Simulizi : Penzi Kabla Ya Kifo
Sehemu Ya Pili (2)
Baada ya ufuatiliaji wake wa kipindi kirefu ndipo aliposoma kwamba msichana huyo alitarajiwa kufanya uzinduzi wa mavazi ya kike aliyoyabuni. Kwa kuwa naye alikuwa mbunifu na alipenda sana mitindo, akaamua kufuatilia kwa ukaribu zaidi.
Hakutaka kukaa nchini Morocco, alichokifanya ni kusafiri mpaka nchini Tanzania ambapo naye alikuwa mmoja wa watazamaji katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Aliyafurahia mavazi yale, aliona kwamba kama angeamua na yeye kutafanyia uzinduzi wa mavazi hayo nchini Morocco basi angepata kiasi kikubwa cha fedha, hivyo akarudi nchini kwake na kuwasiliana na Elizabeth na hivyo kuonana.
“Mbona unanishangaa hivyo?’ aliuliza Rasheed huku akimwangalia Elizabeth kwa macho ya mshangao.
“Unaonekana tajiri sana!”
“Nani? Mimi? Hapana bwana! Mimi si tajiri,” alisema Rasheed huku akitoa tabasamu lililomuacha hoi Elizabeth.
“Hili ni jumba lako?”
“Ndiyo! Ni moja ya vibanda nilivyo navyo!”
“Vibanda? Nalo hili utaliita kibanda?”
“Ndiyo! Nisikilize Elizabeth, maisha yanaanzia mbali sana, nilitoka chini sana mpaka kuwa hapa,” alisema Rasheed.
“Na mimi ninataka kuwa tajiri kama wewe, nitaweza?”
“Hahaha! Elizabeth! Wewe ni bilionea, unataka kingine kipi?”
“Siri za kuwa trilionea!”
“Hahah! Mbona unajua kila kitu!”
“Hapana! Sijui vyote zaidi ya kujituma!”
“Sawa! Nitakufundisha, lakini kwanza tufanye kazi yetu. Nimekwishaanza kufanya matangazo juu ya mavazi yako, hakika utafanikiwa zaidi,” alisema Rasheed.
Walibaki na kuzungumza mambo mengi, kadiri alivyokuwa akimwangalia mwanaume huyo, Elizabeth alizidi kumpenda na kukiri kwamba hakuwahi kumuona mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama Rasheed.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilipofika saa tatu usiku, gari likamfuata na kisha kumchukua kumpeleka katika Hoteli ya Royal Sultan iliyokuwa katikati ya Jiji la Marrakech. Njiani, Elizabeth alikuwa na mawazo tele, bado alimfikiria mwanaume huyo ambaye alionekana kutokuwa na hisia zozote za kimapenzi juu yake.
Gari lilichukua dakika ishirini mpaka kufika katika hoteli hiyo ambapo alipoulizia ilikuwa ni ya nani, akaambiwa kwamba ilikuwa ni moja za hoteli za nyota saba zilizokuwa zikimilikiwa na Rasheed.
Elizabeth akazidi kuchanganyikiwa, wakati mwingine alijiona kama alikuwa ndotoni. Alikuwa bilionea mkubwa lakini kila alipoufikiria utajiri aliokuwa nao Rasheed, alijikuta akiwa masikini ambaye alihitajika kupambana sana mpaka kuwa tajiri kama alivyokuwa mwanaume huyo.
Akapelekwa mapokezini ambapo hapo akapewa kadi maalumu na kuelekea katika moja ya vyumba maalumu, VIP ambapo huko akatulia chumbani na kuanza kufikiria kuhusu mwanaume aliyekutana naye nchini hapo.
“Ni mwanaume mzuri sana, lakini nahisi natakiwa kupambana ili niwe zaidi ya hapa nilipo, lakini mh! Huyu Rasheed asije kuwa kama Edson,” alisema Elizabeth wakati anazima taa na kulala.
Asubuhi ilipofika, akapigiwa simu kwamba tayari gari lilifika mahali hapo kwa ajili ya kumchukua, alichokifanya ni kwenda kuoga na kisha kuvaa nguo zake na safari ya kuelekea nyumbani kwa Rasheed kuanza.
Alipofika huko, akaongozana na mwanaume huyo mpaka katika ukumbi ambao ulitarajiwa kufanyika kwa uzinduzi wa mavazi yake na kisha kuanza kuzungushwa huku na kule.
Japokuwa siku hiyo haikuwa ya tukio kubwa lakini watu walijazana mahali hapo huku wengi wao wakiwa waandishi wa habari ambao walikuwa wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
“Ninajisikia faraja kuwa karibu na trilionea kama wewe,” alisema Elizabeth huku akimwangalia Rasheed usoni.
“Usijali, hata mimi nafurahi kuwa karibu na mtu anayejituma kama wewe, hakika unastahili kuwa ulipo,” alisema Rasheed.
Waliendelea kuzungumza huku wakionekana kuwa marafiki wa kipindi kirefu mno, Rasheed akamtoa Elizabeth mahali hapo na kumpeleka katika hoteli moja kubwa na ya kifahari kuliko zote nchini Morocco.
Huko ndipo alipokutana na mabilionea wengi wa Kiarabu. Kulikuwa na mkutano mkubwa uliohusu namna ya kuuinua uchumi wa Afrika kwa ujumla. Elizabeth alifurahia sana kukutana na watu hao ambao wengine alikuwa akiwasoma kwenye vyombo vya habari na kusikia taarifa zao tu, kukutana nao tu naye alijiona kuwa bilionea mkubwa.
“Ninafurahi kukutana nawe, ni meneja wa kampuni ya mafuta ya Moroccan Oil Investment?” aliuliza Elizabeth, alikuwa akimuuliza mzee moja mwenye ndevu nyingi, aliitwa Bashir Baraak.
“Ndiyo! Wewe ni Elizabeth?”
“Ndiyo! Kumbe unanifahamu?”
“Mwanamke bilionea Afrika, kwa nini tusikufahamu! Nakukaribisha sana katika ulimwengu wa mabilionea,” alisema mzee Bashir huku akiachia tabasamu pana.
Kila mtu aliyemuona Elizabeth ndani ya jengo hilo alifurahia, alikuwa msichana bilionea aliyekuwa akiyaendesha maisha yake kupitia biashara zake mbalimbali. Kila alipokuwa akiwaangalia watu hao, hakuamini, hakujiona kustahili kuwa miongoni mwa watu waliokuwa mahali hapo.
“Unahitaji nini?’ aliuliza mzee Bashir, kikao kizima kilikuwa kimya, japokuwa walifika hapo kwa ajili ya kuzungumzia uchumi wa Afrika, lakini wakaacha vyote na kuanza kuzungumza na Elizabeth.
“Nataka kuwa trilionea!”
“Hilo tu?”
“Ndiyo! Nitafurahi sana kwani kuna mengi ninataka kuyafanya!”
“Ni vizuri, ila kuna vitu unatakiwa kuvifanya kabla ya kuwa trilionea.”
“Vitu gani?” aliuliza Elizabeth huku akiwa na hamu ya kutaka kusikia, akajiweka vizuri kitini.
“Umekuja kufanya nini Morocco?” aliuliza mzee Bashir.
“Kufanya uzinduzi wa mavazi yangu!”
“Sawa! Unaweza ukaanza na hicho kuwa trilionea. Zunguka sehemu mbalimbali, tumia kiasi kikubwa cha fedha katika kutafuta soko. Ngoja nikwambie kitu kimoja, unapoamua kutafuta utajiri, usijali kuhusu muda wako, unapokwenda kuonana na mfanyabiashara mkubwa, ukawekwa mapokezi kwa saa nne bila kutokea, usihuzunike, hata kama baada ya masaa hayo ukaambiwa kwamba mfanyabishara huyo hayupo na urudi kesho, usilalamike, simama na uondoke zako, kesho rudi.
“Unapotafuta mafanikio, ni lazima ujue kwamba kuna kujitoa na kujinyima, hautakiwi kukata tamaa, unapoambiwa fanya jambo fulani, hata kama litahatarisha maisha yako, wewe fanya ila hakikisha hilo jambo halivunji sheria ya nchi.
“Wengi wanatamani kuwa mabilionea, sawa, wanaweza, ila swali ni kwamba wanaweza kupita tulipopita? Wanaweza kupigana kama tulivyopigana? Jibu ni kwamba hawako tayari, kama ni hivyo basi dunia itaendelea kuwa na mabilionea wachache,” alisema mzee Bashir, mabilionea wote waliokuwa kwenye meza ile wakaungana naye.
Muda wote Elizabeth alikuwa akitabasamu tu, maneno aliyokuwa akiambiwa na mzee huyo yalimfurahisha na kumpa nguvu ya kujua kwamba angeweza kusimama na kusonga mbele.
Ni kweli alikuwa bilionea, mwanamke mwenye fedha kuliko wanawake wote barani Afrika, hakutaka kuridhika, hivyo alitamani kuwa trilionea kama matajiri wale waliomzunguka.
“Umaarufu unaweza kuchangia kuwa bilionea? Kama jibu ni ndiyo! Vipi kuhusu nyie? Mbona mmekuwa mabilionea bila kuwa maarufu kabla?” aliuliza Elizabeth, matajiri wote wakaangalia, wakatoa tabasamu, swali hilo liliwafurahisha mno.
“Hapa Morocco kuna sehemu inaitwa Tangier, hii ipo Kaskazini mwa nchi hii, watu wa kule anapotaka kwenda Hispania ambapo ni karibu sana, huwa haendi Rabat au Casablanca kupanda ndege, ili wafike Hispania, wanachokifanya ni kupata mtumbwi tu, wanatumia masaa mawili mpaka kufika Hispania. Ila kama wangekuwa wanakwenda kwanza Rabat au Casablanca, wangetumia saa tano angani, kule wakichukua ndege wanatumia zaidi ya saa kumi mpaka Hispania,” alisema mzee Bashir.
“Unamaanisha nini?”
“Unapokuwa hauna umaarufu, utatumia nguvu nyingi sana mpaka kuwa bilionea, unaweza ukaanzisha biashara yako lakini kama huna watu wanaokufahamu, utakuwa na wakati mgumu kuwauzia watu kile ulichokuwa nacho, ila unapokuwa maarufu, amini kwamba utapata fedha nyingi kwa sababu kila mtu atataka kutumia kile ulichobuni,” alisema mzee huyo.
“Kuna kingine?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo! Katika dunia ya sasa hivi ni vigumu sana kuwaona watu maarufu wakiwa mabilionea, unajua kwa nini? Wengi wanaridhika, wanapopata umaarufu wanaona wamepata kila kitu. Kwa wanaume, wanalala na wanawake wanaowataka, kwa wanawake wanalala na wanaume wowote wanaowataka. Watahitaji nini kama magari wanayo, nyumba wanazo? Wengi wanaridhika na hivyo kushindwa kuendelea mbele.
“Kesho, mtoto wa masikini asiyejulikana anaibuka na kuwa tajiri mkubwa, anapopata umaarufu baada ya kutangazwa kila kona, utajiri wake unaongezeka zaidi, tatizo la watu maarufu wanaridhika sana na ndiyo maana ni vigumu kuwa mabilionea,” alisema Bashir, wenzake wakatingisha vichwa kuonyesha kwamba walikubaliana naye.
“Nashukuru sana, kuna la kuniongezea?”
“Ndiyo!” akaingilia tajiri mwingine, huyu alikuwa Efrahim Noah kutoka Nigeria.
“Kipi?”
“Unatakiwa kuwadanganya watu katika biashara zako,” alisema Efrahim.
“Kuwadanganya?”
“Ndiyo!”
“Kivipi?”
“Kwa mfano umekwenda dukani, ukahitaji kununua kitu, pale ukamuona mwenye duka amekunja ndita, utaweza kwenda siku nyingine?”
“Hapana!”
“Kwa nini?”
“Kwa nini akunje ndita sasa?”
“Yeah! Unatakiwa kutabasamu. Huwa tunapitia katika matatizo mengi sana, wakati mwingine wake zetu wanatukorofisha sana nyumbani, tunakasirika na kuona siku yako imeharibika lakini usithubutu hasira zile ukazipeleka sehemu ya biashara, utafukuza wateja. Unatakiwa kutabasamu kila wakati hata kama moyo wako unawaka moto kwa hasira,” alisema Noah.
“Mmmh!”
“Najua ni ngumu ila unatakiwa ufanye hivyo! Watu wengi wamepoteza wateja kwa kuwa walikuwa na hasira sehemu za kufanyia biashara na mwisho wa siku wanawajibu vibaya wateja, ifanye biashara yako ivutie, ifanye biashara yako iwe bora siku zote, na kitu kinachoweza kufanya hivyo ni tabasamu lako pana,” alisema Noah.
“Sawa! Nitafanya hivyo! Ningependa nifahamu mengine.”
“Jishushe,” aliingilia tajiri mwingine, huyu aliitwa Thomas Khone kutoka Afrika Kusini.
“Kivipi?”
“Unatakiwa kuwa mnyenyekevu kwa kila mtu pasipo kujali kama mtu huyo ni mkubwa, mdogo, masikini au tajiri,” alisema Khone huku akimwangalia Elizabeth machoni.
Siku hiyo ilikuwa ni siku pekee ya kufundishwa namna ya kuwa trilionea mkubwa katika maisha yake, baada ya kupewa njia za kutajirika zaidi, hapo ndipo akaondoka na Rasheed kurudi hotelini.
Bado moyo wake ulikuwa kwenye mapenzi ya nguvu, kila alipokuwa akimwangalia Rasheed, jinsi alivyokuwa, sura nzuri aliyokuwa nayo, alijikuta akiburuzwa mno moyoni mwake.
Alitamani mwanaume huyo azungumze neno lolote la mapenzi au hata kumuonyeshea ishara fulani lakini hilo wala halikufanyika, kila neno alilokuwa akilizungumza mwanaume huyo lilionyesha ni jinsi gani alithamini fedha zaidi ya mapenzi.
“Ungependa kupata nini katika maisha yako?” aliuliza Rasheed.
“Ninatamani kuwa na vingi mno, ila ninahitaji kitu kimoja zaidi,” alijibu Elizabeth.
“Kipi?”
“Mtoto!”
“Kwani huna mtoto?”
“Sina, sijabahatika kuwa na mtoto!”
“Mungu wangu! Pole sana! Na mumeo anasemaje?”
“Sina mume, sijaolewa.”
“Najua, matajiri wengi wanawake huwa hawapendi ndoa, wanahisi kwamba hawawezi kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja,” alisema Rasheed huku tabasamu pana likijiachia usoni mwake.
Waliendelea kuzungumza mengi, baada ya kufika hotelini, Rasheed hakutaka kubaki hapo, alichokifanya ni kuondoka kurudi nyumbani kwake huku akimwambia Elizabeth kwamba kesho yake wangezungumza mengi zaidi.
“Rasheed ananitesa,” alisema Elizabeth huku akilivuta shuka lake kwa ajili ya kulala lakini bahati mbaya kwake usingizi haukuweza kupatikana kirahisi mpaka ilipofika saa sita usiku ndipo hapo alipolala.
Siku ambayo waliitarajia ikafika, watu wengi walikuwa wamekusanyika katika ukumbi uliotarajiwa kufanyika kwa uzinduzi wa mavazi hayo, kila mtu aliyeziona picha za mavazi hayo zilipokuwa zimebandikwa, alikiri kwamba yalikuwa mavazi mazuri mno.
Kiingilio kilikuwa kikubwa lakini watu walijazana na wengine kukosa kabisa nafasi, matangazo yaliyokuwa yametangazwa kwa kipindi kifupi yalisaidia sana, kila mtu akawa na hamu ya kutaka kuangalia jinsi ubunifu huo utakavyokuwa.
Elizabeth na Rasheed walipofika ukumbini hapo, msichana huyo hakuamini alichokiona, idadi kubwa ya watu waliokuwa mahali hapo walimshangaza, hakutegemea kukuta idadi kubwa ya watu kama ilivyokuwa.
Alipoingia, watu wakaanza kupiga makofi kwa shangwe, walikuwa wakimkaribisha ukumbini hapo. Wengi walimfahamu, alikuwa msichana aliyekuwa na fedha kuliko wanawake wote barani Afrika.
Kitendo cha kutangulizana na Rasheed ukumbini hapo kikawapagawisha watu zaidi, hawakuamini kuwaona wawili hao wakiwa mahali hapo pamoja. Waandishi wa habari waliokuwa ukumbini hapo, kama kawaida yao hawakubaki nyuma, wakaanza kupiga picha kila kitu kilichotokea.
“Siamini! Nashukuru sana,” alisema Elizabeth.
“Ahsante, ila usijali sana, nimefanya hivi kwa ajili yako, nataka ufikie utrilionea zaidi ambao kila siku umekuwa ukiuhitaji,” alisema Rasheed .
Usiku wa siku hiyo, kila kitu kikaenda kama ilivyotakiwa, watu wengi walivutiwa na mavazi yale kiasi kwamba hawakutaka kusubiri mpaka yatakapouzwa, wakahitaji mavazi hayo yaanze kuuzwa humohumo ukimbini kitu kilichofanyika kwa haraka sana na hivyo kila vazi kuuzwa kwa dola mia tatu, zaidi ya shilingi laki sita.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Utakwenda kuwa trilionea mkubwa, niamini,” alisisitiza Rasheed.
“Naamini hilo ila bado ninahitaji msaada wako!”
“Usijali, nitakusaidia mpaka utakapokamilisha ndoto zako.”
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki wao, hata Elizabeth aliporudi nchini Tanzania bado aliendelea kuwasiliana na Rasheed. Alimpenda mno, kila siku alihitaji kuwa naye karibu, hakujua ni kwa jinsi gani alimpenda mwanaume huyo lakini kila siku aliogopa kumwambia ukweli.
Sauti yake aliyokuwa akiisikia kwenye simu ilimtetemesha mno, kila wakati alitamani kuisikia kwani ilizitetemesha ngoma za masikio yake ipasavyo. Akawa akiugua moyoni, hofu ilimjaa, hakuwa na jinsi, kama ambavyo Rasheed alivyoonekana kutokujali uhusiano wa kimapenzi, basi naye akamchukulia hivyohivyo.
“Nitaweza kweli kuvumilia? Mmmh! Ngoja nione,” alisema Elizabeth.
Mavazi yake yalipokelewa vizuri, watu waliyanunua na kwa msaada wa fedha kutoka kwa Rasheed ambaye alihusika katika usambazaji, Afrika nzima wakayapokea mavazi hayo yaliyouzwa kwa bei ya chini na wakati matirio yake yalikuwa ni ya gharama kubwa.
Zaidi ya nguo milioni tano ziliuzwa kwa wiki ya kwanza tu kuingia sokoni. Elizabeth akafarijika, akaona ni jinsi gani alikuwa akikubalika barani Afrika. Alijihisi kuogelea katika bwawa la fedha, ila pamoja na hayo yote, pamoja na fedha nyingi alizokuwa nazo na umaarufu mkubwa, bado suala la mtoto liliendelea kukisumbua kichwa chake.
****
“Sukuma...sukuma...” ilisikika sauti ya mwanamke mmoja, alikuwa daktari, alivalia koti kubwa jeupe, ndani ya chumba hicho, kulikuwa na madaktari wengine walioficha pua zao kwa vitambaa vya kijani.
Elizabeth alikuwa juu ya kitanda cha kujifungulia, alikuwa akipiga kelele za maumivu makali, kila alipoacha kusukuma, walimpigapiga mapajani na kumtaka kusukuma zaidi. Kijasho kilimtoka, nguvu zilimuisha lakini hawakuacha kumwambia kuacha kusukuma, bado waliendelea kumsisitizia.
“Na...shin..dw..a” alisema Elizabeh huku akiwa hoi kitandani pale, kijasho kilikuwa kikimtoka.
“Sukuma, anatoka, sukuma, endelea kusukuma,” alisema daktari yule huku wengine wakimpigapiga mapajani.Bado alitakiwa kusukuma, madaktari waliendelea kumsisitiza zaidi, mtoto alikuwa ameanza kutoka, nywele zilianza kuonekana hali iliyoleta matumaini makubwa kwamba ilibakia kiasi kidogo tu msichana huyo aweze kujifungua.
“Anatoka, endeleaaaa...”
“Nashi...ndw...a...siwe...z..i...” alisema Elizabeth huku akiendelea kujitahidi lakini mwili wake ulichoka kabisa.
Baada ya dakika kadhaa, sauti ya mtoto akilia ikaanza kusikika ndani ya chumba hicho, kila daktari akaonyesha uso wenye tabasamu, hawakuamini kama hatimaye msichana huyo alikuwa amejifungua mtoto salama. Uso wa Elizabeth ukaonyesha tabasamu pana zaidi.
“Hongera, umejifungua mtoto wa kike,” alisema daktari huku akimuonyeshea Elizabeth jinsia ya mtoto yule.
“Elizabeth...Elizabeth...” ilisikika sauti ya Candy ikiita.
Elizabeth akashtuka kutoka usingizi, sauti kali ya Candy ilimshtua na kujikuta akiwa kitandani, ghafla, akanyong’oyea mara baada ya kugundua kwamba kila kitu kilichokuwa kimetokea, kuanzia kipindi kile alichokuwa leba akijifungua kumbe kilikuwa ndoto.
Hakuitikia, akakaa kitandani na kuuinamisha uso wake katikati ya miguu yake na kuanza kulia. Moyo wake uliumia mno, hakuamini kwamba kila kitu kilichokuwa kimetokea kumbe kilikuwa ndoto.
Hakukuwa na kitu kilichomuumiza kama hicho, alibaki akitokwa na machozi yaliyolowanisha shuka. Ghafla, mlango ukafunguliwa na Candy kuingia chumbani humo. Hali aliyomkuta nayo rafiki yake ilimshtua, haikuwa kawaida kabisa kumuona akiwa ameamka na kuuinamisha uso wake kama mtu aliyekuwa na majonzi makubwa.
Hakujua kama alikuwa akilia, alichokifanya ni kumsogelea, alipomfikia, akakaa pembeni yake kisha kumshika bega.
“Eliza...” aliita Candy.
“Abeee!” aliitikia Elizabeth kwa sauti iliyosikika kwamba alikuwa akilia.
“Kuna nini tena kipenzi?”
“Candy! Nimeota ndoto...”
“Ndoto! Ni kawaida! Usiogope, hiyo ni ndoto tu...”
“Hapana! Nimeota nikiwa leba najifungua, Candy! Nimeota najif...” alisema Elizabeth lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake akaanza kulia.
Moyo wake uliumia mno, hakuwa na jinsi, kwa kuwa ile ilikuwa ndoto, akaamua kuachana nayo. Akainuka kitandani pale na kuendelea na ratiba yake kama kawaida.
Siku hiyo alipanga kwenda hospitalini, japokuwa alijua kwamba alikuwa na tatizo ambalo halikujulikana lakini alihitaji kurudi tena kwa ajili ya kufanyiwa vipimo kwa mara nyingine ili aweze kujua alikuwa akisumbuliwa na nini.
Mara baada ya kujiandaa, akatoka nje na Candy, wakaingia kwenye gari jingine ambalo nalo lilikuwa la kifahari kisha kuanza kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuonana na daktari wa magonjwa ya wakinamama kwa ajili ya kuzungumza naye. Kwa kuwa alijua kwamba angeweza kuharibu utulivu hospitalini huko, alichokifanya ni kuvaa juba jeusi na nikabu ili asiweze kujulikana.
Hawakuchukua muda mrefu wakaingia ndani ya eneo la hospitali hiyo. Kila mtu aliyeliona gari lile lililoelekea sehemu ya mapokezi akabaki akiliangalia tu, lilikuwa gari la thamani kubwa ambalo haikuwa rahisi kumilikiwa na watu wa kawaida hasa katika nchi kama Tanzania.
Elizabeth na Candy wakateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo. Hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba yule mwanamke aliyevalia juba jeusi na nikabu alikuwa Elizabeth, hivyo wakaishia kuwaangalia tu mpaka walipopotea machoni mwao.
“Nimerudi,” alisema Elizabeth, alikuwa akizungumza na Dk. Kisiju.
“Karibu sana! Unataka nikufanyie nini leo?”
“Tatizo langu lilelile, ninahitaji kupata mimba,” alisema Elizabeth.
“Ila si tulishangalia na hatukukuta tatizo?”
“Kutokukuta tatizo napo ni tatizo! Naomba uniangalie tena,” alisema Elizabeth.
“Basi subiri.”
Dokta Kisiju akaanza kushughulika na vipimo vya Elizabeth, japokuwa alimpima mara kwa mara na kutokugundua tatizo lolote lile lakini hakuwa na jinsi, aliendelea kumshughulikia zaidi kiasi kwamba mpaka anamaliza na kuangalia tena vipimo, ilikuwa ileile kwamba hakuweza kuona tatizo lolote lile.
Bado kichwa cha Elizabeth kilichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kiliendelea mwilini mwake, vipimo vyote alivyopimwa, hakuonekana kuwa na tatizo lolote lile, swali likaja, kwa nini hakupata mimba?CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakuwahi kutoa mimba, hakuwahi kufanya mchezo wowote mchafu ambao aliamini kwamba ungeharibu kizazi chake, kitendo cha kutokushika mimba bado kiliendelea kuwa kitendawili ambacho hakuweza kukitegua kabisa.
Hakuyaacha machozi yake kububujika mashavuni mwake, kazi ilikuwa ni ileile kwamba aliumia siku zote za maisha yake. Candy ndiye alikuwa mtu wake wa karibu aliyemfariji kutokana na hali aliyokuwa nayo.
“Futa machozi Eliza...”
“Hakuna tatizo!”
Alishazoea kulia, alishazoea kuumia, hakuwa na jinsi, hakutaka kuendelea kukaa ndani ya ofisi ile, walichokifanya ni kutoka kwa ajili ya kurudi nyumbani huku kile walichokuwa wamekifuata hospitalini hapo, matokeo hayakubadilika bali kilikuwa ni kilekile cha siku zote.
Walipofika sehemu iliyokuwa na lifti, wakasimama nje kwa ajili ya kuisubiria ili waweze kuingia ndani na kushuka chini. Hapo, kulikuwa na wagonjwa wengi waliokuwa wakipita, wengine walibebwa katika machela, walikuwa hoi, wengine kwa kuwaangalia tu, ungeweza kuhisi kwamba wasingeweza kufika kesho, walikuwa hoi.
Wakati wamesimama hapo, mara akatokea nesi mmoja akikisukuma kiti cha walemavu, katika kile kiti kulikuwa na msichana mdogo aliyepooza, alikuwa ameikunja shingo yake kwenda upande wa kulia huku kiganja chake kikiwa kimeelekea chini na udenda kumtoka mdomoni.
Alipomuona msichana yule mdogo, huruma ikamuingia moyoni mwake, hakutaka kuvumilia, alichokifanya ni kumsogelea na kisha kumwangalia kwa sekunde kadhaa, hata yule nesi aliyekuwa akimsukuma katika kiti kile alibaki akimshangaa tu.
“Anaumwa nini?” aliuliza Elizabeth.
“Amepooza, amekuwa kwenye hali mbaya mno,” alijibu nesi yule.
“Poleni sana! Kwa hiyo hana matumaini ya kupona?”
“Mmmh! Kwa kweli sijui. Hali yake mbaya sana, hapa inatakiwa asafirishwe na kupelekwa nchini India,” alisema nesi yule.
“Si ndiyo mumsafirishe!”
“Tatizo gharama, kaka yake ambaye alimleta binti huyu hana maisha mazuri, ni mtu hohehahe, alipoambiwa kuhusu hilo, alimpiga picha mdogo wake na kupeleka katika Gazeti la Uwazi ili habari itolewe na apate msaada,” alisema nesi yule pasipo kugundua kwamba yule aliyekuwa akizungumza naye alikuwa Elizabeth, msichana bilionea aliyekuwa maarufu kuliko wote barani Afrika.
Lifti ilipokuja, wakaingia na kuanza kushuka chini.
Moyo wake uliguswa kumsaidia mtoto yule, kila alipomwangalia, alihisi maumivu makali moyoni mwake, msukumo mkubwa juu ya kumsaidia uliendelea kumsukuma moyoni mwake, kila alipokuwa akimwangalia, huruma ilizidi kumuingia zaidi.
Candy alionekana kulishtukia hilo, alijua fika kwamba rafiki yake huyo alikuwa ameguswa na hali aliyokuwa nayo binti yule kwani kila alipomwangalia, Elizabeth alikuwa bize kumwangalia mtoto yule.
“Anahitaji kiasi gani kwa ajili ya matibabu?”
“Milioni saba!”
“Sasa atazipata kweli?”
“Mmmh! Nao huo ni mtihani mwingine.”
Elizabeth hakutaka kukubali, alikuwa mwanamke mwenye fedha nyingi ambaye kila siku aliwaambia watu kwamba lingekuwa jambo jema kama unapopata fedha kuwasaidia watu wengine.
Katika maisha yake ya ubilionea alikuwa mtu wa kutoa msaada na kuamini kwamba kila alipoongezewa, ni kwa sababu alitoa sana. Mtoto yule aliyeonekana kuwa hoi, hakutaka kumuacha hivyohivyo, alijiona kuwa na kila sababu ya kuweza kumsaidia.
“Candy!”
“Abeee...”
“Nakuwa na msukumo wa kumsaidia binti huyu,” alimwambia Candy.
“Kweli?”
“Hakika!”
“Basi hakuna tatizo.”
Wakati wanazungumza hivyo, tayari lifti ikafika chini na kuteremka, hawakutaka kuelekea ndani ya gari, walichokifanya ni kufuatilia binti yule alikuwa akipelekwa wapi. Walipoona kwamba amepelekwa katika Wodi ya Mwaisela, wakaondoka zao na kuahidi kwamba wangerudi mahali hapo siku inayofuata.
Siku hiyo Elizabeth alikuwa akimfikiria mtoto yule tu, moyo wake uligubikwa kwa huzuni kubwa kiasi kwamba akakosa furaha kabisa, mawazo juu ya msichana yule mdogo yalikisumbua kichwa chake na kuahidi kuendelea kumfuatilia siku inayofuata ili ajue ni wapi alitakiwa kuanzia kwani kutokana na fedha alizokuwa nazo, milioni saba halikuwa tatizo lolote lile.
Siku iliyofuata aliamka asubuhi na mapema, kitu cha kwanza kabisa kilichokuja kichwani mwake ni kuhusu mtoto aliyekuwa amemuona siku iliyopita aliyemfanya kuwa na msukumo mkubwa wa kutaka kumsaidia kutokana na tatizo kubwa alilokuwa nalo, hakutaka kuchelewa, akaanza kujiandaa tayari kwa kwenda huko hospitali.
Wakati akiendelea kujiandaa, mara simu yake ikaanza kuita, kwa kuwa alikuwa bafuni anaoga, akaamua kuipotezea lakini mara baada ya kutoka tu, kitu cha kwanza alichokifanya ni kuifuata, alipoziona namba tu, alijua ni nani aliyepiga, akampigia.
“Elizabeth! Unakumbuka ahadi yetu?” aliuliza mwanaume wa upande wa pili mara baada ya salamu.
“Ipi?”
“Kutengeneza tangazo na kuingia mkataba!”
“Kwani nilisema lini?”
“Leo, si ndiyo tarehe kumi!”
“Mungu wangu! Nilikuwa nimesahau kabisa.”
“Tupo hapa Mlimani City tunakusubiri,” ilisikika sauti ya mwanaume huyo.
“Nakuja! Nipeni nusu saa,” alisema Elizabeth.
Alikuwa mtu wa biashara tu, jina lake lilikuwa biashara tosha, kila alipokaa, zilionekana fedha tu, alipotembea, watu waliona ni kama fedha zilikuwa zikitembea.
Ili bidhaa zako ziweze kununuliwa kwa wingi, ilikuwa haina budi kumuweka Elizabeth katika bidhaa hiyo au katika matangazo yako, na hivyo ndivyo walivyofanya kampuni ya kutengeneza ngano ya Metropolitan Investment Limited.
Walikuwa wameweka mkataba na msichana huyo kwamba siku hiyo waweze kuonana kwa ajili ya kutengeneza tangazo ili lipate kuonyeshwa katika televisheni, mbali na kutengeneza tangazo hilo hapo Mlimani City pia walitakiwa kuondoka kuelekea Mbezi Beach kama muendelezo wa tangazo hilo.
Hivyo vitu vyote vilitakiwa kufanyika siku hiyo, kama mkataba wa awali walikuwa wameishawekeana na kilichokuwa kimebakia ni mkataba ule wenyewe kwa ajili ya kazi hiyo tu. Alipomaliza kujiandaa, akatoka ndani na kulifuata gari lake, kilichofuatia ni kuanza safari ya kuelekea huko Mlimani City.
Hakuwa na mawazo na binti yule tena, alichokuwa akikifikiria kwa wakati huo ni kutengeneza tangazo na watu hao kwani kazi kama hizo ndicho kitu kingine kilichompa sana fedha. Hakuchukua dakika nyingi akaingia Mlimani City, mara baada ya watu kugundua kwamba hilo gari lilikuwa la Elizabeth tu, wakaanza kulifuata na kulizunguka huku kila mmoja akitaka ateremke.
Umaarufu ulikuwa tabu tupu, hakuwa na raha kabisa, kila alipokwenda, hakukuwa na amani kabisa, kuna wakati alikwenda sehemu kwa ajili ya kutulia tu lakini wingi wa watu ukamfanya kukosa uhuru kabisa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alifika mahali hapo kwa ajili ya kufanya kazi, lakini hata kabla hajateremka kutoka garini, tayari watu walikuwa wamekusanyika wakimtaka kuteremka ili wapige naye picha na hata kumsalimia. Elizabeth akakosa nguvu ya kuteremka na hivyo kuwapigia simu watu wale waliotaka kufanya naye kazi waje na walinzi ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.
“Hebu sogeeni huko, nitawapiga risasi,” alisema mlinzi mmoja, japokuwa alionekana kuwa siriasi, lakini maneno yake yalijaa utani.
“Kaka! Mimi nataka kupiga naye picha tu.”
“Sawa! Kwanza sogeeni kule. Mbona hamuelewi lakini?” alisema mlinzi huyo, hapohapo na walinzi wengine kuongezeka, kila aliyekuja alipiga mikwara.
Wananchi wakasogea pembeni na ndipo Elizabeth akateremka kutoka garini, kila aliyemuona akaanza kushangilia, kumuona msichana huyo ilikuwa kama ndoto, wengine wakashindwa kuamini, walikuwa wakimuona kwenye televisheni na magazetini tu, kuwa hapo tena mbele yao kilikuwa kitu kisichoaminika kabisa machoni mwao.
“Naomba nipige picha nawe,” alisikika msichana mmoja.
“Na mimi nataka kupiga picha nawe,” alisikika msichana mwingine.
Elizabeth hakutaka kujali, kile kilichokuwa kimemleta mahali hapo ndicho kilichotakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo, akaanza kupiga hatua kuelekea sehemu ambayo ingetumika katika kutengenezea tangazo hilo.
Alikuwa katikati ya walinzi, kila mtu aliyekuwa akiliona kundi kubwa la watu hao, naye alikwenda, walipomuona Elizabeth, kila mmoja alitaka kubaki mahali hapo na kumwangalia. Kwa sababu ulinzi ulikuwa ni wa kutosha, moja kwa moja nusu ya tangazo likaanza kutengenezwa, lilikuwa tangazo zuri, lenye mvuto ambalo kila mtu alitamani kulitazama.
Mara baada ya kumalizika, akachukua dakika tano kupiga picha na watu kadhaa kisha kuingia garini na safari ya kuelekea Mbezi Beach kuanza kwa ajili ya kumalizia tangazo hilo.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, siku nzima aliitumia kwenye kutengeneza tangazo hilo tu. Alichoka mno lakini hakuwa na jinsi, maisha yake yalikuwa ni fedha, hakutaka kuishiwa fedha, kila ilipojitokeza, alikuwa tayari kuhakikisha anazichukua kwani alitaka kuwa bilionea mara mia ya vile alivyokuwa.
“Tushamaliza?’ aliuliza Elizabeth, tayari ilikuwa saa kumi jioni.
“Bado, kuna vitu tumalizia kwanza, baada ya hapa, tutapiga sini ya mwisho kisha itakuwa tumemaliza,” alisema jamaa mmoja.
“Sawa.”
Kazi ikaendelea, walikuja kumaliza saa kumi na mbili ambapo walikula na kisha kuondoka. Hapo ndipo Elizabeth alipokumbuka kuhuhusu yule binti mdogo aliyekuwa amemuacha hospitalini, binti aliyekuwa na matatizo makubwa ya kupooza.
Moyoni alijisikia mkosaji, akabaki akiwa na maumivu makubwa ya moyo, akatawaliwa na mawazo kiasi kwamba moyo wake ukanyong’onyea kabisa. Usiku hakulala vizuri, muda mwingi akawa akimuwaza msichana yule mgonjwa na kuahidi kwamba ilikuwa ni lazima kesho aende kumtembelea, ikiwezekana amsaidie kwa matatizo makubwa aliyokuwa nayo.
“Nitakwenda na nitamsaidia tu,” alijisemea na kisha kulala.
Asubuhi Elizabeth aliamshwa na simu yake iliyokuwa ikiita, huku akionekana kuwa na uchovu mwingi tena na macho yakiwa mazito kabisa kutokana na usingizi, akaamka na kuanza kuiangalia simu ile.
Macho yake yakatua katika namba aliyoifahamu kabisa aliyoisevu kwa jina la Meneja. Hakutaka kuchelewa, hapohapo akaipokea simu ile na kuanza kuongea na mpigaji kwani haikuwa kawaida yake kumpigia simu asubuhi namna hiyo.
“Niambie meneja,” alisema Elizabeth kwa sauti ya kichovu.
“Salama tu! Mbona unalala mpaka sasa hivi? Huoni kama tunaweza kuchelewa?” ilisikika sauti ya meneja upande wa pili.
“Kuchelewa na nini?”
“Umesahau jamani?”
“Nimesahau! Kuna kitu?”
“Candy hajakukumbusha kwamba leo tuna safari ya kwenda Uganda?’ aliuliza meneja huyo.
“Uganda! Ugandaaaa! Yeah! Nimekumbuka, kwenye zile tuzo za MPEA?”
“Ndiyo hizohizo!”
“Daah! Sawa! Ngoja nijiandae, mwambie rubani ajiandae,” alisema Elizabeth.
Hakutaka kuendelea kulala tena, tayari kulikuwa na jambo kubwa alilotakiwa kulifanya, alitakiwa kusafiri kuelekea nchini Uganda kulipokuwa kunatolewa tuzo maalumu za watu waliowahamasisha watu wengine kufanya jambo fulani, tuzo hizi ziliitwa MPEA (Motivation People in East Africa) ambazo zilitarajiwa kutolewa nchini humo siku hiyo.
Akaelekea bafuni na kujiandaa kwa safari hiyo. Hakukumbukakama alikuwa na ratiba nzito ya kwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kumuona mtoto aliyekuwa kwenye mateso makali ambaye alijiahidi kwamba angemsaidia.
Alipomaliza kujiandaa, akampigia simu Candy na kumtaka mahali hapo. Wala hakuchukua muda mrefu, ni ndani ya dakika thelathini tu, Candy alikuwa nyumbani hapo ambapo alimwambia kwamba walitakiwa kuondoka kuelekea nchini Uganda.
“Nilikuwa nimekwishasahau shosti wangu,” alisema Candy kwa sauti yake nyororo.
Hawakutakiwa kubaki nchini Tanzania, alichokifanya ni kulifuata gari lake kisha kuondoka nyumbani hapo kuelekea uwanja wa ndege. Walikuwa wamechelewa sana hivyo walitaka kufanya haraka, watumie saa saba angani na kuingia nchini Uganda.
Kwa kuwa tayari rubani wake alikuwa amekwishaambiwa, hivyo moja kwa moja yeye, akiongozana na Candy pamoja na meneja wake, wakaanza kuondoka kuelekea nchini Uganda kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za ugawaji tuzo hizo.
“Hivi ulikumbuka kuhusu yule mtoto?”
“Yupi?”
“Yule wa Muhimbili!”
“Mungu wangu! Sikukumbuka! Nilitaka kwenda jana, nikawa bize, nikapanga kwenda leo, na hii safari, ngoja tutakwenda tukirudi,” alisema Elizabeth huku akionekana kushtuka.
Hapo ndipo mawazo juu ya binti yule yalipoanza kumjia kichwani mwake, alihisi hukumu nzito moyoni mwake, hakuamini kama kwa mara nyingine alikuwa amesahau kumtembelea msichana yule na hivyo kuendelea na maisha yake kama kawaida.
Hakuwa na raha, furaha yote aliyokuwa nayo kipindi cha nyuma ikaanza kupotea. Ndege iliendelea kukata mawingu na ndani ya saa saba tayari ilikuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe uliokuwa jijini Kampala.
Mara baada ya ndege kusimama, Elizabeth na wenzake wakaanza kuteremka ambapo baada ya kufika nje ya uwanja huo, tayari gari maalumu la Hoteli ya Pacific Hilton ilikuwa nje ikiwasubiri, huku akijifichaficha akaifuata gari hiyo na kuingia ndani.
“Karibuni nchini Uganda,” alisema mwanaume mmoja huku uso wake ukipambwa na tabasamu pana.
“Ahsante sana.”
Gari hilo likaanza safari kuelekea katika Hoteli ya Pacific Hilton iliyokuwa katikati mwa Jiji la Kampala. Ndani ya gari, Elizabeth alikuwa kimya, bado mawazo yake yalikuwa yakimfikiria binti yule mdogo ambaye alikuwa akiteseka kitini.
Hakujua ni kwa sababu gani alimfikiria sana binti yule. Ni kweli aliwahi kukutana na watu wengi, waliokuwa na matatizo ambao walihitaji sana msaada wake, lakini kitu cha ajabu sana ambacho hakukitegemea ni uzito aliokuwa nao kwa msichana yule mdogo.
Walipofika hotelini, wakapelekwa chumbani tayari kwa kujiandaa na ugawaji tuzo uliotarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Monrovian uliokuwa pembezoni mwa jiji hilo.
Taarifa zikaanza kutolewa na wahudumu wa hoteli hiyo kwamba mwanamke mwenye nguvu ya ushawishi barani Afrika, Elizabeth alikuwa amefika hotelini hapo. Idadi kubwa ya watu kutoka sehemu mbalimbali hapo Kampala wakafika hotelini hapo kwa ajili ya kumuona msichana huyo aliyekuwa na mafanikio makubwa.
Kwa harakaharaka walikusanyika watu mia mbili nje ya hoteli ile ila kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele, watu walizidi kuongezeka zaidi mpaka kufikia idadi ya watu elfu mbili. Kila mmoja aliyefika mahali hapo alitaka kumuona Elizabeth tu.
Kuwa na mwanamke huyo ndani ya nchi yao ilikuwa ni moja ya bahati ambayo watu wengi walikuwa wakiisubiria. Japokuwa walikaa nje ya hoteli kwa kipindi kirefu lakini hawakuweza kumuona msichana huyo zaidi ya kuambiwa kwamba walitakiwa kufika ukumbini kama walitaka kumuona.
Saa 2 usiku, hafla ya ukabidhaji tuzo ukaanza ndani ya Ukumbi wa Monrovian. Watu walikuwa wengi huku wengi wao wakitaka kumuona Elizabeth tu ambaye mara kwa mara walikuwa wakimsikia kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Hafla ilikwenda vizuri huku Elizabeth akikabidhiwa tuzo moja katika hafla hiyo kitu ambacho kwake kilionekana kuwa kama bahati kubwa kwani kulikuwa na watu wengi ambao kwake walionekana kustahili. Baada ya hafla hiyo kuisha, wakaondoka hotelini hapo.
“Habari yako!” alisikika akisalimia kijana mmoja, kwa kumwangalia, alikuwa kijana nadhifu sana, alikutana naye wakati alipokuwa akiingia hotelini.
“Salama!” aliitikia Elizabeth na kuendelea kupiga hatua.
“Samahani,” alisema kijana yule hivyo Elizabeth kusimama.
“Bila samahani!”
“Nilikuwa nahitaji kitu kimoja kama nitaruhusiwa.”
“Kitu gani?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ningependa ninywe nawe kifungua kinywa kesho asubuhi.”
“Unywe na mimi kifungua kinywa?”
“Ndiyo! Ila samahani kama nimekuudhi!’
Elizabeth alibaki akimwangalia kijana yule, alikuwa mtanashati ambaye alivalia vizuri sana. Watu wote waliokuwa na Elizabeth wakasimama na kuanza kuwaangalia wawili hao, hata baadhi ya wahudumu wa hoteli hiyo walibaki wakiwaangalia wawili hao waliokuwa wakizungumza.
“Ninatarajia kusafiri kesho asubuhi!”
“Hakuna tatizo! Samahani kwa usumbufu,” alisema kijana yule kwa sauti ya chini kabisa, yenye unyenyekevu wa hali ya juu.
Elizabeth akaondoka mahali hapo na kurudi chumbani kwake, akajilaza kitandani huku akianza kufikiria maisha yake toka alipotoka mpaka hapo alipofikia. Alipitia mengi, umasikini wa hali ya juu lakini mwisho wa siku alikuwa bilionea.
Alifarijika sana na alijiahidi kwamba ilikuwa ni lazima kuwasaidia watu waliokuwa na matatizo mbalimbali kwani hakukuwa na njia nyingine ya kuweza kufanikiwa zaidi ya kuwasaidia watu waliokuwa na uhitaji.
Siku iliyofuata hata kabla ya kuondoka hotelini hapo akatakiwa kuonana na mkurugenzi wa hoteli hiyo ambaye alimhitaji kwa ajili ya kumshukuru kutokana na uwepo wake hotelini hapo kwa kuwa ilitangazika sana na watu wengi kuifahamu hata wale waliokuwa nje ya Uganda.
Kama shukrani zake, alihitaji kuonana na msichanahuyo hivyo akatumwa meneja kwa ajili ya kuwasiliana na Elizabeth na moja kwa moja kumpeleka ofisini kwake. Elizabeth hakukataa, alichokifanya ni kuongozana na meneja huyo ambapo mara baada ya kuufikia mlango wa ofisi hiyo, wakaruhisiwa na kuingia ndani.
Macho ya Elizabeth yalipotua kwa mkurugenzi huyo, akajikuta akipigwa na mshangao, hakuamini kama mtu yule aliyekuwa amemuomba nafasi ya kunywa pamoja asubuhi ndiye alikuwa mkurugenzi wa hoteli ile, yaani yeye ndiyealiyekuwa akiimiliki hoteli hiyo.
Alipokaribishwa kitini, mbele, juu ya meza ile kulikuwa na kibao kilichoandikwa Desmond Olotu. Jina hilo halikuwa geni masikioni mwake, alikwishawahi kulisikia sana lakini hakuwahi kuonana na mtu huyo.
Desmond Olotu alikuwa miongoni mwa mabilionea wakubwa barani Afrika, alimiliki visima vya mafuta nchini Nigeria, migodi ya dhahabu Kongo na Afrika Kusini, alikuwa akifanya biashara zake nyingi sehemu tofautitofauti mpaka China ambapo huko alikuwa na kiwanda cha kutengenezea viatu na huku akiwa amewaajiri Wachina ndani ya nchi yao.
Elizabeth hakuamini kama yule bilionea mkubwa aliyevuma sana barani Afrika ndiye yule aliyekuwa mbele yake. Alionekana kuwa kijana mdogo asiyekuwa na maringo yoyote yale, kwa kumwangalia tu, alionekana kuwa kijana mwenye mafanikio makubwa ambaye hakutaka hata kujionyesha.
Elizabeth akabaki akitetemeka huku akijishtukia kutokana na kukataa kunywa kifungua kinywa na mwanaume huyo asubuhi ya siku hiyo. Hakutaka kuonyesha hali yoyote ile, kwake, alijifanya kuwa kawaida japokuwa kila alipofikiria juu ya kukataa kwake kunywa naye chai, kulimuumiza.
Alikuwa binti mdogo wa miaka kumi na mbili, kwa sura, alikuwa mrembo kuliko watoto wote waliokuwa wakisoma katika Shule ya Msingi ya Turiani iliyokuwa Magomeni jijini Dar es Salaam.
Wazazi wake walifariki dunia miaka miwili iliyopita kwa kupata ajali ya gari walipokuwa wakisafiri kwenda Dodoma ambapo ndipo walipokuwa wakiishi kwa kipindi hicho. Baada ya hapo, kaka yake ambaye ndiye alikuwa mtu pekee katika maisha yake ndiye ambaye alibakia, akaamua kumchukua na kumpeleka jijini Dar es Salaam.
Huko, maisha hayakuwa mazuri, kila siku kaka yake huyo aliyeitwa James alikuwa mtu wa kutoka na kwenda kutafuta vibarua vidogovidogo, alipokuwa akifanikiwa kupata kiasi chochote cha fedha, alirudi nyumbani ambapo maisha yaliendelea kama kawaida.
Uzuri wa sura wa msichana huyu mdogo aliyeitwa Glory ulimvutia kila mtu aliyekuwa akimwangalia, si wavulana tu waliotokea kuvutiwa naye bali hata wasichana mbalimbali walitamani kuwa na sura kama aliyokuwa nayo msichana Glory.
Alipoingia darasa la tano, kama ilivyokuwa kwa wazazi wake, naye akapata ajali ya gari baada ya kugongwa wakati akivuka barabara. Dereva ambaye alimgonga hakutaka kubaki, akapiga gia na kukimbia, hivyo akamuacha Glory akiwa chini akivuja damu huku akirusha miguu yake huku na kule kama mtu aliyetaka kukata roho.
Walimu wakachanganyikiwa, wanafunzi wakalia sana, wasamaria wema waliokuwa katika eneo la tukio wakamchukua Glory na kumpeleka katika Hospitali ya Magomeni ambapo hapo hawakukaa naye sana, wakampeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Hali yake mbaya sana,” yalikuwa ni maneno pekee yaliyozungumzwa na kila daktari aliyetoka katika chumba cha upasuaji.
Gloria alikuwa kwenye hali mbaya kweli, alikuwa akiteseka kitandani, mwili wake ulikakamaa, madaktari waliogopa mno na kuona kwamba muda wowote ule binti huyo angeweza kufariki dunia.
Hapo ndipo walipowataka walimu wawasiliane na ndugu yake kwa ajili ya kufika hospitalini hapo, wakafanya hivyo. James alipofika, akachanganyikiwa, mashavu yake yalilowanishwa na machozi yaliyokuwa yakimbubujika, hakuamini kile alichokuwa ameambiwa, hivyo akaanza kupiga kelele akiwataka madaktari wampe ruhusa ya kumuona mdogo wake.
“Nataka nimuone Glory, naomba nimuone Glory,” alipiga kelele James huku akionekana kuchanganyikiwa.
Alionekana kuwa kama chizi, lakini ukweli ni kwamba hali ya mdogo wake ilimtisha mno. Aliogopa, alikumbuka vilivyo kile kilichokuwa kimetokea kwa wazazi wao, hakutaka kumpoteza Glory, alikuwa binti mdogo mno, ndugu yake ambaye alibaki naye katika familia yao.
“Subiri kwanza kijana,” alisema daktari huku akiwa amemshika Glory.
“Dokta! Ninataka nimuone Glory!”
“Usipige kelele, kumbuka hapa ni hospitali,” alisema daktari huyo kwa sauti ya chini.
Matibabu yaliendelea kila siku, hali yake ilikuwa mbaya mno kwani uti wake wa mgongo ulikuwa umepata matatizo na hivyo walichokifanya ili waweze kuwa na uhakika zaidi, Glory akachukuliwa kwa ajili ya kupelekwa katika chumba kilichokuwa na mashine ya CT Scan kwa ajili ya kuangaliwa tatizo hasa lilikuwa nini.
“Mashine inaonyeshaje?”
“Amevunjika uti wa mgongo, ila si sana, kidogo viunga vyake vimeachia,” alijibu daktari mmoja.
“Hebu mpigeni picha ya X ray,” aliagiza dokta mkuu.
Hiyo haikuwa kazi kubwa, walichokifanya ni kumchukua Glory na kumpeleka katika chumba maalumu ambapo akapigwa na mwanga wa X ray na picha kutoa ambayo ilionyesha ni kwa namna gani uti wake wa mgongo ulivyokuwa umevunjika.
“Huyu binti amepooza,” alisema Dr. Kipute, mkononi aliishikilia karatasi ngumu iliyokuwa na picha ya majibu ya uti wa mgongo wa Glory.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Haina jinsi, hapa ni kumpatia matibabu zaidi.”
Hali ilikuwa mbaya kila siku, hakukuwa na siku ambayo Glory alikuwa na nafuu, kila siku alilala kitandani kwake huku akionekana kuwa kama mfu. Alitulia, hakutingishika. Wanafunzi na walimu walifika hospitalini hapo na kumjulia hali, kila aliyemuona kitandani pale, alibaki akilia tu, hali aliyokuwa nayo Glory ilimuhuzunisha kila mtu.
James hakuacha kulia, kila siku alikuwa mtu wa kufuta machozi mashavuni mwake, mdogo wake aliyekuwa akimpenda alikuwa hoi kitandani. Hakujua afanye nini, aliwasikilizia madaktari wangesema nini juu ya hali yake.
Baada ya wiki moja, madaktari wakamwambia kwamba kwa jinsi ugonjwa wake ulivyokuwa isingewezekana kutibiwa nchini Tanzania, alitakiwa kusafirishwa na kupelekwa nchini India ambapo kidogo huko angeweza kutibiwa na kupona kabisa.
“Mmmh!” aliguna James.
“Tatizo nini?”
“Gharama zangu au za hospitali?”
“Unatakiwa kulipia wewe.”
“Nitawezaje? Hata laki moja tu kushika sijawahi kushika,” alisema James.
“Zungumza na watu wa magazeti, nenda hata kwenye Gazeti la Uwazi wakusaidie,” alisema dokta.
Huo ndiyo ushauri aliokuwa amepewa, alichokifanya ni kwenda kwenye ofisi za gazeti hilo na kuwaambia kile alichokuwa akikitaka. Taarifa zikatolewa magazetini na baada ya siku kadhaa, akapata kiasi fulani cha fedha ambazo hizo akazitumia kwa kununulia kiti cha walemavu.
“Kuna fedha zimebaki?” aliuliza dokta.
“Ndiyo! Milioni mbili.”
“Basi sawa! Warudie tena, washukuru lakini wape taarifa kwamba unahitaji milioni saba ili ziwe tisa na asafirishwe,” alisema daktari huyo.
“Sawa. Nakwenda leo hiihii. Ila anaendeleaje?”
“Hivyohivyo! Ila nenda, ukifanikiwa, kila kitu kitakuwa salama,” alisema daktari huyo.
James hakutaka kubaki hospitalini hapo, asubuhi hiyohiyo akaondoka na kwenda katika gazeti hilo kwa ajili ya kuwashukuru na kuwaambia kwamba bado alihitaji kiasi kingine zaidi hivyo asaidiwe katika hilo, habari juu ya ugonjwa uliomsumbua Glory ikatolewa gazetini na watu walioguswa na tukio hilo waendelee kumchangia msichana huyo.
James hakuwa na jinsi, alikuwa na mapenzi mazito kwa mdogo wake, alimpenda mno na hakuwa tayari kumuona akipata shida yoyote ile.
*****
“Bilionea Olotu...” alisema Elizabeth kwa mshtuko.
“Nipo hapa! Karibu sana,” alisema Olotu huku akisimama na kusalimiana.
Bado Elizabeth hakuyaamini macho yake, hakuamini kama yule aliyekuwa mbele yake ndiye yule bilionea mkubwa aliyekuwa akivuma sana barani Afrika. Hakuwahi kukutana naye, hakuwahi kuona hata picha yake zaidi ya kumsoma katika magazeti mbalimbali na mitandano ya kijamii.
Alifurahi, alikuwa bilionea lakini watu aliokuwa akikutana nao walikuwa zaidi yake. Moyoni alifarijika sana, kila alipokuwa akimwangalia Olotu, alijiona akiukaribia utajiri mkubwa kiasi kwamba wakati mwingine alihisi kuchanganyikiwa.
“Unaonekana mdogo mno,” alisema Elizabeth huku akimwangalia Olotu usoni.
“Hahaha! Lakini huwezi amini, nina miaka hamsini na nane sasa hivi,” alisema Olotu na kumfanya Elizabeth kushangaa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kweli?”
“Nakutania. Watu wananiita kijana mdogo, nina umri wa miaka thelathini tu, najiona kuwa mkubwa, miaka inakwenda kwa kasi mno na sijajua ni kwa jinsi gani nitaweza kufanikiwa zaidi ya hapa,” alisema Olotu.
“Watu wanavyosema ndivyo ninavyosema, imekuwaje mpaka kupata utajiri katika umri mdogo namna hiyo?’ aliuliza Elizabeth.
“Kujituma tu, hiyo ndiyo silaha kubwa. Nilikuwa kwenye familia masikini, baba yangu aliendekeza sana mila, alioa wanawake wengi kijijini, zaidi ya saba na alikuwa na watoto sitini,” alisema Olotu.
“Mmmh!”
“Ndiyo hivyo! Sikuupenda umasikini, ili ufanikiwe maishani mwako, haina budi kuuchukia umasikini. Ninaposema kuuchukia umasikini namanisha kwamba inakupasa uamke mapema na kufanya kazi, si kuamka saa sita mchana.
“Unaweza kusema kwamba unauchukia umasikini lakini matendo yako yakaonyesha kwamba wewe ni rafiki mkubwa na umasikini,” alisema Olotu huku akichia tabasamu pana, akasimama, akaifuata chupa ya kahawa na kumimina kahawa, akaanza kunywa.
“Umewezaje kupata masoko nje ya nchi, namaanisha migodi na hatakujenga kiwanda nchini China?’ aliuliza Elizabeth.
“Ujanjaujanja tu,” alisema Olotu na kuanza kucheka.
Elizabeth alijisikia kufarijika, moyo wake ukawa na furaha tele, hakuamini kama mwisho wa siku alikutana na mtu mwingine, bilionea mkubwa barani Afrika. Japokuwa yeye mwenyewe alikuwa bilionea, tena mwenye fedha ndefu lakini moyoni mwake alijiona kuwa na fedha kidogo mno.
“Nimefarijika sana kuwa karibu nawe,” alisema Elizabeth.
“Ila ningependa tuwe pamoja usiku wa leo.”
“Unamaanisha nini?”
“Elizabeth! Wewe ni binti mkubwa, unaelewa kila kitu. Kama ungependa kujua mengi kuhusu mimi, jua kwamba sijaoa,” alisema Olotu.
“Hujaoa? Kwa hiyo unataka tuwe wote kimapenzi?”
“Hahaha! Sikutegemea kama ungeuliza swali kama hilo. Itawezekana kuwa wote kwa siku nzima leo? Nilitamani sana siku nionane nawe,” alisema Olotu.
“Ooppss!” Naomba niende, kuna kitu nakwenda kufanya, ni lazima nirudi Tanzania.”
“Sawa! Basi tuzidi kuwasiliana, nataka siku moja tukae na kuzungumza mengi, hilo tu.”
“Hakuna tatizo,” alisema Elizabeth, hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka huku akiwa ameacha namba yake ya simu kwa bilionea Olotu.
Matumaini yake yakapotea, hakuamini kama mdogo wake angeweza kupona na kuwa kama alivyokuwa kipindi cha nyuma, alihangaika sana kutafuta fedha huku akiwasisitizia waandishi wa habari waitoe tena habari kuhusu mdogo wake ili aweze kupokea michango kutoka kwa watu mbalimbali.
Hakuwa na fedha, kitu pekee alichokuwa akikitegemea kutoka kwa wananchi ni mchango wa fedha tu ili mdogo wake aweze kupelekwa hospitalini na kuwa mzima wa afya. Hapo ndipo chuki kubwa dhidi ya matajiri ilipoanza kujengeka moyoni mwake, hakuwapenda kwa kuwa tu wengi walikuwa na fedha lakini hakukuwa na yeyote aliyejitokeza kumsaidia.
Kiasi cha shilingi milioni saba kilikuwa kidogo mno kiasi cha tajiri mmoja kujitolea na kumsaidia mdogo wake lakini kwa kiasi hichohicho hakukuwa na tajiri yeyote aliyejitokeza kumsaidia hali iliyosababisha wakati mwingine kutamka waziwazi kwamba aliwachukia matajiri.
“Imekuwaje?” aliuliza daktari mara baada ya wiki kupita.
“Bado ninahangaika, nimepata laki tatu tu mpaka sasa hivi,” alijibu James.
“Umekwenda wapi na wapi?”
“Sehemu zote daktari, nimezunguka sana lakini kote huko, nilichoambulia ni hiki,” alisema James.
Hali ya Glory ilikuwa mbaya kitandani, kila siku alikuwa mtu wa kulala kitandani au kama kukaa kitini, aliinuliwa na kutulia hapo. Hakuzungumza kitu chochote kile, mwili mzima ulikuwa umepooza na ni kichwa tu ndicho kilichofanya kazi.
Baada ya wiki moja kukatika, Glory akarudiwa na fahamu, kidogo hayo yakaonekana kuwa mafanikio makubwa kwa kuona kwamba inawezekana angeweza kupona na kuwa mzima kabisa lakini majibu yalikuwa yaleyale kwamba hakuweza kurudi katika hali yake ya kawaida.
“Mungu! Naomba umsaidie Glory, hatuna kitu kingine tunachokitegemea zaidi yako,” hayo yalikuwa maombi ya James kila siku lakini hakukuwa na kilichobadilika.
Hakutulia kabisa, leo alikuwa akienda kwenye magazeti, kesho kwenye redio na sehemu nyingine. Mwili wake ukaanza kupungua, mawazo yalikisumbua kichwa chake mpaka kipindi kingine kuhisi kwamba angeweza kupata vidonda vya tumbo.
“Tatizo nini?” aliuliza mfanyabiashara mmoja, alikuwa mtu mwenye maduka mengi Kariakoo.
“Ninahitaji msaada wako!”
“Hivi tunafahamiana kweli?”
“Hapana mzee, ila mimi ni mwananchi wa kawaida tu.”
“Sawa. Nikusaidie nini?”
Hapo ndipo James alipoanza kusimulia kile kilichotokea, muda wote wa simulizi hiyo alikuwa akibubujikwa na machozi tu. Alisimulia huku akiumia moyoni mwake, picha ya Glory iliyokuwa ikimjia kichwani mwake iliuchoma moyo wake.
“Ninahitaji unisaidie fedha kwa ajili ya kumtibu mdogo wangu,” alisema James huku akiyafuta machozi yake.
“Nikusaidie fedha?”
“Ndiyo!”
“Kijana! Inakuwaje kunifuata mtu kama mimi? Unadhani mimi ni tajiri? Kwa nini usiwafuate watu wenye fedha mpaka kunifuata mimi mwenye vijisenti, tena vya mboga?” aliuliza mzee yule, japokuwa alikuwa na fedha nyingi na hata milioni kumi halikuwa tatizo kwake, lakini hakuwa mtoaji.
“Naomba unisaidie mzee wangu! Mdogo wangu anakufa!”
“Sina fedha, ningekusaidia , kweli tena.”
“Hata laki moja?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mimi ni kama wewe tu, sioni sababu ya kujificha, ningekusaidia tu,” alisema mzee huyo.
Hakuwa na roho ya huruma hata kidogo, japokuwa James aliendelea kumuomba msaada mzee huyo laini hakuwa radhi kumsaidia. Hakuwa tayari kutoa kiasi kikubwa cha fedha na wakati hakuwa na matarajio ya kuingiza baada ya kutoa fedha hizo, hivyo akaamua kumnyima kiasi hicho cha fedha.
James alisikitika mno, chuki yake dhidi ya matajiri ikaongezeka zaidi na kuamua kuwachukia katika maisha yake yote. Aliendelea kutafuta msaada, hakufanya vibarua vyake tena, kitu alichokuwa akikitafuta kwa wakati huo ni fedha tu.
*****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment