa huenda mumewe angerudi mapema nyumbani asije akamkosa kisha akamfuata kwa Irene nako akamkosa ikawa taabu.Baada tu ya kuondoka Dr. Jackson alipiga simu nyumbani kwa msichana wake wa kazi aitwaye Magreth: “Halo mage mama ameshatoka au bado yupo?” Aliuliza ili kuhakikisha. “Ametoka na gari Muda si mrefu.

    Kwani hukumpata kwenye simu yake?” Aliuliza Mage. “Simpati sijui kuna tatizo gani kwenye simu yake alijibu Dr.Jackson kisha akakata simu na kuingia kwenye gari tayari kwa safari ya nyumbani. Aliporudi nyumbani aliingia kwa haraka chumbani na kumchukuwa mtoto Lameck na kuingia naye kwenye gari hatimaye kuliondoa kwa mwendo wa kasi sana. Hali hiyo ilimchanganya sana Mage kwa sababu ndio alikuwa anamwandalia mtoto uji wake. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikosa la kusema kwa sababu hakupata hata nafasi ya kuuliza, kutokana ana haraka aliyokuwa nayo bosi wake. Njiani watu walishangaa mwendo huo wa gari ilikuwa kama gari ya mashindano. Kwa mwendo huo aliwahi kufika maana kwa mbali aliona gari ya Mary ikiingia kwenye kibarabara kidogo ufukweni hapo.

    Baada ya Mary kupaki gari yake alitoka kwa haraka na kuelekea ilipo nyumba ya Ramson na wakati huo huo Dr. Jackson aliipeleka gari yake na kuipaki kando ya gari la mkewe. Taratibu alitoka ndani ya gari na kunyata huku akiwa amejawa na hasira kubwa sana. Alimwona mkewe akikumbatiana na Ramson baada ya Ramson kutoka kwenye nyumba yake. Ni ajabu kuwa hawakumwona kwa haraka Dr. Jackson akija labda ilikuwa ni kwa sababu ya shauku yao ya kuonana.

    Mfuko wa hela ulikuwa kwenye kiti wakati wao walipokuwa wakisalimiana. Kabla hawajamaliza kusalimiana walisikia sauti: “Hapo hapo mlipo msifanye jambo lolote wala kukimbia! Nataka maelezo ya kutosha kila mmoja ajieleze kwa zamu juu ya ubaya huu mnaonitendea.”Alisema Dr. Jackson kwa sauti nzito isiyo na mzaha hata kidogo. Mary na Ramson walipatwa na mshituko usio wa kawaida! Baada ya kugeuka walikutana na mtutu wa bastola! Mary alitamani ardhi ipasuke na kuingia! Alifedheheka sana kubambwa na mumewe katika hali ile akiwa na Ramson. Pamoja na kuiona bastola bado Ramson hakuvumilia aliamua kukimbia. “Simama hapo hapo kabla sijakumaliza!” Alisema Dr.Jackson kwa sauti kali lakini Ramson aliendelea kukimbia. Dr. Jackson alikasirika zaidi na kufyatua risasi iliyompata Ramson mguuni na kuanguka chini na kuachia kelele za maumivu.

    Baada ya kuanguka Dr. Jackson alimfuata kwa mwendo wa haraka akiwa na hasira kali, huku akiwa amemlenga na mtutu wa bastola yake. Ufukwe huo ulikuwa umetulia sana ila kelele za Ramson tu za maumivu. Wafanyakazi wote wa Ramson walitawanyika kwenda kufungasha mahitaji muhimu kwa ajili ya wateja. Kwa hiyo ufukweni hapo alikuwepo Ramson peke yake na wageni wake hao. Unafikiri unaweza kuniharibia familia yangu kisha unikimbie? Umefanya kosa kubwa sana.

    Heri ungesimama tu tukayaongea kuliko kunikimbia.”Alisema Dr. Jackson kwa hasira huku akimsogelea Ramson kwa hatua imara. Kuona vile Mary aliamua kuingilia kati na kwenda kumzuia mumewe. “Tafadhali usimuue Ramson hana kosa mimi ndio mwenye makosa yote mwache tafadhali.” Mary aliyasema hayo huku akimnyang’anya Dr. Jackson bastola yake.

    Wakati wakinyang’anyana kwa bahati mbaya risasi ikatoka kwenye bastola na kumpiga Mary kifuani, mara hiyo akaanguka chini! Jackson alihamaki sana na kuiweka bastola yak echini na kumwinania mkewe huku akipiga kelele.“Mary mke wangu usife! Mke wangu Mary Usife!! Nisamehe kwa hili lililotokea ni hasira tu. Na mimi nimekusamehe kwa yote uliyonitendea.

    Lakini Mary alikuwa tayari amekata roho. Uchungu wake uliongezeka na kutokwa na machozi mengi, huku moyo ukimwuma sana. Hakutaka kufanya hivyo tangu mwanzo; ni jambo lililotokea kwa bahati mbaya tu. Mary alikuwa kila kitu katika maisha yake. Kosa lile alikuwa tayari kumsamehe mkewe na kuendelea kuishi naye. Alizingatia sana maneno ya rafiki yake Mudy alipomwambia:

    “Moyo uliniuma pindi nilipokumbuka jinsi mama alivyokuwa akimsema vibaya mkeo kuwa ni mgumba. Hali hii ikanipa kuona kuwa labda shemeji alifikia mahali akapimwa na kuonekana kuwa hakuwa na matatizo hivyo akaamua kuzaa nje ya ndoa na kuificha siri hiyo japo kwa fedha ili kuficha aibu yake na yako katika ndoa yenu. Ndio maana akagharimika kufanya ujanja ili atoe fedha zote hizo!”

    Maneno hayo yalijirudia rudia katika akili zake huku akilia machozi mengi. Baadaye alikumbuka tena maneno ya mwisho aliyoambiwa na Dr. Mudy wakati wakiagana kuwa:

    “Ninakuamini sana kuwa wewe ni mtu jasiri unayeweza kuvumilia mambo magumu sana katika maisha. Sitaamini macho yangu kama utaonyesha kubadilika katika tabia yako ya mwanzoni. Jikaze na uendelee kuwa jasiri na mvumilivu ili mambo haya yamalizike kwa usalama. Naamini baada ya hapo amani itakuwa kubwa katika maisha yenu.”

    Maneno haya yalikuja kwa nguvu ya aina yake huku yakimsuta sana, kwa sababu tayari ameshafanya mambo ya ajabu kinyume na ushauri huo. Maisha yake aliyaona bure kabisa bila Mary mke wake. Mara hiyo hiyo akaamka na kuchukuwa bastola yake na kumsogelea Ramson aliyekuwa amejisogeza sana akitaka kutoroka. Alipomwona Dr. Jackson anakuja alipiga kelele za kuomba msamaha: “Nisamehe kaka, usiniue tafadhali! Ni ushawishi tu na ibilisi, nisamehe mkubwa wangu!”Sauti yake ilikuwa ya kutetemeka na macho alikuwa ameyatoa kwa woga akiogopa kifo!

    “Ukweli unastahili kufa tena kifo kigumu zaidi ya mtu yeyote, kumbuka makosa yako yote! Umenichukulia mke wangu na kuzaa naye, na ni wewe umesababisha kifo chake. Lakini Mimi sitakuua kama ulivyofikiri, Moyo wangu unauma sana kwa hukumu jinsi nilivyomwua mke wangu japo sikudhamiria!”Alitulia kidogo akiwa anatafakari jambo! Kisha kama aliyeshtuka akamwambia kwa sauti: “Nipe kalamu na karatasi upesi kabla sijageuza mawazo yangu!” Alifoka kwa hasira kali. “Viko pale mezani kwenye kibanda changu kaka!” Alisema Ramson huku akiendelea kutetemeka kwa hofu.

    “Subiri hapo usiondoke ukiondoka nitakuadhibu.” Alisema hivyo Dr.Jackson wakati akikimbilia kibandani. alikaa baada ya kukuta karatasi na kalamu, kisha akaandika mambo mengi sana kwenye karatasi kama mbili hivi. Baada ya hapo alinyanyuka na kwenda aliko Ramson na kumpa zikiwa zimekunjwa.

    “Chukuwa karatasi hizi na ufuate maelekezo yote yaliyopo humo!” Alisema Dr Jackson huku akiwa katika hali mbaya sana iliyotawaliwa na huzuni na hasira. Ramson alizipokea kwa mashaka huku akiwa anaendelea kusihi asamehewe. Hakujua maana ya karatasi hizo.“Ramson Mtoto wako uliyezaa na mke wangu yuko ndani ya gari yangu pale. Nimegundua mambo yote yaliyofanyika na ushahidi wote upo ndani ya dashboad kwenye gari. Sina tena thamani ya kuishi katika dunia hii bila mke wangu Mary!” Dr. Jackson aliyasema hayo huku akimwacha Ramson na kumsogelea mkewe. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipofika ilipo maiti ya Mary alipiga magoti na kuishika huku akiongea maneno ambayo Ramson hakuyasikia kwa sababu ya umbali. Ghafla Ramson alimwona Dr. Jackson akinyanyua bastola kujielekezea kichwani! Alipiga kelele “Usifanye hivyo Brother!” Alijikongoja kujaribu kwenda kumzuia asijiue, lakini maumivu ya mguu yalikuwa makali sana kiasi cha kushindwa kusogeza hatua hata tatu mbele.

    Kelele zake za kutaka kumzuia asijiue hazikufua dafu, mlio wa bastola ulisikiika na mara hiyo Dr. Jackson alianguka kando ya mkewe na kufa hapohapo. Mshituko alioupata Ramson ulikuwa ni mkubwa sana, hivyo alipiga kelele za mfululizo kama kichaa! Ilikuwa wazimu hasa maana mambo yenyewe yalikuwa hayachukuliki katika akili za kawaida!



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog