IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sijui atazaliwa mtoto gani.”
“Labda wa kiume.”
“Mmmh! Mimi napenda awe mtoto wa kike ili na sisi tujivunie kwa mara nyingine.”
“Ila yeye mwenyewe si alitaka wa kiume?”
“Nani?”
“Sangiwa!”
“Ndivyo alivyosema?”
“Ndivyo nilivyosikia, eti kwa sababu ana watoto wengi wa kike, hivyo anataka apate na mwingine wa kiume!”
“Mmmh! Nafikiri hizo ni tetesi tu.”
Yalikuwa ni mazungumzo ya wanawake wawili miongoni mwa watu wengi waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba pekee iliyokuwa imeezekwa bati na kujengwa kwa matofali, nyumba ya mzee aliyeaminika kuwa na fedha nyingi katika Kijiji cha Chibe kilichokuwa mkoani Shinyanga.
Kila mtu alitaka kujua ni mtoto gani ambaye angezaliwa na mke wa Sangiwa aliyekuwa na fedha nyingi kijijini hapo. Watu walimpenda Sangiwa kwa kuwa hakuwa mtu wa majivuno, kile alichokuwa nacho, alitamani wengine pia wakipate.
Kipindi cha nyuma alikuwa na maisha magumu, masikini kama watu wengine, alidharaulika sana kijiji hapo, hakuwa na nyumba kwani wazazi wake walipofariki, hata ile nyumba aliyokuwa akiishi, akafukuzwa.
Alipitia maisha magumu, hakuona afadhali ya maisha hata siku moja, kila siku alikuwa mtu wa kuomba misaada tu, wapo waliokuwa wakimsaidia lakini pia kulikuwepo na wale waliokuwa wakimnyima.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipoona kijijini Chibe maisha yalikuwa magumu, hapo ndipo alipoamua kuhama na kuhamia kijiji cha jirani cha Beda. Maisha hayakubadilika, bado aliendelea kuishi kwenye maisha ya kimasikini hali iliyomfanya kwenda kuomba kazi kwa mzee Mwiku aliyekuwa kijijini hapo.
Kwa kuwa mzee huyo alikuwa na ng’ombe wengi, akampa Sangiwa kazi ya kuwa mchungaji wa mifugo yake. Hilo halikuwa tatizo kwa Sangiwa, kwa kuwa alikuwa na shida, hakuwa na fedha, akakubaliana naye na hivyo kuanza kazi hiyo.
Ilikuwa kazi ngumu mno, kitendo cha kuchunga zaidi ya ng’ombe elfu kumi huku akiwa na wenzake wawili tu ilikuwa kazi kubwa. Kuna kipindi wanyama hao walikuwa wakiingia katika mashamba ya watu, waliwafukuza na hata wakati mwingine kusemwa sana huku wakipokea vitisho vya kila aina.
Waliogopa lakini hawakuwa na jinsi, hawakuachana na kazi hiyo, waliendelea kuchunga kila siku. Walipokuwa wakirudi na kufika nyumbani, walitengewa maziwa na ugali na kuanza kunywa.
Hayo ndiyo maisha waliyotokea kuishi, walikubaliana nayo kwa kuwa hawakuwa na lolote la kuweza kufanya. Urafiki wake na wachungaji wenzake, Milenze na Olembetu ukazidi kukua kwa kuwa kila wakati walikuwa pamoja.
“Umemuona Frida?” aliuliza Milenze.
“Frida gani?”
“Mtoto wa bosi.”
“Amefanya nini?”
“Alivyokuwa akikuangalia!”
“Mimi?”
“Ndiyo! Alikuwa akikuangalia sana, mpaka nikashangaa.”
“Haiwezekani, hawezi kuniangalia hivyo, au kama nilikosea kuvaa hii suruali,” alisema Sangiwa.
“Mmmh! Sidhani. Ila nahisi kuna kitu.”
“Kitu gani?”
“Au anakupenda!”
“Anipende mimi masikini?”
“Hata mimi nashangaa!”
Hakukuwa na mtu aliyejiamini, kila mmoja alijiona kuwa masikini hivyo kupenda na msichana aliyetoka katika familia ya mtu mwenye hela lilionekana kuwa tatizo. Siku hiyo, Sangiwa akaamua kufuatilia kujua kama kile alichokuwa akiambiwa kilikuwa kweli au la.
Walipofika nyumbani, wakatengewa chakula na wasichana wa mzee Mwiku akiwemo huyo Frida. Kama alivyokuwa akiambiwa ndicho kilichokuwa kimetokea, muda mwingi Frida alikuwa akimwangalia mpaka kumfanya kijana huyo kuanza kuogopa.
Alikuwa masikini sana, alikuja kijijini hapo akiwa peke yake, hakuwa na kitu chochote kile zaidi ya zile nguo alizokuwa amezivaa. Alikaribishwa kijijini hapo na mwisho wa siku kupewa kazi na mzee huyo.
Hakutaka kuamini kile kilichokuwa kikiendelea, eti msichana ambaye baba yake alikuwa tajiri ampende yeye masikini asiyekuwa na kitu, kwake ulionekana kuwa muujiza mkubwa.
Sangiwa hakutaka kukubaliana na uhalisia uliokuwepo kwamba alipendwa na msichana huyo, alichokifanya ni kuachana naye na kuendelea na maisha yake kama kawaida.
Frida hakupunguza kumwangalia Sangiwa, kila aipokuwa akikaa, macho yake yalikuwa usoni kwa kijana huyo, alitokea kumpenda mno, moyo wake ukatekwa na hakukuwa na njia nyingine ya kufanya zaidi ya kupanga kumwambia ukweli.
“Hivi atanikubalia kweli?’ alijiuliza.
“Sidhani, lakini mbona kama ananiogopa? Mungu! Naomba anikubalie nitakapomwambia ukweli,” alisema Frida huku mapigo yake ya moyo yakidunda mno.
Hakuwa na jinsi, hakutaka kuendelea kuteseka, alitaka kuhakikisha kwamba mvulana huyo anakuwa wake peke yake. Alitumia muda mwingi sana kujipanga ili pindi atakaporudi basi aweze kumwambia ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.
Ilipofika saa 12 jioni, kwa mbali akaona ng’ombe na wanyama wengine wakianza kurudishwa, hakuwa na wasiwasi kwamba hiyo ilikuwa mifugo yao na miongoni mwa wachungaji wale alikuwepo mvulana aliyekuwa akimpenda sana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walipofika, Frida akaanza kupitisha macho yake kuwaangalia wachungaji wale, kitu kilichoonekana kumshtua sana, Sangiwa hakuwepo. “Mmmh! Sangiwa yupo wapi?” alijiuliza pasipo kupata jibu lolote lile.
Moyo wake ukajawa na presha kubwa, kitendo cha kutokumuona kijana huyo akirudi na wachungaji wale kilimshtua kwa kuona kwamba inawezekana kulikuwa na tatizo, au alikimbia kwani vijana wengi kwa kipindi hicho walikuwa wakitoroka sana kuelekea mjini kutafuta maisha.
Hakutaka kukubali, hakujisikia amani moyoni mwake, kwani hata alipokuwa akiangalia kwa mbali katika njia ile waliyokuwa wakiitumia wachungaji, hakuweza kumuona Sangiwa.
“Naomba nikuulize kitu Olembetu,” alisema Frida, aliamua kumfuata mmoja wa wachungaji wale.
“Kitu gani?”
“Sangiwa yupo wapi?” aliuliza Frida.
“Kuna tatizo lilitokea.”
“Tatizo gani?”
“Kwanza baba yupo?”
“Ndiyo! Yupo.”
“Ngoja nikamuone,” alisema Olembetu.
“Kwanza niambie nini kimetokea,” alisema Frida huku akimvuta Olembetu.
“Nitakuja kukwambia, subiri kwanza,” alisema Olembetu na kuondoka mahali hapo.
Frida akawa na hofu moyoni mwake, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo, aliambiwa kwamba kulikuwa na tatizo lililokuwa limetokea lakini kila alipotaka kufahamu tatizo hilo lilikuwa lipi, akakosa jibu.
Akabaki akiwa na presha kubwa, akabaki mlangoni huku akionekana kuwa na mawazo. Hakuwa na hamu ya kula, hakuwa na hamu ya kufanya jambo lolote lile, akili yake yote ilikuwa ikimfikiria Sangiwa tu.
Wala hazikupita dakika nyingi, mlango ukafunguliwa, baba yake, mzee Mwiku akatoka huku akiwa na hasira kubwa, alichokifanya mzee huyo, akachukua viatu vyake vilivyokuwa mlangoni na kuondoka mahali hapo huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa.
Hali hiyo ikamtia hofu Frida.
***** Wachungaji walikuwa kwenye wakati mgumu, walijitahidi kuwazuia ng’ombe wao kwenda katika mashamba ya watu wengine lakini hali hiyo ilikuwa ngumu kwao. Ng’ombe walikimbilia kwenye mashamba ya watu yaliyokuwa na mavuno mengi na kuanza kula mahindi.
Sangiwa, Olembetu na Milenze
waliendelea kujitahidi kuwazuia ng’ombe wale lakini ilishindikana kabisa.
Waliwafahamu vizuri wakulima, mara kwa mara walikuwa wakipambana nao na hata wakati mwingine kuuana kwa kile kinachosemekana kuwa dharau kutoka kwa wafugaji ambao walionekana kuwaachia ng’ombe wao makusudi na kwenda kuvamia mashamba yao.
Kwa kila ng’ombe aliyekuwa akiingia shambani mwao, walikuwa wakiwakamata, wanawachinja na maisha kuendelea.
Wakati Sangiwa na wenzakeCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
waliposhindwa kuwazuia ng’ombe wale na kuingia mashabmbani, tayari wakajua kwamba ugomvi mkubwa ungetokea kwani mara kwa mara tukio kama hilo linapotokea, wakulima hupandwa na hasira na kuwaua ng’ombe au hata kuwachukua wachungaji wenyewe.
Wote walionekana kuwa na hofu, kitendo cha ng’ombe wale kuingia katika shamba la mzee Matumbo tayari kukaonekana kuwa na ugomvi mzito ambao ungetokea. Vijana wa mzee huyo ambao mara kwa mara walikuwa shambani mule wakilima au hata kuhakikisha mazao yanachungwa, walipowaona ng’ombe wale, wakawakamata.
“Jamani tunaomba mtusamehe,” alisema Sangiwa, alionekana kutia huruma, kosa kubwa la kutokuweza kuwazuia ng’ombe wale kuingia shambani mule, tayari kukaonekana kama kungetokea ugomvi mkubwa.
“Kwa nini mmewaruhusu ng’ombe kuingia shambani kwetu?” aliuliza kijana mmoja, alionekana kuwa na hasira tele.
“Hatukuwaruhusu, tulishindwa kuwazuia,” alijibu Sangiwa huku akionekana kuwa na hofu.
“Tunawaua kama kawaida yetu.”
“Naomba msiwaue, nawaombeni tafadhali,” alisema Olembetu huku akipiga magoti.
Wakati maongezi yakiendelea mahali hapo, ghafla mzee Matumbo akatokea mahali hapo, alipowaona ng’ombe wale shambani kwake, akashikwa na hasira kali mno, akaanza kuwasogelea wachungaji wale huku akionekana kuwa na shari kabisa.
“Kwa nini mmewaruhusu ng’ombe wetu kuingia shambani kwangu?” aliuliza huku akionekana kughadhibika.
“Hatukuwaruhsu mzee, naomba utusamehe, walituzidi nguvu,” alisema Sangiwa.
“Ng’ombe wa nani hawa?”
“Mzee Mwiku.”
“Kamuiteni mwenyewe, la sivyo ng’ombe hawatoki hapa,” alisema mzee yule.
“Mzee, tunakuomba utusamehe.”
“Nimesema kamuiteni, kama hamtaki, mmoja wenu abaki na ng’ombe waende.”
“Hakuna tatizo. Acha nibaki mimi,” alisema Sangiwa maneno yaliyoonekana kuwashangaza wenzake wote.
Hakukuwa na cha kufanya, alitaka mwenyewe kubaki ili mladi wale ng’ombe wachukuliwe na kurudishwa nyumbani. Kwa mzee Matumbo, hakutaka kufanya kitu chochote kibaya, alimheshimu sana mzee Mwiku kwa kuwa walifahamiana sana.
Alikuwa mzee tajiri aliyekuwa na mifugo mingi, alipendwa na watu wengi, si katika kijiji chake bali hata watu wa vijiji vingine walimpenda mzee huyo aliyeonakana kuwa na roho ya huruma na kusaidia watu.
Kutaka kijana mmoja abaki, kwake ilikuwa kama nafasi ya upendeleo, hakutaka kuingia kwenye ugomvi na mzee huyo kwani kama jambo hilo lingetokea, mapigano yake yangekuwa makubwa na kusingeweza kupatikana kwa amani milele.
*
*
Mzee Mwiku alikuwa amechanganyikiwa, alipoambiwa kwamba kijana aliyekuwa akimpenda kuliko wote, Sangiwa alikuwa amezuiwa na mzee Matumbo kulimuumiza na hivyo akaamua kwenda huko yeye mwenyewe.
Mwendo wake ulikuwa ni wa harakaharaka, hakutaka kuangalia nyuma, wakati mwingine alikuwa akikimbia kwa kuona kwamba alikuwa akichelewa.
Binti yake, Frida hakutaka kubaki nyumbani, hakutaka kuona mvulana aliyekuwa akimpenda sana, Sangiwa akamatwe sehemu halafu yeye awe na amani nyumbani, alipomuona baba yake akiondoka, naye akaanza kumfuata kwa nyuma, ila alikuwa mbali.
Kila alipokuwa akipiga hatua kadhaa, alikuwa akijificha, hakutaka kuonekana kabisa. Safari iliendelea, baada ya mwendo wa dakika arobaini na tano, wakaanza kuingia katika sehemu kubwa iliyoonekana kuwa kama shamba kubwa, huko ndipo mzee Mwiku alipokutana na mzee Matumbo.
“Afadhali umekuja,” alisema mzee Matumbo.
“Kuna tatizo?”
“Ndiyo lipo. Unamfahamu huyu?” aliuliza mzee Matumbo,.
“Ndiyo namfahamu, ni kijana wangu.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sawa. Ng’ombe wako walirudi tena shambani kwangu,” alisema mzee Matumbo, tayari kigiza kikaanza kuingia.
“Naomba umruhusu aondoke, sisi tubaki tukizungumza kama wazee,” alisema mzee Mwiku, hilo halikuwa tatizo, Sangiwa akaruhusiwa kuondoka.
Njiani hakutaka kutembea, mwendo wake ulikuwa ni kukimbia tu, alitaka kuwahi nyumbani kwani giza lile lililokuwa likikaribia kuingia, lilimuogopesha sana. Alikimbia mpaka alipotoka nje ya mashamba yale, hakutaka kuangalia nyuma, macho yake yalikuwa mbele tu.
Moyoni alimshukuru Mungu, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, kitendo cha kuruhiswa kuondoka huku akijua kwamba kulikuwa na ugomvi mkubwa baina ya wakulima na wafugaji, kwake aliona kama muujiza.
“Sangiwaaaa.....” ilisikika sauti nyuma yake.
Kwanza akaogopa, tayari giza lilibakia dakika chache kukamilika, alipoisikia sauti hiyo, akaogopa, alijua kwamba alikuwa porini, sasa ni nani alikuwa akimuita, hofu ya kudhani kwamba sauti hiyo ilikuwa ni ya jini au mchawi ikamuingia, hivyo akaongeza kasi.
“Sangiwa nisubiri....Sangiwa nisubiri...” ilisikika sauti ile.
Masikioni mwake haikuwa ngeni, aliifahamu vilivyo, ilikuwa ni sauti ya msichana Frida, lakini pamoja na hayo, hakutaka kusimama.
Aliendelea kukimbia mpaka alipofika umbali fulani, sauti ile iliendelea kumuita, akaona bora asimame, kama ilikuwa ni ya jini kama alivyofikiria, hakuwa na jinsi, alikuwa tayari kufa.
Akageuka nyuma, kwa mbali akaanza kumuona mtu akija kwa kasi, mwili wake ukazidi kutetemeka, mapigo ya moyo yakaanza kumdunda kwa kasi kwa kuona kwamba kulikuwa na hatari ambayo ilikuwa ikimsogelea mbele yake.
Akakosa nguvu za kukimbia, kikafika kipindi akajuta kwa nini alisimama kumsubiria mtu huyo aliyekuwa akija kwa kasi, alipokaribia, akamwangalia, alikuwa msichana aliyevalia gauni refu, alipokaribia zaidi, akagundua kwamba alikuwa Frida.
“We Frida, unafanya nini huku porini?” aliuliza Sangiwa huku akionekana kushangaa.
“Nimekufuata wewe.”
“Umenifuata mimi?”
“Ndiyo! Niliambiwa kwamba upo huku. Nini kilitokea?”
“Hapana, hebu twende nyumbani.”
“Subiri kwanza. Niambie,” alisema Frida.
Kadiri walivyokuwa wakiongea na ndivyo msichana huyo alivyozidi kumsogelea Sangiwa mpaka kumfikia karibu kabisa kama watu waliotaka kukumbatiana. Mapigo ya moyo wa Sangiwa yakazidi kudunda, akazidi kuingiwa na hofu, kuwa na binti wa mzee Mwiku porini, tena usiku, kulimtia hofu.
“Frida...” aliita Sangiwa wakati msichana huyo akishika maeneo ya zipu.
“Nakupenda. Naomba unipe.”
“Unasemaje?”
“Naomba unipe,” alisema Frida.
Hata kabla Sangiwa hajasema chochote, ghafla wakaanza kuzisikia sauti za watu wakija kule walipokuwa, zilikuwa kama sauti za watu watatu, walipozisikiliza vizuri, waliigundua sauti ya mtu mmoja, alikuwa mzee Mwiku.
Kila mmoja akaogopa.
“Baba...” alisema Frida huku akionekana kutetemeka.
***** Akili ya Sangiwa ikacheza fasta, aliona kama asingeweza kufanya kitu cha ziada basi wangeweza kuonekana mahali hapo jambo ambalo lingekuwa baya sana kwake, alichokifanya, tena kwa haraka sana ni kumshika mkono Frida na kisha kumpeleka katika kichaka kilichokuwa pembeni.
“Nyamaza, usipige kelele,” alisema Sangiwa kwa sauti ya chini na Frida kutii.
Walikaa pale mpaka walipomuona mzee Mwiku akipita na watu wengine wawili, alikuwa mzee Matumbo na kijana mwingine, walikuwa wakimsindikiza kuelekea Beda.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Waliendelea kubaki kichakani pale mpaka walipopita na ndipo wakatoka na kusimama huku wakiangalia kule wazee wale walipoelekea.
“Si unaona ulitaka kusababisha tukamatwe,” alisema Sangiwa.
“Naomba unisamehe, lakini ninakupenda Sangiwa,” alisema Frida kwa sauti ya chini.
Sangiwa hakutaka kuelewa kitu chochote, alichomwambia ni kwamba walitakiwa kuondoka mahali hapo na kuelekea kijijini tena kwa kupitia njia nyingine tofauti na ile waliyopita wazee wale.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kwa Frida kumwambia Sangiwa kwamba alikuwa akimpenda. Kwa kijana huyo, mambo yalionekana kuwa magumu, hakutaka kuwa na msichana huyo kwa kuwa alifahamu kwamba mapenzi hayakuwa na siri, hivyo kuna siku baba yake angegundua hilo.
Kwa Frida, maisha yalikuwa magumu, hakutaka kuelewa chochote kile, kila siku ilikuwa ni lazima kutafuta muda maalumu na kuzungumza na Sangiwa. Alimuonyeshea dalili zote kwamba alikuwa akimpenda, hakuona kama kulikuwa na umuhimu wa kuficha chochote kile.
Siku zikakatika, Frida, ambaye alipewa jina hilo kama mrithi wa Mzungu aliyewahi kuja mahali hapo, akaendelea kukua zaidi, maungo yake yakatanuka na kifua chake kujaa kitu kilichomuweka Sangiwa kwenye wakati mgumu.
“Leo nahitaji,” alisema Frida huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikisema. Ilikuwa imepita miaka miwili, katika kipindi chote hicho alikuwa akizungushwa tu.
“Haiwezekani.”
“Kwa nini isiwezekane? Mimi si ni mpenzi wako?”
“Ndiyo! Lakini haiwezekani,” alisema Sangiwa huku akionekana kuogopa.
“Hapana, leo utanipa tu, ukikataa namwambia baba ulitaka kunibaka,” alisema Frida.
Maneno hayo aliyokuwa amezungumza yalionekana kuwa mwiboa mkali moyoni mwa Sangiwa, hakuonekana kutania hata kidogo, alimaanisha kile alichokuwa akikizungumza kwamba endapo asingekubali kufanya naye mapenzi basi ilikuwa ni lazima kumwambia baba yake kwamba alitaka kumbaka.
Kwa Sangiwa ukawa mtihani mgumu, hakutaka binti huyo akamwambie baba yake, alichokifanya, tena kishingo upande ni kukubaliana naye tu na mchezo kufanyika.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kila kitu, wakazidi kupendana kila siku mpaka kikafika kipindi ambacho Sangiwa akaacha mzee Mwiku ajue, na mambo yalipogundulika, Sangiwa akaamua kumuoa msichana huyo na kupewa ng’ombe themanini kama zawadi ya kuanza maisha yake.
Haohao ng’ombe ndiyo waliobadilisha maisha yao, Sangiwa alikuwa na akili ya maisha, kupitia ng’ombe hao, waliongezeka, akaanza kuwakamua maziwa na kisha kwenda kuyauza mjini Shinyanga.
Ilikuwa biashara kubwa na yenye wateja wengi ambapo kidogokidogo akaanza kufanikiwa. Maisha yake yakabadilika na mpaka mwaka mmoja ulipopita, mkewe akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume aliyempa jina la Malima.
Maisha yaliendelea zaidi. Mwaka wa tatu ulipoingia baada ya kuishi maisha ya ndoa na mkewe, wakapata wageni Wazungu kutoka nchini Uingereza ambao walifika hapo kwa ajili ya kueneza elimu ya ufugaji katika vijiji mbalimbali.
Miongoni mwa Wazungu hao wanne waliofika kijijini hapo alikuwepo msichana mrembo aliyeitwa kwa jina la Tatiana.
Wazungu hao walikuwa msaada mkubwa, hawakuwa na maisha ya kifahari kijijini hapo, walisaidiana na wanakijiji wengine kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Tatiana ambaye alionekana kuwa mrembo zaidi, kila siku akawa akiamka asubuhi na kuwakusanya watoto wengi na kuanza kucheza nao. Maisha ya kijijini yakawa tofauti, amani ikatawala, watu wengi wakawapenda Wazungu hao walioonekana kuleta mabadiliko makubwa.
“Ni msichana mrembo, anavutia machoni kwa kila mwanaume,” alisema jamaa mmoja, aliyagandisha macho yake usoni mwa Tatiana aliyekuwa akicheza na watoto.
“Kwa mfano ukawa na msichana kama huyu, yaani kwa mfano tu, halafu akakupenda, hivi si itakuwa balaa kijijini!” alisema jamaa mwingine.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo hivyo! Anavutia sana jamani.”
Tatiana akawa stori ya kijijini hapo, watu waliendelea kumpenda sana. Mpaka mwezi wa sita unaingia baada ya kukaa kijijini hapo, Wazungu wale wakaamua kuondoka kurudi nchini Uingereza kitu kilicholeta majonzi makubwa.
Mwaka uliofuata, Mwiku akapata watoto wawili, walikuwa mapacha, aliwapenda mno, aliwajali na mapenzi zaidi yakawa kwa mkewe. Hiyo ndiyo ilikuwa familia yake, alipata watoto watatu kwa mke wake, hakutaka tena kuwa na mtoto mwingine, alimshauri mkewe kukubaliana naye, wote wakakubaliana kwamba hao ndiyo wangekuwa watoto wa mwisho.
Maisha yalibadilika, baada ya mzee Mwiku kufariki, akaamua urithi wake wote auache kwa mtoto wake, Frida ambaye hakuwa mbinafsi, akawagawana na watoto wengine, kila mmoja akaondoka zake, waliotaka kuuza, waliuliza na waliotaka kuziendeleza mali hizo wakiwemo ng’ombe, walifanya hivyo.
Baada ya mwaka kupita, Sangiwa akashauri wahame hapo na kuhamia katika Kijiji cha Chibe alipozaliwa, Frida hakuwa na kipingamizi, wakahamia huko.
Kila mtu aliyemuona Sangiwa alishangaa, walimfahamu sana, alikuwa kijana masikini ambaye aliondoka kijijini hapo, sasa ilikuwaje awe na mali nyingi, tajiri kiasi hicho?
Alipoingia hapo Chibe tu, kitu cha kwanza ni kujenga nyumba ya kisasa, iliyojengwa kwa matofali na kuezekwa mabati. Kila mwanakijiji akamuheshimu kijana huyo aliyekuwa masikini wa kutupwa kipindi cha nyuma.
“Mume wangu,” aliita Frida.
“Unasemaje mke wangu?”
“Nahisi nina mimba.”
“Unasemaje?”
“Nahisi nina mimba,” alisema Frida huku akiwa amelishika tumbo lake, Sangiwa akachanganyikiwa kwani hakutegemea kupata mtoto mwingie.
“Hebu nione tumbo.”
Akaligusa tumbo la mke wake, Frida.
“Mmmh!” alijikuta akiguna.
*****
Wote wawili hawakutaka kuwa na mtoto lakini haikuwa na jinsi, tayari Frida alikuwa mjauzito kitu kilichomkasirisha kila mmoja. Hawakuwa na jinsi, kile walichokuwa hawakitaki kilikwishatokea hivyo walitakiwa kukubaliana na ukweli wenyewe.
Sangiwa akamuahidi mke wake kwamba angekuwa naye bega kwa bega kuhakikisha mimba inakuwa salama na mwisho wa siku kujifungua mtoto mzuri aliye na afya bora kama alivyofanya vipindi vyote ambavyo Frida alikuwa mjauzito.
Siku zikaendelea kukatika, miezi ikasonga mbele na hatimaye baada ya miezi tisa kukamilika, watu wakajikusanya nje ya nyumba yake kwa ajili ya kusikia ni mtoto wa jinsia gani ambaye angezaliwa siku hiyo.
Kila mtu aliyekuwa mahali hapo alionekana kuwa na furaha, roho nzuri aliyokuwa nayo Sangiwa iliwafanya watu wengi kumpenda na kumtakia mafanikio katika maisha yake yote.
“Natumaini Mungu atakuwa pamoja na mkeo,” alisema mwanaume mmoja, alikuwa akimwambia Sangiwa.
“Natumaini hilo, nina furaha ya ajabu, hatimaye mtoto wangu wa nne anazaliwa,” alisema Sangiwa huku akichia tabasamu pana.
Dakika ziliendelea kusonga mbele, baada ya dakika hamsini, mwanamke mmoja akatoka ndani ya chumba kile, alionekana kuwa na furaha mno huku akiwa na presha kubwa.
Mwanamke yule akaanza kutembea kwa mwendo wa harakaharaka kuelekea kule alipokuwa Sangiwa na wanaume wengine, alikuwa na taarifa nzuri ya kumpa Sangiwa juu ya kile kilichokuwa kimeendelea mule ndani.
“Kuna nini?” aliuliza Sangiwa.
“Hongera sana.”
“Mtoto gani?”
“Wa kike.”
“Unasema kweli?”
“Ndiyo! Ni mzuri kama mama yake,” alisema mwanamke yule.
Sangiwa hakutaka kubaki hapo, alichokifanya ni kusimama na kuanza kuelekea kule ilipokuwa nyumba yake. Kwa kumwangalia tu, wala isingekupa wakati mgumu kugundua kwamba alikuwa na furaha mno.
Alipoifikia nyumba ile, akaufungua mlango na kuingia ndani. Alichokiona ndicho alichoambiwa, mke wake, Frida alikuwa hoi, wanawake waliochukua nafasi za manesi, wakunga walikuwa pembeni yake huku mmoja wao akiwa amembeba mtoto huyo aliyekuwa akilia mfululizo.
Akaanza kupiga hatua mpaka pale aliokuwepo mke wake na kisha kuushika mkono wake. Frida alipomuona mume wake tu, akaachia tabasamu pana.
“Hongera sana me wangu,” alisema Sangiwa.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nashukuru sana.”
“Unamkumbuka Tatiana?”
“Ndiyo!”
“Naomba tumpe jina hilo kama ukumbusho wa Mzungu yule,” alisema Sangiwa.
“Hakuna tatizo.”
*****
Tatiana alikuwa msichana mzuri, uzuri aliourithi kutoka kwa mama yake. Alivutia kwa kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia kiasi cha wengi kusema kwamba angeweza kuwa miongoni mwa wasichana ambao wangekuja kutikisa sana katika Kijiji cha Chibe na vijiji vingine pia.
Alichukua kila kitu kutoka kwa mama yake, kwa kumwangalia, kwa mbali Tatiana alionekana kuwa na mchanganyiko wa rangi, alipendwa na kila mtu huku watu wengine wakitaka kumbeba, mikono yao kuwa na mtoto kama Tatiana ilikuwa ni faraja kubwa.
Frida alimlea mtoto wake kwa mapenzi ya dhati, alikuwa akimbembeleza kila alipokuwa akilia huku kila siku akimnyonyesha kitu kilichomfanya kuwa na afya njema kabisa.
Wakati mwezi wa sita unakatika, Frida akahisi kwamba mtoto wake alikuwa na tatizo kwani kila alipokuwa akiuchezesha mkono wake mbele ya uso wa Tatiana kwenda huku na kule, mboni za Tatiana wala hazikucheza.
“Mmmh!” aliguna Frida.
Hali hiyo ilimshangaza, haikuwa kawaida kwani alikuwa na watoto, tangu walipokuwa na muda huo, kila alipokuwa akiuchezesha mkono wake, zile mboni nyeusi zilikuwa zikihama kwenda huku na kule kuufuata mkono ule.
“Huyu mtoto ana nini?” aliuliza Frida.
“Kwa nini?”
“Mboni zake hazichezi kabisa.”
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo! Hebu jaribu kuchezesha vidole vyako mbele yake,” alisema Frida, alikuwa akimwambia mumewe, Sangiwa ambaye akafanya hivyo, kweli mboni hazikuwa zikicheza.
Hilo likaonekana tatizo kubwa, wazazi hao wakachanganyikiwa, wakajua kwamba kulikuwa na kitu hakikuwa sawa kabisa, walichokifanya ni kusafiri mpaka Shinyanga mjini ambapo huko wakampeleka katika Hospitali ya mkoa ambapo madaktari wakaanza kumpima na kugundua tatizo.
“Poleni sana,” alisema daktari kwa sauti ya taratibu.
“Kuna nini? Mbona pole tena?”
“Mtoto wenu ni mzuri ila ni kipofu.”
“Unasemaje?”
“Tatiana ni kipovu, ana upofu wa kuzaliwa,” alijibu daktari yule.
Frida akashindwa kujizuia, majibu ya daktari yule yalimfanya kuhuzunika na baada ya sekunde chache tu, akaanza kulia kama mtoto huku akimlaumu Mungu kwa kile kilichotokea.
Mume wake, Sangiwa akashindwa kumfariji kwani hata na yeye alikuwa akibubujikwa na machozi tu, moyo wake ulimuuma pia mpaka kufikia kipindi akahisi hasira zake zikipanda dhidi ya Mungu.
Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama mtoto wake wa mwisho ambapo baada ya hapo angejizuia kuzaa tena alikuwa kipofu, kila alipokuwa akimwangalia, moyo wake uliendelea kumuuma mno.
Hawakuwa na jinsi, wakarudi kijijini huku wakiwa na huzuni tele. Hawakutaka kuficha chochote kile, wakawaambia wanakijiji wengine ambao walizipokea taarifa hizo wakiwa na majonzi tele.
“Poleni sana.”
“Asanteni, haina jinsi, kila kitu ni mipango ya Mungu,” alisema Frida huku akiendelea kububujikwa na machozi.
Huo ndiyo uliuwa mwanzo wa kila kitu. Mtoto Tatiana akaanza kukua, alipofikisha mwaka mmoja, akaanza kujifunza kutembea. Hapo ndipo Frida alipoumia zaidi, kila alipomwangalia mtoto wake, alikuwa akipapasa kila alipokwenda, hakuona, aliishi kwa hisia, kuna wakati alikuwa akijikwaa na kudondoka, alisimama na kuendelea tena.
Si Frida tu aliyemuonea huruma Tatiana bali hata wanakijiji wengine. Miaka ikakatika zaidi, uzuri wake ukaanza kujidhihirisha mbele ya watu wengine, baada ya miaka kumi, Tatiana akawa msichana mrembo, alikuwa akisoma lakini vitabu vyake vyote vikiwa na alama za nukta tu.
Hakuona kitu chochote kile, alinyimwa uwezo wa kuona lakini darasani, Tatiana alikuwa mwanafunzi mwingine kabisa. Uwezo wake mkubwa ukamshangaza kila mtu. Wengi walisema kwamba alikuwa genius kwani hata kama hakuwepo shuleni, kile walichokuwa wakifundishwa wanafunzi wengine kilipotoka katika mitihani, alifanya vizuri na kuongoza.
Baada ya kufikisha miaka kumi na tano, Tatiana akamaliza kidato cha nne. Urembo wake, ukaendelea kuwapagawisha wavulana wengi kijijini pale. Alikuwa mkimya, kila alipokaa, pembeni kulikuwa na fimbo yake ambayo ilimuongoza kutembea kila alipotaka kwenda.
“Mama...” aliita Tatiana.
“Unasemaje binti yangu?”
“Hivi kuna siku nitaweza kuona?”
“Mmmh!” kwa kweli sifahamu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Natamani nione, najiona kutokukamilika pasipo kukuona mama yangu kipenzi, ninapenda nione kama wengine mama,” alisema Tatiana huku machozi yakianza kumbubujika.
Frida akashindwa kujizuia, maneno aliyoyazungumza binti yake yaliuchoma moyo wake vilivyo. Ni kweli alijua kwamba binti yake alikuwa na kiu ya kutaka kuona tena lakini hakuwa na jinsi, alizaliwa akiwa hivyo, walimpeleka katika hospitali nyingi lakini huko kote walisema kwamba kama alizaliwa hivyo, asingeweza kuona tena.
Mbali na kuwa kipofu, Mungu alimpa uzuri wa sura na umbo, wanaume wengi waliokuwa wakimwangalia, walimmezea mate lakini msichana huyo hakutaka kukubaliana na mtu yeyote, hakuamini kama hapa duniani kungekuwa na mwanaume ambaye angependa kuwa na mke kipofu.
Uzuri wake wa sura aliokuwa amepewa, haukuwa peke yake bali Tatiana alipewa na uwezo mkubwa wa kuimba. Alikuwa na sauti nzuri, kanisani, alikuwa mwanakwaya, tena yule aliyewaongoza wote.
Alipokuwa akiimba, kila aliyeisikia sauti yake, alikiri kwamba hawakuwahi kumuona msichana aliyekuwa akiimba kwa sauti nzuri kama Tatiana. Kanisa lilipokuwa likiandaa mikutano kijijijini hapo au hata kwenye vijiji vya jirani, Tatiana ndiye alikuwa muimbaji kiongozi, sauti yake, ilizitetemesha ngoma za masikio ya watu wengi.
“Daah! Huyu msichana ana sauti nzuri mno, aiseee, anaimba kama Celine Dion,” alisema kijana mmoja, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wamehudhuria mkutano wa Injili uliokuwa ukiendelea.
“Kweli, hebu isikie inavyojichuja masikioni, aiseeee, hii sauti ya kumtoa nyoka pangoni kaka,” alisema kijana mwingine.
Msichana Tatiana alikuwa akiimba jukwaani, ulikuwa mkutano maalum ulioandaliwa na mhubiri kutoka jijini Mwanza aliyeitwa kwa jina la Christopher Lazaro, mkutano huu uliitwa Deliverence (Ukombozi)
Sauti yake kali na yenye mvuto ndiyo iliyowavuta watu waliokuwa mbali mpaka katika mkutano ule. Hawakuamini kama mtu aliyekuwa akiimba alikuwa binadamu wa kawaida, walipofika hapo na kuangalia jukwaani, msichana Tatiana alikuwa akiendelea kumsifu Mungu tu.
Hakukuwa na mtu aliyegundua kama msichana yule alikuwa kipofu, pale jukwaani, alikuwa akitembea huku na kule lakini waimbaji wenzake walikuwa makini kumwangalia, kama angekosea hatua, wangemuwahi na kumdaka.
Baada ya kipindi cha kusifu na kuabudu, mchungaji Lazaro akakaribishwa na kuanza kuhubiri mkutanoni hapo, mahubiri yaliyochukua dakika arobaini tu kisha mkutano kufungwa.
“Unaimba vizuri sana mpendwa,” alisema kijana mmoja, sauti yake ilisikika vizuri masikioni mwa Tatiana.
“Utukufu kwa Mungu!” alisema msichana huyo huku akiachia tabasamu pana.
“Hivi unaitwa nani?”
“Naitwa Tatiana, wewe?”
“Naitwa Peter Lazaro, mtoto wa huyu mchungaji aliyetoka kuhubiri,” alijibu kijana huyo.
“Nashukuru kukufahamu.”
“Usijali. Unaishi hapahapa kijijini?”
“Ndiyo! Nipo hapahapa.”
“Nimefurahi kukufahamu,” alisema Peter.
“Asante. Karibu tena,” alisema Tatiana.
Uzuri wa msichana huyo ukaichanganya akili ya Peter, hakuamini kama duniani kulikuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa Tatiana, alimwangalia vizuri, sura yake ‘iliita’
Peter hakuwa na raha tena, muda mwingi alionekana kuwa na mawazo huku akitumia wakati dakika kumwangalia Tatiana ambaye alikuwa akifuatwa na watu wengi kisha kupewa pongezi kutokana na huduma aliyoitoa, na kila aliposifiwa, alijibu ‘Utukufu kwa Mungu’.
Mpaka watu wanatawanyika mkutanoni hapo, bado Peter alikuwa akimfikiria msichana huyo kipofu. Kesho ilipofika na mkutano kuanza tena, kitu cha kwanza kabisa mara baada ya kufika uwanjani hapo, Peter akaanza kumtafuta Tatiana, alitaka kuzungumza naye hata kabla mkutano haujaanza.
“Nataka nimuone Tatiana,” alisema Peter, alikuwa akiwaambia baadhi ya wanakwaya.
“Yupo kule ndani, chini ya jukwaa anasali,” alijibu mwanakwaya mmoja.
Peter hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuelekea kule alipoambiwa kwamba Tatiana alikuwa akisali, alipofika, akalifunua turubai lililoziba jukwaa lile kwa chini na kuchungulia, macho yake yakamuona Tatiana akiwa amepiga magoti huku mikono yake akiwa ameikutanisha.
Peter akaachia tabasamu pana, moyo wake uliokuwa na mawazo lukuki juu ya msichana huyo, ukafarijika kupita kawaida, akakenua na kuanza kumfuata msichana huyo, alipomfikia, akasimama pembeni yake.
“Wewe nani?” aliuliza Tatiana mara baada ya kumaliza kusali.
“Peter.”
“Umekuja kufanya nini?”
“Kusali pamoja nawe Tatiana,” alijibu Peter.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tatiana alikuwa akiogopa mno, mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu. Pale walipokuwa, haikuwa sehemu salama hata kidogo, sehemu nzima ilikuwa imefunikwa kwa turubai na walikuwa wawili tu sehemu hiyo. Alichokifanya Tatiana ni kuchukua fimbo yake na kuanza kujiongoza mpaka nje ya jukwaa lile.
Peter alikuwa akimfuata kwa nyuma, moyo wake uliumia sana kwani pamoja na msichana huyo kuwa mzuri vile, alikuwa kipofu kitu kilichomfanya kuwa na hamu ya kufanya muujiza ili msichana huyo aweze kuona.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kila kitu. Peter akafa na kuoza kwa msichana huyo ambaye hakuwa na hisia zozote zile za kimapenzi kwake. Katika siku saba za mkutano huo wa injili, bado Peter alikuwa akijitahidi sana kuwa karibu na Tatiana.
“Unaishi wapi?”
“Hapahapa.”
“Nyumba gani?”
“Kwa mzee Sangiwa.”
“Wala simfahamu huyo.”
“Ukiuliza utapafahamu tu.”
“Sawa. Ningependa tuwe marafiki Tatiana.”
“Marafiki?”
“Ndiyo! Tuwe tunapeana Neno la Uzima,” alisema Peter.
“Mmmh!”
“Nini tena?”
“Kuna urafiki kati ya mwanaume na mwanamke kweli?”
“Hata kama haupo, acha sisi ndiyo tuuanzishe, unaonaje?”
“Sawa, ila shetani asije akaingia kati.”
“Hakuna kitu kama hicho, nakuahidi, tena nitafunga na kuomba asiingie,” alisema Peter.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki wao. Japokuwa kwa Tatiana aliona kuwa urafiki wa kawaida lakini kwa Peter hali ilikuwa tofauti kabisa, kitu alichokifikiria ni msichana huyo kuwa mpenzi wake tu.
Siku hiyohiyo akaamua kufika mpaka kwa kina Tatiana ambapo akakutana na ndugu zake, wazazi wake na kuzungumza nao huku akitambulishwa kama rafiki, mtoto wa mchungaji Lazaro.
“Unaishi wapi?”
“Kwa kawaida ni Mwanza, ila kwa sasa nipo likizo, nasoma hapo Buluba Secondary hapo Shinyanga,” alijibu Peter.
“Kidato cha ngapi?”
“Cha tano.”
“Sawa. Nimefurahi kukufahamu zaidi.”
“Asante.”
Kesho yake, mchungaji Lazaro, timu yake ya wanakwaya na watu wengine wakaanza safari ya kurudi jijini Mwanza. Kwa Peter, yalikuwa ni maumivu makali ya moyo, alimpenda sana Tatiana kiasi kwamba kila siku alitamani sana akae naye karibu na kufanya mambo mengine.
Alikuwa mzuri wa sura, na hata kwenye mambo ya dini, msichana huyo hakuwa nyuma kitu kilichompelekea kuona kwamba endapo angewaambia wazazi wake kuhusu Tatiana wangefurahi pia.
Walipofika Mwanza, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutafuta njia ya kuwasliana na Tatiana, hakujua ni kwa namna gani angeweza kuwasiliana na msichana ambaye alikuwa ndoto ya maisha yake.
“Nitamuandikia barua,” alisema Peter. Alichokifanya ni kuzungumza na baba yake ili apate anuani ya lile kanisa walilokuwa wameitwa kijijini kule kwa ajili ya mkutano, akapewa, hivyo kazi ikabakia kwake kumwandikia barua msichana huyo.
Peter alikuwa amedhamiria kumwandikia barua msichana huyo pasipo kukumbuka kwamba alikuwa kipofu. Siku iliyofuata, akaandika barua ndefu iliyojaza maneno matamu ambapo moja kwa moja akaelekea mjini ambapo huko akaituma kwa njia ya posta tena huku akiwa ameinyunyizia na manukato yaliyokuwa yakinukia vizuri.
Hakutaka kupoteza muda mjini, alichokifanya ni kurudi nyumbani huku akionekana kuwa na furaha tele. Katika kila alilokuwa akilifanya, bado kichwa chake kilimkumbuka msichana huyo ambaye alionekana kuwa kila kitu.
Usiku, usingizi wake ulikuwa wa mang’amung’amu, hakulala hata mara moja kutokana na mawazo mazito aliyokuwa nayo juu ya msichana huyo mrembo.
“Mmmh!” Peter alitoa mguno.
Hapo ndipo alipokumbuka kwamba msichana aliyekuwa amemtumia barua ile, Tatiana hakuwa mzima wa macho, alikuwa kipofu kwa asilimia mia moja, akaanza kujiuliza ni kwa namna gani ujumbe ule ungeweza kumfikia na kuusoma.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Barua ilijaza maneno mengi ya kimapenzi, alifahamu kwamba Tatiana aliheshimika sana kijijini kwa kuwa alikuwa mtu wa dini sana, lakini kitendo cha kumwandikia barua ile kilimaanisha kwamba ni lazima barua ile apewe mtu fulani na kumsomea, je hilo lisingekuwa tatizo kwake?
Tayari akaanza kupata mawazo mengine, hayakuwa mawazo mazuri bali yalikuwa mabaya ambayo aliona kwa namna moja au nyingine ingeweza kumuharibia msichana huyo aliyeaminika sana katika suala zima la dini.
Hakutaka kujali sana, kama kosa alikwishafanya hivyo alichokuwa akikisubiri kwa wakati huo ni kuona kitu gani kingetokea, kama lingekuwa tatizo kwake, basi alikuwa tayari kukabiliana nalo.
****
Tatiana aliendelea kumtumikia Mungu kupitia uimbaji wake kanisani. Moyo wake ulikuwa ukifarijika mno kila alipokuwa akikumbuka kwamba pamoja na kuwa msichana kipofu lakini bado Mungu alikuwa na mipango mingi na maisha yake.
Hali aliyokuwa nayo ilikuwa imekwishazoeleka maishani mwake. Tangu azaliwe, hakuwahi kumuona mtu yeyote zaidi ya kusikia sauti zao huku akiwa na hisia kali kwamba mtu aliyesimama mbele yake alikuwa nani na katika umati wa watu uliokuwa mbele yake, kulikuwa na watu wangapi.
Kila mtu kijijini alimuheshimu msichana huyo ambaye kwa kipindi hicho alikuwa akisubiria majibu ya mtihani wake wa kidato cha nne aliokuwa ameufanya.
Hakumkumbuka Peter, alimchukulia kama rafiki yake wa kawaida ambaye angeweza kuja na kuondoka, kwake, Mungu alikuwa wa kwanza, walifuata wazazi wake na watu wengine, lakini kwa Peter, hakukuwa hata na siku moja ambayo aliweza kumkumbuka.
Baada ya kupita siku kadhaa tangu Peter aondoke kijijini hapo, akasikia kanisani mtu wa matangazo akitangaza kwamba kulikuwa na barua moja ambayo alikuwa ametumiwa Tatiana.
Kwanza kanisa zima halikuamini, si wao tu bali hata Tatiana mwenyewe hakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angeweza kumtumia barua na wakati kila mmoja alifahamu kwamba alikuwa kipofu.
Ukiachana na maswali yote aliyokuwa akijiuliza, pia alijiuliza kuhusu mtumaji wa barua hiyo nani. Hakuwahi kutoa anuani za kanisa kwa mtu yeyote yule, sasa ilikuwaje leo hii apokee barua kutoka kwa mtu ambaye hakuamini kwamba alikuwa akimfahamu?
Hakutaka kujiuliza sana, alichokifanya ni kuchukua barua hiyo na muda wa kwenda nyumbani ulipofika, akaondoka huku akitangulizana na mama yake.
Moyo wake ulikuwa na kimuemue cha kutaka kuona humo ndani ya barua hiyo kuliandikwa nini. Alitamani afike nyumbani haraka iwezekanavyo na amwambie mama yake amsomee barua ile ambapo mpaka katika kipindi hicho, hakumfahamu mtumaji.
Baada ya kufika nyumbani, akaelekea chukmbani kwake na kutulia. Mkononi alikuwa na barua ile, kazi yake kubwa ilikuwa ni kuipapasa tu na kisha kuifungua, hakuweza kuona chochote kile, alichoklifanya ni kumuita mama yake.
“Unasemaje binti yangu?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sijui hii barua nimeandikiwa na nani.”
“Nikusaidie nini Tatiana? Kuisoma”
“Ndiyo! Nataka unisaidie kusoma mama,” alijibu Tatiana huku akinyoosha mkono wake na kumpa mama yake barua ile.
Bi Frida akaipokea na kisha kukaa kitandani pale. Kabla ya kuisoma kwa sauti, akaanza kuisoma kimoyomoyo, akatoa mguno uliomchanganya Tatiana ambaye akashikwa na hamu zaidi ya kutaka kujua kilichoandikwa ndani.
“Inasemaje mama?”
“Ni barua nzuri na mbaya pia.”
“Kwa nini? Nani ameandika?”
“Peter!”
“Peter?”
“Ndiyo.”
“Peter nani?”
“Lazaro! Yule mtoto wa mchungaji.”
“Ameandikaje?”
“Subiri nikusomee,” alisema bi Frida.
Tatiana akajiweka vizuri kitandani pale, alitaka kusikia maneno aliyoyaandika Peter katika barua ile. Alitaka kujua kila neno kwani aliamini kwamba mguno wa mama yake ulitokana na maneno yaliyoandikwa ndani ya barua ile, hivyo naye alitaka kuyasikia. Barua hiyo iliandikwa hivi.... Kwako Tatiana.
Namshukuru Mungu kwa kutufikisha nyumbani salama, nashukuru kwa maombi yako na kanisa kwa ujumla. Sisi huku kwa upande wetu, tupo salama na tunaendelea vizuri na majukumu.
Dhumuni la barua hii ni kutaka kukushukuru kwa kila kitu, hasa kwa kukubali urafiki pamoja nami. Tattie nashindwa kujizuia, naomba unisamehe kama nitakuwa nimekosea sana kwa kuvuka mipaka juu ya kile tulichokuwa tumekubaliana kwamba tuwe marafiki tu.
Kiukweli umetokea kuuteka moyo wangu sana (Kama ni dhambi, Mungu anisamehe). U msichana mzuri sana, mwerevu, na ninafurahia kuona kwamba unampenda Mungu na umetoka katika familia za wokovu kama nilivyo mimi.
Tattie, siwezi kukaa kimya, siwezi kuvumilia kutokukwambia hili kwamba umeuteka moyo wangu vilivyo. Sijui niseme nini, ninakupenda zaidi ya maelezo, kama ningeambiwa ni kitu gani nichague ili niendelee kuwa nacho maishani mwangu, hakika ningekuchagua wewe.
Sitaki kukuchezea, sitaki tuishie hapa, ninataka kuendelea kuishi na wewe milele, ninataka nikuoe na mwisho wa siku nawe uwe mama mchungaji kama alivyokuwa mama yangu. Natamani nikuone, natamani nije tena huko kwa ajili yako tu.
Naomba ujifikirie juu ya hilo na unijibu haraka sana kwani kila ninapokaa chumbani, nahisi kuna siku naweza kufa kwa kukuwaza wewe, na kama si kufa, basi naweza kupata presha itakayonilaza kitandani miaka yote.
Nakupenda Tattie, natumaini kupokea majibu hivi karibuni kama upo tayari kuwa na mimi au ndiyo unaamua kunichinjia baharini.
Mungu akulinde.
Peter Lazaro
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni barua ndefu, baada ya bi Frida kumaliza kuisoma, uso wa Tatiana ulijawa na tabasamu pana, maneno matamu yaliyoandikwa ndani ya barua ile yakaufanya moyo wake kufarijika mno.
Hakujali kama mbele yake alikuwepo mama yake, barua ile iliugusa moyo wake kupita kawaida. Mama yake aliyekuwa mbele yake, akamsogelea na kumkumbatia, bi Frida akashindwa kujizuia, machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.
Tatiana alikata tamaa, hakuamini kama kwenye maisha yake angetokea mwanaume ambaye angetamka kwamba alikuwa akimpenda mno. Mbali na uzuri aliokuwa nao, alikuwa msichana kipofu ambaye angeshindwa kufanya kitu chochote katika maisha yake, kitendo cha kusikia kwamba Peter alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, kwake ikaonekana kuwa faraja kubwa.
Hicho ndicho kilichokuwepo hata kwa mama yake, hakutegemea kama ingetokea siku ambayo angekuja mwanaume na kumwambia kwamba anampenda na alitaka kumuoa na hatimaye waishi milele.
Hata kama walimpenda Mungu, hawakutaka kufanya dhambi lakini barua ya Peter ikawafanya wabubujike na machozi muda wote. “Mama! Ninapendwa....” alisema Tatiana huku akilia kama mtoto.
“Unapendwa mwanangu, Mungu amekuletea mwanaume atakayekuwa bora katika maisha yako,” alisema bi Frida huku akijitahidi kuyafuta machozi yake.
Barua ile, ikaifanya mioyo yao kubadilika na kufurahi sana, ila pamoja na hayo, hawakutaka mzee Sangiwa afahamu chochote kile.
“Nimwambieje?”
“Mwambie umekubaliana naye.”
“Kweli?”
“Ndiyo! Huyu mwanaume ameletwa na Mungu! Hii ni baraka,” alisema bi Frida.
Tatiana akaanza kuandika barua ya majibu. Japokuwa alikuwa kipofu, ila alikuwa na uwezo wa kunyoosha mwandiko, hasa kwenye karatasi.
Ila mbali na hayo, alijua kwamba kulikuwa na mapenzi pasipo maumivu, yaani angependa na kupendwa siku zote, asingeumizwa kitu ambacho hakikuwa kweli, kwa kuwa alikubali kuingia kwenye mapenzi, basi ilimpasa kukubaliana na maumivu pia kitu ambacho hakuwa akikielewa kwa wakati huo.
Hakukuwa na kipindi ambacho Peter alikuwa kwenye presha kubwa kama kipindi hicho, kila siku alikuwa mtu wa kusikilizia kama barua aliyokuwa akiihitaji ilikuwa imeingia au la. Yeye ndiye aliyemwambia baba yake kwamba katika kipindi ambacho atakuwa hapo nyumbani, basi apewe ufunguo wa posta ili aweze kuwa nao.
Hilo halikuwa tatizo, kila siku ilikuwa ni lazima aende kuangalia kwenye sanduku la posta ili kuona kama ametumiwa barua na msichana huyo au hakuweza kuandika kwa kuwa alikuwa kipofu.
Baada ya wiki moja, alipokwenda kufungua sanduku la barua, macho yake yakatua katika bahasha moja ndogo, ilikuwa na karatasi huku kwa juu ya ile bahasha kukiwa na jina lake. Moyo ukamlipuka, hakuamini kama ile barua alikuwa ametumiwa yeye au aliona vibaya, akaichukua na kuanza kuiangalia vizuri, liliandikwa jina lake.
Hakutaka kuchelewa, nyumbani alipaona mbali, alichokifanya, hapohapo akaifungua barua ile, kitu cha kwanza kukutana nacho ilikuwa ni harufu nzuri ya manukato yaliyoichezesha pua yake na kumfanya kusahau kama alikuwa posta kulipokuwa na watu wengi.
“Mungu wangu! Mpaka kopa,” alisema Peter huku akiwa ameifungua bahasha ile na kukutana na mchoro wa kopa.
Nyumbani kulikuwa mbali, hakutaka kwenda kuisoma barua hiyo nyumbani kwao, alichokifanya ni kwenda pembeni na kisha kuifungua.
“Naweza nikanyeshewa na mvua au kugongwa na gari na barua nisiiisome, ngoja niisome hapahapa,” alisema Peter na kukaa chini, pembeni kidogo na sehemu iliyokuwa na masanduku yale ya posta.
Kwako Peter.
Nashukuru kwa barua yako iliyonisisimua, imenifanya kujiona nikiingia kwenye ulimwengu mpya ambao sikuwa nikiutarajia kwamba ningeingia. Siwezi kuandika mengi, ila kila kitu tumshirikishe Mungu kwani yeye ndiye wa kutufanya tuje kuoana.
Nakutakia maisha mema, nakupenda.
Tatiana Sangiwa.
Peter akashusha pumzi nzito, japokuwa mwandiko ulikuwa umepinda lakini aliyaelewa vizuri maneno yaliyokuwa yameandikwa. Pasipo kutarajia akajikuta akiibusu barua ile huku akiwa amekenua meno yake.
Alijisikia kuwa mtu mpya, aliyepewa tumaini jipya la kuishi, hakukuwa na siku ambayo alijisikia kuwa na furaha kama siku hiyo. Akasimama na kuanza kuondoka mahali hapo, kila mtu aliyepishana naye, alikuwa akimsalimia.
Kuanzia siku hiyo, akapata msichana ambaye aliamini kwamba angempenda maisha yake yote. Ulipofika muda wa kurudi shule mkoani Shinyanga, akarudi kuendelea na masomo.
“Nitakwenda kwao tu, siwezi kuvumilia,” alijisema Peter.
Masomo hayakupanda hata kidogo, kichwa chake kilichanganywa na uwepo wa Tatiana, kila siku akawa mtu wa kuliandika jina la msichana huyo huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa na mapenzi makubwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakuwa na siri, alijaribu kuwaambia marafiki zake kuhusu Tatiana. Wengi walimshangaa, ilikuwaje amchague mwanamke kipofu katika maisha yake? Wengine wakapuuzia kwa kuona kwamba Peter alikuwa akiwadanganya.
“Msichana kipofu?”
“Ndiyo!”
“Anaitwa nani?”
“Tatiana.”
“Acha masihara Peter, unahisi leo ni Siku ya Wajinga Duniani?”
“Hapana, nipo siriasi, ninampenda Tatiana,” alisema Peter.
Peter aliwaambia marafiki zake wote kwamba alikuwa na msichana aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, hakutaka kumficha mtu yeyote yule kwani aliamini kwamba msichana huyo ndiye angekuja kuwa mke wake hapo baadae.
Aliendelea kusoma huku mara kwa mara akiwasiliana na Tatiana kwa njia ya barua, kitu pekee alichokuwa akimwandikia ni kwamba angeweza kumuoa na mwisho wa siku kuishi kama mke na mume.
“Nitakuja huko likizo,” aliandika Peter kwenye mmoja wa mistari katika moja ya barua aliyokuwa akiituma.
Aliona siku zikienda taratibu sana kuliko siku nyingine. Macho yake yalikuwa na kiu mno ya kumuona msichana huyo aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati kuliko msichana yeyote yule. Kila alipokuwa akilala usiku, usingizi haukumjia kama siku nyingine, ulikuwa usingizi wa mang’amung’amu mpaka alfajiri.
Siku zilikatika zaidi mpaka siku ile ambayo walifanikiwa kufunga shule na hatimaye kuondoka shuleni hapo. Hakutaka kuelekea Mwanza, kitu alichokifanya ni kuelekea katika Kijiji cha Chibe kwa ajili ya kumuona Tatiana tu.
Njiani, alitamani kuliendesha gari lile kwani alimuona dereva akiendesha taratibu mno. Njia ilikuwa na mashimo mengi lakini hiyo haikuonekana kuwa sababu ya kutosha kumwambia Peter kwamba gari lilitakiwa kuendeshwa hivyo hasa barabara inapokuwa mbaya.
“Nikuulize swali kaka?” alimuuliza jamaa aliyekuwa naye pembeni.
“Swali gani?”
“Umeoa?”
“Ndiyo! Kwani nini?”
“Hivi siku ya kwanza kwenda kuonana na mpenzi wako ambaye ndiye mkeo kwa sasa, ulijisikiaje?” aliuliza Peter huku akiachia tabasamu.
“Kwa nini unauliza hivyo?”
“Nataka kujua tu.”
“Nilijisikia furaha sana kwa kuwa alikuwa mwanamke pekee niliyempenda kwa dhati,” alijibu mwanaume huyo.
“Asante sana kwa majibu yako,” alisema Peter na kuyapeleka macho yake nje huku tabasamu pana likiendelea kuwepo usoni mwake.
Gari lilichukua masaa mawili hatimaye kufika katika Kijiji cha Chibe ambapo Peter akateremsha mabegi yake na kuanza kuelekea ndani ya kijiji kile. Japokuwa hakuwa amezoeleka kijijini pale lakini alikuwa na uhakika kwamba angepokelewa vizuri kwa kuwa tu baba yake alikwishawahi kufanya mkutano wa Injili kijiji hapo.
Alipofika, hatua ya kwanza kabisa ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa mzee Sangiwa, alipofika hapo, akapokelewa vizuri na kukaribishwa.
“Karibu sana Peter,” alisema bi Frida huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
“Nashukuru mama.”
Mgeni alikuwa amefika nyumbani, kila mmoja alikuwa na furaha kumuona, chumba kikaandaliwa kwa ajili yake. Alipewa heshima kubwa kwa kuwa alimuahidi mtoto wao mambo makubwa kwamba angemuona na kuwa mke wake wa ndoa hata kama alikuwa kipofu.
Upendo wa Frida kwa Peter ulikuwa mkubwa, hata mzee Sangiwa alipoambiwa kuhusu Peter, bila kupenda akajikuta akianza kumpenda kijana huyo.
Peter alitulia sebuleni, macho yake yalikuwa yakimwangalia kila mtu aliyekuwa akipita mbele yake. Mtu ambaye alitaka kumuona kwa wakati huo hakuwa mwingine bali Tatiana ambaye alimkumbuka mpaka kuhisi kuumwa.
Alikaa zaidi ya masaa mawili, hakufanikiwa kumuona Tatiana au hata kuisikia sauti yake jambo lililomfanya kuwa na wasiwasi mwingi kwamba kulikuwa na tatizo limetokea kwani kama angekuwepo, angekuwa amekwishaitwa mbele yake kwa ajili ya kuzungumza naye.
“Mama...” aliita Peter.
“Unasemaje mwanangu?”
“Siwezi kulala usiku wa leo pasipo kumuona Tatiana. Yupo wapi?” aliuliza Peter, bi Frida akashtuka.
“Eeeh! Kwani hakukwambia?”
“Kuniambia nini?”
“Kwamba alikuwa anasafiri?”
“Anasafiri? Kwenda wapi?”
“Marekani!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Marekani?”
“Ndiyo!”
“Hapana! Hakuniambia, ilikuwaje?” aliuliza Peter huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Alifuatwa na kwenda Marekani.”
“Alifuatwa na nani?” aliuliza Peter huku akionekana kuwa na presha kubwa, akahisi mwili wake ukinyong’onyea na nguvu kuanza kumuisha. Kijasho chembamba kikaanza kumtoka.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment