Simulizi : Nisamehe Latifa
Sehemu Ya Tatu (3)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Huo ulikuwa mwanzo wa ukaribu wao, wawili hao, Latifa na Liban walikuwa pamoja kila sehemu walipokuwa. Walisoma darasa moja huku kila walipokuwa wakiingia darasani, walikaa karibukaribu hali iliyoyafanya wanaume wote kugundua kwamba wawili hao walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Hiyo haikuwa kazi nyepesi kwa Liban, ni kweli alimpenda mno Latifa lakini kila alipoingizia suala la uhusiano wa kimapenzi, Latifa hakutaka kukubaliana naye, bado maumivu ya Ibrahim yaliendelea kukumbushwa moyoni mwake.
Siku ziliendelea kukatika, Liban hakutaka kusikia wala kuelewa, kila alipoambiwa sitaki, hakukata tamaa, aliendelea kumwambia zaidi mpaka Latifa akachoka na mwisho wa siku, bila kulazimishwa, akajikuta akianzakubusiana na kijana huyo na hatimaye midomo yao kugusana, kilichofuata ni kubadilishana mate tu.
“Ninakupenda Latifa,” alisema Liban, alimkazia macho msichana huyo, hisia kali za kimapenzi zilionekana machoni mwake.
“Ninakupenda pia, lakini.....”
“Lakini nini?”
“Naomba usiniumize,” alisema Latifa kwa sauti ya chini.
“Siwezi kufanya hivyo, siwezi kukufanya kama huyo mpumbavu,” alisema Liban huku akiachia tabasamu pana.
Liban akawa mtu mwenye bahati mno, wanaume wengi chuoni hapo UCLA walijaribu kumfuatilia Latifa lakini mwisho wa siku walikataliwa katakata, kitendo cha Liban kumchukua kulikuwa na wanaume wengi walioumia.
Latifa hakutaka kuliacha penzi la Liban, kwa kipindi kichache alichokuwa naye alimfanya kujisikia amani moyoni mwake, ile furaha ya mapenzi ambayo watu wengi walikuwa wakiizungumzia, ikaanza kuingia moyoni mwake.
Siku zikaendelea kukatika, mpaka mwaka huo unakatika na mwaka mwingine kuingia, wawili hao waliendelea kuwa pamoja huku kila mmoja akimpa mwenzake ahadi ya kuoana na kuishi pamoja.
Mwaka wa pili ulipomalizika, wakati wa likizo ndipo Liban akamwambia Latifa kwamba angependa aende naye nchini India kwa ajili ya kuwaona wazazi wake na hatimaye waweze kufunga ndoa kwani umri ulikuwa unaruhusu.
Latifa hakuamini, hakumkatalia Liban, walikuwa wamebakiza mwaka mmoja tu wamalize chuo hivyo hiyo ikaonekana kuwa nafasi yake kujiandaa kwa ajili ya ndoa, baada ya wiki moja, wakapanda ndani ya ndege na kuelekea India.
Safari kutoka nchini Marekani mpaka India ilichukua masaa ishirini na saba ndipo ndege ilipoanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Indira Gandhi uliokuwa katika Jiji la New Delhi. Ndege iliposimama, abiria wakaanza kuteremka na kuelekea nje ya uwanja huo na kwenda kuchukua mizigo yao.
“Uliwaambia wazazi wako kuhusu mimi?” aliuliza Latifa huku uso wake ukitawaliwa na tabasamu pana.
“Hapana, ila niliwaahidi kwamba nitawafanyia sapraizi.”
“Mmmh!”
“Usiogope kipenzi, wewetwende tu, watafurahi sana mana’ke walinisisitiza sana kuhusu kuoa,” alisema Liban huku akionekana kuwa na furaha tele.
Walipofika nje ya uwanja huo, wakachukua teksi na kuanza kuelekea katika Mtaa wa Aurangzeb uliokuwa hapo New Delhi, mtaa uliokaliwa na matajiri wakiwepo waigizaji kama Aksey Kumar na Sunil Shetty.
Kutokana na wingi wa magari na Bajaj barabarani, walichukua nusu saa mpaka kufika katika mtaa huo. Teksi ikaelekea mpaka kwenye nyumba moja ya kifahari na kuanza kupiga honi, geti likafunguliwa na gari kuingizwa.
Wasichana wawili waliokuwa ndugu zake Liban wakalikimbilia gari hilo kwani walikuwa na taarifa kwamba kaka yao angefika nyumbani hapo siku hiyo.
Nyuso zao zilikuwa na tabasamu pana, hawakuamini kama kaka yao angefika siku ile nyumbani pale kutokea nchini Marekani alipokuwa akisoma. Walishindwa kuzizuia furaha zao, walipomuona akiteremka kutoka garini, wakamsogelea na kumkumbatia kwa furaha.
Hapohapo, mlango wa upande wa pili ukafunguliwa na Latifa kuteremka, hawakuonekana kushtuka kwa kuhisi kwamba yule hakuwa mgeni wao kwani teksi ile ilikuwa imekodiwa na Wahindi walikuwa na tabia ya kukodisha teksi moja zaidi ya watu watatu kutokana na idadi kubwa ya watu.
Wakamwangalia Latifa huku tabasamu yakiendelea kuwepo nyusoni mwao. Liban akaona kwamba hiyo ndiyo ilikuwa nafasi pekee ya kumtambulisha Latifa hata kabla hawajaingia ndani.
“Is she with you?” (Yupo pamoja nawe?) aliuliza dada mmoja.
“Yeah! She is my fiancee,” (Ndiyo! Ni mchumba wangu) alisema Liban huku akiwa na tabasamu pana.
“What do you say?” (Unasemaje?) aliuliza dada mmoja huku akijifanya kutokusikia kile kilichokuwa kimesemwa na Liban. Hivyo akarudia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapohapo, tabasamu yakatoka nyusoni mwao, wakaanza kumwangalia Latifa kwa macho ya chuki, hawakuvutiwa naye hata mara moja. Liban akaligundua hilo, alichokifanya ni kumsogelea Latifa na kumvutia kwake kwani hakutaka ajisikie vibaya juu ya kilichokuwa kikiendelea.
“She is slut..” (Ni mwanamke mchafu..) alisema dada mwingine.
Mpaka kufikia hapo, hakukuwa na kitu cha kuficha kwamba Latifa hakuwa akihitajika ndani ya familia hiyo. Maneno yale yalimchoma mno lakini hakutaka kuonekana kama alichomwa sana, hivyo akaanza kulilazimisha tabasamu usoni mwake.
Hata nguvu za kuchukua begi lake hakuwa nazo, ni Liban ndiye aliyelichukua na kuanza kuelekea ndani. Si dada wale tu waliokuwa wakimchukia Latifa bali kila alipoonekana na watu ndani ya nyumba ile, alikuwa akichukiwa mno, hakupendwa hata kidogo.
Hakupokea mapokezi yale aliyoambiwa kwamba angepewa, mapokezi yale yalikuwa ni ya tofauti sana na maneno ya Liban, akabaki akisononeka moyoni mwake huku akitamani kurudi nyuma na kuondoka.
“Liban. Huyu ni nani?” aliuliza mama yake Liban, alikuwa amemvuta mtoto wake pembeni, japokuwa aliamini kwamba alizungumza kisiri, lakini Latifa aliweza kuyasikia maneno yale.
“Ni mchumba wangu.”
“Hapana. Huyu si mchumba wako, toka lini umeona ndugu zako wakioa wanawake wenye mchanganyiko? Hawa ni wachafu. Haiwezekani, huwezi kuwa na mwanamke mchafu. Mimi kama mama yako, nakwambia simtaki huyu mwanamke, hii ni laana,” alisema mama yake Liban.
“Lakini mama...”
“Nimesema simtaki...” mama Liban alisema kwa sauti kubwa kabisa.
Liban hakuwa na nguvu, alimheshimu sana mama yake na alimuahidi kwamba isingeweza kutokea hata siku moja akamvunjia heshima yake. Kitendo cha kuambiwa kwamba hakuwa akimtaka Latifa kuingia katika familia yao, kilimuuma sana.
Alichokifanya ni kuwapigia simu ndugu zake wengine ili waje wamwambie mama kwamba Latifa alikuwa ni chaguo lake. Kitu cha ajabu, kila ndugu aliyefika mahali pale na kumuona Latifa, hakumtaka, hawakutaka kumuona kabisa Latifa.
“Ni mwanamke mchafu, unatuletea laana kwenye ukoo,” alisema mjomba wake ambaye alimuamini kwamba alikuwa pamoja naye kwa kila kitu.
Ilikuwa ni afadhali kupigwa na risasi au kuchomwa moto, maumivu aliyoyasikia Latifa yalikuwa makubwa mno. Akajikuta akilengwa na machozi na hatimaye kuanza kububujika mashavuni mwake.
Alitamani kupotea ghafla kama mchawi na hatimaye kuibukia Tanzania, hilo halikuwezekana, kila ndugu aliyefika mahali pale, hakumtaka Latifa, sababu kubwa ikiwa ni mchanganyiko wa rangi, aina ya watu ambao walitengwa mno nchini India.
“Kwa nini mimi Mungu?” alijiuliza Latifa huku akianza kulia kama mtoto.
Latifa alitia huruma, kila muda Liban alipokuwa akimwangalia, alitamani kulia, hakukuwa na siku ambayo alimuonea huruma mtu kama siku hiyo. Moyo wake ulimpenda mno msichana huyo, kwake, alikuwa kama pumzi, alikuwa tegemeo kubwa mpaka kumpa ahadi kwamba angemuona na kuwa mama wa watoto wake, lakini mwisho wa siku, ndugu, na watu wengine wa karibu hawakumtaka msichana huyo.
Alitamani kubadilisha matokeo, ndugu zake wakubaliana naye na kuondokana na dhana potofu kwamba Latifa alikuwa na laana kutokana na mchanganyiko wake wa rangi. Ndugu wale hawakutaka kunyamaza, bado waliendelea kulalamika kwamba Liban hakutakiwa kuwa na mwanamke kama Latifa.
Latifa hakutaka kuendelea kubaki nyumbani hapo, alichokifanya ni kusimama, akachukua mabegi yake na kuondoka nyumbani hapo. Kitu kibaya ambacho kilimshangaza sana ni kwamba Liban hakuweza kumfuata, yaani ni kama mwanaume huyo alikubaliana na wazazi wake.
“Ninawachukia watu wa nchi hii,” alisema Latifa huku akilia kama mtoto.
Alitembea barabarani huku kichwa chake kikiwa chini, machozi yalikuwa yakimbubujika, kadiri alivyojitahidi kuyafuta, hayakukata, yaliendelea kutoka zaidi na zaidi. Safari yake hiyo ikaishia mbele ya hoteli kubwa ya Mumbai, hapo ndipo alipoamua kuchukua chumba, hakutaka kukaa sana, akapanga kuondoka kurudi Tanzania siku inayofuata.
****
Mapenzi yalikuwa motomoto, Ibrahim na Nusrat walijiona kuwa miongoni mwa wapenzi waliokuwa wakipendana kwa dhati kuliko watu wowote wale katika dunia hii. Muda wote walikuwa pamoja, walitaniana na kubusiana kila walipokuwa.
Kila mmoja kichwa chake kilifikiria ndoa tu, walipita vizingiti vingi vya wazazi, ndugu, jamaa na marafiki na mwisho wa siku, wote hao walikubaliana waache na hatimaye waweze kufunga ndoa na kuishi pamoja.
Kwa Ibrahim, furaha iliongezeka zaidi, kila alipokuwa akikaa, alimfikiria msichana huyo ambaye kwake alionekana kuwa kila kitu. Baada ya siku kadhaa kupita, Ibrahim akajikuta akianza kuwa karibu na mwanaume mmoja, alionekana kuwa mzee wa makamo, alikuwa na ndevu nyingi zilizokuwa na mvi, alionekana kuchoka hali iliyoonyesha kwamba maisha yalimpiga sana.
Alikutana na mzee huyu wakati akielekea Posta kwa ajili ya kukamilisha michoro yake ambayo alitakiwa kumkabidhi Balozi wa Uingereza kama zawadi pekee kutoka kwa Watanzania kabla ya kuelekea nchini mwake.
Alipokutana na mzee huyo aliyekuwa ombaomba barabarani, akajikuta akifunga breki na kuteremka. Hakujua sababu iliyomfanya kuwa na huruma kiasi hicho, alionekana kuvutiwa na mzee yule, akaufungua mlango na kuanza kumfuata.
“Naomba unisaidie hela ya kula,” alizungumza mzee yule, mavazi yake yalikuwa yamechakaa sana.
“Chukua hii,” alisema Ibrahim huku akimkabidhi mzee yule noti ya shilingi elfu kumi.
Hakutaka kukaa sana, ndani ya gari, alikosa amani, kila wakati alikuwa akimfikiria mzee yule ambaye kwake alionekana kuwa na uhitaji mkubwa. Hakutaka kuficha hisia zake, akampigia simu Nurat na kumwambia kuhusu mzee huyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni vizuri kusaidia watu wasiojiweza,” alisema Nusrat.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki baina ya mzee masikini, ombaomba na Ibrahim. Mara kwa mara alikuwa akimfuata na kuzungumza naye mambo mengi ambayo kwa Ibrahim, yalimsisimua sana.
“Kwa hiyo ikawaje mpaka ukawa ombaomba?” aliuliza Ibrahim, alitegesha masikio yake kumsikiliza mzee yule ambaye pasipo kutegemea, akaanza kububujikwa na machozi, swali aliloulizwa, likazifanya kumbukumbu zake kurudi nyuma, akaanza kulia.
“Duniani kuna watu wabaya sana, duniani hapa, kuna watu wenye roho mbaya sana,” alisema mzee yule masikini.
“Kwa nini?”
“Nimepitia maisha magumu sana, sina kitu, nimepoteza kila kitu maishani mwangu,” alisema mzee yule.
Sauti yake ilikuwa ya chini sana, alizungumza huku akionekana kuwa na maumivu makubwa ya moyo. Kila alipoongea kidogo, alinyamaza, akameza fundo la mate na kuendelea.
Mzee huyo alimuhadithia Ibrahim mambo mengi huku akimbariki kwa kila kitu atakachokifanya katika maisha yake ya mbele. Ibrahim aliporidhika, akamuaga mzee yule tayari kwa kuondoka. Akajikuta akishikwa mkono, akageuka na kumwangalia mzee yule.
“Katika kila ukifanyacho, kumbuka kitu kimoja,” alisema mzee yule, alikuwa amemkazia macho Ibrahim.
“Kitu gani?”
“Usimfanye mwanamke akalia.”
“Nisimfanye mwanamke akalia?”
“Ndiyo! Kila chozi la mwanamke linalodondoka, huwa na laana nzito sana,” alisema mzee huyo.
“Kivipi?”
“Nipo hapa kwa sababu ya chozi la mwanamke, nipo hapa kwa kuwa nilimfanya mwanamke kulia. Hakika ningejua kama haya yangetokea, hakika ningemfanya kuwa na furaha milele, nisingeruhusu kuliona chozi lake,” alisema mzee yule, akanyamaza, akakiinamisha kichwa chake chini, akaanza kulia tena.
“Nyamaza sana mzee. Lakini kwa nini unaniambia hivi?”
“Ni kwa sababu wewe ni rafiki yangu, sipendi upate majanga kama niliyoyapata mimi, ninatamani uje kuwa na furaha kubwa maishani mwako,” alisema mzee yule.
“Maneno yako yananitisha.”
“Si kwamba nakutisha, ila ninakwambia njia za kufanikiwa, njia za kuiepuka laana maishani mwako,” alisema mzee yule.
“Usijali mzee, nitakuwa nikija mara kwa mara,” alisema Ibrahim na kuondoka. Moyoni mwake hakuweza kukumbuka chochote kuhusu Latifa japokuwa maneno yale yaliutesa sana moyo wake.
****
Usiku hakulala, muda wote macho yake yalikuwa wazi huku akiangalia juu tu. Kichwa chake kilikuwa na mawazo lukuki, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea nyumbani kwa mpenzi wake mara baada ya kwenda kutambulishwa.
Mpaka asubuhi inaingia, Latifa hakuwa amepata hata lepe la usingizi, usiku mzima alikuwa na mawazo tu. Hakutaka kuendelea kukaa nchini India, akajiandaa, akawasiliana na ofisi za kampuni ya ndege ya Indian Airlines na kuhitaji kuwekewa tiketi moja ya kwenda nchini Tanzania, hilo halikuwa tatizo.
“Kwa nini nina mkosi hivi? Kwa nini yote haya yananitokea mimi tu?” alijiuliza lakini hakupata jibu, bado alijiona kuwa na mkosi mkubwa maishani mwake.
Ilipofika saa kumi jioni, tena huku akiwa hajaingiza kitu chochote mdomoni, akaondoka hotelini hapo kuelekea uwanja wa ndege na ilipofika saa kumi na mbili jioni, akapanda ndege na kuanza kuelekea nchini Tanzania huku akiwa na majonzi makubwa moyoni mwake.
Kama kulia alilia sana lakini hakubadilisha kitu, kila kitu kilichokuwa kimetokea, kilitokea na hivyo alitakiwa kusahau kila kitu. Alipofika jijini Dar es Salaam, Latifa akapokelewa kwa shangwe kwa kuwa alifanikiwa sana katika elimu yake.
Alikuwa msichana mwenye uwezo mkubwa mno, alijijengea heshima kubwa chuoni kutokana na uwezo wake kuwa mkubwa, kila mtu akajivunia kuwa na mtu kama yeye hasa katika familia ya bi Rachel.
Siku zikaendelea kwenda mbele mpaka pale alipotakiwa kurudi tena chuoni nchini Marekani, akarudi zake. Chuoni huko, hakukutana tena na Liban, mwanaume huyo alikuwa amehama chuo na kuelekea katika Chuo cha Mumbai nchini India, hakurudi tena nchini Marekani.
Uzuri wa Latifa ukaendelea kuwa gumzo, hakujua ni nani aliwaambia watu kile kilichotokea, baada ya wiki kadhaa tu, kila mmoja alifahamu kilichoendelea nchini India na hivyo kumpa pole sana.
Hakutaka kujali tena, kila kitu kilichotokea maishani mwake alikichukulia kama changamoto. Japokuwa kwake ilikuwa ngumu kumsahau Liban lakini hakuwa na jinsi, baada ya miezi miwili tu, kumbukumbu juu ya Liban zikaanza kupotea kichwani mwake.
Uwezo wake wa darasani ulikuwa uleule, watu walimshangaa sana, darasani hakuwa mtu wa kawaida hata mara moja. Wanafunzi wengi walimfuata na kuanza kufundishwa naye, Latifa alikuwa tofauti huku wanachuo wengine wakisema kwamba msichana huyo alikuwa na uwezo mkubwa zaidi ya maprofesa chuoni hapo.
“Naomba kuuliza swali,” alisema Latifa, walikuwa darasani walipokuwa wakisoma.
“Uliza,” alisema profesa huku akiiweka vizuri miwani yake, kila mtu alimheshimu Latifa, hivyo kila alipoinuka na kutaka kuzungumza kitu, watu wote walikuwa kimya.
“Bila shaka mtu wa kwanza kutengeneza gari, alifikiria kuhusu gari tu na wala hakufikiria kwamba kuna mtu angekuja na kutengeneza ndege, si ndiyo?” aliuliza Latifa.
“Ndiyo!” alijibu profesa.
“Hivi kwa nini huyu mtu aliyekuja na kugundua ndege hakufikiria kutengeneza gari lenye miguu kumi badala ya minne?” aliuliza Latifa.
“Unamaanisha nini?”
“Nataka kufahamu tu.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mmmh! Sijui kwa nini hakufikiria hilo.”
“Sawa. Lakini, kama Alexander Bell aligundua simu ya mezani, kwa nini mtu aliyegundua simu ya mkononi asigegundua simu za aina nyingine zinazotumia waya?” aliuliza Latifa.
“Napo sijui.”
“Kuna chochote unachojifunza kutokana na maswali yangu?”
“Hapana. Unamaanisha nini?”
“Kama jopo la madaktari duniani walikaa kwa ajili ya kutafuta dawa za kuua kansa iliyokomaa, wakakosa, hivi hatuwezi kuwa kama mtu aliyegundua ndege na simu za mkononi? Yaani namaanisha kwa kwenda mbele na kufikiria kitu kingine zaidi?” aliuliza Latifa.
“Unamaanisha nini?”
“Najua umeshajua ninachokimaanisha. Ninataka kutengeneza dawa za kuteketeza kansa katika dunia hii,” alisema Latifa kwa kujiamini.
“Unasemaje?” aliuliza profesa huku akiishusha miwani yake na kumwangalia vizuri Latifa.
“Ninataka kutengeneza dawa ya kansa, hiyo dawa itaitwa Morphimousis, nikwambie kitu profesa? Itakwenda kuokoa maisha ya watu wengi, niamini. Hii ndiyo nafasi ya kuwa bilionea ili yule Ibrahim na Liban wanitafute,” alisema Latifa, ghafla machozi yakaanza kumbubujika.
Huo ndiyo ulikuwa uamuzi aliokuwa ameuchukua, alikuwa akisomea masomo ya udaktari hivyo lengo lake kubwa kwa wakati huo lilikuwa ni kuwa daktari mkubwa ambaye angeweka historia katika dunia hii kwa kuweza kukumbukwa katika maisha yake yote, kabla na baada ya kifo.
Darasani alikuwa na akili mno, hakuwa msomaji sana lakini kila ulipokuwa ukija mtihani, kama kawaidayake alikuwa akiongoza kama kawaida yake. Latifa aliendelea kunawili kila siku lakini kwa kipindi hicho, hakutaka kuwa na mwanaume yeyote yule, alitaka kubaki peke yake mpaka atakapokufa.
Siku zilikatika, hapo ndipo alipoamua kuanza kusoma kwa juhudi hata kama alikuwa genius, alitaka kujifunza mambo mengi kuhusu mwili wa binadamu, ni kwa namna gani ulikuwa ukishambuliwa na magonjwa ya kansa na kwa namna gani angeweza kuyadhibiti magonjwa hayo.
Hilo likamfanya kushinda maabara kila siku, likamfanya kutafuta dawa nyingine ambazo alikwenda nazo humo kisha kuanza kuangalia ni kwa jinsi gani angeweza kutengeneza dawa moja ambayo ingekuwa yenye ubora mkubwa sana.
“Dawa zinapatikana kwenye miti, huko ndipo kwenyewe,” alisema Dk. Warren, alikuwa dokta mwenye uwezo mkubwa aliyeweka historia kwa kutengeneza dawa za magonjwa ya mifupa.
“Naweza nikapata wapi hiyo miti?”
“Nenda Amazon.”
“Unamaanisha msitu wa Brazil?”
“Ndiyo!”
Aliamua kwa moyo mmoja kufanya kile alichotaka kukifanya, kwenda nchini Brazil halikuwa tatizo, akajipanga na kisha kuelekea huko. Msitu ulikuwa unatisha sana lakini hakuwa na jinsi, alitakiwa kuingia na kuutafuta mti mmoja ulioitwa Mendozo, mti pekee uliokuwa na uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali, mti pekee ambao magome yake yalitumika kuwatibu Wabrazil.
Alipofika huko, tena huku akiwa na watu watano wenye silaha kali wakaanza kuzunguka msituni kwa malipo makubwa. Ilikuwa kazi kubwa, ya hatari na yenye kuchosha lakini hakutaka kukata tamaa, mbele yake aliyaona mafanikio makubwa, hivyo alitaka kupambana zaidi mpaka anaupata huo mti.
Walizunguka kwa kupumzika kwa kipindi cha wiki nzima na ndipo walipofanikiwa kuupata mti huo, wakachukua magome na kisha kurudi Rio De Janeiro huku kila mmoja akiwa na furaha.
Alipofika hotelini tu, kitu cha kwanza ni kuchukua magome yale na kuanza kuyafanyia kazi, alitaka kujua ni vitu gani vilikuwepo ndani ya miti ile ili mwisho wa siku na yeye aweze kuvitengeneza vitu hivyo au vinavuofanana na hivyo na mwisho wa siku kutengeneza dawa kali na yenye nguvu. Akafanikiwa katika hilo na kurudi nchini Marekani huku akiwa na sample.
“Nakwenda kuwa bilionea,” alisema Latifa, mwili ulichoka sana, alikuwa safarini kurudi nchini Marekani. Moyo wake ukafarijika mno.
Uhusiano wa kimapenzi uliwapa furaha kila mmoja, mipango yao ya ndoa iliendelea kupangwa na siku ya harusi ikawekwa tayari kwa ajili ya harusi hiyo ambayo ilionekana kufana hata kabla ya kufika.
Kila mmoja akawa na kimuemue cha kutaka kuoana, wageni wakaitwa kutoka Uarabuni tayari kwa kuhudhuria harusi hiyo kati ya Nusrat na Ibrahim. Hakukuwa na tatizo lolote lile, kila mmoja, hasa ndugu wa Nusrat walimpenda sana Ibrahim kwani ndiye alikuwa mtu pekee aliyechaguliwa na ndugu yao.
Baada ya wiki moja, hatimaye Ibrahim alivalia kanzu kubwa na kwenda ukweni kuoa. Huko, akajipatia mke wake na hatimaye maisha ya furaha kama mke na mume kuanza. Hakukuwa na mtu aliyefikiria jambo lolote lile baya, kila mmoja aliona kwamba ndoa kuwa furaha tupu pasipo kujua kwamba wakati mwingine, wanandoa hujuta sababu ya kuwafanya kuoa au kuolewa.Hawakujua hilo.
*****
Latifa akawa mtu wa kushinda maabara tu kwa ajili ya kuifanyia kazi dawa yake. Ilikuwa ni kazi kubwa lakini hakutaka kushindwa, kadiri alivyokuwa akiwafikiria wanaume walioutesa moyo wake na kumfanya kulia, hakutaka kukata tamaa kwa kuamini kwamba ni lazima angefanikiwa tu.
Siku ziliendelea kukatika, ndoto yake kubwa kwa wakati huo ilikuwa ni kuwa bilionea mkubwa baada ya kuuza dawa ya magonjwa ya kansa yaliyowatesa watu wengi duniani, hasa Wamarekani na watu wa Ulaya nzima.
Hakutaka kurudi nchini Tanzania, alikuwa bize akitengeneza dawa hiyo kwa kutumia vifaa maalumu. Wakati mwingine hakula chakula chochote kile, alishindakuanzia asubuhi mpaka usiku pasipo kuingiza chochote tumboni mwake, si kwamba hakusikia njaa, alisikia njaa lakini hakutaka kula mpaka ile hatua ambayo alitamani kuifikia kwa siku husika aifikie.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Vitabu vilimsaidia, alitumia muda wa miezi mitatu na ndipo alipoanza kuona mafanikio ya ile kazi aliyoanza nayo kwa kipindi kirefu, dawa ikaanza kukamilika kitu kilichompa furaha mno kwa kuona sasa alikuwa njiani kutimiza ndoto yake.
Hakutaka kufanya siri, alichokifanya ni kumpigia simu Dk. Dickson Myles kwa ajili ya kufika hapo maabara na kumuonyeshea kile alichokuwa amekitengeneza.
“Unaionaje?” aliuliza Latifa, usoni alikuwa na tabasamu pana.
“Ipo vizuri, umefanyaje mpaka ukapata hii dawa?” aliuliza Dk. Myles huku akionekana kushangaa.
“Ni kazi kubwa na ngumu iliyohitaji mtu ujitoe sana, usijali. Nahitaji unifanyie mipango ili niweze kukamilisha kila kitu,” alisema Latifa.
Hakutaka kumwamini mtu yeyote yule, alitumia muda mwingi sana kutengeneza dawa ile na aliona kama angemwambia mtu yeyote yule namna alivyotengeneza dawa ile basi watu wangeweza kuiga na hivyo kutengeneza haraka na kuisambaza hata kabla hajaisambaza yeye. Hakutaka kuona hilo hivyo alifanya kila kitu kuwa siri kubwa.
Baada ya siku tatu, Dk. Myles akafika na Waziri wa Afya nchini Marekani, Bwana Brian Peterson kwa ajili ya kuiona dawa hiyo. Latifa hakuwa na jinsi, aliamini kwamba huo ndiyo ungekuwa mwanzo wake hivyo akamuonyeshea.
Haikuwa dawa ya vidonge, ilikuwa ni ya kimiminika ambayo ilitakiwa kuhifadhiwa kwenye chupa na mgonjwa alitakiwa kunywa na baada ya mwezi mmoja angepona kabisa na kuwa mzima.
Kilichofanyika ni kumpigia simu dokta mkuu wa Hospitali kubwa ya St. Augustino Medical Center ambaye alifika mahali hapo na kuanza kuiangalia. Alikubaliana nayo kwa asilimia kadhaa na hivyo ilitakiwa kufanyiwa marekebisho hata kabla ya kupitishwa na kuanza kutumika.
Kulikuwa na watu wengi mno nchini Marekani waliokuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya kansa hivyo hata tangazo lilipotolewa kwamba kulihitajika wagonjwa wawili waliosumbuliwa na kansa kwa ajili ya kufanyiwa matibabu, walipatikana kwa haraka sana tena huku wengine wakipanga mstari hospitalini kuhitaji matibabu.
Matibabu yakaanza na hatimaye wagonjwa hao kuruhusiwa kuondoka. Latifa alibaki kimya, kipindi cha mwezi mzima ambacho alitakiwa kusubiri alikuwa na presha tele, alikuwa akimuomba Mungu ili dawa ile ifanye kazi kama ilivyotakiwa na hatimaye aweze kuwa bilionea kwa ajili ya kuiuza dawa hiyo ambayo mpaka katika kipindi hicho alikuwa amekwishaisajili.
Siku zilikatika na hatimaye mwezi kumalizika. Wagonjwa wale waliofanyiwa majaribio wakapigiwa simu na kutakiwa kufika katika hospitali hiyo haraka iwezekanavyo. Wala hawakuchukua masaa mengi, wakafika na hivyo kufanyiwa tena vipimo.
Majibu yalipokamilika, jopo la madaktari sitini wakaitwa kwa ajili ya kuipitia ripoti hiyo ya majibu ya wagonjwa wale. Walikaa katika chumba kile kwa dakika kadhaa, ripoti ilipokamilika ikaletwa na kukabidhiwa Dk. Peterson, akashusha miwani yake na kuiangalia vizuri.
“It is impossible!” (Haiwezekani!) alisema Dk. Peterson kwa mshtuko huku akiangalia majibu ya vipimo.
“What do you see?” (Unaona nini?)
Hakujibu swali hilo, alichokifanya ni kuwapa karatasi ile ya majibu na kila daktari kuanza kuiangalia. Kwa miaka yote hawakuwa wamefanikiwa kupata dawa ya kansa, walikuwa na Masters, PhD, leo hii, msichana mwenye digrii moja tu, tayari alifanikiwa kutengeneza dawa ya kansa, kila mmoja akashtuka.
Malumbano yalikuwa yakisikika kutoka katika nyumba moja nzuri na iliyoonekana kuwa ya kifahari iliyojengwa Sinza Mori. Kelele zile zilizokuwa zikiendelea ziliwafanya majirani kutokutulia, kila waliposubiri zipungue japo kidogo, zilizidi kuongezeka zaidi.
Majirani wakashindwa kuvumilia, walisubiri kwa kipindi kirefu sana kuona kelele hizo zikipungua lakini hazikupungua na hivyo kutoka ndani ya nyumba zao na kuwaamuru wanyamaze lakini hawakunyamaza.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa watu hao kulumbana, maisha yao yalitawaliwa na malumbano ya mara kwa mara, kila siku walikuwa kero kwa majirani ambao mara kadhaa waliamua kuwapeleka katika Ofisi za Serikali ya Mtaa lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote ile.
“Hivi unanijua wewe mwanamke?” aliuliza mwanaume mmoja, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, mwili wake ulitetemeka kwa hasira.
“Hivi na wewe unanijua? Unaionaje hii ngozi, unaichukulia poa, sasa utaona,” alisema mwanamke huyo.
“Unajua nitakuua wewe malaya!”
“Uniue mimi! Haloo haloo, eti uniue mimi, thubutu,” alisikika mwanamke huyo.
Huyo alikuwa Ibrahim na Nusrat. Ndoa yao ilifikisha mwaka mmoja lakini iliwaka moto. Hakukuwa na furaha ndani ya ndoa, tangu waoane na kuishi pamoja, maisha yao yalitawaliwa na malumbano ya mara kwa mara.
Walipendana kipindi cha uchumba, tu waliahidiana mambo mengi lakini ndani ya ndoa kila kitu kinaonekana kubadilika. Nusrat yule aliyekuwa, msichana yule mrembo alikuwa amebadilika.
Mara kwa mara alikuwa akirudi nyumbani usiku, tena akisindikizwa na wanaume wake, watoto wa Kiarabu walioonekana kuwa na fedha nyingi, alipofika nyumbani, hakutaka kuzungumza na mume wake, moja kwa moja alikuwa akiingia ndani kulala.
Ibrahim aliumia, alivumilia lakini uvumilivu ulifika mwisho, siku hiyo aliamua kulumbana naye, japokuwa walifanya hivyo mara kwa mara lakini siku hiyo ilionekana kuwa tofauti, alikuwa na hasira mno na kila wakati alikunja ngumi.
Nusrat hakuwa msichana aliyetulia hata kidogo, alikuwa mtu aliyehusudu sana starehe kuliko mambo mengine, mara kwa mara wanapokuwa kitandani, Nusrat hakutaka kufanya tendo la ndoa na mumewe jambo lililomuumiza mno Ibrahim.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mbali na hivyo vyote, pajani mwa msichana huyo karibu kabisa na kiuno kulichorwa tattoo moja yenye alama ya kopa ambayo pembeni iliandikwa ‘Nakupenda Nusrat’. Hicho ndicho kilichomkasirisha sana Ibrahim kwani alijua kwamba kulikuwa na mwanaume aliyeichora tattoo hiyo pajani mwa mke wake, hivyo kila siku walipokuwa wakilumbana, ilikuwa ni lazima kuizungumzia tattoo hiyo.
“Hivi haya ndiyo malipo yako? Hivi haya ndiyo malipo unayonipa baada ya kuuacha moyo wangu ukupende kwa mapenzi ya dhati? Nusrat mke wangu! Hivi ndiyo unaamua kunilipa ubaya kwa wema? Hivi hujui kwamba nilimwacha msichana aliyenipenda kwa ajili yako? ” aliuliza Ibrahim. Hapo ndipo kumbukumbu zake za maisha ya nyuma zikaanza kumrudia kwamba aliwahi kumuacha msichana aliyempenda kwa mapenzi ya dhati kwa ajili ya Nusrat ambaye leo hii alikuwa akileta ujinga ndani ya ndoa. Alishikwa na hasira lakini hakujua ni kitu gani alitakiwa kukifanya.
“Kwani nilikulazimisha umuache? Nilikulazimisha? Hebu niache niondoke, nitarudi kesho, najisikia kukesha klabu leo,” alisema Nusrat kwa dharau kubwa, alikuwa kashavalia, alichokifanya ni kuondoka nyumbani hapo kwenda klabu.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake ya kila siku, kila alipokwenda huko, alirudishwa na wanaume wa Kiarabu wenye gari kitu kilichomuongezea maumivu makali Ibrahim mpaka kufikia hatua ya kutamani kumuua msichana huyo.
*****
“You are very bright Latifa, you are very bright,” (Una akili sana Latifa, una akili sana Latifa) yalikuwa ni maneno yaliyosikika kutoka kwa Dk. Myles, hakuwa akiamini kama kweli ile dawa ya Morphimousis aliyokuwa ameitengeneza Latifa iliweza kuwaponya wagonjwa wale waliosumbuliwa kwa kansa.
Dawa ile ikaanza kutangazwa, Wamarekani na watu wa Ulaya ambao asilimia kubwa walikuwa wagonjwa wa magonjwa ya kansa wakamsifia Latifa na kumpa heshima kubwa japokuwa alikuwa na elimu ndogo na umri mdogo wa miaka ishirini na moja tu.
Jina lake likaanza kutangazwa, vituo vya televisheni vyote vikaanza kumtangaza kama mkombozi ambaye aliletwa duniani ili kuwaokoa watu waliokuwa wakiteseka vitandani. Ingawa Latifa alipewa sifa sana na kuonekana mtu sahihi kuletwa duniani lakini kukaanza kuibuka vuguvugu kati ya Tanzania na Marekani.
Latifa alikuwa Mtanzania lakini alisomea nchini Marekani. Nchi hiyo haikutaka kumuachia Latifa kiholela kwamba aelekee nchini Tanzania na kufanya kazi na wakati elimu kubwa aliyokuwa nayo ilitokea nchini mwao.
Latifa akagombaniwa, jina lake likazidi kupenya masikioni mwa watu wengi duniani. Kwa kuwa Marekani lilikuwa taifa kubwa, wakaamua kutumia nguvu zao nyingi kumtangaza Latifa kama Mmarekani na kuipoteza nchi ya Tanzania kiasi kwamba watu wengi duniani walijua kwamba Latifa alikuwa Mmarekani.
Kupitia dawa yake, akaanza kuingiza fedha, maisha yake yakabadilika, kutokana na ongezeko la wagonjwa wa kansa, Latifa akajikuta akiingiza kiasi cha dola milioni mia moja ndani ya wiki moja tu, hizo zilikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni mbili.
Wakati mwingine alijiona kama yupo ndotoni na muda wowote ule angeamka kutoka usingizini, umaarufu alioupata kwa ghafla sana uliyabadilisha maisha yake. Kila siku aliingiza kiasi kikubwa cha fedha, akanunua jumba kubwa na la kifahari lililokuwa Los Angeles hapohapo Marekani.
Ili kuzuia kila kitu kutoka kwa nchi kama Tanzania iliyokuwa ikitangaza kwamba Latifa alikuwa mtu wao, hapo ndipo Wamarekani wakaamua kumuajiri msichana huyo katika hospitali kubwa ya St. Luis Medical Center iliyokuwa hapohapo nchini Marekani katika Jiji la New York.
Japokuwa hakuwa amemaliza masomo yake lakini Latifa akapewa jina la udaktari rasmi na kuanza kuhudumia wagonjwa katika hospitali hiyo. Uwepo wake mahali hapo, ukawafanya wagonjwa wengi kumiminika, hawakuamini kama msichana huyo ndiye yule aliyekuwa amegundua dawa hiyo iliyomaliza matatizo ya watu wengi.
Aliwakumbuka sana Watanzania, alimkumbuka mlezi wake, bi Rachel lakini kila alipotaka kurudi nchini Tanzania, alizuiliwa kwa kupewa majukumu mengi ya kikazi jambo lililoendelea kuzua mtafaruku mkubwa kati ya Marekani na Tanzania.
Ndani ya mwaka mmoja wa mafanikio yake, Latifa akawa daktari mwenye kiasi kikubwa cha fedha, heshima yake ikaongezeka na akawa bilionea kijana kuliko wote duniani huku akimuacha vibaya mmili wa Mtandao wa Kijamii wa WorkSpace, Williams Peters aliyekuwa na umri wa miaka ishirini na mbili.
“Ni kitu gani ambacho huwezi kukisahamu maishani mwako?” aliuliza Larry King, mtangazaji wa Kituo cha Habari cha CNN.
“Ooppss...” alishusha pumzi Latifa na kuendelea:
“Kuna watu wengi wamejeruhiwa, kuna watu wamepewa vidonda ambavyo haviwezi kupona kamwe hata kama utakuja kuwa na maisha ya mafanikio kiasi gani huko mbeleni. Kwangu, siwezi kumsahau mwanaume anayeitwa Ibrahim,” alisema Latifa na kunyamaza.
“Ndiye nani?”
Latifa akanyamaza, akaingia kwenye hali ya mawazo, ghafla akaanza kububujikwa na machozi. Kila kitu kilichotokea katika maisha yake ya nyuma kikaanza kujirudia kichwani mwake.
Chuki kubwa ikamjaa moyoni mwake, hakumpenda Ibrahim, alimnyima furaha kipindi cha nyuma, alimnyanyasa kisa tu alimpenda. Hakudhania kama ingetokea siku yoyote ile angemsamehe mwanaume huyo. Kama kulia, alilia sana, hakutaka kumpenda hata siku moja na hata kile alichomfanyia katika maisha yake, hakutaka kumsamehe hata mara moja.
“Ninamchukia Ibrahim. Ninamchukia mno,” alisema Latifa huku akiyafuta machozi yake.
“Ndiye nani?”
Hapo ndipo Latifa akaanza kusimulia kile kilichokuwa kimetokea katika maisha yake ya nyuma. Alisimulia tangu siku ya kwanza alipokutana na mwanaume huyo alipomfuata shuleni kwao. Moyo wake ukajawa na maumivu makali mno. Alimpenda na kumpa penzi lake, alimthamini lakini baada ya kusafiri na kuelekea Marekani, kila kitu kikabadilika.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni kitu ambacho sitokuja kukisahau. Hata ikitokea siku nikamuona shetani na Ibrahim wapo porini wanataka kuliwa na simba na nina nafasi ya kumuokoa mmoja, nitamuokoa shetani,” alisema Latifa huku akionekana kumaanisha kile alichokisema, moyo wake ulitawaliwa na chuki kubwa dhidi ya Ibrahim, mwanaume aliyeutesa moyo wake hata zaidi ya Liban.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment