Simulizi : Dead Love ( Penzi Lililokufa )
Sehemu Ya Pili (2)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vipi mpenzi wangu umeshafika nyumbani? Wazazi wako wamekufungulia geti?” sauti nzito ya kiume ilisikika, Abdallah akajikuta akitetemeka kwa hasira kupita kiasi kisha akakata simu.
“Huyu si anajifanya mjanja, sasa ngoja nimuoneshe kwamba mimi ni mjanja zaidi yake,” alisema huku akiingiza namba za siri ambazo aliziona siku moja iliyopita wakati msichana huyo akiziingiza kwenye simu yake.
Simu ilipofunguka tu, kwa kuwa Abdallah alikuwa akifanya kazi kwenye Kampuni ya Planet Link Communication iliyokuwa ikishughulika na teknolojia za kisasa za mawasiliano, alienda moja kwa moja kwenye sehemu ya ‘setting’.
Akaingiza namba fulani ambazo alikuwa akizijua mwenyewe kisha akachukua simu yake na kurekebisha kitu ambacho kitaalamu huitwa GPS (Global Positioning System), mfumo ambao ukiingizwa kwenye simu na kuwekwa namba maalum, ulikuwa na uwezo wa kuonesha mahali mtu mwenye simu hiyo alipo.
Mfumo huo ulikuwa ukitumiwa na kampuni yao kusajili simu au vifaa kama laptop za wateja wao ili kurahisisha upatikanaji wake pindi vinapoibiwa. Baada ya kuhakikisha kila kitu kipo sawa, alijaribu kufungua simu yake kwenye upande wa GPS, akaiona vizuri simu ya Karen kwamba ilikuwa humohumo ndani.
“Lazima nitajua nyendo zake zote,” alisema huku akiinuka na kwenda kufungua mlango, akamkuta Karen amekaa kwenye sofa huku akiwa amejiinamia, akionesha kuwa na mawazo mengi.
“Simu yako inaita, huyo mjomba wako uliyekuwa kwake amepiga,” alisema Abdallah na kumpa msichana huyo, harakaharaka akaifungua na kuangalia namba ya mtu aliyepiga, akazidi kushtuka baada ya kugundua kuwa kumbe simu ilikuwa imepokelewa, akajua lazima Abdallah ameshajua kila kitu.
Hakutaka kumsemesha chochote, akarudi chumbani na kufunga mlango. Hakutoka tena mpaka kulipopambazuka ambapo alipotoka, msimamo wake ulikuwa ni uleule, akamuamsha Karen na kumtaka aondoke.
Kwa jinsi alivyokuwa na jazba, msichana huyo alishindwa kukataa kwani licha ya kumbembeleza sana amsamehe, alikataa, ikabidi achukue kila kilicho chake na kuondoka.
“Lakini nimetokea kumpenda huyu kaka, hata sijui nini kimetokea. Sina kawaida ya kumpenda mwanaume lakini kwa Ibra imekuwa tofauti mpaka najishangaa,” alisema Karen wakati akikatiza mtaani, begani akiwa amebeba begi lake lililokuwa na nguo zake.
Alitembea mpaka kwenye kituo cha Bajaj ambapo madereva walipomuona, kila mmoja alikuwa akimchangamkia, wengine wakimtongoza na wengine kumtania kwani kimuonekano, Karen alikuwa amejaliwa kiasi cha kumfanya mwanaume yeyote aliyekamilika, asiishie kumtazama mara moja.
Hakujali kelele zao, alichagua Bajaj aliyokuwa anaitaka na kumuelekeza dereva sehemu ya kumpeleka.
***
Muda mfupi baada ya Karen kuondoka, Ibra aliamka kitandani na kwenda bafuni kujimwagia maji. Akarudi ndani na kunywa dawa zake kisha akaenda sebuleni, akawasha runinga na kukaa huku mawazo mengi yakiendelea kupita ndani ya kichwa chake.
Japokuwa aliamua kusimamia msimamo wake wa kumtimua msichana huyo baada ya kumuambukiza ugonjwa wa zinaa na vituko vingine alivyomfanyia, hisia zake zilikuwa zikizungumza lugha tofauti kabisa na akili yake.
Japokuwa alishawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasichana kadhaa kabla ya kukutana na Karen, ndani ya nafsi yake alikiri kwamba hakuwahi kukutana na msichana mrembo kama alivyokuwa Karen ingawa pia alikiri kwamba hajawahi kuwa kwenye uhusiano na mwanamke mwenye tabia mbovu kama yeye.
“Anawezaje kunidanganya kwamba anaenda kwa mjomba wake kumbe anaenda kwa mwanaume? Kwa nini anidanganye wakati mwenzake nilikuwa nampenda na nilishakuwa na malengo makubwa juu yake?” Abdallah aliendelea kuwaza huku hisia chungu zikipita ndani ya kichwa chake.
Kwa kuwa alikuwa amewahi sana kuamka kabla ya muda wa kwenda kazini haujafika, aliendelea kukaa sebuleni kwake huku akimuwaza Karen na mambo yote yaliyotokea ndani ya kipindi kifupi tu tangu alipokutana naye. Alishindwa kuelewa Karen ni msichana wa namna gani.
Mara alipata wazo jipya, akainuka na kwenda chumbani kwake ambapo alichukua simu yake na kurudi sebuleni, akakaa kwenye sofa na kufungua sehemu ya GPS (Global Positioning System), akaingiza namba fulani kisha ramani kubwa ya Jiji la Dar es Salaam na mitaa yake ikafunguka huku katikati yake kukiwa na alama nyekundu iliyokuwa inaonesha mahali Karen alipo.
“Atakuwa anaenda wapi?” alisema Abdallah huku akiikazia macho simu yake, kwa ilivyoonesha, Karen alikuwa kwenye chombo cha usafiri kwani alama nyekundu ilikuwa ikihama haraka kuonesha upande aliokuwa akielekea.
“Leo nitajua nyendo zake zote,” alisema Abdallah huku akiwa hajali hatari ambayo itampata endapo bosi wake atagundua kuwa anatumia teknolojia ya kazini kwao kinyume na matumizi sahihi aliyofundishwa.
Baada ya takribani dakika ishirini, Abdallah alisimama huku akiwa bado ameshika simu yake.
“Manzese? Kuna ndugu yake Manzese? Mbona hajawahi kuniambia? Mi nilijua anakwenda Kinondoni kwa mjomba wake?” alisema baada ya simu yake kumuonesha kuwa mwisho wa safari ya Karen ilikuwa ni Manzese Darajani ambapo kwa jinsi ilivyoonesha, alishuka kwenye chombo cha usafiri alichokuwa anakitumia.
Alienda kujiandaa na muda mfupi baadaye, alitoka kuelekea kazini huku muda wote akiwa makini kuangalia simu yake kuona kama kuna mabadiliko yoyote ya sehemu Karen alipokuwa. Mpaka anafika kazini, simu yake ilikuwa ikimuonesha kuwa Karen alikuwa Manzese.
Siku hiyo hata ufanyaji kazi wa Abdallah ulikuwa ni wa kusuasua sana, muda mwingi alikuwa akiutumia kucheza na simu yake, akawa anaangalia mahali msichana huyo alipo ambapo mpaka jioni inafika, bado simu yake ilionesha kuwa alikuwa Manzese.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilipofika muda wa kutoka kazini, Abdallah alitoka na kurudi mpaka nyumbani kwake ambapo alioga harakaharaka, akanywa dawa zake na kurudi sebuleni, akawa anaendelea kuiangalia simu yake.
Ghafla alianza kuona mabadiliko juu ya mahali alipokuwa msichana huyo. GPS ilimuonesha kuwa ameanza kuondoka mahali alipokuwa, akiwa kwenye chombo cha usafiri ambacho hakujua kama ni bodaboda, Bajaj au daladala lakini alichojua ni kwamba alikuwa barabarani.
“Anaelekea wapi?” alijiuliza Abdallah huku akisimama pale alipokuwa amekaa. Akaendelea kuiangalia simu yake ambapo Karen alionekana kuhama kutoka kwenye Barabara ya Morogoro na kukata kona kuingia Barabara ya Shekilango.
“Au anarudi kwangu? Inawezekana ameyajua makosa yake anakuja kuniomba msamaha,” alisema Abdallah huku akiachia tabasamu hafifu.
Japokuwa msichana huyo alikuwa amemfanyia mambo ya ajabu sana, ikiwa ni pamoja na kumuachia gonjwa la zinaa, ndani ya moyo wake alikuwa bado anampendana alijiapiza kuwa atakaporudi na kumuomba msamaha, atakuwa tayari kumpokea.
“Hata hivyo, safari ya msichana huyo iliishia eneo la Sinza Afrikasana na hakuondoka eneo hilo mpaka ilipofika majira ya saa tatu usiku, Abdallah alipochukua jukumu la kutoka na kwenda mpaka eneo hilo kwenda kuangalia alikuwa amefuata nini. Nguvu ya penzi ilimsukuma kufanya mambo ambayo kwa mtu mwingine yangeonekana kuwa ya ajabu.
Alikodi bodaboda na kumuelekeza dereva kumpeleka eneo hilo huku muda mwingi akiwa bize na simu yake, kuangalia eneo alilokuwepo. Kwa jinsi alivyokuwa amevaa, hata kama Karen angemuona, asingeweza kumtambua Abdallah haraka. Dakika kadhaa baadaye, Abdallah tayari alikuwa amefika Sinza Afrikasana, akamlipa dereva wa bodaboda fedha zake na kushuka.
Hata hivyo, kwa kuwa ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kufika eneo hilo nyakati za usiku, alibaki amepigwa na butwaa kutokana na alichokuwa anakiona mbele yake.
Wanawake wengi waliovaa nusu utupu, walikuwa wakipitapita eneo hilo, huku wengine wakionekana kukimbilia magari yaliyokuwa yakisimama pembeni kama wanaogombea kitu. Ilibidi avuke barabara na kusogea upande ule waliokuwepo wanawake hao, ambapo kulikuwa na pilikapilika nyingi utafikiri mchana. Simu yake ilimuonesha kuwa Karen hakuwa mbali na pale alipokuwepo.
Alipovuka barabara tu, alishtukia akizingirwa na wasichana karibu sita, wote wakiwa wamevaa kihasara kiasi cha viungo vyao muhimu kuonekana waziwazi.
“Vipi besti, umenicheki vizuri ninavyolipa? Njoo basi tuongee vizuri baby,” alisema msichana mmoja huku akimshika Abdallah mkono na kuanza kumvutia pembeni. Kabla hata hajapiga hatua moja, mwingine alimshika mkono mwingine na kuanza kumvutia upande wa pili huku naye akimchombeza kwa maneno ya hapa na pale.
Mwingine alimpitia kwa nyuma na kumkumbatia mgongoni, akawa anamvutia kwake, wakawa wanamgombea kama fisi wanaogombea mfupa. Bado Abdallah hakuwa anaelewa kilichokuwa kinaendelea, akabaki amepigwa na butwa utafikiri mjusi aliyebanwa na mlango.
Wakati wakiendelea kumgombea kama mpira wa kona, gari moja la kifahari liliwasili eneo hilo na kusimama mita chache kutoka pale Abdallah alipokuwa, wale wasichana wote wakamuachia Abdallah na kukimbilia kwenye gari hilo, wakawa wanagongana vikumbo kwenye vioo.
“Ebwana vipi, nini kinaendelea hapa?” ilibidi Abdallah amuulize dereva mmoja wa Bajaj aliyekuwa amepaki pembeni kidogo ya barabara.
Akamuitikia huku akicheka, ilivyoonesha alishuhudia kila kitu kilichokuwa kinatokea eneo hilo.
“Hivi hawa wasichana wanajishughulisha na nini usiku wote huu? Isitoshe mbona wote wamevaa kiajabuajabu halafu walikuwa wananivutavuta hapa kama wananifahamu,” alisema Abdallah, badala ya kujibu, yule dereva wa Bajaj akaangua kicheko kwa nguvu kisha akatulia na kumtazama Abdallah ambaye bado alionesha kuwa na shauku kubwa ya kujua kilichokuwa kinaendelea kwenye eneo hilo.
“Hawa ni wajasiriamwili broo.”
“Wajasiriamwili? Ndiyo watu gani?”
“Wauza sukari guru,” alisema dereva huyo wa Bajaj na kuzidi kumchanganya Abdallah, akamuomba amfafanulie, akamueleza kwamba walikuwa ni machangudoa waliokuwa wakifanya biashara haramu ya kuuza miili yao.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“He! Mbona sasa wanafanya ukahaba hadharani namna hii?” alisema Abdallah huku akionekana kushangaa mno, aliendelea kupigwa na butaa, akashuhudia wasichana wawili wakipanda kwenye lile gari kisha likaondoka kwa kasi, wale wengine waliosalia wakaanza kurudi taratibu upande ule Abdalah aliokuwa amesimama, akiendelea kushangaa.
Safari hii hakutaka wamsogelee tena, akawahi kuepusha mbawa zake kwa kujichanganya ndani ya umati mkubwa wa watu waliokuwa wamefurika eneo hilo, wengi wakionesha kulewa. Japokuwa ilikuwa ni usiku, lakini eneo hilo lilikuwa limechangamka mno utafikiri mchana.
Abdallah akatoa simu yake mfukoni ambayo awali aliificha baada ya kuona anazongwa na wale machangudoa, akatazama tena kwenye ramani ya GPS ambapo alama nyekundu ilimuonesha kwamba Karen aliyekuwa akimtafuta, alikuwa upande uleule aliokuwa akielekea.
“Sasa Karen kafuata nini kwenye eneo kama hili?” alijiuliza Abdallah huku akizidi kutembea kuelekea upande ule simu yake ilikomuonesha kwamba Karen alikuwepo. Hatimaye akajikuta ameingia kwenye baa moja iliyokuwa inapiga muziki kwa sauti kubwa, watu wengi wakicheza na kunywa pombe.
Simu yake ilimuonesha kwamba Karen alikuwa ndani ya eneo hilo, akaanza kuangaza macho huku na kule huku mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio kuliko kawaida. Aliendelea kujipenyeza kuelekea ndani ya baa hiyo, huku akishangazwa na jinsi wasichana waliokuwa wakifanya biashara ya uchangudoa walivyokuwa wengi eneo hilo.
Wakati akiendelea kuangaza macho huku na kule, ghafla macho yake yalitua kwa msichana aliyekuwa amezungukwa na wanaume kadhaa, akicheza muziki kwa kukata viuno utafikiri kiuno chake hakina mfupa.
Wanaume wakawa wanamshangilia na kupiga makofi kwa nguvu, naye akawa anazidisha vituko, akaendelea kucheza huku akiwa amempa mgongo Abdallah ambaye aliendelea kupigwa na butwaa kwani hakudhani kwamba kuna wanawake hawana aibu kiasi hicho.
Alipogeuka na kutazama upande ule aliokuwepo Abdallah, kijana huyo alishtuka mno kiasi cha kutaka kudondoka chini kwani miguu yake ilimuisha nguvu ghafla. Msichana aliyekuwa akicheza kwa mbwembwe kiasi kile, akiwa hana hata tone la aibu, hakuwa mwingine bali Karen.
“Mungu wangu,” alisema Abdallah huku akiegamia ukuta palepale alipokuwa amesimama kwani vinginevyo angeweza kudondoka chini. Akafikicha macho yake akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona mbele ya macho yake lakini ukweli haukuweza kubadilika.
Akiwa bado hajui afanye nini, alimuona mwanaume mmoja mwenye mwili mkubwa wa mazoezi, akisimama na kumsogelea Karen, akamkumbatia na kumnong’oneza maneno fulani sikioni kisha akamshika mkono na kuanza kumvuta.
Karen hakuwa mbishi, akawa anamfuata mwanaume huyo aliyeonekana kuwa hodari wa kunyanyua vitu vizito kwa jinsi mwili wake ulivyokuwa umejengeka kimazoezi. Abdallah aliyekuwa akishuhudia kila kilichokuwa kikitokea, alihisi kama mwili wake umekufa ganzi na kupoteza mawasiliano kati ya viungo vya juu na vya chini.
Wazo alilolipata haraka ndani ya kichwa chake, ilikuwa ni kuwafuatilia ili aone walikokuwa wanaelekea. Naye akajipenyeza kwenye umati wa watu huku akitetemeka kuliko kawaida, mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio na kusababisha kijasho chembamba kiwe kinamtoka japokuwa ilikuwa ni usiku.
Safari yake iliishia kwenye gesti bubu iliyokuwa jirani na eneo hilo ambapo alimshuhudia yule mwanaume akiingia na Karen huku akiwa amemkumbatia na kumshika kiuno. Ilibidi atafute sehemu ya kukaa, akajibwaga kwenye fensi ya maua iliyokuwa jirani na gesti hiyo, mwili ukiwa umeisha nguvu kabisa.
Dakika kadhaa baadaye, Karen alitoka lakini tofauti na wakati akiingia, alikuwa akikimbia huku mkononi akiwa ameshika mfuko ambao Abdallah hakujua ndani yake una nini. Akatimua mbio kurudi kule alikotoka na kabla ya kufika, alichepuka pembeni na kuingia kwenye kibanda cha mlinzi mmoja wa eneo hilo kisha mlango ukafungwa.
Abdallah akawa anamfuatilia kwa nyuma huku akiwa makini kuhakikisha hamuoni. Dakika chache baadaye, alitoka akiwa amebadilika utafikiri siyo yeye. Alibadilisha nguo alizokuwa amezivaa na kichwani alivaa wigi lililomfanya awe na mwonekano tofauti kabisa.
Akatembea harakaharaka na muda mfupi baadaye, alikuwa tayari amefika kwenye ile baa, akajichanga na wasichana wengine na kuagiza pombe kali, akakaa kwenye kona moja huku akinywa na wenzake.
Muda mfupi baadaye, yule mwanaume aliyeondoka naye awali, aliwasili kwenye baa hiyo huku akiwa amevaa bukta na singlendi, akaanza kupita huku na kule kama anayemtafuta mtu huku akihema kwa hasira.
Yule mwanaume aliendelea kuzunguka huku na kule kama faru aliyejeruhiwa, akimsaka kwa udi na uvumba Karen lakini kwa kuwa tayari msichana huyo alikuwa amejibadilisha kwa kila kitu, kuanzia mavazi mpaka kichwani alikokuwa amevaa wigi lililomfanya awe na mwonekano tofauti kabisa na ule aliokuwa awali, haikuwa rahisi kumtambua.
Baada ya kuona amemkosa mbaya wake, mwanaume huyo aliyekuwa na mwili mkubwa wa mazoezi, alianza kuwafanyia fujo machangudoa hao, kila aliyekutana naye, alimsukuma na kuangukia kwenye meza zenye vinywaji vya watu wengine au alimkunja na kumnasa vibao, jambo lililosababisha vurugu kubwa.
Muda mfupi baadaye, mwanaume huyo alidhibitiwa ipasavyo na mabaunsa na walinzi waliokuwa eneo hilo, akatolewa nje msobemsobe huku akilalamika kwa uchungu kwamba ameibiwa vitu vyake, zikiwemo pesa nyingi zilizokuwa kwenye waleti aliyoiweka kwenye suruali yake lakini hakuna aliyemjali.
Dakika kadhaa baadaye, hali ya utulivu ilirejea ndani ya eneo hilo. Abdallah bado alikuwa makini kufuatilia kila kilichokuwa kikiendelea, muda wote macho yake yakiwa upande ule aliojificha Karen ambaye safari hii alikuwa akicheka na kugongesheana mikono na wenzake, huku sigara zikiwa hazikauki mdomoni mwake.
“Kwa nini msichana mzuri kama huyu anafanya uchangudoa? Amekosa nini kwenye maisha yake mpaka kufanya kazi ya hatari kiasi hiki? Halafu kwa nini anawaibia wanaume? Hayahofii maisha yake?” Abdallah alizidi kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Muda mfupi baadaye, wanaume wawili waliingia eneo hilo na kuanza kuangazaangaza macho huku na kule. Wanawake wengi waliokuwa eneo hilo, wakifanya biashara haramu ya kuuza miili yao, waliwachangamkia, kila mmoja akawa anatangaza biashara. Wanaume hao waliendelea kuchagua, mmoja macho yake yakatua kwa Karen ambaye alikuwa akivuta sigara na kupuliza moshi mwingi juu, akamsogelea na kumnong’oneza maneno fulani ambayo Abdallah hakuweza kuyasikia kutokana na umbali uliokuwepo kati yao.
Msichana huyo akainuka, kinguo cha nusu uchi alichokuwa amevaa sasa kilionekana vizuri, akashikana mikono na yule mwanaume na kuanza kutoka nje ya baa hiyo iliyofurika watu wengi. Yule mwenzake aliyeingia naye, naye alimpata anayemtaka na wote wakaongozana na kutoka nje ya baa hiyo.
Abdallah hakutaka kulaza damu, naye alitoka na kuanza kuwafuatilia kwa nyuma, hakujua ni jambo gani lililomfanya awe na shauku ya kumfuatilia msichana huyo lakini alijikuta tu akiumia mno ndani ya nafsi yake, akatoka harakaharaka ambapo aliwaona Karen na yule mwanaume wakitokomea gizani.
Akatembea hatua za harakaharaka kuwafuata kule walikokuwa wanaelekea lakini tofauti na mara ya kwanza, safari hii hawakwenda kwenye gesti zilizokuwa vichochoroni bali safari yao iliishia kwenye kile kibanda cha mlinzi ambacho muda mfupi uliopita, msichana huyo aliingia na kuficha vitu alivyomuibia mwanaume waliyekuwa naye gesti.
Abdallah alisogea na kutafuta sehemu ya kujibanza, mahali ambapo aliweza kuona vizuri kilichokuwa kikiendelea ndani ya kibanda hicho. Alijikuta mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio kuliko kawaida, akahisi moyo wake ukiteketea kwa moto mkali.
Kwa mbali akaanza kuhisi machozi yakimchuruzika na kuulowanisha uso wake, akawa anaijutia nafsi yake kwa jinsi alivyojiingiza kwenye mdomo wa mamba kwa kumpenda msichana huyo bila kumjua kwa undani. Akiwa bado anaendelea kutokwa na machozi ya uchungu, alishtukia mtu akitoka kwenye kibanda hicho huku akipepesuka.
Alipomtazama vizuri, aligundua kuwa ni yule mwanaume aliyeingia na Karen muda mfupi uliopita. Kwa hesabu za harakaharaka, tangu waingie hata dakika mbili hazikuwa zimepita hivyo haikuwa rahisi kwamba tayari wawili hao walishakutana kimwili.
Kingine kilichomshangaza Abdallah, wakati mwanaume huyo akiingia kwenye kibanda hicho na Karen, hakuonekana kama amewelewa kiasi hicho lakini muda mfupi tu baadaye, alionesha kuwa tilalila, akabaki anajiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu huku akiendelea kumtazama mwanaume yule aliyekuwa akiendelea kupepesuka.
Muda mfupi baadaye, yule mwanaume ambaye alishafika umbali wa mita kadhaa kutoka kwenye kibanda kile, alidondoka chini kama mzigo, ‘puuh!’. Alijaribu kuinuka lakini alidondoka tena, akalala chini na kujinyoosha bila kujali kwamba pale palikuwa ni barabarani.
Abdallah alibaki amepigwa na butwaa, akiwa bado haelewi kilichotokea, alimuona Karen akitoka kwenye kile kibanda, akiwa tayari ameshabadilisha nguo na kuwa na mwonekano wa tofauti kabisa.
“Mungu wangu, huyu msichana mbona anaonekana ni mtu hatari sana?” alisema Abdallah huku akitoka pale mafichoni alipokuwa amejificha na kuanza kutembea kwa hatua za taratibu kuelekea pale yule mtu alipokuwa amelala. Tayari watu walishaanza kukusanyika kumuangalia kwani halikuwa tukio la kawaida.
Kwa mbali alimuona Karen akivuka barabara na kuhamia upande wa pili kulikokuwa na baa nyingine tofauti na ile ya awali, akaamua kuachana naye kwanza na kwenda kuangalia nini kilichompata yule mwanaume.
“Jamani kanyweshwa madawa ya kulevya huyu, si mnaona alivyolegea?” alisema mwanaume mmoja, wasamaria wema wakasaidiana kumbeba kutoka pale barabarani akiwa hajitambui na kumpeleka pembeni ambako alianza kupewa huduma ya kwanza.
“Madawa ya kulevya?” Abdallah alijiuliza maswali yaliyokosa majibu, akabaki amepigwa na mshangao mkubwa, akiwa haamini kilichotokea. Harakaharaka alianza kutembea kuelekea kule msichana huyo alikokuwa ameelekea huku akipepesa macho huku na kule.
Hatimaye aliingia kwenye baa aliyomuona Karen akiingia, akaanza kujipenyeza kwenye umati wa watu wengi waliokuwa wakiendelea kunywa pombe na kucheza muziki huku akiangaza macho huku na kule. Ghafla alipogeukia pembeni, macho yake yaligongana na ya Karen ambaye naye alionesha kushtuka mno kumuona Abdallah mahali hapo, wakabaki kutazamana.
”Karen!”
“Wewe! Umefuata nini huku?” alihoji Karen huku akionesha kushtuka kuliko kawaida, hakutegemea kabisa kukutana na Abdallah katika mazingira hayo, mapigo ya moyo wake yakawa yanamuenda mbio kuliko kawaida.
“Nimekufuata wewe Karen.”
“Umenifuata mimi? Nani amekuelekeza kuwa niko huku?”
“Mh! Ni stori ndefu lakini nimekuwepo hapa kwa muda mrefu kidogo, nimeona kila kitu ulichokifanya. Kwa nini ulinidanganya? Tafadhali naomba tusogee pembeni tuzungumze.”
“Bwana eeh! Mi sitaki kuzungumza na wewe chochote, sasa hivi nipo kazini, nakuomba uondoke uniache na mambo yangu,” alisema Karen huku akionekana kubadilika na kuvaa uso ambao Abdallah hakuwahi kuuona.
Siku zote alikuwa akijua kwamba Karen ni msichana mpole, mwenye aibu za kikekike na asiyependa makuu lakini kumbe haikuwa hivyo. Upande wa pili wa maisha ya msichana huyo, alikuwa mtu mwingine tofauti kabisa.
“Karen! Tafadhali naomba ku...”
“Nimeshakwambia achana na mimi, kwanza mimi sikujui,” alisema Karen na kuanza kutembea harakaharaka kuondoka eneo hilo. Abdallah hakutaka kukubali kirahisi, alianza kumfuata nyumanyuma huku hata yeye mwenyewe akiwa haelewi ni kitu gani alichokuwa anakitaka.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alishindwa kukubaliana na ukweli wa alichokutana nacho; Karen, mwanamke mrembo mwenye kila sifa za kuwekwa ndani, kumbe alikuwa changudoa mzoefu? Abdallah hakutaka kabisa kuamini. Japokuwa ni yeye ndiye aliyemtimua msichana huyo nyumbani kwake baada ya kumuambukiza ugonjwa wa zinaa alipokutana naye kimwili bila kinga, bado nafsi yake ilikuwa ikizungumza lugha tofauti kabisa.
Aliamini lazima kuna kitu kilichosababisha msichana huyo akaangukia kwenye dimbwi hatari la biashara ya ukahaba na kujikuta nafsi yake ikimwambia kwamba ni lazima afanye kitu kumuokoa ili aachane na maisha hayo.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Karen kumuelewa, alishamwambia muda huo yupo kazini na hahitaji mazungumzo ya aina yoyote lakini bado Abdallah aliendelea kuwa king’ang’anizi.
“Ukiendelea kunifuatafuata nitakupigia kelele za mwizi wenzako wakuchome moto sasa hivi,” alisema Karen kwa nyodo huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.
“Karen, nakuomba unisikilize mama, wala sina shida ya mapenzi na wewe wala kukuharibia kazi yako, nataka kuzungumza na wewe,” alisema Abdallah lakini bado msichana huyo aliendelea kushikilia msimamo wake.
Alipoona Abdallah anazidi kumghasi, alivuka barabara na kuhamia upande wa pili ambapo alijichanganya na machangudoa wengine na kuendelea na biashara. Abdallah naye hakutaka kukata tamaa, licha ya vitisho alivyokuwa anapewa na msichana huyo, bado aliendelea kumfuatilia.
Karen alipoona anazidi kufuatwafuatwa na Abdallah, alimuita dereva wa Bajaj na kuzungumza naye akimuelekeza sehemu ya kumpeleka. Dereva huyo aligeuza Bajaj na kumvusha Karen, akampeleka mpaka kwenye kile kibanda cha mlinzi ambacho msichana huyo alikuwa akikitumia kama stoo yake.
Akashuka na muda mfupi baadaye, alipanda tena kwenye Bajaj na kuanza kuondoka eneo hilo huku akimhimiza dereva aongeze mwendo. Abdallah alikuwa makini kuangalia kila kitu kilichokuwa kinaendelea huku maswali mengi yakipita ndani ya kichwa chake.
Hakutaka kukubali kirahisi, kwa kuwa alishaamua kuutatufa ukweli, alijiapiza kuwa lazima amfuatilie msichana huyo mpaka mwisho kwani mpaka muda huo tayari alishahisi kwamba amemdanganya mambo mengi sana kuhusu ukweli wa maisha yake.
Harakaharaka alikimbilia mahali madereva wa bodaboda walipokuwa wamepaki, akamfuata mmoja na kumpa maelekezo ya kuifuatilia Bajaj ile aliyopanda Karen haraka iwezekanavyo.
Muda mfupi baadaye, tayari Abdallah alikuwa barabarani, dereva wa bodaboda akafanya kama alivyoelekezwa na dakika chache baadaye, tayari walikuwa wameikaribia Bajaj hiyo iliyokuwa inaelekea upande wa Shekilango.
Abdallah alimwambia dereva wa bodaboda apunguze mwendo kidogo ili Karen asishtukie kama alikuwa akimfuatilia, safari ikaendelea mpaka walipofika Shekilango. Japokuwa muda ulikuwa umeenda sana, ikiwa inakaribia kutimia saa nane za usiku, Abdallah hakuchoka wala hakuwa na usingizi.
Baada ya kufika Shekilango, Bajaj iliyombeba Karen ilikata kushoto na kuingia Barabara ya Morogoro kuelekea upande wa Manzese. Wakaendelea kuwafuatilia mpaka walipofika Manzese ambapo dereva wa Bajaj alipunguza mwendo na kuwasha ‘indiketa’ ya upande wa kushoto, nao wakawafuata.
Safari yao ilienda kuishia eneo maarufu Manzese liitwalo Uwanja wa Fisi. Harakaharaka Abdallah alishuka kwenye bodaboda na kumlipa dereva fedha zake, akajichanganya na watu wengi waliokuwa eneo hilo ambalo nalo lilichangamka mno utafikiri ni mchana.
Macho yake yote aliyaelekeza kwa Karen, akamuona akijipenyeza kwenye umati wa watu akiwa ameshika mfuko aliotoka nao kwenye kibanda cha yule mlinzi kule Sinza- Afrika Sana. Naye alijipenyeza kwa tahadhari kubwa kwani alikuwa anajua jinsi eneo hilo lilivyo hatari hasa nyakati za usiku.
Muda mfupi baadaye, walitokezea kwenye uchochoro mwembamba uliokuwa na watu wengi. Abdallah naye akawa anafuata nyumanyuma. Akashangaa kugundua kuwa kumbe uchochoro huo ulikuwa na vyumba kila upande ambavyo vilionesha kuwa makazi ya watu.
Kilichozidi kumshangaza ni kwamba wanawake walikuwa wengi kuliko wanaume na wote walikuwa wamevaa kihasahasara kama wale aliowaacha Afrika Sana. Kwa mbali akamuona Karen akiingia kwenye moja kati ya vyumba vingi vya hadhi ya chini vilivyokuwa eneo hilo.
Akiwa bado anashangaashangaa, alishtukia watu wote eneo hilo wakianza kutimua mbio hovyo huku wakipiga kelele: “Polisi! Polisi! Polisi, jamani msako unapita.” Alimuona Karen akitoka mbio na kuungana na wenzake waliokuwa wanakimbia, ikabidi na yeye aanze kutimua mbio lakini hakufika mbali, polisi wengine wengi waliotokea upande wa mbele wa uchochoro huo, waliwaamuru watu wote kukaa chini huku wakizikoki bunduki zao, wote wakatii amri.
“Hivi hamjui kwamba kufanya uchangudoa ni kosa kisheria? Na nyie wanaume hamjui kwamba kununua machangudoa ni makosa? Lazima mkaozee ndani,” alisema askari mmoja na kuwaamuru wenzake waanze kuwafunganisha mashati watuhumiwa wote, tayari kwa kupelekwa kwenye difenda zilizokuwa zimepaki kwa mbali kisha kuelekea kituoni.
“Haa! Kumbe hawa wote ni machangudoa na wateja wao? Mungu wangu, na mimi si itaonekana nilikuwa nimekuja kununua machangudoa? Kazini wakijua itakuwaje?” alijiuliza Abdallah huku mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio kuliko kawaida. Tayari alishaanza kuiona jela mbele yake, ikabidi atumie akili za ziada.
“Afande, mimi sikuja kununua machangudoa ila nilikuwa napita tu njia,” alisema Abdallah huku akijaribu kujitetea kwa yule askari aliyeonekana kuwa kiongozi wa wenzake. Kwa kuwa alikuwa anajua kwamba mkono mtupu haulambwi, aliingiza mkono mfukoni na kutoa noti ya shilingi elfu kumi na kumkabidhi askari huyo ambaye aligeuka kushoto na kulia, alipoona hakuna aliyekuwa akimtazama, aliipokea na kuingiza mkono mfukoni.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Haya potea!” alisema askari huyo lakini kabla Abdallah hajaondoka, alimsogelea tena askari huyo. Akaingiza tena mkono mfukoni na kutoa noti nyingine ya shilingi elfu kumi ambayo aliikunja na kumkabidhi askari huyo huku akimnong’oneza kitu askari huyo.
“Aroo! Hebu wewe dada kuja hapa,” alisema askari huyo huku akimuoneshea ishara Karen ambaye tayari alikuwa ameshafunganishwa nguo na mwenzake. Askari mwingine akamfungua kisha akasogea pale askari huyo alipokuwa amesimama.
“Una bahati umepata mdhamini, haya poteeni haraka,” alisema askari huyo, Abdallah na Karen wakaondoka haraka eneo hilo huku askari huyo akihakikisha kwamba hawakamatwi tena. Abdallah na Karen wakatimua mbio na kutokomea uchochoroni.
Kwa hofu ya kukamatwa tena, hakuna aliyesimama mpaka walipotokezea mtaa wa pili ambako kulikuwa na watu wengine wanaoendelea na shughuli zao. Abdallah ndiye aliyekuwa wa kwanza kusimama, Karen aliyekuwa anamfuata nyuma yake, naye alisimama huku akitweta kwa nguvu.
“Karen!”
“Nini, we si nilikukataza usinifuate? Kilichokuleta huku ni nini?”
“Badala ushukuru nimekusaidia unaanza kuleta nyodo.”
“Umenisaidia nini? Hata usingenisaidia ningeenda na kesho ningetoka, haya ndiyo maisha yangu,” alisema msichana huyo huku akibetua midomo kwa dharau, jambo lililommaliza kabisa nguvu Abdallah.
“Wala mimi sijaja kwa shari, nashangaa kwa sababu gani unanichukia kiasi hiki, kwani kosa langu ni nini?” ilibidi Abdallah awe mpole kwani Karen alishaanza kumbadilikia. Akaanza kumtuliza kwa kumwambia maneno mazuri kwamba yeye hakuwa na nia mbaya naye isipokuwa nafsi yake ilikuwa ikimwambia kwamba anatakiwa kumsaidia ili aondokane na maisha hayo.
“Unajua mi nakushangaa sana, usiku wote huu unashinda kulala nyumbani kwako na kutulia una kazi ya kuhangaika mitaani kunifuatilia. Kwa kipi kikubwa? Unanidai?”
“Usiseme hivyo Karen, hebu naomba uheshimu mchango wangu kwako, wewe mwenyewe hushangai kwa sababu gani nakufuatilia kiasi hiki?” alisema Abdallah na kuendelea kumbembeleza msichana huyo akubali kumsikiliza. Baada ya kutumia ushawishi mkubwa, Karen alikubali kumsikiliza Abdallah alichokuwa anataka kumwambia.
“Hapa tulipo siyo sehemu salama, naomba kama hutajali, tuondoke pamoja mpaka nyumbani kwangu tukazungumze kwa kirefu.”
“Kama ni mambo ya mapenzi mimi sitaki tena na wewe! Kwanza nilikudanganya nilipokwambia nakupenda, mimi huwa sipendi, naangalia fedha zaidi,” alisema msichana huyo lakini Abdallah akamtoa wasiwasi kwamba shida yake haikuwa mapenzi tena bali alikuwa anataka wakazungumze mambo mengine tofauti kabisa.
Msichana huyo alikubali kwa shingo upande, wakasimamisha Bajaj na kupanda, Abdallah akamuelekeza dereva kuwapeleka Mikocheni alikokuwa anaishi. Japokuwa palikuwa na umbali mrefu lakini Abdallah hakujali kulipa fedha nyingi za nauli.
Safari ya kuelekea nyumbani kwake ikaanza huku kichwani akiendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu msichana huyo. Baada ya takribani dakika arobaini, walikuwa tayari wamewasili Mikocheni, dereva akaanza kukata mitaa kuelekea nyumbani kwa kijana huyo.
Walipofika, alimlipa dereva huyo fedha zake kisha wakateremka na kuingia ndani, Karen akiwa kimya kabisa. Walienda moja kwa moja mpaka kwenye sebule ya kisasa ya kijana huyo, Abdallah akakaa na kumuonesha ishara msichana huyo kuwa naye akae. Alipotazama saa ya ukutani, tayari ilikuwa imefika saa tisa za usiku.
Abdallah alishusha pumzi ndefu na kumgeukia msichana huyo ambaye macho yake yalikuwa hayatulii.
“Kwanza naomba unisamehe kwa kitendo nilichokifanya cha kukufukuza hapa nyumbani kwangu, nilikasirika sana kwa sababu nilienda kupima afya yangu na kujikuta nikiwa na gonjwa la zinaa.”
“Sawa nimekuelewa na wewe naomba unisamehe kwa kukupa gonjwa la zinaa.”
“Usijali, unajua kabla mimi na wewe hatujawa wapenzi, tulikuwa marafiki kwa kipindi kirefu, tukiwasiliana kwa simu na kuchati Whatsapp, Facebook na Instagram kwa hiyo hata kama mapenzi yetu yamekufa, wewe bado ni rafiki tangu.”
“Kwani unataka kusemaje Abdallah, mbona maneno mengi namna hiyo? Mi nimechoka nataka niondoke zangu nikalale.”
“Ninachotaka kukwambia, mimi ni rafiki yako ambaye nimejitolea kwa moyo wangu wote kukusaidia lakini nataka uniambie ukweli wa maisha yako. Hilo tu,” alisema Abdallah huku akimsogelea msichana huyo na kumtazama usoni. Karen naye aliinua uso wake na kumtazama Abdallah, machozi yakaanza kumtoka kwa wingi, akashusha pumzi ndefu na kujiinamia.
“Hata sijui nianzie wapi.”
“Anzia hapohapo,” alisema Abdallah huku akimtaka msichana huyo kutokuwa na hofu yoyote ndani ya moyo wake. Kwa kuwa alimhakikishia kuwa atakachomwambia kitakuwa siri yake, Karen alikubali kumueleza ukweli wa maisha yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwanza nianze kwa kukuomba radhi, nimekudanganya vitu vingi sana lakini kwa kuwa leo nimeamua kukwambia ukweli, naomba ukubali kunisamehe. Jina langu halisi siyo Karen, mimi naitwa Mwanaisha ila wanaolijua jina hilo ni watu wa nyumbani kwetu tu,” alisema msichana huyo na kusababisha Abdallah akodoe macho mithili ya fundi saa aliyepoteza nati.
Msichana huyo aliendelea kumueleza Abdallah historia ya maisha yake na kilichosababisha mpaka akajikuta akiishia kwenye dimbwi la uchangudoa. Abdallah alikaa kimya muda wote huku akimtazama msichana huyo kwa huruma.
“Nakumbuka vizuri jinsi matatizo yalivyoanza kunitokea na kusababisha ndoto zote nilizokuwa nazo maishani mwangu zipotee na kufutika kabisa. Nilikuwa nasoma kidato cha pili, Shule ya Sekondari Magoma, Korogwe mkoani Tanga ambako ndiyo nyumbani kwetu.
“Kwa bahati mbaya, kuna mwanaume alianza kunirubuni akawa ananiambia kuwa ananipenda sana na yupo tayari hata kunisomesha, akawa anataka tuwe wapenzi. Ikawa kila nikienda kwenye duka lake, ananipa zawadi nyingi na kwa sababu sisi kwetu ni maskini, nikawa nashindwa kuzikataa, mwisho tukajikuta tukiwa wapenzi.
“Kwa bahati mbaya zaidi, nilipata ujauzito na kwa kuwa nilikuwa mdogo, sikuweza kujigundua haraka mpaka walimu waliponishtukia shuleni, nikafukuzwa shule na kurudi nyumbani ambako nako wazazi wangu walichachamaa wakitaka nimtaje aliyenipa ujauzito huo.
“Sikuwa na ujanja, ikabidi nimtaje, kesi ilikuwa kubwa sana kwani kipindi hicho ndiyo sheria ya kumfunga jela miaka thelathini mwanaume yeyote anayekutwa na kosa la kumpa ujauzito mwanafunzi ilikuwa imepitishwa.
“Yule mwanaume ambaye tulikuwa tumepishana sana umri, yeye akiwa ni mtu mzima kabisa wakati mimi nilikuwa msichana mdogo, ilibidi ahonge fedha nyingi sana, wakakubaliana na wazazi wangu kwamba anioe na kunitunza mpaka nitakapojifungua.
“Japokuwa sikuwa tayari kuolewa kutokana na umri wangu mdogo, sikuwa na jinsi zaidi ya kuolewa hivyohivyo. Hata hivyo, mwanaume huyo baada ya kuniweka ndani, alianza kubadilika mno, akawa anakunywa sana pombe na kunipiga bila kujali ujauzito wangu.
Kwa bahati mbaya zaidi, siku moja alinipiga sana ujauzito wangu ukiwa na miezi mitano na kusababisha nianguke na kupoteza fahamu. Nilipokuja kuzinduka, nilijikuta nikiwa hospitalini ambapo nilipowauliza manesi, waliniambia mimba yangu imeharibika,” alisema Karen na alipofikia hapo, alishindwa kuendelea, machozi yakawa yanamtoka kwa wingi.
Ilibidi Abdallah afanye kazi ya ziada ya kumbembeleza, alipotulia, aliendelea kueleza jinsi alivyoteseka hospitalini kutokana na mimba hiyo kuharibika.
“Miezi miwili baadaye, niliruhusiwa kutoka hospitalini lakini sikutaka kurudi tena nyumbani. Palepale wakati nimelazwa, kuna mwanamke mmoja alikuwa akimuuguza ndugu yake, aliniambia kuwa kuna ndugu yake anaishi Dar es Salaam anahitaji msichana wa kumsaidia kazi za ndani.
“Akaniunganisha naye ambapo siku hiyo niliporuhusiwa kutoka hospitalini, nilifanya kuwatoroka wazazi wangu, nikapelekwa na yule mwanamke mpaka stendi ya basi, akanipandisha na kumpa maelekezo kondakta ya kunishusha Ubungo kwani bado nilikuwa mdogo na sikuwahi kufika jijini Dar es Salaam,” alisema Karen na kujiinamia tena, akajifuta machozi na kuendelea kueleza jinsi alivyopokelewa jijini Dar es Salaam.
“Yule bosi wangu aliyenipokea, kwa kweli alikuwa na roho nzuri sana kwani siku za mwanzo hakutaka nifanye kazi yoyote mpaka nilipopona kabisa lakini tatizo lilikuwa kwa mume wake na watoto wake wa kiume.
Karen aliendelea kueleza jinsi baba mwenye nyumba huyo alivyomgeuza mtumwa wa ngono ambapo kila siku alikuwa akimuingilia kimwili bila ridhaa yake, muda ambao watu wote wameondoka nyumbani, mkewe akielekea kazini na wanaye kuelekea shuleni.
“Nilishindwa kumwambia mtu yeyote kwani alikuwa ananitishia kwamba nikimwambia mama ataniua kwa bastola yake, ikabidi nifanye kuwa siri yangu, ikawa kila siku ndiyo mchezo wake.”
Msichana huyo aliendelea kusimua jinsi watoto wa kiume wa bosi wake, nao walivyoanza kumtongoza na kumuomba awe mpenzi wao.
“Nilipokataa, walisubiri siku wazazi wao wamesafiri, wakanibaka wote wawili kwa zamu. Kuanzia siku hiyo nikawa nashindwa tena kuwakatalia kwani walikuwa wakitumia nguvu, nikageuzwa na kuwa mtumwa wa ngono, baba yao anafanya mapenzi na mimi na wao wananibaka mpaka nilipokuja kupata ujauzito wa pili.
“Kutokana na aibu niliyokuwa naihisi ndani ya moyo wangu ya kuwachanganya mtu na wanaye mpaka kupata mimba, ilibidi nitoroke bila kumwambia mtu yeyote. Sikuwa na ndugu yeyote Dar na wala sikuwa na nauli ya kurudia kwetu, ikabidi niingie mitaani ndipo siku moja nilipokutana na mdada mmoja aitwaye Chausiku ambaye nilimueleza matatizo yangu.
Alinionea huruma sana, akanichukua na kunipeleka mpaka nyumbani kwake, Manzese Uwanja wa Fisi ambapo baadaye niligundua kuwa alikuwa akifanya biashara ya ukahaba. Akanisaidia kutoa mimba kisha baada ya hapo, na mimi nikawa sina jinsi zaidi ya kujiunga kwenye biashara hiyo.
Nimeifanya kwa kipindi kirefu mpaka sasa nimeshazoea na sidhani kama nitakuja kuiacha kwani napata fedha za kuendeshea maisha yangu bila kumtegemea mtu,” alisema Karen na kumfanya Abdallah ashushe pumzi ndefu na kuishiwa cha kusema.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Umewahi kwenda kupima afya yako kuangalia kama uko salama au tayari umeshapata Virusi vya Ukimwi?” Abdallah alimuuliza Karen swali ambalo hakulitegemea.
...ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment