Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

NISAMEHE LATIFA - 2

     







      Simulizi : Nisamehe Latifa

      Sehemu Ya Pili (2)



      Waliendelea kubaki nchini India mpaka pale Latifa aliporuhusiwa tayari kwa kurudi nyumbani. Hakuwa amepata tatizo lolote lile ambalo lingemfanya kuwa na ugonjwa wowote ule, iwe kifafa, kusahau au kupoteza maisha.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      Alipohadithiwa kile kilichotokea, alibaki akilia huku akimshukuru bi Rachel kwa msaada aliompa. Waliendelea kukaa nchini India kwa wiki kadhaa na ndipo waliporudi nchini Tanzania.

      “Ninataka kuishi na Latifa,” alisema bi Rachel, alikuwa akimwambia Issa.

      “Haiwezekani, bado tunahitaji kukaa naye zaidi, akikuakua, tutakuruhusu uje kumchukua,” alisema Issa.

      “Na mama yake yupo wapi?”

      “Ni stori ndefu sana, kuna siku utajua, kitu cha msingi, acha tuendelee kukaa naye hapa, ukitaka kumuona, usihofu chochote kile, unakaribishwa sana,” alisema Issa.

      Tayari kwa mtazamo wa haraka-haraka Issa aligundua kwamba Latifa alikuwa fedha, hakutaka kumruhusu kuondoka naye kwani alijua kwamba endapo bi Rachel angeamua kumchukua basi asingeweza kuwasaidia.

      Mwanamke huyo alikuwa tajiri, alikuwa na kiasi kikubwa cha fedha, alimiliki vituo vya mafuta, super market na biashara nyingine zilizomuingizia fedha kila siku. Maisha yake yalitawaliwa na fedha, hakuwa na shida, aliishi maisha aliyotaka kuishi siku zote.

      Alichokifanya bi Rachel ni kubadilisha maisha ya Issa, dada yake, Semeni na Latifa pia. Mara kwa mara aliwatumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuwaendeleza katika maisha yao ya kila siku. Baada ya kuhakikisha kila kitu kimekaa sawa, akamhamisha Latifa katika Shule ya Jangwani na kumpeleka katika Shule ya St. Antony iliyokuwa Mbezi Beach.

      Hakutaka msichana huyo apate tabu yoyote ile, alitaka kumsomesha mpaka atakapofikia levo ya juu kabisa kielimu. Shuleni huko, Latifa alionekana kuwa mwiba, uzuri wake ulimpagawisha kila mvulana aliyemwangalia, wasichana wenzake waliovuma kwa uzuri shuleni hapo wakaanzisha bifu na yeye, waliuogopa uzuri wake kwa kudhani kwamba angeweza kuwachukulia wavulana wao.

      “Ninamchukia huyu kinyago, simpendi kweli, sijui kwa nini amehamia hapa,” alisema msichana mmoja, aliitwa Theresa, alikuwa miongoni mwa wasichana waliotesa wanaume kwa uzuri shuleni hapo.

      “Achana naye shoga, asikuumize kichwa, hakuna atakayeweza kutuchukulia watu wetu,” alisema msichana mwingine.

      Uzuri wa Latifa haukuishia hapo bali ulikuwa mpaka darasani, hakukuwa na mwanafunzi aliyemfikia kwa uwezo mkubwa aliokuwa nao. Japokuwa wasichana wengi warembo darasani hawakuwa na makali lakini kwa Latifa hali ilionekana kuwa tofauti kabisa.

      Walimu walibaki wakishangaa, hawakuweza kuamini kama kulikuwa na mtu aliyekuwa na akili nyingi kama alivyokuwa Latifa. Katika masomo yake yote shuleni hapo, alipata alama ya A kitu kilichomfanya kuwa mwanafunzi wa kwanza katika shule hiyo kufaulu kwa kiwango hicho kikubwa.

      “Hapa ni kusoma tu, mapenzi baadaye,” alisema Latifa kila alipofuatwa na wavulana, kwake, masomo yalikuwa chaguo la kwanza.

      ****

      Ibrahim alikuwa kwenye wakati mgumu, muda mwingi alikuwa mtu wa mawazo, hakuamini kama kweli msichana aliyempenda alipata ajali na hivyo kipindi hicho alikuwa hoi kitandani huku akiwa hajitambui.

      Mara kwa mara alikuwa akielekea Muhimbili kwa ajili ya kumuona lakini hakuwa akipata nafasi, na hata kama alikuwa akipata pamoja na wanafunzi wenzake, muda uliotolewa aliuona kuwa mfupi mno.

      Ibrahim alimpenda Latifa, alihitaji kumuona akiamkakutoka katika usingizi wa kifo na hatimaye kuzungumza naye na kumwambia jinsi gani alimpenda na kumuhitaji. Hakuwa na nafasi hiyo tena, kipindi hicho, msichana huyo alionekana kama mfu kitandani.

      Siku kadhaa zikapita, akasikia kwamba msichana huyo alikuwa amepelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu. Moyo wake ukanyong’onyea mno, akakosa nguvu lakini pamoja na hayo, akajiahidi kwamba asingeweza kumsaliti japokuwa hakuwahi kuzungumza naye.

      Ilipopita miezi miwili, akapewa taarifa mbili, moja ilimfurahisha lakini nyingine ilimhuzunisha. Yenye kufurahisha ilisema kwamba Latifa alikuwa amerudi nchini Tanzania lakini ile yenye kuhuzunisha ilisema msichana huyo alikuwa akihamishwa shule na kwenda kusoma shule moja ya watoto wa matajiri.

      Taarifa hiyo mbaya ikawa kama msumali wa moto moyoni mwake, alishindwa kufahamu ni kwa sababu gani lilikuwa jambo gumu kwake kuonana na msichana huyo, baada ya wiki mbili, akaambiwa kwamba msichana huyo alianza masomo katika Shule ya St. Antony iliyokuwa Mbezi Beach.

      “Nitamfuata hukohuko tu,” alijisema Ibrahim.

      Hakutaka kuendelea kubaki katika moyo wa kipweke. Baada ya siku kadhaa akaamua kwenda shuleni huko kwa ajili ya kumuona msichana huyo. Alipofika katika geti la shule hilo, akaomba kuonana na Latifa, akakataliwa na mlinzi aliyekutana naye getini.

      “Hii siyo shule ya uswahilini, huku uzunguni, hebu nenda huko uswahili ukaulizie kiuswahili-uswahili kama ulivyouliza, hapa ukija, unatoa taarifa kwa njia ya simu kwanza,” alisema mlinzi huyo kwa kebehi kwani kila alipomwangalia Ibrahim, alionekana kuwa na maisha mabovu.

      ****

      Makali ya Latifa darasani hayakupungua, kwenye kila mtihani alionyesha kwamba uwezo wake ulikuwa wa juu mno, aliwaongoza wanafunzi wote kiasi kwamba wengi wakaanza kuanzisha bifu naye.

      Wavulana walioendelea kumfuata, mmoja wao aliitwa Maliki Abdullahman. Alikuwa kijana mtanashati mwenye asili ya Kiarabu aliyetoka katika familia ya kitajiri, sura yake ilikuwa ya mvuto iliyowachengua wasichana wengi waliokuwa wakikutana naye barabarani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      Maliki alikuwa gumzo kila kona, wasichana walimsumbua kila siku lakini hakutaka kuwa na msichana hata mmoja. Darasani, uwezo wake haukuwa wa kawaida, alikuwa akikimbizana na Latifa japokuwa walisoma madarasa tofauti.

      Aliwakataa wasichana wengi, hakupenda kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi lakini mara baada ya kumtia Latifa machoni, moyo wake ukamlipuka, hakuamini kama katika dunia hii hasa katika nchi ya Tanzania kungekuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa Latifa.

      “She is so beautiful, I just want to be with her, I will never let her go,” (Ni mrembo mno, ninataka niwe naye, kamwe sitomuacha aondoke) alisema Maliki huku akimwangalia vizuri Latifa.

      Msichana huyo alionekana kuwa msichana wa ndoto zake, kila alipoelekea shuleni ilikuwa ni lazima kwenda katika darasa la kina Latifa kwa lengo la kumuona tu. Moyo wake ukatekwa, hakukuwa na msichana aliyeuteka moyo wake kama alivyokuwa Latifa.

      Alijitahidi kumpiga picha kisiri na kuwa nazo kwenye simu yake, hiyo ikaonekana kutotosha, alichokifanya ni kutafuta namba yake, alipoipata, akajitahidi kuwa karibu naye kimawasiliano lakini msichana huyo alikuwa mgumu kutekeka.

      “Nifanye nini? Ngoja nikamwambie ukweli. Mmh! Ila nitaweza kweli? Mbona naanza kumuogopa!” alijisemea Maliki.

      Kumfuata Latifa ulikuwa mtihani mgumu, alibaki akiumia moyoni mwake huku kila siku usiku akikesha kuziangalia picha zake tu.

      Wakati hayo yote yakiendelea katika maisha ya Maliki, upande wa pili, bado Ibrahim, kijana masikini aliendelea kuteseka moyoni mwake. Safari za kwenda Mbezi Beach hazikuisha, mara kwa mara alikwenda huko na alipofika karibu na eneo la shule hiyo, alikuwa akijificha.

      Gari alilokuwa akiendeshwa Latifa lilipotoka katika eneo la shule, Ibrahim alitoka alipokuwa amejificha na kuanza kuliangalia, hata alipokuwa akimuona msichana huyo kwa mbali, moyo wake uliridhika.

      Hiyo ndiyo ilikuwa tabia yake, aliendelea kufika shuleni hapo lakini ikafika siku ambayo alionekana kuchoka, hakutaka kuendelea tena kujificha, siku hiyo alipanga kuongea na Latifa na kumwambia ukweli.

      Alipofika karibu na eneo la shule hiyo, kama kawaida akajificha na wakati gari lile lilipoanza kutoka, akasogea kule lilipokuwa na kusimama mbele yake, si dereva wala Latifa, wote wakaonekana kushtuka, kile kilichoonekana kilimshtua kila mmoja.

      “Piii…piiii…piii…” dereva alipiga honi lakini Ibrahim hakuondoka, aliendelea kusimama huku lengo lake kubwa likiwa ni kuongea na Latifa siku hiyo.

      “Siondoki mpaka Latifa ashuke garini, nitataka kuzungumza naye tu, siwezi kuteseka siku zote hizo,” alisema Ibrahim huku akiwa amesimama kama askari wa barabarani, honi ziliendelea kupigwa lakini hakuondoka, alisubiri Latifa ateremke.

      Alichokifanya dereva yule ni kuteremka kutoka garini na kuanza kumfuata Ibrahim. Kitendo alichokifanya kijana huyo kilimkera, alimfuata huku uso wake ukionyesha dhahiri kwamba alikuwa amekasirika.

      Ibrahim hakuogopa wala kukimbia, huku dereva akimfuata, macho yake yalikuwa yakiangalia kioo cha mbele cha gari lile huku akijitahidi kuyafinyafinya macho yake ili aweze kumuona Latifa aliyekuwa ndani.

      “Wewe dogo kichaa nini! Mbona unazingua, hebu toka barabarani,” alisema dereva yule kwa sauti iliyojaa ukali.

      “Nataka kuongea na Latifa! Sitoki mpaka niongee na Latifa!” alisema Ibrahim kwa sauti kubwa.

      “Unasemaje?”

      “Nataka kuongea na Latifa, mwambie ashuke kutoka garini,” alisema Ibrahim.

      Maneno aliyoongea na kitendo alichokifanya, alionekana kama kutania, dereva akazidi kushikwa na hasira zaidi, akamshika Ibrahim, akamvuta pembeni na kwenda kumtupia huko huku akimpiga mikwara asirudi barabarani pale.

      Ibrahim alibaki akiwa amechukia, hakuamini kama kweli dereva aliamua kumfanyia kitendo kama kile ambacho kwake alikichukulia kuwa cha kikatili wa hali ya juu.

      “Kuna nini?” aliuliza Latifa huku akishangaa.

      “Yule dogo chizi sana!”

      “Kwa nini?”

      “Eti anataka kuongea na wewe! Unamjua?”

      “Mmmh! Hapana! Ndiyo kwanza namuona leo,” alisema Latifa.

      Dereva akawasha gari lile na kuondoka mahali hapo. Kichwa cha Latifa kikabaki kuwa na maswali mengi juu ya sababu iliyompelekea kijana yule asiyemfahamu kutaka kuzungumza naye.

      Walipompita na gari, alibaki akimwangalia, alijaribu kuvuta kumbukumbu kuona kama alikwishawahi kumuona sehemu yoyote, hakukumbuka chochote kile.

      Huo ndiyo ukawa kama mwanzo wa kila kitu, Latifa akashikwa na kiu, alitaka kusikia kitu ambacho kijana yule alitaka kumwambia. Japokuwa alijitahidi kumtafuta nje ya shule kila alipokuwa akitoka, hakumuona tena, moyo wake ukashikwa na kiu zaidi, moyoni, alijuta sababu ya kutokushuka garini siku ile na kwenda kuongea naye.

      CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      Latifa aliishi kwenye mateso makubwa, kila siku akawa mtu wa mawazo tu akimfikiria kijana aliyekuja kumwangalia ambaye alitaka kuzungumza naye lakini hakuweza kushuka garini.

      Siku ziliendelea kukatika, hamu aliyokuwa nayo moyoni mpaka ikaisha lakini hakufanikiwa kumuona Ibrahim tena. Aliendelea na maisha yake huku akiendelea kufanya vizuri katika masomo yake kwa kuwaongoza wanafunzi wote shuleni hapo.

      Maliki, hakutaka kukata tamaa, kuna kipindi kikafika akaona ni bora kumfuata msichana huyo na kumwambia ukweli lakini hakuwa radhi kuendelea kupata mateso ya moyo. Alichokifanya katika siku ambayo alipanga kumwambia Latifa ukweli, akajiandaa vizuri, hakutaka kuonekana na kasoro yoyote ile, akajivisha ujasiri na kumfuata msichana huyo.

      “Hapana Maliki, sipo tayari kuwa na mvulana yeyote yule,” alisema Latifa, alionekana kumaanisha alichokisema.

      “Latifa, lakini mbona sioni tatizo lolote lile, kama kuna mtu ameuumiza moyo wako, ninataka kuwa daktari kwako, niutibu na upone kabisa, nakuahidi kutokukuumiza,” alisema Maliki huku akimwangalia Latifa machoni. Akamshika mkono ili asiondoke.

      “Maliki, let me go, I’m too young to take care of someone. I’ m just thinking of my studdies, you met me here, you don’t know where I came from, please, let me go,” (Maliki, niache niondoke, mimi ni mdogo mno kumjali mtu. Ninayafikiria masomo yangu, ulinikuta hapa, hujui nimetoka wapi, niache niondoke) alisema Latifa huku akimtaka Maliki amuachie mkono.

      “Laty! What is your problem? Should I say that I’m ready to die for you? Will this make you happy and trust me when I say that I love you?” (Laty! Tatizo lako nini? Natakiwa kusema kwamba nipo tayari kufa kwa ajili yako? Hii itakufanya kuwa na furaha na kuniamini ninapokwambia kwamba ninakupenda?) aliuliza Maliki.

      “Let me go,” (Niache niondoke) alisema Latifa, sauti yake ilitoka kwa juu tena yenye ukali mwingi.

      Maliki akaogopa, ukali alioutumia Latifa ukamtisha, akajikuta akimuachia binti huyo na kuondoka zake. Alimwangalia msichana huyo huku moyo wake ukimuuma mno, hakuamini kama uwezo wake wote wa kuongea aliokuwa nao haukumsaidia hata mara moja na mwisho wa siku kukataliwa huku akijiona.

      Huo wala haukuwa mwisho, alichokifanya ni kuanza kufuatilia msichana huyo alikuwa akitoka kimapenzi na nani. Alifanya uchunguzi wake kwa siku kadhaa lakini hakubaini kitu chochote kile, aligundua kwamba msichana hiuyo alikuwa peke yake.

      Latifa hakuyataka mapenzi, aliamua kuishi peke yake kwani kulikuwa na mambo mengi ya kufanya katika maisha yake. Aliendelea na maisha yake ya kuwakataa wanaume waliokuwa wakimfuatilia kila siku, japokuwa ulikuwa mtihani mzito lakini alihakikisha kwamba anafanikiwa.

      “Malkia Cleopatra....” ilisikia sauti ya msichana mmoja ikimuita jina lake la utani, Latifa akageuka, msichana yule akamsogelea.

      “Unasemaje Lilian?”

      “Kuna mvulana amenipa hii barua, amesema nikupe.”

      “Mvulana gani?”

      “Wala simjui, nimekutana naye hapo nje ya shule, akanipa, akaniambia nikufikishie halafu akaondoka zake,” alisema Lilian.

      “Mmmh!”

      “Unamjua?”

      “Hapana. Ni nani?” aliuliza Latifa.

      “Sijui!”

      Latifa akaichukua barua ile na kuanza kuifungua. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa kasi, mwili ukaanza kumsisimka, moyoni mwake alijua kwamba ni yule kijana aliyemuona siku ile. Alipoifungua barua ile, akaanza kuisoma, barua hiyo iliandikwa hivi....

      Kwako Latifa

      Nimekuwa nikikufuatilia kwa kipindi kirefu, u msichana uliyeuteka moyo wangu, nimekuwa nikiteseka kwa ajili yako kwa kipindi kirefu mno tangu ulipokuwa Sekondari ya Jangwani.

      Najua haunifahamu, lakini unamkumbuka yule kijana aliyetaka kuzungumza nawe siku za karibuni? Yule kijana mchafu, asiyevutia lakini mwenye mapenzi ya dhati kwako?

      Latifa, nimejaribu kila njia kukutana nawe lakini imeshindikana, sina njia nyingine ya kufanya zaidi ya kukuandikia barua hii kwa mwandiko huu mbaya.

      Nilisikitika sana ulipopata ajali, kila siku nilikuwa mtu wa kukuombea dua ili upone na ninamshukuru Mungu kwa kukuponya na kukurudishia afya kama ulivyokuwa kabla.

      Nilihuzunika pia kipindi cha nyuma ulipokwenda nchini India, naikumbuka picha yako ya mwisho kukuona ukiwa hospitalini, ulikuwa kimya huku sura yako ikionyesha kama haukuwa pamoja nasi.

      Latifa, nina mengi ya kuzungumza lakini kubwa zaidi lililobeba hayo mengi, ni kwamba, ninakupenda mno, ninakupenda zaidi ya unavyofikiria.

      Kama ningeulizwa ni kitu gani natakiwa kuwa nacho maishani mwangu sasa hivi, hakika ningekuchagua wewe.

      Ninakupenda Latifa, sijajua ni jinsi gani naweza kulieleza hili, ila ukweli, ni kwamba nakupenda.

      Ibrahim, Sekondari ya Azania.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      Latifa akashusha pumzi nzito, hakuamini kile alichokisoma katika barua ile, akabaki akitabasamu huku akijisikia furaha moyoni mwake. Hakuamini kama barua ile aliandikiwa yeye pasipo kutegemea, kwani ilijaza maneno matamu ambayo hakuwahi kuyasoma kabla.

      Siku hiyo, barua ile ilikuwa karibu yake, hakutaka kuiweka ndani ya begi, muda wote ilikuwa katika mfuko wa sketi yake, kila alipoona kwamba hakukuwa na mwalimu darasani, aliichukua na kuanza kuisoma tena, moyo wake ukafarijika mno.

      Taratibu mawazo juu ya Ibrahim yakaanza kumteka, kila sehemu alipokuwa, aliifikiria barua ile huku muda mwingi akivuta kumbukumbu juu ya kijana huyo ambaye alimuona mara moja tu katika kipindi walichokuwa wakipita na gari kurudi nyumbani.

      Moyo wake ukawa na hamu kubwa, akatamani kumuona huyo aliyeandika maneno matamu yaliyoukuna moyo wake vilivyo. Kwa sababu chini kabisa aliandika kwamba alitokea katika Shule ya Wavulana ya Azania, kesho akawa huko.

      Uzuri wake uliendelea kuwa gumzo, wengi waliomuona walimkumbuka, alikuwa miongoni mwa wasichana walioziteka shule zote za ukanda wa mjini kuanzia Azania, Kisutu, Jangwani na shule nyingine za Kihindi.

      Siku hiyo hakwenda shule, alitaka kuitumia siku hiyo kumuona mvulana huyo tu. Kila mvulana aliyepishana naye, aligeuka nyuma na kumwangalia, alionekana kuwa na uzuri usio wa kawaida, wanaume wakware, wakashindwa kuvumilia, wakabaki wakimuita kwa kumpigia miluzi tu.

      Latifa hakujali, alipofika shuleni hapo, akamuulizia Ibrahim kwa lengo la kutaka kumuona mvulana huyo.

      “Wapo wengi, unamuulizia yupi?” aliuliza mlinzi.

      “Wala simfahamu, ila alijitambulisha kwa jina la Ibrahim.”

      “Sawa! Kwa jinsi ninavyokuona, atakuwa Ibrahim Jumanne. Jamaa fulani msafimsafi hivi, ngoja nikuitie,” alisema mlinzi yule na kuondoka mahali hapo.

      Latifa alibaki sehemu ya mlinzi akisubiriwa kuitiwa mtu aliyekuwa akimhitaji. Japokuwa haikuwa ikiruhusiwa mpaka mtu kwenda kwenye ofisi ya walimu, lakini mlinzi alishindwa kuvumilia, hakukubali kuona akikataa kumsaidia msichana mrembo kama Latifa.

      Aliporudi, aliongozana na kijana aliyeonekana kuwa mtanashati, alipendeza alivyovaa na alinukia vizuri. Kijana huyo alipomuona Latifa, akashtuka, hakuamini kama aliuliziwa na msichana mrembo kama alivyokuwa, akamsogelea huku akiachia tabasamu pana.

      “Niambie mrembo!” alisema kijana huyo.

      “Safi tu! Kaka, samahani, siyo huyu,” alisema Latifa huku akimwangalia mlinzi.

      “Mmmh! Siyo huyo? Basi muulize huyohuyo atakuwa anamfahamu,” alisema mlinzi yule.

      Hapo ndipo Latifa alipoanza kumueleza huyo Ibrahim juu ya mtu aliyekuwa akimhitaji shuleni hapo. Kichwa cha mvulana huyo kikaanza kuwapekua Ibrahim wote waliokuwepo shuleni hapo, kila aliyemfikiria, hakulingana na maneno aliyokuwa akielezea Latifa.

      “Huyo wala simfahamu!”

      “Kaka, naomba unisaidie kunitafutia huyu Ibrahim, muulizie hata shule nzima, ukifanikiwa, nakupa zawadi, chukua hii kwanza,” alisema Latifa huku akimkabidhi Ibrahim shilingi elfu kumi kama kumhamasisha katika suala zima la kumtafuta Ibrahim. Jamaa akaenda kumtafuta.

      Moyo wa Latifa ulikuwa kwenye mapenzi ya dhati, hakuwa radhi kuondoka na kurudi nyumbani na wakati yule aliyekwenda kumtafuta hakuwa amemuona. Alikaa sehemu hiyo ya mlinzi huku akiongea naye, kila neno aliloliongea, alionekana kuwa na uhitaji wa kumuona kijana huyo.

      Zilipita dakika thelathini, Ibrahim yule akarudi na vijana watano waliokuwa na jina kama lake. Latifa akaanza kuwaangalia watu hao, japokuwa kipindi cha nyuma wakati Ibrahim alipokuja shuleni kwao hakumuona vizuri lakini kila alipowaangalia wavulana wale, moyo wake ulimwambia kwamba kipenzi chake hakuwepo.

      “Hapana! Hawa ndiyo wote?” aliuliza Latifa.

      “Hapana. Kuna mmoja amebaki, leo hajaja, mtoromtoro na mchafumchafu fulani hivi, nikaona siyo tatizo nikikuletea hawa wenzangu, achana na yule, hawezi kuwa yeye, kwanza kuna demu huwa anampigia misele huko Mbezi,” alisema Ibrahim.

      “Ninataka kumuona pia,” alisema Latifa.

      “Yupi? Huyo mchafumchafu?”

      “Ndiyo! Huyohuyo! Nataka kumuona, inawezekana akawa mchafu kimwili, ila moyoni akawa na mzigo mzito wa mapenzi yangu, nahitaji kumuona, naomba unitafutie au kunipeleka kwao, nitakupa kiasi chochote utakachotaka, naomba nikamuone,” alisema Latifa huku akionekana dhahiri kuwa na uhitaji wa kumuona kijana huyo.

      “Lakini inawezekana siye yeye, huoni kama utasumbuka?”

      “Kusumbuka kwa ajili ya mapenzi, si tatizo kaka yangu, hata angekuwa wapi, ningemfuata. Ili niujutie usumbufu, kama siye yeye, basi nitajuta, ila kama ni yeye, hakika nitakuwa na furaha moyoni mwangu,” alisema Latifa. Mapenzi yalimteka na kumtumbukiza kwenye bwawa la mahaba.

      ****

      Siku hiyo Latifa alidhamiria kuonana na kijana aliyejitolea kumpenda kwa mapenzi ya dhati, Ibrahim. Mara baada ya kuzungumza na kijana huyo mtanashati ambaye alimfuata na kumwambia kwamba mvulana aliyekuwa akimtaka hakuwa shuleni hapo, akataka kwenda kumuona.

      Latifa hakutaka kurudi nyumbani pasipo kumuona Ibrahim, kilichotokea, akaanza kupelekwa Magomeni Kagera alipokuwa akiishi Ibrahim. Walipofika huko, kijana yule mtanashati akaelekea katika nyumba hiyo na kumuita Ibrahim waliyemfuata.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      “Hayupo.”

      “Amekwenda wapi?”

      “Hatujui, labda rudini jioni-jioni hivi,” alisema mwanamke mmoja waliyemkuta, alikuwa mama yake Ibrahim.

      “Ila hapa si ndiyo kwao?”

      “Ndiyo!”

      “Basi nitarudi baadaye,” alisema Latifa.

      Hilo wala halikuwa tatizo, kwa sababu alikuwa amekwishapafahamu alipokuwa akiishi Ibrahim, akaahidi kurudi tena baadaye. Moyo wake ukaridhika, kitendo cha kuifahamu nyumba ile akajiona mshindi, alichokifanya ni kumpa Ibrahim yule shilingi elfu kumi nyingine na kuondoka.

      Ilipofika saa 11:03 jioni, Latifa alikuwa tena nyumbani hapo, muda huu, ulionekana kuwa bahati kwa upande wake, mvulana aliyekuwa akimtafuta, aliyetaka kumuona alisimama mbele yake, hakuyaamini macho yake kwamba yule kijana aliyeandika maneno matamu yaliyoutetemesha moyo wake ndiye huyo aliyekutana naye.

      Umasikini ulimtafuna mno Ibrahim, hakuonekana kuwa na uwezo kifedha kwani hata mavazi aliyokuwa ameyavaa, yalionyesha ni jinsi gani alivyokuwa masikini. Japokuwa alikuwa katika hali hiyo, kitendo cha kumuona Latifa tu kilimfurahisha, kikamrudishia furaha kubwa moyoni mwake.

      “Umependeza,” Ibrahim alimwambia Latifa mara baada ya salamu, tabasamu pana lilikuwa usoni mwake.

      “Nashukuru. Hapa ndiyo nyumbani?”

      “Ndiyo! Ninaishi na mama.”

      “Na baba yupo wapi?” aliuliza Latifa lakini Ibrahim hakujibu kitu, akabaki kimya huku uso wake ukibadilika na kuonyesha majonzi.

      “Pole sana Ibrahim,” alisema Latifa huku akimshika mkono Ibrahim kwa kugundua kwamba baba yake alikuwa amefariki dunia.

      “Usijali. Siamini kama umekuja kunitafuta, subiri, nina zawadi yako,” alisema Ibrahim huku akianza kupiga hatua kuelekea ndani.

      Wala hakuchukua muda mrefu, akarudi nje huku akiwa na karatasi moja kubwa, iliyokunjwa, akamgawia Latifa, alipoikunjua, akakutana na sura yake, picha iliyochorwa kipindi yupo hospitalini huku akiwa ametundikwa dripu.

      “Ni mimi?” aliuliza Latifa huku akichia tabasamu pana.

      “Ndiyo! Hiki ndicho kilikuwa kipindi kigumu nilichowahi kukutana nacho maishani mwangu, niliumia mno, sikutarajia kumuona msichana ninayempenda akiwa kimya kitandani. Latifa, barua imeeleza kila kitu, hii picha ni kama kupigilia msumari wa mwisho moyoni mwako juu ya upendo niliokuwa nao kwako,” alisema Ibrahim kwa sauti ya mahaba.

      Hapo ndipo Latifa alipogundua kwamba mbali na mvulana huyo kuwa na mapenzi mazito juu yake, pia alikuwa mchoraji mzuri. Alipoiangalia picha ile, haikuonekana kama imechorwa, ilionekana kama imepigwa kwa kamera. Latifa akashindwa kuvumilia, pasipo kutarajia, akajikuta akimsogelea Ibrahim na kumkumbatia.

      ****

      Walihisi kwamba wao ndiyo walikuwa watu wa kwanza duniani kupendana kama walivyokuwa wakipendana, muda mwingi walikuwa pamoja huku wakizungumzia mambo mengi ambayo kwa namna moja au nyingine yaliufanya upendo wao wa dhati uweze kukua na kuwa zaidi ya hivyo ulivyokuwa.

      Siku zikaendelea kukatika huku siku zikizidi kusonga mbele mpaka kufika siku ambayo wawili hao wakamaliza masomo yao ya kidato cha nne na hivyo kukaa nyumbani. Waliitumia nafasi hiyo kufanya mambo mengi likiwepo mapenzi ambalo kwa wao wote lilikuwa suala gumu mno.

      Matokeo yalipotoka, Latifa alikuwa amefaulu vizuri lakini kwa Ibrahim, hakuwa amefanya vizuri kabisa. Alionekana kuwa na majonzi lakini mpenzi wake, Latifa ndiye aliyekuwa mfariji wake namba moja, kila alipokuwa akiyafikiria matokeo yale, Latifa alimsogelea, alimkubatia na kumwagia mabusu mfululizo mashavuni mwake.

      Kidogo, moyo wake ulijisikia afueni huku hata matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne yakaanza kupotea kabisa.

      Kwa sababu bi Rachel alikuwa na mtoto wake aliyekuwa akisoma nchini Marekani, hivyo hakutaka Latifa aendelee kusoma nchini Tanzania, alichokifanya ni kuomba ruhusa kwa mzee Issa kwamba alitaka kumpeleka msichana huyo nchini Marekani.

      “Kwa hiyo unataka kumpeleka kwa Wazungu?” aliuliza mzee Issa huku akionekana kutokuamini alichokuwa akikisikia.

      “Ndiyo. Atakwenda kusoma katika shule anayosoma mtoto wangu,” alisema bi Rachel.

      “Sawa, hakuna tatizo, ila mtoto mwenyewe atataka?”

      “Nitaongea naye.”

      Hilo halikukuwa tatizo kwani hata Latifa alipofikishiwa taarifa hiyo, akakubaliana naye na hivyo kumwambia Ibrahim kwamba alitakiwa kuondoka nchini Tanzania na kwenda Marekani kusoma.

      “Mmmh!”

      “Nini tena mpenzi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      “Wazungu wananiogopesha mno, hawatoweza kunilia tunda langu?” aliuliza Ibrahim.

      “Najiamini, najitunza, hakuna kitu kama hicho, niamini,” alisema Latifa na kumkumbatia Ibrahim.

      “Ila usiache kuchora mpenzi, naamini utafanya makubwa mno,” alisema Latifa na Ibrahim kukubaliana naye.

      Hakukuwa na kipindi alichokuwa na huzuni kama kipindi hicho, Ibrahim hakuamini kama furaha yote na ya kipindi chote ndiyo ilitakiwa kuishia wakati huo.

      Japokuwa Latifa alijitahidi kumwambia Ibrahim kwamba kusingekuwa na kitu chochote ambacho kingebadilika na angeendelea kulitunza penzi lake, lakini Ibrahim hakuliamini hilo.

      Usiku hakulala, mawazo yake yalikuwa kwa Latifa tu. Aliwasiliana naye simuni na kumwambia juu ya wasiwasi wake wa kuporwa msichana wake lakini binti huyo aliendelea kumsisitizia kwamba alikuwa wake peke yake.

      Siku zikaonekana kukatika kwa kasi sana, siku ya safari ilipofikia, Ibrahim akaonekana kama mgonjwa, mpaka ndege ya Shirika la Ndege ya American Airlines inapaa, tayari machozi yalikwishambubujika vya kutosha mashavuni mwake.

      Ndege ilichukua saa kadhaa kufika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amsterdam ambapo wakabadilisha ndege na kupanda nyingine iliyowapeleka mpaka katika Jiji la Atlanta, sehemu ambapo Latifa alitakiwa kuanza masomo yake katika Shule ya St. Luis II iliyokuwa katikati ya jiji hilo.

      Siku ya kwanza tu ambayo alipelekwa shuleni hapo, wanaume wote wakapigwa na butwaa, msichana mgeni, kutoka barani Afrika katika nchi masikini ya Tanzania alionekana kuwa na uzuri usio wa kawaida.

      Alikuwa msichana wa Kichotara mwenye mvuto, hipsi zilizojaa na chini ya pua yake kuwa na kidoti kilichosindikizwa na vishimo viwili mashavuni mwake. Alimvutia kila mmoja.

      Siku hiyo akasajiliwa kuanza masomo shuleni hapo huku akiwa na mtu wake wa karibu, mtoto wa bi Rachel aliyeitwa Dorcas.



      Latifa akatokea kupendwa shuleni hapo kutokana na uzuri aliokuwa nao. Wanaume wengi walimtolea macho lakini hakukuwa na mtu aliyethubutu kumfuata. Hakukuwa na aliyefikiria kwamba msichana huyo alitokea nchini Tanzania, shule nzima walifikiri kwamba Latifa alitokea nchini Nigeria.

      Hakukuwa na Mzungu aliyetaka kuanzisha uhusiano na msichana yeyote wa Kinajeria, waliwafahamu wasichana hao, walikuwa wajanja na wengi wao walikuwa matapeli na kama ukiwa nao zaidi, kuna siku wanakuibia kila kitu ulichokuwa nacho.

      Ukaribu wa Latifa na Dorcas ukawapa wasiwasi zaidi, miongoni mwa watu waliokuwa wakorofi hata kuwasogelea alikuwa msichana Dorcas. Hakuwa msichana aliyewapenda wavulana, aliwachukia mno na chanzo cha kuwachukia kilikuwa ni jamaa aliyeitwa Michael Okonkwo, kijana wa Kinaijeria ambaye alimuibia vitu vyake vyote chumbani kwake zikiwepo fedha.

      “Kuwa makini Latifa,” alisema Dorcas.

      “Makini na nini?”

      “Wanaume! Wanaume wa huku ni wabaya sana, ukizubaa tu, umelizwa, hasa Wanaijeria” alisema Dorcas.

      “Usijali, nitakuwa hivyo.”

      Dorcas hakutaka kuishia hapo, alianza kumsimulia mambo yote yaliyokuwa yakitokea shuleni hapo likiwepo suala la Wanaijeria kuwa wezi na matapeli wakubwa. Latifa akaogopa, hakutaka kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu yeyote yule.

      Siku ziliendelea kukatika, alipoanza masomo ndipo watu walipojua kwamba mbali na uzuri aliokuwa nao, Latifa alikuwa mtu hatari darasani. Hakujali kama alikuwa katika ardhi ya ugenini, alichokuwa akikifanya ni kuwaongoza kwa alama nyingi darasani.

      Ndani ya miezi sita tu, tayari jina lake lilikuwa miongoni mwa wanafunzi waliokuwa na kipaji darasani. Hakusoma sana, muda mwingi aliutumia chumbani lakini kila ulipokuwa ukija mtihani, Latifa alitisha kwa kupata alama za juu.

      “Nataka uhusiano naye,” alisema jamaa mmoja, alikuwa mvulana mtanashati, Muhindi kutoka Jijini Mumbai nchini India.

      Liban alikuwa miongoni mwa watu waliovutiwa na Latifa, kila siku katika maisha yake alitamani kuwa karibu na msichana huyo. Alimpenda kwa moyo wake wote, hakuwa tayari kumuona msichana huyo akimkosa na ndiyo maana kila siku alikuwa akimtafuta katika rada zake.

      Kuwa na Latifa halikuwa jambo dogo, hakuingilika kwa kuwa tayari alikwishaambiwa maneno mengi na Dorcas juu ya tabia za wanaume wengi shuleni hapo. Moyo wake ulikuwa mgumu na hata Liban alipoanza kumchombezachombeza, Latifa hakuwa tayari.

      Mbali na hilo, bado kichwa chake kilimfikiria mpenzi wake Ibrahim aliyekuwa nchini Tanzania. Hakutaka kumsaliti, alijitahidi kuutoa moyo wake kwa hali zote lakini si kumsaliti mvulana huyo. Japokuwa alikuwa kijana masikini, moyo wake ulikuwa na hamu ya kuishi naye milele.

      ****

      Ibrahim akuwa na akili darasani, alifeli vibaya lakini mbali na akili hizo, Mungu alimpa kipaji cha uchoraji. Alipenda kuchora, kila siku katika maisha yake, asilimia kubwa alikuwa akitumia kuchora.

      Alitafuta ajira magazetini, alikataliwa kwa kuwa hakuonekana kama alifaa kufanya kazi hiyo ya uchoraji. Ibrahim hakutaka kuishia hapo, aliendelea kuchora zaidi huku mbele yake akiyaona mafanikio makubwa.

      Alichokifanya ni kutafuta sehemu maalum ya kufanyia kazi zake za kuchora. Hapo, akaandika bango kwa watu waliokuwa wakitaka kuchorwa, mteja wa kwanza kabisa kumpata alikuwa Nusrat, msichana wa Kiarabu aliyefika mahali hapo na kutaka kuchorwa huku akiwa na mpenzi wake.

      “Kiasi gani?” aliuliza Nusrat.

      “laki moja na nusu kwa mtu mmoja.”

      “Sawa. Chukua hii picha, naomba unichore hivihivi, picha iwe kwenye manila kubwa, nitakuja wiki ijayo kuichukua,” alisema Nusrat huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi hicho cha fedha na kumkabidhi Ibrahim.

      Macho ya Nusrat hayakutulia, kila alipokuwa akimwangalia Ibrahim, alionyesha kwamba alikuwa na kitu fulani moyoni mwake, hakutaka kukiweka wazi kwani alionekana kuwa na hofu kubwa kwa kuwa tu mpenzi wake alikuwa pembeni yake.

      Japokuwa hakutaka kuonyesha chochote kile, lakini ukweli ni kwamba alitokea kumpenda kijana huyo, hasa kipaji chake cha uchoraji ambacho kilimdatisha mno.

      Nusrat alikuwa msichana mrembo aliyevutia kwa kila kitu, macho yake malegevu, umbo lake la kimisi na hipsi zilizojaa vilizidi kuongeza uzuri wa muonekano wake.

      Japokuwa alipewa siku maalum kufika mahali hapo kwa ajili picha yake ingekuwa imekamilika lakini kwake ilionekana kuwa ngumu kusubiri. Alitokea kumpenda mno Ibrahim na asingekuwa tayari kuendelea kusubiri na wakati kila siku moyo wake ulikuwa kwenye mateso makali. Alichokifanya ni kuanza kuelekea kule alipokuwa akichorewa picha yake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      Kila siku alipofika hapo, alikuwa mtu wa kupiga stori tu huku muda mwingi akitumia kukaa mikao ya hasarahasara ili kumpagawisha Ibrahim. Kwa kijana huyo ilikuwa ni shida mno lakini akaamua kuvumilia kwani aliwajua wasichana vilivyo.

      “Unajua sana kuchora, hivi ulijifundisha au kipaji?” aliuliza Nusrat.

      “Kipaji tu. Mungu aliniumba nikiwa hivi,” alijibu Ibrahim.

      “Hongera sana wangu, unajitahidi sana,” alisema Nusrat.

      Kila siku akawa mtu wa kutoa pongezi tu kwa Ibrahim. Hakukuwa na siku ambayo hakwenda mahali hapo na kujifanya kuulizia picha yake na wakati moyoni mwake alimpenda.

      Alivumilia mno mpaka kikafika kipindi hakutaka kuendelea kuwa na uvumilivu, aliamua kuufumbua mdomo wake na kumwambia ukweli jinsi alivyokuwa akijisikia, kwamba alimpenda mno na hakuwa akilala kwa ajili yake.

      Ibrahim alivyoambiwa, hakushtuka, alilitegemea hilo kwani dalili za mvua zilikwishaanza kuonekana kwa mawingu kutanda angani, hivyo akachukulia suala hilo kuwa kawaida sana.

      “Umechelewa mno Nusrat, nina mtu tayari, ninampenda na ananipenda pia,” alisema Ibrahim.

      “Haiwezekani, sidhani kama nimechelewa Ibrahim. Nimetokea kukupenda, siwezi kukaa kimya kwani ninausababishia moyo wangu maumivu mazito, ninaomba uwe wangu, hata ukinifanya kuwa mtu wa pili, nitakuwa tayari kwa hilo lakini si kukukosa,” alisema Nusrat huku akionekana kuwa na uhitaji wa kuwa na kijana huyo.

      Msimamo wa Ibrahim ulikuwa uleule kwamba hakutaka kuwa na binti huyo kwa kuwa tayari alikuwa na mpenzi wake aliyeahidiana naye mambo mengi, Latifa.

      Siku zikaendelea kukatika, Nusrat hakukoma, alijua kwamba alikataliwa lakini hakutaka kuchoka, kila siku alifika mahali hapo na kuendelea kumwambia maneno matamu kwa kuamini kwamba kuna siku moyo wake ungebadilika na kukubaliana naye.

      Alipoona kwamba Ibrahim anaendelea kuweka msisitizo kwamba alikuwa na mpenzi wake, hapo ndipo alipotumia njia nyingine ambayo aliamini kwamba angefanikiwa kwa urahisi mno, akaanza kutumia zawadi.

      Kila alipofika hapo, alikuwa na vitu mbalimbali alivyoamini kwamba vingeweza kumpagawisha kijana huyo, kitu alichomwambia ni kwamba aliamua kumpa zawadi hizo kutokana na ugumu aliokuwa akiupata katika kumchorea picha yake.

      Siku za kwanza ilikuwa ngumu kukubaliana na msichana huyo lakini baada ya kulia sana huku akilalamika kwamba hakuwa akithaminiwa, Ibrahim akaamua kuzipokea zawadi hizo kama fulana, chokleti na hata wakati mwingine kuletewa fedha.

      Taratibu Nusrat akaanza kuyabadilisha maisha ya Ibrahim, kiasi kikubwa cha fedha alichokuwa akimpa, alikitumia katika kuyaendeleza maisha yake kwa kununua vitu vingi vya ndani na hata kulipia kodi ya chumba alichokuwa amepanga baada ya kuhama nyumbani.

      Kukataa kwake kuwa mpenzi wake, mwisho wa siku msichana huyo akasisistiza kwamba wawe marafiki wa kawaida ili kumtoa wasiwasi, Ibrahim akakubaliana naye pasipo kugundua kwamba hiyo ilikuwa moja ya njia aliyoitumia msichana huyo kumteka.

      Urafiki ulipokua, Nusrat akaanza kumuomba Ibrahim kutoa mitoko mbalimbali. Hilo halikuwa jambo gumu, kwa kuwa walikubaliana kwamba walikuwa marafiki tu, kijana huyo hakuwa na wasiwasi wowote ule.

      Kuwa karibu na Nusrat, kutoka na kwenda sehemu mbalimbali, kupokea zawadi zake na hata kuwa naye bize kwenye simu kuongea naye nyakati za usiku kukaanza kuubadilisha moyo wa Ibrahim. Taratibu akaanza kumsahau Latifa huku akiupa nguvu msemo usemao ‘Fimbo ya mbali haiui nyoka’.

      Baada ya ukaribu wao kudumu miezi miwili, mambo yakabadilika, wakaanza kubusiana na mpaka kubadilishana mate kitu kilichoufanya moyo wa Ibrahim kuendelea kumsahau kabisa Latifa, na miezi minne ilipokatika, akasahau kama alikuwa na msichana aliyeitwa kwa jina la Latifa, penzi la Nusrat likauteka moyo wake.



      Liban hakutaka kukata tamaa hata mara moja, alimpenda sana Latifa na hivyo asingeweza kukaa kimya na kuona msichana huyo akipita. Kila siku shauku yake kubwa ilikuwa ni kuzungumza na msichana huyo lakini hakuweza kuipata nafasi hiyo.

      Latifa hakuwa msichana mwepesi, hakuwa kama wasichana wa Kizungu ambao ukiwaambia kwenda kula chakula cha usiku, basi hukubaliana nawe na usiku huohuo kuwa wapenzi. Kwa Latifa, alitamani kuishi kama Mtanzania kwa kuamini kwamba lingekuwa jambo gumu kupatikana kwa kuwa alilelewa kama Mtanzania.

      “Ninampenda sana Latifa,” alisema Liban.

      Ni kweli moyo wake ulichanganyikiwa mno, japokuwa alipata nafasi ya kusoma na Latifa darasa moja lakini hakuwahi kupata nafasi ya kuzungumza naye, msichana huyo alionekana kuwa siriasi sana.

      Siku zikiendelea kukatika mpaka Liban aliposema kwamba imetosha, kama kuteseka, aliteseka mno, huo ukawa wakati wa kumfuata Latifa na kumwambia ukweli wa moyo wake, kama atakubali, awe mpenzi wake na kama atakataa, basi abaki na maumivu yake moyoni.

      “Ninakupenda Latifa,” alisema Liban kwa sauti ndogo aliyohakikisha kwamba aliitoa kimahaba.

      “Najua, unafikiri nilikuwa sijui! Najua sana.”

      “Nashukuru. Kwa hiyo inakuwaje?”

      “Kuhusu nini?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      “Kuwa nami.”

      “Haiwezekani.”

      “Kwa nini?”

      “Nina mpenzi wangu, ninampenda, ninamjali na kumthamini, mbaya zaidi, siwezi hata kumsaliti,” alisema Latifa.

      Hakuwa muongeaji sana, alipoona kwamba amemaliza kile alichokizungumza na Liban, akasimama na kuondoka zake. Maneno ya Latifa yalikwenda na maumivu makali moyoni mwa Liban, hakuamini kama angeweza kuambiwa maneno yenye kuchoma moyo wake kama yale.

      Alimwangalia Latifa alivyokuwa akiondoka, alionekana mrembo hasa lakini hakuwa na cha kufanya, kama kukataliwa, alikataliwa, ikambidi awe mpole tu.

      Siku zikaendelea kukatika, japokuwa kwa upande wa Tanzania, Ibrahim aliamua kuanza uhusiano wa kimapenzi na msichana mwingine lakini kwa Latifa hakutaka kabisa kufanya hivyo, hakujua kilichokuwa kikiendelea, hakujua kwamba mwanaume yule aliyempa moyo wake na kumsisitizia kwamba alitakiwa kuwa nao makini tayari alianza kuwa na mwanamke mwingine.

      Alimpenda mno, hakuwa akikaa zaidi ya saa moja pasipo kumbukumbuka. Kila alipoziangalia picha za Ibrahim, aliuhisi moyo wake ukiwa kwenye uhitaji mkubwa wa kuwa naye. Hakutaka kumsaliti, kwa jinsi alivyokuwa akimpenda, alihisi kwamba alionekana kila alipokuwa, yaani Ibrahim alikuwa akimfuatilia vilivyo.

      Darasani aliendelea kuongoza, mpaka mwaka mzima unamalizika na matokeo kutoka, Latifa alikuwa amefanya vizuri kuliko wanafunzi wote shuleni hapo, matokeo yake yakawa ni ya alama za juu na kufunika alama zilizowekwa na genius Michael Rudzic, Mrusi aliyewahi kusoma hapo mwaka 1967 ambaye alishikiria rekodi ya kufaulu kwa alama nyingi.

      “This is impossible,” (Hii haiwezekani) alisikika mwalimu mmoja mara baada ya kupata matokeo ya mitihani ile.

      “She has the highest scores than what Rudzic got in 1967, she has broken the Rudzic’s record and make her own record,” (Ana alama za juu zaidi ya alizopata Rudzic mwaka 1967, amevunja rekodi ya Rudzic na kuweka rekodi yake mwenyewe,) alisema mwalimu huyo huku akionekana kutokuamini, ikambidi avue miwani yake na kuyaangalia vizuri matokeo yale.

      Huo ndiyo ulikuwa ukweli, mara baada ya rekodi ya mwanaume genius kutoka nchini Urusi kudumu shuleni hapo kwa miaka mingi, hatimaye msichana kutoka Afrika, tena katika nchi iliyojiita Masikini, Tanzania alikuwa amefanya vizuri na kuvunja rekodi hiyo.

      Moto wake ulimuogopesha kila mtu, wanafunzi wengine wakaanza kumtolea macho kwa kuona kwamba msichana huyo alikuwa na akili za ziada. Mpaka shule zinafungwa nchini Marekani kwa kujiandaa na majira ya joto, tayari Latifa alijipatia umaarufu mkubwa shuleni hapo.

      “Tunarudi Tanzania,” alisema Dorcas.

      “Ahsante Mungu! Sasa ni wakati wa kumuona tena mpenzi wangu, nilimkumbuka sana, Mungu, naomba moyo wa kumpenda mara mia zaidi ya nilivyompenda kipindi cha nyuma,” alisema Latifa huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.

      Kwa wakati huo, alihisi moyo wake kuwa kwenye mapenzi mazito zaidi ya kipindi kilichopita, alimpenda mno Ibrahim na hakuwa tayari kumpoteza, kwake, mvulana huyo alikuwa na nafasi kubwa hata zaidi ya mtu yeyote yule.

      Siku ambayo walikuwa ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Americans Airlines, Latifa aliiona ndege ikichelewa kufika Tanzania, alitaka iende kwa kasi kuliko ilivyokuwa ikienda kwa wakati huo, muda wote mawazo yake yalikuwa kwa mpenzi wake, alimpenda na kumthamini sana.

      Moyo wake ulijawa na upofu, hakujua kile kilichokuwa kikiendelea nchini Tanzania, mvulana aliyekuwa akimpenda na kumthamini, mvulana aliyempa thamani kubwa ya moyo wake, aliyemfanya kumkataa Liban, wakati huo alikuwa kwenye mapenzi ya dhati na msichana wa Kiarabu, Nusrat.

      ****

      Latifa alikuwa kwenye presha kubwa, kitendo cha kufika nchini Tanzania, kesho yake akaanza kumtafuta Ibrahim kwenye simu. Ilikuwa kazi kubwa kwani kila namba aliyokuwa akimpigia miongoni mwa zile alizokuwa nazo, hakuwa akipatikana.

      Ilimuumiza mno, alitaka kumuona mpenzi wake kwa kuamini kwamba kwa kipindi hicho alikuwa mzuri zaidi, yaani tofauti na alivyokuwa kipindi cha nyuma. Hakuacha, kila siku alimtafuta simuni lakini matokeo yalikuwa yaleyale, hakupatikana.

      “Au alibadilisha simu? Hapana, inawezekana amezima tu,” alijiuliza na kujipa jibu.

      Si kwamba hakupafahamu alipokuwa akiishi kijana huyo, alipafahamu lakini kitu cha kwanza alichokitaka ni kumfanyia sapraizi juu ya uwepo wake nchini Tanzania kwa kuamini kwamba angeshtuka mno.

      Baada ya kukaa kwa siku mbili pasipo simu yake kupatikana, hapo ndipo alipoamua kwenda nyumbani kwao, Manzese kwa ajili ya kumuulizia, kwani tayari alikwishahisi kwamba kulikuwa na tatizo.

      “Hayupo, alitoka na msichana mmoja hivi, demu wake,” alisema msichana mmoja aliyemkuta katika nyumba hiyo ya kupanga.

      “Unasemaje?”

      “Amegonganisha magari nini?”

      “Unamaanisha nini?”

      “Kwani wewe nani?”

      “Naitwa Latifa.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      “Basi siyo wewe, yule anaitwa Nusrat, ni mzuri kama ulivyo wewe japokuwa umemzidi kidogo tu,” alisema msichana huyo.

      “Sijakuelewa unamaanisha nini.”

      “Kwani wewe ni nani kwake?”

      “Mpenzi wake.”

      “Kwa hiyo ana mademu wawili? Mmoja Muhindi na mmoja Mwarabu, kweli jamaa noma,” alisema msichana yule.

      “Bado anaishi hapa?”

      “Hapana, alihama, kahamia Magomeni.

      Latifa hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, akasimama na kuelekea ndani ya gari lake, hata kabla hajaliwasha, akauegemea usukani wa gari lile na kuanza kulia. Moyoni aliumia, hakuamini kile alichokisikia kwamba mpenzi wake, aliyempenda, aliyetumia muda mwingi kwa ajili yake, leo hii alikuwa katika uhusiano na msichana mwingine.

      Alilia na kulia, muda wote alijutia uamuzi wake wa kuwa na Ibrahim kiasi kwamba kuna wakati alijiona kuwa mtu mjinga alisiyestahili kupenda wala kupendwa.

      “Kwa hiyo ana mademu wawili!? Mmoja Muhindi na mmoja Mwarabu, kweli jamaa noma,” maneno ya dada yule yakajirudia kichwani mwake na kumfanya kuumiza zaidi.

      “Haiwezekani,” alisema Latifa na kuteremka garini.

      Akamfuata msichana yule na kumuomba amuelekeze alipokuwa amehamia, kwa kuwa hakuwa anapafahamu, akamuelekeza sehemu aliyokuwa akifanyia kazi yake ya kuchora, Latifa akarudi garini na kuanza kuelekea huko.

      Hakuwa makini barabarani, kichwa chake kilikuwa kimevurugika mno, mapenzi aliyoyapenda na kuyathamini, leo hii yalimfanya kubadilika na kuwa kama chizi. Alipofika karibu na Ubalozi wa Marekani, ilibakia kidogo tu agonge, bila utaalamu wa dereva mwenye gari ndogo, tayari angesababisha ajali.

      “Mungu wangu! Ni nini hiki?” alijiuliza huku akijishangaa.

      Aliendesha mpaka karibu na eneo ulipokuwa Ukumbi wa Maisha klabu ambapo kulikuwa na wachoraji wengi wa picha za kubandikwa ukutani. Hakutaka kuteremka, alibaki garini akianza kuangalia huku na kule kuona kama angeweza kumuona Ibrahim.

      Wala hakuchukua muda mrefu, mtu aliyekuwa akitaka kumuona maeneo hayo, alifanikiwa kumuona, alikuwa amekaa chini huku akichora kama kawaida yake. Japokuwa aliambiwa maneno mengi, lakini akajikuta akifarijika, kwa mbali uso wake ukaanza kuawa na tabasamu pana.

      Maneno yote aliyoambiwa na msichana yule yakaanza kupotea na kumuona mtu mbaya ambaye hakutaka kuuona upendo wake na Ibrahim ukiendelea kama kawaida. Huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana, akaushika mlango kwa ajili ya kuteremka.

      Hata kabla hajafanya hivyo, mara akamuona msichana mmoja mrefu, mrembo mwenye nywele nyingi mpaka mgongoni akitembea kumfuata Ibrahim, akaacha kutoka garini na kuangalia kwa makini.

      Msichana yule alipomfikia Ibrahim, akamfumba macho kwa nyuma kama wafanyavyo watoto na kisha kumbusu shavuni.

      Yalikuwa ni zaidi ya maumivu, yalikuwa ni zaidi ya moto mkali uwakao moyoni mwake. Moyo wake ukawaka moto, akahisi kama kulikuwa na mtu aliyemfuata huku akiwa ameshika msumali wa moto na kisha kuuchoma moyo wake.

      Kilichokuwa kikiendelea mahali pale, hakikuweza kuaminika moyoni mwake, hakuamini kama Ibrahim yuleyule aliyekuwa akimpenda na kumpa kila kitu alichotaka, leo hii alikuwa na msichana mwingine. Akashindwa kuteremka garini, akabaki humohumo na kuendelea kulia kama mtoto, picha aliyokuwa akiiona, hakika ilimuumiza.

      “Ibrahim....” alijikuta akiita, hakutaka kubaki garini, akatoka na kuanza kuwafuata huku akiwa na hasira kali.

      Latifa alitembea huku akiwa na hasira kali moyoni mwake, kile alichokuwa akikiona mbele yake, kiliuchoma moyo wake mno, akawa hataki kusikia la mtu yeyote yule, alichokitaka mahali hapo ni kumvamia Ibrahim na kupambana naye.

      “Ibrahim...” alimuita mvulana huyo.

      Ibrahim alipogeuka na macho yake kumwangalia Latifa, hakuzungumza kitu, hakuonekana kushtuka, alimwangalia msichana huyo, ghafla, tabasamu pana likaanza kuonekana usoni mwake, tabasamu lililoufanya moyo wa Latifa kuumia zaidi.

      “Ibrahim mpenzi, nini kimekupata? Mbona unanifanyia hivi? Au kwa sababu ulijua sipo karibu nawe?” aliuliza Latifa huku akilia kama mtoto.

      “Latifa! Mbona unakuja huku ukiongea hovyo kama chizi? Hebu punguza munkari kidogo, kaa chini, vuta pumzi mrembo,” alisema Ibrahim.

      Aliongea kidharau mno, sauti yake ilionyesha ni kwa jinsi gani alikuwa na dharau kwa msichana huyo. Alimwangalia kuanzia juu na kumshusha mpaka chini, kisha akampandisha tena.

      Mapenzi ya Nusrat yalimchanganya, akawa haoni, hasikii chochote kile, moyo wake ulitawaliwa na msichana huyo wa Kiarabu. Latifa aliongea sana, alilia sana lakini kila alipomwangalia, bado uso wake ulikuwa na tabasamu pana.

      “Umemaliza?” aliuliza Ibrahim, Latifa aliendelea kulia.

      “Unaifanyia hivi? Yaani leo unanifanyia hivi?”

      “Umemaliza?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      “Ibrahim...!”

      “Umemaliza?”

      Latifa hakuweza kunyamaza, siku hiyo ilikuwa ni siku mbaya maishani mwake, siku iliyouchoma moyo wake, hakuamini kile alichokiona, alimpenda mno Ibrahim, moyo wake ulitekwa na mvulana huyo, alimthamini, aliwakataa wanaume wengi kwa ajili yake.

      Mbali na hayo yote, alipoteza muda wake mwingi lakini mwisho wa siku, mvulana yuleyule aliyekuwa akimpenda, yuleyule aliyekuwa akimthamini alimfanyia jambo baya, alimsaliti kwa msichana mwingine wa Kiarabu, yalikuwa ni maumivu makali mno.

      “Acha kulia Latifa kana kwamba huyajui mapenzi. Mapenzi ni safari tu, mapenzi yanafanana na mchezo wa mpira, kuna wakati mwingine unachezewa faulo, yeah! Hata kwenye mapenzi faulo zipo, usitegemee dakika zote mchezo utakuwa na amani tu. Kwenye mapenzi, hizi ndiyo faulo, unaweza kumpenda asiyekupenda, au unaweza kumjali mtu asiyekuwa na habari na wewe, sasa unajiliza nini? Hebu nyamaza, endelea na safari, machozi yako hayaweza kuuahirisha mchezo huu, pigana dada,” alisema Ibrahim maneno yaliyoungwa mkono na Nusrat.

      “Kumbe ndiyo haka kadada ulikokuwa unakazungumzia?” aliuliza Nusrat.

      “Yeah! Ndiyo hakahaka, unakaonaje baby?”

      “Mmmh! Sasa kanajiliza nini?”

      “Achana naye. Hakujua kama fimbo ya mbali haiui nyoka? Hebu tuendelee na mambo yetu,” alisema Ibrahim.

      Alijua kwamba kuna watu waliumizwa mapenzini, alijua kwamba kuna watu walidharaulika kwa wapenzi wao, lakini kwa kile alichokuwa amefanyiwa siku ile, kilikuwa ni zaidi ya dharau, kilikuwa ni zaidi na maumivu makali moyoni mwake.

      Alimwangalia Ibrahim, hakutaka kuamini kama yule ndiye kijana yuleyule aliyekuwa akimfuatilia shuleni kwao, kijana mchafu, asiyejua hata kuchana nywele, mwenye nguo zilizochakaa, asiyekuwa na uwezo wowote ule.

      Leo, kijana huyohuyo aliyejaribu kuyabadilisha maisha yake ndiye aliyesimama mbele yake na kumletea dharau, moyo wake ulimuuma mno, kuna kipindi alihisi kama alikuwa usingizini, alikuwa akiota ndoto mbaya na muda mfupi angeshtuka kutoka usingizini.

      “Nashukuru, nashukuru Ibrahim,” alisema Latifa huku akirudi garini.

      “Poapoa, msalimie bwana Issa, mwambie naendelea vizuri,” alisema Ibrahim na hapohapo Nusrat kuanza kucheka, kicheko kilichotoka kwa dharau kubwa, kicheko kilichoongeza maumivu makali moyoni mwa Latifa.

      “Utakuja tu,” alisema Latifa, akaufungua mlango wa gari na kuingia ndani. Alichanganyikiwa kupita kawaida.



      Latifa alichanganyikiwa mno, kitendo cha kuona mpenzi wake aliyempenda na kumthamini akiwa amezama katika mapenzi ya mwanaume mwingine, moyo wake ulimuuma mno.

      Akaliegesha gari lake katika eneo la maegesho ya magari nyumbani kwao na kisha kuteremka. Akaanza kutembea harakaharaka kuufuata mlango wa kuingia ndani kwao. Mashavu yake yaliloanishwa na machozi yaliyokuwa yakimbubujika kwa maumivu makali, kwa kuwa hakukuwa na mtu mwingine ndani ya nyumba zaidi ya mfanyanyakazi wa ndani, akaingia chumbani kwake.

      Akakifuata kitanda, akakikalia na kuuchukua mto na kuuegemea huku akijifuta machozi yaliyokuwa yakimbubujika. Taswira za tukio lililopita ziliendelea kujirudia kichwani mwake kama mkanda wa filamu na kadiri alivyoendelea kukumbuka, aliumia zaidi.

      “Ibrahim....nimekufanya nini mpenzi? Kwa nini umeamua kuniumiza hivi? Kwa nini mpenzi? Naomba unionee huruma, rudi kwangu, ninaumia, naomba uje kunifariji,” alisema Latifa huku akilia kama mtoto.

      Huo ulikuwa mwanzo wa maumivu makali. Alimpenda sana Ibrahim na hakutaka kuona akiondoka kirahisi mikononi mwake. Alikumbuka kwamba alipoteza muda wake mwingi kumfikiria, aliwakataa wanaume wengi kwa ajili yake, leo kuona akiondoka mikononi mwake, tena kirahisi namna ile, lilikuwa jambo gumu mno.

      Alichokifanya, siku iliyofuata akaondoka na kurudi kulekule Osterbay, sehemu walipokuwa na wachoraji wengi, alitaka kumuona kwa mara nyingine Ibrahim kwani hakuamini kama kile kilichotokea jana kilikuwa cha kweli au la.

      Alipofika hapo, akamkuta Ibrahim akiwa peke yake, akateremka garini na kuanza kumsogelea. Kitendo cha Ibrahim kumuona Latifa, akakunja sura yake, hakufurahishwa na uwepo wake mahali hapo.

      Ibrahim hakumpenda Latifa, kitendo cha kusogelewa, akaanza kumtukana. Alimtukana na kumdhalilisha kwa kumuita malaya, kumshobokea mtu asiyempenda. Latifa aliumia sana lakini neno moja tu ndilo alilokuwa akimwambia kwamba alimpenda.

      “Ninakupenda,” alisema Latifa huku akilia kama mtoto na watu wakiwa wamesogea kuangalia kilichokuwa kikiendelea.

      “Huna hadhi ya kutembea na mimi, mbona unakuwa na shobo wewe binti, hebu jiangalie, una hadhi ya kutembea na mimi? Kama nilishawahi kutembea na wewe hiyo kitambo tu, sahau, hebu toka niendelee na kazi yangu,” alisema Ibrahim kwa sauti ya juu, watu wote waliokuwa wakipita njia, wakasimama, na hata waliokuwa wakiyaendesha magari yao, walipoliona tukio hilo, wakasimama na kuwaangalia.

      “Ninakupenda.....”

      “Mimi sikupendi. Tokaaaaaaa....”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      “Ninakupenda, ninakupenda Ibrahim, naomba usinifanyie hivi, kumbuka tulipotoka, kumbuka ulivyokuwa nyuma, yakumbuke maisha yako Ibrahim, msichana uliyenaye hakupendi, hata kama angeikuta hali uliyokuwa nayo zamani asingekupenda, Ibrahim, naomba ukumbuke, naomba vuta kumbukumbu mpenzi wangu,” alisema Latifa huku akianza kulia.

      “Nani mpenzi wako? Mimi mpenzi wako? Hebu toka huko, unaniambia kuhusu historia inanihusu nini?” alisema Ibrahim kwa dharau, tena akiona sifa kwa watu waliowazunguka.

      “Dada nenda zako tu, huoni aibu hilo limwanaume linavyokukashifu,” alisikika msichana mmoja akiongea, alionekana kushikwa na hasira.

      Bado Latifa hakuwa radhi kuondoka. Maneno aliyoongea Ibrahim yalimuumiza mno lakini hakutaka kuondoka kirahisi. Alijua fika kwamba mvulana huyo alikuwa akimpenda mno ila kutokana na uwepo wa Nusrat ndiyo uliombadilisha moyo wake. Hakutaka kukubali, alichokitaka kwa wakati huo ni kuyarudisha mapenzi ya Ibrahim kwake kitu kilichoonekana kuwa kigumu kama kudeki bahari.

      Kila alichokifanya kilishindikana, akarudi nyuma, akaingia garini, akapandisha vioo na kuanza kulia. Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kukataliwa na mvulana huyo, alipoliwasha gari lake na kuondoka, moyo wake ukajiahidi kwamba asingerudi tena mahali hapo.

      “Kuna nini? Mbona unalia sana?” aliuliza Dorcas.

      “Kichwa kinauma.”

      “Sasa ndiyo ulie namna hiyo?”

      “Ndiyo.”

      Alichokifanya Dorcas ni kutoka chumbani na kwenda kumchukulia dawa, akampa na kunywa. Bado kilio kiliendelea, hakunyamaza kwani kila alipokumbuka, moyo wake ulimuuma mno.

      Aliendelea na maisha yake nchini Tanzania, baada ya kukatika miezi miwili, yeye na Dorcas wakarudi nchini Marekani kuendelea na maisha huku moyo wake ukiwa na jeraha kubwa la mapenzi, chuki dhidi ya Ibrahim ikaanza kuchipua moyoni mwake.

      ****

      Kilikuwa kipindi cha baridi kali nchini Marekani, theluji zilidondoka ardhini na kuzifunika kabisa barabara kiasi kwamba ilikuwa ngumu mno kwa magari kupita kwani sehemu kubwa ya ardhi ilikuwa imefunikwa na theluiji hizo zilizoendelea kudondoka.

      Kilikuwa kipindi kibaya mno ambacho hakikupendwa na Wazungu wengi kwani kiliwapa tabu sana wakati wa kuelekea kazini hata vyuoni kutokana na msongamano mkubwa wa magari uliosababishwa na magari makubwa yaliyokuwa na kazi ya kusafisha barabara kwa kuziondoa theluji hizo.

      Katika kipindi hicho ambacho theluji zilikuwa zikidondoka, msichana Latifa alikuwa amejikunyata kitandani, alikuwa akihisi baridi kali mno kiasi kwamba hata lile branketi alilokuwa amejifunika aliona kutokumsaidia kabisa.

      Mbali na baridi hilo, mashavu yake yalilowanishwa namachozi yaliyoendelea kumbubujika kila alipokuwa akikumbuka kile kilichotokea nchini Tanzania. Mapenzi mazito aliyokuwa nayo moyoni mwake yaligeuka na kuwa sumu kali yenye kuumiza ambayo iliujeruhi moyo wake kwa kiasi kikubwa mno.

      Hakutaka kwenda darasani, alitamani kuendelea kubaki chumbani mule kwani kwa jinsi moyo wake ulivyokuwa kwa kipindi hicho, hakuona kama angeweza kusoma vizuri kutokana na jinsi alivyojisikia.

      Huku akiendelea kumfikiria Ibrahim na mambo yote aliyomtendea, mara simu yake ikaanza kuita, alipoichukua na kuangalia jina, alikuwa Liban, mvulana wa Kihindi ambaye hakuacha kumwambia kwamba alimpenda.

      “Where are you?” (Upo wapi?) lilikuwa swali la kwanza alilouliza Liban.

      “In my room. What do you want?” (Chumbani kwangu. Unahitaji nini?)

      “I want to see you,” (Nataka nikuone)

      “It is impossible, I’m busy, see you later, bye,” (Haiwezekani, nipo bize, tutaonana baadaye, kwa heri) alisema Latifa na kukata simu.

      Moyo wake uliwachukia wanaume, kila aliyekuwa akimwangalia, alimuona kuwa Ibrahim ambaye kwake alimchukulia kuwa na roho mbaya. Kwa Liban, hakubaki kimya, bado aliendelea kumpigia simu msichana huyo lakini hakuwa akiipokea kabisa.

      Liban hakuridhika, mara baada ya kuona simu yake haikuwa ikipokelewa, akaanza kumtumia meseji nyingi za kimapenzi huku akiendelea kusisitiza ni kwa jinsi gani alikuwa akimpenda msichana huyo.

      Kwa Latifa, ni kama moyo wake aliuvisha koti, hakutaka umuone mtu yeyote yule, alihitaji kuishi peke yake katika kipindi chote cha maisha yake. Mwaka huo ukakatika na mwingine kuingia.

      Hakutaka kurudi nchini Tanzania, alitaka kuendelea kuishi hukohuko hivyo akaomba ruhusa kwa mama yake mlezi, bi Rachel ambaye alimkubalia japokuwa moyoni alijisikia vibaya.

      Siku ziliendelea kukatika, uzuri wa latifa haukupungua, kila siku alionekana mrembo kupitiliza, wanaume waliendelea kumbabaikia lakini hakuwa radhi kuwa nao tena kipindi hicho.

      Baada ya kumaliza mwaka wa mwisho wa kusoma elimu ya sekondari ndipo alipoanza masomo ya biashara katika Chuo cha UCLA ((University of California, Los Angeles).

      Hapo, bado sifa za uzuri wake ziliendelea kuwa gumzo kila sehemu, watu hawakuacha kumsifia, kila alipopita, wanaume walibaki midomo wazi. Latifa hakuwa na habari na mtu, alihamia chuoni hapo peke yake baada ya kufanya vizuri katika masomo yake.

      Baada ya kusoma kwa mhula wa kwanza, akakutana tena na mtu aliyekuwa akimfuatilia sana toka kitambo, huyu alikuwa Liban. Latifa alipomuona tu, akashtuka, hakutegemea kumuona mwanaume huyo chuoni hapo.

      “Unafanya nini hapa?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

      “Nimekuja kusoma, kama wewe.”

      “Kumbe ulifaulu?”

      “Ndiyo! Nilipelekwa nchini India kusoma, ila nisingeweza kuwa mbali nawe, hata kama unanikataa, siyo tatizo, kukuona kila siku moyo wangu unafarijika,” alisema Liban maneno yaliyoanza kuubadilisha moyo wa Latifa.



      ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog