Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 3

 







    Simulizi : Niliishi Dunia Ya Peke Yangu

    Sehemu Ya Tatu (3)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Mwili wangu ulikuwa katika hali ya unyonge kama mgonjwa macho yalikuwa yamevimba kidogo na kuwa mekundu kutokana na kulia sana kila nilipokumbuka kutengana na familia niliyo izoea kwenda kuishi sehemu nisiyoijua. Lakini bado niliamini sikutakiwa kuogopa chochote zaidi ya kuondoka na kuwa tayari kukabiliana na lolote nitakalo kutananalo. Waliponiona waliitana na kuzungumza kwa muda kisha walikuja kwa ajili ya maombi na kunieleza jioni ya siku ile kutakuwa na kikao cha kuzungumzia matatizo yangu kwa kina. Sikutaka kuwabishia niliwakubaliana, waliondoka na kuniacha na mama ambaye aliendelea kunitia moyo na kuamini nitayashinda yote yanayonikatisha tamaa. Nilikubaliana naye na kufanya kazi zote za muhimu za asubuhi ikiwa pamoja na kuandaa chakula cha mchana. Baada ya kuoga na kujiandaa kutoka niliomba kwa mama nitoke mara moja. “Ester mwanangu kwa nini usipumzike tu leo maana nakuona haupo sawa.” “Hapana mama baada ya maombi ya asubuhi sasa hivi nipo sawa wala usihofu.” “Umesema unakwenda wapi?” “Kwa Suzana kuna kitabu cha maombi alisema atanipa.” “Basi usichelewe.” “Sawa mama.”niliagana na mama na kuelekea ofisini kwa baba. Nilikwenda hadi ofisini kwa baba, aliponiona alinichangamkia na kunikaribisha kwa bashasha. “Karibu Ester.” “Asante baba.” “Karibu mama yangu, karibu kwenye kiti,” alisema huku akinyanyuka toka nyuma ya meza yake kwa kunikaribisha kama mgeni maalumu, ilikuwa ina tofauti na siku za nyuma nilipokwenda ofini kwa baba nilipotumwa na mama, alinikaribisha kwa heshima lakini si kwa kunyanyuka kitini na kuzunguka meza. Alikikaribisha akionesha moyo wa upendo ambao nilijifikia jinsi ya kuachana nao, nilikumbuka

    mapenzi ya awali ambayo alinifanyia kiasi cha kusahau matatizo yote ya nyuma. Kosa alilofanya ni kunibaka ambalo nalo nilimsamehe lakini Mungu naye akatoa ushahidi wake wa mimi kushika mimba. Lakini hakuwahi kunitendea kitu chochote kibaya zaidi ya kunilea kama mtoto wake wa kunizaa ndiyo maana niliamua kumsamehe aliponiomba msamaha japo historia yake ya nyuma ilionesha ana huruma ya mamba kukulia ukiwa nje ya maji ukiingia unakugeuza kitoweo. “Za nyumbani mama?” aliniuliza kwa unyenyekevu. “Nzuri tu baba.” “Mmh! Sasa kwa hiyo bado una msimamo wako?” “Baba nina imani tumeisha zungumza kinachotakiwa ni utekelezaji,” sikutaka kulegeza msimamo wangu. “Sawa, mzigo huu hapa hesabu mwenyewe,” baba alisema huku akiweka bahasha ya fedha juu ya meza. “Kama zipo sawa sina umuhimu wa kuzihesabu nakuamini,” nilisema huku nikichukua bahasha. “Lakini kwa nini hukutaka tufanye zoezi dogo tu.” “Zoezi gani?,” sikumuelewa alikuwa na maana gani. “La kutoa hiyo mimba kwanza ni changa isingesumbua.” “Naomba kauli hiyo uachane nayo, labda unaona hasara fedha zako, nitaondoka hata kwa miguu bila senti tano yako na kwenda kufia mbele ya safari.” “Hapana Ester, ni mawazo yangu tu wala si lazima.” “Sasa baba nilikuwa na wazo jingine,” baada ya kuona msimamo wangu nilimueleza ninachowaza. “Wazo gani?” “Nataka nikitoka hapa nisirudi nyumbani.” “Unakwenda wapi?” “Ndiyo safari yangu imeanza, jioni nitapanda malori mpaka Iringa na kesho asubuhi nipande basi mpaka Dar.” “Ulipoondoka nyumbani na mizigo yako ulimuaga vipi mama yako?” “Sikuondoka na kitu chochote zaidi ya nilivyo hapa.” “Amemwambiaje mama yako?” “Nimekwambie nimefuata kitabu cha maombi kwa shoga yangu.” “Kwa hiyo utaondoka vipi bila nguo zako?” “Inabidi iwe hivyo kwa vile siwezi kutoka nyumbani na mzigo bila kuulizwa mswali. Kingine sasa hivi hali nyumbani imechafuka.” “Imechafuka! Una maana gani?” “Nimekuwa nikiulizwa maswali ya mitego na mama ambayo huenda majibu yake anayo anasubiri kauli yangu kukamilisha.” “Una maana gani?” “Toka siku ya kwanza mama alikuwa na wasiwasi huenda umenibaka, nilimkatalia bado alikuwa

    na wasiwasi na majibu yangu. Jana alinibana na maswali mazito huku akitaka niseme umenibaka nilikataa lakini bado alikuwa na mimi mpaka nilipomdanganya nitampa jibu kesho. Huoni nikirudi leo nyumbani sitakuwa na majibu ya maswali ya mama? ”

    “Alisema hivyo?” “Kuhusu nini?” “Kuwa nimekubaka?” “Hajasema ila ndicho anachokitaka nikiseme, amesema ana maono, ameota kuna kitu kimetendeka ndani lakini nakificha, pia kuna jambo zito la aibu linakuja na kuniomba niseme ukweli. Kuna ukweli gani zaidi ya mimi kusema kuwa umenibaka?” “Kwa nini unang?ang?ania kubakwa, unafikiri hakuna kitu kingine anachokiwaza juu yako?” “Kutokana na historia yako chafu ya siku za nyuma, swali la jana si la kwanza, kuna siku aliniuliza kama kweli umenibaka ungekuwa ni mwisho wa ndoa yenu. “Amenieleza uchafu wako wa siku za nyuma hadi akalazimika kuondoka nyumbani.” “Nimekuelewa, basi itabidi nikupe fedha ukanunue nguo za kuanzia maisha.” “Siyo mbaya nikipata na begi kabisa.” Baba alivuta droo na kutoa laki mbili, akanipatia. “Kanunue nguo, ila kitu chochote kikitokea nijulishe, nitakuongeza fedha ukanunue na simu ili nijue maendeleo yako kwa vile umeondoka na damu yangu.” “Hakuna tatizo.” “Ukimaliza weka vitu vyako sehemu yenye usalama ili uje uniage, sawa mama?” “Sawa baba.” Baada ya kuniongeza fedha niliondoka hadi mjini na kununua mahitaji yangu muhimu ya nguo, simu sikuihitaji kwa vile ingekuwa chanzo cha kujiingiza kwenye matatizo hata namba ya simu ya baba sikuihitaji tena kwa vile nilipanga kwenda kuanza maisha mapya sehemu nisiyoijua, sikutaka kusumbuliwa na mtu yeyote. Baada ya kuviweka vitu vyangu vizuri kwenye begi, majira ya saa kumi na moja na nusu jioni nilipanda gari ndogo hadi nje ya mji ili niwe na uhakika na safari yangu. Nilifika katika mji majira ya saa kumi na mbili jioni. Mji ule ulikuwa umechangamka sana, kwa vile sikutaka watu wanizoee, nilikwenda kwenye duka moja ambalo kaka mmoja alikuwa akiuza bidhaa na kumuomba msaada wa kuwekewa begi langu ili nifanye mipango ya usafiri wa lori. Nilimwamini kuwa asingeweza kulipekua begi langu kwa vile asingeweza kufikiria kama ndani kulikuwa na kitu cha maana. Nilitoka hadi sehemu yanapoegeshwa malori, nilimkuta kaka mmoja akibadilisha tairi. “Habari kaka?” Nilimsalimia. “Nzuri tu dada yangu,” alinijibu huku akinyanyua uso wake na kunitazama. “Samahani kaka, wewe ni dereva?” nilimuuliza. “Vipi, una shida gani?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Nahitaji msaada wa lifti mpaka Iringa.” “Dereva amelala mpaka usiku.” “Lakini si mnaondoka leo?” “Ndiyo, majira ya saa nne usiku.” “ Dereva anaamka saa ngapi?” “Mpaka saa moja na nusu, atakuwa ameamka.” “Basi nilikuwa naomba lifti au hata fedha naweza kulipa ili nifike Iringa.” “Hakuna tatizo una mizigo?” “Nina begi tu.” “Basi nitakusaidia.” “Nitakuwa pale dukani.” “Hakuna tatizo dada yangu.” Nilirudi dukani na kumuomba yule kaka kiti ili nipumzike, nilimshukuru mwenye duka japokuwa alikuwa mwanaume lakini alikuwa na roho ya ukarimu. Majira ya saa mbili yule kaka alinifuata na kunitaka nipeleke mzigo kwenye gari. Nilifanya vile kwa sababu nilikuwa nimekwisha kula niliamua kukaa ndani ya gari. Majira ya saa nne usiku tuliondoka, lori lile lilikuwa linakwenda Dar es Salaam kutokana na maelezo ya dereva lakini wala sikutaka kwenda nao hadi Dar. Niliamua kuwadanganya kuwa naishia Iringa ili niweze kuondoka na mabasi ya asubuhi yake. Nilimshukuru Mungu tuliingia Iringa alfajiri na kwa bahati nzuri niliteremshiwa karibu na kituo cha mabasi. Niliwashukuru kwa msaada wao wa kunisafirisha bure. Baada ya kuniteremsha wao waliendelea na safari ya Dar, kwa vile sikutaka msaada wa kila kitu niliwaacha waondoke. Sikuwa mgeni sana Iringa kwani kabla mama hajafariki niliwahi kufika naye zaidi ya mara mbili. Nilikwenda kukata tiketi katika basi la Upendo linalokwenda Dar. Baada ya kukata tiketi niliingia kwenye basi na kukaa kwenye siti yangu kusubiri basi liondoke. Majira ya saa kumi na mbili na nusu basi liliondoka kituoni. Nilitulia huku nikimuomba Mungu nifike salama japo sikujua nitafikia wapi. Niliamini kutokana na maelezo ya msichana mmoja aliwahi kurudi nyumbani baada ya kupachikwa mimba na baba mwenye nyumba na kunusurika kuuawa na mkewe baada ya kugundua mimba ilikuwa ni ya mumewe, nilijua sitapata tabu. Maelezo yake yalinipa ujasiri jinsi alivyoweza kuingia Dar bila kuwa na mwenyeji na kuweza kupata kazi. Kwa upande wangu japo hali yangu ya ujauzito ilikuwa bado haijaanza kuonekana, nisingeweza kwenda kutafuta kazi ya ndani kwani ningekuwa mzigo. Nikiwa nimezama kwenye mawazo nililiona basi likiacha mji wa Iringa na kuutafuta Mkoa wa Morogoro. Moyoni nilikuwa tayari kuishi maisha yoyote na niliamini mateso yangu yalikuwa na mwisho.

    Safari iliendelea huku nikimuomba Mungu nifike salama, bahati nzuri tulisafiri bila tatizo na kuingia jijini Dar majira ya saa kumi na moja jioni. Baada ya kushuka kwa kweli nilichanganyikiwa nianzie wapi maana jiji lilivyokuwa limejengeka tofauti kubwa na nilipotoka. Kituoni kulikuwa na mabasi mengi na watu wengi, lakini sikutaka kuonesha ugeni kwa kuamini naweza kuibiwa kutokana na taarifa nilielezwa jiji la Dar kuna matepeli wengi. Wakati nikiwaza nifanye nini nilimuona dada mmoja aliyekuwa na mtoto wa kike miaka minne niliyesafiri naye kwenye basi moja. Niliamini anaweza kunisaidia kwani nilikuwa nalingana naye kwa maumbile. “Samahani dada,” nilianza kumsemesha baada ya kumsogelea alipokuwa akiweka mizigo yake vizuri. “Bila samahani.” “Eti dada wewe ni mwenyeji hapa?” “Ndiyo kwani vipi?” alinijibu huku akinitazama. “Tulikuwa kwenye basi moja, nimefika lakini nashangaa simuoni mwenyeji wangu,” nilitengeneza uongo ili nipate msaada wa kuondoka mule ndani kituo cha mabasi ambacho kilinichanganya. “Kwani wewe umetokea wapi?” “Mbeya, lakini safari hii nimeanzia Iringa.” “Ndugu yako anakaa wapi?” “Tandika,” nilijibu sehemu niliyokuwa naifahamu kwani sehemu nilizokuwa nazisikia ni Magomeni, Kinondoni, Masaki, Tandika, Mbagala na Oysterbay. “Namba yake ya simu unayo?” “Nimeitafuta kwenye begi siioni.” “Jamani ndugu yangu sasa itakuwaje?” yule dada aliniuliza kwa sauti ya huruma. “Yaani hata mimi nimechanganyikiwa mtu aniagize na kuahidi atakuja kunipokea halafu asionekane, sasa nitakuwa mgeni wa nani katika jiji hili linalotisha kwa utapeli.” “Umeishawahi kufika hapa?” “Ndiyo mara yangu ya kwanza.” “Mwenyeji wako jina anaitwa nani?” “Koleta.” “Ni mwanamke?” “Eeh dada! Ni rafiki yangu nilisoma naye.” “ Anafanya kazi gani?“ “Ni baamedi.” “Kwani na wewe umekuja kufanya kazi hiyo?” “Hapana, mimi alinieleza kuna kazi za ndani kwa Wahindi,” nilitengeneza mazingira ya ukweli ili nipate msaada. “Mmh! Sasa utafanya nini kwa vile muda umekwenda na mwenyeji wako haonekani?” “Kwa kweli nimechanganyikiwa hata sijui nifanye nini?” “Kwa nini usiende kukaa sehemu ya kupokelea wageni ili umsubiri?” “Dada yangu kama ameshindwa kuja kunipokea kabla gari halijafika atakuja kunitafuta sehemu asiyoijua?” “Kwa hiyo nitakusaidia vipi ndugu yangu?” aliniuliza huku akiwa na maswali atanisaidiaje. “Nilikuwa naomba msaada wa kulala kwako leo ili kesho nijue nifanye nini.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Si umesema wewe ni mgeni hapa jijini?” “Ndiyo.” “Sasa hiyo kesho utafanyaje utarudi kwenu?” “Ni kweli mimi ni mgeni lakini maisha nayajua, nikitulia leo kesho nitajua nifanye nini siwezi kurudi nyumbani, nimekuja kutafuta maisha.” “Mmh! Sawa kwa vile mwanamke mwenzangu na umekuja kutafuta maisha nitakuchukua, mengine yatajulikana baadaye.” Nilishukuru kimoyo kwa kuamini maisha ya Jiji la Dar nitayaweza kwa vile mwanzo wangu ulikuwa mzuri. Ili kumuonesha sina matatizo nilimweleza akodi teksi hadi kwake nitalipa. “Dada unakaa wapi?” “Keko Toroli.” “Ni mbali kutoka hapa?” “Siyo mbali ni daladala moja tu.” “Kwa nini tusichukue teksi?” “Mmh! Ni fedha nyingi.” “Hapana dada nilitalipa mimi.” “Mmh! Sawa.” Alikwenda kuchukua teksi ambayo ilitubeba hadi Keko Toroli, kwa kweli mji wa Dar ulionesha umejengeka pia watu na magari yalikuwa mengi sana tofauti na nilipotoka. Tulifika nyumba aliyopanga ilikuwa chumba cha uani, chumba hakikuwa kikubwa pia hakuwa na vitu vingi, ilionesha na yeye ndiyo alikuwa akianza maisha. Chumbani alikuwa na kitanda cha futi nne kwa sita, jiko la mafuta, la mkaa, ndoo tatu za maji, sufuria chache kwa kweli alikuwa na vyombo vichache sana. “Karibu ndugu yangu haya ndiyo maisha yetu ya Dar,” mwenyeji wangu alinikaribisha. “Mbona kawaida tu.” Nilishukuru yule dada alikuwa na moyo wa upendo kwani hakunifahamu lakini alinipokea vizuri. Huo ndiyo ukawa mwanzo wangu wa kuingia Jiji la Dar na kuanza maisha mapya.

    Kwa vile nilikuwa na malengo yangu niliamini kama nami nitatoa msaada wa chakula kwa mwenyeji wangu, ingenisaidia kujipanga hata kujua anajishughulisha na nini kitu ambacho kitanisaidia kujua cha kufanya. “Samahani dada yangu,” nilimweleza usiku tukiwa kitandani kabla ya kulala. “Bila samahani.” “Nina imani una mtu.” “Una maana gani?” “Mwanaume anayekusaidia kupunguza ukali wa maisha.” “Ndugu yangu yaani maisha ya mjini naishi kiujanjaujanja tu, huyu mtoto hata baba yake simjui.” “Ulimpataje?” “Ndugu yangu kazi zetu za kuzunguka ovyo kutafuta riziki.” “Kazi gani hiyo?” “Kwanza nilipofika nilikuwa mfanyakazi wa ndani, maisha yalikuwa magumu kwani mshahara

    ulikuwa mdogo lakini kazi nzito ndipo nilipompata shoga yangu mmoja niliyetoka naye kijijini na kunivuta kwenye kazi ya ubaamedi ambayo kidogo ilinisaidia.” “ Nimeshasikia kuwa mshahara wake ni mdogo tofauti na kazi yenyewe ya kupigwa na baridi usiku?” “Ni kweli lakini hao mabaamedi wanajenga kupitia kazi hiyo hiyo.” “Wanajenga? Wanajenga vipi?” “Kazi ile unaweza kupata bwana wa kukuoa au kukuhonga fedha nyingi, wengine tunatumia ujanja kuwazidishia bili wateja au kupewa ofa za bia ambazo hatunywi bali tunachukua fedha na maisha yanasonga.” “Mmh! Mimi nina aibu sana kazi hiyo nitaiweza?” “Utaiweza tu, hata mimi nilikuwa hivyo hivyo lakini njaa mbaya inakufanya mtu usichague kazi.” “Hivi nikiwa na fedha kidogo ninaweza kufanya biashara gani ya kuweza kunipatia riziki?” “Kama shilingi ngapi?” “Laki mbili.” “Mmh! Unaweza kufanya biashara ya kununua nguo na vipodozi na kuvikopesha.” “Wateja wapo?” “Wapo, unajua mara nyingi wanawake wa uswahilini huwa hawawezi kulipa mara moja, lakini ukiwapa walipe baada ya mwezi wanaweza kudunduliza na kukulipa.” “Nilikuwa na wazo la kukuomba tuifanye kazi hiyo pamoja ili tuachane na kazi ya baa,” niliamini huenda kazi hiyo ikatukomboa. “Hakuna tatizo.” Tulikubaliana kuifanya biashara ile ambayo niliamini kidogo ina heshima tofauti na ile ya ubaamedi. Kwa vile usiku ulikuwa umekwenda sana tulilala kuitafuta siku ya pili. *** Nilianza kwa kuyabadili maisha ya shoga yangu kwa kufanya biashara ya kukopesha vipodozi na nguo za kike. Nilimshukuru Mungu kutokana na hali ya ukaribu aliyonifanyia shoga yangu aliyekuwa akiitwa Salome au mama Konso. Kutokana na ucheshi wangu niliweza kuzoeleka haraka mtaani, kila mmoja alinipenda. Nilijikuta na wakati mgumu wa kuamua niishi katika dini gani, wazo lilikuwa kurudi katika dini yangu ya zamani. Kwa vile mwenyeji wangu alikuwa muumini mzuri wa Kikristo niliamua kubaki katika dini yangu hiyo mpya. Pamoja na kuwa nilikuwa na fedha nyingi lakini sikutaka kujionesha wala kuzitumia kwa fujo. Niliamua tuhame nyumba ile ya zamani na kwenda kukaa sehemu nyingine, kutoka Keko Toroli tukaenda kukaa Temeke kwa Sokota. Tulihamia kwenye nyumba ambayo ilikuwa na umeme na kununua vitu vya ndani ambavyo viliweza kutuweka katika watu wenye maisha yenye unafuu tofauti na awali nilivyomkuta shoga yangu.

    Nilimshukuru Mungu biashara yetu ilikwenda vizuri mpaka siku moja shoga yangu aliponieleza kuwa amepata bwana wa kukaa naye. Japo jambo lile lilikuwa zuri lakini kwangu lilikuwa pigo, hasa kwa kuzingatia kuwa tumbo langu nalo lilikuwa likikua siku hadi siku. “Ester si kwamba nakukimbia la hasha nami nataka kuishi maisha yangu, hata wewe huwezi kukaa hivi siku zote lazima kuna mtu atajitokeza na kukutaka utaishi naye, kama ulivyonieleza dereva teksi anavyokubembeleza kukuoa na kuwa tayari kuilea mimba yako.” “Sasa ndugu yangu ni heri ungekuwa unakaa karibu, Gongo la Mboto nikishikika itakuwaje?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Usiombe mabaya, ukijisikia tu nijulishe, nitakuja mara moja ndugu yangu.” Sikuwa na jinsi, Salome alihamia Gongo la Mboto kwa bwana?ake ambaye alikutana naye katika biashara zake. Katika vitu alivyonishukuru shoga yangu ni kumbadilisha kutoka katika kutoheshimika mpaka maisha ya kuonekana mtu mbele za watu na hatimaye kupata bwana aliyekubali kukaa naye kama mke na mume. Kwa vile nilikuwa nimeshakuwa mwenyeji maeneo yale, nilipata msichana wa kazi wa kunisaidia kazi ndogondogo za ndani. Ujauzito nao ulianza kuniendesha na kunifanya niwe nyumbani muda mwingi. Kwa vile Salome pamoja na kuwa kwa mumewe alikuwa akifuata biashara na kuzigawa. Siku moja usiku baada ya kazi zangu za asubuhi nilisikia maumivu makali ya tumbo, ukali wa maumivu ulisababisha nipoteze fahamu. Niliposhtuka nilijikuta hospitali na pembeni yangu alikuwepo shoga yangu Salome na msichana wangu wa kazi. Nilipopepesa macho niliona chupa ya damu pembeni yangu niliyokuwa naongezewa. Nilishtuka na kuvuta kumbukumbu zangu baada ya kufanya usafi wa chumbani kwangu na kushikwa na maumivu makali ya ghafla ya tumbo. Baada ya maumivu makali, sikuelewa kilichoendelea mpaka nilipojikuta hospitali. Nikiwa katikati ya lindi la mawazo, Salome alinisemesha kwa sauti ya chini. “Vipi Ester, unajisikiaje?” “Hata sijui nini kinaendelea kwani vipi?” Nilijikuta nauliza kwa vile sikuelewa nilifikaje hospitalini tena nikiwa naongezewa damu. “Nilipigiwa simu na Mere kuwa umeanguka ghafla na huzungumzi huku ukitokwa na damu nyingi. Nilichanganyikiwa na kuja mbio, huwezi kuamini mshtuko nilioupata kutokana na Mere alivyokuwa akizungumza huku akilia, nilichokumbuka ni pochi ya fedha na kuwahi kuja huku. Nilikodi bodaboda mpaka hapa, viatu na khanga nimechukulia kwako. “Shoga kuna kitu gani ulichofanya?” “Kitu gani! Una maana gani kusema hivyo?” nilishindwa kumuelewa anamaanisha nini.

    “Damu niliyokuta imekutoka utafikiri umechinja mbuzi.” “Mungu wangu!” nilishtuka kusikia vile. “Mbona unashtuka?” “Sasa damu zinitoke kama kumechinjwa mbuzi nimefanya nini?” “Kwani ilikuwaje?” Nilimwelezea hali iliyonipata muda mfupi baada ya kumaliza usafi wa chumbani kwangu. “Mmh! Sasa kutokwa na damu nyingi kiasi kile, tena inanuka sana kunatokana na nini?” “Kwani daktari anasemaje?” “Kwa kweli muda mwingi alikuwa akikushughulikia, sikupata muda wa kumuuliza.” “Kwani muda huu ni saa ngapi?” “Saa kumi jioni.” “Mmekula?” “Mbona unauliza kula badala ya afya yako?” “Nina imani toka asubuhi mpo na mimi hospitali?” “Ni kweli, lakini la muhimu ni afya yako.” Mara aliingia daktari na kuja moja kwa moja kwenye kitanda changu. “Pole,” aliniambia kwa sauti ya chini huku akinishika begani. “Asante.” “Unaendeleaje?” “Naweza kusema sijambo, japo sijajua hali yangu kwa vile bado nimelala kitandani.” “Kwa jinsi ulivyokuja na sasa ulivyo hujambo sana.” “Kwani daktari tatizo kubwa ni nini?” “Tumbo.” “Nasikia damu zimetoka nyingi, ujauzito wangu una usalama?” “Upo salama.” “Ooh! Afadhali maana nilikuwa na wasiwasi huenda umetoka.” “Vipi chakula mmemletea?” daktari alimgeukia Salome. “Ndiyo, tumefanya kama ulivyotuagiza.” “Basi mpeni ale kisha apumzike, kesho nina imani atatoka.” Baada ya kusema vile aliondoka na kutuacha chumbani, Salome alikuwa ameniletea mtori. “Mmh! Shoga mtori huu umetengeneza saa ngapi?” “Nimenunua hotelini.” “Mmh! Mzuri sana, wanajitahidi,” nilisema baada ya kupiga vijiko vitatu vya mtori. “Lakini unajisikiaje?” wakati nikiendelea kula Salome aliyekuwa amekaa pembeni yangu aliniuliza akiwa anachezea nywele zangu. “Najiona nipo sawa.” “Pole sana shoga yangu.” “Asante sana, yaani nashukuru sana kwa kuwahi kuja, sijui bila wewe ningekuwaje?”

    “Yote mipango ya Mungu, tushukuru kwa yote aliyoyafanya kwa ajili yetu.” Baada ya kula chakula nilidungwa sindano na kupumzika na kuwaacha Salome na msichana wangu wa kazi wakirudi nyumbani.

    Siku ya pili kabla ya kuruhusiwa kutoka niliitwa ofisini kwa daktari, baada ya kuingia na kutulia, daktari alikuwa akiandika kitu kwenye karatasi kisha akaniita jina langu. “Ester.” “Abee.” “Pole sana.” “Ahsante.” “Umeolewa?” “Hapana.” “Nani mwenye ujauzito?” “Mimi mwenyewe.” “Japo inaonesha hupendi mambo yako kujulikana, nilikuwa nataka kukueleza jambo ambalo lingekuwa vizuri uwe na mwenzako.” “Ni kweli ujauzito wangu hauna baba.” “Umekuja kwa njia ya roho mtakatifu?” “Nilibakwa,” niliamua kukata shauri. “Ooh! Pole sana.” “Ahsante.” “Sasa napenda nikueleze kuwa ujauzito wako umetoka.” “Eti?” nilishtuka. “Pole sana najua itakuuma lakini inaonekana ulikuwa na tatizo la muda mrefu ambalo hukuliwahisha hospitali.” “Mmh! Nimeamini wa moja havai mbili.” “Lakini kwa upande wangu naona mshukuru Mungu kwa kukuondolea kitu ambacho kama kingekuwepo kingekuongezea maumivu ya kubakwa.” “Ni kweli, lakini bado mwanangu angekuwa hana hatia na wala nisingeweza kuwaza kubakwa zaidi ya kumlea, niliamini yeye ni zawadi yangu kutoka kwa Mungu.” “Basi imekuwa bahati mbaya nina imani Mungu atakupatia mwanaume wa halali na watoto wa halali.” “Mmh! Sina budi kukubaliana na yote yaliyotokea nina imani kila kitu ni mapenzi ya Mungu.” “Kwa vile afya yako tokea jana imeendelea vizuri, baada ya matibabu yaliyokwenda vizuri nitakuruhusu ila kama kuna tatizo lolote usisite kurudi hapa haraka, kadi nitakayokupa itakusaidia kukuonesha kuwa ni mteja wetu.” “Ahsante.” “Kwa hiyo sasa hivi unakaa na nani?”

    “Peke yangu.” “Huna mzee?” “Sina, nipo peke yangu.” “Na jamaa aliyekulipia matibabu ni nani yako?” “Nani kanilipia?” nilishtuka kusikia kuna mtu kanilipia gharama zote za matibabu. “Anaitwa Victor.” “Aah! Kumbe ni Victor?” nilishtuka kumsikia ni yeye, kweli yule kaka alikuwa amepania pamoja na kumwekea vikwazo vya kutokuwa pamoja naye, bado alikuwa karibu yangu. “Unamjua?” “Ndiyo.” “Ni nani yako?” “Ni rafiki yangu wa kawaida.” “Kwa hiyo upo singo?” “Ndiyo.” “Huna mtu?” “Sina, mbona maswali mengi?” “Jamani mti wenye matunda si ndiyo unaopigwa mawe.” “Ni kweli, lakini kwa sasa sihitaji mtu.” “Basi ukihitaji nipo Dokta Hashimu.” “Sawa dokta japo sihitaji kwa sasa.” “Hata baada ya miaka kumi, jina langu naomba ulipe upendeleo maalum.” “Tumuombe Mungu.” Baada ya kuruhusiwa nilirudi nyumbani kwa teksi ya Victor aliyekuwa yupo jirani na hospitali. Nilipofika sikuwa na budi kumshukuru Victor kwa ubinaadamu wake. “Ahsante Victor kwa yote uliyonifanyia.” “Kawaida tu Ester, yote nayafanya kwa ajili ya kukuonesha jinsi gani ninavyokuthamini.” “Mungu atakuzidishia.” “Ahsante.” Baada ya kuachana na Victor na Salome kurudi kwake nikiwa kitandani nimejilaza, niliwaza mambo mengi juu ya matukio yote ninayokutana nayo, nilijikuta nikiungana na Dokta Hashimu kuwa ni heri mimba ile imetoka kwa vile sikuitarajia. Moyoni niliamini huenda ndiyo maisha yangu mapya baada ya mateso ya muda mrefu. Kutoka kwa ujauzito hakukuniuma sana, niliona kawaida japokuwa majirani walinipa pole huku wakiniombea kwa Mungu anipatie mtoto wa kuziba pengo lile. Kwa vile Victor alionesha mapenzi ya dhati nilikubali kumkabidhi moyo wangu na kuwa mwanaume wangu wa kwanza nikiwa Dar.

    HaikupatikanaCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Kwa hiyo upo tayari kuninunulia gari mpenzi?” “Ndiyo, lakini mpaka zifike milioni tatu na laki tano ili tupate zuri kama la Muddy, gari lile hata likiwa sokoni lazima mteja alichukue.” “Basi lipo zuri zaidi ya lile tena milioni tatu tu.” “Mmh! Milioni tatu lisiwe ni bodi tu, injini siku mbili tu gari juu ya mawe.” “Kwa nini unasema hivyo?” Victor aliniuliza. “Bei yake mbona ndogo kuliko gari la Muddy?” “Kama nilivyokwambia siwezi kununua kitu kibovu, jamaa anataka kununua gari lingine ndiyo maana analiuza, kwanza halikuwa teksi lilikuwa la kwake la kutembelea, lilikuwa uani kutoka ilikuwa ni siku moja moja, ukiliona kama jipya.” “Mmh! Victor acha kunitia upepo, ina maana taarifa za kuuzwa kwa gari ulikuwa nazo mapema?” “Tena hii ni bahati kama kweli tutalinunua, taarifa alinipa kwa vile mimi ni mtu wangu wa karibu sana, tena ananiamini na aliniomba nimtafutie mteja, hii si kazi ya kwanza hata ile gari ya Rama mimi ndiye nililiuza na kupata laki mbili cha juu. Kwa gari hili alitaka milioni tatu tu, zikizidi zangu.” “Kwa hiyo unataka kuniambia ni zuri kuliko la Muddy?” “Wee toa fedha uone kitu cha ukweli mbona tutawapiga bao,nakuhakikishia ndani ya mwaka mmoja litazaa gari jingine.” “Usiniambie? Lakini si nasikia kuna sijui usajili ili kulifanya kuwa teksi?” “Hiyo hela iliyobaki itamaliza kila kitu.” “Basi mjulishe tunalitaka kabla mtu mwingine hajatokea kuliwahi,” nilijikuta nikipata kimuhemuhe cha kupata gari ili mpenzi wangu asipate manyanyaso, niliamini gari hilo litakuwa la kwetu hata kama hesabu isipotimia hatutagombezana. “Tena nampigia hapa hapa unasikia naweka loud speker ili usikie.” Baada ya kusema vile alimpigia simu mwenye gari ambayo iliita kidogo na kupokelewa upande wa pili. “Haloo Victor vipi?” “Poa Maheb, za saizi?” “Poa, vipi mambo mazuri nini?” “Eeh! Mteja kapatikana.” “Kwa ngapi?” “Kwa kiasi ulichoniambia.” “Cha juu kiasi gani, ili mteja akija nisiharibu mambo?” “Maheb, kumbe wife alikuwa na kibubu chake, tena alitusikia tukilizungumzia gari la Muddy si ndiyo akasema anaweza kulinunua la bei hiyo.” “Acha uongo Victor unafikiri nitataka cha juu chako, kama ningekuwa nakitaka nisingekutajia

    kiasi kidogo kama hicho, nimefanya hivyo kwa vile wewe ni mtu wangu wa karibu sana.” “Haki ya Mungu, tena ninavyozungumza wife yupo pembeni anasikia kila kitu.” “Kwa hiyo anataka lini?” “Eti lini mpenzi?” Victor aliweka simu pembeni na kuniuliza. “Hata leo,” nilimjibu kwa vile fedha zangu nilikuwa naziweka ndani sikuwahi kufungua akaunti ya benki. “Maheb nina imani umemsikia mwenyewe.” “Mmh! Kweli alikuwa na usongo, sasa fanya hivi kwa vile nipo mbali kidogo biashara tuifanye kesho mapema.” “Saa ngapi?” “Asubuhi kuanzia saa mbili mpaka saa nne, saa sita nina safari ya kwenda Zanzibar tena mtakuwa mmenisaidia sana.” “Basi kesho, usiku mwema.” “Hakuna tatizo, nakutakieni na ninyi usiku mwema.” Victor alikata simu na kunigeukia, ilionekana pamoja na kuzungumza bado hakuniamini. “Ester kweli fedha hiyo ipo au unatania, unajua jamaa ni mtu wangu sana ndiye anayenibeba mambo yakienda kombo mjini.” “Mmh! Naona huamini hebu ngoja.” “Nilikwenda kwenye kabati la nguo na kuchukua mfuko wa rambo na kurudi nao kitandani, kisha nilizimwaga fedha juu ya kitanda. Nilimwona Victor macho yakimtoka kama kaona meli barabarani. “Mpenzi zote hizi unaziweka ndani?” “Nani anajua?” “Lakini nyumba inaweza kuungua, kwa nini usiweke benki?” “Kwangu si muhimu kwa vile zipo kwenye hali ya usalama, wewe ulijua kama nina fedha kiasi hiki?” “Hata.” “Basi hesabu ili kesho na wewe uwe bosi.” Victor alizihesabu fedha zote huku akijikuta akirudia zaidi ya mara tano kutokana na kutetemeka na kuzidondosha, kuna wakati alisahau mahesabu. “Victor jamani mbona unanitia aibu, milioni tatu tu umechanganyikiwa je, zingekuwa kumi?” “Siyo kwamba nimechanganyikiwa bali siamini.” “Basi amini mpenzi wangu.” Baada ya kutulia, alizihesabu na kuzikuta zikiwa shilingi milioni tatu na laki mbili. “Zipo sawa.” “Basi toa hizo tatu zingine utamalizia mambo mengine.” Victor baada ya kutoa laki mbili, milioni tatu aliziweka kwenye mfuko kusubiri siku ya pili kwenda kununua gari letu.

    Maskini siku hiyo nilimuonea huruma Victor alikuwa na furaha ya ajabu alinikumbatia kwa furaha, kwake ilikuwa kama miujiza fulani ambayo hakuitegemea.

    Tulilala mpaka siku ya pili ambayo tulikutana na huyo Mwarabu Maheb. Tulichanya mchakato wote wa mauziano uliokwenda vizuri na kukabidshiwa vitu vyote muhimu na kadi ya gari. Baada ya makabidhiano gari likawa letu rasimi. Japo ilikuwa na jila la mwenye gari lilikuwa langu lakini niliamini ile ni yetu. Victor alidizi kunishukuru kwa kumtoa kwenye kazi ya manyanyaso. “Yaani siamini nashukuru sana mpenzi wangu kwa yote uliyonifanyia, sijakueleza ya moyoni lakini nilikuwa na mpango wa kuacha kazi kwani manyanyaso yalizidi. Leo hii na mimi naweza kusimama mbele za watu na kuonekana mtu. Nakuahidi kufanya kazi kwa nguvu zote ili isijutie uamuzi wako wa kununua gari.” “Wala usifike huko mpenzi wangu, usitumie nguvu sana shida yangu si fedha bali uwe na uhuru na kazi yako, pia uifanye kazi bila wasiwasi.” “Nimekuelewa, lakini chetu ndicho kinatakiwa tukihangaikie sana.” “Nimekuelewa.” Huo ndio ukawa mwanzo mpya wa maisha yaliyojaa furaha na faraja kwangu na Victor, nami biashara zangu zilitoka mtoto wa kike kwa muda mfupi nilinenepa na kupendeza machoni mwa watu. Mpenzi wangu naye alifanya kazi kwa bidii iliyoonesha matunda kila wiki tuliweka fedha zaidi ya ile aliyokuwa akipeleka kwa tajiri yake. Ndani ya miezi sita toka tununue gari tuweza kununua kiwanja maeneo ya Tabata Segerea na kukusanya nguvu za ujenzi. Wakati huo niliona ule ndiyo ulikuwa muda mzuri wa mimi kutafuta mtoto baada ya kuridhika na muda nilioamua kupumzika. Kwa vile hali yetu ya maisha ilikuwa imeimalika kwa kipato kuongezeka tulifunga ndoa na kuwa mke na mume, baada ya ndoa ilichukua miezi miwili kushika mimba. Ilikuwa kama inasubiri ndoa kwani nilikuwa nimekwisha kubali kubemba mimba hata bila ya ndoa. Siku zilikatika mambo yenu nayo yalizidi kutunyookea nami nilizidi kumshukuru Mungu ujauzito wangu uliendelea vizuri. Muda ulipotimu nilijifungua salama mtoto wa kike ambaye nilimpa jina la mama yangu mzazi Fatuma kama kumbukumbu yake. Kila mmoja alishangaa mimi mkristo kumwita mwanangu jina la fatuma. Niliwaeleza jina si dini kila mmoja alinielewa. Siku zilikatika maisha nayo yalitunyookea duka nalo lilizidi kupanuka na kuweza kuajili wasichana wawili ambao walifanya kazi vizuri ya kuuza duka kipindi chote nilipokuwa nikimlea mwanangu. Mume wangu baada ya kukusanya fedha ambayo nilichanganya na yangu kidogo kwa ajili ya kuanza ujenzi. Fedha ilikuwa kama milioni nne na nusu ambazo tulipanga kuanzia kunyanyua nyumba, siku mbili kabla ya kuanza mchakato baada ya wapimaji kupima kiwanja na kutueleza mpaka nyumba kusimama ilitakiwa milioni kumi na tano. Kwa vile kwa mwezi tulikuwa na uhakika wa kuingiza zaidi ya laki nne mpaka tano tuliamini nyumba ingesimama taratibu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Usiku wa kuamkia siku tuliyopanga kuanza ujenzi mume wangu alipigiwa simu kuwa kuna gari zuri linauzwa kwa bei ya kutupa ya milioni tatu na laki mbili. Taarifa zile kidogo zilimchanganya Tony na kumuona kuna kitu ninahitaji kumsaidia. “Vipi mpenzi mbona kama habari hizi zimekushtua?” nilimuuliza kwa sauti ya upole. “Ni kweli.” “Kwa nini?” “Isingekuwa tumekubaliana kujenga nyumba tungelinunua, nina imani tukiwa na gari mbili ndani ya miezi sita nyumba itanyanyuka bila kuchukua fedha za dukani.” “Siku zote huwa sipendi kukuona ukiumia kwa jambo linalowezekana kutatulika.” “Sawa, lakini sipendi kila jambo niamue mimi.” “Ndiyo sababu ya kuwa baba wa familia, nina imani kila ukifanyacho kina faida yake.” “Kama ni hivyo basi tulinunue hilo gari litatuongezea kipato.” Siku ya pili tuliongeza teksi ya pili, mume wangu kama kawaida alimtafuta dereva mzuri tena mwenye bidii ya kazi. Miezi mitatu ya kwanza tulianza kujenzi wa nyumba yetu. Niliamini duniani hakuna mwembamba mume wangu alinenepa na kuwa na kitambi alionekana kweli mtu mwenye fedha. Maisha yangu yalivyobadilika sikuamini na mimi nitakuwa mtu wa kufanyiwa kazi hata kuwalipa watu mshahara. Niliamini siri ya maisha aijuae Mungu peke yake, kutokana na mateso niliyopata mwanzo wa maisha yangu niliamini kabisa nilikuwa nikiishi dunia ya peke yangu lakini kumbe penye matatizo makubwa mbele kuna faraja kubwa.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog