Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

PENZI BILA MAUMIVU - 2

 







    Simulizi : Penzi Bila Maumivu

    Sehemu Ya Pili (2)



    Alikuwa miongoni mwa matajiri wakubwa nchini Marekani ambao walimiliki mali nyingi huku akiwa na kiasi cha dola bilioni arobaini katika akaunti yake. Mwanaume huyu aliyekuwa na mke mmoja aitwaye Posh, alibahatika kupata watoto watatu tu katika maisha yake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikuwa na kila kitu alichokuwa akikihitaji, aliendesha magari ya kifahari na kununua nyumba zilizokuwa na hadhi ya kukaliwa na watu wenye fedha nyingi kama yeye.

    Mzee huyu aliyejulikana kwa jina la Garrett Warren alikuwa mfanyabiashara mkubwa aliyekuwa akijiingiza mamilioni ya dola kila siku. Maisha yake yalikuwa ya kifahari na alipendwa na watu wengi kwa kuwa tu alikuwa mtu wa kuisaidia jamii.

    Alimpenda Mungu, alivisaidia vyuo vingi vya dini, aliwasaidia watoto yatima na hata wale waliokuwa wakiishi katika maisha ya kimasikini. Katika mambo yote aliyokuwa akiyafanya, aliamini kwamba hakukuwa na mtu ambaye alifilisika baada ya kuwasaidia watu.

    Baada ya miaka mingi kupita huku akijihusisha na biashara mbalimbali, ndipo alipopata wazo moja kwamba ilikuwa ni lazima aanzishe kipindi maalumu kwenye luninga ili aweze kuwatafuta waimbaji bora nchini Marekani na kuwashindanisha huku mshindi akijinyakulia kitita cha dola milioni moja ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni moja kwa fedha ya Kitanzania.

    Wazo hilo likapitishwa, akamwambia mkewe ambaye alimpa jina la shindano hilo liitwe American Pop Idol. Alichokifanya, kupitia televisheni yake, akaanza kutangaza kwamba waimbaji walikuwa wakihitajika huku kiwango hicho cha fedha kama zawadi kikiwekwa wazi kitu kilichowachanganya watu wengi na hivyo kujisajili.

    Sehemu ambayo fainali ilitakiwa kufanyika ilikuwa jijini California ila mashindano madogomadogo yalitakiwa kufanyika katika kila jiji nchini Marekani. Ndani ya siku saba tu, tayari watu zaidi ya milioni moja walikuwa wamejiandikisha hivyo mchakato kuanza.

    American Pop Idol likawa shindano lililomuingizia kiasi kikubwa cha fedha kupitia matangazo na wadhamini, utajiri wake uliongezeka huku shindano hilo likichukua miezi sita na hatimaye mshindi wa shindano hilo kupatikana huku yeye kama yeye akiwa ameingiza kiasi cha dola bilioni tano.

    “This is good business, I thank God for giving me this idea,” (Hii ni biashara nzuri, asante Mungu kwa kunipa wazo hili) alisema bwana Warren huku akiangalia kiasi cha fedha kilichoingizwa ndani ya akaunti yake.

    Hakuishia hapo, bado alihitaji kutengeneza fedha zaidi, kila mwaka akawa na kazi ya kuandaa shindano ambalo lilimfanya kuwa maarufu huku likimuingizia fedha nyingi. Mwaka wa tano ulipofika baada ya mchakato wa usajili wa shindano hilo kuanza, hapo ndipo alipoamua kwenda nchini Tanzania.

    Alikwenda huko huku lengo lake kubwa likiwa ni kupanda mlima Kilimanjaro na kutembelea mbuga za wanyama pamoja na familia yake wakiwemo watoto wake, Laurent, Jessica na kaka yao mkubwa Smith.

    Walipofika huko, wakafanya kama walivyokuwa wamepanga na hivyo kutaka tena kusafiri mpaka Butiama, Musoma kwa ajili ya kuangalia makumbusho ya Mwalimu Julius Nyerere aliyezikwa huko.

    “Tunakwenda huko, lakini nina wazo,” alisema bwana Warren, alikuwa akimwambia mkewe huku safari ikiendelea.

    “Wazo gani?”

    “Tumejitahidi sana kufanya shindano la American Pop Idol nchini Marekani kwa kuwashirikisha Wamarekani, hivi hatuwezi kuwatafuta Watanzania wenye uwezo nao wakaenda huko kushindana?” aliuliza bwana Warren.

    “Inawezekana, lakini tutawapataje hao washiriki kutoka huku?”

    “Hakuna tatizo, nahisi tunaweza kwenda makanisani, huko, kuna waimbaji wengi tu, nahisi hatutoshindwa, halafu shindano letu litakuwa la kihistoria,” alisema bwana Warren.

    “Na mimi nina wazo.”

    “Lipi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa nini tusiwashindanishe Wamarekani na hawa Waafrika waliopo huku?” aliuliza bi Stellah.

    “Wazo zuri sana, tuanze mchakato.”

    Hicho ndicho walichokifikiria kwa wakati huo, walichokifanya mara baada ya kufika Musoma, moja kwa moja wakaanza kutembelea makanisani kutafuta waimbaji ambao waliwaona kustahili kushindana katika shindano lao.

    Ilikuwa kazi kubwa ambapo baadae wakaamua kuwaachia watu ili waendelee kuwatafuta waimbaji wengine wengi kwa ajili ya mchakato huo huku matangazo yakianza kutangazwa nchini Marekani kwamba shindano la American Pop Idol mwaka huo lingekuwa la aina yake kwani Wamarekani wangepata nafasi ya kushindana na Waafrika, kila mmoja akalisubiria kwa hamu.

    *****

    “Do you really want best singers?” (Hivi kweli mnahitaji waimbaji bora?) aliuliza jamaa mmoja, alikuwa akizungumza na bwana Warren.

    “Yes, we do. Do you know anyone who can sing?” (Ndiyo, tunahitaji. Unamfahamu yeyote anayeweza kuimba?) aliuliza bwana Warren.

    “Just wait,” (Subirini) alisema kijana yule na kusogea pembeni.

    Alichokifanya ni kuchukua simu yake na kupiga sehemu fulani, baada ya sekunde kadhaa, alikuwa akizungumza na mtu simuni. Alikuwa akimuuliza kuhusiana na muimbaji mmoja ambaye kwake alimuona kuwa bora zaidi, muimbaji huyo alikuwa Tatiana.

    Alipoambiwa kwamba msichana huyo alikuwepo kijijini, akawaambia Wazungu wale kwamba muimbaji huyo ambaye alikuwa bora kwa kipindi hicho, alikuwa kijijini. Safari yao ya kwenda Butiama ikasitishwa hivyo kuanza safari ya kuelekea Shinyanga.

    Hawakuchukua masaa mengi wakafika huko ambapo wakaanza kuelekea katika Kijiji cha Chibe. Ilikuwa safari ndefu na ya kuchosha mno lakini hawakutaka kukata tamaa, walihitaji kumuona muimbaji huyo ambaye aliendelea kusifiwa na kijana yule kwamba alikuwa na sauti nzuri mno.

    Walipofika Chibe, moja kwa moja wakaingia ndani kabisa ya kijiji kile na kijana yule kuwapeleka mpaka kwa mzee Sangiwa. Hapo, akaanza kuwaambia wazazi wa Tatiana kwamba wale walikuwa wageni wao na walikuwa hapo kwa kuwa walihitaji waimbaji wazuri.

    “Ila umewaambia kwamba binti yangu ni kipofu?” aliuliza mzee Sangiwa.

    “Hapana, sasa wewe si ndiyo uwaambie.”

    “Sasa kwani mimi najua Kizungu? Waambie wewe,” alisema mzee huyo na kijana huyo kuwaambia.

    “Wamesema hakuna tatizo, wanataka kusikia jinsi anavyoimba.”

    Hapohapo Tatiana akaitwa na kuanza kuambiwa juu ya ugeni ule, hakuamini kama kweli alisimama mbele ya Wazungu waliotaka aimbe ili kama atakuwa yupo vizuri basi wamchukue na kwenda naye Marekani, akafanya hivyo.

    Sauti yake kali ilimfanya kila mtu kutokuamini kama sauti ile ilikuwa ikiimbwa na mtu, walikwishazoea kuzisikia sauti zile kutoka studio ambazo zilichanganywa na mashine, lakini siku hiyo, wakakutana na msichana aliyekuwa akiimba kiasi kile.

    Hawakutaka kupoteza muda, Tatiana akaonekana kustahili kushirikia shindano hilo, walichokifanya ni kuomba kumchukua, hilo wala halikuwa tatizo.

    “Naomba wasimuuze binti yangu,” alisema bi Frida.

    “Hakuna tatizo, hakiwezi kutokea kitu kama hicho.”

    “Sawa. Tunakuamini.”

    Hakukuwa na cha zaidi mahali hapo, kwa kuwa walikuwa wamekwishakubaliana, walichokifanya ni kumwambia Tatiana ajiandae tayari kwa kusafiri na kuelekea nchini Marekani kushiriki shindano hilo lililoendelea kujinyakulia umaarufu huku kwa wakati huo, mshindi alitakiwa kuvuna dola milioni tano, zaidi ya bilioni kumi za kitanzania.

    Tatiana hakuonekana kuwa na raha, moyo wake ulikuwa ukimuwaza Peter tu. Alijua ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alikuwa akimpenda, alimthamini japokuwa alikuwa kwenye hali ya upofu.

    Alijua fika kwamba angeumia mno endapo angemwambia ukweli kwamba alitakiwa kusafiri kuelekea nchini Marekani, hivyo alichokifanya ni kubaki kimya tu.

    Baada ya mwezi mmoja wa maandalizi kufanyika, bwana Warren na mkewe, Stellah wakafika kijijini hapo na kumchukua Tatiana kwa ajili ya kuelekea nchini Marekani. Tatiana hakuamini kile kilichokuwa kikitokea, katika maisha yake yote hakuwahi kutoka nje ya kijiji kile, aliyapenda mazingira ya hapo lakini kitendo cha kuambiwa kwamba alitakiwa kuondoka, kilimsononesha mno.

    “Nakutakia ushindi mwema Tatiana,” alisema mama yake.

    “Asante mama. Naomba msimwambie Peter, akiniulizia, mwambieni ninampenda sana na hakuna zaidi yake. Namuahidi kuwa naye maisha yangu yote,” alisema Tatiana huku akilia.

    “Nitamwambia tu.”

    “Nitashukuru mama. Mwambie kwamba ninampenda....please mama mwambie kwamba ninampenda,” alisema Tatiana.

    “Nitamwambia kila kitu.”

    Hakukuwa na cha kupoteza mahali hapo, walichokifanya ni kuanza safari kuelekea Dar es Salaam ambapo huko wangechukua washiriki wengine watano na kukamilisha idadi ya washiriki ishirini kutoka mikoa mingine.

    Mchakato huo haukufanyika Tanzania tu bali kwenye kila nchi huku Waafrika elfu moja waliokuwa na uwezo wa kuimba vizuri wakitakiwa kwenda nchini Marekani kitu kilichoonekana kuwa faraja kwa familia zao, na wote hao waliwaombea watoto wao ushindi mkubwa kwani waliamini kwamba maisha yao yangebadilika.

    “Tunakwenda Marekani sasa, wewe unaitwa nani?” aliuliza msichana mmoja aliyekuwa amekaa na Tatiana.

    “Naitwa Tatiana, wewe?”

    “Mimi naitwa Maria. Nimefurahi kukufahamu,” alisema Maria.

    “Na mimi pia nimefurahi kukufahamu.”

    “Nikwambie kitu Tatiana?”

    “Niambie, kitu gani?”

    “U msichana mrembo sana, sijawahi kuona. Una sura nzuri mpaka nakuonea wivu,” alisema Maria.

    “Kweli?”

    “Hakika.”

    “Utukufu kwa Mungu,” alisema Tatiana, muda huo walikuwa kwenye ndege wakielekea jijini Dar es Salaam.



    Kwa jinsi uso wa Peter ulivyokuwa tu, tayari alionyesha kwamba muda wowote ule machozi yangeanza kumbubujika. Bi Frida akaanza kumuelezea kile kilichokuwa kimetokea mpaka binti yake kuchukuliwa na kuelekea nchini Marekani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Moyo wa Peter ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kile alichokisikia lakini kutokana na hali ilivyoendelea, hakuwa na jinsi kuamini kila kilichokuwa kikielezwa mbele ya masikio yake.

    Moyo wake ulinyong’onyea huku kipindi kingine akihisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kuwa na msichana huyo mrembo, hata nguvu ya kuendelea kukaa kijijini hapo hakuwa nayo tena.

    Angewezaje kukaa kijijini na wakati yule aliyemfanya kuwa mahali hapo hakuwepo? Kila alipofikiria kwamba ni kwa jinsi gani angeendelea kukaa kijijini hapo, akakosa jibu.

    “Kwa hiyo atarudi lini?”

    “Bado hatujajua, nahisi mpaka atakapotoka kwenye mashindano,” alijibu bi Frida.

    Kwa kuwa muda ulikuwa umekwishakwenda sana, Peter hakuwa na jinsi, siku hiyo akalala hapohapo kijijini japokuwa muda mwingi kitandani alikuwa na mawazo tele juu ya mpenzi wake huyo.

    Hakupata usingizi kwa haraka kama ilivyokuwa siku nyingine, alibaki akibimbirika kitandani tu, kila alipogeuka, taswira ya uso wa Tatiana ilikuwa ikionekana kichwani mwake jambo lililomfanya kukosa usingizi mpaka ilipofika saa kumi alfajiri.

    “Ninataka kuondoka,” alisema Peter, alikuwa ameamka asubuhi huku mwili wake ukiwa umechoka mno.

    “Mbona mapema?”

    “Sina amani kukaa hapa, Tatiana hayupo, unafikiri nitaendeleaje kuishi hapa mama?” aliuliza Peter.

    “Sawa, hakuna tatizo. Ila siku ya mwisho alivyoondoka alisema nikwambie kwamba anakupenda, anakupenda na kukupenda sana anataka umuoe na muishi pamoja,” alisema bi Frida.

    “Kweli?”

    “Ndiyo! Huo ndiyo ujumbe pekee alioniambia kuhusu wewe,” alisema mwanamke huyo.

    “Nashukuru, ninampenda pia.”

    Siku hiyo Peter hakutaka kuendelea kubaki kijijini hapo, alichokifanya ni kuondoka. Njiani alikuwa na mawazo tele, bado alimkumbuka Tatiana, lengo lake kubwa la kwenda kijijini kule lilikuwa ni kuonana naye, akae naye na kumuahidi mambo mengine mengi ambayo angejitahidi kuyafanya pamoja naye likiwepo suala la kumuoa na kuishi naye mpaka kifo kiwatenganishe.

    “Tatiana, ninakupenda mpenzi, naomba urudi haraka nchini Tanzania, hakika sitoweza kukusaliti, nakuahidi kuwa nawe maisha yangu yote,” alisema Peter huku akiangalia nje, mawazo juu ya Tatiana yalikuwa mengi mno.

    *****

    Ndege iliendelea kukata mawingu huku msichana Maria akiendelea kumsifia Tatiana kutokana na uzuri mkubwa aliokuwa nao. Sifa zile zikaendelea mpaka zikaonekana kumchosha Tatiana kwani kwenye kila sentensi kumi alizokuwa akiziongea Maria, aliingizia suala la uzuri wake.

    Safari iliendelea zaidi mpaka walipoingia Dar es Salaam ambapo wakapelekwa katika Hoteli ya Kilimanjaro na kisha kuambiwa kwamba walitakiwa kusubiri kwa wiki mbili mpaka mchakato wa kuwakusanya waimbaji wengine kutoka mikoa mbalimbali utakapokamilika.

    Huko, kila siku walikuwa wakichukuliwa na kupelekwa ufukweni ambapo walikuwa wakifanya mazoezi ya kuimba ili kujiweka sawa hata kabla ya kwenda nchini Marekani kwa ajili ya mashindano.

    Uzuri wa Tatiana ulikuwa gumzo mno, japokuwa alikuwa kipofu lakini alionekana kumvutia kila mtu. Mbali na uzuri wake, sauti yake ilikuwa nzuri ambayo ilizitetemeza ngoma za masikio ya kila mtu aliyekuwa akiisikia.

    Tatiana alikuwa kama kiongozi, kila walipokuwa wakiimba, yeye ndiye aliyechaguliwa kuwapanga wenzake na mpangilio wa sauti ukiwa sauti ya kwanza, ya pili, ya tatu mpaka besi.

    Maandalizi hayo yaliendelea kufanyika kila siku, asubuhi na mapema waliamka na kwenda katika ufukwe na kufanya mazoezi hapo. Kila mmoja alionyesha uwezo wake huku hata walimu ambao waliitwa mahali hapo mara kwa mara waliwapa mazoezi mazito ya sauti huku wakiamini kwamba mshindi wa shindano hilo angetoka mahali hapo.

    “Namfundisha mshindi wa shindano hili hapa,” alisema mmoja wa walimu ambaye alionekana kuwa mchangamfu mno.

    “Natumaini mshindi wa shindano hili atatoka hapa. Jamani, kuna siku mtanitafuta na kuniambia kweli mwalimu Luciana utabiri wako ulikuwa mkubwa. Mnakwenda Marekani, huko, wala msiogope, wale hawazaliwagi na vipaji, wale wanaingia darasani na kujifunza, ila nyie, niaminini, mna vipaji vya kuimba, na mshindi yupo kati yetu,” alisema mwalimu Luciana maneno yaliyomfariji kila mmoja.

    Mazoezi yaliendelea kila siku, badala ya wiki moja kama walivyoambiwa walichukua wiki mbili mpaka kumaliza mazoezi hayo huku wale waimbaji kutoka mikoa mbalimbali wakiwa wamekwishafika na kujumuika pamoja.

    Kila mmoja aliyekuwa akimwangalia Tatiana, alikiri kwamba msichana huyo alikuwa mzuri kwa umbo na sura japokuwa alikuwa kipofu.

    Tatiana alizoeana na Maria sana, yeye ndiye alikuwa rafiki wake wa dhati, kila alipokuwa, msichana huyo alikuwa pembeni yake na huku akichukua jukumu la kumuongoza kila alipotaka kwenda.

    Baada ya wiki mbili kutimia, bwana Warren akafika jijini Dar es Salaam, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuwaita na kisha kuwaweka katika chumba cha mkutano na kuanza kuzungumza nao.

    Alitumia muda mwingi kuwatoa wasiwasi na wajisikie huru na kwamba wangeweza kushindana mpaka kushinda, hata yeye aliamini kwamba mshindi wa shindano lile kwa mwaka ule angetokea barani Afrika japokuwa hakujua ni nchi gani.

    “Jua kwamba wewe ni mshindi, sijajua kwa nini, moyo wangu unaniambia kwamba mshindi wa shindano hili anatokea Afrika japokuwa sijajua ni nchi gani. Ila ninachoamini, mshindi anatokea katika kundi hili la watu,” alisema bwana Warren huku uso wake ukiwa na tabasamu tele.

    Baada ya wiki moja nyingine, washiriki hao wakapanda ndege binafsi ya bwana Warren na familia ya mzee huyo na kuanza safari ya kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya kushindana katika Shindano la kumtafuta kumtafuta mwanamuziki bora lililoitwa American Pop Idol, ila kwa kipindi hiki liliitwa America & Africa Pop Idol.

    *****

    Matangazo yalibandikwa kila kona nchini Marekani, mengine yakatangazwa sana kwamba lile shindano lililokuwa likisubiriwa kwa hamu, American & Africa Pop Idol lilikuwa limebakiza mwezi mmoja kabla ya kuanza.

    Watu waliokuwa na uwezo wa kuimba waliendelea kujiandikisha, kila mmoja alitaka kuonyesha uwezo wake na mwisho wa siku kuchukua kitita cha dola milioni tano kilichokuwa kimewekwa.

    Fedha zilikuwa nyingi mno na kila mmoja alizitolea macho. Maandalizi yaliendelea kufanyika zaidi huku Wamarekani wengi waliokuwa wamejiandikisha katika shindano hilo, waliwaita walimu wao waliokuwa na kazi ya kuwafundisha namna ya kuimba vizuri ili mwisho wa siku mmojawapo aweze kushinda kitita hicho cha fedha.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakukuwa na Mmarekani ambaye alitaka kuona fedha hizo zikichukuliwa na mtu mwingine kutoka nje ya Marekani, kwa sababu shindano lilikuwa lao, liliandaliwa nchini mwao na kufanyika humo, hivyo walifanya kila juhudi kuhakikisha kwamba hata fedha hizo zinakwenda katika akaunti ya mtu yeyote ila awe Mmarekani.

    Wakati ndege kutoka nchini Tanzania inawasili uwanjani, watu zaidi ya elfu tano walikuwa wamekusanyika mahali hapo kwa ajili ya kuwaona watu hao waliotoka barani Afrika tena katika nchi kama Tanzania ambayo haikuwa ikijulikana sana.

    Washiriki hao walipokuwa wakiteremka, kila mmoja alibaki akiwaangalia, kwa muonekano wao wa nje, walionekana kutokuwa na uwezo wowote ule jambo lililowapelekea Wamarekani wengi kuwadharau kwamba hawakuwa na uwezo wowote ule.

    Mbali na Watanzania hao waliokuwa wakiingia uwanjani muda huo, Waafrika wengine walikuwa wamekwishaingia na tayari walikwishaanza mazoezi katika Ukumbi wa Abraham Lincoln Theatre uliokuwa katika Jiji la California.

    Watanzania hao wakachukuliwa na kisha kupelekwa katika Hoteli ya Cassavana Hill iliyokuwa pembezoni mwa Ufukwe wa Julien. Huko, wakakutana na Waafrika wenzao ambapo moja kwa moja urafiki wao ukaanzia hapo huku wakijipa moyo kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kuchukua ushindi katika shindano hilo.

    “Where do you come from?” (Umetoka wapi?) aliuliza Maria.

    “ Monrovia, Liberia. My name is Nathan, my pleasure to meet you Maria) alisema mwanaume mmoja mwenye sura nzuri aliyekuwa akizungumza na Maria, rafiki yake Tatiana.

    Kwa kumwangalia, ungeweza kusema Nathan alikuwa Mtusi. Alikuwa mwanaume mrefu aliyekuwa na mwili mwembamba, sura yake, iliwavutia wanawake wengi waliokuwa wakimwangalia. Hakuwa mzungumzaji sana, alikuwa mkimya na mpaka alipokuwa akizungumza na Maria, msichana huyo ndiye aliyeanza kuzungumza naye.

    Moyo wa Maria ulikwishatekwa na kijana huyo, alipomwangalia kwa mara ya kwanza tu, alihisi moyo wake ukifurukuta, hakujiweza, alitokea kumpenda Nathan kupita kawaida na ndiyo maana alishindwa kujizuia kabisa.

    Mazoezi yalianza rasmi. Mbali na uzuri wa Nathan uliokuwa ukiwapagawisha wasichana wengi katika ukumbi huo lakini uzuri wa msichana Tatiana ndiyo uliokuwa gumzo zaidi. Alikuwa kipofu lakini uzuri wa sura yake ulimfanya kila mwanaume kuvutiwa naye.

    Tatiana hakuwa na habari, kitu pekee alichokuwa akikifahamu ni kwamba alifika nchini Marekani kwa kuwa tu kulikuwa na shindano la kumtafuta muimbaji bora, suala la kuwadatisha wanaume wengi wala hakulifahamu.

    “I can’t tolerate, I must see her,” (Siwezi kuvumilia, lazima nikutane naye) alisema Nathan.

    “Whom do yo want to see?” (Unataka kumuona nani?)

    “Sorry man! I miss my home buddy,” (Samahani bwana! Nimepakumbuka nyumbani mshikaji) alisema Nathan.

    Alikuwa na mawazo juu ya Tatiana tu kiasi kwamba alijikuta akiropoka pasipo kujua kwamba kijana aliyekuwa naye karibu alikuwa amemsikia na hivyo alitaka kufahamu mtu aliyetaka kumuona. Uvumilivu ukamshinda Nathan, akajikuta siku hiyohiyo akimfuata msichana Tatiana kwa ajili ya kuzungumza naye tu, alitaka kumwambia ukweli wa moyo wake kwamba alikuwa akimpenda sana.

    “Tatiana....” aliita Nathan.

    “Nathan...” aliita Tatiana, Nathan akashtuka.

    “Umenijuaje?”

    “Nimeweza kukujua tu, nawajua wote humu ndani.”

    “Umenishangaza sana. Umejiandaaje na ushindani?”

    “Kawaida tu, nataka dunia iamini kwamba nina kipaji cha kuimba. Siangalii fedha zao, ningependa nionyeshe uwezo wangu tu,” alijibu Tatiana.

    “Kwa hiyo hutaki fedha?”

    “Unapokuwa na kipaji, fedha zitajileta tu, ngoja niionyeshe dunia kwamba kulekule nchini Tanzania, tena kijijini kabisa kulikuwa na mtu aliyekuwa na kipaji cha kuimba,” alisema Tatiana.

    Kila alipokuwa akizungumza, Nathan alikuwa akimwangalia Tatiana usoni tu, bado kichwa chake kilikuwa kikijiuliza kama kweli msichana aliyekuwa na uzuri ule alipatikana kweli duniani au alikuwa ameshushwa kutoka Mbinguni.

    “Nathan...” aliita Tatiana.

    “Naam.”

    “Naomba usiniangalie sana, nasikia aibu,” alisema Tatiana.

    “Nisikuangalie sana?”

    “Ndiyo!”

    “Kwani nilikuwa nakuangalia sana?” aliuliza Nathan huku akishangaa msichana huyo alijuaje.

    “Ndiyo!”

    Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa ukaribu wao. Wasichana wengi walionekana kuumizwa na ukaribu wa Tatiana na Nathan kwa kuwa kila mmoja alitaka kuwa karibu na mvulana huyo aliyekuwa na sura nzuri.

    Kwa Maria ndiye aliyeonekana kukasirika zaidi, wivu mkali ukamkamata moyoni mwake, alimpenda mno Nathan na hakutaka mvulana huyo awe na msichana yeyote zaidi yake.

    Kitendo cha Tatiana kuanzisha ukaribu na Nathan tayari kwake kukawa na maumivu makali ya moyo kiasi kwamba kila alipokuwa akiwaona, alisikia kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake.

    Taratibu chuki ikaanza kujengeka dhidi ya Tatiana, hakutaka kumshikia fimbo yake na kumuongoza tena kama ilivyokuwa zamani, alichokifanya ni kumsusa hivyo Nathan kuchukua jukumu hilo ambalo likamfanya kuwa karibu zaidi na msichana huyo.

    Siku zikaendelea kukatika, japokuwa kila mmoja alikuwa muimbaji lakini waliikubali sauti ya Tatiana ambayo iliwasisimua wote waliokuwa wakiisikia. Sauti ile ikawavunja moyo na kuona kwamba ilikuwa ni lazima wao kuwa wasindikizaji na msichana huo kuchukua ushindi katika shindano hilo.

    “Unajua kuimba,” alisema Nathan.

    “Nashukuru! Hata wewe unajua.”

    “Najua ila si kama wewe. Unanifurahisha sana, unautetemesha mtima wa moyo wangu kila nikusikiapo,” alisema Nathan huku akimshika mkono Tatiana pale walipokaa, Tatiana akashtuka.

    “Nathan! Kuna nini?”

    “Sikiliza Tatiana!”

    “Kuna nini?”

    “Nimeshindwa kuvumilia.”

    “Kuvumilia nini?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nataka nikwambie ukweli wa moyo wangu,” alisema Nathan.

    “Ukweli upi?”

    “Kwamba ninakupenda.”

    “Unanipenda?”

    “Ndiyo! Ninataka nikuoe kama ikiwezekana,” alisema Nathan, moyo wa Tatiana ukapiga paaaaaaa!

    “Unataka......”

    “Nikuoe! Usiwe na wasiwasi, ninataka niwe nawe, haijalishi tutaishi wapi, ukitaka Tanzania, sawa, Liberia, sawa pia ila ukweli, popote pale lakini mwisho wa siku nataka kuwa na wewe, uwe mama wa watoto wangu,” alisema Nathan, hapohapo Tatiana akaanza kububujikwa na machozi, maneno aliyoongea Nathan, yaliugusa moyo wake



    Peter alikuwa na mawazo tele juu ya mpenzi wake ambaye kwa kipindi hicho hakuwepo nchini Tanzania. Kila wakati, alionekana kuwa na mawazo mengi huku wakati mwingine akijilaza kitandani kwa ajili ya kupata usingizi lakini haukuweza kuja kabisa.

    Alimpenda mno Tatiana kuliko msichana yeyote yule, alimthamini sana lakini mwisho wa siku aliamua kuondoka nchini Tanzania pasipo kumuaga. Moyoni aliumia lakini hakuwa na jinsi, aliamua kukubaliana na hali iliyojitokeza na hivyo kuaanza kumsubiria.

    Aliposikia kwamba kulikuwa na shindano kubwa la muziki lilitaka kuanza nchini Marekani, akili yake ikamwambia kwamba hicho ndicho kilichopelekea msichana wake kuchukuliwa na kupelekwa nchini Marekani.

    Alichokifanya, kwa kuwa lilikuwa likitangazwa sana, ndipo alipoamua kuanza kufauatilia kwenye mitandao juu ya washirika ambao wangeshiriki katika kinyang’anyiro hicho.

    Zaidi ya watu elfu kumi walikuwa wamejiandikisha ila alichokifanya ni kwenda kwenye sehemu ya watu kutoka barani Afrika, hapo ndipo alipoliona jina la msichana wake, Tatiana.

    Akalibonyeza jina hilo, picha ya Tatiana ilitokea. Alichanganyikiwa, uzuri wake ukampagawisha zaidi kiasi cha kuona kama alikuwa akiibiwa mali yake huko nchini Marekani.

    Akakosa raha, moyo wake ukapoteza amani, alichokifanya ni kuanza kumuomba Mungu ili kama itawezekana basi aweze kumlinda na kusitokee mtu yeyote yule kulichukua penzi lake

    “Natumaini atarudi tu, nitataka nimwambie ukweli kwamba nimeshindwa kuvumilia, hata kama itawezekana, aje kulala nyumbani,” alisema Peter.

    *****

    Nathan akapata wakati mgumu wa kumbembeleza Tatiana na kumfuta machozi yaliyokuwa yakimtoka. Aliguswa na machozi yale, hakutaka kuona msichana huyo akilia huku yeye akiwa moja ya sababu iliyomfanya kuwa hivyo.

    Alijaribu kumbembeleza lakini hakuacha kumwambia ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake. Mapenzi ya msichana huyo yakamlevya, hakutaka kusikia kitu chochote kwa wakati huo zaidi ya kuwa na Tatiana tu.

    Siku zikaendelea kukatika, wiki zikasonga mbele na hatimaye siku ambayo watu walikuwa wakiisubiria kwa hamu kufikia. Watu elfu kumi waliokuwa wamejiandikisha nchini Marekani, wakachunjwa mpaka kufika watu elfu moja, kwa maana hiyo, Afrika ilitoa watu elfu moja na Marekani ikatoa idadi hiyo ya watu.

    “Kesho ndiyo kesho, mpambano unaanza,” alisema mtangazaji mmoja wa Redio ya Number One.

    Siku iliyofuata, mpambano mkali wa kuimba ukaanza. Majaji waliandaliwa kwa ajili ya kuanza kazi zao. Kila mmoja alikuwa makini katika uimbaji, watu wengi waliokuwa wakisimama mbele ya jukwaa katika ukumbi waliopangiwa alikuwa makini kuhakikisha kwamba hatoki nje ya biti.

    Zaidi ya watu elfu tano walikuwa wakikusanyika ndani ya ukumbi huo, televisheni nyingi za Marekani zilikuwa zikionyesha shindano hilo lililovuta hisia za watu wengi duniani kwa kipindi hicho.

    Ka sababu alihitajika mtu mmoja tu, watu wakaanza kuchujwa. Kila mtu aliyeambiwa kwamba asingeweza kuendelea, alikuwa akilia tu huku wale waliofanikiwa kuvuka wakiwa watu wenye furaha kwa kuona kwamba wanakaribia kunyakua kitita kile cha fedha.

    “You are the best Tatiana,” (Wewe ni bora Tatiana) alisema jaji mmoja, alikuwa akimwangalia Tatiana aliyesimama jukwaani huku mkononi akiwa na kipaza sauti, alikuwa amekwishamaliza kuimba.

    Uwezo wa Tatiana ulikuwa gumzo kwa kila mtu aliyekuwa akilifuatilia shindano hilo, watu wengi walivutika kwa ajili ya kumsikiliza Tatiana aliyeonekana kuwa na kipaji hasa cha kuzaliwa.

    Sauti yake ilikuwa na mvuto, watu wengi walikuwa wakikifuatilia kipindi hicho kwa kuwa tu kulikuwa na msichana aliyekuwa na sauti nzuri na kali hata zaidi ya mwanamuziki Celine Dion.

    Wamarekani wakaanza kumuogopa Tatiana kwa kuwa ndiye aliyeonekana kuwa kizuizi kikubwa katika kuuchukua ushindi huo. Washiriki wao walikuwa wazuri lakini kila wapokuwa wakimsikiliza Tatiana, msichana huyo alionekana kuwa moto wa kuotea mbali.

    Hawakujua ni kitu gani walichotakiwa kufanya ili heshima ibaki nchini kwao. Hawakutaka kutulia, baadhi yao, kitu walichoona kufaa kufanywa ni kucheza na majaji wale tu.

    “Jamani huu si mchezo wa chumbani, kumbeba mtu yeyote yule litakuwa kosa kubwa kwa kuwa shindano linaonekana dunia nzima,” alisema jaji mmoja.

    “Sasa unataka ushindi uende kwa mtu ambaye si Mmarekani?”

    “Tunaangalia uwezo wa mtu tu, vinginevyo, heshima ya shindano hili litashuka,” alijibu jaji huyo.

    Stori za kutaka kupewa ushindi Wamarekani zikaanza kuvuma, zilisikika kila kona na mwisho wa siku kumfikia bwana Warren aliyeonekana kupandwa na jazba.

    Alichokuwa akikiangalia kwa wakati huo ni fedha tu, kitendo cha kusema fulani alikuwa mshindi na wakati watu wote waliona kilichokuwa kikiendelea ilikuwa ni sawa na kulishusha thamani shinano hilo.

    Alichokifanya ni kuwaita majaji na kuongea nao. Japokuwa aliwaonya sana lakini bado tetesi zikaanza kusikika kwamba lile suala la kuibeba nchi ya Marekani lilikuwa palepale hivyo kuamua kuwaondoa majaji hao na kuwaleta wengine.

    Alichokuwa akikihitaji ni heshima ya shindano tu, alikwishajua kwamba endapo wangepata mshindi aliyeonekana kutokufaa basi sifa ya shindano hilo ingeshuka hivyo hata wadhamini kulipuuzia, kabla ya kitu hicho kutokea, akaamua kuwawahi kwa kuwaondoa majaji hao.

    Kati ya watu elfu kumi waliokuwa wakishindana katika kinyang’anyiro hicho, ni watu mia tano tu ndiyo waliokuwa wamebaki. Mpaka kufika hapo, tayari idadi kubwa ya washiriki walikuwa wamekwishaondoka nyumbani kwao hivyo wale waliobakia wakachukuliwa na kupelekwa Las Vegas kulishuhudia jiji hilo.

    Si Tatiana wala Nathan, wote wawili walikuwa wamebaki ndani ya kinyang’anyiro hicho, uwezo wao katika uimbaji ulikuwa mkubwa kiasi kwamba kila mtu alikuwa akiwahofia. Ukaribu wao haukupungua, kila siku bado waliendelea kuwa pamoja huku msichana Maria ambaye naye alinusurika kutolewa zaidi ya mara tatu akiendelea kuumia moyoni mwake kiasi kwamba uwepo wake ndani ya nchi hiyo uligeuka na kuwa maumivu makubwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Washiriki wakapangiwa hoteli nzima ya nyota tano jijini humo, watu wawili walilala katika chumba kimoja kwa staili ya ‘double’. Japokuwa bwana Warren alitumia fedha nyingi lakini aliingiza kiasi kikubwa cha fedha kiasi cha kufanya utajiri wake kuongezeka.

    Huku akiwa chumbani kwake, mara Tatiana akaanza kusikia simu ikiita. Hakuweza kuinuka kwenda kuipokea zaidi ya msichana aliyekuwa naye chumbani humo, Angelia ambaye alikuwa Mmarekani kwenda kuipokea na kuanza kuzungumza na mtu wa upande wa pili.

    “Naweza kuzungumza na Tatiana?” ilisikika sauti kutoka mapokezini.

    “Bila shaka. Wewe nani?”

    “Ni dada wa mapokezi hapa. Kuna mgeni wake,” alisikika dada huyo wa mapokezi.

    “Mgeni gani?”

    “Smith Warren,” alisikika.

    Hapohapo Angelina akamfuata Tatiana na kumuinua kitandani kisha kumuongoza mpaka katika simu ile kwa lengo la kuzungumza na msichana wa mapokezi. Kitu kikubwa alichokisema ni kwamba kulikuwa na mtu ambaye alikuwa akihitaji kumuona kwa wakati huo, mtu huyo aliitwa Smith.

    Hilo halikuwa tatizo, alimfahamu Smith kama mtoto mkubwa wa bwana Warren. Mara ya kwanza kumuona kijana huyo ilikuwa nchini Tanzania kipindi walichokuja kwa ajili ya kumfuata, hivyo kwake hakuwa na wasiwasi hata kidogo.

    Angelina akamuongoza mpaka mapokezini, hapo, Smith alikuwa akimsubiria kitini. Alipomuona tu msichana huyo, akasimama, uso wake ukaachia tabasamu pana na kuanza kuwasogelea.

    “Tatiana, habari yako!” alisema Smith huku akiwa ameachia tabasamu pana.

    “Salama tu, u mzima Smith?”

    “Nipo poa. Tunaweza kutafuta sehemu tukakaa na kuzungumza?” aliuliza Smith.

    “Kuna nini? Kuna tatizo limetokea nyumbani?”

    “Wewe twende, utajua hukohuko, ila usihofu, ni jambo la kawaida tu,” alisema Smith hivyo kuanza kumuongoza msichana huyo huku akimwambia Angelina arudi tu chumbani kuendelea na mambo yake.

    Smith akamchukua Angelina na kwenda naye katika mghahawa mdogo uliokuwepo hotelini hapo. Wakiwa hapo, akaagizia kahawa na Tatiana akiagizia maziwa na kuanza kunywa. Muda wote huo Smith alibaki akimwangalia msichana huyo kwa umakini sana.

    “Smith...!”

    “Tatiana....!”

    “Kuna tatizo?”

    “Hapana, hakuna tatizo.”

    “Sasa kuna nini?” aliuliza Tatiana.

    “Usiwe na pesha, kunywa kwanza, kuna mengi ya kuzungumza nawe,” alisema Smith.

    “Mmmh!”

    “Ndiyo hivyo!”

    ****

    Kwa jina aliitwa Smith Warren, alikuwa mtoto wa kwanza wa bilionea Warren ambaye kwa kipindi hicho alikuwa tajiri wa ishirini duniani. Smith alikuwa kijana mpole, mtaratibu sana aliyesoma kwa kiwango kikubwa.

    Akiwa na umri wa miaka ishirini na tatu, tayari alikuwa na digrii mbili za biashara kutoka katika Chuo cha Mississippi cha nchini Marekani kitu kilichomfanya kuziendesha baadhi ya biashara za baba yake pasipo tatizo lolote lile.

    Wanawake walimpenda Smith kwa kuwa alikuwa mtoto wa bilionea hivyo waliamini kama wagekuwa naye basi maisha yao yangekuwa mazuri. Smith hakuwa na habari na msichana yeyote yule, kitu pekee alichokuwa akikifikiria kwa wakati huo ni kusoma zaidi na kufanya mambo mengine hasa kusimamia biashara za baba yake.

    Siku ziliendelea kukatika mpaka siku ile alipoambiwa na wazazi wake kwamba walitakiwa kwenda nchini Tanzania kwa lengo la kutembelea mbuga za wanyama na kupanda Mlima Kilimanjaro.

    Kwake ilikuwa ni furaha tele, hakuwahi kufika nchini Tanzania hivyo kufika huko kungemaamaanisha kwamba angekuwa na furaha zaidi kwa kubadilisha hali ya mazingira, hasa hali ya hewa,

    Walipofika huko, wakafanya kila kitu na hata wazo la kuliboresha shindano la American Pop Idol lilipotolewa, kwake aliliona wazo zuri kufanyika. Walifanya kila kitu kilichotakiwa kufanywa, siku ambayo waliambiwa kwamba kulikuwa na msichana aliyekuwa akiimba sana, akajikuta akiwa na kiu ya kutaka kumuona msichana huyo.

    Wakaelekea Shinyanga mpaka katika Kijiji cha Chibe, alipomuona msichana huyo, uzuri wake na sauti yake, akajikuta akianza kumpenda kwa mapenzi ya dhati.

    Uzuri wa Tatiana ukamchanganya mno, hakuamini kama angeweza kukutana na msichana mrembo kama alivyokuwa Tatiana tena akiwa ndani ya nchi masikini kama Tanzania.

    Alibaki akimwangalia Tatiana ambaye alikuwa kipofu, moyo wake ukazama katika penzi la dhati hali ambayo hakuwahi kuihisi tangu azaliwe. Alijitahidi kuvumilia lakini kamwe hakuacha kuuthaminisha uzuri wa Tatiana.

    Siku hiyo waliporudi hotelini, mawazo yae yalikuwa juu ya msichana huyo aliyeonekana kuwa na uzuri wa ajabu. Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndicyo ambavyo alizidi kumpenda msichana huyo kwa mapenzi ya dhati kutoka moyoni mwake.

    “I really love her from the bottom of my heart,” (Ninampenda sana kutoka katika mtima wa moyo wangu) alisema Smith huku akionekana kulewa kwa penzi juu ya msichana huyo kipofu.

    Siku zikakatika mpaka ile siku ambayo waliamua kurudi nchini Marekani. Katika kipindi chote hicho alikuwa akimfuatilia msichana huyo ambaye aliendelea kuuteka moyo wake vilivyo.

    Walipofika Marekani, alipewa kazi kubwa ya kufuatilia biashara mbalimbali za baba yake nchini Urusi na China. Kila kitu alichokuwa akikifanya kwa wakati huo alikifanya harakaharaka ili amalize na kurudi nchini Marekani kumuona Tatiana ana kwa ana.

    Akiwa nchini Urusi, alilifuatilia shindano la American & African Pop Idol katika televisheni, uwezo wa Tatiana ulimshangaza, alifahamu kwamba alijua kuimba lakini katika shindano hilo alionekana kuwa moto wa kuotea mbali.

    Kila siku alikuwa akiwaita marafiki zake aliokuwa nao nchini Urusi na kuwaambia waangalie kile kilichokuwa kikiendelea, aliwaamia kwamba alimfahamu sana Tatiana na walimtoa barani Afrika tena ndanindani kabisa kitu walichokikataa marafiki hao kwa kuamini kwamba msichana huyo alitoka Afrika Kusini.

    Alihakikisha anafanya vitu vyote mpaka alipomaliza na ndipo alipoamua kurudi nchini Marekani ambapo akapata nafasi ya kuendelea kulifuatilia shindano hilo kwa ukaribu zaidi.

    Ili kuonyesha ni jinsi gani alikuwa amedata kwa penzi la msichana huyo, kila siku alikuwa akielekea sehemu ya mazoezi, alipofika huko, alikuwa kimya pembeni akiwaangalia wanamuziki hao waliokuwa wakifanya mazoezi kwa nguvu zote.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ukaribu wa Tatiana na Nathan ukamtia mashaka, ukamfanya kuanza kuona wivu kupita kawaida, kila alipokuwa akiwaangalia, ukaribu ule ukaanza kumuumiza mno. Hakujua kama watu hao walikuwa wapenzi au marafiki kama walivyokuwa wengine, alichokifanya ni kuanza kufuatilia.

    Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumfuatilia Nathan. Akagundua kwamba mvulana huyo alikuwa ametoka nchini Liberia katika Jiji la Monrovia hivyo hakuwa na haki ya kuwa na msichana huyo kwani yeye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kumuona nchini Tanzania.

    Hakutaka kuendelea kuumia zaidi, alichokifanya ni kuanza mishemishe za kuonana na Tatiana. Siku ambayo walichukuliwa na kupelekwa katika Jimbo la Nevada ndani ya Jiji la Las vegas, hapo ndipo alipoamua kumfuata hotelini ili japo apate nafasi ya kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.

    Alipokwenda hotelini na kuitiwa msichana huyo, mapigo yake ya moyo yakaanza kumdunda mno, akahisi akizidi kumpenda msichana huyo zaidi ya kipindi kilichopita. Kila alipokuwa akimwangalia, uso wake ulijawa na tabasamu pana kiasi kwamba akajiona kushindwa kuvumilia kwa mapenzi yake.

    “Niambie kuna nini,” alisema Tatiana huku akinywa maziwa aliyoletewa.

    “Tatiana...”

    “Abeeee.”

    “Kuna kitu ninataka kukwambia, nimeshindwa kuvumilia, naomba nijiweke wazi kwamba nina....” alisema Smith na kukaa kimya.

    “Una nini?”

    “Ninakupenda mno, ninataka uwe mke wangu wa ndoa,” alisema Smith.

    Moyo wa Tatiana ukashtuka, hakutegemea kusikia kile alichokuwa amekisikia mahali hapo, alihisi kama masikio yake yalizembea kusikiliza kile alichokizungumza Smith mbele yake, akauliza tena na tena lakini jibu la Smith lilikuwa lilelile kwamba alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati.

    “Smith....”

    “Naomba usiniambie neno la kuniumiza Tatiana, nimetokea kukupenda tangu nilipokuona kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, umekuwa msichana mwenye uzuri wa ajabu ambaye siwezi kumuacha akapita, Tatiana, umeuteka moyo wangu, sitaki kuona ukiolewa na mtu mwingine tofauti na mimi, ninakupenda Tatiana,” alisema Smith huku akimshika Tatiana mkono wake uliokuwa juu ya meza.

    “Hapan Smith...” alisema Tatiana huku akianza kububujikwa na machozi.

    “Kwa nini hapana? Kwa nini unataka kuniumiza hivi?”

    “Smith....nina mpenzi...”

    “Hapana Tatiana, siwezi kuamini hilo, nimekuwa nikikufuatilia kwa kipindi kirefu, ni bora kama unanikataa unikatae kwa sababu nyingine lakini si kunidanganya kwamba una mpenzi. Tatiana, ninataka kukufanya kuwa mke bora, naomba uwe mpenzi wangu na mwisho wa siku nikuoe,” alisema Smith huku naye akianza kububujikwa na machozi.

    Hicho kilikuwa kipindi kigumu katika maisha yake, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, iweje wanaume wawili watokee ghafla katika maisha yake na kumwambia kwamba walikuwa wakimpenda?

    Hapo ndipo alipoanza kumkumbuka Peter, mwanaume wa kwanza kumwambia kwamba alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, huyo ndiye aliyekuwa na moyo wake, huyo ndiye aliyekuwa amemteka vilivyo, hakujua sababu ya wanaume hao kuibuka ghafla namna hiyo.

    “Naomba nikupe muda wa kujifikiria, na hongera sana kwa sauti nzuri uliyobarikiwa,” alisema Smith na kisha kumuinua msichana huyo kumrudisha ndani ya hoteli.

    *****

    “Wewe ni mpenzi wangu Tatiana, haiwezekani kuona ukiolewa na mtu mwingine, siwezi kuona harusi hii ikitokea,” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja akiongea kwa hasira sana huku mkononi akiwa ameshika chupa ya pombe kali aina ya John Walker.

    Mwanaume huyo alisimama katika mlango wa kanisa, alionekana kuwa mlevi, nywele zake zilikuwa timutim. Kanisani hapo kulikuwa na watu wengi waliokuwa wamekuja kuhudhuria harusi iliyokuwa imetangazwa sana kati ya Tatiana na mwanaume wa Kizungu. Msichana Tatiana alisimama mbele ya kanisa hilo huku akiwa na mwanaume wa Kizungu aliyevalia suti nyeupe.

    Ilikuwa ni siku ya harusi yake, mwanaume huyo wa Kizungu alikuwa Smith aliyekuwa kwenye mshangao mkubwa mara baada ya kumuona mwanaume huyo mlevi akiingia kanisani na kutaka mchungaji asifungishe ndoa, alikuwa Peter.

    Kichwani akawa na mawazo, mwanaume yule alikuwa nani na alikuwa na uwezo gani wa kusimamisha ndoa ile isifanyike? Kila alipojiuliza, alikosa jibu kabisa.

    Tatiana hakuzungumza kitu, alikuwa akimwangalia mwanaume yule huku akiwa kimya kabisa, kilio cha kwikwi kikaanza kusikika kutoka kwake, alikuwa kwenye kipindi kingine kigumu kuliko vipindi vyote maishani mwake.

    Wazazi wake ambao walikuwa kwenye viti vya mbele kabisa walibaki wakimwangalia mwanaume yule aliyeonekana kuwa chakari kutokana na pombe kali alizokuwa akinywa.

    Huku kanisa likiwa limetaharuki, mara mtu mwingine akaingia kanisani humo akiwa hoi, mwili wake ulijeruhiwa na alikuwa na bandeji kubwa mwilini mwake. Alipomuona, alimkumbuka vilivyo kwamba mwanaume huyo alikuwa Nathan, alisimama kule mlangoni na kuanza kuzungumza kwa sauti kubwa,

    “Tatiana....” alianza kusema Nathan na kuendelea:

    “Hata kama umenifanyia hivi, kuniua ili uolewe na huyu Mzungu wako, kumbuka ni jinsi gani ninakupenda, kumbuka ni jinsi gani tulivyokuwa pamoja,” alisema Nathan, watu wote waliokuwa kanisani wakabaki kimya.

    Smith alionekana kuwa na hasira mno, kila alipokuwa akiwaangalia watu hao alishikwa na hasira zaidi hali iliyompelekea kuchomoa bunduki yake iliyokuwa kiunoni na kisha kuanza kuwasogelea watu wale.

    Kila mmoja akagundua kile kilichokuwa kikitaka kutokea, kwa kasi ya ajabu, Tatiana akaanza kumfuata Smith, alipomfikia, akamshika mkono ili asifanye kile alichotaka kufanya. Hiyo haikuweza kuzuia, alichokifanya Smith ni kuwanyooshea bunduki na kisha kuwafyatulia risasi.

    “Noooooooooo......” alipiga kelele Tatiana.

    Ilikuwa ni moja ya ndoto mbaya na iliyomsisimua kupita kawaida. Alikuwa akipiga kelele zilizomfanya Angelina kushtuka kutoka usingizini na kumwangalia rafiki yake huyo. alichokifanya ni kumuuliza nini kilikuwa kimetokea lakini Tatiana hakujibu kitu chochote zaidi ya kulia tu.

    “Tell me what’s wrong with you,” (Niambie una nini?)

    “It was a nightmare,” (Ilikuwa ndoto mbaya)

    “Oooh! It was just a nighmare, don’t cry Tattie,” (Oooh! Ilikuwa ndoto mbaya tu, usilie Tattie) alisema Angelina huku akimkumbatia.

    Tatiana hakuwa na raha tena, moyo wake ulikuwa kwenye mawazo mazito juu ya ile ndoto mbaya aliyokuwa ameiota, moyo wake ulimuuma sana kwani hakutegemea kitu kama kile kutokea katika maisha yake.

    Aliichukulia ndoto ile kuwa miongoni mwa ndoto mbaya na hakika isingeweza kuwa kweli kwani piga ua alijiahidi kutokuolewa na mwanaume yeyote yule zaidi ya Peter aliyemuacha nchini Tanzania.

    Siku ziliendelea kukatika kama kawaida. Shindano lile liliendelea kwenda mbele kama kawaida na walipobaki watu hamsini wa mwisho, kwa bahati mbaya kwake, Nathan akawa amechujwa katika shindano hilo na kutakiwa kurudi nchini kwake huku akikabidhiwa kitita cha dola elfu kumi (zaidi ya milioni ishirini) kama kifuta jasho.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Fedha halikuwa tatizo katika maisha yake, alitoka familia ya mzee aliyekuwa na fedha nyingi nchini Liberia. Baba yake alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na fedha nyingi kwa kujishughulisha na biashara ya madini huku akimiliki migodi mbalimbali ya almasi nchini humo.

    “Tatiana, siwezi kuondoka, bado ninahitaji kuwa karibu nawe,” alisema Nathan.

    Hilo halikuwa tatizo kwa Tatiana lakini suala la kuendelea kubaki ndani ya hoteli hiyo ilikuwa kinyume ya kile kilichokuwa kikiendelea na kilikuwa nje ya uwezo wa Tatiana. Kuwa karibu na msichana huyo hakuzuiliwa lakini hakutakiwa kuwepo ndani ya hoteli hiyo kwa kuwa hakuwa mshiriki tena.

    Kila kitu kikaonekana kuwa kigumu kwa Nathan, kile kilichokuwa kikiendelea kilimuumiza mno kwani ilikuwa ni lazima arudi nyumbani na amuache msichana huyo nchini Marekani.

    Kitu kilichomuumiza mno kichwa ni kwamba mpaka kipindi hicho msichana huyo hakuwa amekubaliana naye kama alikuwa tayari kuwa naye kimapenzi au la, alitakiwa kuondoka kurudi Liberia.

    Hiyo ikawa nafasi kubwa kwa Smith, kitendo cha Nathan kuondolewa nchini hapo, moja kwa moja akamfuata Tatiana na kumwambia kwamba alitaka kumleta mtu maalumu kwa ajili ya kumsaidia katika kila kitu likiwemo suala la kumuongoza kila atakapotaka kwenda na gharama zote zingekuwa chini yake.

    Tatiana akakubaliana naye na kazi kuanza mara moja. Kila siku wawili hao wakawa wakikutana, Smith alijitahidi kumuonyeshea Tatiana kwamba alikuwa akimpenda kwa kumaanisha na hakuwa akimtamani hata mara moja.

    Mapenzi yalimlevya hivyo akataka Tatiana naye awe katika hali hiyo jambo lililohitaji kazi kubwa tena ya kujitoa mpaka aingie katika ulimwengu wa mapenzi kama alivyokuwa yeye.

    Baada ya siku wiki chache, tayari watu walioingia kwenye tano bora wakajulikana, kulikuwa na Waafrika wawili tu, yaani Tatiana na msichana Febby Grace kutoka nchini Ghana. Shindano lilikuwa kubwa na lilileta sana msisimko.

    Katika hatua hiyo, walichukua mwezi mzima kujiandaa huku wakitembezwa sehemu mbalimbali na kukutanishwa na walimu wengi wa muziki ambao wote hao waliushangaa uwezo mkubwa aliokuwa nao Tatiana.

    Alikuwa na sauti nzuri mno, kila alipokuwa akiimba wimbo wowote ule, sauti ilipangiliwa kiasi cha walimu kukiri kwamba hawakuwahi kukutana na mtu aliyekuwa na sauti nzuri kama Tatiana.

    “Sitochoka kukwambia kwamba nakupenda Tatiana,” alisema Smith, hayo yalikuwa maneno yake ya kila siku alipokuwa akikutana na Tatiana.

    “Najua.”

    “Unanipenda?”

    “Swali gumu sana Smith.”

    “Lakini linaweza kujibika, si ndiyo?”

    “Naomba uniache kwa kipindi hiki, si unajua siyo kizuri sana?”

    “Najua, lakini hebu niambie japo niridhike,” alisema Smith.

    “Nitakujibu.”

    Hilo halikuwa tatizo, Smith hakutaka kuwa na haraka, aliamini kwamba ilikuwa ni lazima Tatiana akubali kuwa naye na hatimae amuoe na kuwa mke wake. Hakujali kama msichana huyo alikuwa na mpenzi wake au la, alichokuwa akikijua yeye ni kwamba kuna siku msichana huyo angekuwa mpenzi wake tu.

    Siku ziliendelea kukatika na hatimaye siku ambayo fainali ilitakiwa kufanyika ikatangazwa, watu wote duniani wakaanza kuisubiria kwa hamu. Tatiana alionekana kuwa na wasiwasi moyoni mwake lakini kila siku Smith alikuwa na jukumu kubwa la kumtia moyo kwamba angeshinda shindano hilo.

    “Niamini Tatiana, unajua sana, wewe ni bora zaidi ya hawa wote,” alisema Smith huku akimwangalia Tatiana usoni.

    “Kweli?”

    “Ndiyo! Wewe ni bora zaidi ya mtu yeyote yule,” alisema Smith.

    Maneno yale yakamtia moyo Tatiana, hakuamini kama angeweza kupata mtu ambaye angemtia moyo namna ile katika kipindi kigumu kama kile ambacho alihitaji faraja kubwa kutoka kwa mtu wake wa karibu.

    Pasipo kupenda, pasipo kulazimishwa, Tatiana akajikuta akimbusu Smith shavuni na kuhama kisha kuanzakubadilishana mate. Moyo wake ukabadilika, hakumkumbuka tena Peter, mtu ambaye alikuwa naye kwa karibu kipindi hicho alikuwa Smith tu na ndiyo maana alikuwa radhi kumpa ladha ya mate yake kwa mara ya kwanza kabla ya mwanaume yeyote yule, naye, mapenzi yakaanza kumchanganya huku Peter akisahaulika kwa kasi.



    Japokuwa shule zilikuwa zimefunguliwa lakini Peter hakutaka kurudi shuleni, moyo wake ulikuwa na hamu ya kujua juu ya lile shindano ambalo kila wiki lilikuwa likionyeshwa katika televisheni.

    Moyo wake ulifurahi mno, kitendo cha kuona Tatiana akiendelea kuwa juu kutokana na umahiri wake kilimpa moyo sana kwa kuona kwamba msichana huyo angefanikiwa na kuchukua ushindi katika shindano lile.

    Kura za awali zilionyesha kwamba Tatiana alikuwa akiongoza kwa asilimia 70 tofauti na wengine ambao waligawana hizo thelathini zilizobakia. Tatiana alipendwa na kila mtu, si kwa hali yake tu aliyokuwa nayo bali hata uzuri wake katika uimbaji uliwafanya watu wengi kuamini kwamba msichana huyo alizaliwa akiwa na kipaji cha kuimba.

    Peter alikuwa makini, alipenda kufuatilia kila kitu kuhusu msichana huyo. Wazazi wake walijua kila kitu kilichokuwa kikiendelea, walifahamu ni kwa namna gani Peter alikuwa akimpenda msichana Tatiana hivyo hata alipokuwa bize na televisheni badala ya kwenda shule alipokuwa akisoma, hawakutaka kumghasi sana.

    Siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ikawadia, siku hiyo peter alijiweka vizuri kochini huku moyo wake ukiwa na furaha kubwa kwamba hatimaye siku hiyo ndiyo mpenzi wake angetangazwa na kuwa mshindi wa shindano hilo. Kwa Tanzania, shindano hilo lilikuwa likionyeshwa saa mbili asubuhi huku Marekani, hasa katika Jiji la New York ikiwa ni saa nnembili usiku wa jana yake.

    Dola milioni tano zilikuwa fedha nyingi mno ambazo kila mtu alizitolea macho, shindano lile liliendelea kupata watazamaji hasa katika kipindi kile cha mwishomwisho akiwemo Peter ambaye hakutaka kubanduka mbele ya televisheni yake.

    “Mungu! Naomba Tatiana ashinde,” alisema Peter huku akiikutanisha mikono yake.

    Ilikuwa ni siku ya Jumapili lakini Peter hakwenda kanisani, siku hiyo alishinda nyumbani kwani alitaka kufahamu kile kilichokuwa kikiendelea, kama mpenzi wake atachukua ushindi au la.

    Baada ya wanamuziki waalikwa kuitwa na kutumbiza, washindani wakaanza kuimba nyimbo zao na walipoaliza, wakaambiwa wajipange kwa ajili ya mshindi kutangazwa, kila mtu aliyekuwa akifuatilia shindano lile, moyo wake ukaanza kumdunda kwa nguvu.

    *****

    “Nathan, speak out, I want to hear what you are about to tell me,” (Natha zungumza, ninataka kusikia hicho unachotaka kuniambia) ilisikika sauti ya msichana mrembo, alikuwa akizungumza simuni na Nathan.

    “We are not going to get married,” (Hatutoona)

    “Why?” (Kwa nini?)

    Nathan hakutaka kujibu swali hilo, alibaki kimya na baada ya sekunde tatu akakata simu. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makubwa, alijua ni kwa jinsi gani msichana huyo alikuwa akimpenda na kumthamini, alikumbuka mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kabla ya kwenda nchini Marekani ambapo huko alikutana na Tatiana ambaye aliamini alikuwa akimpenda kama alivyokuwa akimpenda.

    Hakutaka kusikia lolote lile kutoka kwa msichana wake wa kipindi kirefu, Dassy, moyo wake ulikuwa umezama kwa msichana Tatiana kwa asilimia mia moja na hakukuwa na nafasi nyingine ya kumuingiza msichana yeyote akiwemo huyo aliyekuwa ameongea naye, Dassy.

    Dassy alikuwa msichana mrembo ambaye alifanikiwa kunyakua taji la urembo la Liberia miaka miwili iliyopita. Mara baada ya kuchukua taji hilo, wanaume wengi wakaanza kumtolea macho akiwemo Nathan ambaye alikuwa hali, hanywi kwa ajili ya msichana huyo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alimsumbua sana lakini baada ya mieizi mitatu ya kumfuatilia, Nathan akawa mwanaume mwenye bahati kubwa baada ya kuuteka moyo wa Dassy. Mahusiano ya kimapenzi yakaanza rasmi, wawili hao wakawa pamoja kila sehemu waliyokwenda huku kila mmoja akimuonyesha mwenzake ni kwa namna gani alikuwa akimpenda.

    Baada ya uhusiano huo kudumu kwa kipindi kirefu, hapo ndipo walipoamua kupanga mikakati ya kutaka kufunga ndoa, ila kwa kuwa kulikuwa na shindano la kuimba nchini Marekani na Nathan alibahatika kupata nafasi, akazungumza na wazazi wake kwa kuwaambia kwamba atakaporudi nchini Liberia basi angeweza kumuoa msichana huyo, wazazi wa pande zote mbili wakakubaliana naye.

    Nathan alirudi, wazazi wote walifurahi lakini alionekana kubadilika mno. Hakuwa Nathan yule aliyemthamini Dassy, huyu alikuwa Nathan mwingine ambaye hakutaka kusikia kitu chochote kile kuhusu msichana huyo.

    Hilo liliwashtua mno wazazi, wakaamua kumuita na kumuweka kikao ili awaambie ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, Nathan hakuficha, akawaambia ukweli kwamba alipokwenda nchini Marekani, alikutana na msichana wa Kitanzania ambaye alitokea kumpenda kwa dhati.

    “Whaaaaaaaaat?” (Niniiiiiiii?) aliuliza mama yake huku akionekana kutokuamini.

    “This is my decision mom, I will never get married with Dassy,” (Huu ni uamuzi wangu mama, kamwe siwezi kumuona Dassy) alisema Nathan.

    Japokuwa wazazi hawakuamini kile kilichokuwa kimezungumziwa lakini ule ndiyo ulikuwa uamuzi wake alioamua kuuchukua kwa wakati huo. Hakutaka kuwa na msichana Dassy ambaye alimsifia sana kutokana na uzuri wake, msichana pekee aliyekuwa akimpenda kwa wakati huo alikuwa Tatiana tu.

    Dassy alilia na kulia, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea kwamba hatimaye mpenzi wake, Nathan hakutaka kuwa naye tena. Hakuridhika na ile simu, aliamini kwamba Nathan aliamua kufanya vile kwa kuwa tu walikuwa wakizungumza simuni, hivyo akaanza kumtafuta. Alipompata, akaanza kuzungumza naye.

    “Kile ndicho nilichokimaanisha Dassy! Siwezi kuwa nawe, nimempata msichana mwingine,” alisema Nathan huku akionekana kumaanisha alichokizungumza.

    “Nathan, naomba usinitanie, niambie ukweli.”

    “Naonekana kama natania?”

    “Niambie ukweli.”

    “Ndiyo huo! Siwezi kuwa nawe.”

    Alivyokuwa akiongea, Dassy alifikiri kwamba Nathan alikuwa akitania lakini ukweli ni kwamba alimaanisha kile alichokuwa akikizungumza mbele yake. Dassy aliumia zaidi moyoni mwake lakini hakuwa na jinsi, huo ndiyo ukawa mwisho wa uhusiano wake na Nathan.

    Akili ya Nathan ikatulia kwa Tatiana, kila siku alikuwa akilifuatilia shindano lile lililoonekana kushika kasi kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele. Moyo wake uliendelea kumpenda Tatiana, kila alipokuwa akimwangalia, alijipongeza kwa kufanya uamuzi ulio sahihi wa kumuacha Dassy kwa ajili ya Tatiana.

    Siku zikaendelea kukatika mpaka siku ya fainali ya shindano lile ilipowadia. Kama kawaida yake, Nathan akakaa sebuleni kwa ajili ya kuona ni nani angechukua ubingwa ule. Japokuwa matokeo ya awali yalisema kwamba Tatiana alikuwa akiongoza lakini hakutaka kujifariji kwani alijua kwamba hata Marekani napo fitina zilikuwepo pia.

    “ Mungu, naomba umpe ushindi Tatiana, Mungu, nakuomba sana ufanye hilo,” alisema Nathan huku akiona washiriki watano wa mwisho wakiwa wamekaa tayari mbele ya ukumbi tayari kwa matokeo kutangazwa. Mapigo yake ya moyo yakaanza kumdunda.

    *****

    Tatiana hakuamini kile alichokuwa amekisikia kwamba alikuwa ametangazwa na kuwa mshindi wa shindano hilo lililodumu kwa miezi sita. Alisikia vizuri kwamba akitajwa jina lake lakini hakuamini kama alisikia vizuri au alikuwa amesikia jina jingine lililofanana na lake.

    Kilichomshtua na kuamini kwamba alikuwa ametajwa yeye ni kelele za watu waliokuwa ukumbini pale ambao walikuwa wakilitaja jina lake kwa shangwe kubwa. Hapo ndipo akaamini kwamba yeye ndiye aliyeibuka mshindi katika shindano lile.

    Furaha iliyoje! Alishindwa kuamini, hakuendelea kusimama, akajikuta akichuchumaa chini na kuanza kulia kama mtoto. Kile kiasi cha dola milioni tano ambazo zilikuwa ni zaidi ya bilioni kumi zilikuwa zake.

    Majaji wote wakasimama na kuanza kumfuata Tatiana aliyekuwa amezungukwa na washiriki wengine na kisha kumkumbatia kwa fuaraha, walikuwa wakimfariji, aache kulia kwani ule ulikuwa ni ushindi wake, alikuwa amejipatia kiasi kikubwa cha fedha ndani ya siku 180 tu.

    Kila mtu aliyekuwa akifuatilia shindano lile alishangilia kwa kuona kweli haki ilitendeka, yule mtu aliyekuwa amestahili kuchukua ushindi ule, aliuchukua kitu kilichompa sifa sana bwana Warren kwa kuonekana kwamba hauwa na shindano lililokuwa na upendeleo.

    Hapohapo vyombo vya ahabari vikaanza kutangaza juu ya ushindi ule, kila sehemu, picha za Tatiana akilia jukwaani zilikuwa zikionekana, kwa kipindi cha dakika kadhaa tu, tayari akawa maarufu mkubwa duniani.

    “Tattie, don’t cry baby, I told you you are the best ever,” (Tattie, usilie kipenzi, nilikwambia wewe ni bora haijawahi kutokea) alisema Smith huku akimkumbatia Tatiana.

    Watu kutoka ukumbini pale tayari walikwishajazana jukwaani na kila mmoja kutaka kumshika Tatiana ambaye kwa kipindi hicho alikuwa msichana mwenye uwezo mkubwa kifedha japokuwa hakuwa bilionea kama wengine.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa Smith, hicho ndicho kilikuwa kipindi maalumu cha kuionyesha dunia kwamba msichana yule aliyekuwa bora kwa kuimba duniani, alikuwa mpenzi wake. Pasipo kujiuliza chochote kile, pasipo kuogopa kamera wala kujua kwamba watu wawili waliokuwa wakimpenda sana Tatiana walikuwa wakilifuatilia shindano lile kwenye televisheni, hapohapo akamkumbatia Tatiana kwa nguvu kisha kuanza kubadilishana mate kitu kilichoshangiliwa sana na watu waliokuwa pale ukumbini.

    *****

    Ilikuwa ni zaidi na kupigiliwa msubali wenye ncha kali moyoni mwake au kuteketezwa na moto huku akijiona, maumivu aliyokuwa ameyapata Peter yalikuwa makubwa yalioufanya mwili wake kuanza kutetemeka na kijasho chembamba kuanza kumtoka.

    Hakuamini kile alichokuwa akikiona mahali pale, msichana aliyekuwa akimpenda, aliyempa nafasi kubwa moyoni mwake, alikuwa amesimama jukwaani na mwanaume mwingine kisha kubadilishana mate naye.

    Alihisi wivu mkali ukiuchoma moyo wake, hasira zake zikawaka, pasipo kutarajia, machozi yakaanza kububujika mashavuni mwake. Hakuendelea kuangalia kwani kadiri alivyokuwa akiangalia na ndivyo alivyozidi kuumia zaidi, akajikuta akiizima televisheni na kukimbilia chumbani.

    Huko hakunyamaza, akaanza kulia kwa sauti ya juu kama mtoto. Wafanyakazi wa nyumba ile wakaogopa kwa kuhisi kwamba inawezekana kulikuwa na msiba, hivyo wakaanza kuelekea chumbani kwa Peter lakini mlango ulifungwa kwa ndani.

    Walijaribu kuugonga lakini haukufunguliwa, bado kilio cha Peter kiliendelea kusikika ndani ya chumba kile, kilio kilichochanganyikana na maumivu makali ya moyo wake.

    “Peter...fungua mlango,” alisema mfanyakazi mmoja, alikuwa mama mtu mzima.

    Peter hakutaka kufungua mlango, bado aliendelea kubaki ndani huku akilia tu. Alishinda ndani asubuhi mpaka mchana. Mchungaji Lazaro aliporudi kutoka kanisani, akaambiwa kile kilichokuwa kimetokea.

    “Kisa nini?” aliuliza.

    “Hata sisi hatufahamu, tulisikia tu akilia,” alijibu mfanyakazi yule.

    Mchungaji Lazario akaelekea chumbani kwa Peter, akajaribu kuufungua mlango lakini ulikuwa umefungwa kwa ndani. Mama Peter akawa na wasiwasi kwamba inawezekana kulikuwa na jambo baya lilikuwa limetokea, hivyo kuendelea kuuliza zaidi.

    “Hatujui chochote mama, tulikuwa jikoni tukasikia tu akilia tu,” alisema mfanyakazi yule.

    Mchungaji Lazaro na mkewe wakaanza kumuita na kumtaka kuufungua mlango lakini Peter hakufanya hivyo, aliendelea kuufunga mlango ule na hakutaka kuufungua kabisa jambo lililowatia hofu wazazi hao kwa kuhisi kwamba inawezekana Peter alikuwa amejidhuru chumbani, hivyo wakaanza kufanya mchakato wa kuuvunja mlango.

    *****

    Kilichotokea kwa Peter ndicho kilichotokea kwa nathan pia, hakuamini kile alichokuwa akikiona katika televisheni kipindi kile, hakuamini kama kweli msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wote, Tatiana alikuwa akibadilishana mate na mwanaume ambaye alikuwa akimuona mara kwa mara wakati walipokuwa wakifanya mazoezi, Smith.

    Moyoni aliumia mno na kilichomuumiza zaidi ni kwamba alimuacha msichana Dasy kwa sababu ya Tatiana lakini mwisho wa siku, msichana huyo alikuwa na mwanaume mwingine kabisa. Nathan akashindwa kuvumilia, kile alichokuwa amekiona kwenye televisheni kilimchanganya na kumuumiza mno, akajikuta akianza kububujikwa na machozi.

    “Haiwezekani! Tatiana hawezi kufanya hivi,” alisema Nathan huku akionekana kuwa na hasira.

    Alionekana kama kichaa, alitembea huku na kule pale sebuleni huku akilia tu, kila alipokuwa akiwaangalia wawili wale kwa jinsi walivyokuwa wamekumbatiana baada ya kubadilishana mate, aliendelea kuumia zaidi.

    “Tatiana, nimemuacha Dassy kwa ajili yako! Haiwezekani, lazima ulipe hili,” alisema Nathan huku wakati mwingine akiongea kama kichaa.



    Kiasi cha dola milioni tano kikaingizwa ndani ya akaunti ya Tatiana aliyokuwa amefunguliwa na kuunganishwa na benki moja nchini Tanzania. Bwana Warren hakutaka binti huyo akatwe katika fedha zile kama kodi ya serikali, alichokifanya ni kuongeza kiasi kingine ambacho kilikatwa na Tatiana kupata kiasi chote pasipo makato yoyote yale.

    Moyo wake ulifurahia, hakuamini kama tangu siku ya kwanza alipokwenda nchini Tanzania kumbe ndiyo alikuwa akimfuata mshindi wa shindano lile. Aliyakumbuka maneno yake ambayo mara kwa mara alikuwa akiwaambia washiriki walipokuwa nchini Tanzania kwamba alikuwa na hisia kabisa kwamba mshindi wa shindano lile angetokea katika nchi hiyo japokuwa hakujua ni nani.

    Kilichoongeza furaha zaidi kwa bwana Warren ni kile kitendo cha mtoto wake kubusiana na Tatiana, hakuamini kama hali ilikuwa namna ile, akabaki akitabasamu tu kwani hata naye, mbali na upofu aliokuwa nao Tatiana, alivutika na uzuri aliokuwa nao.

    Akamfuata binti huyo palepale mbele ya ukumbi ule na kumkumbatia huku akiwa na furaha kubwa. Waandishi wa habari waliendelea na kazi zao za kupiga picha kwani hata hali ile waliyokuwa nayo mahali pale, ilionyesha dhahiri kwamba mzee huyo alifurahishwa na mengi katika ushindi wa Tatiana.

    “Do you remember what I told you six months ago?” (Unakumbuka nilichowaambia miezi sita iliyopita?) aliuliza bwana Warren.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “I do remember,” (Nakumbuka) alisema Tatiana huku akiyafuta machozi yaliyokuwa yakimbubujika.

    “This is God’s plan, He wants you to move from poverty to wealth,” (Huu ndiyo mpango wa Mungu, hutaka wewe utoke kwenye umasikini mpaka utajiri) alisema bwana Warren huku akiachia tabasamu pana.

    Kila kitu kikakamilishwa siku hiyo, baada ya hapo, ikapangwa sherehe ya kumpongeza Tatiana kutokana na ushindi aliokuwa ameupata na wenzake walioingia kwenye tano bora, hivyo tarehe ikawekwa wazi, ilikuwa ni wiki mbili kuanzia siku hiyo.

    Akachukuliwa chumba katika moja ya hoteli ya nyota saba jijini New York, huko akakaa na wenzake wanne huku wakiisubiria hiyo sherehe ya kuwapongeza huku kwa bwana Warren, akianza kufanya mikakati wazazi wa washindi walioingia tano bora waweze kufika nchini Marekani kusherehekea na ndugu zao.

    “Kwa hiyo wazazi wangu watakuja huku?” aliuliza Tatiana.

    “Ndiyo! Mipango inaanza kupangwa. Tatiana, unaanza kuelekea kwenye utajiri mkubwa endapo utafanya mipango madhubuti juu ya fedha zako,” alisema Smith.

    “Nitajitahidi kufanya kila liwezekanalo mpaka niwe bilionea, ila itawezekana?” aliuliza Tatiana.

    “Kwa nini ishindikane?”

    “Huoni jinsi nilivyo?”

    “Tatiana, nikwambie kitu?”

    “Niambie.”

    “Tabasamu kwanza,” alisema Smith, Tatiana akaachia tabasamu pana lililotoka moyoni.

    “Nimewasiliana na Dk. Stephen Buffet kutoka Denver, Colorado kwa ajili yako.”

    “Ndiye nani?”

    “Ni mtaalamu wa magonjwa ya macho, nimezungumza naye na ni kwamba utatakiwa kuelekea huko kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa macho yako ili uweze kuona kwa mara ya kwanza,” alisema Smith.

    “Nione?”

    “Ndiyo!”

    “Itawezekana vipi? Nimezaliwa hivihivi Smith.”

    “Tatiana! Kuna wengi walizaliwa hivyo lakini mwisho wa siku wakapona kabisa. Gharama yake ni kubwa lakini nitagharamia mimi mwenyewe, ninataka uone, upo tayari?” aliuliza Smith.

    “Nipo tayari mpenzi.”

    “Sawa. Sherehe ikishakwisha, tutakwenda huko,” alisema Smith na kisha kukumbatiana. Huo ndiyo ukawa usiku wa kwanza kwa wawili hao kufanya mapenzi na Tatiana kutolewa usichana wake.

    “Nitakupenda milele kwa hii zawadi uliyonipa,” alisema Smith, hakuamini kumkuta Tatiana akiwa bado hajaingiliwa na mwanaume yeyote yule.

    “Nitakupenda pia mpenzi,” alisema Tatiana na kukumbatiana kwa furaha.

    *****

    Furaha ilikuwa kubwa katika Kijiji cha Chibe, watu hawakuamini kile walichokuwa wamekisikia kwamba msichana aliyeondoka kuelekea nchini Marekani kutokea katika kijiji hicho, Tatiana alikuwa amechukua ushindi kwa kuwa muimbaji bora katika shindano lile lililokuwa likiendelea nchini huko kwa miezi sita.

    Wazazi wake, mzee Sangiwa na mkewe walizidiwa na furaha, kila walipokuwa wakifurahia, walionekana kama vichaa fulani. Hawakufikiria zaidi kuhusu fedha, kitu pekee walichokuwa wakikifurahia kwa wakati huo ni heshima tu kwa kujua kwamba nchi yao na kijiji chao, vyote hivyo vingetangazika mno.

    Baada ya wiki moja ya furaha yao, Wazungu wanne wakafika kijijini hapo na kuwaambia kwamba mzee Sangiwa na mkewe walitakiwa kuondoka nao kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya kuhudhuria sherehe ya kumpongeza mtoto wao kwa kile kilichokuwa kimetokea.

    Furaha zao zikaongezeka maradufu, taarifa ile walioletewa na Wazungu wale ikawapa furaha ya ajabu kiasi kwamba wakaenda kanisani kesho yake na kutoa sadaka ya shukrani.

    “Kwa hiyo ndiyo tunakwenda kwa Wazungu, hukoooooo, kule alipotoka Michael Jackson,” alisema mzee Sangiwa huku akionekana kuwa na furaha tele.

    Mipango ilishasukwa, baada ya wiki mbili, wazazi hao wakachukuliwa na safari ya kuelekea nchini Marekani kuanza mara moja. Njiani, ndani ya ndege hawakuamini, kuna wakati mwingine walihisi kwamba walikuwa ndotoni na muda wowote ule wangeamka na kujikuta wakiwa chumbani wamelala.

    Safari hiyo ilikuwa ni kwenda Marekani kwa kuelekea Accra nchini Ghana ambapo huko walitakiwa kuwapitia wazazi wa Febby na kisha kuunganisha mpaka nchini Marekani kwani ni washirika wawili tu kutoka Afrika ndiyo waliokuwa wameingia kwenye tano bora.

    “Ndiyo Ulaya hiyo tunakwenda, kumbe ndani ya ndege kuzuri sana,” alisema mzee Sangiwa huku meno yote thelathini na mbili yakiwa nje. Ndege iliendelea kukata mawingu tu.

    *****

    Tatiana hakuamini kama waliosimama mbele yake walikuwa wazazi wake, japokuwa alikuwa kipofu lakini hisia zilimfanya kugundua kwamba watu waliokuwa wamesimama umbali mdogo kutoka alipokuwa walikuwa wazazi wake.

    Uso wake ukajawa na tabasamu pana na kuanza kusogea kule mbele kwa lengo la kuwafuata huku akiwa na fimbo yake mkononi. Alipoona kwamba amewafikia, akaiachia fimbo na kuitanua mikono yake kama mtu aliyesubiri kuwakumbatia watu fulani, wakamsogelea na kumkumbatia kwa furaha.

    Hawakuami kama binti yao mrembo alikuwa amefanikiwa kuchukua ushindi ule uliokuwa ukitamaniwa na kila mtu, huo, kwao ukaonekana kuwa muujiza mkubwa na walimshukuru sana Mungu kwa kila kilichotokea.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Alichokifanya Tatiana ni kuwatambulisha wazazi wake kwa Smith, mbaya zaidi aliwatambulisha kama mpenzi wake ambaye alikuwa na mipango ya muda mrefu ya kufunga naye ndoa.

    “Unasemaje?”

    “Huyu ndiye atakayenioa mama, ninampenda na ananipenda,” alijibu Tatiana.

    Wazazi walibaki na mshangao lakini hawakutaka kuzungumza kitu, walichokifanya ni kusubiri mpaka sherehe hiyo ifanyike na kumalizika. Hapo, hata ile furaha waliyokuwa wamekuja nayo ikapotea, mioyo yao ilimfikiria Peter tu ambaye alijitoa sana kwa ajili ya binti yao na alikuwa akimpenda Tatiana kwa penzi la dhati.

    Siku ya sherehe ilipofika, kama kawaida ikatangazwa sana. Tatiana hakuwa yule wa kipindi cha nyuma, huyu wa sasa hivi alikuwa tajiri mkubwa, aliheshimika na kutangazwa sana kila kona. Umaarufu mkubwa duniani ulikuwa ukimnyemelea, alitafutwa sana na waandishi wa habari ambao walitamani kusikia mengi sana kutoka kwake.

    Sherehe ilipokwisha, wazazi hao walitaka kuzungumza na binti yao, maneno aliyowaambia kwamba alikuwa amempata mwanaume mwingine ambaye alijitolea kumuoa, yaliwashtua kwani kitu walichokuwa wakikifahamu ni kwamba Peter bado alikuwa kwenye mapenzi ya dhati kwa binti yao.

    “Hivi ulisemaje vile?” aliuliza mama yake.

    “Nimempata mwanaume ambaye nahisi nina mapenzi naye ya dhati,” alijibu Tatiana.

    “Hivi unajua unachokisema?”

    “Ndiyo mama.”

    “Na vipi kuhusu Peter?”

    “Mama! Kile kilikuwa kipindi cha nyuma, nilikuwa mtoto hivyo wakati mwingine sikuwa na maamuzi , sasa nimekua mama,” alisema Tatiana.

    “Yaani miezi sita tu unasema ulikuwa mtoto, kweli?”

    “Ndiyo mama. Ninampenda Smith,” alisema Tatiana kwa ujasiri mkubwa.

    Mioyo yao ilichomwa na kitu kikali zaidi ya sindano, hawakuamini kile walichokisikia kutoka kwa binti yao. Mioyo yao ilikuwa kwa Peter tu, hawakutaka kusikia habari za mwanaume yeyote yule, kitu walichokitaka ni kuona binti yao akiwa na Peter tu.

    “Hapana! Wala sikubaliani na wewe Tatiana.”

    “Baba! Mkubaliane na mimi, msikubaliane nami, hilo wala sijali, ninachokisema ni kwamba ninampenda Smith,” alisema Tatiana huku akionekana kumaanisha alichokuwa akikisema.

    Hawakuwa na jinsi, binti yao alikuwa ameamua kitu kilichokuwa kigumu kukubalika mioyoni mwao, hawakutaka kumuingilia sana zaidi ya kumsisitizia kwamba wao kama wazazi walitamani kumuona akiwa na Peter kwani ndiye mwanaume aliyeonyesha kuwa na mapenzi naye ya dhati na si kama ilivyokuwa kwa Smith.

    Siku zikaendelea kukatika, baada ya wiki moja sherehe kumalizika, wazazi hao wakarudi zao nchini Tanzania huku wakimuacha Tatiana akijiandaa kwenda Colorado kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa macho kwa daktari mkubwa aliyekuwa akisifika nchini Marekani.

    Hakuwa na shida ya hela, Tatiana alikuwa tajiri mkubwa tu na kwa matibabu yale uliotarajiwa kufanyiwa, asingetumia fedha zake, gharama zote zilikuwa kwa Smith tu.

    Siku mbili baadae walikuwa ndani ya ndege binafsi ya Smith na safari ya kuelekea Colorado kuanza. Ndani ya ndege Tatiana alionekana kuwa na furaha tele, hakuamini kama ndani ya siku chache zijazo angeweza kuona kama walivyokuwa watu wengine.

    Kil alipokuwa akiisikia sauti ya Smith, alimpenda mno, alikuwa na shauku kubwa ya kutaka kumuona uso kwa uso ili awe huru zaidi wa kufanya mambo mengi na ikiwezekana hata kuoana.

    Saa nane mchana walikuwa wakiingia katika Jimbo la Colorado, ndege yao ikaanza kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Denver na kisha kuingia ndani ya gari maalumu lililoandaliwa kwa ajili yao na safari ya kuelekea hotelini kuanza.

    Kitendo cha kufika Denver tu tayari kikampa uhakika Tatiana kwamba ndani ya siku chache zijazo angeweza kuona kitu ambacho kingemfanya kuwa na furaha kuliko siku nyingine katika maisha yake.

    Katika kipindi chote cha safari yao kuelekea hotelini, Smith alikuwa akitumia muda mwingi kumsifia Dk. Buffet tu kwamba alikuwa daktari mtaalamu wa magonjwa ya macho kitu kilichompa uhakika Tatiana wa kuweza kuona tena.

    Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika Hoteli ya Everest ambapo wakateremka na kuchukua chumba hapo. Usiku mzima walilala huku wakiwa wamekumbatiana tu, walifanya vitu vyote ambavyo wapenzi wangeweza kufanya wawapo faragha.

    Kwa Tatiana, hakumkumbuka kabisa Peter, alimsahau mwanaume huyo na hakutaka kukumbuka kama katika maisha yake aliwahi kukutana na mwanaume mwenye jina kama hilo. Smith alimteka, alimpenda na kumuona mwanaume wa kweli ambaye aliletwa duniani kwa ajili yake tu.

    “Kesho ndiyo tunakwenda kumuona daktari, upo tayari?” aliuliza Smith huku wakiwa wamekumbatiana tu kitandani.

    “Nipo tayari mpenzi.”

    “Basi sawa. Nitafurahi kama ukiona jinsi dunia inavyokwenda. Nakupenda sana mpenzi,” alisema Smith huku akiachia tabasamu pana.

    “Nakupenda pia.”

    Asuhbuhi ilipofika, wawili hao wakaamka na kisha kujiandaa kwenda katika Hospitali ya Mount Sinai Medical Center iliyokuwa katikati ya Jiji la Denver ambapo huko wangekutana na daktari huyo wa magonjwa ya macho na kuanza kumtibu Tatiana ugonjwa huo ili aweze kupona.

    Wakachukua gari na kuanza kuelekea huko ambapo baada ya dakika ishirini, walikuwa wamekwishaingia ndani ya jengo la hospitali hiyo na kuelekea ilipokuwa ofisi ya daktari huyo.

    “Karibuni sana,” aliwakaribisha Dk. Buffet.

    “Asante sana. Ndiyo tumekuja,” alisema Smith huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.

    Walikuwa wamekwishazungumza simuni juu ya kitu gani kilichotakiwa kufanywa mahali hapo hivyo hawakuwa na sababu ya kujielezea sana. Alichokifanya Dk. Buffet ni kumchukua Tatiana na kuelekea naye katika chumba cha uchunguzi kilichokuwa na mashine nyingi kwa ajili ya kuwapima wagonjwa uwezo wao wa kuona na hata wale waliokuwa vipofu kabisa.

    “Mkalishe hapo,” alisema Dk. Buffet na kisha Smith kumkalisha Tatiana katika kiti kilichokuwa pembeni kabisa ya chumba kile.

    Alichokifanya Dk. Buffet ni kutayarisha vifaa vyake kwa ajili ya kuanza kazi. Hatua ya kwanza kabia aliyoifanya ni kuyaangalia macho ya Tatiana huku akiyamulika kwa tochi. Hayakuonekana kuwa na tatizo lolote lile zaidi kitu kilichomfanya kugundua kwamba inawezekana tatizo kubwa likawa kwenye mishipa inayoyafanya macho hayo yawe na nguvu ya kuona.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ana tatizo kubwa la mishipa, kuna uwezekano ikawa imelegea, ni tatizo kubwa lakini pia linatibika endapo nitapewa muda zaidi wa kufanya hivyo,” alisema Dk. Buffet.

    “Hakuna tatizo, ninachotaka ni kumuona akiona tu, hakuna jingine.”

    “Basi hakuna tatizo. Kazi ni kubwa na itachukua mwezi mzima.”

    “Hata kama mwaka, ninachohitaji ni kumuona akiona tena.”

    “Basi sawa.”

    “Kwa hiyo kazi inaanza lini?”

    “Leoleo, tena sasa hivi.”

    “Nashukuru sana,” alisema Smith, akamwangalia Tatiana usoni kisha kumbusu shavuni.

    “Nakupenda mpenzi,” alimwambia.

    “Nakupenda pia.”

    “Unakwenda kuona, ninamwamini sana daktari huyu, hautakiwi kuhofia chochote kile,” alisema Smith.

    “Asante mpenzi, hata mimi naamini hilo.”

    Alizungumza naye kwa mara ya mwisho kabla ya kazi ile kuanza rasmi. Dk. Buffet aliwapa nusu saa kuzungumza na kisha kumuomba Smith atoke chumbani na yeye kubaki na mgonjwa ambapo mara moja kazi ikaanza.

    *****

    Peter hakuwa na furaha tena, akili yake ilichanganyikiwa na hata aliporudi shuleni hakuwa akisoma kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma. Kichwa chake kilimfikiria zaidi Tatiana ambaye aliamua kulitupa pezi lake na kumchukua mwanaume mwingine.

    Kila alipokuwa akilikumbuka tukio lile lililofanyika ukumbini, moyo wake ulimuuma mno na kujikuta akimchukia msichana huyo. Muda mwingi Peter alikuwa na mawazo tele, wakati mwingine kila alipokuwa akikaa peke yake, alikuwa akibubujikwa na machozi tu, moyo wake ulijaza maumivu makali yasiyokuwa na mfano.

    Hali ya kuwa na mawazo mengi yakamfanya kutokusoma kabisa, muda mwingi alikuwa akimfikiria msichana huyo ambaye aliweka doa kubwa moyoni mwake.

    Siku zikaendelea kukatika zaidi, hakusoma tena kwani kila alipokuwa akishika daftari kwa ajili ya kusoma, hakuwa akielewa chochote kile zaidi ya kutumia muda mwingi akimfikiria Tatiana.

    “Peter...” aliita rafiki yake.

    “Naaam!”

    “Una nini rafiki yangu?”

    “Kwani kuna nini?”

    “Unaonekana kuwa na mawazo sana, halafu hata kusoma husomi, kila siku unalala tu bwenini, tatizo nini?” aliuliza rafiki yake huyo.

    “Hakuna kitu, muda mwingi najisikia uchovu tu.”

    “Hapana! Nahisi kuna kitu. Hebu niambie rafiki yangu naweza kukusaidia,” alisema rafiki huyo.

    “Usijali. Hakuna kitu.”

    Hakutaka kumshirikisha mtu yeyote juu ya kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake. Kila siku maumivu yale aliyachukulia kama yake na hakutakiwa kumshirikisha mtu yeyote yule. Siku ziliendelea kukatika, mpaka muda wa kufanya mitihani ya mwisho ulipofika, wakafanya na Peter kuelekea Shinyanga kabla ya Mwanza, alitaka kuonana na wazazi wa msichana huyo tu.

    Kama kawaida safari ilikuwa ndefu lakini baada ya masaa kadhaa akafika katika Kijiji cha Chibe na moja kwa moja kuelekea nyumbani kwa mzee Sangiwa. Kijiji kilikuwa kimebadilika, hakikuwa kijiji kilichokuwa na nyumba nyingi za nyasi, kulianza ujenzi wa kujenga nyumba kubwa za matofali ambazo zilitolewa kwa ajili ya wanakijiji tu.

    Mbali na hiyo, kulikuwa na bomba kubwa lililopitishwa chini, shida ya kuchota maji haikuwepo tena. Hakukuwa na haja ya kwenda kuchota maji kisimani, wanakijiji waliwekewa mabomba ya maji huku umeme ukiwa umeletwa kwa wingi kijijini hapo. Kwa kifupi, Tatiana alikuwa akikibadilisha kijiji hicho.

    Kitendo cha kumuona mvulana huyo akiingia ndani ya nyumba yao, mioyo yao ikawa kwenye maumivu makali, walijua ni kwa jinsi gani alikuwa na maumivu moyoni kutokana na kile kilichokuwa kikiendelea.

    “Mama! Kweli Tatiana hatorudi?” aliuliza Peter huku akilengwa na machozi.

    “Hatujajua. Ngoja tusubiri, tutajua hivi karibuni. Amekuwa akituma fedha kwa ajili ya maendeleo ya kijiji na familia, kuhusu kurudi, bado hatujajua,” alijibu bi Frida.

    Peter akajikuta akianza kububujikwa na machozi yaliyokuwa yamemlenga kwa kipindi kirefu, bado hakuwa akiamini kama huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kila kitu. Mapenzi yalipotoea, msichana aliyekuwa akimpenda sana alikuwa ameruka.

    Siku iliyofuata akaamua kurudi jijini Mwanza huku moyoni akiwa na maumivu makali ya moyo. Alipofika Mwanza Mjini, magazeti mengi yalikuwa na habari ya Tatiana. Alikuwa msichana maarufu aliyeiwakilisha Tanzania kuliko mtu yeyote yule.

    Aliifanya Tanzania kuzungumzwa na watu wengi waliokuwa barani Ulaya na nchini Marekani, katika nchi zote zilizokuwa na maendeleo, mtu aliyekuwa akizungumzwa kwa kipindi hicho alikuwa Tatiana tu.

    Kipindi cha nyuma alikuwa na upofu, ila kwa kipindi hiki, hakuwa kipofu tena, alikuwa mzima na aliona vizuri kabisa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tatiana, sitokuacha kukupenda, najua kuna siku utarudi tu,” alijisemea Peter huku akionekana kuumia moyoni mwake.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog