Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

NINGE - 4







    Simulizi : Ninge

    Sehemu Ya Nne (4)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikatamani kuombaomba haopa na pale lakini nikalikumbuka lile gazeti ambalo yule bwana alinisomea likitoa taqarifa kuwa nilikuwa nahusika na mauaji na kisha kukimbia nikiambatana na majambazi wenzangu, taarifa zile ziliniwekakatika utata nikihofia kuwa iwapo mtu mmoja atanigundua basi atatoa taarifa polisi kisha nitakamatwa na kukamatwa nikiwa katiika hali niliyokuwanayo sioni ni kwa namna gani ningeweza kujitetea na kueleweka.

    Na kama uwezekano wa kujitetea ulikuwa mdogo basi bila shaka kifungo gerezani kilikuwa haki yangu.

    “Dah kufungwa bila makosa…..” niliumia kuwaza hivi.

    Lakini ningeendelea vipi kuishi eneo lile huku nikiwa na njaa, ni lazima tu yangenikuta mabaya.

    Nikaamua tena kujitosa, nikaenda katika mgahawa nikamuona msichana wa makamo yangu akiwa anaosha vyombo.

    Nikajongea pale nikiwa kama nilivyokuwa bila viatu miguuni.

    “Habari za asubuhi dada yangu…” nilimsalimia huku nikiombea awe anakijua Kiswahili.

    Alinitazama kisjha akanijibu, “nzuri, karibu kaka”

    Akaendelea na shughuli yake ya kuosha vyombo huku na mimi nikijiuliza ni neno gani sahihi la kumueleza msichana yule akanielewa.

    Kila neno niliona si neno sahihi, akasita kuosha vyombo akanitazama, safari hii akanitazama miguu yangu isiyokuwa na viatu.

    “Karibu….” Akaniambia tena….

    “Dada yangu nina njaa kali sana, kama unalo la kunisaidia tafadhali nakusihi…. Nisaidie.” Nilijikuta namueleza hilo lililonijiakatika kinywa changu.

    Alisita kuosha vyombo kisha akanitazama machoni kwa muda kiasi kisha akasimama.

    “Unaitwa nani wewe…” akaniuliza swali lile lililonitisha, nilihisi huenda amegundua kuwa ni mimi yule muuaji ninayetafutwa.

    “Naitwa Kevin..” nilimdanganya ili nijue ni kitu gani alikuwa akihitaji kutoka kwangu zaidi.

    Baada ya kujitambulisha akanitazama tena kwa sekunde kadhaa kisha akaniambia kitu.

    “Huwa sina ukawaidawa kusaidia mtu yeyote yule kwa sababu wengi ni waongo, wavivu wa kufanya kazi na wanaopenda vya dezo.. ila naona kitu kwako Kelvin… ingia ndani .” alinieleza dada yule kisha akaendelea kuosha vyombo nami nikashukuru na kuingia mgahawani.

    Baada ya muda aliniletea supu na chapatti mbili.

    Nilikula kwa kujitahidi nile taratibu lakini sikuweza nilikula upesi upesi kwasababu nilikuwa na njaa kali sana.

    Nilimaliza na kumshukuru sana yule dada, nikamuaga kuwa ninaondoka akaniita.

    “Wewe ni mgeni eneo hili.. nakuona leo kwa mara ya kwanza Kelvin” alizungumza nikatikisa kichwa kukubaliana naye akanisogelea na kunieleza kuwa niishi kwa tahadhari kubwa sana, kuna wimbi la wachuna ngozi na vibaka limelindima pale Tunduma.

    Kauli yake ile ilinifanya niingiwe na ubaridi mkali sana. Nilitetemeka na tumbo nalo likaunguruma kwa sababu dada yulealikuwa akizungumzia kitu ambacho siku hiyo nilikuwa nimekishuhudia, kuona wenzangu wakichunwa ngozi huku wakiwa hai hadi wanakufa.

    “Kwani wewe ni mwenyeji wa wapi..” aliniuliza.

    Nilikosa jibu nikainama chini, nilitaka kumwongopea yule dada tena lakini sikuona kama ni sahihi kwa sababu kwa kiasi alinipa mwanga jinsi gani niweze kujihadhari.

    Nilinyanyua macho yangu na kumtazama, nilijaribu kuzuia machozi yasinitoke lakini sikuweza, nilikuwa nalia kwa sababu nilishuhudia mauaji ya kikatili sana na nikajiona kuwa nipo katika foleni ile.

    “Kelvin nina miaka mitatu sasa nafanya biashara eneo hili, nakuona kabisa kuwa una tatizo wewe. Sikia, hapa Tunduma watu wengi sana huwa wanaachwa solemba na wenzao, wanaambiwa subiri hapa kisha inakuwa moja kwa moja, kila biashara haramu inapatikana hapa kwa sababu ya uwingi huu wa watu. Hivyo kama na wewe umeachwa solemba fanya upesi urudi kwenu kwa sababu hapa sio sehemu sahihi ya kuishi bila kuwa na kazi ya kufanya…..huu mwaka hapafai kabisa, miaka iliyopita paliwa na amani sana sijui hawa wachuna ngozi ni watu kutoka wapi, naamini sio watanzania…” alizungumza nikaingilia mazungumzo yake.

    “Lakini nimewasikia wakizungumza Kiswahili…” nilimweleza.

    Akashtuka na kuifunga kanga yake vyema, akataka kunihoji mara sauti ikasikika.

    “Mama danny niongeze chapatti huku, na mchuzi kidogo.” Ilikuwa sauti ya mteja mgahawani.

    “Tafadhali usiondoke Kelvin…” aliniita kwa jina lile bandia nililokuwa nimejitambulisha. Nilibaki nimesimama pale huku taratibu nikijipa onyo kuwa nisije kumfananisha msichana yule kama Rahma mtoto wa mwenyekiti wa mtaa niliyemueleza siri zangu na kisha akatabasamu na kunicheka nilipokuwa nimepiga magoti huku nikiwa nimefungwa kamba.

    Baada ya muda alirejea bila shaka ni baada ya kutoa huduma.

    Alianza kuzungumza na mimi akiniuliza nini maana ya kauli yangu, nikamjibu kijuu juu tu kuwa nilikuwa nimekoswakoswa kuchunwa ngozi.

    Sikumuelezea zaidi chanzo cha kufika pale kwa sababu sikutaka kujivua nguo kwa kila mtu hii ilikuwa hatari sana….

    Wakati tunaendelea kuzungumza, mara akapita mwanaume akiwa amevalia suti, yule dada akamuona.

    “Ehee… ngoja nisubiri hapa Kelvin usiondoke tafadhali…”

    Akaondoka upesi na kumfikia yule mwanaume, alipofika wakawa wanazungumza huku mara kwqa mara akielekeza mikono kuja mahali nilipokuwa na baada ya muda akawa amemshika mkono yule mwanaume na kuja naye upande ambao nilikuwa nimesimama.

    Mwanaume yule alikuwa amevaa miwanio nyeusi na alikuwa mbabe kwa kumtazama tu.

    “Askari!!!” nilitahamaki huku mwili ukishikwa na ganzi kali.

    Nikabaki nimesimama nisijue ni kitu gani cha kufanya, na wao wakazidi kusogea……

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    JIFUNZE.

    WALISEMA kuwa maisha ni shule, bila shaka ewe unayeifahamu shule unafahamu kuwa katika safari ya shule kuna mitihani, mingine utafaulu na mingine utafeli. Ukifeli mtihani mmoja usikate tamaa bali weka jitihada zaidi ili ufaulu mtihani mwingine.

    Mlango mmoja katika maisha ukifungwa, kuna milango mingine elfu kwa maelfu imefunguliwa.

    Maisha ni shule…….SOMA.



    WALIZIDI kusogea, nikataka kukimbia lakini nikakumbuka mara kadhaa nilizojaribu kukimbia niliishia kufyatuliwa risasi na kuishia kukamatwa. Ni heri kama alikuwa anakuja kunikamata anikamate tu bila kunidhuru.

    Yule dada alipofika pale akawahi kunitazama machoni kisha akanikonyeza, sikujua nini hasa maana yake na mara akazungumza.

    “Aliyenipa ile pesa nd’o huyu na amekuja hapa kunidai….” Akasita na kumtazama yule bwana mwenye suti.

    “Mdai gani huyu bwana sista unanizingua mi hela sina nilikwambia nikipata nitakupa…” alijibu kwa jeuri yule bwana.

    “Michael tafadhali naomba hiyo pesa acha masihara basi mbona mimi sijawahi kudharau kazi ya mtu, au kisa mimi msichana eeh” alihoji huku akionekana kukerwa na majibu ya yule bwana.

    “Yaani utasababisha hata wateja waaminifu niache kuwa nawakopesha, sasa wewe unadhani naendeshaje biashara, nimewapikia wafanyakazi wako wamekula halafu hela unanifanyia hivi kwanini lakini??” alizidi kulalamika.

    Yule mwanaume hakuonekana kujali yale malalamiko, akageuka ili aweze kuondoka.

    “Michael…. Michael sitaki tuvunjiane heshima… nakuheshimu Michael….” Yule dada alimsihi. Yule mwanaume akazidi kuondoka.

    “Ngoja sasa nikuonyeshe mimi ni nani…” akaongea kwa sauti ya chini kisha akailegeza kanga yake akaitoa kiunoni na kubakiwa na pensi ndani maarufu kwa jina la nyanyapuzo kwa miaka ya tisini…

    Sikujua ni kipi binti yule anaweza kumfanya yule bwana mwenye mwili mkubwa hadi afikie hatua ya kuvua kanga kama anaenda kupambana na msichana mwenzake.

    Nilitaka kumzuia lakini sikuwa nimezoeana naye sana.

    Nikabaki kumsuhudia, akafika na kumshika mkono Mixchael, kisha akamuuliza iwapo atampa pewsa yake au hatanmpa. Yule bwana akamjibu kwa nyodo.

    “Sikupi na cha kunifanya huna Malaya mzoefu wewe…”

    Ni hapo nikalishuhudia sakata ambalo sikuwahi kuliona hata siku moja katika maisha yangu.

    Yule binti akavuta koti la yule bwana, yule bwana ikabidi ainame kufuatana na anapovutwa, alipoufikia usawa wa yule binti, akarukiwa kichwa kilichouchapa mdomo wake barabara, akatokwa nay owe la maumivu huku akitukana kila aina ya matusi. Yule binti upesi akainama akachota mchanga chini upesia akamwagia machoni, sasa watu wakawa awamejaa wakishuhudia ule ugomvi.

    “Ole wake mtu aniachanishe.. niacheni nilivyo.. nataka aniambie huo umalaya nilifanya naye lini ama aliniona naufanya wapi, yaani pesa zangu hataki kunilipa na matusi kanitukana..” alifoka dada yule wakati mwanaume mmoja alipotaka kuachanisha ugomvi ule.

    Sasa yule Michael hakuwa akiona na alipokea kipigo kitakatifu.

    Kama hiyo haitoshi yule dada akamvua koti la suti na shati lake akabaki kifua wazi.

    Alikuwa amempa kipigo kikali haswa.

    “Na ninaendelea kufungua biashara yangu kama kawaida siogopi mtu mimi…” aliongea kwa ghadhabu huku akiondoka na zile nguo.

    “Yaani anaiiita mimi Malaya… mimi kabisa ananiita Malaya….” Akazungumza peke yake akionekana kana kwamba hajaridhika na kipigo alichomgawia bwana Michael.

    Akatembea hadi nilipokuwa nimesimama akafika na kunitazama.

    Akanitazama kwa muda mrefu kisha machozi yakaanza kumtoka, nikamsogelea na kumkumbatia. Ni mimi pekee niliyekuwa mtu wake wa karibu kwa dakika zile.

    “Pole ni mitihani ya maisha tu…” nilimnong’oneza.

    “Ila nd’o ananiita mimi Malaya mzioefu.. kwanini aniite hivi eeh!! Kwanini??” alilalamika, na hakika alionekana kuguswa sana na kauli ya yule bwana.

    Nikiwa bado nimesimama na yule dada, bwana Michael akasimama, sasa alikuwa anaweza kuona tena, kwa zile aibu akataka kupambana kurudisha heshima. Na kuna watu walionekanja kumjaza kichwa ili aweze kumwadhibu yule dada.

    Nilitambua kuwa yule bwana atampiga vibaya sana dada aliyenipa chakula, na isingekuwa sawa mimi kushuhudia kitu hiki, nikajivika ujasiri. Na kwa machozi ya yule dada nikajikuta na,kuwa jasiri sana.

    “Ni heri uondoke kwa amani ulichopata kinakutosha, usidiriki kumgusa dada yangu…” nilizungumza kwa kujiamini huku hasira zikinionyesha wazi kuwa yule bwana si lolote si chochote.

    Nilikuwa nimeshiba tayari chakula cha yule dada kivipi sasa nisikitumie kile chakula kumtetea.

    Bwana Michael hakuonekana kutishwa na mkwara wangu na jambo hili nilikuwa nalipenda tangu shuleni, niliwaeleza mwanzoni mwa simulizi hii kuwa nilikuwa sipo tayari kuonewa hata siku moja shuleni.

    Nanilipenda sana mtu aliyejiamini kuwa anao uuwezo wa kuniadhibu asijue na mimi nina uwezo gani.

    Akafika kichwakichwa pale akimtaka dada.

    Nilitokwa na ngumi moja kali, huenda ilikuwa kali kuliko zote nilizowahi kupiga.

    Ikamwingia barabara mdomoni, mdomo ambao tayari ulikuwa umepasuliwa kwa kupigwa kichwa ukapasuka mara ya pili.

    Akaanguka chini nikakunja ngumi na kumsihi tena asithubutu kuendeleza ugomvi ule.

    Kweli akagwaya na kutoa maneno ya kidhaifu, eti ipo siku yetu anatupangia.

    Kwa kauli ile alijikuta akizomewa.

    “Inabidi nifunge banda langu, kashaniharibia siku mjinga huyu. Sitapika chakula cha mchana leo….” Alinieleza yule binti. Kisha akanitazama tena machoni, “Asante kwa kunipigania… ulisema unaitwa nani vile..”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naitwa Kessy…”

    “Ooh nilisikia Kelvin pale mwanzo…”

    Nikatabasamu. Nikaongozana naye akafunga banda lake tulipotoka nje akaniuliza, “Sasa utalala wapi Kessy??”

    Nilimtazama bila kusema lolote, akaendelea….”Kama vipi twende basi kwetu huko, utalala kule halafu kesho utajua nini cha kufanya kaka yangu sawa…”

    “Asante sana dada….. dada nani vile!!” na mimi nilimuhoji.

    “Naitwa Tusekile…”

    “Nilisikia wakikuita mama Danny…” nilimuhoji…

    “Yote hayo majina yangu ila niite Tusekile itafaa zaidi..” alinijibu huku tukitembea kuelekea kituo cha daladala.

    Tukapata daladala na kuondoka.

    Hatukwenda vituo vingi tukashuka.

    “Kumbe kwenu sio mbali eeh…”

    “Yah sio mbali sana.. niliamua kuishi huku kwa sababu ni jirani sana na eneo langu la biashara.” Alinijibu huku akiongoza njia.

    Tulitembea hadi tukakifikia chumba kimoja, akafungua mlango tukaingia ndani.

    Tulifika na kuketi kitandani, maana chumba hakikuwa na viti.

    “Ila sijisikii amani kabisa kulala hapa leo sijui kwanini na mama aliwahi kunambia kuwa nikisikia sauti ndani yangu ni heri niiheshimu..” alizungumza akiwa mwenye mashaka. Mimi sikuwa msemaji nsana bado nilikuwa mgeni.

    “Kessy naomba nioge halafu tuondoke kwa tukio lililotokea leo sina amani ghafla…” alinisihi, nikamuunga mkono kwa kutikisa kichwa kukubali.



    Kweli baada ya kuoga, tukatoka ilikuwa yapata saa nane mchana. Tukatoka na kuketi mahali ambapo tulikuwa tunaiona nyumba yake.

    Tulikuwa tunakunywa soda, Tuse akiwa na mkoba wake mkubwa begani na kila mara alikuwa akitazama huku na kule.

    Kweli ikawa kama alivyokuwa amechezwa machale yale. Baada ya kama saa zima hivi nyumba ile ilizungukwa na maaskari ambao walikuwa wamevaa sare zao.

    “Si nilikwambiaaa…” alisema huku akiuweka sawa mkoba wake, tukasimama tuweze kuondoka eneo lile hali haikuwa shwari tena.



    JIFUNZE



    Rafiki hazaliwi akiwa na alama ya kuja kuwa rafiki yako siku za usoni, rafiki huja kutokana na matukio. Rafiki wa kweli ni yule atakayesimama nawe wakati wa ugumu na kukufanya kuwa imara.

    Rafiki dhaifu atacheka nawe wakati ukiwa katika furaha tu……

    Thamini urafiki ni ngao katika maisha…..



    UZURI ni kwamba sehemu ile tuliyokuwa tumekaa nyuma yake palikuwa na njia, tukapita pale na kwenda hadi barabarani tukapanda gari ya kutufikisha Mbeya mjini.

    Tukiwa ndani ya gari kuna abiria wawili walianzisha maongezi, walikuwa wakizungumzia juu ya kibanda cha kuuzia chakula ambacho kilikuwa kimechomwa moto. Kila mmoja alitoa sababu zake, huyu akisema kuwa katika kibanda kile wachuna ngozi walikuwa wanakutana kwa ajili ya kusuka mipango yao, mwingine alipinga na kudai kuwa mmiliki wa kibanda kile alikuwa ni jambazi hivyo wananchi wenye hasira kali walikuwa wameamua kukichoma kama namna ya kulipiza kisasi.

    “Kha we naye bwana sasa kale kasichana unasema kalikuwa kajambazi au??” aliuliza katika namna ya kusanifu bwana yule.

    “Hah! Kwani jambazi huwa ana sura basi, yeyote tu anaweza kuwa jambazi…” alikazia bwana yule huku akiungwa mkono na abiria mwingine ambaye aliendeleza mjadala kwa kulaani vitendo vya uchunaji ngozi za wanadamu vilivyokuwa vimeshamiri.

    Tuse aliniinamia sikioni na kunieleza kuwa ni yeye anayezungumziwa na kuwa ni kibanda chake kimetiwa moto na watu wabaya.

    Hata kabla hajaniambia vile kichwani nilikuwa nimewaza tayari kuwa alikuwa ni yeye anayezungumziwa.

    “Naomba nilale katika mapaja yako sitakiwi kuonekana sura yangu kuna tatizo hapa….” Aliniambia kisha akapenyeza na kujilaza katika mapaja yangu.

    Laiti kama angejua jinsi na mimi nilivyokuwa na hofu ya kuonwa sura yangu kutokana na mikasa kadhaa niliyokuwa nimepitia angenionea huruma ama la ungekuwa mwisho wa kuniamini.

    “Ila tukifika mjini hakuna kitakachoharibika…” alizungumza huku akiwa amenilalia.

    Safari ilikuwa ndefu kiasi chake hadi kufika Mbeya mjini.

    Tukatelemka na kutembea kwa miguu kwa mwendo mrefu, Tuse hakutaka tupande tena gari, aliamini kuwa halikuwa jambho salama hata kidogo.

    Kweli nilimuunga mkono hata mimi niliona kuwa halikuwa jambo la heri hata kidogo. Tukatembea sana wakati huo nikiwa nimevaa kandambili ambazo alinipatia Tuse nilipoenda katika kile chumba chake.

    Hatimaye tukafika eneo ambalo aliniambia kuwa libnaenda kwa jina la Soweto. Akanieleza kuwa ni pale alizaliwa na kukulia pale…. Tukapinda kona mbili tatu hatimaye tukaifikia nyumba.

    Akabisha hodi mlango ukafunguliwa na mwanamke aliyekuwa amevalia gauni refu la kulalia pamoja na sweta.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Shkamoo mama…” Tuse alimsalimia mwanamke yule na mimi pia nikasalimia.

    “Nd’o mkwe wangu…” alisema yule mama huku akitabasamu.

    Tuse akamchukua mkono na kufanya kama anataka kumuuma, yule mama akapiga kelele kisha wakakumbatiana. Nikatambua wazi kuwa mama na mwana wale walikuwa na mazoea ya karibu sana. Na walikuwa ni marafiki.

    “Kessy karibu ndani, huyu ni mama yangu mzoee tu ana matatizo naona ni uzee unamsumbua…” alizungumza kimasihara Tuse.

    Nikaingia ndani huku nikiwa nimetawaliwa na amani tele.

    Tuliketi pale sebuleni, na moja kwa moja Tuse akanitambulisha kwa mama yake kwa ufupi na kisha akaelezea chanzo cha kuwa pamoja hadi wakati ule kuanzia ugomvi hadi katika kuiona nyumba ikivamiwa na kusikia juu ya kibanda cha Tuse kuchomwa moto.

    “Kessy huyu ni mama yangu zamani aliitwa mama Tuse lakini sasa hivi anaitwa mama lao….” Alizungumza Tuse kisha akasita na kuendelea “Nilikwambia kwa mama huyu hakiharibiki kitu na nd’o maana likawa kimbilio la kwanza kabisa.”

    Nikatikisa kichwa kukubaliana naye.

    “Nimekufungulia kibanda mwanangu wamekichoma moto, nimekupangishia chumba wamekuvamia na bunduki….. alizungumza kwa sauti ya chini mama yule ambaye simulizi zile wala hazikumtetemesha na sikujua ni kwanini lakini baadaye nilikuja kufahamu.

    Akajikohoza kidogo kisha akaendelea, “Bwana mwenye suti akagoma kulipa deni ukamdai akasema wewe ni Malaya mzoefu…. Mwanangu mimi wewe ni Malaya si ndo alichomaanisha…” aliendelea kuzungumza peke yake sisi tukiwa kimya.

    “Sikilizeni wanangu, kuna watu wanajaribu kuifanya nchi hii ni mali yao kabisa halali na wanaweza kufanya lolote ambalo wanajisikia kufanya, kitu ambacho sio sahihi. Mimi nimekaa sana Dar es salaam nimeyaona mambo haya, nimekaa sana Iringa nikaona mambo haya. Dawa ya kuitafuta haki yako ni kuwa ngangari na akili nyingi sana kichwani….kuna watu wapo kwa ajili ya kuumiza tu wenzao na wakibaki kutazamwa wataumiza wengi sana…. Mimi sipo tayari kuona mtu anaumizwa nd’o maana mikasa ya ANTI EZEKIEL na HILA yote ilinihusu…..na huu mkasa usiokuwa na jina na wenyewe utanihusu….” Akasita akanitazama machoni, na kisha akanitupia swali, “Na wewe sura yako mbona sio ngeni sana machoni kwangu…”

    Nikainama chini na kulazimisha tabasamu, Tuse akawahi kuzungumza…”We mama nawe umewahi kumuona wapi?? Umbe tu…”

    “Subiri ajibu basi yeye mwenyewe mtoto wa kike mbona hivi….” Mama lao alimshushua Tuse kidogo.

    “Ni kweli usemalo mama kuna uwezekano umewahi kuniona mahali naninajisikia huru kabisa kusema hili ambalo sijamueleza Tuse…” nilizungumza nakisha nikaelezea mkasa mzima ulionikumba hadi kuwa pale nikaelezea hadi picha zangu kutolewa magazetini kwa makosa ambayo sijayafanya.

    Nilipomaliza kusimulia, Tuse akiwa amepigwa na butwaa, mama lao yeye alisimama na kuanza kuzunguka huku na kule huku akiwa na tabasamu pan asana usoni.

    “Looh!! Nilihisi kabisa hili jambo linanihusu moja kwa moja ama kivyovyote vile. Na leo nimepata majibu sasa….” Alizungumza vile na kuendelea kusimulia jinsia livyolifuatilia kwa ukaribu tukio la mwanamke kuuwawa kwa kuchomwa visu na mume wake na kisha kutoweka na baadaye kusemekana kuwa ni mtoto wake aliyemchoma visu.

    Mama lao alisimulia mambo mengi kuonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa amelifuatilia sana jambo lile.

    Baada ya mazungumzo marefu sana hatimaye Tuse aliingia jikoni na kuandaa chakula tukala na kisha tukapumzika, Tuse akilala chumbani kwa mama yake na mimi nikilala kile chumba alichotakiwa kulala Tuse.

    Asubuhi pakapambazuka na kuingia katika vita kuu ya mwisho ambayo ilikuwa ni aidha haki inapatikana na kila mmoja kuwa huru ama la haki ifungwe pingu kisha sisi soye tuishie pabaya kabisa.

    Mama lao akaamua kuwa vita hii inaenda kuamuriwa jijini Dar es salaam.

    Kumbe maisha yangu ya kijijini yalinifanya nisiijue mikasa ya mama lao ambayo aliwahi kushiriki, ndo maana nikawa siamini kuwa mwanamke anaweza kuwa mpiganaji kiasi cha kusema kuwa tunaenda dar katika vita na yeye ndiye amiri jeshi mkuu.

    Moyoni sikuaminmi kabisa, ila kumbukumbu za jinsi Tuse alivyokabiliana na yule bwana aliyegoma kulipa deni zikanifanya niamini kuwa utata ule alikuwa amerithi kutoka kwa mama yake.

    Siku hiyo mapema safari ikapagwa kuwa siku inayofuata tutasafiri wote kwenda jijini Dar.

    Mimi, Tuse na yeye mwenyewe amiri jeshi mkuu mama lao.



    JIFUNZE.

    Nguvu ya mwanamke ni KUJIAMINI…..



    Safari nzima ilitawaliwa na hekaheka za hapa na pale kama inavyokuwa safari nyingine za kawaida. Mama lao alikuwa mnunuzi mkubwa mara anunue korosho mara kanunua biskuti, machungwa na chochote ambacho kilimpendeza.

    Nilijifunza kuwa mama lao alikuwa mwanamke ambaye anafanya jambo ambalo anataka yeye bila kutazama watu watamtazama vipi, ilimradi tu hawaletei makwazo yoyote yale basi alifanya kwa heri!!

    Tulifika jijini Dar es salaam majira ya saa moja na nusu usiku, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kabisa kuingia katika jiji lile lakini mama lao pamoja na Tuse Yule mwanaye wa kike walidai kuwa walikuwa ni wenyeji sana tu wa jiji lile.

    “Ningeweza kukuacha ulale na Tuse lakini nimewaona mpo kama …” kabla hajamalizia kutoa kauli yake ambayo mimi na Tuse tulikuwa tumeielewa tayari mara Tuse akamziba mdomo ili asiendelee kuzungumza lolote lile.

    Kama kawaida yao mama na mwanaye waliokuwa wamezoeana na kutaniana kama mtu na dada yake.

    Vilichukuliwa vyumba viwili katika nyumba ya kulala wageni kimoja kilikuwa kwa ajili yangu na kingine alilala Tuse na mama yake. Lakini ili kuwaficha wamiliki wa nyumba ile ya kulala wageni tulilaghai kuwa chumba kimoja nalala mimi na Tuse halafu kingine analala mama lao.

    Nyumba hizi huwa haziruhusu watu wa jinsia moja kulala chumba chenye kitanda kimoja, lakini naona siku hizi utaratibu huu unajifia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati mimi nawaza kuwa baada ya kupata chakula ulikuwa muda wa kulala haikuwa vile katika akili ya Tuse na mama yake, bila shaka mama lao alikuwa amemuambukiza mambo mengi sana Tuse.

    Wakati najigeuza kuusaka usingizi vizuri nilisikia chumba kinagongwa, nikatulia bila kusema neno lolote mlango ukagongwa tena.

    Nikasimama na kusogea mlangoni kasha nikauliza ni nani alikuwa mlango sauti ya mama lao ikajibu.

    Nikafungua mlango akaingia, hakuwa peke yake…..

    “Washa taa” sauti ya kiume ikasema…..

    Nikawasha, na hapo nikajikuta natazamana ana kwa ana na mwanaume ambaye alikuwa hana mguu mmoja na alikuwa anatembelea gongo, sikumtilia maanani sana kumtazama usoni kwa sababu mwenyeji wangu mimi alikuwa ni mama lao nilingoja anieleze ni kitu gani kilikuwa kinaendelea.

    “Dogo… huyu jamaa anahusika katika kukitafuta kile ambacho tunakitafuta… msikilize na umpe ushirikiano bila kujalisha ni kwa muda gani. Amini kuwa hakitaharibika kitu…..” alizungumza na hakungoja kusikia iwapo kuna kitu nitajibu, akaondoka na kuufunga mlango kwa nje kwa kutumia funguo.

    Sikujua hata ni kipi kilikuwa nia yake ya kufanya vile.

    Yule mtu akajikokota na kuketi.

    Akaliweka gongo lake pembeni, akajipekua mfukoni na kutoka na karatasi jeupe na penseli, akaviweka mezani na hapo akatulia kasha akakohoa kidogo.

    “Dodo… samahani ninakuita dogo kwa sababu ndo nilivyoambiwa kuwa unaitwa dogo…..” alizungumza na mara kengele za hatari zikagonga katika kichwa change nilikuwa nimewahi kuisikia sauti hii mahali lakini akili yangu haikufanya upesi kutambua kuwa ni wapi nimewahi kusikia.

    “Hamna shida hata ukiniita hivyo inafaa tu mimi ni mdogo kwako…” nilizungumza huku nikiwa bado najiuliza kuwa nimemfananisha ama ni kweli alikuwa yeye ambaye akili yangu inawaza.

    Kitendo change cha kujibu lile swali kikaibua hisia Fulani kwake ambazo nilizigundua, alikuwa ameshtuka kwa kiasi Fulani.

    “Dogo ni wewe ama nafananisha sauti… nilidhani kuwa ulikufa??” ile sauti ikaniuliza na nikiwa sijajua nini cha kujibu mara ghafla akanitazama usoni.

    Naam! Nilikuwa natazamana moja kwa moja na macho ya afande wanchera, Yule afande ambaye alikuwa pamoja na afande Saimoni waliokuja kunikamata kule kijijini kwa kesi ya kuwa nimemuua mama yangu kasha kukimbia, kabla hawajanifikisha palipostahili tunakutana na watekaji na wauaji wa Gadna wanaanza kurushiana risasi baadaye tunafanikiwa kutoroka lakini tunapata ajali ya gari.

    Sasa alikuwa na mimi chumbani hana mguu mmoja na uso wake ukiwa umebondeka bondeka.

    Nilikuwa nimepagawa nikidhani kuwa mama lao alikuwa amenileta mjini kwa ajili ya kuniuza, nilijikuta nakata tamaa kabisa.

    “Sasa nazifuta fikra zote nilizokuwa nikiziamini na wanazoziamini watu wengi kuwa wewe ulikuwa muuaji na wale waliokuja kupambana na sisi walikuwa wenzako… “ alisita kuzungumza akanitazama tena na kasha akaendelea.

    “Afande saimoni alipoteza maisha katika ajali ile, gari ilipopata ajali alijaribu kuruka lakini hakufanikiwa akanasa kwenye vyuma gari ikamponda vibaya sana…..” akasita tena akawa anatazama hewani, nikatambua kuwa alikuwa anadhibiti machozi yake yasimwagike, akauma meno yake kasha akaendelea. “Saimoni alikuwa rafiki yangu sana na alikuwa kama mdogo wangu wa karibu sana… mimi kama unionavyo hapa nilipoteza mguu wangu na ilikuwa bahati sana kupona…”

    Aliendelea kusimulia afande Wanchera, akanieleza jinsi alivyolala muda mrefu kitandani hadi kujikuta akiipoteza ajira yake akiwa palepale kitandani. Akaelezea jinsi familia yake ilivyoondolewa katika zile nyumba za kipolisi kwa sababu baba hakuwa polisi tena.

    Akazungumza mengi na baadaye akanieleza kuwa baada ya kutoka hospitali akiwa si polisi tena na zile pesa alizopewa kama pole zikiwa zimekaribia kumuishia akaamua kurejea katika fani yake ya zamani, fani ya uchoraji na hicho ndo kitu ambacho kimemkutanisha na mama lao.

    Yupo pale kwa ajili ya kuchora sura ambazo nilizishuhudia zikimtesa Gadna na kumuua vibaya.

    Nilijikuta nashusha pumzi zangu na kumuonea huruma kubwa bwana wanchera, kwa sababu hali aliyokuwanayo ilionyesha wazi kuwa alikuwa yu katika wakati mgumu sana kimaisha.

    Nikatumia fursa hiyo kumueleza pia makubwa niliyopitia, kuanzia pale niliporejewa na fahamu na kujikuta katika mikono ya watu walionipeleka Zambia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilielezea kila kitu na pia nikaelezea sura nilizoziona kati ya watu waliokuwa wakimtesa Gadna hadi kumuua.

    Wakati naelezea ndipo nikaona maajabu ya vipaji vilivyo katika nchi yetu, mimi nikiwa nazungumza Wanchera alikuwa anachora, na baada ya muda akainuka na kunipa ile karatasi.

    Mungu wangu!!! Nilikuwa naitazama sura ya Yule muuaji wa Gadna.

    Damu ilinisisimka sana na kujikuta narejea katika tukio lile baya kabisa la kutisha sana.

    Baada ya hapo alienda mlangoni, safari hii hakutumia lile gongo lake badala yake alirukaruka kwa kutumia mguu mmoja tu, nikajikuta natokwa machozi kumtazama afande wanchera akirukaruka namna ile.

    Akili yangu ikanikumbusha kuwa hakuna aijuaye kesho yake na mwanadamu hujafa hujaumbika.

    Aliufikia mlango akagonga mara mbili akatulia kasha akagonga tena mara tatu.

    Baada ya muda kidogo mlango ukafunguliwa mama lao akaingia.

    Akaufunga mlango na kuketi kitandani.

    “Mbona kama mlikuwa mnaomboleza vijana?” alituuliza huku akitusaili kwa kututazama macho yetu.

    Hakuna aliyemjibu, na yeye hakuuliza mara ya pili.

    “Afande sasa inamaana ilishindikana kabisa kuwekewa walau mguu wa bandia…” nilimuuliza.

    Mama lao hakushtuka hata kidogo, akaendelea kuitazama picha ile kwa ukaribu kabisa.

    “Ni stori ndefu dogo ila naamini kuwa utafahamu siku moja” akasita akamgeukia mama lao.

    “Anti shika hizi…” akampatia pesa.

    “Za nini tena hizi…” mama lao akahoji.

    “Mimi ni mwenzenu nipo pamoja nanyi katika tukio hili, nilikuwa sijakueleza kiundani na huenda hata nisingekueleza kama nisingekutana na huyu dogo….” Wanchera akamsimulia mama lao kila kitu kama kilivyotokea.

    Ebwana eeh! Mama alao aliduwaa sana, akamuita Tuse.

    Akamsimulia, na hapo tukajikuta tumeunda jeshi la watu wanne.

    Na ile picha mama alo na Wanchera walikuwa wameitambua kabisa kuwa ni ya nani.

    Na wakati uleule mipango ikaanza kusukwa jinsi ya kujua ni kitu gani kimejificha nyuma ya pazia.

    Afande wanchera akatuahidi kuwa yeye hatasimama msitari wa mbele kwa sababu anatambulika kuwa aliwahi kuwa askari. Lakini akatueleza kuwa atatushauri mbinu za kutumia, akatupa onyo kuwa tusithubutu hata kidogo kulifikisha suala hili polisi, akatueleza kuwa Yule bwana katika picha alikuwa ana mtabndao mkubwa sana angeweza kubadili kila ukweli kuwa uongo.

    Mama lao akatabasamu kasha akamueleza afande wanchera kuwa wazo la kwenda polisi halipo katika kichwa chake.

    Na hapo akaleta mpango ambao sikutegemea kuwa mama Yule anaweza kuuleta, ulikuwa mpango ambao hata ningepewa miaka mia nisingeweza kuusuka.

    Na safari hii chambo katika mtego huu alikuwa ni Tusekile mtoto wa mama lao.

    Nikakiri kuwa sio tu tembea uyaone, bali kumbwa pia na mikasa ili ujifunze.

    Lakini usije ukajiundia mikasa maksudi kamwe!!!

    Mpango huu ukapangwa kufanyika haraka iwezekanavyo.



    JIFUNZE.

    KESHO… ni neno jepesi sana kutamka lakini ni kitu ambacho hakuna hata mmoja wetu ambaye anakimiliki.

    Unaweza kuwa tajiri sana, una vuiwanda, nyumba na mali nyingi sana lakini kitu ambacho hauwezi kukimiliki kwa kutumia pesa zako ni KESHO!!!

    Mshukuru Mungu kila anapokuamsha salama asubuhi ukiwa unavuta pumzi hizi za bure kabisa!!!



    Punde baada ya mama lao kuifahamu sura ambayo iliyokuwa imechorwa na afande wanchera ambaye sasa alikuwa na ulemavu wa kudumu.

    Alimweka chini Tuse na kumueleza kuwa ule ulikuwa ni wakati wake wa kucheza karata ambazo mchangaji atakuwa ni mama lao lakini yeye Tuse atatakiwa kuzicheza vyema.

    Mama lao akamueleza Tuse kuwa atatakiwa kujiweka karibu kabisa na huyo bwana ambaye mama lao alimpa jina la kaburu. Japokuwa halikuwa jina lake halisi alipenda litumike jina hilo.

    Tuse hakushtushwa na taarifa ile hata kidogo bila shaka alijua ni kiasi gani mama yake anajua kuzichanga karata zake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya hapo mama lao akaondoka na Tuse kwenda chumba chao na mimi nikabaki na afande Wanchera katika kile chumba.

    Nilipata nafasi ya kumuuliza maswali mengi sana bwana huyu juu ya mambo yanavyokuwa yakienda hasahasa katika suala zima la siasa. Nilimuuliza ni kwanini basi viongozi wawanie madaraka kiasi kile.

    Wanchera alicheka kisha akaniambia kuwa nijitahidi sana nisije kuingia katika siasa kwa sababu unaweza kuwa mwanasiasa safi lakini ukishaamua kujiingiza tu katika siasa unajikuta ni mwanasiasa siasani.

    Yaani unavuka mipaka ya siasa na kuwa na tabia nyingi nyuma yako, usiye na huruma, muongo na wsengine wanavuka hatuana kujikuta wakiingia katika ushirikina.

    “Mdogo wangu… siasa isikie tu. Usiifuate kama kweli unapenda kubaki salama…” akasitaakanitazama, “Unajua Gadna kisa tu alitangaza nia ya kuwania ubunge na vile anapendwa basi ndo kashapotezwa katika ramani, kuna watu wanadhani eti walizaliwa kuwa viongozi kwa maisha yao yote…. Akitokea tu mtu wa kuwapinga, wanamfanya wanavyojua wao…..”

    Alinielezea kiundani na kisha akaanza kuniuliza juu ya mama lao, akaniuliza Yule mama alikuwa akijiamini nini kujiingiza katika jambo hili ambalo linaonekana kuwa zito sana.

    Sikuwa na majibu yaliyonyooka ya kumpatia, nilichomwambia ni kwamba hata mimi sijui lakini mama Yule anajiamini sana.

    Baadaye afande wanchera alisinzia huku akiniacha mimi nikiwa bado napepesa macho nikiusaka usingizi.

    Nilikuwa nafikiria mengi sana, mwisho nikamuomba sana Mungu atuongoze katika jambo hili liweze kuisha kwa haki kupatikana.

    Sijui saa ngapi nilisinzia lakini nilikuja kushtuka afande wanchera akinitikisa na kunisihi niamke.

    Nikaamka na kusugua macho yangu nikamkuta mama lao pale chumbani, upesi nikajistiri vizuri.

    “Bila kuoga wala kufanya lolote njoo…” akaniita Yule mama, nikamfuata nyuma.

    “Ingia katika chumba kile kisha urejee baada ya dakika tano na unieleze chochote ambacho utaona kinafaa kunieleza…” alinipa maelekezo yale. Nikafuata huku nikiwa nimejawa na hofu, yaani nilikuwa muoga wa kila kitu… nikatembea nikakifikia chumba na kukifungua.

    Asalaaale!! Macho yangu yalilazimika kufumba na kufumbua upesiupesi ili niweze kuamini ama kutoamini kile nilichokuwa natazamana nacho.

    Alikuwa ni binti mrefu, mwenye umbo la kuvutia mweusi na weusi wake ulifaa zaidi laiti kama angekuwa mweupe huenda angeharibika.

    Macho yake malegevu na tabasamu usoni lilimfanya kuwa mmoja kati ya wasichana ambao hauwezi kusita kuwaita warembo.

    “Mambo!!” akanisalimia huku akizidi kutabasamu.

    “Wewe mtoto toka sasa imetosha alaa!!” nilishtushwa na sauti ya mama lao.

    Nikatoka nikiwa na aibu zangu, sikuwa naamini bado kuwa Yule alikuwa ni Tuse, alikuwa amerembwa akarembeka.

    Wakati natoka mama lao akasema, “Huyu hapa anakujia ofisini kwako anaomba umpatie kazi utamnyima??”

    Nilisimama nikacheka kidogo kisha nikasema, “Naomba nisiwe muongo mama, mimi ningempa zaidi ya kile alichokiomba!!”

    Mama lao akacheka kwa sauti ya juu, Tuse naye akacheka.

    “Wanaume ni viumbe dhaifu sana, yaani sio tu dhaifu nyie ni wajinga mno. Huwa sijui akili zenu zinawaza nini, yaani mkiona wanja, poda, mavazi ya kung’ara tayari mnachanganyikiwa kabisa. Hivi haya madude huwa yanawapa faida gani…. Hovyo kweli!!” mama lao akatoa dongo lenye ukweli ndani yake nikajifanya sijasikia kabisa. Ila lilinichoma kwa sababu ni kweli kabisa, sijui wanaume huwa tunakuwaje tu.

    Hii ikanikumbusha ule upuuzi wangu niliofanya eti kumueleza Yule Rahma mtoto wa mwenyekiti kila kitu kilichotokea na hatimaye kujikuta matatani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ila kwa uzuri ule wa Tusekile ni heri ningeonekana mjinga tu lakini walah!! Ningempa kazi na zaidi ya kazi!!

    Hakika kama mama lao alipanga kumtumia mwanaye Yule kama chambo basi nilianza kuziona dalili za ushindi njenje. Lakini katika dalili zile za ushindi na wivu nao ukachukua nafasi yake!! Nikaanza kuhofia itakuwaje iwapo Tuse ataingia vibaya katika mtego!!!



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog