IMEANDIKWA NA : NEA MAKALA
*********************************************************************************
Simulizi : Usaliti Wa Kiapo
Sehemu Ya Kwanza (1)
TONY ni kijana mtanashati na mwenye muonekano maridhawa, tabasamu lake limekuwa likihadaa nyoyo za wasichana wengi. Sauti yake tulivu isiyo na mitetemo ilizidi kuwaburudisha wengi pindi ipenyapo masikioni mwao. Umaarufu wa Tony ulichagizwa na upekee wa falsafa na misimamo yake binafsi, kamwe hakuruhusu mtu afanye maamuzi kwa niaba yake. Juhudi na ubunifu katika kila alichokifanya ukampa Tony heshima ya kipekee na kuwa kifani kwa vijana wa rika lake.
Tony ni mtu anayependa kusoma na kufatilia vitabu na majarida mbalimbali ya wanafalsafa na wanasaikolojia, kwake yeye mwanamke ni kiumbe dhaifu kinachoendeshwa kwa hisia na mihemko lakini mwanaume siku zote ni bora anayeongozwa na nguvu ya kufikiri kwanza kisha hisia na mihemko huja baadaye. Misimamo yake ilimuaminisha kuwa Mapenzi ya kweli hupatikana zaidi kwenye riwaya na tamthilia, mwanamke yupo kwa ajili ya kumfurahisha na kumburudisha mwanaume, hivyo kwake kuwa na uhusiano na msichana zaidi ya mmoja halikuwa jambo la kushangaza. Tony ni kati ya vijana wachache waliojaliwa kuwa na maneno matamu na makali ambayo aliyatumia kama silaha ya kukata nyoyo za warembo wengi.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***************
Ni jioni moja tulivu iliyopambwa na mawingu mepesi huku mvua za rasharasha zikipunguza vumbi la mji mdogo na wa kitalii Bagamoyo, Sauti za ndege wanaorejea katika viota vyao zilichagiza kutoa melodi tamu masikioni mwa wapenzi wawili walioketi ndani ya sebule yao kubwa na yenye kupendeza wakiongea na kufurahi.
“Tony asante kwa mapenzi unayonionesha, nakili kuwa wewe ni mwanaume wa pekee sana,” alisema Theresa.
Theresa au Tedy amefahamiana na Tony kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa, lakini kwa jinsi alivyompenda Tony ni kama amekuwa akifahamiana naye kwa kipindi cha miaka, ukweli alihisi amechelewa sana kuwa naye.
“Tedy wewe ni msichana mrembo na mwenye uzuri wa asili mimi ni wako nawewe ni wangu tuu,” Tony alijibu huku akiishika mikono ya mpenzi wake.
“Kuwa nami hivi siku zote, niahidi kuwa tutakuwa pamoja hata baada ya kifo, mi nawe ni moyo mmoja katika miili tofauti, kuwa nami usiniache Tedy,” aliendelea kuongea maneno ambayo moja kwa moja yalimfanya mwanadada yule kupata msisimko wa ajabu na kujihisi kuwa yeye ni msichana mwenye bahati kuliko wengine wote.
“Asubuhi kwangu haijakamilika bila uwepo wako, napenda kukuona mchana na jioni kadharika, wewe ni maumivu yasiochosha, nitakupenda daima.”
Tony alizidi kuzama na kuchukua nafasi kubwa moyoni mwa binti yule, wakati akiendelea kuongea na kumfanyia vituko vya hapa na pale ghafla simu yake ikaita, kuiangalia akakuta ni swahiba wake wa siku nyingi Darmian, akakaa sawa na kuipokea,
“Niaje wa obey!”
“Hakuna cha obey wala uswazi leo, kisanga kinakuja kwako”, alijibu Darmian.
“Nini?” Tony alishtuka kusikia kauli hiyo ya rafiki yake.
“Yaani hadi dakika hii, ninavyozungumza Vanessa anakaribia kufika kwenu sasa kama upo bado na Tedy jua kazi unayo,” alisema Darmian na kukata simu.
Taharifa ile ilimchanganya kidogo Tony japo alikuwa mtu wa kuchanganya sana wasichana lakini haikutokea hata siku moja akawakutanisha, anayafahamu vizuri sana maumivu ya mapenzi. Alijitahidi kila awezavyo asije gonganisha magari, mabadiliko yale ya muda mfupi yalimshtua kidogo Tedy na kuanza kuhoji,
“Vipi mpenzi mbona umebadirika ghafla kuna tatizo gani?”
“Hamna kitu nipo sawa”
“Mbona kama unahofu hivi?”
Tony akashindwa kutoa majibu mazuri kwa mpenzi wake, akajikuta njia panda asijue afanye nini ili kuepusha fumanizi ambalo ndani ya muda mfupi linaweza kutokea. Wakati akiendelea kufikiri, akapata wazo la kumpigia tena Darmian ili aone kama anaweza kumsaidia kumzuia Vanessa asifike nyumbani. Akapiga simu ikaita kwa muda mrefu bila majibu, wakati akiendelea kuyafanya hayo Tedy nae akaanza kupata wasiwasi asielewe nini kimemkuta mwanaume wa ndoto zake.
“Babe! Mboni hivyo sikuelewi ujue,” alisema Tedy huku akisogea zaidi alipo mpenzi wake.
Tony akasimama na kusogea mbali kidogo na alipokaa Tedy, akatembea umbali mfupi kisha akageuka na kumtazama mahabuba wake kwa tabasamu zito.
“Dunia yangu ipo mikononi mwako, wewe ni zaidi ya paradiso kwangu, uko kama mashairi nami ni muziki, wewe ni matamanio yangu, nami ni mpendwa wako”
Maneno yale yakaondoa hofu ambayo Tedy alikuwa ameshaanza kuipata akajikuta akifurahi mno, lakini wakati Tony anayaongea hayo tayari Vanessa akawa amefika mlangoni hivyo akaanza kupiga makofi ya pongezi kwa Tony. Vanessa akashtuka sana alipokutanisha macho yake na Tedy, vivyo hivyo Tedy nae akabaki katika sintofahamu kuona uwepo wa msichana mwingine pale japo hawakuwa wakifahamiana wala kuonana kabla. Tedy akajikuta akisimama kumtazama Vanessa ambaye alikuwa akipiga hatua fupi fupi kuelekea alipo Tony.
Tony hakuonesha kushtuka ila akajikuta akiangua kicheko kilichowashangaza Tedy na Vanessa, akachukua rimoti na kuwasha muziki kwa sauti ya juu kidogo. Akamfata Tedy na kuanza kucheza naye alipokaa sawa akamgeukia Vanessa ambaye alionekana kama anataka kuuliza kitu lakini maswali yote yaliisha baada ya Tony kumshika mkono ivyo naye akajikuta anatulia, wakacheza muziki kwa muda wa kama dakika 5, kisha Tony akazima na kukaa chini, nao pia wakafanya vile vile.
Tony akachukua maji na kumimina kwenye Bilauri ya shaba na kunywa hili kuburudisha Koo lake lililokauka. Kisha akawatazama Vanessa na Tedy kwa uchangamfu wa hali ya juu,
“Nimeamini msemo ule wa kuwa mwanamke ni pambo la nyumba, uzuri wenu umeifanya nyumba yangu kuwa kama paradiso ndogo, harufu ya manukato yenu..............aaah so good” akashusha pumzi ndefu.
“Tedy huyu anaitwa Vanessa ni wifi yako,” Tedy akatoa tabasamu na kumpa mkono Vanessa.
Akamgeukia Vanessa na kusema maneno yale yale aliyosema kwa Tedy, Vanessa nae akatabasamu, alivyoona ametoa utambulisho ambao utakuja kuibua maswali ambayo hasingeweza kuyapatia majibu akatafuta namna ya kufanya hili wasigunduane kuwa ni wake wenza, Tony akafikiri kidogo kisha akamgeukia Vanessa na kumwambia,
“Wewe sio mgeni hapa, naomba ukajichukulie kinywaji ukipendacho na nikipendacho alafu tuje tusherekee”.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Van bila kusita akanyanyuka na kuelekea kule ambapo vinywaji vinaifadhiwa. Tony alivyoona Van ameenda akamsogelea Tedy na kumshika kiuno kisha kwa sauti ya taratibu akamwambia,
“Kuwa huru mpenzi wifi yako hana noma,” kisha akamsogeza karibu zaidi na kumbusu.
“Sawa honey nitakuwa huru”
Jibu lile lilimfurahisha Tony ambaye aliamua kutumia nguvu kubwa kucheza na akili za wasichana hao hili wasije kugundua kuwa wote wana nafasi sawa kwake, akaamua kucheza mchezo huo wa kumfanya mmoja dada na mwingine mpenzi kwa kuwatambulisha kila mmoja kuwa ni wifi wa mwenzie. Hama kweli mwanamke ni kiumbe kinachoongozwa na hisia bila kuwa na uwezo wa kufikiri kwa haraka, sijajua kwanini warembo wale hawakuhoji zaidi wakabaki kusadiki maneno yake na kila mmoja kujiona bora.
Tony akamwachia Tedy ambaye hakutamani kuachiwa hata kwa dakika moja,
“Honey naona wifi yako anachelewa kurudi ngoja nikamwangalie kwanza amekutwa na nini,” alisema Tony na kuanza kupiga hatua ndefu kuelekea kule alipo vanessa, lakini kabla hajafika akakutana naye njiani.
Tony akamshika mkono na kurudi naye kwenye stoo ya Vinywaji. Nyumba ya Tony ni kubwa mno na alitumia ubunifu wa hali ya juu kuhakikisha kila hitaji linakuwa na sehemu yake, alijitahidi kuweka maktaba ndogo ambapo huwa anajisomea vitabu na majarida mbalimbali, pia kukawa na sehemu ya kuhifadhia vinywaji tofauti na kwenye jokofu. Tony hakuacha kutenga sehemu maalumu kwa ajili ya kufanyia sala zake kwa Mungu japo changamoto za ujana zilimzidi nguvu.
Akaichukua ile chupa ya mvinyo aliyoishika Vanessa na kuiweka pembeni, hakupoteza muda akamvuta kwa karibu na kuanza kumbusu, Mapigo ya moyo ya Vanesaa yakaanza kwenda mbio kuliko kawaida,
“Kwanini umekuja bila kunitaarifu mapema, ona sasa nakosa uhuru wa kukubusu kutokana na heshima yangu kwa wifi yako”
“Samahani mpenzi sikuwa nafahamu kama una mgeni leo,” Vanessa alijibu.
Tony akaendelea kuvuluga akili ya mwanadada yule kwa kumshika na kumbusu kila mahali,
“I real missed you (nimekupeza sana),” alisema Tony
“I missed you too honey (nimekupeza pia mpenzi), Van akarudisha majibu.
Tony alivyoona amefanikiwa kwa kiwango kikubwa akamwachia Van na kuichukua ile chupa ya mvinyo,
“Twende wifi yako asije kujisikia mpweke”.
Wakaongozana hadi alipo Tedy kisha kwa pamoja wakafungua mvinyo ule na kuanza kuunywa taratibu huku wakisindikizwa na muziki laini.
******************
Darmian baada ya kuona kuwa Tony alimpigia sana bila ya yeye kujibu akahisi hali ya hatari kichwani mwake. Ingawa alichoshwa na tabia ya rafiki yake ya kucheza na nyoyo za wasichana wengi kwa wakati mmoja lakini akaamua atafute namna ya kwenda kumsaidia hivyo akaamua ampigie rafiki yake mwingine,
“Oyah upo wapi wewe?” akauliza Darmy baada ya simu kupokelewa.
“Ndio nimetoka kazini naelekea nyumbani,” akajibu Yassir.
“Sasa tukutane basi hapo Mapinga twende kwa Tony naona ana tatizo kidogo”
“Tatizo!” akauliza Yassir kwa mshangao.
“Ndio! Jamaa naona leo kapata fumanizi”.
“Duuh! Kwa hiyo kawakutanisha Mirrium na Vanessa au?”.
“Aah! Mirrium mbona alishaachana naye kitambo sasa hivi ana mwingine anaitwa Tedy”.
“Duuh! Kweli ni shida, poa nipe dakika 10 nitakuwa hapo”
“Sawa usikawie asee”.
Darmian akakata simu na kuanza safari ya kuelekea walipopanga kukutana na Yassir.
Baada ya muda mfupi wakawa wamekaribia kabisa kufika nyumbani kwa swahiba wao, wakakuta geti limerudishwa tuu halikufungwa vizuri na kwa kuwa walishazoea kwenda mara kwa mara, wakaingia bila kusubili kukaribishwa. Wakapita katika bustani iliyo mbele ya nyumba na moja kwa moja hadi kwenye mlango mkubwa, lakini kabla hawajaingia ndani wakashangaa kusikia watu wakiongea na kufurahi. Maswali yakaanza kuzunguka vichwani mwao, shauku ya kutaka kujua nini kilichojili ikaongezeka.
Wakasikia watu wakiongea na kucheka mno, wakatazamana kwa mshangao kidogo sababu walijua wangekuta ugomvi mzito. Kwa pamoja wakaingia ndani na kukuta Tony akiwafanyia vituko vilivyowafurahisha mno, Tony alivyowaona akashusha pumzi ndefu na kunyoosha mikono juu kushukuru,
"Karibuni sana," akawakaribisha.
"Asante," Darmy akaitikia.
"Mambo zenu warembo," Yassir akawasalimu.
Tedy na Van nao wakaitikia na kwa pamoja wakakaa na vinywaji vikaongezwa wakaendelea kunywa na kuongea hili na lile.
Darmy akaendelea kufikiri juu ya mchezo alioucheza Tony asipate jibu akatamani kujua nini kilijili lakini hakuweza kuuliza kwa wakati ule. Ikamlazimu avute subira Zaidi hadi warembo wale watakapoondoka, matamanio yake yalitimia baada ya muda mfupi pale Vanessa na Tedy walivyoaga kwa pamoja kuwa muda umeenda na wanahitaji kurejea majumbani mwao. Tony alihofia mno kwa wasichana wale kama wangeongozana peke yao lolote lingetokea katika maongezi yao, akafikiri kitu kidogo kisha akasema,
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vanessa Subiri kidogo acha nimsindikize Tedy”
“Kweli Van endelea kubaki nasi kidogo, kwanza mama hana shida alafu nyumbani ni hapo tuu karibu, acha Tony amsindikize Mgeni sisi tuendelee kupiga soga,”alisema Yassir.
Van bila kipingamizi akakubali, Darmy akamuangalia Tony na kumuonesha ishara ya dole gumba kuashiria kuwa asihofu kila kitu kiko sawa.
Tony akatoka na kimwana yule na kuwasha gari tayari kwa safari ya kumrudisha kwao,
“Asante mpenzi nimefurahi sana kuwa na wewe leo, hata wale rafiki zako na yule wifi yangu kwakweli ni wachechi mno,” Tedy alisema.
“Usijali mpenzi, nafanya yote kuhakikisha unafurahi”
Jibu lile liliiburudisha nafsi ya Tedy pasipo kujua kuwa ana wenzake wengi tuu, safari iliendelea hatimaye wakafika, Tedy akamtazama Tony kisha akambusu na kushuka kwenye gari.
Tony akamsindikiza kwa macho hadi alipoingia ndani akageuza gari na kurejea kwake ambapo akamchukua vanessa na kumfikisha nyumbani kisha akawasindikiza na maswahiba zake,
“Ebhana eenh leo umewezaje kuwa na wanawake wawili kwa wakati mmoja na wasifahamiane?” Yassir akafungua maongezi maana ya kimya kifupi kupita.
“Nilicheza tuu na saikolojia zao, nikaizuia hofu kwangu na kumfanya kila mmoja afurahi kwa nafasi yake,” akajibu Tony.
“Ila uoni kama ni hatari kuendelea kuwachanganya hivi, kwanini usichague mmoja ukatulia naye,” Yassir akaendelea kusema.
Kauli ile ilimfanya Tony afunge breki ya ghafla ambayo iliwashtua wote, kisha akapiga piga usukani kwa hasira na kumgeukia Yassir,
“Lini umekuwa na kichwa cha panzi kiasi cha kusahau yote ndani ya muda mfupi, leo hii wewe umekuwa wa kuniambia nitulie na msichana mmoja,” Tony aliongea kwa hasira mno.
“Kweli Tony wakati umefika lazima ufanye maamuzi magumu, chagua yule unayeona unampenda kuliko wengine,” Darmy naye akaongozea.
“Kupenda! Mnajua nini nyinyi kuhusu kupenda, mmesahau kisa cha mpendwa kupenda asipopendwa akatendwa na kwenda, lakini kule alikopendwa hakupenda!”.
Tony akashusha pumzi ndefu kisha akaendelea kuongea,
“Ninyi ni marafiki zangu wa muda mrefu sana, najua mna nia njema kwangu lakini kwa hili naomba mniache tu”
“Kweli sisi ni rafiki zako lakini unatupa wakati mgumu sana, hivi hao wanawake wakija kugundua kuwa unawachezea watatufikilia vipi sisi. muda ndio huu funika yaliyopita na usonge mbele, binafsi leo ndio mara ya mwisho siwezi tena kujiingiza kwenye ujinga wako,” aliongea Yassir kisha akafungua mlango na kushuka kwenye gari na kuondoka, Darmy nae akafanya vile vile na kumuacha Tony akiwa mwenye kuwaza sana.
Tony ni mmoja kati ya waongozaji wa filamu wenye mafanikio na upekee katika kazi zake, ubunifu, umakini na kujituma kwake kukaifanya kampuni ya STUDIO 7 MEDIA LTD. kukua na kutambulika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, mbali na mtazamo hasi juu ya wanawake lakini hakuwanyima fursa ya kufanya kazi walau kwa majukumu machache.
Upekee wa kampuni hiyo ndio uliosaidia kupata nafasi ya kuingia ubia na kampuni moja ya kikorea iliyofahamika kwa jina la TAE XHIANG SUNG GROUP, kampuni hii imejikita Zaidi katika maonesho ya mitindo na matangazo mbalimbali hivyo kwa kampuni ya Tony ilikuwa nafasi muhimu sana ya kuzidi kutanua wigo wa kazi yake.
Ni asubuhi moja tulivu yenye mawingu mepesi yaliyofanya siku hiyo kuwa na baridi kiasi, Tony akiwa kitandani akashtushwa na mlio wa simu yake, akaamka na kuangalia akagundua kuwa ni alarm aliyoitega ili imuamshe. Siku hiyo alikuwa na kikao cha muhimu sana, kitakachotoa mpango kazi kati ya kampuni yake na ile kampuni ya kikorea iliyofungua tawi hapa nchini, hivyo ikabidi ajiandae haraka tayari kwa ajili ya safari ya kwenda Ubungo plaza ambapo kikao kimepangwa kufanyika. Alipojaribu kuwasha gari likakataa kuwaka, hakupoteza muda kujua tatizo ni nini akaamua atumie usafiri wa umma kwa siku hiyo. Gari lilisimama karibu kila kituo jambo ambalo lilimkera Tony na akaanza kuona dalili za kuchelewa kikao.
Walipofika maeneo ya makongo wakakuta kuna foleni kubwa uliyoenda hadi mwenge na alivyotazama saa yake akaona amebakiwa na nusu saa kabla ya kikao kuanza, ikabidi ashuke na kupanda pikipiki. Akamuhimiza dereva wa pikipiki ile aongeze mwendo ili aweze kuwahi. Nausifu ujanja wa dereva yule kwani alijitahidi kupenyapenya kukwepa foleni ile lakini walipofika maeneo ya mawasiliano dereva alipoteza umakini kidogo na kujikuta akielekea kuivaa gari ndogo aina ya Ferrari akajitahidi kufunga breki lakini akuweza na kujikuta akiigonga kwa nyuma. Wote wakaanguka na kwa bahati nzuri hakuna aliyeumia zaidi ya ile pikipiki na gari, ndani ya sekunde kadhaa watu wakawa wamezunguka eneo lile, ugomvi ukazuka na wote wakataka kumpiga dereva wa pikipiki kwa kutokuwa makini.
“Jamani msimfanye chochote huyu dereva, kosa ni langu mimi ndiye niliyekuwa nikimchochea aongeze mwendo kwani nina kikao cha muhimu nahitaji kuwahi,” Tony alitoa utetezi wake.
“Mpumbavu wee! kikao ni muhimu kuliko usalama wako?” akasema mwananchi mmoja ambaye sikumfahamu Jina Lake.
“Naweza kusema hivyo ila tafadhalini sana msifanye lolote na naomba kuongea na mwenye gari sina muda zaidi wa kukaa hapa,” alisema Tony.
Mzozo uliendelea na ndani ya muda mfupi akatokea msichana ambaye kuwepo kwake tuu, kulifanya watu wote wakae kimya na kila mmoja aliduwazwa na uzuri wake. Akasogea akaliangalia lile gari kisha akamuangalia dereva wa pikipiki na kisha kumtazama Tony, ama kwa hakika ukimuangalia analipsi za kuvutia, kidevu ndio sisemi kitu jamani, macho yake ang’avu yalifanya nyoyo za vidume wengi kukimbia zaidi ya kawaida, umbo namba nane na mwenye mvuto zaidi ya maua wanaume wengi wakajikuta wakitaka kuonesha ubavu wao kumsaidia mrembo yule,
“Samahani sana dada yangu ni bahati mbaya tuu,” aliongea dereva wa pikipiki.
Yule mwanadada akamuangalia kwa dharau sana kisha akasonya,
“Unajua thamani ya hii gari? Unajua ni kiasi gani cha pesa unachotakiwa kulipa kwa ajili ya hii gari, nafikiria kukuweka polisi kwa muda hadi utakapolipa pesa yangu,” aliongea mrembo kwa dharau na hasira kidogo.
“Naomba nilipe mimi gharama za kutengeneza gari lako, haya yote yametokea kwa sababu yangu” Tony akazungumza.
Yule msichana akamuangalia Tony kisha akacheka kwa dharau sana, Tony alivyoangalia saa yake akagundua kuwa zimebaki dakika 5 kikao kuanza akakosa Amani na akahofu zaidi nini kitatokea endapo atakikosa kikao kile muhimu.
“Tafadhali dada yangu nina haraka mno, naomba tusifanye mambo kuwa makubwa binafsi nitalipa deni hili”
“Lipa sasa hivi! Asiondoke bila kulipa huyo! Wamezoea hao!” yalikuwa maneno ya baadhi ya watu waliokuwa eneo lile.
Tony akamshika mkono mrembo yule na kumsogeza pembeni lakini kitendo kile kikamchukiza mara dufu msichana yule, akanyanyua mkono wake na kumzaba kofi Tony, asee nafsi ilimuuma mno akatamani ajibu mapigo lakini akajiona mjinga endapo atafanya tukio lile, akajitahidi kujizua kisha akamuangalia usoni mwanadada yule,
“Huna hadhi ya kuhushika mkono huu masikini wewe na usirudie tena kunigusa, kwa kuwa umenianza mimi namaliza lazima ulale kituo cha polisi leo, unajua mimi ni nani?” msichana aliendelea kuongea kwa vitisho.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tony alizidi kuumia nafsini kwani hata siku moja hakukubali kudhalilishwa na mwanadamu hasa wa kike, hasira zikampanda akamwangalia mwanadada yule kisha akajikuta anacheka mno,
“Sawa fanya unalojisikia ila huyu dereva muache aende,” Tony akasema na kumpa kiasi kidogo cha fedha dereva yule wa pikipiki ambaye alishangaa sana ukarimu wa Tony kwani toka aanze kufanya kazi ile hakuwahi kukutana na mteja wa namna ile akashukuru na kuondoka.
Mrembo bado akawa na nia ya kumdhalilisha Tony mbele ya watu ambao wengi walishaanza kupiga picha na kurekodi kwa simu zao tayari kwa kuziachia kwenye mitandao ya kijamii, Tony akatoa kitambulisho chake cha taifa na akatoa namba zake za simu na kumkabidhi yule msichana,
“Nakuamini na naomba uniamini, peleka gari yako gereji yeyote kisha baada tu ya kikao kuisha nitakuja hapo kulipa gharama zote, nitumie ujumbe wenye malekezo ya hiyo gereji kwa sasa naomba uniache niende”
Tony akusubili kuambiwa nenda akaanza safari baada tu ya msichana yule kuipokea ile dhamana, ya kitambulisho.
*************
Kikao kikaanza bila hata ya Tony kuwasili, wadau wakaanza kujadili mambo mbalimbali juu ya uendeshwaji wa kampuni izo mbili ilipofika zamu ya STUDIO 7 MEDIA LTD kuelezea namna kazi itakavyoenda kila mmoja akashangaa kutokumuona mkurugenzi wa kampuni hiyo, ikabidi mkurugenzi wa kampuni ya kikorea asimame na kuongea kwanza,
“Nasikitika katika kikao cha kwanza mshirika mwenzetu kushindwa kufika, hii inanipa wasiwasi kidogo mimi kama mwakilishi na msimamizi wa kampuni hii ya TAE XHIANG SUNG GROUP kwa hapa Tanzania, japo sijajua ni sababu gani zilizomfanya hadi muda huu asiweze kufika lakini huu naweza kuuita uzembe usiweza kuvumilika,” aliongea Martha ambaye ni msimamizi wa kampuni ile.
Martha ni msichana anayejiamini mno katika kila analolifanya, yeye asili yake ni mtanzania japo kwa muda mrefu sana alikuwa nchini Korea kimasomo na kubahatika kufanya kazi huko huko ivyo kampuni aliyokuwa akiifanyia kazi kufungua tawi hapa nchini ilitokana na juhudi zake binafsi,
“Tumeipa nafasi kampuni ya STUDIO 7 MEDIA LTD kwa kuwa tuliamini ni kampuni yenye watu makini na ubunifu mwingi katika kazi lakini huu uzembe…………” kabla hajaendelea kuongea akajikuta anaduaa kumuona Tony akiingia huku akihema sana, Martha akajikuta anashindwa kuendelea kusema alichokusudia kusema,
“Lakini huu uzembe…lakini…..lakini….!” akajikuta anarudia maneno huku macho yake yakishindwa kutoka alipo Tony.
Tony aliposikia mwanadada yule anashindwa kumalizia sentensi zake akanyanyua kichwa na kutazama ili afahamu japo kwa kinaga ubaga nini tatizo, daah naye akashikwa na bumbuazi kukuta ni Mtu ambaye anamfahamu, mapigo ya moyo yakaenda mbio zaidi, akageuka kwa jirani yake na kumuuliza,
“Huyu msichana ana cheo gani?”
“Huyu ndie mkurugenzi wa kampuni uliyoingia nayo ubia”
Fikra zikaenda mbali zaidi, kila mmoja akawa anashangaa juu ya tukio lile, Tony akawa anapiga piga meza kuonesha mfadhaiko.Martha akakohoa na kikao kikaendelea, Tony akaomba radhi kwa kuchelewa, wadau wakaelewa na wakafikia makubaliano namna ya kuanza kazi. Kikao kilifungwa na wakapena mikono ishara ya umoja lakini ilipofika zamu ya Tony kupeana mkono na Martha, Tony akakwepa na kuanza kuondoka lakini kabla hajatoka akasikia anaitwa,
“Mr. Tony nakuomba mara moja,” ilikuwa ni sauti ya mmoja ya wadau wa ile kampuni ya kikorea akihitaji kuzungumza machache.
Tony akasogea alipo yule mdau ili kusikiliza nini alichoitiwa,
“Mimi ni msaidizi wa bibie hapa, hivyo natumai utatupa ushirikiano wa kutosha katika kila jambo,” alisema yule mdau.
“Shaka ondoa” Tony akajibu.
“Kwa kuwa wakurugenzi wote mpo mimi nafikiri mngepata muda wa kukaa na kuona jambo gani lianze kufanyiwa kazi”
“Ni kweli ukizingatia muda unazidi kwenda na upinzani wa kibiashara ni mkubwa,” Martha akaongezea.
“Lolote mtakaloamua nipo tayari ila kwa sasa kuna mahali nawahi tutaonana wakati mwingine” akasema Tony na kuanza kuondoka.
Ukweli Tony hakufuraishwa kabisa kufanya kazi na mrembo yule alitamani hata avunje mkataba ila kila alivyofikiria kuhusu mafanikio atakayoyapata kutokana na ubia ule ikabidi avumulie.
Akaangalia simu yake na kukuta ujumbe mfupi uliomuelekeza mahali Fulani ambapo alitakiwa afike, bila kuchelewa akaanza safari na ndani ya dakika 45 akawa amefika. Ilikuwa ni gereji moja kubwa na ya kisasa iliyopo maeneo ya sinza iliyotambulika kwa jina la Mdidi Auto Garage. Alipoangaza huku na kule akakutana na sura ya mwanadada yule ambaye asubuhi alikuwa na ugomvi nae, akasogea hadi alipo na kumwambia,
“Nimerudi kulipa deni langu”
“Kaka naomba uniletee hiyo lisiti ya malipo” akasema yule msichana na ndani ya dakika lisiti ikaletwa Tony akashtuka alipoisoma, akakuta anatakiwa kulipa laki saba na nusu pesa za kitanzania (Tsh. 750,000).
“Mbona pesa nyingi kiasi hiki, na nikiangalia gari lilivyoumia haviendani” Tony akasema.
“Usitake nikuabishe lipa pesa kama huna sema,”
“Sawa nitalipa nipe dakika 15”
“Poa kila la kheri”
Tony hakuwa na pesa hizo mfukoni ikabidi aombe msaada kwa rafiki zake ambao jana yake tuu walikorofishana ila haikusumbua kitu kwani waliweza kumsaidia kwa kutumia mitandao ya simu. Tony akasogea hadi zilipo huduma za kutolea pesa kwa njia ya mtandao na akafanikisha hilo. Akarudi na kukabidhi zile pesa kisha akasogea kwa yule msichana na kumwambia,
“Samahani sana kwa usumbufu ila ulichonifanyia leo usikisahau”
“Una maana gani”
“Ya kawaida tuu, naomba unikabidhi kinachonistahili”
Msichana akapekua pochi yake kuangalia kitambulisho alichokabidhiwa na Tony kama dhamana ya uaminifu lakini hakukiona, akatoa kila kitu pembeni na kupekua kila mahala lakini hakufanikiwa kukipata. Akakaa chini na kuanza kutafakari wapi alipokiacha kitambulisho kile, akakumbuka kuwa amekiacha nyumbani kwao, ugumu ukaja ataanza vipi kumwambia Tony kuwa amesahau kitambulisho,CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vipi ujakiona kitambulisho! Nina mambo mengi ya kufanya, nimeshalipa deni lako nikabidhi istahiki yangu niende,” akasema Tony.
“Samahani kaka yangu nimekisahau kitambulisho chako nyumbani”
Tony akamtazama sana msichana yule akajikuta hajui amfanye nini,
“Ila kama hutojali nitakuletea popote ulipo jioni hii” aliendelea kuongea mwanadada yule huku hofu kidogo ikimtawala.
Tony akatabasamu na kuanza kuondoka bila kutoa jibu lolote, wakati anaondoka akafikiri vingi sana na akajikuta akiongea kimoyo moyo,
“Kwa kuwa umenianza, hakika sitokuacha, unawezaje kunidhalilisha kiasi kile”.
Jioni ya siku hiyo ilikuwa ngumu sana kwa Tony akajikuta akizama katika dimbwi la mawazo akiyafikilia zaidi matukio ya siku hiyo kuanzia yule mrembo ambaye hakulifahamu jina lake na yule mkurugenzi mwenza aliyemfahamu kwa jina la Martha. Kila alivyofikiri kuhusu kuwa karibu na Martha ndivyo moyo wake ukajikuta ukijawa na hasira hasa baada ya kukumbuka miaka kadhaa iliyopita.
“Martha kwanini umekuja katika katika maisha yangu, japo si rahisi ila natamani uende mbali nami, kwa muda mrefu hakutokea mwanamke ambaye angeusimamisha moyo wangu walau kwa dakika na kunifanya nimfikirie yeye tuu, lakini wewe umeweza hilo, nakuchukia na lazima ulipie hili,” alisema Tony huku akinywa mvinyo wake taratibu.
“Nitayafanya maisha yako kuwa magumu kuliko kawaida, niko radhi kufanya lolote, liwe la kielevu au la kipumbavu, nitahakikisha unashuka na kuwa mtu wa chini.”
Wakati akiendelea kufikiri hayo simu yake ikaita kuangalia ilikuwa namba ngeni ikabidi aipokee,
“Hallo”
“Hallo! Naongea na Tony”
“Ndio! Nani mwenzangu?”
“Mimi ni Jamilah”
“Jamilah wa wapi?”
“Ooh! Tony unamaswali mengi nipo maeneo ya Bunju kwa sasa, niambie nikuone wapi ili nikukabidhi kitambulisho chako”
“Njoo Mapinga”
“Sawa dakika 15 nitakuwa huko”
Simu ikakatwa na mawazo juu ya Martha yakakata ghafla, Tony akajiandaa haraka huku akinuia kuwa lazima mrembo yule alipie ule uzalilishaji alioufanya juu yake, akapanga kufanya kila aliwezalo amnase mwanamke yule kimapenzi.
Baada ya dakika 15 Jamilah akawa ameshafika maeneo ya Mapinga na kabla hajampigia simu kujua alipo, Tony nae akawa ameshafika maeneo hayo. Tony alitumia takribani dakika moja kuuangalia uzuri wa msichana yule hakika alikubali kweli Jamilah ameumbwa akaumbika. Mrembo yule naye akabaki ameduwaa kwani alimuona Tony tofauti na alivyokuwa asubuhi na kadri alivyozidi kusogelewa na Tony ndivyo alivyozidi kuchanganyikiwa kwa utanashati wake, akajikuta anababaika kuongea asijue aseme nini,
“Siwezi kukupa kitambulisho chako hapa, tutafute sehemu iliyotulia tukae walau tuzungumze kidogo,” alisema Jamilah.
“Sawa twende ukapaki gari yako pale alafu tutaenda huko”
Jamilah akaenda kupaki gari yake sehemu aliyoelekezwa na Tony kisha wakasogea katika mgahawa uliyo karibu akaagiza kinywaji lakini tony akakataa na kusema kuwa alishakunywa alipotoka ivyo hajisikii kunywa chochote, jibu hilo lilimfanya Jamilah nae kughairi kuagiza kinywaji,
“Tony samahani sana kwa kile kilichotokea leo”
“Huna haja ya kuomba msamaha ila mimi ndio natakiwa kuomba radhi”
“Hapana Tony ukweli kila nikifikiria niliyokufanyia leo, moyo wangu unauma sana na sikujua kuwa wewe ni mtu mwema na mkarimu kiasi hiki, nilijisikia aibu pale niliposahau kitambulisho chako nyumbani na nilitegemea utanifanyia kama niliyokufanyia ila uko tofauti mno”
“Yameisha hayo mimi nishasahau”.
Tony alijibu japo moyoni alikuwa na hasira sana juu ya huyo msichana ila akaamua kuigiza mwema hili atomize lile analolitaka.
Jamilah akatoa kitambulisho na kumkabidhi Tony, nae akakipokea na kushukuru, wakaongea mengi na taratibu mazoea yakaanza, usiku ukaingia na wakaagana huku wakiahidiana kuonana tena siku zijazo. Uchangamfu na vituko vya Tony vilitosha kumloga Jamilah na kujikuta kutamani kuwa karibu na mkaka huyo tena na tena.
BAADA YA MIEZI MITATU
Ushirika wa kampuni mbili ukawa mkubwa na maarufu katika macho na masikio ya watanzania wengi, umaarufu huu haukuishia Tanzania tuu ulivuka mipaka na kuenea katika nchi nyingi za Asia hasa zilizo karibu na Korea. Tony alijitahidi kutengeneza Makala mbalimbali zilizoonesha mitindo yenye utamaduni wa kiafrika na kiasia, Kama utafatilia vizuri mpenzi msomaji Afrika na Asia tamaduni zao zinafanana kwa kiasi kikubwa tofauti na zile tamaduni za Ulaya na Amerika. Kila mmoja alifurahia mafanikio hayo na kukaandaliwa na sherehe maalumu kwa ajili ya kupongezana. Sherehe hiyo ikapangwa kufanyika katika moja ya hoteli za kitalii zilizopo katika fukwe za bahari ya Hindi katika mji mdogo wa Bagamoyo. Wafanyakazi wote wakataalifiwa hivyo kila mmoja akawa akiisubiri siku hiyo kwa hamu zote.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku ya siku ikafika Tony akiambata na maswahiba zake Darmy na Yassir ambapo kila mmoja alikuwa katika suti moja matata sana, Siku hiyo iliwafanya waonekane wa tofauti sana,
“Tangulieni ndani kuna mtu namsubili,” akasema Tony.
“Duuh! Kama kawaida yako,” Yassir akadakia.
“Haya nani huyo anayekuja leo, Vanessa au Tedy?” Darmy akauliza.
“Si Tedy wala si Van, ila ni…..acha iwe surprise mtamuona akifika”
Darmy na Yassir wakatazamana kisha wakaingia ndani bila kuongeza neno, Tony akaendelea kusubili na ndani ya muda mfupi mwanadada mwenye urembo wa asili akawasili. Tony alitumia dakika moja kuthibitisha kuwa yule ni binadamu au malaika,
“Hakika mwanamke ni sawa na waridi lenye kuvutia na kunukia vizuri, kama ilivyo kazi ya waridi kupendezesha nyumba ndivyo ilivyo kazi ya mtu mke kumburudisha na kumstarehesha mtu mume,” Tony akasema hayo maneno moyoni, akaachia tabasamu zito na akuweza kuzuia mikono yake kumkumbatia mwanadada yule pindi alipomkaribia.
Kwa pamoja wakaongozana ndani wakaangaza huku na huko wakakuta kuna meza tupu, wakajongea na kukaa hapo, Uzuri wa binti yule ulizua gumzo kubwa kwa wageni wote waliolikwa kwenye sherehe hiyo. Darmian na Yassir wakashindwa kuvumilia kule walipokaa,
“Ebhana eenh! Umeona kule,” Darmy akasema.
“Wapi tena?” Yassir akauliza.
“Kule kwenye meza ile”
“Wee! Yule mtoto mzuri vile Tony kamtolea wapi”
“Mhmh! Kwani wewe ndio umemfahamu leo?”
“Daah! Yule jamaa sijui anauchawi gani, yeye tuu kila siku anaibua wapya”
“Ila usifikirie sana labda anaweza kuwa rafiki tuu”
“Aah! Kama ni rafiki yake tuu, nitaomba aniachie mie yule mtoto”
“Wewe mjinga si umeoa acha tamaa nitakusemea mie”
“Daah! Vunga jamaa yangu ila twende palepale walipo”
Wakati wakiinuka kuelekea alipo Tony, Mshehereshaji akashika kipaza sauti na kuomba wageni waalikwa wote wasogee katika viti vya mbele hili sherehe iweze kuanza. Darmy na Yassir wakafika alipo Tony wakatabasamu na kukaa, ikabidi utambulisho mfupi ufanyike hili kuwafanya wawe huru zaidi katika maongezi yao,
“Jamilah hawa ni rafiki zangu wa karibu sana, huyu ni Darmian na huyu ni Yassir,” akawageukia rafiki zake na kuendelea utambulisho.
“Oyah ni shemeji yenu”
“Eenh! Shemeji!” Yassir akajikuta akiuliza kwa mshangao zaidi.
“Kwani ujasikia au ndio mbwembwe,” akasema Darmy.
“Nafurahi kuwafahamu,” Jamilah akasema huku akiwapa mikono wale maswaiba wa Tony.
Sherehe ikaanza kwa watu mbalimbali kuongea na kuonesha wazi kufurahishwa na juhudi za kampuni hiyo katika kukuza utamaduni wa Nchi, ikafika zamu ya mgeni rasmi ambaye pia ni naibu waziri wa Utamaduni, Habari na Michezo. Waziri alifuraishwa sana na hatua ya kampuni ya Korea kuja kuwekeza nchini kwetu, na hii imesaidia sana kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wengi aidha Waziri alishukuru pia kwa kuutangaza utamaduni wa nchi yetu.
Ikafika hatua ya utoaji Tuzo kwa viongozi wa kampuni zote mbili, TAE XHIANG SUNG GROUP ikawa ya kwanza kuitwa kupokea Tuzo ya heshima. Taa zikazimwa na macho ya wote yakawa katika zulia jekundu ambapo kwa mwendo wa madaha kabisa mwanadada ambaye naweza kusema yeye ni zaidi ya mrembo akawa akitembea kueleka jukwaani, Darmy na Yassir wakashtuka mno wote kwa pamoja wakajikuta wakisema,
“Martha…!”
Jina lile lilivyopenya kwenye masikio ya Tony akajikuta akiangusha glasi aliyoishikiria mkononi mwake, taratibu akanyanyua shingo yake na kutazama kwenye zulia jekundu. Moyo ukamuenda mbio zaidi, Jamilah akabaki kuwashangaa asijue lolote, wakati akiendelea kushangaa Martha akawa ameshafika jukwaani na kupokea Tuzo ile. watu wakampongeza kwa makofi mengi kisha akasogea pembeni, Waziri akaendelea tena kwa kutoa tuzo kwa kampuni zalendo, jina la Tony likaitwa naye bila kuchelewa akamshika mkono Jamilah na kuongozana naye lakini kabla hajaenda Yassir akataka kumzuia kwa sababu aliona hatari ya kufanya vile. Waandishi wa habari walikuwa wengi eneo hilo hivyo kila tukio lilinaswa na kamera zao, Darmy na Yassir walifikiri itakuaje kwa Vanessa na Tedy ambao bila shaka watafatilia habari juu ya tukio hilo. Tony hakujali akaongozana na Jamilah, muonekano wao usiku huo ni kama maharusi, watu walishangilia mno, hali ilikuwa tofauti kwa Martha, alionesha wazi kuchukizwa na tukio hilo nafsi yake ilikaangika mno akapaona pale mbele pachungu. Wakafika jukwaani na Waziri mwenye zamana akatoa Tuzo ile.
Mshehereshaji akampa Martha kipaza sauti walau aongee machache, lakini hakuweza kusema kitu zaidi ya machozi kumtiririka, Tony alipoona vile akafurahi mno na kujisemea moyoni,
“Pole sana Martha, huu ni mwanzo tuu, picha kamili linakuja”
Mshehereshaji alivyoona Martha anashindwa kuongea akaamishia kipaza sauti kwa Tony, naye akakipokea na kuvuta pumzi ndefu kisha akasema,
“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mungu kwanza, ambaye naamini kwa nguvu zangu nisingeweza kuwa hivi nilivyo leo. Pia shukrani kwa rafiki zangu wa karibu sana, Darmy na Yassir, Shukrani pia kwa wafanyakazi na uongozi mzima wa TAE XHIANG SUNG GROUP na shukrani za kipekee kwa Martha”. CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipolitaja hilo jina kila mmoja akashangaa, watu wakawa kama wanaangalia picha la kihindi hasa baada ya Tony kugeuza shingo na kumtazama mrembo yule ambaye hatukujua kilio chake ni cha furaha au huzuni, japo alijitahidi kwa kiasi kikubwa kujenga tabasamu usoni mwake.
“Martha, nimejifunza mengi kupitia wewe, tamu na chungu vyote nimevijua asante sana,”
Akarudisha kipaza sauti na kumshika mkono Jamilah tayari kwa kuelekea kwenye nafasi yake.
Sherehe ikaisha na safari ya kurudi majumbani ikaanza Tony akaambata na marafiki zake pamoja na Jamilah, njia nzima kila mmoja akawa kimya hamna aliyejaribu kuuliza kitu. Tony alionekana mwenye mawazo mengi jambo lilimpa wakati mgumu Jamilah kuelewa nini kinazunguka vichwani mwao, wakafika Mapinga Darmy na Yassir wakashuka na Kuelekea makwao, Tony akageuka na kumtazama Jamilah,
“I want to spend this night with you, (nataka kuwa nawe usiku huu)”
“Its ok, am yours (sawa mimi ni wako tuu),” akajibu Jamilah huku akiupapasa mkono wa Tony kuashiria amekubali mualiko ule.
Safari ikaendelea na hatimaye wakafika nyumbani kwa Tony, Jamilah alishangazwa na ukubwa wa nyumba ile,
“Ina maana nyumba yote hii unaishi mwenyewe?”
“Ndio, naishi peke yangu”
“Mhmh! Umewezaje kuishi upweke kiasi hiki?”
“Aah! siwezi kuona upweke wakati wewe upo hapa”
“Wazazi au ndugu zako wako wapi?”
Jamilah akajikuta anauliza maswali mengi ambayo hayakuwa na umuhimu sana kwa wakati ule, Tony alivyoona Maswali yanazidi kuwa mengi akamsogelea Jamilah na kumshika kiuno kisha akamsogelea karibu zaidi na kumtazama usoni,
“Sasa nani…… anaye….ku…..pi….kia,” Jamilah akajikuta akihema kwa kasi mno na kushindwa kumalizia sentensi yake. Tony akamuangushia tabasamu zito na kumwambia,
“Acha nyoyo zetu zizungumze sasa, unachokihisi au ninachofikiri ni vigumu kukielewa, nataka usiku huu uwe wa kihistoria katika maisha yetu,”
“Tony nashindwa kujizuia kusema kuwa nakupenda sana, nifanye niwe wako siku zote”
“Shiiiii! Usiseme kitu”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tony alizidi kumkoleza mrembo yule kwa maneno yaliyopenya moja kwa moja mtimani, aliugundua udhaifu wa Jamilah mapema sana hivyo akakoleza chumvi na ndani ya muda mfupi mwanadada yule akawa anahisi kama yupo dunia nyingine.
“Samahani sana Jamilah,”
Tony akasema japo kwa hali aliyokuwa nayo Jamilah muda huo akuelewa kitu, Tony akatumia nafasi hiyo kutimiza matakwa ya mwili wake.
****************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment