Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

A LIVING DREAM ( NDOTO INAYOISHI ) - 3

 







    Simulizi : A Living Dream ( Ndoto Inayoishi )

    Sehemu Ya Tatu (3)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Luciana hakuonekana kuwa na raha, alikuwa mwenye huzuni mno. Mawazo juu ya Patrick yalikiumiza kichwa chake. Kuna wakati alikuwa akijutia kile alichokuwa amekifanya lakini pia kuna kipindi kingine alikuwa akijiona kufanya kitu sahihi kwa kuwa aliusikiliza moyo wake na hata uwepo wa Emmanuel ulimpa faraja tele.

    Kumbukumbu mbaya za maisha yaliyopita ndizo zilizomuumiza zaidi, alikumbuka siku zote ambazo alitumia pamoja na Patrick kuwasiliana na hata zile siku walizokuwa wakikutania chini ya mbuyu kule Bagamoyo na kuzungumza mengi huku wakiwekeana ahadi kwamba wasingeweza kuachana milele.

    Hilo ndilo lililomnyima raha kabisa, kitendo cha kukumbuka kwamba walisimama chini ya mbuyu, wakachanana vidole vyao na kila mmoja kulamba damu ya mwenzake, kilimuumiza moyo wake.

    “Kwa nini nilifanya ujinga ule? Kwa nini nilikuwa na akili za kitoto?” alijiuliza Luciana pasipo kupata jibu lolote lile.

    Hakutaka kujali tena, kwa sababu kila kitu kilichopita, kilipita, aliona ni bora kama angeendelea na maisha yake kama kawaida.

    Hakupunguza ukaribu wake na Emmanuel, japokuwa muda mwingi hakuwa na raha lakini akajitahidi kumuonyeshea Emmanuel unafiki wa furaha ingawa moyo wake ulikuwa tofauti kabisa.

    Siku zikaendelea kukatika mpaka siku za kufanya mitihani ya Taifa ya Kidato cha Sita kukaribia. Kwa sababu alikuwa amejiandaa vya kutosha, aliamini kwamba angeweza kufaulu vizuri na kuanza na masomo ya chuo.

    “Nakutakia mafanikio mema, natumaini utafaulu tu, wewe kichwa sana,” alisema Emmanuel.

    “Asante mpenzi. Hata mimi nakutakia mafanikio mema pia, una akili sana mpenzi,” alisema Luciana.

    Siku ya mitihani zikafika na wanafunzi kukusanyika madarasani mwao. Kwa Luciana, bado kichwa chake kiliendelea kumuuma, hakuamini kama kwa kipindi kirefu vile mawazo juu ya Patrick yangeendelea kumtesa kiasi kwamba hakujisikia furaha katika mahusiano aliyokuwa nayo.

    Wanafunzi wote walikuwa wametulia kimya darasani na mwalimu aliyetakiwa kulisimamia darasa hilo ndiye aliyekuwa akitoa maelezo juu ya nini kilitakiwa kufanyika. Huku maelezo hayo yakiendelea, hakuna mtu aliyejua nini kilitokea, ghafla, Luciana akasimama na kuanza kuisukumasukuma meza iliyokuwa mbele yake huku akianza kuzitimua nywele zake alizokuwa amezichana vizuri.

    “Vipi tena?” aliuliza msimamizi huyo.

    Wanafunzi wote wakashtuka, hali aliyokuwa nayo Luciana, tena iliyomtokea ghafla, dakika chache kabla ya kuanza mitihani yake ilimpa hofu kila mmoja.

    Hali ya kusukumasukuma meza na kuzitibuatibua nywele zake iliendelea zaidi mpaka kufikia hatua ya kuanza kuongea peke yake.

    “Nini kinaendelea?” aliuliza mwalimu wa shule hiyo, alisikia kelele darasani humo na kuamua kwenda, alipofika, hata yeye alionekana kushangaa juu ya kile kilichokuwa kikiendelea.

    “Hatufahamu! Ameanza kupiga kelele ghafla,” alijibu msimamizi wa mtihani.

    Hicho ndicho kilichotokea, Luciana akaanza kuwa kichaa ambaye baada ya dakika kadhaa, akaanza kuvua nguo zake. Wanafunzi waliokuwa darasani humo, wavulana wenye nguvu wakamsogelea na kumshika vilivyo, wakamtoa nje ambapo wanafunzi wa kidato cha tano wakamchukua na kumuingiza katika gari la mwalimu mkuu na kuanza kumpeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo haikuwa mbali kutoka hapo.

    “Daaah! Demu mkali, cheki, amekuwa kichaa,” alisema mwanafunzi mmoja aliyekuwa garini, Luciana alikuwa akiongea peke yake huku udenda ukimtoka.

    “Kweli uchawi noma, mtu kawa kichaa siku ya pepa, kweli hii kali aiseee. Oya Juma, mshike vizuri miguu, asije akakushinda nguvu akajirusha nje ya gari,” alisema mwanafunzi mwingine.

    Walipofika hospitalini, Luciana akapokelewa na madaktari ambao wakamchukua na kumpeleka katika chumba kimoja, huko, wakamlaza kitandani na kumfunga kwa kamba ngumu.

    Pale kitandani, Luciana hakutulia, bado alitamani kujiondoa na kuondoka zake. Hali ilionekana kumsikitisha kila mtu, msichana mrembo, leo hii alibadilika na kuwa kichaa, ilikuwa ni stori iliyovuma katika sehemu zote hasa kwenye ukanda huo wa mjini.

    ****

    Mara baada ya kupata taarifa kwamba mpenzi wake alikuwa amechanganyikiwa na kuwa kichaa, Emmanuel akapatwa na mshtuko mkubwa, hakuamini kile alichokuwa amekisikia kwamba kipenzi cha moyo wake, alikuwa kichaa, dakika chache kabla ya kuanza mtihani wa kumaliza kidato cha sita.

    Mtihani wa kwanza ulipomalizika, harakaharaka akaenda hospitalini hapo, alipofika, akaomba kumuona Luciana, kwa kuwa ulikuwa muda wa kuwaona wagonjwa, akaruhusiwa kuingia katika chumba kile.

    Kile alichokuwa amekisikia ndicho alichokuwa akikiona chumbani mule, Luciana alikuwa amefungwa kamba kitandani pale, japokuwa alikuwa akihangaika kutaka kujinasua kutoka kitandani pale lakini akashindwa kabisa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Wazazi wake walikuwa pembeni yake, mama yake, bi Asteria alikuwa akilia tu, hakuamini kama binti yake alikuwa amechanganyikiwa na kuwa kichaa kwa asilimia mia moja.

    Luciana, msichana mrembo, aliyesifika kwa uzuri na upole, leo hii, alibadilika kabisa na kuwa msichana mwenye nywele timtim huku kila wakati udenda ukimtoka na kuongea peke yake.

    “Luciana....” alijikuta akiita Emmanuel.

    Alishindwa kuvumilia kabisa, akajikuta akianza kububujikwa na machozi, kila kilichokuwa kikiendelea kilionekana kuwa kama moja ya ndoto mbaya na ya kusisimua mno.

    Hali ya Luciana haikubadilika, na kadiri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo aliendelea kubadilika na kuchanganyikiwa zaidi. Akawekwa katika chumba kimoja kikubwa cha watu waliokuwa wamechanganyikiwa na akili.

    Kila siku, Emmanuel alikuwa na jukumu kubwa la kumtembelea hospitalini pale na kumwangalia. Alisikitika, alihuzunika mno lakini hali iliyokuwa ikiendelea haikuweza kubadilika.

    Mawazo yakamsonga Emmanuel, akajikuta akianza kupoteza hamu ya kula, akawa mtu wa mawazo mno huku wakati mwingine akijikalia chumbani na kuanza kulia kama mtoto mdogo.

    Mpaka matokeo yanatoka na kufaulu mtihani wa taifa na kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, bado Luciana hakupata nafuu, aliendelea kuwa kichaa kitu kilichoonekana kwamba angeendelea kubaki hivyo mpaka atakapokufa.

    Wasichana wengi chuoni walimpenda Emmanuel, upole wake ulikuwa kivutio kwa wasichana hao. Sura yake ya kitoto ambayo ilipendezeshwa na vishimo viwili mashavuni kila alipokuwa akitabasamu, vikawaacha wasichana hoi.

    Hawakutaka kulaza damu, kuwa na Emmanuel kilikuwa moja ya vitu vitu vilivyowasumbua wasichana wengi chuoni hapo, hivyo kila mmoja alikuwa na muda wake wa kwenda kumshawishi Emmanuel ambaye alionekana kuwa mgumu hasa kutekeka kimapenzi.

    “Tatizo nini Emmanuel?” aliuliza Juke, miongoni mwa wasichana waliokuwa wakitikisa kipindi hicho.

    “Juke! Naomba uniache, sipo sawa kabisa,” alisema Emmanuel.

    “Tatizo nini? Niambie labda naweza kukusaidia!”

    “Haiwezekani! Wewe niache tu.”

    Baada ya siku kadhaa, watu wakafahamu kile kilichokuwa kimetokea, sababu kubwa ya Emmanuel kuwakataa wanawake wazuri ni kwa sababu alikuwa na mpenzi wake ambaye alipatwa na ukichaa wakati akijiandaa kufanya mtihani wa taifa.

    “Pole sana kaka, nimesikia kile kilichotokea,” alisema mwanachuo mmoja.

    “Kipi?”

    “Kuhusu shemeji! Kweli kuna binadamu wana roho mbaya,” alisema mwanachuo huyo.

    Kila siku Emmanuel alikuwa akienda katika hospitali hiyo ya Taifa kwa ajili ya kumuona mpenzi wake tu. Kila alipofika, alikwenda katika eneo la wodi ile ya vichaa na kuwekwa sehemu ambayo ingekuwa rahisi kwake kumwangalia mpenzi wake.

    Kila alipokuwa akimwangalia Luciana, alijisikia kuwa na maumivu makali moyoni mwake, hakuamini kama mwisho wa kila kitu ungekuwa namna ile. Alimpenda sana na kumthamini, kitendo cha kuwa kichaa kilimaanisha kwamba asingeweza kumuoa, yaani ndoto zote ambazo alimwambia kipindi cha nyuma zingebaki na kuwa historia tu.

    “Luciana, nini kilitokea mpenzi?” aliuliza Emmanuel huku akibubujikwa na machozi.

    Luciana hakuonyesha mabadiliko yoyote yale, mpaka Emmanuel anamaliza mwaka wa tatu chuoni hapo, bado mpenzi wake aliendelea kuwa kichaa vilevile. Japokuwa bado msichana yule aliendelea kubaki katika hali ile, kitu cha ajabu ni kwamba Emmanuel hakutaka kumuoa msichana yeyote yule, kila alipokuwa akishauriwa amuoe msichana yeyote na aachane na yule Luciana kichaa, alikataa katakata kwa kuamini kwamba ingetokea siku ambayo msichana huyo angepona na kuwa mzima kabisa.

    “Kuna siku atapona tu Esta, niamini hilo,” alisema Emmanuel.

    “Amekaa kwa miaka mingapi?”

    “Kama minne hivi.”

    “Basi amini hawezi kupona. Emmanuel, utampendaje kichaa?” aliuliza Esta, mmoja wa wasichana waliokuwa wakimsumbua mno.

    “Naomba usiniingilie, naomba usimseme Luciana, tutagombana,” alisema Emmanuel.

    “Mmmh! Sawa. Ila ninakuhitaji Emmanuel, ninahitaji kuwa na wewe,” alisema Esta.



    Alionekana kichaa, hakuwa na ufahamu wa kitu chochote kilichopita lakini kwa Emmanuel bado alimpenda msichana huyo. Moyo wake ulitekwa vilivyo, hakutaka kusikia lolote lile, mapenzi yake ya dhati bado yalikuwa kwa Luciana tu.

    Kila siku katika maisha yake aliamini kwamba msichana huyo angeweza kupona lakini hilo halikuweza kutokea. Mpaka mwaka wa tano unaingia, bado Luciana aliendelea kuwa kichaa vilevile, tena wakati huu akiwa amevurugwa kabisa, mbaya zaidi, hata mwili wake ulikuwa umepungua mno, alionekana kama mtu aliyekuwa akiugua ugonjwa wa UKIMWI, mwili wake ulikongoroka kwa kiasi kikubwa kutokana na kutokula mara kwa mara.

    Bado wanawake waliendelea kumshangaa Emmanuel, alionekana kuwa na moyo wa ajabu mno. Kitendo chake cha kuwakataa na kuamua kuwa na kichaa yule kiliwashangaza mno.

    Mapenzi mazito aliyokuwa nayo kwa Luciana, yakawafanya watu kuona kwamba hata naye alikaribia kuwa kichaa. Alifanikiwa maishani mwake, alikuwa na kazi nzuri, alijiendeleza katika biashara zake huku karatasi zote za umiliki wa biashara zake zikionyesha kwamba alikuwa akichangia na Luciana.

    “Kumbe umeoa hata kuambiana kaka,” alisema mfanyabiashara mwenzake, Joakim.

    “Hapana! Sijaona. Yaani nioe wewe usijue!”

    “Hahaha! Hebu acha utani, na huyu Luciana ni nani?”

    “Msichana wangu.”

    “Yupo wapi sasa? Mbona hujawahi kunionyesha? Au unataka nikutane naye mtaani nimrukie?” aliuliza Joakim huku akicheka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Hahaha! Hakuna bwana, kuna siku utamjua tu.”

    “Sawa. Ila fanya mishe kaka, umri unakwenda tu, au unataka mtoto wako akuite babu?”

    “Hapana. Usijali, nitaoa tu.”

    Hicho ndicho kilichokuwa kikimuumiza kichwa Emmanuel. Ni kweli alitamani sana kuoa lakini suala kubwa ambalo lilimchanganya ni kitendo cha Luciana kuwa kichaa. Hakuwa radhi kuona akimuoa msichana mwingine, mtu pekee aliyekuwa akimpenda alikuwa Luciana tu.

    Alivumilia mno na miaka iliendelea kukatika lakini hakuwa tayari kuona akiingia katika mahusiano ya kimapenzi na msichana mwingine zaidi ya kichaa huyo.

    “Nitamuoa hata kichaa, kweli tena, ngoja nianze kufanya mishemishe, hata kama kichaa, nitamuoa tu,” alisema Emmanuel.

    Hakutaka kuficha hilo, alichokifanya ni kuwaambia wazazi wake kwamba uamuzi aliokuwa ameufikia ni kufunga ndoa na Luciana tu kwa kuwa hakumuona msichana mwingine ambaye alistahili kuwa mke wake zaidi ya huyo.

    “Umechanganyikiwa?” aliuliza mama yake huku akionekana kushtuka.

    “Hapana mama, ni maamuzi tu.”

    “Haiwezekani, utakuwa umechanganyikiwa tu.”

    Hakutaka kuambiwa kitu chochote kile, moyo wake ulikuwa kwenye bwawa la mahaba kwa Luciana. Alichokifanya ni kuwafuata wazazi wa Luciana na kuwaambia ukweli kile alichokuwa amekifikiria, wazazi hao wakapigwa na butwaa, hawakuyaamini maneno ya Emmanuel kwamba alitaka kumuoa binti yao hata kama alikuwa kichaa.

    ****

    Huo ndiyo uamuzi aliokuwa ameufikia na hakutaka kushauriwa na mtu yeyote yule. Alimpenda Luciana na hakutaka kusikia lolote lile zaidi ya kumuoa na kuwa mke wake wa ndoa.

    Alionekana kuchanganyikiwa lakini yeye mwenyewe alijiamini kwamba alikuwa na akili timamu na hata uamuzi aliokuwa ameufikia, ulitoka moyoni mwake na wala hakushinikizwa na mtu yeyote yule.

    “Emmanuel...unasema unataka kumuoa Luciana?” aliuliza mama yake, japokuwa alikuwa amekwishawaambia lakini hawakutaka kuamini hata kidogo.

    “Ndiyo mama, ninataka kumuoa.”

    “Hapana. Hebu kwanza nenda ukajifikirie vizuri.”

    “Nimekwishajifikiria mama. Ninataka kumuoa Luciana,” alisema Emmanuel.

    Mama yake hakutaka kukubali, alikwishaona kwamba mtoto wake alimaanisha kile alichokuwa amekisema na hivyo alihitaji nguvu za ndugu zake ili waweze kuzungumza na Emmanuel na kumshuri kwamba hakutakiwa kufanya kile alichotaka kukifanya.

    Ndugu waliposikia uamuzi wa Emmanuel, kila mmoja akamshangaa, alionekana kwamba ni msomi aliyefanya vizuri chuoni kwao lakini kitendo cha kutaka kumuoa kichaa, kilimshangaza kila mmoja.

    Walichokifanya, wakamuita kikao, wajomba, mashangazi zake na ndugu wengine walikuwa wamemzunguka, waliongea naye huku wakimwambia madhara ambayo yangeweza kutokea lakini kwa Emmanuel, hakutaka kukubali, bado uamuzi wake ulikuwa uleule kwamba alidhamiria kumuoa msichana Luciana.

    “Emmanuel....upo sawa kweli?” aliuliza shangazi yake.

    “Nipo sawa shangazi, ninataka kumuoa Luciana.”

    “Luciana! Huyuhuyu kichaa?”

    “Ndiyo shangazi. Siwezi kumuacha Luciana. Mnajua ni jinsi gani ninampenda, mnajua ni wapi tulipotoka, tuko shuleni, leo hii ni mwaka wa tano, siwezi kumuacha, ninachoamini ni kwamba kuna siku atarudi katika hali yake ya kawaida,” alisema Emmanuel huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikiongea, hakutaka kupata ushauri mwingine wowote ule, alichokuwa akikitaka ni kumuoa Luciana tu.

    “Atarudi katika hali yake lini? Amekwishakuwa kichaa, hawezi kurudi Emmanuel, ushauri wangu kama shangazi yako, achana naye, wewe panga mambo yako na usimwangalie yeye tena,” alisema shangazi yake.

    “Hapana. Huu ni uamuzi wangu na sitaki ushauri tena, cha msingi, jiandaeni na harusi, ipo karibu na ishaanza kunukia,” alisema Emmanuel, hakuonekana hata kuwa na chembe ya utani.

    Japokuwa walizungumza naye mambo mengi lakini hawakuweza kuubadilisha uamuzi wake, msimamo wake ulibaki kuwa uleule kwamba alitaka kumuoa msichana huyo ambaye alikuwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiugua ugonjwa wa kichaa.

    Alichokifanya Emmanuel ni kusafiri kwa mara nyingine tena kuelekea Bagamoyo ambapo huko akakutana na wazazi wa Luciana na kuendelea kuwasisitizia kwamba mchakato wake wa kutaka kumuoa binti yao bado ulikuwa ukiendelea kama kawaida.

    “Nimekuja kuwaambia kwamba mpango wangu unaendelea, nimekwishazungumza na wazazi wangu, ndugu, wote wamekubaliana nami,” alisema Emmanuel.

    “Wamekubaliana nawe? Una uhakika?” aliuliza baba Luciana.

    “Ndiyo. Kinachosubiriwa ni harusi tu.”

    “Sawa. Umepanga kufunga ndoa lini?”

    “Hata mwezi ujayo. Kwa sababu tunapendana, hakuna tatizo,” alisema Emmanuel.

    Alivyokuwa akizungumza, ilionekana kama mwanamke aliyetaka awe mke wake alikuwa mzima wa afya njema, hakuonekana kuwa na tatizo lolote lile. Msimamo wake mkali ndiyo uliowashangaza watu wote kwamba ilikuwaje atamani kumuoa Luciana, msichana kichaa na aachane na wasichana wengine, tena wazima wa afya waliotaka kuwa naye?

    Emmanuel hakutaka kusikiliza neno la mtu yeyote yule, tena alipoona kwamba watu wengi walikuwa wakimpigia simu na kumfuata nyumbani huku wakimshauri kwamba hakutakiwa kumuona Luciana, akaamua kuzima simu na kuhamia hotelini.

    Huko, bado mawazo yake yalikuwa kwa msichana huyo, alikumbuka namna walivyopendana na kufanya mambo mengi yaliyoyaamsha mapenzi yao na kupendana zaidi. Picha za Luciana alizokuwa nazo simuni mwake ndizo zikawa faraja kubwa kwake, kila wakati alikuwa akiziangalia kitu kilichomfanya kuona furaha moyoni mwake.

    Mpaka kufikia hatua hiyo, tayari alikwishawaandaa marafiki zake kwenye kamati ya harusi, watu waliotakiwa kufuatilia kila kitu kikiwepo ukumbi, mavazi, chakula na vitu vingine.

    Hakutaka kumshirikisha mtu yeyote katika mchango wa harusi hiyo kwani hakutaka watu wachangishe kwa kuepuka lawama, alichokifanya ni kuhakikisha watu wanapewa taarifa siku ya kufunga harusi hiyo na kuhudhuria kanisani tu.

    “Rachel! Vipi kuhusu shela?” aliuliza Emmanuel simuni.

    “Ndiyo nipo kwenye hatua za mwisho Emma.”

    “Na mliongea na watu wa suti?”

    “Ndiyo.”

    “Wamesemaje?”

    “Iko poa, ileile uliyotaka.”

    “Nyeusi?”

    “Yeah! Wamekwishaiandaa, waliinunua kutoka Afrika Kusini.”

    “Basi sawa. Wasiliana na Saluni ya Monalisa, waambie kabisa kwamba wiki ijayo ndiyo kila kitu kikamilike,” alisema Emmanuel.

    “Sawa. Hakuna tatizo.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Rachel. Naomba usiniangushe, naomba usiniangushe!”

    “Sawa! Hakuna tatizo.”

    Baada ya kukaa hotelini siku zote hizo huku wakati mwingine akiwasiliana na wanakamati wake kuhusiana na namna ambavyo maandalizi yalivyokuwa yakienda, siku nazo ziliendelea kuyoyoma mpaka kufikia siku moja kabla ya tukio lile laharusi kufanyika kanisani.

    Marafiki zake wote walikuwa na taarifa hivyo wakajiandaa kuona harusi hiyo kwa hamu kubwa. Waandishi wa habari ambao walisikia tetesi juu ya harusi hiyo, wakaamua kujiandaa kwa ajili ya kuhudhuria kwa kuamini kwamba wangeweza kupata kitu chochote kile.

    Siku hiyo mchana, tayari Emmanuel na wazazi wa Luciana walikwishafika katika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kuzungumza na madaktari juu ya mpango wake wa kufunga ndoa na mmoja wa vichaa waliokuwepo mahali hapo.

    Madaktari wote waliosikia kuhusu suala hilo, wakamshangaa Emmanuel, ilikuwaje mpaka aamue uamuzi mgumu namna ile? Je hakukuwa na wasichana wengine wazuri mpaka kuamua kufunga harusi na Luciana, msichana aliyekuwa katika hali ya ukichaa kwa miaka mitano?

    “Kijana! Upo sawa kweli?” aliuliza Dk. Mshana, alikuwa mtaalamu wa magonjwa ya akili hospitalini hapo.

    “Nipo sawa dokta.”

    “Kweli unataka kumuoa msichana huyu?”

    “Ndiyo!”

    “Hapana. Hilo ni suala gumu sana, sisi kama madaktari, hatuwezi kuruhusu suala hilo,” alisema Dk. Mshana.

    “Unasemaje?”

    “Hatuwezi kuruhusu suala hilo.



    ” alisema Dk. Mshana.

    “Unasemaje?”

    “Hatuwezi kuruhusu suala hilo. Yaani haiwezekani kumruhusu chizi kutoka ndani ya himaya yetu, tena kwenda kufunga ndoa, hilo ni suala gumu mno,” alisema Dk. Mshana.

    Emmanuel akaishiwa nguvu, kwanza akaanza kuongea kwa sauti kubwa huku akimsisitizia daktari huyo kwamba alifika mahali hapo kwa sababu alitaka kumchukua Luciana na kwenda kufunga naye ndoa kanisani, daktari huyo hakuonekana kumuelewa, bado msisitizo wake ulikuwa palepale kwamba asingeweza kuruhusu tukio kama hilo litokee.

    Emmanuel akachanganyikiwa!

    ****

    Emmanuel hakutaka kukubali, alitumia kiasi kikubwa mno cha fedha kwa ajili ya maandalizi ya harusi yake na Luciana, hakutaka kuona jambo hilo likishindikana, alichokitaka ni kufunga ndoa na msichana huyo tu.

    Japokuwa alimuelezea Dk. Mshana juu ya gharama zake lakini dokta huyo aliendelea kusisitiza kwamba jambo hilo lisingeweza kutokea hata mara moja, hivyo alitakiwa kuondoka mahali hapo kurudi nyumbani.

    Alipoona ameshindwa kabisa, akawaomba wazazi wa Luciana waweze kuzungumza na daktari huyo ili akubaliane na suala lake la kumuoa binti yao. Japokuwa walitumia muda mrefu kuzungumza na daktari huyo, tena kwa kumuahidi kwamba wangeweza kuwa makini naye, Dk. Mshana akakubaliana nao.

    “Nashukuru sana,” Emmanuel alijikuta akishukuru kwani hakuamini kama kazi ya kumuomba daktari yule ingekuwa nyepesi nama ile.

    Siku hiyo usiku, Emmanuel hakulala, muda wote alikuwa akiifikiria kesho yake kwamba ni furaha ya namna gani angekuwa nayo katika kipindi ambacho angepewa nafasi ya kumvisha pete Luciana na kuwa mke wake wa ndoa.

    Japokuwa ndugu, jamaa na marafiki waliweka vikwazo vingi kwamba hakutakiwa kumuoa msichana huyo lakini mwisho wa siku alikuwa akitarajia kufunga ndoa na msichana huyo mrembo.

    Mawazo juu ya kule walipotoka hayakuisha, alikumbuka kila kitu, toka siku ya kwanza alipokutana na msichana huyo mrembo mpaka kipindi alichokumbwa na ugonjwa huo.

    “Hatimae anakuwa mke wangu, nitampenda milele,” alijisemea Emmanuel na kupitiwa na usingizi.

    Asubuhi alipoamka, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwapigia simu wanakamati wake na kuwauliza juu ya hatua waliyokuwa wamefikia. Walimwambia kwamba kila kitu kilikuwa tayari na ni muda wa kufungwa kwa harusi hiyo ndiyo uliokuwa ukisubiriwa.

    Alichokifanya, akawaelezea wazazi wake ambao walimwambia kwamba ndugu wa Luciana walikuwa wamekwishafika kutoka Bagamoyo, wote walikuwa mahali hapo kwa ajili ya kushuhudia kile kilichotarajiwa kufanyika.

    Hiyo ilikuwa miongoni mwa harusi zilizovuma kwa kipindi hicho, kwa kila aliyesikia kwamba Emmanuel alitaka kumuoa kichaa, alitaka kushuhudia kwa macho yake ni kitu gani kingeendelea kanisani humo.

    Saa mbili asubuhi, wazazi wa Luciana wakafika hospitalini hapo na kuomba ruhusa ya kumchukua binti yao na kuondoka naye. Halikuwa jambo jepesi kumzuia Luciana asifanye fujo, iliwachukua zaidi ya saa moja, wakaweza kumdhibiti tena kwa kutumia msaada wa watu wengine wanne, wanaume wenye nguvu walioonekana kushiba hasa.

    “Wapi hiyo?” aliuliza mwanaume mmoja.

    “Saluni,” alijibu bi Luciana.

    “Saluni?”

    “Ndiyo.”

    “Kufanya nini?”

    “Kumseti bibi harusi.”

    “Bibi harusi! Huyu ndiye yule kichaa anayetarajiwa kuolewa?”

    “Ndiyo!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Mmmh! Kumbe huyu ndiye yule tuliyekuwa tukisikiasikia?” aliuliza mwanaume mwingine.

    “Ndiye huyuhuyu. Naomba mtusaidie naahidi kuwalipa kiasi fulani cha fedha,” alisema baba Luciana.

    Kwa sababu wafanyakazi wa Saluni ya Monalisa walikwishaambiwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea, hata alipoletwa Luciana hakukuonekana kuwa na tatizo kubwa. Walichokifanya ni kumchukua na kumfunga kamba ngumu zilizokuwa zimekwishaandaliwa.

    Siku hiyo, saluni hapo ilikuwa ni balaa, kila wakati Luciana alikuwa akileta fujo kiasi kwamba alivunja baadhi ya vitu na baba yake kuahidi kuvilipa. Japokuwa wafanyakazi wa saluni hiyo walipata kazi kubwa lakini mwisho wa siku wakafanikiwa kuzitengeneza nywele zake na hivyo kulipwa kiasi chote walichokuwa wakikihitaji, kuanzia huduma na vitu vilivyoharibiwa.

    Saa tano na nusu asubuhi, tayari kanisa lilikuwa limefurika, zaidi ya watu elfu mbili walikuwa wamekusanyika kanisa hapo kwa ajili ya kushudia harusi hiyo ambapo kijana Emmanuel, msomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikuwa akimuoa msichana kichaa ambaye alikuwa mpenzi wake wa siku nyingi, Luciana.

    Waandishi wa habari hawakukosa, japokuwa ilikuwa ngumu kuwafahamu kwa kuwa walionekana kama wapiga picha wa kawaida, lakini walifika kanisani hapo kwa kuwa walitaka kuona ni kitu gani kingeendelea kanisani hapo.

    Picha zilipigwa, vigelegele vya wakinamama vilikuwa vikisikika kila kona kanisani hapo. Kila mmoja alionekana kuwa na furaha lakini wengine walikuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona ni kwa namna gani harusi hiyo ingeweza kufungwa.

    Baada ya dakika ishirini huku presha za watu zikiwa juu, gari dogo likafika kanisani hapo, baadhi ya watu waliokuwa kanisani humo wakatoka nje na kuangalia ni nani aliyekuwa akiteremka.

    Gari lilipambwa kwa maua yenye mvuto pamoja na mapambo ya kila namba yaliyolifanya livutie huku ubavuni kuwa na mapambo mengine yaliyoandika majina yao. Mlango wa nyuma ukafunguliwa na Emmanuel kuteremka huku akiwa na mpambe wake.

    Alipendeza mno. Suti nyeusi ilimkaa vizuri, shati jeupe lililokuwa liking’aa lilionekana kwa mbali huku tai nyekundu ikiwa imetulia vema shingoni mwake. Yeye na mpambe wake wakaanza kuingia kanisani humo, vigelegele viliendelea kusikika kila kona, waliokuwa na mchele, waliutupa hewani, ulipomwagika, ulionekana kuwa kama ishara ya kushangilia.

    Wanawake wa Kichaga hawakunyamaza, walikuwa wakiimba nyimbo zao za uchagani na kucheza kwa furaha, kitendo cha kijana wao kupata ‘jiko’ siku hiyo kiliwafurahisha mno.

    Walipofika mbele, wakasimama na kuanza kumsubiria bibi harusi. Mchungaji wa kanisa hilo, John Mwabukusi alisimama mbele kabisa, mkononi alikuwa na Biblia huku uso wake ukipendezeshwa vizuri na miwani ya macho.

    “Fredrick, ndiyo naaga ubachela aiseee, daaah!” alisema Emmanuel, alikuwa akimwambia mpambe wake.

    “Karibu sana kaka. Usiogope ndoa, ni kitu chepesi mno,” alisema Fredrick huku akitoa tabasamu.

    “Ni kwa miaka mingi nimekuwa nikilisubiria hili, hatimae, nimefanikiwa.”

    “Yeah! Ninachokuhusia, mpende sana mke wako, tena umpende zaidi ya unavojipenda,” alisema Fredrick.

    “Nadhani hilo limedhihirika, sidhani kama utakuwa na wasiwasi nami.”

    Wala haukuchukua muda mrefu, gari la bibi harusi likaanza kuingia ndani ya eneo la kanisa hilo. Watu wengi waliokuwa kanisani wakatoka nje ili kumuona huyo bibi harusi. Gari lile liliposimamishwa, mlango ukafunguliwa na bibi harusi kuteremka.

    Alipendeza mno, shela jeupe alilokuwa amelivaa na mapambo yaliyokuwa yametumika kumpamba yalimvutia kila mmoja. Luciana hakuwa peke yake, alikuwa na mpambe wake wa kike huku wanaume watatu wenye nguvu wakiwa wamemshika vilivyo ili kumzuia asilete fujo.

    Japokuwa alishikwa kwa nguvu lakini bado Luciana hakutaka kutulia, alikuwa akihangaika huku na kule kama njia mojawapo ya kutaka kujinasua kutoka katika mikono ya watu wale waliokuwa wamemshika.

    Emmanuel alipoona mke wake mtarajiwa akiingia, naye akaanza kupiga hatua kuelekea kule kulipokuwa na mlango kisha kuungana na mchumba wake, wakaanza kupiga hatua kwenda mbele huku wakinamama wa Kichaga wakiendelea kupiga vigelegele vya shangwe.

    Walipofika, kitu cha kwanza kabisa alichokifanya mchungaji ni kuifungua Biblia yake na kisha kuanza kuhubiri Neno la Mungu kuhusu ndoa, alipomaliza, akahitaji pete ziletwe mikononi mwake, zilipoletwa, akaanza kuwaangalia washirika kanisani mule.

    “Kabla sijafungisha ndoa hii, kuna mtu yeyote anataka kupinga ndoa hii isifungwe?” aliuliza mchungaji.

    Kila mtu macho yake aliyageuza huku na kule kuona kama kulikuwa na mtu yeyote aliyesimama. Kanisa zima lilikuwa kimya na hakukuwa na mtu yeyote aliyesimama hivyo mchungaji kurudia mara ya pili lakini majibu yalikuwa yaleyale. Aliporudia mara ya tatu, mara mwanaume mmoja akasimama na kuanza kuelekea mbele ya kanisa lile.

    Kila mtu akapigwa na butwaa, kijana yule aliendelea kupiga hatua kwenda mbele, machozi yaliendelea kububujika mashavuni mwake kwa uchungu. Kila mmoja akabaki akimwangalia, Emmanuel hakumfahamu mtu yule alikuwa nani, na hakujua kama alikuwa akisogea mbele ili kuipinga harusi hiyo au la.

    Alipofika mbele, kitu cha kwanza akaanza kumwangalia Luciana, machozi ya uchungu yaliendelea kumbubujika. Kusingekuwa na maelezo yoyote ya kuthibitisha kwamba mtu huyo alikuwa kwenye hali gani, uso wake tu, ulionyesha ni jinsi gani alikuwa ameumia.

    Kijana huyo alikuwa Patrick!

    ****

    Hakukuwa na mtu aliyemfahamu kijana yule, Emmanuel alibaki akimwangalia Patrick, alionekana kuwa kijana mgeni machoni mwake na hakufahamu kama aliwahi kumuona sehemu yoyote ile.

    Wazazi wa Luciana walionekana kumkumbuka kijana huyo lakini hawakukumbuka sehemu waliyowahi kumuona. Walikuwa wakijiuliza huku wakijaribu kuvuta kumbukumbu zao lakini hawakuweza kukumbuka kabisa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Machozi yaliendelea kumbubujika Patrick, hakuamini kama kweli mpenzi wake wa kipindi cha nyuma aliyewahi kuwekeana naye ahadi kwamba wangeoana, leo hii alikuwa akiolewa na mwanaume mwingine kabisa.

    Alipoyahamisha macho yake na kutua usoni mwa Emmanuel, akaukunja uso wake, alionekana kuchukia mno kumuona mwanaume huyo mahali hapo. Akajua kabisa huyo ndiye aliyesababisha mpaka msichana huyo aondoke mikononi mwake na hatimae kutaka kumuoa yeye.

    “Mama! Kwa nini mmenifanyia hivi?” aliuliza Patrick huku akibubujikwa na machozi tu. Kanisa zima lilikuwa kimya.

    “Wewe ni nani?” baba Luciana aliingilia kwa kuuliza swali.

    “Mmenisahau? Hamumkumbuki Patrick, hamkumbuki kitu chochote kuhusu mimi?” aliuliza Patrick.

    “Patrick?”

    “Ndiyo. Ni yuleyule niliyekuwa nikimwambia Luciana kwamba ninampenda, nilielewana naye sana lakini nashangaa leo hii mnataka mnisaliti na kumuozesha kwa mwanaume mwingine!” alisema Patick huku machozi yakiendelea kumbubujika.

    “Mbona unatuchanganya Patrick!”

    “Nawachanganya nini?”

    “Umesema kwamba tunakusaliti, sasa kosa letu? Si binti yetu ndiye alitaka kuolewa na huyu Emmanuel!”

    “Hapana! Luciana hakutaka kuolewa na huyu, alitaka kuolewa na mimi. Niliahidiana naye mengi sana, niliilamba damu yake chini ya mbuyu kule Bagamoyo kwamba hakuna kitakachonitenganisha naye zaidi ya kifo, baba, kwa nini mnanifanyia hivi?” aliuliza Patrick huku akiendelea kulia kama mtoto mdogo. Wazazi wa Luciana wakabaki kimya.

    “Angalia, hata barua zake hizi hapa, unaona, tulikuwa tukiandikiana sana na kuhusiana juu ya upendo wetu, kuwa waaminifu mpaka nitakapomuoa. Huyu mwanaume si anayestahili kuwa mume wa Luciana, mimi ndiye ninastahili, mvueni suti mnivishe mimi,” alisema Patrick.

    Kila aliyekuwa akimwangalia Patrick kanisani pale alimuonea huruma, alikuwa akilia mfululizo huku machozi yakiendelea kumbubujika mashavuni mwake. Hakukuwa na kipindi kilichomuumiza mno maishani mwake kama kipindi hicho.

    Aliwaona wazazi wa Luciana kuwa wasaliti, walikuwa wakimuozesha binti yao kwa mwanaume mwingine pasipo kumpa taarifa. Alijua kwamba Luciana alimkataa hasa baada ya kumwambia kwamba alipata mwanaume mwingine lakini Patrick hakutaka kukubali kabisa.

    Malumbano yakaanza kutokea kanisani hapo, Luciana, msichana kichaa akaanza kugombaniwa na kila mmoja. Vurugu zikaanza kutokea kanisani pale kiasi kwamba mchungaji Mwabukusi akaacha shughuli ya kuwafungisha ndoa maharusi wale.

    Watu waliokuwa wamekaa vitini, wakashindwa kuvumilia, wakasimama na kuanza kusogea kule mbele. Hakukuwa na aliyetulia, kila mtu alizungumza lake mahali pale.

    Luciana hakuwa akielewa kitu chochote kile, akili zake zilimruka hivyo kubaki akiongea peke yake huku wanaume wale waliokuwa wamemshika kuendelea kumshika zaidi.

    “Luciana ni mke wangu mtarajiwa,” alisema Emmanuel.

    “Hapana. Ni wangu. Nimetoka naye mbali sana



    , mimi ndiye niliyemtoa usichana wake, haiwezekani, huyu ni wangu,” alisema Patrick huku akimshika mkono Luciana.

    Hicho kikaonekana kuwa kituko, waandishi wa habari wakabaki wakitabasamu tu, kwa vuguvugu lililokuwa likitokea, liliwapa uhakika kwamba habari hiyo ingewapa sana fedha hivyo waliendelea kupiga picha tu.

    “Nimesikia umesema Luciana alinyonya damu yako!”

    “Ndiyo!”

    “Kivipi?”

    Hapo ndipo Patrick alipoanza kusimulia kile kilichokuwa kimetokea, toka siku ya kwanza alipokutana na msichana huyo, walipoanza kuwa karibu na hatimae kuwa wapenzi. Hakuficha kitu chochote kile, aliendelea kulisimulia kanisa mpaka siku walipokutana katika mbuyu wa kichawi na kuwekeana ahadi kwamba wasingeweza kuachana na kama ingetokea mmoja kumuacha mwenzake, basi alistahili kuishi kwa huzuni maisha yake yote.

    Historia ya maisha yao ya nyuma aliyokuwa akiihadithia ilimsikitisha kila mtu hata Emmanuel mwenyewe aliyekuwa akiisikiliza alimuonea huruma Patrick lakini hakutaka kumuacha Luciana awe naye.

    “Pole sana, stori yako imesikitisha sana, ila kukuachia Luciana, haiwezekani, hapa hatuongelei mbuyu, damu wala huzuni, hapa tunaongelea harusi tu, hayo mengine ni maneno ya mkosaji tu,” alisema Emmanuel huku akionekana kumaanisha alichokuwa akikiongea.

    “Mchungaji, endelea kufungisha ndoa,” alisema baba Luciana.

    “Bado hamjaelewana, mmenichanganya mpaka mimi mwenyewe,” alisema mchungaji Mwabukusi.

    “Lakini mimi si ndiye ninatakiwa kumuoa! Hili lijamaa limekuja tu, halina hata uthibitisho kwamba Luciana alikuwa mpenzi wake, kama ukiwa na mtu, bila pete au mtoto, sasa hapo utakatazaje ndoa kufungwa? Lete vithibitisho kaka,” alisema Emmanuel.

    Aliloliongea lilikuwa jambo la msingi mno, kitendo cha Patrick kutotaka ndoa hiyo ifungwe alitakiwa awe na vithibitisho vyovyote ambavyo vingeonyesha kwamba kweli ndoa ile haikutakiwa kufungwa kwa kuwa Luciana alikuwa mtu wake.

    Hilo lingewezekana kama angekuwa amemuoa kabla, hivyo alikuwa mke wake au alizaa naye na hivyo akaachwa solemba. Kila alichokuwa akiulizwa kwamba ni nini alikuwa nacho kama ushahidi wa kuizuia ndoa ile isifungwe, hakukuwa na chochote kile.

    “Kwa hiyo ndoa inafungwa?” aliuliza Patrick huku akionekana kughadhibika.

    “Ndiyo!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Kwa nini sasa?”

    “Si hauna uthibitisho wowote ule. Ndoa inafungwa,” alisema mchungaji Mwabukusi, washirika wote wakarudi vitini huku Patrick akiwa amesimama pale mbele, alikuwa akitetemeka kwa hasira kupita kawaida.

    “Haiwezekani! Haifungwi ndoa hapa!” alisema Patrick, kwa mwendo wa haraka akatoka nje, hakukuwa na aliyejua mtu huyo alifuata nini, hakuna aliyejali, walibaki wakimwangalia Patrick aliyeukaribia mlango wa kutokea, ili kumkebehi na kumuonyeshea kwamba hafai, kanisa zima likaanza kucheka kitendo kilichomfanya mwanaume huyo kushikwa na hasira kali mno.

    Alipotoka nje ya kanisa tu. Luciana akalegea, watu wakashtuka, walipomuachia, akaanguka chini kama mzigo na kutulia. Walipoyasikilizia mapigo yake ya moyo, yalikuwa yakifunda kwa mbali mno.

    “Amekufa?”

    “Hapana, ila nahisi anaelekea kufa, mapigo yake ya moyo yapo chini sana.”

    “Mungu wangu!” alisema mama Luciana na kuanza kuangua kilio kanisani hapo. Kila mmoja pale mbele alionekana kuchanganyikiwa, Luciana alionekana kubakiza dakika chache kuendelea kuvuta pumzi ya dunia hii.

    ****



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog