Simulizi : I Killed My Beloved One (Nilimuua Nimpendaye)
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ILIPOISHIA:
“Nataka matatizo yako yakishaisha uwe balozi wa wanawake na watoto, nataka watu wajifunze kitu kutokana na matatizo yaliyokukuta, naamini utaniunga mkono,” alisema yule mama kwa sauti ya chini ambayo hakuna mwingine aliyesikia zaidi yangu.
SASA ENDELEA...
Nilitingisha kichwa kuonesha kuwa nimekubali alichoniambia, kisha akarudi mpaka kwenye kiti chake na kukaa. Kuna jambo ambalo walikuwa wakilijadili kabla hatujaingia lakini uwepo wetu uliwafanya waache kila kitu.
Yule mama mkurugenzi akamuita mmoja wao pale kwenye kiti chake na kumpa maagizo fulani kisha yeye akainuka na kukusanya vitu vyake pale mezani na kutuaga, akasema ana safari ya mkoani kikazi lakini tusiwe na wasiwasi kwani yupo pamoja na sisi katika kila hatua.
Alipoondoka, wale wanaharakati nao walikusanya vitu vyao, wakatuambia na sisi tuwafuate. Tukatoka mpaka nje ambapo tulikuta tayari kuna gari limeshaandaliwa, tukaingia pamoja na wale wanaharakati na safari ya kuelekea Muhimbili ikaanza.
Baada ya muda, tuliwasili Muhimbili, tukawa wa kwanza kushuka na kuwaongoza wale wanaharakati mpaka kwenye wodi aliyokuwa amelazwa mama. Tukiwa kwa mbali, tulimuona mama akiwa anatoka nje, mkononi akiwa amebeba ndoo, nadhani alikuwa akienda kufua.
Alipotuona, aliacha kila kitu, akawa anatukimbilia huku akiliita jina langu. Jamani mama alikuwa na nafuu kubwa sana, yaani ilikuwa ni lazima uambiwe kwamba siku chache zilizopita alikuwa anafungwa kamba vinginevyo usingeweza kuamini. Alipotufikia, alinikumbatia kwa nguvu na kuniinua kwa furaha.
Aliponiachia, alimkumbatia pia kaka yangu kisha tukamtambulisha kwa wageni. Alifurahi sana kukutana nao, akawashika kila mmoja mkono na kuwashukuru sana kwa jinsi walivyoisaidia familia yetu. Nilimuona mama akilengwalengwa na machozi, nafikiri ni kwa sababu ya furaha aliyokuwa nayo.
“Najua kuna watu wengi sana wanaoteseka huko mitaani ambao nao wanahitaji kupata msaada wenu lakini Mungu aliwaongoza mpaka kwenye familia yangu, sina namna ya kuwashukuru,” mama alisema kwa hisia huku akiendelea kutokwa na machozi ya furaha.
Ilibidi aache kila kitu alichokuwa anafanya, tukatafuta sehemu nzuri kwenye kivuli cha mti na kwenda kukaa, mama akaendelea kuwashukuru wale wanaharakati kutoka Tamwa huku akiwaeleza jinsi alivyopitia kipindi kigumu kwenye maisha yake.
“Pole sana, lakini sasa hivi unajisikiaje kiafya?”
“Namshukuru Mungu naendelea vizuri sana, daktari amesema leo naweza kuruhusiwa kurudi nyumbani, ushauri wa kisaikolojia niliopewa na Dismas Lyassa umenisaidia sana,” alisema mama, kauli iliyomfurahisha kila mmoja. Ni kweli mama alikuwa na nafuu kubwa mno kiasi kwamba hata mimi nilikuwa siamini.
Unajua jambo ambalo watu wengi hawalijui, kuna mamilioni ya watu wanaugua magonjwa ambayo hospitalini hayawezi kuonekana kwenye vipimo lakini kumbe tatizo lipo kwenye akili. Naweza kusema msongo wa mawazo ni hatari kuliko ugonjwa wowote unaoujua kwa sababu unaathiri akili ambayo katika mwili wa binadamu ndiyo injini.
Ili kuthibitisha hilo, hebu waangalie vichaa au wendawazimu wengi wanaozurura mitaani, ukijaribu kufuatilia historia zao, utagundua kuwa waliwahi kutokewa na matukio makubwa ambayo walishindwa kuyahimili na mwisho wakaishia kuwa vichaa. Najua hata mama tusingemhangaikia, na yeye angeishia kuokota makopo na kushinda kwenye madampo akichezea uchafu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mama aliongea mambo mengi sana mbele ya wale wanaharakati wa Tamwa, alitoa ushuhuda mzito kuhusu maisha yake na kuwaomba wale wanaharakati wamsaidie kumtoa kwenye hatia ya kushiriki kumuua baba.
“Lakini si umesema makubaliano yako na Jimmy hayakuwa kumuua mumeo bali kutoroka na mali zake?”
“Ndiyo, Jimmy aliniahidi kuwa tutaenda kuishi sehemu ambayo hakuna mtu yeyote atakayejua tulipo lakini nikashangaa anabadilika na kuandaa tukio lililoyakatisha maisha ya mume wangu kipenzi,” alisema mama huku akijifuta machozi yaliyokuwa yanamtiririka kwa wingi.
“Usijali, tutakusimamia kama tulivyomsimamia mwanao na wala hutahusishwa kwa namna yoyote kwenye kesi hiyo kwa sababu kwanza mshtakiwa namba moja tayari ameshakufa.”
“Nitashukuru sana.”
“Usijali, lakini pia inabidi ukamuombe msamaha Mungu wako kwa ulichokitenda na uishi kwa sala na toba, najua hata kama kisheria usipopatikana na hatia, bado hutakuwa huru ndani ya moyo wako mpaka utakapotubu na kumrudia Mungu wako,” alisema mwanaharakati mmoja wa Tamwa ambaye alionekana kuifahamu vizuri dini.
Tulikaa pamoja kwa muda mrefu, wale wanaharakati wakamhakikishia mama kuwa wataendelea kuwa pamoja naye katika kila hatua na kuhakikisha haki zake zote za msingi alizodhulumiwa na Jimmy zinarudi kwenye mikono yake. Nilimuona mama akifurahi mno, akiwa ni kama haamini alichokisikia.
Baadaye tuliwasindikiza, wakaondoka kisha tukarudi kwenye wodi aliyokuwa amelazwa mama, kila mtu akawa anamshangaa mama kwa jinsi alivyobadilika ndani ya muda mfupi. Wengi walitupongeza kwa jinsi tulivyoamua kujitoa kwa moyo wote kuhakikisha mama anapona.
Daktari alipokuja kuwatembelea wagonjwa wake, aliridhishwa kabisa na maendeleo ya mama, akaturuhusu turudi nyumbani lakini akatuambia kuwa tuwe tunampeleka mama kila wiki kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya afya yake. Siku hiyo ilikuwa ya furaha kubwa kwa mama, mara kwa mara machozi ya furaha yalikuwa yakimbubujika akiwa ni kama haamini.
Aliwaaga kwa furaha wagonjwa wenzake, manesi waliokuwa wanamhudumia na daktari wake kisha tukachukua kila kitu chetu na safari ya kurudi nyumbani ikaanza. Safari hii tulikodi teksi iliyotupeleka mpaka nyumbani.
Tulipofika nyumbani, tayari wadogo zetu walikuwa wametoka shuleni, walipomuona mama wote wakamkimbilia huku wakipiga kelele kwa furaha, wakamrukia mwilini na yeye akawakumbatia kwa nguvu, kila mmoja akawa anatokwa na machozi ya furaha.
Tulisaidiana kushusha mizigo kwenye gari na kuiingiza ndani, nikaenda kumsafishia mama chumba chake na kupanga kila kitu vizuri wakati yeye akiendelea kufurahi na wanaye wengine sebuleni. Siku hiyo ilikuwa muhimu sana kwenye historia ya maisha yetu kwani tulikuwa ni kama tumezaliwa kwa mara nyingine.
Niliingia jikoni na kuandaa chakula kizuri kwa ajili ya familia yote, kilipoiva tukasaidiana kuandaa. Tukala, kunywa na kufurahi huku tukimshukuru Mungu kwa miujiza aliyotutendea kwenye maisha yetu.
Tulikaa sebuleni mpaka karibu saa tano za usiku, ikabidi mama atukatishe na kuwaambia wadogo zetu wakalale kwani asubuhi walitakiwa kuwahi shuleni. Na mimi nilipotaka kwenda kulala, mama aliniambia nimsubiri kwani alikuwa na mazungumzo na mimi.
Nilikubali, nikaenda kuhakikisha wadogo zangu wote wamelala vizuri kwenye chandarua ili wasing’atwe na mbu kisha nikamfuata mama chumbani kwake. Kwanza alirudia tena kunishukuru kwa ujasiri mkubwa niliouonesha katika kipindi ambacho familia yetu ilikuwa ikipitia kwenye misukosuko ya hali ya juu.
Akaniuliza swali ambalo lilikuwa sawa na mwiba mkali kwenye moyo wangu:
”Matatizo yako ya kizazi yamefikia wapi?”
Sikutegemea kusikia swali hilo, hata sijui ni kwa sababu gani. Nafikiri ni kwa sababu sikuwa tayari kukubaliana na habari zozote mbaya kuhusu kizazi changu ambacho kiliharibiwa nilipopelekwa na Jimmy kutolewa ujauzito.
Nilishindwa kumjibu mama chochote, nikajishika tumbo langu na kuanza kuvuta kumbukumbu jinsi nilivyoteseka baada ya kutolewa ujauzito vibaya. Mama aliligundua hilo, akanikumbatia kwa upendo na kuniambia kuwa nisiogope sana, inabidi kesho yake tuende hospitali kupima kwa mara ya mwisho ili tujue mbivu na mbichi.
“Lakini mama, wewe ndiyo kwanza umetoka hospitali leo, kwa nini usipumzike kwanza haya mambo mengine yatafuata baadaye?”
“Hapana Eunice, wewe ni mwanangu na mimi ndiye ninayejua uchungu wako,” mama alisema kwa hisia, wasiwasi mkubwa ukazidi kunizonga kwenye moyo wangu. Hakuna kitu ambacho nilikuwa nakiogopa kama kuambiwa kwamba kizazi changu kimeharibika.
Hata hivyo, nilijipa moyo mwenyewe baada ya kukumbuka siku za mwisho kabla tukio la kifo cha Jimmy halijatokea. Nilikumbuka jinsi nilivyopingana na mpango wa madaktari kunifanyia upasuaji eti wanitoe kizazi changu ambacho kwa maelezo yao ya awali, kiliharibiwa vibaya wakati nilipotolewa ujauzito.
Nilikumbuka jinsi mpango huo ulivyokufa baada ya kutumia dawa ambazo zilifanya uchafu wenye harufu uliokuwa unanitoka uache na maumivu ya tumbo kupungua taratibu mpaka nilipopona kabisa na daktari kuniambia kwamba hakukuwa tena na haja ya kunifanyia upasuaji kwani nilikuwa naendelea vizuri.
Nilishusha pumzi ndefu na angalau nikawa na uhakika kidogo kwamba naweza kuwa salama. Sikutaka kuendelea kuzungumza tena na mama kwa sababu kwanza nilikuwa nimechoka, muda nao ulikuwa umeenda sana na pia habari za kwenda hospitali zilinitoa kwenye mudi.
Niliagana na mama na kuenda chumbani kwangu, nikajilaza kitandani huku moyoni nikimshukuru Mungu kwa kumponya mama. Haikuchukua muda, nikapitiwa na usingizi mzito. Sikushtuka mpaka kesho yake alfajiri. Nikawahi kuamka kama kawaida yangu na kuanza kuwaandalia chai ndugu zangu wanaoenda shuleni.
Nikawaamsha na kuwasaidia kujiandaa, walipoondoka nilianza kufanya usafi wa nyumba nzima. Mpaka mama alipoamka, alinikuta tayari nimeshamaliza kazi zote, tukasalimiana na kujuliana hali kisha tukaenda sebuleni kwa ajili ya chai.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa kuwa wadogo zangu wengine walikuwa wameshaondoka kwenda shule, tulibaki watatu tu, mimi, kaka Gisla na mama. Tukiwa tunaendelea kupata kifungua kinywa, kaka alimwambia mama kuhusu suala la sisi kurudi shuleni, nikamuona akisitasita kidogo, nadhani ni kwa sababu bado hakuwa na uhakika wa kupata pesa.
“Usijali kuhusu ada, wale watu wa Tamwa wamesema watatulipia kwa kipindi chote wakati taratibu za kisheria za kurudisha fedha na mali zote zilizochukuliwa na Jimmy kijanja kutoka kwako zikiendelea,” nilisema, kauli ambayo ilimfurahisha sana mama.
Akainua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu kisha akaongea jambo ambalo lilizidi kutupa matumaini kwamba kweli mama alikuwa akirejea kwenye hali yake ya kujitambua kama zamani.
Alisema tuende kwanza hospitali kufuatilia mambo yangu kisha baada ya hapo, tumpeleke kwa padri akaungame na kutubu dhambi zake zote, ikiwemo ile kubwa ya kumsaliti baba na kuwa chanzo cha kifo chake.
Tulifurahishwa sana na alichokisema kwani hata Dismas Lyassa alitushauri kitu kama hicho, pia hata wale wanaharakati wa Tamwa pia walitushauri hivyohivyo. Kweli tulipomaliza kula, tulijiandaa wote watatu na safari ya kuelekea hospitali ikaanza. Safari hii hatukutaka kwenda Muhimbili tena kwa sababu hata Amana ningeweza kufanyiwa vipimo.
Njia nzima nilikuwa natetemeka huku nikitamani muujiza utokee. Nilijiapiza kuwa endapo nikikutwa nipo salama, kamwe haitakuja kutokea kwenye maisha yangu nikaja kutoa mimba tena, iwe kwa hiyari au kwa lazima.
Tulifika Amana, tukateremka kwenye Bajaj na kuongoza moja kwa moja kuelekea ndani ya hospitali hiyo, tukafuata taratibu zote za hospitalini kisha tukaelekezwa kwenda kwenye ofisi ya daktari wa magonjwa ya wanawake. Hofu iliyokuwa ndani ya moyo wangu, naijua mwenyewe. Tulipofika, ilibidi kaka abaki nje, tukaingia mimi na mama ambapo alinisaidia kueleza kila kitu kilichonitokea.
Kwa kweli nilijisikia aibu sana kwa sababu sikuwa nataka kila mtu ajue kwamba nimewahi kutoa ujauzito lakini kama wasemavyo wahenga, mficha maradhi, kifo humuumbua.
Yule daktari, mwanamke wa makamo ambaye kichwa chake kilikuwa na mvi kiasi, alinilaza kwenye kitanda maalum na kuanza kunifanyia vipimo. Anajua mwenyewe utaalamu aliokuwa anatumia kwani baada ya kuniangalia kwa kutumia mashine fulani ambayo ipo kama kompyuta, alishusha pumzi ndefu na kumgeukia mama.
Alimwambia kwamba nina bahati kwa sababu mwili wangu umejitibu wenyewe na kujiunga sehemu ya kizazi iliyopata matatizo kipindi kile nilipotolewa ujauzito. Akanigeukia na kuniambia nimshukuru sana Mungu na endapo nikirudia tena kutoa ujauzito, huenda ndiyo ikawa siku yangu ya kufa.
Nilimuapia kwamba kamwe sitathubutu tena kufanya mchezo huo hatari, hata iweje. Akawa anaandika baadhi ya vitu kwenye karatasi ambalo aliliweka kwenye faili, akatuandikia majibu ya vipimo na kuendelea kunisisitizia kuhusu kuachana na mambo ya wanaume na kukazania masomo.
Tulimshukuru sana, nikakumbatiana na mama kwa nguvu huku machozi yakinitoka. Tukaagana naye na kutoka mpaka nje, tukamkuta kaka akiwa anatusubiri kwa shauku naye akitaka kujua nini kimetokea. Nilimkimbilia na kumkumbatia kwa nguvu, nikamweleza kuwa nipo salama, taarifa ambazo na yeye alizipokea kwa furaha kubwa kiasi cha kulengwalengwa na machozi.
Tulitoka huku wote tukiwa na furaha kubwa kwenye mioyo yetu kwani milango iliyokuwa imefungwa na Jimmy kwenye maisha yetu, sasa yote ilikuwa ikifunguka, mmoja baada ya mwingine.
Simsemi vibaya kwa sababu marehemu hasemwi ila kiukweli Jimmy alitusababishia matatizo makubwa sana kwenye maisha yetu kiasi kwamba sitakuja kumsahau mpaka siku ya mwisho ya uhai wangu. Hata hivyo, licha ya yote hayo, bado namuombea kwa Mungu ampumzishe mahali pema peponi na ampunguzie adhabu siku ya kiama kwa sababu hakupata hata nafasi ya kutubu dhambi zake kabla hajafa.
Basi tuliondoka hospitalini hapo na kurudi kwanza nyumbani kisha baada ya kupumzika, tukatoka wote watatu na safari ya kuelekea kanisani ikaanza kwa ajili ya kumpeleka mama kuungama na kutubu dhambi zake.
Tulipofika kanisani, tulienda moja kwa moja katika ofisi za mchungaji. Kaka ndiyo alitangulia mbele, akagonga mlango, sauti nzito ya mchungaji ikasikika ikitukaribisha. Sote tuliingia ndani ya ofisi hiyo na kukaribishwa kwenye viti, tukakaa kisha mama akaanza kuzungumza na mchungaji.
Alianza kwa kujitambulisha yeye kisha akatutambulisha na sisi kwa mchungaji, wote tulinyanyuka na kumsalimia mchungaji kwa kupeana naye mikono. Baada ya muda kidogo, mama alituomba tutoke nje ili apate muda wa kuzungumza na mchungaji. Ilibidi mimi na kaka tutoke nje na kumpa mama nafasi kama alivyoomba.
Mama alianza kwa kumueleza mchungaji kila kitu kilichotokea katika maisha yake. Hakuficha kitu, japokuwa tulikuwa nje tuliweza kusikia kila kitu kilichokuwa kinaendelea. Alipomaliza kumueleza, uso wake wote ulikuwa umejawa na machozi.
Mchungaji ambaye kwa muda wote huo alikuwa akimsikiliza mama kwa makini, alishusha pumzi ndefu na kusimama pale alipokuwa amekaa. Akatembea taratibu kumfuata mama na kumshika begani, akawa anambembeleza na kumpa maneno ya kumtia faraja ambayo kwa kiasi kikubwa yalimsaidia mama.
“Hata Biblia inasema kwamba sote tunahitaji msamaha kutoka kwa Mungu, kitabu cha Mhubiri 7:20, Biblia inasema: Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani ambaye anafanya mema tu hajawahi kufanya dhambi.”
“Kwa kuwa Mungu ni mwenye upendo na huruma, yupo tayari kutusamehe. Kitabu cha 2 Petro 3:9, kinasema: Yeye hutuvumilia maana hapendi mtu yeyote apotee bali wote wafikirie toba. Yesu alikufa juu ya msalaba kwa sababu ya dhambi zetu ili tuendelee kuwa hai kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23).CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mchungaji aliendelea kumtolea mama maneno ya vifungu vya Biblia huku akimwambia kuwa hajachelewa kutubu na kuungama dhambi zake. Baada ya mchungaji kumjenga mama kiimani, alitoka naye na kuelekea chumba cha kuungamia ambapo alimuongoza kwenye sala ya toba.
Iliwachukua zaidi ya nusu saa kufanya kazi hiyo, walipomaliza walitoka na kurudi katika ofisi ya mchungaji na sisi tukaitwa na kuanza kuhubiriwa neno la Mungu. Pia mchungaji akatufundisha kuwa tusiache kufanya ibada hasa kwenye siku hizi za mwisho ambazo dunia inaelekea ukingoni. Alitufundisha pia namna ya kuishi na mama na kumsaidia kuondokana na majuto ya dhambi na kutusisitizia kuwa tuwe tunasoma sana Biblia.
Baada ya hapo, mchungaji alitufanyia maombi sote kwa pamoja kisha akatusisitiza kila Jumapili tuwe tunaenda kanisani. Tulimshukuru sana mchungaji, tukaagana naye na kuanza safari ya kurudi nyumbani.
Tuliporudi nyumbani, tulimshukuru Mungu kwa miujiza aliyotutendea, mimi na mama tukaenda jikoni kuandaa chakula cha jioni kwa ajili ya familia kwani tayari muda ulikuwa umeenda sana. Kilipoiva, tulikula na wadogo zetu ambao tayari walikuwa wamesharejea kutoka kanisani na sote tukaenda kupumzika.
Nikiwa nimejilaza chumbani kwangu, niliendelea kukumbuka mambo yote yaliyotokea kwa siku hiyo kuanzia asubuhi. Nilimshukuru sana Mungu wangu na niliamini kweli yeye ni muweza wa yote. Nilimshukuru pia Mungu kwa kuniokoa na janga la kizazi changu kutoharibika baada ya kutoa ujauzito ambapo sasa nilikuwa na uwezo wa kubeba mimba na kuzaa kama wanawake wengine.
Pia nilimshukuru sana Mungu kwa miujiza aliyoendelea kumtendea mama yetu, sikutegemea kama familia yetu ingekuja kuwa na furaha tena kama zamani. Niliwaza mambo mengi sana mpaka nilipokuja kupitiwa na usingizi mzito, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka ilipofika alfajiri.
Jogoo wa kwanza alipowika, tayari nilikuwa nimeshaamka, nikapiga magoti na kuanza kusali kama mchungaji alivyotufundisha kisha nikachukua Biblia yangu na kuanza kusoma.
Baada ya kumaliza kupitia neno la Mungu, nilitoka chumbani kwangu na kwenda kuanza kufanya usafi wa nyumba nzima kama ilivyo kawaida yangu na kuwatengea chai wadogo zangu wanaowahi kwenda shule, walipomaliza kupata kifungua kinywa, niliwasindikiza kwenda kupanda gari la shule kisha mimi nikarudi na kuendelea na kazi za nyumbani.
Baadaye mama aliamka na kukuta nimeshamaliza kazi zote, tukasalimiana kwa furaha kisha nikamuuliza kama amekumbuka kusali na kusoma Biblia kabla hajaendelea na shughuli nyingine. Alinishangaza aliponiambia kuwa kuanzia saa tisa za usiku alikuwa macho akisali, kulia na kusoma Biblia ili Mungu wake amsamehe.
Nilifurahi sana kwani ilionesha kweli mama anajutia yote yaliyotokea. Muda mfupi baadaye, kaka naye aliamka ambaye naye swali la kwanza baada ya kusalimiana na mama, alimuuliza kama amekumbuka kusali na kusoma Biblia. Mama alimjibu kama alivyonijibu mimi, nikamuona naye akifurahi kuliko kawaida.
Baada ya wote kumaliza kuoga, tulikaa sebuleni kwa ajili ya kupata kifungua kinywa huku tukiendelea kupiga stori za hapa na pale. Jamani kweli Mungu mkubwa, ule upendo na amani vilivyokuwa vimetoweka kwa kipindi kirefu kwenye familia yetu, sasa vilirudi kwa kasi, tena maradufu. Nilijisikia furaha mno ndani ya moyo wangu.
Tukiwa tunaendelea kupata kifungua kinywa, tulisikia mlango wa mbele ukigongwa, kaka akainuka na kwenda kuangalia ni nani aliyekuwa anagonga asubuhi yote ile. Sote tukatulia na kusikiliza kwa makini, tukamsikia akiwapokea wageni kwa furaha na kuwakaribisha ndani.
Kumbe walikuwa ni wale wanaharakati wa Tamwa, wanasheria walionisaidia katika kesi yangu pamoja na yule mama mkurugenzi wa Tamwa (nilisema sitamtaja jina kwa sababu maalum). Sote tulisimama na kuwakaribisha wageni wetu kwa furaha kubwa. Tuliwakaribisha chai lakini wakasema wao tayari wameshakunywa hukohuko walikotoka.
Ilibidi tuache kila kitu na kwenda kukaa nao kwenye masofa huku tukiwa na shauku kubwa ya kusikia kama wana ujumbe wowote waliotuletea. Wote walifurahishwa mno na maendeleo yangu pamoja na ya mama, kila mmoja nikamsikia akimshukuru Mungu kwa miujiza iliyotokea.
Baada ya hapo, yule mkurugenzi wa Tamwa ambaye ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kufika pale nyumbani, alivunja ukimya kwa kueleza kuwa kikubwa kilichowaleta pale, ni kuhusu mali za marehemu baba. Sote tulijiweka vizuri kwenye viti vyetu, tukiwa na hamu kubwa ya kusikia anataka kuzungumza nini.
Akatuambia kuwa wao kwa kushirikiana na wanasheria wao, wamejitahidi kwa kadiri ya uwezo wao kupigania haki zetu za msingi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mali zote zilizozchukuliwa na Jimmy kwa hila, zinarudi kwenye mikono yetu lakini walikutana na kikwazo kikubwa ambacho ni saini za mama kuonekana katika mikataba yote feki iliyohalalisha mali za familia yetu kuhamishiwa kwenye himaya ya Jimmy.
“Lakini tumefikia hatua nzuri sana na tunaamini kwamba tukishirikiana, tutafanikisha hii kazi kubwa iliyopo mbele yetu,” alisema yule mkurugenzi kisha akaanza kutueleza tulichokuwa tunatakiwa kukifanya.
Jambo la kwanza, ilikuwa ni kuongozana nao tukiwa na mama mpaka mahakamani ambako wanasheria wao wangemsaidia mama kubatilisha saini zake zote alizoweka kwenye nyaraka mbalimbali alizosainishwa na Jimmy kijanja. Wakatuhakikishia kwamba endapo zoezi hilo likimalizika vizuri, basi mali zote zilizoporwa na marehemu Jimmy enzi za uhai wake, zingerudishwa kwetu.
Harakaharaka sote tulienda kujiandaa na baada ya muda mfupi, tulitoka na ule ugeni mpaka nje ambako magari mawili waliyokuja nayo, yalikuwa yamepaki. Tukaingia na safari ya kuelekea mahakamani ikaanza huku njiani wote wakitupa matumaini kwamba kila kitu kitaenda sawa.
Baada ya dakika kadhaa, tayari tulikuwa tumewasili mahakamani.
Mimi na kaka tukaambiwa tubaki pale nje kwenye vivuli vya miti kisha wao wakaingia ndani na mama. Tuliendelea kuzungumza mambo mbalimbali na kaka yangu, huku mawazo yetu yote yakiwa ni kwenye suala la kurudi upya shuleni.
Baada ya takribani saa mbili, tuliwaona wakitoka huku wakiwa wameongozana na mama ambaye safari hii alionekana kuchangamka sana, tofauti na awali. Wakatufuata mpaka pale tulipokuwa tumekaa kisha mama akatuambia kuwa kazi imeisha. Akatukumbatia kwa furaha kisha tukaongozana mpaka kwenye magari.
Kabla hatujapanda, tuliagana kabisa na yule mkurugenzi pamoja na wenzake, wao wakapanda kwenye gari moja kisha sisi tukapanda kwenye lingine tukiwa na dereva tu ambaye alipewa maagizo ya kuhakikisha anatufikisha nyumbani. Safari ikaanza huku tukiwa na na shauku kubwa ya kwenda kumuuliza mama juu ya kilichotokea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pia kabla yule mkurugenzi hajaagana na sisi, alituambia kuwa tuhakikishe tunarudi shuleni haraka iwezekanavyo kwa sababu tayari walishazungumza na uongozi wa shule na kukamilisha masuala ya malipo kwa hiyo kilichokuwa kimebaki ilikuwa ni mimi na kaka kwenda kuripoti shuleni.
Safari iliendelea hadi tulipofika nyumbani, tukateremka kwenye gari na kuagana na dereva, tukashikana mikono, mama akiwa katikati na kuingia ndani ambako alianza kutusimulia jinsi alivyokula kiapo maalum mle ndani wakati sisi tukiwa nje.
Alitupa matumaini makubwa sana kwamba kila kitu kitakuwa sawa baada ya siku chache kwa sababu wale watu wa Tamwa walikuwa wakiifanya kazi yao ipasavyo. Tulifurahi sana, tukamuuliza kama ikitokea mali zote zilizoachwa na marehemu baba zikarudishwa mikononi mwake atafanya nini?
“Sitarudia tena kufanya ujinga wowote, haraka sana nitawaandikisha wanangu kuwa wamiliki halali kwa sababu naweza kuanguka leo hata kesho nikafa na kuwaacha kwenye mateso makubwa wanangu.
“Haya yaliyotokea yamenifundisha kitu kikubwa sana, hivi mmewahi kujiuliza kama ningekufa kabla hamjakutana na wanaharakati wa Tamwa au kama ningechanganyikiwa jumla mngeishi vipi kwenye kwenye hii dunia?” mama alituuliza swali ambalo ama kwa hakika lilitugusa.
Ni kweli kama mama angetangulia mbele za haki au asingepona matatizo yake ya akili, tungeishi maisha ya kuhangaika sana. Yaani ilikuwa ni kama miujiza tu kwa Mungu kuamua kuiunganisha tena familia yetu japokuwa baba hakuwepo duniani.
Tulizungumza vitu vingi sana na mama siku hiyo, akatuasa kuwa elimu ndiyo urithi pekee ambao utatusaidia katika maisha yetu ya baadaye hivyo tutakaporudi shuleni tusifanye kabisa mchezo na elimu.
Pia alinigeukia na kuanza kunipa nasaha, akinisihi kuwa makini na wanaume wasije wakanilaghai na kuniharibia maisha kama ilivyotokea kwa Jimmy. Akaniambia kuwa nijitunze sana na kusahau yote yaliyotokea, akili zangu nizielekeze kiwenye masomo mpaka nitakapokuwa mtu mzima, nipate mchumba na kuolewa kwa heshima.
Alimuasa pia kaka naye kuwa makini kwa sababu hata wanawake nao siku hizi wamebadilika mno hivyo asimuamini mtu yeyote mpaka atakapokuwa mkubwa na kumpata mke bora wa maisha yake.
Baada ya hapo, tuliendelea na kazi nyingine za kawaida za pale nyumbani huku kila mmoja akiisubiri kwa hamu siku inayofuatia ambayo ndiyo tulipanga kwenda kuanza shuleni.
Kila mmoja kwa wakati wake aliendelea kujitayarisha huku tukishirikiana pia kufanya kazi mbalimbali za pale nyumbani mpaka wadogo zetu waliporudi shuleni. Hatimaye siku hiyo ikapita, ikafika siku tuliyokuwa tunaisubiri kwa hamu kubwa ya kurudi shule.
Mimi na kaka tuliwahi kuamka siku hiyo kuliko siku nyingine zote, tukaanza kujiandaa kwa kuvaa sare mpya za shule tulizonunuliwa na wale wanaharakati wa Tamwa na mabegi mapya. Tuliendelea kujitayarisha na wadogo zetu walipoamka, walikuta tayari tumeshavaa sare za shule.
Siku hiyo mama ndiyo alitusaidia kuandaa kifungua kinywa, familia nzima tukakaa mezani huku kila mmoja akiwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake. Hatimaye baada ya kumaliza kupata kifungua kinywa, mama alitusindikiza na kututakia masomo mema, akawapeleka wadogo zetu sehemu yao ya kusubiria gari la shule.
Mimi na kaka Gisla kwa sababu tulikuwa tukisoma shule tofauti, tukaenda eneo ambalo zamani tulikuwa tukisubiria gari la shule ambapo tuliwakuta wanafunzi wenzetu ambao karibu wote walionekana kutushangaa.
Japokuwa tulikuwa na wakati mgumu kujibu maswali ya kila mmoja, mimi na kaka tulikubaliana kwamba jibu letu liwe moja tu, kwamba mama yetu alikuwa akiumwa sana ndiyo maana tuliacha kwenda shule kwa muda.
Kweli kila aliyekuwa akituuliza sababu za kutoonekana shuleni kwa kipindi chote hicho, jibu letu lilikuwa ni hilohilo. Baadaye gari la shule lilikuja na tukapanda pamoja na wanafunzi wenzetu mpaka shuleni. Moja kwa moja tukaenda kuripoti kwenye ofisi ya mkuu wa shule kama tulivyoelekezwa na wale wanaharakati wa Tamwa.
Ilivyoonesha tayari mkuu wa shule alikuwa na taarifa zetu kwani alitupokea kwa uchangamfu, kitu ambacho siyo kawaida yake, akatupa pole kwa matatizo yote yaliyotokea kisha akanyanyua simu ya mezani na kuzungumza na upande wa pili. Muda mfupi baadaye, tulimuona mwalimu wa taaluma au Academic Master kama tulivyozoea kumuita akiingia kwenye ofisi ya mkuu wa shule. Kama ilivyokuwa kwa mkuu wa shule, mwalimu huyo naye alitusalimia kwa kutushika mikono huku akitupa pole sana kwa yaliyotupata.
Tulijisikia faraja kubwa ndani ya mioyo yetu kuiona kwamba kumbe kuna watu walikuwa wakijali kuhusu kilichotutokea. Mkuu wa shule akampa maelekezo mwalimu wa taaluma kwamba ahakikishe tunasoma yale masomo waliyofundishwa wenzetu katika kipindi ambacho hatukuwepo shuleni.
Baada ya hapo, mkuu wa shule alitutakia masomo mema kisha tukatoka na mwalimu wa taaluma ambaye alitupeleka mpaka ofisini kwake, kisha akamuita mwalimu wa darasa wa kaka Gisla ambaye alipofika, naye alimpa maelekezo kama aliyopewa na mkuu wa shule. Akatoka na kaka kuelekea darasani kwao kwani tulikuwa tukisoma madarasa tofauti.
Muda mfupi baadaye, mwalimu wetu wa darasa, Madam Joyce naye alikuja pale ofisini, akafurahi mno kuniona kiasi cha kumfanya anikumbatie kwa nguvu, mwalimu wa taaluma alipomaliza kumpa maelekezo, alinishika mkono, tukatoka naye na kuelekea mpaka darasani.
Wanafunzi wote walipigwa na butwaa wakati tukiingia, huku wengine wakilitaja jina langu kwa mshtuko, mwalimu akawatuliza na kuwaeleza kuwa nilikuwa na matatizo makubwa ya kifamilia ndiyo maana sikuwepo shuleni kwa kipindi hicho chote. Akawaambia wanipe ushirikiano wa kujifunza yake ambayo wenzangu walifundishwa kipindi ambacho mimi sikuwepo.
Nikaenda kukaa kwenye dawati langu huku wanafunzi wenzangu wengi wakija kunipa mikono ya pole, kwa kweli nilifarijika mno na kujiona nimekuwa mpya. Hatimaye ndoto zangu za kurudi shuleni kuendelea na masomo zikawa zimetimia. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni hapo ndipo nilipoamini kwamba kumbe kila jambo huja kwa sababu maalum hapa duniani na ukiona giza linaongezeka, ujue mapambazuko yamekaribia.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment