IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
UMASIKINI ulikuwa chanzo cha mimi kugundua mapema kabisa tofauti kubwa iliyokuwepo kati ya baba na mama yangu. Nililala na mama na baba yangu chumba kimoja hadi nilipoanza darasa la kwanza. Hapo ndipo uhalisia ukauzidi nguvu ule ukimya wa kuzuga kuwa kila kitu kipo sawa na hapo tukalazimika kuhamia nyumba ambayo ilikuwa na chumba na sebule.
Usiku baada ya kupata chakula natoa meza na kutandika godoro langu na kulala.
Awali lilikuwa jambo la kawaida lakini hadi nafikia namaliza darasa la sana akili ilikuwa imefunguka na kinagaubaga nilitambua kuwa haikuwa jambo la afya hata kidogo kulala pale sebuleni huku chumba kile kilichokuwa wazi sehemu ya juu kikiyaruhusu masikio yangu kusikia kila kilichokuwa kikiendelea chumbani kwa wazazi wangu.
Nilizaliwa peke yangu kwa wazazi wale wawili lakini sikuwa peke yangu kwa baba yangu wala kwa mama yangu.
Mama alikuwa na mtoto wa nje na baba alikuwa na watoto wawili wanje.
Niliwahi kuwaona mara moja tu japokuwa sikutambulishwa moja kwa moja kuwa wale ni ndugu zangu. Hivyo nilijiongeza tu, lakini ukiniuliza mpaka sasa jibu langu ni kwamba nimezaliwa peke yangu.
Na hata yote yaliyotokea yalinitokea peke yangu.
Huwa inafika kipindi nasema laiti kama ningelijua ningelilazimisha nitambuylishwe kwa ndugu zangu.
Lakini neno ninge lilichelewa kuja na ni kawaida yake kuchelewa!!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliendelea kuishi sebuleni huku kila siku akili yangu ikinasa jambo ambalo lilikuwa likinichukiza sana.
Baba yangu mzazi alikuwa hana sauti kabisa mbele ya mama yangu, na mbaya zaidi kuna kipindi alikuwa akipigwa nami nilikuwa nikisikia kila kutu.
Hakika nilifedheheka sana lakini sikuwa na lolote la kufanya. Nilikuwa mtoto, maisha yakaendelea.
Nilifanikiwa kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza lakini alikuwa mama yangu aliyuekataa nisiende shule eti kuna shamba ni heri nilime kwanza ili ipatikane pesa ya kutosha na mwaka unaofuata nitaenda shule.
Ilikuwa kama mama alivyosema baba hakuwa na neno la kubadilisha kilichozungumzwa.
Hivyo sikuendelea na shule na haikuwa kwa mwaka mmoja ilikuwa moja kwa moja hadi ujana wangu.
Sawa nilijua mama yangu alikuwa akimnyanyasa baba yangu lakini sikujua inakuwaje mwanaume mzima kunyanyaswa na mwanamke. Nilijitazama mimi kwa jinsi nilivyokuwa imara sana shuleni dhidi ya wanafunzi wenzangu sikuwa nikionewa na aliyethubutu kunionea nilimkabili na kumfunza adabu.
Sasa kama mimi niliweza kufanya yale inakuwa vipi niwe nilizaliwa na baba mnyonge kama yule??
Hii iligoma kabisa kuniingia akilini na laiti kama baba asingefanana nami kwa sura basi ningeweza kuamini kuwa huenda si baba yangu wa kunizaa.
Mawazo yale yalibaki kama yalivyo na hatimaye nikajikubali kuwa sitasoma nikaendelea kulima huku nikilala sebuileni na kuendelea kuzisikia fujo za baba na mama kila siku.
Walikuwa wakipigana na kutukanana.
Sikujua nini chanzo!!
Nilibaki kuwa msikilizaji tu!!
Miaka ikakatika hadi siku ile ambayo utata ulikuja!!
Nilikuwa na umri wa miaka kumi na saba tu wakati huo lakini usingeweza kukubali kwa macho. Nilikuwa nina mwili uliokomaa na pia nilikuwa na umbile refu.
Hii ni kutokana na kufanya kazi ngumu za kujiingizia kipato kwa sababu kwa kipindi hico mama alinambia kuwa nimekuwa mkubwa tayari hivyo ninachotakiwa kufanya ni kuelewa kuwa nipo katika umri sahihi wa kujitafutia na mimi kula yangu.
Nilijiuliza sana inawezekana vipi mama wa kunizaa afikie hatua ya kunitamkia maneno yale, sasa najitafutia vipi ilhali hata elimu sina na yeye ndiye aliyetoa kauli ili nisiendelee na masomo.
Maisha yakaendelea!!
____
Mapenzi bila pesa kufanikiwa kumpata unayemuhitaji huwa ni kazi ngumu sana tena isokuwa na ujira zaidi ya matusi kutoka kwa mlengwa.
Mimi pia ni mwanadamu licha ya ugumu wa maisha pale nyumbani bado hisia za mapenzi zilikuwa palepale.
Niliangukia kwa mtoto wa mwenyekiti wa mtaa wetu ambaye enzi hizo nilisoma naye shule ya msingi lakini mwenzangu aliendelea hadi akafanikiwa kumaliza kidato cha nne na hatimaye kuingia chuo cha mambo ya hoteli sasa alikuwa kijijini tena.
Hakika hatukuwa tukifanana kuanzia namna ya kuzungumza hadi kutembea na kusalimia na watu. Mwenzetu kila kitu alifanya katika namna anayoijua yeye.
Sikuyajali haya yote nikasema kuwa ni huyu ninayehitaji kumuoa.
Na hapo nikawa nimejipa adhabu nyingine mpya kabisa, karaha za nyumbani na hofu ya kumtamkia Rahma kuwa nilikuwa nikihitaji kuanzisha naye mahusiano.
Ili kuiridhisha nafsi yangu nikawa najitahidi mara kwa mara kwenda katika duka la mwenyekiti wa mtaa ambapo Rahma alikuwa akiuza kwa muda wakati huo akisubiri kupangiwa mahali pa kufanya kazi.
Nilikuwa naridhika sana kusalimia na Rahma na kupiga soga hapa na pale japokuwa hakuwa hakionyesha ushirikiano sana, hivyoihivyo mimi nilikuwa naridhika.
Na ikafikia hatua sura na sauti ya Rahma ikawa tiba ya maradhi yangu. Maradhi ya kukerwa na vurugu za wazazi wangu.
Sikujua itafika siku ya kuzungumza na Rahma kwa kirefu lakini ile siku ilifika bila mimi kujua kama ni siku sahihi ama la!
Niliamini katika kile nilichoamini.
Sikujua kuwa haikuwa siku sahihi lakini kwa wakati ule sikujua!!
____CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni siku ya ijumaa, hapakuwa na utaratibu maalumu kwa baba yangu kwenda msikitini. Kwa kifupi hakuwa akijali sana juu ya jambo hili, na hivyo kuniambukiza mimi, hata mimi sikuwa naijali sana dini.
Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo!!!
Lakini ijumaa hii ilikuwa ya tofauti sana. Baba yangu alishindia msikitini na alishiriki swala zote kuanzia alfajiri.
Na siku hii alishinda akiwa amevaa kanzi tu.
Nilimsikia mama yangu akicheka sana kila baba alipokuwa akirejea kutoka katika swala moja.
Alipocheka baba yeye alikuwa mkimya tu bila kusema neno lolote.
Jioni mida ya saa kumi na moja jioni nikiwa dukani kwa mwenyekiti nikipiga soga na Rahma nilimuona baba yangu akizungumza na mtu ambaye alikuwa anauza visu.
Hatimaye nikamuona akinunua kisu. Badala ya kukibeba kikawaida tu hakufanya vile alitazama kushoto na kulia kisha upesi akaifunua kanzu na kukificha kisu kile.
Hapo tayari alikuwa amefanya malipo.
Akaondoka na kwenda zake, bahati nzuri hakuniona!!
Sikujali sana kuhusu tukio lile alilofanya baba, nilikuwa najali zaidi kuyatazama macho ya Rahma kuliko tukio alilokuwa akifanya baba yangu.
Sikujua na sikujali ni kitu gani kitaendelea.
Baada ya kuishiwa na kuongea nilitoweka na kuingia katika kibanda cha mama lishe akanihudumia nilichotaka na saa mbili usiku nilikuwa nyumbani.
Kama kawaida kulala sebuleni, nikaanza kupangua meza na beseni la kuwekea vyombo.
Alaa! Sikukiona kisu kipya alichokuwa amenunua baba na mbaya zaidi sikujua kama alikuwa ndani ama la!!
Nilitamani kuuliza kwa mara ya kwanza lakini nafsi ilisita sana.
Nilishangazwa na ukimya ule katika chumba cha wazazi wangu, hawakuwa wanalumbana wala kujibizana lolote lile kama ilivyokuwa kawaida yao. Hili lilinishangaza sana.
Nilijaribu kulala lakini usingizi haukunipitia hadi majira ya saa tano usiku ndipo nilipopatwa na usingizi nikalala.
Hata hapa sikulala sana majira ya saa tisa usiku nilikuwa nikitazamana na dari lililotoboka likinidhihaki.
Nilijigeuza huku na kule lakini bado sikuweza kusinzia.
Akili yangu ilizunguka na hatimaye nikajikuta natabasamu nilipogundua kuwa nilikuwa nakosa usingizi kwa sababu baba na mama hawakuwa wakilumbana.
Mazoea yana tabu jama!!
Hatimaye asubuhi ikafika na mwanga ukatawala, nikatoa godoro langu ambalo huwa naliweka chumbani na baba akitaka kulala analitoa nami nalikuta sebuleni.
Sasa ilikuwa asubuhi na nilihitaji kulipeleka godogo chumbani.
Nikabisha hodi lakini chumba kilikuwa kimya.
Nikajaribu tena sikujibiwa, nikaamua kusukuma mlango kama mama atanitukana anitukane tu.
La haula!! Nilichokutana nacho ilikuwa ni filamu ya kutisha sana miguu iliishiwa nguvu sikuweza kupiga hatua mbele wala kurudi nyuma.
Kijasho kikaanza kunitoka.
NILIBAKI nikiwa wima huku nitetemeka vibaya sana, macho yangu yalikuwa yakitazama na mwili wa mama yangu akiwa anaogelea katika dimbwi kubwa la damu.
Koo langu lilikauka nikashindwa kusema neno lolote lile, nikaanza kurudi nyuma nyuma hatimaye yale mauzauza yakaenda mbali na macho yangu, na hapo nikaona ile haikuwa sehemu stahiki ya kuendelea kukaa.
Nikatoka nje huku tumbo likiwa linaniuma sana, kila mtu niliyemuona na akathubutu kunisemesha basi bila hiari yangu nilijikuta sijibu kitu chochote kile.
Nilizunguka huku na kule huku taswira ikirejea siku iliyopita nilipokuwa dukani. Nilimuona baba yangu akinunua kisu na nilipofika nyumbani sikukikuta kisu kile.
Ina maana baba alikuwa amepanga kumuua mama kikatili namna ile. Nilijiuliza lakini hakuwepo wa kunipatia jibu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akili zangu zilikuwa zimepevuka haswa na nilitambua moja kwa moja kuwa nipo matatani ikiwa tu baba yangu hataonekana. Na mle ndani kuna mwili wa mama yangu ambaye haikuhitajika ushahidi wa daktari kuthibitisha kuwa alikuwa amekufa kwa sababu utumbo wote ulikuwa nje na jinsi damu zilivyogandamana pale chini, bila shaka aliuwawa masaa mengi yaliyopita.
Kuna uwezekano kabisa ule ukimya niliokuwa nimeusikia usiku uliopita na kuhisi kuwa baba na mama yangu kwa mara ya kwanza walikuwa katikaamani na maelewano basi nilikuwa najidanganya. Mama yangu alikuwa amekufa zamani sana na nililala na mwili wa mama yangu mle ndani.
Kufikiria kuwa nililala usiku mzima na maiti mle ndani damu yangu ikasisimka.
Ngoja nikueleze jambo hapa, kiukweli wanasema upendo wa mama hauna cha kufananisha lakini nakiri kwa kinywa changu nikiwa na akili timamu kuwa mama yangu yule huenda hakuwa mama wa kunizaa kwa sababu sikuwahi kuuona upendo wake waziwazi. Hivyo hata tukio hili la mauaji haya lilinisisimua sio kwa sababu aliyekufa alikuwa mama yangu la, bali nilisisimka kwa sababu nilikuwa nimelala na maiti huku nikiamini kuwa nilikuwa nimelala na na wazazi wangu waliokuwa hai.
Majira ya saa nne asubuhi nilipita jirani na nyumba yetu, hapakuwa na hekaheka zozote, bila shaka utambuzi ulikuwa bado.
Nikaona ni jambo jema ikiwa nitajisalimisha tu kwa balozi wa nyumba kumikumi nimueleze kila kitu jinsi nilivyokiona. Hii ingeniweka mimi katika upande salama.
Nilipofika nyumbani kwa balozi nikiwa bado nimetawaliwa na hofu kubwa nilimkuta mtoto wake, akanieleza kuwa baba yake alikuwa amempeleka mama yake hospitalini lakini alikuwa amekaribia kurudi.
Nilitamani kumsubiri lakini nikaona si vibaya nikizunguka hapa na pale na kisha nitarejea.
Ni hapa ndipo nilipoanzia kutawaliwa na kauli za ninge…. Ninge… ninge…
Ningejua ningemsubiri hadi atakapofika.
Lakini bahati ilikuwa mbaya kwa upande sikuweza kumsubiri.
Wakati nazurura hapa na pale nikaingia katika mgahawa, nikaagiza chai na kitumbua kwa kutumia senti kadhaa nilizokuwanazo mfukoni.
Nilikunywa taratibu ili muda uende mbele zaidi na nikirejea nyumbani kwa balozi nikute amerejea nimueleza lililokuwa linanikabili.
Baada ya kumaliza kunywa chai, nilitoka nje kuwaachia nafasi wateja wengine waweze kuketi, na ni hapa nilipomuona msichana aliyekuwa akiutesa moyo wangu.
Nilimuona Rahma kwa mbali, moyo ukapiga kwa nguvu na nikaanza kukimbia hadi nilipomfikia dada yule.
Kama nilivyosema hapo awali kuwa mwenzangu alikuwa amesoma kunipita hivyo alikuwa anazo chembechembe za dharau.
Licha ya kumwambia kuwa nilimkimbilia kwa muda mrefu hadi kumfikia hakujali sana badala yake alinisalimia kikawaida na kuniangalia kikawaida tu.
Jambo hili liliniumiza sana,.
Wakati mwingine ukikosa la kuongea ni heri usiongee kabisa neno lolote lile.
Nilipomaliza kusalimiana na Rahma nilijikuta nakosa la kuongea lakini nikiwa natamani kuendelea kuwa karibu na Rahma.
Ni hapa nikamweleza kuwa kuna jambo zito sana linanikabili.
‘’Rahma..kukukimbilia kote huku mwenzako nina jambo nahitaji kukueleza, na ninakueleza kwa sababu we ni msichana ama ni mtu wangu wa karibu sana ambaye nakuamini kuwa unaweza kunishauri vizuri sana. Na ninatamani kuwa mtu wako wa karibu zaidi lakini mwenzangu naona haunitazami kwa jicho ninalokutazama mimi….’’ Nilianza kuzungumza huku kiuwazi kabisa nikitambua kuwa nilikuwa namuhofia sana binti yule.
Bila shaka ni kutokana nna jinsi alivyojiweka katika daraja la aliyeelimika.
‘’Ongea nakusikiliza Kassim’’ alizungumza kwa sauti iliyojaa maringo huku akinitazama kwa lile jicho lake lililokuwa likinitesa kila siku.
Ni hapo nikajikuta namwaga mchele mahali nilipohisi kuna kuku mmoja kumbe nilikuwa nakosea sana.
Nikamueleza Rahma juu ya tukio lililotokea nyumbani kwetu, simulizi ile ikamfanya Rahma anisogeze kando tukaketi kabisa ili kuzungumza kwa kina.
Kitendo cha kuketi na kusikilizana vyema na Rahma kilinifanya nijisikie fahari sana na hapo nikaona nimekaribia kabisa kumnasa msichana yule.
Nilijieleza kila kitu katika namna ambayo nahisi hata balozi mwenyewe nisingeweza kumweleza kwa mapana kiasi kile.
Rahma alinipa pole huku akiniuliza mara mbilimbili ikiwa nilikuwa ninao uhakika na nilichokuwa nakisema.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sijui nilishikwa akili kiasi gani na yule binti maana kama ile haitoshi nilijikuta nikivuka mipaka na kumweleza kuwa mimi ninahisi kuwa yule hakuwa mama yangu mzazi, mama yangu yupo mahali fulani na ipo siku tutaonana. Nikamweleza Rahma kuwa sikuwa nimeumizwa kabisa na kifo cha mama yule ambaye alikuwa akimnyanyasa baba yangu kila siku. Wakati mwingine hadi kumpiga alikuwa anampiga…
Hawezi kuwa mama yangu yule…. Nilikataa.
Sikukumbuka kuwa maneno yanayomtoka mtu yana hatari zaidi kwa sababu neno likitoka halirudi na kila mmoja ataliweka katika tafsiri anayoijua yeye mwenyewe. Mimi niliongea tu ilimradi kumfurahisha Rahma na kumfanya awe mtu wangu wa karibu zaidi…..
Baada ya pale tukaachana na Rahma baada ya kuwa ameniruhusu nimsindikize kidogo.
Sikumbuki kama kuna kitu chochote alinishauri kuhusiana na tukio lile baya kabisa na la kutisha.
Alipoondoka niliamua kwamba niende shambani kulima pamoja na rafiki zangu kisha baadaye ndipo nitaenda kwa balozi wa nyumba kumi kumueleza kilichotokea.
Hilo lilikuwa kosa kubwa sana, kwani kile kitendo tu cha kwenda shambani huku nyuma mambo yalikuwa mambo.
Rafiki yangu mmoja alifika mbio mbio pale shambani huku akihema juu juu, kwa pamoja tukasita kuendelea na zoezi la kulima.
Alishusha pumzi zake mara kadhaa huku akionyesha mkono kuelekea huko alipotoka.
‘’Kassim, kassim kuna tatizo nyumbani kwenu, nyumba imezungukwa na maaskari… unaitwa huko na maaskari.’’ Alinieleza yule kijana huku akionekana kuwa amepagawa sana.
Kitendo cha kusikia kuwa ninaitwa na maaskari nikaingiwa na ubaridi mkali katika mwili wangu. Niliogopa sana kwa sababu kamwe nilikuwa sijawahi kupelekwa kituo cha polisi…..
Nikajikuta nafanya jambo la kipuuzi sana, nikakimbia bila kujua ni wapi ninapoelekea.
Laini ningelijua nisingelikimbia..
Huu ukabaki kuwa msemo tu lakini nilikuwa nimekimbia tayari…….
Kukimbia huko nikawa nimejiingiza katika majanga yanayosababisha leo hii unasikiliza simulizi hii….
NILIKIMBIA sana bila kuchoka na bila kujua ni nini hatma yangu, nilichoamini kuwa kukimbia itakuwa tiba kwangu. Niliendelea kwenda mbele lakini nilipofika mbali zaidi nikakumbuka kuwa kukimbia tatizo sio namna ya kulitatua natakiwa nifanye namna nyingine ya kulikabili tatizo.
Lakini tayari nilionyesha kulikimbia tatizo bila shaka kitendo changu cha kukimbia kitakuwa kimeniweka matatani na nikijirudisha mikononi mwa polisi wataondoka na mimi kama mtuhumiwa wa mauaji yale.
Mapigo yangu ya moyo yalienda mbio sana nikijiuliza ni kitu gani hiki kinanitokea katika maisha yangu haya ya kimasikini tena nikiwa na umri mdogo tu japo sio umri wa kuitwa mtoto bali kijana.
Niliendelea kuwa vichakani hadi majira ya jioni, na kigiza kikaanza kuingia kikiambatana na ubaridi. Ni hapa ndipo nikatambua wazi kuwa sipo eneo salama hata kidogo, lakini ni kitu gani ambacho ningeweza kufanya ili niwe salama.
Sikuwa na lolote ambalo ningeweza kufanya zaidi ya kujirudisha katika mikono ya watu wale waliokuwa wakinitafuta.
Jambo hili sikuliafiki hata kidogo katika kichwa changu, na ni hali hii ya kuendelea kukosa maamuzi iliyozidi kulifanya jambo lile kuwa zito zaidi.
Majira ya saa moja usiku kwa mujibu wa saa yangu nilijitoa katika vile vichaka, jambo la kushukuru ni kwamba ule ulikuwa msimu wa maembe hivyo nilikula maembe yaliyotapaa katika miti iliyosongamana katika vile vichaka.
Wakati naanza kutoka kichakani nilisikia mchakacho kama wa watu kutembea hivi.
Nikajificha tena kichakani ili kama kuna mtu aweze kupita kwanza ndipo na mimi niendelee kutembea, hakika nilikuwa nikimuhofia kila mtu ambaye ningeweza kukutana naye kwa wakati ule.
Picha ya mwili wa marehemu mama yangu ilikuwa ikinitawala katika taswira yangu. Lakini kwa sasa nilihisi kama nilikuwa nimeshuhudia tukio la kutisha sana na nikawa namsimulia yule binti mtoto wa mwenyekiti kana kwamba lilikuwa tukio la kawaida tu.
Na mimi likaanza kunitisha nilivyokuwa nalifikiria….
Baada ya muda kidogo ule mchakacho ukazidi kusogea eneo nilipokuwa, nilitaka kukurupuka nitoke mbio lakini nilisita miguu ilikuwa imeishiwa nguvu kabisa na nilihisi kuwa siwezi kupiga hatua nyingi kabla sijakamatwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Naam, nikaendelea kutulia, kundi la watu watano lilifika na kuweka kituo katika upande wa pili wa kichaka ambacho nilikuwa nimejificha. Kwa upenyo mdogo uliokuwepo katika kichaka kile nilijikuta nikiona kila kilichokuwa kikiendelea, mtu mmojak kati ya watu wale watano alikuwa amefunikwa macho yake kwa kitambaa cheusi. Baada ya kufikishwa eneo lile alifunuliwa kitambaa na hapo nikaweza kumuona vyema kabisa.
Alikuwa ni mtu ambaye haikuwa mara ya kwanza kumuona, kwa wakati ule pale sikuweza kumtambua jina lake, lakini niliifahamu sura ile.
Alipofunguliwa kitambaa nilimuona akitaka kuzungumza lakini akaambulia ngumi kali sana mdomoni akabaki kuvuja damu, alikuwa amechoka sana na alikuwa akihema juu juu sana.
‘’Ukithubutu kuongea lolote tutakuua vibaya kuliko tulivyopanga kukuua…’’ bwana mmoja alimkaripia kisha nikaiona na yeye sura yake kidogo.
Hapo hofu ikaniingia na nilibaki kulishuhudia tukio lile huku mwili wangu wote ukiingiwa na ubaridi mkali sana.
Nilikuwa mwenye hofu ambaye nilitambua kuwa nikifanya kosa lolote lile la kutikisika basi nitakuwa nimejiingiza katika utata mwingine mpya tena huu usingekuwa na msalia mtume iwe isiwe tu ningeuwawa.
Kuogopa kule kujitikisa kukanifanya niendelee kutazama kila kilichokuwa kinaendelea, yule bwana niliyekuwa naitambua sura yake alikabwa shingo yake kwqa nguvu sana kisha akaachiwa na kuanza kukohoa huku akitapika hovyo na kutema damu.
‘’Zipo wapi..’’ aliulizwa.
‘’Zipo wapi nakuuliza…’’ jamaa alisistiza huku akiwa amemmulika na tochi usoni.
Nilikuwa natetemeka sana, nilijiuliza itakuwaje ile tochi ikigeuziwa upande niliokuwa mimi, mkojo niliusikia ukichuruzika, hata kuuzuia sikuweza.
Niliendelea kutulia nikingoja litakalotokea, sikujua hata ni kitu gani walichokua wakimlazimisha awaambie kilipo.
Baada ya zoezi la kwanza kugonga mwamba huku yule bwana akizidi kusisitiza kuwa hajui lolote lile, bwana mmoja alitoa msumeno. Akausogeza katika shingo ya yule bwana aliyekuwa amechoka huku akivuja damu.
‘’Msiniueee…’’ alilalamika kwa sauti iliyokuwa ikikwaruza kwaruza.
‘’Nakuuliza kwa mara ya mwisho zipo wapi.. usipojibu naichinja shingo yako hadi unakufa.. nadhani nisiseme sana ngoja nikuonjeshe…’’ alisema yule bwana kisha akauchukua mkono wa yule bwana na kuupitishia ule msumemo mara mbili akipeleka mbele kisha nyuma.,
Yule bwana alipiga kelele kubwa sana, mimi mkojo ukazidi kunichuruzika. Nilikuwa sina nguvu kabisa, yaani baada ya kushuhudia tukio baya kabisa la kuuona mwili wa mama yangu ukiwa umepoteza uhai kwa kuchomwa visu sasa nashuhudia hatua kwa hatua jinsi mtu anavyoteswa kwa nia ya kumuondolea uhai wake.
‘’Kimyaa…’’ akakaripiwa huku damu ikimchuruzika kama bomba vile alitulia tuli, machozi yakimtoka, udenda na mabonge ya damu mdomoni.
Alisikitisha kumtazama, ni kama nilikuwa nimeketi katika banda la kuonyesha filamu nikitazama mojawapo ya filamu ambayo mwisho wa siku wale wote waliokufa katika vipande vya filamu hiyo wataendelea kuwa na uzima wao.
Lakini hii haikuwa filamu, walikuwa wanaume wanaozungumza Kiswahili kabisa wakimfanyia kitu kibaya kabisa mwenzao ambaye alikuwa akiongea Kiswahili pia.
‘’Zipo wapi… ukinijibu nitafikiria kukuacha hai.. usipojibu sitakuwa na namna tena nitakuchinja nakwambia Guda….’’ Yule bwana alimuita kwa jina ambalo sikuwahi kulisikia, ni kweli nilikuwa sijui jina lake lakini niliwahi kulisikia na halikuwa hilo.
‘’Zipo nyumbani kwa Bonge, zipo chumbani kwake katika sanduku….’’ Alijibu huku akitetemeka sana, bila shaka alikuwa na hofu kuu juu ya kifo ambacho kilikuwa sentimeta chache sana kutoka pale alipokuwa.
Baada ya jibu lile wale wanaume waliosalia walizungumza kichini chini kisha wakawa kama wanataka kumuacha bwana yule, lakini ghafla wakamvamia. Mmoja akamkanyaga shingo ikawa chini halafu mmoja ambaye alikuwa anamdhibiti kuanzia mwanzo alimkaribia.
‘’sali sala zako za mwisho mzee… hakuna kutoka salama katika mdomo wa mamba….’’ Alizungumza na hapo akainama kama anayetaka kuchinja kuku, yule bwana akatokwa na mayowe makubwa sana ya hofu na mimi sikuweza kuvumia zaidi nikatokwa na mayowe makubwa sana huku nikikurupuka kutoka katika kichaka kile.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
‘’kamata huyu upesi asiondoke hai…’’ niliisikia amri ikitoka kwa nyuma yangu huku mimi nikitimua mbio huku nikiyumba yumba na kuanguka mara kwa mara.
Nilikimbia huku nikisikia vishindo vikinifuata kwa nyuma huku wakitoa maonyo makali kuwa iwapo sitasimama watafyatua risasi.
Akili haikutaka kubadili maamuzi ilinisihi niendelee kutimua mbio kwa nguvu zote.
Nikatimua mbio zaidi huku nikianza kuchoka na wale watu wabaya wakinikaribia….
Uzuri ni kwamba uenyeji wa eneo ulikuwa umenibeba sana. Ni kweli nilikuwa si mtu wa kwenda sana eneo lile mara kwa mara lakini niliijua njia ile na mimi nilikuwa mweneyji kupita wao.
Pailipokuwa na mabonde wao hawakujua niliwasikia tu wakianguka chini huku wakitukana matusi mazito.
Hatimayew tukaufikia mto, mto ambao tangu utoto wangu ulikuwa mto tuliokuwa tunaenda kuoga na kuogelea. Nilitabasamu kidogo huku pia nikifanya dua kuu mmoja kati yao asiwe na ujuzi katika suala la kuogelea.
Naam, ilikuwa kama nilivyotaraji, nilipojitupa kwenye maji wao walibaki kutoa vitisho tut u kuwa watanipiga risasi. Sikuwajali nikazidi kukata maji huku nikikumbuka vitisho kuwa mida ya usiku katika mto ule huwa kuna mamba wanafanya kuingia na kisha alfajiri sana wanaondoka.
Sikuwa na njia mbadala zaidi ya kuendelea kuifuata tahadhali hii dhahania kuliko kuwasikiliza watu wale ambao nimewashuhudia wakimuua mtu nimjuaye.
Hatimaye nilifika ng’ambo ya pili. Palikuwa kimya sana, nilisikia kwa mbali sana mbwa wakibweka. Nikatambua kuwa kwa namna yoyote ile kuwa jirani na mahli nilipokuwa basi kuna miji ya watu.
Nikataka kuiita hali ile kuwa ni nafuu lakini nikakumbuka kuwa siku hiyo palikuwa pametokea tukio fulani la kutisha nyumbani halafu mimi nikakimbia.
Kukimbia kule kukanifikisha katika majanga mengine, nikajishauri na hatimaye nikaona ni heri kukabiliana na wanakijiji wanaweza kunionea imani lakini sio watu wale ambao wameshirikiana kumtesa na kisha kumuua yule bwana ambaye alikuwa amewaeleza kilipokuwa kile walichokihitaji.
Nikaendelea kukimbia hadi nilipoyafikia makazi ya kwanza, nikabisha hodi na kufunguliwa mlango na mwanaume makini aliyeshika panga mkononi mwake na tochi mkononi.
Akaniuliza mimi ni nani, nikajieleza kwa ufupi. Akaniuliza ni kitu gani natafuta usiku huo, nikamueleza kuwa nilikuwa nahitaji hifadhi hadi asubuhi kutokana na matatizo ambayo yamejitokeza huko nilipotoka.
Akanikaribisha bwana yule akanielekeza kuwa nitalala pale sebuleni kwa sababu huko chumbani alikuwa pamoja na mchumba wake aliyekuwa amekuja kumtembelea. Uzuri wa maisha ya kijijini sio sawa na mjini, kijijini hakuna mashaka makubwa kama ilivyo mjini, halafu ujamaa bado unapatikana huko!!
Nilimshukuru sana, nikajilaza pale sebuleni nikapitiwa na usingizi. Huku mazingira yale nikiyaona kama yaliyokuwa nyumbani kwetu nilikuwa nalala sebuleni baba na mama wakiwa chumbani.
Alfajiri sana niliondoka nikimuaga yule bwana, hakunijibu bila shaka alikuwa bado usingizini. Nikaufungua mlango na kuonddoka.
Nikawa napita njia nisiyokuwa na uelewa nayo vizuri.
Mara kwa mbali nikawaona wanawake wakiwa na ndoo zao, ilikuwa kawaida katika kijiji chetu shida ya maji.
Niliendelea kutembea hadi nilipopishana nao huku nikiwapa salamu.
Sikugeuka nyuma kujua kama kuna lolote walikuwa wakijadiliana kuhusu mimi, lakini ghafla walianza kunipigia mayowe makali sana wakisema kuwa mimi ni muuaji. Mayowe yao yakasafiri mbali sana na kuwafikia wanaume waliodamkia mashambani asubuhi ile wakatoka walipokuwa na kuungana na wanawake wale.
Kelele zikawa kubwa sana nikakosa sehemu sahihi ya kwenda maana kila kona nilisikia kelele za kutishiwa maisha, wengine wakiwa na mapanga na mashoka, wengine makwanja na majembe.
Nikapiga magoti chini ndugu msikilizaji na kisha kuinyanyua mikono yangu juu. Huku neno ninge likipita katika kichwa changu.
‘’laiti ningelijua ningeliondoka usiku kabisa kabla watu hawajaamka’’ nilijisemea huku nikisubiri kuona ni kitu gani kitajiriCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wanaume wanne walifika mbele yangu wakiwa pamoja na akina mama.
‘’huyu amemuua mama yake, na kisha amekimbia…’’ mwanamke mmoja aliwaelezea wale wanaume huku akionekana kumaanisha moja kwa moja kile alichokuwa akikisema.
‘’Jamani mimi….’’ Nilitaka kuzungumza lakini ghafla ubapa wa panga ukatua katika mgongo wangu. Nilihisi nimechanika mgongo kutokana nay ale maumivu, sikujua kuwa ule ulikuwa ubapa tu.
‘’kaa kimya kabisa….’’ Alinikoromea yule bwana ambaye alinipiga na ule ubapa wa panga. Nikatulia tuli yule mwaname akaendelea kuzungumza.
‘’walikuja mapolisi kumkamata akakimbia, wakasema tukimuona popote tupige kelele akamatwe…’’ akamaliza kujieleza.
Maneno yake yakawatia hasira wale mabwana na mmoja kati yao akanivamia na kunipiga kibao kikali sana usoni. Nikaisikia harufu ya damu, baadaye ikaanza kunivuja mdomoni na puani.
Niliogopa kusema neno lolote lile kwa sababu nilikuwa nimechimbwa mkwara wa nguvu sana.
Nikiwa bado navuja damu mwanaume mmoja alifika pale akiwa ameshika kamba, akafika na kunirukia teke kali kana kwamba nilikuwa katika majaribio ya kupambana naye.
Niliangukia kisogo, akanigeuza nikawa nimelalia tumbo akaichukua mikono yangu na kuifunga kwa nguvu sana huku akinitusi kila lolote alilojisikia kutukana.
Uso wangu ulikuwa umegandamizwa vibaya sana katika ile ardhi yenye matope kiasi kwamba nikawa siwezi kupumua vizuri.
Baada ya kunikaza barabara na zile kamba huku zikinichana chana vibaya, alinigeuza.
Jicho lake jekundu sana likanitazama.
‘’unaitwa nani wewe muuaji…’’ aliniuliza kwa ghadhabu.
‘’mimi sio muuaji…’’ nilimjibu nikiwa katika maumivu.
Bila kusema neno lolote alinipiga teke kali katika mbavu zangu kisha akanieleza.
‘’nimekuuliza jina lako kijana…’’
Nilitaja jina langu, akawatazama wenzake na kisha kuniuliza ni kitu gani kinafuata baada ya kumfunga kamba zile.
‘’tumpeleke serikali za mitaa ama kwa mwenyekiti wa mtaa….’’ Alijibu kijana mmoja. Kisha wakajadili kwa alfajiri ile kuwa ni heri kwa mwenyekiti wa mtaa kwani serikali za mitaa ofisi bado hazijafunguliwa.
Wakaninyanyua na kunilazimisha nitembee, huku wakinizunguka kila kona.
Nilitembea huku nikijiuliza ni aibu kiasi gani naenda kukutana nayo ninapoenda kukutana na Rahma ambaye ni mtoto wa mwenyekiti wa mtaa.
Lakini kwa akili nyingine nikahisi kuwa ile si aibu bali ukombozi pekee maana ni yeye pekee rahma ambaye nilikuwa nimemsimulia kila kitu kilivyotokea hadi mama yangu kukutwa akiwa amekufa na baba yangu kukimbia.
Nilitembezwa hovyohovyo, huku nikihangaika sana kupiga hatua vizuri kwa sababu nilikuwa nimefungwa mikono yangu yote miwili kwa nyuma. Nilianguka hawakujali walinichukulia kama mtu hatari sana ambaye yale yote waliyoona napitia ilikuwa stahili yangu kabisa na sikupaswa kuonewa huruma hata kidogo.
Hatimaye tukafika nyumbani kwa mwenyekiti, kwa jinsi nilivyokuwa nasindikizwa na makelele mengi tulimkuta mwenyekiti akiwa nje tayari anatusubiri.
Katika kundi lile nikamuona na rahma akiwa peku peku, usoni mwake alionesha tabasamu..
Nilishangaa sana.
Wakati mimi nawaza kuwa nipo pamoja naye na atanitetea nikashangaa kuona anatabasamu….
Kichwani nikajiuliza kuwa ikiwa ni huyu rahma pekee ninayemtegemea kuniokoa katika hili, halafu sasa anatabasamu ni nani ambaye ataweza kunitetea.
Nikapata jibu kuwa hakuna mtu mwingine wa kunitetea zaidi ya kujitetea mimi mwenywe.
Na hapo nikajikuta nipo katika kufanya maamuzi na lolote litakalokuwa liwe tu.
Nikakusudia kukimbia…..
Nilihesabu hatua kadhaa kabla ya kuamua kufanya nilichotaka kufanya.
Lakini ile nafikia hatua ya tatu.. mara gari la polisi likaingia kwa fujo kali sana pale tulipokuwa.
Nguvu zikaniisha miguuni…
Nikaanguka na kujikuta nimepiga magoti tu nikilia….
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
JIFUNZE.
MAISHA yana mitihani mikubwa sana, jifunze kupitia mitihani wanayopitia wenzako ili siku ukikabiliana na mtihani wowote ule ujue ni jinsi gani kuwa mvumilivu wakati unakabiliana na mtihani huo.
MAISHA NI SHULE….. JIFUNZE.
0 comments:
Post a Comment