Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

USALITI WA KIAPO - 4

 







    Simulizi : Usaliti Wa Kiapo

    Sehemu Ya Nne (4)



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Martha huyu bila shaka unamfahamu na huyu ni rafiki yangu pia anaitwa Darmian au Darmy kwa kifupi”

    “Sawa nafurahi kuwafahamu,” alisema Martha huku akiwapa mkono.

    “Sasa jamani mimi natoka ila narudi muda si mrefu,” alisema Yassir.

    “Wee unaenda wapi saa hizi, mida hii” Tony akasema.

    “Vunga kidogo, pigeni stori na mrembo huyo nakuja”.

    “Tony mimi ni shabiki yako sana, ukweli napenda jinsi unavyoimba natamani nami ningejua kuimba lakini ndio hivyo si kipaji changu,” alisema Martha huku akitabasamu.

    “Nashukuru sikuwahi kufikiria kama naweza kuwa na shabiki kama wewe,” Tony akajibu.

    “Daah! Usanii raha kweli ushanizidi kete jamaa” Darmy akasema, Tony akajikuta akicheka japo Martha hakuwa ameisikia vizuri kauli ya Darmy.

    Baada ya dakika 10 Yassir akawa amerudi akiongozana na msichana mwingine na mwenye mvuto wa kipekee.

    “Mhm! Huyu mjinga hawa warembo anawatolea wapi?” Darmy akamuuliza Tony kwa sauti ya chini.

    “Hata mimi sifahamu”

    “Jamani eenh! Huyu ndio shemeji yenu anaitwa Grace na nimefahamiana na Martha kupitia yeye sababu wao ni marafiki” Yassir akawatumbalisha.

    Baada ya hapo wakaagana na wale wasichana na kuingia kwenye Bajaji ambayo iliwapeleka moja kwa moja hadi mtaani kwao. Njiani mazungumzo yakaendelea,

    “Hivi wale wasichana umefahamiana nao vipi?” Darmy akauliza.

    “Wale wasichana nilikutana nao ukumbini, nilianza kumuona Grace ikabidi nianze kulia shida ila akawa anielewi, Mungu fundi Tony ukapanda jukwaani, kabla hujaanza kuimba ikabidi nianze kusema yale mashairi (yalinikuta kama yako rafiki, aliuteka moyo wangu nikajiweka usoni pake kabla ya macho yangu, akauktaili moyo huu na kuniacha kilema…). Taratibu nikaona mtoto aniangalia kisha akauliza, Unamaana gani? Mimi nikamjibu kuwa nampenda Zaidi ya neno kupenda. Nikaona anaanza kunielewa hivi, apo apo nawe ndio ukaanza kuimba tena maneno yale yale, nikajifanya kama kumpotezea akaanza kuniuliza, “kwani Tony unafahamiana naye?”, aah hapo ndio nikaona ngoja nimmalize kabisaa, nikamwambia mimi ndiye mwalimu wake yaani mashairi na nyimbo anazoimba mimi ndio nazitunga”.

    Kufika hapo wote wakajikuta wakiangua kicheko hadi dereva wa bajaji naye akacheka bado kidogo apoteze umakini na kuingia mtaroni.

    “Duuh sasa siku ukigundulika kama hujui kuimba wala kutunga hamna atakayekutetea!” Darmy akasema.

    “Mhm! Acha kunitia mkosi hadi aje kugundua itakua baadae sana labda muamue kuuza gazeti”.

    Muda wote Tony alikuwa anacheka tuu kwa ule mchezo ambao Yassir ameucheza hakika haukuwa wa kitoto.

    “Tony kuna mzigo wako Martha ameniambia nikupe”.



    Yassir akatoa kikadi kidogo chenye mawasiliano na kumkabidhi Tony. Wakati huo wakawa washafika mtaani kwao, wakamlipa dereva wa bajaji na kila mmoja akashika njia yake.

    Tony anaishi na dada ake wa pekee ambao kiukweli ndugu hao wanapendana sana, wanashauriana na kusaidiana kwa kila hali, Wazazi wao walifariki miaka kadhaa iliyopita. Maisha yao yalikuwa yakawaida, hayakuwa ya juu sana wala ya chini sana, Biashara ndogo ndogo zilizoachwa na wazazi wao ziliwasaidia katika kupata ridhiki ya kila siku.

    “Hongera mdogo wangu, japo sikuwa ukumbini ila nilikuwa nakufatilia kwenye luninga, ukweli najivunia kuwa na ndugu kama wewe”

    “Hongera nawe dada, kwani bila msaada na ushauri wako nisingalifika hapa nilipo sasa”

    “Nakupenda sana mdogo wangu”

    “Nakupenda pia dada”. Yalikuwa maongezi mafupi kati ya Tony na dada yake kabla ya kuingia chumbani kwake na kulala.



    ************************



    Siku zikazidi kusonga hatimaye mchujo ukapita na Tony akafanikiwa kuingia fainali ambapo washiriki watano watashindana kumpata mshindi mmoja. Tarehe ikatangazwa na wasanii maarufu ndani na nje ya nchi wakaalikwa kushuhudia ni nani atakayeibuka kuwa mwenye kipaji Zaidi ya wengine. Kila mshiriki akawa anajiandaa kwa anavyoweza kuhakikisha anaibuka mshindi, Kwa upande wa Tony hakuwa na wasiwasi kwani alijua wazi hakuna anayeweza kumshinda.

    “Wewe ndiye jaji mkuu, hakikisha Tony hapati ushindi badala yake mtangazeni Daniel kuwa mshindi wa huo mchuano”.

    “Ilo haliwezekani, watanzania wanamkubali sana Tony na hata ukiangalia Daniel uwezo wake ni mdogo ukilinganisha na Tony” CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sawa nitajua mimi cha kufanya, Daniel lazima awe mshindi”.

    Yalikuwa maongezi kati ya jaji mkuu na mzee mmoja mwenye uwezo wa kipesa, anaushawishi mkubwa katika vyombo vya habari na mitandao kutokana na pesa alizonazo lolote atakalotaka liwe linakuwa. Na uamini kuwa palipo na pesa hamna litakaloshindikana, jina lake maarufu ni Pedeshee Mkwanja.

    “Unafikiria kufanya nini?” jaji akauliza

    “Daniel ananifaa sana katika shughuli zangu na nimemuahidi ushindi kama zawadi yangu ya kwanza katika kukubali kuungana nami”.

    Mzee akaingia mfukoni na kutoa kibunda cha pesa na kumkabidhi jaji, kisha akatazama huku na huko na kumwambia,

    “Hii ni zawadi yako, hakikisha ufungui kinywa chako na kumwambia yeyote juu ya haya tuliyoyaongea”

    “Sawa kuwa na Amani”

    Pesa inashawishi sana,jaji yule hakuweza kuikataa, akapokea kitita kile cha pesa na kukisunda mfukoni tayari kwa kumnyima haki Tony.



    ***********************



    Kadri siku ya fainali ilivyokuwa inakaribia ndivyo umaarufu wa Tony ulizidi kuongezeka katika vyombo mbali mbali vya habari na hata katika mitandao ya kijamii, wengi walikua na uhakika kuwa kijana huyo ndiye anafaa kutwaa taji la “Tanzania Got Talent”.

    “Tony hivi karibuni vyombo vya habari, mitandao ya kijamii havitakuwa na la kuandika juu yako badala yake mimi nitatawala,” alisema Daniel baada ya kuona taarifa za Tony.



    Hakuna aliyejua mipango ya siri inayofanyika kumuangusha Tony, kila mmoja akawa anaisubiri siku ya fainali kwa hamu zote. Baada ya mazoezi mazito Tony akakaa na rafiki zake wakipeana ushauri juu ya iyo siku ya fainali,

    “Usiwaze sana ndugu yangu, huna mpinzani kaka” Darmy akaongea na Yassir akadakia

    “Daah! Mimi hapa nafikiria nitokeje siku hiyo, alafu ukipewa tuzo lazima nije na mimi walau niuze jukwaani”

    “Wewe unataka kuuza si kwa sababu ya Grace!”

    “Aah! Umejuaje asee, yaani siku hiyo acha, kwanza swaga zinaongezeka yaani mtoto akinicheki aone kama majaji wamekosea kutoa tuzo”

    “Unamaana gani?” Darmy akauliza

    “Mimi ndiye ningepewa badala ya Tony”.

    Muda wote huo Tony hakuongea neno akabaki kuwasikiliza na kufurahi,

    “Ukweli najisikia furaha sana kuwa na marafiki ambao ni kama ndugu kwangu, ninyi mmekuwa sehemu ya muhimu sana katika maisha yangu, sitowasahau kamwe”.

    “Aah! Kawaida tuu usijali, tupo pamoja katika kila hali”.

    “Asanteni sana”.

    “Tony eenh! Baadae hivi kuna sehemu nataka unisindikize,” Yassir akasema.

    “Wapi tena..?”

    “Wee kubali kwanza kisha nitakwambia tutakapoelekea”.

    “Sawa tutaenda”.

    “Nawe Darmy vipi?”

    “Aah! Mimi siendi popote leo!”

    “Acha hizo bhana, twenzetu sio ishu kila siku kukaa kitaa”

    “Poa tutaenda,” Darmy akajibu.

    “Tukajiandae basi saa moja jioni tunaenda,” alisema Yassir.

    “Sawa, ila hujasema tunaenda wapi?”

    “Mtajua huko huko”

    “Mhmh haya bhana”.



    *********************



    Muda waliopanga kukutana kwa ajili ya safari ukawadia, kama ilivyokuwa kawaida usafiri wao mkubwa ni bajaji hivyo wakamuita dereva wao wasikuzote, bila kupoteza muda akaja na kuianza safari.

    “Oya suka ongeza mwendo tumechelewa sana,” alisema Yassir.

    “Sawa bosi usijali! Si umesema ni tabata Chang’ombe?”

    “Yeah pale Chikoho hotel”

    “Poa dakika chache tutakuwa tumefika!”

    “Fanya kweli suka”.

    Tony na Darmy hawakujua wanapoelekea hadi waliposikia toka kwa dereva, wakamgeukia Yassir na kumuuliza,

     “Mhmh! Wewe jamaa Chikoho hotel tunaenda akufanya nini?”

     Kabla hajawajibu, simu ya Yassir ikaita na kwa haraka Zaidi akaipokea,







    “Nipe dakika chache tuu tutakuwa hapo, tumekaribia,” alisema Yassir na akakata simu.

    Baada ya dakika mbili wakafika, wakashuka na kuingia hotelini. Wakapanda hadi ghorofa ya 7, walipofika tuu watu wote wakasimama na kushangilia hasa baada ya kumuona Tony. Grace akasogea na kumkumbatia Yassir,

    “Sikuamini kama kweli ungekuja kwenye sherehe hii ya siku yangu ya kuzaliwa”

    “Hamna lishindikanalo katika nguvu ya mapenzi” Yassir akajibu.

    Tony na Darmy wakabaki wameduwaa wasijue nini kinachoendelea.

    “Twende ukawasalimie rafiki zangu,” alisema Yassir.

    “Sawa” Grace akajibu.



    Grace akasogea walipo Tony na Darmy akawasalimu na kuwakaribisha katika sherehe iyo. Baada ya Muda mfupi sherehe ikaanza.

    “Mabibi na mabwana napenda kumkaribisha bwana Yassir atufungulie sherehe hii kwa maneno machache”

    Mc akamkabizi Yassir kipaza sauti na kila mmoja akawa na shauku la kutaka kujua nini atakachokisema kama ufunguzi wa sherehe ile.

    “Nimepata sapoti yako dunia imenivuta, kuanza mahusiano nawe kila mara najihisi mpya, wewe ni kila kitu kwangu, wewe pekee ndiye unipaye Amani ya moyo na niwewe pekee moyo wangu umeamua kukupenda. Nakupenda sana Grace, Happy birthday.” 

    Watu wote wakajikuta wakishangilia kwa makofi na vigelegele, hamna aliyetegemea kama Yassir anaweza kuwa na ujasiri wa kuelezea hisia zake wazi wazi vile.

    “Nakupenda pia Yassir,” Grace akajibu.

     Baada la jibu ilo furaha na shangwe viliongezeka maradufu sehemu ile, watu walikunywa na kula wapendacho.

    “Mashairi yako mwenzio kayafanyia mazuri, kiulaini kaopoa mrembo” Darmy akamnong’oneza Tony wote kwa pamoja wakajikuta wakicheka.

    “Mambo zenu”

    Ilikuwa sauti tamu ambayo kwa hakika kuisikia tuu huishiwi hamu, sauti hiyo iliwafanya Darmy na Tony kuacha kucheka na kutazama ni nani hasa mmiliki wa ile sauti, walipotaza kila mmoja akajikuta akiduwaa,

    “Safi tuu” Darmy akajibu.

    “Mboni mnanishangaa?”

    “Aah! Hivi wewe ni Martha”. CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yeah ni mimi nilifahamiana nanyi usiku ule mashindano” Martha akajibu na kukaa katika kiti kilichopo karibu na Tony.

    “Nafurahi kuonana nanyi tena”,

    “Nasi pia tumefurahi” Darmy akajibu.

    Muda wote huo Tony kama kawaida yake hakuongea kitu Zaidi ya kutabasamu na kusapoti maongezi kwa ishara. Tony hakuwa na maneno mengi alipenda kukaa kimya muda mwingi na kutafakari sana kabla hajaongea au kufanya lolote.



    Muda wa kucheza muziki ukafika, watu wakanyanyuka katika viti na kuanza kusakata rumba kwa kila mitindo iliyowajia vichwani mwao. Utundu wa Dj ukamshawishi Darmy kuinuka na kwenda mbele kuonesha uwezo wake wa kudansi.

    “Mmhmh! Vipi nawe si mpenzi wa kucheza kama mimi?” Tony akamuuliza.

    “Kama ukikubali kucheza nami basi sitokuwa na kipingamizi,” alisema Martha.

    “Hapana mimi sijisikii kucheza muziki leo,” alijibu Tony.

    “Nami pia sijisikii”

    “Mhmh! Ayah!” alisema Tony.

    “Hivi Tony rafiki yako hakukupa kadi yenye mawasiliano yangu”

    “Ndiyo Alinipa!”

    “Sasa kwanini hujawahi kunitafuta?”

    “Sikuwa na sababu ya kukutafuta ndio maana sikukutafuta”.

    Majibu ya Tony yakawa yanamnyima raha Martha ambaye siku nyingi alivutiwa na kijana huyo alijenga Imani kuwa iposiku atakuwa naye. Ndoto zake zikawa kama zinakaribia kutimia hasa baada ya kukutana na Tony,

    “Tony mbona unachokiandika na kukiimba ni tofauti na unachokiishi?”

    “Kivipi?”

    “Tony ushawahi kupenda?”

    “Ndiyo nilipenda, ninapenda na nitaendelea kupenda”.

    Martha akashtuka kidogo kusikia jibu la Tony, hofu ya kukosa nafasi kwa mwanaume huyo ikamjia, lakini akajipa moyo na kuendelea na mazungumzo.

    “Ulijisikiaje pale unapoitaji kitu toka kwa yule umpendaye na akashindwa kukupa?”

    “Uwa sihitaji kitu kilicho nje ya uwezo wa wale niwapendao, ninachohitaji huwa nakipata kwa hiyo siwezi kujua jibu la swali lako”

    “Kwani Tony kwa kuangalia bado ujajua au kuelewa nini nahitaji toka kwako?”

    “Martha si kila kionekanacho uhakisi uhalisia, hivyo sio rahisi mimi kukigundua mpaka utakapo nitamkia kwa kinywa chako”

    “Tony kiukweli mimi…”

    “Wewe nini?”

    “Tony….:”



    Martha akajikuta anashindwa kumalizia sentensi yake baada ya kumtazama Tony ambaye hakuonesha ushirikiano kwa kile alichokisema. Akanyanyuka na kwenda mbele walipo watu, akaomba kipaza sauti na kupewa. Kisha akaomba watu wote wamsikilize na wote wakaacha kucheza hili kumpa nafasi Martha azungumze kile alichodhamiria.

    “Embu niambie kwa nini moyo wangu umevurugika, kila ninapokuona nahisi kama tumefahamiana kwa miaka mingi, unaonekana huna uzoefu wa mambo yahusuyo moyo, kile ninachofikiri ni ngumu kukwambia”.

    Martha aliduwaza wengi alipoanza kuimba nyimbo hiyo ambayo iliimbwa na Tony kwenye mchujo wa ishirini bora, wote wakamgeukia Tony wakitaka aungane na Martha katika kuimba ile nyimbo. Tony akawa anasita kwenda kuimba sababu tayari alishajua nini mwanadada yule anahitaji hivyo kwa kutumia nyimbo akawa akifikisha ujumbe, alisita lakini mwishoe akapewa kipaza sauti akaungana nae kushusha mashairi, hakika waswili hao waliifanya siku ile kufana sana, kila mmoja aliburudika na kuridhika. Sherehe iliisha saa 6.47 usiku na kila mmoja kurejea nyumbani kwake.

    “Tony eenh! Ukweli Martha amekuelewa sana fanya mazuri kaka” Yassir akafungua mjadala baada ya kimya kirefu kupita ndani ya bajaji waliyoikodi iwarudishe nyumbani.

    “mhm! Achana na habari hizo!” Tony akajibu.

    “Ila huku kuna jambo testa (wasichana warembo) yaani hata kama ningeambiwa nichague sijui ningemchagua nani!” Darmy akaongea.

    “ila Tony ungegoma kuimba muda ule ungeniua chalii yako, pale nilivyokua mbele nilikuwa najipamba mno, nimekuleta ufanye shoo, basi ndio mtoto kazidi kunielewa na ile mistari yako daah noma saana!”

    Wote wakacheka sababu siku zote Yassir ni mtu wa vituko na huwa anaunganisha matukio na kujitengenezea stori yake itakayomnufahisha.



    ************



    Saa 48 zikawa zimesalia kabla ya fainali kufanyika, Tony akawa anatoka mazoezini na siku iyo hakuongozana na rafiki zake. Akawa akitembea taratibu huku akiimba, mara ghafla kundi la watu 6 walioshiba vizuri wakamzunguka. Tony akasimama na kuwatazama, Jamaa mmoja mrefu mnene mwenye sura ya kutisha akamwambia Tony,

    “Kama unahitaji maisha yako basi achana na mashindano, usiwepo siku ya fainali”,

    “Siwezi kuacha mashindano katika hatua hii, tafadhali niacheni niende,” alisema Tony.

    Yule jamaa akafura kwa hasira akampiga Tony kibao kilichompeleka moja kwa moja chini.

    “Kwani ninyi ni akina nani na mnahitaji nini toka kwangu?”

    Hakupewa jibu Zaidi ya kipigo katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

    “Mchukueni mpelekeni sehemu yetu”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Bila huruma Tony akabebwa na kuingizwa kwenye gari, wakamfunga macho asione wanapoelekea. Gari lilitembea kwa haraka na baada ya nusu saa likafika sehemu na kusimama, Tony akatolewa na kuingizwa kwenye chumba ambacho kina vumbi na harufu kali mno, apo apo mafua yakamshika vumbi likampalia akajikuta akihema kwa shida huku akikohoa mfululizo.

    “Kwani nimefanya dhambi gani hadi kunihukumu hivi?” Tony akauliza.



    Hamna aliyemjibu wakamfungia humo na kuondoka, hewa ikawa nzito sana akajikuta anashindwa kuhema. Tony alipata shida sana, akajitahidi kupaza sauti yake walau apate msaada wa kutoka humo lakini hamna aliyemsikia, akajitahidi kutoka alipokuwa hakuweza kamba zilizokuwa mikononi na miguuni mwake zilimzuia kufanya hivyo. Hali yake ikazidi kuwa mbaya, akahisi kichwa kinamuuma sana, macho yakawa mazito akaanza kuona giza na taaritibu akajikuta ameanguka sakafuni, haikupita muda wale waliomteka wakafungua mlango, walipoona amepoteza fahamu wakachukua maji na kummwagia,

    “kazi yetu imakamilika tumuachie aende zake sasa,” waliambiana wale watekaji.







    Papo hapo Tony akazinduka toka kwenye usingizi mzito, akashangaa kumuona dada yake akilia na maswahiba wake wakiwa pembeni.

    “Umekutwa na nini Mdogo wangu, toka usiku wa jana hadi sasa ni saa 11 jioni ndio unaamka”

    Tony akashangaa sana, akataka kusema jambo lakini sauti haikutoka ghafla akaanza kupiga chafya na kukohoa mfululizo, homa ikapanda na akawa na joto kali mwilini.

    “Hali yake imerudi kama mwanzo sasa tumpeleke hospitali,” alisema Darmy.

    Tony hakuamini kuwa yale yote yaliyomtokea ilikuwa ni ndoto ingawa ndoto ile iliambatana na ukweli. Sauti yake ikakata akawa anaongea kwa shida sana, mafua na kifua hamna tofauti na ilivyokuwa katika ndotoni.

    “Daktari vipi hali ya mgonjwa wetu?” Dada yake Tony akamuuliza pindi daktari alivyomaliza kumfanyia vipimo mdogo wake.

    “Unahusiana vipi na mgonjwa?”

    “Ni mdogo wangu wa damu”

    “sawa twende ofisini”.

    Daktari akaongozana na Dada yake Tony hadi ofisini, akachukua faili na kuandika vitu flani kisha akamtazama na kumwambia,

    “Hali aliyonayo mdogo wako imenishangaza sana, nikawaita madaktari wenzangu lakini wote tukabaki na mshangao, kwani mgonjwa ameanza kuumwa lini?”

    “Daktari hadi jana, mdogo wangu alikuwa mzima wa afya, lakini alishikwa na usingizi mzito mno ambao kila nilivyojaribu kumuamsha hakuamka, nikaona tuu anachemka ikabidi niwe namkanda kwa maji ya baridi hadi alipoamka na kuona hali imezidi kuwa mbaya ndio tukafikia uamuzi wa kumleta hapa”.

    Daktari akashusha pumzi ndefu kisha akawa kama anafikiri kitu ambacho hakupata jibu lake,

    “Mbona waniacha njia panda dokta, vipi hali ya mdogo wangu?”

    Daktari akamuangalia dada yake Tony kisha akamwambia

    “hivi umesema unaitwa nani?”

    “Naitwa Rozina”

    “sasa Rozina kiukweli, tumempima mdogo wako kila ugonjwa lakini anaonekana hana tatizo lolote yuko salama tuu”

    “dokta unawezaje kusema yu salama akiwa katika hali hiyo”.

    “Nimekua daktari kwa Zaidi ya miaka 17 sasa mdogo wako yupo salama na sioni sababu ya kuendelea kumuweka hapa, hivyo ni vyema ukarudi nae nyumbani na nitamwandikia dawa za kutuliza homa na kukata hayo mafua. Kadri ya muda utakavyozidi kwenda atakuwa mzima tu, wala usiwe na wasiwasi,” alisema daktari.



    *****************



    Taarifa za kuugua kwa Tony zilienea haraka mno, nchi zima ikapoa kila mmoja akawa anaongea lake kuhusu ugonjwa wa Tony, Magazeti yakabeba vichwa vya kila aina baadhi yalipambwa kwa maandishi makubwa “Ushirikina wamuondoa Tony mashindanoni” mengine “Hatimaye wafanikiwa kumzuia Tony”, hamna aliyejua sababu halisi ya ugonjwa wa Tony, kadri ya muda ulivyozidi kwenda ndivyo hali yake ikazidi kuwa mbaya.

    “Dada embu tuhangaike hata kwenye mambo ya jadi hali hii si ya kawaida” akasema mmoja wa majirani zake.

    “Namtumaini mungu aliyetuumba haina haja ya kuangaika uko mdogo wangu atakuwa sawa tuu”.

    Watu wengi wakajitokeza kumuona Tony kila mmoja alikuwa na oni lake wapo waliosema wamuombee kwa mungu na wapo walioshauri waende kupiga ramli uenda akawa amelogwa lakini misingi ya kidini, iliyojengwa kwa wanandugu hawa toka wakiwa wadogo ilikuwa ni migumu mno, hivyo haikuwa rahisi kwa dada mtu kushawishika kumpeleka mdogo wake katika tiba za asili.



    *****************************



    Majaji na washiriki wengine wakaenda kumjulia hali, wote waliofika walishindwa kuzuia machozi yasiwatoke maana katika masaa machache tuu, afya ya Tony ilidhoofika kama mgonjwa aliyeumwa kwa muda mrefu.

    “Haina budi tukate jina la Tony kwenye mashindano sina uhakika kwa hali hii kama ataweza kushiriki”.

    “Haina haja ya kulifuta jina lake, Tony kesho atakuwepo kwenye fainali”

    Watu wote wakashtuka sana waliposikia kauli ile walipogeuka kutazama, akawa ni mwanadada yule yule mrembo kweli kweli Martha.

    “Liache tuu hadi mwenyewe atakaposema lifutwe”.

    Jaji akakubali kisha wakaaga na kuondoka pamoja na washiriki wengine.

    “Halo jaji! Pedeshee Mkwanja naongea hapa, bila shaka kazi yangu umeiona hivyo hamna kipingamizi tena kwa Daniel kuwa mshindi wa shindano hilo”

    “Nimeiona ila umemfanyaje mtoto wa watu?” jaji akauliza.

    “Hahahahaha! Itakuwa vyema kama utafatilia mambo yako na kusahau yale yasio kuhusu,” alisema Pedeshee Mkwanja na akakata simu.

    Martha akajitahidi kufanya kila awezalo kuhakikisha Tony anarudi katika hali yake ya kawaida. Akachukua majukumu yote katika kumhudumia mgonjwa,

    “Tony leo ni siku ya fainali, sisi sote tunatamani uinuke na kwenda kuimba” Martha akamwambia Tony ambaye hakuwa na sauti ya kuongea, ukweli aliumia sana na hali ile aliyekuwa nayo.

    “Kunywa haya maji ya tangawizi nina Imani yatafungua koo lako”

    Wakati anakunywa maji yale yatangawizi tayari Yassir akawa ashachanganya asali na mdalasini ambayo husaidia kukata mafua. Baada ya kunywa izo dawa ghafla mwili wake ukaanza kuchemka na akawa anaunguza mno, kichwa kikamuuma sana, akawa akilalamika

    “Dada sizani kama nitapona, nahisi mwisho wangu umefika,” aliongea Tony kwa shida mno.

    Dada aliposikia hayo presha ikapanda naye akajikuta akianguka na kupoteza fahamu. Wakamfanyia huduma ya kwanza, na kumtenga kidogo na mdogo wake. Martha akajitahid kila awezalo kuhakikisha Tony anakuwa sawa. Baada ya muda mfupi dada akawa amezinduka na jambo la kwanza lilikuwa kumuulizia Tony wake, wakamsihi aendelee kupumzika kwani hali ya Tony ilikua inaleta matumaini. CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ***************************



    Hayawi hayawi sasa yamekuwa katika ukumbi wenye wa Diamond Jubilee, ukumbi ambao ulijaa umaarufu mkubwa Sana jijini Dar es Salaam. Watu walijaa kusubiri ni nani atakayeibuka mshindi katika shindano la TGT. Muda ukafika hatimaye washiriki wakaanza kupanda na kuonesha utaalamu wao wa kuimba, hakika upinzani ulikuwa mkali mno, haikuwa rahisi kwa mtu wa kawaida kujua nani atakayeibuka mshindi siku iyo. Washiriki wanne wakamaliza mzunguko wao wa kwanza jukwaani, sasa ikawa ni zamu ya mshiriki wa tano ambaye ni Tony, Mc alipotaja jina la Tony kila mmoja akawa na shauku kubwa maana wote waliamini kuwa Tony ndiye anayestahili kuwa mshindi, katika hali yake ya kuugua akajikongoja hadi jukwaani na akakabidhiwa kipaza sauti. Kabla hajaongea lolote mashabiki wakaanza kushangilia kwa nguvu mno, wapo walio lia kwa furaha,wapo waliotabasamu na wapo waliochukia kumuona jukwaani. Akanyoosha mkono juu kuwaomba watu wanyamaze na wote wakatii, kila alivyojaribu kuongea sauti ikagoma kutoka,akajitahidi tena na tena lakini hakuweza kutoa sauti, katika jitihada zake akajikuta anawaliza mashabiki waliokuja kushuhudia fainali ile, kwani akuweza kuongea lolote watu wote wakainamisha vichwa chini si walio ukumbini wala wale wanaofatilia kupitia luninga, wote walipoa. Tony akarudisha kipaza sauti na kushuka jukwaani, Mc akajitahidi kuwarudisha watu katika hali ya kawaida na mambo mengine yakaendelea. Fainali ilimalizika kwa Daniel kutangazwa kuwa mshindi, japo wengi hawakurizika na ushindi aliopewa Dany kwani hakuwa na uwezo mkubwa sana kuwashinda vijana wengine.

    “Hongera sana kijana, nimekupa ulichohitaji sasa ni zamu yako kulipa fadhila” akaongea Mzee Mkwanja baada ya Daniel kupokea tuzo ile.

    “Nipo tayari kufanya lolote mzee wangu”

    “Hahahaha! Safi sana kijana, nimependa ujasiri wako na utanifaa sana, kapumzike baada ya wiki moja kazi itaanza”. Baada ya maongezi hayo mafupi wakaagana na kila mmoja akashika njia yake.



    **********************



    “Martha umekuwa mtu wa muhimu sana katika maisha yangu, sikutegemea kama utakuwa upande wangu hasa katika kipindi hiki cha ugumu, sina cha kukulipa”

    “Shii! Usiseme kitu Tony, una utajiri mkubwa mno, ivyo ukisema huna cha kunilipa unakosea”

    “Unamaanisha nini?”

    “Mhmh! Sio kitu!”

    “Martha”

    “Tony”





    Kadri siku zilivyokuwa zikienda ndivyo Martha na Tony walijikuta wakizama katika bahari ya huba, wasitamani kuokolewa, Mapenzi yao yaliota mizizi, shina hatimaye matawi yaliyovutia wengi. Afya ya Tony ilirejea katika hali ya kawaida hivyo akawa anaendelea na shughuli zake za kila siku. Hakuna aliyesahau kipaji chake cha kuimba lakini kila alivyojaribu kutafuta nafasi mambo yalikuwa magumu upande wake, wengi walimkejeli na kumkatisha tamaa, haina maana kuwa hawezi ila wengi waliogopa kupoteza nafasi zao endapo wangeruhusu. Martha akawa mstari wa mbele kuhakikisha anakitendea haki kipaji hiko akawa na ushawishi mkubwa hadi Tony akafanikiwa kuingia studio na kurekodi nyimbo.



    *******************************



    Siku moja Tony aliamua kumtembelea mjomba wake anayeishi Tukuyu, mkoani Mbeya.Akaambatana na kipenzi cha moyo wake katika safari hiyo, Safari ilikuwa ndefu kidogo kutokana na gari waliyopanda kutoweza kwenda kwa kasi kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha siku hiyo. Toka saa 12.00 asubuhi walijikuta wakifika uyole saa 3 usiku na hapo bado safari ya kwenda Tukuyu. Wakaamua washuke Uyole na kuingia katika moja ya nyumba za wageni zilizopo eneo hilo.



    “Bora tupumzike maana na baridi hili kwenda huko tunaweza kujikuta tunafika saa 5,” alisema Tony na Martha akaridhia.

    Baada ya kulipia wakakabidhiwa funguo na kuoneshwa chumba chao, Tony na Martha wakaingia huku kila mmoja akionesha kumfurahia mwenzie,

    “Baridi hili leo si nitaganda mie,” alisema Martha.

    “Uwezi kuganda wakati mumeo niko hapa,” Tony akajibu.

    “Hahahaha! Haya kwa hiyo tutakula nini usiku huu”

    “Sema wewe”

    “Mimi nataka chipsi na mishikaki ila iwe ya moto”

    “Basi hata mimi nitakula iko”

    Tony akatoka na kumuacha Martha ambaye aliamua kuingia bafuni kuoga hili kupunguza uchovu wa safari. Baada ya nusu saa Tony akarejea, kisha kwa pamoja wakashariki kula chakula kile. Baada ya hapo Tony akaingia bafuni kisha usingizi ukawanyemelea na wote wakalala.



    *************

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni siku nyingine Tena, baada ya kuamka Salama na kujiandaa, wakasogea hadi kituo cha mabasi na Wakachukua usafiri ambao uliwapeleka moja kwa moja hadi Tukuyu. Walitumia saa 2.30 hadi kufika kwa mjomba wake na Tony. Wakamkuta mjomba akiwa amekaa chini ya mti wa maembe, mjomba alipomuona Tony alifurahi sana akainuka na kumkumbatia

    “Karibu sana uncle!”

    “Asante sana Uncle!”

    “Naona umeniletea mwali leo”

    “Hahaha! Uncle ujaacha tuu”

    “Ila mjomba umechagua mwali amenoga huyu”

    “Mhmh! Uncle hata kukutambulisha sijakutambulisha!”

    “Hahaha! Haya karibuni sana”



    Baada ya kusalimiana, Mjomba akawakaribisha kwenye mkeka ulipo chini ya mti huo nao wakakaa, Mjomba akawa na shauku sana la kutambulishwa ugeni ule,

    “Uncle! Huyu ni rafiki yangu anaitwa Martha na Martha huyu ndiye mjomba wangu aliyebaki”

    “Nafurahi kumfahamu” Martha akajibu kwa kutabasamu.

    “ila Tony mboni kama sielewi elewi hivi!?”

    “Uelewi nini uncle?”

    “Urafiki gani kati ya mwanaume na mwanamke au ndio mkwe huyu? Maana nyie vijana wa siku hizi mhm”,

    Tony akajikuta akicheka mno, ukweli mjomba yake alikuwa ni mtu mcheshi na mwenye vituko mno.

    “Aaah! Uncle bhana huyu rafiki tuu,” alisema Tony.

    “Mhmh! Huo urafiki wa kulala pamoja wa wapi tena mwanamke na mwanaume,” alisema Mjomba.

    Wote wakajikuta wakiangua kicheko, ukweli mjomba alifurahi sana kupokea ugeni huo.

    “Uncle! Shangazi yuko wapi?”

    “Yupo shamba ila hatochelewa kurudi”

    “Aah! Basi ngoja nimfate huko huko shamba”

    “Mhmh! Hata kupumzika kidogo uncle”

    “Nimepapeza mno, acha nikaangalie mazingira”

    “Sawa uncle ila huyu mwali uniachie hapa”

    “Hahahaha! Uncle bhana! Huyu yupo”.



    Safari ya kwenda shamba ikaanza huku kila mmoja akifurahishwa na mazingira ya njiani, wakatembea huku wakishangaa huku na huko hatimaye wakatokea kwenye mto.Walipofika hapo Tony akamwambia Martha wapumzike kidogo kisha wataendelea na safari,

    “Mhmh kwani bado mbali sana?” Martha akauliza.

    “Hapana si mbali, tukuvuka huu mto tunapandisha kidogo kisha tunakunja kulia na hapo tutakuwa tumefika”.

    “Basi twende kwanza alafu tutakuja kukaa hapa wakati wa kurudi”.



    Tony akakubaliana na wazo la Martha kisha safari ikaendelea, baada ya dakika kadhaa wakafika shambani, wakaangaza huku na kule lakini hawakumuona shangazi.Wakaingia hadi katikati ya shamba wakamkuta shangazi akichimba mihogo, shangazi aliposikia hatua za watu akageuka na kutazama, hakuamini macho yake kumuona Tony eneo lile.Shangazi akaweka panga chini na kuinuka Tony akamsogelea na kumkumbatia,

    “Khaaa! Tony mwanangu umekua hivi”

    “Shikamoo shangazi”

    “Marhaba mwanangu za siku”

    Kabla Tony hajajibu Shangazi akamtazama Martha na akazidi kutabasamu,

    “Naona umeniletea mwali hadi huku, hakika mungu awabariki na nimefurahi sana leo,” alisema Shangazi.



    Martha akasogea na kumsalimu shangazi kisha wakakaa na kuongea mambo kadhaa, Martha akavutiwa mno na mazingira ya shamba hilo akauliza na kuelezwa mengi na shangazi yake Tony.

    “Shangazi hapa tutanogewa na kazi zitalala, acha nikusaidie mizigo na tutakutana nyumbani,” alisema Tony baada ya kuona muda unaenda na mazungumzo hayaishi.

    Shangazi akacheka mno, hakuamini kama vijana hao wa mjini wanaweza kubeba mizigo ile na kufika nayo nyumbani.

    “Ninyi vijana wa mjini na mizigo ya shamba wapi na wapi?, acha tuu nitaibeba mwenyewe,” alisema Shangazi.

    “Aah! Anti usijali tutaibeba mimi na Tony”



    Martha akamtoa shaka shangazi yake Tony na bila kupoteza muda wakabeba ile mizigo na safari ya kurudi nyumbani ikaanza. Walipofika mtoni ikawalazimu kutua mizigo yao na kukaa kando ya mto. Kabla hawajaongea chochote ghafla kukatokea upepo mkali, uliotingisha na kuangusha baadhi ya miti iliyo eneo hilo. Tony na Martha wakaogopa mno wakatamani kukimbia lakini upepo ulikuwa mkali ivyo haikuwa rahisi kwa wao kukimbia, ikabidi wakumbatiane kwa nguvu, huku kila mmoja akiwa amefumba macho asitake kuona lolote likiwadhuru.Baada ya muda mfupi hali ile ikatulia na kukawa shwari kabisa, Tony akafungua macho na kumuona Martha akiwa bado katika hali ya woga.

    “Nyanyuka twende”

    “Hapana siwezi kwenda naogopa mno”

    Tony ikabidi acheke na cheko lake likamfanya Martha afungue macho nae hakuamini kama hali ile imepita. Wakachukua mizigo yao na taratibu wakaendelea na safari,

    “Mhm! Hivi Martha ulitaka kuniambia nini?”

    “Aah! Yaani ule upepo umenishtua mno hata nililotaka kuongea silikumbuki”



    Wakawa wanaongea huku wanatembea, wakafika sehemu moja hivi, wakamkuta mzee ambaye hawakumtambua akiwa chini asiweze kutembea. Tony alipomuona akashusha mzigo na kumwambia Martha wamsaidie mzee yule ambaye hawakuwa wanafahamu hata anapoishi ila waliamini lazima atakuwa mmoja wa wanakijiji ambacho mjomba wake anaishi. Wakamsogelea na walipomchunguza wakagundua mzee ameteguka mguu, wakasaidiana kumwinua na kumuweka sehemu nzuri, baada ya muda mfupi mzee akaanza kukohoa mfululizo, ikabidi Tony amwache Martha na kukimbia hadi mtoni ambapo alikata jani la mgomba na kulitumia kuchota maji. Kisha akarudi kwa haraka kumpatia mzee yule, taratibu akanywa maji yale kisha akafungua macho na kuwatazama wawili wale,

    “Wajisikiaje sasa?” Martha akamuuliza,

    “Najihisi vyema tofauti na awali, shukrani kwenu,” alijibu mzee yule.

    “Usijali mzee wangu, kwasasa tuambie kwako ni wapi tukusindikize,” Tony akaongea.





    Mzee akatabasamu kisha akawatazama usoni Tony na Martha kwa makini sana, akakohoa kidogo na kuzungumza,

    “Samahani kwa kuwachelewesha safari yenu, msiwe na shaka, na kwa ninavyojisikia sasa naweza kufika kwangu bila wasiwasi”

    “Mhm! Babu bado hauko sawa tunaomba tukusindikize”.

    Babu akatazama angani kisha akawatazama tena akawa kama anafikiri kitu, kisha akawatazama tena na kuwaambia,

    “Muda umeenda sana, kwenu watakuwa na wasiwasi na washaanza kuwatafuta, nendeni haraka ila jambo moja zingatieni maisha yenu yatajawa na furaha endapo wawili ninyi mtakuwa pamoja”.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tony na Martha wakajikuta wakitamani kuuliza mengi kwa mzee yule lakini hakuwapa nafasi ya kuuliza, akawaonesha njia ya kuifata. Wakajitwika mizigo yao na kuanza kufata njia ile, hawakusemeshana hadi walipotoka kabisa msituni na kuingia katika makazi ya watu, wakatembea kidogo na wakakutana na wanakijiji walioambatana na mjomba wake Tony, mjomba alipowaona akafurahi na akawasogelea;

    “Mmetupa wasi wasi sana mlikuwa wapi hadi usiku huu?”

    Tony na Martha akili zao zikafunguka na kugundua kweli ulikuwa usiku lakini kila walipojaribu kukumbuka matukio waliyokutana nayo waliona hayazidi saa moja sasa walipoambiwa ni usiku wakachanganyikiwa kidogo. Hawakuongea lolote wakaongozana hadi nyumbani kisha Mjomba akawashukuru wanakijiji kwa kujitoa kumtafuta mpwa wake.



    Baada ya kila mmoja kuingia bafuni kujimwagia maji na kuondoa uchovu, wakakaa mahala pamoja na mjomba akawa wa kwanza kuvunja ukimya, akawatazama Tony na Martha kisha akakohoa kidogo na kuzungumza,

    “Tony, embu nidadavulie nini hasa kiliwakuta hata kututia hofu kwa maana kiza kilishatanda”

    Tony hakuwa na sababu ya kuficha, akaeleza kila kilichotokea, kuanzia ule upepo mkali hadi kukutana na mzee yule waliyemsaidia, baada ya kuelezea hayo yote, mjomba na shangazi wakawa kama wanatafakari wasijue nini la kusema japo nyuso zao zilionesha kutabasamu,

    “Mimi sioni haja ya kuwaficha na ukweli yule mzee mliyokutana naye si binadamu wa kawaida kama tulivyo sisi, wengi husadiki kuwa yeye ndiye mkuu wa msitu ule.

     Anaweza kutoa Baraka kwa wema na kuwaadhibu waovu, ninyi mlienda kama wachumba na mkamsaidia kwa pamoja hivyo katika maisha yenu Baraka zitakuwepo kama ninyi mtaendelea kuwa pamoja. Kile kimbunga kiliashiria majaribu katika dunia halisi hivyo jitahidi kuyashinda katika maisha yenu kukumbatiana kwenu kuliashiria kuweka agano au kiapo ambacho mnatakiwa mkitunze na kukieshimu,” alisema Mjomba.



    Tony na Martha ndiyo wakapa picha halisi juu ya mambo yale yaliyotokea, walifurahi sana kuona mapenzi yao yamepata kibali mbele za wengine na hata wale waliojaliwa kuwa na maono ya mbele.

    “Mjomba ukweli nampenda sana huyu mwanamke, mambo yakikaa sawa tutafika kwa paroko hili tupate kibali mbele ya Mungu,” alisema Tony.

    Martha pia akamgeukia Tony na kumwambia kuwa hata yeye anampenda ten asana na wala haitotokea kwa yeye kumtenda.

    “Zingatieni haya niliyowaambia, na kumbuka kuwa ukishamwambia mtu unampenda ni sawa na kuingia agano kuwa hutoona pengine hivyo jitahidi kuepuka vishwawishi na mjaliane kwenye hisia zenu, mimi na mjomba wenu tumedumu huu mwaka wa 23 sasa lakini ukituangalia ni kama vile tumetongozana jana,” alisema Shangazi na wote wakacheka.

    Usiku ulikuwa mkubwa sana na wote wakahisi usingizi mjomba akawaruhusu kwenda kupumzika na mengine watayaongea kadri siku ziendavyo.



          BAADA YA JUMA MOJA



    Martha na Tony wakawa wamesharudi jijini Dar-es-salaam na shughuli nyingine za kimaisha zikawa zinaendelea. Martha alifanya Usahili wa kwenda kusoma chuo kikuu cha Selou kilichopo jiji la Selou nchini Korea ya kusini. Mungu akajalia akapita katika usahili ule na kupata nafasi Moja kati ya tano za kwenda nchini humo kimasomo Zaidi.



    Ni ijumaa tulivu kabisa kila mtu akifikiri ni vipi ataitumia wikiendi yake, kwa upande wa Martha, Maandalizi ya safari ya kwenda kuendelea na masomo yakawa tayari, ivyo akaona ni vyema akatumia wikiendi hii kuagana vizuri na barafu wa moyo wake Tony. Katika kipindi hiki kila mmoja alionesha ni kiasi gani atatafunwa na upweke pale umbali utakapokua kikwazo katika mapenzi yao.Hatahivyo kila mmoja alikuwa na Imani kubwa juu ya mwenzie,

    “Martha nimekuzoea sana mpenzi, sijui vipi nitaishi ila naahidi kuwa mvumilivu na muaminifu, sitoruhusu msichana yeyote aingie moyo mwangu hadi pale utakaporejea”

    “Nakupenda sana Tony, nakuahidi uaminifu na uvumilivu pia, tuombe Mungu maana vishawishi ni vingi”

    Wawili hao wakakumbatiana kwa mabusu tele, kila mmoja akihuzunika moyoni mwake. Saa zikaenda mbio hatimaye siku ya safari ikawadia Tony akamsindikiza mpenziwe hadi uwanja wa ndege, muda ukawadia wakaagana kwa kumbato na kukumbushiana ahadi zao.



    ************************



    Wanajamii husema mwanadamu ni kiumbe anayebadilika kutokana na wakati na mazingira, kadri siku zilivyozidi kwenda ndivyo mawasiliano kati ya Tony na kipenzi chake Martha yalivyozidi kufifia. Tony hakuwa na wasiwasi juu ya hiyo hali alijua labda mpenzi wake amebanwa na masomo lakini kila akifikiria kuhusu siku za awali mambo hayakuwa kama yalivyokuwa sasa, Walizoea kujuliana hali walau mara mbili kwa siku lakini sasa Martha amebadilika mno.

    “Tony una nini mdogo wangu, mbona umenyongea kiasi iko”

    “Dada mie hata sielewi yaani, unajua sasa ni muda mrefu sana sijawasiliana na Martha”

    “Mhmh! Umejaribu kumpigia hapatikani?”

    “Sio hapatikani dada yaani kila nikipiga simu haipokelewi na hata nikimtumia meseji hajibu, nashindwa kuelewa ana shida gani?”

    “Hauna namba za mtu anayesoma nae umuulize”

    Kauli iyo ya dada ikampa Tony tumaini jipya akakumbuka jinsi alivyokuwa akiongea na kuchati na marafiki zake Martha ambao wanasoma chuo kimoja, akatabasamu kisha akamwambia dada yake,

    “Nina namba za rafiki zake nitawatafuta niwaulize”

    “Sawa mdogo wangu fanya ivyo”



    Baada ya mazumgumzo hayo, Tony akaingia chumbani akajilaza kitandani akachukua simu yake na kuingia mtandaoni, kwa bahati nzuri akakuta Martha yupo online bila kuchelewa Tony akatuma meseji lakini hakujibiwa ikabidi atume tena na tena lakini meseji zikawa zinasomwa tuu majibu asipate. Hali iyo ikamtesa sana Tony asielewe nini kimemkuta mpenzi wake, akaamua amtafute mmoja kati ya rafiki zake amuulize kulikoni, majibu aliyoyapata ama kwa hakika yaliuvunja moyo wake.

    “Samahani Tony kwa haya nitakayokwambia, kiukweli hata sisi tunaumia ila hatuna jinsi ni maamuzi yake, Martha kwa sasa yupo kwenye uhusiano mpya na kila tunapoongea kuhusu wewe, mwenzetu hataki kutuelewa”.

    Tony alijikuta akiangalia meseji aliyotumiwa na mmoja kati ya marafiki wa Martha, akutaka kuamini hilo akakumbuka ahadi na kiapo walichopeana, akajikuta chozi likimtoka.

    “Aneth naomba unisaidie kitu”

    “Sema tuu Tony”

    “Naomba fanya kila uwezalo niongee na Martha”

    “Sawa nitajitahidi kwa hilo”



    Baada ya maongezi mafupi na Aneth ambaye wanasoma chuo kimoja na Martha, Tony akashusha pumzi ndefu huku nafsi yake ikikaangika, hakutaka kuamini hata chembe kile ambacho Aneth amekisema. Akaamua aingie Facebook ili achunguze walau picha za Martha cha ajabu akakuta ameblokiwa hivyo hawezi kuona chochote, wazo la kuingia instagram likamjia alipoingia napo akakuta vile vile ameblokiwa, roho ilimuuma mno taratibu akaanza kusadiki yale maneno aliyoambiwa na Aneth.

    “Kwanini uliuteka moyo wangu hili hali ulijua utakuja kuumiza, kwa nini ulinitega nikategeka ilihali ukupanga kudumu nami….”

    Tony akajikuta anachukua kipande cha karatasi na kuandika maneno hayo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





    Martha ni mmoja kati ya wasichana wa kiafrika, waliokuwa na mvuto usiokuwa na kifani katika chuo kikuu cha Selou nchini Korea kusini.Uzuri wake uliwavutia wengi si wanaume pekee ata wasichana wenzake walipenda kuwa karibu nae.Wavulana wengi toka mataifa mbali mbali walijaribu kurusha ndoano zao hili waone endapo kama wataweza kuuteka moyo wa binti huyo lakini yeye alijua vyema kilichompeleka katika nchi hiyo ya kigeni ni masomo na si mambo mengine, hata hivyo tayari moyoni mwake kuna mtu amevuta kiti na kukaa hivyo haikuwa rahisi kwake kumkubali mwanaume yeyote tofauti na Tony.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog