Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

THE LOVE YOU HAD BEFORE (PENZI ULILOKUWA NALO KABLA) - 3

 







    Simulizi : The Love You Had Before (Penzi Ulilokuwa Nalo Kabla)

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Mapenzi yalizidi kuwa motomoto, kila siku walikuwa pamoja huku wakisaidiana katika kila kitu. Luciana yule wa kipindi cha nyuma alibadilika kabisa, akawa si mtu wa kukosa chuo, kila siku ilikuwa ni lazima kuhudhuria huku akitamani kuwa karibu na Dickson kila wakati.

    Maisha aliyopitia nyuma, yalibaki na kuwa historia, hakuwa msichana yule wa kuhusudu fedha, alikuwa mtu aliyekuwa tayari kwa maisha ya kufunga ndoa na kuwa na mume wake.

    Kwa Dickson, alikuwa na mawazo mno, hakufikiria sana kuhusu Evadia, aliamua kwa moyo mmoja kuachana na msichana huyo, watu ambao walimuumiza sana kichwa chake walikuwa wazazi wake tu.

    Hakujua angewaambia nini, hakujua angeanzia wapi kuwaambia kwamba alipata msichana mwingine ambaye alionekana kustahili kuwa mke wake, alijua kwamba wangeongea sana lakini kama mwanaume, wakati mwingine akapiga moyo konde na kusonga mbele.

    “Mbona una mawazo?” aliuliza Luciana.

    “Hakuna kitu mpenzi.”

    “Hebu niambie ukweli kwanza.”

    “Hakuna kitu, niamini.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ziliendelea kukatika, penzi likazidi kuchipuka, Dickson akawa si kitu pasipo Luciana na kwa msichana huyo ikawa hivyohivyo. Baada ya kukatika miezi kumi, hapo ndipo chuo kikafungwa kwa ajili ya likizo ndefu kwani napo kilikuwa kipindi ambacho nchi hiyo ya Venezuela ilikuwa ikielekea katika uchaguzi mkuu.

    Wakaondoka na kurudi barani Afrika. Kabla ya kurudi nchini Tanzania, Dickson aliataka kupitia nchini Rwanda, atambulike kwa wazazi wa Luciana hata kabla ya kufunga ndoa, baada ya saa kadhaa, wawili hao walikuwa nchini Rwanda.

    “Nimefurahi sana kufika nchini kwenu, hakika watu wenu ni wakarimu sana,” alisema Dickson huku akionekana kuwa na furaha mno.

    Walifika katika Jiji la Kigali, mishemishe ziliendelea kila kona, watu walionekana kuwa bize kuitengeneza nchi yao baada ya machafuko yaliyotokea mwaka 1994. Hakukuwa na mtu aliyekaa kiholelaholela, kila mmoja alionekana kuwa na kiu ya kuibadilisha nchi yake.

    Baada ya safari ya dakika thelathini, wakafika katika mtaa uliokuwa pembeni wa Jiji la Kigali, Mtaa wa Mwongozo ambapo gari likaingia katika barabara ya vumbi na baada ya dakika kadhaa likasimama nje ya nyumba moja iliyoonekana kuwa ya kawaida sana.

    Watu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walipoliona gari hilo likiingia ndani ya eneo la nyumba hiyo, wakatoka nje ili kushuhudia ni nani ambaye angeteremka, aliposhuka Luciana, wote wakamkimbilia na kumkumbatia kwa furaha.

    Majirani hawakutaka kuwa mbali, nao wakasogea kule kulipokuwa na gari lile na kuanza kumwangalia Luciana. Alionekana kuwa mrembo hasa, alipendeza machoni mwa kila mtu aliyekuwa akimwangalia, kwao, alionekana kuwa mrembo hata zaidi ya alivyokuwa kipindi cha nyuma.

    “Très proche soeur Luciana,” (Karibu sana Luciana) alimkaribisha mama yake, alizungumza Kifaransa kama ilivyokuwa nchini humo.

    “Thank you,” (Asante) Luciana aliitikia kwa Lugha ya Kingereza, hakutaka kumuacha mpenzi wake katika sintofahamu.

    Wote kwa pamoja wakaanza kuelekea ndani. Dickson hakuzungumza kitu, mahali hapo alikuwa kimya tu na muda wote ule uso wake ulijawa na tabasamu pana. Alionekana kufurahia kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo, kila mmoja alimchangamkia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walipofika ndani, kitu cha kwanza alichokifanya Luciana ni kumtambulisha kwa wazazi wake kwamba alikuwa mpenzi wake ambaye walipanga mambo mengi kuhusu ndoa, wazazi, ndugu na jamaa wote wakakubaliana naye, wakampokea na kuwabariki kwa kila kitu ambacho wangekifanya likiwa hilo la kuishi milele.

    “Yeye ni Mtanzania?” aliuliza mama yake.

    “Ndiyo!”

    “Nimefurahi, nawapenda sana Watanzania,” alisema mama yake Luciana.

    Siku hiyo wakalala hapo na siku mbili baadaye wakaanza safari ya kuelekea nchini Tanzania. Njiani, Dickson alikuwa na mawazo tele, hakujua ni kitu gani alitakiwa kuwaambia wazazi wake kwani kitendo cha Luciana kuwa mpenzi wake, aliamini kwamba kisingepokelewa kwa mikono miwili.

    “Nitawaambia chochote tu, kwanza Evadia simtaki tena,” alisema Dickson.

    “Unasemaje?” aliuliza Luciana.

    “Kwani nimesema chochote?”

    “Nimesikia ukiongea!”

    “Hapana!Labda umesikia vibaya!”

    “Mhh!Sawa mpenzi,” alisema Luciana, hapohapo akamuegemea Dickson begani na kupitiwa na usingizi.

    Muda wote huo, Dickson alikuwa kwenye presha kubwa.





    *****

    **********

    ***********

    Safari iliendelea, japokuwa Luciana alilala njiani lakini kwa Dickson alikuwa macho safari nzima. Kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, aliwafikiria wazazi wake kwa kuona kwamba wangekataa yeye kuwa na msichana huyo kwa kuwa alimwacha msichana waliyemfahamu, msichana mpole, asiyekuwa mzungumzaji, Evadia.

    Ndege ilichukua saa kadhaa ndipo ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo wakateremka na kufuata taratibu zote kisha kukodi teksi ambayo ikaanza kuwapeleka mpaka Msasani alipokuwa akiishi.

    Njiani, bado Dickson hakuonyesha uchangamfu ambao ulizoeleka machoni mwa Luciana, alionekana kuwa na kitu kilichokuwa kikimtatiza moyoni mwake, Luciana hakutaka kukubali kuiona hali hiyo kitu kilichompelekea kuuliza.

    “What’s wrong with you?” (Kimekukuta nini?) aliuliza Luciana.

    “What?” (Nini?)

    “I’m asking you! What’s wrong with you?” (Ninakuuliza kimekukuta kitu gani?)

    “Nothing.” (Hakuna kitu)

    “Are you sure?” (Una uhakika?)

    “Yes!” (Ndiyo!)

    “But, you look weird!” (Lakini unaonekana tofauti)

    “Luciana! Nothing wrong, trust me,” (Luciana! Hakuna tatizo, niamini) alisema Dickson.

    Luciana hakutaka kuuliza swali jingine, alichokifanya ni kuyapeleka macho yake nje na kuanza kuangalia mazingira. Hakuwa na raha, kitu alichohisi ni kwamba mpenzi wake huyo kulikuwa na kitu kilichomfanya kuwa katika hali ile ila alimficha tu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakujali, alichokifanya ni kupuuzia na safari kuendelea. Walichukua dakika kadhaa na ndipo walipofika nje ya jumba moja la kifahari, dereva akapiga honi na mlinzi kutoka nje, akaenda kuongea na dereva, alipoona kwamba gari hilo lilimbeba Dickson, akafungua geti.

    “Karibu kaka!” mlinzi alimkaribisha Dickson.

    “Asante.”

    Wakaingia ndani huku mlinzi akitangulia na mabegi. Hapo ndipo Dickson alipoonekana dhahiri kwamba alikuwa na hofu moyoni mwake. Luciana aliendelea kuwa na wasiwasi lakini hakutaka kuuliza swali kwani majibu aliyopewa ndani ya gari yalionyesha kabisa kwamba mpenzi wake hakutaka maswali zaidi.

    Walipofika sebuleni, wakatulia, akamuita dada wa kazi ambaye akafika mahali hapo na kuambiwa kwenda kuwaita wazazi wake, mfanyakazi yule akafanya kama alivyoambiwa.

    Hazikupita dakika nyingi, wazazi wake wote wawili wakafika sebuleni hapo, walifurahi kumuona kijana wao lakini walipoyapeleka macho yao pembeni, wakamuona msichana ambaye alikuwa mgeni machoni mwao, wakahisi kwamba huyo ndiye alikuwa Luciana waliyeambiwa.

    Hawakuonyesha kinyongo, hawakuonyesha hali yoyote ya mshtuko kwani walijua hilo lingeweza kutokea, walichokifanya ni kuwakaribisha nyumbani hapo. Dickson hakutaka kunyamaza, alichokifanya ni kuwaambia wazazi wake juu ya Luciana.

    “Huyu ni mchumba wangu,” alisema Dickson.

    “Uchumba huo umeanza lini?” aliuliza mama yake.

    “Chuoni. Nimeona kwamba yeye ni msichana mzuri, mwerevu na anayejua kupenda ambaye kama tutatengeneza maisha pamoja, naamini itakuwa ni furaha yangu ya milele,” alisema Dickson.

    “Karibu sana Luciana.”

    “Asante mama.”

    Hakukuwa na maswali mengi, wazazi wake walipomuona msichana huyo wakaridhika naye, walimpenda kwa sababu alikuwa na sura nzuri ila mbali na hilo, walikuwa na majonzi mioyoni mwao kwani msichana pekee waliyekuwa wamemzoea alikuwa Evadia tu.

    Baba yake hakutaka kuvumilia, alichokifanya baada ya Luciana kuanza kuzoea mazingira ya humo ndani ni kumuita kijana wake pembeni kwa lengo la kuzungumza naye.

    “Hivi ulifikiria nini?” aliuliza baba yake.

    “Kivipi?”

    “Kuhusu huyu msichana.”

    “Hakuna kitu, nimegundua kwamba ni msichana mzuri, ana sifa zote za kuwa mke,” alijibu Dickson.

    “Una uhakika?”

    “Asilimia mia mbili.”

    “Sawa. Na vipi kuhusu Evadia?”

    “Nilimwambia ukweli kwamba nimempata msichana mwingine.”

    “Ila hukuona kama angeumia?”

    “Unafikiri ningefanyaje? Sikuwa na jinsi, ila nilimpa nafasi ya kuwa na mwanaume mwingine,” alijitetea Dickson.

    “Mmmh! Aya, hakuna tatizo. Uamuzi ni wako, kazi yetu kubwa ni kukuunga mkono,” alisema baba yake maneno yaliyomfanya Dickson kuwa na furaha mno, akashindwa kuvumilia, akamkumbatia baba yake.

    Laurence alipotea ghafla, hakuonekana tena hospitalini hapo. Kila mmoja alikuwa na hofu, walijiuliza mahali alipokwenda kijana huyo lakini hakukuwa na aliyejua, na hata alipouliza Matilda, jibu lake lilikuwa lilelile kwamba hakujua mwanaume huyo alielekea wapi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku zikaendelea kukatika, Evadia aliendelea kubaki kitandani pale, kama kulia, alilia sana lakini hakukuwa na kitu chochote kilichobadilika. Hakukuwa na mtu ambaye alimfanya kuwa katika maumivu makali kama msichana huyo.

    Kuna wakati alikuwa akijuta kuonana na Laurence, chuki ya taratibu ikaanza kujitengeneza moyoni mwake, mapenzi aliyokuwa nayo juu ya mwanaume huyo yakaanza kupotea kabisa.

    Mama yake ndiye alikuwa mfariji pekee aliyebaki naye, ingawa Matilda alifika hospitalini hapo mara kwa mara na kumwambia kwamba inawezekana hapo baadaye Laurence akarudi tena lakini kwa msichana huyo jambo hilo halikuweza kumbadilisha chochote kile.



    Mikakati ya kutafuta figo kwa mtu mwingine ikaanza hospitalini hapo, watu mbalimbali walifika kwa ajili ya kutoa figo lakini kila walipopimwa majibu yalikuwa yaleyale kwamba vinasaba vyao havikuendana kabisa na vya Evadia jambo lililofanya upasuaji kutokufanyika hivyo Evadia kuwa kwenye hali mbaya.

    “Hivi nitapona kweli mama?” aliuliza Evadia.

    “Utapona tu, Mungu atakutia nguvu.”

    “Kweli?”

    “Niamini. Hujui kwamba Yesu ni Mponyaji?”

    “Najua.”

    “Basi amini hilo. Kama aliponya wengine, basi jua kwamba hata wewe atakuponya,” alimfariji mama yake.

    Siku zikaendelea kukatika, ulipofika mwezi wa pili tangu awe kitandani, Dk. Panzini akaingia ndani ya chumba kile huku uso wake ukionekana kuwa mwenye furaha tele.

    “Kuna nini?” aliuliza mama Evadia.

    “Laurence amerudi.”

    “Unasemaje?” aliuliza Evadia huku akijitahidi kukaa kitandani lakini akashindwa.

    “Laurence amerudi. Ngoja nimuite.”

    Badala ya kuwa na furaha, Evadia akaanza kulia kitandani pale. Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kile alichokisikia kutoka kwa daktari yule. Alimchukia Laurence, hakumpenda kwa sababu tu alimtoroka hospitalini hapo na kwenda asipopafahamu.

    Baada ya dakika kadhaa, Laurence akaingia ndani ya chumba kile. Alionekana vilevile, mwanaume aliyepigwa na maisha ambaye uso wake ulijawa na tabasamu pana, alipomuona Evadia, hapohapo akaanza kumfuata pale kitandani kisha kumuinamia.

    “Mpenzi....” aliita.

    Evadia hakuitikia, alibaki akimwangalia Laurence mahali pale huku akionekana kuwa mwenye hasira. Uso wake ule, ndita alizokuwa amezikunja hazikumfanya Laurence kuliondoa tabasamu lake, aliendelea kulitoa huku akimwangalia msichana huyo kitandani pale.

    “Naomba uondoke Laurence,” alisema Evadia.

    “Niondoke? Niende wapi?”

    “Nimesema naomba uondokeeeee...” alisema Evadia kwa hasira.

    “Hapana! Siwezi kuondoka, siwezi kukuacha peke yako,” alisema Laurence huku akipiga magoti.

    Evadia hakuzungumza kitu chochote, alibaki akilia kitandani pale, moyo wake ulimuuma mno, kila alipomwangalia Laurence na jinsi alivyomtoroka hospitalini hapo alibaki akiumia na hakuona kama alitakiwa kumsamehe mwanaume huyo.

    Msimamo wake ulikuwa uleule kwamba Laurence alitakiwa kuondoka ndani mule kitu ambacho hakukubaliana nacho hata kidogo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sasa si uondoke,” alisema mama Evadia.

    “Mama! Siwezi kuondoka, ninampenda Evadia, siwezi kumuacha peke yake akiteseka.”

    “Hapana! Kama ungekuwa unampenda, usingemkimbia katika kipindi kigumu kama hiki. Mwangalie jinsi alivyo, angalia jinsi alivyokonda kwa ajili ya mawazo. Laurence, naomba uondoke na umuachae binti yangu,” alisema mama Evadia huku akionekana kumaanisha alichokisema.

    “Siwezi! Kwa sababu nina mapenzi mazito kwa Evadia, siwezi kuondoka,” alisema Laurence, akasimama, akavuta kiti na kutulia. Mara hapohapo Matilda akaingia, yeye mwenyewe kumuona Laurence wodini mule alishangaa.



    “Karibu Matilda,” alimkaribisha Laurence.

    “Laurence! Ulikuwa wapi?” lilikuwa swali lililotoka kwa Evadia.

    “Nani? Mimi?”

    “Ndiyo!”

    “Nilipata tatizo, nilikwenda mbali.”

    “Wapi?”

    “Mwanza!”

    “Kufanya nini?”

    Laurence alibaki kimya kwa muda, alionekana kuwa mtu mwenye mawazo mengi. Kichwa chake kikaanza kufikiria kwa haraka juu ya kitu alichotakiwa kukizungumza mahali hapo. Wote waliokuwa ndani ya chumba kile walibaki wakimwangalia, walitaka kusikia Laurence alikuwa wapi.

    “Nimekuwa nikimpenda sana Evadia, amekuwa msichana muhimu sana kwangu. Kumuona kitandani akiugua, kilikuwa kitu kilichoniumiza sana, sikupenda kumuona akiteseka, hivyo niliondoka kwenda Mwanza,” alisema Laurence.

    “Kufanya nini huko?”

    “Kutafuta pesa.”

    “Ila pesa zipo, si nimetoa pesa kwa ajili ya kuwasaidia?”

    “Najua. Ila wakati mwingine niliona bora nitafute pesa kama mwanaume, nisingeweza kukubali kuona msichana wangu akiteseka kitandani,” alisema Laurence.

    “Sawa. Kuna kingine?”

    “Ndiyo! Tena cha muhimu kabisa,” alijibu Laurence.

    “Kitu gani?”

    “Nataka kutoa figo yangu kumsaidia Evadia,” alisema Laurence, kila mmoja humo ndani akashtuka, mpaka Dk. Panzini.

    “Utoe figo yako?”aliuliza Dk. Panzini.

    “Ndiyo! Ninataka kumpa figo yangu moja Evadia.”

    “Mmmh!”

    Kwa kumwangalia tu usoni mwake, alionyesha ni kwa jinsi gani alimaanisha kile alichokisema mahali pale. Kichwa chake kilimuuma kila siku, alimfikiria msichana huyo aliyekuwa kitandani, jinsi alivyoteseka, hakupenda kuliona hilo likitokea hivyo kitu cha mwisho kabisa alichoamua kukifanya ili kumrudishia furaha msichana huyo ni kwamba alitaka kutoa figo yake ili ipandikizwe kwa Evadia.

    Evadia mwenyewe hakuonekana kuamini kile alichokisikia, ila swali kubwa likaja je, vinasaba vya figo lake vingeendana na vya mwanaume huyo au ingekuwa kama wale wengine?

    “Na vipi kuhusu vinasaba?” aliuliza Evadia.

    “Najua Mungu atafanya jambo, sidhani kama yupo tayari kukuona ukiteseka kitandani hapa,” alijibu Laurence.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa hiyo unataka kumpa figo yako?” aliuliza Dk. Panzini.

    “Ndiyo! Ninataka kwa asilimia mia moja.”

    “Sawa.”

    Huo ndiyo uamuzi alioufikia, hakutaka kuona msichana wake akiendelea kuteseka kitandani pale. Alichokifanya Dk. Panzini ni kumwambia amfuate kwa ajili ya kupima ili kuona kama vinasaba vyake vingekuwa vinafanana na vya Evadia.

    Evadia alibaki chumbani mule na mama yake, japokuwa kwa kipindi kirefu aliahidi kwamba angemchukia Laurence lakini kwa kile alichojiwekea nadhiri kukifanya kikazifanya hasira zake kupungua kwa kiasi kikubwa hivyo kubaki chumbani mule wakifarijiana.

    Zilipita dakika arobaini na ndipo Laurence na daktari yule waliporudi ndani ya chumba kile. Kwa kuwaangalia tu ungejua ni kitu gani kilikuwa kimetokea, wote wawili nyuso zao zilijawa na tabasamu pana, tabasamu yaliyoonyesha kwamba kulikuwa na habari nzuri.

    “Kuna nini?” aliuliza Matilda.

    “Habari njema ni kwamba vinasaba vya Laurence vinaendana na vya Evadia,” alijibu Dk. Panzini.

    Hakukuwa na aliyeamini kile alichokisikia kutoka kwa Dk. Panzini, watu wengi walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kumtolea figo Evadia lakini mwisho wa siku hakukuwa na mtu aliyefanikiwa katika hilo.





    Leo hii, baada ya watu zaidi ya mia mbili kufika hospitali hapo na kutokufanikiwa, mwanaume aliyekuwa akimpenda, aliyemthamini kumbe vinasaba vyake viliendana na vile alivyokuwa navyo yeye.

    Hasira zote zikatoweka, akauhisi moyo wake ukianza kumpenda tena Laurence. Siku hiyo ilikuwa ni furaha kwa kila mtu, Laurence hakujutia uamuzi wake wa kutoa figo kwa ajili ya msichana aliyekuwa akimpenda, alikuwa radhi kwa kila kitu na ndiyo maana aliamua kufanyika kwa jambo hilo.

    “Ninakupenda Evadia,” Laurence alimwambia Evadia.

    “Nashukuru mpenzi! Nashukuru kwa kila kitu,” alisema Evadia, akashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumtoka.

    “Usijali. Kwa maana hiyo, zile fedha zilizobaki, tutafanyia biashara nyingine kwa ajili ya maisha yetu,” alisema Laurence.

    “Hakuna tatizo.”

    Kiasi kilichokuwa kimebaki kilikuwa ni milioni ishirini na saba, milioni tatu zilitumika. Mama Evadia hakuchoka kumshukuru Laurence, kila wakati alimwambia dhahiri kwamba alimshukuru kwani alikuwa msaada mkubwa kwa binti yake.

    Siku iliyofuata, asubuhi na mapema Laurence akafika katika chumba hicho, siku hiyo alijiandaa kwa ajili ya upasuaji ambao ungemfanya kutolewa figo yake na kupandikizwa katika mwili wa msichana Evadia.

    Mara baada ya kufika, akaitwa katika ofisi ya daktari yeye na mama Evadia pamoja na Matilda na kuanza kupewa elimu juu ya kile ambacho kingekwenda kufanyika huku akipewa karatasi kwa ajili ya kusaini kwamba alikuwa tayari kwa kila kitu.

    “Unatakiwa kusaini hapa, hii ni oparesheni, chochote kinaweza kutokea,” alisema Dk. Panzini.

    “Hakuna tatizo.”

    Laurence akachukua karatasi hiyo na kuanza kusaini. Muda wote moyo wake ulikuwa na wasiwasi, hakuwahi kufanyiwa upasuaji na siku hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza hivyo kitendo cha kuambiwa kwamba alitakiwa kufanyiwa upasuaji huo kilimtia woga moyoni mwake.

    Alipomaliza kusaini, akachukuliwa na kupelekwa katika chumba maalumu, huko, akavuliwa nguo zake na kuvarishwa vazi maalumu kisha kulazwa katika machela ambayo ilisukumwa mpaka katika chumba kilichoandikwa Theatre (chumba cha upasuaji).CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wala hazikupita dakika nyingi, machela nyingine ikaingizwa ndani ya chumba kile na juu yake alikuwepo msichana Evadia. Alipomuona mpenzi wake chumbani mule huku akiwa tayari kwa ajili ya upasuaji ule, akatoa tabasamu pana. Alichokifanya Laurence ni kuunyoosha mkono wake kisha kuushika mkono wa Evadia.

    “Ninakupenda mpenzi,” alimwambia.

    “Ninakupenda pia mpenzi na asante kwa kila kitu.”

    “Ninafanya hivi kwa ajili yako, si unajua hilo?”

    “Najua mpenzi.”

    “Sawa.”

    Tayari Dk. Panzini na madaktari wenzake walikwishafika chumbani humo, kila mmoja alikuwa tayari kwa ajili ya upasuaji huo. Kazi hiyo ilitakiwa kufanywa kwa umakini mkubwa kwani endapo wangekosea hata sehemu moja basi ingemaanisha kwamba mmoja wapo au wote wawili wangefariki dunia.

    Kabla ya upasuaji kuanza, madaktari wale wakashikana mikono na kuanza kusali kila mtu kwa dini yake, walipomaliza, wakachukua nusu kaputi na kisha kuwawekea, wala hazikupita dakika nyingi, wawili hao wakapitiwa na usingizi mzito, kilichoendelea, hakukuwa na aliyekifahamu, upasuaji ukaanza kufanyika.

    Nje ya chumba kile, mama Evadia alikuwa na hofu, hakutulia, kila wakati alikuwa akiomba Mungu kwamba upasuaji ule ukamilike na hivyo binti yake arudi na kuwa kama alivyokuwa kipindi cha nyuma.

    Kwa Matilda, hakutulia, kichwa chake kilikuwa na maswali mengi kwamba ilikuwaje bosi wake, Laurence akubali kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kutolewa figo kisa msichana?

    Alifahamu kwamba alikuwa na fedha nyingi, alikuwa na uwezo wa kuwatafuta watu wengine tena kwa gharama zozote zile na mwisho wa siku kumpata mtu ambaye vinasaba vyake vingeendana na vya Evadia kisha kumlipa na figo ya huyo mtu kutolewa.

    Kila kitu alichojiuliza alikosa jibu ila kwa sababu mapenzi yalikuwa na nguvu kuliko mauti, akaamua kuachana naye kwa kuamini kwamba bosi wake aliamua kutoa figo yake kwa kuwa alimpenda sana msichana Evadia.



    Madaktari waliendelea na kazi yao ya kutoa figo ya Laurence kwenda kwa msichana Evadia. Nje ya chumba kile bado mama Evadia alikuwa na mawazo tele. Saa ziliendelea kukatika huku akiendelea kubaki kwenye benchi pamoja na Matilda.

    Kwa kumwangalia Matilda, aliendelea kuwa kwenye hali ya sintofahamu kwani alionekana kujiuliza juu ya ujasiri alioufanya nao mwanaume huyo wa kuutoa figo yake na kumpa msichana aliyekuwa akimpenda sana, Evadia.

    Saa zilianza kukatika mahali pale, waliendelea kuvumilia, hali ilionekana tofauti na walivyotegemea kwani upasuaji ulikuja kumalizika saa tatu usiku, saa kumi na mbili tangu madaktari waanze upasuaji ndani ya chumba kile.

    Mara baada ya kila kitu kumalizika, Laurence akachukuliwa na kupelekwa nje, alikuwa kitandani, machela ilisukumwa kuelekea katika chumba cha wagonjwa mahututi, alipofikishwa humo akapewa muda wa mapumziko.

    Wala hazikupita dakika nyingi naye Evadia akatolewa ndani ya chumba kile, hakuwa akijitambua, alikuwa hoi juu ya machela na ilikuwa ikisukumwa kuelekea katika chumba cha mapumziko.

    Si mama Evadia wala Matilda ambaye aliruhusiwa kuingia ndani ya vyumba hivyo, walizuiliwa kwani wagonjwa walihitaji muda zaidi wa kupumzika kabla ya kuendelea na mambo mengine.

    Matilda alifika hospitalini hapo kila siku, kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilitakiwa kuwa siri, hakutakiwa kufahamu mfanyakazi yeyote yule juu ya hali aliyokuwa nayo Laurence kwamba aliamua kutoa figo yake moja kwa ajili ya kumsaidia mpenzi wake.

    Siku zikakatika, baada ya wiki mbili, wote walikuwa wakiendelea vizuri. Walizungumza ingawa si kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma. Walionekana kuwa na afya nzuri kidogo. Mama Evadia alipata nafasi ya kuwatembelea wote wawili, tena kwa zamu, baada ya madaktari kuona mama huyo akihangaika huku na kule, wakaamua kuwaweka wagonjwa hao katika chumba kimoja.

    “Unajisikiaje?” aliuliza mama Evadia, alikuwa akimuuliza binti yake.

    “Najisikia vizuri kidogo,” alijibu Evadia kwa sauti ya chini.

    “Asante Mungu!”

    Hapohapo akamfuata Laurence ambaye naye alikuwa ndani ya chumba hichohicho, alipomfikia akamuuliza kuhusu hali yake, naye alikuwa kama Evadia, hakuwa akijisikia vizuri sana kwani bado mshono ulikuwa ukimuuma.

    Siku ziliendelea kukatika, kila siku Matilda alipoingia wodini na kumwangalia bosi wake machoni, aliyaona mapenzi yaliyokuwa yakionekana kwa msichana Evadia. Laurence alikuwa tayari kwa kila kitu na hakuonekana kama alikuwa tayari kumpoteza msichana huyo.

    “Bosi..” aliita Matilda.

    “Shiiiii....”

    “Samahani, nimesahau. Unajisikiaje?” aliuliza Matilda.

    “Najisikia vizuri kidogo, bado kidonda kinaponapona kwanza,” alijibu Laurence.

    “Pole sana.”

    “Asante sana.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya mwezi mmoja, wote wawili wakaruhusiwa kutoka hospitalini. Hakukuwa na mtu yeyote aliyeruhusiwa kufanya kazi zozote kwani walikuwa walitakiwa kupumzika kwa kipindi kirefu pamoja na kutofanya kazi zozote nzito kwani bila hivyo mishono waliyokuwa nayo ingeweza kuleta matatizo mengine.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog