Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

DEAD LOVE ( PENZI LILILOKUFA ) - 4

 





    Simulizi : Dead Love ( Penzi Lililokufa )

    Sehemu Ya Nne (4)



    “Si naongea na wewe Karen?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sijui jamani mpenzi wangu, labda walinijua kipindi cha nyuma lakini sasa hivi nimekuwa mtu mpya kwa hiyo usijali,” alisema Karen na kumshika begani Abdallah, akashusha pumzi ndefu na kuamua kupuuzia kila kitu.

    Walifika nyumbani ambapo walianza kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu maisha yao ya baadaye na jinsi watakavyokuwa wanasaidiana kuhakikisha Karen anaondokana kabisa na utumiaji wa madawa ya kulevya.

    “Leo nimezaliwa upya Abdallah, nakuahidi nitakuwa mwanamke mwema sana mpaka mwenyewe ushangae. Miongoni mwa wanaume waliopata bahati kuwa na wanawake wazuri, basi na wewe jihesabu,” alisema Karen kwa sauti ya chini huku akionesha kumaanisha kile alichokisema.

    Maneno hayo yalionekana kumfariji sana Abdallah, akamkumbatia kwa nguvu na kumwagia mvua ya mabusu. Licha ya kasoro nyingi alizokuwa nazo Karen, Abdallah alitokea kumpenda mno na hakuwa tayari kukata tamaa mpaka aone mwisho wa msichana huyo.

    Kama isingekuwa mapenzi ya dhati, pengine huenda angeamua kuachana naye mapema kabisa hasa pale alipomuambukiza gonjwa la zinaa lakini kwake ilikuwa tofauti.

    Alimshuhudia kwa macho yake akifanya biashara ya ukahaba na baadaye akagundua kuwa kumbe pia alikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya lakini bado aliendelea kujipa moyo kwamba ipo siku Karen atabadilika na kuwa mwanamke bora.

    Maisha yaliendelea, Karen akahamia kabisa nyumbani kwa Abdallah ambapo walikuwa wakiishi pamoja kama mume na mke japokuwa hawakuwa wameoana kihalali. Kila siku Abdallah alikuwa akihakikisha lazima Karen aende Hospitali ya Mwananyamala kunywa dawa ya methadone.

    Kutokana na kuzingatia vizuri dozi pamoja na maelekezo mengine aliyokuwa amepewa, ikiwemo kufanya mazoezi kila siku, kula chakula bora, kunywa maji mengi ya kutosha na kupata muda wa kupumzika, ndani ya kipindi kifupi tu Karen alikuwa amebadilika mno.

    Kama ungekutana naye na kuambiwa kwamba huyo ndiye Karen aliyekuwa anafanya kazi ya uchangudoa na kutopea kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, usingeweza kuamini kabisa. Alibadilika mno, ngozi ya mwili wake ilitakata na kunawiri vizuri, uzuri wa sura na umbo lake ukazidi kuongezeka, jambo lililompa furaha kubwa Abdallah.

    Wakati mwingine alikuwa akimtazama msichana huyo, haamini kama kweli yupo kwenye himaya yake. Akili yake ilitulia sana, ule utoro na uzembe aliokuwa akiufanya kazini, uliisha kabisa, maelewano na viongozi wake kazini yakazidi kuimarika kwani sasa alikuwa akifanya kazi kwa kujituma na kwa ufanisi mkubwa.

    Siku kadhaa baadaye, aliongezewa mshahara kazini kwake huku bosi wake akimpa moyo wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kumuahidi kuwa akiendelea hivyo, atapandishwa cheo na kuzidi kuongezewa mshahara.

    Hakuna kipindi ambacho Abdallah aliishi kwa amani na furaha kama hicho, kila kitu chake kilikuwa kikifanikiwa kwa kishindo. Kufanikiwa kumbadilisha Karen na kuishi naye vizuri, ilikuwa ni sawa na kufungua milango ya riziki.

    Mapenzi kati yao yalizidi kushamiri, Karen akawa anafanya kazi zote anazotakiwa kufanya mke wa mtu, kuanzia kumfulia nguo Abdallah, kuzinyoosha, kuzipanga vizuri kabatini, kumuandalia chakula kizuri na kumhudumia kwa kila kitu.

    Abdallah alijiona kama mfalme, hadhi yake ikazidi kupanda kwani kila muda alikuwa akionekana kuwa nadhifu na mtulivu, hali iliyosababisha watu wengi wazidi kumheshimu.

    “Kupendwa ndiyo huku kipenzi changu, lazima nikuoe uwe mke wangu halali,” alisema Abdallah jioni moja ya wikiendi, akiwa amekaa ufukweni na Karen, wakipunga upepo huku wakicheza michezo mbalimbali kwa furaha. Hakuna ambaye hakuwaonea wivu alipowatazama kwa jinsi walivyokuwa wanapendana na kupendezana.

    Uzuri wa Karen ulizidi kuwa tishio, kila alipokuwa anapita ilikuwa ni lazima nyuma aache gumzo kubwa. Hata wale wanaume ambao walishawahi kukutana nao kipindi akifanya biashara yake ya uchangudoa, walikuwa wakimshangaa kwani alikuwa amebadilika mno.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku zilizidi kusonga mbele, maisha yakizidi kuwanyookea. Kwa kuwa kwa kipindi chote hicho Karen alikuwa akikaa tu nyumbani, Abdallah alimpa wazo jipya.

    “Unaonaje ukienda kusomea kozi yoyote chuoni ili kesho na keshokutwa na wewe uwe na kazi yako?” alisema Abdallah, wazo ambalo lilimfurahisha sana Karen. Kwa kipindi kirefu alikuwa akitamani sana kusoma ili aje kuwa na kazi yake lakini hilo halikuwezekana kwani hakukuwa na mtu wa kumsaidia.

    Kutokana na furaha aliyokuwa nayo, alishindwa kuyazuia machozi yasimtoke na kuulowanisha uso wake. Akamkumbatia Abdallah kwa nguvu huku akiendelea kutokwa na machozi ya furaha. Ndoto zake zilizokuwa zimezimika kwa kipindi kirefu, sasa zilianza kufufuka upya.

    Kwa kuwa kipato cha Abdallah alichokuwa analipwa kazini kwake kilikuwa kikubwa, walikubaliana kwamba Karen aende kusomea kozi ya Hotel Management and Tour Guiding (Usimamizi wa Hoteli na Kuongoza Watalii), mipango ya kuanza kutafuta chuo ikaanza ambapo siku mbili baadaye, Abdallah alirudi nyumbani akiwa na fomu ya kujiunga na Chuo cha Planet Link College kilichokuwa Mwenge jijini Dar es Salaam.

    Furaha aliyokuwa nayo Karen siku hiyo, ilizidi siku zote katika maisha yake, muda wote akawa anamkumbatia Abdallah na kumwagia mvua ya mabusu.



    Aliamini kurudi kwake shule kutayabadilisha mno maisha yake.

    Siku kadhaa baadaye, Karen alianza masomo, Abdallah akajitahidi kumpatia kila kitu muhimu kwa ajili ya chuo, jambo lililozidi kumpa furaha msichana huyo. Kutokana na uzuri wake, ndani ya kipindi kifupi tu tangu aanze chuo, tayari alikuwa gumzo, kila mtu akiuzungumzia uzuri wa kipekee wa msichana huyo.

    Wanaume wakware nao hawakuwa nyuma, kila mmoja kwa wakati wake akawa anajaribu kumtongoza msichana huyo lakini mwenyewe kwa sababu alishaamua kubadilika, hakuwa na muda tena. Penzi lake aliamua kumkabidhi Abdallah pekee baada ya kuwa amehangaika sana na dunia.

    Hata wanaume walipokuwa wakitumia njia mbalimbali kumlaghai, mwenyewe alikuwa akiwapuuza kwani hakukuwa na kitu kipya kwenye maisha yake, kama starehe alishazifanya sana, anasa ndiyo usiseme. Akili zake zote alizielekeza kwenye masomo kwani hilo ndiyo jambo pekee aliloamini linaweza kuyabadilisha maisha yake.

    Maisha yalizidi kusonga mbele, Karen akiwa anasoma huku mapenzi yake na Abdallah yakiwa yamekolea kisawasawa. Kwa jinsi walivyokuwa wanaishi kwa upendo, ungeweza kudhani wawili hao walioana miaka mingi iliyopita.

    Kwa upande wa Abdallah, naye aliendelea kuchapa kazi kwa moyo mmoja kazini kwao. Kama alivyokuwa ameahidiwa, akapandishwa cheo na kuzidi kuongezewa mshahara, jambo lililomfurahisha sana.

    “Nyota zetu zinaendana mpenzi wangu, yaani sasa hivi kila ninachokigusa kinabadilika na kuwa almasi,” Abdallah alimwambia Karen jioni moja wakiwa wanapunga upepo wa bahari, kwenye Ufukwe wa Msasani, mahali ambapo mara kwa mara Abdallah alikuwa akipenda kwenda na mpenzi wake huyo.

    “Kweli kabisa mpenzi wangu, maisha yangu yamebadilika sana baada ya kukutana na wewe, yaani muda mwingine nahisi kama nipo kwenye ndoto, naomba usiniache ‘habi’ wangu, nakupenda sana mwenzio.”

    “Siwezi kukuacha Karen, kama nimeweza kukuvumilia kwa kipindi chote hicho mpaka sasa umebadilika namna hii, kwa nini nikuache? Nakupenda sana, wewe ndiyo mwanamke wa maisha yangu,” alisema Abdallah kwa sauti ya kubembeleza.

    Japokuwa kulikuwa na watu wengi ufukweni jioni hiyo, wawili hao hawakuona aibu kukumbatiana na kugusanisha ndimi zao, wakawa wanaelea kwenye ulimwengu mwingine huku wanaume wakware waliokuwa eneo hilo wakimuonea wivu Abdallah kutokana na uzuri aliokuwa nao Karen.

    Waliendelea na mchezo huo kwa muda mrefu, mithili ya njiwa aliyekuwa akiyalisha makinda yake. Baadaye waliinuka na kwenda kuogelea baharini, huku wakicheza na kufurahi pamoja. Kila mmoja alishasahau kabisa matatizo aliyowahi kupitia siku za nyuma.

    Siku hiyo ilipita, furaha, amani na mapenzi ya dhati vikazidi kuyatawala maisha yao. Miezi kadhaa baadaye, Karen akiendelea na masomo, asubuhi moja alitokewa na jambo lililowapa hofu wote wawili. Wakati wakipata kifungua kinywa, ili Karen aende chuoni na Abdallah aende kazini kwake, msichana huyo alianza kutapika mfululizo.

    “Umepatwa na nini mpenzi wangu,” alisema Abdallah huku akimsaidia Karen ambaye tayari alishachafua nguo alizokuwa amevaa.

    “Naskia kichefuchefu kika...” hakumalizia kauli yake, akawa anaendelea kutapika mfululizo. Awali, wote wawili walihisi huenda msichana huyo amepatwa na malaria au homa kali, ikabidi Abdallah apige simu kazini kwao kuomba ruhusa ya saa chache kwa ajili ya kumpeleka Karen hospitali.

    Kwa kuwa jirani na walipokuwa wanaishi kulikuwa na kituo kidogo cha afya cha mtu binafsi, wawili hao walienda kwa ajili ya kumpima Karen ili kubaini kilichokuwa kinamsumbua. Hata hivyo, baada ya kufika na kumweleza daktari alivyokuwa anajisikia na baadaye kuchukuliwa vipimo, Karen hakubainika kuwa na tatizo lolote kiafya.

    “Mara ya mwisho uliziona lini siku zako za hedhi?” daktari alimuuliza Karen baada ya kuangalia majibu yake, swali hilo likawafanya msichana huyo na Abdallah watazamane. Siku nyingi zilikuwa zimepita bila msichana huyo kuona siku zake za hedhi, jambo ambalo halikuwa kawaida.

    Alipomjibu daktari, aliwashauri wapime pia na ujauzito, wakafanya hivyo kisha wakatoka na kwenda kukaa kwenye benchi, kusubiri majibu. Muda mfupi baadaye, daktari aliwaita.

    “Vipimo vinaonesha una ujauzito wa mwezi mmoja,” alisema daktari, kauli iliyomfanya Karen ainuke kwa kasi pale alipokuwa amekaa huku akipiga kelele na kumrukia Abdallah mwilini. Wakakumbatiana kwa furaha huku kila mmoja akiwa haamini.

    Kwa jinsi walivyokuwa wanapendana, hiyo ilikuwa ni habari njema mno kwao. Hawakutaka kuendelea kukaa tena hospitalini hapo, wakaondoka huku kila mmoja akiwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake, wakarudi nyumbani kwao, kila mmoja akichekacheka kama mwendawazimu.

    Huo ukawa mwanzo wa ukurasa mwingine wa maisha yao ya kimapenzi, Abdallah akazidi kumpenda msichana huyo huku akimdekeza mno, jambo lililomfanya Karen ajione ni mwanamke wa kipekee chini ya jua.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa kuwa bado ujauzito ulikuwa mdogo, walikubaliana aendelee na masomo kama kawaida mpaka utakapokuwa mkubwa ambapo atasimama kwa muda mpaka atakapojifungua.

    Siku zilizidi kusonga mbele, mapenzi yao yakiwa yameshamiri kuliko kawaida. Hata hivyo, kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele, mahudhurio ya Karen kwenda kupata dozi ya methadone hospitalini yalianza kulegalega bila Abdallah kujua.

    Mwisho akaamua kuacha kabisa ingawa bado alikuwa akimdanganya Abdallah kwamba anaendelea na dozi kama kawaida. Ile hali ya kuteseka na ‘arosto’ ikaanza upya kumrudia Karen.



    Baada ya kuona anateseka sana na arosto, Karen aliamua kwenda kutafuta madawa ili avute japo kidogo kuondoa maumivu makali aliyokuwa anayahisi kwenye kila kiungo cha mwili wake kiasi cha kumfanya awe anatetemeka sana.

    Alitoka bila hata kumpa taarifa Abdallah ambaye alikuwa kazini akiendelea na majukumu yake ya kawaida na kukodi Bajaj iliyompeleka mpaka Kinondoni. Kwa kuwa alikuwa akifahamu sehemu zote anazoweza kupata madawa hayo kwa urahisi, haikumuwia vigumu.

    Akafanikiwa kupata kete kadhaa alizorudi nazo mpaka nyumbani kwake na kujifungia milango yote kisha akajidunga kwa kutumia bomba la sindano alilolinunua wakati akirudi kuchukua madawa hayo, Kinondoni.

    Muda mfupi baadaye, tayari alikuwa mtu mwingine tofauti kabisa, akielea kwenye ulimwengu wa peke yake. Kama kawaida yake, baada ya ‘kubembea’ sana, alipitiwa na usingizi mzito, akalala palepale alipokuwa amekaa wakati akijidunga madawa hayo.

    Alikuja kuzinduka muda ukiwa umeshaenda sana, alipotazama saa ya ukutani alishangaa kugundua kuwa tayari ilishatimu saa kumi na moja za jioni. Harakaharaka akaamka na kuficha ushahidi wote kwani alijua muda si mrefu Abdallah atarejea kutoka kazini.

    Akaenda bafuni kujimwagia maji kisha akarudi na kuanza kujipamba ili isiwe rahisi kwa Abdallah kugundua chochote. Kweli alifanikiwa kwani Abdallah aliporejea muda mfupi baadaye, hakugundua chochote.

    Tofauti yake ni kwamba alichangamka kuliko siku nyingine, muda wote tabasamu pana likiwa limeupamba uso wake. Siku hiyo ilipita bila Abdallah kugundua chochote, kesho yake asubuhi akawahi kuamkia na kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini.

    “Leo huendi chuo?” Abdallah alimuuliza Karen baada ya kumuona anazidi kuvuta shuka wakati muda wa kwenda chuo ulikuwa umefika. Akadanganya kwamba alikuwa hajisikii vizuri kutokana na ujauzito wake.

    “Basi pumzika kipenzi changu, usiende popote,” alisema Abdallah huku akimbusu msichana huyo tumboni kama alivyokuwa akifanya mara kwa mara baada ya kugundua kuwa tayari alikuwa mjamzito.

    Abdallah aliendelea kujiandaa kisha akaondoka na kumuacha Karen amelala. Muda mfupi baadaye, Karen naye aliamka na kwenda kujifungia milango yote kwani tayari alishaanza kuteswa na arosto. Kwa kuwa kete za madawa ya kulevya alizochukua jana yake hakuwa amezimaliza, aliamua kujidunga tena asubuhi hiyohiyo.

    Akachukua bomba la sindano na kujichoma kwenye mshipa mkubwa uliokuwa kwenye mkono wake wa kushoto. Muda mfupi tu baadaye, tayari alikuwa akielea kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa baada ya kujidunga madawa hayo ya kulevya.

    Muda mfupi baadaye, alipitiwa na usingizi mzito kama ilivyokuwa jana yake. Alipokuja kuzinduka, tayari ilikuwa ni saa kumi za jioni, akaenda kuoga na kuficha ushahidi wowote ili Abdallah akija asijue chochote.

    Taratibu akajikuta akirudi kulekule kwenye janga hatari la matumizi ya madawa ya kulevya. Jitihada zote alizofanya Abdallah kumsaidia mpaka akaanza kutumia dozi ya dawa ya methadone, ilikuwa sawa na sifuri japokuwa Abdallah mwenyewe hakuwa akijua chochote.

    Siku iliyofuatia, Karen hakwenda tena chuoni na baada ya Abdallah kuondoka tu, alijiandaa kwa safari ya kuelekea tena Kinondoni kutafuta madawa ya kulevya kwani tayari alishamaliza kete zote.

    Fedha za matumizi alizoachiwa na Abdallah, zote alizitumia kununulia kete za madawa hayo kwani alitaka achukue ya kumtosha siku kadhaa. Akarudi nyumbani ambapo kazi iliendelea kama kawaida.

    Aliendelea kubadilika kitabia taratibu baada ya kuwa madawa hayo yameshamuingia mwilini kiasi cha kutosha, kibaya zaidi akawa anatumia dozi kubwa kuliko ilivyokuwa kipindi cha kwanza kabla hajaanza matibabu ya dawa ya methadone.

    “Mbona siku hizi unakuwa unachokachoka sana mpenzi wangu? Chuo huendi tena halafu hata rangi ya ngozi yako imeanza kubadilika, una nini?” Abdallah alimuuliza Karen siku moja baada ya kuanza kuona mabadiliko makubwa kuanzia kwenye tabia na mwonekano wake.

    “Huyu mtoto wako tumboni ndiye anayesababisha yote haya,” alisema Karen huku akilishika tumbo lake na kumfanya Abdallah aamini alichokuwa anamwambia. Hakuwa akijua kwamba mwenzake tayari amesharudia tena matumizi ya madawa ya kulevya.

    Karen naye aliendelea kufanya jambo hilo siri, akawa anatoka mara kwa mara bila Abdallah kujua chochote na kwenda kununua madawa hayo. Fedha alizokuwa anapewa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, zote zikawa zinaishia kwenye madawa hayo na kwa kuwa safari hii alikuwa akitumia dozi kubwa zaidi, fedha zikawa hazitoshi.

    Akaanza tabia nyingine ya kuwa anachukua vitu vya thamani ndani ya nyumba hiyo na kwenda kuviuza kwa bei ya hasara ili apate fedha za kuongezea madawa hayo ya kulevya. Alianza kwa kuuza simu zake mbili za bei mbaya alizokuwa amenunuliwa na Abdallah kama zawadi.

    Alipoulizwa akasingizia kwamba zimeibiwa na vibaka wa mtaa huo. Abdallah akamuamini msichana huyo lakini kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele, ndivyo vitu vya thamani vilivyokuwa vinazidi kupotea ndani ya nyumba hiyo katika mazingira ya kutatanisha.

    Abdallah hakutaka kuwa anamhoji sana kwa sababu aliamini hali yake ya ujauzito ndiyo inayomsumbua mpenzi wake huyo kiasi cha kukosa umakini na kusababisha vitu viwe vinapotea hovyo. Wala hakuhisi kabisa kwamba Karen alikuwa akimfanyia uhuni.

    Kutokana na kuendelea kutumia dozi kubwa ya madawa hayo wakati akiwa mjamzito, mimba yake iliharibika kabla hata haijafikisha miezi mitatu na kusababisha msichana huyo atokwe na damu nyingi sana.

    Abdallah alipompeleka hospitali, vipimo vilionesha kuwa tayari ujauzito umeharibika, jambo ambalo lilimuumiza mno Abdallah moyo wake, akajikuta akishindwa kuyazuia machozi yasimtoke na kuulowanisha uso wake.



    Hizo zilikuwa ni habari mbaya sana kwake hasa ukizingatia jinsi alivyokuwa akimpenda msichana huyo na kutamani siku zisonge mbele haraka ili amzalie mtoto mzuri kama yeye.

    Machozi yalizidi kumtoka kwa wingi huku Karen akiwa amejiinamia pembeni na kujikausha huku naye akijifanya kuwa na huzuni. Kwa jinsi alivyokuwa anatumia dozi kubwa ya madawa ya kulevya, ilikuwa ni lazima ujauzito huo utoke, jambo ambalo hata mwenyewe alikuwa akilijua.

    Baada ya kuhuzunika na kutokwa machozi mengi, Abdallah alimfuata tena daktari akitaka kufahamu chanzo kilichosababisha mkewe atokwe na ujauzito huo.

    Kwa kuwa vipimo vya awali vilishaonesha kuwa msichana huyo alikuwa na kiwango kikubwa cha madawa ya kulevya katika mwili wake, alijishauri kama amueleze ukweli Abdallah au asimamie maadili ya kazi yake ambayo yanaeleza kuwa ugonjwa ni siri kati ya mgonjwa mwenyewe na daktari tu.

    “Kwani ni nani yako huyu mgonjwa?”

    “Ni mke wangu.”

    “Mkeo? Mmeshafunga ndoa? Maana mnaonekana bado vijana wadogo.”

    “Hatujafunga lakini tupo kwenye maandilizi ya kufanya hivyo,” Abdallah alimwambia daktari huyo na baada ya kuona anazidi kushikilia msimamo wake, aliamua kutumia ule usemi wa wahenga kwamba penye uzia penyeza rupia.

    Alitoa noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi na kumshikisha daktari huyo na kumtaka amdokeze sababu iliyofanya mimba ya mpenzi wake huyo iharibike. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa kuwa tayari alishapewa kitu kidogo, ilibidi amueleze ukweli kwamba Karen alikutwa na kiwango kikubwa cha madawa hatari ya kulevya kwenye damu yake na hiyo ndiyo sababu ya mimba hiyo kuharibika.

    “Mungu wangu, Karen amerudia kutumia madawa ya kulevya?” Abdallah alisema kwa sauti ya juu, ikabidi daktari huyo aanze kumhoji kama alikuwa anafahamu kwamba mpenzi wake anatumia madawa ya kulevya.

    Akamueleza kila kitu kuanzia jinsi alivyomgundua kwa mara ya kwanza kisha jitihada alizoanza kuzifanya mpaka alipompeleka hospitali kuanza dozi maalum ya methadone ili kumaliza kabisa tatizo lake la uteja.

    Daktari huyo naye alimpa ushauri kwamba kama alishawahi kutumia methadone lakini amerudia tena, ilitakiwa juhudi za makusudi kumsaidia kwani vinginevyo ambacho kingetokea baadaye ni msichana huyo kuzidi kuongeza dozi kadiri siku zinavyosonga mbele na mwisho kuishia kujiovadozi na kufa.

    “Inatakiwa umsaidie kwa lazima, hata ikibidi kutumia nguvu fanya hivyo kwani kinachofuata ni kifo tu, madawa ya kulevya ukiyarudia kwa mara ya pili huwa ni hatari sana, lazima ufe,” alisema daktari huyo huku naye akionesha kumuonea huruma Abdallah.

    Alimpa ushauri wa kujikaza na kwenda kuzungumza na mpenzi wake huyo kwa upole kuhusu suala hilo. Pia akamsisitiza kuwa ahakikishe anampeleka hospitali mara kwa mara kwa ajili ya kusafishwa tumbo lake baada ya mimba hiyo kuharibika, jambo ambalo Abdallah alilikubali.

    Akatoka mpaka nje ambako Karen alikuwa amekaa, akionesha kutojali kuhusu chochote kilichotokea. Alipomuona Abdallah anakuja, alivaa uso wa huzuni na kujifanya anasikitika sana.

    Abdallah alienda na kumchukua bila kumsemesha chochote, wakatoka hadi nje ambapo walipanda Bajaj na kuondoka kuelekea duka la madawa kununua baadhi ya dawa walizoelekezwa kisha kuelekea nyumbani kwao.

    Njia nzima hakuna aliyemsemesha mwenzake chochote, ukimya ulitawala mpaka walipofika nyumbani kwao. Kwa kuwa Abdallah alikuwa na hasira kali dhidi ya msichana huyo, hakutaka kuzungumza naye chochote kwanza, akangoja hasira zake zipungue.

    Kwa muda wote huo aliendelea kumhudumia kwa upole kama hakuna chochote kilichotokea, akahakikisha amekunywa dawa zote alizoandikiwa hospitalini kisha akamtafutia chakula. Wakala pamoja na kwenda chumbani kupumzika kwani kila mmoja alikuwa amechoka sana.

    Muda mfupi baadaye, Karen alipitiwa na usingizi mzito lakini Abdallah bado hakuweza kupata hata lepe la usingizi, akawa anaendelea kufikiria kwa kina juu ya nini cha kufanya. Ghafla alipata wazo la kuutumia muda huo kupekua ndani ya nyumba hiyo kama anaweza kupata ushahidi kwamba ni kweli Karen alikuwa amerudia matumizi ya madawa ya kulevya.

    Kwa kuwa walishaishi pamoja kwa muda sasa, Abdallah hakupata shida kujua mahali msichana huyo anakoficha vitu vyake ambavyo hataki mtu mwingine avione.

    Baada ya kupekua huku na kule, hatimaye alifanikiwa kukuta bomba la sindano ambalo ndilo msichana huyo alilokuwa akilitumia kujidunga na kete kadhaa ambazo bado zilikuwa hazijatumika pamoja na mabaki ya kete nyingine nyingi ambazo tayari zilikuwa zimeshatumika.

    Mpaka hapo alikuwa na uhakika kwamba Karen hawezi kumbishia chochote kwani alikuwa na ushahidi wote mkononi. Akarudi kitandani na kumsubiri msichana huyo azinduke kutoka usingizini ili aanze kumhoji juu ya kilichotokea.

    Alipoona anachelewa kuzinduka kutoka usingizini, ilibidi amuamshe na kumtaka aende kuoga kwanza kisha akirudi kuna jambo muhimu anataka wajadiliane.

    “Kwani kuna nini jamani?”

    “Wewe fanya kama nilivyokwambia,” alisema Abdallah huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara. Karen akafanya kama alivyoambiwa ambapo muda mfupi baadaye alirejea kutoka bafuni, akapatwa na mshtuko mkubwa baada ya kuona Abdallah alikuwa ameweka mezani ushahidi wote kuonesha kwamba bado msichana huyo alikuwa akiendelea kutumia madawa ya kulevya.

    “Nataka ukae hapa na kunipa maelezo ya kila kitu kuhusu huu upumbavu wako unaoufanya,” alisema Abdallah huku akionesha kupandwa na jazba, Karen akaanza kutetemeka kwani hakujua nini itakuwa hatma yake.



    “Nisamehe mpenzi wangu.”

    “Nikusamehe? Hivi una akili timamu wewe? Mimi nahangaika kwa ajili yako lakini mwenyewe huoneshi kujionea huruma hata kidogo. Nini kimekufanya urudie tena kutumia madawa ya kulevya? Unakosa nini kwangu?” alisema Abdallah kwa jazba huku mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio kuliko kawaida.

    Karen alikuwa amemtibua mno na kumfanya ahisi kwamba huenda alifanya chaguo lisilo sahihi kumpenda. Hakuwahi kudhani kwamba msichana huyo anaweza kurudia tena kutumia madawa ya kulevya hasa kutokana na jinsi alivyokuwa anamdekeza, akihakikisha anapata kila alichokuwa anakihitaji.

    Karen alijiinamia chini, Abdallah akawa anaendelea kumfokea kwa hasira, hali iliyosababisha msichana huyo aanze kutokwa na machozi. Aliendelea kumsema kwa muda mrtefu, Karen akawa anajifanya anajutia sana makosa aliyoyafanya.

    Hata hivyo, ilikuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa, tayari sumu ya madawa ya kulevya ilikuwa imeshaingia upya kwenye mwili wake na alikuwa tayari kufanya chochote kuhakikisha anapata madawa hayo kila siku ili kukabiliana na arosto ambayo sasa ilikuwa ikimsumbua kama mwanzo kabla hajaanza kutumia Methadone.

    Abdallah alipoona msichana huyo anaonesha kujutia alichokifanya, alianza kuzungumza naye kwa upole, akamueleza jinsi alivyoumizwa na kitendo cha yeye kutumia madawa ya kulevya wakati alikuwa anajua fika kwamba ana ujauzto wake.

    “Nisamehe mpenzi wangu, ni shetani tu alinipitia, nakuahidi nikipona tu nakubebea mimba nyingine na kutimiza ndoto zako za siku nyingi za kuitwa baba,” alisema Karen. Kwa kuwa Abdallah alikuwa na mapenzi ya dhati na msichana huyo, alimuamini alichokisema.

    Akaendelea kumsisitiza kuwa ni hatari sana kwake kutumia madawa ya kulevya baada ya kuwa alishaanza kutumia Methadone, Karen akawa anaitikia kila kitu kwani alichokuwa anataka, ni mazungumzo hayo kufikia mwisho tu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya Abdallah kuamini kwamba msichana huyo alikuwa amemuelewa, alichukua yale madawa yaliyokuwa yamebaki pamoja na bomba la sindano alilokuwa analitumia msichana huyo kujidunga na kutoka navyo nje, akaenda kuvitupa kwenye choo cha shimo kwenye nyumba ya jirani, akarudi ndani na kumkuta Karen anaendelea kujiliza ili kumuaminisha kwamba na yeye ameguswa sana na kilichotokea.

    Alifanikiwa kumhadaa kwani zile hasira zote alizokuwa nazo Abdallah ziliyeyuka kama theluji juani na sasa wakawa wanazungumza mazungumzo ya kawaida. Usingeweza kudhani ni Abdallah huyohuyo ndiye muda mfupi uliopita alikuwa akitaka kupasuka kwa hasira, ama kweli mapenzi ni kama upofu.

    Siku hiyo ilipita, kesho yake Abdallah akajiandaa kwa ajili ya kuelekea kazini huku Karen akibaki nyumbani.

    “Tafadhali naomba usitoke kwenda sehemu yoyote, hakikisha unakula vizuri na kunywa dawa,” alisema Abdallah, msichana huyo akamsisitiza kwamba kutokana na jinsi alivyokuwa anajisikia maumivu makali ya tumbo baada ya ujauzito wake kuharibika, asingeweza kwenda sehemu yoyote.

    Abdallah alitoka na kuelekea kazini lakini muda mfupi tu baadaye, Karen alijiandaa harakaharaka na kutoka kuelekea tena Kinondoni kwani tayari arosto ilishaanza kumsumbua na hakuwa na uwezo wa kuhimili mateso aliyokuwa anayapata.

    Alipotoka nje, hakutaka kutembea mpaka kituo cha daladala, akaenda kwenye maegesho ya Bajaj ambapo alipanda kwenye Bajaj ya yule kijana aliyewapeleka hospitalini siku kadhaa zilizopita.

    Kwa kuwa Karen alikuwa akikutana na wanaume wengi, wala hakumkumbuka dereva huyo wa Bajaj ingawa mwenyewe alikuwa akimkumbuka vizuri, akapanda na kumuelekeza sehemu ya kumpeleka, muda mfupi baadaye wakawa tayari wapo barabarani wakielekea Kinondoni.

    Baada ya kufika, Karen alimlipa dereva huyo fedha zake kisha akashuka na kuelekea moja kwa moja kwenye mtaa aliokuwa akinunua madawa hayo. Kutokana na jinsi alivyokuwa amebanwa na arosto, aliona akisubiri mpaka arudi kwake, atakuwa amechelewa sana.

    Akamlipa muuzaji fedha zake kisha akaomba ajidunge hapohapo. Kwa kuwa kulikuwa na sehemu ambayo watumiaji wengine wengi wa madawa ya kulevya walikuwa wakiitumia kujidunga, muuzaji huyo alimuelekeza ambapo muda mfupi baadaye, tayari Karen alikuwa ameshajidunga.

    Akawa ‘anabembea’ kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa, baadaye akapitiwa na usingizi. Aliendelea kulala eneo hilo kwa muda mrefu mpaka baadaye madawa hayo yalipopungua nguvu, akainuka na kuagiza kete nyingine kadhaa ambazo aliondoka nazo na kuianza safari ya kuelekea Mikocheni.

    Kwa jinsi alivyokuwa amelewa baada ya kujidunga madawa hayo, haikuwa rahisi kwake kujificha. Kila mtu aliyekuwa akipishana naye, alikuwa akigeuka na kumtazama mara mbilimbili.

    Lilikuwa ni jambo la ajabu sana, msichana mrembo kama Karen, ambaye alionesha kutoka familia bora, kuonekana mchana wa jua kali akiwa amelewa madawa ya kulevya kiasi hicho! Alitia huruma.

    Ilimchukua muda mrefu sana mpaka kufika Mikocheni, kutokana na kuzidiwa na madawa, wala hata hakuwa na akili ya kukodi Bajaj, aliposhuka kwenye daladala alianza kutembea huku akipepesuka kuelekea nyumbani kwake. Watu wote waliokuwa wamezoea kumuona akiwa ameongozana na Abdallah, wakawa wanamshangaa wakiwa ni kama haamini.

    “Yule demu teja, tena kuna kipindi alikuwa anafanya biashara ya uchangudoa Manzese na Afrika Sana. Namsikitikia sana yule jamaa anayeishi naye, eti anajifanya anampenda kinoma wakati demu mwenyewe alishashindikana, atamuua kwa ngoma,” kijana mmoja alikuwa akiwaambia wenzake, waliokuwa wamekusanyika kwenye kituo cha Bajaj, wakimshangaa msichana huyo.

    Mwenyewe wala hakuwa na habari, aliendelea kujikongoja mpaka alipofika ndani, akajitupa kwenye sofa na muda mfupi baadaye, tayari alikuwa amepitiwa na usingizi mzito.

    Abdallah akiwa hana hili wala lile, baada ya kumaliza majukumu yake ya kikazi alirejea nyumbani. Tofauti na siku zote, alishangaa alipofika kwenye mtaa aliokuwa anaishi kugundua kuwa watu wengi walikuwa wakimtazama huku wakionekana kama wanajadiliana jambo fulani.

    Hakuwa na taarifa juu ya chochote kilichotokea huku nyuma wakati yeye akiwa kazini. Hali iliendelea hivyohivyo, watu wengi wakawa wanamjadili bila mwenyewe kuelewa tatizo lilikuwa nini. Hakujali sana, akaenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwake.

    Alipofika, jambo la kwanza lililomshangaza, mlango aliukuta ukiwa wazi, kitu ambacho halikuwa kawaida. Alipoingia ndani, alishtuka kumkuta Karen akiwa amelala juu ya sofa, bila hata kuvua viatu huku miguu yake ikionesha kuwa na vumbi jingi kuashiria kwamba kuna sehemu alikuwa ameenda.

    Alipomsogelea na kumchunguza vizuri, aligundua kuwa alikuwa amelewa chakari baada ya kujidunga madawa ya kulevya. Awali alihisi alijidungia madawa hayo humohumo ndani lakini alipojaribu kupekua huku na kule, hakuona ishara yoyote, akagundua kuwa kumbe msichana huyo siku hiyo alijidunga madawa hayo hukohuko alikotoka.

    Ni hapo ndipo alipopata picha kwa nini watu walikuwa wakimshangaa na kumjadili wakati akirejea kutoka kazini. Kutokana na uchungu aliouhisi ndani ya moyo wake, alikaa kwenye sofa jingine na kujiinamia, machozi yakaanza kumtoka kwa wingi na kuulowanisha uso wake.



    Alijisikia uchungu mkali sana ndani ya nafsi yake, kuna wakati alikuwa anajuta kwa nini aliingia kichwakichwa kwenye penzi la msichana ambaye hakuwa akimjua. Ule usemi wa wahenga kwamba utamu wa mkakasi ndani kipande cha mti, ulikuwa ukitimia kwake.

    Kwa uzuri na sifa zake za nje, hakuna mtu ambaye angeweza kudhani alikuwa na kasoro kubwa kiasi hicho upande wa tabia yake. Abdallah aliendelea kujiinamia pale kwenye sofa kwa muda mrefu, macho yake yakabadilika rangi na kuwa mekundu kutokana na kulia kwa muda mrefu.

    Majira ya kama saa mbili za usiku, Abdallah akiwa amekaa palepale kwenye sofa, Karen alizinduka baada ya kuwa amelala kwa saa nyingi mfululizo. Akashangaa kumkuta Abdallah amekaa pembeni yake huku akiwa amejiinamia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Harakaharaka alikurupuka na kutaka kukimbilia bafuni kuoga kama ilivyokuwa kawaida yake lakini Abdallah akamzuia.

    “Kwa nini tunashindwa kuelewana? Mara ngapi nimekwambia sipendi tabia yako ya kutumia madawa ya kulevya?”

    “Nisamehe mpenzi wangu,” alisema Karen huku mdomo wake ukiwa mzito kuonesha kwamba madawa aliyotumia bado hayakuwa yameisha mwilini mwake.

    “Hii ni mara ya mwisho, sitazungumza nawe tena, siku nitakayokukuta umetumia tena madawa ya kulevya huo ndiyo utakuwa mwisho wa mimi na wewe. Nimechoshwa na jinsi unavyonitia aibu, angalia mtaa mzima leo gumzo ni mimi na wewe, nimechoka,” alisema Abdallah huku akipiga meza kwa hasira.

    Karen kama ilivyokuwa kawaida yake, alijifanya kushuka chini na kumuomba msamaha Abdallah huku akiahidi kwamba hatarudia tena. Hata hivyo, alichokuwa anakisema kilikuwa kikitokea mdomoni tu kwani ukweli ni kwamba hakuna kazi ngumu kama kujitoa kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.

    Abdallah alimruhusu msichana huyo aende kuoga ambapo muda mfupi baadaye, alirudi chumbani na kukaa nyuma ya ‘dressing table’, akaanza kujipodoa na kujiremba.

    Kwa jinsi alivyobadilika baada ya kumaliza kujipodoa, usingeweza kuamini kwamba ndiyo Karen huyohuyo ambaye saa kadhaa zilizopita alikuwa hajitambui kutokana na kutumia kiwango kikubwa cha madawa ya kulevya.

    “Kutokana na upumbavu ulioufanya leo, siwezi kuendelea kuishi na wewe kwenye huu mtaa, kesho nitaenda kutafuta chumba sehemu nyingine sasa ole wako urudie tena ulichokifanya leo,” Abdallah alisema huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.

    Usiku huo hakukuwa na mtu aliyemsemesha mwenzake kama ilivyokuwa kawaida yao, wakalala mpaka kesho yake asubuhi. Abdallah akawahi kuamka na kujiandaa kisha akaelekea ofisini kwake kwa lengo la kwenda kusaini kisha kuomba ruhusa.

    Alikuwa amedhamiria kweli kuhama mtaa huo kwani aibu aliyokuwa anaihisi ndani ya moyo wake ilikuwa kubwa sana. Baada ya kufika kazini, alisaini kisha akaomba ruhusa na kuondoka, breki ya kwanza ilikuwa kwa madalali wa Makumbusho. Akazungumza nao kuhusu suala lake la kutafuta chumba mitaa hiyo.

    Kwa kuwa alikuwa na fedha mfukoni, muda mfupi tu baadaye alifanikiwa kupata nyumba nzuri, upande mzima huku ndani ikiwa na kila kitu. Akaenda kukutanishwa na mwenye nyumba ambapo alimlipa na kuandikishiana mkataba.

    Siku hiyohiyo alitafuta gari kubwa kwa ajili ya kwenda kumhamisha Mikocheni alikokuwa anaishi. Aliporudi akiwa na gari pamoja na watu wa kumsaidia kuhamisha vyombo, alimkuta Karen akiwa ndani. Vitisho alivyomtolea usiku wa siku iliyopita kidogo vilisaidia.

    Kazi ya kuhamisha vyombo ikaanza. Kutokana na wingi wa samani za kisasa alizokuwa nazo Abdallah iliwachukua zaidi ya saa mbili kuifanya kazi hiyo.

    Kitu kingine ambacho Abdallah alikibaini wakati kazi ya kuhamisha vyombo ikiendelea, ni kwamba ndani ya nyumba yake kulikuwa na mabaki mengi ya madawa ya kulevya ambayo Karen alikuwa akiyaficha baada ya kumaliza kujidunga.

    Kwa kuwa tayari alishampa onyo la mwisho na mwenyewe akakiri kwamba hatatumia tena madawa hayo, hakusema chochote zaidi ya kumsaidia kuyaficha ili wale vijana waliokuwa wakiwasaidia kuhamisha vyombo wasiyaone.

    Baada ya kazi hiyo kukamilika, waliondoka na safari ya kuelekea Makumbusho kwenye makazi mapya ikaanza. Walipofika, wale vijana waliwasaidia kushusha vyombo na kuvipanga ndani, kazi iliyowafikisha mpaka jioni ya siku hiyo. Hatimaye Abdallah na Karen wakawa wameyaanza maisha mapya, mahali ambapo hakuna mtu aliyekuwa akiwafahamu.

    Abdallah alikuwa akiendelea kumsisitiza Karen kwamba endapo atarudia tena kufanya mambo ya ajabu, hatakuwa na cha kufanya zaidi ya kuachana naye.

    Kwa kuwa Karen alikuwa anajua kwamba bila kupata tiba ya Methadone hataweza kuvumilia arosto ya madawa, aliamua kujifanya mjinga, kesho yake akajipeleka tena mwenyewe Hospitali ya Mwananyamala na kumueleza daktari wake kwamba alikuwa amerudia tena madawa ya kulevya hivyo alikuwa anaomba kupatiwa msaada kama ilivyokuwa mwanzo ili aachane na tabia hiyo hatarishi.

    Kwa kuwa Dokta Kyaruzi, mkuu wa kitengo cha kusaidia waathirika wa madawa ya kulevya alikuwa akimfahamu, aliamua kumsaidia. Karen akawa ameanza upya kunywa dawa za Methadone huku daktari akimsisitiza mara kwa mara kwamba endapo atarudia tena madawa ya kulevya, basi kifo kilikuwa kikimuita.

    Siku zikawa zinazidi kusonga mbele huku msichana huyo akijitahidi kuachana kabisa na matumizi ya madawa ya kulevya. Hali hiyo ilimfurahisha sana Abdallah, mapenzi kwake yakaongezeka huku akimsimamia msichana huyo kuhakikisha anaendelea na masomo yake ya chuo ambayo aliyakatisha baada ya kuanza upya kutumia madawa ya kulevya.

    Mwezi wa kwanza ukapita, ukaja wa pili na hatimaye wa tatu, wawili hao wakawa wanazidi kupendana huku mambo yao mengi yakiwanyookea. Hata hivyo, kama walivyosema wahenga kwamba la kuvunda halina ubani, miezi kadhaa baadaye, Karen alirudia tena kutumia madawa ya kulevya, jambo ambalo liliupasua mno moyo wa Abdallah.

    Kwa kuwa alishajiapiza kwamba msichana huyo akirudia tena madawa ya kulevya hatakuwa na namna zaidi ya kumuacha, safari hii aliamua kushikilia msimamo wake kwani aliamini akiendelea kumchekea, anaweza kuja kumsababishia matatizo makubwa zaidi.

    “Nataka leo nikirudi nisikukute hapa nyumbani kwangu, nimechoshwa na upumbavu wako,” alisema Abdallah kwa hasira.

    Hata hivyo, japokuwa mdomoni alikuwa akiyazungumza hayo, moyo wake ulikuwa ukizungumza lugha tofauti kabisa. Hakuwa tayari kumuacha msichana huyo aondoke katika maisha yake kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hali hiyo ilisababisha abaki na maumivu makubwa ndani ya moyo wake, siku hiyo hata kazini hakuweza kukaa kabisa kutokana na jinsi alivyokuwa anajisikia vibaya. Akatoka na kwenda kwenye ufukwe aliokuwa anaupenda, Msasani Peninsula, Kawe jijini Dar es Salaam ambako alitafuta sehemu tulivu na kukaa.

    Kwa jinsi alivyokuwa akimpenda msichana huyo, alishindwa kuyazuia machozi yasiulowanishe uso wake, akawa anaendelea kulia kwa uchungu huku muda mwingine akifikia hatua ya kumkufuru Mungu wake kwa kuruhusu msichana aliyekuwa anampenda kwa moyo wake wote, kuwa na tabia za ajabu kiasi hicho.

    Kutokana na jinsialivyokuwa amezama kwenye mawazo machungu, hata wingu kubwa la mvua lilipoanza kujikusanya angani, wala hakuwa na habari, aliendelea kukaa palepale ufukweni, juu ya mchanga alipokuwa amekaa tangu mwanzo, machozi yakiendelea kumtoka.

    Hata manyunyu yalipoanza na kusababisha watu wote waliokuwa wamekaa ufukweni kukimbia kujikinga na mvua, yeye alikuwa mbali mno kimawazo kiasi cha kutoelewa kilichokuwa kinaendelea.



    Winfrida, mhudumu wa kike wa hoteli iliyokuwa ufukweni mwa bahari ya Msasani Peninsula, Kawe jijini Dar es Salaam alikuwa akikimbia huku na kule kukusanya chupa ambazo wateja wake walikuwa wameziacha ufukweni baada ya hali ya hewa kubadilika ghafla.

    Akjiwa anaendelea kukusanya chupa, huku manyunyu ya mvua yakiwa yameanza kuongezeka, anga likiwa limegubikwa na wingu zito la mvua, ghafla alionakitu kilichomshtua.

    Alikuwa ni kijana mtanashati aliyekaa juu ya mchanga, akiwa amejiinamia, akiwa hana habari kabisa na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa yaliyotokea. Japokuwa manyunyu ya mvua yalikuwa yakiuloiwanisha mwili wake, badio alikuwa amejiinamia vilevile.

    Winfrida alijaribu kumuita lakini hakuonesha kushtuka wala kutringishika. Wingula mvua lilizidi kutanda na sasa ngurumo za radi zilikuwa zikisikika na kufanya hali iwe ya kutisha mno. Hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa amesalia ufukweni mpaka muda huo zaidi ya watu hao wawili.

    Tayari mvua kubwa ilikuwa imeshaanza kumwagika, ikabidi Winfrida amkimbilie yule kijana pale alipokuwa amekaa na kumshika mkono. Ni hapo ndipo alipozinduka kutoka kwenye dimbwi la mawazo machungu alilokuwa amezama ndani yake kwa muda mrefu.

    Harakaharaka akainuka na kuanza kukimbia kumfuata Winfrida aliyekuwa anaendelea kumsemesha lakini wakawa wanashindwa kuelewana kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inamwagika.

    Kijana huyo hakuwa mwingine bali Abdallah ambaye alikuwa kwenye kipindi kigumu sana ndani ya moyo wake kutokana na vituko alivyokuwa akifanyiwa na msichana aliyetokea kumpenda kwa moyo wake wote, Karen ambaye sasa aligeuka na kuwa mwiba mkali ndani ya moyo wake.

    Japokuwa alikuwa amechukua uamuzi mgumu wa kuamua kuyakatisha mahusiano yao kutokana na kugundua kuwa msichana huyo alikuwa amerudia tena kwa mara nyingine tabia yake hatari ya kutumia madawa ya kulevya, moyo wake ulikuwa ukizungumza lugha nyingine tofauti kabisa.

    Bado alikuwa akimpenda sana Karen na alitamani abadilike na kuwa vile alivyokuwa anataka ili waishi pamoja na baadaye kufunga ndoa na kuwa mume na mke halali, lakini hilo lilionekana kuwa gumu sana, hali iliyosababisha apitia kipindi kigumu sana maishani mwake.

    Hata hivyo, aliamua kushikilia msimamo wake wa kutengana na Karen kwani aliamini kama kweli msichana huyo alikuwa na mapenzi ya dhati kwake, anaweza kubadilika na kuacha kabisa matumizi ya madawa ya kulevya ili waendelee kuishi pamoja.

    “Umepatwa na nini?” kauli ya Winfrida ndiyo iliyomzindua kutoka kwenye lindi zito la mawazo, akiwa tayari wameshafika kwenye sehemu ya pili ya hoteli hiyo ambayo haikuwa ikifikiwa na mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kumwagika.

    Kila mtu alikuwa akimshangaa Abdallah kwani alionesha dhahiri kutokuwa kwenye hali yake ya kawaida na muda mfupi baadaye, radi kubwa ilipiga na kusababisha umeme ukatike, eneolote likamezwa na giza nene huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha. Muda mfupi baadaye, mishumaa iliwashwa.

    Winfrida akamfuata tena Abdallah na kuendelea kumuuliza kilichomtokea. Licha ya Winfrida kurudia kumuuliza mara kadhaa, bado hakujibu chochote huku maji ya mvua yaliyomlowanisha Abdallah yakimsaidia kuficha ukweli kwamba alikuwa analia.

    Winfrida hakukata tamaa, aliendelea kumsubiri Abdallah atulie ili amwambie kilichokuwa kinamsumbua, muda mfupi baadaye, Abdallah aliingiza mkono mfukoni na kutoa fedha, akamuagiza mhudumu huyo amletee maji ya kunywa. Muda mfupi baadaye, Winfrida alikuwa tayari amesharejea na safari hii, naye aliamua kuvuta kiti kabisa, huku akionesha kuwa na shauku ya kutaka kujua kilichokuwa kimemtokea Abdallah mpaka akawa kwenye hali ile.

    Abdallah alipoona msichana huo amekaa kwenye kiti kilichokuwa kinatazamana naye, huku akiwa anamtazama usoni kwa huruma, alishusha pumzi ndefu na kumuangalia Winfrida ambaye bado alikuwa ametulia, akisubiri kusikia chochote kutoka kwa Abdallah.

    Kabla hajazungumza chochote, simu ya mkononi ya Abdallah ilianza kuita mfululizo, akaiangalia namba ya mpigaji lakini badala ya kupokea, alijiinamia tena na kuanza kulia, safari hii kwa uchungu zaidi kuliko mwanzo, jambo lililomfanya Winfrida abaki njia panda.

    “Jamani kwani kuna nini? Mbona sikuelewi? Huyo Karen ndiyo nani?”

    “Niache tu dadaangu, acha dunia iniadhibu kwa sababu nilishindwa kusikia la mkuu, acha leo nivunjike guu,” alisema Abdallah huku akijifuta machozi na kamasi zilizokuwa zinamtoka kwa wingi.

    Winfrida aliendelea kumsisitiza amwambie lakini hakuwa tayari, akaendelea kuumia ndani ya moyo wake mithili ya mtu aliyepokea taarifa za msiba. Mvua iliendelea kunyesha kwa muda mrefu, ilipokuja kukatika, tayari ilikuwa ni usiku, watu wakaanza kutoka, kila mmoja akitafuta njia ya kuelekea kwake.

    Abdallah naye aliinuka na kuagana na Winfrida, akamshukuru kwa wema wake na kumwambia kwamba wakijaaliwa, ipo siku watakutana tena. Japokuwa bado Winfrida alikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichomtokea kijana huyo mtanashati, alishindwa kumzuia kuondoka.

    Abdallah alipofika kwenye lango la kutokea, Winfrida alikumbuka kitu, akasimama na kumuita Abdallah kisha akaanza kumkimbilia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Samahani kama nakusumbua, hii hapa ni namba yangu ya simu, unaweza kunipigia muda wowote utakaokuwa na mudi ya kuzungumza na mimi,” alisema Winfrida huku akimkabidhi Abdallah namba iliyokuwa imeandikwa kwenye tishu. Akaachia tabasamu hafifu na kuipokea kisha akaendelea na safari yake, huku akikwepa madimbwi ya maji yaliyosababishwa na mvua hiyo.

    Hatimaye alipata usafiri uliomfikisha mpaka Makumbusho alikokuwa amehamia kutoka Mikocheni alikokuwa anaishi awali. Akateremka kwenye daladala na kuvuka barabara, akaanza kutembea taratibu kuelekea nyumbani kwake ambako aliamini atakuta Karen ameshaondoka kama alivyomwambia asubuhi ya siku hiyo baada ya kugundua kuwa alikuwa amerudia matumizi ya madawa ya kulevya.

    Hatimaye aliwasili kwenye nyumba aliyokuwa anaishi lakini akiwa getini tu, alipatwa na mshtuko baada ya kukutana na mazingira yasiyo ya kawaida. Akasimama kwa sekunde chache na kuanza kuangalia huku na kule. Kitu cha kwanza kilichomshtua ilikuwa ni kuona soksi yake moja ikiwa getini.

    Alipotazama vizuri chini kwa msaada wa taa za nje, aliona pia nguo zake nyingine zikiwa zimedondoka, akapiga moyo konde na kuamua kusonga mbele ili akajionee kilichotokea.

    Alipofika kwenye mlango wa kuingilia ndani kwake, alipigwa na butwaa zaidi baada ya kugundua kuwa mlango ulikuwa wazi kabisa wakati yeye aliufunga kabla ya kuondoka. Huku akitetemeka, aliingia ndani na hali aliyokutana nayo, ilimchanganya kuliko kawaida.

    ...

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog