Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

THE LOVE YOU HAD BEFORE (PENZI ULILOKUWA NALO KABLA) - 2

 







    Simulizi : The Love You Had Before (Penzi Ulilokuwa Nalo Kabla)

    Sehemu Ya Pili (2)



    Mama Evadia hakutaka kutulia nyumbani, alihisi hasira moyoni mwake, alichokifanya ni kuondoka nyumbani hapo na kuelekea kwa akina Dickson ambapo huko akawaambia wazazi wa kijana huyo kila kitu kilichokuwa kimeendelea. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wazazi hao hawakuamini, waliuliza mara mbilimbili kama alikuwa na uhakika na kile alichokizungumza, mwanamke yule aliwaambia kwamba kila kitu kilikuwa wazi, alipoona hiyo haitoshi, akampigia simu Evadia na kumtaka kuelekea nyumbani kwa kina Dickson ambapo alifanya hivyo haraka sana.

    “Ni kweli Evadia?” aliuliza baba yake Dickson.

    “Ni kweli! Ameniambia amepata mwanamke mwingine.”

    Wazazi hao wakashtuka, hawakutegemea kusikia kile walichokisikia mahali pale, walibaki wakimwangalia msichana yule, walipigwa na mshangao mkubwa. Walimfahamu kijana wao, waliyajua mapenzi mazito aliyokuwa nayo kwa msichana yule, leo hii kusema kwamba hakuwa akimhitaji kwa sababu alikuwa amepata mwanamke mwingine, mioyo yao ilisikia maumivu makali.

    “It is impossible,” (Haiwezekani)

    “Ndiyo hivyo!” alisema Evadia na kuanza kulia kwa uchungu. Maumivu yake ya moyo, hakika hayakuweza kupungua. Dickson alimchanganya mno.



    Kwa jina aliitwa Luciana Pentezel, msichana mrembo aliyetoka nchini Rwanda. Kwa kumwangalia tu, usingekuwa na wakati mgumu wa kusema kwamba Luciana alikuwa miongoni mwa wasichana wazuri waliowahi kuumbwa katika sayari hii.

    Alikuwa na sura nyembamba ya Kitusi, macho makubwa yaliyomuonyesha kwamba muda wowote ule usingizi mzito ungempata, alikuwa na lipsi nene huku meno yake yakiwa meupe kabisa.

    Kwa sura alivutia mno, kila mwanaume aliyemwangalia Luciana alibaki na kumbukumbu kwamba katika maisha yake aliwahi kumuona msichana aliyekuwa na urembo wa ajabu.

    Japokuwa nchini venezuela kulikuwa na wasichana wengi warembo lakini kwa Luciana kila msichana alikaa pembeni, chuoni hapo alikuwa gumzo, kila alipopita, wanaume walimwangalia kwa matamanio makubwa.

    Luciana hakuwa msichana wa tofauti, hakuwa na maringo, alipewa kuzungumza na kila mtu kitu kilichomfanya kupendwa mno.

    Katika mambo yote hayo, uzuri wote aliokuwa nao, Luciana alihusudu sana pesa, alipenda pesa sana zaidi ya alivyokuwa akimpenda Mungu. Kila alipokaa, alitamani pesa ziwe zimemzunguka, kila alipopita alitamani akanyage pesa kwenda sehemu yoyote aliyotaka kwenda.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, hakuwahi kuwa katika uhusiano na mwanaume asiyekuwa na pesa. Alitoka katika familia ya kimasikini, alikwenda nchini Venezuela kama bahati tu hivyo alivyofika, alitaka kurudi nchini Rwanda huku akiwa na heshima ya juu kabisa, atafute pesa popote zilipo ili mwisho wa siku atakaporudi nchini Rwanda basi awe na utajiri wa kutosha.

    Uzuri wake ukawavuta wanaume wengi, walipogundua kwamba msichana huyo alihusudu sana pesa, wakamfuata na pesa zao na kisha kulala naye. Luciana hakuwa msichana mwenye kujali, alitembea na kila mtu aliyekuja kwake na kutanguliza pesa mbele.

    Kila alipopata mimba, kwake ilikuwa ni bahati mbaya tu, hivyo akatoa na maisha kuendelea kama kawaida. Siku zikakatika, wanaume wakazidi kutembea naye, wakampa pesa nyingi mpaka kufikisha kiasi cha dola milioni mbili, zaidi ya milioni mia nne.

    Alijiona kuwa tajiri, alijiona kuwa na sauti kubwa mara atakaporudi nchini Rwanda. Hakukoma, hakuacha, bado msururu wa wanaume uliendelea kujipanga huku kila aliyekuja kulikuwa na sharti kubwa la kuacha pesa mezani, kiasi kikubwa cha pesa ambacho hata wakati mwingine kilifika dola elfu tano, zaidi ya milioni kumi, kwa watu wenye pesa, hawakujiuliza, walitoa kiasi hicho cha fedha ili mradi mwisho wa siku walale naye tu.

    “Kuna mvulana amekuja chuo,” alisikika rafiki yake aitwaye Serena, msichana kutoka nchini Ethiopia aliyekuwa anamuunganishia kwa wanaume wengi hapo chuoni.

    “Mvulana gani?”

    “Ni Mtanzania, mzuri sana.”

    “Kweli?”

    “Ndiyo!”

    “Ana pesa?”

    “Mmmh! Sijui!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa bila pesa, hata sidhani kama kuna mtu anaweza kuwa mzuri. Uzuri wa kweli ni pesa tu, hivyo vingine mbwembwe,” alisema Luciana huku akibinua mdomo wake.

    Hicho ndicho alichokifikiria, hakuamini kama duniani kulikuwa na wanaume wazuri, kwake aliamini katika pesa, kwamba unapokuwa na pesa, hata kama wewe ni mbaya bado utaonekana mzuri tu.

    Kila siku Serena alimwambia kuhusu mwanachuo mpya aliyekuja kujiunga chuoni hapo, mwanaume mwenye uzuri wa sura ambaye alitoka nchini Tanzania. Kila siku Luciana alikuwa bize na wanaume wenye pesa ambao walimfuata na magari ya thamani chuoni hapo.

    Alipelekwa katika kumbi za starehe, kulala kwenye hoteli za gharama ilikuwa kawaida yake, hakujuta kuwa mzuri, kila siku ilikuwa ni lazima kumshukuru Mungu kwa uzuri aliompa ambao muda huo aliona faida yake kubwa.

    “Luciana!”

    “Abeee!”

    “Kesho una ratiba gani?”

    “Nakwenda kwa Arnandro!”

    “Mmh! Yule si muuzaji wa madawa ya kulevya?”

    “Ndiyo! Kwani mimi nakwenda kuuza? Si nakwenda kuchuma pesa tu,” alisema Luciana.

    “Mmh! Ila kuwa makini.”

    “Usijali.”

    Alitembea na watu wengi mno, wenye pesa ambao walitamani kuwa na wanawake wazuri. Kwa Luciana hakutaka kujali kitu chochote kile, alichokuwa akikifikiria kwa wakati huo kilikuwa pesa tu.

    Hakujali kama mtu fulani alikuwa muuzaji wa madawa ya kulevya au alizipata pesa kwa njia haramu, alichokuwa akikiangalia ni mfuko wake kujaa pesa tu. Alizibabaikia pesa, utajiri mkubwa ukaanza kunukia maishani mwake, hakufikiria kurudi Rwanda, hata kulipokuwa na likizo, alihakikisha kwanza anatafuta fedha kwa juhudi zote na ndiyo arudi huko.



    “Ulikuwa unasemaje siku ile?” aliuliza Luciana.

    “Siku gani?”

    “Kuna siku uliniambia kwamba kuna mwanaume amefika chuo ni mzuri sana.”

    “Bado unakumbuka tu?”

    “Ndiyo! Ninataka kumuona.”

    “Yupo chuo.”

    “Leo lazima niende, sikwenda siku nyingi, nitataka kumuona,” alisema Luciana.

    “Basi usijali. Twende.”

    Alifanya mambo mengi, alifanya ufuska mpaka kufikia hatua kuona kwamba ilikuwa imetosha. Alikusanya kiasi kikubwa cha pesa, akaunti yake ikajaa pesa, hakukuwa na kitu alichokihitaji kwa wakati huo zaidi ya kuwa na mwanaume mmoja tu.

    Mtu aliyekuwa akimfikiria kwa wakati huo ni huyo mwanaume aliyeambiwa kwamba alikuwa mzuri wa sura, mvulana aliyewavutia wanawake wengi lakini hakukuwa na yeyote aliyefanikiwa kumpata.

    Kwake, Luciana hakuwa na tatizo lolote, alijua kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni lazima mwanaume huyo amkubali kwa sababu tu alikuwa mzuri wa sura, msichana aliyependwa na wanaume wote, waliokuwa na fedha na hata wale ambao hawakuwa na kitu.

    Kilipita kipindi kirefu hakuwa amekwenda chuo. Siku ambayo alifika chuoni hapo, wanaume walipomuona, macho yakawatoka, msichana huyo alipotea kwa kipindi fulani na siku hiyo ambayo alifika chuoni hapo alionekana kuwa mrembo hasa, mara tano ya jinsi alivyokuwa kipindi cha nyuma.

    Alifika chuoni hapo kwa lengo la kumuona mwanaume aliyezungumzwa sana na rafiki yake, mwanaume aliyekuwa mzuri wa sura ambae aliamini kwamba hata yeye mwenyewe angeweza kumpenda.

    “Yupo wapi?”

    “Nani?”

    “Si huyo mwanaume uliyesema ni mzuri!”

    “Twende kule, nilimuona sehemu ya kulia chakula,” alisema Selina.

    Hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kwenda sehemu iliyokuwa ikihusika na uuzaji wa chakula. Walipofika kule, wakaanza kuyapeleka macho yao huku na kule na kwa bahati nzuri macho yao yakatua kwa mwanaume waliyekuwa wakimtafuta.

    “Luciana....”

    “Abeee...”

    “Mwanaume mwenyewe yule pale,” alisema Selina huku akimuonyeshea Luciana sehemu aliposimama mwanaume huyo.

    Luciana alipomuona, kwanza akatoa mguno, hakuonekana kuamini kama duniani kulikuwa na mwanaume mzuri kama alivyokuwa yule ambaye alionyeshewa mahali pale. Moyo wake ukaanza kubeba kitu kizito, shauku kubwa ikamuingia moyoni mwake, akajikuta akiwa hajiwezi.

    “Selina...is that the one?” (Selina...yule ndiye mwenyewe?) aliuliza Luciana huku akionekana kutokuyaamini macho yake.

    “He is the one.” (Ndiye mwenyewe)

    Luciana hakutaka kubaki mahali hapo, hakuona kama alitakiwa kusimama zaidi, akili yake ilichanganyikiwa mno, hakuamini kama katika dunia hii kungekuwa na mwanaume mzuri kama alivyokuwa yule aliyeonyeshewa, tena kutoka barani Afrika.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akashindwa kuvumilia, akajikuta akianza kupiga hatua kumfuata. Mahali pale kulikuwa na gumzo, kitendo cha msichana Luciana kuonekana mahali hapo kilimchanganya kila mwanaume aliyemwangalia.



    Umaarufu wake, uzuri wake uliwadatisha watu wengi, wanaume wakabaki kimya huku wakimwangalia, hawakuamini kama yule Luciana ambaye kila siku alionekana kuwa mrembo, leo alikuwa mara tano ya zaidi ya urembo aliokuwa nao kabla.

    Alipomfikia kijana yule, akamshtua kwa kumshika bega, alipogeuka, macho ya mwanaume yule yakatua usoni mwa msichana aliyeonekana kuwa mrembo mno, msichana ambaye urembo wake alihisi kwamba hakuwahi kuuona sehemu yoyote ile.

    “My name is Luciana, a beautiful girl you have never met,” (Jina langu ni Luciana, msichana mrembo ambaye haujawahi kukutana naye) alisema Luciana huku akiachia tabasamu.

    “My name is Dickson.” (Ninaitwa Dickson).

    Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa wawili hawa kukutana, walipoonana kwa mara ya kwanza, kila mtu akatokea kumpenda mwenzake. Wasichana walichanganyikiwa na uzuri aliokuwa nao Dickson lakini kwa upande wa pili hata wanaume walichanganyikiwa na uzuri aliokuwa nao Luciana.

    Wawili hao wakatengeneza muunganiko wa hatari, kila aliyekuwa akiwaangalia alibaki akitabasamu tu kwani watu hao kama walijua jinsi walivyokuwa wazuri, hivyo waliamua kuchaguana.

    Katika kipindi cha kwanza Dickson alimkumbuka sana msichana wake aliyemuachana nchini Tanzania, Evadia, aliwasiliana naye mara chache chache lakini baada ya kuwa karibu na Luciana, akaanza kumsahau msichana huyo aliyekuwa nchini Tanzania.

    Penzi likamteka, hakuwa na sababu ya kumpenda msichana kama Evadia, kwake, alimuona msichana huyo kuwa wa kawaida sana, msichana masikini ambaye aliamini katika maisha yake asingeweza kumsaidia kwa lolote lile.

    Baada ya kuwa na Dickson, hata maisha ya Luciana yakabadilika, hakuwa kama jinsi alivyokuwa kipindi cha nyuma, akaacha tabia yake ya kufuata wanaume wengi, alijiahidi kwamba angekuwa mwaminifu na hicho ndicho kilichotokea.

    Kwa Luciana, akafika, hakutaka kusikia lolote lile kutoka kwa mwanaume yeyote yule. Wanaume wengi wakaendelea kumchombeza kwa maneno matamu tena wengine wakiweka pesa mezani lakini moyo wa Luciana ulibadilika kabisa, alichokifikiria kwa wakati huo hakikuwa pesa tena, yalikuwa ni mapenzi ya dhati ambayo aliyapata kutoka kwa Dickson ambaye alikuwa amemuacha msichana aliyekuwa naye nchini Tanzania, Evadia kwa ajili yake.



    Moyo wake ulijeruhiwa, kama ni mtu, tayari aliumwa na nyoka hivyo hata alipokuwa akiguswa na ujani, alishtuka. Moyo wake ukabadilika, kitendo alichofanyiwa na Dickson kilimuumiza mno na kujiahidi kwamba milele yote asingeweza kuwa na mwanaume hivyo alipaswa kumkatalia kila mwanaume aliyekuja mbele yake.

    Chuki kubwa ikamkamata moyoni mwake, hakuamini kama wanaume aliokuwa akiwachukia kipindi hicho, kulikuwa na mwanaume mwingine ambaye alianza kumfuatilia, mwanaume asiyemfahamu ambaye aliamua kuacha kazi zake kwa ajili yake.

    Alipomuona Laurence akimfuatilia, alichukia, aliyachukia mapenzi hivyo hakutaka kuwa na mwanaume yeyote yule. Mama yake alilifahamu hilo, kila alipomuona Laurence, alimfukuza kwa kumwambia aondoke kwani binti yake hakutaka kuonana naye.

    “Ninahitaji kumuona Evadia,” alisikika Laurence.

    “Evadia!”

    “Ndiyo mama!”

    “Huwezi kumuona.”

    “Kwa nini jamani?”

    “Nimesema huwezi. Hunielewi?”

    “Siwezi kukuelewa mpaka nimuone,” alisema Laurence.

    Japokuwa alikatawaliwa sana na Evadia lakini hakutaka kusikia, hakutaka kuacha kumfuatilia, kwake, msichana huyo alionekana kuwa kila kitu, alimpenda kwa mapenzi ya dhati kutoka moyoni, hakutaka kuwa na msichana mwingine zaidi ya Evadia tu.

    Mama yake Evadia alimkatalia kuonana naye tena huku akimtaka kuondoka nyumbani hapo lakini Laurence hakutaka kuondoka. Maisha aliyokuwa akiyaleta mahali hapo yalionekana kuwa kama filamu fulani ya kimapenzi lakini kile kilichokuwa kikitokea, alikimaanisha kwa asilimia mia moja.

    “Siondoki mpaka nimuone Evadia,” alisema Laurence huku akikaa nje ya nyumba ya kina Evadia.

    Mama Evadia hakutaka kujali sana, alichokifanya ni kuingia ndani na kuufunga mlango huku tayari ikiwa saa moja usiku. Laurence hakutaka kuondoka mahali hapo, wakati mwingine hata yeye mwenyewe alibaki akijishangaa kwamba ilikuwaje amng’ang’anie msichana mmoja namna hiyo, hakutaka kujali sana, aliendelea kusubiri zaidi na zaidi na hata kama ingewezekana kulala mahali hapo, alikuwa tayari.

    Mbu walimuuma, aliwaua na kuendelea kumsubiri msichana huyo. Alikuwa ndani, hakutaka kuingia kumfuata, alitaka msichana huyo atokea na kuzungumza naye kwani siku moja kwake pasipo kuona ilikuwa ni adhabu kali ya kaburi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Muda ulizidi kuyoyoma, saa mbili ikaingia, saa tatu, saa nne, saa tano lakini bado Laurence hakuondoka mahali hapo.

    Ndani, Evadia alikuwa ametulia kitandani, moyo wake ulimuuma mno, bado alikuwa kwenye maumivu makali ya kukataliwa na mwanaume aliyempenda kwa moyo wa dhati.

    Alilia usiku kucha, kila siku akawa mtu wa kumlalamikia Mungu kwa kile kilichotokea, alijutia kitendo chake cha kuwa na mwanaume huyo ambaye mwisho wa siku alimsababishia maumivu makali ya moyo.

    Mama yake alipomwambia kwamba Laurence alikuwa nje akimsubiria, alikunja uso wake, alionekana kuwa na hasira kali mno. Hakutaka kuwa na mwanaume yeyote kwa kipindi hicho, alitaka kubaki peke yake, aishi peke yake na hata kama angezeeka, alitamani kuzeeka akiwa peke yake.

    Ilipofika saa tano na nusu usiku, Evadia akaelekea sebuleni ambapo akalifuata pazia chakavu na kuchungulia nje, alimuona Laurence amekaa kibarazani huku akiwa amejikunyata, baridi lilimpiga na mbu kumng’ata lakini hakutaka kuondoka mahali hapo.

    Huruma ikamuingia, akajikuta akiufuata mlango na kuufungua, akasimama mlangoni na kumwangalia Laurence ambaye naye alibaki akimwangalia machoni, tabasamu likaanza kuonekana usoni mwake.

    Laurence hakutaka kuishia hapo tu, alichokifanya ni kusimama na kumfuata Evadia pale mlangoni aliposimama na kuanza kuzungumza naye.

    “Hii yote kwa ajili yako,” alisema Laurence, alikuwa akianza kutetemeka kwa baridi kali la usiku.

    “Laurence...”

    “Nakusikiliza.”

    “Naomba uniache, sipo sawa,” alisema Evadia.

    “Najua Evadia. Macho mekundu, umenyong’onyea, ila naweza kukupa furaha maishani mwako,” alisema Laurence.

    “Najua Laurence....ila naomba uniache.”

    “Siwezi Evadia. Niambie tatizo nini.”

    “Basi tu.”

    “Hapana! Kuna kitu! Naweza kukupa mawazo pia, unachotakiwa ni kuniamini tu.”

    “Naomba tufanye siku nyingine. Rudi nyumbani.”

    “Unadhani nitakuwa na furaha? Unadhani nitakuwa katika hali ya kawaida? Evadia, ninakupenda, unalijua hilo, siwezi kurudi nyumbani huku nikikuacha katika hali hiyo, naomba uniambie, nini kinaendelea,” alisema Laurence huku akionekana kulengwa na machozi.

    “Mapenzi yanauma Laurence.....” alisema Evadia, hapohapo akaanza kububujikwa na machozi.

    Laurence akasikia maumivu makali moyoni mwake, alichokifanya ni kumsogelea zaidi Evadia kisha kumkumbatia, akaanza kumbembeleza kwa kumpigapiga mgongoni. Hakutaka kumuona msichana huyo akilia, akiumia kwa kitu chochote kile.

    Kwa jinsi alivyokuwa akiumia, hata naye maumivu yake yalikuwa vilevile. Machozi ya Evadia yakatiririka na kuulowanisha mgongo wake kwani bado walikuwa wamekumbatiana tu.

    “Usilie...”

    “Inauma Laurence....”

    “Ninaahidi kukupa furaha na kukusahaulisha kwa kila kitu,” alisema Laurence.



    Utajiri wake mkubwa aliokuwa nao ulikuwa siri kubwa, hakutaka Evadia afahamu au hata mama yake ajue hali halisi ya maisha yake. Jina lake lilikuwa kubwa nchini Tanzania lakini bahati mbaya watu hawakuwa wamemuona hivyo kuwa na shauku ya kutaka kujua kwamba huyu bilionea Laurence alikuwaje, alifananaje na aliishi vipi.

    Hakuacha kwenda nyumbani kwa kina Evadia, kidogo kwa wakati huo hali ilikuwa afadhali, msichana huyo hakuwa mtu wa kuwa na majonzi wakati wote, kwa Laurence, mwanaume huyo alijitahidi kumpa furaha.

    Hakumpa ruhusa msichana huyo kufika nyumbani kwake, alichokuwa akikifanya ni kumfuata kwao na kuzungumza naye, kama walitakiwa kutoka, walitoka kwenda sehemu, walizungukazunguka na kurudi.

    “Laurence...” aliita Evadia.

    “Naam.”

    “Hivi unaishi wapi?”

    “Kwani hupajui?”

    “Sipajui.”

    “Kweli?”

    “Kweli! Hujaniambia.”

    “Naishi Manzese Midizini.”

    “Na unafanya kazi wapi?”

    “Mmh! Mbona maswali mengi jamani?”

    “Kwani ni vibaya nikijua?”

    “Si vibaya sana, ila usijali. Nafanya kazi katika Ofisi ya Kata ya Manzese, nimeajiriwa pale kama fundi umeme,” alijibu Laurence.

    “Kumbeee!”

    “Ndiyo! Samahani kwa kukuficha kwa muda mrefu.”

    “Usijali.”

    “Leo wapi?”

    “Twende popote pale, nitakuwa na furaha kwa kuwa nipo pamoja nawe,” alijibu Evadia.

    Kwa kipindi chote hicho, Laurence hakutaka kumwambia ukweli Evadia namna alivyokuwa. Alijifanya kuwa mtu wa kawaida, hakutaka kujulikana kwa msichana huyo kama alikuwa bilionea.

    Waliondoka nyumbani kwa kina Evadia na kwenda Manzese Darajani, huko, walisimama juu na kupiga picha. Kwa Evadia ilikuwa ni furaha pekee, aliwahi kuwa na mwanaume mwenye fedha na matokeo yake kilichotokea ni kitu kilichomuumiza mno.

    Leo hii alikuwa na mwanaume mwingine, alikuwa bilionea mkubwa nchini Tanzania lakini Evadia hakufahamu hilo, kila alipomwangalia Laurence, jinsi alivyokuwa akivaa, simu aliyokuwa akiitumia, alionekana mtu wa kawaida sana.

    Walisimama katika daraja la Manzese, walikuwa wakiangalia huku na kule, kila mmoja alionekana kuwa na furaha mno. Evadia alifarijika sana, upendo wa dhati alioupata kwa mwanaume huyo ulikuwa tofauti kabisa.

    “Najifunza mengi sana kutoka kwako mpenzi,” alisema Evadia, Laurence akashtuka kusikia hivyo kwani kwa kipindi chote hicho hakuwahi kuitwa mpenzi.

    “Kama yapi?”

    “Ni bora kuwa na mpenzi asiyekuwa na kitu kuliko kuwa na mpenzi mwenye fedha,” alisema Evadia.

    “Kwa nini?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wenye fedha wanaringa, wanajiona wao ndiyo wao, ila mkikutana masikini msiokuwa na kitu kama tulivyo, kila kitu kinakwenda sawa,” alisema Evadia huku akiachia tabasamu.

    “Najua hilo mpenzi. Maisha ya mapenzi ni mapenzi, fedha haina nafasi katika mapenzi,” alisema Laurence.

    Walizungumza mambo mengi, bado Evadia hakujua mtu aliyekuwa naye alikuwa wa namna gani. Kitu alichokijua ni kwamba Laurence alikuwa masikini wa kutupwa, aliyaamini maneno yake kwamba alikuwa mtu asiyekuwa na fedha, yaani alikuwa fukara kama alivyokuwa.

    Baada ya kuzungumza naye kwa kipindi kirefu darajani, wakateremka na kuanza kuondoka mahali hapo. Walitakiwa kupanda daladala kutoka hapo Manzese mpaka Mburahati lakini hilo lilishindikana kwani kwa maneno ya Laurence, mfukoni hakuwa na kitu.

    “Kwa hiyo?” aliuliza Evadia.

    “Tutembee tu, au una hela yoyote hapo?”

    “Mmh! Sina.”

    “Basi tutembee, baadaye nitarudi hukuhuku Manzese,” alisema Laurence.

    Wakaanza kutembea huku wakizungumza mambo mengi. Ilikuwa ni ngumu mno kwa Evadia kugundua kwamba mtu aliyekuwa naye alikuwa bilionea mkubwa Tanzania, tena hata yeye mwenye alimsikia sana.

    Katika kipindi chote hicho Laurence alionekana kuwa na furaha mno, kuwa na Evadia katika maisha yake hakika kilikuwa kitu kilichompa furaha sana katika maisha yake. Walichukua dakika arobaini wakafika nyumbani kwa kina Evadia, wakamkuta mama Evadia akiwa nje.

    “Nimemrudisha nyumbani,” alisema Laurence mara baada ya salamu.

    “Sawa. Karibu tena Laurence.”

    “Asante mama.”

    Laurence akamsogelea Evadia na kumbusu shavuni, alipomaliza, akaondoka zake kurudi nyumbani. Alipofika njiani, akasimamisha bodaboda, akapanda na kuelekea nyumbani. Kila kitu alichokuwa akikifanya, alikifanya kimakusudi, hakutaka apendwe na msichana huyo kwa sababu ya fedha tu.



    Siku iliyofuata, asubuhi na mapema Laurence akajiandaa kwa ajili ya kwenda kumtembelea mpenzi wake. Kwa wakati huo, hata kazi hakutaka kufanya, alitaka kuweka mambo sawa kabisa, hakutaka kuwa bize na kazi kwani ukaribu wake na Evadia ulikuwa kitu cha muhimu kuliko vitu vingine.

    Alipomaliza kujiandaa, kama kawaida yake akachukua bodaboda na kuelekea huko. Njiani, mawazo yake yalikuwa kwa Evadia tu, alimuona kuwa na thamani mno, alipenda zaidi ya mtu yeyote katika dunia hii.

    Alipofika nyumbani kwa kina Evadia, kitu kilichomshangaza ni kwamba mlango ulikuwa umefungwa kitu ambacho hakikuwa kawaida kabisa. Laurence akachanganyikiwa, alijaribu kuufungua mlango ule, ulikuwa umefungwa kwa ufunguo, hakuishia hapo, alichokifanya ni kuanza kuita, ukimya mkubwa ulitawala ndani.

    “Evadiaaaa...Evadiaaaa...” aliita huku akiwa amesimama nje ya nyumba ile, hakukuwa na sauti yoyote iliyosikika kutoka ndani.

    Alijaribu kuzunguka mpaka nyuma ya nyumba ile huku akiendelea kuita lakini bado ukimya uliendelea kutawala mahali hapo. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kimeendelea, alichokifanya ni kwenda kwa majirani na kuwauliza juu ya hali iliyokuwa ikiendelea mahali pale.

    “Walikwenda hospitali asubuhi sana,” alijibu jirani mara baada ya kuulizwa.

    “Nani anaumwa?”

    “Evadia. Ugonjwa wake uleule.”

    “Upi?”

    “Wanasema figo yake moja ina matatizo na ndiyo maana mara kwa mara anazimiazimia,” alijibu jirani huyo.

    “Wamekwenda hospitali gani?”

    “Mmh! Sijui! Ila nadhani Palestina, nenda huko kajaribu kumtafuta,” alijibu jirani huyo.

    Laurence akachanganyikiwa, kile alichoambiwa kilimchanganya kichwa chake. Akabaki akijiuliza juu ya ugonjwa uliokuwa ukimsumbua mpenzi wake, hakuwa ameambiwa kabla japokuwa kuna siku mama yake Evadia alimwambia kwamba alizimia.

    Hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka nyumbani hapo, kwa kasi kubwa na kuelekea huko hospitali. Akachukua bodaboda na kuelekea huko huku akionekana kuchanganyikiwa mno.

    Japokuwa dereva alikuwa akiendesha bodaboda kwa mwendo wa kasi, yeye aliona akiendesha kwa mwendo mdogo hali iliyomfanya kumwambia dereva huyo aongeze kasi.

    “Vuta moto kaka! Vuta moto mpaka pikipiki ipae,” alisema Laurence.

    “Kaka! Kwa magari haya, tutakufa.”

    “Kufa si tatizo, unaogopa kufa?”

    “Mmmh!”

    “Wewe ongeza kasi, hizi hospitali zimewekwa kwa ajili yetu.”

    Alisema Laurence na hivyo dereva wa bodaboda kufanya kama alivyotaka mteja wake.

    Kama kuchanganyikiwa, Laurence alichanganyikiwa mno, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, msichana aliyempenda, aliyeonekana kuwa kila kitu katika maisha yake alikuwa hoi hospitalini.

    Hakukuwa na kitu kilichomuumiza kichwa kama hicho, kila alipomwambia dereva bodaboda aongeze kasi, aliona aliendesha kwa kasi ndogo japokuwa dereva huyo aliongeza kwa kiasi kikubwa.

    Baada ya dakika chache, wakafika katika Hospitali ya Sinza Palestina na hapohapo Laurence akaruka kutoka katika bodaboda na kuanza kukimbia kuelekea ndani, yaani hata kumlipa dereva hela yake hakukumbuka kabisa.

    “Nimekuja kumuulizia mgonjwa wangu,” alisema Laurence, alikuwa amemsimamisha nesi mmoja aliyekuwa akipita mbele yake.

    “Nani?”

    “Anaitwa Evadia.”

    “Mmmh! Nenda kule kwa upande wa magonjwa ya wakinamama,” alisema nesi yule, hapohapo Laurence akaanza kuelekea huko.

    “Braza, hujanilipa hela yangu,” alisema dereva bodaboda baada ya kumsogelea. Hapohapo Laurence akaingiza mkono mfukukoni na kutoa noti ya shilingi elfu kumi, hakutaka kusubiri chenji, akaondoka zake.

    Laurence alionekana kuwa na haraka. Hakutaka kupoteza muda mahali hapo, alichokifanya ni kuelekea kule alipokuwa ameelekezwa, alipofika, akakuta kundi la wanawake wakiwa wamekaa kwenye mabenchi yaliyokuwepo mahali pale, kila mmoja akaanza kumwangalia.

    Laurence akayapitisha macho yake huku na kule, yakagongana na macho ya mama yake Evadia, hapohapo akaanza kumfuata.

    “Kuna tatizo gani mama?” aliuliza Laurence.

    “Evadia anaumwa.”

    “Anasumbuliwa na nini?”

    “Figo yake moja haifanyi kazi vizuri, huwa inafeli,” alisema mama yake Evadia, Laurence akashusha pumzi ndefu na nzito.

    “Yupo wapi kwa sasa?”

    “Amelazwa ndani, daktari aliniambia nisubiri nje, wanamshughulikia,” alijibu mwanamke huyo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Laurence akaungana naye mahali pale. Wote wawili walionekana kuwa na mawazo lukuki, Laurence alikuwa akimfikiria mpenzi wake tu kwamba ni kwa namna gani angeweza kupata matibabu yanayotakiwa.

    Hakutaka kuonekana kama ana fedha nyingi, hakutaka ajulikane kama alikuwa bilionea lakini kwa jinsi hali ilivyokuwa ikienda, alionekana kuwa na wasiwasi kwamba ilikuwa ni lazima ijulikane kwani asingekubali kuona msichana aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati akifa.

    Walikaa kwa saa mbili ndipo walipofuatwa na daktari na kuambiwa kwamba waende ndani kumwangalia Evadia. Kitendo cha Laurence kumuona mpenzi wake akiwa kimya kitandani, moyo wake ukanyong’onyea, huzuni ikaanza kuugubika moyo wake, akashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumbubujika.

    “Amka mpenzi, amka unitazame,” alisema Laurence huku machozi yakiendelea kumbubujika.

    Evadia alikuwa kimya kitandani, kwa kumwangalia, lisingekuwa jambo jepesi kuamini kwamba mtu huyo bado alikuwa hai, kuna kipindi Laurence alionekana kuwa na hofu hivyo kusikiliza mapigo yake ya moyo ili kuona kama yalikuwa yakiendelea kudunda au yalisimama, aliyasikia yakidunda.

    Wakati wakiendelea kumwangalia msichana huyo kitandani pale, mlango ukafunguliwa na daktari mmoja, mwanamke aliyevalia koti refu jeupe kuingia ndani ya chumba kile.

    “Bado hajafumbua macho dokta,” alisema Laurence huku mashavu yake yakiwa yamelowanishwa na machozi.

    “Naomba nizungumze nanyi, mnaweza kunifuata,” alisema daktari yule.

    Hakukuwa na mtu aliyebisha, walichokifanya ni kusimama mahali pale na kisha kumfuata daktari yule ambaye safari yake iliishia ndani ya chumba kimoja, ilikuwa ni ofisi yake.

    Wakaingia ndani na kukaribishwa katika viti vilivyokuwa humo ndani. Walipokaa, daktari yule akachukua miwani yake iliyokuwa mezani na kuivaa, akachukua mafaili yaliyokuwa mezani mwake na kuyaangalia vilivyo.

    “Kuna nini?” aliuliza Laurence huku akionekana kuwa na hofu tele.

    “Mgonjwa wenu anatakiwa kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi,” alijibu daktari yule.

    “Tatizo nini?”

    “Anasumbuliwa na figo, haiwezi kufanya kazi kama inavyotakiwa,” alijibu daktari yule.

    “Sawa!Hakuna tatizo.”

    Laurence hakutaka kusikiliza sana daktari alisemaje, aliufahamu ugonjwa huo, watu wengi walikuwa wakifa kwa kukosa figo moja tu iliyokuwa na nguvu, aliuogopa ugonjwa huo, alikuwa tayari kuona lolote likitokea lakini si kumuona mpenzi wake huyo akifariki dunia.

    Siku iliyofuata, Evadia akarudiwa na fahamu, hawakutaka kuzungumza naye, waliambiwa kutokufanya hivyo, wakamchukua na kuelekea katika hospitali ya Taifa. Walipofika huko, msichana huyo akapewa kitanda na madaktari kuanza kazi yao.

    “Unajisikiaje?” aliuliza Laurence huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.

    “Naendelea vizuri. Nashukuru kwa kuwa nami hatua kwa hatua,” alisema Evadia huku akijitahidi kutoa tabasamu pana.

    “Mbona haukuniambia kwamba unaumwa?”

    “Niliogopa kufanya hivyo.”

    “Kwa nini?”

    “Basi tu. Kwa jinsi ulivyokuwa ukinipenda, nilihisi kamba ungehuzunika zaidi,” alisema Evadia.

    “Hata kama mpenzi, ulitakiwa kuniambia.”

    “Naomba unisamehe.”

    “Usijali.”

    Walikaa na kuzungumza mengi, mama yake alikuwa pembeni yake, kila wakati alionekana kuwa mtu mwenye furaha mno, hakuamini kama binti yake kidogo angeendelea vizuri kama ilivyokuwa.

    Mara baada ya kukaa naye kwa dakika thelathini, mlango ukafunguliwa na daktari wa kiume kuingia, alikuwa mzee mwenye ndevu nyingi, alipoingia tu, akawataka kutoka nao nje.

    “Kuna nini?”

    “Njooni mara moja.”

    Akawachukua na kuelekea nao ofisini mwake. Tayari wawili hao walionekana kuwa na hofu, uso wa daktari yule ulionekana kuwa na jambo kubwa lililokuwa likitokea ambalo kwa namna moja au nyingine hakutaka kulizungumza mbele ya mgonjwa wodini mule.

    “Kuna nini?” aliuliza Laurence huku akionekana kuwa na hofu.

    “Figo moja ya mgonjwa wenu haifanyi kazi kama inavyotakiwa, ni lazima tufanye kidney transplant,” alisema daktari.

    “Ndiyo nini hiyo?” aliuliza mama yake Evadia.

    “Tumuwekee figo moja kwani kati ya mbili alizokuwa nazo, moja imeharibika na haifanyi kazi kama inavyotakiwa,” alijibu daktari huyo aliyeitwa Haji Mukhandi.

    “Hiyo figo nyingine tutaitoa wapi?” aliuliza mama yake Evadia.

    “Hilo ni swali gumu kwa sasa, figo haipatikani bure, ni lazima kitolewe kiasi cha fedha ili kumhamasisha mtu kutoa figo yake kwa ajili ya mgonjwa,” alijibu Dk. Mukhandi.

    “Kiasi gani?”

    “Si chini ya milioni ishirini.”

    “Unasemaje?” aliuliza mama yake Evadia huku akionekana kushtuka.

    “Ndiyo hivyo.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mama Evadia akachanganyikiwa, hakuamini kile alichoambiwa kwamba zilihitajika zaidi ya milioni ishirini ili binti yake aweze kuwekewa figo nyingine ili arudi katika hali yake ya kawaida.

    Moyoni mwake alifikiria ni kwa namna gani angeweza kupata kiasi hicho cha fedha kwani kilikuwa kikubwa sana ambacho kamwe asingeweza kukipata. Alihisi moyo wake ukimuuma sana, hakuwa na fedha, hakuwa na kitu chochote kile, kwa maana hiyo kitendo cha binti yake kuwa na figo moja inayofanya kazi kilionekana kuwa kitu cha hatari sana na ndiyo maana mara kwa mara alikuwa mtu wa kuzimiazimia tu.

    Mbele yake aliona giza, hakujua pa kuanzia, kitu pekee alichokifikiria ni kurudi mitaani na kuomba michango kutoka kwa watu wengine, ndugu, jamaa na marafiki, lakini hata kama angewachangangisha watu wengi, kiasi kilichohitajika kilikuwa kikubwa mno.

    “Kwa hiyo tufanyeje?” aliuliza Laurence huku akionekana kuwa mwenye majonzi.

    “Nitakwenda mitaani kuomba michango,” alijibu mwanamke huyo huku akijaribu kuyafuta machozi yaliyokuwa yakimbubujika mashavuni mwake.



    Japokuwa mama Evadia alijitahidi kwa nguvu zote kuzunguka huku na kule kwa ajili ya kutafuta mchango ili binti yake abadilishwe figo lakini kiasi alichokipata hakikuweza kufika kama kilivyotakiwa.

    Mbele yake aliona giza kubwa, hakujua ni kipi alichotakiwa kufanya kipindi hicho. Miaka ya nyuma alimpoteza mume wake, leo hii, binti yake pekee aliyebaki katika maisha yake alikuwa akiumwa mno na hali yake ilikuwa mbaya sana.

    Alishinda akilia, kila alipokwenda hospitalini, alikaa pembeni ya binti yake na kuanza kulia kama kawaida yake. Laurence hakuacha kufika hospitalini hapo, kila siku alifika, alishinda na Evadia, walizungumza mengi huku akimpa moyo kwamba angepona na kurudi katika hali ya kawaida kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

    Maneno hayo yalimtia nguvu Evadia, hakutegemea kupata mwanaume ambaye angejitolea kama alivyojitolea Laurence. Alifahamu fika kwamba mpenzi wake huyo alikuwa masikini wa kutupwa lakini hiyo haikuwa sababu ya kutaka kutokuwa naye, huyohuyo masikini ndiye ambaye leo hii alikuwa naye katika kila hatua aliyopitia hospitalini pale.

    Wakati wote watatu wakiendelea kuwa ndani ya chumba kile, ghafla mlango ukafunguliwa na Dk. Mukhandi kuingia ndani, uso wake ulikuwa tofauti na jinsi alivyokuwa kipindi cha nyuma, alionyesha tabasamu pana. Kila mtu aliyemwangalia daktari huyo akajua kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.

    “Kuna habari njema,” alisema daktari huyo, wote wakasimama na kumwangalia.

    “Habari gani?” aliuliza Laurence huku akijifanya kushtuka.

    “Kuna mtu amejitokeza na kutoa milioni thelathini kwa ajili ya Evadia,” alisema daktari huyo, kila mmoja akashtuka.

    “Milioni thelathini?”

    “Ndiyo!”

    “Nani?” aliuliza Laurence huku macho yake yakiwa na mshtuko mno.

    “Anaitwa Matilda John, mwanamke mmoja, alisema anafanya kazi Umoja wa Mataifa, alizipata taarifa za Evadia hivyo ameamua kumsaidia,” alijibu daktari.

    “Mwanamke? Mhh! Alijuaje kama Evadia anaumwa na anahitaji kiasi hicho cha fedha?” aliuliza Laurence.

    “Hata mimi sijui, imekuwa ni miujiza mno ambayo haikuwahi kutokea,” alijibu daktari huyo.

    Kila mmoja alibaki na maswali moyoni mwake, hakukuwa na mtu aliyefahamu hilo zaidi ya Laurence ambaye kiasi kile cha fedha alikitoa yeye kupitia kwa mfanyakazi wake aitwaye Matilda ambaye alifika hospitalini hapo na kujifanya msamaria mwema.

    Hakutaka kitu chochote kile kijulikane, na hata daktari alipokuwa akiwaambia kuhusu jambo hilo, hata yeye mwenyewe alijifanya kuwa na mshangao na aliuliza maswali mengi kama kuwapa upofu watu hao wasijue kitu chochote kile.

    Kwa kuwa kiasi hicho cha fedha kilitolewa, kilichofuata ni kuwekwa kwa matangazo katika baadhi ya magazeti ambapo wakaandika kwamba mtu yeyote aliyekuwa tayari kutoa msaada wa figo alitakiwa kufika hospitalini hapo.

    Wiki iliyofuata, zaidi ya watu mia moja wakawa wamefika hospitalini hapo tayari kwa kupimwa ili kuangalia vinasaba kama vinaendana na vinasaba vya Evadia.

    “Ila nitahitaji milioni ishirini,” alisema jamaa mmoja kwa kutoa figo yangu.

    “Hakuna tatizo, njoo ndani,” alisema Dk. Mukhandi.

    Waliwapima watu wote ili kuona kama vinasaba hivyo viliendana, kitu kilichomuumiza kila mtu, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa tayari kutoa figo yake ambaye vinasaba vyake vilifanana na vinasaba vya Evadia.

    “Mungu wangu!” alisema Dk. Mukhandi.

    “Kuna nini?”

    “Hakuna mtu ambaye vinasaba vyake vinaendana na Evadia.”

    “Unasemaje?”

    “Ndiyo hivyo!”

    “Watu wote hao hakuna?”

    “Hakuna.”

    Kila mmoja alichanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani kilichotakiwa kufanyika mahali hapo. Mama Evadia na Laurence wakaitwa ndani ya ofisi ya daktari na kuambiwa kile kilichokuwa kimetokea, kila mmoja alisikitika mno.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Imeshindikana?” aliuliza Laurence.

    “Ndiyo! Hakuna hata mmoja!” alijibu daktari yule. Kilio kikaanza kusikika kutoka kwa mama yake Evadia.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog