Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

I KILLED MY BELOVED ONE (NILIMUUA NIMPENDAYE) - 2

 







    Simulizi : I Killed My Beloved One (Nilimuua Nimpendaye)

    Sehemu Ya Pili (2)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa muda mfupi tu niliomfahamu Jimmy, nilitokea kuvutiwa sana na haiba yake ya upole na ucheshi. Nilivuta kumbukumbu za jinsi nilivyokutana naye kwenye mazingira ya hatari alipotaka kunigonga na gari lake wakati nikirudi shuleni nikiwa na mawazo.

    Nilikumbuka jinsi alivyoonesha uungwana na kunipa pole kwa tukio hilo, kisha akanipa lifti mpaka karibu na nyumbani na kuniachia kiasi kikubwa cha fedha. Nilizidi kuvutiwa naye kwa jinsi alivyokuwa anaongea kwa upole kwenye simu.

    Japokuwa nilikuwa mgeni kabisa katika mambo ya mapenzi, kwa mara ya kwanza nilijihisi kumpenda Jimmy na kutamani awe mpenzi wangu. Sikujali hata tofauti ya umri iliyokuwepo kati yetu. Sijui mawazo hayo yalitoka wapi kwani kabla ya hapo, sikuwahi kuwa na mpenzi na hata wavulana waliokuwa wakinitongoza, nilikuwa nikiwatukana sana.

    Nilichelewa sana kulala siku hiyo, mawazo juu ya Jimmy yalinisahaulisha kabisa hisia chungu nilizokuwa nazo kutokana na jinsi mama alivyokuwa akiiongoza familia yetu baada ya kifo cha baba.

    Baadaye usingizi ulinipitia, nikalala mpaka kesho yake asubuhi kulipopambazuka ambapo kama kawaida niliwahi kuamka na kuanza kufanya shughuli mbalimbali za nyumbani. Nikafanya usafi wa ndani na nje ya nyumba, nikawafulia wadogo zangu nguo zao kisha nikaanza kuandaa kifungua kinywa.

    Siku hiyo mama hakuondoka kama ilivyokuwa kawaida yake, alishinda chumbani kwake akiwa amejifungia mlango. Hata kifungua kinywa kilipokuwa tayari, hakutoka kujumuika nasi, alilala mpaka saa sita mchana, ndiyo akaamka na kutoka nje.

    Kwa upande wangu, siku hiyo nilishinda na simu, kila nilipokuwa nakwenda sikuiacha nikihofia Jimmy anaweza kupiga halafu akanikosa. Ilipofika saa nane, nikiwa jikoni namalizia kupika chakula cha mchana, simu iliita, nilipotazama namba ya mpigaji, alikuwa ni Jimmy.

    Harakaharaka nikainuka na kukimbilia chumbani kwangu, nikajifungia mlango na kupokea simu. Kama kawaida yake, Jimmy alinichangamkia na kuniambia kuwa tayari ameshaninunulia simu hivyo tukutane pale aliponishusha jana yake.

    Nilimkubalia, nikaenda kumalizia kupika kisha nikawaacha ndugu zangu wanaendelea kula, nikaenda bafuni kuoga harakaharaka kisha nikaenda kujiandaa. Japokuwa haikuwa kawaida yangu kujipodoa au kutumia muda mrefu nyuma ya kioo, siku hiyo nilifanya hivyo kwani sikutaka niende kuonana na Jimmy nikiwa na dosari yoyote.

    Baada ya kuridhika na jinsi nilivyokuwa nimependeza, nilitoka bila mtu yeyote kujua nakwenda wapi, nikatokomea mitaani na kwenda mpaka pale aliponishusha jana yake. Japokuwa mwenyewe alikuwa anajua pale ni jirani kabisa na kwetu, ukweli ni kwamba tulikuwa tukiishi mtaa wa tatu kutoka eneo hilo. Sikutaka afahamu nyumbani kwetu kirahisi.

    Nilipofika, nilisimama huku nikiangaza macho huku na kule, mara nikasikia muungurumo wa gari, alikuwa ni Jimmy lakini akiwa kwenye gari lingine tofauti na lile la jana yake. Akalisogeza na kusimama jirani kabisa na pale nilipokuwa nimesimama, akateremsha kioo huku tabasamu pana likiwa limeupamba uso wake.

    Baada ya kusalimiana kwa uchangamfu, alinionesha kwa ishara kwamba niingie ndani ya gari, nikazunguka na kuingia.

    Alitoa kiboksi na kunikabidhi, akaniambia nifungue mwenyewe na kujionea kilichokuwa ndani. Nilikishika na kufungua, nilichokutana nacho hakika sikuamini. Ilikuwa ni simu nzuri ya kisasa, ikiwa bado mpya kabisa.

    “Whaoooo! Nzuri sana,” nilisema kwa sauti huku nikiwa nimeikodolea macho simu hiyo ya ‘kuslaidi’, akanisaidia kuitoa kwenye karatasi na kuiunganisha vizuri kisha akaiwasha, nilishindwa kuificha furaha niliyokuwa nayo.

    Kwa kuwa tulikuwa tumekaa jirani, sijui nini kilitokea lakini nilijikuta nimemkumbatia Jimmy na kujilaza kwenye kifua chake, na yeye akanionesha ushirikiano kwa kunikumbatia.

    “Ahsante sana Jimmy,” nilisema kwa sauti iliyotokea puani huku nikimtazama kwa macho yangu mazuri. Baada ya sekunde kadhaa, tuliachiana, nikamshukuru tena kisha nikaagana naye, nikateremka na yeye akawasha gari lake na kuondoka, nikabaki nimesimama palepale, nikamsindikiza kwa macho mpaka alipopotea na gari lake.

    Harakaharaka nikaondoka na kurudi nyumbani huku ile simu mpya nikiificha kwani sikutaka mtu yeyote aione. Kwa bahati nzuri, hakuna aliyeniona wakati naingia, nikaenda moja kwa moja mpaka chumbani kwangu na kujifungia, nikaanza kuikagua vizuri ile simu.

    Ilikuwa na mambo mengi mazuri ya kufurahisha na kuvutia, kuanzia kamera, redio, na vitu vingine vingi. Nilifurahi mno siku hiyo, nikajilaza kitandani huku nikiendelea kuufikiria ukarimu aliokuwa nao Jimmy. Kwa kitendo hicho alichonifanyia, nilijikuta nikizidi kumpenda maradufu, muda wote nikawa namuwaza.

    Kumbukumbu za jinsi tulivyokumbatiana naye na hali niliyoihisi baada ya kitendo hicho, zilinifanya nijihisi kama napaa angani. Nikajikuta naanza kuweweseka na kulitaja jina la Jimmy, nikaukumbatia mto wangu na kuanza kujigeuzageuza kitandani huku nikiendelea kulitaja jina lake.

    Nikashtuka baada ya kusikia mlango wa chumba changu ukigongwa, nikakurupuka na kwenda kuificha simu chini ya kitanda kisha nikausogelea mlango.

    “Simu yangu ipo wapi? Mbona leo kutwa nzima umeshinda nayo kwani unawasiliana na nani?” kaka yangu aliniuliza maswali mfululizo lakini sikumjibu zaidi ya kumrudishia simu yake aliyokuwa ameniazima tangu jana yake.

    Nilihakikisha nimefuta namba ya Jimmy ndiyo nikampa kwani sikutaka kaka yangu aelewe chochote kinachoendelea kutokana na malezi tuliyolelewa. Nilipompa simu yake, alikaa pembeni ya kitanda changu, akanitaka tubadilishane mawazo kuhusu mambo yaliyokuwa yanafanywa na mama.

    Tofauti na siku nyingine zote ambapo mimi ndiyo nilikuwa naonekana kushikia bango mabadiliko ya mama, safari hii nilimwambia kaka kuwa tuachane naye. Sikutaka kabisa kuendelea kujadiliana kuhusu ishu za mama kwani nilijua zitaniongezea mawazo.

    Akili yangu kwa muda huo ilikuwa ikimuwaza Jimmy pekee hivyo nilihitaji muda wa kukaa peke yangu. Kaka alinishangaa lakini alipoona nimeshikilia msimamo wangu, hakuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana na mimi, akatoka na kuniacha mwenyewe chumbani akiwa hajui kwamba nimepata simu mpya, tena ya bei mbaya.

    Nikaukumbatia tena mto wangu na kuendelea kumvutia hisia Jimmy. Ndani ya kipindi kifupi tangu nifahamiane na mwanaume huyo, nilikuwa nimezama kabisa ndani ya dimbwi la mapenzi lakini mtihani mkubwa niliokuwa nao, ulikuwa ni namna ya kumfikishia ujumbe wa kilichomo ndani ya moyo wangu.



    Nilijua nikimueleza kwamba nampenda, ataniona sijatulia au atahisi sijalelewa vizuri kama wanawake wa Kiafrika wanavyotakiwa kuwa, nikawa naendelea kuteseka. Niliendelea kuitazama ile simu aliyonipa kama zawadi, furaha ikazidi kuugubika moyo wangu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku hiyo nilishinda chumbani kwangu nikimuwaza Jimmy mpaka jioni nilipokuja kushtuliwa na wadogo zangu ambao waliniuliza kama siku hiyo hatuli kwani giza lilishaanza kuingia kukiwa hakuna maandalizi yoyote jikoni.

    Nilikurupuka harakaharaka na kutoka mpaka gengeni ambapo nilinunua mboga kwa kutumia fedha nilizopewa na Jimmy, nikarudi ndani na kuanza kuandaa chakula cha usiku. Niilifanya kila kitu harakaharaka, baada ya muda chakula kikawa kimeshaiva, nikaandaa kisha tukajumuika mezani na ndugu zangu. Mimi ndiyo nilikuwa wa kwanza kunawa mikono.

    Nikaenda chumbani kwangu na kuwaachia maagizo wadogo zangu kuwa wote wakimaliza kula waondoe vyombo na kusafisha meza. Nikajifungia mlango na kujilaza kitandani, nikawa nachezeachezea simu yangu huku nikiwa na shauku kubwa ya kuzungumza na Jimmy.

    Kwa bahati nzuri, ni kama na yeye alijua kilichokuwa ndani ya moyo wangu kwani muda mfupi baadaye, simu yangu ilianza kuita, nilipotazama namba ya mpigaji, alikuwa ni Jimmy. Sijui ni kitu gani kilichotokea lakini ghafla nilianza kuhisi mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio sana, nikajikaza na kupokea simu.

    “Vipi Eunice, mzima,” alisema Jimmy kwa uchangamfu kama ilivyokuwa kawaida yake, nikahisi sauti yake ikipenya mpaka ndani ya moyo wangu, hofu ikapungua na kujikuta nikiachia tabasamu, tukaendelea na mazungumzo yetu.

    Aliniuliza kama kesho yake nitakuwa na nafasi kwani kuna mahali anataka nimsindikize. Nilijishaua kwa muda kwani sikutaka aelewe kwamba nilisimamishwa masomo kutokana na kukosa ada, nikamdanganya kwamba nitakuwa shuleni mpaka jioni.

    Japokuwa nilikuwa nampenda sana, sikutaka kujirahisisha kwa kuogopa kushusha hadhi yangu, nikaendelea kumdengulia mpaka mwenyewe akaahirisha na kusema basi tutakutana Jumamosi, saa nane mchana. Baada ya mazungumzo marefu, tulitakiana usiku mwema kisha akakata simu.

    Nikaanza kujilaumu kwa nini sikukubali ombi lake la kumsindikiza huko alikokuwa anataka kwenda. Nilijiona mjinga kwa kusingizia kwamba nitakuwa shuleni wakati ukweli ni kwamba sikuwa nikienda. Nikaendelea kumuwaza mpaka usingizi uliponipitia.

    Siku zikawa zinasonga mbele huku akinipigia simu mara kwa mara, kunitumia meseji nzuri na kunirushia vocha kwenye simu yangu. Nikajikuta nikizidi kumpenda ingawa bado sikuwa na ujasiri wa kumueleza nilichokuwa nakiwaza. Hali kadhalika, naye hakuwa amenitamkia neno lolote la mapenzi ingawa alionesha kunijali na kupenda kuwa karibu nami.

    Hatimaye Jumamosi iliwadia, siku ambayo Jimmy aliniambia kuna sehemu anataka nimsindikize. Niliwahi sana kuamka siku hiyo, nikaanza kufanya kazi za pale nyumbani kwa bidii ili niwahi kumaliza. Nilijiapiza kuwa lazima saa nane mchana niwe nimeshafika pale tulipokubaliana kukutana na Jimmy.

    Ilipofika saa sita za mchana, tayari nilikuwa nimeshafanya usafi kila sehemu na kuwapikia chakula ndugu zangu, nikawawekea kwenye ‘hotpot’ kisha nikaenda bafuni kuoga.

    Nilipomaliza, nilirudi chumbani kwangu na kuanza kujipodoa. Safari hii nilitumia muda mrefu zaidi nikiwa nyuma ya kioo kwani nilikuwa na vipodozi vingi nilivyovinunua kwa kutumia fedha alizonipa Jimmy.

    Nilipomaliza kujiandaa, nilichagua gauni zuri ambalo lilinipendeza sana, nikiwa najiandaa kuondoka bila kuweka bayana nakwenda wapi, nilishtuka baada ya kusikia sauti ya mama nje. Nilishangaa kwa sababu haikuwa kawaida yake kurudi nyumbani mchana.

    Nilipomsikiliza vizuri, nilibaini kuwa alikuwa na hasira sana kwani alikuwa akimfokea kila mtu. Hata hivyo, sikutaka kujua nini kilichomuudhi. Ili kukwepa maswali mengi, nilisubiri mpaka aingie chumbani kwake, nikatoka kimyakimya bila mtu yeyote kuniona.

    Saa nane juu ya alama, tayari nilikuwa nimefika pale tulipokubaliana na Jimmy, baada ya kusimama kwa muda mfupi, nikamuona akija na gari lake. Akateremka na kunikumbatia, tukasalimiana kwa uchangamfu kisha akanifungulia mlango, nikaingia kwenye gari na kukaa kushoto kwake, akaondoa gari bila mimi kujua tunakwenda wapi.

    “Naomba usichelewe kunirudisha nyumbani kwa sababu nimefanya kutoroka tu, mama yangu ni mkali sana,” nilimwambia Jimmy huku nikimrembulia macho yangu mazuri, nikamuona ananitazama kama anayepania jambo fulani ndani ya moyo wake.

    Aliniitikia kwa kutingisha kichwa huku uso wake ukiwa umejawa na tabasamu pana, mtoto wa kike nikazidi kuchanganyikiwa. Aliendesha gari kwa muda mrefu, mara tukatokezea kwenye jengo kubwa la kisasa lililokuwa limeezekwa kwa makuti upande wa mbele.

    Bila hata kuuliza, nilijua pale ni hotelini, mlinzi akafungua geti na Jimmy akaingiza gari mpaka kwenye maegesho.

    “He! Kumbe tumekuja baharini?” nilimuuliza kwa mshangao baada ya kubaini kuwa kumbe hoteli hiyo ya kifahari, ilikuwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi, upepo mwanana ukipiga kutokea baharini na kunifanya nijisikie kama nipo peponi.

    Japokuwa mimi na ndugu zangu tulikulia Dar es Salaam, hatukuwa na mazoea ya kutembelea sehemu za starehe kama hizo. Nakumbuka kwa kipindi chote cha maisha yangu, niliwahi kwenda ufukweni mara moja tu, tena ikiwa ni safari ambayo iliandaliwa na walimu wetu shuleni.

    Kitendo cha Jimmy kunileta ufukweni, kilinifurahisha kuliko kawaida. Baada ya kupaki gari vizuri, tuliteremka na kuelekea upande wa ufukweni ambapo kulikuwa na miamvuli na viti vya kisasa, huku watu mbalimbali hasa Wazungu wakiwa wamejipumzisha wakipunga upepo.

    “Jisikie huru Eunice,” Jimmy aliniambia huku akiwa amenishika mkono, akanielekeza sehemu ya kukaa huku akitumia muda mwingi kunitazama, hasa usoni na kifuani kwangu. Nikaanza kuhisi aibu za kikekike. Nikajikaza na kukaa, akamuita mhudumu.

    “Utakunywa nini?” Jimmy aliniuliza huku akiendelea kunitazama, nikamjibu kwamba soda inatosha, jambo ambalo alilipinga sana.

    “Unakunywa soda kwani wewe mgonjwa?” aliniuliza huku akitabasamu, akaniambia anataka kunionjesha kitu cha tofauti.

    “Lakini mimi sinywi pombe,” nilimkatisha lakini akanitoa wasiwasi kwamba hata yeye huwa hanywi pombe, akaniambia anataka kuagiza mvinyo laini ambao tutakunywa wote. Sikumpinga kwani hata huo mvinyo sikuwa naujua ni kitu gani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tuletee Red Merlot chupa moja na glasi mbili,” alisema Jimmy huku akitoa kadi inayofanana na ya ATM, akampa yule mhudumu kisha akaendelea kunipigisha stori. Nilimuuliza kwa nini amempa mhudumu kadi badala ya fedha, akacheka sana na kuanza kunielewesha kwamba yeye hufanya manunuzi kwa kutumia kadi za malipo na siyo fedha ‘keshi’.

    Alinifafanulia kwa kina mpaka nikamuelewa. Muda mfupi baadaye yule mhudumu nadhifu akaja akiwa amebeba chupa kubwa iliyokuwa na maandishi ya Red Merlot, akaiweka mezani na glasi zake ndefu kisha akaanza kuifungua.

    Baada ya kumaliza kufungua, alimrudishia Jimmy kadi yake kisha akaondoka. Akachukua glasi yangu na kumimina kinywaji kile ambacho kilikuwa na rangi nyekundu kisha akanisogezea, na yeye akamimina glasi yake kisha akanitaka tugongesheane ‘chiazi’, nikafanya hivyo na sote tukafurahi sana na kuanza kunywa.

    “Mh! Kumbe tamu hivi,” nilisema huku nikipiga funda la pili, Jimmy akatabasamu bila kujibu kitu, kwa mara nyingine akanikazia macho usoni na kwenye kifua changu, nikakwepesha macho yangu kwa aibu za kikekike.



    “Mbona unaniangalia sana Jimmy?”

    “Eunice, wewe ni mzuri sana, nimejikaza nisikwambie lakini naona nashindwa. Umeumbika kama malaika?” alisema Jimmy, kauli iliyozidi kunifanya nione aibu kwani sikuwahi kusifiwa kiasi hicho na mwanaume. Japokuwa na mimi nilikuwa nampenda sana Jimmy, bado aibu zilinitawala kiasi cha kunifanya nikose uhuru.

    Jimmy aliendelea kunipamba kwa maneno matamu, akikisifia karibu kila kiungo cha mwili wangu, nikawa naendelea kunywa mvinyo kama njia ya kujificha na aibu nilizokuwa nazihisi.

    Wakati nikiendelea kunywa, nilianza kuhisi kama nimeanza kulewa kwani kuzungumza kwangu kulibadilika, nikawa nahisi mdomo umekuwa mzito huku muda mwingi nikiutumia kucheka na kurembua macho.

    Nadhani Jimmy aliyaona mabadiliko hayo, akawa anazidi kunichombeza kwa maneno matamu huku muda mwingine akinigusa sehemu mbalimbali za mwili wangu, nikajikuta nikisisimka kupita kawaida.

    Alimuita tena mhudumu na kumuagiza atuletee kuku mzima wa kuchoma na chipsi. Akaniambia wakati tunaendelea kusubiri chakula, tukanyooshe miguu kwa kutembea kwenye mchanga wa bahari, wazo nililolikubali bila kipingamizi.

    Nilipojaribu kusimama, nilijihisi kuishiwa nguvu, nikagundua kuwa ule mvinyo niliokuwa naufakamia kwa fujo, ulikuwa na kilevi ambacho sasa kilishaanza kufanya kazi. Jambo ambalo nililipenda kuhusu mvinyo huo ni kwamba kwa kadiri nilivyokuwa naendelea kunywa, ile hofu niliyokuwa nayo juu ya Jimmy ilikuwa ikizidi kupungua.

    Nikawa sitetemeki tena wala aliponikazia macho kifuani na usoni sikuogopa tena zaidi ya kuzidi kuyarembua macho yangu mazuri, nikamuona alivyokuwa anazidi kuchanganyikiwa. Alinishika mkono na kunisaidia kutembea, tukaelekea kwenye mchanga wa bahari huku akiendelea kunichombeza kwa maneno ya hapa na pale.

    “Kwa nini haniambii haraka kwamba ananipenda? Au hajavutiwa na mimi? Lakini mbona ananisifia sana? Lazima atakuwa ananipenda,” nilijiuliza maswali mengi kichwani wakati tukiendelea kutembea taratibu kwenye mchanga, nikajikuta nimejilaza kwenye bega lake kimahaba, naye akapitisha mkono wake na kunishika kiunoni, jambo lililozidi kunifanya nichanganyikiwe.

    Tukasogea mbali ambako hakukuwa na watu, tukatafuta sehemu nzuri na kukaa huku Jimmy akiendelea kunifanyia vituko vya kimahaba. Sijui nini kilitokea lakini nilijishtukia nimemkumbatia Jimmy kwa nguvu, na yeye akafanya kama mimi, nikawa napumua kwa kasi kama nilikuwa nakimbizwa na mnyama mkali.

    “Eunice!” Jimmy aliniita kwa sauti ya huba.

    “Abee,” niliitikia huku nikimtazama kwa macho yangu ambayo sasa yalikuwa mithili ya mtu aliyetoka usingizini.

    “Najihisi kukupenda sana, kwani una mpenzi?” aliniuliza Jimmy huku akiwa amenikazia macho usoni. Nilifurahi sana kumsikia akisema maneno hayo kwani kiukweli na mimi nilitokea kumpenda sana ingawa sikuwa na ujasiri wa kumtamkia zaidi ya kumsubiri yeye ndiyo aseme.

    “Nilitingisha kichwa kuashiria kwamba sikuwa na mpenzi kama alivyoniuliza, na mimi nikawa namtazama usoni huku macho yangu yakizidi kulegea. Nikamuona anausogeza uso wake karibu kabisa na wangu kisha tukagusanisha ndimi zetu.

    Sikuwa na uelewa wowote kuwa watu wanapogusanisha midomo yao huwa wanafanya nini, nikabaki nimezubaa nikitegemea yeye ndiyo anioneshe cha kufanya. Mara kwa mara nilikuwa nawaona watu runingani kwenye tamthiliya wakifanya kama vile Jimmy alivyokuwa anataka kufanya lakini sikuwa naelewa ni kitu gani wanachofanya.

    Jimmy alifanya kazi yake vizuri ya kunifundisha nini cha kufanya, ndimi zetu zikawa zinagusana na kusababisha nijihisi hali ya tofauti kabisa ambayo sikuwahi kuihisi tangu nizaliwe.

    Sijui ni kwa sababu ya mvinyo niliokuwa nimekunywa au mapenzi niliyokuwa nayo kwa kijana huyo kwani hata alipotaka kuniachia, niliendelea kumng’ang’ania kwa nguvu huku mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio.

    Tulikuja kushtuliwa na mhudumu ambaye alitupa taarifa kwamba chakula tulichokuwa tumeagiza, kilikuwa tayari. Kwa aibu tukainuka pale tulipokuwa tumekaa, tukarudi kwenye viti vyetu huku mimi nikitazama chini muda wote.

    Tulipofika tulikuta kuku mzima ameandaliwa mezani kama Jimmy alivyokuwa ameagiza, tukaanza kula taratibu huku akinitolea minofu na kuniwekea upande wangu.

    Kitendo hicho kilinifanya niamini kwamba ni kweli Jimmy ananipenda sana kwani wakati mwingine alikuwa akinilisha kisha kunipiga mabusu. Hatukujali watu waliokuwa wanatutazama pembeni, tukaendelea kula raha.

    Mara simu ya Jimmy ilianza kuita mfululizo lakini badala ya kuipokea, alikuwa akiikata na kuonesha kutofurahishwa kwake na mtu aliyekuwa anampigia. Mpigaji naye hakuchoka, mara kwa mara akawa anapiga na kusababisha usumbufu mkubwa kwa Jimmy, nilimuona akibadilika na uso wake ukawa na mikunjo ya hasira.

    “Kwani ni nani anayekusumbua?” niliuliza kwa hofu kwani sikujua namna ambavyo angelipokea swali langu lakini kwa bahati nzuri, alionesha tabasamu hafifu kisha akaniambia wala nisijali sana kwani ni mambo yake ya kazi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipoona hali ile haijanifurahisha, aliamua kuizima simu yake na kuiweka mfukoni, tukaendelea kula huku tukifanyiana mambo mbalimbali yaliyozidi kunifanya nijione kama malaika. Baada ya kumaliza kula, Jimmy aliagiza chupa nyingine ya Red Merlot, akawa ananihimiza ninywe.

    Kwa kutotaka kumuudhi, kweli nilionesha bidii kunywa, ikafika mahali nikawa sijitambui tena kutokana na kulewa, muda wote nikawa nataka Jimmy anikumbatie. Sikuelewa tena kilichoendelea mpaka nilipokuja kuzinduka na kujikuta nipo sehemu ambayo sijawahi kufika.

    “Hapa ni wapi?” nilijiuliza baada ya kufumbua macho, mwili wangu wote ukiwa na uchovu uliopitiliza. Nilijikuta nimelala kwenye kitanda cha kisasa kilichokuwa na mashuka laini yanayonukia vizuri. Kuta za chumba hicho zilikuwa zimenakshiwa kwa rangi nzuri huku kukiwa na mapambo ya kifahari ukutani.

    Nilipoinua kichwa na kutazama pembeni, niligundua kuwa nipo chumbani ingawa sikujua ni chumba cha nani na nimefikaje. Nilishtuka zaidi baada ya kugundua kuwa nilikuwa nimelala na nguo yangu ya ndani tu, jambo ambalo siyo kawaida yangu.



    Niliendelea kushangaa huku na kule nikiwa siamini kabisa, nilipotazama saa ya ukutani iliyokuwa ndani ya chumba hicho, niligundua kwamba tayari ilikuwa ni saa kumi na mbili za asubuhi.

    “Mungu wangu, nimelala nje? Nitajibu nini kwa mama,” nilijiuliza huku nikipeleka mikono yangu kwenye ‘ikulu’ yangu kwani nilianza kukumbuka kilichotokea jana yake. Nilikumbuka jinsi nilivyoenda ufukweni na Jimmy ambapo tulifanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kunywa mvinyo mpaka nikapoteza ‘network’.

    Kwa harakaharaka nilijua aliyenifanyia yote hayo ni Jimmy na akili yangu ikanituma kuamini kwamba lazima atakuwa ameniingilia kimwili. Hata hivyo nilishangaa kuikuta ikulu yangu ikiwa salama kabisa kuonesha kwamba ‘glasi’ yangu haikuwa imevunjwa.

    Nikiwa naendelea kujiuliza maswali yaliyokosa majibu, nilishtuka baada ya kusikia mlango wa chumba hicho ukifunguliwa, akaingia Jimmy aliyekuwa amejifunga taulo tu, nikashtuka sana na kuanza kutetemeka kwa hofu. Japokuwa nilikuwa nampenda sana Jimmy, niliona kama mambo yanaenda harakaharaka sana.

    Jimmy ni kama alijua hofu niliyokuwa nayo moyoni, akanionesha dhahiri kwamba hakuwa akifikiria nilichokuwa nakiwaza akilini. Alinisogelea pale kitandani na kuniuliza naendeleaje, nikaanza kumlaumu kwa nini amesababisha nilale nje ya nyumbani kwetu. Akaniambia nisiwe na wasiwasi kwani nipo kwenye mikono salama na atanisaidia kuwaeleza wazazi wangu kilichotokea.

    Kidogo hofu ilipungua, akaniambia niamke ili nikaoge. Akanirushia taulo na kunielekeza bafu lilipokuwa. Kwa aibu za kikekike nikainuka huku nikiendelea kushangaa jinsi nyumba hiyo ilivyokuwa nzuri, ikiwa imepambwa kwa vitu vya thamani kubwa utafikiri tupo Ulaya. Sakafu yote ilikuwa na marumaru za kisasa pamoja na zulia la bei mbaya.

    Nilienda mpaka bafuni ambapo nilikutana na sinki kubwa lililokuwa na maji ya uvuguvugu huku povu jingi la sabuni ya kuogea likinukia vizuri. Japokuwa nilikuwa mgeni na mambo hayo, sikutaka kuonesha ushamba, nikajikaza na kuoga harakaharaka kisha nikarudi chumbani na kuvaa nguo zangu.

    Nilikuta tayari Jimmy ameshavaa nguo zake na kuandaa kifungua kinywa chumbani, akanikaribisha kwa uchangamfu. Wakati tukiendelea kupata kifungua kinywa, niliona kitu juu ya meza ambacho kilinishtua sana.

    Ulikuwa ni mkufu wa kike ambao kwa kumbukumbu za harakaharaka nilihisi kuna sehemu niliwahi kuuona. Nikajaribu kuvuta kumbukumbu lakini sikukumbuka nimewahi kuuona wapi. Sikutaka tena kuendelea kupata kifungua kinywa, nikabadilika.

    “Huu mkufu ni wa nani?” nilimuuliza Jimmy huku nikiwa tayari nimeshaushika mkononi. Jimmy ni kama alizielewa hisia zangu, akaanza kunieleza kwamba mkufu huo ni mpya na ameununua kama zawadi kwa ajili ya mama yake.

    Sijui ni kwa nini nilikuwa namuamini sana Jimmy kwani aliponiambia hivyo tu, nilishusha pumzi ndefu na kukubaliana na alichokisema, akanihakikishia kwamba nisiwe na wasiwasi hata kidogo kuhusu yeye kwani hana mwanamke mwingine zaidi yangu na ndiyo maana hakuwa na haraka na penzi langu.

    “We hushangai tumelala wote usiku kucha, tena ukiwa hujitambui kwa mvinyo lakini sijakugusa wala kukufanya chochote? Amini kwamba nakupenda kwa dhati na lengo langu siyo kukuchezea bali nataka nikuoe kabisa,” alisema Jimmy kwa sauti ya upole, nikajikuta nikishindwa kujizuia, nikamkumbatia na kumbusu shavuni, na yeye akanifanyia hivyohivyo.

    Tuliendelea kupata kifungua kinywa huku Jimmy akinisemesha mambo mbalimbali. Tulipomaliza, nilimuaga kwamba nataka kuondoka kurudi nyumbani, akainuka na kwenda kufungua droo ya kitanda chake na kutoa noti nyingi za shilingi elfu kumikumi.

    Akanikabidhi huku akiniambia kuwa niangalie vizuri ramani ya nyumba hiyo ili siku nyingine nikitaka kuja nisipotee. Kidogo nilisita kumuitikia kwani ukweli ni kwamba tangu niingie ndani ya nyumba hiyo, kulikuwa na kila dalili kwamba Jimmy haishi peke yake. Haikuwa rahisi kwa mwanaume kama yeye kuifanya nyumba iwe safi kiasi hicho, niliamini lazima kuna mwanamke anaishi naye ingawa sikuwa na uhakika na hilo.

    “Unaniruhusu niwe nakuja mwenyewe hapa kwako, siku nikikutana na mke wako je?”

    “Mimi sina mke Eunice, wewe ndiyo chaguo langu, kuwa huru na pachukulie hapa kama nyumbani kwako, umenielewa mpenzi!” alisema Jimmy, kama kawaida yake kwa sauti ya kubembeleza.

    Mtoto wa kike nikajikuta namuamini kupita maelezo. Alinitoa mpaka nje ambapo kwa macho yangu nilishuhudia magari manne ya kifahari yakiwa yamepaki uani. Nilipoitazama nyumba hiyo kwa nje, niliishia kuguna kwani ama kwa hakika ilikuwa nzuri mno.

    “Hapa ni kwako na kila kitu kilichopo hapa ni kwa ajili yetu, mimi na wewe,” Jimmy aliniambia wakati akinielekeza kuingia ndani ya gari, nikatabasamu kwa furaha kwani ilikuwa ni zaidi ya miujiza kwangu.

    Akawasha gari kisha tukaondoka, tukiwa njiani ndipo mawazo juu ya nitakachomjibu mama kuhusu mahali nilikolala yalipoanza kunisumbua.

    “Ulisema utanisaidia kumueleza mama yangu juu ya mahali nilikolala?”

    “Yaah! Kazi ndogo sana hiyo, tutapitia hospitali ambapo tutazungumza na daktari mmoja rafiki yangu akuandikie kwamba ulianguka ghafla na kupoteza fahamu tangu jana hivyo wakalazimika kukupa ‘bed rest’.

    “Ukifika nyumbani jitahidi kuonesha kwamba unaumwa kweli na kwa sababu utakuwa na vyeti vya hospitali kazi itakuwa nyepesi,” Jimmy aliniambia kwa kujiamini, nikajikuta ile hofu yote ikiniisha.

    Kama alivyosema, kweli tulipitia kwenye hospitali moja ya kisasa ambapo Jimmy alinipeleka moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya daktari mmoja ambaye ilionesha wanafahamiana sana, akamueleza mpango wake ambapo daktari huyo alifanya kama alivyoambiwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Cheti kikaandikwa kwamba eti nilifikishwa hospitalini hapo nikiwa sijitambui na kwa kuwa sikuwa na uwezo wa kuzungumza wala kueleza ndugu zangu wapo wapi, walilazimika kunipa ‘bed rest’ mpaka nilipozinduka siku ya pili. Ilikuwa ni mbinu kali ambayo niliamini lazima mama ataikubali.

    Baada ya hapo, tuliondoka na kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwetu. Tukiwa njiani, simu ya Jimmy ilianza kuita mfululizo kama ilivyokuwa jana yake lakini hakuipokea, akawa anaikata kila ilipoita.

    Nilishangazwa sana na tabia hiyo ya Jimmy, sikuelewa ni nani alikuwa akimpigia na kwa nini alikuwa hataki kupokea simu yake. Sikutaka kumuuliza chochote kwa kuhofia kumuudhi.

    “Watu wengine bwana, yaani mtu anakupigia simu kama anakudai hadi inakuwa kero, siwezi kupokea simu yoyote ya kazi nikiwa na wewe mpenzi wangu,” Jimmy alisema huku akiizima kabisa simu yake, sikumjibu kitu zaidi ya kuonesha tabasamu hafifu.

    Safari iliendelea hadi tukafika pale tulipokuwa tukikutania na Jimmy, jirani na nyumbani kwetu. Kabla sijateremka kwenye gari, alinibusu kwenye mdomo wangu na kuniambia kuwa nisisahau yote tuliyozungumza.

    Akaniahidi kuwa kesho yake atakuja kunichukua tena, nikashuka huku nikiwa na furaha kuliko kawaida. Nilimsindikiza kwa macho mpaka alipopotea kwenye upeo wa macho yangu.

    Nikiwa nimesimama palepale, nilitoa pochi yangu ndogo na kuanza kuhesabu fedha nilizopewa na Jimmy. Sikuamini macho yangu baada ya kugundua kuwa zilikuwa shilingi laki mbili. Nilijiuliza maswali mengi sana yaliyokosa majibu wakati nikitembea kuelekea nyumbani.

    Iweje Jimmy anipe fedha nyingi kiasi kile huku akionesha kutokuwa na haraka ya penzi langu? Ilifika mahali nikaamini kwamba huenda ni kweli Jimmy alikuwa anataka kunioa na siyo kunichezea na kuniacha. Nikajikuta nikizidi kumpenda maradufu.

    Nilipofika nyumbani, tayari nilishavaa uso wa ugonjwa, nikamfuata mama moja kwa moja chumbani kwake na kutaka kumueleza kilichonitokea. Cha ajabu nilimkuta mama akiwa kwenye hali iliyoonesha kwamba alikuwa akilia kwa muda mrefu.

    Ilivyoonesha kumbe hata hakuwa na taarifa kwamba sikulala ndani kwani aliponiona tu, aliniuliza kama nimeshawapikia chai ndugu zangu. Nilipomjibu kwamba bado, aliniambia nikafanye hivyo huku yeye akiendelea kulia, muda mwingi akionekana kuhangaika na simu yake.



    Nilitoka na kwenda kuzungumza na kaka yangu ambaye jambo la kwanza aliniuliza nilipolala, kabla sijamjibu nilimuuliza kuhusu mama, akaniambia kuwa tangu jana yake alikuwa amejifungia chumbani kwake akilia kwa uchungu, akanitoa wasiwasi kwamba hata hakuwa akijua kwamba sikulala ndani, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama kaka yangu.

    Ushahidi wa uongo niliotaka kumuonesha mama, niliutumia kwa kaka yangu, akashtuka sana kusikia nilikuwa nimelazwa. Nilipomuonesha na vyeti, akaamini kwamba ni kweli ila nikamuomba asimwambie mama chochote.

    Kwa kuwa kaka yangu hakuwa na makuu, alinielewa. Akaanza kunieleza kuhusu mama ambapo aliniambia kuwa tangu jana yake alikuwa akilia huku akiongea mwenyewe kama mwendawazimu.

    Tulijaribu kuulizana kinachomliza lakini hakuna aliyekuwa na jibu. Nikawaandalia chai ila kwa kuwa mimi nilikuwa nimeshiba, nilienda chumbani kwangu kupumzika, hisia tamu juu ya Jimmy zikiendelea kupita kichwani mwangu.

    Nikiwa katikati ya hisia tamu, taswira ya Jimmy ikiendelea kupita ndani ya kichwa changu, nilishtuka baada ya kusikia mtu akigonga mlango wa chumba changu kwa nguvu. Nikajifunga kitenge na kwenda kufungua, nikakutana uso kwa uso na kaka yangu.

    “Dada Eunice, hebu kajaribu kumuuliza mama kinachomfanya aendelee kulia kwa muda wote huo, huenda kuna tatizo kubwa limempata,” kaka yangu aliniambia.

    “Siwezi kaka, si unajua bado naumwa na nahitaji kupumzika? Nenda wewe atakusikiliza na huenda akakwambia kinachomsumbua.”

    “Hapana Eunice, wewe ndiyo tunakutegemea na isitoshe, upo karibu na mama kuliko sisi watoto wa kiume,” alisema kaka huku akiendelea kuning’ang’aniza. Kiukweli nilikasirika kwa sababu alinihamisha kutoka kwenye ulimwengu wa raha na kunirudisha mahali ambapo sikuwa nikipapenda.

    Tangu mama aanze kutuzungusha kutulipia karo ya shule na kutufanya tuendelee kusota nyumbani, sikuwa nikimpenda tena na kumchukulia kama mwanamke katili ambaye hakuwa na nia nzuri kwenye maisha yetu ya baadaye. Pia alionesha dhahiri kushindwa kuiongoza familia tangu baba alipotutoka, jambo lililozidi kunifanya nimchukie. Haikuniingia akilini kwamba mali zote na fedha alizoacha marehemu baba zilikuwa zimeyeyuka na kuisha haraka kiasi hicho wakati hata nusu mwaka ulikuwa bado haujapita tangu baba atutoke.

    Nilihisi lazima kuna mchezo mchafu mama anaufanya kuhusu mali alizoziacha baba ingawa sikujua kwa haraka ni mchezo gani. Baada ya kaka yangu kuniambia hivyo, nilijifikiria kwa muda huku nikijishauri kama niende au nisiende. ILIPOISHIA:

    Kaka alipoendelea kunisisitiza, nilipiga moyo konde na kuamua kwenda hivyohivyo, nikavaa vizuri na kwenda kumgongea mama mlango. Niligonga kwa muda mrefu lakini hakufungua, nikawa namsikia akiendelea kuangua kilio cha kwikwi kama mtu aliyepokea taarifa mbaya. Niliendelea kugonga kwa nguvu, mama akafungua huku macho yake yakiwa yamevimba na kuwa mekundu sana.

    “Samahani mama nahitaji kuzungumza na wewe japo kwa ufupi.”

    “Hapana, sijisikii vizuri kwa sasa, nahitaji kukaa peke yangu, tutazungumza baadaye.”

    “Lakini mama, unafikiri unatuacha kwenye mazingira gani iwapo hutaki kutushirikisha kwenye tatizo linalokufanya uwe kwenye hali hiyo? Kwani kuna tatizo?”

    “Nimeshakwambia siwezi kuzungumza kwa sasa, mbona huelewi we mtoto?” alisema mama kwa sauti ya ukali kidogo, akausukuma mlango na kuubamiza, nikabaki nimesimama mlangoni huku nikiijutia nafsi yangu kwa kukubali kutimiza nilichoambiwa na kaka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilibidi nimrudishie majibu kaka na kumweleza kila kitu nilichojibiwa na mama. Nilimuona akisononeka sana kutokana na jinsi mama alivyonijibu. Sikutaka kuendelea kujadili tena kuhusu vituko vya mama, nikaenda kujifungia chumbani kwangu kwani bado nilikuwa nikijihisi uchovu.

    Niliendelea kumfikiria Jimmy kwa muda mrefu mpaka nilipopitiwa na usingizi, nikalala fofofo japokuwa nje jua lilikuwa linawaka. Nilikuja kushtuliwa na wadogo zangu waliokuwa wanagonga mlango kwa nguvu, nikajilazimisha kuamka na kwenda kuwasikiliza.

    “Dada njaa inauma, katupikie chakula,” alisema mdogo wangu wa mwisho, nilipotazama saa kwenye simu yangu, nilishtuka baada ya kugundua kuwa tayari ilikuwa ni saa nane za mchana.

    Harakaharaka nilienda bafuni kujimwagia maji kisha nikarudi chumbani na kuchukua noti moja ya shilingi elfu kumi kati ya zile nilizopewa na Jimmy jana yake. Nikakimbia hadi gengeni ambapo nilinunua mahitaji muhimu kisha nikarudi na kuanza kuandaa chakula cha mchana.

    Wakati nikiendelea na kazi hiyo, nilikumbuka kuwa tulikuwa tumeahidiana na Jimmy kukutana ambapo aliniambia atanifuata nyumbani kwetu, nikaongeza kasi ya kuandaa chakula cha mchana. Nilipoivisha tu, sikutaka kusubiri kula, nikaenda tena bafuni kuoga kisha nikajifungia chumbani kwangu na kuanza kujipodoa. Nikatumia muda mwingi nyuma ya ‘dressing table’ mpaka nilipohakikisha nimependeza.

    Nikaanza kuchagua nguo za kuvaa. Kila niliyoichukua niliona haifai, nikabadili zaidi ya mara tano mpaka nilipopata gauni langu ambalo sikuwa nikipendelea kulivaa kwani lilikuwa fupi na lilikuwa likikiacha kifua changu wazi.

    Sijui kwa nini niliamua kulichagua hilo wakati siku zote nilikuwa natamani kuligawa kwani sikuzoea kuvaa nguo fupi zinazoacha maungo yangu wazi. Nikiwa naendelea kujiandaa, ujumbe mfupi uliingia kwenye simu yangu kutoka kwa Jimmy akinitaarifu kwamba ameshafika.

    “Jimmy akiniona mwenyewe atadata na roho yake,” nilijisema wakati nikijizungusha mbele ya kioo. Kwa kuwa nguo hiyo iliacha wazi sehemu kubwa ya mapaja yangu mazuri na kifua changu kibichi, niliona siyo vizuri kutoka nyumbani huku kila mtu akiniona, nikavaa khanga kwa juu na kujitanda ushungi.

    Bila kumuaga mtu, nilitoka harakaharaka na kuwaacha ndugu zangu wakiendelea kula chakula cha mchana, nikakaza mwendo na kwenda mpaka sehemu yetu ya kukutania ambapo nilimkuta Jimmy ameshawasili akinisubiri.

    Aliponiona, alinikumbatia na kunibusu mdomoni, kwenye mashavu na shingoni, na mimi nikafanya hivyohivyo bila kujali watu ambao wangeweza kutuona. Sijui ndiyo upofu wa mapenzi au kitu gani kwani nikiwa na Jimmy, nilikuwa na uwezo wa kufanya mambo ambayo sikuwahi kuyafanya ilimradi tu nimuone akifurahi.

    “Whaooo, umependeza,” alisema Jimmy baada ya mimi kuvua khanga na ushungi niliokuwa nimeuvaa wakati natoka nyumbani, nikabaki na kigauni changu. Jimmy akanifungulia mlango wa gari, nikatabasamu huku nikiyarembua macho yangu mazuri.

    Na yeye akaingia na safari ya kuelekea nyumbani kwake ikaanza. Tulipofika kwake, alinikaribisha kwa uchangamfu, nilipoingia ndani tu, alinibeba juujuu na kuanza kuniangushia mvua ya mabusu tena, akanibeba kama mtoto mpaka chumbani kwake, akanibwaga kitandani kisha nikamuona akiufunga mlango kwa funguo.

    Akavua shati lake kisha suruali, akanisogelea pale kitandani huku akionekana kuchanganyikiwa kabisa, akawa anapumua kwa nguvu kama ametoka kukimbia marathon.

    Nikampokea na kumkumbatia kifuani kwangu kwa mahaba, tukagusanisha ndimi zetu na kuanza kuelea kwenye ulimwengu wa tofauti huku mapigo ya moyo wangu yakiongezeka kama ilivyokuwa kwa Jimmy.

    Hata sijui nini kilitokea, tukajikuta wote tupo kama tulivyotoka kwenye matumbo ya mama zetu. Japokuwa ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kuwa katika hali ile na mwanaume, nilijitahidi kuonesha kwamba na mimi siyo mtoto.

    Nikaendelea kujikaza na kuonesha ushirikiano kwa kila kitu alichokuwa anakitaka Jimmy, tukawa tunaelea kwenye ulimwengu wa tofauti huku nikijihisi hali ambayo sikuwahi kuihisi tangu nazaliwa.

    Furaha yangu ilitibuka ghafla, sijui Jimmy alifanya nini kwani nilihisi maumivu makali mno, nikauma meno lakini haikusaidia kitu, nikajikuta napiga kelele kwa nguvu lakini bado haikusaidia kitu. Jimmy hakuwa tena na huruma na mimi.

    Siwezi kusahau kwa jinsi nilivyojisikia maumivu siku hiyo, mpaka Jimmy ananiachia, eneo lote likabadilika na kuwa kama machinjioni. Nikawa naendelea kulia kwa uchungu huku nikijiuliza niliyaanzaje mambo hayo.



    Jimmy alinibembeleza na kuniambia kuwa eti sasa nimeshakuwa mkubwa, akaniahidi vitu vingi vizuri ambavyo angalau vilinifanya nijihisi ahueni. Jimmy alinibeba na kunipeleka bafuni ambapo nilijimwagia maji huku nikiendelea kuhisi maumivu makali.



    Tuliporudi ndani, alinipa vidonge vya kutuliza maumivu.

    “Na hii ndiyo zawadi yako kwa hiki ulichonifanyia leo,” alisema Jimmy huku akinivalisha shingoni mkufu mzuri uliokuwa unang’ara.

    Akaniambia kuwa huo ni mkufu wa dhahabu na aliununua maalum kwa ajili yangu. Nikamshukuru sana, kama hiyo haitoshi, alifungua tena droo iliyokuwa pembeni ya kitanda chake na kutoa bunda la noti nyekundu, akahesabu kadhaa na kunipa.

    Nilimshukuru sana na kumuaga kwamba nataka kurudi nyumbani kwani sikuwa nimeaga.

    Alinisindikiza hadi nje, akanisaidia kupanda kwenye gari lake kwani hata kutembea kwangu kulikuwa ni shida tupu. Akanipeleka mpaka pale tulipokutania, nikashuka kisha tukapungiana mkono wa kwa heri, akageuza gari lake na kuondoka kwa kasi.

    “Sijui mama akiniuliza nitamwambia nini?” nilijiuliza wakati nikipiga hatua fupifupi kuelekea nyumbani, nikichechemea kutokana na maumivu.

    Kwa bahati nzuri, nilipofika nyumbani, hakuna mtu aliyeniona wakati nikiingia, nikanyata hadi chumbani kwangu ambapo nilijifungia na kujitupa kitandani, nikawa naendelea kuugulia maumivu.

    Kwa bahati nzuri siku hiyo hakuna mtu aliyenishtukia lakini kama wahenga walivyosema kuwa mwonja asali haonji mara moja. Kutokana na mapenzi mazito niliyokuwa nayo kwa Jimmy, licha ya kwamba aliniumiza sana mara ya kwanza, nilijikuta nikitamani tena kukutana naye.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wiki moja baadaye, yale maumivu ya awali yakiwa yamepungua sana, nakumbuka ilikuwa ni Jumapili asubuhi, nilimpigia simu Jimmy na kumwambia kuwa nataka kuonana naye muda ule. Hakupinga ombi langu, akaniambia kuwa na yeye alikuwa na hamu kubwa ya kuonana na mimi. Akanielekeza kuwa nipande bodaboda yeye atalipa.

    Mtoto wa kike sikulaza damu, nikajipara harakaharaka nikapendeza haswaa, nikauvaa ule mkufu wa dhahabu niliopewa na Jimmy kisha nikatoka kinyemela mpaka mtaa wa pili, nikakodi bodaboda iliyonipeleka mpaka nyumbani kwa Jimmy. Kwa kuwa mwenyewe nilikuwa na fedha zangu, nilimlipa dereva wa bodaboda kisha nikagonga geti, muda mfupi baadaye Jimmy alikuja kunifungulia.

    Akanikumbatia kwa mahaba na kunikaribisha ndani. Kwa mara nyingine nikampa mwili wangu na kumuachia afanye anachotaka. Tofauti na mwanzo, safari hii sikuumia sana, nikajitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kumfurahisha Jimmy nikiamini yeye ndiyo mume wangu na baba wa watoto wangu. Siku hiyo tulikaa muda mrefu mpaka majira ya saa kumi za jioni, nikaondoka nikiwa nimechoka kuliko kawaida.

    Kama kawaida, Jimmy alinisindikiza mpaka pale tunapokutania siku zote. Tulipofika alinikumbatia kwa nguvu na kunibusu kila sehemu, akanishukuru kwa yote niliyomfanyia na kunisifia kuwa eti japokuwa nilikuwa mdogo na mgeni wa mambo ya kikubwa, nilimpa raha ambazo hakuzitegemea.

    Nilicheka kwa aibu na kutazama chini, akanibusu tena kisha akafungua ‘dashboard’ ya gari lake na kutoa bunda la noti nyekundunyekundu, akanibusu tena kisha tukaagana. Nikashuka na kusimama pembeni, nikamuangalia wakati anageuza gari lake kisha akanipungia mkono na kuondoka.



    Harakaharaka nikaanza kujikongoja kuelekea nyumbani huku nikijiuliza nitamjibu nini mama endapo nitamkuta kwani haikuwa kawaida yangu kuondoka bila kuaga na kuchelewa kurudi kiasi hicho. Kwa bahati nzuri, wakati naingia hakuna mtu yeyote aliyeniona, nikapitiliza chumbani na kujifungia mlango, nikajibwaga kitandani huku nikihisi uchovu wa hali ya juu.

    “Ngo ngo ngo!” Nilisikia mlango wa chumba changu ukigongwa, harakaharaka nikabadilisha nguo na kujifunga kitenge ili nionekane nilikuwepo muda wote, nikainuka na kwenda kufungua mlango.

    “Ulikuwa wapi muda wote huo?”

    “Nilikuwa nimelala mama.”

    “Umelala? Yaani una usingizi gani mpaka nikugongee mlango namna hiyo? Unajua hii ni mara ya ngapi nakuja kukugongea mlango?”

    “Sikwenda popote mama, najisikia vibaya sana ndiyo maana nilikuwa nimelala.”

    “Hivi unanifanya mimi bibi yako si ndiyo? Unafikiri mimi sikupitia huko? Utanieleza ukweli leo,” alisema mama huku akionesha kuwa na hasira, akanishika kwa nguvu, akanivutia kwake na kutaka kuanza kunishushia kichapo lakini ghafla aliacha na kuonekana akiwa amepigwa na butwaa.

    “Umeupata wapi huu mkufu?” alisema huku akiuchunguza vizuri mkufu wa dhahabu niliokuwa nimepewa na Jimmy kama zawadi. Nilishindwa cha kujibu, nikawa najiumauma huku nikianza kutetemeka kwa hofu. Nilijilaumu kwa nini wakati navua nguo sikukumbuka kuuvua na mkufu huo.

    Sijui ni nini kilichomtokea mama kwani ghafla aliushika na kuuvuta kwa nguvu, ukakatika. Akauchukua na kuondoka kwa kasi chumbani kwangu huku akiendelea kuuchunguza kwa makini mkufu huo. Nilibaki najiuliza maswali yaliyokosa majibu kuhusu kilichotokea.



    Nikabaki chumbani kwangu ambapo harakaharaka nilizificha fedha nyingi nilizopewa na Jimmy chini ya godoro langu nikiwa na uhakika kuwa mama atarejea tena baada ya muda mfupi lakini haikuwa hivyo. Niliendelea kukaa kwa hofu kubwa lakini mama hakurudi, zikapita dakika, nusu saa na hatimaye saa moja ikawa imeisha.



    Sikuelewa kwa nini imekuwa hivyo, ikabidi nitoke chumbani kwangu na kuelekea kwenye chumba cha mama, kichwani nikitunga uongo kwamba nikifika nimdanganye kwamba huo mkufu ni wa rafiki yangu Nancy kisha nimuombe msamaha.



    Nilipoukaribia mlango wa chumba cha mama, nilimsikia akizungumza kwenye simu na mtu, huku akionesha kuwa na jazba kali kuliko kawaida. Ikabidi nijibanze na kuanza kumsikiliza.

    “Mwanaume shetani sana wewe, yaani sikutegemea kama unaweza kunifanyia ufirauni mkubwa kiasi hiki. Yaani siku zote hizo nakupigia simu hutaki kupokea kumbe una lako jambo. Ulikuwa unanitafutia sababu si ndiyo? Sasa lazima utakufa kama mwenzako,” alisema mama kwa hasira kisha nikasikia kishindo kikubwa kilichofuatiwa na mlio wa simu iliyopasuka.

    Nilibaki nimeduwaa huku hofu ikizidi kuongezeka ndani ya moyo wangu kuliko awali. Akili ikanicheza haraka kwamba endapo mama atatoka na kunikuta pale mlangoni, naweza kumkasirisha zaidi. Harakaharaka nikanyata na kuondoka kurudi chumbani kwangu. Ile naingia tu, nilisikia mlango wa chumba cha mama ukifunguliwa, akatoka na kutembea harakaharaka kuja chumbani kwangu.



    Kufumba na kufumbua mama aliingia chumbani kwangu na kuja kunivaa mwilini kwa nguvu. Uso wake ulikuwa umefura kwa hasira kama nyoka kobra huku macho yake yakiwa mekundu kama amevuta bangi. Akaanza kunipiga kwa hasira kiasi cha kusababisha damu zianze kunitoka puani kwa wingi, nikajua nisiposema ukweli juu ya mahali nilikokuwa anaweza kuniua.



    Ikabidi nimsihi aache kunipiga na kuahidi kumueleza ukweli wa kila kitu. Huku akihema kwa nguvu, mama aliniachia na kunitishia kwamba nikijaribu kumdanganya chochote, ataniua. Nikawa najifuta machozi na damu huku nikijiandaa kusema ukweli. Ghafla tukashtushwa na mlio wa simu yangu kuonesha kwamba kuna meseji imeingia.

    Mama akanitolea macho akiwa haamini kama na mimi namiliki simu.



    “Una simu? Eunice una simu? Tangu lini? Hebu ilete haraka sana,” alisema mama huku akizidi kupagawa kwa hasira.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sikuelewa nini hasa kilichomfanya mama akawa kwenye hali hiyo. Huku nikitetemeka, nilienda mahali nilipokuwa nimeificha simu yangu, nikaitoa na kuiangalia kabla sijamkabidhi mama. Moyo ukanilipuka kugundua kuwa meseji iliyoingia ilitoka kwa Jimmy. Nikawa najishauri kama nimpe simu mama au nisimpe.



    Wakati naendelea kubabaika, mama bado alikuwa amesimama mbele yangu, akihema kwa nguvu kama faru dume. Kufumba na kufumbua alinipokonya simu, licha ya kujitahidi kumzuia sikuweza kummudu, akaanza kuipekua.

    Cha kwanza alienda sehemu ya meseji na kuifungua, akatulia kwa sekunde kadhaa wakati akiisoma meseji iliyokuwa imeingia muda ule. Mapigo ya moyo yalikuwa yakinienda mbio kuliko kawaida, kijasho chembamba kikawa kinanitoka.

    “Huu ndiyo upumbavu unaoufanya eeeh! Huyu uliyemsevu Honey ni nani?” mama alifoka huku akiwa amenikodolea macho, akiwa ni kama haamini alichokiona. Nikiwa naendelea kujiumauma, alinikunja tena na kuanza kunishushia kipigo cha mbwa mwizi akitaka nimueleze nimepata wapi simu na yule niliyekuwa nachati naye mambo ya mapenzi ni nani.

    Kutokana na kipigo cha nguvu alichokuwa ananishushia, niliamua tu kumueleza ukweli kwani sikuwa na jinsi.

    “Anaitwa Jimmy, ni mpenzi wangu amesema atanioa.”

    “Jimmy? Jimmy gani?”

    Nilianza kumfafanulia mama, cha ajabu alionesha kama anamfahamu ingawa sikuwa na uhakika. Kwa maswali aliyokuwa ananihoji, ilionesha kabisa anamfahamu. Nilipomweleza ukweli, alizidi kupandwa na hasira, akaendelea kunipiga mpaka akanipasua usoni, juu kidogo ya jicho.

    Damu nyingi zilizokuwa zinanitoka ndiyo zilizofanya aache kunipiga, akaondoka na ile simu hadi chumbani kwake na kuniacha naendelea kuugulia maumivu makali niliyoyapata.

    Kaka yangu Gisla ndiye aliyekuja kunisaidia, akanifuta damu na kunisafisha kidonda hicho pamoja na kuuchua mwili wangu kwa maji ya moto. Na yeye alishangaa sana kusikia kuwa nimeanza mambo hayo kwani haikuwa kawaida yangu kabisa.

    Alinipa pole lakini akanisisitiza kuwa makini kwani dunia ya sasa imeharibika. Kwa jinsi nilivyokuwa namheshimu kaka, niliupokea ushauri wake. Akaendelea kunichua mwilini mpaka alipomaliza.

    Tangu mama alipoingia chumbani, hakutoka tena wala sikusikia akiendelea kunifokea kama ilivyokuwa kawaida yake. Muda ulizidi kuyoyoma na hatimaye giza likaingia. Kwa jinsi nilivyokuwa najisikia vibaya, sikuweza hata kupika siku hiyo.

    Nikawa nimejifungia chumbani kwangu. Nilishtushwa na mtu aliyekuwa anagonga mlango kwa nguvu, nikajikongoja na kwenda kufungua. Nikakutana na kaka yangu Gisla ambaye aliniambia kwamba kuna tatizo limetokea.

    “Tatizo gani tena kaka?” nilisema huku nikivaa nguo vizuri. Akaniambia kwamba mama ameanguka ghafla wakati akijaribu kutoka chumbani kwake. Harakaharaka tukatoka na kaka mpaka pale alipokuwa ameangukia mama, huku tukiwa na wasiwasi mkubwa.

    Ni kweli mama alikuwa amelala sakafuni, akiwa hajitambui. Sikujua ni kitu gani kimemtokea na licha ya kuniadhibu vikali, nilijikuta nikimuonea huruma. Tukasaidiana na kaka kumnyanyua, tukamrudisha chumbani kwake.

    Kaka akatoka kufuata teksi nje kwa ajili ya kumkimbiza hospitali kwani hali yake ilikuwa mbaya kiasi cha kumfanya ashindwe hata kupumua. Kwa kuwa nilikuwa na fedha nyingi za akiba nilizopewa na Jimmy, hatukupata shida kuhusu usafiri.

    Tukaondoka na kaka mpaka Muhimbili ambapo mama alipokelewa na kulazwa kwenye kitanda chenye magurudumu, akakimbizwa wodini na madaktari na manesi wakaanza kuhaha kuokoa maisha yake.

    Tulipomuuliza daktari mmoja juu ya kilichomtokea mama, alituambia kuwa amepatwa na mshtuko wa ghafla wa moyo ndiyo maana alianguka. Akatuhakikishia kwamba tusijali, atapona.

    Kwa kuwa na mimi nilikuwa na majeraha mengi mwilini niliyoyapata baada ya kupigwa na mama, ukichanganya na ‘suluba’ niliyoyapata kutoka kwa Jimmy, nilimuomba daktari anipe dawa za kutuliza maumivu kwani mwili wote ulikuwa ukiwaka moto.

    Akanipaka dawa na kunifunga bandeji kwenye majeraha ya usoni kisha akanipa vidonge vya kutuliza maumivu. Tukaendelea kumuuguza mama huku na mimi nikiugulia maumivu makali niliyokuwa nayasikia kutokana na kichapo nilichokipata kutoka kwa mama.

    Usiku huo mimi sikurudi nyumbani, tulikubaliana kwamba nibaki na mama hospitali wakati kaka yeye alirudi kwenda kuangalia usalama wa nyumba na wadogo zetu ambao walikuwa wakihitaji uangalizi wa karibu. Nikalala wodini na mama.

    Kesho yake asubuhi, kaka alinifuata hospitali na tukabadilishana, mimi nikarudi nyumbani kupumzika. Kwa kuwa chumbani kwa mama kulikuwa wazi, nilishindwa kukaa muda mrefu bila kuwasiliana na Jimmy ambaye sasa alikuwa ameshauteka moyo wangu kabisa.

    Nilimheshimu na kumuona kama mtu wangu wa karibu sana, hasa baada ya kumruhusu kuujua mwili wangu, akiwa ndiyo mwanaume wa kwanza maishani mwangu. Nikaenda chumbani kwa mama na kuanza kupekua huku na kule nikitafuta simu yangu.

    Nilifanikiwa kuipata ingawa ilikuwa imezimwa. Harakaharaka nikarudi chumbani kwangu na kujifungia, nikaanza kumpigia Jimmy. Tofauti na siku zote, simu iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa mpaka ilipokata. Nikahisi labda Jimmy alikuwa mbali na simu. Nikajaribu tena na tena lakini bado hali ilikuwa ileile, mwisho simu ikazimwa kabisa.

    Nilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. Hata hivyo sikutaka kumuwazia mabaya Jimmy wangu, nikajilazimisha kuamini kwamba huenda aliibiwa simu au aliiacha sehemu na yeye kwenda mbali. Jioni ilipofika, nilijiandaa na kwenda hospitali kulala na mama ambaye bado alikuwa hajarejewa na fahamu zake.

    Kwa siku mbili mfululizo, mama hakuwa amerejewa na fahamu, hali iliyoanza kututia wasiwasi, tukawa tunahaha tukiwa hatuelewi nini cha kufanya. Moyoni nilijihisi kuwa na hatia sana kwani niliamini mimi ndiyo chanzo cha yote. Jimmy naye hakuwa akipatikana tena kwenye simu licha ya kujitahidi kumpigia mara kwa mara.

    Siku ya tatu, mama alifumbua macho yake ingawa bado hakuwa na uwezo wa kuzungumza wala kufanya chochote. Tulifurahi sana na kumshukuru Mungu kwa miujiza yake. Kesho yake akaanza kuzungumza ingawa bado alikuwa ni kama amechanganyikiwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nakumbuka vizuri alianza kupata uwezo wa kuzungumza usiku wa kama saa sita hivi ambapo alizinduka kutoka usingizini na kuanza kuniita kwa jina langu. Kwa kuwa bado nilikuwa sijapitiwa na usingizi, niliamka haraka na kwenda kumsikiliza.

    Japo alikuwa akizungumza kwa taabu, huku akilia, niliweza kumuelewa ambapo aliniambia kwamba wanaume ni watu wabaya sana wanaoweza kufanya ukajuta kuzaliwa. Aliongea mambo mengi kwa mafumbo, nilijitahidi kuwa makini lakini mengine nilikuwa siyaelewi.

    Haikuwa kawaida kwa mama kuzungumza kwa busara kiasi hicho kwani tangu kifo cha baba, tulizoea kumsikia akifoka muda mwingi. Moyoni nikaanza kupatwa na wasiwasi kwani niliwahi kusikia kwamba ukiona mgonjwa anaongea sana, ujue anakaribia kuaga dunia.

    “Mama! Mamaa! Usiondoke mama,” nilisema huku nikitokwa na machozi kwani mama alikuwa akiongea kwa uchungu sana kama mtu anayetaka kukata roho. Cha ajabu, alinijibu kwamba hafi ila cha moto anakiona, nikamuuliza alikuwa anamaanisha nini kusema vile lakini bado aliendelea kuongea kwa mafumbo.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog