Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

HUWEZI KUUA MAITI - 2







    Simulizi : Huwezi Kuua Maiti

    Sehemu Ya Pili (2)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa mara nyingine alipiga tena mluzi na kundi jingine kubwa la ndege aina ya Tai liliibuka na kuanza kuzizingira helkopta hizo lakini muda mfupi baadaye bibi Nyanjige alishangaa kuona ndege wengi wakianguka ardhini wakiwa wamekufa na kuijaza ardhi! Alishindwa kuelewa ni kitu gani kilitumika kufanya mauaji hayo ya ndege wake.



    Alipomuokota ndege mmoja na kumnusa ndipo aligundua ndege wake waliuawa kwa sumu kali aina ya DDT! Helkopta zilizidi kusogea eneo alilokuwa na alishuhudia mipira ya maji ilimwaga aina Fulani ya maji maji na mvuke angani ndege wake wakazidi kuporomoka na hatimaye anga ikabaki wazi bila ndege hata mmoja.



    Kifo cha ndege kilimtisha na alipoona hivyo alipiga mluzi kuamuru jeshi jingine liingie kazini na nzige wengi walivamia anga kwa makundi makundi lakini kama ilivyokuwa kwa ndege nzige nao waliporomoshwa kwa makundi makundi hadi ardhini.



    Kuona hivyo bibi Nyanjige alianza kukata tamaa kwani aliona ni kiasi gani jeshi lake lilikuwa limepuputika, alikuwa amebaki na jeshi la tembo peke yake na hakujua kama tembo hao wangeweza kuhimili vishindo vya vita kali iliyokuwa mbele yake.



    Wakati akiwaza hayo ghafla alianza kuwaona Tembo wakiduwaa na kuketi chini na hata yeye mwenyewe alianza kuhisi kulewa na muda mfupi baadaye bibi Nyanjige alipoteza fahamu kabisa na kulala ardhini, madawa yaliyokuwa yakimwaga na helkopta angani yalimlewesha bibi Nyanjige pamoja na Tembo wake. Kabla hajapoteza fahamu zake zote ni kitu kimoja tu alichowaza kichwani mwake. angefanywa nini baada ya kukamatwa KWA VIFO ALIVYOSABABISHA.

    *

    *



    Meli zilizobeba askari wa nchi kavu wa Tanzania ziliingia katika mji wa Kalemii nchini Kongo na kubebwa katika magari tayari kwa safari ya kwenda msituni! Kulikuwa pia na vifaru vipatavyo sabini kwa ajili ya vita hiyo pia vilishushwa na kuendeshwa kuelekea msituni tayari kwa mapambano.



    “Ni lazima akamatwe” Alisema kiongozi wa majeshi ya kongo yaliyojitolea kuyasaidia majeshi ya Tanzania mara baada ya kuwapokea askari wa Tanzania.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tayari vita hiyo ilishachukuwa sura kubwa kuliko ilivyotegemewa kila askari alikuwa na hasira kali dhidi ya bibi Nyanjige na wengi walitamani kumwona huyo bibi aliyeitingisha dunia kwa uwezo wake mkubwa wa kushawishi wanyama kufanya mauaji ya kikatili, lilikuwa si jambo rahisi kuamini.



    “Baada ya helkopta kumwaga sumu na kuwaua wadudu na pia kuwalewesha Tembo, ndege za kulipua mabomu zitapita na kuusambaratisha msitu baada ya kazi hiyo jeshi la nchi kavu litaingia msituni na kukamilisha kazi!” Alisema mkuu wa majeshi ya Tanzania.



    Wakati jeshi la nchi kavu likiingia msituni ilitolewa amri kuwa helkopta zote zilizokuwa zikipita angani na kumimina sumu zisitishe zoezi hilo kwanza ili kutoa nafasi kwa ndege za kudondosha mabomu na ndege kama kumi hivi ziliruka na kuingia msituni ambako milipuko ya mabomu ilisikika kila mahali, wakati huo askari wa miguu waliendelea kutembea taratibu kuingia msituni.



    Kwa jinsi mabomu yalivyolipuka hakuna mtu hata mmoja aliyeamini bibi Nyanjige angekuwa hai mpaka wakati jeshi la waenda kwa miguu linaingia msituni, kwani msitu ni kama uligeuzwa nje kuingia ndani! Ulifukuliwa kila mahali hapakuwa na mahali pa mtu kujificha.

    “Ni lazima huyu bibi atakuwa amekufa lakini maiti yake ni ni lazima itafutwe twende nayo hadi Tanzania Rais wetu akaione bibi huyu amesababisha vifo vya watu wengi mno” Hayo ndiyo maongezi yaliyoendelea midomoni mwa askari wengi waliotembea kuingia msituni.



    Baada ya mashambulizi ya mabomu yaliyodondoshwa na ndege nyingi angani, ilifuata hatua ya mwisho ya jeshi la nchini kavu kwa lengo la kwenda kupambana na tembo kama wangekuwa hai na kumkamata bibi Nyanjige ama kuitafuta maiti yake hadi ipatikane na kuondoka nayo! Kwa fikra za askari wengi vita hiyo ilikuwa imefika mwisho



    Jeshi la askari wasiopungua elfu tano liliuvamia msitu huo mkubwa kwa ajili ya kazi hiyo, kila mahali walikopita walishangaa kuona idadi kubwa ya tembo wakiwa wamekufa na kusambazwa kabisa na mabomu lakini hawakumwona bibi Nyanjige mahali popote kila mtu aliamini bibi huyo alikufa katika mashambulizi hayo.

    *

    *



    Hakikuwa kitu rahisi kwa bibi Nyanjige kufa kama walivyotegemea kwani dakika kama ishirini hivi kabla ya jeshi la nchi kavu halijauvamia msitu, bibi alirejewa na fahamu zake na kukuta kila upande wa mwili wake kuna Tembo mkubwa mnene aliyekufa na aliponyanyuka na kukaa kitako macho yake yalipambana na shimo kubwa lililochimbuliwa alijua hiyo ilikuwa ni kazi ya mabomu.



    Aliendelea kusikia milipuko sehemu mbalimbali msituni, ndege zilikuwa zikidondosha mabomu, kwa hali hiyo ingawa alikuwa amelewa aliweza kunyanyuka na kujikongoja akipita katikati ya msituni chini ya miti michache iliyokuwa imebaki mbele alisimama alipoiona helkopta iliyoungua huku pembeni mwake kukiwa na maiti za wanajeshi wawili waliokuwa.



    Wazo la kujiokoa lilimwijia kichwani mwake kwa sababu alijua wakati wowote angekamatwa, aliivamia moja ya maiti hizo na kuivua magwanda na kuyavaa na akachukua pia kofia na kuivaa kichwani mwake, alipomaliza tu kufanya hivyo alisikia nyasi nyuma yake zikitingishika na aliamini haukuwa upepo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walikuwa ni maaskari wa nchi kavu wa Tanzania! Walioibuka kutoka katikati ya nyasi wakiwa na silaha zao mikononi, moyo wa bibi Nyanjige uliingiwa na hofu kubwa na alianza kutetemeka akijua ni lazima angetiwa nguvuni na kuuawa. Pamoja na kuwa bibi kizee lakini alikuwa shupavu kuliko umri wake, alijiangusha karibu kabisa na maiti aliyoivua magwanda.



    Kwa jicho la pembeni aliwashuhudia askari wakitembea kuelekea mahali ilipokuwa helkopita iliyoungua, kila mmoja wao alisikika akiongea kwa huzuni hasa walipoziona maiti zikiwa zimelala pembeni, wao waliamini miili yote mitatu iliyolala chini ilikuwa maiti hawakujua kama mtu waliyekuwa wakimsaka alikuwa miongoni mwa miili hiyo.



    “Masikini hawa ni askari wetu kabisa. Hakyanani huyu bibi tukimtia mikononi tutamchanana vipande viwili!” Alisema mmoja wa askari hao kwa hasira huku akirukaruka kuonyesha hasira aliyokuwa nayo.

    Wengi wa maaskari walipoziona maiti hizo walilia machozi kwa uchungu na kila mmoja wao alionyesha hasira aliyokuwa nayo juu ya bibi Nyanjige.



    Bibi Nyanjige alisikia kila kitu kilichoongelewa na askari hao na kuzidi kuingia na hofu! Alibana mbavu ili asionekane akihema, alijua kama angegundulika ni lazima wangemuua kikatili kuliko ilivyowahi kutokea duniani.

    “Sasa tufanye nini?” Mmoja wa maaskari alimuuliza mkuu wa jeshi.



    “Tusonge mbele vijana wengine wachukue hizi maiti tatu wazipeleke hadi tulipoyaacha magari, wazipakie wakati tukisubiri utaratibu wa kuzirudisha nyumbani baada ya vita ya leo, sawa?” Alisema mkuu wa majeshi na vijana watatu walijitokeza wakaimana na kuibeba miili hiyo begani hakuna hata mmoja aliyehisi kuwa mmoja kati ya miili waliyoibeba ulikuwa ni wa mtu hai! Bibi Nyanjige alizidi kubana pumzi.



    Alilala begani kwa mmoja wa maaskari hao bila kujitingisha huku akihema mara moja kila baada ya dakika moja ili asingundulike! Alijua kama mbavu zake zingecheza ni lazima askari angeshtuka na kupiga kelele na huo ndio ungekuwa mwisho wake.



    Mpaka wanafika yalipokuwa magari na kuitupa miili hiyo ndani ya gari hakuna askari hata moja aliyehisi mwili mmoja kati ya walioipakia ulikuwa ni wa bibi Nyanjige tena akiwa hai.



    Maaskari waliondoka mbio kuwafuata wenzao msituni na muda mfupi baadaye maiti zilizidi kusombwa na kurundikwa ndani ya gari huku bibi Nyanjige akiendelea kugandamizwa na kuumia! Maiti zaidi ya hamsini zilipangwa juu yake.



    “Hawanipati ng’o”Aliwaza bibi Nyanjige huku akizididi kutiririkiwa na damu kutoka katika miili ya watu waliokufa.





    Msako wa kumsaka bibi Nyanjige porini uliendelea kwa masaa karibu kumi na mbili bila mafanikio yoyote! Nyumba yake ilisambaratishwa na mashimo mengi yalifukuliwa akitafutwa lakini bado hakuonekana mahali popote wanajeshi walikata tamaa na kuamini alikuwa amekufa.



    Miili mingi ya tembo wakiwa wamekufa ilionekana kila mahali msituni, ndege na nzige waliokauka pia walionekana ardhini ilikuwa si rahisi kuiona ardhi sababu ya wingi wa ndege na nzige walioifunika.

    Siku hiyohiyo jioni iliamriwa maiti zote zilizokuwa zimekusanywa zisafirishwe kurudi Tanzania wakati kukiwa na mpango kamambe wa kuendelea na operesheni kumsaka bibi Nyanjige siku ya iliyofuata.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kauli hiyo ya mkuu wa majeshi maiti zote zilianza kuhamishwa kutolewa kwenye gari na kufungwa katika mifuko maalum ya nailoni tayari kwa kusafirishwa kurudishwa Tanzania, bila kugundulika bibi Nyanjige alifungwa ndani ya mfuko na kupakiwa katika ndege maalum iliyoandaliwa.



    Dakika kama mbili hivi baada ya kuwekwa katika mfuko wa nailoni akiwa amepangwa ndani ya ndege bibi Nyanjige alianza kukosa hewa! Alihisi angekufa sababu ya kukosa hewa safi, Kwa kutumia meno yake makali alitoboa tundu katika mfuko wake na kuitega pua yake kwenye tundu hilo akawa anavuta hewa taratibu kutoka nje.

    *

    *



    Ndege ilipoingia Dar es Salaam saa nne ya usiku maiti zote zilipakuliwa na kupakiwa ndani ya gari maalum lililoandaliwa tayari kwa kuzipelekea chumba cha maiti cha hospitali ya jeshi iliyoitwa Military general hospital kuhifadhiwa katika chumba chenye baridi ili zisiharibike zikisubiri operesheni imalizike na wote waliokuwa wazikwe siku moja kwa heshima ya jeshi.



    Masaa matatu baada ya kuingizwa katika chumba cha maiti baridi kali iliyokuwemo ndani ya chumba hicho ilimfanya bibi Nyanjige ahisi mwili wake ukiganda aligundua asingeweza kuendelea kuwa ndani ya chumba hicho kwa muda mrefu kabla roho yake haijatoka.



    Kwa nguvu zake zote za kizee alijitahidi na kuutoboa mfuko wa nailoni uliomfunga akatoka nje na kupenya katikati ya maiti nyingine na kusimama wima ndani ya chumba cha maiti huku akitetemeka mwili mzima. Alijitahidi na kuusogelea mlango mkubwa wa kuingilia chumba cha maiti na kujaribu kuutingisha lakini ulikuwa mgumu alitaka atoke nje na kuondoka zake!



    Aliposhindwa kuufungua alibaki ameduwaa.

    Kwa masaa karibu sita aliketi pembeni ya mlango akiendelea kupigwa na baridi, alijaribu kufikiri ni kwa njia gani angeweza kujiokoa kutoka ndani ya chumba hicho lakini alishindwa, mara ghafla alisikia jogoo likiwika akafahamu tayari ilikuwa ni alfajiri na kuamini masaa machache baadaye mlango ungefunguliwa. ****************



    Baadaye alianza kuona mwanga wa jua ukipenyeza kwenye madirisha na muda mfupi baadaye aliusikia mlango wa chumba cha maiti ukitingishwa akajua kulikuwa na mtu aliyetaka kuufungua! Bibi Nyanjige alikimbia na kwnda kujificha nyuma ya kabati kubwa iliyokuwemo ndani ya chumba hicho.



    Akiwa nyuma ya kabati alishuhudia mlango ukifunguliwa na mtu aliyevaa mavazi ya kijeshi aliingia na kwenda kuketi nyuma ya meza iliyokuwa mbele ya kabati alilojificha! Mtu huyo alichukua kalamu na daftari na kuanza kuandika mambo ambayo bibi Nyanjige hakuyaelewa.



    Dakika chache tena baadaye aliingia mwanamke aliyevaa mavazi ya kijeshi akiwa na fagio kubwa mkononi, bibi Nyanjige alielewa mwanamke huyo alitaka kufanya usafi na ni lazima angemwona alishindwa angefanya kitu gani kujiokoa, alifikiria kukimbilia upande mwingine alijua angeonekana na kuamua kubaki hapo hapo.



    Askari wa kike alianza kufagia taratibu akielekea nyuma ya kabati kubwa, bibi Nyanjige alitetemeka mwili mzima akijua mwisho wake tayari ulikuwa umefika! Alibaki akitetemeka wakati mfagiaji akielekea nyuma ya kabati, bibi Nyanjige hakujua ni kitu gani kingetokea.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Huku akitetemeka bibi Nyanjige alinyata taratibu na kuizunguka kwa mara ya pili kabati kuelekea upande mwingine ili kumkwepa muuguzi akapanda kwenye ngazi na kulala katikati ya maiti mbili bila muuguzi kugundua, alimwona muuguzi akiendelea kufagia kuizunguka kabati, bibi alijua kama angebaki nyuma ya kabati ni lazima angekamatwa.





    “Mungu amesaidia swali ni kwamba

    nitatokaje humu ndani?” Alijiuliza bibi Nyanjige bila kupata jibu.

    Alitaka sana kutoka chumba cha maiti mapema kabla maiti za wanajeshi hazijakaguliwa asubuhi hiyo jambo ambalo kwa uhakika alijua lingehatarisha usalama wake! Kwa idadi kubwa ya vifo vya wanajeshi alivyosababisha alikuwa mtu aliyesakwa kuliko hata gaidi Carlos!





    Baada ya kumaliza kufagia muuguzi alitoka nje na kuufunga mlango wa chumba cha maiti nyuma yake na giza likarejea tena! Bibi Nyanjige aliutumia muda huo kuvua nguo za kijeshi alizokuwa nazo mwilini mwake na kubaki na gauni lake la kawaida, alizitupa nguo hizo sakafuni na kuendelea kulala katikati ya maiti akizidi kutafakari njia ya kujiokoa na kifo kilichokuwa mbele yake.



    Mara mlango ulifunguliwa safari hii hakuingia muuguzi peke yake aliongozana na kundi la wanaume kumi na mbili.

    “Maiti yenu ipo palee kwenye zile ngazi pembeni ya kabati!” Alisema muuguzi huku akizionyesha maiti ambazo bibi Nyanjige alilala katikati yake! “Hapa lazima nijikaushe vinginevyo mtu mzima nitaabika!” Aliwaza bibi wakati wanaume wale wakizidi kuikaribia ngazi aliyolala.



    “Nyie wanaume hebu mmoja wenu aje atie kwanza saini kwenye kitabu cha kuchukulia maiti yenu!” Muuguzi aliwaeleza na wanaume wote walisita na mmoja wao alikwenda hadi kwenye meza na kutia saini kwenye kitabu!

    “Haya nendeni mkachukue zipo maiti mbili moja ndiyo yenu!”

    “Sawa!”



    Wanaume hao waliondoka kuelekea kwenye ngazi na walipozifikia walishangaa kuona kukuta kuna maiti tatu moja ya mwanamke ikiwa imelala katikati ya maiti mbili na sakafuni kukiwa na mavazi ya kijeshi!

    “Nesi!”

    “Mnasemaje?”

    “Mbona kuna maiti tatu wakati wewe umesema ni mbili?”

    “Mungu wangu wee!” Bibi Nyanjige aliwaza moyoni mwake na kujua tayari mambo yalishaharibika alizidi kubana pumzi na mbavu kama mtu aliyekufa siku tatu kabla ya siku hiyo!Macho yake aliyafunga vizuri na mdomo wake kuuacha wazi! Ilikuwa si rahisi hata kidogo kuamini kuwa mtu aliyekuwa mbele yao alikuwa mzima.



    “Nyie chukueni maiti yenu muondoke, hata kama zipo nne nini kinachowasumbua?” Muuguzi alijibu, jibu hilo lilimfurahisha sana bibi Nyanjige.

    Baada ya jibu hilo wanaume hao waliushika mwili wa bibi Nyanjige na kuuweka pembeni kisha wakachukua maiti yao na kuishusha chini, wakaibeba na kuanza kutoka nayo nje ya chumba cha maiti!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akili ya bibi Nyanjige ilifanya kazi kwa haraka haraka kama kompyuta! Alitaka kuitumia nafasi hiyo kuokoa maisha yake. Alipomwangalia muuguzi mezani alikuta ameinamisha kichwa chake akiandika mambo fulani kwenye vitabu vyake bila kuwaangalia watu waliokuwa wakitoka na maiti.



    “Huu ndio wakati wenyewe!”, Alisema bibi Nyanjige na kuruka na kutua sakafuni bila mlio wala kelele.

    “Yes! Hiyo inaitwa staili ya paka mwizi maarufu wa mboga!” Alisema bibi Nyanjige akiisifia staili aliyotumia kuruka.



    Alinyata kwa kasi ya Chui akiwafuata wanaume waliobeba maiti kwa nyuma! Moyo ulikuwa ukimdunda kwa kasi ya ajabu wasiwasi wake ulikuwa ni muuguzi kunyanyua uso au watu aliokuwa akiwafuata kugeuka nyuma na kukuta mwanamke akiwafuata, alijua ni lazima wangeshangaa na kupiga makelele na hilo lingemaanisha kukamatwa.



    Alitembea mpaka nje ya chumba cha maiti bila kugundulika hakuna mtu kati ya wanaume wote waliokuwemo ndani ya chumba cha maiti aliyegeuka na kuangalia nyuma. Maiti ilipofikishwa nje watu wote waliokuwepo waliangua kilio kwa uchungu hakuna mtu aliyeonekana kujali kitendo cha bibi Nyanjige kuonekana akitoka chumba cha maiti.



    Ilionekana wazi mtu aliyekufa alikuwa tegemeo la watu wengi na alikuwa kipenzi cha watu! Ili kuficha tatizo lake bibi Nyanjige aliangua kilio kikali kuwazidi hata wafiwa waliokuwepo nje ya chumba hicho watu wote waligeuka na kujiuliza bibi huyo alikuwa nani! Ni hapo ndipo alipogundua kilio chake kilikuwa kikali na kupunguza kidogo sauti.



    “Mh! Wasije wakanishtukia bure!” Aliwaza bibi Nyanjige lakini mpaka hatua hiyo aliamini tayari alishanusurika kifo!

    *

    *

    Maiti ilipakiwa ndani ya gari na watu wengine walipanda katika mabasi mawili yaliyokodishwa kwa ajili ya kubeba watu kwenda chumba cha maiti, bibi Nyanjige hakutaka kuipoteza nafasi hiyo alipanda ndani ya basi mojawapo akiwa mtu wa tano tu kabla ya watu wengine kupanda.



    “Siwezi kupanda daladala wakati usafiri upo! Na kwa staili hii hawanipati ng’o na hata wakinipata watakuwa wamehangaika vya kutosha!”Aliwaza bibi Nyanjige wakati akitembea kuelekea kwenye kiti cha nyuma kabisa cha basi na kuketi.



    Wanawake wengine watatu walimfuata na kukaa karibu naye, walionekana kumshangaa kwa sababu hakuwa na khanga wala kitenge zaidi ya gauni chafu alilovaa!Bibi Nyanjige aliishtukia hiyo na kuamua kukizamisha kichwa chake katikati ya mikono kama mtu aliyekuwa akilia kwa uchungu, watu wengi ndani ya basi walihisi alikuwa shangazi au mama wa marehemu kwa uchungu alioonekana kuwa nao!



    “Nikifika huko nyumbani kwao, nitateremka na kwenda zangu stesheni ya treni na kama lipo nitaondoka leo hii hii kwenda Mwanza nataka nikajifiche kwenye kisiwa cha Rubondo pia kuna wanyama wengi sana nataka niunde jeshi jingine ili nipambane nao tena upya! Nataka niifundishe dunia somo ambalo haitalisahau, safari hii nitamwaga Tembo na Nzige mjini watu wabanane!” Aliwaza bibi Nyanjige.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Bibi!” Aliita msichana mmoja aliyekaa kiti jirani na bibi Nyanjige tayari gari ilishaanza kuondoka hospitalini.

    “Mbona huna khanga?”

    “Nimedondosha mjukuu wangu!”

    “Wapi bibi?”

    “Sikumbuki!”



    “Haya chukua hii hapa ikusaidie kidogo!”Alisema binti huyo wakati akimkabidhi bibi Nyanjige khanga aliipokea na kujifunika nayo kichwani badala ya sehemu nyingine za mwili! Hakutaka kuonekana sura kwa kuogopa kujulikana!”

    *

    *



    Basi lilikwenda kwa kasi likipita maeneo ya Mwenge, Morocco kuelekea kivuko cha kwenda Kigamboni.

    “Jamani kuna mtu kazidi nini humu ndani,mbona mwenzenu kakosa kiti?” Utingo wa gari hilo aliuliza baada ya kuona kijana mmoja amesimama wima wakati gari ilikuwa na uwezo wa kubeba watu ishirini na waliopanda basi hilo kwenda chumba cha maiti walikuwa shirini na hakuna aliyesimama!



    Abiria walianza kuangaliana ili kujua ni nani alikuwa amezidi! Bibi Nyanjige alizidi kutetemeka ndani ya khanga aliyojifunika alijua ni lazima angegundulika na si ajabu wangemfikisha polisi! Aliendelea kuomba Mungu amsaidie ili asigundulike.



    “Acha tu braza mimi nitasimama!” Alisema kijana huyo huku akisogea mbele kuelekea kwa dereva.

    “Njoo ukae hapa!” Alisema dereva akimwita kijana huyo akakae kwenye eneo la karibu na gia ya basi alikaa na kujisikia vizuri! Watu wote ndani ya gari walikuwa kimya, kwikwi za bibi Nyanjige tu ndio zilisikika ndani ya khanga aliyojifunika kichwani.

    *

    *



    Dakika tano tangu magari yaondoke chumba cha maiti,wanajeshi wakiwa na mkuu wao wa hospitali ya jeshi waliingia chumba cha maiti na kuanza kuzikagua maiti za wanajeshi, zilipohesabiwa walishangaa kukuta maiti moja haipo!

    Walipojaribu kuzunguka chumba cha maiti wakitafuta maiti moja walishangaa kukuta mavazi ya kijeshi yametupwa sakafuni, walipomuuliza muuguzi mtunza chumba cha maiti alionekana kutofahamu lolote juu ya mavazi hayo wasiwasi mwingi uliwaingia.



    “Kuna watu wamechukua maiti mpaka sasa hivi?”

    “Ndiyo!”

    “Ni wa wapi?”

    “Ni wenyeji wa Kigamboni!”

    “Balozi wao ni nani?”

    “Kessa Mwambeleko!”

    “Wana simu yoyote waliyokuachia?”

    “Ndiyo!”

    “Hebu tupatie hiyo namba yao tujaribu kuuliza!”

    “Ni 0744 382856!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mmoja wa wanajeshi hao alikuwa na simu ya mkononi palepale alibonyeza namba zilizotajwa na kuanza kusikiliza sikioni mwake.

    “Mko wapi?” Ndilo swali aliloanza kuuliza.





    “Tupo feri tunasubiri boti wewe ni nani?” Aliuliza upande wa pili.

    “Mimi ni mwanajeshi wa jeshi la ulinzi nipo chumba cha maiti cha hospitali ya Jeshi, nina wasiwasi mtakuwa mmechukua maiti tofauti!”

    “Maiti tofauti! Kivipi?”

    “Tunahisi mmechukua maiti ya mwanajeshi aliyeuawa Kongo!”

    “Hapana hiyo si kweli tuliyemchukua ni ndugu yetu kabisa na mimi ni mdogo wake kabisa!”



    “Hebu subirini hapa hapo mlipo!” Mwanajeshi huyo aliamuru na muda mfupi baadaye yeye na wenzake waliingia ndani ya gari la jeshi kuelekea kivukoni, ilichukua kama muda wa dakika kumi kufika na kuomba jeneza lifunguliwe ili maiti ikaguliwe.



    Yalitokea mabishano makali wanajeshi wakidai maiti irudishwe chumba cha maiti lakini mdogo wa marehemu hakukubaliana nao mpaka mtu mmoja alipotoa picha ya marehemu na kuifananisha na maiti iliyokuwa ndani ya jeneza ndipo walipokubali na kuondoka!

    Muda wote huo bibi Nyanjige alikuwa amejifunika khanga kichwani akitetemeka hakutaka sura yake ionekane na alimshukuru Mungu kuwa mpaka wakati huo hapakuwa na mtu aliyekwisha mshtukia! Alipanga wakifika kigamboni achoropoke na kutoroka msibani kurudi mjini ambako angetafuta usafiri wa treni kumpeleka Mwanza.





    *

    *

    Kupotea kwa maiti moja katika chumba cha maiti kuliwashangaza viongozi wengi wa jeshi la wananchi na uongozi wote wa hospitali! Walishindwa kuelewa ni jambo gani hasa lilitokea mpaka maiti kupotea wengi walihisi iliibiwa, lakini kwanini iibiwe? Hilo ndilo lilikuwa swali ambalo halikupata jibu.



    Mwanajeshi mtunza chumba cha maiti mkuu pamoja na msaidizi wake walikamatwa na kuwekwa rumande ya jeshi ili uchunguzi juu ya kupotea kwa maiti hiyo ufanyike.

    *

    *



    Kama kuna makosa aliyowahi kuyafanya katika maisha yake bibi Nyanjige ni kitendo chake cha kuzihamisha karatasi alizoandika matukio yote muhimu akiwa porini huko Kongo kutoka katika gauni lake na kuziweka katika magandwa ya jeshi aliyojivisha ili kuepuka kugundulika na kusahau kuzitoa karatasi hizo wakati wa kuyavua magwanda.



    Ni karatasi hizo zilizofanya wanajeshi wagundue ni nani aliyetoroka! Ziliposomwa kila mtu alijua bibi Nyanjige aliingia nchini akiwa katika maiti zilizoletwa kutoka Kongo na kutoroka akiwa chumba cha maiti.

    “Aisee nimeamini huyu bibi ni hatari sijui anatumia uchawi pia?”Aliuliza jenerali Mwita Mitiro katika kikao cha wakuu wa jeshi la polisi na jeshi la Wananchi kilichoitishwa kulijadili suala la bibi Nyanjige haraka.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa tufanye kipi maana tayari huyu bibi keshatutoroka!”

    “NI LAZIMA AKAMATWE!” Alisema mkuu wa jeshi la polisi na kuagiza simu ipigwe haraka sana huko kongo ili zoezi la kumsaka bibi Nyanjige lisimamishwe wanajeshi waliokuwa Kongo hawakuamini walichokisikia, walifikiri ni uongo.

    “Kafika vipi Tanzania?” Alihoji kiongozi wao.



    Viwanja vyote vya ndege, stesheni za reli, vituo vya mabasi, bandari vyote viliwekwa chini ya ukaguzi mkali, iliagizwa mabasi yote yaliyosafiri yasimamishwe na kukaguliwa bibi Nyanjige akitafutwa kwa udi na uvumba! Msako mkali mno kila mahali wanajeshi waliingia mitaani na kusaidiana na polisi kufanya msako wa nyumba hadi nyumba!



    Watu walipigwa na vibibi vizee zaidi ya mia moja waliofanana kidogo na bibi Nyanjige walitiwa mbaroni na kuhojiwa katika vituo mbalimbali vya polisi, vituo vya televisheni na redio vilitangaza juu ya kuingia kwa bibi Nyanjige nchini na picha yake ilionyeshwa, ili kurahisisha kukamatwa kwake zawadi ya shilingi milioni hamsini ilitangazwa.



    Msako ulikuwa mkali mno kila sehemu ya jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, magari yote yalisimamishwa na kukaguliwa, abiria wote katika stesheni ya reli walikaguliwa na wanajeshi hamsini walipangwa kuondoka na treni siku hiyo na wengine ishirini kusafiri na meli ya kwenda Mtwara ikifikirika bibi Nyanjige angeondoka na usafiri huo! Bibi Nyanjige alitafutwa kama Osama Bin Laden.



    Mpaka wanafika kigamboni bibi Nyanjige hakuwa na habari kuwa maiti ilipelekwa huko kwa ajili ya kutolewa heshima za mwisho peke yake! Akiwa huko aligundua kuwa maiti ilikuwa isafirishwe kwenda mkoani Kilimanjaro kwa mazishi, taarifa hizo ndizo zilimfanya abadilishe mawazo yake ya safari badala ya kwenda Mwanza aliamua kwenda Moshi na magari ya msiba lengo lake likawa kwenda kwenye mbuga za wanyama za Ngorongoro na Serengeti ambako angetulia na kuaanzisha jeshi jingine jipya na wanyama.



    “Tena huko kuna wanyama wengi zaidi ninafikiri jeshi langu safari hii litakuwa kubwa sana kuna uwezekano hata wa kuwapata Tembo wengine kutoka Kenya kwenye mbuga za Maasai Mara! Wasiponikamata katika muda wa wiki mbili nitakuwa nimekwisha unda jeshi kubwa kuliko nililokuwa nalo Kongo!”Aliwaza bibi Nyanjige.



    Mpaka Chalinze basi lao lilishasimamishwa zaidi ya mara tatu kwenye vizuizi barabarani lakini maaskari walipogundua kuwa lilibeba watu waliokuwa safarini kwenda kwenye mazishi waliliachia liendelee na safari.



    Bibi Nyanjige alifurahi kupita kiasi lakini wakati wanakaribia kuimaliza Chalinze askari polisi na wanajeshi watano wakiwa na bunduki mikononi walisimama katikati ya barabara na kulisimamisha gari lililobeba maiti pamoja na basi lililobeba abiria, waliingia ndani ya basi na kuliacha gari lililobeba maiti! Moyo wa bibi Nyanjige ulibadilisha kasi.



    “Jamani sisi tunawahi mazishi hawa wote unaowaona humu ndani ni watu tunaowapeleka mazishi huko Marangu Moshi!”

    “Sawa lakini kuna mtu tunamtafuta ni lazima tukague mzee! Tumeagizwa hivyo na mkuu wetu wa kazi!” Alisema mmoja wa maaskari.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “MAMA YANGU!” Bibi Nyanjige aliongea ndani ya khanga aliyojifunika aliyasikia maongezi yote ya maaskari na dereva, mkojo ulitaka kumpenya kwa woga na aliomba Mungu ili muujiza utokee wanajeshi hao wasipande ndani ya basi lakini haikuwa hivyo walipanda na kusimama ndani ya basi.



    “Jamani tunawaomba wote mtoe ushungi na vilemba vichwani mwenu ili nyuso zenu zionekane wazi kuna mtu tunamtafuta samahani sana kwa usumbufu utakaojitokeza, tusipompata mtaendelea na safari yenu!”

    “Mtu mwenyewe ni nani?” Aliuliza dereva.



    “Bibi Nyanjige!” Alijibu mwanajeshi mmoja.

    “Yule aliyeua watu mia na hamsini kwa sumu?”

    “Ndiyo! Tena ni zaidi ya mia na hamsini kamaliza wanajeshi wetu wengi sana huko Kongo!”

    “Aisee! Lakini humu ndani hayumo mimi ningemwona!” Alisema dereva.



    Bibi Nyanjige akiwa kiti cha nyuma alishindwa kufunua nguo yake kichwani, machozi yalimtoka humohumo ndani ya khanga aliyojifunika, aligundua hapakuwa na njia yoyote ile ya kujiokoa! Huo ndio ulikuwa mwisho wa safari yake ya kukimbia!



    Wanajeshi walizidi kumsogelea wakipita na kuangalia mtu mmoja baada ya mwingine! Tena kwa uangalifu mkubwa kila mmoja wao akiwa na picha ndogo ya bibi Nyanjige mkononi.



    Bibi Nyanjige alizidi kutetemeka ndani ya Khanga aliyojifunika kichwani, alielewa wazi hapakuwa na njia yoyote ya kujiokoa kutoka mikononi mwa wanajeshi waliokuwa wakimsaka! Aliamini mwisho wa uhai wake ulikuwa umefika na kilichokuwa kikimsubiri mbele yake hakikuwa kingine zaidi ya kamba shingoni, alijua kwa mauaji aliyoyafanya ni lazima angenyongwa na kufa!



    “Ehne! Wewe mama hebu jifunuee hicho kilemba chako!” Mwanajeshi mmoja alimwambia mwanamke aliyekaa kiti kilichokuwa mbele ya kiti cha bibi Nyanjige na aliyekuwa akifuata baada ya mama huyo alikuwa bibi Nyanjige mwenyewe! Bila ubishi mama huyo alijifunua kilemba chake na kuuacha uso wake wazi, hakufanana na mtu waliyekuwa wakimtafuta.



    “Haya wewe mwanamke mwenye khanga kichwani hapo kwenye kona hebu ondoa hiyo khanga yako!” Alisema askari huyo.

    Pamoja na ushujaa wake bibi Nyanjige alisikia nguo zake za ndani zikilowana, tayari mkojo ulishampenya! Alijadili kwa muda mrefu kuhusu kuitoa khanga kichwani au la kwani alijua kufanya hivyo kungemfanya akamatwe! Na kukamatwa kwake kungemaanisha kifo.



    “Wee mwanamke husikii unajifanya kusinzia siyo?” Askari aliuliza kwa ukali.

    “Ah bwanae hebu tuachane nao hawa twende chini tukasubiri magari mengine!” Askari mmoja alisema baada ya kuona taa za gari zikimulika kutoka kwa nyuma yao na wote kwa pamoja waliteremka hadi chini kuliwahi gari lililokuwa likija.



    Kitendo hicho cha askari kilimfanya bibi Nyanjige ashushe pumzi ndani ya khanga aliyojifunika, hakuamini kama sakata hilo lilikuwa limekwisha! Kwa mara ya kwanza katika maisha yake alijikuta akiamini kuwa Mungu husikia kilio cha wenye shida.

    “Hapo ndio nilishakufa!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Dereva aliliondoa gari huku akilalamika kwa kupotezewa muda wake, walitumia kama dakika thelathini eneo hilo moja! Hata watu wengine ndani ya basi walisikika wakilalamikia kitendo hicho, bibi Nyanjige naye aliendelea kuhema kwa nguvu ndani ya khanga yake, hakuwa tayari kujifunua kwa kuogopa kugundulika kwani tayari kila mtu ndani ya basi hilo alikuwa na habari juu ya kusakwa kwake.





    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog