IMEANDIKWA NA : AZIZ HASHIM
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
Upepo wa bahari ulikuwa ukivuma kwa nguvu na kusababisha mawimbi makubwa ya maji yawe yanapiga kwa nguvu ufukweni, yakizoa mchanga na kuupeleka bahari kisha kurudi tena.
Kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele, ndivyo upepo ulivyokuwa ukizidi kuongezeka huku wingu jeusi likianza kutanda angani. Watu wote waliokuwa wakiufurahia upepo wa baharini, sasa walianza kuuona kuwa kero kwani ulikuwa ukiambatana na baridi kali huku kijua cha jioni kilichokuwa kikiwaka, kikimezwa na wingu zito jeusi.
Watu waliokuwa wamekaa ufukweni, waliendelea kupungua kwa kasi na muda mfupi baadaye, ufukwe ulikuwa kimya kabisa huku ngurumo za hapa na pale zikianza kusikika kuashiria mvua kubwa iliyokuwa ikitaka kunyesha.
Licha ya hali kubadilika na kuwa mbaya kiasi hicho, bado kuna mtu mmoja alionekana kuendelea kukaa juu ya gogo kubwa la mnazi, akionekana kuwa mbali kimawazo kiasi cha kushindwa kutambua mabadiliko ya hali ya hewa yaliyotokea ghafla.
Mhudumu wa kike wa ukumbi maarufu uliopo ufukweni mwa bahari, Kunduchi Beach Club aitwaye Winfrida ambaye alikuwa akikimbia huku na kule kukusanya chupa za vinywaji alivyowahudumia wateja wake kabla mvua haijaanza kunyesha, ndiye aliyegundua kwamba kuna mtu alikuwa amesalia ufukweni, akiwa hana dalili za kuondoka.
“We kaka! Kakaaa! Tunafunga geti kule, huoni mvua kubwa inayokuja? Ingia ndani,” alisema Winfrida huku akiendelea kukusanya chupa za bia na soda na kuziweka kwenye kreti, alipaza sauti lakini bado yule mtu aliendelea kujiinami, hali iliyomlazimu kumsogelea.
Tayari manyunyu ya mvua yalikuwa yameanza kudondoka, huku giza likiwa limetanda ghafla, ngurumo za radi zikisikika huku na kule na kuifanya hali kuzidi kuwa ya kutisha.
“Kaka, we kaka,” alisema Winfrida, safari hii akiwa amemgusa mtu huyo na kumtingisha, taratibu mtu huyo akainua uso wake na kumtazama Winfrida, ghafla na yeye akaonekana kushtuka kwani ilionekana hakuwa akijua kilichokuwa kikiendelea.
“Umepatwa na nini kaka? Huoni mvua inayokuja? Twende haraka unaona geti linafungwa kule,” alisema Winfrida huku akimshika mkono na kumuinua, akabeba kreti lake lililokuwa limejaa chupa tupu na kuanza kukimbia. Huku nyuma, yule mtu naye alisimama na kuanza kumfuata huku akiendelea kushangaa hali ya hewa kwani ilionesha imebadilika haraka mno.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walipoingia kwenye geti tu, mlinzi aliyekuwa anawasubiri alifunga, wakakimbiampaka kwenye ukumbi mkubwa ambapo waliwakuta watu wengi wakiwa wamejistiri mvua, huku kila mmoja akionekana kumshangaa mtu huyo.
Muda mfupi tu baadaye, mvua kubwa ikaanza kunyesha, ikiwa imeambatanana upepo mkali sambamba na radi zilizofanya watu wote kuzidi kuingia ndani ya ukumbi huo na kujibanza kwenye kona.
“Inamaana ulikuwa umelala au? Nisingekushtua bado ungekuwa kulekule ufukweni,” Winfrida alimuuliza mtu huyo ambaye kwa kuwa sasa walikuwa kwenye mwanga wa taa, aliweza kumuona vizuri usoni na kubaini kwamba kumbe alikuwa analia. Akaweka kreti lake chini na kumsogelea.
“Inaonekana ahaupo sawa, nini kinachokusumbua?” aliuliza Winfrida lakini kauli yake ilionekana kama imeenda kutonesha donda ambalo bado halikuwa limepona kwenye mtima wa kijana huyo, aliyekuwa amevaa kitanashati.
Machozi yakaanza kumtoka kwa wingi na kutiririka mpaka chini ya kidevu chake, yakapotelea kwenye ndevu zake alizokuwa amezinyoa vizuri. Ghafla umeme ulikatika baada ya radi moja kupiga kwa nguvu, giza likatawala eneo lote la ukumbi huo.
Harakaharaka Winfrida alimshika mkono kijana huyo na kumuongoza kutembea mpaka upande kulipokuwa na kaunta, akavuta viti viwili , kimoja akampa kijana huyo ambaye bado hakuwa anaelewa nini kilichokuwa kinamsumbua, akakaa huku akiendelea kulia.
Kama isingekuwa umeme kukatika ghafla, huenda watu wengi wangemuona jinsi alivyokuwa anamwaga machozi kama chemchemi ya maji, akajiinamia kwenye meza ambapo aliendelea kulia kwa kwikwi kwa muda mrefu, huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha.
“Pole sana lakini kulia pekee hakuwezi kukusaidia chochote, tafadhali niambie unaitwa nani, unatokea wapi na nini kilichokusibu mpaka ukawa kwenye hali kama hii,” alisema Winfrida kwa sauti ya upole, mtu huyo akashusha pumzi ndefu na kutoa kitambaa mfukoni mwake, akajifuta machozi na kamasi na kumtazama Winfrida.
“Ahsante kwa kunishtua kule ufukweni, ahsante sana,” alisema kijana huyo huku akiendelea kujifuta machozi, Winfrida akatingisha kichwa kama ishara ya kupokea shukrani hizo.
“Naitwa Abdallah au Dulla kama wengi wanavyopenda kuniita,” alijibu kijana huyo, Winfrida akamkazia macho usoni ambapo kwa msaada wa mshumaa uliokuwa umewaswa kaunta, aliweza kumuona vizuri, akendelea kumtazama akiwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia kilichomfanya awe kwenye hali kama hiyo.
“Ni mambo ya kawaida ya dunia ndiyo yaliyonifanya niwe kwenye hali kama hii, wala usijali ila nashukuru sana kwa msaada wako,” alisema Dullah huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa noti ya shilingi elfu tano.
“Naomba unisaidie maji ya kunywa ya Kilimanjaro,” alisema huku akimkabidhi Winfrida fedha hiyo. Alipoinuka na kueleka kaunta, Dullah alitoa simu yake mfukoni na kuibonyeza, akashangaa kugundua kuwa kumbe tayari ilikuwa imefika saa moja kasoro za jioni.
Akajishangaa kukaa ufukweni muda mrefu kiasi hicho kwani kumbukumbu zake zilimuonesha kuwa wakati anafika ufukweni hapo, ilikuwa ni saa tano za asubuhi. Akageuka upande mwingine na kugundua kuwa kulikuwa na watu wengi eneo hilo, wote wakiwa wamejificha mvua iliyokuwa ikiendelea kumwagika kwa wingi, ikiambatana na upepo na radi nyingi.
Muda mfupi baadaye, Winfrida alirudi na kumletea maji kama alivyoagiza, akamfungulia na kumkabidhi chenji, akakaa palepale alipokuwa amekaa awali. Dullah alimimina maji kwenye glasi na kuyanywa yote, alipoishusha glasi, ilikuwa tupu.
Akashusha pumzi ndefu na kumuangalia Winfrida ambaye bado alikuwa ametulia, akisubiri kusikia chochote kutoka kwa Dullah.
Kabla hajazungumza chochote, simu ya mkononi ya Dullah ilianza kuita mfululizo, akaiangaalia namba ya mpigaji lakini badala ya kupokea, alijiinamia tena na kuanza kulia, safari hii kwa uchungu zaidi kuliko mwanzo, jambo lililomfanya Winfrida abaki njia panda.
“Jamani kwani kuna nini? Mbona sikuelewi? Huyo Karen ndiyo nani?”
“Niache tu dadaangu, acha dunia iniadhibu kwa sababu nilishindwa kusikia la mkuu, acha leo nivunjike guu,” alisema Dullah huku akijifuta machozi na kamasi zilizokuwa zinamtoka kwa wingi.
Winfrida aliendelea kumsisitiza amwambie lakini hakuwa tayari, akaendelea kuumia ndani ya moyo wake mithili ya mtu aliyepokea taarifa za msiba. Mvua iliendelea kunyesha kwa muda mrefu, ilipokuja kukatika, tayari ilikuwa ni usiku, watu wakaanza kutoka, kila mmoja akitafuta njia ya kuelekea kwake.
Dullah naye aliinuka na kuagana na Winfrida, akamshukuru kwa wema wake na kumwambia kwamba wakijaaliwa, ipo siku watakutana tena. Japokuwa bado Winfrida alikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichomtokea kijana huyo mtanashati, alishindwa kumzuia kuondoka.
Alipofika kwenye lango la kutokea, Winfrida alikumbuka kitu, akasimama na kumuita Dullah kisha akaanza kumkimbilia.
“Samahani kama nakusumbua, hii hapa ni namba yangu ya simu, unaweza kunipigia muda wowote utakaokuwa na mudi ya kuzungumza na mimi,” alisema Winfrida huku akimkabidhi Dullah namba iliyokuwa imeandikwa kwenye tishu. Dula akaachia tabasamu hafifu na kuipokea kisha akaendelea na safari yake, huku akikwepa madimbwi ya maji yaliyosababishwa na mvua hiyo.
Kwa kuwa muda ulikuwa umeenda sana, Dullah alipotoka nje ya hoteli hiyo, alilazimika kuchukua usafiri wa Bajaj ili umsogeze mpaka eneo analoweza kupata daladala. Kwa bahati nzuri, alipotoka tu, alikutana na dereva wa Bajaj aliyekuwa anarudi kumpeleka abiria.
Akampungia mkono na kusimama, muda mfupi baadaye, tayari walikuwa wakiondoka eneo hilo.
“Umesema unaelekea wapi?”
“Nipeleke mpaka pale njia panda, panaitwaje vile?”
“Mbuyuni.”
“Yaah! Hapohapo, nataka nikapande daladala za kuelekea Mwenge,” alisema Dullah huku akijitahidi kurudi kwenye hali yake ya kawaida. Safari iliendelea, wakapita eneo la Mtongani, Kunduchi na muda mfupi baadaye, tayari walikuwa wamewasili Mbuyuni. Akamlipa dereva wa Bajaj na kusimama kituoni pamoja na abiria wengine wachache.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Muda mfupi baadaye, gari liliwasili na kusimama, wakapanda na safari ya kuelekea Mwenge ikaanza huku bado Dullah akionesha kuwa na mawazo mengi ndani ya kichwa chake. Akiwa njiani, simu yake ilianza tena kuita, akaitoa mfukoni na kutazama namba ya mpigaji lakini badala ya kupokea, aliikata na kuizima kabisa.
Safari ikaendelea mpaka alipofika Mwenge, akashuka na kutafuta gari lingine lililompeleka mpaka Makumbusho alikokuwa anaishi. Tofauti na Kunduchi alikotoka, Makumbusho umeme haukuwa umekatika na ilivyoonesha, mvua haikunyesha kwa kiwango kikubwa kama alikotoka.
Akateremka kwenye daladala na kuvuka barabara, akaanza kutembea taratibu kuelekea nyumbani kwake ambako baada ya kukumbwa na matatizo makubwa ya kimapenzi, alikuwa akiishi peke yake. Alitembea akiwa kimya kabisa, hata marafiki zake aliozoea kutaniana nao kila jioni wakati akirudi kutoka kwenye mihangaiko yake, siku hiyo hakuwa na stori nao kabisa.
Hatimaye aliwasili kwenye nyumba aliyokuwa anaishi lakini akiwa getini tu, alipatwa na mshtuko baada ya kukutana na mazingira yasiyo ya kawaida. Akasimama kwa sekunde chache na kuanza kuangalia huku na kule. Kitu cha kwanza kilichomshtua ilikuwa ni kuona soksi yake moja ikiwa getini.
Alipotazama vizuri chini kwa msaada wa taa za nje, aliona pia nguo zake nyingine zikiwa zimedondoka, akapiga moyo konde na kuamua kusonga mbele ili akajionee kilichotokea.
Alipofika kwenye mlango wa kuingilia ndani kwake, alipigwa na butwaa zaidi baada ya kugundua kuwa mlango ulikuwa wazi kabisa wakati yeye aliufunga kabla ya kuondoka. Huku akitetemeka, aliingia ndani na hali aliyokutana nayo, ilimchanganya kuliko kawaida.
Sebule ilikuwa tupu kabisa, hakukuwa na chochote kilichosalia zaidi ya nguo chache zilizokuwa juu ya zulia. Masofa yake ya kisasa aliyoyapata kwa taabu, hayakuwepo, runinga kubwa ya flat screen iliyokuwa ukutani nayo haikuwepo pamoja na vitu vingine vya thamani vilivyokuwa sebuleni hapo.
Mapigo ya moyo yakawa yanamuenda mbio kuliko kawaida, alijikaza na kusonga mbele, akaingia chumbani na kuwasha taa. Alichokutana nacho kilimfanya ashindwe kuvumilia, chumba chote kilikuwa tupu kabisa huku kukiwa hakuna chochote kilichosalia zaidi ya chaga za kitanda na vitu vingine vidogovidogo.
Akatoka nje mbio mpaka kwenye mlango wa mama mwenye nyumba, akagonga kwa nguvu. Muda mfupi baadaye, mlango ulifunguliwa na mama mwenye nyumba wake ambaye alionekana kumshangaa sana.
“Vipi mwenzetu, sisi tunajua mmeshafika Bagamoyo? Au kuna kitu umekisahau?” alihoji mama huyo mwenye nyumba, kauli iliyozidi kumshangaza Abdallah ‘Dullah’.
“Bagamoyo? Mama mbona sikuelewi? Nimekuta mlango wangu umevunjwa na vitu vyote ndani ya nyumba havipo,” alisema Abdallah huku akitetemeka, kauli iliyomshangaza sana mama huyo mwenye nyumba.
“Mbona Karen alikuja na watu hapa akasema umemtuma kuja kuhamisha vitu kwa sababu umehamishiwa Bagamoyo kikazi? Tena sote tumemsaidia kutoa vyombo nje na kuvipakiza kwenye gari,” alisema mwanamke huyo, Abdallah akashindwa kujizuia na kukaa kwenye ngazi, akaanza kuangua kilio kama aliyepokea taarifa za msiba.
“Kwani kuna nini jamani?” alihoji mama huyo mwenye nyumba huku na yeye akitoka nje kwa mshangao. Ilibidi Dullah aanze kumueleza ukweli kwamba hakuwa amemtuma Karen kufanya chochote kama alivyowadanganya.
“Kwa hiyo kumbe alikuwa anatudanganya? Mungu wangu, watu wote humu ndani tumemsaidia kutoa vyombo na kuvipakiza kwenye gari,” alisema mama huyo mwenye nyumba huku akiwa amejishika mikono kichwani.
Lilikuwa ni tukio la ajabu sana lililowaacha wote midomo wazi, ikabidi wapangaji wengine wote nao watoke nje kutaka kujua kulikoni.
“Pole sana kaka, hiyo yote ni mitihani ya dunia,” alisema mpangaji mwingine ambaye chumba chake kilikuwa kikipakana na cha Abdul.
“Lakini si ulikuwa umeshamchumbia? Kwa nini usiende kuwapa taarifa wazazi wake ili wakusaidie upate vyombo vyako?”
“Ni stori ndefu sana jamani, nyie acheni tu, wale hawakuwa wazazi wake bali wahuni wa mitaani aliowapandikiza waonekane kama ni wazazi wake, najuta sana yaani natamani nife hata leo,” alisema Abdul huku akiendelea kulia kwa uchungu.
Kila mmoja alimuonea huruma, mpangaji mwenzake mmoja wa kiume akajitolea kumpa hifadhi kwani kwa hali aliyokuwa nayo usiku huo, kama asingepata mtu wa kumsimamia huenda angejidhuru na pengine hata kuyakatisha maisha yake.
***
Agosti 12, 2009
Ubungo, Dar es Salaam.
Jua lilikuwa kali sana jijini Dar es Salaam na kusababisha wapita njia wengi waliokuwa bize kila mmoja na shughuli zake, watokwe na jasho jingi kwenye miili yao. Wauzaji wa maji ya baridi na vitambaa vya kufutia jasho waliitumia vizuri fursa hiyo, wakawa wanafanya biashara kwa wingi.
Abdallah Maghembe, kijana mtanashati ambaye ndiyo kwanza alikuwa ameanza kufanya kazi kwenye kampuni kubwa ya Planet Link Communications iliyopo Mikocheni baada ya kuhitimu masomo yake ya chuo kikuu, alikuwa amesimama pembeni, huku muda mwingi akionekana kuwa bize na simu.
“Haloo! Umesema uko wapi? Nipo hapa Ubungo karibu dakika arobaini zinaelekea kuisha sasa, mbona sikuoni?” alisikika kijana huyo akizungumza na mtu wa upande wa pili kwa kutumia simu yake ya kisasa (smart phone).
“Fanya haraka basi si unajua muda wa kazi huu, nimefanya kutoroka tu mara moja nije kuonana na wewe,” alisema kijana huyo kisha akakata simu. Akatoa kitambaa na kujifuta jasho jingi lililokuwa linamtoka.
Alikuwa ametoroka kazini kwao, Mikocheni kwa ajili ya kwenda kuonana na msichana ambaye kwa kipindi kirefu walikuwa wakiwasiliana tu kwenye simu na mitandao ya kijamii, Karen.
Muda mfupi baadaye, msichana aliyekuwa amevalia kinadhifu, akiwa amejipamba sana mwilini mwake, alionekana akitokea upande wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani, akawa anatembea taratibu kwani alivaa viatu virefu ambavyo vilihitaji staha wakati wa kutembea.
“Nimeshafika hapa sheli,umevaaje?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimevaa shati la pinki na suruali nyeusi, nimechomekea. Wewe umevaaje?”
“Nimevaa kimini cha rangi ya bluu na topu nyeupe, natokea upande huu wa stendi ya Ubungo.”
“Ooh! Ok, sawa nimeshakuona,” alisema Abdallah huku mapigo ya moyo yakianza kumwenda mbio baada ya kumuona kwa mbali msichana aliyekuwa anaenda kukutana naye. Urembo wake wa nje tu ulitosha kumtetemesha kila mwanaume aliyekamilika, Abdallah akajikuta akianza kuishiwa pozi.
Hata hivyo, alipiga moyo konde na kuanza kutembea kikamavu kuelekea msichana huyo alikokuwa anatokea, muda mfupi baadaye wakawa wameshakutana.
“Whaoo! Umependeza sana,” Abdul alijikaza na kusema huku sauti yake ikionesha dhahiri alivyokuwa na wasiwasi, Karen akaachia tabasamu pana na kusababisha meno yake meupe yaonekane vizuri.
“Ahsante, na wewe umependeza sana, kumbe ndivyo ulivyo handsome hivyo?” alisema Karen wakati akipeana mkono na kijana huyo, wakasogea pembeni kidogo ambapo walitambulishana vizuri kwani siku hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza kwa wawili hao kukutana ana kwa ana.
Kwa kipindi kirefu walikuwa wakiwasiliana kwa simu na mitandao ya kijamii tu. Kwa kuwa hapakuwa na sehemu tulivu kwa wawili hao kuzungumza eneo hilo la Ubungo ambalo lilipambwa na pilikapilika nyingi, walikubaliana kwamba wachukue usafiri mpaka Mlimani City, ili wakafahamiane zaidi.
Taratibu waliondoka eneo hilo na kuvuka barabara huku kila mmoja akiwa kimya, wakaenda kwenye kituo cha Bajaj na kuchagua moja ya kupanda huku Abdul akimuelekeza dereva sehemu ya kuwapeleka. Hatimaye baada ya dakika kadhaa, waliwasili Mlimani City, Abdul akamlipa dereva wa Bajaj fedha zake kisha wakateremka na kutafuta sehemu nzuri ya kukaa.
“Unatumia kinywaji gani?”
“Juisi ya Rosella,” alisema msichana huyo huku akikwepesha macho yake yaliyoonekana kujaa aibu za kikekike. Muda mfupi baadaye, vinywaji vililetwa mezani hapo ambapo Abdul aliagiza maji ya baridi. Wakawa wanakunywa kimyakimya mpaka kijana huyo alipoamua kuuvunja ukimya.
“Enhee! Hebu niambie namba yangu ya simu uliipata wapi?”
“Niliipata baada ya kukosea namba ya rafiki yangu Mwantumu tuliyesoma naye kama nilivyokusimulia siku ile ya kwanza.”
“Mh! Kweli Mungu mkubwa, yaani unakosea namba halafu baadaye tunakuja kuwa marafiki tulioshibana kama hivi! Najisikia furaha sana kukufahamu,” alisema Abdul huku akitoa tena mkono na kumpa msichana huyo.
“Kwani we unaishi wapi? Nataka nikapajue nyumbani kwako,” alisema Karen na bila hiyana, Abdul akamkubalia kwani kwake aliiona hiyo kama bahati ya mtende kuota jangwani hasa kutokana na uzuri wa msichana huyo. Mara kwa mara akawa anamtazama msichana huyo usoni huku akiwa bado haamini kama kweli amekutana naye kwa mara ya kwanza baada ya kuwa wanachati kwa kipindi kirefu.
Baada ya kumaliza vinywaji, waliinuka na taratibu wakaanza kutembea kutoka eneo hilo la Mlimani City.
“Kwani wewe nyumbani ni wapi?” Abdul naye alimuuliza msichana huyo, akamgeukia na kumuangalia kwa macho yake makubwa aliyokuwa anajua namna ya kuyalegeza, akaachia tabasamu pana na kumjibu:
“Jamani Abdallah, si nilikwambia natoka Arusha na leo ndiyo nimeshuka Ubungo?”
“Oohoo! Nilisahau, nisamehe kama nimekukwaza kukuuliza tena.”
“Wala hujanikwaza chochote,” alisema msichana huyo na kuongeza kwamba alikuwa amekuja kumtembelea shangazi yake anayeishi Kinondoni lakini hatakaa kwa muda mrefu jijini Dar.
Waliendelea kutembea mpaka walipofika nje, wakasimamisha teksi na kuingia, wakakaa siti ya nyuma ambapo msichana huyo alijitanua bila wasiwasi na kusababisha mapaja yake yaonekane waziwazi, Abdallah ambaye alikuwa na ugonjwa wa kupenda ‘totoz’, akameza funda la mate kwa uchu na safari ikaendelea.
Njiani, msichana huyo aliendelea kumfanyia vituko vya hapa na pale ikiwemo kumlalia begani eti kwa kisingizio kwamba amechoshwa na safari ndefu ya kutoka Arusha. Waliendelea na safari mpaka nyumbani kwa Abdallah ambaye ndiyo kwanza alikuwa ameyaanza maisha.
Japokuwa alikuwa akiishi kwenye nyumba yenye vyumba viwili tu, alikuwa na vitu vingi vya thamani ambavyo alivinunua siku chache zilizopita, baada ya kupewa mkopo kazini kwao kwa ajili ya kuyaanza maisha mapya.
“Karibu, hapa ndiyo nyumbani kwangu,” alisema Abdallah huku akianza kuvua viatu vyake kwenye kapeti zuri, msichana huyo naye alifanya hivyo, akaingia ndani ambapo alimsifia kijana huyo kwa jinsi alivyokuwa akiishi maisha mazuri.
“Utanashati wako wa nje unafanana kabisa na maisha unayoishi, hongera sana,” alisema msichana huyo wakati akikaa kwenye sofa na kuendelea kuangaza macho huku na kule.
Abdallah alifungua friji dogo na kutoa vinywaji, wakakaa na kuendelea kunywa huku mazungumzo yakizidi kushamiri. Msichana huyo akataka Abdallah akamuoneshe sehemu aliyokuwa analala, bila hiyana wakaingia hadi kwenye chumba kilichokuwa kimepambwa na kitanda kikubwa na samani nyingine nzuri.
Akazidi kumwagia sifa lukuki kutokana na maisha aliyokuwa anaishi. Waliendelea kuzungumza mambo mbalimbali lakini kwa sababu shetani wa ngono alikuwa tayari ameshapanda kwenye kichwa cha Abdallah, ukichanganya na vituko alivyokuwa anafanyiwa na msichana huyo, muda mfupi baadaye walijikuta wakianza kufanyiana vituko vya kimapenzi.
Mambo yaliendelea hivyo na mwisho wote wakajikuta wakiwa kama walivyotoka kwenye matumbo ya mama zao. Uzuri wa msichana huyo ulimfanya Abdallah awe mwehu kabisa, wakaangukia dhambini kwa mara ya kwanza, tena bila tahadhari ya aina yoyote.
Ni mpaka alipokidhi haja zake, ndipo Abdallah aliporejewa na akili zake, akawa anajishangaa kwa jinsi alivyoweza kumuamini msichana huyo wakati ndiyo ilikuwa siku ya kwanza wanakutana ana kwa ana na kujikuta wakivunja amri ya sita.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hata hivyo, bado akili yake ilikuwa imezingirwa na ukungu wa urembo wa msichana huyo, waliendelea kucheza na kufanyiana vituko mbalimbali vya kimapenzi. Hakukumbuka hata kurudi tena kazini, muda wote walikuwa wamejifungia ndani, huku msichana huyo akimuonesha mapenzi motomoto yaliyozidi kumchanganya.
Abdallah alikuja kushtuliwa na simu yake iliyokuwa inaita mfululizo, alipotazama namba ya mpigaji, alikuwa ni meneja wake kazini aliyekuwa anataka kujua yupo wapi hadi wakati huo kwani alipoondoka, aliaga kwamba angerejea baada ya muda mfupi.
“Nipo mbali kidogo bosi na kuna foleni, nafikiri nitachelewa kurudi,” alisema Abdallah kwa sauti ya woga kisha simu ikakatwa. Harakaharaka akaamka na kukimbilia bafuni ambapo alijimwagia maji na kurudi chumbani, akamtaka msichana huyo naye afanye hivyohivyo.
Akaenda kuoga na kurudi chumbani ambapo alimkuta tayari Abdallah ameshajiandaa, tayari kwa kuondoka na kurudi kazini kwenda kukamilisha taratibu za kazi. Hata hivyo, alipomtaka msichana huyo naye ajiandae waondoke pamoja, alimkatalia kwa kisingizio kwamba alikuwa amechoka na alihitaji muda wa kupumzika.
Kutokana na mazingira yalivyokuwa, alishindwa kumkatalia, tena mwenyewe akamsisitiza kwamba akiondoka amfungie mlango kwa nje na akirudi atamkuta anamsubiri. Abdallah alifanya kama alivyoelekezwa, akaondoka na kumfungia msichana huyo ndani.
Japokuwa kwa upande mwingine alikuwa akijilaumu kwa kutochukua tahadhari zozote alipokutana na msichana huyo, upande mwingine alijipongeza kwa jinsi alivyofanikiwa kumnasa msichana huyo mrembo kiulaini.
Alitoka na kukodi bodaboda iliyomkimbiza mpaka kazini kwao, Mikocheni. Akafika na kumkuta bosi wake amefura kwani alitumia saa nyingi za kazi vibaya, jambo ambalo halikuwa likikubalika kwenye ofisi hiyo. Kwa kuwa hakuwa na mazoea ya kutegea kazi, alisamehewa.
Akaendelea kufanya kazi huku akili zake zote zikimuwaza Karen. Taswira ya jinsi msichana huyo alivyokuwa ameumbika, ilikuwa ikijirudia kichwani mwake, mara kwa mara akawa anachekacheka mwenyewe na kujipongeza.
Alifanya kazi harakaharaka na muda wa kutoka ulipofika tu, yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kutoka ofisini, akakodi tena bodaboda iliyomkimbiza mpaka nyumbani kwake. Kabla hajafika, alishuka na kwenda kwenye kibanda cha chipisi ambapo aliagiza chipsi kuku alizobeba mpaka nyumbani kwake.
Akapokelewa kwa uchangamfu na Karen ambaye muda wote alikuwa amelala na kujifunga mtandio mwepesi. Wakala chakula hicho pamoja kisha wakajifungia tena ndani ambapo waliendelea kujivinjari kwenye bahari ya huba yenye kina kirefu. Cha ajabu, licha ya muda kuendelea kuyoyoma, msichana huyo hakuwa na dalili zozote za kuondoka.
“Vipi, tutalala mpaka kesho?” Abdallah aliuliza kimitego akitegemea msichana huyo atamwambia anaondoka lakini akakutana na swali juu ya swali.
“Kwani we unataka niondoke au nibaki?” alihoji Karen huku akimpapasa taratibu Abdallah kifauni, akajikuta akijiingiza mwenyewe mtegoni kwa kumwambia kuwa asiondoke.
Waliendelea kupiga stori za hapa na pale na kuogelea kwenye bahari ya huba mpaka walipopitiwa na usingizi. Kwa mara ya kwanza, Abdallah akawa amelala na mwanamke ndani ya nyumba yake mpaka asubuhi, jambo ambalo hakuwahi kulifanya hata siku moja.
Aliwahi kuamka ambapo alimuamsha Karen naye ajiandae lakini katika hali iliyozidi kumchanganya, msichana huyo alimwambia amfungie mlango kwa nje yeye aende kazini kwani bado alikuwa na uchovu anataka kupumzika.
Abdallah alibabaika kidogo lakini kwa sababu hakutaka kumuudhi msichana huyo, alikubali. Akaandaa kifungua kinywa ambapo walikaa pamoja mezani na kula kisha baada ya hapo, Abdallah aliondoka kwa makubaliano kwamba atarudi mchana kumpelekea chakula.
Alipofika kazini, Abdallah alianza kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu msichana huyo. Japokuwa alikuwa mrembo, alishangaa ni kwa nini haoneshi kuwa na haraka za kuondoka nyumbani kwake, akakosa majibu.
Aliendelea pia kujilaumu kwa jinsi alivyomuamini haraka na kujikuta akiogelea naye kwenye dimbwi la huba bila kuchukua tahadhari yoyote. Hata utendaji wake wa kazi siku hiyo haukuwa kama kawaida yake, alionesha kuwa na mawazo mengi.
Ilipofika saa saba mchana, muda ambao kwa kawaida wafanyakazi katika kampuni yao hutoka kwa ajili ya kwenda kupata chakula cha mchana, Abdallah alitoka kazini na kuianza safari ya kurudi nyumbani. Akapita kwenye mgahawa maarufu wa Break Point, mahali ambapo alikuwa na mazoea ya kwenda kula chakula cha jioni.
Akatoa simu yake ili ampigie Karen na kumuuliza chakula anachotaka kula mchana huo lakini simu hiyo ilionesha inatumika. Akaamua kutumia uzoefu, akamnunulia chipsi kuku kisha na yeye akaagiza chakula chake, akaondoka na kurudi nyumbani kwake.
Alipokaribia, alijaribu tena kupiga simu ya Karen lakini bado ilikuwa inatumika, akaamua kuachana nayo kwani tayari alikuwa amefika jirani na anapoishi. Alipofika mlangoni, aliweka vifurushi vyake chini na kuanza kuvua viatu lakini ghafla alisikia sauti kama ya Karen ndani ikionesha alikuwa akizungumza na simu.
Ilibidi atege sikio kusikia alikuwa anazungumza nini na mtu gani muda wote huo. Cha ajabu, aligundua kwamba Karen alikuwa akizungumza na mwanaume tena kwa jinsi mazungumzo yaao yalivyokuwa, ilionesha kama wana uhusiano wa kimapenzi.
Mapigo ya moyo yakaanza kumwenda mbio, kijasho chembamba kikawa kinamtoka huku akishindwa kujua afanye nini. Akiwa bado hajui afanye nini, simu yake iliita mfukoni, alipoitoa mlio wake ukasikika mpaka ndani ambako Karen alishtuka na kukata simu haraka.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akainuka na kufungua pazia ambapo alimuona Abdallah ambaye naye alijifanya anamalizia kuvua viatu, akajitahidi kuilazimisha furaha ndani ya moyo wake na kuvaa tabasamu bandia.
Akamalizia kuvua viatu na kuchukua vifurushi vyake, akaingia ndani ambako Karen alimdaka juujuu kwa mabusu motomoto huku akimwambia kwamba alikuwa amemmisi sana kwa muda wote aliokuwa kazini.
“Nakupigia simu yako muda mrefu naona inatumika, ulikuwa unaongea na nani?” Abdallah alijikaza kiume na kumuuliza, Karen akambadilishia Kiswahili na kumlainisha kwa maneno matamu huku akimdanganya kwamba alikuwa akizungumza na mjomba wake anayeishi jijiji Dar es Salaam.
“Alikuwa ananielekeza kwake, anasema leo niende,” alisema msichana huyo huku akiyarembua macho yake kiasi cha kumfanya Abdallah aamini kwamba alichokuwa anaambiwa kilikuwa ni kweli.
Akashusha pumzi ndefu na kutuliza moyo wake, wakakaa mezani na kuanza kula chakula alichokuwa amemletea. Muda wa kawaida ambao wafanyakazi wanaruhusiwa kutoka kwenda kula ulimalizika lakini bado Abdallah alikuwa nyumbani kwake, tena akiwa hana dalili za kuondoka kutokana na jinsi alivyokuwa amebanwa kimahaba na msichana huyo.
Walipomaliza kula, walijikuta wakiangukia tena ‘mswambweni’, wakaogelea kwenye bahari ya huba kwa muda mpaka walipokifikisha chombo pwani.
Karen ndiye aliyekuwa wa kwanza kuamka, akaenda kujimwagia maji bafuni na aliporudi, Abdallah naye alifanya hivyohivyo. Wakaanza kujiandaa, Abdallah kwa ajili ya kurudi kazini huku msichana huyo akimwambia kwamba anakwenda nyumbani kwa huyo mjomba wake.
Moyoni Abdallah alifurahi kwamba ule mzigo sasa alikuwa anaenda kuutua lakini akaishiwa nguvu baada ya kuona msichana huyo, ameacha vitu vyake vingi, ikiwa ni pamoja na nguo kwa maelezo kwamba angerudi baada ya siku chache.
Alishindwa cha kujibu, wakatoka pamoja na kukodi Bajaj ambayo ilimpitisha kwanza Abdallah ofisini kwake kisha ikampeleka Karen kwenye safari zake.
“Mbona umechelewa kurudi lunch time? Ulikuwa wapi?” meneja alimuuliza Abdallah huku akiangalia saa yake ya mkononi. Ni kweli alikuwa amezidisha sana muda kwani badala ya kurudi saa saba na nusu kama sheria ilivyo, yeye alirudi saa kumi kasoro za jioni. Akapewa onyo jingine la mdomo.
Aliingia na kwenda sehemu yake ambapo alianza kufanya kazi ambazo zilikuwa zimerundikana mezani kwake. Ghafla alianza kusikia maumivu kwenye sehemu zake za siri, akainuka haraka na kuelekea chooni ambapo alipotaka kujisaidia haja ndogo, maumivu yalizidi kuongezeka maradufu, alipojikaza sana, alishangaa akitokwa na vitu kama usaha kwenye sehemu zake za siri.
Tukio hilo lilimshtua mno Abdallah kwani tangu alipoanza kujihusisha na michezo ya kikubwa, hakuwahi hata mara moja kutokewa na hali kama hiyo. Akawa anakumbuka maelezo waliyokuwa wanapewa na mwalimu wao wa somo la Biology kipindi alipokuwa anasoma sekondari kwamba hizo ni dalili za magonjwa ya zinaa.
“Mungu wangu, nimepata ugonjwa wa zinaa?” alisema huku akiendelea kuduwaa, mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio kuliko kawaida. Kwa jinsi mazingira yalivyokuwa, alijua kuwa hakuna mtu mwingine aliyemuambukiza gonjwa hilo isipokuwa Karen.
Alitoka na kurudi sehemu yake ya kazi lakini alishindwa kufanya chochote, mawazo mengi yakawa yanapita ndani ya kichwa chake, akijilaumu sana kwa uzembe alioufanya wa kushiriki tendo na Karen bila kuchukua tahadhari yoyote wakati hakuwa akimjua wala kumuamini.
Alitamani kuomba ruhusa ili aende hospitalini lakini alipofikiria kwamba muda mfupi tu uliopita ametoka kupewa onyo kali kutokana na tabia yake ya kutegea kazi, aliamua kujikaza kisabuni.
Aliendelea kumfikiria Karen, akashindwa kuamini kwamba msichana mzuri kama yule ambaye mwanaume yeyote akimuona lazima atamani kuwa naye, anaweza kuwa anatembea na maradhi hatari kiasi hicho.
Muda uliyoyoma na hatimaye saa za kutoka kazini ziliwadia, harakaharaka akatoka na japokuwa siku hiyo kulikuwa na mechi ya mpira wa miguu kati ya timu yake ya Arsenal aliyokuwa anaipenda sana dhidi ya Liverpool uliokuwa unaoneshwa kwenye runinga kubwa iliyokuwa kwenye mgahawa uliokuwa karibu na kazini kwao, hakutaka kuangalia kabisa.
Alikodi Bajaj na kumueleza dereva kumkimbiza kwenye Hospitali ya Micco, Sinza aliyokuwa akitibiwa kila anapoumwa. Japokuwa alikuwa akijisikia aibu sana kumwambia mtu yeyote juu ya kilichompata, hakuwa na ujanja zaidi ya kwenda kumweleza ukweli daktari.
“Umeshiriki ngono bila kinga ndani ya siku chache zilizopita?” daktari alimuuliza Abdallah, akatingisha kichwa kuonesha kukubali huku akijisikia aibu kubwa ndani ya moyo wake.
Daktari alimuandikia vipimo na kumuelekeza kuelekea maabara ambapo baada ya muda, alichukuliwa vipimo vyote alivyoandikiwa. Dakika kadhaa baadaye, aliitwa tena chumba cha daktari ambapo aliambiwa kuwa majibu yameshatoka na imebainika kwamba ameambukizwa ugonjwa wa Kaswende.
“Kaswende?”
“Ndiyo, ili utibiwe inabidi ukamlete mwenzako mliyeshiriki naye kwenye tendo ili mpate tiba kwa pamoja,” alisema daktari huyo lakini ikabidi Abdallah aongope kwamba mwenzake alikuwa amesafiri kwani kwa maumivu aliyokuwa akiyahisi, kamwe asingeweza kuendelea kusubiri.
Daktari alimuelewa lakini akampa ushauri wa kuwa makini siku nyingine na kutoshiriki tendo la ndoa bila kuchukua tahadhari ya kutumia kinga. Pia alimuasa kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu na kuachana na tabia ya kurukaruka na wanawake kwani anaweza hata kupata gonjwa hatari la Ukimwi.
Baada ya hapo alimuandikia dawa ambazo alipaswa kuzitumia kwa muda wa siku saba, akamshukuru na kwenda kulipia dawa kisha akaondoka kurudi nyumbani kwake huku chuki dhidi ya Karen ikiugubika moyo wake. Alijiapiza kuwa siku atakayorudi, atamtupia kila kitu chake nje na kumpiga marufuku kukanyaga nyumbani kwake.
Alirudi nyumbani kwake akiwa na mawazo mengi ndani ya kichwa chake na jioni hiyohiyo akaanza kutumia dawa alizoandikiwa. Muda ukayoyoma na baadaye akalala usingizi mzito kutokana na dawa alizokuwa anatumia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alikuja kuzinduka alfajiri baada ya kusikia mlango wa sebuleni ukigongwa kwa nguvu. Akashtuka na kuangalia saa yake, akagundua kuwa tayari ilikuwa ni saa kumi na moja alfajiri, akawa anajiuliza ni nani anayeweza kuwa anamgongea usiku wote huo.
Akiwa bado hajui cha kufanya, alisikia dirisha la chumbani kwake likiwa linagongwa kwa nguvu, akaamka na kufungua pazia kimyakimya, hakuyaamini macho yake kugundua kuwa ni Karen ndiye aliyekuwa anagonga.
“Abdallah nifungulie mpenzi wangu, nimepatwa na matatizo mwenzio,” alisema Karen kwa sauti iliyoonesha kweli alikuwa kwenye matatizo makubwa, Abdallah akajifikiria kwa muda kisha akaamua kupiga moyo konde na kwenda kumfungulia.
Alipofungua tu mlango, Karen hakusubiri kukaribishwa, aliingia mpaka ndani huku mavazi aliyokuwa amevaa yakimshangaza mno Abdallah kwani hakuwahi kumuona akiwa amevaa hivyo. Juu alikuwa amevaa kitopu kilichoishia juu ya kitovu na kuliacha tumbo lake lote likiwa wazi. Kama hiyo haitoshi, kinguo hicho kilikuwa kikiangaza, jambo lililomfanya aonekane kama hajavaa kitu.
Chini alikuwa amevaa kikaptura kifupi kilichoyafanya maungo yake yaonekane waziwazi, Abdallah akabaki amepigwa na butwaa. Harakaharaka akakimbilia kwenye nguo zake alizokuwa ameziacha, akachukua khanga na kujifunga kwani naye alikuwa akiona aibu kwa jinsi alivyovaa.
“Umetoka wapi usiku wote huu?” alihoji Abdallah huku akijaribu kuvaa uso wa ‘usirias’ kwani zile hasira za kuambukizwa ugonjwa wa zinaa na msichana huyo, zilianza kupanda baada ya kumuona.
“Nimetoka kwa mjomba lakini kuna matatizo yametokea ndiyo maana nimeondoka usiku.”
“Matatizo gani?”
“Mjomba anapigana na mke wake sijui wameanziana nini ndiyo nikaona nikimbie wasije wakauana nikawa shahidi.”
“Kwa hivyo ulivyovaa umetoka kwa mjomba wako kweli?”
“Ndiyo, jamani Abdallah mbona huniamini,” alisema msichana huyo huku akimsogelea na kutaka kumkumbatia lakini akamtoa na kumrudisha nyuma.
“Mbona unanuka pombe? Hebu niambie ukweli umetoka wapi?” alisema Abdallah, safari hii hasira zikiwa zimeshampanda, akamsogelea na kumkunja shingoni.
“Unaniumiza Abdallah, unaniu...” alilalamika Karen lakini alishindwa kumalizia kauli yake kwa jinsi alivyokuwa amekabwa.
“Na nitakuumiza kweli, nataka uniambie ukweli, ulikuwa wapi?”
“Si nilikuaga kwamba naenda kwa mjomba Kinondoni?”
“Mwanamke muuaji sana wewe,” alisema Abdallah na kumsukuma msichana huyo kwa nguvu, akaenda kuangukia juu ya ‘dressing table’ iliyokuwa pembeni ya chumba hicho. Almanusra apasue kioo kwenye meza hiyo ya kujipambia, akabaki anashangaa kwani Abdallah alionesha kubadilika sana.
Hakuwa tena yule mwanaume mpole, mcheshi ambaye muda wote alikuwa akizungumza kwa upole, tabasamu likiwa limeupamba uso wake. Alibadilika mno na kwa jinsi alivyoonekana, alikuwa tayari kufanya chochote usiku huo.
“Kwani tatizo ni nini mpenzi wangu? Mbona umenibadilikia ghafla?”
“Nani mpenzi wako? Mwanamke muuaji sana wewe, sitaki kuamini kama umekuja kwa ajili ya kuvuruga maisha yangu, nakuchukia, nakuchukia sana Karen!” alisema Abdallah ambaye sasa alishindwa kuendelea kusimama, akakaa chini na kuegamia kitanda huku machozi mengi yakiendelea kumtoka.
“Kwani kuna nini? Tafadhali niweke wazi, nimekukosea nini?” alisema Karen kwa upole, huku akiinuka kutoka pale alipokuwa ameangukia.
“Hujui! Unajifanya hujui siyo?” alifoka Abdallah huku akifungua droo ya kitanda na kutoa karatasi ya majibu pamoja na dawa alizokuwa amepewa hospitalini.
“Kama ulikuwa unajijua una maradhi yako, kwa nini usiniambie tutumie kinga? Unataka kuniua si ndiyo?” Abdallah alizidi kufoka, Karen akajishika mdomoni kwa mshangao, pombe zote alizokunywa zilimuisha. Akaokota kile cheti cha daktari na kuanza kusoma majibu ya vipimo alivyochukuliwa. Akazidi kupigwa na butwaa.
“Unashangaa nini? Kumbe wewe malaya si ndiyo?”
“Hapana Abdallah, unakosea kunitukana, ina maana kukubali ombi lako la kuwa wapenzi ndiyo unaniona mimi malaya?”
“Mshenzi wa tabia wewe, kwanza bahati yako sasa hivi ni usiku, ningekutimua muda huuhuu, sitaki majadiliano na wewe, kukipambazuka tu, chukua kila kilicho chako uondoke na sitaki kuja kukuona tena,” alifoka Abdallah na kusababisha baadhi ya majirani waanze kushtuka usingizini kutokana na zogo hilo.
Abdallah aliinuka pale alipokuwa amekaa, akajifuta machozi na kuchukua mkoba uliokuwa na nguo za Karen, akautoa sebuleni na kumwambia atalala sebuleni mpaka asubuhi na kukipambazuka tu, aondoke na asirudi tena. Akamshika mkono na kumtoa mpaka sebuleni na kumbwaga kwenye sofa.
Yeye akarudi chumbani na kujifungia mlango kwa ndani. Akajitupa kitandani na kuendelea kuwaza huku akitweta kwa hasira zilizochanganyikana na huzuni. Alijiona mjinga sana kwa kukubali kuingia kirahisi kwenye mtego wa msichana yule aliyeonekana kuwa hajatulia kabisa.
Akiwa amejilaza kitandani, alisikia simu ikiita. Akadhani ni simu yake, alipoangalia, aligundua kuwa simu yake haikuwa ikiita, ikabidi ainuke na kuanza kuangaza macho huku na kule, akaona kuna simu ilikuwa sakafuni, ikabidi ainuke na kwenda kuiokota.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akagundua kuwa kumbe ilikuwa ni simu ya Karen, akaichukua na kuanza kutazama namba ya mpigaji. Alishangaa ni mtu gani anaweza kuwa anampigia simu Karen usiku kiasi hicho. Alitamani kuipokea lakini akajikuta akisita, simu ikaendelea kuita mpaka ilipokata.
Akiwa bado ameishika mkononi, ilianza tena kuita, ikabidi ajikaze kisabuni na kuipokea, kabla hata hajazungumza chochote, alisikia sauti ya kiume ikizungumza upande wa pili.
ITAENDELEA
...
0 comments:
Post a Comment