Simulizi : Ninge
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dakika kumi baadaye Tuse mrembo pamoja na mama yake waliingia pale chumbani kwetu. Kisha mama lao akatueleza kwa ufupi mpango wake.
Kwa pamoja tukaubariki, akamsindikiza Tuse katika mkakati huo.
Aliondoka pale akitusihi tusithubutu kuzurura kwa sababu mimi sura yangu bado ilikiwa sura ambayo inatakiwa sana, tena kutakiwa huko kulikuwa kwa mabaya mno.
Kama Yule Kaburu alikuwa na watu wake serikalini hivyo angeweza kunimaliza hata kabla sijapata nafasi ya kusimama mahakamani!!
Tukaamua kutii amri!!
Mama lao alikuwa na namba za simu ya Wanchera akamuahidi kuwa kwa lolote lile atampigia.
Tulibaki pale ndani kwa masaa mengi sana, tuliongea, tukalala tukaamka tukala, bado mama lao alikuwa hajarejea wala kutoa taarifa yoyote.
Majira ya saa mbili usiku mama lao akampigia simu Wanchera na kumueleza kuwa wakati wa kazi ulikuwa umefika.
“Mwambie huyo dogo avae kofia azibe hako kasura kake…. “ niliisikia sauti ya mama lao kwenye spika.
Na hata baadaya kukata simu wanchera akanieleza mahali tunapotakiwa kwenda, nikajiandaa na kuvaa kofia kama alivyoagiza mama lao. Na hapa nikawa mtu wa kumfuata nyuma Wanchera kwa sababu mimi sikuwa mwenyeji kabisa wa jiji hilo la dar.
Tulipanda daladala na kushuka kituo Fulani ambacho hakikuwa kimechangamka sana.
Tukapenya mitaa kadhaa, hatimaye tukakifikia kibanda cha chipsi, Wanchera akanyanyua simu aweze kumpigia mama lao. Lakini kabla hajafanya hivyo mara mama lao alikuwa amefika tayari.
“Twendeniupesi sana huyu mjinga asije akamuambukiza mwanangu magonjwa, mbona nitamuua akifanya hivyo.” Mama lao alizungumza kwa ghadhabu huku akinekana kujiamini sana.
Tulimfuata nyuma mama lao.
“Jamani hakuna kutegeana tukifika ni aidha mazungumzo halafu kazi, lakini kama akitaka iwe kazi kweli aipate kazi.” Alizungumza mama lao huku akipiga hatuia ndefu ambazo zilionekana kumzidi afande wanchera lakini alijikaza kikakamavu tu, bila shaka mazoezi ya kijeshi enzi hizo yalimsaidia zaidi hadi wakati huu.
Hatimaye tukaifikia nyumba ya kulala wageni iliyokuwa ya kiwango cha kawaida tu.
“Tazama lile ni gari la serikali, dah! Ama kweli si kila mtu alizaliwa kuwa mtawala…” afande wanchera alilalamika alipoona gari likiwa limeegeshwa pale na akatambua wazi kuwa kuna kiongozi wa serikali alikuwa akiisaliti ndoa yake katika nyumba ile.
Tulipenyeza hadi pale mapokezi.
“Karibuni jamani… vyumba vimejaa samahani” dada wa mapokezi akiwa anajipodoa uso wake uliokithiri kwa mkorogo alitueleza hata bila kutusikiliza tulichokuwa tunahitaji.
“We mjinga nani amekwambia kila mtu anayekuja hapa anahitaji chumba… kazi kujipodoa tu wakati umri ushakuacha!!” alijibu mama lao. Bila shaka alifanya kwa maksudi ili amkere Yule dada.
Hakika alimkera maana alivimbiana sana na laiti kama mama lao angeongeza dongo jingine Yule dada angepasuka mbele yetu!!.
“We malaya unasemaje??” aliwaka Yule dada huku akiufungua mlango na kutoka ili amkabiri mama lao.
Alipotoka tu mama lao akamshika mkono kisha akatoa kitambulisho na kumsogezea machoni.
“Bila shaka unajua kusoma mpuuzi wewe, tupo kazini sisi..” akasita na kugeuka, “Afande wanchera hakikisha hamna simu inapigwa kutoka hapa kwenda popote pale, dogo wewe tunaenda wote ndani……” alitoa amri mama lao safari hii sauti yake ilikuwa tofauti kabisa, alikuwa anaonyesha hasira za waziwazi.
Amakweli mpambano ulikuwa umeanza…
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tulitembea huku macho ya mama lao yakiwa yanasoma namba na majina ya vile vyumba vya nyumba ile ya kulala wageni.
Hatimaye tukakifikia chumba kilichoandikwa nambari 18. Tukasimama pale kisha mama lao akausogelea ule mlango na kusikiliza kwa sekunde kadhaa kabla hajagonga hodi.
Kimya kikatanda akaugonga mlango tena.
Sauti ya kiume ikakohoa kisha ikauliza.
“Nani wewe??”
Mama lao hakujibu kitu akanivuta na kuninong’oneza, “Ni yeye, hakikisha kamera yako inakuwa makini sana… …”
Nikabaki kushangaa, mbona mimi sikuwa na kamera alimaanisha kamera gani mwanamama huyu.
“Kamera?” nilimuuliza huku nikiwa nimetaharuki kiasi fulani.
Akanivuta kisha akanipiga kwenzi kali kichwani. Kisha akanisogeza karibu yake tena akaninong’oneza tena, “Kamera ni macho yako dogo… na nikisema piga picha namaanisha upigane…” wakati anamalizia kusema yale mlango ukasikika ukifunguliwa.
Na mara ukatoka uso, uso ulionitisha na kuufanya mwili wangu uingiwe na ubaridi mkubwa sana.
“Samahani sijui kama mmeelekezwa chumba sahihi?” alituuliza Yule bwana ambaye kwa mara ya kwanza nay a mwisho nilimuona akimtesa Gadna na kumuua.
Mama lao akawa kama anayeshangaa kiasi kabla hajafanya ambalo sikuwa nikilitegemea hata kidogo.
Hakika ilistaajabisha, mama lao alizunguza kwa sauti ya chini sana huku akionekana kumsihi Yule bwna kitu.
Mtindo huu wa mama lao ukamfanya Yule bwana kuwa makini na kusogeza sikio ili aweze kumsikia vyema mama lao.
Hilo lilikuwa kosa ambalo mama lao alisubiri kwa hamu litokee. Yule bwana alipoweka sikio ili amsikize mama lao, mama lao naye akasogea nyuma kidogo kisha akakitupa kichwa chake kwa kasi kubwa sana.
Kikampiga Yule bwana sikioni akajikuta akiuparamia mlango na kutua ndani, sekunde iliyofuata mama lao alikuwa yu ndani ya kile chumba akaniamuru na mimi niingie, nikafanya vile.
Na hapo macho yangu badala ya kumshuhudia Yule bwana anayetapatapa pale chini yalimshuhudia Tuse mtoto wa mama lao akiwa katika upande mmoja tu wa kanga.
Tulipogonganisha macho akanikonyeza huku akitabasamu. Nilisisimka sana.
“Hebu vaa nguo zako na wewe….” Nilimsikia mama lao ghafla akimkoromea mwanaye aliyekuwa amejibweteka kitandani.
Ndugu msikilizaji, umewahi kuamini kuwa hata katika vita mapenzi huweza kuibuka??
Kama haujawahi kuamini basi ni kwa sababu haujawahi kukutana na Tuse mtoto wa kinyakyusa Yule….
Nisiseme sana siku nikipata muda nitamuelezea kiundani!!
Tuse alijizoazoa akavaa nguo zake, na hapo Yule bwana akasimama na kutaka kupambana na mama lao.
“Kijana ni kweli una nia ya ….” Kabla hajamalizia kauyli yake Yule bwana akarusha teke kali likamtulia mama lao mbavuni. Mama lao akatokwa nay owe la wastani. Yowe ambalo lilimaanisha kuwa mambo si mazuri sana.
Tuse akiwa bado hajavaa nguo zake vizuri hakusubiri kuambiwa akaruka kutoka pale kitandani mzimamzima akampiga ngumi kali ya mgongo Yule mwanaume, kwa jinsi alivyojikunja hauhitaji yeyote wa kukuelezea kuwa maumivu yalimuingia vizuri kabisa.
Alipojinyoosha mama lao alikuwa amefika na kuizungusha mikono yake kwa nyuma.
Yule bwana akaanza kupiga kelele na hapo sasa mama lao akaitumia fursa ile kumuuliza maswali.
Alimuuliza juu ya Gadna na ni kitu gani walimfanya na ni nani amesimama nyuma ya mambo haya yote.
Yule bwana akasema hamfahamu Gadna, mama lao akaikunja mikono zaidi na hapo akamchimba mkwara.
“Nakuuliza swali lile lile kama la awali lakini ukithubutu kutoa jibu lilelile la awali nakuahidi kuwa huu utakuwa mwisho wako wa kuwa na mikono, nitaikata maana sijui kuvunja!!” alichimba mkwara wenye uzito wa tembo mama Yule.
Yule mwanaume akalegea na kukiri kuwa anahusika katika kumuua Gadna. Akajieleza kuwa yeye ni mtumwa tu hakuwa na nia ya kuua bali aliagizwa na bosi wake.
“Huyu bosi nd’o nalihitaji sana jina lake” aliuliza mama lao bila kujali uchungu aliokuwa akipitia Yule jamaa.
Ni hapo Yule bwana alipotoa jibu ambalo lilitustaajabisha sana, alitaja kuwa aliyetoa agizo hilo alikuwa ni Yusuph Kirenge.
Nani hakulijuajina hili lilipokuja suala la medani za kisiasa, nani angekubishaia kama ungesema kuwa Kirenge alikuwa mwanasiasa wa kuigwa.
Sasa inakuwaje anashiriki fitna nzito kama hii.
Tenainayohusisha roho ya mtu kupotea katika namna ya mateso makubwa vuile.
Yule bwana alioyekuwa amelegezewa kidogo mikono yake alisema kuwa bwana Kirenge alikuwa mwanasiasa wa aina yake ambaye alitenda maovu kimyakimya huku akiwahadaa wananchi kwa kuwa msemaji sana bungeni lakini ile ilikuwa ni kiremba tu alikuwa amejivika.
Mwanasiasa chipukizi aliyetangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo mojawapo jijini Dar bwana Gadna alikuwa akitembea kifua mbele baada ya kuibaini mikataba ambayo bwana kirenge alikuwa ameingia na mamia ya wananchi maskini wa Tanzania. Yaani wakati wananchi wakilia juu ya mikataba ambayo serikali inasaini na watu wan je kirenge yeye aliwakandamiza walewale wanaolia.
Alinunua mazao ya wananchi kwa bei ya chini sana, aliwatishia wananchi kuwa wasipomuuzia maeneo atawafanyia fitna maeneo yao yauzwe nawaishie kupata pesa kiduchu, kwa sababu waliiogopa mserikali na walikuwa kijijini hakuna sauti yao iliyosikika popote pale.
Aliyeyafichua haya alikuwa ni Gadna, Kirenge aligundua na njia pekee ya kumnyamazisha ilikuwa kumlazimisha kutoa zile nyaraka za ushahidi na baada ya hapo amwondoe duniani.
Mpango ukafanyika na kutimia!!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yule bwana alisema mengi yaliyokuwa ya kuumiza sana lakini mwisho wa yote aliapa kuwa hakuwa akifahamu kabisa juu ya zile nyaraka kwa sababu hawakuwa wamezipata bado kwani alipowaelekeza Gadna kuzichukua palikuwa pagumu kuingilika na vile alikuwa amekufa tayari uzito ulikuwa umepungua sana.
Mama lao akamuuliza ni wapi zilikuwa zile nyaraka, akajieleza vyema.
Mama lao akamueleza kuwa usiku huohuo wanaenda eneo hilo na liwalo na liwe!!
Mama lao alidai kuwa kuna mambo mengi nyuma ya pazia hayawezi kuwa haya tu…
Sijui ni kwa nini yeye aliamini vile alivyoamini.
Akamchimba tena mkwara Yule mwanaume na kumwambia kuwa akijaribu kuleta udanganyifu wowote ule watakapokuwa nje basi kitakachomtokea kamwe hatakaa aamini.
Yule mwanaume akafanya tabasamu hafifu kisha akaapa kuwa hatafanya jambo lolote lile.
Tukaufungua mlango na kutoka nje.
Hatukupiga hata hatua nne mbele, tukaona kundi la wanaume wapatao wane wakitembea kwa kasi kuja eneo tulipokuwa.
Yule mwanaume akatabasamu zaidi na mwisho akacheka.
Mimi na mama lao tulipagawa sana.
Tuse yeye alikuwa anavaa bado chumbani….
Mama lao akatoka na tusi zito katika kabila yake ya kinyakyusa!!
Unashangaa nilijuaje kuwa hilo ni tusi wakati mimi si mnyakyusa…
Tuse alinifundisha kidogo…..
TUKIWA bado katika mshangao ule wa aina yake mara ghafla, Yule mateka wetu akamgeukia mama lao na kumtandika ngumi ya usoni, mama lao akatokwa na kilio kikubwa huku akiyumbayumba.
Ile anajiweka sawa na wale wanaume wanne walikuwa wamefika na kutuzunguka.
Ndugu msikilizaji mimi nilikuwa mgeni katika mambo haya ya kupambana ana kwa ana japokuwa nilikuwa nimeona mapambano kama haya mengi tu katika mkasa huu ambao ulikuwa umenifanya niwe mojawapo kati ya watu wachache wanaoweza kuelezea kwa vitendo juu ya ule usemi wa neno ninge huja wakati yameshatokea tayari.
Wale mabwana walitoa pingu, nikashangaa sana kwa sababu nilijua wazi kuwa watu wale ni watu wabaya na wala si watu kutoka serikalini sasa inakuwaje wanakuwa na uwezo wa kumiliki pingu na kuzitumia watakavyo.
Mama lao ambaye sasa alikuwa ameegemea ukutani akihema kwa nguvu sana, ni kama alikuwa haoni kile kilichokuwa kinaendelea pale na jinsi walivyokuwa wa,kimsogelea wakiwa na pingu zao.
Huenda hata mimi nilikuwa simjui vyema mama lao kama yeye alivyokuwa akijijua uwezo aliokuwanao, hivyo kadri ya matukio nami nilikuwa najifunza juu ya mama huyu.
Ilikuwa ghafla!! Naam ilikuwa ghafla haswa…..
Mama lao alipayuka kwa sauti ya juu.
“Dogoo piga picha…” nikakumbuka upesi kuwa aliniambia kuwa maana ya kupiga picha ni kupigana, aliposema vile mara Tuse naye akatoka mle chumbani akiwa na kioo ambacho kilikuwa ndani ya kile chumba, alifika bila kusita akambamiza nacho Yule mateka wetu kichwani kikamchana vibaya akaanguka chini, mama lao hakuchelewa akamuwahi mwanaume mmoja na nitumie nafasi hii kumpa pole kwa sababu hakujua uzito wa kichwa cha Yule mama, alipomuona mama lao analeta kichwa nay eye akaleta kichwa wakutanishe.
Ulisikika mlio mkubwa na na Yule bwana akapiga yowe dogo huku akiweweseka na kutua chini.
“Mpo chini ya ulinzi!! Usitikisike wala kugeuka nyuma.” Ilisikika sauti ya amri kali sote tukatulia kama tulivyo, uzuri ni kwamba sisi tulimuona huyo aliyekuwa akiamrisha kutulia kama tulivyo.
Alikuwa ni afande Wanchera, kwa wakati ule usingeweza kucheka lakini baadaye ilifurahisha sana afande hakuwa na chochote mkononi bali alikuwa ameweka vidole vyake kama bunduki hivi.
Mama lao hakupoteza muda akamkamata mwanaume mmoja, Tuse naye akamkabili mwanaume mwingine hii ilimaanisha kuwa Yule mwanaume aliyebaki alikuwa halali yangu.
Kaa karibu na uwaridi ili na wewe unukie.
Hii ndo ilinitokea, nikamkabili yule mwanaume nikiwa na imani kuwa ikiwa mwanamke anaweza inakuwaje mimi nisiweze.
Hakika nilifanikiwa kwa kiasi fulani.
Lakini asiyejua hajui tu msikilizaji…
Watu wale walikuwa wametambua wazi kuwa maisha yao yalikuwa hatarini na walijua kuwa wakiendelea kutii amri ile basi kila kitu kitaharibika.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yule ambaye nilithubutu kumkabili, ghafla alinisukuma na nikiwa sijajua nini cha kufanya mara nilishtushwa na ubaridi katika mbavu zangu na mara ubaridi ule ukapotea na kisha kuwa maumivu makali. Nilibaki kujipinda nikiwa nasikilizia maumivu yale, nilipojishika nilikutana na mpini.
Nilikuwa nimechomwa kisu.
Nilianguka chini nikiwa nimejishika mbavuni huku nikilia, nikiwa pale chini nikamuona yule mtu akigeuka ili aweze kukimbia, lakini nikapata nafasi ya kushuhudia faida za mazoezi ya kijeshi.
Afande wanchera hakuwa na mguu mmoja lakini alichofanya.
Alistahili pongezi zote.
Afande alilitoa gongo lake kwapani akaruka kwa kutumia mguu wake mmoja na mara akazungusha lile gongo lake na kutua vyema katika katika kisogo cha bwana aliyenidunga kisu. Akapepesuka na kutua chini.
Wanchera akiwa bado amesimamia mguu mmoja alikuwa amechachamaa, wale wanaume wawili walipojaribu kuwadhibiti mama lao na Tuse, aliingia kwa kasi akiwa na lile gongo akalizungusha katika namna isiyosimlika na kuwapiga wote wawili kwa ustadi mkubwa sana.
Halafu upesi kaichukua pingu na kuwazungushia katika mikono yao.
Na hapo akanyanyua simu yake na kupiga.
“Unampigia nani??” aliuliza mama lao.
“Ikiwa tunao huu ushahidi na serikali ishindwe kutusaidia basi hatuna serikali… napiga simu kwa kamanda mkuu…” alizungumza kwa amri za kiaskari na hapo kwa mara ya kwanza nikamuona mama lao akiwa mpole kabisa.
Afande wanchera akapiga simu akazungumza na kutoa uelekeo walipokuwa.
“Tuse na we dogo ondokeni hapa, Tuse hakikisha unamfikisha hospitali akapatiwe huduma. Hicho kisu hakina sumu hivyo hapatakuwa na madhara makubwa zaidi ya jeraha … likitokea lolote baya msisite kuwa wakombozi wetu….” Wanchera alisema, mama lao akaunga mkono hoja, na hapo nikaondoka na kwenda nikiwa na Tuse mrembo!! Urembo wake sasa sikuutambua vizuri kwa sababu nilikuwa naugulia maumivu.
Punde tuliingia katika zahanati moja, upesi Tuse akatoa rushwa ili tusiulizwe maswali mengi. Nesi mwenye njaa akaipokea akaenda kugawana na daktari. Nikahudumiwa upesi, kweli kama alivyosema wanchera halikuwa tatizo kubwa, yule bwana alikuwa amechoma kwenye nyama tu hakuwa ameudhuru mfupa wowote.
Baada ya nusu saa nilikuwa natembea kwa kuchechemea lakini sikuwa naumia sana.
Baada ya takribani nusu saa eneo lile lilikuwa limetawaliwa na jeshi la polisi, watu wale na suti zao walichukulia pamoja na akina mama lao. Walipoondoka na sisi tukaondoka na Tuse akalipia teksi tukaufuata ule msafara kujua nini hatma ya jambo lile.
Tatizo dereva hakuwa mwepesi sana, gari lile likatupotea na kushindwa kujua ni wapi walikuwa wameelekea.
Tuse alimfokea sana yule jamaa na kisha akasema kuwa hatalipa pesa yoyote.
Kwa upole yule bwana akatushusha huku akiwa mwenye manung’uniko.
Usiku ulikuwa mnene sana, Tuse akashauri tutafute mahali tupumzike ili siku inayofuata tufuatilie kwa ukaribu zaidi ni nini kinaendelea.
Ilikuwa kama Tuse alivyosema, tukatafuta nyumba ya kulala wageni iliyokuwa ya gharama nafuu.
Tukajihifadhi huko huku kila mmoja akiwa na wazo lake juu ya nini kimewatokea Mama lao na afande Wanchera.
Alfajiri wote tulikuwa macho kabisa, pale chumbani palikuwa na runinga.
Tuse akaiwasha na kujaribu kufuatilia habari kadha wa kadha.
Hatimaye ikaja ile habari tuliyokuwa tunaisubiri kwa hamu kubwa.
Ilikuwa sauti ya kiume ya msomaji wa habari ile.
“Kundi la watu kumi lililokuwa likijihusisha na siasa chafu huku likigandamiza tabaka tawaliwa ambalo ni masikini kabisa limefikishwa mikononi mwa polisi kwa jitihada za wasamaria wema wapenda haki akiwemo yule mwanamke wa shoka ajulikanaye kwa jina la mama lao. Mwili wa kiongozi wao mkuu bwana Kirenge ambaye pia alikuwa ni mbunge katika jimbo lake umekutwa ukiwa porini bila uhai, inasadikika kuwa alijiua kwa kujipiga risasi nbaada ya wenzake kukamatwa wakiwa na mpango mzito katika nyaraka walizokuwa wamebeba.
Hii ni tahadhari kwa watanzania na wasiokuwa watanzania wanaodhani kuwa serikali yetu imelala, wanasahau kuwa hata wananchi pia ni serikali.
Wanatakiwa kuelewa kuwa Tanzania ipo macho kabisa na haipo tayari kuona mambo ya kikatili kama hayo yakiendelea kutokea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Leo majira ya saa nne patakuwa na mkutano wa waandishi wa habari, serikali inatoa rai kwa vijana wawili shupavu katika kulitetea taifa Tusekile na mwenzake aitwaye dogo kujitokeza katika ofisi za mkuu wa polisi Kinondoni bila kuogopa lolote kwa sababu wao ni mashujaa…..”
Tuse aliizima runinga kisha akanigeukia, akatoa lile tabasamu lake zuri lililokluwa na salamu fulani ndani yake.
Nikalijibu lile tabasamu kisha nikasimama na kumkumbatia kwa nguvu zote.
Tukajiandaa na kuondoka tukiwa na amani tele.
Tulifiika eneo lile hata kabla ya saa nne…
Muda ulipofika tuliingia pale ofisini, na hapo tukapokelewa kwa heshima tele tukiwa kama mashujaa.
Ile hali ya kupokelewa kishujaa ikanifanya nikumbuke ile kauli ya ninge…
Nikajisemea kwa sauti ya chini, ningeikimbia vita hii ningeupata wapi ushujaa huu.
Tulitulia mahali baadaye wakaingia watu wengine, walikuwa wanne, nilimtambua mama lao na afande wanchera kwa mbali lakini wale wengine wawili nilikuwa sijawatambua ila mmoja ni kama nilikuwa nimewahi kumuona.
Wakaendelea kusogea hadi walipofika.
Nikatazama na yule mtu, ndugu msikilizaji huwezi amini alikuwa ni baba yangu.
Baba yangu mzazi, alikuwa na pingu mikononi mwake.
Alikuwa ananitazama lakini hakuonesha kunikumbuka hata kidogo…..
Nilipagawa sana…….. nikajiuliza ni kitu gani kinaendelea na kwa nini iwe katika siku hii.
“Dogo vipi mbona unamtazama sana huyu jamaa…” mama lao alinihoji.
Nikajaribu kuzungumza lakini sauti haikutoka vizuri, nikajikohoza na kisha nikawaeleza kuwa yule mtu anafanana kabisa na baba yangu mzazi ambaye sijawahi kumuona tena tangu litokee lile tukio la mama yangu kuuwawa.
Niliposema ile kauli, yule mtu wan ne ambaye nilikuwa nimemgundua kuwa ni askari tayari alishtuka, sikujua ni kitu gani kilichokuwa kimemshtua.
Na katika kusema kwangu vile yule mwanaume akanyanyua uso wake na kunitazama vyema zaidi usoni.
“Kessy,… ni wewe mtoto wangu…” alizungumza huku sauti ikishindwa kutoka vyema…..
Afande alipiga simu akazungumza kidogo kuna mtu alikuwa anamuita.
Punde aliyeitwa akafika, wakanichukua mimi na baba na kwenda faragha.
“We dogo una uhakika huyu ni byako…”
“Ndio kwa asilimia zote kabisa…” nilijibu bila kutetereka.
Afande akashusha pumzi na kisha akaelezea kuwa baba yangu alijipeleka kituoni tangu aliposikia kuwa ninatafutwa na polisi kwa kosa kumuua mama yangu, aliwaeleza polisi kuwa mimi sihusiki hata kidogo ni yeye ndiye aliyemuua mama yangu.
Polisi hawakumuamini hata kidogo na walipompa taarifa mkuu wa polisi wilayani hapo akatoa amri kuwa mtu huyo apelekwe katika ofisi yake kwa sababu asingeweza kuhukumiwa kisa tu amejitaja kuwa yeye ni muuaji.
Polisi alivyomaliza kuzungumza baba alinitazama kisha akalazimisha kutabasamu,
“Kessy nilimuua mke wangu, ilibidi tu kufanya vile mwanangu…. Mama yako hakuwa kiumbe wa kawaida hata kidogo. Alinifanyia mengi mabaya mwanangu, alikutenda wewe pia sana.
Alikuhangaisha ukiwa mdogo hadi unavyokuwa, kisa tu yeye hakuwa na uwezo wa kuzaa.
Kessy nimekutana nawe leo kwa mipango ya Mungu….. nimekutana nawe ili ujue kuwa yule hakuwa mama yako bali mke wangu mimi, na uliona alichokuwa kinifanyia. Sio kwamba sikuwanao uwezo wa kumwadhibu lakini tangu nikiwa mdogo sikufundishwa kupiga mwanamke, ndo maana uliona mama yako akinipiga na kujiona kuwa yeye ni mbabe sana, hayo yote nikayafumbia macho mwanangu, mama yako akaona hiyo haitoshi akadai kuwa mimi nd’o mwenye matatizo ya kuzaa hivyo akaanza vitisho kama utani vile akasema atatafuta mwanaume mwingine. Nikadhani anafanya utani na hawezi kufanya kitu kama kile.
Baadaye akaanza kuninyimba unyumba ama ananipa siku anayotaka yeye, na nikaanza kusikia tetesi mtaani kuwa mama yule anajihusisha kimapebnzi na vijana kadha wa kadha.
Nilijisikia aibu sana hivyo nikaendelea kumtetea mama yako. Samahani kwa kuendelea kumuita mama yako naomba umchukulie hivyohivyo, nilipokuwa nikimuuliza ananijia juu na kuendelea kujiona yeye ni mbabe ananitukana matusi mazito na siku hii akapitiliza na kunitukania mama yangu, Kessy mwanangu niliumia sana nikaamua kulala maana ningeendelea kuzozana na mama yako nadhani ni siku hiyo nd’o ningempiga hadi nimuue. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku iliyofuata nikamuomba ushauri rafiki yangu alichoniambia ni kwamba niende kutazama afya yangu kisha nikiwa salama nimpe talaka yule mwanamke na kisha kuendelea na maisha yangu.
Ni siku hiyo nilipogundua kuwa mama yako licha ya kunidhalilisha na kunitukana hadi kumtukana mama yangu bado alikuwa amefanikiwa kuniambukiza gonjwa hatari la Ukimwi.
Kufikia dakika hiyo mimi nilikuwa wa kufa tu…
Nikashindwa kuiongoza akili yangu, nikaona kuwa siku sahihi ilikuwa hiyo. Lakini niamini mwanangu sikupanga kuua, nilizungumza na mama yako lakini yale majibu yake na kunionyesha waziwazi kuwa ana wanaume wengine nikaona isiwe tabu nikamtandika makofi na hatimaye kikatokea hicho ulichokiona. Acha nikafie jela mwanangu, hata bila jela bado mimi ni wa kufa tu.
Nakupenda sana Kessy!! Naamini sasa upo huru hawatakusumbua tena. Rudi kijijini kautangaze Ukimwi, kawaambie wanakijiji kuwa upo na unaua.”
Baba alimaliza kuzungumza akanisogelea na kunibusu katika paji langu la uso.
Baba yangu alikuwa anatia huruma sana, si mimi tu hata wale maaskari walikuwa wamesononeka.
Sasa niliweza kumtazama vyema usoni, ngozi yake ilikuwa imechujuka sana na macho yake yalikuwa yamebonyea kwenda ndani.
“Mnahitaji kwa mkuu!!” sauti ya askari mwingine ilituita na hapo tukasimama kumfuata, tulifika na kuzungumza kwa dakika kadhaa na mkuuyule akatusifu na kutupatia zawadi nono.
Baba yangu akabaki na pingu zake akarejeshwa katika karandinga akanipungia mkono, nilijikuta natokwa machozi kwa sababu nilijua kuwa huo ni mwisho wa kumuona baba yangu akiwa hai nilitambua kuwa atakufa na alikuwa tayari kufa!!
Nilikumbuka kumueleza mkuu wa kituo juu ya yule bwana aliyeniokoa kutoka katika janga la kuchunwa ngozi nikamtajia na lile jina la baba yake. Wakaniahidi watalishughulikia hilo upesi sana!!!
Naam, baada ya kutoka pale nilimtazama tena Tuse. Nilipomtazama nikaikumbuka ile kauli ya baba yangu kuwa Ukimwi upo na unaua.
Ule urembo wa Tuse ukapukutika nikamuona kama binti wa kawaida kabisa, matamanio niliyokuwanayo yakayeyuka kabisa.
Tuliondoka, tukapata muda wa kuketi na kufahamiana wote wanne kwa pamoja yaani afande Wanchera, mama lao Tuse na mimi.
Siku iliyofuata mama lao na Tuse wakapanda gari kurejea Mbeya. Na afande Wanchera akanisindikiza kijijini kwetu ili tu nikakitangazie kijiji yale aliyoniagiza baba yangu.
Ile siku ninafika nilikuta kwa mjumbe pakiwa na sherehe, ilikuwa ni sherehe ya kumuaga rahma aliyekuwa anaenda katika kituo cha kazi alichokuwa amepangiwa.
Watu walishangaa sana kuniona tena pale kijijini, na ulemukawa wakati muafaka wa kuwasimulia kila kilichotokea.
Kwa kutumia kipaza sauti nilienda na kusimulia kila hatua niliyopitia, nikaelezea jinsi Rahma alivyonisaliti lakini sikumlaumu kwa sababu alifanya nafsi yake ilivyomtuma, nikaelezea juu ya gonjwa hatari la Ukimwi na jinsi ambavyo marehemu mama yangu alimuambukiza baba yangu, nikakisihi kijiji kijitahidi kujua afya zao kabla ya kuendelea na harakati zozote zile.
Maneno yangu yalikuwa kama msumari wa moto yaliwachoma lakini wakabaki tuli wakinisikiliza.
Nilipomaliza hapo nikaisikia nafsi yangu ikiwa katika utulivu kabisa alichoniagiza baba yangu nilikuwa nimelitimiza.
Wakati wanakijiji wakinipigia makofi kwa nguvu sana, nilifumba macho yangu na kujisemea.
“Ningepata wapi nafasi ya kuwa mwalimu kama sio mitihani hii”
JIFUNZE!!
NDOA zinatawaliwa na SIRI ambazo wanazijua wanadoa wenyewe, naam!! Ni vyema kutunza siri za ndoa, lakini kuna baadhi ya wanandoa wanatunza siri ambazo zinawatafuna wao wenyewe, mtazame baba Kessy, ametunza siri kwa sababu ya kulinda tu ndoa yake na heshima ya mkewe lakini kumbe anazalisha mengine makubwa.
Baba Kessy amechukua sura mbili akiwa mfano wa kuigwa kwa wanandoa kwa jinsi anavyotunza siri, lakini si mfano wa kuigwa kwa wale wanaohisi kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI basi ndo mwisho wa maisha.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Amini kuwa ikiwa umepata maambukizi huo sio mwisho wa maisha….
Yapo maisha baada ya maambukizi na ni maisha ya furaha tu hasahasa ukiwa umefuata ushauri nasaha.
Napenda kusema neno moja kwako msomaji, jifunze kupokea furaha sawa na huzuni….. tabu na raha ziliumbwa kwa ajili yetu wanadamu…
MWISHO
0 comments:
Post a Comment