Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

MVUA YA HUBA - 3

 







    Simulizi : Mvua Ya Huba

    Sehemu Ya Tatu (3)

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Maisha ya vitisho toka kwa mtu asiyejulikana yaliendelea kwa Luis, akatamani awashirikishe wazazi wa Lucy lakini alihofu uenda atasababisha matatizo mengine kwa familia ile.

    Kadri siku zilivyozidi kusonga ndivyo Luis na Lucy walivyozidi kuzoena, ukiwatazama unaweza kufikiri ni mapacha waliozaliwa na mama mmoja. hisia tofauti zikaibuka kati ya watu walio waona wengine wakafikiri kuwa wawili hao wameshazama katika dimbwi la huba lakini wao hawakuwa na wazo hilo.



    Jumamosi moja Lucy alimuomba Luis amsindikize mjini kwa ajili ya kununua mahitaji mbalimbali, bila kipingamizi Luis aliridhia. Wakatembea na kufika sehemu yenye mzunguko wa barabara, Luis akatangulia kuvuka akifuatiwa na Lucy, ghafla gari ndogo aina ya toyota nissan ikaja kwa kasi na kutaka kuwavaa wote wawili. Katika hali ya kustaajabisha zaidi akatokea kijana mmoja aliyekuwa mwepesi wa mbio na mwenye nguvu za misuli akamsukuma Luis pembeni na wakati huo huo akamvuta Lucy kumuepusha na ajali hiyo. watu walioshuhudia ilo wakaona kama mchezo wa kuigiza japo ni kweli kijana huyo ameyaokoa maisha ya vijana hao wawili.

    "Kuweni makini mvukapo barabara" alisema kijana huyo.

    Lucy alishindwa kuongea lolote zaidi ya mwili wake kutetemeka kwa hofu, ilimchukua dakika kadhaa kung'amua juu ya jambo lile.

    "Shukrani kaka sitosahau hili ulilotufanyia leo, Mungu akubariki na kukuzidishia," alisema Luis ambaye alipata michubuko kwenye mikono na mguu wake wa kushoto baada ya kusukumwa na kijana aliyewasaidia.

    "Usijali binadamu tupo kwa ajili ya kusaidiana na naona shemeji hapa amepatwa na mshtuko kidogo ni vyema ukarejea nae nyumbani akapumzike" alijibu kijana yule.

    "Hahahaha! kaka huyu ni kama dada yangu misingi ya uhusiano wetu si wa namna hiyo"

    "Daah! Nisamehe sana niliwaona toka mkiwa upande ule wa barabara, akili yangu haikuwa na shaka juu ya nyinyi wawili kuwa wapenzi ndiyo maana nikasema kauli hii"

    "Usijali wengi wanahisi hivyo lakini sivyo ilivyo"

    "Mimi naitwa Izack ni afisa masoko katika kampuni ya moja ya usafirishaji iliyopo Kihonda, sijui ninyi wenzangu?"

    "Mimi naitwa Luis na huyu anaitwa Lucy yeye ni daktari bingwa na mimi ni mwanamuziki"

    "Ooh! Mna majina yanayoshahabiana sishangai kwa wawili ninyi kuwa na urafiki mkomavu, nafikiri tusipoteze muda zaidi niwaache mkapumzike na haya ni mawasiliano yangu," alisema Izack huku akitoa kadi ndogo iliyo na mawasiliano ya namba za simu na anuani ya barua pepe.

    Luis alimsindikiza Lucy na kumsimulia mama yake kila kilichojiri, mama alishtuka sana juu ya jambo hilo. Hakuielewa hatima ya bintiye kwani kila alipoikaribia furaha ndipo huzuni ilimwandama. Mama akaifikiria ajali iliyotaka kuwapata muda mfupi uliopita na akavuta kumbukumbu juu ya ajali iliyotokea na kusababisha kifo cha mkwewe, akapatwa na hisia huenda kuna mchezo mchafu unaochezeka.



    *************

    Michubuko midogo aliyoipata Luis ikafanya aanze kuhisi maumivu, ikabidi apitie hospital wakamsafisha na kumueka dawa. Wakati akiwa njia kurejea nyumbani simu yako ikaita alipoangalia akakuta ni namba mpya kwa mara nyingine, akabonyeza kitufe cha kupokelea na kuiweka sikioni.

    "Hiyo ni rasharasha tuu gharika inakuja" ilisikika sauti iliyo upande wa pili na kabla Luis hajasema lolote simu ikakata.

    Luis akafikiri maneno yale akaunganisha na tukio la mchana akahisi vinauhusiano mkubwa na asipokuwa makini anaweza kujikuta matatani Zaidi.

    “Huyu mtu anahitaji nini kwa Lucy? Kwanini anayafanya haya yote?” alijiuliza Luis.



    *************

    Akili ya Izack haikutulia toka macho yake yalipotua kwa Lucy, muda wote aliitazama simu yake akitegemea kuona ujumbe mfupi au kupigiwa na mrembo huyo. Mara zote aliposikia simu ikiita aliikimbilia kwa haraka lakini hakuwa mtu yule ambaye yeye moyo wake unamuhitaji.

    “Kupenda ni sawa na kuwa mtumwa, kupelekeshwa na kufanya vitu ambavyo yawezekana hutamani kuvifanya, mhmh! Lucy u drive me crazy, sijui nitaanzia wapi kukwambia kilichopo moyoni mwangu naisubili simu yako. Najua utapiga ndani ya muda mfupi ujao” alisema Izack ambaye kwa hakika alionekana kuweweseka kwa penzi la Lucy japo hakuliweka bayana.

    Chumba cha Izack kilipambwa na picha za Lucy zilizoning’inizwa ukutani, muda mwingi Izack husogea kati ya moja ya picha zilizo kwenye kuta za chumba na kusema,

    “Naamini utakuwa wangu”



    Maneno hayo yalimtia nguvu Izack na kumfanya kutotetereka katika ndoto ya kuushinda moyo wa Lucy. Wakati huo hakujua lolote juu ya mpango haramu wa kuangamiza kila kiumbe kinachomsogelea Lucy kwa nia ya kuwa naye kimapenzi. Akajikuta anaweka tamanio bila kuelewa kwamba laweza kumsababishia matatizo.

    Muda mfupi baadae simu yake ya mkononi ikaita, kwa haraka mno akabonyeza kitufe cha kupokelea na kuiweka sikioni,

    “Hallo”

    “Hallo”

    “Nani mwenzangu?” alisema Izack baada ya kuisikia sauti ya kiume.

    “Mimi ni Izack”

    “Izack yupi?”

    “Mchana wa Leo uliokoa maisha yetu tulipokuwa hatarini kwa kugongwa na gari lililopoteza muelekeo na kuja upande wetu”

    Izack akatabasamu akaona njia ya kumpata Lucy inafunguka yenyewe, akashusha pumzi ndefu na kusema,

    “Sawa nimekukumbuka ndugu yangu, vipi dada yako anaendeleaje?”

    “Anaendelea vizuri tu”

    “Vipi naweza kupata mawasiliano yake”

    “Ndiyo nitakutumia”

    “Nitashukuru sana”



    Luis akatuma mawasiliano ya Lucy kwa Izack bila kuelewa Izack ana kusudio gani Zaidi kwa Lucy ambaye kwa wakati huo alimuona kama dada yake. Baba yake Izack alikuwa pembeni akisikiliza na kutazama kila kitu ambacho mwanaye alikuwa akifanya. Akamsogelea na kumshika bega kisha akamwambia,

    “Mwanangu najua unamawazo mengi juu yangu, ila kumbuka kanuni ya maisha kuwa kila kilichochakavu hakina budi kukipisha kipya, baba yako kwa kiasi kikubwa nimekula chumvi. Ni wakati wako sasa kuifiiria kesho yako itakuaje, siku hazigandi na uzee huu karibu angalia watoto zake badala ya kukuita baba wakakuita babu. Nakuombea umpate mwezi mwema utakayejenga naye familia na kuondoka katika dimbwi hili la upweke wa moyo”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nina furaha nikiwa nawe baba yangu hata hivyo nitayazingatia na kuyafanyia kazi uliyoniambia,” alisema Luis.

    “Ubaki katika busara na hekima hii siku zote za maisha yako”

    Maongezi ya siku hii yalimfanya Luis kuanza kufikiri kuhusu kuwa na familia kwa mara ya kwanza. Akili yake ikazunguka na kutafuta nani hasa anayeweza kuwa mwenza wake haikupata mtu Zaidi ya kugota kwa Lucy.

    Akakumbuka maneno ya Izack “naona shemeji hapa amepatwa na mshtuko kidogo ni vyema ukarejea nae nyumbani akapumzike" jinsi alivyojibu na Izack alivyoendelea kusema "Daah! Nisamehe sana niliwaona toka mkiwa upande ule wa barabara, akili yangu haikuwa na shaka juu ya nyinyi wawili kuwa wapenzi ndiyo maana nikasema kauli hii"

    Akaendelea kumuweka Lucy akilini mwake toka siku ya kwanza alipomuona hadi siku waliyokoswa na ajali. Akatabasamu na akaamini jambo aliloambiwa na baba yake litatimia siku chache zijazo.

    ************

    Mbio za kulisaka penzi la Lucy likaanza kwa vijana wawili ambao kila mtu hajajua kama mwenzie ana lengo sawa na lake. Izack akapata nafasi ya kuanzisha urafiki na Lucy ambao kwa kiasi kikubwa ulididimiza ukaribu kati ya Lucy na Luis. Izack alikuwa vizuri kifedha hivyo alimudu kumtembeza Lucy katika kila kona ya Tanzania, jambo hili likamshtua kidogo Luis ambaye hakuwa anazielewa vizuri hisia zake kwa wakati huo.

    Ulikuwa ni usiku mnene mno Luis hakuweza kupata usingizi kutokana na kufikiria changamoto iliyojitokeza katika harakati za kuweka wazi hisia zake kwa Lucy. Baba yake wakati anatoka kwenda kujisaidia akaona mlango wa chumba cha mtoto wake ukiwa wazi na taa ikiwa bado inawaka akaendelea na safari yake na aliporejea akaingia chumba cha mtoto wake na kumkuta akiwa mwenye kuwaza sana.

    “Sio kawaida kwa wewe kuwaza hivi, yawezekana likawa swala nyeti sana,” alisema baba yake Luis.

    “Baba ni kama vile sijielewi siku hizi”

    “Kivipi?”

    “Nahisi kuumia moyoni ninapokosa kumuona au kuongea na Lucy, natamani niwe karibu yake muda wote, ghazabu unipanda ninapomuona Izack akimkaribia baba sielewi nimekuaje na haya yote yanasababishwa na nini?”

    “Hama hakika mganga hajigangi, Luis wewe ni mashuhuri kwa tungo za huba, unayeweza kufanya umma wa wasichana kuvutika na unachozungumza. Leo hii unashindwa kugundua kama umeingia katika mapenzi? Unampenda Lucy!”

    “Yeah nampenda Lucy” alijibu Luis.

    “Ni wakati wako wa kumwambia kuwa unampenda”

    “Eenh! Baba nampenda tu kawaida, haiwezekani kwa mimi kumpenda hivyo mimi, mtu mwenyewe yupo kama chizi chizi”

    “Acha kuvunga nenda kamwambie kilichopo moyoni mwako”

    Maneno hayo yakamtia nguvu Luis na kujiapiza nafsini mwake kuwa kabla jua halijazama siku ya kesho lazima aweke wazi hisia zake kwa Lucy.

    *************************

    Lucy alifurahishwa na ukaribu wa Izack, Kumbukumbu za Mumewe zikaanza kufifia kadri muda zilivyozidi kusonga. Mchana wa siku hiyo jiji la Morogoro lilitawalia na joto kali mno, Lucy aliamua kukaa katika bustani iliyo nyuma ya nyumba yao akawa akisoma riwaya ya “USALITI WA KIAPO” iliyotunga na mtunzi mashuhuri Afrika Mashariki “NEA MAKALA”. Riwaya hiyo ilimgusa sana Lucy akaduwazwa jinsi kiapo kilichosalitiwa kikitoa adhabu katika mapenzi na jinsi watu wanavyolaumiana. Lucy aliogopa kidogo lakini alipoikumbuka ile Kauli ya kwamba kifo tu ndicho kitakachowatenganisha basi akajipa tumaini hata kama akipenda tena hakuna madhara. Akaendelea kuwaza na kuwazua hadi ufahamu wake ukahama kabisa katika dunia hii, hakuweza kutambua kama Luis alifika eneo hilo na amekaa karibu yake akimtazama.

    “Mhmhmh! Nina uzoefu wa nadharia vitendo sivielewi, nimezoea kuyaandikia lakini kuyafanya ujasiri umenikimbia. Kweli huku ni kupenda au kuchanganyikia, sioni kasoro japo hamna mwanadamu hasiye na kasoro, ooh! Luis mimi nimetegwa nikategeka, lazima nimwambie leo” alinena Luis na nafsi yake huku akiendelea kumtazama msichana yule ambaye kwa sasa alionekana mrembo maradufu.

    Lucy aliendelea kuwa katika hali ya kufikiri mno, hakuutambua uwepo wa Luis hadi pale alipogeuza shingo yake na kumtazama. Lucy alishtuka mno,

    “Wewe umefika saa ngapi hapa!” aliuliza Lucy kwa mshangao.

    “Muda tuu”

    “Sasa mbona hujanishtua?”

    “Sikutaka kukusumbua” alijibu Luis.

    Luis akatabasamu na akawa kama anafikiri kitu kisha akashusha pumzi ndefu na kumsogelea Luis karibu akamkazia macho na kusema,

    “Toka nimekufahamu nimekuwa mwenye furaha isiyo na kifani, umenifanya nione kuwa mimi bado nina thamani katika hii dunia, japo nilijiapiza kutokuufungua moyo wangu kwa mwanaume yeyote yule ila kwako nimeshindwa. Sijutii na wala sioni haya kukwambia kuwa nakupenda si kama rafiki tuu bali yule mtu aliyenyeshewa na kuloa kwa mvua ya huba iliyotoka kwenye anga lako. Nitafurahi kama utanipa hifadhi ndani ya moyo wako”

    Maneno hayo yalimfanya Luis kuhisi kama amepigwa na shoti ya umeme, akajikuta akisimama na kupiga hatua fupi kurudi nyuma. Hakujua aseme nini kwani hakulitegemea hilo japo alienda pale kwa lengo la kuelezea hisia zake kwanza. Lucy akasimama na kusogea Zaidi alipo Luis,

    “Naijua falsafa ya wanaume kuwa mnaanza kufikiri kabla ya kuweka wazi hisia zenu, je hili ninalokwambia ni gumu? Huwezi kunipa jibu leo? Nikupe siku, wiki au mwezi wa kufikiri?” aliuliza Lucy.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Luis akajikuta akirudi tena kukaa bila kutegemea kiukweli hakuwahi kuambiwa maneno yale japo yeye alizoea kuyaandika na kuimba kwenye nyimbo zake. Kila alipojaribu kutamka alishindwa aseme nini, japo moyo wake tayari ulishamkubali mrembo yule. Kubabaika kule kukamfanya Lucy acheke mno, alicheka hadi kukaa chini kabisa kwenye nyasi zilizofyekwa kwa namna iliyofanya zivutie. Luis akashangaa kumuona Lucy akicheka,

    “Kipi kinachokuchekesha?” aliuliza Luis.



    “Kumbe hivi ndivyo atakavyoshtuka kama nikimwambia maneno haya” alijibu Lucy.

    Jibu lile likamshtua na kumchanganya Zaidi Luis ambaye alifikiri maneno yale alikuwa akiambiwa yeye, akamuangalia tena Lucy na kusema,

    “Maneno haya yanamaana gani?”

    “Maneno hayo nafikiria kumwambia mtu ambaye ameuteka moyo wangu lakini nakosa ujasiri ndiyo maana nimeyajaribu kwako. Je ikitokea msichana amekuambia hivyo utamchukuliaje?”

    “Kama akisema kwa kumaanisha na kama moyo wangu utamridhia basi sitokuwa na kipingamizi cha kuwa nae” alijibu Luis.

    “Mhmh! Hautofikiri kuwa yeye ni Malaya? Na hautofikiri kuwa kama ameweza kukwambia hivyo wewe je hakuna wanaume wengine aliokwisha waambia?”

    “Binadamu wote wana haki sawa katika kuelezea hisia zao kwa watu wawapendao hivyo kama ningalikuwa mimi nisingefikiri kwa namna mbaya”

    “Asante sana Luis! Wewe ni Zaidi ya rafiki kwangu na siwezi kukuficha hili, ukweli nimejikuta nikitamani kuwa karibu na Izack, moyo wangu unakereketa nisipopokea simu yake au hata kuona ujumbe mfupi toka kwake. Siwezi kuvumilia Zaidi nahitaji kumwambia ukweli” alisema Lucy.



    Daah! Kwa mara ya kwanza Luis alianza kuhisi chungu ya penzi hata kabla hajalionja, akahisi kama mtu ameshika kisu kikali na kuukata moyo wake vipande vipande. Machozi yakamtoka bila yeye mwenyewe kuelewa kuwa analia, Lucy akaiona ile akashangaa sana. Akamsogelea Luis ambaye tayari akili yake ilishaama maana maumivu aliyoyasikia hakujua ni kwa namna gani ataweza kustahimili.

    “Hey! Are you okey? (wajisikiaje sasa)”

    “Yeah! Am fine (niko poa)”

    “Then why are you crying? (kwanini unalia?)”

    Luis hakuwa na jibu la swali hilo, hakuwa tayari kufichua siri ya moyo wake, hakuwa tayari kumpa wakati mgumu Lucy ambaye alishampenda mwanaume mwingine. Luis akailazimisha furaha ingali moyoni mwake kulikuwa na msiba, akacheka huku machozi yakimtoka, akasogea na kumkumbatia Lucy.

    “Nalia kwa sababu nimefurahi kuona moyo wako umefunguka, naamini sasa hautokaa upweke wala kuongea mambo yako ya ajabu. Nitaendelea kuwepo kila utakonihitaji” alisema Luis.

    “Luis sina la kukulipa ila nichukulie kama mdogo wako wa kike ninayehitaji ulinzi wa kaka”

    Kauli hiyo ilididimiza kabisa ndoto za Luis na akapata jibu kuwa msichana yule anamchukulia yeye kama kaka na si vinginevyo. Wahenga wanasema hasiyekubali kushindwa si mshindani, hivyo katika kinyang’anyiro kile Luis akakubali kuwa ameshindwa.

    “Nenda! Usichelewe naamini atakuwa anakusubili mahali, kamwambie kama ulivyonambia mimi bila kupunguza wala kuongeza chochote naamini atakuelewa”

    “Asante kaka yangu”

    Luis hakuwa na la ziada ikabidi aage na kuondoka huku akiwa mwenye maumivu makali moyoni mwake, hakutamani kupanda usafiri wowote, akatembea huku machozi yakimbubujika.

    “Sitamani mapenzi yakamuumiza mwingine kama yalivyoniumiza mimi, manung’uniko ya moyo acha yabaki moyoni husiyatoe hadharani, yawezekana umenisahau Niseme nini sasa! Moyo wangu wahuzunika hata machozi kunibubujika, niseme nini tena? Nilikupa furaha yote, nilikujaza tabasamu nyakati zote. Kama ilivyo maji kuwa ishara ya uhai ndivyo nilivyoyatunza mapenzi haya kwa uaminifu, lakini akaja mtu mwenye kung’ara mithili ya mbalamwezi ukamkaribisha na akaijaza sehemu iliyotupu ya moyo wako. Kwa hakika hili ndilo kosa nililolifanya, sikuwahi kukutamkia lolote lile kabla, na kama ungeli kubali usingelienda mbali nami, hamna atakayeelewa maumivu haya ninayopitia” alisema Luis huku akitembea bila kuelewa mahala gani anakwenda.



    Wakati akiendelea kutembea akajikuta akivuka barabara bila kuangalia, watu wakapiga yowe la kumzuia asivuke lakini hakusikia. Maneno yale ya kutotamani mapenzi kumuumiza mwingine kama yalivyomuumiza yeye yalizidi kuzunguka kichwani mwake. Luis alishtusha na gari lililofunga breki miguuni mwake,

    “Wewe bwege kama umechoka kuishi kafie mbele sio kutuletea mkosi barabarani” alisema dereva wa gari hiyo ndogo ya abiria.



    Luis hakusema kitu Zaidi ya kuinamisha kichwa na kufunga mikono yake ishara ya kuomba radhi, kwa wakati huo kifo kilikuwa bora kuliko mfukuto ule aliousikia moyoni mwake. Akaendelea na safari hadi alipokutana na sehemu yenye miti, akakaa chini na kuinamisha kichwa chake huku bado machozi yakimtoka.



    ************************

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Uzuri wako ni mashuhuri kama anga, aliye hapa na aliye sehemu yeyote ya dunia ulishuhudia, tabasamu lako tamu Zaidi ya sharubati iliyochanganywa na asali, sauti yako sasa, kama ingekuwa ni kituo cha redio basi ningeisikiza hiyo kila ninapokuwa. Shule imekupa fani ya utabibu wa mwili ila Mungu amekupa kazi ya kuutabibu moyo wangu. Nakupenda Lucy”

    Maneno hayo yalitoka katika kinywa cha Izack mara baada tu ya wawili hao kuonana katika mgahawa uliopo kwenye hoteli moja maarufu mjini Morogoro. Lucy alifurahi sana kwani kabla hajasema tayari alishakubaliwa na kabla hajaomba tayari alishapewa. Lucy akakubali na Izack akamuomba wajongee mbele hili wacheze muziki, Dj akaweka muziki laini ambao uliwafanya wawili hao wacheze wakiwa wamekalibiana Zaidi. Izack alionesha mwenye kufurahi muda wote akatamani siku hiyo iwe siku ya kwanza ya kumbusu Lucy, akaongeza ukaribu Zaidi na kushika kiuno cha Lucy kisha taratibu akapeleka lipsi zake, lucy akafumba macho na kuwa tayari kuzipokea. Wakati Izack akiwa karibu Zaidi kuufikia mdomo wa Lucy ghafla akakumbuka maneno ya marehemu mumewe,

    “Lucy mke wangu! Wewe ni mwanamke mzuri kuliko wote ambao macho yangu yamebahatika kuwaona, nakupenda sana,”

    Kauli hiyo ikamfanya Lucy ajitoe mikononi mwa Izack na kuanza kupiga hatua fupi kurudi nyuma, moyo ukaenda kasi mno, Lucy hakuweza tena kukaribiana na Izack akarudi kwenye meza waliyokaa na kuchukua mkoba wake tayari kwa safari ya kurejea nyumbani. Izack alihisi amemkosea mno Lucy kwa kutaka kumbusu kwa siku hiyo ya kwanza, akamkimbilia na kumwambia,

    “Am so sorry! I was out of control (Samahani nilijikuta nikishindwa kujizuia)”

    “Its okay (Usijali)” alijibu Lucy huku akiendelea na safari yake.

    Izack akamuomba amsindikize nyumbani kwani giza lilishaingia lakini Lucy alikataa na kutoka nje ambapo alikodi gari (TAX) iliyompeleka hadi nyumbani kwao. Njia Lucy alijiuliza maswali mengi ambayo hakuelewa yanatoka wapi.

    “Nimekuaje mimi! Kwanini sauti ya mume wangu ijirudie kichwani mwangu kwa wakati ule? Wapi nilipokosea?” alijiuliza Lucy.



    Hadi giza linaingia Luis alikuwa bado amekaa mahala pale akiwa amejikunyata kama kifaranga aliyetelekezwa na mama yake. Simu yake ikaita na akakuta namba ngeni akaipokea na kuiweka sikioni,

    “Nilikwambia wewe ni gugu usiye nafaida nyikani, ila mimi ndiye ngano bora niliyevunwa na kuwekwa ghalani. Huwezi shindana nami”



    Ilisikika sauti iliyo upande wa pili wa simu na kabla ya Luis hakusema kitu simu ikakata. Luis akaanza kuunganisha matukio picha ya Izack ikamjia kichwani mwake akawaza uhenda yule si mtu mzuri japo hakuwa na uhakika juu ya hilo.

    “Ushindani wangu haukuwa wazi kwa yeyote hata mimi sikuwa natambua kama nilikuwa nashindana na mtu mwingine katika kuupata moyo wa Lucy. Sasa yeye amejuaje? Ni kweli Izack ni mtu mbaya au kuna mtu mwingine anayetengeneza haya mambo ili nimchukie mtu aliyeokoa maisha yangu? Hakuna marefu yasiyo na ncha ipo siku nitajua lililopo nyuma ya pazia” alisema Luis na kunyanyuka pale alipokaa tayari kwa kuelekea nyumbani.



    Mwendo wa Luis ulikuwa kama wa mtu aliyekata tamaa, akafika nyumbani na kukaa kwenye kiti kilichopo sebuleni. Baba yake alishuhudia mfadhaiko uliopo kwa kijana wake, akamsogelea na kuketi karibu nae.

    “Mwanangu mahusiano ni sawa na chupa na mfuniko, zipo chupa za duara zinazofunikwa kwa mfuniko wa duara, zipo chupa za mraba zenye kufunikwa kwa mifuniko ya mraba na ipo ya pembe tatu yenye kufunikwa na mfuniko wenye umbo hilo hilo. Kama ilivyo ngumu kwa chupa ya duara kufunikwa na mfuniko wa pembe tatu ndivyo ilivyo ngumu kwa mahusiano. Mapenzi hayalazimishwi ila huja kwa kutengenezwa na kumbuka kuwa kila kitu hutokea kwa sababu, naamini malkia wa moyo wako yupo mahali akisubili wakati ufike hili uungane naye usikate tamaa mwanangu wewe ni mwanaume, usioneshe udhaifu”

    Maneno hayo yalikuwa kama maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu kwani yaliweza kupunguza maumivu yaliyo kwa Luis na kuchipusha tumaini jipya.

    “Baba umejuaje kama sijafanikiwa”

    “Hahaha! Luis mwanangu kila siku nakwambia vitendo vinakelele nyingi kuliko maneno, macho yangu yalipotua kwenye uso wako nimeyajua mafadhaiko yako hivyo kama mzazi sina buni kukutia nguvu na kukwambia kuwa kesho nayo siku, Mungu atakupa nafasi nyingine unayostahili”

    “Najihisi ni mwenye bahati sana kuwa na baba kama wewe, nathubutu kusema hamna Zaidi yako, nakupenda sana na Mungu azidi kukuweka mzee wangu”

    Waliendelea kuongea huku baba akizidi kumfariji na kumtia moyo Zaidi mwanaye, kadri ya mshale wa saa ulivyozidi kusogea ndivyo Luis alijikuta akirejea katika hali ya kawaida.



    BAADA YA MIEZI MIWILI



    Uhusiano kati ya Izack na Lucy ukakomaa na kuota mizizi, Izack akaona ni wakati sahihi kwa wao kuweka mahusiano yao wazi kwa familia zao.

    “Lucy mpenzi siku nyingi zimepita sasa, sitaki tuendelee kuishi hivi nataka tuweke mahusiano yetu wazi na hatimaye tuunganishwe kwenye ndoa takatifu” alisema Izack.

    “Ni kweli usemayo lakini nivumilie kidogo mpenzi kila kitu kitakuwa sawa”



    Kwa muda wote huo Lucy hakumruhusu Izack ambusu wala kufanya naye chochote Zaidi ya kumbatio na kushikana mikono. Msimamo huo wa Lucy ulimpa wakati mgumu Zaidi Izack ambaye alikuwa mkware kiasi cha kuwa na matamanio makubwa kwa mpenzi wake. Akatamani mambo yaende kwa haraka hili awe na uhuru na mwanamke huyo ambaye ameuteka moyo wake,

    “Sawa nipo tayari kusubiri hadi pale utakapokuwa tayari” alijibu Izack.

    “Thank you (Asante)”

    “Never mention! It’s my pleasure (Usijali)”



    Wazazi wa Lucy walifurahishwa na hali aliyonayo binti yao, wakaahidi kuitunza furaha ile kwa gharam yeyote. Wakapanga kuonana na wazazi wa Izack waone uwezekano wa kupitisha ndoa baina ya wawili hao. Japo kiutamaduni hawakuwa na nafasi ya kufanya hivyo isipokuwa upande wa kiume. Taharifa ya uhusiano kati ya Lucy na Izack ikafika kwa wazazi wa Lucas nao hawakuwa na kipingamizi Zaidi ya kumtakia kila lililo jema maana aliteseka sana alipompoteza mumewe.



    **************



    Kama ilivyo kwa misemo ya wahenga kuwa mvumilivu siku zote hula mbivu, Lucy akaridhia Izack amchumbie na maandalizi kwa ajili ya tukio hilo yakaanza. Wakati mambo yakikaribia kukamilika kabisa Luis anaibuka na kuhitaji kuonana na Lucy, alishangazwa kidogo na mapokezi aliyoyapata alipofika nyumbani kwa kina Lucy kwani watu walionekana kama kupuuzia uwepo wake, hamna aliyemsemesha wala kumjulia hali. Hakujali hayo shida yake kubwa ilikuwa ni kuonana na Lucy japo kwa wakati huo ilikuwa ngumu mno, katika kuangaza huku na huko akamuona mama yake Lucy kwa haraka akamsogelea na kumuomba wazungumze pembeni,

    “Mama Shikamoo!”

    “Marahaba mwanangu! Karibu na utusamehe maana kila mtu anashughuli nyingi leo”

    “Mama uliomba niwe mtoto wako nami nikaridhia, Lucy amekuwa kama dada kwangu ningependa kutoa maoni yangu juu ya huu uchumba utakaofungwa leo” alisema Luis huku akionekana mwenye wasiwasi tele na aliyekosa kujiamini hata kidogo.

    “Sema mwanangu mimi nakusikiliza”

    “Binafsi nahisi kuwa Izack si mtu sahihi kwa Lucy”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sentensi hiyo ikamfanya mama yake Lucy aduae mno akamtazama Luis kuanzia juu mpaka chini hasiweze kuelewa kuwa maneno yale aliyamaanisha au alikuwa akitania.

    “Luis unamaana gani unaposema kuwa Izack si mtu sahihi kwa mwanangu? Je wewe ndiye Sahihi?” aliuliza mama yake Luis.

    “Sio hivyo mama ila…”

    “Basi ishia hapo hapo sihitaji kuusikia upuuzi wako, mimi najua kuwa unampenda Lucy ila bahati haikuwa upande wako hivyo mwache mwanangu afurahie maisha yake mapya” alisema mama Lucy bila kumpa nafasi Luis ya kuongea.

    “Lakini mama…”

    “Kijana tulikupokea na kukuona kama mtoto wetu ila kwa haya sitojutia kukwambia ondoka katika nyumba yangu na sihitaji kukuona maana huna nia njema na familia hii”

    “Sawa naondoka ila fanya kila uwezalo kuzuia hili” alisema Luis kisha akageuka nyuma na kutaka kuondoka.

    Shingo yake ilipogeuka akakutana uso kwa uso na baba yake Lucy ambaye alikwishayasikia yote yaliongeleka. Akamwangalia Luis kwa ghazabu mno,



    “Nilizani wewe ni nuru uliyekuja kuiangaza familia hii ila sivyonilivyofikiri maana umekuwa giza unayeitaji kuipoteza furaha iliyotawala hapa Luis nenda na usifikirie kurudi tena hapa” alisema baba yake Lucy kwa ukali mno.



    Luis aliangusha machozi baada ya kuona kuwa hana namna ya kufanya kuzuia uchumba ule kati ya Izack na Lucy. Baada ya matukio ya vitisho kumkuta Luis aliamua kufanya uchunguzi binafsi juu ya mtu aliyekuwa akiyafanya hayo. Mwisho wa uchunguzi akagundua kuwa Izack hakuwa mtu mwema hata kidogo matatizo yote aliyoyapitia Lucy chanzo kilikuwa ni Izack. Wakati akiondoka akakumbuka simulizi aliyopewa na mmoja kati ya watu ambao hawakutaka wafahamike juu ya Izack.



    **************



    Izack kiuhalisia si afisa masoko kama alivyojitambulisha kwa Lucy, yeye ni mmoja kati ya wanajeshi ambao wanafanya kazi kitengo tofauti na alichokuwa akifanya Lucas. Izack alikuwa mwanaume wa kwanza kumuona Lucy kabla ya Lucas, alianza kujenga upendo mkubwa bila kuweka wazi hisia zake, hakuwa na ujasiri wa kuonana na Lucy ambaye kwa kipindi hiko alikuwa bado ni mwanafunzi wa udaktari. Lucy alikuwa mwanamke asiyeyumbishwa katika msimamo wako kwa kipindi hiko Izack alikuwa mmoja kati ya wavulana wengi waliokataliwa na Lucy. Haikuwa bahati kwa Lucy kwani hakuweza kumkumbuka Izack wala kukumbuka kile alichomfanyia.

    Tokea kipindi hiko ambacho Izack alikuwa mafunzoni na Lucas akiwa mmoja kati ya wafunzwa wenzake alijiapiza kulipata penzi la msichana huyo kwa gharama yeyote hile. Hakuwa tayari kudharirika kiasi kile maana kila siku wenzake walimcheka na kumkejeli kwa kutokukubaliwa na Lucy.



    Mwaka mmoja baadae Lucas akawa mmoja kati ya wanajeshi kumi waliochaguliwa kwenda kuendelea na mafunzo Zaidi nchini Cuba na hapo ndipo alipokutana na Lucy kwa mara ya kwanza. Katika nchi ile ngeni Lucy alifurahi kukutana na mtu mwenye uraia sawa na wakejapo walisoma vyuo tofauti haikuwa sababu ya wao kutokuwasiliana na hata kutembelea. Urafiki wao ulipokomaa ndipo penzi likachipua.

    Lucas alikuwa wa kwanza kuhitimu na kurejea nchini kisha mwaka mmoja baadae Lucy akafatia, wakatambulishana kwa wazazi na pande zote mbili kuridhia.



    Tarehe ya harusi ikapangwa na taharifa zikasambazwa kwa ndugu, jamaa na marafiki. Izack hakuamini macho yake alipokabidhiwa kadi ya mwaliko wa harusi ile, alitamani ardhi ipasuke atumbukie humo kiukweli hakutamani kushuhudia jambo lile. Akajenga chuki kubwa kwa Lucas pamoja na Lucy akiamini kuwa watu hao ndio sababu ya yeye kupoteza furaha yake. Izack aliweka kiapo kuwa hatojali ni miaka mingapi itamchukua hadi yeye kuwa na Lucy na aliapa kuangamiza mwanaume yeyote atakayemsogelea Lucy.



    Historia hiyo ilimuumiza kichwa sana Luis ambaye alishajua kuwa Lucy amempenda adui yake, hakuna aliyemuunga mkono katika hilo akabaki peke yake hasijue la kufanya. Wazo la kumpigia simu Lucy likaja akachukua simu ya mkononi na kutafuta namba ya Lucy kisha akaipiga kwa bahati mbaya simu haikupatikana. Akarudia kupiga Zaidi ya mara sita lakini majibu yalikuwa vile vile kuwa simu haipatikani, alihisi kuishiwa nguvu akabaki kusubili miujiza ambayo labda itaweza kumuokoa Lucy kutoka mikononi mwa fedhuli yule.



    ****************



    Jioni ya siku hiyo wageni mbalimbali walihudhuria kwenye tafrija fupi ya kumchumbia Lucy iliyofanyika nyumbani kwao. Nyumba yao ilikuwa ni kubwa hivyo haikuwa shida kupokea wageni Zaidi ya 50 kwa wakati mmoja. Wazazi wa Izack wakahudhuria eneo hilo, izack akiwa sambamba na rafiki zake, Lucy siku hiyo alivaa gauni refu la rangi ya pinki lililomfanya aonekane mrembo Zaidi, Izack alivaa suruali nyeusi juu akiwa na shati la kaki lililoshonwa kwa mitindo ya kisasa.

    Muda ukawadia wawili hao wakasimama mbele ya hadhara tayari kwa Izack kumvisha Lucy pete ya uchumba. Izack akapiga goti na kumtazama usoni Lucy kisha akasema,



    “Will you marry me? (Naomba nikuoe)”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lucy hakujibu kitu Zaidi ya kuhisi mapigo ya moyo yakienda kwa kasi mno, joto la mwili likapanda kiasi cha kuanza kusikia kizunguzungu, upepo mkali ukavuma na kufanya wageni waalikwa kutoona vizuri kilichokua kikiendelea mbele. Lucy akahisi kuishiwa nguvu na papo hapo akaanguka chini na kupoteza fahamu. Izack akachanganyikiwa mno hakuamini kama katika siku muhimu hiyo anashindwa kumvika pete msichana yule ili awe wake. Tahayaruki inakuwa kubwa mno katika eneo hilo, mmoja kati ya madaktari waliyoudhuria hafla hiyo anasogea na kupima mapigo ya moyo ya Lucy na kukuta yameshuka mno. Daktari anawahimiza kuwa anahitaji huduma ya haraka hivyo wajitahidi kumuwahisha hospitali kabla mambo hayajaaribika Zaidi.

    “Eenh! Mungu ni mambo gani haya unayoyafanya juu ya binti yangu, kwanini kila akiikaribia furaha unamyang’anya.



    Najua sisi tu wa dhambi mbele yako lakini adhabu hii ni kubwa hatuwezi kuibeba, tafadhali mponye binti yangu” alisema mama yake Lucy huku machozi yakimtoka.

    Watu wakasaidiana kumbeba Lucy na kumuingiza ndani ya gari, kwa haraka Zaidi Lucy akawaishwa hospitali.



    *TANGANYIKA 1917*



    “Ni muda mrefu sasa umepita toka binti huyu apoteze fahamu na wewe umekuwa hapa siku zote kumlinda, nafikiri wakati umefika sasa wa wewe kwenda kufnya majukumu mengine”

    “Sitamani kurejea maskani kwangu ingali huyu binti bado yupo katika hali hii, huyu ndiye tegemeo pekee lililobaki ili kuokoa maisha ya chifu Lukemo”

    “Mhmh! Lukoha chifu yu hoi taabani, hajiwezi kwa lolote mimi nafikiri ni wakati wa kumuachia chifu aende kupumzika kuliko kuwa katika adha ile”

    “Usirudie tena hiyo kauli, chifu atapona tuu naamini”



    Yalikuwa mazungumzo kati ya Lukoha ambaye alikuwa mlinzi wa chifu na kiongozi wa jeshi lote la Sanzani na mzee mmoja ambaye alikuwa kama mshauri katika mambo yahusuyo siasa.

    “Wewe ni kiumbe huru kata hizi nyororo zilizokufunga tafuta furaha yako,” alisema mzee yule ambaye alifahamika kwa jina la Kahise.

    “Furaha yangu ni kumuona chifu akirejea katika afya yake ndiyo maana nipo hapa kuhakikisha binti huyu anapata haueni kwa haraka” alisema Lukoha.



    Wakati wawili hao wakiendelea kuongea wakakatishwa na chafya aliyoipiga lucy au Mwenda wa miaka hiyo. Mwenda akatazama asielewe mahala alipo, akafikicha macho na kuangaza tena papo hapo moyo wake ulilipuka kwa mshangao hasa baada ya kuona sura ya Lukoha, mwanaume aliyefanana na Lucas kwa kila kitu. Maswali mengi yakatiririka kichwani mwake akakumbuka tukio la mwisho aliloliacha katika dunia ile ya 2017 ni alikuwa katika tafrija ya kuvikwa pete na Izack. Lukoha akamtazama Lucy kwa tabasamu zito, akashindwa kuizuia furaha aliyokuwa nayo akamkumbatia binti yule bila kujali ilikuwa ni kinyume na miiko ya Sanzani.

    “Akhsanteni sana mizimu ya Sanzani ombi langu la kila siku limetimia,” alisema Lukoha.

    Lucy akashindwa kuongea lolote Zaidi ya kuduwazwa na lile kumbatio ambalo likafanya akili yake isimame kwa sekunde kadhaa, akahisi mwili ukishikwa na msisimko wa ajabu,

    “Lucy mimi nimekuaje bila shaka nimerudishwa Sanzani, Ooh Mungu wangu nini hiki ninachojisikia juu ya mwanaume huyu?”





    “Tulia hivi usijiangaishe Zaidi, siwezi kuelezea furaha niliyonayo moyoni mwangu baada ya kukuona umerejewa na fahamu” alisema Lukoha.

    “Vipi chifu hali yake?” aliuliza Lucy.

    “Hali bado si shwari, kwa sasa chifu ni nusu mfu nusu hai, naamini utaweza kumponya chifu wetu” alisema Lukoha.

    “Je vipi swala la ndoa bado lipo kama ilivyopangwa?” aliuliza Lucy.

    “Mhmhm! Mwenda ndoa ishapita wewe ni mke halali wa chifu Lukemo”

    “Mmewezaje kupitisha ndoa ingali sikuwa najitambua?”

    “Mama yako alisimama badala yako hivyo muunganiko kati yako na chifu Lukemo ukakamilika kwa namna hiyo”

    “Hapana hilo haliwezekani! Siitambui hiyo ndoa” alisema Lucy au mwenda wa kipindi hiko kisha akainuka bila kusema lolote, mwili wake haukuwa na nguvu ya kutosha alipiga hatua chache na kujikuta akipepesuka kama mlevi, kabla ya mwili wake haujagusa ardhi Lukoha akachomoka mithiri ya mshale na kumzuia Lucy kwa mikono yake miwili.

    “Malkia wangu usalama wako ni wathamani kuliko maisha yangu, hatima ya Sanzani hii mikononi mwako, hivyo kwa wakati huu pumzika kidogo na ule vizuri ili kurejesha nguvu ulizopoteza kisha nitakusindikiza kwa mumeo na utimize jambo ambalo wengi tumekuwa tuklisubilia” alisema Lukoha.



    Mwenda akajikuta akicheka huku machozi yakimtoka kila alipomwangalia Lukoha alizidi kuchanganyikiwa hasijue nini hasa mpango wa Mungu juu ya maisha yake. Aliizuia ndoa kati yake na chifu Lukemo pia akazuia uchumba kati yake na Izack mwanaume aliyetokea kumpenda bila kutarajia kama haitoshi akamrudisha kwa Lukoha ambaye hakuonesha dalili yeyote ya kumpenda mwenda.

    “Kama ni kweli kila kitu hutokea kwa sababu, kwangu mimi imezidi sasa, eenh Mungu nini matokeo ya haya yote? Maisha yangu yamegubikwa na simanzi na upweke kwanini hunipi nafasi hata ya kufurahi na watu niwependao?” alijiuliza Lucy kwa sauti isiyosikikita hata kwa mtu aliye umbali wa sentimita tatu toka alipo yeye.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ******************



    Taharifa ya kurejewa fahamu Mwenda zikasambaa kama harufu ya mzoga uliooza, wanakaya zote za sanzani wakarejewa na tumaini kuu kuwa chifu wao atapata matibabu. Siku chache baadae Mwenda kapelekwa alipo chifu Lukemo, wakati wakiikaribia Zaidi nyumba ya chifu wakasikia kilio kikubwa kilichogubikwa na simanzi nzito. Sauti ya kilio kile ikamfanya lukoha atimue mbio kama swala anayefukuzwa na samba ili ageuzwe kitoweo. Bila hodi Lukoha akaingia mpaka ndani na kumkuta mke mkubwa wa chifu akilia, alipotazama pebeni akakuta watoto wa kike kwa wakiume wachifu nao wakilia kwa majonzi, akasogea hadi alipolala chifu na alipomtazama akagundua kuwa chifu Lukemo mauti yamekwisha mfikia. Akahisi miguu ikiishiwa na nguvu machozi yakamtoka na katika kipindi hiko Mwenda naye akawa anaingia, mke wa chifu alipomuona Mwenda akamrukia kwa hasira na kumlaumu kuwa yeye ndiye chanzo cha kifo cha mumewe.

    “Binti ni mchawi sana wewe! Sitamani kukuona ondoka hapa umemuua mume wangu,” alisema mke mkubwa wa chifu.

    Watoto wengine wa marehemu chifu wakaamka na kumshambulia Mwenda kwa maneno ya fedhea, Mwenda hakuweza kuvumilia akageuka na kutimua mbio. Lukoha naye akatoka na kumfata Mwenda,

    “Malkia wangu si busara wewe kuondoka na kuuacha mwili wa mumeo ndani” alisema Lukoha.

    “Naomba nikuulize swali, hivi unaelewa maana halisi ya ndoa wewe?”

    “Ndoa uhusisha moyo mmoja imara ulioridhia kuungana na nyoyo nyingine ili kuzipa faraja na Amani, kwa mantiki hiyo nadhani jibu umelipata”

    “Hahahahahahaha!”

    Alicheka Mwenda bila kusema neno lolote maana jibu la Lukoha ni wazi lilionesha ubinafsi wa hali juu, kwanini ndoa iwe ya mtu mmoja mwenye nguvu zidi ya watu wengi dhaifu. Hivi ni kweli mwanamke ni kiumbe dhaifu kama wengi wanavyoamini? Mungu aliumba mtu mume kwanza kisha baadae akamletea mtu mke kutoka katika moja ya mbavu zake, sasa iweje kuwe nan yoyo Zaidi ya moja.

    “Mbona unacheka nimekosea kujibu au?”

    “Ndiyo umekosea! Ila nakupa nafasi kwa kukuuliza swali lengine” alisema Mwenda.

    “Sawa Uliza”

    “Je sanzani hii ina watu aina ngapi?”

    Lukoha akakaa kimya kidogo, akafikiri kwa sekunde kadhaa kisha akamtazama Mwenda ambaye alionekana kumaanisha kwa kila alichokiongea,

    “Mhmh! Ukweli Sanzani ilikuwa na watu wengi mno ila toka wajerumani waje na kuteka baadhi ya watu sina idadi kamili” alijibu Lukoha.

    “Ndio unajiita mlinzi mtiifu wa Milki ya chifu ukiwa na upeo finyu kiasi hiko, kwangu mimi hufai hata kuwa mlinzi wa mifugo yangu maana unaweza kuinyanyasa kwa kutokufikiri kwako”



    Jibu hilo lilimgazibisha na kumshangaza sana Lukoha kwani haikuwahi kutokea kwa yeye kudhalauriwa kiasi kile.



    “hata ukichukia au ukiamua kuniua hapa sitobadirisha kauli yangu, wewe ni sawa na mbwa unayefata matakwa ya bwana wako, akikupigia mbija na akikutaka uende popote pawe pa shali au pema wewe u radhi bila kufikili, ndoa inahusisha nyoyo mbili zilizojengwa katika misingi ya upendo na kuaminiana je huku ndoa ipo hivyo? Sanzani ina watu wa aina mbili wenye tabia tofauti tofauti. Utofauti watabia zao hatuwezi kusema wao wanajinsia nyingine tofauti na ya kiume au ya kike. Hivyo kwa mtu mmoja kuoa watu wengi Zaidi ni unyanyasaji ni wapi nilipopewa nafasi ya kuelezea hisia zangu….Leo nalaumiwa kwa kifo cha chifu Sanzani hii imejaa udhalimu na ubatili mtupu napachukia mno” alisema Mwenda huku machozi yakimtoka.



    Maneno yale yalipenya vyema mtimani mwa Lukoha, akajkuta akimpisha njia binti yule na kuinamisha kichwa chake,



    “Wewe ni msichana wa tofauti mno umefungua masikio yangu nenda katafute furaha yako ilipo” alisema Lukoha.

    Mwenda akafurahi kusikia kauli ile, akageuka na kuanza kuondoka lakini kabla hajafika mbali akasimama na kugeuka. Akakuta bado lukoha akimtazama. Mwenda akarudi kwa kasi alipo Lukoha na kumkumbatia,



    “Umekuwa wa mwanaume wa kwanza kunielewa toka nilipokanyaga ardhi hii ya Sanzani, siwezi kuondoka ingali mwili wa chifu upo ndani nitasubili hadi maziko yatakapokamilika” alisema Mwenda





    Lukoha akafurahi na kurejea tena ndani akiongozana na Mwenda, hakuna aliyeongea tena maana wote simanzi iliwatawala.



    *********************

    Taratibu za mazishi ya Chifu zikakamilika kisha wananchi wote wa Sanzani wakashiriki katika kumsindikiza chifu kwenye nyumba yake ya milele. Wiki moja baadae balaza la wazee na washauri likakaa na kuamua kumteua mtoto wa kwanza wa chifu arithi kiti cha baba yake. Tarumbeta iliyoambatana na ngoma ikapigwa na wananchi wote wa sanzani wakakusanyika katika uwanja ambao wamezoea kukutana. Mzee mmoja akasimama na wananchi wote wakainamisha vichwa vyao kutoa heshima kisha mzee yule akasema,



    “Ndugu zangu wa Sanzani wote twajua kuwa chifu Lukemo hatunaye tena, hivyo basi sisi kama wazee, washauri na viongozi wa ibada tulifanya maombi kwa mizimu yetu juu ya kumpata mtu atayerithi kiti cha chifu Lukemo, na leo tunamtangaza Ng’arika kama chifu wetu mpya”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Watu wote wakashangalia kwa nderemo na vifijo, hakuna aliyeweka pingamizi juu la hilo maana wote walikuwa na Imani kubwa kwa Ng’arika. Chifu Ng’arika ameshahabiana na marehemu baba yake kwa kiasi kikubwa, umbo na hata matendo huwezi kuwatofautisha. Ng’arika alikuwa ni mrefu na mwenye mwili mkubwa uliojengeka vizuri kutokana na kazi ngumu alizokuwa akizifanya.

    “Kwa swala la mke wa 14 wa chifu Lukemo ambaye ni Mwenda huyu atarithiwa na kuwa mke wa Majariwa ambaye ni mdogo wa mwisho wa chifu Lukemo”

    Kauli ile ikamshtua Zaidi Lucy ambaye alifikiri kuwa ameepuka msalaba wa kuwa katika ndoa hasiyoipenda. Watu wote wakashangilia kwa mara nyingine na kumuona Mwenda kuwa ni msichana mwenye bahati, Mwenda akawaangalia wananchi wale akaiona furaha iliyo kwenye nyuso zao. Kwake yeye ilikuwa ni kama msiba, hakutamani hata kidogo jambo lile litokee.



    “Kwa wakati huu ataendelea kuwa chini ya Ulinzi wa Lukoha hadi pale mume wake atakapokuja kumchukua na kuelekea naye TUNGI ulipo utawala mdogo wa Majariwa” aliendelea kusema mzee huyo.

    Msafara wa majariwa kuelekea Sanzani ulikumbwa na kashikashi toka kwa wajerumani na kufanya achelewe mazishi ya kaka yake. Tofauti na taharifa ya Tanzia hakujua lingine lolote lililoamriwa huko aendako.



    ************

    Siku moja Mwenda akahitaji kutoka katika milki ya chifu Lukemo na kwenda kumsabahi mama yake, Lukoha akawa na jukumu la kumsindikiza ili kuhakikisha usalama wa malkia huyo. Njiani kila mmoja alikuwa kimya huku Mwenda akionekana kufurahia Zaidi mazingira yaliyomo njiani.

    “Katika dunia yetu ni aghalabu sana kukutana na mazingira haya” alisema Mwenda.

    “Unamaana gani?”

    “Nazungumzia dunia ijayo, kila kitu hakipo kama ilivyo sasa isipokuwa kwa sehemu chache tu”

    “Bado sielewi nini unachozungumza” alisema Lukoha.

    “Dunia ile hatuitaji kutembea kwa farasi au punda kwenda umbali mrefi isipokuwa kuna magari, pikipiki, ndege na meli kwa safari za maji”

    “Mhmh! Malkia!” aliita Lukoha kwa mshangao.

    “Mimi siitwi Mwenda kama wewe unavyodhani mimi ni mtu niliyetoka dunia ijayo na kuletwa huku”

    “Mhmh! Mwenda bila shaka umepitia mambo mengi sana na nilifikiri akili yako imepona kumbe bado” alisema Lukoha.

    “Nimesikia msafara wa chifu Majariwa umekwama kutokana na kushambuliwa na wajerumani ila miaka sio mingi sana utawala huu utakufa na utakuja utawala mwingine japo bado utakuwa hautupi uhuru maana wote ni wakoloni” alisema Mwenda.



    Lukoha akamtazama binti huyo na kumsikiliza kwa makini mno, wakati akimsikiliza ghafla akasikia muungurumo wa simba, bila kukaa vizuri akaona mnyama huyo akija kwa kasi upande wao. Mwenda aliogopa mno, akakosa nguvu ya kujitetea hakuelewa akimbie au apambane, Lukoha akamsogelea na kumvuta pembeni kwa bahati mbaya wote wawili wakateleza na kuanguka kwenye mteremko mkali uliowapeleka moja kwa moja kwenye mto. Lukoha hakumwachia mkono Mwenda alijitahidi kumkinga walipokutana na mawe au matawi ya miti, tukio lile lilikuwa la kipekee sana kwa Mwenda akakumbuka siku ambayo mume wake alimtaka afunge mkanda vizuri akakumbuka ajali ile iliyowakuta ambayo iligharimu maisha ya mumewe na yeye kuwa salama.



    “Vipi malkia uko salama”

    “Ndiyo niko sawa shukrani kwako”

    “Usijali malkia ni wajibu wangu”

    Mwenda akamtazama vizuri Lukoha na kugundua kuwa alikuwa na majeraha kadhaa kwenye mwili wake,

    “Naona hali yako si shwari ngoja nitafute namna ya kuyatibu majeraha yako”

    “Wala usijiangaishe malkia ni majeraha madogo haya alafu ni hatari kwa wewe kuzunguka peke yako, tupumzike kidogo naamini nitakuwa sawa” alisema Lukoha.



    Ukweli Lukoha aliumia sana ila hakutaka kuliweka wazi hilo mbele ya Malkia huyo sababu ni wajibu wake kutoa ulinzi. Kadri muda ulivyozidi kwenda ndivyo hali ya lukoha ilizidi kuwa mbaya alishikwa na homa kali mno. Mwenda akajaribu kila namna aliyoweza akashindwa kumsaidia, ikabidi aukague vizuri mwili wa Lukoha ili agundue ni kipi hasa kilichokuwa kikimsibu. Akamkagua kuanzia utosini hadi unyayoni na alipoangalia vizuri kwenye kisigino akaona jeraha la tofauti kidogo, alipolichunguza Zaidi akagundua kuwa Lukoha aliumwa na nyoka bila yeye kuelewa. Sumu ya nyoka ilikuwa kali mno kwani ndani ya muda mfupi ngozi ya Lukoha ikabadilika toka rangi ya maji ya kunde na kuwa nyeusi. Mwenda alichanganyikiwa Zaidi kwani hakuwa na utaalamu wa dawa za miti shamba,



    “Malkia wangu wakati wangu wa kuungana na chifu Lukemo umewadia hata hivyo nina furaha ya kuwa na wewe katika dakika hizi za mwisho”

    “Hapana Lukoha huwezi kufa na kuniacha mimi, kumbuka uliweka ahadi ya kunilinda tafadhali Lukoha….”



    Kabla Mwenda hajamalizia kauli yake Lukoha akakohoa na kutoa povu jeupe kisha papo hapo akaanguka chini na kupoteza fahamu. Kwa haraka mwenda akatafuta kitu chenye ncha kali na kumchanja Lukoha sehemu aliyeng’atwa na nyoka. Akatumia kinywa chake kunyonya sumu iliyosambaa katika mwili wa Lukoha ili aone kama itaweza kusaidia, alifanya hivyo kwa Zaidi ya dakika 5 bila kuona badiriko lolote katika mwili wa Lukoha. Akasogea hadi kifuani na kusikiliza mapigo ya moyo, kwa bahati aliyasikia kwa mbali sana, ikabidi atumie viganja vyake vya mikono kushtua moyo wa Lukoha. Alifanya hivyo mara kadhaa huku akiendelea kuyasikiliza lakini hakufanikiwa Zaidi ya kuzidi kupungua.



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwenda alijikuta akitoa machozi hasielewe afanye nini Zaidi kunusuru maisha ya Lukoha, akakaa pembeni kidogo huku akimuomba Mungu amuepushe na balaa lile. Muda mfupi baadaye akamuona Lukoha akiweweseka akamsogelea na kupima mapigo yake ya moyo na kukuta yamerejea katika hali ya kawaida, akamshukuru Mungu kwa hilo na akaendelea kusubili hadi giza lilipoanza kuchukua nafasi ya jua, Lukoha akawa bado hajarejewa na fahamu. Mwenda akaona ni hatari Zaidi kama wataendelea kukaa eneo hilo kwa usiku huo, akamuacha Lukoha na kwenda kutafuta mahali penye usalama kidogo. Katika kuzunguka kwake akaona pango ambalo lilionekana kutumika kwa kila baada ya kipindi flani, akaona sehemu hiyo ni sahihi kwa wao kupumzika. Akarejea alipo Lukoha na kukuta bado fahamu hazijarejea, akamkokota hadi kwenye pango, akatafuta kuni na kuzipanga kisha akapekecha vijiti ili kuwasha moto utakaowasaidia kuwapatia joto na kufukuza wanyama au wadudu hatari. Akaendelea kuwa karibu na Lukoha ila kutokana na uchovu wa siku hiyo akajikuta akipitiwa na usingizi. Lukoha akafumbua macho yake na kujikuta yupo katika mazingira mapya alipotazama pembeni akamwona Mwenda akiwa amelala, mwili wake ulikuwa mzito mno akajitazama sehemu alizopata majeraha akakuta amesafishwa vizuri na kupakwa dawa akamtazama mwenda kwa tabasamu zito.



    “Sitoisahau siku hii ya leo umekuwa msaada mkubwa katika kuyanusuru maisha yangu” alisema Lukoha japo Mwenda hakuweza kumsikia kutokana na kupitiwa na usingizi mzito.

    Lukoha akajaribu kusimama ili kuangalia vizuri mazingira waliyopo lakini akashindwa na kujikuta akianguka chini kwa kishindo kilichomshtua Mwenda.

    “Usijiangaishe bado hauna nguvu ya kutosha” alisema Mwenda.

    Lukoha akajikongoja na kukaa vizuri huku akimtazama mwenda aliyejaa na wasiwasi mkubwa juu ya hali aliyekuwa nayo.

    “Nafikiri itatulazimu kubaki hapa kwa siku saba Zaidi hili uweze kurejea katika hali yako ya kawaida, japo tutakumbana na changamoto ya chakula ila nitajitahidi kuzunguka nione kama kuna watu jirani ambao wanaweza kutupatia msaada wa chakula ikishindikana tutatumia hata matunda ya mwituni” alisema Mwenda.

    “Ningepata nafasi ya kutoa taharifa kwa chifu naamini wangekuja kutupatia msaada” alisema Lukoha.

    “Nitatafuta pia njia ya kufanya hivyo wewe pumzika tuu” aliendelea kusema Mwenda.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog