Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

JULIANA - 3

 







    Simulizi : Juliana

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Kwa kuwa naye alijua kwamba msichana huyo alikuwa akimfuata, akaongeza mwendo, japokuwa Halima alikuwa akiita ili asimame lakini hakusimama, aliendelea kutembea kwa mwendo wa haraka.

    Moyo wake ukawa na hofu kubwa, aliufahamu mtandao wa Global Publishers, aliamini kwamba kama picha zake zingetolewa katika mtandao huo, mwisho wa siku zingemaliziwa katika magazeti kitu ambacho kingemfanya kupata aibu ya mwaka ambayo hakuwahi kuipata maishani mwake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakukuwa na picha za utupu alizowahi kupiga zaidi ya zile ambazo alijipiga na kumtumia Gideon, moyo wake ukaanza kujuta, kitendo chake cha kuonyesha mapenzi kwa mwanaume huyo kwa kuamini kwamba angependwa kukaonekana kuanza kumtia aibu ambayo hakuwahi kuifikiria kabla.

    “Naomba unisubiri wewe kaka,” alisema Halima huku akikimbia kumfuata Fred.



    Fred akasimama, msichana huyo akamsogelea, alikuwa akihema kwa nguvu, alichoka kukimbia, tayari macho yake yalibadilika, yakawa mekundu kwani tayari machozi yalianza kukusanyika machoni mwake. Alimwangalia mwanaume huyo huku akionekana kutia huruma sana, kwa sababu alikuwa amedharauliwa, naye akamuonyeshea dharau msichana huyo kwa kumwangalia juu mpaka chini, halafu akamsonya.



    “Naomba uifiche aibu hii!” alisema Halima.

    “Eti msichana mzuri unatuma picha kwenda kwa mwanaume, hata aibu huoni. Sasa dawa yako moja tu, picha zako nawapa watu wa magazeti ya udaku ili ukome, tutafanya kama tulivyofanya kwa msichana Salma,” alisema Fred, yote ilikuwa ni kumtisha msichana huyo, hakukuwa na kitu kilichotokea, ila aliamua kulitumia jina la Salma kwa kuamini kwamba msichana huyo angeamini kwamba kulikuwa na mtu ambaye naye alifanyiwa mchezo kama huo.



    “Naomba unihurumie kaka yangu!”

    “Nikuhurumie wewe! Wewe nguchiro, wewe kibweka! Naanzaje kwa mfano?” aliuliza Fred kwa nyodo na kuanza kuondoka.



    Halima aliendelea kulia, alichanganyikiwa, alichokuwa akikiona mbele yake ni aibu nzito ambayo hakujua angeificha wapi sura yake. Huo haukuwa muda wa kumlaumu Gideon kwa kile alichokuwa amekifanya bali alitakiwa kupambana kuhakikisha kwamba picha zake hazitolewi kwenye mitandao ya kijamii na magazetini.



    Hakutaka kujiuliza kama mwanaume huyo kweli alikuwa na picha zake au la, jibu alilokuwa nalo ni kwamba alikuwa nazo kwani kama hakuwa nazo, alijuaje kama alipiga picha za utupu na kumtumia mwanaume? Hakutaka kuona akiadhirika na watu kugundua kile kilichokuwa kimetokea.



    Akawafikiria wazazi wake, akawafikiria marafiki zake na ndugu zake, endapo picha zake zingeanza kusambaa na kuzipata, nini kingetokea? Jamii ingemchukuliaje kama tu wangegundua kwamba yeye ndiye aliyepiga picha zile za utupu? Je, chuo kingeweza kumvumilia kuwa naye kama mwanafunzi wao, kitendo cha picha hizo kuwa hewani kilimaanisha ndiyo ungekuwa mwisho wa kusoma chuoni hapo.



    “Naomba usitume picha hizo, nitakupa chochote utakachotaka,” alisema Halima huku akimwangalia Fred, macho yake tu yalionyesha kumaanisha alichokuwa akikisema.

    “Hahaha! Mimi nataka vingi sana! Huwezi kunipa vyote,” alisema Fred huku akimwangalia msichana huyo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Niamini! Nitakupa kitu chochote utakachotaka!” alisema Halima huku akiomba hasa.

    “Sawa. Nahitaji milioni mia moja. Ukizipata, njoo nazo kesho,” alisema Fred huku akimwangalia msichana huyo.

    “Jamani wewe kaka!”



    “Sasa mbona sikuelewi! Unaniambia utanipa chochote, nimekwambia mkwanja unaanza kulialia,” alisema Fred.

    “Naomba uniambie kingine. Nakuomba!”

    “Basi tukutane pale Jumanj hotel tuzungumze kidogo manake kuna waandishi washanipigia simu wanataka kuzinunua picha zako,” alisema Fred, kichwa chake kilikuwa makini sana kwenye kutengeneza mikwara ya harakaharaka.



    “Sawa kaka yangu! Nitakuja!”

    Wakakubaliana ni muda gani walitakiwa kuonana mahali hapo. Halima alijua kile ambacho kingekwenda kutokea huko, lawama zake nyingi zilikuwa kwa Gideon ambaye hakuonekana kujali na aliamua kufanya hivyo kwa ajili ya kumkomoa tu.



    Hakutaka kuwasiliana na Gideon, alitaka kumaliza tatizo lililokuwa mbele yake kwanza kwani kama angemwambia mwanaume huyo, alikuwa na uwezo wa kuwatumia picha hizo wanaume wengine kitu ambacho kingekuwa kibaya zaidi.



    Kwa Fred, moyo wake ulikuwa na furaha tele, muda wote alikuwa akicheka kwa furaha. Kwa kipindi kirefu alimtamani msichana huyo, alimvutia lakini hakujua angempata vipi lakini leo, alikuwa na uhakika wa kuwa na msichana huyo chumbani.

    Hakutaka kuvumilia, akampigia simu Gideon na kumshukuru sana kwani kwa tekniki aliyokuwa ameitumia hatimaye alikuwa akienda kukamilisha jambo ambalo hakuwahi kulifikiria maishani mwake.



    “Kaka kwanza nashukuru sana. Mtoto kajaa! Nakutana naye baadaye! Hii ndiyo dawa yao hawa wanaowatumia wanaume picha za hasarahasara. Nashukuru sana mkombozi kwa kuniunganisha na mtoto Halima, kama kawa mtoto mwingine akileta shobo za kukutumia picha za utupu, nisakizie mimi mzee wa kumalizia, wewe ziasisti kama Ozil vile,” alituma ujumbe wa maneno kwenda kwa Gideon.



    Wakati Fred akituma ujumbe huo uliokwenda katika simu ya Gideon, hakujua kwamba mwanaume huyo alikuwa akioga na ujumbe huo ulipoingia, mtu aliyekuwa karibu na simu yake alikuwa Juliana.



    Haraka sana baada ya kuona ujumbe umeingia katika simu ya mpenzi wake, hakutaka kuchelewa, akaichukua simu hiyo, akatoa password na kisha kuufungua ujumbe huo.

    Kwanza mtumaji hakuwa na hofu naye, alimfahamu, alikuwa rafiki wa mpenzi wake lakini ujumbe ambao uliandikwa katika simu hiyo ndiyo uliomtia hofu.



    Akahisi mwili wake ukitetemeka kwa hasira, hakuamini alichokuwa akikiona. Machozi yakaanza kumlenga, hasira kali ilimkamata, alimfahamu Halima, alikuwa msichana mrembo na hakuamini kama msichana huyo aliwahi kumtumia picha za utupu mpenzi wake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa kuwa Gideon alikuwa ameanza kuoga, akaenda sehemu ya picha, akazitafuta picha hizo, akazikosa, hakutaka kusubiri, alikuwa akifanya mambo hayo harakaharaka huku akitetemeka, akaenda WhatsApp na kulitafuta jina la msichana huyo, alipoliona, akaona ikiwa imeblokiwa. Hakutaka kuridhika, aliamini kulikuwa na kitu.



    Akatoa block kisha kumtumia ujumbe mfupi uliosomeka ‘Simu yangu noma, njoo huku 0256780953’ kisha akamtumia na kuzifuta meseji hizo. Akatulia kusikiliza ujumbe kutoka kwa msichana huyo katika laini yake nyingine, alihitaji kujua ukweli juu ya msichana huyo.

    Gideon akatoka kuoga, akalivua taulo lake na kukaa kitandani. Alimwangalia mpenzi wake, Juliana, kwa jinsi alivyoonekana, hakuonekana kama alivyokuwa ameelekea bafuni, alibadilika na kwa jinsi uso wake ulivyokuwa, ilionyesha kabisa kwamba kulikuwa na kitu.



    Hakujua ni kitu gani kilitokea, ila cha kwanza kabisa akaiangalia simu yake, alitaka kujua kama ilikuwa salama. Akatoa password na kuingia huku akizuga kuangalia kama kuna ujumbe au kupigiwa simu.



    Akaenda kotekote, hakukuta ujumbe wowote wala simu iliyopigwa kwani wakati Juliana ametuma ujumbe kwa Halima, aliufuta ujumbe wake. Gideon akajiridhisha kwamba hakukuwa na kitu kibaya, sasa kwa nini mpenzi wake alibadilika hivyo?



    “Kuna nini? Mbona upo hivyo?” aliuliza Gideon huku akimwangalia Juliana.

    “Hakuna kitu! Kichwa kinaniuma sana, kimeanza ghafla, yaani sina raha mpenzi,” alisema Juliana huku akikishika kichwa chake.

    “Pole sana jamani! Hebu sogea huku kwanza,” alisema Gideon, Juliana akasogea na kisha kumkumbatia.



    Alilihisi joto la mwili wa msichana huyo, lilikuwa kali lililomfanya kujisikia vizuri kabisa kutokana na uwepo wa mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha. Walikumbatiana kwa dakika kadhaa na msichana huyo kuaga, siku hiyo hata kusindikizwa hakutaka.



    Njiani alikuwa na mawazo tele, moyo wake ulimuuma, kitu kilichokuwa akilini mwake ni kwamba Gideon alikuwa akitoka kimapenzi na Halima. Kwa nini amsaliti? Kwa nini mchukue msichana huyo na wakati alikuwa naye kipindi hicho.



    Akafungua WhatsApp kupitia kwa namba yake nyingine ambayo alimpa Halima. Alitaka kuangalia kama kungekuwa na ujumbe wowote ule, kabla ya kufanya chochote akabadilisha picha na kuweka ya Gideon.



    Alikaa na kuangalia huko, hakukuwa na ujumbe wowote ule lakini baada ya dakika chache akapokea ujumbe kutoka kwa msichana huyo ambaye alikuwa akilalamika.



    “Kwa nini umenifanyia hivi?” aliuliza Halima kwa kupitia ujumbe mfupi WhatsApp, tena aliweka na emoj ya kulia.

    “Nimekufanyaje jamani?” aliuliza Juliana kwa namba ile aliyojifanya Gideon.

    “Hebu niambie kitu kimoja! Unanipenda?” aliuliza Halima.

    “Daah! Unanipa wakati mgumu sana! Kwani wewe unanipenda?” aliuliza Juliana.

    “Ndiyo! Tena sana lakini sijui kwa nini umekuwa ukinikataa!” alijibu Halima.

    “Kwani nilikwambiaje?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Najua una mpenzi! Unampenda sana lakini naomba unipe nafasi. Ninakupenda mno, kinachoniumiza, nimekutumia picha zangu za utupu, umenitukana, mbaya zaidi umekwenda kumpa rafiki yako! Kwa nini unanifanyia hivi jamani Gideon?” aliuliza Halima huku akilalamika.



    Mpaka kufika hapo, tayari Juliana alipata picha juu ya kila kitu kilichokuwa kimetokea. Akashusha pumzi nzito, akashukuru Mungu kwani ni kweli msichana huyo alimpenda mpenzi wake lakini Gideon alimuonyeshea msimamo thabiti kwa kumwambia kwamba alikuwa na mtu na asingeweza kuwa naye.



    Moyo wake ukazidi kumpenda mwanaume huyo, alionekana kuwa imara, mwenye msimamo ambaye hakuwa akiteteleka hata kama alipendwa na msichana mrembo kiasi gani.

    “Kama nilivyokwambia! Siwezi kumuacha mpenzi wangu kwa ajili yako,” aliandika Juliana.



    “Sawa. Ila ulichonifanyia sijapenda,” aliandika Halima.

    Juliana akaamua kuachana na msichana huyo na kuendelea na mambo yake. Bado moyo wake ulikuwa kwa Gideon, alijua fika kwamba mpenzi wake huyo alikuwa mzuri wa sura, aliwatetemesha wanawake wengi hivyo kitendo cha kutokuwa naye karibu kilimaanisha kwamba angewapa nafasi wanawake wengine kumfuatafuata.



    Mapenzi yakaendelea mpaka walipomaliza chuo. Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya Gideon ni kwenda nyumbani kwa kina Juliana na kuzungumza na wazazi wake. Aliwaambia ukweli jinsi alivyokuwa akimpenda msichana huyo na alikuwa na malengo naye ya kumuoa na kuwa mke wake maisha yake yote.



    “Una uhakika unampenda binti yangu?” aliuliza Mzee Marcel huku akimwangalia Gideon.

    “Ninampenda mzee! Nisingekuwa nampenda, nadhani nisingefika mahali hapa,” alijibu Gideon huku akitoa tabasamu pana.



    “Basi sawa. Kama mmependana mimi nitasema nini sasa! Sina msemo au mama hapa,” alisema Mzee Marcel na kumgeukia mkewe.

    “Hata mimi sina! Cha msingi ni kumuomba Mungu mpaka watakapofunga ndoa,” alisema mama yake Juliana.



    Baada ya miezi minne, wawili hao wakafunga ndoa na kuwa mume na mke. Kwa kuwa Gideon hakuwa akijiweza sana, akapewa milioni hamsini kwa ajili ya kufanya biashara. Hiyo ilikuwa nafasi kubwa kwa mwanaume huyo, hakutaka kuona akishindwa, akaingia katika kazi ya kilimo, akakodi mashamba na kuanza kulia mahindi na nafaka nyingine.



    Hiyo ndiyo ikawa biashara iliyomuinua kutoka pale alipokuwa. Akaanza kutengeneza pesa pamoja na mkewe. Muda wote walishirikiana wao wawili, biashara ikakua, wakaingiza mamilioni ya shilingi na kufanikiwa kuwa matajiri wakubwa.



    Ndani ya kipindi kifupi, wakajenga jumba lao kubwa na la kifahari na kununua nyumba nyingine. Wakawekeza katika ardhi na kila kitu walichokuwa wakikifanya, Mungu akawabariki zaidi na kuyafanya maisha yao kuwa na furaha, amani na mapenzi tele.

    “Nikwambie kitu mume wangu?” aliuliza Juliana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Niambie!”

    “Sikuona siku zangu! Nina uhakika kwamba nina mimba,” alisema Juliana huku akimwangalia mumewe kwa uso uliokuwa na tabasamu pana.

    “Kweli?”

    “Kweli tena!”



    Gideon akamsogelea mkewe na kumkumbatia. Moyo wake ukawa na furaha tele, hakuamini kama mkewe alikuwa na mimba kwani kitu pekee alichokuwa akikihitaji sana kipindi hicho kilikuwa ni mtoto tu.



    Alikuwa na kila kitu, utajiri, alikwenda alipotaka kwenda lakini suala la kutokuwa na mtoto ndilo lililokuwa likimtesa usiku na mchana, kitendo cha mkewe kusema kwamba alihisi alikuwa na mimba, kikampa fura tele.

    Baada ya wiki mbili, akaenda kupima, akaambiwa kwamba alikuwa mjauzito kitu kilichompa furaha.



    Mapenzi yakaongezeka, kila wakati Gideon alikuwa akimpigia simu mkewe kumjulia hali. Alimuomba Mungu kila siku kwamba siku ya kujifungua mkewe ajifungue salama kabisa.

    “Hamjambo!” alisalimia Gideon huku akimwangalia mkewe.

    “Hatujambo?”



    “Ndiyo! Si mpo wawili! Wewe na huyo hapo,” alisema Gideon huku akicheka.

    “Hahah! Hatujambo! Tumekumisi tu!”

    “Kweli?”

    “Yeah! Hasahasa huyu hapa,” alisema Juliana huku akimuonyeshea mumewe tumbo lake.



    Gideon akamsogelea, akalishika na kisha kuweka sikio lake katika tumbo lile. Lilikuwa dogo, halikuanza kuonekana lakini kwake hakutaka kushindwa, alihitaji kuonyesha mbwembwe zote hata kabla mtoto hajazaliwa.



    Kutokana na furaha kubwa aliyokuwa nayo, Gideon akaanza kuwaambia marafiki zake wengi kuhusu ujauzito ule, kila alipotembea alijiona kuwa kidume kwani kulikuwa na wanaume wengi ambao hawakuwa na watoto, kwake, alijiona kuwa na nguvu kuliko wote.



    Malenzi mema kwa mkewe yakaongezeka, akazidi kumjali, mapenzi yakanoga sana mpaka alipotimiza miezi tisa na hatimaye kwenda kujifungua, akafanikiwa kupata mtoto wa kike waliyempa jina la Jesca.

    “Ni mtoto mzuri sana,” alisema rafiki yake huku akimwangalia mtoto huyo.

    “Kweli?”



    “Yeah! Kachukua kila kitu kutoka kwa mama! Ila hivi vikono hivi ni vya baba pyua,” alisema rafiki huyo na kuanza kucheka.

    Hiyo ndiyo ikawa furaha yao, ndiyo ikawa mwanzo wa kupendana zaidi na zaidi. Gideon hakuwa akitulia kazini, kila siku alikuwa akirudi nyumbani mapema kabisa, alipofika, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumbeba mtoto wake, kwake alikuwa kila kitu, alikuwa tayari kupoteza kila alichokuwa nacho lakini si mtoto huyo.



    Wakawa karibu zaidi na mtoto wao, walimpenda na kumpa kila kitu alichotakiwa kupewa. Miezi ikakatika, siku zikaenda mbele, waliendelea kumpenda kila siku huku wakiahidi kumfanyia mambo mengi katika maisha yake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipofikisha umri wa miaka miwili, akaanza chekechea katika Shule ya Watoto ya Livingstone Day Care ambayo ilikuwa ikisomwa na watoto wa matajiri tu. Walitaka kumpa elimu bora, hawakupenda kumuona akipokea elimu ya kawaida kwa kuamini kwamba hakukuwa na kitu ambacho kingemkomboa zaidi ya kuwa na elimu tu.



    Mtoto alipofikisha miaka minne, wakapanga kupata mtoto mwingine kwa kuwa tayari Jesca alikuwa mkubwa. Wakajadiliana na kukubaliana kwamba kusingekuwa na tatizo lolote lile kama tu wangepata mtoto wa pili.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog