Simulizi : Penzi Kabla Ya Kifo
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila mmoja alitaka kushuhudia harusi iliyokuwa ikizungumziwa kila kona, wengine walisema kwamba ingevunja rekodi nchini Tanzania na kujitengenezea historia yake.
Kuolewa kwa Elizabeth halikuwa jambo la kukaa kimya, utajiri na umaarufu wake uliendelea kutikisa barani Afrika kiasi kwamba chochote kile ambacho ungefanya, basi ilikuwa ni lazima kumzungumzia yeye.
Hapo ndipo watu wenye akili zao, watu waliozaliwa kwa ajili ya kutafuta fedha duniani wakaanza kufanya kile walichoamini kwamba kingewaingizia fedha. Jarida la Teenegers lililokuwa likitoka kila mwezi nchini Tanzania likatoa kopi za haraka zaidi ya elfu sabini ambapo mbele kabisa kulikuwa na picha kubwa iliyomuonyesha Elizabeth akiwa na James tena huku wakiwa kwenye mavazi ya harusi, kila aliyeliona jarida lile, aliingiza mkono mfukoni, akatoa fedha na kulinunua.
Wachumba hao walilipwa fedha nyingi na jarida hilo ila kiasi ambacho Teengers waliingiza ni kingi mno kutokana na watu wengi kulinunua. Kila kona ndani ya Tanzania, stori zilikuwa ni harusi ambayo ilitarajiwa kufanyika mwezi mmoja mbele.
Wazungu wengi, hasa wale waliokuwa maarufu duniani wakafika nchini Tanzania, walifika mapema kwani mbali na uudhuriaji wa sherehe hiyo pia walikuwa wakitaka kufanya utalii katika mbuga mbalimbali za wanyama.
Siku zikakatika, Elizabeth akaishi kwa presha kubwa, hakutegemea kwamba muda wa siku chache zijazo angeitwa mke wa mtu fulani. Kila alipokuwa akionana na mpenzi wake ambaye kwa kipindi hicho waliamua kuishi tofauti ili wakumbukane, walizungumzia mambo mengi kuhusu harusi hiyo, namna ambavyo watu watasherehekea.
Bado James hakuamini, kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwake kilionekana kuwa kama ndoto ambapo baada ya muda fulani angeshtuka kutoka usingizini. Alijiona kuwa na fedha nyingi mno, kupitia kiasi cha shilingi bilioni moja alichokuwa amepewa, kikamfanya kufungua biashara zake, fedha zikaanza kuingia.
Alimshukuru Elizabeth kwa kila kitu na ndiyo maana hakutaka kumuacha, aliyabadilisha maisha yake kwa ujumla hivyo alitaka kuishi naye mpaka kifo kitakapowatenganisha.
“Elizabeth...” aliita James.
“Nipo kipenzi.”
“Umebadilisha maisha yangu, siamini kwa kila kitu kinachoendelea,” alisema James kwa sauti ndogo, alionekana kumaanisha alichokuwa akikizungumza.
“Usijali James, nimefanya hivi kwa kuwa ninakupenda sana. Upo tayari kuishi nami milele?” alisema Elizabeth na kuuliza.
“Nipo tayari, naahidi kukupenda maisha yangu yote.
Kila walipokuwa wakikaa, walijikuta wakipendana kwa mapenzi ya dhati, hawakuisha kukumbatiana, walibusiana na kufarijiana kwa kila kitu. Hakukuwa na mtu aliyetaka kuona mwenzake akiondoka mikononi mwake.
Siku ziliendelea kukatika, baada ya siku nyingi kupita, hatimaye ikabaki wiki moja wawili hao kuoana. Hapo ndipo tetesi zile zilizokuwa zikisikika hatimaye zikawa kweli, harusi ile isingefungiwa kanisani kama zilivyo harusi nyingine bali ingefungiwa ndani ya ndege.
“Unasemaje?’ aliuliza jamaa mmoja.
“Harusi inafungiwa kwenye ndege.”
“Jamani! Huyu Elizabeth mbona anafanya kufuru hivi.”
“Hela hizo kaka! Watu wana hela mpaka hawajui wafanye nini,” alisema jamaa mwingine.
Hizo zilikuwa habari nyingine zilizotengeneza vichwa vingi vya habari katika magazeti mbalimbali. Watu hawakuamini kile kilichokuwa kimesikika kwamba harusi hiyo ingefungiwa ndani ya ndege, ilikuwa ni kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, hakukuwa na harusi yoyote ile ambayo iliwahi kufungiwa ndani ya ndege, tena ikiwa angani.
“Nataka niache historia hapa Tanzania,” alisema Elizabeth, alikuwa akiwaambia marafiki zake.
“Tena kweli shosti, watu wamekusakama sana.”
“Ndiyo nimewafungia kazi sasa,” alisema msichana huyo na kugongesheana mikono.
Hicho ndicho kilichoendelea, masaa yaliendelea kukatika kama kawaida, watu wakaendelea kusambaziana habari kuhusu harusi hiyo ambayo ilianza kutikisa hata kabla haijafanyika. Watu wengi wakatoka nchini kwao na kuelekea Tanzania, kila mtu alitaka kujionea mwenye jinsi harusi ile itakavyofana.
Mabilionea mbalimbali, viongozi wa serikali na watu wengine wote walifika nchini humo, hakika harusi ya Elizabeth na James ilitingisha vyombo vingi vya habari.
Baada ya masaa mengi kukatika, hatimaye siku ambayo watu walikuwa wakiisubiria kwa hamu ikawadia. Asubuhiasubuhi mishemishe zikaanza, watu wengi walikuwa radhi kutokwenda makazini mwao lakini walitaka kuhakikisha wanashiriki katika harusi hiyo.
Mchungaji Williams John wa Kanisa la Lutheran lililokuwa New York nchini Marekani akafika nchini Tanzania tayari kwa kufungisha ndoa hiyo iliyokuwa na mbwembwe nyingi, ndoa iliyokuwa na umaarufu mkubwa kuliko zote zilizowahi kufanyika.
Macho ya watu wengi duniani yakawa nchini Tanzania, watu wakataka kufahamu kile kilichokuwa kikiendelea. Wapo waliokuwa wakiponda kwamba haikutakiwa kufanyika harusi kubwa na ya gharama kiasi hicho lakini wapo wengine waliojitokeza na kupongeza.
Watu wakaombwa kukutana katika Kanisa la Praise And Worship lililokuwa Masaki, hapo ndipo ambapo maharusi walipotakiwa kukutana, wachukuane na kuelekea uwanja wa ndege ambapo wangepanda ndege kisha harusi kufungwa angani, baadaye warudi tena kanisani hapo.
Saa 5:29 asabuhi maharusi wakaanza kuingia kanisani hapo, watu waliokuwepo ndani hawakutulia, kelele za shangwe zilisikika, wengine wakasimamasimama na kutaka kuangalia kule nje walipokuwa wakitokea maharusi hao.
Rais wa nchi na mawaziri wengine nao walikuwemo kanisani humo, ulinzi ulikuwa mkubwa kila kona, hakukuwa na mtu aliyekuwa na wasiwasi hata kidogo. Wanawake wa Kichaga wakaanza kushangilia kwa sauti za juu, hawakuamini kama binti yao siku hiyo angeolewa baada ya maneno mengi ya watu.
James hakuwa na wazazi, waliokuwemo kanisani humo walikuwa ndugu zake wengine, wajomba na mashangazi zake. Mbele kabisa alikuwepo mdogo wake, Glory aliyekuwa kwenye kiti chake, aliangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, alitoa tabasamu pana, kitu peke ambacho hakuweza kufanya ni kuutingisha mwili wake kuanzia kifuani kwenda chini.
Maharusi wakaanza kupiga hatua kuingia ndani ya kanisa hilo, walipofika mbele kabisa, mchungaji akasimama na kuanza kuzungumza maneno machache huku pembeni akiwemo mkalimani wake.
Alizungumza kwa muda na ndipo akaomba pete ziletwe, akazishika na kisha kuanza kuzibariki, baada ya hapo akawaambia watu wasubiri ili aende na maharusi hao pamoja na wageni waalikwa uwanja wa ndege tayari kwa kuchukua ndege kisha kufunga harusi ndani ya ndege hiyo.
Hilo halikuwa tatizo, ndani ya dakika ishirini tayari walikuwa maeneno ya uwanja wa ndege ambapo kulikuwa na watu wengi waliotaka kuwaona maharusi hao wakiingia ndani ya ndege tayari kwa kufunga ndoa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila mtu aliyewaona wakiteremka, aliwapiga picha, walionekana kuwa na furaha sana, kila mtu aliyekuwa akiwaangalia, hakuamini kama kweli mmoja wa watu wale alikuwa Elizabeth aliyejaa skendo za kutembea na wanaume wengi, leo hii, eti alikuwa akiolewa.
Waandishi wa habari walifuatilia kila kilichokuwa kikiendela, walitoka nao kanisani na muda huo walikuwa uwanja wa ndege, kwa kuwa walikuwa na vitambulisho maalumu, haikuwa kazi sana, waliruhusiwa kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Baada ya kuteremka kutoka garini, walichokifanya ni kuenda kwenye eneo la uwanja huo huku watu wote macho yao yakiwaangalia kiasi kwamba kwa wale wasiojua kilichokuwa kikiendelea, walibaki wakishangaa tu.
Walipoifikia ndege, hawakutakiwa kuingia, wakaambiwa wasubiri, mchungaji akaingia ndani ya ndege ile, kitu cha kwanza alichokifanya ni kuanza kuibariki ili iwe na utakaso tayari kwa kufungiwa ndoa kisha kuwaruhusu kuingia, watu wengine wakatakiwa kusubiri nje. Walipopanda, ndege ikapaa.
“Angalianeni,” aliwaambia mchungaji na wao kufanya hivyo, wazazi wa Elizabeth, ndugu wa James, rais na familia yake, waziri mkuu na familia yake, wote walikuwa ndani ya ndege hiyo wakifuatilia kila kitu huku vijana wengine watano wakiwa humo kwa ajili ya kuimba.
Mchungaji akazichukua pete zile na kuanza kuziangalia, akawaangalia maharusi wale ambao muda wote walikuwa kwenye tabasamu pana huku wakionekana kutokuamini kile kilichokuwa kikitarajiwa kutokea mahali pale.
“Elizabeth...upo tayari kuolewa na James?”
“Ndiyo nimekubali.”
Alilirudia swali hilo kwa James mara tatu, baada ya hapo, akamgeukia James na kumuuliza swali kama lile, James naye akajibu kama alivyojibu Elizabeth na hivyo kuruhusu wawili hao kuvarishana pete.
Wakati kitendo hicho kikitarajia kufanyika, kila mtu aliyekuwa humo sura yake ilikuwa kwenye tabasamu pana, hawakuamini kama mwisho wa siku msichana huyo alikuwa akiolewa, hata rais, uso wake ulikuwa na tabasamu pana, kwanza kushiriki harusi hiyo, kwake ilionekana kuwa heshima kubwa. Wakajiandaa kuvarishana pete.
“Mchungaji....” alisema Elizabeth, alionekana kama mtu aliyeshtuka jambo fulani, tayari James alikwishamshika mkono wake kwa ajili ya kumvarisha pete.
“Ndiyo Elizabeth!”
“Sitaki kuolewa,” alisema Elizabeth, watu wote waliokuwepo mahali pale wakashtuka.
“Unasemaje?”
“Sitaki kuolewa...” alirudia Elizabeth huku akiutoa mkono wake mkononi mwa James. Kila mmoja akamshangaa.
James akachanganyikiwa.
Hakukuwa na mtu aliyemuelewa, kila mmoja alimshangaa Elizabeth kwa kile alichokisema kwamba hakutaka kuolewa mahali hapo. Wengine walihisi kwamba ulikuwa ni utani lakini walivyomwangalia, hakuonekana kuwa na utani hata kidogo.
Hawakujua tatizo lilikuwa nini, Elizabeth alimaanisha kile alichokuwa akikisema kwamba hakutaka kuolewa. James akabaki akimwangalia, alipokuwa akitania jambo, alifahamu vilivyo na hata alipokuwa akimaanisha, alifahamu pia.
Kwa jinsi alivyokuwa akimwangalia msichana huyo, alionekana kumaanisha kile alichokuwa akikizungumza kwamba hakutaka kuolewa na James jambo lililoendelea kumshangaza kila mtu aliyekuwa ndani ya ndege.
“Unasemaje?” aliuliza mama yake.
“Mama! Sitaki kuolewa.”
“Hapana! Elizabeth! Umechanganyikiwa?”
“Mama! Nina akili timamu, sitaki kuolewa,” alisema Elizabeth, hata rais akamshangaa, naye akasimama na kumuuliza Elizabeth kama alikuwa akimaanisha alichokizungumza, jibu lake likawa lilelile, hakutaka kuolewa.
“Hapana! Nahisi kuna tatizo.”
Elizabeth akachomoka pale alipokuwa na kuwafuata marubani, akawapa amri kwamba ndege iteremshwe haraka iwezekanavyo. Kila aliyemwangalia, alishindwa kuamini kile kilichokuwa kimetokea.
James akamfuata na kumuuliza tatizo lilikuwa nini lakini Elizabeth akabaki kimya tu, hakutaka kuzungumza kitu chochote kile zaidi ya kumsisitizia rubani ashushe ndege chini ili akaendelee na mambo yake.
“Elizabeth....”
“Nimesema sitaki kuolewaaaaaaa,” alisema Elizabeth kwa sauti kubwa, alikuwa akimwambia James.
Ndege ikaanza kushushwa, James akakosa nguvu, akakifuata kiti na kutulia, kijasho kikaanza kumtiririka, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, baada ya safari ndefu iliyojaa furaha, mahaba tele mwisho wa siku msichana aliyetegemea kumuoa alikataa kuolewa, tena katika hatua ya mwisho tu, kabla ya sekunde thelathini kuwa mke wake.
Japokuwa wote ndani ya ndege hiyo walikuwa wakimbembeleza Elizabeth akubali kuolewa lakini hakukubali, aliendelea kuweka msimamo wake kwamba hataki kuolewa, alitaka aachwe na maisha yake.
“Jamani naomba mniache,” alisema Elizabeth.
“Tatizo nini?” aliuliza rais.
“Hapana! Sitaki kuolewa, hilo tu, naomba mniache.”
“Hivi unamaanisha kweli au?”
“Mnanionaje? Mnahisi natania? Mtaona ndege ikitua, hapo ndipo mtakapoamini ninachokisema,” alisema Elizabeth.
Kama kumbembeleza, walifanya hivyo sana lakini mwisho wa siku, alikataa na kusisitizakwamba hakutaka kuolewa kabisa. Glory aliyekuwa kwenye kiti chake, alibubujikwa na machozi, moyo wake uliumia sana kusikia kwamba Elizabeth, mtu aliyekuwa akimpenda mno aliamua kukataa kuolewa na kaka yake.
Watu waliokuwa chini hawakujua kile kilichokuwa kikiendelea ndani ya ndege, walikuwa na furaha, walishangilia kwa kuamini kwamba kila kitu kilikwenda kama kilivyotakiwa. Mara wakaanza kuiona ndege ile ikianza kushuka chini, waandishi wa habari wakaanza kuipiga picha huku kelele za shangwe zikisikika kila kona.
“Wanameremetaaaaa....wanameremetaaaa....” walisikika wanawake wakiimba kwa sauti nyororo.
Ndege iliposimama, mlango ukafunguliwa na hapohapo Elizabeth kutoka. Watu wakaanza kusogea kule ndege iliposimama, msichana huyo alipoanza kushuka ngazi, watu wakapiga mayowe ya shangwe.
Elizabeth hakusimama, alionekana kuwa tofauti kabisa, alionekana kama mtu mwenye hasira nyingi, akaanza kupiga hatua kuelekea kule watu walipokuwa. Hakukuwa na aliyeelewa kilichokuwa kikiendelea, walimshangaa msichana huyo, uso wake haukuonyesha kama mtu aliyetoka kufunga ndoa ndani ya ndege ile, alipowafikia, hakuzungumza chochote kile, akapenya katikati ya watu na kuondoka zake.
“Eeeh! Jamani! Kuna nini tena?” aliuliza mwanamke mmoja.
“Hata mimi nashangaa...” alisema mwanamke mwingine.
Elizabeth hakutaka kukaa ndani ya eneo la uwanja huo, alichokifanya ni kuingia ndani ya gari la maharusi na kisha kumwambia dereva aondoke mahali hapo huku kama kawaida waandishi wakiendelea kupiga picha ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
“Jamani! Nini kinaendelea tena? Mbona hatuelewielewi hapa,” aliuliza mwanamke fulani, alionekana kuwa na mzuka wa kutaka kujua.
“Hata mimi nashangaa aisee...hebu tuwaone wale waliokwenda kwenye ndege,” alijibu mwanaume mmoja, macho ya watu wote yakaelekea katika ndege ile.
Mtu aliyefuata alikuwa rais na familia yake, naye kwa kumwangalia usoni alioekana kutokuwa na furaha kabisa, hakuwa kama alivyokuwa mwanzo wakati anaingia ndani ya ndege ile. Mbali na yeye, familia yake, waziri na familia yake, wote hawakuonekana kuwa na furaha kabisa.
Baada ya wote waliokuwa ndani ya ndege ile kuteremka, mtu wa mwisho kabisa kuteremka alikuwa James, kwa kumwangalia tu ungegundua kwamba hakuwa sawa, macho yake yalikuwa mekundu kutokana na kulia sana ndani ya ndege.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Bado hakuwa akiamini kile kilichokuwa kimetokea, alibaki akiwatazama watu wale waliokuwa mahali pale. Moyo wake uliumia mno. Kuna wakati alikuwa akijutia uamuzi wake wa kuwa na msichana huyo, alijiona kutokuwa mwanaume sahihi wa maisha yake.
Alikumbuka mambo mengi waliyowahi kupitia, mambo yaliyowafanya kufurahi, kuyaona mapenzi yakiwa juu kabisa na wakati mwingine kujiona wakipendana zaidi ya watu wote duniani. Kila alipokuwa akikumbuka kila kitu walichokuwa wamekifanya pamoja, aliumia mno moyoni mwake.
“Kuna nini?” kila mtu aliuliza swali hilo.
“Hakuna harusi,” alijibu mjomba wake James jibu lililoanzisha minong’ono mahali pale.
“Amesemaje?”
“Amesema hataki kuolewa....”
“Eehh! Kwa nini tena?” aliuliza mwanaume mmoja.
Hakukuwa na kitu kilichoendelea, kile alichokisema mjomba wake James ndicho kile kilichokuwa kimetokea, hakukuwa na harusi, bibi harusi alikataa kuolewa huku akiwa ameshika pete mkononi. Kila aliyesikia lile, hakuamini masikio yake, wakati mwingine walifikiria kwamba hayo yalikuwa maigizo tu, ila mbele ya rais, hakika hakukuwa na maigizo yoyote yale.
Maneno hayo yakaanza kusambaa kila kona kwamba Elizabeth alikataa kuolewa na James, hakukuwa na mtu aliyejua sababu, hakukuwa na mtu aliyefikiria jambo hilo kwamba lingetokea kwani kwa jinsi Elizabeth alivyokuwa na hamu ya kuolewa, kwa jinsi watu walivyokuwa wakimsakama, hakika kufanya jambo kama lile lilimshangaza kila mtu.
“Nini kilitokea jamani? Mbona amekataa kuolewa? Au ndiyo anatafuta kiki?” aliuliza mwanamke mmoja.
“Jamani! Cha msingi waulizwe watu waliokuwa mule ndani ya ndege, hakuta ajuaye ukweli wowote ule,” alisema jamaa mwingine.
Magazeti yakaandika sana kile kilichokuwa kimetokea ndani ya ndege, kwa sababu kulikuwa na waimbaji na ndugu za James, wao ndiyo walioelezea kile kilichokuwa kimetokea, kila aliyesikia, alihuzunika sana, alimuonea huruma James kwani waliona ni jinsi gani mwanaume huyo alivyokuwa ameumia.
Watu wengi walimlaumu Elizabeth, alikuwa msichana mpole, mwenye kiu kubwa ya kuolewa, aliyekuwa radhi kutafuta ndoa kwa gharama yoyote ile lakini siku ya harusi, alikataa kabisa kuolewa.
Waandishi wa habari hawakutaka kurudi ofisini, walitaka kujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea, walipenda kuandika kitu chenye maelezo mengi, hivyo walichofanya ni kumtafuta mwanadada huyo mrembo.
Walipofika nyumbani kwake, wakapewa jibu kwamba hakuwepo, alifika nyumbani hapo, akavua shela la harusi kisha kuingia ndani, alipotoka, alitoka na begi dogo kisha kuondoka zake, alipoelekea, hakukuwa na aliyejua.
“Kwa hiyo hamjua amekwenda wapi?” aliuliza Imelda Mtema, mmoja wa waandishi bora kabisa nchini.
“Hatujui kabisa dada yetu,” alijibu mlinzi mmoja.
“Sawa!” alisema Imelda na kuondoka nyumbani hapo.
Moyo wa Rasheed uliumia vilivyo, hakuamini kama kweli alikataliwa na Elizabeth, alichoamua ni kurudi nchini Morocco na kufanya kile alichotaka kufanya. Hakukubali kuona akimkosa msichana huyo mrembo, kwake, ilikuwa ni bora kukosa kitu chochote kile lakini si kumkosa Elizabeth.
Mara baada ya kufika nchini Morocco majira ya saa sita mchana, akawasiliana na rafiki yake, bilionea mwenzake, Abdallahman Saleh na kumuuliza sehemu ambayo angeweza kupata mganga mzuri kwani kulikuwa na kazi kubwa aliyotaka kufanya.
“Kazi gani?” aliuliza Abdallahman.
“Wewe niambie ni nani anaweza.”
“Wapo wengi lakini tatizo ni kwamba hiki ni kipindi kibaya cha kazi,” alisema Abdallahman kwenye simu.
“Kwa nini?”
“Tunasubiri mwezi uandame leo ili kesho tuanze kufunga,” alijibu Abdallahman.
Hapo ndipo kumbukumbu zake ziliporudi na kukumbuka kwamba muda huo Waislamu duniani kote walikuwa kwenye maandalizi makubwa kwa ajili ya mfungo wa Ramadhani ambao ulitarajiwa kuanza siku inayofuatia.
Hakuwa na jinsi, aliuheshimu mwezi huo kuliko kitu chochote kile, alichokiona ni kusubiri ili mwezi uandame na hatimaye kwenda kufanya kazi ile aliyotaka kuifanya. Hakuona njia nyingine, hakuona kama angeweza kumpata Elizabeth kirahisi, alitaka kutumia upande wa pili, kumchanganya msichana huyo mrembo kwa kutumia dawa za kishirikina na hatimaye kumchukua jumla.
Hakuwa na furaha, mwezi huo ambao ulichukuliwa kama kipindi maalumu cha watu kuwa karibu na Mungu, kwake ilionekana kuwa kinyume chake, mawazo juu ya msichana Elizabeth yaliendelea kuuchanganya moyo wake kiasi kwamba kila siku alikuwa mtu wa kutenda dhambi kupitia mawazo yake, yaani kila siku alikuwa mtu wa kufikiria ngono tu kwa Elizabeth.
Alivumilia mpaka mwezi ulipokwisha na ndipo alipompigia simu Abdallahman na kumkumkumbushia kile walichozungumza naye kabla mwezi wa Ramadhani haujaanza. Walichofanya ni kupanga muda wa kuonana ili waweze kulizungumzia suala hilo na kuona ni mganga gani ambaye alitakiwa kufanya kazi hiyo kubwa.
Saa tisa mchana walionana katika Mgahawa wa Allah Akbar uliokuwa katikati ya Jiji la Rabat karibu na msikiti wa Masjid Al Ribat, walikutana mahali hapo kwa ajili ya kuzungumzia jambo ambalo Rasheed alitaka kumwambia mwezi mmoja uliopita.
“Kuna nini?”
“Ninataka unielekeze kwa mtu ambaye anaweza kunisaidia,” alisema Rasheed.
“Kukusaidia nini?”
“Kuna msichana ninamtaka, nimeshindwa kumpata,” alijibu Rasheed.
“Msichana gani?”
“Ni msichana aitwaye Elizabeth, yule bilionea.”
“Ulikuwa ukimtaka?”
“Ndiyo! Ninamtaka mpaka sasa hivi.”
“Si alikuja hapa miezi kadhaa iliyopita, kwa nini hukumwambia?”
“Sikiliza, kuna mengi yalitokea, unaweza kunisaidia kwanza?”
“Hakuna tatizo.”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hilo wala halikuonekana kuwa tatizo, Abdallahman alikuwa akiwafahamu watu wengi alioamini kwamba wangeweza kumsaidia Rasheed kwa kile alichokuwa akikihitaji, alichokifanya ni kumwambia waende sehemu ambayo ndipo kulipopatikana mganga mzuri ambaye aliwafanyia watu kazi zao mbalimbali yakiwemo mazindiko.
Kwa huyo mganga, ndipo viongozi wengi walipokwenda, walihudumiwa na kutatuliwa matatizo yao, wagonjwa walipelekwa na kuponyeshwa na hata wale waliokuwa na majini, walipopelekwa huko, majini yale yalitulizwa.
Aliaminika kuliko waganga wote hapo Rabat, mganga huyu aliitwa Sued Kharim, mmoja wa waganga maarufu sana. Hata Rasheed alipoambiwa kuhusu mganga huyo, hapo ndipo alipopata picha, alilisikia jina hilo, halikuwa geni masikioni mwake.
“Namuamini, nilisikia sana sifa zake,” alisema Rasheed.
Hakukuwa na cha kusubiri, kilichofuata ni kwenda kwa mganga huyo aliyekuwa akiishi pembezoni mwa jiji hilo. Walitumia muda wa dakika arobaini ndipo gari lao likaanza kuingia katika eneo moja kubwa, lilikuwa na michanga mingi, kwa mbali lilionekana kuwa kama jangwa fulani, hapo ndipo alipokuwa akiishi mganga huyo.
Wakasimamisha gari lao na kuanza kuifuata nyumba moja iliyoonekana kutengenezwa kwa maboksi, nje kulikuwa na ngamia watatu wakiwa wamefungwa kamba. Nje ya nyumba ile kulikuwa na watu kama watano, wote hao walikuwa wakisubiri huduma kutoka kwa mganga huyo.
Hawakuteremka, kwa kuwa Sued alikuwa na msaidizi wake, hasa yule aliyekuwa akiwapokea wageni, walipomuona, wakamuita huku wakiwa garini kwani hawakutaka kuonekana na mtu yeyote yule. Msaidizi yule akawafuata.
“Samahani kidogo.”
“Bila samahani.”
“Tunahitaji kumuona mzee, si yupo?”
“Ndiyo!”
“Ila hatutaki tuonekane, sijui unaweza kutusaidia vipi?” aliuliza Abdallahman.
“Nendeni kule nyumba ya nyumba, kuna mlango mwingine wa kuingilia.
“Sawa! Hakuna tatizo.”
Walichokifanya ni kuelekea huko nyuma ya nyumba ile, walipofika, wakaegesha gari na kumsubiria yule msaidizi ambaye akafika na kuwaongoza mahali walipotakiwa kuwa. Aliwafahamu wote, walikuwa mabilionea wakubwa nchini Morocco, akazungumza nao na kuwaambia kwamba angewafuata karibuni na yeye kuondoka.
“Jua kwamba umefanikiwa, huyu mganga ni kiboko,” alisema Abdallahman huku akionekana kumaanisha alichokuwa akikizungumza.
“Nitashukuru sana.”
Msaidizi yule hakuchukua muda mrefu, akawarudia na kisha kuwaambia kwamba mganga Sued alikuwa akiwasubiri wao tu, hivyo wakainuka na kuanza kuelekea huko. Walipofika mlangoni, kitu cha kwanza wakaambiwa waingie kinyumenyume, hilo halikuwa tatizo, wakafanya hivyo.
Hapo ndipo Rasheed akaanza kumwambia mganga kile alichokuwa akikihitaji ambacho kilimpeleka kuwa ndani ya nyumba hiyo. Alimwambia mganga Sued hatua kwa hatua, tangu siku ya kwanza alipokutana na Elizabeth, alivyouchukulia uzuri wake kuwa kitu cha kawaida mpaka pale alipoota ndoto nzuri na kugundua kwamba msichana huyo anaweza kuwa mwanamke wake wa ndoto.
“Ni kazi nyepesi mno.”
“Naomba unisaidie mtaalamu.”
“Hakuna tatizo!”
Mganga Sued akasimama na kisha kulifuata kapu lake lililokuwa pembeni, akatoa tunguli moja kubwa, achana na zile zilizokuwa zimetundikwa kila kona ndani ya chumba kile, hakutoa hiyo tu bali akatoa na hirizi moja nyeusi tii ambapo kwa kuiangalia tu, Rasheed alionekana kuogopa.
“Huwa situmii ushirikina wa kitabu,” aliwaambia na kuendelea:
“Ninaoutumia ni huu wa kutumia tunguli tu, kila kitu kitakuwa sawa, wala msijali,” alisema mganga Sued.
Akachukua karatasi moja nyeupe kabisa na kumwambia Rasheed aandike jina lake na la msichana aliyekuwa akimtaka, akafaya hivyo. Mganga akaichukua ile karatasi na kuyaangalia yale majina, akaanza kuzigawa zile herufi kinyota na mwisho wa siku kupata jibu kwamba majina yale yaliangukia kwenye nyota ambayo haikuwa ngumu kabisa, ilikuwa miongoni mwa nyota nyepesi kuliko zote.
“Ni wepesi mno, sikuwahi kufanya kazi kwa watu wepesi namna hii,” alisema mganga Sued.
“Kwa hiyo tutafanikiwa?”
“Ndiyo! Kwa asilimia mia moja.”
“Nashukuru sana.”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapo ndipo mchakato ulipoanza. Walichukua muda wa nusu saa huku mganga Sued akizungumza maneno yasiyoeleweka, mwisho kabisa akachukua ubani na kuuwasha huku akichukua shuka jeusi na kujifunika kwa lengo la kuzungumza na majini yake, baada ya kutumia muda wa dakika kadhaa, akanyamaza na kuanza kuwaangalia usoni.
“Kinachofuata?”
“Nendeni, kila kitu tayari, atakufuata yeye mwenyewe, ukifanikiwa, inshalaah, unaweza kuniletea chochote kile” alisema mganga Sued na hivyo Rasheed na Abdallahman kuondoka mahali hapo.
Alichokifanya mganga Sued ni kutuma jini mahaba ili liende moja kwa moja kwa msichana Elizabeth na kumvuruiga akili yake juu ya Rasheed. Kweli kioo chake cha kiganga akajiona kufanikiwa, jini lile likamuingia Elizabeth tena ikiwa siku ya harusi, kwake, ulionekana kuwa ushindi mkubwa.
******
“Rasheed! Kwa nini nilikukataa? Kwa nini sikukwambia ukweli kwamba ninakupenda? Naomba unisamehe mpenzi, naomba unisamehe kwa kila kitu nilichokifanya, kwa kukukataa na kuumiza moyo wako,” alisema Elizabeth.
Ndege ilikuwa ikikata mawingu, iliondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya jijini Nairobi. Miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya ndege ile alikuwepo Elizabeth ambaye alionekana kuwa na mawazo lukuki.
Tangu awe bilionea, hiyo ndiyo ilikuwa siku yake ya kwanza kupanda ndege ya abiria, mara zote alikuwa akitumia ndege yake binafsi ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam, ndiyo ile aliyokuwa ameiacha wakati alipokataa kufunga ndoa na James.
Moyo wake ulikuwa kwenye mapenzi mazito kwa Rasheed, alijikuta akimpenda mwanaume huyo kuliko mtu yeyote katika maisha yake. Kama kupenda, kipindi hicho alipenda mpaka hatua ya mwisho kabisa, alijikuta akishindwa kabisa kuvumilia, na wakati huo alikuwa akielekea nchini Morocco kuonana na mwanaume huyo aliyetokea kumpenda.
Hakutaka kuzungumza na mtu yeyote ndani ya ndege, alikuwa kimya huku moyo wake ukiwa na mawazo tele juu ya Rasheed. Kwake, kwa kipindi hicho alionekana kuwa mwanaume mzuri ambaye aliamini kwamba endapo angekuja na kuwa mume wake, hakika angekuwa na maisha mazuri, yenye furaha na upendo wa dhati kuliko kwa mwanamke yeyote yule.
Safari ilichukua saa ishirini na tano na ndipo ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sale uliokuwa hapo Rabat. Iliposimama, abiria wakaanza kuteremka akiwemo Elizabeth ambaye alipitia katika mlango wa watu maalumu.
Alipofika nje, hakutaka kuchelewa, kwa kuwa alikuwa akipafahamu nyumbani kwa Rasheed, akakodi teksi na kuanza kuelekea huko. Kadiri dakika zilivyoendelea kukatika na ndivyo alivyozidi kumpenda mwanaume huyo, alijikuta akishindwa kabisa kukumbuka kile kilichotokea nchini Tanzania, akamsahau James, alichokuwa akikumbuka kwa wakati huo ni Rasheed tu.
Teksi ilichukua dakika kumi ndipo ikafika nje ya nyumba kubwa ya kifahari, gari likaegeshwa nje ya geti lile na kisha dereva kupiga honi, geti dogo likafunguliwa na mlinzi mmoja aliyekuwa na bunduki kutoka nje.
“Nikusaidie nini?’ aliuliza mlinzi huku akiwa hajamuona Elizabeth.
“Nimemleta mgeni wenu.”
“Yupo wapi?”
“Huyo hapo nyuma,” alijibu dereva yule, Elizabeth aliyekuwa nyuma akashusha kioo.
“Oooh! Elizabeth, karibu sana,” alisema mlinzi yule huku akiufungua mlango wa gari lile na Elizabeth kuteremka.
Mara baada ya kumlipa dereva gharama yake aliyoihitaji, akachukuana na mlinzi na kuelekea ndani ya eneo la nyumba ile kisha kuelekea ndani kabisa, akakaribishwa kochini na kutulia. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda mno, hakuamini kama baada ya safari ndefu, tayari alikuwa amefika nchini Morocco na muda wowote ule angemuona mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.
Wafanyakazi wa ndani walipomuona, walionekana kufurahi mno, walimfahamu Elizabeth tangu siku ya kwanza alipofika nchini humo. Alikuwa msichana mcheshi, mwenye roho nzuri na ambaye alikuwa huru kuzungumza na mtu yeyote yule.
Wakamkaribisha na kumpatia kinywaji huku wakimwambia amsubiri Rasheed ambaye kwa kipindi hicho alikuwa msikitini akiswali.
Baada ya dakika kumi, Rasheed akatokea mahali hapo, Elizabeth alipomuona mwanaume huyo, akashindwa kuamini, akamrukia na kumkumbatia kwa nguvu, hakuamini kwamba mwisho wa siku alikutana na mwanaume huyo aliyeuteka moyo wake.
Kumbatio alilompa lilikuwa maalumu, alilopenda kuwapa watu aliowapenda kwa moyo wote, Rasheed akajifanya kushangaa, alijua kipi alichokifanya lakini kwa wakati huo, aliujenga uso wake kuwa kwenye mshangao mkubwa.
“Elizabeth...” alimuita kwa sauti ya chini.
“Nipo mpenzi!”
“Sijakuelewa...”
“Ninakupenda mno, nimetoka Tanzania kwa ajili yako, tena nilikuwa nikiolewa,” alisema Elizabeth huku akimmwagia mabusu mfululizo.
“Bado sijakuelewa...”
“Hujanielewa nini mpenzi?”
“Yote unayonifanyia.”
“Ninakupenda, naomba uwe wangu,” alisema Elizabeth huku akimwangalia mwanaume huyo usoni.
Rasheed akabaki kimya, alimwangalia Elizabeth usoni huku akijifanya hajui kilichokuwa kikiendelea, alichokifanya ni kujitoa mikononi mwa msichana huyo na kwenda pembeni, akatulia kochini na kuanza kumwangalia Elizabeth.
Ni kweli alikuwa mzuri, aliumbika, alikuwa na mvuto mkubwa lakini kwa kuwa aliamini kwamba asingeweza kutoka mikononi mwake, basi aanze kuleta pozi fulani hivi. Elizabeth akaanza kumsogelea Rasheed mahali pale alipokuwa na kisha kukaa karibu yake.
Akaanza kumwambia jinsi alivyokuwa akimpenda mwanaume huyo, hakulala, hakula wa kunywa kwa ajili yake, alitumia saa zaidi ya ishirini njiani kwa ajili yake tu, kubwa kuliko zote ni kwamba alikuwa akiolewa na mwanaume mwingine, akakataa kuwa mume wake kwa ajili yake.
“Kwa nini umemkataa mwanaume huyo?” aliuliza Rasheed.
“Kwa sababu ninakupenda.”
“Kweli?”
“Ndiyo!”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni nani? Ndiye yule James?”
“Ndiyo!”
“Sawa! Nihakikishie kama kweli unanipenda!”
Alichokifanya Elizabeth ni kukisogeza kinywa chake na kuanza kubadilishana mate na mwanaume huyo. Rasheed alijisikia msisimko wa ajabu, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, kwake, kilionekana kuwa kama ndoto ambapo baada ya muda mfupi angeshtuka na kujikuta akiwa kitandani.
Hapo ndipo alipoanza kuamini nguvu za kishirikina, hapo ndipo alipoamini kwamba kulikuwa na waganga waliokuwa wakimaanisha pale waliposema kwamba walikuwa na madawa ya kuponya magonjwa au kufanya jambo lolote ambalo kwa macho ya kibinadamu yasingeweza kufanyika.
Hapo ndipo mapenzi yao yalipoanzia, Rasheed alimpenda mno Elizabeth lakini msichana huyo hakujua kwamba kila kitu kilichokuwa kikiendelea, hasa mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa mwanaume huyo yalikuwa ni nguvu za giza. Hakulijua hilo, kila alipokuwa akimpenda, alijua kwamba alimpenda kikawaida kumbe kulikuwa na nguvu za kishirikina nyuma yake.
Kile kilichotokea kilimshangaza kila mtu, hakukuwa na aliyeamini kwamba msichana Elizabeth ambaye kila siku alikuwa akiomba Mungu aolewe eti ndiye aliyemkataa mume wake mtarajiwa kanisani, sekunde chache kabla ya kuvarishana pete na kuwa mume na mke.
Magazeti yaliandika, kila mtu aliyesoma taarifa zile alishtuka, hakukuwa na mtu aliyeamini kile kilichokuwa kimetokea. Ilikuwa ni aibu kubwa mno, mbele ya rais, mbele ya waziri mkuu na watu wengine maarufu, mbele ya watu waliokuwa na heshima zao, Elizabeth alikuwa amekataa kuolewa na James.
Hakukuwa na aliyejua tatizo lilikuwa nini, hakukuwa na aliyejua ni kitu gani kilitokea mpaka msichana huyo kufanya kitu kama kile kilichokuwa gumzo nchini nzima, kikasambaa na kuwa Afrika Mashariki nzima.
Kila mtu aliyechangia, alichangia lake na kumlaumu Elizabeth kwani kama kumuacha mwanaume huyo, angemuacha kabla na si kusubiri kipindi kama hicho, kipindi ambacho James alikuwa na uhakika kwamba angemfanya mwanamke huyo kuwa mke wake wa ndoa.
Alishinda akilia, alipokea meseji mbalimbali kutoka kwa watu wengi ambao walimpa pole kwa lile lililotokea lakini pole za maneno hazikuweza kuiondoa huzuni moyoni mwake, haikuweza kuyapunguza maumivu moyoni mwake, kilichokuwa kikiendelea, ni kuumia moyo na kuhisi kama alichomwa na kitu chenye ncha kali.
“Pole sana James,” alisema rafiki yake mkubwa, Boniface.
“Ahsante sana, ila kwa nini Elizabeth ameamua kufanya hivi?” aliuliza James.
“Kwani uliwahi kumfanyia kitu kibaya?”
“Hapana!”
“Hamkuwahi kugombana?”
“Hapana!”
“Hata kukuonyeshea kinyongo siku moja?”
“Hapana! Hakuwahi kufanya jambo lolote lile baya ambalo lingenifanya nihisi vibaya, nashangaa, ni ghafla sana, kwa nini lakini?’ aliuliza James huku akibubujikwa na machozi.
Alimpenda mno msichana hyo, kwake, alikuwa kila kitu zaidi ya mtu yeyote yule, kila alipokuwa akikumbuka jinsi walivyokuwa pamoja, walipofanya vitu vingi wakiwa pamoja mpaka siku ya harusi yao, moyo wake uliumia mno.
Hakuamini kama kweli Elizabeth ndiye aliyefanya kile alichokifanya, wakati mwingine alishindwa kuamini, alikaa chumbani huku akiziangalia picha za msichana huyo, wakati mwingine alizishika na machozi yake kuangukia katika flemu za picha, yalikuwa machozi ya uchungu, machozi yaliyoelezea ni jinsi gani alikuwa ameumia moyoni mwake.
Faraja yake kubwa ndani ya nyumba alikuwa mdogo wake, Glory ambaye kila siku ilikuwa ni lazima kuzungumza naye. Kama ilivyo kwake, hata kwa Glory ilikuwa ni maumivu makali, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea ndani ya ndege.
Alimpenda mno Elizabeth, alikuwa msichana wa kipekee mno maishani mwake, alimsaidia kwa kipindi kirefu, alimfanyia mambo mengi likiwepo suala la kumpeleka nchini India na Ujerumani kwa ajili ya matibabu.
Leo hii, msichana huyo ambaye kila siku alimuita wifi hakuwa mikononi mwa kaka yake, alikuwa ameondoka, alikimbia na kuelekea pasipojulikana kitu kilichomuumiza sana, hakujua mahali ambapo msichana huyo angeweza kupatikana.
Kila siku swali moja tu ndilo alilokuwa akimuuliza kaka yake juu ya mahali alipokuwa Elizabeth aliyekuwa amemzoea. James hakujibu kitu, kila alipomuona mdogo wake huyo akibubujikwa na machozi mashavuni mwake, aliumia moyoni lakini hakuwa na la kufanya.
“Atarudi,” alisema James.
“Lini?”
“Sijajua, ila atarudi,” alisisitiza James.
Hakuwa na jibu jingine la kumpa zaidi ya hilo, alijua kwamba inawezekana Elizabeth asirudi lakini hakutakiwa kumwambia ukweli juu ya hisia zake, alichokitaka ni kumtia moyo na kumwambia kwamba Elizabeth angerudi na kumuoa.
*****
Hakukuwa na mtu aliyefahamu mahali msichana mrembo Elizabeth alipokwenda mara baada ya kukataa kufunga ndoa na James. Maswali yakawa mengi mtaani, kila mtu alitaka kufahamu mahali alipokuwa, walitaka kumfuata kwa lengo la kujua sababu, kwa nini aliamua kumkataa James sekunde chache kabla ya kufunga ndoa.
Baada ya wiki kupita ndipo tetesi zikaanza kusikika kwamba msichana huyo alikuwa na bilionea wa Kiarabu aliyeishi nchini Morocco, Rasheed. Kila aliyeziona taarifa zile, hakuziamini, zilionekana kuwa tetesi ambazo kamwe hazikuaminika mioyoni mwao.
Mtandao wa Skypee ambao ndiyo uliotoa taarifa hizo ukaanza kutafuta picha na ndani ya siku kadhaa, wakazipata picha za wawili hao wakiwa katika Kisiwa cha Hawaii nchini Marekani wakila raha kama wapendanao.
Huo ndiyo ukawa mwisho wa tetesi zile, hapo ndipo watu walipojua kile kilichokuwa kikiendelea kwamba msichana Elizabeth hakuwa na James tena bali alikuwa ameangukia katika mikono ya mwanaume mwingine, bilionea mwenzake aliyeogelea fedha pamoja naye, Mwarabu mwenye sura nzuri, Rasheed.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watanzania wakakasirika lakini hasira zao hazikuweza kubadilisha kitu chochote kile, ukweli ukaendelea kubaki palepale kwamba msichana huyo, bilionea wa Kitanzania alikuwa kwenye penzi la dhati na mwanaume mwingine mwenye fedha kama alizokuwa nazo.
“Kweli matajiri kwa matajiri,” alisema mwanamke mmoja, alikuwa akiwaambia wenzake.
“Mmmh! Jamani huyu Elizabeth kweli katudhalilisha Watanzania,” alisema mwanamke mwingine, alionekana kuumia moyoni mwake.
Kila mtu aliyezipata taarifa zile, alimsikitikia James, umasikini wake ukamfanya kuachwa na mwanamke mrembo. Alipoletewa taarifa kwa mara ya kwanza, hakuamini, alitaka kuziona picha za msichana huyo akiwa na mwanaume huyo, akaonyeshewa Gazeti la Ijumaa, alipoziona, akakaa kochini, miguu ilikosa nguvu, akahisi akipoteza nguvu ya kuona, giza likamtawala na mwisho wa siku akapoteza fahamu.
“Jamani njooni mnisaidie,” alisema rafiki yake ambaye ndiye aliyempeleka gazeti lile lenye picha.
Msichana wa kazi na mlinzi wakatokea sebuleni pale, walihokifanya ni kumbebea na moja kwa moja kumpeleka hospitalini ambapo huko wakapewa taarifa kwamba alikuwa na msongo wa mawazo.
Alimpenda mno Elizabeth, hakuwahi kufikiria kwamba kuna siku angeweza kumpoteza mikononi mwake, alichokiamini ni kwamba angeendelea kuwa naye maisha yake yote, yaani mpaka kifo kiwatenganishe.
Kile alichokuwa amekifikiria, kikaenda tofauti, akaachwa solemba kitu kilichomletea mawazo kila siku. Hospitalini hapo, alilala chali huku dripu ikining’inia juu yake, hakuwa amerudiwa na fahamu, alikuwa kimya kabisa huku pembeni yake wakiwepo marafiki zake.
Baada ya saa tano kupita ndipo akarudiwa na fahamu. Kitu cha kwanza kukiona kilikuwa ni dripu iliyoning’inizwa juu yake na iliendelea kupitisha maji katika mshipa wake. Hakutaka kujiuliza alikuwa wapi, alijua kwamba ilikuwa ni hospitali, swali lililokuja kichwani mwake, alifikaje?
Kumbukumbu zake zilipoanza kujirudia kichwani ndipo akakumbuka kila kitu kwamba mara ya mwisho alikuwa sebuleni akiangalia picha ya Elizabeth akiwa na bilionea wa Kiarabu, Rasheed. Bila kutegemea, akajikuta akibubujikwa na machozi mashavuni mwake.
“Usilie kaka,” alisema mdogo wake, Glory huku akiwa kwenye kiti chake cha mataili.
Maumivu ya moyo wake yalikuwa makubwa mno, aliendelea kulia kitandani pale japokuwa mdogo wake mgonjwa aliyepooza akijaribu kumbembeleza zaidi. Bado hakuamini kile alichokuwa akikipitia, kila kitu kilionekana kuwa kama ndoto katika maisha yake.
Watu mbalimbali walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali, alikuwa mtu maarufu, alijulikana Tanzania nzima, kupitia nyota kali ya Elizabeth, naye akajikuta akiwa supastaa mkubwa nchini Tanzania.
“Pole sana James,” alisema Waziri Mkuu, bwana Jackimbute Pius aliyekwenda kumtambelea hospitali..
“Ahsante sana mkuu.”
Si huyo tu, waliendelea kumiminika viongozi wengi na watu maarufu nchini Tanzania, wote hao walifika mahali hapo kwa ajili ya kumjulia hali James ambaye alikuwa hoi kitandani. Katika kipindi hicho cha shida, kipindi alichokuwa hoi kitandani hapo ndipo alipokuja kufahamiana na msichana Siah Kobiro, muigizaji wa Tamthiliya ya Kipupwe iliyokuwa ikirushwa katika Kituo cha Televisheni cha Global.
“Pole sana James! Mungu atakutangulia,” alisema Siah huku akimwangalia James usoni.
“Nashukuru sana, ila sijajua mwenzangu nani!”
“Haunifahamu?”
“Hapana! Lakini sura yako si ngeni! Nani mwenzangu?” aliuliza James huku akimwangalia msichana huyo kwa umakini.
“Naitwa Siah! Yule wa Kipupwe...”
“Ahh! Kumbe! Unaendeleaje?”
“Nipo salama tu.”
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo, kila siku Siah alikuwa akifika hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali James ambaye alikuwa akiendelea vizuri kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele. Baada ya siku tatu, akatoka hospitalini, magazeti yalimwandika sana, mitandao ya kijamii, kote huko jina lake lilivuma.
Alipendwa sana, kitendo cha kuachwa solemba kiliamsha mapenzi ya watu kwake, hawakumuacha, walimuonyeshea ni jinsi gani walikuwa wakimpenda. Ukaribu wake na Siah, ukamfanya msichana huyo kila siku kufika nyumbani kwake na kukaa karibu naye huku akimjulia hali Glory kila siku.
Baada ya waandishi wa habari kumfuma Siah akiingia ndani ya nyumba ya James hapo ndipo walipoanza kumwandika kwamba inawezekana msichana huyo alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na James.
Kila mtu ambaye aliziona taarifa zile, alimshukuru Mungu kwa kuamini kwamba sasa mawazo ya James kwa msichana wake, Elizabeth yangekwisha kwani msichana huyo alikuwa amekuja na kitu kipya moyoni mwake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Japokuwa ukaribu uliendelea na mwisho wa siku kujikuta wakilala pamoja lakini moyo wa James haukuweza kumsahau Elizabeth, alikuwa mwanamke aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati.
Hali hiyo haikutokea kwake tu bali hata kwa Glory ambaye mara kwa mara alikuwa akilia huku akimtaka Elizabeth arudi nyumbani kwani alikuwa kwenye upweke wa hali ya juu.
Kiasi cha shilingi bilioni moja alichopewa kabla siku ya harusi ndicho kiasi hichohicho kilichoyabadilisha maisha yake. Alikifanyia biashara kiasi hicho na hatimaye kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Japokuwa alionekana kuwa tajiri, lakini fedha bila mapenzi kutoka kwa mtu aliyempenda ilionekana kuwa si chochote, si lolote. Alichokuwa akikihitaji katika maisha yake ni kuwa na Elizabeth tu, ndiyo, alifahamu kwamba kulikuwa na wanawake wengi waliompenda lakini moyo wake ulikufa na kuoza kwa msichana huyo tu.
“Ninakupenda James,” alisema Siah kwa sauti nyororo.
“Nakupenda pia.”
“Lakini mbona hauna furaha?”
“Mbona nipo poa tu.”
“Hapana! Hauna furaha hata mara moja, hebu niambie tatizo nini,” alisema Siah huku akimwangalia mpenzi wake huyo usoni.
“Sina tatizo.”
“Mmmh! Kweli?”
“Hakika.”
Huzuni haikujificha usoni mwake, mawazo hayakumuisha, kila alipokaa, alimkumbuka msichana Elizabeth, alikuwa mtu pekee aliyeupiga chapa ya moto moyo wake, chapa ile haikuweza kutoka, kila siku katika maisha yake alimkumbuka msichana huyo.
Hata kama msichana gani angemfuata katika maisha yake, bado Elizabeth alidumu moyoni mwake. Wakati mwingine alibaki chumbani kwake, humo, alilia mno, alishindwa kuelewa sababu iliyomfanya Elizabeth kumuacha na kumfuata bilionea Rasheed.
Picha alizokuwa akiziona magazetini, zilimuumiza mno, alisononeka sana, hakuwa na nguvu. Kulia ilikuwa sehemu ya maisha yake, hakutaka kunyamaza, kila siku alishinda chumbani kwake akilia, mateso yalimuumiza mno.
“Nyamaza kaka! Elizabeth atarudi tu,” alisema Glory huku naye akibubujikwa na machozi.
Mwezi mmoja ulipita lakini maumivu juu ya Elizabeth yalikuwa makubwa, yaani ilionekana kama aliachwa siku iliyopita. Kama kulia, alilia sana, kama kuhuzunika alihuzunika sana lakini hakukuwa kilichobakia, ukweli ukaendelea kubaki palepale kwamba Elizabeth hakuwa naye tena, alikwenda kwenye mikono ya mwanaume bilionea.
****
“Ninakupenda mpenzi, hakuna zaidi yako moyoni mwangu,” alisema Elizabeth kwa sauti nyororo huku akiwa kifuani mwa mpenzi wake, Rasheed.
“Nakupenda pia, ila kwa nini ulinikataa?”
“Mmmh! Hata mimi nashindwa kuelewa kwa sababu gani,” alisema Elizabeth huku akianza kukipapasa kifua cha Rasheed kilichokuwa na nywele nyingi.
Hiyo ilikuwa wiki ya pili yangu wawili hao wawe pamoja, walikuwa wamesafiri kwa kipindi cha wiki mbili mfululizo kwenda katika fukwe mbalimbali nchini Marekani kwa ajili ya kula raha tu. Maisha yao yalitawaliwa na furaha, kila mmoja alimpenda mwenzake kupita kawaida.
Huko, walionyeshana mahaba niue, mapenzi ya njiwa kwa kukaa pamoja na kulishana vyakula walivyotaka. Mpaka katika kipindi hicho, Elizabeth hakumfikiria James, hakukumbuka kama kulikuwa na mtu aliyeitwa kwa jina hilo, na hata alipomkumbuka, alijishangaa ni kwa sababu gani alimpenda mwanaume kama huyo.
Walikaa nchini Marekani kwa kipindi cha mwezi mmoja na ndipo walipoamua kuondoka na kuelekea nchini Hispania na kutulia katika Ufukwe wa Ibiza. Huko, kama kawaida yao, walitumia fedha, hakukuwa na kitu kilichoendelea zaidi ya kutumia fedha tu.
Walichukua chumba katika hoteli kubwa, walikodisha magari ya thamani na kuyatumia popote pale walipokuwa, kwao, fedha haikuwa tatizo kabisa, walichokuwa wakikiangalia ni kwa namna gani wangeweza kuzitumia.
“Mpenzi...” aliita Elizabeth.
“Sema kipenzi!”
“Ninahitaji mtoto.”
“Unahitaji mtoto?”
“Ndiyo! Sitaki kingine chochote, ninahitaji mtoto, naomba tuzae wote,” alisema Elizabeth kwa sauti nyembamba ya kumtoa nyoka pangoni.
Hilo bado liliendelea kuwa hitaji la maisha yake yote, alikuwa akihitaji mtoto kwa hali na mali, kama fedha, alikuwa nazo nyingi, kila kitu alichokuwa akikitaka katika maisha yake, alikipata, mtoto ndiye ambaye alikuwa akimhitaji kwa kipindi hicho.
Hilo wala halikuwa tatizo, kwa kuwa Rasheed alikuwa akimpenda sana Elizabeth, kilichotokea ni kuanza kumtafuta mtoto lakini hawakuweza kufanikiwa hata kidogo, hata dalili za kuonyesha kwamba alikuwa mjauzito hazikuweza kuonekana.
Furaha haikuwepo, alipewa mapenzi yote aliyokuwa akiyataka lakini kitendo cha kukosa mtoto kilimpa shida sana, kilimsumbua maishani mwake na kilimkosesha furaha moyoni mwake.
Hakuacha kuwaona madaktari, katika kila nchi aliyotua, alikuwa akielekea katika hospitali kubwa na kuwaona madaktari, alitaka kuambiwa tatizo lilikuwa nini, cha ajabu alipofika huko, akaambiwa kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile.
“Sasa kwa nini sipati mtoto?”
“Hata sisi hatufahamu! Ila kwenye mashine zetu unaonekana uko poa kabisa,” alisema Dk. Bonny wa Hospitali ya Mtakatifu Agatha iliyokuwa nchini Hispania.
Japokuwa katika maisha yake alihangaika sana kutafuta mtoto lakini hapo napo akajikuta akianza kuhangaika tena. Walikutana wote wawili wakiwa mabilionea hivyo suala hilo halikuwa kazi kubwa, katika kila nchi ambayo walikwenda kula raha walipitia na hospitali za huko kuangalia kama wangeweza kufanikiwa katika suala zima la kuweza kupata mtoto.
“Tutaendelea kujaribu kila sehemu, wewe wala usijali,” alisema Rasheed.
Baada ya matembezi yaliyochukua miezi miwili kwa ajili ya kula raha tu hatimaye wakaamua kurudi nchini Morocco ambapo huko maisha yaliendelea kama kawaida. Watu wengi hasa marafiki wa Rasheed wakatokea kumpenda Elizabeth, alionekana kuwa mwanamke mzuri kuliko hata Waarabu waliokuwa nchini humo.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Japokuwa magazeti mbalimbali yaliandika kuhusu uhusiano huo na kama ingewezekana basi Rasheed atengwe kwa kuwa alikuwa akiishi na mwanamke kinyume na dini lakini mwisho wa siku nguvu ya hela ikaonekana kuwa kubwa kuliko hata dini yenyewe.
Waliokuwa wakisema sana, wakanyamaza, wakamuacha bilionea huyo aendelee na maisha yake kama kawaida. Elizabeth hakubadilika, alifuatwa mara kwa na kuambiwa kwamba alipaswa kuvaa ushungi au juba lakini hakutaka kufanya hivyo.
“Nivae ili iweje?” aliuliza Elizabeth kila alipoambiwa.
“Mwanamke kujisitiri ndiyo anavyotakiwa kuwa,” alisema mwanamke mmoja.
“Hadi hapa nimejisitiri vya kutosha, siwezi kuvaa zaidi ya hapa,” alijibu Elizabeth, hapo alikuwa amevaa gauni lililomfika ugokoni na kichwani alivalia kofia ya jua.
Watu hawakunyamaza, Morocco nzima walikuwa wakimjadili Elizabeth lakini hakubadilika, magazeti yakaandika na kuandika lakini bado hali ilikuwa vilevile. Rasheed aliambiwa sana kuhusu Elizabeth lakini kutokana na mapenzi mazito aliyokuwa nayo kwa msichana huyo akashindwa kufanya lolote kile, akawa mtu wa kuyapitisha maneno katika sikio la kulia na kutokea sikio la kushoto, hakujali kabisa.
*****
“Ninakupenda James! Ninakupenda kwa moyo wangu wote,” alisema Siah kwa sauti ndogo karibu na sikio la James.
“Najua Siah! Najua kwamba unanipenda.”
“Na wewe unanipenda?”
“Kwani unanionaje?”
“Ndiyo nataka kusikia kutoka kwako,” alisema Siah.
“Ninakupenda pia.”
Miezi miwili ilipita lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote yale, James aliendelea kumkumbuka msichana wake kana kwamba alikataliwa siku iliyopita. Siah hakukata tamaa, kitu pekee alichokuwa akikijua kwamba ingetokea siku ambayo moyo wa James ungemsahau kabisa Elizabeth na kukubaliana naye kwa asilimia mia moja.
Kipindi hicho ndicho ambacho Siah alikuwa akiigiza Filamu ya Love Has Fallen Apart, ilikuwa filamu nzuri iliyoandaliwa nchini Tanzania lakini waongozaji wake walitoka Afrika Kusini. Filamu ilijaa mapenzi, ilielezea jinsi watu walivyokuwa wakiumizwa katika maisha ya kimapenzi.
Filamu ile ilipokamilika, siku ya uzinduzi Siah akaenda na James katika Ukumbi wa Mlimani City ambapo hapo ndipo uzinduzi ulipotarajiwa kufanyika. Watu walipomuona James, walishindwa kuvumilia, wakamfuata na kuanza kupiga naye picha, walivutiwa naye mno.
Alitoa tabasamu lakini wengi waliliona tabasamu lile kuwa bandia, lilionyesha dhahiri kwamba moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno. Walioligundua hilo walimuonea huruma, hawakupenda mvulana mpole na mwenye uzuri wa sura apitie kile alichokuwa akipitia.
Wakati filamu inaanza mpaka kufikia katikati, James alikuwa akilia tu, kila kitu alichokuwa akikiona kilimkumbusha maisha yake aliyoishi na Elizabeth. Mashavu yake yalilowanishwa na machozi, kutokana na mwanga hafifu uliokuwemo humo, Siah hakuweza kugundua lolote lile.
“Naomba tuondoke mpenzi,” alisema James, alikuwa akimwambia Siah.
“Kwa nini jamani!”
“Hakuna kitu, naomba tuondoke,” alisisitiza James.
“James mpenzi! Unajua kwamba hii ni filamu niliyoigiza?”
“Najua!”
“Unajua kwamba baada ya hapa watu watataka kupiga picha nami?”
“Najua!”
“Naomba tusubiri iishe! Nakuomba mpenzi,” alisema Siah kwa sauti ya chini na ya kubembeleza.
James hakuwa na jinsi, japokuwa filamu ile ilimuumiza sana lakini akavumilia kwani haikuwa imebakiza dakika nyingi mpaka kumalizika. Machozi hayakumkauka, bado iliendelea kumuumiza mno kwani kila hatua alikuwa akimfikiria Elizabeth tu.
Filamu ilipomaliza, wakatoka nje ya ukumbi ule, kila mtu alibaki akimpongeza Siah kutokana na umahiri wake aliouonyesha katika filamu ile. Watu wakaanza kupiga naye picha za ukumbusho huku James akiwa pembeni kabisa, tena uso wake wake akiwa ameulazimisha kuwa na tabasamu pana.
Wakati James akimwangalia Elizabeth aliyeonekana kuwa na furaha mno kupiga picha na mashabiki zake, ghafla James akaanza kusikia simu yake ikianza kutetemeka. Hapohapo akaitoa mfukoni na kuangalia namba ya mtu aliyekuwa akimpiga, alikuwa mfanyakazi wa nyumbani.
“Theodora, kuna nini? Mbona usikuusiku?” aliuliza James huku akionekana kuchanganyikiwa. Hakukuwa na neno lolote alilolisikia kutoka kwa Theodora zaidi ya kilio tu. James akachanganyikiwa.
****
Simu aliyoipokea ilitoka kwa dada wa nyumbani ambaye hakuzungumza kitu chochote zaidi ya kulia tu. James akashtuka, hakujua sababu ya kilio cha msichana huyo kiasi kwamba kukawa na vitu vingi vikaanza kumiminika kichwani mwake, na kitu kimoja kikubwa ni kuhusu uvamizi wa majambazi.
“Theodora...” aliita kwa mara nyingine lakini Theodora hakuzungumza kitu chochote kile.
Moyo wa James ukaanza kudanda kwa kasi, haikuwa kawaida kwa dada huyo wa nyumbani kumpigia simu usiku namna hiyo kama hakukuwa na tatizo lolote lile, kwa wakati huo, ilikuwa saa saba usiku, alimpigia simu na hakuwa akizungumza kitu chochote kile zaidi ya kulia tu.
Wakati akiendelea kuiacha simu sikioni tena huku kijasho chembamba kikianza kumtoka, msichana wake, Siah akamfuata na kuanza kumwangalia. Hakuonekana kuwa katika hali ya kawaida, alionekana kuwa na hofu, mwili wake ulimtetemeka huku kwa mbali kijasho kile kikionekana.
“James....” aliita Siah kwa sauti ya chini huku akimshika bega, hapohapo James akashtuka.
“Siah..!”
“Kuna nini? Mbona hivyo?” aliuliza Siah huku simu ikiwa sikioni mwa James.
“Theodora amepiga simu na kuni....” alisema James lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, akasikia sauti ya Theodora ikiongea kwenye simu.
“Glory...” ilisikika sauti ya Theodora.
“Glory! Amefanya nini?” aliuliza James, lakini hata kabla hajapewa jibu, hapohapo simu ikakatwa.
James alichanganyikiwa, hakuona kama kulikuwa na sababu ya kuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya, huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa akaanza kuondoka huku akikimbia, Siah hakutaka kubaki peke yake, naye akaanza kumkimbiza.
Kila mtu aliyeliona tukio hilo alishangaa, hawakujua sababu iliyowafanya wapendanao hao kukimbia kuelekea nje na wakati bado shughuli ya kupiga picha ilikuwa ikiendelea. Walichokifanya nao ni kuelekea kule nje kwani tayari kukaonekana kuwa na tatizo.
James akafika nje, moja kwa moja akaanza kuelekea sehemu ilipokuwa gari lake, alipolifikia, akaufungua mlango na kuingia ndani, hata kabla hajawasha gari, naye Siah akafika, akafungua mlango na kuingia ndani.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuna nini James?” aliuliza Siah lakini James hakujibu kitu, akawasha gari na kuondoka mahali hapo.
Safari ya kurudi nyumbani ikaanza, James alionekana kuwa na hofu moyoni mwake, tayari alijua kwamba kulikuwa na tatizo lililokuwa limetokea, kitendo cha Theodora kulitaja jina la mdogo wake kulimchanganya mno.
Siah alijitahidi kumuuliza maswali mengi kwa lengo la kutaka kujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea lakini James hakuongea kitu chochote kile zaidi ya kutilia umakini barabarani. Walichukua dakika tano tu, wakafika nyumbani, hata kabla mlinzi hajafungua geti kubwa ili aliingize gari, tayari akatoka garini na kulifuata geti dogo ambalo mlinzi alifungua na kuingia ndani.
“Kuna nini?”
“Hakuna kitu.”
“Hakuna tatizo ndani?”
“Sijui! Labda Theodora anajua chochote, ila sijaona chochote kibaya,” alijibu mlinzi.
James akaanza kuelekea ndani, alionekana kuchanganyikiwa, alipoufikia mlango wa kuingia sebuleni, akaufungua na kuingia ndani. Kama kawaida sebule ilikuwa kimya mno, alichokifanya ni kuelekea chumbani kwa Glory.
Hata kabla hajaingia ndani, tayari akasikia kilio kutoka kwa dada wa nyumbani, alikuwa akilia huku akiongea maneno ya kutaka kumuamsha Glory. Mpaka kufikia hatua hiyo, James akachanganyikiwa zaidi, akaufgungua mlango na kuingia ndani.
“Theodora, kuna nini?’ aliuliza James lakini hata kabla hajajibiwa swali lake, tayari alimfikia Glory aliyekuwa kimya kitandani.
Alijaribu kumuamsha Glory kitandani pale, alikuwa kimya, James hakutaka kuamini alichokuwa akikiona, aliendelea kumuasha Glory na kwa kumuita kwa sauti ya juu kabisa huku akimshikashika shavuni lakini msichana huyo alikuwa kimya kitandani pale.
Alichokifanya ni kuupeleka mkono wake katika kifua cha Glory, moyo ulikuwa ukidunda kwa mbali mno, tayari akaona kwamba kulikuwa na tatizo na kama asingefanya kitu cha ziada basi mambo yangekuwa magumu zaidi.
Walichokifanya ni kumuinua na kuelekea naye nje. Tayari machozi yalianza kumbubujika James, hakuamini kile alichokuwa akikiona mbele yake, alimpenda sana mdogo wake, baada ya kuondoka kwa Elizabeth, mdogo wake huyo ndiye alikuwa kila kitu katika maisha yake.
Walipofika nje wakaingia garini na kumwambia Siah aendeshe gari kuelekea katika Hospitali ya Mtakatifu Maria ambayo haikuwa mbali kutoka hapo walipokuwa. Ndani ya gari James bado aliendelea na juhudi zake za kumuamsha Glory lakini bado ukimya ulikuwa mkubwa, hata shingo na kichwa chake ambvyo mara kwa mara vilikuwa vikitingishika, muda huo vilitulia na kulegea kabisa.
Walipofika hospitalini, harakaharaka machela ikavutwa na manesi waliokuwa nje na kumuweka Glory juu kisha kuanza kuisukuma kuelekea ndani. Walipofika ndani kabisa karibu na chumba kilichoandikwa Theatre, wakaambiwa wasubiri nje.
“Nesi!” aliita James.
“Unasemaje James.”
“Nataka kuingia ndani!”
“Subiri hapa kwanza, hautakiwi kuingia humu,” alisema nesi yule.
“Lakini ni mdogo wangu!”
“Hata kama! Nakuomba usubiri kwenye viti hivyo,” alisema nesi yule, akaingia ndani na kufunga mlango.
Hakuwa najinsi, kichwa chake kilichanganyikiwa mno, hakuamini kama mambo yote yaliyokuwa yakitokea yalimtokea katika maisha yake. Alikuwa na mawazo mno juu ya msichana aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, Elizabeth, mwisho wa siku msichana huyo akamuacha katika kipindi kigumu, sekunde chache kabla ya kumalisha pete na kuwa mke wake wa ndoa.
Wakati kichwa chake kikiwa na mawazo mengi, tayari tatizo jingine lilikuwa limetokea, mtu pekee ambaye alikuwa amembakiza katika maisha yake, Glory alikuwa hoi, hakujua alipatwa na nini, alikuwa kwenye dakika za mwisho kuvuta pumzi ya dunia hii.
Machozi hayakukauka, alichanganyikiwa mno mpaka kujiona kama angekwenda kuwa chizi dakika chache baadaye. Pale kitini alipokuwa, Siah alitumia muda huo kumfariji mpenzi wake huyo kwani yeye ndiye alikuwa mfariji pekee aliyekuwa amebaki katika maisha yake.
“Nyamaza James! Nyamaza kipenzi,” alisema Siah, hata naye kwa mbali machozi yalikuwa yakimlenga.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwa nini mimi? Kwa nini Mungu ananionea hivi?’ aliuliza James.
“Hapana! Yote muachie Mungu! Ila kumbuka kwamba kila anachokifanya hakina makosa, Mungu anafanya mambo sawasawa na mipango yake. Kumbuka, yeye ndiye ameshika kila kitu, amini kwamba Glory atapona na kuwa mzima,” alisema Siah.
Japokuwa alitumia maneno mengi kumfariji lakini James hakufarijika, aliendelea kuumia mno, bado moyo wake haukuamini kile alichokuwa akikipitia wakati huo. Hakuacha kumlaumu Mungu, wakati mwingine aliona huyo ndiye alitakiwa kulaumiwa kutokana na kila kitu kilichokuwa kikitokea.
Wakati wakiwa hapo, mara daktari mmoja mwenye ndevu nyingi, aliyevalia koti kubwa jeupe akatokea, hakuzungumza nao chochote kile, alichokifanya ni kuingiandani ya chumba kile. James akasimama, hakuona kama kulikuwa na sababu ya kukaa chini, akausogelea mlango ule na kuanza kuliita jina la mdogo wake.
Alilia na kulia, kila alipoona ukimya ukiendelea kuwa mkubwa ndani ya chumba kile na ndivyo alivyozidi kuwa na wasiwasi juu ya hali aliyokuwa nayo Glory.
*****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment