Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

NISAMEHE LATIFA - 1

  





    IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Nisamehe Latifa

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    Msichana mrembo mwenye asili ya Kihindi, Nahra Patel alikuwa akilia huku akikimbia kwa kasi kuelekea sehemu kulipokuwa barabara ya lami. Jasho lilimtoka, alikuwa akihema kwa nguvu, japokuwa alionekana kuchoka lakini hakutaka kusimama.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Miguuni mwake hakuwa na viatu na alikimbia katika sehemu zilizokuwa na mibamiba, lakini Nahra hakusimama, aliendelea kusonga mbele, cha ajabu hata miba haikumchoma, na kama ilimchoma, hakusikia maumivu yoyote yale.

    Machozi yalitiririka mashavuni mwake, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini msichana mrembo kama yeye, aliyesifiwa na wanaume kwamba alikuwa mithili ya malaika, leo hii alikuwa amefukuzwa kama mbwa na mwanaume ambaye kila siku alimuona kuwa ndoto ya maisha yake.

    “Deo, mimi? Hapana! Kwa nini? Nimekufanya nini?” aliuliza maswali mfululizo lakini hakupata jibu, wakati huo alikuwa akikaribia barabara ya lami.

    Alipofika barabarani, akatulia chini, pembezoni kabisa mwa barabara hiyo na kuanza kulia huku akiwa amekiingiza kichwa chake katikati ya mapaja yake. Machozi yaliendelea kumtoka, kila alipokumbuka namna alivyokimbizwa na mwanaume aliyemchukulia kama mume wake wa baadaye, moyo wake ulimuuma mno.

    Hakuwa na sehemu ya kwenda na wala hakuwa na fedha. Wazazi wake hawakutaka kumuona kabisa kwa sababu alikuwa amebeba mimba ya kijana mwenye ngozi nyeusi na wakati yeye alikuwa Mhindi.

    Mapenzi yake ya dhati, kung’ang’ania kwake kuwa na Deo ndiyo kulimfanya leo kuwa katika hali hiyo. Hapo barabarani, alikuwa mtu wa kujuta tu, kila alipokumbuka maisha aliyopitia, alibaki akimlaani Deo.

    “Ubungo buku...Ubungo buku,” ilisikika sauti ya kondakta wa daladala moja iliyokuwa ikipita mahali hapo.

    Nahra akauinua uso wake na kuiangalia daladala iliyosimama mbele yake, akasimama na kuanza kuifuata, alipoifikia akaingia ndani na kuondoka.

    Ndani ya daladala, kila mwanaume alikuwa akimwangalia kwa matamanio, alikuwa msichana mrembo wa Kihindi mwenye sifa zote za kuitwa Malkia Cleopatra. Kwa sababu ilikuwa ni usiku na gari halikuwa na taa ndani, hakukuwa na mtu aliyeyaona machozi yake japokuwa uzuri wake ulionekana.

    “Unalia nini tena Kajool?” aliuliza mwanaume aliyekaa naye, alimuita jina la muigizaji maarufu wa kike wa filamu za Kihindi, Nahra hakujibu swali hilo, bado kilio cha kwikwi kiliendelea kusikika.

    Kuanzia hapo Kibaha mpaka anaingia Dar es Salaam, alikuwa mtu wa kulia tu, kumbukumbu za maisha aliyokuwa akiishi na Deo zilijirudia kama mkanda wa filamu kitu kilichomuumiza na kumliza zaidi.

    Mpaka daladala inaingia Ubungo, tayari ilikuwa saa mbili usiku, Nahra akateremka na kusimama kituoni pamoja na watu waliokuwa wakisubiri usafiri.

    “Niende wapi?” alijiuliza Nahra, jibu lililokuja ni kwamba alitakiwa kwenda kwa wazazi wake waliokuwa wakiishi Masaki.

    Baada ya dakika kumi, akapanda daladala iliyokuwa ikielekea Masaki na safari ya kuelekea nyumbani kwao kuanza. Kama kawaida, bado alikuwa mtu wa kulia tu, kilio chake cha kwikwi hakikuisha, baada ya dakika thelathini, akafika nje ya geti la nyumba yao, akaanza kugonga.

    “Nahra, umefuata nini, baba yako ataniua,” aliuliza mlinzi aliyefungua geti, hakuamini kumuona Nahra mahali hapo tena.

    “Naomba niingie, nataka kuonana na baba,” alisema Nahra.

    “Hapana. Naogopa Nahra. Siku ile alitaka kunipiga risasi, siwezi kukuruhusu,” alisema mlinzi huyo huku akianza kulifunga geti hilo.

    “Ninataka kuingia ndani Chichi, niache niingie nikaongee na baba yangu,” alisema Nahra huku akianza kulia tena, akaanza kulisukuma geti ili mlinzi asilifunge.

    Msimamo wa mlinzi ulikuwa uleule, hakutaka kumruhusu Nahra kuingia ndani. Baada ya kulazimisha sana tena kwa kusukumana, Nahra akafanikiwa kuingia ndani ya eneo la nyumba yao. Akaanza kuufuata mlango wa kuingilia sebuleni na kuanza kuugonga.

    Baada ya dakika tano, mlango ukafunguliwa na wazazi wake wote wawili kutoka ndani. Macho yao yalipotua kwa binti yao aliyekuwa akilia huku akiomba msamaha, baba yake, mzee Patel akabadilika, akakunja uso kwa hasira.

    “Umefuata nini hapa? Umefuata nini wewe mbwa?” aliuliza mzee Patel huku akionekana kuwa na hasira kali, Nahra hakujibu kitu, alichokifanya mzee huyo ni kurudi ndani, kama kawaida yake alikuwa ameikumbuka bunduki yake.

    Mama yake, bi Aishani alimtaka Nahra aondoke kwani alijua fika mumewe alifuata bunduki lakini Nahra hakutaka kuondoka, alikuwa tayari kupigwa risasi na kufa, ila si kuondoka nyumbani hapo.

    Msimamo wa Nahra ulikuwa palepale, hakutaka kuondoka mahali hapo, alikuwa radhi kumuona baba yake akimpiga risasi na kufa lakini si kukubali kirahisi kuondoka nyumbani hapo.

    Alikuwa akilia, alijiona kunyanyaswa kwa kile kilichotokea, kitendo cha kutengwa na ndugu zake kisa alikuwa na mimba ya mtu mweusi kilimuumiza mno. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakukuwa na mtu aliyemuelewa, hata mama yake, mtu pekee aliyekuwa akimuonyeshea mapenzi ya dhati siku za nyuma, katika suala hilo alikuwa tofauti naye.

    Mlango ukafunguliwa, mzee Patel kutoka huku mkononi akiwa na gobole, alichokifanya, huku akionekana kutetemeka kwa hasira, akamnyooshea Nahra gobole lile tayari kwa kumfyatulia risasi.

    “Niue tu, we niue baba, ila jua kwamba nilimpenda Deo na nisingeweza kumuacha, kama mnaona nilifanya makosa, wewe niue tu kwani hata wewe utakufa tu,” alisema Nahra, alikuwa amepiga magoti huku akilia kama mtoto.

    Bila bi Aishani kulipiga gobole lile, basi risasi iliyotoka ingeweza kumpiga Nahra kifuani. Mdomo wa gobole ukaenda pembeni, risasi ikatoka na kupiga ukutani. Japokuwa mtoto wao alikuwa amefanya makosa yaliyoonekana kuwa makubwa kwa kuzaa na mtu mweusi lakini hakuwa radhi kumuona Nahra akipigwa risasi na kufa.

    “Punguza jazba,” alisema bi Aishani huku akimsihi mume wake asimuue Nahra.

    “Usinizuie, niache nimuue huyu malaya, ametuzalilisha sana, acha nimuue,” alisema mzee Patel huku akionekana kuwa na hasira mno.

    Bado Nahra aling’ang’ania kubaki mahali hapo, hakuwa na pa kwenda usiku huo, kama walivyokuwa wazazi wake, hata ndugu zake wa Kihindi walikuwa wamemtenga, sababu ilikuwa ni ileile ya kuwa na mimba ya mwanaume mweusi.

    Mbali na ndugu zake, mwanaume aliyekuwa amempa mimba, Deo alikuwa amemfukuza nyumbani kwake. Hakutaka kuondoka, kama kuuawa, alikuwa tayari kufa lakini si kuondoka nyumbani hapo.

    “Chichi, mtoe huyu mbwa mara moja,” alisema mzee Patel, mlinzi akasogea Nahra na kumshika Nahra, akaanza kumbeba juujuu.

    Japokuwa hakupendezwa na jambo lile lakini hakuwa na jinsi, alitekeleza amri ya bosi wake kwamba Nahra alitakiwa kutolewa ndani kinguvu.

    “Niacheeee, nimesema niacheeee, nimesema sitokiiiiiiiii,” alisema Nahra huku akipiga kelele.

    Hiyo wala halikusaidia, Chichi akafanikiwa kumtoa Nahra ndani ya nyumba hiyo. Kwa sababu mvua ilianza kunyesha na ardhi kuanza kulowanishwa na maji, Nahra hakujali, akakaa chini na kuendelea kulia.

    Katika maisha yake yote, hicho kilikuwa kipindi kigumu kuliko vyote, hakuamini kama kweli wazazi wake walimfukuza kama mbwa kisa tu alizaa na mwanaume mweusi. Hata kama alikuwa Muhindi, akajikuta akianza kuwachukia Wahindi wote kwa kile alichokuwa amefanyiwa.

    “Sitorudi tena nyumbani na sitorudi tena kwa Deo, acha niendelee na maisha yangu,” alisema Nahra na kisha kusimama, akaanza kuondoka.

    Alitembea kwa mwendo wa taratibu, mvua kubwa iliendelea kunyesha na kumlowanisha mno lakini hakusimama sehemu kwani nyumba zote za Masaki zilikuwa za kifahari zilizokuwa na uzio mkubwa.

    Wakati mwingine alijuta kupewa mimba na Deo kwa kuwa tu jamii yake ilimtenga lakini kuna kipindi aliona kwamba hakutakiwa kujilaumu, kile kilichokuwa kimetokea, kilitokea hivyo alitakiwa kusonga mbele.

    Dakika ziliendelea kusonga mbele, mpaka anafika kituoni, tayari ilikuwa ni saa tano usiku, akakaa hapo na kuanza kusubiri daladala japokuwa mkononi hakuwa na fedha yoyote ile. Baada ya dakika thelathini, daladala ndogo (hiace) ikasimama hapo na kupanda.

    Safari ya kuelekea Magomeni ikaanza, hakuwa na ndugu yeyote lakini kitu pekee alichokitaka ni kufika huko tu. Mawazo yalimtawala, hakujua ni sehemu gani alitakiwa kwenda kuishi. Huku akifikiria ni wapi alitakiwa kwenda, kichwani mwake likaja jina la mwanaume mmoja, huyu aliitwa Mithun, mwanaume wa Kihindi ambaye alimpenda lakini alimkataa kwa sababu alikuwa na Deo.

    “Nitakwenda Kariakoo kwa Mithun, nitamuomba anisaide,” alijisemea Nahra.

    Alipofika Magomeni, akadaiwa nauli lakini hakuwa nayo. Kondakta hakuwa mkorofi, kwa muonekano wa Nahra alionekana kuwa na matatizo, akamruhusu kuondoka, safari ya Kariakoo ikaanza huku ikiwa ni saa nne usiku.

    Akaanza kutembea kwa miguu, sehemu pekee aliyokuwa akiihofia ilikuwa ni Jangwani tu. Huku akiwa amefika maeneo hayo ya hatari, mbele yake akawaona vijana wawili wakiwa wamesimama, naye akasimama, ila kabla hajafanya kitu chochote, akashtukiwa akipigwa kofi moja zito kwa nyuma.

    Wakati anaugulia maumivu, akajikuta akibebwa msobemsobe na kuingizwa vichakani, wanaume wengine wanne waliokuwa na pensi walikuwa wakimsubiri huku wakionekana kuwa na tamaa ya ngono, walitaka kumbaka Nahra. Alijaribu kupiga kelele ili asaidiwe lakini hakukuwa na msaada wowote ule.

    Nahra aliendelea kupiga kelele, wanaume wanne waliokuwa wamesimama mbele yake walikuwa wakihangaika kufungua bukta zao huku wakizichana nguo zake. Hakukuwa na mtu yeyote aliyesikia kelele hizo alizokuwa akipiga japokuwa zilitoka kwa sauti ya juu.

    “Naanza mimi,” alisema mwanaume mmoja.

    “Fastafasta, usinogewe na mtoto wa Kihindi,” alisema jamaa mwingine.

    Usiku huo ulikuwa ni usiku wa kuumiza mno maishani mwake, wanaume hao wanne wakaanza kumuingilia kinguvu tena kwa zamu. Alipomaliza huyu, alikuja yule.

    Nahra alisikia maumivu makali, kiuno chake kikaanza kukaza, kelele alizokuwa akizipiga, zikaanza kupungua kwani kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo alivyokuwa akiumia zaidi.

    Hakuchukua muda mrefu, huku akiendelea kuingiliwa kichakani pale, mbele yake akaanza kuona giza, akajitahidi kuyafumbua macho yake, haikuwezekana, hapohapo akapoteza fahamu huku wanaume wale wakiendelea kumuingilia kama kawaida, tena kwa zamu.



    Deo alikuwa kimya chumbani kwake, machozi yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake, hakuamini kile kilichotokea, kumfukuza Nahra nyumbani kwake kilikuwa moja ya vitendo kilichomuuma mno.

    Alimpenda Nahra kwa mapenzi ya dhati, hakuwa tayari kumuona msichana huyo akipata shida yoyote ile, japokuwa alikuwa msichana wa Kihindi, kwake haikuwa tatizo, alikuwa akimpenda hivyohivyo.

    Wazazi wa Nahra walionekana kuwa tatizo kwake. Mara baada ya kumpa mimba msichana huyo na kuhamia kwake kwa kuwa wazazi wake walimfukuza, wazazi hao wakawatuma wanaume wawili waliokuwa na bunduki, walichokuwa wakikitaka ni kuona Deo akimfukuza Nahra nyumbani hapo, vinginevyo, wangemuua.

    Huo ulikuwa mtihani mkubwa maishani mwake, alimpenda Nahra, hakutaka apate tabu yoyote ile, kitendo cha kuambiwa amfukuze msichana huyo kilikuwa kigumu, akakataa.

    Watu hao walipoona kwamba kitu hicho hakikufanyika, wakarudi kwa mara ya pili, wakati huu walionekana kuwa na hasira zaidi, kila walipomwangalia Deo usoni, waliyakumbuka maneno ya mzee Patel ambaye aliwaambia wamuue tu.

    “Kijana, fanya tunachokwambia. Tumeagizwa tuje kukuua, hatuwezi, tunakuonea huruma. Fanya hivyo, tunakupa siku moja ya ziada, kesho tukija, tunakuja na sura tofauti na hizi,” alisema mwanaume mmoja huku akimwangalia Deo usoni.

    Kwa jinsi walivyoonekana, kwa maneno yao yaliyowatoka midomoni mwao ilionyesha kabisa watu hao walimaanisha kile walichokiongea, Deo akakubaliana nao kishingo upande.

    Siku hiyo usiku ndiyo ilikuwa siku ya kumfukuza Nahra nyumbani hapo. Alifanya hivyo huku moyo ukimuuma mno, kila alipomwangalia msichana huyo, alijisikia huruma, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali.

    “Nahra, naomba unisamehe, sikutaka kukufukuza, wazazi wako ndiyo waliolazimisha kufanya hivi, ninakupenda Nahra,” alisema Deo huku akimuona Nahra akikimbia, machozi yalikuwa yakimmbubujika msichana huyo, baada ya hapo, hakujua Nahra alikimbilia wapi, usiku huo, kwake ukawa usiku wenye mateso mengi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nitamtafuta tu,” alisema Deo huku akijipa uhakika kwamba angeweza kumuona tena Nahra aliyekuwa na mimba yake.

    ****

    Nahra alikuja kupata fahamu asubuhi, alikuwa katika majani yenye unyevuunyevu, mwili wake ulikuwa ukimuwasha. Pamoja na kuwashwa huko, alikuwa akisikia maumivu makali chini ya kitovu.

    Akaanza kujiuliza sababu ya yeye kuwa mahali hapo, hakukumbuka kitu chochote kile, alibaki akishangaa mpaka kumbukumbu zilipokaa sawa na kuanza kukumbuka kila kitu kilichotokea usiku uliopita, Nahra akaanza kulia, akajiangalia, sehemu zake za siri zilikuwa zimeharibiwa vibaya, akaendelea kulia mfululizo huku akijiinua kuelekea barabarani.

    Kila mtu alibaki akimshangaa, alionekana msichana mrembo mno lakini muonekano wake ulikuwa tofauti kabisa, alikuwa msichana mchafu mno, kwa jinsi uzuri wake ulivyokuwa, hakutakiwa kuwa kama alivyokuwa.

    “Hata kama nimechafuka na hata kama nimebakwa, bado ninahitaji kumuona Mithun, ni lazima nimfuate na anisaidie, sina kimbilio jingine zaidi yake,” alisema Nahra.

    Kila alipopita, watu walimshangaa, hakuwa akitembea kawaida, alikuwa akichechemea kama mtu aliyekanyaga mwiba. Alitembea hivyohivyo mpaka alipofika maeneo ya Fire ambapo akaunganisha mpaka Mtaa wa Twiga, mtaa uliokuwa na maghorofa mengi, huko ndipo alipokuwa akiishi Mithun.

    “Mungu, naomba Mithun anikubalie, anisamehe kwa kila kitu niweze kuwa naye, asahau kila kitu kilichotokea maishani mwetu,” alisema Nahra, tayari alikuwa amefika katika mlango wa nyumba ya kina Mithun, akaanza kugonga mlango, moyo wake ulijawa hofu.

    Wala hazikupita dakika nyingi, mlango ukafunguliwa, mtu aliyekuwa akimuhitaji ndiye aliyefungua mlango, alikuwa Mithun.

    Mwanaume huyo alibaki akimwangalia Nahra huku uso wake ukiwa kwenye mshangao mkubwa. Hakuamini kama yule aliyesimama mbele yake alikuwa Nahra yule aliyekuwa akimfahamu au alikuwa mtu mwingine.

    Alikuwa mchafu mno, nguo zake zilikusanya majanimajani huku zikiwa zimetapakaa tope, kwa kumwangalia tu, Mithun alijisikia kinyaa.

    “Nikusaidie nini?” aliuliza Mithun huku akijitahidi kujizuia kupumua kupitia pua yake, maji yaliyokuwa yameilowanisha nguo ya Nahra, yalikuwa yakinuka.

    “Naomba unisamehe,” alisema Nahra huku akijitahidi kupiga magoti chini.

    Alikuwa akilia kwa maumivu makali, alijua kwamba alifanya makosa kumkataa mwanaume huyo aliyekuwa na lengo la kumuoa na kumkubali Deo aliyekuwa amemfukuza kama mbwa.

    Macho yake yalionyesha kila kitu, alikuwa akiomba msamaha lakini Mithun hakujali. Alikumbuka vema kila kitu kilichotokea katika maisha yake ya nyuma na binti huyo.

    Alimpenda Nahra na kuahidi kumuoa lakini maamuzi ya msichana huyo yalikuwa kwa Deo, mwanaume mweusi aliyempa mimba na kumtimua.

    “Unanuka Nahra,” alisema Mithun maneno yaliyomuumiza mno Nahra, ila kwa kuwa alikuwa na uhitaji, akavumilia.

    “Naomba unisamehe Mithun.”

    “Nikusamehe ili iweje? Na hicho kitumbo ukipeleke wapi? Nikusamehe wewe? Ulivyonikataa kwa maneno ya dhihaka! Nahisi umepotea njia. Kwanza unanuka sana, hivi ulioga jana?” alisema Mithun na kuuliza kwa dharau.

    Kilio cha Nahra kikaongezeka zaidi, hakuamini kama maneno yale yote yalitoka Mithun. Alijitahidi kuomba msamaha lakini matokeo yale aliambulia maneno ya kejeli tu, hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, akaondoka zake huku akilia.

    “Nitakwenda wapi mimi? Nitaishi vipi mimi? Bora nikajiue tu, siwezi kuendelea kuishi,” alijisemea Nahra na huku akipiga hatua kuelekea nje ya ghorofa hilo.

    Huo ndiyo ulikuwa uamuzi alioufikia, hakutaka kuendelea kuishi tena, mateso na maumivu aliyoyapitia yalitosha kabisa kumfunza, hivyo alitaka kujiua kwa kuamini kwamba angekwenda kupumzika.

    Akaanza kukimbia kuelekea Kariakoo Relini huku lengo lake kubwa ni kwenda Mivinjeni. Hakukuwa na kitu alichokifikiria zaidi ya kujiua tu, alitaka kuiondoa roho yake kwa kulala kwenye reli na treni kupita juu yake.

    Mara baada ya kufika Kariakoo Relini, akachukua Barabara ya Kilwa na kunyoosha nayo kama alikuwa akienda Bandarini. Alipofika Mivinjeni, akaanza kuelekea katika reli iliyokuwa chini ya daraja ambako kulikuwa na vyumba vingi vya reli ya kati.

    “Nitajiua tu,” alijisemea Nahra na kujibanza sehemu huku akisubiria treni ipitie na yeye kulala relini. Aliyachoka maisha yake hiyo ndiyo sababu iliyompelekea kutaka kujiua siku hiyo. Hakutaka kuendelea kuishi na wakati watu wote aliokuwa amewaamini hawakutaka kuishi na yeye.

    Moyo wake ulimuuma, hakukuwa na kitu kingine alichokiona kuwa suluhisho la maisha yake zaidi ya kujiua tu. Alidhamiria kufanya hivyo kwa kuamini kwamba asingeweza kuumizwa tena, asingeweza kulia tena, huko atakapokuwa, angeishi maisha matamu milele na kuepuka ghadhabu za dunia hii.

    “Pooooooo,” ilisikika honi ya treni ya mizigo, alipoisikia honi hiyo, akachungulia kwa jicho moja kutoka pale ukutani alipojibanza. Treni ile ya mizigo ilikuwa ikija kwa kasi.

    Ilikuwa imetoka kituoni na kuanza safari yake, alipoiona treni hiyo kwa mbali, Nahra akasubiri mpaka ikaribie na ndiyo aende kujilaza relini na hatimaye aweze kufa na kuyaepuka mateso aliyokuwa akiyapata.

    “Nisamehe Mungu! Mateso yamezidi, acha tu nijiue ili wazazi wangu wapumzike, wasinichukie tena. Pia nisamehe kwa kukiua hiki kiumbe unachokitengeneza tumboni mwangu. Mungu, sifanyi hivi kwa kupenda, najua unayajua maisha ninayopitia,” alisema Nahra huku treni ile ikiendelea kusogea zaidi.

    Nahra aliendelea kuisubiria,treni ilibakisha kama hatua mia mbili kabla ya kufika pale alipotaka kujilaza. Kichwa chake kilitawaliwa na mawazo tele, alikuwa tayari kujiua lakini si kuendea kuishi kwa mateso kama aliyokuwa akiishi.

    “Bora nife tu, sina haja ya kuendelea kuishi,” alisema Nahra.

    Baada ya sekunde kadhaa, treni ilikuwa mbali kama hatua mia moja, alichokifanya Nahra, akakimbilia relini na kujilaza. Machozi yalimbubujika mashavuni mwake, hakuamini kama maisha yake yote aliyokuwa akiishi, mwisho wa siku alikuwa amefikia hatua ya kujiua.

    “Nisamehe Mungu, sikupenda kujiua, ila sina jinsi. Acha nife na mwanangu aliyepo tumboni,” alisema Nahra, treni ya mizigo ilikuwa ikija kwa kasi, na ilibakisha hatua arobaini tu za miguu ya binadamu kabla ya kumkanyaga pale relini alipokuwa amelala. Muda wote treni ilikuwa ikipiga honi lakini Nahra hakutoka relini, alidhamiria kujiua kwa kukanyagwa na treni hiyo.

    Huku treni ikiwa imebakiza kama hatua thelathini za miguu ya binadamu huku Nahra akiendelea kulala relini pale na macho yake yakiwa yamefumba, ghafla akashtuka akishikwa mikono na kuanza kuvutwa.

    Hapo, akayafumbua macho yake kuangalia ni nani aliyekuwa akimvuta. Macho yake yakatua kwa kijana mmoja mchafumchafu, aliyevalia pensi ya jinzi chakavu huku mdomoni mwake akiwa na sigara.

    “Toka hapo, njoo huku,” alisema kijana yule huku akimvuta Nahra kutoka katika reli ile.

    Kwa kuwa kijana yule alikuwa na nguvu Nahra akajikuta akitolewa katika reli ile na treni kupita kwa kasi kubwa.

    “Unataka kujiua?” aliuliza jamaa yule huku akimwangalia Nahra machoni, alikuwa akimshangaa tu.

    “Ungeniacha nife, sitaki kuishi, naomba uniache nife,” alisema Nahra huku akilia kama mtoto.

    “Hapana. Kwani kuna nini? Mbona msichana mrembo unataka kujiua, hebu nieleze, kuna nini,” alisema kijana yule huku akimwangalia Nahra usoni.

    Kwake, Nahra alikuwa msichana mrembo kuliko mwanamke yeyote aliyewahi kumuona machoni mwake, kitendo cha binti huyo kutaka kujiua kilimshtua mno.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nahra hakusema kitu, alibaki akilia tu. Bado moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, kiu ya kutaka kujiua iliendelea kumkamata moyoni mwake. Lawama zake zote zilikuwa kwa mwanaume huyo aliyemtoa relini, hakujua ni aina gani ya maisha aliyokuwa akiyapitia, hakujua ni jinsi gani moyo wake ulikuwa kwenye chuki kubwa dhidi ya wazazi wake na hata ndugu zake.

    “Kuna nini Mhindi wewe?” aliuliza mwanaume yule.

    “Nataka kufa.”

    “Kwa nini? Umechoka kula ugali?”

    “Hapana kaka, nataka kufa tu.”

    “Hebu kwanza tutoke hapa, unaweza kuniletea msala,” alisema mwanaume yule na kuanza kuondoka mahali pale.

    Wakatoka sehemu ile karibu na reli ile na kwenda juu kulipokuwa na daraja ambapo wakavuka na kuanza kutembea pembezoni mwa Barabara ya Kilwa huku wakielekea Kariakoo Relini.

    Nahra alikuwa akilia tu, alikitamani mno kifo kuliko kitu chochote kile, hakuamini kama kweli mwanaume huyo alikuwa amemuokoa na wakati alidhamiri kujiua.

    Alikasirika, alimkasirikia kijana huyo. Hakutaka kuzungumza chochote kile, machozi yaliendelea kumbubujika tu mashavuni mwake.

    “Nini kinaendelea?” aliuliza mwanaume yule.

    Hapo ndipo Nahra alipoanza kusimulia kile kilichokuwa kimetokea maishani mwake tangu alipoanza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Deo, alipopata mimba iliyompelekea kufukuzwa na wazazi wake na hata ndugu zake ambao hawakutaka hata kumuona.

    Historia ya maisha yake ilimshtua mwanaume yule aliyejitambulisha kwa jina la Issa, naye akajikuta akianza kuwachukia Wahindi.

    “Kwa hiyo hauna pa kuishi?” aliuliza Issa.

    “Sina. Sina chochote katika maisha yangu.”

    “Basi poa, kama vipi wapotezee tu, twende tukaishi gheto kwangu,” alisema Issa kwa lafudhi za kihuni.

    “Unaishi wapi?”

    “Tandale Kwa Mtogole.”

    “Mmmh!”

    “Nini tena?”

    “Gari unapandia wapi?”

    “Hahah! Hapa hakuna gari, tunakwenda kwa ngondi tu, tunazama hapo mbele, tunaibukia Jangwani, tukizama tena Magomeni, tunaibukia Tandale, dakika tano tu, tupo gheto,” alisema Issa huku akicheka, alikuwa akiongea maneno ya mtaani zaidi.

    Kutoka katika maisha ya fedha aliyokuwa akiishi, kutembelea magari, leo hii, kila kitu kilikuwa kimebadilika. Japokuwa Issa alionekana kijana mhuni asiyekuwa na chochote, lakini hakutaka kukataa kwenda kuishi kwake. Hakuwa na kitu, huyo Issa aliyeonekana kuwa mhuni, kwa matatizo aliyokuwa nayo, kwake alionekana kuwa msaada mkubwa. Hivyo akakubaliana naye na kuanza kwenda naye huko Tandale.

    ****

    Alichoka sana, kila wakati alikuwa akipumzika, jua lilimchoma mno huku akitokwa na jasho jingi. Issa hakutaka kujali, bado walikuwa wakiendelea na safari kwa miguu kama kawaida. Alipokuwa akipumzika, Issa alisimama na kumsubiri huku akimtia moyo kwamba ilibakia umbali kidogo kufika Tandale hivyo alitakiwa kuvumilia.

    Kwa muonekano tu, Issa alikuwa kijana masikini asiye na kitu chochote cha maana nyumbani kwake. Alionekana kupigwa mno na maisha na kila alipofikiria kama kijana huyo angekuwa msaada mkubwa kwake, moyo wake ukakataa hilo.

    Walichukua zaidi ya saa moja na nusu, wakafika Tandale Kwa Mtogole. Chumba kilikuwa shaghalabaghala, hakikuwa na mpangilio, kilionekana kwamba kwa zaidi ya mwezi mzima hakukuwa na usafi wowote uliofanyika.

    Nahra akashusha pumzi ndefu, muonekano wa chumba kile uliomchosha mno. Aliyaonea huruma maisha yake, hakuamini kama kuanzia siku hiyo hapo ndipo alipotakiwa kuishi.

    “Hapa ndiyo gheto, karibu sana mrembo,” alisema Issa huku akiachia tabasamu pana.

    “Mmmh! Kuzuri,” alisema Nahra, harufu mbaya ya chumbani mule, ikaanza kuiumiza pua yake. Hilo wala hakujali sana, alichokuwa akikihitaji, ni sehemu ya kuishi tu.



    Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo moyo wa Deo ulivyozidi kuuma, hakuamini kama tayari msichana aliyempenda kwa moyo wote, Nahra hakuwa mikononi mwake tena.

    Moyo wake ulikuwa kwenye majuto makubwa, japokuwa alipewa vitisho vya kuuawa endapo tu asingemfukuza Nahra lakini kumuachia likaonekana kuwa kosa kubwa kwake kwani hata kama angemchukua na kuondoka naye kwenda kuishi sehemu nyingine, aliamini watu hao wasingeweza kumpata.

    Hakutaka kukaa nyumbani, alijiona kuwa na uhitaji mkubwa wa kumtafuta msichana huyo aliyeondoka nyumbani kwake usiku wa saa mbili.

    Alichokifanya siku hiyo ni kuondoka nyumbani, sehemu ya kwanza ambayo ilimjia kichwani mwake ni kwenda kumuulizia nyumbani kwao, Msasani.Alipofika huko, mtu wa kwanza kabisa kuonana naye alikuwa mlinzi, Chichi.

    “Namuulizia Nahra,” alisema Deo huku akionekana kutokuwa sawa.

    “Daah! Deo, hata salamu?”

    “Nimechanganyikiwa kidogo. Mambo vipi!”

    “Poa. Nahra hayupo.”

    “Hayupo! Si alikuja hapa jana usiku? Chichi, usinifiche bwana, mimi mweusi mwenzako, naomba uniitie Nahra,” alisema Deo huku akionekana kutokuwa sawa kabisa, alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.

    “Deo, siwezi kukuficha kitu, mbona zamani nilikuwa nakuitia freshi tu. Jana Nahra alikuja hapa home, mdingi wake aliwaka kinoma, akamtimua kama mbwa,” alisema Chichi.

    “Unasemaje?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo hivyo. Mzee katili sana, alimfukuza kama hamjui. Hapa unaweza kuniletea msala, mzee akikuona anaweza kukuua na kunifukuza kazi, kama vipi wewe jiachie tu,” alisema Chichi.

    “Sawa. Haina noma, niende wapi sasa? Nikamtafutie wapi?”

    “Sijajua. Popote pale wewe nenda tu,” alisema Chichi, akaingia ndani na kufunga geti.

    Deo akabaki nje, alichanganyikiwa, hakujua ni wapi alitakiwa kuanzia kumtafuta msichana wake, bado alichanganyikiwa mno na hakujua mahali alipokuwa msichana wake aliyekuwa na ujauzito wake.

    Hakuwa na jinsi, kwa sababu alitakiwa kuondoka na hapo nyumbani ndiyo sehemu pekee ambayo aliamini angeweza kumkuta Nahra, akaondoka zake na kurudi nyumbani huku uso wake ukiwa na huzuni mno.

    *****

    Maisha hayakuwa ya kawaida, kuishi na mtu ambaye hakuwa na malengo yoyote yale zaidi ya kuendekeza pombe na kuishi kwa kuuza vyuma chakavu, yalikuwa maisha magumu mno.

    Issa hakuwa mwanaume aliyekuwa akimhitaji, lakini kwa wakati huo, hakuliangalia hilo, aliona ni bora kuishi naye hivyohivyo tu kwani hakuwa na sehemu nyingine ya kwenda, kama kwa mpenzi wake, alifukuzwa, kwa wazazi wake ndiyo kabisa hawakutaka kabisa kumuona, hivyo hapo kwa Issa kulionekana kuwa msaada mkubwa wa maisha yake.

    Tofauti na matarajio yake, Issa hakumtaka kimapenzi hata siku moja, kila siku walikuwa wakilala wote lakini hakukuwa na siku aliyokuwa akimgusa kitu kilichomfanya Nahra kufikiria vibaya.

    Marafiki wa Issa hawakukauka, uzuri wa Nahra ulikuwa gumzo mtaani, kila wakati, wanaume walifika nyumbani hapo na mtu pekee waliyekuwa wakitaka kumuona alikuwa Nahra tu.

    Issa alikuwa mkali kwa kila mwanaume aliyemtaka Nahra, hakutaka mtu yeyote amuingilie msichana huyo na wakati alikuwa kwenye ngome yake. Wapo waliokuwa wakimfuata kwa pesa ili awaunganishie wawe naye lakini vyote hivyo, Issa aliendelea kukataa.

    Siku ziliendelea kukatika, miezi ikasonga mbele mpaka tumbo la Nahra kuanza kuonekana. Hapo, Issa aliendelea kuhangaika zaidi, hakutaka kukaa nyumbani, alijitahidi kutoka kwenda mihangaikoni ili kuhakikisha kwamba chakula kinapatikana cha kutosha kwa ajili ya Nahra aliyekuwa mjauzito.

    Baada ya miezi tisa kutimia, Nahra akajifungua mtoto mzuri wa kike ambaye alimpa jina la Latifa. Japokuwa alikuwa mtoto mdogo, uzuri wa sura yake haukuweza kujificha, alipokuwa akicheka, akitabasamu na hata kulia, bado uzuri wake ulikuwa palepale.

    “Amechukua sura yako, mmmh! Katoto kazuri,” alisema Issa huku akimwangalia Latifa.

    “Ahsante.”

    “Kwa hiyo ndiyo baba yake alimkataa?”

    “Ndiyo.”

    “Duuh! Makubwa.”

    Kila alipomwangalia mtoto wake, Latifa, Nahra aliumia, mawazo juu ya Deo yakaanza kumtawala. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali hakuamini kama mtoto aliyekuwa amezaliwa alikataliwa na mwanaume aliyezaa naye.

    Siku zikakatika na mawazo kuzidi kumuumiza. Latifa alipofikisha kipindi cha miezi miwili tu, Nahra akaanza kuvuta sigara na kunywa pombe za kienyeji, hakufanya hayo kwa kuwa alipenda, alijitahidi kuyaondoa mawazo juu ya Deo kwa kuwa mlevi na mvutaji.

    Sigara na pombe ya kienyeji, gongo hazikumpenda, ghafla, tena ndani ya miezi mitatu tu, afya yake ikaanza kubadilika, mwili ukaanza kupungua na vipele kuanza kumtoka.

    Afya ikazidi kudhoofika zaidi, na mwisho wa siku, akabaki mifupa mitupu, gongo aliyokuwa akiinywa, iliuteketeza mwili wake.

    Mwili uliendeea kupungua kila siku, sehemu yake kubwa aliyokuwa akiishi kwa wakati huo ilikuwa klabuni tu. Japokuwa Issa alikuwa mlevi na mvutaji sigara mzuri lakini kwa Nahra alionekana kuwa zaidi yake.

    Uzuri wake haukupungua japokuwa mwili wake ulichoka mno kutokana na unywaji wa pombe za asili na uvutaji sigara. Maisha yake yakazidi kupoteza dira, wale waliokuwa wakimfuatilia, hawakumfuatilia tena, walevi aliokuwa akinywa nao klabuni ndiyo waliopata nafasi ya kumchukua na kufanya naye mapenzi.

    Kwa sababu hakuwa na fedha, mlevi yeyote yule aliyemsaidia kiasi cha shilingi mia tano kwa ajili ya kununua kikombe kimoja cha gongo, naye alikuwa akimuweka kwenye foleni ya kufanya naye mapenzi usiku ndani ya choo cha klabuni hapo.

    Kwa Latifa, hakupokea malezi bora, kila siku aliachwa nyumbani na hata kama ilitokea siku mama yake kumchukua na kwenda naye klabuni, alipolilia maziwa, alipewa kiasi cha pombe kunywa.

    “Wewe mwanamke, utamuua huyo mtoto! Unampa gongo!” alisema mlevi mmoja, alikuwa akimwangalia Nahra kwa mshangao.

    “Achana na mimi, usifuatilie maisha yangu, fanya kilichokuleta,” alisema Nahra huku akiona kila kitu alichokuwa akikifanya kuwa sawa.

    Walevi wengine hawakupenda kuona jambo hilo likiendelea kutokea, walichokifanya ni kumwambia Issa ambaye alionekana kuchukizwa na kitendo hicho na hivyo kumchukua Latifa na kumpeleka kwa dada yake, Semeni aliyekuwa akiishi Manzese Midizini.

    Pombe zilizidi kumkolea Nahra, wakati mwingine hakuwa akirudi kabisa nyumbani, pombe zilimkolea na kulala hukohuko klabuni.

    Issa alikuwa kwenye wakati mgumu, japokuwa alimchukua mwanamke huyo kwa ajili ya kumsaidia lakini kwa kipindi hicho, kwa kiasi fulani alikuwa akijuta.

    Kila siku ilikuwa ni lazima kumfuata Nahra klabuni na kumrudisha nyumbani, japokuwa lilikuwa zoezi gumu kwake lakini hakuwa na jinsi, alifanya kila kinachowezekana kuhakikisha Nahra analala nyumbani kwake.

    Mwaka wa kwanza ukakatika, Nahra aliendelea kubaki katika hali ya ulevi mkubwa, na mpaka mwaka wa pili unaingia, tayari alikuwa mnywaji mkubwa kuliko wanywaji wote waliomtangulia.

    “Mtoto wangu yupo wapi?” aliuliza Nahra, mwili wake ulikuwa umekonda mno huku ukiwa na vipele vingi.

    “Yupo kwa dada yangu. Ameanza shule, usihofu kitu chochote kile,” alijibu Issa.

    “Nataka kumuona mtoto wangu,” alisema Nahra kwa staili ya kulalamika.

    “Utamuona tu. Usijali.”

    “Lini?”

    “Wewe unataka lini?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Leo.”

    “Kwa leo haitawezekana. Tufanye keshokutwa,” alisema Issa.

    Siku ziliendelea kukatika, Issa hakutaka kumruhusu Nahra kumuona mtoto wake. Alijua fika kwamba alifanya makosa lakini alijaribu kuepuka matatizo ambayo yangeweza kutokea endapo tu mwanamke huyo angekutana na mtoto wake.

    Nahra hakuacha kumuulizia Latifa, kila siku ilikuwa ni lazima amuulize Issa kuhusu mtoto wake na jibu lake lilikuwa lilelile kwamba angekwenda naye Manzese kumuona.

    Mwezi wa kwanza ukakatika tangu amuulizie Latifa, mwezi wa pili na wa tatu ikakatika na hatimaye mwaka mzima kukatika. Afya yake iliendelea kuzorota huku vipele vikiendelea kumsumbua mwilini mwake.

    “Twende hospitali,” alisema Issa.

    “Hapana. Siwezi kwenda.”

    “Kwa nini?”

    “Naogopa sindano.”

    “Hapana. Utakwenda tu.”

    Afya ilikuwa yake lakini kwenda hospitali ilikuwa mbinde. Alichokifanya Issa ni kumbeba na kuanza kuondoka naye kinguvu. Muda wote Nahra alikuwa akilalamika kwamba hakutaka kwenda hospitalini lakini Issa hakujali, aliendelea kumbeba mpaka walipofika katika Hospitali ya Halmashauri, Tandale.

    “Apelekwe Muhimbili kwa vipimo zaidi,” alisema daktari mwenye sura ya upole na huruma, Dk. Mariamu.

    Issa hakuchoka, kwa sababu alikuwa na kiasi fulani cha fedha, akachukua bajaji na safari ya kuelekea Muhimbili kuanza. Walipofika huko, vipimo vikachukuliwa na Nahra kuonekana kuwa na ugonjwa hatari wa UKIMWI.

    Hiyo ilikuwa taarifa mbaya kwake, msichana aliyekuwa na mvuto kiasi cha kuwatetemesha wanaume wengi, leo hii alikwisha kabisa na kuambukizwa ugonjwa hatari wa UKIMWI.

    Nahra alilia sana lakini kilio chake hakikubadilisha kitu, mtu pekee aliyekuwa akimfariji alikuwa Issa tu.

    Siku zikaendelea kukatika, vipele vikaongezeka mwili huku ukiendelea kupungua mpaka kufikia hatua ya kuanza kupata mabakabaka fulani mwisho wa siku nywele zake kuanza kunyonyoka, zote hizo zilikuwa dalili za ugonjwa hatari wa UKIMWI.

    Nahra aliendelea kuisha, aliharibika na kila siku alikuwa mgonjwa. Japokuwa kila siku alitamani sana kwenda klabuni kulewa lakini kwa hatua aliyofikia, hakuwa na nguvu za kuweza kusimama. Akawa mtu wa ndani tu.

    “Ninakufa Issa, ninataka kumuona mtoto wangu,” alisema Nahra huku akitia huruma kitandani.

    Issa hakuwa na cha kufanya, ni kweli kwa muonekano aliokuwa nao alionekana kutokuwa na muda mrefu kuendelea kuishi, alichokifanya ni kwenda kumchukua Latifa na kumletea.

    Alikuwa amefanana naye kwa kila kitu kuanzia uzuri na hata ngozi ya mwili. Nahra alibaki akimwangalia mtoto wake tu, machozi yakaanza kumbubujika mashavuni pale alipokumbuka kwamba alikuwa mfu aliye hai.

    Huo ukawa muendelezo wa mateso aliyoyapata, mara kwa mara alikuwa akiletewa mtoto wake na kuanza kumwangalia, moyo wake ulimuuma, alikuwa akiyauma meno yake kwa hasira na kuwapa lawama zote wazazi wake na Deo ambao walimfanya kuwa hapo.

    Kila kitu kikabadilika, mtu pekee aliyekuwa akiyaangalia maisha yake ya mateso kitandani pale alikuwa Issa tu. Siku zikakatika, mwili wake ulizidi kukonda na vipele kuongezeka, kwa kumwangalia tu, usingebaki kimya, machozi yangekulenga na kusema kwamba Nahra alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakipitia mateso makali.

    “Issa, kama nitakufa, naomba umsomeshe mtoto wangu mpaka chuo kikuu,” alisema Nahra huku akionekana kukata tamaa.

    “Usijali, nitajitahidi, hata kama nitakosa fedha, nitakopa tu.”

    “Issa, nilikwishawahi kukuelekeza nyumbani, si ndiyo?”

    “Ndiyo.”

    “Utaweza kupakumbuka?”

    “Nafikiri nitaweza.”

    “Basi hapo ndipo utakapotakiwa kwenda endapo utapata tatizo lolote kuhusu fedha,” alisema Nahra.

    “Wataweza kunisaidia kweli?” aliuliza Issa.

    “Watakusaidia tu, huyu ni mjukuu wao na si mtoto wao, hana kosa, watakusaidia tu, amini hilo.”

    “Sawa, nitajaribu japokuwa sina uhakika, nikipata tatizo, nitakwenda huko, nisipopata, hawatoniona,” alisema Issa ambaye kila alipomwangalia Nahra, moyo wake ulimuuma mno.

    Siku hiyo Nahra aliongea kwa shida sana, ilipofika saa saba mchana, mateso aliyokuwa akiyapata kitandani yakaisha na kukata roho. Huo ukawa msiba mkubwa kwa Issa, alibaki akilia sana lakini machozi yake hayakuweza kubadilisha kitu chochote kile, Nahra alifariki kwa Ugonjwa wa UKIMWI.

    Alichokifanya Issa ni kuelekea nyumbani kwa kina Nahra, japokuwa alielekezwa juu kwa juu lakini alifanikiwa kufika huko. Mtu wa kwanza kabisa kumpa taarifa za msiba alikuwa mlinzi wa getini, Chichi ambaye aliwapelekea taarifa wazazi wake Nahra.

    “Acha afe, tulimwambia azae na mtu mweusi,” alisema mzee Patel, Mhindi aliyekuwa na roho mbaya.

    Japokuwa Wahindi wengine walipewa taarifa kuhusu msiba wa Nahra lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyejitokeza kwenda huko, walibaki majumbani mwao wakiendelea kuyafurahia maisha.

    Kitendo alichokifanya Nahra cha kukubali kuzaa na mtu mwenye ngozi nyeusi, Deo kiliwachukiza mno, hawakutaka kumuona, hawakumpenda na hata hawakutaka kuufikiria uzao wake, kwao, uzao wa Nahra ukawa ni uzao wenye laana.

    Baada ya kila kitu kumalizika na Nahra kuzikwa, Issa akawa na jukumu kubwa na zito la kumlea mtoto Latifa. Kila alipomwangalia, moyo wake ulimuuma mno kwani sura yake ilimkumbusha Nahra.

    “Wazazi wa Nahra wana roho mbaya sana, wamemkataa Nahra na uzao wake wote,” Issa alimwambia dada yake, Semeni aliyekuwa na jukumu la kukaa na Latifa.

    “Kisa?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kazaa na mtu mwenye ngozi nyeusi, ni hatari sana.”

    Latifa alikuwa mtoto mkimya, hakuwa mtoto wa kulialia kama ilivyokuwa kwa baadhi ya watoto. Hakukuwa na shida ya kumlea, kwa Semeni, alimchukulia kama mtoto wake wa kumzaa, huduma zote alizokuwa akiwapa watoto wake wa kuwazaa, alikuwa akimpa Latifa pia.

    Mwaka wa kwanza ukakatika na wa pili kuingia, Latifa aliendelea kukua huku uzuri aliokuwa nao ukiendelea kuonekana zaidi, ulipofika mwaka wa pili, watu wakaanza kupigishana kelele kwa kudai kwamba Latifa angeweza kuwa mwanamke mrembo kuliko wanawake wote duniani, uzuri wake ulimdatisha kila mtu.

    “Aiseee! Kama malaika!” alisema jamaa mmoja.

    “Kwani ushawahi kumuona malaika?” jamaa mwingine akauliza huku akicheka.

    “Sijawahi, lakini huyu kama malaika, amini hilo.”

    Uzuri wa Latifa ukawa gumzo Manzese nzima, kila aliyekuwa na hamu ya kutaka kumuona mtoto mzuri alikuwa akiambiwa kwenda nyumbani kwa Semeni kumuona Latifa.

    Mwaka wa tatu ulipoingia, Latifa akaanzishwa shule ya chekechea. Miongoni mwa watoto waliokuwa wakimya, Latifa alikuwa mmojawapo, hakuwa mzungumzaji kabisa, hakuwa mtundu, alipokuwa akikaa muda huu, hadi muda wa kutoka alikuwa hapohapo.

    Mbali na ukimya wake, walimu wakagundua kitu kimoja kwamba Latifa hakuwa mtoto wa kawaida, uwezo wake darasani ulikuwa ni wa juu mno. Yeye ndiye alikuwa mwanafunzi wa kwanza kujua kusoma na kuandika japo kwa mwandiko mbaya.

    Uwezo wake huo ukawashangaza walimu wote, hawakuamini kama kungekuwa na mtoto ambaye angeweza kufanya vitu hivyo kwa haraka kama alivyokuwa Latifa.

    Hata mitihani ya shuleni hapo ilipokuwa ikija, Latifa alikuwa akiongoza jambo lililowafanya walimu kumpeleka darasa jingine la juu kwani uwezo wake ulikuwa ni wa kitofauti kabisa. Kwa kifupi tungesema Latifa alikuwa genius.



    Mpaka anaanza darasa la kwanza, Latifa alikuwa mtoto mwenye uwezo mkubwa darasani, katika kila mtihani, alikuwa akifanya vizuri kitu kilichowashangaza sana walimu kwani hakukuwa na mwanafunzi yeyote aliyewahi kusoma shuleni hapo huku akiwa na akili nyingi kama Latifa.

    Mbali na uwezo wake darasani, Latifa alikuwa mtoto mrembo ambaye usingeweza kumwangalia mara moja na kuyaamisha macho yako. Mchanganyiko wake wa rangi ulivichanganya vichwa vya watu wengi kiasi kwamba wengine wakatabiri kuwa angekuwa miongoni mwa wasichana watakaoitikisa Tanzania.

    Miaka ilikatika zaidi, mpaka Latifa anaingia kidato cha kwanza katika Shule ya Wasichana ya Jangwani, uzuri wake uliendelea kuwatikisa watu wengi wakiwepo wavulana waliokuwa wakisoma katika Shule ya Wavulana ya Azania.

    “Kuna demu nimekutana naye, ni mkali balaa, anasoma hapo Jangwani, aisee huyo demu ni shida,” alisikika mwanafunzi mmoja akiwaambia wenzake.

    “Yupo vipi?”

    “Muhindi si Muhindi, Mswahilini si Mswahili, ni noma.”

    “Hahaha! Utakuwa unamzungumzia Latifa.”

    “Latifa! Latifa yupi?”

    “Kuna msichana wa kidato cha kwanza, ni mzuri ile mbaya, halafu ana akili kinoma,” alisema mwanafunzi mwingine.

    Stori juu ya uzuri wa Latifa ndizo zilizokuwa zikisikika, uzuri wake uliendelea kumdatisha kila aliyemwangalia. Watu wakazidi kuambiana kuhusu Latifa kiasi kwamba binti huyo akaanza kupata umaarufu katika shule hizo mbili.

    ****

    Miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakimpenda Latifa alikuwa Ibrahim Musa, kijana mtanashati aliyekuwa akisoma katika Shule Wavulana ya Azania. Kila siku alipokuwa akisikia stori kuhusu Latifa, Ibrahim alihisi moyo wake ukitetemeka kwa mahaba mazito.

    Hisia kali za mapenzi juu ya msichana huyo zikamtawala, kila alipokaa, alimfikiria Latifa na hata katika kipindi cha kuondoka shuleni hapo, hakuwa tayari kuondoka mpaka pale alipomuona msichana huyo.

    Kwa mwaka mzima Ibrahim aliendelea kumfuatilia Latifa, hakuwahi kuzungumza naye, alimuogopa, ni mara nyingi alipanga kumfuata lakini kila alipotaka kumsogelea, mapigo yake ya moyo yalidunda mno na hofu kumjaa. Wavulana wengine walimfuata Latifa lakini mwisho hakukuwa na mvulana yeyote aliyekubaliwa.

    Kila alipowaangalia wavulana waliomfuata Latifa na kujiangalia yeye, alijiona kutokuwafikia hata mara moja. Hakuwa mvulana tajiri, alitoka katika familia masikini ambayo haikuwa na mbele wala nyuma.

    Ibrahim alikuwa kama Latifa, japokuwa alikuwa kijana masikini lakini alikuwa na uwezo mkubwa darasani, katika kila mtihani aliofanya, aliongoza kwa maksi nyingi kiasi kwamba alikuwa gumzo kwa walimu wote.

    “Nataka kuwa daktari, ila daktari bila kuwa na mke mrembo haiwezekani, Latifa atanifaa,” alisema Ibrahim.

    Moyo wake uliendelea kuumia kila siku, kumfuata Latifa na kumwambia ukweli aliogopa sana. Mwaka mwingine ukaingia na kupita, mwaka wa tatu ulipoingia, Ibrahim akashindwa kuvumilia, hakuwa tayari kujiona akiteseka na wakati kulikuwa na mtu ambaye angeweza kuyatuliza mateso yake ya moyo.

    Siku hii alikuwa amejipanga vilivyo, alivalia nadhifu huku akiwa amevipiga kiwi viatu vyake. Aliipanga siku hiyo kuwa maalumu kuzungumza na msichana huyo, kumwambia kila kitu kilichokuwa kikiusibu moyo wake.

    Baada ya kufika shuleni, hakutaka kutoka darasani, alivumilia mpaka muda wa kutoka. Kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele, mapigo yake ya moyo yakawa yanaongeza kasi ya udundaji, alipenda kuonana na Latifa lakini moyo wake ulijawa hofu kubwa.

    Baada ya kengele kutoka, moja kwa moja akaelekea nje ya shule na kusimama barabarani. Macho yake yalikuwa katika geti la shule ile ya wasichana, alikuwa akimsubiria Latifa tu.

    “Leo lazima kieleweke, siondoki mpaka nizungumze naye,” alijisemea Ibrahim.

    Dakika ziliendelea kusonga mbele huku wanafunzi wakiendelea kutoka, alikuwa kama mtu anayewahesabu wanafunzi hao, mpaka mwanafunzi wa mwisho anatoka ndani ya ndani ya shule, Latifa hakuwepo.

    “Mmmh! Hajafika au alipita ila sikumuona?” alijiuliza Ibrahim.

    Hakutaka kuvumilia kusimama nje, alichokifanya ni kuelekea ndani ya shule ile na kukutana na walinzi, akaanza kuwauliza kuhusu Latifa, kwa sababu alikuwa maarufu, halikuwa tatizo.

    “Hauna habari nini?” aliuliza mlinzi mmoja.

    “Habari gani?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ibrahim aliyasikia mapigo ya moyo wake yakidunda kwa nguvu, hofu ikamuingia, akajikuta akianza kusali kimoyomoyo mlinzi yule asimpe taarifa mbaya kuhusu Latifa kwa kuamini kwamba moyo wake ungemuuma sana.

    “Latifa alipata ajali asubuhi, nimesikia hali yake mbaya sana, aligongwa na gari hapo Jangwani na amepelekwa hospitalini huku akiwa hajitambui. Tetesi zinasema kwamba anatakiwa kusafirishwa kupelekwa India kwa matibabu zaidi,” alisema mlinzi yule, Ibrahim akachanganyikiwa.

    “Unasemaje?” aliuliza Ibrahim kwa mshtuko.

    “Ndiyo hivyo, yaani leo watu wamemmisi sana, si unajua alivyokuwa mkali,” alisema mlinzi yule.

    Ibrahim hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alihisi kuchanganyikiwa, alichokifanya ni kuanza kutimua mbio kuelekea Muhimbili kumwangalia, alionekana kama chizi, mapenzi yaliuendesha moyo wake vilivyo.

    ****

    Ulisikika mlio mkubwa wa gari, watu wakapiga mayowe, wengine wakashika vichwa vyao, hawakuamini walichokiona, msichana mdogo aliyevalia sare za shule aligongwa na gari, alirushwa juu, akazungushwa, alipotua chini, hakutingisha, akatulia tuli.

    Damu zilimtoka mfululizo, shati lake jeupe alilolivaa, ilikuwa vigumu kujua kama lilikuwa jeupe au jekundu, lilitapakaa damu hali iliyoonyesha kwamba msichana huyo alikuwa ameumia vibaya.

    Watu waliokuwa pembezoni mwa barabara wakaanza kumfuata, dereva aliyekuwa amemgonga, hakukimbia, akateremka na kumfuata mahali pale alipoangukia. Kila mtu aliyemuona msichana huyo, alishika kinywa chake kwa mshtuko, kwa muonekano, msichana yule alionekana kufariki dunia palepale.

    Kilichofanyika ni kumbeba na kumpeleka katika gari lile lililomgonga na safari ya kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuanza. Hakukuwa na mtu yeyote aliyegundua kwamba msichana aliyegongwa alikuwa Latifa, uso wake ulijaa damu huku akiwa ameumia vibaya kichwani.

    “Mungu wangu! Huyu atakuwa amekufa,” alisema jamaa mmoja huku yeye na wenzake wakiwa garini kumpeleka Latifa hospitali.

    Alipofikishwa hospitalini, akachukuliwa na kupelekwa katika chumba kilichoandikwa Theatre mlangoni, yaani chumba cha upasuaji. Kitu cha kwanza alichofanyiwa ni kuwekewa mashine ya hewa safi.

    “Inatupasa tufanye kitu vinginevyo anaweza kufariki,” alisema daktari mmoja, bingwa wa upasuaji hospitalini hapo, Dk. Lyaruu.

    “Kitu gani?”

    “Mapigo yake ya moyo yapo chini, nipe CPR,” alisema Dk. Lyaruu.

    Hapohapo mashine ya kushtulia mapigo ya moyo, Cardiopulmonary Resuscitation (CPR) ikaletwa na moja kwa moja kuanza kuyashtua mapigo ya moyo ya Latifa ambayo yalikuwa chini mno.

    Kila kitu kilichofanyika mahali hapo, kilifanyika kwa harakaharaka, baada ya kuona kwamba mapigo yake ya moyo yanaanza kurudi katika hali yake, wakamtundika dripu na kuanza kuisikilizia hali yake.

    Tayari wanafunzi walikwishaanza kukusanyika hospitalini hapo, kila mmoja alipatwa na mshtuko, taarifa waliyokuwa wameisikia kwamba mwanafunzi mwenzao aliyekuwa akisifika kwa urembo shuleni, Latifa alikuwa amepata ajali mbaya ya gari iliwashtua mno.

    Hali iliyokuwa ikiendelea hospitalini hapo ilizidi kuwatia hofu wanafunzi kiasi kwamba kila mmoja akabaki akisali kimoyomoyo ili Mungu atende muujiza na hatimaye aweze kurudi katika hali yake ya kawaida.

    “Ubongo wake umetikisika, hili ni tatizo kubwa, hebu subirini, muandaeni, nitarudi sasa hivi kuanza naye,” alisema Dk. Lyaruu.

    Dk. Lyaruu akatoka ndani ya chumba hicho na baada ya dakika chache, alikuwa kwenye chumba kikubwa kilichokuwa kikitumika kwa kufanyia mikutano au vikao vya dharura.

    Jopo la madaktari wanne likakutana, wote walikuwa mahali hapo kwa ajili ya kuizungumzia hali aliyokuwa nayo Latifa. Baada ya kufanyiwa uchunguzi, ripoti zikawekwa mezani na kuanza kujadiliwa.

    “Ni ajali mbaya, ripoti zinaonyesha kwamba ubongo wake umetikisika na damu kuvilia kichwani, kuna vitu vinne vinaweza kutokea kama tusipofanya kitu fulani,” alisema Dk. Lyaruu na kuendelea:

    “Kitu cha kwanza mgonjwa anaweza kupatwa na kichaa, hii ni hatari sana kwa afya yake,kitu cha pili mgonjwa anaweza kupoteza kumbukumbu zake jambo ambalo na jambo la tatu, mgonjwa anaweza kupata kifafa, lakini mbaya zaidi, anaweza kufariki,” alisema Dk. Lyaruu, madaktari wote walikuwa kimya wakimsikiliza.

    Ilikuwa ni taarifa mbaya wasiyoitegemea, msichana mdogo ambaye alipata ajali na kuletwa hospitalini hapo alipatwa na tatizo kubwa lililoashiria kifo chake endapo tu asingeweza kutibiwa kwa ufasaha na kwa haraka.

    Alikuwa msichana mdogo mno kupata mateso kama yale aliyoyapata. Msichana mrembo, mwenye akili nyingi, leo hii alipata ajali mbaya na kuufanya ubongo wake kutikisika.

    “Kwa hiyo ili tuyaokoa maisha yake, ni lazima tulifungue fuvu lake, tuitoe damu hiyo, kama tutashindwa, haina budi kumsafirisha kuelekea nchini India,” alisema Dk Lyaruu, kila mmoja ndani ya chumba kile akashusha pumzi ndefu.

    Kikao hicho cha dharura kikafungwa na kila mtu kuondoka katika chumba hicho. Vichwa vyao vilifikiria ni kitu gani kilitakiwa kufanyika ili Latifa aweze kupona na kurudi katika hali ya kawaida.

    Hawakutaka kumuona akichanganyikiwa au kumbukumbu zake kufutika, hawakutaka kumuona akipatwa na ugonjwa wa kifafa, la zaidi, hawakutaka kumuona akifariki dunia, walitaka kumtibu na mwisho wa siku awe kama alivyokuwa kabla.

    “Dokta, nini kinaendelea?” aliuliza mwanamke mmoja, alikuwa yule dereva aliyemgonga Latifa kwa gari.

    “Subirini kwanza, kuna kitu kinatakiwa kufanyika,” alijibu Dk. Lyaruu huku akiwa na haraka.

    “Nipo radhi kutoa kitu chochote kile, ninahitaji huyu mtoto apone, naomba mumsaidie,” alisema mwanamke yule huku akianza kububujikwa na machozi.

    Alionekana kuchanganyikiwa, kitendo cha kumgonga Latifa kwa gari kilimchanganya. Kila alipokaa, hakutulia, alisimama na kuzunguka huku na kule, alionekana kama chizi.

    Sehemu hiyo ya kusubiria kuwaona wagonjwa hakuwa peke yake, zaidi ya wanafunzi kumi walikuwepo mahali hapo huku kila mmoja akitaka kumuona Latifa, ambaye alikubalika, leo hii alikuwa hospitalini huku akiwa hajitambui.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya dakika ishirini, madaktari watatu na manesi wanne wakaingia ndani ya chumba cha upasuaji. Walipofika, kitu cha kwanza wakashikana mikono kwa kumzunguka Latifa na kuanza kumuomba Mungu kwa dini zao ili aweze kuwasaidia katika upasuaji uliokuwa unakwenda kufanyika ndani ya chumba hicho.

    Kitu cha kwanza walichokifanya ni kumuingiza katika mashine kubwa iliyokuwa na kipimo kiitwacho Magnetic Resonance Imaging (MRI). Hicho kilikuwa kipimo maalumu ambacho hutumika katika kuangalia ni sehemu gani ya ubongo wa mwanadamu iliyokuwa imepata tatizo fulani.

    Hiyo ndiyo ilikuwa hatua ya kwanza kabisa ambayo walitakiwa kuichukua ndani ya mashine ile. Kikamera kidogo ambacho kiliunganishwa na kompyuta iliyokuwa chumbani mule ikaanza kuchukua kile kilichokuwa kikiendelea.

    Kila daktari akashtuka, hawakuamini kama donge kubwa la damu ambalo lilivilia ndani ya ubongo wa Latifa lilikuwa kubwa kiasi kile. Japokuwa waliwahi kupokea wagonjwa wengi wa tatizo kama lile lakini hawakuwahi kumpata mgonjwa aliyekuwa na donge kubwa la damu kama ilivyokuwa kwa Latifa.

    “Hapa kazi ipo, sidhani kama itawezekana,” alisema Dk. Pius, alikuwa mtaalamu mwingine wa upasuaji hospitalini hapo.

    “Ooppss…! Sikujua kama damu inaweza kuwepo kwa wingi kiasi hiki. Hili ni tatizo kubwa, inatakiwa ahamishwe haraka kwenda kwa wataalamu zaidi, vinginevyo, anaweza kufariki,” alisema Dk. Lyaruu.

    Hospitali ambayo ilikuwa vichwani mwao kwa haraka sana ni Ganga Medical Center iliyokuwa nchini India, huko ndipo alipotakiwa kupelekwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji ambao ungegharimu dola elfu kumi, zaidi ya shilingi milioni ishirini.

    “Ni fedha nyingi, atazipata vipi?” aliuliza Dk. Lyaruu.

    “Labda tukazungumze na yule mwanamke aliyemgonga, tukishindwa, tuwaruhusu waandishi wa habari wa Gazeti la Uwazi waitoe taarifa yake gazetini, naamini ataweza kupata kitu chochote kile,” alisema Dk. Pius.

    Walichokifanya ni kumfuata mwanamke yule ambaye muda wote alikuwa mtu wa kulia tu. Walipomwambia kwamba Latifa alitakiwa kusafirishwa nchini India kwa ajili ya matibabu, akakubaliana nao kulipia kila kitu, si milioni ishirini tu, hata ingekuwa mia moja, alikuwa radhi kufanya hivyo.

    Mawasiliano na Hospitali ya Ganga yakaanza kufanyika. Mtoto mwenye sura nzuri, aliyekuwa na akili darasani, aliyetoka katika familia ya kimasikini ambapo mama yake alifariki kwa ugonjwa wa UKIMWI, alihitaji kupelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu ya kuondoa donge kubwa la damu ubongoni mwake, kila kilichokuwa kikiendelea, Latifa alikuwa kwenye usingizi wa kifo, hakufahamu chochote kile.





    Mawasiliano baina ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Ganga ya nchini India yakafanyika na siku mbili baadaye, Latifa, Issa, yule mwanamke aliyemgonga, bi Rachel walikuwa ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Indians Airlines wakielekea nchini India.

    Kama kulia, bi Rachel alilia sana lakini haikusaidia kumuinua Latifa kitandani pale, bado alikuwa amepoteza fahamu, yaani toka alipomgonga kwa gari, hakuwa amerudiwa na fahamu mpaka siku hiyo.

    Safari nzima ya kutoka nchini Tanzania kuelekea India, Latifa alikuwa akipumulia kwa msaada wa mashine ya hewa safi. Kama aliyokuwa amelazwa nchini Tanzania, alikuwa vilevile mpaka walivyokuwa wakiingia nchini India.

    Gari la wagonjwa kutoka Ganga Medical Center lilikuwepo uwanjani hapo na baadhi ya madaktari waliokuja kumpokea Latifa aliyekuwa hajitambui. Mara baada ya ndege kusimama na abiria wote kuteremka, naye Latifa akateremshwa huku akiwa juu ya machela, wakamuingiza ndani ya gari na kuondoka naye.

    Walichukua dakika ishirini njiani, wakafika katika hospitali hiyo ambapo moja kwa moja machela ikateremshwa na kuanza kusukumwa ndani ya hospitali hiyo kwa ajili ya kuanza kazi ya upasuaji ambayo ingewachukua kwa zaidi ya mwezi mzima mpaka kuhakikisha kwamba Latifa amekuwa katika hali nzuri.

    Kabla ya kitu chochote kuanza, madaktari mabingwa wa upasuaji wakakutana katika chumba maalumu na kuanza kufanya mkutano wa dharura. Zaidi ya madaktari saba walikuwa ndani ya chumba hicho, ripoti kutoka nchini Tanzania katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikawekwa mezani na kuanza kuijadili.

    Kikao hicho kilichukua saa moja, kikamalizika na kugundua kwamba Latifa alikuwa amepata tatizo ambalo kitaalamu huitwa Subdural Haematoma, tatizo ambalo husababishwa na mkusanyiko mkubwa wa damu katika ubongo.

    Baada ya kila kitu kuwa sawa, mara moja oparesheni ikaanza kufanyika ndani ya chumba kile. Mlango ulikuwa umefungwa, ukimya ulitawala ndani ya chumba kile, upasuaji ule haukuwa mdogo, sehemu ndogo ya utosini ikachanwa na kisu kikali na kuanza kuangalia ndani.

    Ilionekana kuwa kazi kubwa, madaktari walikuwa wametulia wakiifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa mno. Walichukua saa nane, upasuaji ukakamilika, wakaziba sehemu waliyoiachana huku donge lile la damu likiwa limetolewa.

    “What is going on? What about operation? Is it successful done? We want to see her,” (Nini kinaendelea? Upasuaji ulikuwaje? Ulifanyika kwa mafanikio? Tunataka kumuona) alisema bi Rachel huku akionekana kuwa na wasiwasi.

    “It is successful done, you have to wait for twelve hours, you can go now and be back tomorrow” (Imefanyika kwa mafanikio, mnatakiwa kusubiri kwa masaa kumi na mbili, mnaweza kuondoka na kurudi kesho) alisema daktari aliyetoka katika chumba cha upasuaji ambaye koti lake kubwa lilikuwa na kichuma kilichoandikwa Dr. Patesh Munil.

    Hawakuwa na jinsi, walichokifanya ni kuondoka hospitalini hapo huku ikiwa tayari imetimia saa 2:17 usiku. Kila mmoja alikuwa na mawazo, mioyoni mwao walikuwa wakiendelea kumuombea Latifa aweze kurudi katika hali yake ya kawaida.

    “Mungu naomba umponye!” alisema bi Rachel huku akiwa amepiga magoti chumbani kwake, tayari mashavu yake yalilowanishwa na machozi yaliyokuwa yakimtoka.

    Siku iliyofuata, asubuhi na mapema walikuwa hospitalini hapo. Walitulia katika viti vya watu wanaosubiria wagonjwa, alipotokea Dk. Munil na kuwaona, akawataka kumfuata ambapo akaenda nao mpaka katika chumba kile alicholazwa Latifa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kama alivyoletwa ndivyo alivyokuwa kitandani pale, kila mmoja akashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kuwabubujika mashavuni mwao kwani picha waliyokuwa wakiiona iliwaumiza mno.

    Latifa, binti mrembo na mwenye akili, kichwa chake kilifungwa bandeji huku puani akiwa na mashine iliyomsaidia kupumua.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha waliyokuwa wakiishi, kila siku ilikuwa ni lazima wafike hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali msichana huyo. Siku ya kwanza ikakatika, siku ya pili ikaingia na kukatika, mpaka wiki inamalizika, bado Latifa hakuwa amefumbua macho.

    “Atakufa?” aliuliza bi Rachel.

    “Hapana, hawezi kufa, Mungu wetu ni mkuu, atamponya tu,” alisema Dr. Munil ambaye alionekana kuwa na imani kubwa.

    ****

    Bado Latifa aliendelea kuwa kitandani hapo, kila siku ukimya ulikuwa sehemu ya maisha yake, hakuwa akizungumza kitu chochote kile na hata kula alikuwa akila kwa kutumia mipira maalumu ambayo iliunganishwa puani mwake.

    Kila siku ilikuwa ni huzuni kwao, kwa bi Rachel, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, kila siku alikuwa akimuomba Mungu aweze kumponya binti huyo ili moyo wake urudi kwenye amani kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

    Wiki zikakatika na hatimaye mwezi wa kwanza kumalizika, bado Latifa aliendelea kuwa kitandani pale. Mwezi mwingine ulipoingia, kidogo kwake ikaonekana kuwa nafuu, akaanza kwa kukunja vidole vya mikono yake, manesi waliokuwa ndani ya chumba hicho hawakutaka kubaki humo, wakatoka kwa kasi kumfuata Dk. Munil na kumwambia kile kilichokuwa kimeendelea chumbani.

    “Kuna nini?” aliuliza Dk. Munil.

    “Dokta, dokta, mgonjwa ameanza kukunja vidole vyake,” alisema nesi mmoja huku akihema kama mtu aliyekimbia umbali mrefu.

    “Mgonjwa gani?”

    “Latifa.”

    Dk. Munil hakutaka kubaki ofisini kwake, kwa kasi ya ajabu akachomoka na kuanza kuelekea katika chumba alichokuwemo Latifa. Hakutaka kuamini, mgonjwa huyo alikuwa amekaa kitandani kwa muda wa mwezi mzima bila kutingisha kiungo chochote kile, alivyoambiwa kwamba alikuwa akikunja vidole vyake, alitaka kuhakikisha hilo.

    “Kuna nini?” aliuliza bi Rachel ambaye alikuwa nje ya chumba kile.

    “Subirini.”

    “Kwa nini tusubiri? Manesi walitoka wakikimbia, wewe unatuambia tusubiri! Kuna nini?” aliuliza bi Rachel huku Issa akiwa pembeni akimsikiliza.

    Dk. Munil hakutaka kujibu swali hilo, akaingia ndani kwa ajili ya kujihakikishia kwa macho yake. Alipofika ndani ya chumba hicho, moja kwa moja macho yake yakatua kwa Latifa aliyekuwa kitandani, akayapeleka macho yake katika vidole vyake, kwa mbali vilikuwa vikitikisika.

    “Amepona,” alijikuta akisema Dk. Munil huku akipiga magoti chini na kumshukuru Mungu.

    Alichokifanya Dk. Munil ni kumuita bi Rachel na Issa ndani ya ofisi yake na kuanza kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea ambacho kwao kilionekana kama muujiza mkubwa.

    Kila mmoja alijikuta akimshukuru Mungu kwa matendo makuu aliyoyafanya. Baada ya siku mbili, Latifa akaanza kufumbua macho yake na baada ya siku chache mbele, akaanza kuongea japo kwa sauti ya chini kabisa.

    “Hakupata tatizo lolote?” aliuliza bi Rachel.

    “Hakupata. Tulitegemea angeweza kusahau kila kitu lakini haikuwa hivyo, tukahisi kwamba angeweza kupata ukichaa lakini haikuwa hivyo pia, ni mzima wa afya, hili ni jambo la kumshukuru Mungu sana,” alisema Dk. Munil.

    “Kwa hiyo ni lini hali yake inaweza kutengemaa kabisa?”

    “Hivi karibuni, nadhani baada ya mwezimmoja.”

    “Tunashukuru sana.”

    Waliendelea kusubiria hospitalini hapo huku kila mmoja akitaka kuona Latifa akirudi katika hali yake kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma. Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo hali yake iliendelea kuwa nzuri na baada ya mwezi mmoja iliyosemwa, akaanza kuongea kama kawaida.

    “Ilikuwaje?”

    “Ulipata ajali.”

    “Mungu wangu!”

    “Ila tunashukuru Mungu umepona.”

    “Kwa hiyo hapa nipo hospitali gani? Agha Khan? Mbona Wahindi wengi?”

    “Hapana. Hapa upo India.”

    “Mmmh! Na wewe nani?” alimuuliza bi Rachel.

    Hakutaka kuficha, moyo wake ulikuwa ukimsuta kila alipotaka kukaa kimya. Hapo ndipo alipoamua kumwambia Latifa ukweli juu ya kila kitu kilichokuwa kimetokea, hakutaka kuficha kitu chochote kile, aliamua kumwambia ukweli kwani tayari mtu huyo alikuwa amepona.

    Moyo wa bi Rachel ukaanza kumpenda Latifa. Katika maisha yake yote, alikuwa amepata mtoto mmoja tu ambaye kwa wakati huo alikuwa nchini Marekani akisoma. Jina la mtoto huyo aliitwa Dorcas.

    Mara baada ya kumzaa mtoto huyo, kwa bahati mbaya bi Rachel akapata ajali mbaya ya gari akiwa na mume wake. Mume wake, bwana Michael Mshana akafariki palepale huku yeye akiharibika kizazi chake na kutokuweza kubeba mimba tena.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akaishia kuwa na mtoto mmoja tu, hakupata mwingine tena, huyo ndiye mtoto aliyekuwa akimpenda. Kitendo cha kuwa karibu na Latifa kikamfanya kutamani kuendelea kuishi na msichana huyo, hakujua Latifa alikuwa nani, hakujua kama ana wazazi wake au la, kitu alichokitaka ni kuishi naye tu.

    “Nitamuomba niishi naye, nimsomeshe, nitatumia hata utajiri wangu wote ili mradi afike pale ninapotaka afike. Halafu nilisikia wakisema kwamba yeye ni genius, kama ni kweli, nitampeleka Marekani katika shule ya watoto wenye vipaji akasome, nadhani huko maisha yake yatabadilika,” alijisema bi Rachel, kila alipomwangalia Latifa, alijisikia furaha moyoni mwake. Kuhusu fedha, kwake hakuwa na tatizo lolote lile.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog