Simulizi : Mtu Wa Ufukweni (The Beach Man)
Sehemu Ya Tatu (3)
Mandhari ya ufukwe yalianza kuchukuwa kasi katika kuwa bora kila siku. Watu waliokuwa wanakuja kila mwisho wa juma walizidi kuwa wengi. Ramson alipata marafiki walioahidi kumletea viboti vya kutembezea watalii, katika maeneo mbalimbali baharini. Kuna visiwa vyenye historia nyingi ambavyo vinaweza kuwa na kumbukumbu nyingi. Ramson ametamani kupata boti za kuwatembezea baadhi ya watalii watakaopenda kutembelea maeneo hayo.
Hizo ni ndoto ambazo anaendelea kuzifanyia kazi kila siku ili kuinua kipato na kuridhisha moyo wake, kwa kufikia malengo yake ya kimaendeleo.Ringo alikuwa akijishughulisha kwa bidii sana katika kufungasha bidhaa mjini na kuwauzia wateja pia alisimamia mazingira. Kwa namna hii walipiga hatua kubwa ya kimaendeleo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila hatua walipongezana na kukaa mahali ili kutathimini faida na hasara lakini ilikuwa ni aghalabu sana kupata hasara katika kazi yao hiyo. Kwa Ramson Ringo alifanyika kuwa ndugu yake kabisa. Alifarijika kuona kuwa hata Ringo alimchukulia vilevile. kilichoweka muhuri juu ya undugu wao ni uaminifu na bidii yao. Walishirikiana kwa mambo yote na hata mawazo yao hayakutofautiana.
Kitu kingine hawakutaka pombe, wala tabia za kujihusisha na mambo ya uhuni hayakuwepo vichwani mwao Walizingatia miiko waliyojiwekea kuwa ndio msingi wa maendeleo yao kama wakiishika. “Unajua kama tusingejiwekea miiko hii hapa tulipofikia pangebakia katika ndoto?” Alisema Ramson siku moja walipokuwa katika kikao chao cha kujadili maendeleo ya ufukwe wao.
“Ni kweli Rafiki yangu. Daah unajua nimeheshimu sana mipango yako mtu wangu. Katika maisha yangu sijawahi kuwaza kuwa tunaweza kuwa wamiliki wa sehemu nzuri hivi. Ungeniuliza mapema juu ya suala hili ningepiga mahesabu ya mamilioni ya mtaji kumbe ni bidii na maarifa tu!” Alisema Ringo huku akishangaa aina ya maendeleo yalivyokuja kwao.
“Mtu wangu naweza kusema kuwa hii ni hatua ndogo sana. Hatujafika popote ila tayari tumepata fununu tu ya kule tunakotaka kwenda. Unajua mara zote ukijiona uko juu bila kuangalia walioko juu zaidi yako, unaweza kujibweteka. Lakini mara kwa mara unapopiga hatua fulani usiridhike kuwa uko juu. Jambo la kufanya Kila unapopiga hatua angalia juu, Utakapowaona wengine walivyo juu kimaendeleo kuliko wewe, jipange na utamani kufika pale walipo na kuzidi, hii ndio chachu ya kimaendeleo siku zote.
Unajua Rafiki yangu maendeleo ni nia na juhudi kwa kile unachotamani ukipate. Hapa tulipo tunamshukuru Mungu tunapata riziki yetu ya kila siku. Tunaweza kubadilisha mavazi kila siku tukitaka. Pia tunaweza kufanya vitu vingi kiasi kwa uwezo wa Mungu. Lakini bado hatujapiga hatua ya kimaendeleo. Tunatamani usafiri wa kufungashia bidhaa zetu mjini. Tunatamani boti za kuwatembezea wateja wetu baharini, tunatamani pia kujenga nyumba za maana hapa ufukweni na kuzifanya hoteli kwa ajili ya wageni wetu.
Tunaangalia mbele zaidi kuwa siku moja tuwe na Hoteli za kitalii mahali hapa. Ukiangalia mipango hiyo na ukirudi kuangalia hapa tulipo lazima ujione kuwa bado uko chini sana.” Alisema Ramson kwa utulivu kuonyesha kuwa kichwani kwake bado mipango iko mingi inayohitaji kufikiwa. “Kweli Rafiki yangu unaangalia mbali sana.” Alisema Ringo kwa msisimko. Maelezo yako yanahamasisha na kutia ujasiri wa kufanya kazi kwa bidii.
Najua kama Mungu ametuwezesha kufika hapa tulipo tutashindwaje kufikia malengo hayo uliyoyasema? Hii ni hatua ya kwanza mbele yetu tunazo hatua nyingi sana zinazohitajika kutufikisha katika kila kimoja cha hayo malengo uliyonayo.” Alisema kwa hamasa Ringo. “Naamini kila jambo litafikiwa katika yote tuliyopanga.” Alisema Ramson kwa uhakika kisha akaamka kwenda kupokea wageni waliokuwa wanapaki gari lao.
“Yule jamaa ameleta Mabarafu?” Aliuliza wakati akiendelea kutembea kuwaendea wageni wake. “Ataleta saa sita maana yalikuwa bado kuganda sawa sawa.” Alijibu Ringo kwa sauti.
* * *
Ilikuwa ni ajali mbaya sana. Ajali iliyotokea mjini Tanga kwenye barabara iitwayo Taifa Road. Gari ndogo ilikuwa ikitokea maeneo ya Mabanda ya papa kwenda maeneo ya Mjini kati. Gari hili lilikuwa likienda kasi sana inaelekea Dreva wake alikuwa na haraka sana. Gari hili mara tu lilipokuwa kwenye raundi about ya barabara ya kumi na tano lilikutana na pikipiki iliyotoka soko mjinga.
Mwendesha pikipiki hakuwa akiangalia na badala yake alikuwa akitaka kupitiliza ili kwenda ng’ambo akiambaa ambaa na barabara hiyo ya kumi na tano kwenye maduka ya vyakula.Alipokuwa katikati ya barabara ya Taifa road kabla hajaifikia barabara nyingine pacha na ile, ndipo gari lile lilipogonga pikipiki ile vibaya. Gari liliserereka kwa kukosa mwelekeo kisha liliingia kwenye mfereji wa barabara hiyo. Dreva wa pikipiki alikufa hapohapo. Ndani ya gari walikuwepo abiria wawili pamoja na Dreva, abiria wote walifariki dunia lakini dreva alivunjika mguu wa kushoto na kupata majeraha mengi usoni.
Miongoni mwa abiria walikufa kwenye ajali hiyo alikuwepo Ringo! Ringo alitoka asubuhi hiyo ufukweni ili awahi kununua bidhaa mjini. Ilikuwa ni Jumamosi kwa hiyo wateja ni wengi sana ufukweni. Hivyo waliagana na Ramsoni kufungasha bidhaa za kutosha, ili wateja wasikose mahitaji muhimu. Kabla hajafika kwenye vidaladala vya kumpeleka mjini, alikutana na rafiki yake Kejo aliyekuwa na gari.Alijipakia ndani ya gari hilo ndani yake akiwepo mtu mwingine, mbali na Kejo aliyekuwa akiendesha.
Kwa ufupi ulikuwa ni msiba mwingine wa kutisha na kusikitisha sana kwa Ramson, baada ya kupewa habari. Moyo wake ulimuuma sana, kwa kumkosa tena mtu muhimu kwake na kwa shuguli zake. Ramson alisimamia msiba huo kama wa ndugu yake kabisa.
Kila kitu alihakikisha kinafanyika kwa viwango vikubwa. Alisafirisha yeye mwili wa aliyekuwa rafiki yake na kusimamia mambo yaliyopungua kwa ajili ya matayarisho ya mazishi. Mwisho wa yote aliwapa wazazi wa Ringo kiasi cha fedha, kilichokuwa mgao wa fedha kwa ushirikiano na mtoto wao. Kisha aliahidi kuendelea kuwahudumia kama kukumbuka ushirikiano wake na Mtoto wao katika kazi zake.
* * *
Baada ya miezi miwili Ramson akiwa katika maeneo yake ya kazi alipata wageni. Ni kawaida yake kupata wageni kila siku lakini wageni wa leo walikuwa hawajawahi kufika ufukweni hapo, walikuwa ni mwanamme na mwanamke. Walionekana watu hawa ni matajiri kutokana na uonekano wao, pia Usafiri wao ulikuwa wa thamani sana. Baada ya kupaki gari waliteremka na kuja mbele ya Ramson kwa hatua za taratibu, wakiwa wameshikana mikono. Ukweli walikuwa wamependezana sana.
“Karibuni sana Wageni wangu.” Alikaribisha Ramson. “Asante sana habari za hapa?” Aliitikia yule wa kiume. “Nzuri sana karibuni sana. Mimi naitwa Ramson lakini Rafiki zangu hupenda kuniita The Beach Man! Karibuni mjisikie vizuri kuwepo hapa.” Alisema Ramson. “Asante Mimi naitwa Jackson Kigoi kwa fani ni Dokta hivyo watu wamezoea kuniita Dr.Jackson, huyu niliyenaye ni Mke wangu mpenzi anaitwa Mrs Mary Jackson.” Alisema Jamaa huyo aliyejitambulisha kama Jackson.. kisha akaendelea..“Kuja kwetu hapa ni ili tujipumzishe na kuogelea. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tumepata taarifa juu ya ufukwe huu kuwa ni mzuri na mmiliki wa eneo hili ni mkarimu sana na ndivyo tunavyojionea hapa.” Alimalizia kutoa utambulisho Dr.Jackson huku mkewe akitoa tabasamu kumuunga mkono kwa maneno yake. “Labda ni kweli! Karibuni sana ndugu zangu. Sijui kama mtahitaji vifaa vya kuogelea?” Aliuliza Ramson kwa uchangamfu. “Mimi sina shida ila mwenzangu inabidi umpatie puto maana asije akatupa mitihani hapa hajui kuogelea kabisa.” Alisema Dr.Jackson.
“Hamna shida kabisa Dr,” Alisema Ramson huku akiingia kwenye kibanda kimojawapo na kutoa Puto moja na kumkabidhi Mke wa Dr. nao wakaondoka na kuelekea kwenye maji. Baada ya hapo aliendelea na kazi zake nyingine. Mpaka baada ya muda wa masaa mawili alipoitwa tena na wateja wake hao kwa ajili ya kuwaelekeza bafu iliyowekwa tayari kwa ajili yao ili kujisafisha kwa maji safi. Ramson aliwaelekeza na baadaye walipokuwa tayari walimlipa kwa huduma zote.
Hapa mahali tumepapenda sana pana huduma nzuri na mazingira yake yanavutia. Alisema Dr. Jackson au unasemaje mke wangu?,” Aliuliza Dr. Jackson huku akimgeukia mkewe. “Kwa kweli ni pazuri sana,” Aliitikia na kutabasamu tutakuwa tunakuja hapa kila mara alimalizia Mrs Jackson. “Nashukuru sana kama mmependezewa na huduma zangu na wakaribisha sana,” Alisema Ramson huku akiwasindikiza wakati wakielekea kwenye gari lao.
Baada ya kuingia garini walimpungia na kuondoka taratibu. Ramson akarudi kuhudumia wateja wengine. Kwa ujumla alikuwa na mawazo mengi mazuri kwa jinsi alivyokuwa anapata wateja kila wakati. Kubwa na la kupendeza ni pale wanaposifia eneo lile kuwa ni zuri. Sifa hizo zilichangia sana kutia bidii, katika kuuboresha ufukwe huo. Ramson alikuwa tofauti sana na watu wengi katika namna ya kupokea sifa kwa jambo fulani. Wengine wanaposifiwa hukaa wakarithika na sifa hizo.
Ila Ramson huchukulia kuwa kusifiwa kwake ni changamoto za kumfanya asonge mbele kwa kufanya vizuri zaidi. Dr. Jackson na mkewe walimpa changamoto nyingine, ambayo kwake ilikuwa ni chachu ya kufanya mambo makubwa zaidi. Alipata ari nyingine ya kuboresha huduma ufukweni hapo. Mawazo yake yakawa katika kutafuta jinsi ya kufanya vizuri zaidi ili kuzifikia ndoto zake.
* * * *
Ulikuwa ni mchana uliokuwa na jua kali pamoja na joto. Mchana huu ulikuwa wa faida sana kwa Ramson kwani ulivuta wateja wengi waliotaka kupunguza joto, kwa kuogelea na wengine kupunga upepo tu ufukweni hapo. Watu wengi walihitaji vinywaji baridi ambavyo vilikuwepo vya kila aina. Akisaidiana na wasaidizi wake katika kuuza aliwauzia wateja wake soda Juice na Ice cream za aina mbalimbali.
Kwa ujumla watu waliburudika sana na kutamani kuja tena katika ufukwe huo kutokana na huduma zake kuwa nzuri. Wakati Ramson akiwahudumia watu mara jamaa mmoja alimsogelea karibu, “Ramson!”Aliita jamaa huyo kwa sauti ya mshangao! Ramson alipogeuka hakuamini macho yake, alikuwa ni Richard rafiki yake. “Richard ni wewe rafiki yangu?” Ramson alisema hivyo na kumkumbatia rafiki yake.
“Kwa kweli leo ni siku njema sana, karibu Richard.” Alisema Ramson huku akimwelekeza mahali pazuri pa kukaa ili wazungumze. “Chidy njoo uchukuwe vinywaji hivi uwapelekee wale watu pale mtu na mkewe sawa?” Ramson alimwagiza kijana wake wa kazi. Njoo hapa rafiki yangu yeye na rafiki yake walikaa kwenye mwamvuli mmoja uliojengewa kwa ajili ya kuleta kimvuli.
“Hatimaye ndoto zako zimetimia Ramson,” Alisema Richard huku akionyesha kumshangaa Rafiki yake. “Ni kweli Richard nashukuru sana kwa ajili ya hatua hii, japo bado ndoto ni nyingi zinazosubiri kutimizwa,” Alisema huku akitabasamu. “Kwa kweli sikutegemea kuona haya ninayoyaona leo. Alisema Richard kisha akatulia kidogo wakati akipokea juisi yake aliyoletewa na mfanyakazi.. kisha akaendelea
“Ulipozungumzia mambo ya Beach mimi nilichukulia kwa uzito mdogo sana. Japo sikudharau maono yako lakini sikufikiri kuwa utakifikia mapema hivi. Hongera sana Ramson.” Alisema Richard huku akiangaza angaza macho kwenye maeneo mbalimbali.“Asante sana rafiki yangu, ndio hivyo maisha yalivyo... Kutumia Fursa ni jambo la muhimu sana.
Kuna Fursa nyingi sana zinazotokea katika maisha ya mtu. Afya njema ni fursa mojawapo kwa upande wake, Ujana pia ni fursa, na mawazo yenye msukumo wa kufanya jambo fulani nayo ni fursa. Kuna aina nyingi za Fursa ila nimetaja hizi chache ili niweze kuzizungumzia. Kwa ujumla wake fursa zote hizi hutokea mara moja moja na hazirudii tena . Mfano ujana: “Ujana unapokuja na mtu akashindwa kutumia ujana wake vizuri ujana huo unapoondoka hauwezi kurudi tena hata kama ungefanya nini!
Nguvu za ujana ni nyingi sana, lakini zinakabiliwa na changamoto nyingi pia. Matumizi mabaya ya ujana kwa njia ya tamaa tu huharibu fursa ya mtu. Wengi wameutumia ujana wao vibaya na kukosa kuweka kumbukumbu nzuri za maisha yao baada ya wao kuzeeka au kufa. Kwa upande wa afya njema ni moja ya fursa tuliyopewa na Mungu.
Matumizi ya afya zetu njema yazingatie kuwa kuna wengi hawajiwezi aidha ni wagonjwa ama wamepungukiwa na viungo muhimu katika miili yao. Ikiwa mtu ni mzima wa afya asipoutumia uzima huo iko siku atakuja kujilaumu; kwa kuwa hata uzee nao utakuwa kikwazo cha kufanya mambo mengi muhimu. Tunapokuja kwenye mawazo yenye msukumo wewe ni shahidi.
Ninakumbuka nilikushirikisha zaidi juu ya maazimio yangu kuhusu kufanya kazi za ufukweni. Najua ulikuwa hujanielewa mpaka tunaachana wakati ule. Ila niliambulia kwako jina zuri sana lililonifaa, kwani uliniita The Beach Man! Kweli rafiki yangu niliamua kuwa mtu wa ufukweni na kuishi ufukweni. Mahali hapa pakawa ndio nyumbani kwangu nimewekeza chochote nilichokipata katika ufukwe huu.”Ramson Alikohoa kidogo kisha akaendelea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwa kupitia mawazo hayo nimefaulu kutengeneza kituhiki, kitu ambacho kwa maneno tu hakiwezi kuonekana wala kushikika!Karibu sana Ufukweni kwa rafiki yako.” alihitimisha Ramson Hotuba yake. “Asante sana Ramson kwa fundisho lako lenye kuambatana na mfano huu mzuri na halisi. Nimevutiwa na maono yako makubwa sana, unaona mbali sana Ramson.” Alisema Richard.
“Wewe uko wapi sasa?” Aliuliza Ramson. “Baada ya kuachana nilikwenda tena kwa baba mkubwa na kumwomba anisaidie kiasi cha hela za Mtaji ambazo nilitarajia kufungua biashara fulani.Nilikuambia kuwa baba yangu huyo hawezi kuacha kunisaidia, lakini kabla hajanisaidia anatanguliza maneno mengi sana ya masimango. Baada ya masimango hayo hunipatia kiasi kile nilichomwomba au zaidi.
“Lakini safari hiyo niliyomwendea alikuja na jambo tofauti, hakunipa hela bali alinipeleka kuchukuwa kozi ya Uongozi nchini Marekani. Miaka miwili ilinitosha kuajiriwa kwenye kampuni ya usafirishaji iliyoko Jijini Dar-es-Salaam.” Alisema Richard. “Aaaaah! hongera sana rafiki! Ni hatua nzuri sana.” Alisema Ramson. “Asante na hivi ninavyoongea mimi ndiye meneja wa kampuni hiyo ambayo nimeitumikia kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.”
“Hongera sana Richard.” Ramson alimpongeza rafiki yake na kuongea mengi sana kabla hawajaachana. “Kwa hiyo umekuja kumwona baba mkubwa?” Aliuliza Ramson wakati wakiagana. “Ndiyo nimekuja kumwangalia afya yake Yeye kashakuwa mzee sasa.” Alimalizia huku akitabasamu na kupanda ndani ya gari yake tayari kwa kuondoka. “Kwaheri Ramson nitakutembelea tena wakati mwingine.” Alisema. “Asante kwaheri Richard!” Alisema Ramson huku akipunga mkono kuagana na Richard.
* * *
Ilikuwa ni siku ya Jumatano mchana Ramson alipopata mgeni. Mgeni huyohakuwa mwingine bali alikuwa ni Mary au Mrs Dr. Jackson. Mary alipoegesha gari lake alimsogelea Ramson mahali alipokuwa amekaa akipunga upepo. Wooooow Mrs Dr. Karibu sana.” Alisema Ramson akimkaribisha. “Asante sana Ramson, naona umepumzika habari za tangu tuachane?” Mrs Dr.Jackson aliuliza huku akijikalisha kando ya Ramson.
“Ninashukuru karibu Mrs. Dr. Leo umekuja peke yako?” Aliuliza Ramson. “Dr. Jackson amepata safari, amekwenda Uingereza kuongeza masomo yake ya Udaktari.” Alijibu Mary. “Atachukuwa muda gani kumaliza amasomo yake?” Aliuliza Ramson huku akijiweka sawa kwenye kiti. “Atakaa huko miaka mitatu.” Alijibu kwa hali fulani ya unyonge kidogo Mary,kisha akanyanyuka na kusimama. “Naomba puto nimekuja kuendelea kujifunza kuogelea.” Alisema Mary.
Ramson alinyanyuka na kuelekea kwenye kibanda cha kuhifadhia Maputo na kumchukulia moja, “Hili linakufaa sana unaweza kulitumia kwa njia zozote, hata kulala juu yake wakati ukichoka kuogelea” Alisema Ramson na kumkabidhi puto lililokuwa kama kitanda. “Lakini ningehitaji uje unifundishe maana kwa kweli sijui lolote kuhusu kuogelea.” Alisema Mary baada ya kupokea puto hilo.
“Sawa nitakuja tangulia kuna mambo niyaweke sawa kwa ajili ya wateja.” Ramson alijibu na kuchukuwa chombo cha kuchotea maji na kwenda kuchota maji yaliyokuwepo kwenye pipa na kujaza ndoo mbili na baadaye aliuzipeleka kwenye bafu mbili tofauti. Baada ya kazi hiyo alimfuata Mary aliyekuwa anachezea maji kwenye kina kidogo.
“Sogea kule mbele kwenye maji mengi.” Alisema Ramson wakati akianza kuinga kwenye maji. Walisogea mpaka kwenye kina kirefu cha maji na Ramson alimfundisha Mary jinsi ya kuogelea kwa muda mrefu. Kwakuwa Mary alikuwa mwepesi kuelewa aliweza kushika mitindo miwili ya kuogelea. Mpaka wanatoka kwenye maji alikuwa anajua kuogelea kiasi. “Ramson nashukuru sana kwa kunifundisha. Wewe ni mwalimu mzuri sana.” Alisema Mary akishukuru. “Asante sana Mary kwa shukrani zako, wewe pia ni mwanafunzi mzuri sana, maana ni mwepesi wa kuelewa unapofundishwa.
Kwa sasa hata nisipokufundisha tena mitindo mingine itatokana na ubunifu wako tu katika kuchezea maji.”Alisema Ramson na kumwelekeza ilipo bafu ili akaondoe maji ya chumvi.“Aaaah! Mi mbona bado nahitaji uendelee kunifundisha? siku moja tu haitoshi kunifanya nijue kuogelea mwenyewe.” Alisema Mary wakati akielekea bafuni. “Sawa Mary nitakufundisha tena siku ukija.” Alisema Ramson.
Baada ya Mary kumaliza kuoga alitoka bafuni na kumuaga Ramson. “Ramson kwaheri naweza kukutembelea siku nyingine.” Alisema wakati akielekea ilipo gari yake. “Karibu Mary ukiweza waalike na marafiki zako ili waje kupunga upepo na kuogelea.”Alisema Ramson. “Kwa hilo usiwe na wasiwasi nitafanya hivyo.” alisema Mary wakati akiingia kwenye gari lake na hatimae kuliondoa taratibu.
* * *
Mwenyekiti wa kijiji cha Tabu yanini siku moja nyakati za Asubuhi alimtembelea Mzee Kihedu. Alikuwa na mazungumzo mengi lakini moja ya mazungumzo hayo lilikuwa juu ya Ramson. “Bwana Kihedu habari za kijana wetu Ramson? Nilimwona wakati wa msiba wa bibi yake lakini baada tu ya kumaliza mambo yote aliondoka, japo nilihitaji sana kuongea naye.”
Alisema Mwenyekiti. “Kwa kweli ndugu mwenyekiti kijana Ramson anaendelea vizuri sana huko aliko. Sijasikia tatizo lolote juu yake na pia maisha yake yanaendelea vizuri.” Alijibu Mzee Kihedu huku akimimina kahawa kwake na kwa Mwenyekiti. “Unajua bwana Kihedu moyo umeniuma sana baada ya kugundua kuwa Ramson hakuwa mwizi.
Kubwa sana linaloniumiza ni jinsi nilivyomfukuza hapa kijijini, nikishirikiana na wanakijiji. Nilitafuta sana nafasi hii ili nije tu kuzungumza na wewe, ili unikutanishe na Ramson nimwombe msamaha na kuitisha mkutano wa kijiji. Ninakusudia kumtakasa kwa wanakijiji kwa ubaya tuliomzushia.” Alisema mwenyekiti kwa unyenyekevu sana. “Ndugu mwenyekiti ninashukuru kwa kusikia kutoka kwako kuwa Ramson sio mwizi!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hicho kilikuwa ni kidonda ndani ya moyo wangu, kwa mjukuu wangu kuitwa Mwizi na kukataliwa na kijiji. Ilinigharimu sana kufikiri na kuvumilia maumivu hayo kwa muda mrefu. Ila niseme tu kuwa Ramson kwa sasa yuko vizuri na hana kinyongo chochote na wewe wala wanakijiji. Niligundua hili pale alipokuja kwa ajili ya msiba wa bibi yake.
Baada ya kumaliza msiba alisifu ushirikiano ulioufanya wewe na wanakijiji kwa ajili ya mambo yote ya mazishi. Alikusifu kwa mambo yote hasa jinsi ulivyokuwa mstari wa mbele katika shughuli nzima ya msiba.”“Enhee! alisemaje kuhusu tatizo lile?” Alidakia mwenyekiti! “Nilipozungumzia masaibu yaliyompata, alichosema Ramson ni kwamba kijiji kilitumika kumpeleka mahali ambapo alipaota siku nyingi, ili akaweke makao yake. Aliongeza kuwa kama kijiji kisingefanya hivyo asingefikia ndoto zake hizo. Kwa sasa Ramson anamiliki biashara zake ufukweni huko Tanga. Maisha yake yanaenda vizuri na tayari ameajiri watu kadhaa wa kumsaidia katika biashara na miradi yake.
Katika ufukwe huo anapata wageni wengi sana mpaka wazungu. Kwakweli ndugu mwenyekiti hata Ramson angepewa magari na hela nyingi, hawezi kuja tena kukaa hapa kijijini. Hayo ndiyo niliyoyaona kwake.” Alihitimisha Mzee Kihedu kutoa maelezo. “Hayo ni sawa bwana Kihedu. nafurahishwa na maendeleo yake pia, lakini nitahitaji siku moja aje ili niitishe mkutano na kumwondolea shutuma zile.
Hilo ni deni ninalodaiwa kulilipa kwake na utu wake niliouharibu kwa maneno yasiyo ya kweli.” Alisema mwenyekiti kwa msisitizo. “Sawa ndugu Mwenyekiti nitafanya hivyo, akirudi kuniangalia nitamwambia aje mwonane wenyewe.” Alisema Mzee Kihedu. “Sawa sawa kabisa bwana Kihedu, nitashukuru nikionana naye mwenyewe ili kulizungumzia hilo.”
Alisema Mwenyekiti huku akiweka kikombe cha kahawa mezani na kunyanyuka. “Mbona unasimama ndugu mwenyekiti, bado kahawa ipo tuendelee kunywa kuna mengi ya kuzungumza.” Alisema Mzee Kihedu. “Bwana Kihedu ngoja niende mazungumzo hayaishi. Tutakuwa na muda mzuri wa mazungumzo hayo. Kwa sasa ngoja niwahi shamba, kuna vijana wametangulia na mke wangu kwa kazi ya kuangua nazi. Mama Batuli ana kazi nyingi, naenda kusimamia maswala ya nazi pamoja na ubebaji.”
Alisema Mwenyekiti huku akiusogelea mlango. Mzee Kihedu alinyanyuka na kumsindikiza mpaka nje ya nyumba yake. “Sawa Mwenyekiti wangu nikutakie siku njema.” Aliaga Mzee Kihedu. “Na wewe pia.” Alisema hayo na kuondoka kisha Mzee Kihedu alirudi ndani na kujiandaa kwa majukumu ya siku hiyo mpya.
* * *
Asubuhi hii ilikuwa ya harakati nyingi kwa Mary. Alikuwa akipanga hiki na kupangua kile ili mradi alikuwa yuko na shughuli nyingi sana. Mawazo pia yalikuwa mchanganyiko kwenye kichwa chake, ndio maana akajipatia shughuli nyingi hata ambazo hazina umuhimu. Mawazo yake yalikuwa juu ya Beach Man! Mtu huyu wa Ufukweni alimchanganya kwa aina ya maisha yake. Alisikia kuwa pale Ufukweni ni yeye aliyepatengeneza.
Cha kusisimua ni kwamba Kijana huyo alianzisha sehemu hiyo akiwa hana hata hela. Alihamia tu mahali hapo akitokea kijijini kwao, kidogokidogo akajikongoja mpaka kufikia hatua hiyo. Mawazo yake hayakuwa na sababu ya msingi katika kuyachukulia umuhimu wa kiasi kile! Hata siku moja hajawahi kufikiri kuanzisha mradi unaofanana na ule.
Hata yeye angeulizwa ni kwanini anafikiri kwa kiwango hicho juu ya mradi wa Ramson, asingekuwa na jibu la maana. Ila alipokuwa katikati ya mawazo hayo alishtuliwa na simu iliyokuwa inaita. Alipoangalia kwenye kioo cha simu alikutana na Jina la Irene!..“Halo Irene habari za asubuhi? Aliitikia Mary kwa bashasha! “Habari ni nzuri sana Mary nimekumiss sana ndio maana nikakupigia, kama una nafasi uje tujumuike wote kwa chakula cha mchana.” Alisema Irene.
“Asante rafiki yangu ni kama uliyejua kuwa niko mpweke sana leo.” Alisema Mary. “Sawa basi karibu sana ndugu yangu” Alisema Irene na kukata simu. Mary akakusanya nguo na kuzirudisha mahali pake taratibu huku akijiandaa kuelekea kwa Irene. Baada ya kuoga na kujiweka sawa alitoka na kumwaga msichana wake wa kazikuwa anatoka kidogo, angerudi baada ya muda si mrefu sana. Kisha akazama ndani ya gari yake na kuiondoa kwa mwendo wa taratibu.
Mwendo wake ulimfikisha nyumbani kwa rafiki yake kwa muda muafaka, kwani alimkuta akiwa anaandaa chakula mezani. “Woooooow rafiki yangu!” Alisema Irene baada ya kumwona Mary akiingia ndani ya sebule. “Wooooow! Irene mambo vipi?” Aliuliza Mary wakikumbatiana. “Kwa kweli mambo ni mazuri karibu sana Mary. Nimekukumbuka sana asubuhi. Sababu ya kukukumbuka ni juu ya biashara yetu. Niliona kama tunaweza kuiboresha zaidi ingetuingizia faida kubwa sana.”
Unajua ni siku nyingi zimepita bila kukaa kikao cha kujadili habari ya maendeleo ya biashara?” Alisema Irene. “Ni kweli kabisa Irene! Wazo lako ni la manufaa makubwa sana.” Alisema Mary huku akiliendea sofa na kujikalisha. “Mary naona ungekaa mezani kabisa kwa sababu umekuja kwa wakati chakula tayari.” Alisema Irene na Mary alinyanyuka na kusogea mezani taratibu.
“Mwanamke kwa kwenda na wakati wewe! Saa saba kamili chakula tayari mezani!” Alitania Mary huku akijikalisha kwenye kiti kinachokabili meza kubwa ya duara. “Si unajua tena rafiki yangu miili yetu haijengwi na matofali! Chakula ndio kinachotengeneza kila kitu katika mwili wa mwanadamu, usipojijali unafikiri utakuwaje?” Alisema Irene wakati akifunua bakuli la chakula maarufu kama hot port. Baadaye alimsogezea Mary pamoja na mboga, kusudi ajipakulie mwenyewe. Mary alifanya hivyo na baadaye wakaingia katika mazungumzo yao, wakati wakipata chakula. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mazungumzo ya biashara yalipokwisha waliingia kwenye mada mchanganyiko. Waliongelea lolote waliloona linafaa kuliongelea ilimradi kusogeza muda.“Unajua Irene unapitwa na mengi?” Alisema Mary katika kuanzisha mada mpya. “Yapi rafiki yangu?” Aliuliza Irene huku akijiweka sawa kwenye kiti chake.“Hivi ulishawahi kufika Mwahako Beach?” Aliuliza Mary kiushabiki. “Wala sijawahi kufika kwani kuna nini cha ajabu huko?” Aliuliza Irene.
“Si ndio rafiki yangu ninakuambia kuwa unapitwa na mambo mengi? Mwahako kuna bonge la Beach! Si unasema hapa Tanga hakuna ufukwe uliotulia? Basi nenda kauangalie Ufukwe wa Mwahako utaupenda mwenyewe!” Alisema Mary kwa namna ya mpiga debe! “Tanga kuna ufukwe wa maana kweli kama fukwe za wenzetu?” Aliuliza Irene. “Kama wapi?” Mary aliuliza pia. “Kama Mombasa?” Unajua Mary mimi nimependa sana fukwe za Jirani zetu wale.” Wamefanya ubunifu wa hali ya juu sana na kujaribu kuwekeza kwa nguvu zote, hadi watalii wakatamani kuwa wanatembelea fukwe hizo.
Mombasa wamepiga hatua kubwa sana kwa njia hiyo.” Alisema Irene. “Ni kweli Irene sio wewe tu hata mimi ni mmoja wa washabiki wa Fukwe za jirani zetu Wakenya. Mara kwa mara mapumziko yetu na Dr. tunapenda kutembelea kwenye Fukwe hizo. Ila wiki kama mbili zilizopita Dr. alinipa habari za kuwepo kwa ufukwe mzuri maeneo ya Mwahako. Na mimi sikuamini kwa kuambiwa tu bali siku tuliyoenda ndipo nilipoamini kwa macho yangu.
Labda wewe pia siku tukienda utakubali baada ya kuona mwenyewe mandhari yaliyopo hapo.” Alisema Mary. “Okay Twende lini? maana umenihamasisha mpaka nimehamasika! natamani nipaone mahali hapo.” Alisema Irene. “Hakuna shida nitakupeleka huko hata kesho ukitaka. Nitaangalia nafasi kisha nitakuambia jioni ratiba yangu.
Itakuwa nzuri sana Irene utafurahi pia kumwona The Beach Man, ni mtu mwenye bidii na mtanashati sana muda wote. Anapendeza sana kama ufukwe wenyewe unavyopendeza!” Alisifia Mary.Nafikiri wewe umeshampenda huyo The beach Man unayemsema, maana unavyomsifia!
Alisema Irene kwa mashaka huku akionyesha mshangao. “Umejaribu kuwa karibu na ukweli, sina la kukubishia ila nahitaji ushauri wako juu ya hili.” Alisema Mary kwa aibu kidogo. “Unataka kuvunja ndoa yako? Mimi simo siwezi kuwa mshauri wako katika hili.” Alisema Irene kimbea huku akijichekesha kwa sauti.
“Hakuna neno rafiki yangu mimi naona ni vizuri kesho tufike huko kusudi ukashuhudie mandhari ya ufukwe mambo mengine tutayaongelea tukiwa katika eneo hilo sawa? Kwa sasa sina maneno mengi ya kuongea.” Alisema Mary. “Vipi wewe kuhusu Shemeji? mmekubaliana ndoa ikafungiwe wapi?” Aliuliza Mary. “Kwakweli rafiki yangu mpaka sasa nimechanganyikiwa.” Alisema Irene wakati akiweka juice mezani.
“Jiwekee juisi unayoipenda kati ya hizi hapa na kama huna chaguo lako hapa sema nikutolee nyingine.” Alisema Irene. akiwa kapanga chupa mbalimbali za Juisi mezani. “”Hizi zote nazipenda nitakunywa yoyote kati ya hizi usisumbuke kutoa nyingine. Alisema Mary. Mwenzangu uko juu kuhusu mambo ya matunda. Juisi zote hizo ni kwa ajili yako tu na msichana wako wa kazi?” Alisema Mary kwa mshangao.
“Kwakweli mimi kuhusu matunda mtu haniambii kitu. Ninatengeneza Juisi za matunda ya kila aina, kusudi kujenga na kulinda mwili. Si unajua kuwa Miili haina spea kwa hiyo tunapaswa kuilinda na kuitunza ili isipatwe na uharibifu.” Alizungumza hayo huku akisogeza glasi kwa rafiki yake.“Nimekuelewa rafiki uko sawa kabisa. lakini nimekuuliza habari ya ndoa yenu mmepangaje naona bado hujanijibu vizuri.” Mary alikumbusha. “Ni kama nilivyokuambia rafiki yangu kuwa ndoa yenyewe ina mambo ya kuchanganya tu.
“Unajua kwenye mahusiano kama hayo halafu kukiingizwa vipingamizi kibao inasumbua sana kichwa?” Alisema Irene kwa umakini sana. “Mvutano gani tena?” Si ulisema shida ilikuwa ni nyinyi kuamua mahali pa kufungia ndoa kati ya Kanisani au msikitini? Nikafikiri labda mmepata maamuzi watu waanze vikao vya maandalizi.” Alisema mary.“Bado hatujapata maamuzi ya maana rafiki yangu unajua swala la kubadili dini kwa upande wetu sio tatizo ila wazazi ndio wanaoleta vipingamizi.
Sijajua la kufanya na hata mwenzangu amechanganyikiwa kabisa.” Alisema Irene kwa masikitiko kidogo. “Sawa Irene lakini kama imeshindikana kufungia kanisani au Msikitini, fanyeni uamuzi wa kufungia bomani, kusudi kila mtu abaki na dini yake?” Alishauri Mary.“Mary unafikiri ni rahisi kufanya hivyo? Bado maamuzi yanabaki kwa wazazi wetu. Hakuna kati yetu aliyefikiria suala la kufungia ndoa Serikalini.
Ila wazo hili ni jema nitajaribu kulipenyeza kwa mwenzangu alipeleke kwa wazazi wake tuone kama linaweza kuleta matokeo.” Alisema Irene. “Basi rafiki yangu jaribu kumpa njia hiyo halafu tusikilizie kama itakubaliwa.” Alisema May huku akinyanyuka na kuaga kuwa anaondoka. “Mbona mapema sana Mary kwani unakimbilia nini?” Alisema Irene kwa mashangao kidogo.“Kuna mambo naenda kuyaweka sawa rafiki yangu. Nafikiri tuonane tu kesho mchana ili tuelekee Beach si ndivyo tumekubaliana?” Alisema Mary.
Sawa rafiki yangu Nitajiandaa kisha nitakujibu kama nitakuwa okay hiyo kesho kuhusu kwenda Ufukweni.” Alisema Irene wakati akinyanyuka kitini kwa ajili ya kumsindikiza rafiki yake.“Sawa naomba iwe hivyo ili tukazungumzie mambo yetu huko ninahitaji sana ushauri wako.” Alisema Mary huku akitabasamu.
“Ushauri kuhusu nini? Si nimekuambia kuwa sitashiriki kukushauri ikiwa unataka kupoteza ndoa yako, kwa ajili ya mtu wa ufukweni utajijua mwenyewe!” Wote walicheka na Mary alipanda kwenye gari. Hujajua nataka ushauri gani unarukia tu mambo,” alisema Mary huku akimpungia mkono rafiki yake na kuondoa gari taratibu na baadaye, akatoweka nje ya geti.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Haikuwa hiyari yake kabisa kuingia katika uhusiano huu! Moyo wake ulimuuma kila wakati, kwani hakuwahi kuwa na uhusiano na mwanamke yeyote tangu udogo wake. Sio kwamba alikuwa na tatizo la hasha. Alikuwa anajiepusha sana na mambo hayo ili ajiwekee malengo yake na kufikia ndoto zake. Aliwaona vijana wengi waliopoteza malengo yao, kwa kujihusisha na wanawake. Hakupenda kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi kabla ya ndoa.
Alikutana na vishawishi vingi sana, toka kwa wasichana na wanawake wenye ndoa zao. Wengi wakimsifia kuwa alikuwa na umbo zuri la kimazoezi na sura yake iliwavutia. Lakini kwake hakutoa nafasi ya kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi. Mazoezi na uchapakazi ni vitu vilivyoondoa kabisa hamu ya kujihusisha na mapenzi. mawazo yake aliyaelekeza kwenye ndoto zake za kimaendeleo na alifanya bidii sana ili azifikie ndoto hizo.
Leo ilikuwa tofauti kabisa, kwani ile nadhiri aliyojiwekea ilivunjika tena kwanjiaambayo kamwe hakuitarajia. Ilikuwa ni njia tofauti na ndoto zake. Njia mbaya ya kuingia katika uhusiano na mke wa mtu! Ramson alikuwa akijifikiria jinsi alivyoingia katika uhusiano huo mbaya. Alimfananisha Mrs.Doctor na Delila alivyomrubuni Samson, hata akaanguka katika mikono yake na kupoteza nguvu zake alizopewa na Mungu.
Ushawishi wa Mary juu ya anguko hilo, ulisababisha Ramson ajikute tayari ndani ya uhusiano huo. Uhusiano huu ulikuwa umeshafungua ukurasa mwingine kabisa katika moyo wake. Hakuwa tena na ujanja kila wakati akawa kama mtumwa wa mapenzi, kwani hisia zake zikawa zimetekwa mateka na mwanamke huyo. Lakini kila wakati alifikiria jinsi ya kujinasua kwenye uhusiano huo.
Ilikuwa siku ile aliyofika Mary na Mwenzake aitwaye Irene katika ufukwe huo, ndipo Mary alipomtamkia maneno ya kumtaka wawe na uhusiano wa kimapenzi. Kukataa kwake hakukuwa na nguvu mbele za mwanamke huyo. Alimwahidi kufika ufukweni hapo siku iliyofuata, ili wazungumze vizuri kuhusu hilo. Siku aliyoahidi kuja Mary ilikuwa ni siku ya katikati ya wiki. Kwa kawaida siku hizi huwa wateja hawaji ufukweni hapo na kama watakuja basi ni mmoja mmoja.
Siku aliyosema atakuja ilifika naye akaja. “Unajua Ramson vile nilivyokuambia jana ninamaanisha? Labda tu huelewi kuwa ninakupenda kwa kisi gani.” Alisema Mary kwa sauti ya kushawishi. “Mary hilo sahau kabisa dada yangu. kiukweli maisha yangu nayapenda na sihitaji kuyahatarisha na hatimaye kuyapoteza kijinga kiasi hicho.” Alisema Ramson kwa dhati huku akionyesha msimamo. “Ni hatari gani unayoizungumzia Ramson?” Aliuliza tena Mary.
“Hatari! Hujui kuwa wewe ni mke wa mtu? isitoshe huu sio wakati wake wa mimi kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi. Ninangojea wakati wangu ufike ili nioe na ndipo nitakapoingia rasmi kwenye mambo hayo.” Alisema Ramson. Lakini Mary alifanya kazi kubwa sana ya ubembelezi na kuahidi kuwa itakuwa ni siri kubwa kati yao. na mwisho wake Ramson akaingia kwenye mahusiano hayo.
* * * *
Ilikuwa ni hali ngeni kwake kwani kila wakati alisumbuliwa na kichefu chefu na hali ya uchomvu usio na sababu. vipimo mbalimbali vya kidaktari havikubaini lolote katika mwili wake. Hiyo ni hali mpya kwake naye aliamua kuikubali kuwa ni sehemu ya tatizo lake maana haikutibika. Siku moja asubuhi alimpigia simu rafiki yake Irene: “Halo rafiki yangu nimevumilia kukuambia lakini naona haina maana kukuficha maana unaweza kunisaidia.” Alisema Mary kwa unyonge.
“Una nini rafiki yangu.” Aliuliza Irene kwa mashaka kidogo. “Unajua nina mwezi sasa ninasumbuliwa na kichefuchefu, uchomvu na wakati mwingine ninatapika. Nimekwenda kupima kwa Daktari lakini bado hakujaonekana ugonjwa wowote.” Alisema Mary kwa sauti ya kukata tamaa. “Hiyo inaweza kuwa ni habari njema rafiki yangu ila umakini unahitajika hapo ili usije ukapoteza ndoa yako.
”Alisema Irene kwa uchangamfu. “Unamaanisha nini rafiki yangu? yaani kuumwa kwangu ni habari njema?” Alisema Mary kwa hamaki. “Mary hiyo ni mimba rafiki yangu, amini usiamini na kama bado hujanielewa nenda tena kwa Daktari umwambie akupime ujauzito utakuja kuniambia.” Alisema Irene kwa uhakika.
“Sawa rafiki yangu nitakwenda leo kupima mapema sana kuanzia wakati huu.” Alijibu Mary kisha akakata simu. Hakuchukuwa muda mrefu sana alikwenda kwenye Zahanati iliyokuwepo jirani katika mtaa wao na kumwomba nesi aliyemkuta ampime ujauzito. Majibu yaliyotoka karibu yamtie kichaa kwa furaha. Alifurahi sana kwa sababu aliishi katika ndoa yake kwa muda wa miaka minne bila mafanikio.
Masimango na kejeli za mawifi vilimchosha na kumtia aibu. Kila wakati alijihisi kama alikuwa sio mwanamke aliyekamilika, kwa kukosa mtoto katika ndoa yake. Mume wake mara chache sana alilalamika kuhusu hilo, lakini baadaye alinyamaza kimya na kumtia moyo, kuwa kila kitu kingeenda sawa kwani Mungu ana wakati wake.
Maneno ya mume wake hayakumfanya ajisikie huru kwa kuwa huo ulibaki kuwa ukweli na kilema katika familia. Mawifi nao hawakukoma kupiga vijembe vya masimango kuhusu tatizo lake. Kupata kwake ujauzito kulimfanya ampende zaidi Ramson na kumwona wa maana kuliko mume wake.
Suala hilo lilisababisha ampigie simu kwa haraka baada ya kurudi kutoka kwenye vipimo vyake. Ramson alipokea habari hizo kwa hofu kidogo, akihofia usalama wa maisha yake kwa kuingia katika uhusiano na mke wa mtu. Kwakweli haikuwa habari njema kwake kama ilivyokuwa kwa Mary. Ilimtia mashaka na kuona wazi kuwa tayari maisha yake yamekuwa hatarini. Baada ya kumjulisha Ramson akampigia rafiki yake Irene simu na kumwambia kuwa ameshapima na kwamba tayari yeye ni mjamzito kama alivyotangulia kumwambia. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kweli mwenzangu wewe ni mtaalamu! Vile ulivyoniambia ni kweli kabisa.” Alisema kwa furaha sana Mary. “Sawa rafiki lakini umeshamjulisha mumeo kuwa umepata ujauzito?” Irene alimwuliza kwa shauku. “Hilo nimelisahau mwenzangu, kwa furaha nimeishia kumjulisha Ramson badala ya mume wangu.” Alisema Mary kizembe, baada ya kukumbushwa kuwa ingekuwa bora amwambie mumewe kuwa alimwacha na ujauzito.
“Kumwambia Ramson ni kosa kubwa litakalokugharimu mambo mengi sana.” Alikohoa kidogo Irene kisha akaendelea. “Suala la mimba hakupaswa kuambiwa kabisa huyo jamaa, badala yake ungembambikizia mumeo kwa ajili ya kulinda ndoa yako. Ila hujachelewa bado hebu mpigie mumeo , kwa sababu tangu aondoke mpaka sasa ni miezi miwili tu mjulishe kuhusu hali yako.”Alishauri Irene na kukata simu.
Hii hali ilimchanganya sana baada ya kupewa mbinu hii na rafiki yake. Tayari alishajiona amefanya jambo la kijinga na litakalomgharimu sana, katika kulinda siri hii isivuje na kumfikia mumewe. Jioni ya siku hii ilibidi apige simu kwa mumewe na kumwelezea kuhusu hali yake. “Dear nina jambo la furaha sana nataka kukujulisha” Alisema Mary baada ya kuongea machache na mumewe ya kujuliana hali na maendeleo ya masomo pamoja na biashara baina yao. “Ni jambo gani hilo mke wangu?” Aliuliza Dr. Jackson kwa shauku.
Tangu uondoke nimekuwa nikisumbuliwa sana na kichefu chefu na wakati mwingine ninachoka sana mwili wangu.” Alisema Mary na kutulia kidogo. “Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa habari njema ndio huko kutapika na kuchoka mwili? Acha utani kama hakuna maelezo mengine hebu kapime upate dawa huenda ni malaria.” Alisema Dr. Jackson kwa bashasha. “Kwani mimi sijui habari njema?” Alihamaki Mary.
“Kama ungenisikiliza vizuri ningekujulisha habari yenyewe lakini unaonekana una haraka.” Alisema Mary… kisha akaendelea. “Nilikwenda Hospitali na kupimwa vipimo vyote lakini haikuonekana malaria wala ugonjwa wowote. Nikawa sina la kufanya kwa muda mrefu kidogo. Ila nilivyomjulisha rafiki yangu Irene akanishauri nikapime ujauzito, ndipo vipimo vilipobaini kuwa nina ujauzito wa kama miezi miwili hivi.
Kwa hiyo nina habari njema kuwa hatimae umeniachia ujauzito.” Alisema Mary kwa hamasa. “Woooow!!! unasema kweli mke wangu?” Alisema Dr. Jackson kwa furahakubwa sana. “Ni ukweli kabisa nina ujauzito na hatimaye aibu itakuwa imekwisha ya kuonekana kuwa mimi ni mgumba!”…. “Achana nayo hayo mke wangu hebu tuangalie mambo yetu.
Nafurahi kusikia habari hizo endelea na vipimo kuhusu afya yako na kufuata masharti ya madaktari kuhusu kujitunza na mtoto aliyeko tumboni sawa mke wangu?” Alisema Dr. Jackson.. “Sawa Mume wangu nitafanya hivyo.” Kisha simu ikakatika.
* * *
Mawazo yalikuwa ni mengi sana kiasi cha kumkosesha usingizi. Hakujua kuwa atayakwepa vipi masaibu yaliyo mbele yake. Mawazo yake yalikosa kumpa jibu la kuepuka aibu iliyoko mbele yake. Aliona kuwa hakuwa na budi kutumia mbinu zaidi kusudi kuficha tatizo hilo. Lakini ni mbinu gani?
Hakupata jibu na hili ndilo lililokuwa tatizo lake. Mwishowe akaona atafute tena mawazo kwa rafiki yake. Irene rafiki yake alikuwa na mbinu nyingi. Alimshauri aende kumwona Ramson na kukubaliana kuwa mtoto atakayezaliwa awe wa Jackson mume wake ili kumwepushia tatizo.
Baada ya ushauri huo Mary alienda kumtembelea Ramson na kumwambia kuhusu kuficha siri ile kuhusu mtoto atakayezaliwa. “Unajua Ramson ni kweli tulishirikiana hadi mimi kupata ujauzito huu lakini kumbuka kwako na kwangu litakuwa tatizo. Mimi ni mke wa mtu. Ikiwa itajulikana kuwa mtoto huyo ni wa kwako nitakuwa nimekuweka katika wakati mbaya sana na mimi pia ndoa yangu inaweza isiwepo tena.” Alisema Mary kwa utulivu ili kumvuta Ramson amwelewe.
“Ni kweli kabisa Mary hayo unayoyasema lakini unataka kuniambia itaishia tu kuficha siri hii kwa upande wangu? Utafanyaje ili nisahau kuwa mtoto sio wa kwangu wakati ukweli utakuwa unajulikana kati yetu wawili? Unafikiri nitakuwa mjinga kiasi cha kuona mtoto wangu analelewa na baba mwingine, wakati nikijua kabisa kuwa ni damu yangu? Hebu niambie la kufanya ili ninyamaze Mary.” Alisema Ramson kwa utulivu sana lakini kwa uzito wa hali ya juu.
“Ni sawa Ramson umesema kweli kuwa huwezi kuvumilia juu ya hili lakini kumbuka utaniponza mimi na wewe pia utakuwa hatarini. Kwa hiyo nimeona ni vizuri unifichie siri, kusudi tusiingie katika shida. Wewe unaonaje labda pia naomba unipe mawazo yako.” Alisema Mary kwa mtego akihitaji kusikia kutoka kwa Ramson kuwa angesemaje. “Unajua Mary tangu mwanzo nilikataa kuingia katika uhusiano na wewe! nilijua yanaweza kutokea mambo mabaya sana mbeleni.
Lakini kwa sababu tayari mambo yametokea kama hivi ni vizuri ujue kuwa mimi ni mwanamme. Usidhani kuwa mimi ni mwoga kiasi hicho. Siwezi kuikana damu yangu, kama mtu anaweza kuhiyari kufa kwa ajili ya kuilinda familia yake, kwanini mimi niwe mwoga katika kumpigania mtoto ambaye nina uhakika kuwa ni wangu?” Alisema Ramson kwa ujasiri wa hali ya juu na kuongeza mashaka kwa Mary!
“Ni kweli lakini Ramson utaniingiza kwenye shida na mume wangu. Labda naomba sana uifiche siri hii na mimi nitakupa kiasi cha fedha.” Alisema Mary kwa sauti ya kubembeleza.“Hapo ninaweza kukuelewa Mary, lakini ni kiasi gani utanipa kitakachonifanya nisahau mtoto wangu?” Aliuliza Ramson. “Sema wewe Ramson” Alijibu Mary. “Sawa kwa kukusaidia ili usiachane na mumeo nipatie Shilingi million ishirini najua kwenu hela sio tatizo. Nafanya hivyo kwa sababu sitaki matatizo yakutokee. Alisema Ramson kwa kuonyesha huruma.
“Kama nikikupa kiasi hicho hutaifanya siri hii itoke?” Aliuliza Mary huku uso wake ukionyesha tabasamu. “Siwezi kutoa siri ila ikiwa tu utanipa hela hizo zote.” alisema Ramson kwa uhakika. “Sawa Ramson nitakupatia hela hizo lakini kwa awamu, Kesho nitakuletea nusu yake na Dr. Akirudi nitakupatia nusu nyingine maana kuna hela tuliziweka Fixid Account.
Asante sana kwa kukubali kunifichia siri hii alisema Mary huku akimkumbatia Ramson. “Ila jambo moja ukumbuke.” Alisema Ramson kisha akaendelea. “Mumeo akirudi hicho kiasi cha fedha unipatie mapema sana. Hilo ndio sharti kinyume na hapo nitaghairi makubaliano yetu sawa?” ….”Sawa Ramson nitafanya hivyo.” Alisema Mary. Baada ya mazungumzo hayo Mary na Ramson walipatana kukutana kesho yake nyakati za jioni. Kisha wakaagana na Mary akarudi mjini.
Ulikuwa ni mtihani mwingine ambao ulijitokeza tena katika maisha yake. Hakupenda kukosea ila tayari aliingia katika mtego ambao hakupenda awepo ndani yake. Akili yake ilivurugika alipofikiria kuwa itakuwaje ikiwa Dr. Jackson akigundua kuwa amekuwa na uhusiano wa Kimapenzi na mkewe.
Hakupata nafuu yoyote hata pale alipofikiria kuhusu fedha alizomwambia Mary ampe. Kilikuwa ni kiasi kikubwa sana, lakini hakikutosha kumpa amani kwenye hatia ile. Moyo wake ulikuwa hautulii wakati huo. Lengo lake lilikuwa ni kuuhama mji ikiwa mambo yatagundulika. Fedha ile atakayopewa alikusudia kuiweka Benk Dr. Akirudi, azikusanye kwa pamoja na kuukimbia mji. Hayo ndiyo malengo ya Ramson kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment