Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

SONONEKO - 2

 







    Simulizi : Sononeko

    Sehemu Ya Pili (2)



    ILIPOISHIA



    Sikutaka kabisa kuendelea kuwepo maeneo yale ya sebuleni kwani huenda hali ya hewa ingechafuka na kuzuka balaa kubwa.

    “Namshukuru Mungu kama naye ni mzima wa afya”. Ilinikuta nikiwa mlangoni kuingia chumbani kwetu.



    SASA ENDELEA



    Nikiwa chumbani nilibadilisha nguo haraka haraka na kwenda kujimwagia maji ili kuondoa uchovu pamoja na mawenge niliyokuwa nayo.



    Nilibadili nguo safi na zile chafu nikaziweka katika kapu la nguo chafu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kisha nikaelekea sebuleni ambako alikuwako mke wangu.

    Pale nilimkuta mke wangu amekwishaandaa staftahi tayari na alikuwa akinisubiri mimi tu ili tuweze kujumuika pamoja.



    “Chai hii tamu sana mke wangu hakika wewe ni fundi wa mapishi”. Nilijibaraguza pale kumsifia mke wangu kwa lengo la kuficha madhambi yangu niliyoyatenda usiku uliopita.



    “Ahsante sana mume wangu. Pia kuna jambo moja ambalo nataka kukushirikisha mume wangu”. Aliongea mke wangu huku akinitazama machoni.



    Moyo wangu ulinipasuka paa! Nilihisi mambo huenda yalikuwa yameharibika. Nilidhani kwamba mke wangu alikuwa tayari kashagundua usaliti ambao nilikuwa nimemfanyia. Nilitamani ardhi ipasuke nami nitumbukie na kujificha humo.



    “Jana nilikwenda hospitali kupima baada ya kujiona kwamba afya yangu ni tofauti. Majibu yameonesha kwamba nina ujauzito wa miezi miwili”.



    Sikuyaamini macho yangu na masikio yangu kwa kile ambacho nilikuwa nikikisikia. Ni jambo ambalo nilikuwa nikiliomba kwa muda mrefu sasa kwa mwenyezi Mungu ya kwamba atujaalie kupata mtoto.



    “Waaaaaaoooow! Wasema kweli mke wangu? Dah! Yaani siyaamini masikio yangu. Ahsante sana mke wangu kwa kunipa zawadi hii adhimu. Nakupenda sana mke wangu na nitazidi kukupenda milele”. Niliongea kwa furaha kubwa sana maneno ambayo sidhani kama yalikuwa na ukweli ndani yake kwa sababu kama ningekuwa nampenda mke wangu nisingethubutu kumsaliti hata siku moja.



    Nilisimama kutoka pale nilipokuwa na kumfuata mke wangu. Nilimkumbatia na kumpa mabusu mengi na motomoto ambayo yalimpa wehu mke wangu na niliihisi furaha yake ambayo aliikosa kwa muda mrefu kutoka kwa mume wake.



    Mke wangu Rose alijisikia furaha kubwa sana kwa mapenzi ya dhati kabisa ambayo nilimwonyesha bila kutarajia siku ile kwani ni kwa kipindi kirefu sana sijawahi kumwonesha kwamba namjali.



    “Sasa itabidi nianze kuhudhuria kliniki mume wangu na tunapaswa kuhudhuria pamoja kwa ajili ya maelekezo ya afya ya mama na mtoto na familia kwa ujumla”. Mke wangu aliniambia kwa msisitizo.



    “Wala usijali mke wangu yaani hata kama hiyo kliniki iko ulaya mi nitakupeleka tu. Nakupenda sana mke wangu”. Nilimwambia Rose mke wangu maneno ambayo yalimfurahisha na kuuona uso wake umechanua kwa furaha kubwa sana.



    Tuliendelea kupata kifungua kinywa pamoja pale mezani huku tukibadilishana mawazo kwa vicheko vilivyoambatana na furaha kubwa sana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kumaliza kupata chai mimi nilimuaga mke wangu kwamba nakwenda katika majukumu yangu ya kila siku huku nikimwahidi kwamba nitawahi kurejea baadaye. Mke wangu alinitakia kila la kheri katika mizunguko yangu.



    Siku ile mchana wote niliupitisha kwa Maggie huku tukipeana mahaba tele. Siku hiyo nilimpa penzi moto sana zaidi ya lile ambalo nilimpa usiku wa jana yake.



    Maggie alizidi kuchanganyikiwa nami na kuahidi kwamba hatakuwa radhi kunipoteza kutoka katika mikono yake kwa hali yoyote ile.



    Alasiri ya siku ile nilimuaga Maggie kwamba nilikuwa naenda kunyosha nyosha miguu kwa marafiki zangu hivyo tutakutana kesho.



    “Kwa nini usirudi kuja kula chakula cha usiku honey mbona mimi nitakuwa mpweke mpenzi”. Aliniambia Maggie kwa sauti ya kubembeleza sana iliyokuwa ikitokea puani.



    “Nitakuja kesho mpenzi wangu wala usijali. Nakupenda sana darling”. Nilimwambia maneno hayo huku nikimuaga kwa kumpa busu zito sana ambalo lilimchanganya sana.



    Maggie ilibidi akubaliane na mimi ingawa alikuwa hajaridhika kutoka moyoni kwa mimi kukataa kurudi usiku ule kula chakula pamoja naye.



    Baada ya kutoka kwa Maggie moja kwa moja nilinyoosha kwenda nyumbani. Nilikuwa nina imani kwamba siku ile mke wangu angefurahi sana kwani hakuna siku ambayo nimewahi kurudi nyumbani mapema kama siku ile tena huku nikiwa safi kabisa.



    Pia siku ile nilikuwa sijapata pombe hata kidogo hali ambayo ilikuwa haijawahi kutokea kabisa hata siku moja katika maisha yetu kwani kila siku nilikuwa nikirejea nyumbani nikiwa chapachapa kwa kilevi.



    Kwa kifupi mke wangu alikuwa si mlevi na alikuwa ni mtu ambaye alikuwa akimcha Mungu sana. Yaani nilikuwa na bahati kubwa sana kuwa na mke mwema na bora kama huyu ingawa mimi mwenyewe nilikuwa sijitambui.



    Nilipofika nyumbani nilishangaa sana kwa hali niliyoikuta pale. Mke wangu alikuwa amenuna kweli. Nilimsalimia lakini alinijibu kwa unyonge sana kama mtu ambaye alikuwa ni mgonjwa vile.



    Niliogopa kwa kweli. Nilijua hapa tayari mambo yalikuwa yameharibika. Tumbo lilianza kuniunguruma.



    Nilijipa moyo kwamba litakalokuwa na liwe. Lakini moyoni nilikuwa na hofu sana kwani mwili wangu ulikuwa umejaa sana madhambi ya uzinzi na ulevi kuanzia unyayoni mpaka utosini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliendelea kujibaraguza pale sebuleni kwa kumwongelesha mke wangu lakini hola. Nilishangaa sana. Mbona mke wangu asubuhi nilimwacha katika hali ya furaha kabisa na tukaagana kwa chereko, nderemo na vifijo sasa saa hizi imekuwaje tena.



    Ama kweli Stanley mimi nilikuwa na mtihani mkubwa sana leo hii.

    Lakini mambo haya nilikuwa najitakia mwenyewe hivyo hata sikuilaumu nafsi yangu. Ulikuwa ni ulimbukeni na tamaa zangu za ngono ndizo ambazo zilikuwa zikiipiga dafrao ndoa yangu



    Hali ilizidi kuwa tete pale sebuleni. Mke wangu alikuwa amenuna hasa. Mimi nilikuwa nikishika na kuacha kila kifaa ambacho nilikuwa nikikiona mbele yangu.



    Mara nishike rimoti, mara nijifanye kusoma magazeti, mara nitandike vizuri vitambaa, mara nipige mluzi, mara niimbe yaani ilimradi kujibaraguza tu.



    Mke wangu alikuja pale sebuleni na kuketi katika sofa lililokuwa mkabala na lile ambalo nilikuwa nimekaa mimi. Alinitazama kwa muda wa kama dakika mbili usoni bila ya kuzungumza chochote.



    Hatimaye niliyashuhudia machozi yakimtoka mke mke wangu kutoka katika mboni za macho yake na kuporomoka kupitia katika mashavu yake laini kuelekea kidevuni na kuanguka kifuani mwake.



    Dah! Hali ile ilinihuzunisha kwa kweli na kuipatia nafsi yangu unyonge wenye mashiko. Nilimwonea huruma mke wangu kuwa katika hali ile ya simanzi ambayo alikuwa nayo kwa muda ule.



    Nilitamani nisimame nimfuate na kumkumbatia ili kumfariji lakini nilikuwa na hofu kwamba chanzo cha machozi yake ilikuwa ni mimi kumsaliti. Nilinywea kimya kama kondoo anayesubiri kuchinjwa huku macho yangu yakiona aibu kumtazama mke wangu kipenzi.



    “Stanley mume wangu, hivi unafahamu ya kwamba mimi ninakupenda sana kuliko wanaume wote hapa duniani?”. Mke wangu aliniuliza swali ambalo lilinishtua kidogo.



    Kwa mwanaume wa kawaida swali hili lilikuwa ni swali la kawaida sana lakini kwangu mimi ambaye nimezoea uzinzi na kutoka nje ya ndoa yangu lilikuwa ni swali lenye maana kubwa sana.



    “Ndiyo nafahamu mke wangu kwani hilo liko wazi kabisa”. Nilijikakamua kujibu kwa upole huku nikiwa nimenywea kwani nilikuwa ninafahamu kuwa mambo yalikuwa yamekwisha haribika.



    “Sasa naomba unieleze kwa dhati toka moyoni mwako jana ulilala wapi?” Mke wangu Rose aliongea huku akiwa amenikazia macho.

    Mungu wangu! Mambo yalikuwa yamekwishaharibika. Tumbo langu lilianza kuunguruma tena sasa sifahamu lilikuwa ni tumbo la uharo au ilikuwa ni hofu. Halafu kwa mbali nilianza kuhisi kama kizunguzungu hivi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Pia nilianza kuihisi baridi wakati kulikuwa na joto kali sana la kutumia feni kabisa. Hakika nilikuwa katika kimuhemuhe.



    “Si nilikwambia kwamba ninalala kwa rafiki yangu Morris kwa sababu ya kuzuiwa na ile mvua kubwa ya jana usiku!” Nilijaribu kumjibu mke wangu huku sauti yangu ikiwa na uoga ndani yake.



    Unajua unapokuwa umekosa, ni lazima mtu unakosa ujasiri kabisa. Hata kama ni mwanaume wa shoka ni lazima utanywea tu ila utajitutumua tu lakini mh!



    “Sasa mbona nguo zako zina harufu ya manukato ya kike?” Mke wangu alinitandika swali ambalo lilinipa kiwewe kidogo na kunifanya nikose jibu kwa muda kidogo.



    “Unajua…. Unajua……. Unajua asubuhi nilipanda daladala …… ah! Hapana nilimpa lifti mwanamke ambaye alikuwa amejipulizia manukato hayo”. Mh! nilijigonga kwa kweli kwani mimi huwa sipandi daladala nina usafiri wangu binafsi na ndio gari niliyokuja nayo asubuhi.



    “Sawasawa mume wangu nakubaliana kabisa na wewe. Sasa je, na ile nguo ya ndani ya kike uliyokuwa umeivaa imetoka wapi?”. Mke wangu alinipachika swali jingine la moto.



    Duh! lilikuwa ni swali lililonipandisha presha yangu. Kizunguzungu kilizidi na sikuelewa nitajibu vipi ili nieleweke.

    *****************





    Yaani penzi la Maggie jana lilinipagawisha hata asubuhi nilipokuwa nikivaa nguo kumbe badala ya kuvaa chupi yangu niikuparamia “mkwego” wa Maggie bila kutambua na kuutundika mwilini mwangu.



    Hata asubuhi kwa sababu ya kihoro nilichokuwa nacho sikuwa makini kujikagua mavazi yangu. Dah! Bonge la faulo.



    “Unajua mke wangu …….. unaju…… unajuua…..yah!.... you know ….. unajua nilikuwa nataka nikufanyie surprise. Niliinunua ile nguo ili nije nikukabidhi kwa mtindo wa pekee nikiwa nimeivaa. Ni surprise tu mke wangu”. Nilijigongagonga pale huku nikitoa maelezo ambayo yalikuwa hayaeleweki kabisa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ok, nimekuelewa mume wangu mpenzi, sasa mbona chupi yenyewe ilikuwa imetumika kabisa. Je, hapo utaniambia nini?”. Rose mke wangu aliniuliza kwa sauti yake ileile yenye upole uliotukuka.



    “Nili…. Nili….. nilitaka …….. nilikuwa…….!” Midomo yangu iligoma kabisa kupatana na kuunda uongo ambao ningeweza angalau kumfanya mke wangu aweze kuniamini hata kidogo tu.



    “Pole mume wangu najua unapata shida sana namna ya kunijibu swali hili lakini mimi ni mtu mzima naelewa kila kitu. Wewe ndio baba wa nyumba mimi sina lolote la kusema mume wangu”. Mke wangu aliongea maneno ambayo yalinichoma moyo na kunifanya mtu mzima niporomokwe na machozi.



    Baada ya maneno hayo mke wangu alisimama huku akilia kwa uchungu na kuelekea chumbani kwake. Alijitupa juu ya kitanda huku akilia sana.



    Nilimfahamu vyema Rose mke wangu. Anapokuwa katika hali ile haikupaswa kumsemesha chochote. Alitakiwa aachwe hivyohivyo alie weeeee! Ndipo hasira zake hupungua na huamua kusamehe yote.



    Lakini la safari hii lilikuwa kubwa sana la kurudi na “mkwego” wa kike nyumbani dah! Stanley mimi nilikuwa hatari sana.



    Nilisimama kutoka pale sofani na kutoka nje. Nililifuata gari langu la kifahari aina ya “Toyota surf” na kuliwasha. Kwa mwendo wa kasi nilipotea kutoka maeneo yale ya nyumbani kwangu.

    Kwa upande wa wakati ilikuwa ni majira ya saa moja na dakika kumi na mbili jioni.



    Niliikamata barabara kuu ya Tunguhza ambayo ilinichukua mpaka katika mtaa wa Mateku. Katika mtaa huu palikuwa na baa moja maarufu sana ambayo mimi huipenda sana. Baa hii ilikuwa ikiitwa “Highway Bar”.



    “Mariam mambo vipi?” Hebu nipatie “Le grande Cologne” tano hapo mezani fasta fasta”. Nilimwambia muhudumu yule wa baa ile ambaye nilikuwa nimezoeana naye kwani hapo awali nilikwishafanya naye ngono mara kadhaa na hata ninapokuwa na hamu ya mwanamke mara nyingi huwa nazini na huyu dada mrembo wa hapa baa.



    “He! Bosi Stanley kulikoni tena mbona hivi. Hujanywa siku saba nini?” Aliuliza Mariam kwa mshangao na kwa utani kwani “Le grande Cologne” ni pombe ya kifaransa ambayo ilikuwa ni kali sana na yenye kilevi asilimia tisa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Acha longolongo zako wewe, lete pombe hapa au wataka nikupe mambo nini?” Nami nilimchombeza kwa maneno ya bashasha kwani Mariam alikuwa ni mtani wangu.



    “He he he he he! Unalo babuuuuuu! Hapa leo hupati kitu”. Aliongea Mariam kwa mbwembwe huku akiniletea vinywaji nilivyoviagiza katika ile meza niliyomwelekeza.



    “Haya kaa hapo mwanamke kula pombe toka kwa mpenzi wako wa nguvu Stanley”. Nilimwambia Mariam ambaye alikuwa tayari amekaa hata kabla ya kukaribishwa kwani alikuwa akiufahamu utaratibu mzima.



    “Eenh! Nipe maneno darling, mbona leo uko tofauti kabisa kulikoni”. Alihoji Mariam baada ya kunigundua kwamba siku ile nilikuwa tofauti kabisa toka muda ule nilipokuwa nimeingia pale baa.



    “Dah! Eeh bwana mwenzio leo nimelikoroga kweli na natamani hata dunia ipasuke na mimi nijitumbukize ndani yake ili nijifiche”. Nilianza kumweleza Mariam ambaye licha ya kuwa ni mpenzi wangu lakini pia alikuwa ni rafiki yangu mkubwa sana.



    “Imekuwaje tena? Mbona wanitisha mwana wa mwenzio?” Alihoji Mariam huku akiionesha dhahiri hofu ambayo alikuwa nayo.



    “Tulia mwanamke nikupe mkanda mzima. Basi si nilipata mwanamke mmoja kwa ajili ya kupooza hamu……” Mara Mariam alinikatisha.



    “Hebu ishia hapo hapo, wewe si nilikwishakukataza habari za kuzoazoa wanawake. Hivi unafikiri kwamba mimi siumii kwa matendo yako hayo ya kuchukua wanawake hovyo. Mi nakupenda sana na nahitaji uwe na mimi pekee. Naumia unapotoka na wanawake wengine”. Aliongea Mariam akioonesha dhahiri alimaanisha kile alichokioongea.



    “Sawa lakini mimi si nilikwishakwambia toka awali kwamba siku nikiwa na hamu ya haya mambo na wewe ukiwa mbali ni lazima nitachukua mwanamke mwingine. Halafu pia wewe si unafahamu ya kwamba mimi nimeoa. Sasa je, kwani mke wangu naye haumii mimi ninapotoka na wewe?”. Niliongea maneno ambayo yalimchoma sana Mariam.



    “Haya bwana we endelea tu kuniumiza. Hivyo si ndivyo ambavyo unapenda. Haya hebu endelea kunisimulia huo upuuzi wako”. Mariam aliongea hukua akionesha wazi alikuwa amekereka kwa mimi kutembea na mwanamke mwingine zaidi ya mke wangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo hivyo bwana. Baada ya mambo yetu haya si nikarudi asubuhi nyumbani. Sikujikagua kumbe nilikuwa nimevaa nguo ya ndani ya yule binti niliyekuwa naye. Moto uliowaka huko nyumbani nashindwa hata namna ya kuuzima”. Nilimwambia Mariam huku nikiwa naendelea kuzibugia zile pombe mithili ya buge.



    “Pole bwana lakini mambo haya unajitakia mwenyewe. Mtindo wako wa kuzoazoa wanawake ndio ambao unakusababishia matatizo hayo”. Mariam aliongea maneno ambayo yalikuwa na mantiki ndani yake lakini alisahau kuwa hata yeye pia alikuwa ni miongoni mwa hao wanawake ambao nilikuwa nikiwazoazoa.



    Tuliendelea kula pombe mpaka zikatufahamu kuwa sisi ni akina nani. Mariam naye katika kubugia pombe alikuwa ni mtaalamu sana.



    Na hilo ndilo ambalo nilimpendea kwani mara nyingi alikuwa akinipa kampani ya kutosha si unajua utamu wa pombe ni sharti muwe wengi.



    Kuna kipindi fulani Mariam alilazimika kusimama na kuniacha pale mezani peke yangu kwani alikwenda kuhudumia wateja wengine. Alipowahudumia alirudi na kuendelea kujumuika nami katika kuzitandika pombe.



    Siku ile nilizinywa pombe kupita kiasi. Utashi na akili zangu vilihama kabisa na nikawa sijitambui. Mariam kidogo ndo alikuwa msaada kwani yeye hakulewa sana kama mimi kwa sababu yeye alikuwa ni muhudumu na alitakiwa aendelee kuwa na ufahamu kwa lengo la kuifanya kazi yake vyema bila ya dosari.

    *******************

    Yalikuwa ni majira ya asubuhi ya saa nne ndipo ambapo nilizinduka kutoka katika usingizi mzito sana. Kichwa kilikuwa kikinigonga sana kutoka na pombe ambazo nilikuwa nimezipiga usiku wa kuamkia leo.



    Mwanga mkali wa jua ulikuwa ukiingia kupitia madirisha makubwa ya chumba cha kulala ambacho kwa wakati ule kilikuwa kimefunguliwa mapazia na kuingiza hewa safi pamoja na nuru ya kutosha sana ambayo ilileta burudani safi.



    Mke wangu alikuwa anapenda kuyatunza mazingira ya nyumba yetu kikiwemo chumba chetu cha kulala katika hali ya usafi na unadhifu mkubwa sana. Nyumba yetu muda wote ilikuwa inapendeza na kuvutia sana.



    Sikuelewa nilifikaje mle chumbani kwani kumbukumbu zangu zilinikumbusha kwamba kwa kudra za mwenyezi Mungu nilifanikiwa kuliendesha gari kutoka baa na kufika salama nyumbani ingawa humo njiani nilinusurika kuwagonga watu wasio na idadi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Pia nilikwishanusurika kama mara tano kugongana na magari mengine na pia niliponea chupuchupu kuzivaa nguzo za taa za barabarani.



    Nilipofika katika geti la kuingilia nyumbani kwangu nikaona nisiwasumbue waliokuwa wamelala ndani kwa kupiga honi bali nishuke na kulifungua mimi mwenyewe kwani funguo za geti hata mimi nilikuwa nazo.



    Niliposhuka chini kutoka garini, nilikula mweleka mmoja matata ulionifanya nidondoke chini na kutapika kiasi fulani cha pombe ambayo nilikuwa nimeibugia. Baada ya hapo nilipoteza fahamu.



    Nilijitazama mwilini. Nilishangaa baada ya kujikuta nipo katika mavazi ya kulalia huku mwili wangu ukionekana nadhifu ikimaanisha nilikuwa nimeoga. Mh! Haya yalikuwa makubwa tena.



    Niligeuza kichwa changu na kutazama upande wa pili wa chumba ambapo nilimwona mke wangu akiwa amejikunyata huku akiwa ameukumbatia mdoli mmoja mkubwa ambao nilimnunulia zamani sana kama zawadi katika kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa.

    Machozi yalikuwa yakimporomoka huku akilia taratibu kwa kwikwi ndogondogo.



    “Pole sana mume wangu, wajisikiaje sasa?”. Mke wangu aliniuliza swali ambalo lilitia aibu na kunifanya nimshangae sana mwanamke huyu. Hivi alikuwa ni mwanamke wa namna gani huyu?.



    Licha ya madhambi, mateso na kila aina ya ubaya niliomfanyia lakini bado alikuwa na huruma nami Stanley mwanaume mwenye roho mbaya iumizayo wanawake.



    Kwa kweli niliumia sana moyoni kwa mapenzi ya dhati ambayo mke wangu alikuwa nayo juu yangu lakini mimi nikiwa na akili zangu timamu kabisa nilikuwa nikijitahidi kuyabomoa.



    Kweli wanawake wameumbwa tofauti kabisa na ni watu wavumilivu sana na wenye mapendo ya dhati kwa wenza wao.

    Niliona hata aibu kumjibu mke wangu maana nafsi yangu ilikuwa ikinisuta ndani yangu. Ni kweli nafsi ilinisuta hasa.



    Bila kutarajia nilijiona nikiporomokwa na machozi ya uchungu kutoka moyoni mwangu. Nilijilaani kwa nini nilikuwa nikimwumiza mwanamke huyu wa pekee ambaye alikuwa na mapenzi ya dhati juu yangu.



    Je, hivi yeye aliumbwa kuipata tabu hii ambayo alikuwa akiipata. Hivi hakustahili kuipata furaha katika maisha yake. Je, ni nani wa kuisababisha furaha katika maisha yake?

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakika nilikuwa ni mimi. Mwanaume ambaye nilikuwa sijui kupenda ninapopendwa wala kumjali mtu anayenipenda na kunijali.

    ***************



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog